Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. George Natany Malima (15 total)

MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, naomba kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni adhma ya Serikali kuunganisha miji yote ya mikoa na wilaya kwa barabara za lami; na kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hii kiuchumi kwa wananchi wa Mpwapwa, je, Serikali ipo tayari kuipa kipaumbele maalum barabara hii ili ikamilike mapema?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Malima, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara hii ni muhimu na ndiyo maana hata hapa tunapoongea yeye atakuwa ni shahidi kwamba mkandarasi yuko site akiwa anajenga hizo kilometa 5. Naamini katika bajeti ijayo tutaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuendeleza hiyo barabara.
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa tatizo la maji katika Mji wa Mpwapwa limekuwa la muda mrefu. Na kwa kuwa, Serikali imekiri kwamba, ni kweli limekuwa la muda mrefu na kwamba, wana mpango wa kuchimba visima viwili katika eneo la Kikombo ili kuongeza upatikanaji wa maji katika mji ule.

Je, ni lini uchimbaji huu wa visima hivi viwili utakamilika ili watu wa Mpwapwa nao wapate unafuu wa shida ya maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; mwezi Januari timu kutoka Wizara ya Maji ilikuja kutembelea katika Jimbo langu, tulikagua miradi miwili ya maji mmoja katika Kijiji cha Vingh’awe na mmoja katika Kijiji cha Manhangu; na mradi ule wa Vingh’awe ulitengenezwa siku nyingi, lakini historia iliyopo ni kwamba ulipochimbwa miundombinu ilijengwa chini ya kiwango; ulifanya kazi siku tatu tu mabomba yalipasuka, lakini tenki ambalo lilijengwa below standard pia nalo lilibuja lote halafu ule mradi ulikufa, lakini mradi wa Manhangu pia una story inayofanana.

Je, Serikali inasemaje kuhusu hili, maana walikuja kukagua na wakaahidi kwamba wataifanyia matengenezo ili ifanye kazi. Je, ni lini watakuja kurekebisha hiyo miradi miwili?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika,ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa George Malima, Mbunge wa Mpwapwa kama ifuatavyo:-

Swali lake la kwanza ni lini mradi ule unakwenda pesa zitapelekwa ili mradi uendelee kutekelezwa. Jibu lake kwa sababu mradi uko ndani ya mwaka wa fedha huu 2020/2021 Mheshimiwa Mbunge nakuhakikishia kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha kwa maana ya mwezi Juni hii fedha itakuwa imefika na tutasimamia utekelezaji wake kwa karibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ameongelea kuwa mwezi Januari kuna timu kutoka Wizarani ilikwenda na ni kweli. Miradi hii anayoiongelea ya Vingh’wale pamoja na Manhangu kwa pale Mpwapwa ni kati ya miradi ya ule mpango wa vijiji kumi ambao Wizara imekuwa ikiifanyia kazi na vijiji hivi kwa hakika vilikuwa na changamoto kubwa sana ya maji, lakini kwa awamu hii sisi tumejipanga kuhakikisha kuona kwamba miradi ile kwenye ile programu ya vijiji kumi tunakwenda kuisimamia ambayo ina vijiji takribani 177 vyote tunakwenda kuhakikisha tunarekebisha pale ambapo kidogo palikuwa na mapungufu. Lakini vilevile tutahakikisha wananchi wetu wanakwenda kupata maji safi na salama na ya kutosheleza.
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa Korongo hili kwa msimu wa mvua wa mwaka 2020 na mwaka 2021, nyumba 29 za wananchi zimechukuliwa na maji.

Je, Serikali ina mpango gani kupitia Mfuko wa Maafa kuwasaidia wananchi hawa ambao wameathirika kwa kuchukuliwa na nyumba zao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ili kuona ukubwa wa tatizo hili, ni muhimu sana Waziri na timu yake ya wataalam wa mazingira kutembelea eneo hili ili kuona wenyewe uharibifu ambao umetokea pale: Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kufuatana nami katika eneo lile ambalo imetokea shida hii ajionee mwenyewe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Spika, ahsante. Awali ya yote naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Malima kwa juhudi yake ya ufuatiliaji katika mto huo na Jimbo lake kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, pili, nampa pole Mheshimiwa Mbunge kwa maafa ambayo yametokea katika mvua zilizopita. Ni kawaida ya Serikali, inapotokea maafa katika sehemu yoyote kufuatilia, kufanya tathmini na kuwafariji watu hao ambao wamepata maafa katika sehemu mbalimbali. Kwa hiyo, nimtoe shaka kwamba, Serikali itafuatilia na itakwenda kuwafariji watu waliopata maafa katika sehemu hiyo.

