Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Florent Laurent Kyombo (34 total)

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali naomba kuongeza maswali ya nongeza mawili kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza niishukuru Serikali kupitia Mheshimiwa Dkt. Magufuli, lakini pia na Waziri wa Wizara ya Maji pamoja na Naibu Waziri kwa usimamizi mzuri wa mradi unaoendelea katika Jimbo la Nkenge wa Kyaka Bunazi wa bilioni 15.1 na Mheshimiwa Naibu Waziri nikushukuru sana juzi ulitoka kule kuangalia maendeleo ya mradi.

Mheshimiwa Spika, mradi huo unahudumia vijiji saba katika Kata za Kyaka na Kasambia lakini kata zingine na vijiji ambavyo vimezunguka mradi huo. Je, ni lini Serikali itaongeza thamani ya mradi ya huo ambao una tenki lenye zaidi ya lita milioni mbili kuzunguka Kata za Nsunga, Mutukula, Bugorora, Bushasha ili thamani ya mradi iweze kuongezwa?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili Wilaya ya Misenye ambayo ni ndani ya Jimbo la Nkenge, ina vyanzo vingi vya maji na vyanzo hivi ni pamoja na Mto Kagera, lakini tuna Mto wa Ngono. Je, ni lini Serikali itaona ni vizuri kutumia vyanzo hivyo vya maji kuweza kupeleka maji katika vijiji ambavyo vinazunguka vyanzo hivyo vya Kata za Kakunyu, Kilimile, Mabale pamoja na Miziro? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nipende kujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge na niseme kwamba mradi huu mkubwa ambao umeutambua na Mheshimiwa Waziri alifika pale na nikupongeze wewe binafsi kwa namna ambavyo umekuwa ukitoa ushirikiano katika Wizara yetu na nikuhakikishie tu kwamba mradi huu kuongezwa thamani tayari michakato imeanza na wataalam wetu wanafika huko hivi karibuni na kila kitu kitakwenda sawa kama ambavyo uliweza kuongea na Mheshimiwa Waziri alipokuwa ziarani katika jimbo lako.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kutumia vyanzo vingine vya maji ili kukidhi na kuondoa shida ya maji katika vijiji vile vingine Mheshimiwa Mbunge nikuahidi tu kwamba tunatarajia kufikia mwezi Juni, tutakuwa tumekamilisha hatua mbalimbali za kuona namna gani tunaibua vyanzo vipya lakini vyanzo vile vilivyoko tunaviboresha na kuona mtandao wa maji unaendelea kutawanyika katika jimbo lako vijiji vyote ambavyo havina maji kwa sasa viweze kupata maji. Ahsante.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwa majibu ya Serikali na nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri na weledi katika masuala yote ya barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza na swali la kwanza ni barabara ya Katoma - Bukwali ambayo ni barabara inaunganisha nchi yetu nanchi ya Uganda na ni barabara muhimu kwa uchumi kwa wananchi wa kata za Gera, Ishozi, Bwanjai, Kashenye na Kanyigo; barabara hiyo yenye kilometa 39.5 nishukuru Serikali sasa hivi kilometa nne zimeanza kujengwa kwa kiwango cha lami na je ni lini kilometa 35.8 zilizobaki zitawekwa kwenye bajeti na kuweza kukamilishwa kwa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili ni barabara ya Bunazi - Nyabiyanga - Kasambya - Kakindo na Minziro ambayo barabara hiyo inaunganisha Makao Makuu ya Wilaya pamoja na nchi yetu ya Uganda lakini kuwa ni barabara kiungo kwa wananchi wote wa Tanzania kila mwezi Januari wananchi wanaenda kuhiji katika eneo takatifu la Mtakatifu Yohana Maria Muzeyi aliyezikwa hapo na ni mojawapo ya mashahidi 22 wa Uganda.

Je, ni lini barabara hiyo yenye kilometa 35.8 na yenyewe itaweza kutengenezwa kwa kiwango cha lami nakushukuru kwa nafasi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika,kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo, Mbunge wa Nkenge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyoitaja ya Katoma - Bukwali tayari ipo inaendelea kujengwa na kilometa
4.2 kama alivyosema zinajengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana na mimi kwamba bado wakandarasi wawili wako site wakiwa wanaendelea kufanya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwa kilomita ambazo tunaamini kilometa 2.2 zitakamilika mwezi Aprili na Serikali bado inaendelea kutafuta fedha na katika bajeti ijayo barabara hii tunaamini kwamba itapata fedha kuendelea kukamilishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara alizozitaja zote hizo za vijiji mbalimbali na kata mbalimbali tunatambua kwamba ni muhimu kwa uchumi wa wananchi wa Nkenge na bado Serikali tunaahidi kwamba itaendelea kuzikarabati na pale fedha itakapopatikana kuzijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lililoko Singida Magharibi ni sawa na lililoko katika Jimbo la Nkenge, Wilaya ya Misenyi na hasa wananchi wa Misenyi chakula kikubwa ni ndizi na baada ya kukumbwa na ugonjwa wa mnyauko ambao haujapata majibu majibu mpaka leo, wananchi wamejielekeza katika kulima mazao mengine mbadala. Mazao hayo yameendelea kushambuliwa na wanyama aina ya ngedere na hivyo kufanya wananchi hao kuhangaika sana kupata chakula.

Je, Serikali ina utaratibu gani kuweza kudhibiti wanyama hao waharibifu? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kyombo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, labda tu niseme kitu kimoja na nimuombe Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya maswali hapa tuweze kukutana na sisi kama Wizara tuko committed kupeleka wataalamu ili tuweze kupata solution ya wanyama hawa.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nishukuru kwa nafasi ya swali la nyongeza, lakini niseme sijaridhika kabisa na majibu ya Serikali. Changamoto hii ipo tangu mwaka 78 ambapo sasa hivi ni takribani miaka 43 mpaka leo. Nilivyotumwa na wananchi wa Nkenge kuja kuleta malalamiko ya wananchi mwezi wa saba ndipo timu ikatumwa.

