Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Mwanaidi Ali Khamis (14 total)

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha kwa majibu yake mazuri na amenipa mwongozo na yametoa matumaini, lakini nina maswali mawili mdogo ya nyongeza: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa ni wengi walioweka amana zao pale walitumia viinua mgongo vyao kuweka amana katika Benki ya FBME, hasa kule kwetu Zanzibar nilikotoka. Amesema wamelipwa wateja nusu na waliobakia bado hawajalipwa na watakaolipwa watalipwa kutokana na fedha ambazo watapata amount ambayo haitazidi 1,500,000/=; na kwa kuwa hii benki ni ya nje; na kwa mujibu wa Sheria ya Benki na Financial Institutions, BOT ndio wenye dhamana ya kukaribisha mabenki ndani, swali langu;’ je, ni lini watalipwa fedha zao zote kwa sababu, benki hii haijafilisika FBME?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni lini Benki Kuu ya Tanzania itaacha kuingiza benki hovyo hovyo kama hizi za kutoka nje zikaleta madhara katika nchi yetu? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Hassan King kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza alilouliza Mheshimiwa King amesema kwamba, lini wateja hao ambao wana amana zao katika benki ya FBME watapatiwa fedha zao. Kama nilivyoeleza katika jibu la msingi, wateja waliokuwa na amana zaidi ya shilingi 1,500,000 watalipwa kiasi kitakachobaki chini ya zoezi la ufilisi wa benki ambapo kwa mujibu wa sheria na taratibu kiasi kitakacholipwa kitategemea fedha zitakazopatikana kutokana na kuuza mali za benki husika. Suala hili liko chini ya mujibu wa sheria, kwa hivyo sheria zitakapomalizika Mheshimiwa King basi, wateja wote wenye amana katika benki hiyo watalipwa pesa zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; anaulizia lini benki zitatoa ukomo wa kuchukua benki ambazo hazina faida katika nchi yetu. Mheshimiwa King jibu lako la pili naomba nilichukue ili nikalifanyie kazi na nitakujibu kwa barua ili uelewe maelezo zaidi katika Serikali yetu, uweze kupata ufafanuzi zaidi wa kupata jibu lako sahihi. Ahsante. (Makofi)

