Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Florent Laurent Kyombo (13 total)

MHE. FLORENT L. KYOMBO Aliuliza: -

Kata za Gera, Ishozi, Ishunju, Kanyigo, Kashenye, Bwanjai, Bugandika, Kitobo, Buyango na Ruzinga katika Jimbo la Nkenge zina shida kubwa ya maji licha ya kwamba zipo kwenye mwambao wa Ziwa Victoria.

Je, ni lini Serikali itawafikishia wananchi wa kata hizo maji kutoka Ziwa Victoria kama inavyofanya kwa mikoa mingine inayopata maji kutoka katika ziwa hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo, Mbunge wa Nkenge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya maji katika vijiji 32 ambapo imetenga jumla ya shilingi bilioni 2.084 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika Wilaya ya Misenyi.

Aidha, Wilaya ya Misenyi inatarajiwa kunufaika na Mradi wa Maji wa Maziwa Makuu kupitia Ziwa Victoria ambapo Mtaalam Mshauri anaendelea na usanifu wa kina unaotarajiwa kukamilika mwezi Mei, 2021 na ujenzi wa mradi kuanza mwaka wa fedha 2021/2022. Vijiji 11 vitanufaika ambavyo ni Ishunju, Luhano, Katolerwa, Kyelima, Kashenye, Bushango, Kigarama, Bweyunge, Bukwali, Kikukwe na Bugombe.
MHE. FLORENT L. KYOMBO Aliuliza:-

Pamoja na kazi nzuri ya miradi ya kutengeneza barabara Nkenge, viongozi wetu kwa nyakati tofauti wameahidi kufanya maboresho ya miundombinu ya barabara za Kabyaile/Shozi – Njiapanda ya Gera, Minziro – Mutukula, Kaja Hospitali ya Mugana (Bwanja).

Je, ni lini barabara hizo zitatengenezwa ili kuondokana na kero hizo zinazowapata wananchi wanaotumia barabara hizo kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo, Mbunge wa Nkenge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mutukula – Minziro (kilometa 15.8) ni barabara ya ulinzi na pia ni moja ya ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Barabara hiyo inatakiwa kufunguliwa na tayari kilometa mbili zipo na zinatumika. Kilometa 13.8 zilizosalia zinapita katika mashamba na Hifadhi ya Msitu wa Minziro na zitaendelea kufunguliwa kwa awamu. Makisio ya ujenzi wa barabara hiyo yamefanyika na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS)ambapo jumla ya shilingi bilioni 3.63 zinahitajika kwa ujenzi wa kiwango cha changarawe na shilingi bilioni 9.994 zinahitajika kwa ujenzi wa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara zingine ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja, Serikali itaendelea kuziboresha ili kuhakikisha kuwa zinapitika vizuri katika majira yote ya mwaka. Ahsante.
MHE. FLORENT L. KYOMBO Aliuliza:-

(a) Je, ni kwa nini Jeshi la Wananchi wa Tanzania lisifuate utaratibu, ili kumiliki eneo la wananchi wa Kitongoji cha Byawamala, Kijiji cha Bulifani, katika Kata ya Kyaka, badala ya kuhamia eneo hilo kwa nguvu na hivyo kuibua mgogoro kuhusu eneo hilo?

(b) Je, ni kwa nini eneo hilo lisigawanywe kwa Jeshi na Wananchi kwa kuwa eneo hilo ni kubwa na limekuwa pori kwa sasa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WIZARA YA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo, Mbunge wa Nkenge, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, eneo la jeshi linalotambulika kama Kiteule cha 21- KJ lipo Bulifani, Kyaka, Wilaya ya Misenyi. Eneo hili lilitumika wakati wa Vita vya Uganda kwa kujikinga na kuyashambulia majeshi ya Nduli Idd Amin Dada. Mpaka sasa eneo hilo bado lina mahandaki yaliyotumika wakati wa vita. Hivi sasa eneo hili linakaliwa na askari wetu na limekuwa Kiteule cha 21-KJ Kaboya.

Mheshimiwa Spika, mwezi Julai, 2021 timu ya wataalamu wa ardhi kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa walikwenda kutembelea eneo hilo na kufanya tathmini ya uthamini na upimaji. Eneo hili litaingizwa kwenye mpango wa miaka mitatu ya kuondoa migogoro iliyopo katika maeneo yote ya jeshi, mpango ambao umeanza Aprili, 2021. Naomba wananchi wawe na subira katika kipindi hiki kifupi kilichobakia.

Mheshimiwa Spika, eneo hili halitaweza kugawanywa kwa wananchi kwa kuwa, lipo kwa matumizi ya jeshi na eneo hili limekaa kimkakati zaidi. Nakushukuru.
MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawatambua watu wenye haki ya Uraia ili wapate Vitambulisho vya Taifa pamoja na kuwapa Uraia watu ambao siyo raia lakini wameishi nchini kwa zaidi ya miaka kumi na tano?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kuwa na afya na leo kushiriki kwenye kikao cha Bunge.