Mheshimiwa Spika, unaweza ukaona majibu ya Serikali. Anayelalamikiwa ni Wizara ya Ulinzi, ameenda yeye na JKT, hakuna kuhusisha Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, hakuna kuhusisha halmashauri, hakuna kuhusisha Mbunge aliyeleta malalamiko, hatuoni nia ya dhati ya kuweza kutatua tatizo hilo.

Mheshimiwa Spika, swali langu la msingi, kama ni kweli tunatambua kazi nzuri ya jeshi letu, Wizara ya Ulinzi kama ni kweli wanahitaji hilo eneo kuna utaratibu wa kuchukua eneo. Na swali langu la msingi lilikuwa ni hilo, kama linatakiwa kuchukuliwa na jeshi letu la ulinzi na usalama kwa nini wasifuate taratibu za Serikali ili eneo hilo basi lichukuliwe kwa mujibu wa taratibu? Hilo ni swali langu la kwanza.

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Anaposema kwamba, hilo eneo halitagawiwa kwa wananchi:-

Mheshimiwa Spika, siamini kama hiyo timu waliyounda ilienda site kwa sababu, wananchi wanaishi katika eneo hilo miaka 43 iliyopita. Sasa maana yake leo katika swali langu la pili atuambie hao wananchi walioko katika eneo hilo watapelekwa wapi? Nakushukuru.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo, Mbunge wa Nkenge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, maeneo kama haya ambayo yanashika historia, lakini pia tunafahamu kwamba, eneo hili linalosemwa ndio lilitumika kama base dhidi ya Vita ya Kagera mwaka 78. Lakini tunafahamu pia madhara makubwa na madhila makubwa waliyoyapata watu wa Kagera na hususan wa maeneo haya. Maneno haya ya Mheshimiwa Mbunge na concern anayoiweka hapa inanifanya nitafakari zaidi na niombe kwa ruksa yako, acha tuchukue maoni yake na twende tukatafakari zaidi namna bora zaidi ya kutekeleza jambo hili kwa maslahi ya nchi, lakini kwa maslahi pia, ya watu wetu walioko katika eneo hili. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa nafasi. Wilaya ya Misenyi ni Wilaya yenye Kata 20. Inavyo vituo vya afya viwili ambavyo havina watumishi kabisa pamoja na Idara za Elimu na Kilimo. Je, ni lini Serikali itaweza kutupatia watumishi wa kutosha ili watoe huduma nzuri kwa wananchi wa Wilaya ya Misenyi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha ujao 2021/2022 Serikali na Ofisi ya Rais – TAMISEMI tumeomba vibali vya ajira takribani 12,000 kwa ajili ya watumishi wa kada mbalimbali katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa na hivyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Mheshimiwa Kyombo kwamba katika mgawanyo wa watumishi katika Mwaka ujao wa fedha tutahakikisha tunaitazama Halmashauri ya Misenyi kwa jicho la karibu ili tuendelee kuboresha huduma za afya katika vituo hivi ambavyo havina watumishi lakini pia katika kada nyingine katika halmashauri hiyo na kote nchini kwa ujumla wake.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi na niipongeze Serikali kwa juhudi madhubuti za kuboresha ujenzi wa vituo vya afya, zahanati pamoja na hospitali:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Misenyi ni wilaya ambayo ina kata 20, lakini mpaka sasa inavyo vituo vya afya viwili. Sasa ni lini zamu ya Wilaya ya Misenyi itafikiwa angalao kuongezewa vituo vya afya kwa juhudi kubwa ambazo zimekuwa zikifanywa na Serikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Florent Kyombo, Mbunge wa Nkenge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo hili la Nkenge na Halmashauri ya Misenyi kwa ujumla wake Serikali imeweka kipaumbele cha kuhakikisha inafanya tathmini ya maeneo ambayo yatapewa kipaumbele cha kuanza kujenga zahanati, lakini pia vituo vya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali katika mwaka ujao wa fedha imetenga kujenga vituo vya afya 121, lakini katika miaka mingine inayofuata ya fedha pia, tutahakikisha tumeweka kipaumbele cha kujenga vituo vya afya kwa hivyo, Jimbo hili la Nkenge na Halmashauri ya Misenyi pia, ni moja ya halmashauri ambazo zitapewa kipaumbele. Nashukuru.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi, viongozi wetu wa Kitaifa kwa nyakati mbalimbali wamefanya ziara ndani ya Wilaya ya Misenyi na kuahidi ujenzi wa barabara za lami. Barabara ya Mutukula kwenda Minziro lakini vilevile barabara kutoka Kadieli Kata ya Ishozi mpaka Gela njia panda. Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi za viongozi wetu wapendwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Florent Kyombo, Mbunge wa Misenyi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara ya Mtukula hadi Minziro iliahidiwa na anakubaliana na mimi kwamba kuna kazi tayari imeshanza. Baada ya kukamilisha kwa kiwango cha changarawe na kuifungua basi tutafanya kazi ya pili itakuwa ni kuisanifu kwa ajili ya kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara aliyoitaja ya pili ni barabara ambayo tayari ameshakuja mara kadhaa ofisini ni barabara ambayo ilikuwa inahudumiwa na Wakala wa Barabara (TARURA) na tayari tunafanya mawasiliano na wenzetu ili tuone namna ya kuipandisha hadhi lakini itategemea na wao watakavyoleta mapendekezo yao ili barabara hiyo kwa umuhimu wake iweze kuchukuliwa na TANROADS kama itakuwa imekidhi vigezo. Ahsante.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru tena kwa nafasi. Ni mara ya pili nauliza swali kama hili katika Bunge lako Tukufu, lakini kwa imani kubwa niliyonayo kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, ndugu yangu, Mheshimiwa Engineer Masauni na Mheshimiwa Sagini, naamini sasa hili suala litakwenda kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Jimbo la Nkenge, Wilaya ya Misenyi, hasa Kata za Mutukura, Kakunyu, Minziro na maeneo mengine wamekuwa na mila na desturi zinazofanana kabisa na Nchi ya Uganda. Sisi tunaongea Ruganda lakini majina unayoyakuta upande wa Tanzania ni sawasawa na unayoyakuta upande wa Uganda. Wataalam wetu wa Uhamiaji wamekuwa wanatumia kigezo hicho kuwa-judge kwamba siyo raia kwa sababu ya lugha na majina yale.