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili. Mimi pamoja na timu yangu ya wataalam, niko tayari kabisa kufuatana na yeye baada ya Eid El-Fitr twende wote kuona hali ilivyo Inshallah. (Makofi)
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa daraj ala Godegode linalounganisha majimbo mawili yaliyoko katika Wilaya ya Mpwapwa lilichukuliwa na maji msimu wa mvua wa mwaka 2020 na kusema ukweli uchumi wa wananchi wa Majimbo haya mawili, Jimbo la Kibakwe na Jimbo la Mpwapwa yanategemea sana uwezo wa daraja hili, lakini pia tukizingatia kwamba daraja hili ujenzi wake uko kwenye Ilani ya Uchaguzi 2020/2025.

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa daraja hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Malima Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimuombe Mheshimiwa Malima baada ya session hii tuweze kuonana ili kama daraja limeondoka, kujenga daraja inaweza ikachukua muda, lakini tuna madaraja ya chuma ambayo yanaweza yakatumika kwa muda wakati Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kujenga hilo daraja kwa muda mrefu. Lakini kwa maana inaunganisha Halmashauri au Wilaya mbili nadhani itakuwa ni busara tuonane nae ili tuone na wataalam kupitia Bunge hili Mkoa huu wa Dodoma basi waende wakafanye tathmini ili tuweze kuona kama tunaweza tukajenga daraja la muda wakati tunatafuta fedha ya kujenga daraja la kudumu ili shughuli za uchumi na usafirishaji na usafiri wa wananchi ziweze kufanyika katika kipindi cha muda mfupi. Ahsante. (Makofi)
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, pamoja na jibu zuri la Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza ni kwamba, pamoja na uchakavu wa hospitali hii, lakini hatuna gari la wagonjwa: Je, ni lini Serikali italeta gari la kubebea wagonjwa (ambulance)?

