Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. John Michael Sallu (7 total)

MHE. JOHN M. SALLU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini naomba Serikali ituhakikishie kwamba, katika kipindi hicho cha miezi tisa kweli huu mradi unaweza kumalizika maana tuna shida kubwa sana ya maji pale. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kitandula kwa kuwasilishwa na Mheshimiwa John Sallu kwamba, Serikali tumejipanga ndani ya miezi tisa mradi utakamilika na tunaendelea kuongeza nguvu kuhakikisha ikiwezekana kabla ya miezi (9) kufika iwe imekamilika.
MHE. JOHN M. SALLU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Kule handeni kuna barabara inayotoka Magore - Turiani mpaka Handeni. Barabara hii ina ahadi nyingi za viongozi wa Serikali na vile vile barabara hii inaunganisha Mkoa wa Tanga na Morogoro na ni barabara fupi kwa kuja Jijini Dodoma.

Sasa niulize, ni lini Serikali itamalizia kile kipande cha Turiani - Handeni kwa kiwango cha lami? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa John Marco Sallu, Mbunge wa Handeni Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia barabara zinazopita katika jimbo lake. Kwa swali alilouliza, nataka nimhakikishie kwamba dhamira ya Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan ni kuifungua Tanzania; na kuifungua Tanzania ni kuhakikisha kwamba miundombinu na hasa barabara zinajengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja ya Magole - Turiani hadi Handeni ni sehemu ya barabara inayotoka Korongwe - Handeni - Mzia -Turiani - Magole kwenda Kilosa hadi Mikumi. Barabara hii iko kwenye mpango, kwa hiyo, Serikali inatafuta fedha, maana imeshajenga Magole hadi Turiani; sasa hivi inatafuta fedha za kujenga Turiani kwenda Handeni.

MHeshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba iko kwenye mpango wetu na hata kwenye vitabu vya bajeti inaonekana hivyo. Kwa hiyo, avute Subira, barabara itakamilishwa kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. JOHN M. SALLU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Kata ya Sindeni pana Kituo cha Afya cha Tarafa ambako mawasiliano ni shida kabisa. Vilevile katika Mji wa Mkata ambako ni Makao Makuu ya Halmashauri, imejengwa Hospitali ya Halmashauri pamoja na Makao Makuu ya Halmashauri kilometa nne tu kutoka katikati ya mji, lakini mawasiliano yanasuasua: Je, ni lini Serikali itafanya hatua za makusudi kabisa kuhakikisha taasisi hizo za kiserikali zinapata mawasiliano ili mifumo ifanye kazi na wananchi kupata huduma stahiki haraka iwezekanavyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa John Marko Sallu, Mbunge wa Handeni Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ushirikiano wake mzuri ambao ametupatia hasa pale nilipofanya ziara katika Jimbo lake. Katika eneo hili ambalo ni la Sindeni, natambua kabisa kwamba kuna changamoto ya mawasiliano ambapo kulikuwa na mnara uliokuwa umejengwa kilometa 21 kutoka Makao Makuu ya Kata ambao haukuweza kufikisha huduma ya mawasiliano maeneo ambapo hiki Kituo cha Afya kilipojengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimuahidi kwamba wataalamu wetu wataenda pale, watafanya tathmini, watakapojiridhisha ni namna gani tufanye, basi tutaingiza katika mpango wa utekelezaji. Kwa upande wa Kata ya Mkata ni kilometa nne. Kwa aina ya spectrum ambazo tunatumia nine hundred na eighteen hundred, ukiangalia hapa bado iko katika range. Kikubwa hapa, tutaenda kuliangalia tatizo ili tuweze kuongeza nguvu ya minara iliyopo katika Kata hii ya Mkata ili kuhakikisha kwamba Halmashauri na Hospitali zilizopo katika maeneo haya ambayo ni kilometa nne, zinapata huduma ya mawasiliano bila kuwa na changamoto yoyote, ahsante.
MHE. JOHN M. SALLU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa barabara ya Sindeni – Kwedikwazu ni barabara muhimu na kuna idadi kubwa ya watu na vilevile inatumika kutoa mazao mengi; na kipindi cha mvua inasumbua sana. Je, ni lini Serikali itaitengeneza barabara hiyo kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa John Marko Saluu, Mbunge wa Jimbo la Handeni Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba Serikali ina mpango wa kuhakikisha barabara zile zenye shida kutafuta fedha ili tuzitengee na kuzijenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge najua anafanya kazi nzuri ya kuwatetea wananchi wake katika Jimbo la Handeni Vijijini, kwa hiyo katika hilo nimwambie tu kwamba kadri tutakavyopata fedha basi eneo lake tutalizingatia sana.
MHE. JOHN M. SALLU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, kwa hiyo wananchi wa Handeni tunategemea hivi karibuni michakato itaanza, nina swali moja la nyongeza.