Mheshimiwa Spika, swali langu; je, ni lini Serikali itatambua hayo mahusiano ya ukaribu ya mila na desturi wananchi wakapewa haki yao ya uraia na waweze kupata pia vitambulisho vya NIDA? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa sheria, kama aliyoitaja Naibu Waziri ya mwaka 1995 ya Uraia inaruhusu mwananchi ambaye amekaa katika nchi yetu kwa muda wa takribani miaka saba hadi kumi kwa tabia njema aweze kupata uraia wa Tajnisi. Sasa Mheshimiwa Waziri au Naibu Waziri, hamuoni ni muda muafaka twende wote katika kata hizo tukae na wananchi tuwaongoze wajaze fomu waweze kupata uraia na kuishi kwa amani katika nchi yao? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Kyombo kwa namna anavyofuatilia kwa karibu maslahi ya wananchi wake, hususan anaoona wanakosa uraia ambao wanastahili.

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema, bahati nzuri vigezo anavifahamu, ametaja uraia mwema lakini viko vigezo vingine ambavyo vipo kwa mujibu wa sheria, kwa haraka nitaje vichache: -

Mheshimiwa Spika, tunasema kabla ya tarehe ya kuwasilisha maombi yake ya uraia awe alikuwepo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miezi 12 mfululizo; kwamba katika kipindi cha miaka kumi kabla ya muda wa miezi 12 awe ameishi ndani ya Jamhuri ya Muungano kwa kipindi kisichopungua miaka saba; awe na ufahamu wa kutosha wa Lugha za Kiswahili na Kiingereza au Kiingereza; awe mwenye tabia njema. Hiyo ni moja, lakini mbili za mwisho, awe amechangia au ameshiriki katika kukuza uchumi wa Taifa na mwisho aahidi kwamba akipata uraia anayo nia ya kuendelea kuishi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo ikiwa amekidhi vigezo hivi kwa kweli ana haki ya kupewa uraia.

Mheshimiwa Spika, ombi lake la pili, mimi na Waziri wangu, tuko tayari kuongozana naye na wataalam wetu ili kuona changamoto ambayo wanakabiliana nayo wananchi hawa walioko mpakani. Kuzungumza lugha ya nchi jirani hakiwezi kuwa kigezo cha kumnyima mtu uraia kwa sababu hali ya mipakani iko hivyo katika maeneo yote. Nashukuru.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi. Kwanza nakiri kwamba nimekuwa mtumishi wa TFDA kwa miaka kumi. Niseme, kuhamisha bidhaa za chakula na vipodozi kumekinzana na dhana nzima duniani ya udhibiti wa bidhaa hizo. Ukiangalia nchi zote duniani; uende Marekani bidhaa za chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba, zote zinadhibitiwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, duniani pote ndivyo ilivyo, lakini TFDA imekuwa ni kioo katika East Africa. Wamefundisha Rwanda, wamefundisha hadi Tanzania Visiwani leo tuna ZFDA. Kwa hiyo, kuhamisha kwenda kwenye Bureau of Standards ni jambo ambalo kidunia wanatushangaa. Je, ni lini sasa Serikali italeta sheria hapa ibadilishwe ili hizi bidhaa zidhibitiwe kulingana na matakwa ya kikanda na kimataifa? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri. Kwanza amesema ni practice ya kidunia na pia amesema kwamba TFDA ni mfano kwa East Africa. Nataka kumwambia, ni ya kwanza kwa Afrika nzima. Ndiyo sasa hivi inaongoza kwa Afrika nzima kwa zile standards za kidunia. Kwa hiyo, kwa Afrika ni ya mfano, hata nchi zilizoendelea kuliko sisi tumewapita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi mimi kama ambavyo nimejibu swali la msingi, naona kuna element hapo, lakini kwa sababu walioamua kubadilisha ilikuwa ni suala la kisheria na Bunge likaleta hapa Sheria Na. 8 ya Fedha ilivyobadilishwa ndiyo uamuzi ukafanyika, kwa hiyo, kabla ya kusema tutafanya nini, naomba mtupe muda wa kufanya uchambuzi wa kina kwa kushirikiana na Wizara husika ili tulete maamuzi hapa tusije tukaingilia mambo ambayo yanaweza yasitekelezeke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tunaelewa concern yenu Wabunge, tunaelewa concern ya swali la msingi. Tutaendelea kulichungulia vizuri na kushirikiana na wadau husika ili tuweze kuona tuendeje. (Makofi)
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Mheshimiwa Spika, kwenye swali la msingi la vipodozi fake kweli ni janga la Kitaifa.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba vipodozi vinapendezesha (beautifying) lakini kazi kubwa ya vipodozi ni za kiafya katika ngozi na mwili. Swali langu la msingi ni kwamba, ni lini Serikali itahamisha bidhaa za vipodozi kutoka Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara kwenda Wizara ya Afya ambapo kuna wataalam wa vipodozi hivyo ili tuweze kulinda afya ya jamii? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Florent Kyombo (Mb) kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika ni kweli vipodozi ni sehemu ya bidhaa ambayo ipo kwenye kundi la dawa. Sasa, kwasababu ni ushauri Serikali tunalichukua ili tuweze kuona namna gani tutaliweka hili suala liweze kutumiwa kwenye sehemu sahihi kama sio Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, nakushukuru.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nakushuru kwa nafasi.

Mheshimiwa Spika, Serikali iliahidi kuwajengea Wananchi wa Jimbo la Nkenge Wilaya ya Misenyi barabara ya Mtukura kwenda Minziro na nikupongeze Mheshimiwa Naibu Waziri na wewe ulifika na barabara hiyo sasa imeamza kujengwa, lakini ahadi ilikuwa ni ujenzi wa kiwango cha lami; je ni lini sasa barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kyombo, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii ilikuwa inafunguliwa na tumeishaifungua na baada ya kuifungua hatua inayofuata nikufanya upembuzi na usanifu na ndiyo tunavyoelekezwa na ilani kwamba barabara zote ziwe kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge hiyo barabara itafanyiwa upembuzi na usanifu wa kina kadri fedha itakavyokuwa inapatikana, ahsante.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na pongezi kubwa kwa Serikari kwa ujenzi wa vituo vya afya unaoendelea sasa, vipo vituo vya afya ambavyo vimejengwa kipindi cha nyumba lakini mpaka sasa havina watumishi wa kada ya afya wa kutosha: -

Je, ni lini sasa Serikali itapeleka watumishi hao ili wananchi wapate huduma inayostahili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kyombo, Mbunge wa Nkenge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilijibu swali hili kama ulivyoelekeza. Tunatambua kwamba kuna changamoto ya uhaba wa watumishi katika kada ya Afya.