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Ni lini Waziri atafanya ziara katika hospitali hii ya Wilaya ya Mpwapwa ili ajionee hali halisi ya hospitali ile? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa George Natany Malima, Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mwaka huu wa fedha atapata gari la wagonjwa kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya katika Halmashauri ya Mpwapwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, nilifanya ziara mwezi wa Nne mwaka huu katika Hospitali ya Mpwapwa, lakini nipo tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge kwenda kufanya ziara tena kuona namna ya kuboresha huduma pale. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Naishukuru Serikali kwa kutoa fedha kuchimba bwawa la umwagiliaji katika Kata ya Chunyu, Namhambi: Je, ni lini kazi hii itaanza?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Malima, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mkandarasi anayejenga mradi wa skimu ya umwagiliaji ya Msagali, hivi sasa yuko site ameanza mobilization na ni kati ya wale Wakandarasi 21 ambao walisaini mikataba pale Nanenane Mbeya na tunategemea muda wowote aanze kazi hiyo. Vile vile bwawa ambalo linajengwa pale likikamilika litakuwa na uwezo wa kutoa lita za mita za ujazo milioni 92. Kwa hiyo, ni habari njema kwa wana-Mpwapwa na kwa bahati nzuri mkandarasi yuko site tayari. (Makofi)
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza: Sambamba na visima hivi viwili kuchimbwa Mpwapwa Mjini, lakini mwaka wa 2021 kilichimbwa kisima kimoja katika Shule ya Sekondari ya Berege na mpaka sasa hivi akijaanza kufanya kazi: Je, ni lini kisima hiki nacho kitaanza kutoa huduma kwa wanafunzi wale wa Shule ya Sekondari ya Berege?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kwamba, kuna Miradi mitatu ya maji inatekelezwa katika Jimbo la Mpwapwa katika Kata ya Ving’hawe, Lupeta na Kijiji cha Igojiwani Kata ya Mima, lakini kasi ya utekelezaji wake imekuwa hafifu; je, nini tamko la Wizara kuhusu utekelezaji hafifu wa miradi hii? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge George Malima, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusema, miradi yote ambayo imeanza kutekelezwa Waheshimiwa Wabunge ni lazima ikamilike.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu ambao utekelezaji wake Mheshimiwa Mbunge George ameuona ni hafifu, tutausimamia. Mradi namna mkataba umesainiwa tutajitahidi ukamilishwe ndani ya wakati. Kwa kisima kilichochimbwa shuleni, pia ni moja ya mikakati ya Wizara kuhakikisha maeneo kama haya ya shule au hospitali na vituo vya afya yanapata huduma ya maji safi na salama bombani. Hivyo kisima hiki kilichochimbwa pia tunakuja kukifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa agizo kupitia Bunge lako Tukufu, Watendaji wa Mkoa wa Dodoma wanaofanya kazi maeneo haya, wahakikishe wanatoa hizi sintofahamu haraka iwezekanavyo.
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza: Katika Mji wa Mpwapwa kuna eneo dogo sana ambalo liliwekwa taa zamani, lakini taa hizi muda mwingi hazifanyi kazi: Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati taa hizi ili ziweze kufanya kazi angalau katika eneo hilo dogo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Mheshimiwa Rais amejenga daraja kubwa la TANESCO katika Mji wa Mpwapwa; daraja hili limejengwa katika eneo lenye miti mingi, kwa hiyo, husababisha giza nene wakati wa usiku. Mazingira hayo yanahatarisha usalama wa watumiaji. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakubaliana nami kwamba jambo la kuweka taa katika eneo hili ni la dharura lisilohitaji kusubiri taratibu za manunuzi? Kama jibu ni ndiyo; ni lini wataweka taa katika daraja hilo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa George Natany Malima, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, taa tunazoweka ni kwenye Barabara ambazo ni za TANROADS na kilometa 2.5 naamini tutakuwa tumepita pia kwenye maeneo hayo anayoyasema na hata tutayawekea lami na kuweka taa. Kwa hiyo, nina hakika kwa kilometa mbili na nusu tutakuwa tumekamilisha taa katika Mji wa Mpwapwa. Kama kutakuwa na changamoto ya hizo taa, nitaomba Mheshimiwa Mbunge tuweze kuonana ili tulichukue kama ni jambo la namna yake ili tuweze kuangalia kama hizo taa zinarekebishika ama tutaweka taa nyingine.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la pili, kama nimemsikia kuhusu daraja ambalo liko katika Mji wa Mpwapwa; limeshakamilika na tunatambua kwamba kuna mmomonyoko mkubwa ambao unaendelea. Sisi kama TANROADS kwa maana ya ujenzi, linahusisha watu wengi; watu wa mazingira, watu wa bonde la maji, na pia TAMISEMI kwa maana ya kwamba ni wadau. Sisi tunaweza tukajenga lakini kwa kushirikiana na hao wadau, na Mheshimiwa Mbunge tulishaongea naye kwamba Serikali imelichukua kwa wadau wote, tuone namna ya kuweza kudhibiti mmomonyoko ambao unaendelea ambao pia utahatarisha hilo daraja.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba liko, linafanyiwa kazi na Wizara zinazohusika kuweza kulijenga hilo daraja, kwa maana ya kurekebisha hizo kingo za daraja la huo Mto Mpwapwa.
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Shule ya Sekondari ya Berege yenye Kidato cha Tano na cha Sita ina idadi kubwa ya wanafunzi lakini ina upungufu mkubwa wa mabweni. Je, ni lini Serikali itajenga mabweni katika shule hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, Serikali itajenga mabweni katika Shule ya Sekondari Berege kule Wilayani Mpwapwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Nitoe wito kwa Mkurugenzi wa Halmashauri kuanza kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni haya katika Shule ya Sekondari Berege na kisha kuleta maombi vilevile Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ajili ya kuweza kutafutiwa fedha ya kuweza kuendelea na ujenzi wa mabweni hayo.
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Iwondo umefikia asilimia 80 lakini fedha za kumalizia asilimia 20 iliyobaki zimekwisha. Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kituo hicho ili wananchi wa kata hiyo waweze kupata huduma?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Kituo cha Afya cha Kata ya Matomondo kimekamilika na sasa kinatoa huduma lakini kuna upungufu mkubwa sana wa watumishi na hasa kada ya madaktari. Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza watumishi katika kituo hicho cha afya ili wananchi wa Kata ya Matomondo waweze kufurahia huduma ya afya? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa kwamba Serikali inajenga vituo hivi vya afya kwa awamu. Niwapongeza kwa kujenga kituo cha afya hiki cha Iwondo mpaka kufikia hatua ya asilimia 80 na bado asilimia 20 ya fedha kwa ajili ya ukamilishaji.

Mheshimiwa Spika, nitoe wito kwa Mkurugenzi wa Halmashauri kufanya mahesabu tufahamu hii asilimia 20 iliyobaki ni sawa na shilingi ngapi ili tuweze kuona namna ya kupata fedha Serikali Kuu pia na namna ya kupata fedha kutoka kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya kukamailisha ujenzi wa kituo hiki cha afya.

