Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. John Michael Sallu (4 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. JOHN M. SALLU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Namshukuru Mwenyezi Mungu, namshukuru Mwenyekiti wa Chama chetu cha Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, nashukuru Chama chetu cha Mapinduzi, nashukuru wananchi wa Handeni Vijijini na wadau wote walionifanya niwepo hapa ili kuwatumikia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli napongeza sana juhudi zilizofanywa katika kuandaa Mpango huu. Namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa kuandaa Mpango mkakati utakaotutoa sehemu moja kwenda sehemu nyingine. Ndugu zangu si dhambi kushukuru na kupongeza juhudi zilizofanywa katika kuanzisha miradi mikubwa katika nchi hii ambapo ni msingi mkubwa wa maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchache wa muda, nitaanzia na bwawa kubwa la Stigler’s Gorge. Bwawa hili la Mwalimu Nyerere litazalisha umeme wa maji megawatt 2,115 ambapo ndiyo rahisi duniani kote. Kwa hiyo, utachagiza maendeleo makubwa kwa viwanda vyetu vikubwa, vya kati na vidogo. Hivyo, itatusaidia sana sisi wananchi wa Handeni Vijijini kuongeza thamani ya mazao yetu kwani sisi ni wakulima wazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na kuanzisha viwanda hivyo ambavyo tayari vimeshaanza na tuna mikakati ya kuvutia wawekezaji, vilevile maji na barabara ni muhimu. Ili mazao hayo yaweze kufika kwenye viwanda, ndugu zangu lazima tufanye mpango mkakati bajeti ya TARURA iongezeke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile viwanda vinaendana na maji. Naomba Wizara yetu ya Maji tukitoka hapa tuwe na mpango mkakati ili tuongeze pesa ili wananchi wetu wa vijijini wapate maji safi na salama na kuweza kuendesha mitambo hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni upanuzi mkubwa wa bandari zetu. Bandari zetu zimepanuliwa sasa lazima tutafute mbinu chochezi ziweze kufanya kazi zituingizie pato. Kwa mfano, wananchi wa Mkoa wa Tanga tumeshuhudia meli kubwa ya mita 200 ambayo ilibeba tani 55,000 za Clinker kwa ajili ya kwenda Rwanda. Meli hiyo iliondoka pale Tanga ikiwa tupu, sasa lazima tutafute mbinu chochezi ili bandari zetu ziweze kubeba mizigo kuingiza na kutoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara ya Madini iweze kusaidia wachimbaji wetu wadogo wa chuma na madini ya viwandani kwani Handeni Vijijini tuna madini ya chuma na madini ya viwandani kwa wingi sana. Wachimbaji wadogo wamejitahidi, pale tuna takribani tani zaidi 50,000 imelala pale chini ambapo waliingia mkataba na Dangote lakini kwa bahati mbaya haijachukuliwa. Kama tungeweka mbinu chochezi basi tani hizo zingeondoka na meli hiyo na bandari yetu ingefanya kazi, Halmashauri ingepata siyo chini ya shilingi milioni 600, bandari yenyewe ingepata mapato siyo chini ya dola milioni 150 kwa sababu mzigo huo wa tani takribani 50,000 gharama yake ununuzi (FOB) huwa ni dola milioni 4. Kwa hiyo, ndugu zangu naomba tutafute namna chochezi Wizara ya Madini ikitusaidia ili tuweze kuwahudumia wachimbaji wetu hawa wadogo tuweze kuhamasisha uingizaji wa pesa kwa kutumia bandari yetu ya Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. JOHN M. SALLU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami nichangie kwenye Wizara hii ya Kilimo. Kwanza niwape hongera sana Waziri, Naibu Waziri, Makatibu na watendaji wote wa Wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya kusukuma gurudumu letu la kilimo. Nikija upande wa mbegu, mbegu ni kitu muhimu sana katika kilimo, kwa bahati nzuri uzalishaji wa mbegu wa ndani sasa unaanza kupanda kulinganisha na miaka ya nyuma ambako zaidi ya asilimia 70 ya mbegu ilikuwa inaagizwa