Moja ya mikakati ni pamoja na Serikali kuajiri. Katika mwaka wa huu wa fedha 2021/2022 Serikali inatarajia kuajiri. Waziri wa Nchi atakapokuwa ametangaza ajira hizi, maana yake tutaainisha na kupeleka maeneo yale ambayo yana uhaba mkubwa wa watumishi kuhakikisha kwamba huduma za afya huduma za Afya zinaanza. Kwa hiyo, hilo ndilo jibu la msingi na niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba tutazingatia maeneo yote ambayo hayana watumishi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi. Wananchi wa Kata Kakunyu, Wilaya ya Misenyi ambapo ni mpakani mwa nchi yetu na Uganda, wamejenga kituo cha polisi mpaka kuezeka.

Je, ni lini sasa Serikali itawaunga mkono kumalizia kituo hicho wapate huduma za kipolisi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kyombo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema, wananchi wamejenga kituo, wanahitaji msaada wa kumalizia. Hatua watakayoanza ni kutathmini kiwango gani cha fedha kinatakiwa ili kukamilisha kituo hicho ili kuona kama tunaweza tukatumia sehemu ya fedha ya tuzo na tozo kwa ajili ya ku- support vituo hivi ambavyo viko mpakani. (Makofi)
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naipongeza Wizara ya Maji kwa miradi inayotekelezwa ndani ya Jimbo la Mkenge Wilaya Misenyi, lakini miradi hiyo ya Igayaza, Byamte, Baishozi, Rutunga na Lwamachi Nakitobo imesimama kwa sababu ya kasi ndogo ya wakandarasi kwa kukosa fedha ambapo wameshaomba certificate Wizara ya Maji. Je, ni lini sasa wakandarasi hawa watalipwa ili miradi iweze kukamilika kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kyombo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari wiki iliyopita tumeanza kulipa wakandarasi, hivyo huenda na mkandarasi huyo akawemo ndani ya ile listi na tunaendelea kulipa. (Makofi)
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Kwa nyakati tofauti viongozi wetu wa kitaifa waliahidi wananchi wa Wilaya ya Misenyi kutengeneza barabara ya Mutukula kwenda Minziro, na kwa bahati nzuri Naibu Waziri alikwenda kutembelea eneo hilo, akapokelewa kwa shangwe, lakini mpaka leo barabara hii haijatengenezwa pamoja na kuingizwa kwenye bajeti.

Je, ni lini barabara hiyo ya Minziro - Mutukula itatengenezwa wananchi wapate huduma na kuinua shughuli za kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kyombo, Mbunge wa Misenyi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara hii nilitembelea. Ni barabara ambayo inafunguliwa upya. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa haikuwa kwenye mtandao, kwa hiyo, inaweza isionekane, lakini azma ya Serikali ni kuifungua na kuijenga hii barabara. Ahsante.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Naipongeza Serikali na hasa katika Jimbo langu la Nkenge wilaya ya Misenyi. Ndani ya kipindi cha mwaka mmoja nimejengewa minara minne na hivyo kupunguza tatizo la mawasiliano. Hata hivyo, kama tunavyojua Jimbo la Nkenge linapakana na nchi ya Uganda muda mwingi tunapata mawasiliano ya simu na redio kutoka nchi Jirani. Je, ni lini sasa Serikali itaendelea kumaliza changamoto ya minara katika kata nyingine zilizobaki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa sababu nakumbuka tulifanya ziara mpakani kule, tukatembea wote, tukajionea hali halisi. Baada ya kuona hiyo hali ya changamoto ya mawasiliano, Serikali iliamua kumpelekea minara minne ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja. Kwa hiyo tumpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuridhia kuleta fedha kwa ajili ya ujenzi wa minara katika Jimbo la Misenyi. Ahsante.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini pia niendelee kuipongeza Serikali kwa fedha walizotuletea tulizipokea na barabara inaendelea kujengwa.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali imeshasema kwamba itaendelea kuihudumia barabara hiyo mpaka itakapopandishwa hadhi, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, ni hatua gani imefikiwa ya barabara hiyo kupandishwa hadhi kutoka TARURA kwenda TANROADS kwa sababu ina vigezo vyote vinavyostahili?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; je, ni nini mkakati wa Serikali kwa barabara za namna hiyo ambazo zina vigezo na zinaunganisha Nchi ya Tanzania na nchi za jirani ili ziweze kuwekwa katika mkakati wa kuzipandisha hadhi kutoka TARURA kwenda TANROADS? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo, Mbunge wa Jimbo la Nkenge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara zikishatoka katika ngazi ya TARURA ili zipandishwe hadhi zinakwenda Wizara ya Ujenzi ambao ndio wasimamizi wa TANROADS. Kwa hiyo, hatua ya sasa zipo huko ambapo wanafanya uchambuzi wa mwisho, wakishamaliza nafikiri watatangaza kwenye Gazeti la Serikali kwa taratibu ambazo zimewekwa.