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa. Nataka tu niongezee kakipengele kadogo kale ambako kanaongelea lini hawa watu watapata fedha. Kwa benki hii ambayo Mheshimiwa Mbunge ameuliza utaratibu huu ambao ameuelezea Mheshimiwa Naibu Waziri umekuwa mrefu kwa sababu benki hii ilikuwa ina-operate katika nchi mbili. Kwa maana hiyo, ule utaratibu wa mufilisi kuweza kukusanya madeni na kukusanya na mali zote ili azibadilishe ziwe fedha ili aweze kuwalipa wale wateja ambao amana zao zilikuwa zinazidi kile kiwango cha awali ambacho wanapewa pale benki inapokuwa kwenye mufilisi, kikamilike. Kwa hiyo, hicho kikishakamilika hapo ndipo ambapo mufilisi ataweza kufanya hiyo kazi ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameisema na hawa wateja waweze kupata hizo fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili la pili ambalo Mheshimiwa muuliza swali ndugu yangu King amesema ni lini Benki Kuu itaacha kuruhusu mabenki yaingine hovyo hovyo. Nimhakikishie kwamba, mabenki hayaingii hovyo hovyo na Serikali inafanya due diligence kwa kila benki inapotaka kufanya kazi hapa nchini na ndio maana Benki Kuu iliingilia kati ilipoona baadhi ya mabenki hawaendi sawasawa na vile ambavyo yanatakiwa yafanye kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe rai tu kwa wananchi wetu kwa sababu, huwa kuna report zinazotolewa kila miezi mitatu na kunakuwepo na mkutano mkuu wa wadau wa benki na sisi tuwe tunafuatilia ili tuweze kuona mienendo ya benki. Tusisubirie tu Benki Kuu ambaye ni msimamizi aweze kufanya jukumu hilo ambalo linawahusu pia, wadau wadau wa benki ambao wanatakiwa watoe muongozo kwa benki yao. (Makofi)
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa wewe ni miongoni mwa watu waliofika Jimboni kwetu na kuona namna ambavyo tunalima miwa kwa bidii kwa kufuata kauli ya Mheshimiwa Rais ya nchi kujitegemea katika suala zima la sukari; na kwa kuwa hao wenye viwanda ndio waliopewa vibali vya kuingiza sukari inayopungua katika nchi yetu, je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka mwekezaji mwingine wa kiwanda ili kuondoa monopolism ya kiwanda ambacho kipo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Waziri na Mawaziri husika katika sekta hii ya kilimo na viwanda na biashara, watakuwa tayari kuambatana nami baada ya Bunge hili, kwenda kuwasikiliza wananchi hasa wakulima wa miwa Jimboni kwangu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abubakari, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, Serikali inaona umuhimu wa kuongeza uwekezaji wa viwanda vya sukari nchini hasa katika Kiwanda cha Kilombero ili kuongeza uzalishaji wa sukari nchini. Kwa upande wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero, Serikali na mbia mwenza, iko katika majadiliano ya kupanua kiwanda hiki na hatimaye kuongeza uzalishaji wa sukari ili miwa yote inayolimwa iweze kutumika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, napenda kumwahidi Mheshimiwa Abubakari kwamba niko tayari kuongozana naye pamoja na wataalam wangu kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina ili kujionea hali halisi ya uzalishaji katika kiwanda hicho, pale tutakapopata nafasi mara baada ya mkutano huu wa Bunge kuahirishwa. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UWEKEZAJI): Mheshimiwa Spika, ahsante na naomba kuongezea majibu kwa majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba Serikali iko kwenye mazungumzo na wawekezaji kadhaa angalau watatu ambao wana nia ya kuwekeza katika kujenga viwanda vipya vya sukari. Naamini kwa mazungumzo hayo, tukiwapata tutapunguza sana tatizo la sukari na nia ya Serikali ni kuona kwamba katika mwaka mmoja ujao tunajitosheleza kwa mahitaji ya sukari hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili ni kwamba, wiki ijayo baada ya Bunge hili mimi na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo tuna ziara katika Mkoa wa Morogoro na tutajitahidi tufike pia jimboni kwa Mheshimiwa ili kuweza kuona changamoto. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini Lukumbule ni lango kubwa ambalo wafanyabiashara wanapita kupeleka bidhaa zao Msumbiji na wale wanaotoka Msumbiji wanapita Lukumbule kuleta Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali imekubali kufanya tathmini na kwa kuwa wananchi wa Tanzania wanaopeleka bidhaa Msumbiji mara nyingi hunyang’anywa mali zao kwa kukosa documents za kusafirisha mizigo yao kwenda Msumbiji.

Je, Serikali haioni haja ya haraka kufanya tathmini hiyo ili kuhakikisha wananchi wetu wa Tanzania wanaoenda Msumbiji hawanyang’anywi mali zao mara kwa mara? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa Jimbo la Tunduru Kusini lina miji mitano mikubwa; Nalasi, Mchoteka, Malumba, Lukumbule pamoja na Misechela ambayo ina wafanyabiashara wengi na miji hiyo iko zaidi ya kilometa 80 kutoka ilipo Ofisi ya TRA Tunduru Mjini.

Je, Serikali haioni haja ya kupeleka agencies katika maeneo hayo ili wafanyabiashara wale waweze kulipa kodi zao wakiwa katika maeneo yao ya biashara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeona umuhimu wa ushauri wa Mheshimiwa Mbunge. Kwa hiyo, ushauri tumeupokea na tutaufanyia kazi kwa mujibu wa sheria na miongozo iliyowekwa na pale tutakapopata majibu basi tutamfikishia majibu kwa haraka sana. (Makofi)
MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri lakini naomba niulize maswali ya nyongeza mawili kama ifuatavyo:-

Swali la kwanza; ni dhahiri kuwa Taifa letu linahitaji wawekezaji wengi kutoka Mataifa mengine, lakini naamini itakuwa ni ngumu kupata wawekezaji ikiwa hawa tu tulionao wanashindwa kuwekeza kutokana na mrundikano mkubwa wa kodi zilizoko ndani ya Taifa letu.