kutoka nje, hapo niwape hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Waziri ameainisha kwamba ataipa nguvu kubwa ASA ili iweze kuzalisha mbegu kwa wingi. Lakini hapo hapo naishauri Serikali isiwasahau wazalishaji binafsi kwa kuwawekea mazingira rafiki ili waweze kuzalisha kwa wingi kwani mpaka sasa hivi wazalishaji binafsi wanazalisha asilimia 90 ya mbegu. Kwa hiyo, hatutakiwi tuwaache nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watafiti wetu wa mbegu wanafanya juhudi kubwa kutengeneza mbegu zenye tija lakini mara nyingi zinaishia kwenye makabati, hazipati kutangazwa vya kutosha ili wananchi wakazifahamu. Ushauri wangu hapa, turudishe lile zoezi la kugawa mbegu kwa ruzuku. Wananchi wakipewa mbegu kwa ruzuku wakulima wadogo wadogo wataanza kutambua zile mbegu mpya zilizokuja na hivyo ikifikia kununua watakuwa wanazitafuta kwa majina zile mbegu mpya watalaam wetu walizozitengeneza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukija kwa upande wa umwagiliaji. Sisi wa Handeni vijijini tuna mto mkubwa unapita pale mto wa Pangani ambao haukauki mwaka mzima. Tuna mabonde mazuri ya umwagiliaji ambayo nilikuwa naomba Serikali iyatolee macho. Bonde la Masatu lililoko Kata ya Segera na Bonde la Jambe lililoko Kwamgwe. Kwa kutumia umwagiliaji, tunaweza kutengeneza mazao ya mbogamboga ambayo yanaweza kusaidia sana kiuchumi pamoja na ku-export nje ya nchi tukapata hela za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile kwenye mazao ya matunda, kwenye matunda, sisi wa Handeni Vijijini tunazalisha sana matunda ya maembe pamoja na michungwa. Lakini kwa bahati mbaya tumevamiwa sana na wadudu waharibifu wa matunda hayo. Nzi weupe, kwa hiyo, naomba Wizara itoe macho itusaidie janga hili ambalo linadhuru sana machungwa na miembe iliyoko kwenye kata takriban 10. Nikizitaja kata ambazo zimeathirika sana ni Kata ya Kwedizinga, Segera, Mgambo, Kabuku, Kabukundani na Kwamgwe. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali itoe macho ili iweze kutusaidia janga hili la wadudu waharibifu.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa muda niliopata. Naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini
MHE. JOHN M. SALLU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Vilevile, naipongeza sana Wizara kwa kazi nzuri waliyofanya ya kuifikisha sekta yetu ya madini hapa tulipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natajikita zaidi kwa wachimbaji wadogo. Wachimbaji hawa wana mchango mkubwa sana kwenye sekta ya madini na kwenye pato la Serikali kwa jumla. Kama ilivyoelezwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ukiangalia upande wa madini ya dhahabu, wachimbaji wadogo wamechangia asilimia 30; kwa kweli nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, nawapongeza sana wachimbaji wadogo kwani ndiyo wagunduzi wakubwa wa madini ndani ya nchi yetu, pamoja na kwamba hawana vifaa. Migodi yote inayochimbwa karibuni wamegundua wao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wachimbaji hawa wadogo tunatakiwa tuwashike mkono, Serikali pamoja na Wizara tutafute namna sahihi ya kupata mikopo yenye riba nafuu. Napenda kuyashauri mabenki yatafute namna ya kuzungumza na wachimbaji ili wajue hasa sekta inakwendaje, kwa sababu inaonekana hawaamini kuwakopesha wachimbaji wadogo, lakini nina imani wakikaa kwa pamoja watakuja na namna sahihi ya wachimbaji hawa kuweza kupata mikopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawakaribisha mabenki kwenye Jimbo langu la Handeni Vijijini, tuna vijiji zaidi ya kumi ambavyo vinachimba dhahabu; vijiji zaidi ya saba vinachimba feldspars; vijiji viwili vinachimba dolomite. Kwa hiyo, tuna vijiji zaidi ya 30 ambavyo vina madini mbalimbali, mabenki waje tukae