Mheshimiwa Spika, la pili, mkakati wa Serikali ni kuhakiksha barabara hizo kwanza kwa sasa zinapitika wakati wote na kulingana na mahitaji ya wakati uliopo na wakati ujao, maana yake tutaendelea kuzingatia ili kama zinahitaji kupandishwa hadhi zitafanyika hivyo, kama haitahitajika basi tutaendelea kuzihudumia ili zipitike wakati wote, ahsante sana.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pia niipongeze Wizara na Mheshimiwa Naibu Waziri aliyetembelea Wilaya ya Misenyi na kuahidi kufunga minara katika kata kumi na mpaka sasa ameongea kata tatu zimeshafungiwa minara bado kata saba. Je, ni lini sasa kata hizo zitamaliziwa kufungiwa minara ili wananchi wapate mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kuna kata ambazo tuliziingiza katika utekelezaji wetu na tayari hatua za awali za ujenzi huo zimeshaanza. Hivyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuwa na subira wakati utekelezaji huu ukiendelea kufanyika kwa wakandarasi wetu wa ndani.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Naomba niongezee maswali mawili ya nyongeza: -

Mheshimiwa Spika, barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 12 kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri ni ya muhimu sana kwa wananchi wa eneo hilo ikitokea Lubira, Kyabunaga, Bugango mpaka mpakani.

Je, sasa ni lini Serikali itaona umuhimu wa barabara hiyo kwakuwa inakidhi vigezo vyote vya kuhudumia na TANROAD ipandishwe hadhi kwenda kule iwe imepata bajeti ya uhakika?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, barabara ya kutokea Kiwanda cha Kagera Sugar kwenda Kijiji cha Bubali imekuwa ina changamoto kwa muda mrefu na inahitaji matengenezo makubwa.

Je, ni lini barabra hiyo itatengewa bajeti ili iweze kutengenezwa na wananchi waweze kutumia barabara hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza la Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mbunge ameomba barabara hiyo kupandishwa hadhi na jukumu hilo kubwa linafanywa na wenzetu wa TANROADS, kwa kuwa Serikali ni moja basi sisi tutalipokea hilo ombi ka niaba ya TANROADS na watakwenda kulifanyia kazi kwa kufuata zile taratibu ambazo zinatakiwa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara ya Kagera Sugar kwenda Bubali ambapo ameainisha hapo ni lini itapangiwa fedha, mimi nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba nitawaagiza Maneja wa TARURA wa Wilaya na Mkoa wa Kagera waende wakafanye tathmini ili sisi tutafute fedha kwa ajili ya barabara hiyo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Mabasi ya abiria yanayosafiri kutoka Mkoa wa Dar es Salaam kwenda Mkoa wa Kagera na Nchi jirani ya Uganda kupita Wilaya ya Misenyi hulazimika abiria kulala katika Mji wa Kahama na wananchi kupata adha kubwa usiku kucha.

Mheshimiwa Spika, katika Pori la Biharamulo kuna vituo vya polisi vingi kila baada ya kilometa chache ambayo ni pongezi kubwa kwa Serikali.