Mheshimiwa Spika, pili, kituo cha afya ambacho kinatoa huduma, Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt, Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka miwili na nusu imeajiri jumla ya watumishi wa sekta ya afya wapatao 17,000 ambao wamepangwa katika vituo mbalimbali kikiwepo kituo hiki. Zoezi hili ni endelevu na tutatoa kipaumbele kwa ajili ya kituo hiki cha afya cha Mpwapwa, ahsante.
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, pamoja na ujenzi wa njia mpya ya kusambaza umeme bado upatikanaji wa umeme katika Wilaya ya Mpwapwa na hasa maeneo ya vijijini siyo ya kuridhisha. Ni nini tamko la Serikali juu ya kuondoa tatizo hili kabisa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni lini Serikali itaanza zoezi la kubadilisha nguzo za miti ambazo zimekaa kwa miaka mingi na nyingi zimechakaa na kuanza kuweka nguzo za zege? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa George kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nianze na la pili kama nilivyosema kwenye jibu la msingi kuanzia mwaka wa fedha ujao, fedha imeshatengwa, itatengwa na kwa ajili ya kuweza kubadilisha nguzo zilizochakaa kuweka za zege, waya na vikombe na maeneo kama hayo.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali la kwanza; kwanza nipende kuwaambia Waheshimiwa Wabunge kwamba tarehe moja na tarehe mbili tutaleta habari njema ya faraja kwa Watanzania kutoka kwa Mheshimiwa Rais kupitia bajeti ambayo tutakuja kuisoma hapa ikiwa imetengwa takribani shilingi bilioni 500 kwa ajili ya kuboresha Gridi ya Taifa na maeneo yanayohusika na Gridi ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwenye eneo hili, eneo la Mpwapwa litapata maendeleo ya ziada kwa sababu imetengwa pesa kwa ajili ya kujenga kitu kinaitwa switch station pale Mbande ambacho sasa kitapunguza urefu wa njia ya kutoa umeme Zuzu kwenda mpaka pale na tukishakijenga station pale Mbande itatoka na njia nne mojawapo itakuwa ikienda Mpwapwa. Kwa hiyo, itafikisha umeme kwa urahisi na utakuwa ni umeme mkubwa.
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, vitendo vya uhalifu vimekithiri sana katika Kata ya Berege iliyopo Jimbo ya Mpwapwa. Je, Serikali itajenga lini Kituo cha Polisi ili kukabiliana na wimbi hili la uhalifu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Malima, Mbunge wa Mpwapwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba baadhi ya maeneo hasa Miji inayokua na kuchipua ikiwemo Wilaya ya Mpwapwa kuna kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu. Kama nilivyowahi kusema hapa, uhalifu ni zao la jamii lakini si jambo jema kufanywa na vijana wetu ambao wanazo fursa mbalimbali wakizitumia wanaweza kupata riziki zao bila kulazimika kuleta uhalifu katika jamii. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kulitaka Jeshi la Polisi ngazi ya Mikoa, Wilaya na Kata kuimarisha shughuli za usimamizi wa usalama wa raia na mali zao lakini kuchukua hatua thabiti dhidi ya vijana au watu wanaojihusisha na matendo ya uhalifu. Nashukuru sana.
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, Jimbo la Mpwapwa lina changamoto kubwa sana ya mawasiliano na hasa katika Kata za Luhambi, Lupeta, Mlembule, chitemo na Ihondo. Je, ni lini Serikali itaweka minara ya mawasiliano ili kutatua tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Mpwapwa Kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa maeneo mengi nchini bado yana changamoto ya mawasiliano. Lakini kwa maelekezo ya Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi ni kweli maeneo ni makubwa lakini hatuwezi kuyatekeleza ndani ya mwaka mmoja. Na ndio maana tunapanga mpango wa mwaka mmoja, tunapanga na mpango wa miaka mitano tunaamini kabisa kwa kipindi ambacho kuanzia sasa mpaka 2025 maeneo mengi yatakuwa yamepata suluhisho la mawasiliano kwa ajili ya wananchi wetu, nakushukuru sana.

MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, vitendo vya uhalifu vimekithiri sana katika Kata ya Berege iliyopo Jimbo ya Mpwapwa. Je, Serikali itajenga lini Kituo cha Polisi ili kukabiliana na wimbi hili la uhalifu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa George Malima, Mbunge wa Mpwapwa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba baadhi ya maeneo hasa Miji inayokua na kuchipua ikiwemo Wilaya ya Mpwapwa kuna kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu. Kama nilivyowahi kusema hapa, uhalifu ni zao la jamii lakini si jambo jema kufanywa na vijana wetu ambao wanazo fursa mbalimbali wakizitumia wanaweza kupata riziki zao bila kulazimika kuleta uhalifu katika jamii. Kwa hiyo, nichukue nafasi hii kulitaka Jeshi la Polisi ngazi ya Mikoa, Wilaya na Kata kuimarisha shughuli za usimamizi wa usalama wa raia na mali zao lakini kuchukua hatua thabiti dhidi ya vijana au watu wanaojihusisha na matendo ya uhalifu. Nashukuru sana.
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, ni lini Barabara ya Kongwa – Mpwapwa itaanza kujengwa?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, tayari mkandarasi alishapatikana, kwa hiyo, kinachosubiriwa sasa hivi ni kumkabidhi site. Ahsante.