Mheshimiwa Spika, pia nimshukuru Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kuniamini kuwa mmoja wa wasaidizi wake katika nafasi ya Naibu Uwaziri. Ahadi yangu kwake ni kutekeleza majukumu haya kwa uadilifu, uaminifu na bidIi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho, nikupongeze kwa kuchaguliwa kwa kura zote kuwa kiongozi wetu wa Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo sasa, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo, Mbunge wa Nkenge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na zoezi la kuwatambua na kuwapatia vitambulisho wale wote wanaostahili. Aidha, zoezi hili ni endelevu kwa kuwa kila mwaka idadi ya watu wanaofikisha umri na vigezo vya kutambuliwa na kusajiliwa inaongezeka. Aidha, idadi ya wageni wakazi na wakimbizi wanaoingia nchini imekuwa ikiongezeka na hivyo kuhitaji kusajiliwa na kutambuliwa ili kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na utaratibu wa kuwapatia uraia wa Tanzania (Tajnisi) wageni ambao wanaomba uraia wa Tanzania ikiwa wamekidhi sifa na vigezo vya kutajnisiwa uraia kwa mujibu wa Sheria ya Uraia Sura ya 357, Toleo la Mwaka 2002 na Kanuni zake. Ahsante.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO K.n.y. MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga uwanja wa ndege wa Omukajunguti?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo, Mbunge wa Nkenge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango wa kujenga Kiwanja kipya cha Ndege katika eneo la Omukajunguti, mkoani Kagera ili kuwezesha ndege kubwa ziweze kuruka na kutua.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, utekelezaji wa mradi huu utaanza kwa kadri ya upatikanaji wa fedha baada ya Serikali kukamilisha taratibu za utwaaji wa ardhi na ulipaji wa fidia. Ahsante.
MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakasimu kwa TANROADS Barabara ya Kibaoni, Kakunyu hadi Bugango wakati taratibu za kupandisha hadhi zikiendelea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo, Mbunge wa Jimbo la Nkenge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Kibaoni, Kakunyu hadi Bugango ina sehemu mbili ambazo zinahudumiwa na Wakala mbili za barabara ambazo ni TANROADS na TARURA. Sehemu ya kwanza ya barabara hiyo inaanzia Kibaoni hadi Kakunyu yenye urefu wa kilomita 76 ambayo inahudumiwa na TANROADS na sehemu ya pili inaanzia Kakunyu hadi Bugango yenye urefu wa kilomita 12.4 ambayo inahudumiwa na TARURA.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa mwaka 2022/2023 kupitia TARURA imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 200 kwa ajili ya matengezo ya barabara kutoka Kakunyu hadi Bugango yenye urefu wa kilomita 12.4 kwa kiwango cha changarawe.

Aidha, Serikali itaendelea kuhudumia barabara hiyo na kuhakikisha inapitika wakati wote hadi hapo taratibu za kupandishwa hadhi zitakapokamilika.
MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaitengea bajeti barabara inayounganisha Uganda na Tanzania ya Kibaoni - Kakunyu kwenda Bugango mpakani ambayo iko chini ya TARURA wakati taratibu za kupandishwa hadhi zikiendelea ili iweze kupitika wakati wote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo, Mbunge wa Nkenge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hiyo ya Kakunyu - Bugango ni muhimu kwa kuwa inaungaisha Nchi jirani ya Uganda pia hutumika katika kukuza shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa Missenyi.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu huo, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ilitenga jumla ya Shilingi Million 41.08 kwa ajili ya matengenezo ya barabara hiyo katika maeneo korofi yenye urefu wa kilomita 3.0 na kazi hiyo imefanyika na kukamilika.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Serikali imeendelea kuona umuhimu wa kuhakikisha kuwa wananchi wa Missenyi wanaweza kufika katika mpaka wa Bugango kwa kutenga jumla ya Shilingi Milioni 34.92 katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya matengenezo ya barabara nyingine iliyopo jirani iitwayo Missenyi Ranchi - Bugango jumla ya kilomita 17.3 ambapo Mkandarasi yupo eneo la kazi anaendelea ukamilishaji wa matengenezo hayo. (Makofi)
MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza: -

Je, lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kukamilisha Mradi wa Skimu ya Umwagiliaji wa Kyakakera uliopo katika Kata ya Kyaka?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo Mbunge wa Nkenge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Skimu ya umwagiliaji ya Kyakakera ni miongoni mwa skimu zinazounda Bonde la Mto Ngono lenye ukubwa wa hekta 11,700 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ambapo kupitia bajeti ya mwaka 2022/2023 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetenga fedha kwa ajili ya kufanya mapitio ya upembuzi yakinifu na kufanya usanifu wa kina. Mpaka sasa, Serikali ipo katika hatua za kukamilisha manunuzi ya kumpata mshauri mwelekezi atakayefanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, katika Mpango na Bajeti ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Bonde la Mto Ngono limetengewa bajeti ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji ambapo jumla ya hekta 3,000 zimepangwa kuendelezwa katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji na Skimu ya Kyakakera itakuwa miongoni mwa skimu za awamu ya kwanza zitakazoendelezwa wakati wa utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika Skimu ya Bonde la Mto Ngono.
MHE. FROLENT L. KYOMBO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaongeza minara au kuboresha mawasiliano katika kata zote 20 za Wilaya ya Misenyi?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA NA HABARI, alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Frolent Laurent Kyombo Mbunge wa Nkenge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imetekeleza miradi ya mawasiliano iliyokamilika katika kata 10 za Wilaya ya Missenyi. Kufikia mwezi Machi, 2023 tayari ujenzi wa minara 13 imekamilika na inatoa huduma katika teknolojia ya 2G na 3G.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali Serikali imeshapata watoa huduma wa kufikisha huduma za mawasilioano katika Kata za Bugorora, Kasambya, Mutukula na Kakunyu ambapo tayari zimeshapata watoa huduma, ahsante.
MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza: -