Je, ni lini sasa mabasi yanayotoka katika Mkoa wa Dar es Salaam kwenda Mkoa wa Kagera na Nchi ya Uganda kuruhusiwa kusafiri mpaka kufika bila wananchi kulala njiani na kupata adha kubwa?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kyombo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali lake linafanana na swali ambalo la msingi ambalo Mheshimiwa Taska Mbogo ameuliza. Hivyo niombe majibu ambayo nimeyajibu kwenye swali la msingi yaendelee kubakia hivyo hivyo.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa majibu ya Serikali japo niseme nina imani sana na Mheshimiwa Bashe na Mheshimiwa Antony Mavunde kwa sababu skimu hii imekuwa ni muda mrefu imetelekezwa bila mafanikio. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, skimu hii imeshatumia zaidi ya shilingi milioni 944 ambazo hazikuleta tija yoyote. Je, ni nini commitment ya Serikali kuhakikisha kwamba sasa inaumalizia mradi huo na unakuwa na tija kwa wananchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Wakulima wa eneo hilo walisimamishwa kuendelea na ulimaji katika skimu hiyo mwaka 2013, leo ni miaka 10 tunapoongea hakuna chochote kinachoendelea. Naomba Serikali itoe matumaini kwa wananchi hao kuweka commitment kwamba sasa skimu hii inaenda kukamilishwa na wananchi wanarudi pale kwa ajili ya kulima kilimo cha umwagiliaji na kuleta tija katika maisha yao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni commitment. Nataka nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, ni dhamira ya Serikali ya kuhakikisha ya kwamba tunaendeleza kilimo cha umwagiliaji kupitia miradi mbalimbali. Mradi wa Kyakakera ambao umekaa muda mrefu ni mkombozi mkubwa wa wakulima. Tumekwisha mwelekeza Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kuhakikisha wanalipitia eneo hili na tulikamilishe kwa haraka ili wakulima wetu waanze kutumia mradi huu kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, sisi wenyewe hatupendi kumwona Mkulima amekaa bila kufanya kilimo lakini mradi huo ulikuwa chini ya DADP na ziko changamoto ambazo zilijitokeza katika utekelezaji wa hii miradi na hivi sasa tumejikita kuhakikisha kwamba tumejenga miradi ambayo itakuwa ni bora na ya kudumu muda mrefu ili wakulima wetu wasipate shida. Miaka 10 ya wakulima ni mingi nataka nikafute kilio hicho kwamba Mkurugenzi Mkuu akienda huko aifanye kazi hiyo vyema wakulima hao waweze kuanza kulima mapema kabisa katika msimu unaokuja hivi karibuni.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali na niipongeze baada ya kipindi cha miaka miwili baada ya ziara ya Naibu Waziri, katika jimbo langu tumekwishapata minara Minne mipya. Pia, nashukuru katika bajeti mpya sasa hiyo minara mipya minne ikienda kujengwa tutaielekeza katika maeneo yanayohusika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Misenyi, kama ilivyo mpakani mwa Nchi ya Uganda imekuwa na changamoto kubwa ya mawasiliano. Sasa ni lini minara mingine itajengwa katika Kata za Bugandika, Kilimilile, Buyango, Kitobo, Bwanjai na Mabale ili kuweza kufanya wananchi wa maeno hayo waweze kupata mawasiliano mazuri katika jimbo letu?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili, wananchi wa Wilaya ya Misenyi, wamekuwa wakipata mawimbi ya redio ya nchi jirani ya Uganda. Ni lini sasa Serikali itaweka nia ya dhati kuhakikiasha kwamba wananchi wanafaidi mawasiliano ya mawimbi ya radio ya nchi yetu? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kyombo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunafanya feasibility study kwa ajili ya kupeleka huduma ya mawasiliano katika Kata ya Bugorora na Kakunyu hapakuwa na minara imejengwa. Lakini kwa sasa tumegundua watoa huduma kwa kutumia uwekezaji wao wamekwisha jenga minara katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa minara ambayo tulikuwa tumepanga kupeleka pale sasa tutaihamishia na kupeleka Kata ya Minzilo na tutapeleka katika eneo la Kashenye. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, wananchi wa eneo hilo pamoja na maeneo ya Kitobo na Kanyigo wote tutawaweka katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipengele cha pili, eneo la Misenyi lina changamoto ya huduma ya usikivu wa redio. Pia, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tayari ametoa fedha kwa ajili ya kwenda kujenga kituo katika eneo la Kyerwa ambapo tukishafunga mtambo wetu pale utaweza kufikisha huduma ya redio katika maeneo ya Misenyi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Wananchi wa Kata Kilimilile wamejenga zahanati kwa nguvu ya wananchi na wafadhili na hiyo zahanati ina majengo ya wodi ambazo hazitumiki kwa sababu hadhi ya zahanati hairuhusiwi kulaza wagonjwa: Je, sasa ni lini Zahanati hiyo ya Kata ya Kilimilile itapandishwa hadhi ili iweze kutoa huduma katika Kata za Mabale na Kilimilile kwa wananchi hao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua nafasi hii mbele ya Bunge lako Tukufu kumwelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera kufika katika Zahanati ya Kilimilile katika Kata ya Kilimilile kufanya tathmini na kuona yale majengo ambayo yamejengwa kama yanakidhi vigezo vya kuweza kupandisha zahanati hii kuwa kituo cha afya na taarifa hii kuwasilishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Naye nampatia mwezi mmoja ili iweze kuwa imefanyika tathmini hii.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa maelezo mazuri ya Serikali na niipongeze Serikali kwa kweli dawa zipo kwenye vituo vyetu na wananchi wanapata dawa. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, ni nini mkakati madhubuti wa Serikali kuhakikisha kuwa dawa hizi zinazopatikana sasa hivi ziendelee kupatikana katika vituo vya afya?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tupate ufafanuzi wa utaratibu uliowekwa pale mgonjwa anapokosa dawa katika hospitali na duka linalomilikiwa na hospitali ili sasa apate dawa kwa ajili ya tiba inayohusiana na matibabu yake, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT FESTO J. DUGANGE) K.n.y. WAZIRI WA AFYA: Mhehimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mkakati wa kuhakikisha kwamba baadhi ya dawa ambazo zinakosekana zinapatikana, moja, tumeelekeza na kusisitiza vituo vyote vya Serikali vifungue maduka ya dawa. Mbali na dispensing za hospitali zenyewe lakini wafungue maduka ya dawa ndani ya hospitali zenyewe, na wahakikishe yale maduka yana dawa zote zilizopo katika ngazi ya kituo husika; ili mgonjwa akikosa dawa pale dispensing aweze kuwa-referred ndani ya hospitali kwenda kuchukua dawa kwenye duka la dawa la hospitali. Kwenye mkakati huo tumeweka kwamba dawa zote lazima zipatikane kwenye duka, ikiwa ni alternative ya filling kutoka dispensing.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, utaratibu ni kwamba mara mgonjwa akiandikiwa cheti cha dawa na kwenda dirisha la dawa kupata dawa zile akapata chache na moja kakosa anaandikiwa cheti kidogo kwa ajili ya kwenda kwenye duka la dawa na kupata dawa zile; na tutaendelea kusimamia utaratibu huo.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali katika eneo ambalo imeongelea la kudhibiti kweleakwelea, viwavijeshi, nzige na wanyama wengine waharibifu, lakini katika eneo hilo suala la ngedere ni ngumu sana kulidhibiti kwa aina ya kupitia kilimo anga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Wilaya ya Missenyi imekuwa ni janga kubwa na sisi kama wananchi kupitia juhudi za Mbunge na Waheshimiwa Madiwani tulitafuta suluhisho la kununua dawa aina ya carbofuran ambayo inaua ngedere hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua mchango wa Waheshimiwa Madiwani na Mbunge kununua dawa hiyo; je, Serikali haioni kuna haja ya ku–support juhudi hizo kuchangia hizo fedha au kuelekeza Halmashauri ikatenga bajeti kwa ajili ya kununua dawa hiyo ili wananchi sasa wakilima waweze kuvuna?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Tunajua Serikali imefanya kazi kubwa katika kupambana na suala la mnyauko, lakini mpaka sasa hivi bado unaleta usumbufu katika maeneo yetu.

Je, ni hatua gani ambayo Serikali imefikia katika kufanya utafiti ili sasa tuweze kupata suluhisho la kudumu la ugonjwa wa mnyauko? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili la kwanza la kuhusu dawa ambayo inatumika pale Missenyi nataka nichukue fursa hii kumuelekeza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya waende kuangalia dawa hiyo ambayo inatumika, na kama ina ufanisi sisi kama Serikali pia, tutaunga mkono kwa ajili ya kutatua changamoto hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusu mkakati wa kudumu; kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi, moja kati ya kazi kubwa ambayo tunaendelea kuifanya hivi sasa ni kuhakikisha kwanza kabisa tunang’oa na kuchoma moto mashina yale yote ambayo yalikuwa yana ugonjwa wa mnyauko ili ugonywa huu usisambae, lakini la pili, tunawajengea uwezo Kituo chetu cha Utafiti wa Kilimo cha TARI - Maruku, ili waweze kufanya utafiti na badae kuzalisha miche bora ambayo itakuwa na ukinzani na ugonjwa huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka ujao wa fedha tumetenga shilingi milioni 800; shilingi milioni 400 inakwenda kwa ajili ya utafiti na uzalishaji wa miche bora ya migomba. (Makofi)
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakazi wa Mkoa wa Kagera wamekuwa wakipata adha kwa kukosa stendi ambayo iko ndani ya Manispaa ya Bukoba, ambayo Mbunge wa Jimbo ndugu yangu Steven Byabato amekuwa akifatilia.