Sasa nataka kujua je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kulichukua jambo hili na kufanya marekebisho ya sheria za kodi ili wananchi wetu waweze kufanya biashara kwa uhuru? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa TRA wamekuwa na utaratibu wa kufanya makadirio ya kodi wanapofika kwenye biashara za watu; ni nini tamko la Serikali katika hili maana TRA wamekuwa wakiwakadiria watu kodi kubwa ambazo zinazidi mitaji yao na kusababisha watu wengi kufilisika na kufunga biashara. Ni nini tamko la Serikali kwa hiki kinachoendelea leo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Stella Fiyao kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kutokana na mazingira mazuri na rafiki hakuna ukandamizaji wa kodi kwa wananchi/wafanyabiashara atakayekimbia kwa kufanya biashara kwa sababu ya kulipa kodi kubwa ambazo Serikali imeziweka kiurafiki na kulipa kodi kwa sheria na utaratibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la pili la Mheshimiwa Stella Fiyao kuwa kama Mheshimiwa anaona kuna kodi kandamizi ambazo wafanyabiashara wanapatiwa basi tungemuomba atuletee changamoto hizo na Serikali itazifanyia kazi kwa mujibu wa sheria na mipango yote iliyowekwa katika Serikali. (Makofi)
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa sheria inawaruhusu wachezesha bonanza kulipa asilimia 0.03 ya mapato yao, nataka kumuuliza Waziri, je, ni nani anayejumlisha mapato yao kwa mwaka?

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Wachina hawa wanaochezesha mabonanza wanarundika pesa zao nyumbani wala hawapeleki benki. Mfano mzuri ilitokea Morogoro, ulipofanyika msako Morogoro walikutwa na bilioni 2.5, ukafanyika msako Arusha wakakutwa na bilioni 5.0 ndani. Sasa sisi kama Halmashauri kupata ile asilimia tunayoitaka kwenye levy tunaipataje? Je, Serikali wako tayari kuruhusu kwamba, kule Halmashauri tuweke makufuli pamoja pale kwenye zile slot machine, ili wanapoenda kufungua watendaji wetu tujumuike nao ili tuweze kupata hesabu vizuri kwa ajili ya kukusanya hiyo service levy? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Musukuma, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi wanaohusika na ukusanyaji wa mapato ya service levy ni Mamlaka ya Serikali za Mitaa wenyewe kwa mujibu wa sheria iliyowekwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, naomba kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Musukuma kwamba, anajali na anaijali Serikali kwa kuangalia uchumi wa nchi unavyokwenda. Hata hivyo, Mheshimiwa Musukuma ushauri wake tumeuchukua na tutaufanyia kazi kwa mujibu wa sheria kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kama ilivyo sheria. (Makofi)
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakubaliana na Serikali kwamba kifungu cha 9 (1)(j) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 kinaipa mamlaka PPRA kufanya kazi nyingine ikiwemo ya kuandaa mifumo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri atakubaliana kwamba mfumo huu wa TANePS umeandaliwa na wataalam wa nje kupitia mradi uliofadhiliwa na Benki ya Dunia; lakini atakubaliana na mimi, kwamba Serikali kupitia wataalam wa ndani kupitia Wizara ya Fedha imeandaa mifumo ambayo inafanya kazi kwa ufanisi mkubwa ukiwepo huu wa GPG, MUSE na GSPP.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Juzi tumeona Mheshimiwa Rais wakati anapokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, ameonesha nia ya kuitaka serikali kuwa na mifumo michache ili kuongeza ufanisi.

(i) Je, Serikali haioni kwamba kuendelea kuwa na mifumo mingi kwenye taasisi nyingi itaendeleza urasimu badala ya ufanisi?