Barabara itokayo Chalinze mpaka Segera, hasa kile kipande kinachoanzia Manga mpaka Segera zinatokea ajali nyingi sana na kupoteza nguvu kazi kubwa sana ya nchi hii, na sababu kubwa ni wembamba wa barabara na kona nyingi.

Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kufanya maboresho kwenye barabara hiyo ili tuweze kuondoa vifo hivi vya wananchi wa kitanzania na majeruhi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa John Marko Sallu, Mbunge wa Handeni Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mhshimia Mwenyekiti, barabara ya Chalinze hadi Segera ni barabara ambazo ni barabara standard kwa maana ina upana wa mita 6.5 kwa maana kila upande mita 3.25 na hizo ndiyo barabara zilizo nyingi. Ninatambua kwamba ni kweli kuna ajali nyingi zinataokea lakini ambacho tumekifanya tumetenga fedha kwa ajili ya kufanya economic study na usanifu wa barabara hiyo kwenye maeneo ya miinuko, kona na kuhakikisha kwamba barabara hii ipanuliwe hasa kwenye maeneo ambayo watu wameongezeka kwenye vijiji na kuongeza upana wa mabega.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafanya economic study na feasibility study ambayo tutaanza mara moja kwa ajili ya kupunguza ajali ili watu waweze kuonana kwa umbali, ni barabara ambayo imeinuka sana, ukilinganisha na yaani embankment yake ni ya juu. Kwa hiyo, hilo tumeshaliona na Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kufanya hiyo study na economic study. Ahsante.
MHE. JOHN M. SALLU: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini kule kwenye Tarafa ya Kwamsisi ni tarafa iliyoko pembezoni sana. Sasa ni lini Serikali itaona umuhimu wa kujenga Kituo cha Afya katika Kata ya Kwa Msisi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Handeni Vijijini tuna upungufu mkubwa sana wa watumishi, takribani tuna upungufu wa zaidi ya asilimia 60. Sasa je, ni mkakati gani wa Serikali katika kupambana na upungufu huo wa watumishi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA YA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la kwanza la Tarafa ya Kwamsisi ni lini itapata kituo cha afya; nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika mwaka wa fedha 2024/2025, tarafa hii na Kata ya Kwa Msisi itatengewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya.

Mheshimiwa Spika, nikienda katika swali lake la pili la upungufu wa watumishi, kama ambavyo wote ni mashahidi katika Bunge lako hili tukufu, Serikali inaendelea kuajiri na hivi sasa kuna ajira zaidi ya 21,000 ambazo zimetangazwa na Serikali itaendelea kuajiri vile vile kadri ya uwezo wake wa kibajeti na katika hawa watumishi 21,000 ambao wanaajiriwa hivi karibuni vile vile Handeni Vijijini watapata watumishi.
MHE. JOHN M. SALLU: Mheshimiwa Spika, Jimbo letu la Handeni Vijijini lina vitongoji takribani 770; sasa ni lini Serikali itaona umuhimu wa kupeleka umeme wa REA katika vitongoji hususani vile ambavyo vina kaya nyingi? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa John Marko Sallu, Mbunge wa Handeni Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama tulivyoeleza katika Bajeti yetu ya Wizara ya Nishati kwa mwaka ujao wa fedha Serikali imeanza program mahususi ya kupeka umeme vitongojini na tumetenga shilingi bilioni 140 kama sehemu ya maandalizi ya kazi hiyo ambayo itaongezeka kasi yake pale ambapo tutakuwa tumepata rasilimali za kutosha, lakini ni kweli kwamba baada ya kupeleka umeme katika maeneo mengi ya vijijini, maeneo ambayo yanasubiri umeme ni ya vitongoji na vitongoji hivyo katika Wilaya ya Handeni Vijijini pia vitazingatiwa katika mipango ya Serikali ya kupeleka umeme vitongojini.