nao tutafute namna sahihi ya kuweza kuwakopesha wachimbaji wadogowadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja kwa upande wa GST. GST inatakiwa itoe mchango mkubwa kwenye kuangalia wapi pana madini na kwa kiasi gani. Katika Jimbo langu la Handeni Vijijini, tuna madini ya chuma, graphite na dhahabu lakini wachimbaji wale hawawezi kujua chuma kile tulichokuwa nacho pale kiko kingi kiasi gani au graphite ile iko nyingi kiasi gani. Vilevile hii ni faida kwa Serikali kwani tukijua tuna graphite kiasi gani na tuna madini ya chuma kiasi gani, tunaweza kujipanga tuone tufanyeje kwa sababu kupanga ni kuchangua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la uongezaji thamani madini. Jambo hili tukilitumia vizuri litatusaidia sana kwenye upande wa ajira za vijana wetu, kwani uongezaji thamani madini siyo lazima madini ya dhahabu au almasi peke yake, kuna madini ya viwandani ambayo yanaweza kutumika kutengeneza vitu mbalimbali. Kwa mfano, insulators za umeme na vito mbalimbali, nina maana vipuri vya akina mama vinaweza kutengenezwa kutokana na madini ya feldspars.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwa mfano nchi ya China, utakuta insulators zinatengenezwa na viwanda vidogo sana, ni kama SIDO type. Kwa hiyo, tukiweza kutafuta ujuzi tukawapa watu wetu ujuzi, kama vile ambavyo imefanyka kwenye vikundi vya akina mama na vijana kupewa ujuzi wa kutengeneza sabuni na batiki, basi tukatengeneza namna vijana wakapata ujuzi wa kutumia malighafi hii ya madini ya viwanda, itatusaidia sana kuongeza ajira kwa vijana wetu na kuongeza pato la madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haya machache, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. JOHN M. SALLU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nianze na shukrani. Naishukuru sana Serikali yetu sikivu. Namshukuru sana mama kwa kuja na bajeti hii bajeti sikivu. Hapa nipende kumpongeza ndugu yangu Waziri, Mheshimiwa Mwigulu, Naibu wake na watendaji wote walioko chini yake kwa kuandaa bajeti hii Sikivu, iliyosikiliza mawazo mengi ya Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli namshukuru sana mama kwa jinsi ambavyo ametukumbuka kwenye barabara. Sisi wa vijijini kwa kutuongezea zile hela za TARURA zimetusaidia sana na zitasaidia sana kusisimua maendeleo ya kilimo kule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najikita zaidi kwenye kilimo kwa sababu Jimbo langu linashughulika zaidi na kilimo, kwa hiyo, katika ile asilimia 65 ya watu wanaoshughulika na kilimo na jimbo langu tumo. Kwa kweli asilimia moja ya bajeti ni ndogo sana kwa kilimo, kwa sababu kilimo kwa sababu kilimo kimebeba asilimia 65 ya wananchi. Ili tuweze kupata maendeleo kwenye nchi yetu, tunahitaji asilimia 65 ya wananchi kuisisimua ili iweze kulima kwa tija. Ili iweze kulima kwa tija tunahitaji Maafisa Ugani wa kutosha pamoja na mbinu za kuwaelimisha ili waweze kulima kwa tija kwani mazao yanayopatikana sasa hivi ndani ya heka moja yako chini sana hayana tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile katika kusisimua wakulima hawa soko ni muhimu sana la ndani na nje. Soko la ndani linaweza kusisimuliwa zaidi kwa kuwa na mbinu za kutengeneza viwanda vidogo vidogo ambavyo vitaleta tija ya ku-add value, kuongeza thamani mazao yetu. Kwa hiyo, taasisi husika zinatakiwa hapa Serikali iziangalie kama alivyosema mwongeaji aliyepita, kuna hizi CAMARTEC watakiwa waje na mbinu ya kuhakikisha kwamba tunapata viwanda vidogo vidogo ambavyo vitasaidia kusisimua uchumi kule vijijini. Uzuri ni kwamba ndugu zetu wa REA wamejitahidi umeme unaenda kila mahali, kwa hiyo sasa ni jukumu la viwanda hivi kusisimuliwa ili viweze kuleta tija kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, soko