Je, Serikali haioni kuwa kufutwa kwa Form 2c katika huduma ya Bima ya Afya inakosesha mgonjwa kupata dawa iliyokosekana hospitali aliyotibiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT FESTO J. DUGANGE) K.n.y. WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo, Mbunge wa Nkenge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, maamuzi ya Serikali ya kusitisha matumizi ya fomu za dawa (Form 2C) katika vituo vya kutolea huduma za afya yalifanyika kwa kuzingatia manufaa yake, ikiwemo utekelezaji wa maelekezo ya watoa huduma wote wa Serikali. Kwamba kuwe na utaratibu wa kuanzisha maduka ya dawa yanayomilikiwa na hospitali na hivyo kuongeza mapato ya ndani ya hospitali. Pia kuepusha usumbufu kwa wananchi wa kutafuta dawa nje ya hospitali na hivyo kusabisha lawama zisizo za lazima kwa Serikali. Vilevile na kuepusha vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa katika eneo la dawa dhidi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Wizara imevielekeza vituo vya kutolea huduma kuweka utaratibu wa Mgonjwa kupata dawa iliyokosekana hospitali aliyotibiwa ili kuepusha usumbufu kwa wananchi. Ahsante.
MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza: -

Je, lini Serikali itatafuta suluhisho la kudumu la kudhibiti wanyama waharibifu wa mazao na ugonjwa wa mnyauko?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo, Mbunge Nkenge wa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Kilimo kila mwaka hutenga fedha kwa ajili ya kudhibiti makundi mbalimbali ya wanyama waharibifu wa mazao hususani panya, kweleakwelea, viwavijeshi na nzige.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2022/2023, jumla ya shilingi bilioni 4.9 zimetolewa kwa ajili ya kudhibiti wanyama hao. Aidha Serikali inaendelea kuimarisha timu ya kusimamia kilimo anga ambapo ndege moja iliyokuwa mbovu imesharekebishwa na taratibu za kununua ndege mpya zinaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na ugonjwa wa mnyauko katika mazao mbalimbali ikiwemo ndizi, viazi, maharage na kahawa, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzalisha miche bora yenye ukinzani na magonjwa ya mnyauko; kutoa elimu kwa wakulima na Maafisa Ugani kuhusu kukata au kung’oa mashina yote yaliyoathirika na kuyachoma moto ili kuzuia kusambaa kwa ugonjwa na kuzalisha miche bora kutoka mashina yaliyoathirika kutumia teknolojia ya tissue culture ambayo inasaidia kusafisha na kuzalisha miche ambayo haitakuwa na ugonjwa huo.
MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatenga bajeti ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya pamoja na Vituo vya Afya Misenyi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo, Mbunge wa Jimbo la Nkenge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 na hadi kufikia Mei, 2023 kiasi cha shilingi bilioni 1.5 zimekwishatumika katika ujenzi wa majengo saba ya Hospitali ya Wilaya ya Misenyi na kiasi cha shilingi milioni 500 kilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha kimkakati cha Kanyigo kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Serikali imetenga shilingi milioni 800 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Misenyi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenge bajeti kwa ajili ya ujenzi na ukamilishaji wa miundombinu msingi katika hospitali na vituo vya afya kote nchini vikiwepo vya Halmamashauri ya Wilaya ya Misenyi.
MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza: -

Je, ni lini wananchi wa Jimbo la Nkenge ambao hawajapata Vitambulisho vya Taifa au Namba za Usajili watatambuliwa kama raia wenye haki na kupatiwa vitambulisho hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo, Mbunge wa Jimbo la Nkenge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ina jukumu la kuhakikisha upatikanaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi ikiwemo wananchi wa Jimbo la Nkenge. Katika Mkoa wa Kagera jumla ya wananchi 1,009,653 wamesajiliwa na kutambuliwa baada ya maombi yao kuhakikiwa. Jumla ya vitambulisho 310,847 vimezalishwa kwa ajili ya wananchi wa mkoa huo. Katika Wilaya ya Misenyi inayojumuisha jimbo la Nkenge wananchi 85,439 wamesajiliwa na kutambuliwa na jumla ya wananchi 32,235 wamepatiwa Namba za Utambulisho ambazo wanazitumia katika kupata huduma mbalimbali. Aidha, vitambulisho 24,694 vimezalishwa na kugaiwa kwa wananchi wa Wilaya hiyo. Nashukuru.