Je, ni lini sasa Stendi hiyo itajengwa ili kuweza kusaidia wananchi wa Mkoa wa Kagera?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kyombo kuhusu stendi ya Manispaa ya Bukoba. Serikali itapeleka fedha hizo pale maandiko haya yatakuwa yamepitiwa na kuona sustainability.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni miradi ya kimkakati, na kwa kuwa ni ya kimkakati lazima ioneshe sustainability, kwamba watakapopatiwa fedha na kujenga miradi hii basi halmashauri itaweza kuingiza mapato ya kujiendesha. Kwa hiyo pale ambapo tutamaliza mchakato wa ku-review andiko hili lililoletwa na Manispaa ya Bukoba tutawasilisha Wizara ya Fedha ili nao waweze kutenga fedha kwa ajili ya stendi hii.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Dkt. Ishengoma Kikoyo, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa malengo ya Serikali ni kuhamasisha uchumi ambao ni shindani katika ununuzi wa kahawa;

Je, Serikali haioni sasa itoe kibali cha wanunuzi binafsi kushindana na AMCOS kununua kahawa moja kwa moja kutoka kwa wakulima?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa kahawa inaendeshwa kwa Bodi ya Kahawa;

Je, Serikali haioni kwamba ni muda mwafaka kuleta Sheria ya Bodi ya Kahawa hapa Bungeni ikafanyiwa marejeo ili kuendana na uchumi wa sasa? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi, Serikali imeweka utaratibu ambao unaruhusu pia wawekezaji binafsi kununua kupitia katika AMCOS, ambapo wao wanakusanya. Na ninaomba tu niliweke wazi hapa lieleweke vizuri; AMCOS hanunui kahawa, anachokifanya yeye ni ku-aggregate na baadaye ndipo wanunuzi binafsi wanakwenda kununua kupitia kahawa iliyokusanywa. Kwa hiyo tutakachokifanya ni kuboresha mazingira zaidi ili wakulima wanufaike na bei lakini vilevile na waagizaji binafsi wapate uhakika wa kahawa yao.

Mheshimiwa Spika, la pili, kuhusu marejeo ya sheria; kutokana na kuwa na Agenda Maalum ya 10/30, hivi sasa tunafanya marejeo katika sheria zetu zote ili kuhakikisha kwamba zinaendana na mipango tuliyonayo ya kukuza sekta ya kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, ikiwemo sheria ambayo pia inaongoza zao la kahawa.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Serikali ya Awamu ya Tano iliahidi kuwajengea wananchi wa Minziro barabara ya kutoka Mutukula kwenda mpaka Minziro, na ni faraja kwamba Naibu Waziri alikuja akatembelea barabara hiyo na sasa hivi imeanza kufumuliwa: Je, lini sasa barabara hiyo itakamilika kwa kiwango cha lami kutoka Mutukula kwenda Minziro?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, barabara hii tulitembea na Mheshimiwa Mbunge, mimi nilishaitembelea. Kitu cha kwanza kilikuwa ni kuifungua hiyo barabara, na kitu cha pili tutakachofanya sasa ni kuifanyia usanifu. Ni barabara muhimu kwa sababu ipo kwenye uchumi na pia ni barabara ya ulinzi ambayo ni moja ya vipaumbele vya kujenga barabara kwa kiwango cha lami kwa mujibu wa sera zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya kuifungua yote tutaifanyia usanifu ikiwa ni maandalizi ya kuijenga kwa kiwango cha lami, ahsante.

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze kwa majibu mazuri ya Serikali, na ni kweli majengo saba yamejengwa. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, katika majengo hayo hatuna wodi ya watoto, akina baba, akina mama pamoja na theatre;

Je, ni lini sasa wodi hizo zitajengwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, ili hospitali hiyo iendane na kutoa huduma ya haraka kama ambavyo speed ya ujenzi imeenda inahitaji kuunganishwa na barabara ya lami ambayo iliahidiwa na kiongozi wa kitaifa.

Je, na barabara hiyo ambayo iko chini ya TARURA ni lini itajengwa kwa kiwango cha lami kuelekea katika hospitali iweze kutumika itakapo funguliwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Kyombo, la kwanza hili la kutokuwa na wodi ya watoto, akina baba na theatre vile vile katika Hospitali ya Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nilikuwa nimeshasema kwenye majibu yangu ya msingi kwamba Serikali imetenga shilingi milioni 800 katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 ambayo itakwenda kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Hospitali hii ya Wilaya ya Misenyi na watapata wodi ya watoto, baba na vilevile theatre. Ni lengo la Serikali hii ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba miundombinu katika sekta ya afya ipo ya kutosha kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali lake la pili la barabara inayounganisha hospitali. Barabara hii ina urefu kama wa kilomita nne kutoka kwenye barabara kuu inayokwenda Mtukula ambayo ni barabara ya TANROADS. Hivyo naomba nichukue nafasi hii mbele ya Bunge lako Tukufu kumwelekeza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kagera kwenda kufanya tathmini ya barabara hii na kuiweka katika mipango yetu kwa ajili ya kutafuta fedha na kuweza kuijenga ili wananchi waweze kufika hospitali kupata huduma za afya kwa wakati.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mpaka wa Mutukula ambao ni mpaka wa Tanzania na Uganda ndani ya Wilaya ya Misenye ni mpaka ambao kiuchumi unakusanya mapato makubwa, lakini wafanyabiashara wa pale wanakabiliwa na utitiri wa tozo ambazo kama mazingira mazuri ya kiwekwa biashara hiyo itakua…

SPIKA: Swali lako.

MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, ni lini sasa Serikali itaboresha mazingira ya biashara katika mpaka wa Mutukula?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ipo katika jitihada za kuweka mazingira mazuri ya kibiashara, kwa hiyo, siyo tu sehemu ambayo ameitaja Mheshimiwa Mbunge, sehemu zote ambazo ziko mipakani na ambazo sio za mipakani tutajitahidi kuondoa changamoto hiyo ya biashara. (Makofi)
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Lazaro Londo, inaonekana fedha ambayo imetengwa kwa ajili ya barabara hiyo haitoshi. Sasa ni nini comment ya Serikali kuhakikisha kwamba barabara hiyo inatengewa fedha za kutosha ili iweze kujengwa na kukamilika na wananchi waitumie?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, barabara hii ya Kisanga, Malolo na Uleling’ombe ni barabara ambayo inatumika kama barabara mbadala kipindi barabara ya kwenda Iringa ya lami inapokuwa ina hitilafu. Je, nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba barabara hii inatengenezwa na inatumika kipindi chote cha mwaka? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. NDUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo yaliyoulizwa na Mheshimiwa Florent Kyombo kwa niaba yake, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tumetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii lakini fedha haitoshi. Kimsingi tunafahamu kwamba safari ni hatua, tunaanza na hatua moja tunakwenda na hatua nyingine, angalau Serikali imeanza kuweka fedha, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kutafuta fedha kukamilisha barabara hiyo.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hii barabara nyingine ambayo inaunganisha maeneo haya muhimu ya Kata hizi mbili ya Kisanga na Uleling’ombe nayo iko kwenye mpango. Nimeeleza hapa na tutahakikisha kwamba tunaendelea kutafuta fedha kujenga barabara hizi kadri ya upatikanaji huo. Ahsante. (Makofi)
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Lazaro Londo, inaonekana fedha ambayo imetengwa kwa ajili ya barabara hiyo haitoshi. Sasa ni nini comment ya Serikali kuhakikisha kwamba barabara hiyo inatengewa fedha za kutosha ili iweze kujengwa na kukamilika na wananchi waitumie?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, barabara hii ya Kisanga, Malolo na Uleling’ombe ni barabara ambayo inatumika kama barabara mbadala kipindi barabara ya kwenda Iringa ya lami inapokuwa ina hitilafu. Je, nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba barabara hii inatengenezwa na inatumika kipindi chote cha mwaka? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. NDUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo yaliyoulizwa na Mheshimiwa Florent Kyombo kwa niaba yake kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tumetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii lakini fedha haitoshi. Kimsingi tunafahamu kwamba safari ni hatua, tunaanza na hatua moja tunakwenda na hatua nyingine, angalau Serikali imeanza kuweka fedha, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kutafuta fedha kukamilisha barabara hiyo.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hii barabara nyingine ambayo inaunganisha maeneo haya muhimu ya Kata hizi mbili ya Kisanga na Uleling’ombe nayo iko kwenye mpango. Nimeeleza hapa na tutahakikisha kwamba tunaendelea kutafuta fedha kujenga barabara hizi kadri ya upatikanaji huo. Ahsante. (Makofi)
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nishukuru kwa nafasi, na naipongeza Serikali kwa majibu mazuri, lakini ndani ya muda mfupi wameweza kutengeneza vitambulisho. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; Wilaya ya Misenyi kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri, imetengeneza vitambulisho 24,000 lakini mpaka sasa ni vitambulisho 5,000 vimegawiwa kwa wananchi. Shida kubwa ni kwamba wananchi wanatakiwa kuhakikiwa kwa mara nyingine, hii imekuwa ni kero kubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Misenyi na hivyo wananchi kuona kwa kweli kuona kwamba sio sahihi kuhakikiwa mara ya pili.

Je, ni nini tamko la Serikali kuhusiana na usumbufu huo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, sasa kuna baadhi ya wananchi ambao walikuwa hawajafikiwa kwa ajili ya kujaza fomu kwa ajili ya kupata vitambulisho ikiwa ni pamoja na wale ambao wamefikisha umri wa miaka 18 ambao wametiza sasa vigezo sasa vya kupata vitambulisho.

Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha na wananchi hao wanafikiwa kwa ajili ya kupata vitambulisho? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kyombo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu idadi ndogo ya wananchi waliogaiwa vitambulisho 5,000 tu kati ya wananchi 24,694 ambao vitambulisho vyao vimetoka, nitoe tu maelekezo kwa wenzetu wa NIDA Mkoa wa Kagera na hususan Wilaya ya Misenyi kwamba wakati wanawahakiki mwanzo mpaka vitambulisho vinatoka bila shaka walikuwa wamejiridhisha. Hata hivyo, pale ambapo kuna mashaka kwamba huenda wanaokwenda kutoa vitambulisho siyo raia wa Tanzania wana haki ya kufanya uhakiki mara ya pili; lakini uhakiki huo usiwe sehemu ya usumbufu kwa wananchi kwa sababu haieleweki kwa nini wananchi 5,000 pekee kati ya 24,000 ndiyo wapate. Kwa hiyo, waharakishe uhakiki huo ili wanaostahili kweli waweze kupewa vitambulisho vyao.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la mkakati wa Serikali, tumelijibu kwa nyakati tofauti kwamba tulikuwa na changamoto ya kimkataba kati ya Serikali na Mkandarasi, lakini changamoto hiyo imemalizwa na mkataba umeuhishwa mwezi Machi, 2022; kwa hiyo, wakati wowote kuanzia sasa vitambulisho vingine vitazalishwa na watu wengine ambao wamefikisha miaka 18 wataendelea kutambuliwa kwa madhumuni ya kupewa vitambulisho vyao. Nashukuru.
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viongozi wetu wamekuwa wakitoa ahadi kwa wananchi kwa ajili ya matengenezo ya barabara, na Rais wetu wa Awamu ya Tano alitoa ahadi ya kutengeneza barabara Kabia ile Kata ya Ishozi kuja mpaka njia panda ya Gera ambayo inasimamiwa na TARURA, lakini mpaka leo barabara hiyo haijatengenezwa ambayo imekuwa ni maswali mengi kwa wananchi na kuona kwamba, ahadi za viongozi hazitekelezwi.

Je, ni lini sasa barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami, ili sasa wananchi waweze kupita katika barabara hiyo kwa urahisi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Kyombo, Mbunge wa Nkenge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, ahadi za viongozi zote zipo katika mipango yetu na kila ahadi ambayo inatolewa lazima tutafute fedha ili utekelezaji wake uwepo. Kwa hiyo, waondoe shaka wananchi, tutatekeleza ahadi hiyo. Ahsante.