(ii) Kwa kuwa mfumo huu ukiuangalia na kwa language iliyoandikwa na wataalam hao wa nje haikuzingatia business concept ya nchi, yetu na mfumo huu umekuwa na matatizo mengi, hata siku mbili zilizopita mfumo huu ulikuwa chini na kuleta matatizo makubwa kwenye manunuzi.

Je, haoni kwamba ni wakati muafaka sasa kupitia kurugenzi yetu ya taarifa za mifumo ya fedha pale Hazina tutapunguza gharama kwa ku-integrate mfumo huu na mifumo ambayo nimeitaja hapo juu? (Makofi).
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Silaa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa mfumo wa TANePS tayari umeshaunganishwa na mifumo mingine ya GPS na taratibu zinaendelea ili kuunganisha na mifumo mingine ya serikali ikiwemo mifumo ya MUSE nakadhalika ili kupunguza gharama za uendeshaji Serikalini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Slaa, ni kama alivyoeleza Mheshimiwa Rais katika hotuba yake ya juzi alipokuwa akipokea taarifa za CAG; kuhusu kuunganisha mifumo ya malipo yote ya Serikali ili kubaki na mifumo michache ili kupunguza gharama za uendeshaji. Kwa hivyo, Mheshimiwa Rais amesema kwamba tuwe na mifumo michache ambayo inaweza kuendesha Serikali na kupunguza gharama za Serikali ili kuondoa usumbufu na upotevu wa fedha za Serikali. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali bado kuna tatizo. Wengi wa wateja waliokuwa wa benki hii ambayo ilifutiwa leseni pamoja na wanahisa ni wanyonge, ni watu ambao wasingeweza kusubiri kwa muda mrefu wakisubiri amana zao zilipwe. Pamoja na kwamba kuna ambao walilipwa 1,500,000/= kwa kupitia DIB naona kwamba suala la muda ni changamoto. Wateja wengi hawataweza kusubiri kwa muda mrefu kiasi hiki, sasa hivi ni miaka mitatu na miezi mitatu tangu benki hii ifutiwe leseni.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali itamke bayana, je, ni lini itamaliza tatizo hili kwa kulipa amana zote kwa wana hisa na wateja ambao walikuwa wa benki hii?

