Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Additional Questions to the Prime Minister from Hon. Anton Albert Mwantona (1 total)

MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Spika, nadhani kila mtu anajua faida ya mradi wa makaa ya mawe pale Kiwira Coal Mine. Kwanza huu mradi ulikuwa unazalisha ajira zaidi ya 2,500 kabla haujaisha na mara kwa mara suala hili limejadiliwa hapa kwenye Bunge lako tukufu. Mwaka 2006 iliahidiwa na Wizara hii kwamba huu mradi utaanza mara moja, chini ya Naibu Waziri kipindi kile, Mheshimiwa Dkt. Medard Kalemani; mwaka 2018 pia ikajadiliwa hivyo kwamba mradi utaanza mara moja, sasa hivi tunaambiwa tena kwamba wako katika hatua za mwisho.

Je, ni lini ukarabati wa mgodi huu wa mawe utakamilika na tunategemea kuajiri watu wangapi? Kwa sasa hivi katika sehemu hii ndogo tumeajiri watu 28 tu lakini capacity ya kwanza ilikuwa ni watu 2,500.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni lini Serikali itatoa ahadi ya uhakika kwa sababu 2016 tumeahidiwa, 2018 tumeahidiwa, sasa hivi tunaambiwa tena mradi utaanza; ni lini Serikali itatoa ahadi ya uhakika ambapo sasa tutapata ajira za kutosha kwa wananchi lakini pia tutapata za huduma za kiuchumi kwa Wilaya za Rungwe, Kyela pamoja na Ileje? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyotoa majibu katika swali la msingi, ni kweli kwamba Shirika liko katika maongezi na TANESCO ili kukamilisha hatua za mwanzo kwa ajili ya uchimbaji kuanza. Napenda Mheshimiwa Mbunge ajue kwamba taratibu za uchimbaji zinahusisha upembuzi yakinifu kwa sababu unapokuja kuwekeza unawekeza fedha nyingi. Kwa hiyo, tunapokuwa tunasema kwamba upembuzi yakinifu unafanyika, lengo ni kwamba tunapoingia katika uchimbaji tuweze kuingia kwa namna ambayo tunajua kile kilichopo, fedha inayoingizwa na hatimaye kupata faida.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu tuko katika maongezi na kuhitimisha hatua hizi, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili litafanyika baada ya kuhitimisha hatua hizi za mwanzo. Ajira zinazotarajiwa kupatikana tunaweza tukazipata baadaye baada ya kuwa tumemaliza upembuzi wote yakinifu kwa ajili ya mradi.

Mheshimiwa Spika, napenda kutoa majibu hayo.