la nje ndugu zetu wa TANTRADE wanajitahidi, naomba na sisi wafanyabiashara tujitahidi kutafuta soko la nje kwa kadri iwezekanavyo kwa sababu ukiangalia wenzetu jirani wanauza sana nje mazao yetu sisi. Mazao yetu mengi yanapitia Kenya. Kwa hiyo hapa kuna jambo la kujifunza. Kwa mfano, kilimo cha mbogamboga na matunda ambapo kwenye jimbo langu tuna eneo kubwa sana wanalima machungwa na maembe pamoja na mbogamboga, kata takribani 14. Hapa nashauri lijengwe soko la matunda pale Segera ili liweze kurahisisha matunda haya kukusanywa na kuweka soko la Kimataifa pale ambapo litakuwa na majokofu ya baridi kwa ajili ya matunda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa napo pana kitu cha kujifunza kwa sababu baada ya kukusanya na kununua mazao haya ya matunda na mbogamboga tunatakiwa tuyapeleke nje, lakini bandari zetu bado hazijawa imara kusafirisha mazao haya. Maana ukiangalia kwa sasa hivi mazao mengi ya mbogamboga na matunda yanapitia Bandari ya Mombasa, hata yale maparachichi ya Njombe mengi yanapitia Mombasa badala ya kupitia Bandari ya Dar es Salaam au ya Tanga. Sasa hapa tuna kitu cha kujifunza. Serikali ikae na wafanyabiashara ili iweze kuona tuna upungufu gani ambao bandari zetu ya Tanga na Dar es Salaam haiwezi kusafirisha mbogamboga na matunda kwa urahisi kiasi ambacho kinawafanya wakapitie kwenye bandari nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuongelea suala la umwagiliaji, kwa sababu umwagiliaji utaongeza sana tija kwa wakulima wetu. Sisi wa Handeni Vijijini tunapitiwa na Mto mkubwa wa Pangani ambapo tungeweza kutumia vizuri Bonde ya Masatu na Bonde la Kwamgwe ambapo maji yameshafanya kazi ya kuzalisha umeme sasa yanaenda kutupwa tu baharini. Kwa kutumia mabonde haya tungeweza kusisimua sana kilimo kwa wananchi na kuleta tija na hatimaye kuongeza kipato cha wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mito ya msimu ambayo wakati wa mvua inaleta tafrani kubwa kwenye madaraja yetu. Sasa hii mito ya msimu tungeweza kuyakinga maji na tukayatumia kwa ajili ya umwagiliaji wa mbogamboga na matunda, tungeongeza tija kubwa kwa wananchi wetu. Mito hiyo ni kama vile Mto Msangazi na Mto Mnyuzi ambayo inakatiza katika eneo kubwa la Jimbo la Handeni Vijijini ambapo tukiitumia vizuri, basi tutatengeneza mazingira bora ya wakulima na hivyo kuongeza tija na kipato kwa ujumla na hatimaye kuongeza pato la halmashauri na nchi kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nije kwenye suala la zile mashine za kukusanyia kodi. Mashine zile zinahitaji mtandao wa simu (network) na eneo kubwa la Jimbo la Handeni Vijijini hatuna network ya kutosha. Hivyo tunatumia mashine ambazo zinaweza kukusanya kodi offline lakini inabidi lazima mkusanyaji huyo wa kodi atoke aende kutafuta mtandao ili aweze ku-reconcile data zake. Sasa hicho kipindi cha kwenda kutafuta mtandao na kupanda kwenye mti kupata mtandao ina maana kuna malori ya mizigo yanapita pale, kwa hiyo kuna mapato tunakosa. Hivyo, Wizara husika naomba itusaidie, mtandao upatikane katika maeneo yote ili tuweze kukusanya mapato ya halmashauri kadri inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sina budi kushukuru upatikanaji wa mbinu mbadala ya kupata hela ya kuchangia TARURA kwa sababu tukiimarisha TARURA tutaweza kutoa mazao yetu kwenda sokoni na bei itakuwa nzuri kwani sasa hivi kuna mazao yanaharibika na kuozea mashambani kwa kukosa barabara nzuri. Hivyo, nasihi ule ukusanyaji wa vyanzo ambavyo tumevipanga hapa ufanyike vizuri na Fungu lilindwe vizuri ili kweli lipelekwe kutengeneza barabara zetu za TARURA zipitike mwaka mzima ili tuweze kutoa mazao na tupate maendeleo tarajiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii na naunga mkono hoja. (Makofi)