Mheshimiwa Naibu Spika na ninaomba hapa ni- declare interest, kwamba mimi mwenye nilikuwa mwanahisa wa benki hii nasubiri hiyo pesa kwa miaka mitatu sasa, ningeipata ningenunua hata ng’ombe. Naomba majibu ya Serikali.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa John kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi, Bodi ya Bima ya Amana bado inaendelea na zoezi la ufilisi wa mabenki na itakapokamilisha ufilisi wateja wote waliozidi zaidi ya shilingi 1,500,000/= watalipwa fedha zao kulingana na mapato yaliyokusanywa na kupatikana kutokana na benki husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, Mheshimiwa Mbunge, changamoto ambazo wanazipata katika benki ya amana mpaka sasa hivi ni wale ambao waliokopeshwa fedha hizo bado wanaendelea kuwa na ugumu wa kulipa. Hata hivyo Serikali inaendelea kutafuta taratibu nyingine ili kuhimiza wale waliokopeshwa kulipa madeni hayo ili wateja wanaodai fedha zao katika benki hiyo waweze kulipwa kwa haraka. Ahsante.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, akina mama wa Mkoa wa Tanga ni watafutaji na wachapakazi, wamejiunda kwenye vikundi lakini wanakosa tija kwa kukosa elimu ya kuandaa maandiko ya miradi na namna ambavyo wanaweza kuunganishwa kwenye taasisi za fedha ili waweze kupata mikopo. Je, ni lini Serikali italeta makongamano hayo ambayo Serikali imeyafanya katika mikoa mingine kwenye Mkoa wa Tanga ili akina mama hawa na wenyewe waweze kupata ujuzi huo kwa ajili ya kuendeleza shughuli za ujasiliamali?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, elimu ni kitu endelevu; makongamano pekee yanaweza yasikidhi ile haja ya akina mama wa Mkoa wa Tanga. Je, ni kwa namna gani sasa Serikali inajipanga kuimarisha Ofisi za Maendeleo ya Jamii kwenye Halmashauri zetu ili ziweze kutoa elimu hii ya uandishi wa maandiko ya miradi pamoja na kuwasaidia akina mama na taasisi za kifedha badala ya kutegemea zile za Halmashauri peke yake?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Husna, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi, hadi sasa Serikali imeshafanya makongamano katika mikoa mitano kati ya mikoa 26 nchini. Katika mikoa hiyo 26 Tanga ni mkoa mmojawapo kati ya mikoa 21 ambayo haijapata mafunzo hadi sasa. Tunategemea kupata rasilimali fedha na baada ya kupata rasilimali fedha hizo tutafanya makongamano hayo katika mikoa iliyobaki. Nimuombe tu Mheshimiwa Husna awe mstahamilivu kwa hili, Serikali tumeshajipanga kuendesha makongamano hayo wakati wowote tutakapopata fedha hizo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili Mheshimiwa Husna amesema vipi tutawezesha halmashauri ili wanawake waweze kupata elimu. Serikali imeshaanza kuweza halmashauri nchini na katika mwaka 2000 imeandaa miongozo ya utoaji mikopo kwa ajili ya vikundi mbalimbali vya wanawake ikiwemo kuwapatia elimu ya ujasiliamali na mafunzo ya uendeshaji wa biashara kabla na baada ya kupata mikopo. Hata hivyo, mwongozo huo umeambatanishwa na mfano rahisi wa andiko la miradi ulioandikwa na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika kutoa elimu kuhusu namna ya kuandaa andiko hilo.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Husna kwa kuwapigania wanawake wa mkoa wake ili waweze kupata elimu ya kiuchumi kwa ajili ya kuondoa umaskini.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, sheria zilizopo bado kuna changamoto kubwa sana katika eneo hili na ndiyo maana hata Chama cha Mapinduzi kwenye Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025 kimeliona hili na kimeahidi kwamba kitaelekeza Serikali kwenye ukurasa wake wa 145 inasema hivi; “Chama cha Mapinduzi kitaelekeza Serikali kuimarisha huduma za usuluhishi wa migogoro ya ndoa na matunzo kwa watoto.” Kwa msingi huu naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza, je, Serikali haioni saa ipo haja ya kurekebisha sheria zilizopo ili gharama ya matunzo ya watoto iendane na hali ya uchumi wa sasa na maisha ya sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili kwa kuwa vitendo vya masuala ya familia vimezidi kushamiri; je, Serikali haioni sasa iko haja ya kuanzisha Mahakama ya Familia (Family Court) kama walivyofanya kwenye Mahakama ya Ardhi ili masuala haya ya matunzo ya watoto yaweze kubebwa kwa uzito unaostahili na kupanua wigo wa haki? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. MWANAIDI ALI KHAMISI): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaungana na Mheshimiwa Mbunge kuwa kuna haja ya chombo maalum kitakachokuwa kinashughulikia masuala ya familia. Ushauri wake tumeupokea na tutaufanyia kazi kulingana na sheria zilizopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, Serikali iweke kiwango cha matunzo kitakachozingatia hali ya uchumi ya sasa kusaidia matunzo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi kuwa huduma za matunzo ya watoto umetolewa kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 kifungu cha 44(a) na (e) sheria hii imeipa mamlaka Mahakama kufanya maamuzi ya kuzingatia mambo yafuatayo; kuangalia kipato cha wazazi wote wawili, ulemavu wowote na uwezo wa kipato cha mzazi katika jukumu la kutunza mtoto, wajibu wa majukumu ya mzazi katika kutoa matunzo kulinganisha na majukumu ya kutoa matunzo kwa watoto, gharama za maisha katika eneo ambalo mtoto anaishi na haki nyingine za kisheria ambazo mtoto anahitaji kupatiwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, changamoto ya wanawake kutelekezewa watoto imekuwa kubwa sana; je, Serikali haioni umuhimu wa kubadilisha kuleta mabadiliko ya Sheria ya Ustawi wa Jamii Bungeni ili iendane na hali halisi ya maisha ya sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. MWANAIDI ALI KHAMISI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hawa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, tumelipokea ombi la Mheshimiwa Mbunge na tutalifanyia kazi kwa mujibu wa sheria zilizopo ili wanawake waweze kupata haki zao kikamilifu. (Makofi)
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kutokana na majibu ya Mheshimiwa Waziri kwanza niipongeza Serikali kwa kuona kuna haja ya kuwa na mpango mkakati wa Taifa wa kutokemeza ukatili. Hata hivyo, inashangaza kuona Serikali yenyewe imejiwekea asilimia 50 tu kutokomeza matendo haya, ifikapo 2022.

Mheshimiwa Spika, malengo haya bado yako chini na tunawapa mwanya…

SPIKA: Mheshimiwa Zaytun nenda kwenye kuuliza swali.

MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; je, Serikali haioni kama kuna haja ya kujiwekea malengo ya juu ambayo yatadhibiti matendo haya na kukomesha?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa vitendo hivi vingi vinafanyika kwenye ngazi za kata na za vitongoji lakini madawati ya kijinsia mengi yapo kwenye ngazi za wilaya. Je, Serikali haioni kama kuna haja ya kushusha huduma hii kwenye ngazi za chini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. MWANAIDI ALI KHAMISI): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Zaytun kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika jibu langu la msingi nilieleza kuwa, mpaka sasa Serikali imeshaanzisha madawati 420 ya jinsia ya watoto kwa vituo mbalimbali nchini. Aidha, ningependa kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa huduma za wahanga wa ukatili zinafanyika katika kila Kituo cha Polisi na kila Kituo cha Polisi kimewekwa chumba maalum kwa ajili ya kuwahudumia wahanga hao.

Mheshimiwa Spika, vilevile wahanga hao wa ukatili uhudumiwa na Polisi ambao masuala yao yote huanzia katika Vituo Vidogo vya Polisi na kumalizia Vituo Vikubwa vya Polisi kwa ajili ya kushughulikiwa zaidi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili Mheshimiwa Zaytun, ni kweli kuwa kuna sababu ambazo zinasababisha vitendo vya ukatili wa kijinsia ni uwepo wa imani za ushirikina. Serikali ishaanza kushughulikia suala hili ili kutekeleza mpango wa Taifa na kutokomeza ukatili dhini ya wanawake na watoto. Aidha, nimuahidi kuwa nitalifuatilia suala hili na kuhakikisha wanawake wote wa Arumeru na Monduli wanakuwa salama pasipo na kunyanyaswa. Pia ni watake Maafisa wa Maendeleo ya Jamii Arumeru na Monduli kupanga mpango kazi maalum ili kuwaendeleza wananchi wa Arumeru kukabiliana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji. Ahsante.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na majibu ya Serikali kwamba nchi yetu inaongozwa kwa mujibu wa sheria mbalimbali. Swali la kwanza; kwa kuwa sheria hizi huwa zinafanyiwa marekebisho kadri uhitaji unavyotokea au wakati. Je ni lini sasa Serikali italeta marekebisho ya sheria hii ili kuwapa nafasi nzuri zaidi waathirika kuripoti haya matukio?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa Vituo hivi vya Mkono kwa Mkono ni vichache, vinakadiriwa kuwa
14 nchini na uhitaji ni mkubwa kwa sababu tunahitaji kuwatunza wale waathirika kwenye vituo hivyo kabla ya mashauri kukamilika ili kulinda uchunguzi. Je Serikali ina mpango gani sasa kwa ajili ya kuongeza vituo hivi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Husna, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la kwanza kwa nini dawati hilo halishirikishwi na vituo vya hospitali; kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi dawati hili hushirikiana na Vituo vya Mkono kwa Mkono na pia hushirikiana na Jeshi la Polisi, huduma za afya pamoja na wanasheria ili kuhakikisha kwamba waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia hupata huduma stahiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuongezea kwamba, sio kila wahanga waathirika wa vitendo vya ukatili wa jinsia, wanahitaji huduma za afya; waathirika wengine wanahitaji huduma za kisheria, unasihi, na msaada wa kisheria ili kuona kwamba wanapatiwa huduma stahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, je ni lini sasa Serikali litaleta marekebisho hayo Bungeni. Napenda kumweleza Mheshimiwa Mbunge kwamba, hadi sasa hatujapata ugumu wa marekebisho ya sheria ya masuala ya ukatili wa kijinsia. Kwa hivyo nimwombe Mheshimiwa Husna atuletee marekebisho au maboresho ya dawati hili ili Serikali iweze kuangalia zaidi maboresho hayo na muathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia aweze kupata huduma na kuweza kuleta malalamiko yake bila ya kuwa na hofu kwa kutumia sheria ambazo zimewekwa. (Makofi)
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali moja la nyongeza. Kutokana na majibu yaliyotolewa na Serikali, inaonyesha ni dhahiri ni Halmashauri mbili tu kati ya Halmashauri 184 nchi nzima ambazo zimepatiwa pikipiki. Hali hii inaonyesha jinsi ambavyo upo uhitaji mkubwa katika Halmashauri nyingine. Je, Serikali ina mkakati gani wa makusudi kuhakikisha kitengo hicho kinawezeshwa kibajeti katika Halmashauri zote? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. MWANAIDI ALI KHAMISI): Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Josephine kwa kufuatilia Maafisa hawa na kuona umuhimu wa kazi zao wanazozifanya.

Mheshimiwa Spika, ni kweli Maafisa hawa wana changamoto kubwa ya vitendea kazi. Mimi mwenyewe binafsi baada ya kumalizika Bunge la Bajeti niliweza kutembelea mikoa mitatu pamoja na Wilaya zake, yaani Mkoa wa Tabora, Iringa na Ruvuma na nimekutana na Maafisa hawa wa Ustawi wa Jamii wakanielezea changamoto zao.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Wizara inaendelea na mikakati ya kuwasiliana na wadau wa Maendeleo ya Jamii ili pamoja na miradi ambayo wanaitekeleza na wadau hao, kuwawezesha Maafisa hawa wa Jamii kuendelea kupata vifaa vya kufanyia kazi kulingana na mazingira yao waliyokuwa nayo.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inawajali sana wafanyakazi pamoja na wananchi wake. Kwa hili tumelipokea na tutaendelea kulifanyia kazi suala hili la upatikanaji wa vitendea kazi kwa mikoa yote nchini Tanzania. Ahsante, napenda kuwasilisha.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa fursa hii.

Mheshimiwa Spika, kutokana na uhalisia kwamba halmashauri zetu nyingi nchini zina changamoto sana ya miundombinu. Serikali haioni kuna haja ya kubadilisha usafiri kutoka kwenye pikipiki na kuwapatia magari maafisa maendeleo ya jamii hawa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa urahisi na kwa uwanda mkubwa? Kwa mfano, kipindi cha mvua mtu huyo atatumiaje pikipiki maana yake atakuwa analowa, hawezi kutekeleza majukumu yake. Serikali haioni umuhimu wa kuwanunulia magari maafisa maendeleo ya jamii ikiwa ni pamoja na Jimbo la Momba?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. MWANAIDI ALI KHAMIS): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali moja la nyogeza la Mheshimiwa Condester kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli, maafisa hawa wanatembea kwa pikipiki kwa ajili ya kufuatilia wafanyakazi hawa au vitendo mbalimbali vinavyotokea katika jamii. Serikali kama nilivyoeleza imejipanga kuzungumza na wadau ambao wanaendeleza maendeleo haya ya jamii ili kuhakikisha kwamba maafisa hawa hawatopata tabu katika kazi zao katika mazingira yao ya kazi kwa mujibu wa sheria zilizopo, ahsante nashukuru. (Makofi)