Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. George Natany Malima (8 total)

MHE. GEORGE N. MALIMA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya kuanzia Njia Panda ya Kongwa hadi Mpwapwa Mjini yenye urefu wa takribani kilometa 30 ambayo ipo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 2025?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Natany Malima, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa barabara ya Njia Panda ya Kongwa hadi Mpwapwa ulianza kutekelezwa kwa kujengwa kwa kiwango cha lami kuanzia mwaka wa fedha 2013/2014. Ujenzi huu ulianza baada ya kukamilika kwa kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina mwaka 2013 uliohusisha barabara ya Mbande – Kongwa Junction. Kongwa Junction – Ugogoni kilometa 17.5, Kongwa Junction – Mpwapwa – Ving’awe kilometa 38.85 na Mpwapwa – Gulwe – Kibakwe kilometa 46.93.

Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilika kwa kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, ujenzi kwa kiwango cha lami ulianza, ambapo hadi sasa ujenzi wa sehemu ya Barabara ya Mbande – Kongwa Junction kilometa 16.7 umekamilika. Serikali kwa sasa inaendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Njia Panda ya Kongwa hadi Mpwapwa. Katika mwaka wa fedha huu tunaondelea nao Serikali imetenga shilingi bilioni 4.95 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami katika mji wa Mpwapwa. Ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Njiapanda ya Kongwa hadi Mpwapwa utaendelea kutekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imeendelea kutenga fedha za matengenezo mbalimbali ya barabara hizi ili ziendelee kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka huu wa fedha 2020/2021 jumla ya shilingi bilioni 1.1 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara ya Pandambili – Saguta – Mpwapwa – Ng’ambi na shilingi milioni 751.596 kwa ajili ya matengenezo ya barabara ya Manchali – Ng’ambi – Kongwa Junction – Hogolo Junction ambapo barabara ya Njiapanda ya Kongwa hadi Mpwapwa imezingatiwa. Ahsante.
MHE. GEORGE N. MALIMA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo la muda mrefu la uhaba wa maji kwa wananchi wa Mji wa Mpwapwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Natany Malima, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua tatizo la muda mrefu la uhaba wa maji katika mji wa Mpwapwa. Katika kutatua tatizo hilo, mikakati ya muda mfupi na muda mrefu imekuwa ikitekelezwa. Kwa upande wa mikakati ya muda mfupi, mwaka 2020/2021 Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuchimba visima virefu viwili katika eneo la Kikombo. Ujenzi wa bomba kuu kutoka katika visima hivyo viwili mpaka katika tanki la Vingh’awe, kuongeza mtandao wa maji katika maeneo ya pembezoni ambayo ni Vijiji vya Vingh’awe na Behero. Aidha, kazi nyingine itakayofanyika ni kufunga pampu mpya kwenye kisima cha Kikombo ambacho kitaongeza uzalishaji wa maji katika kisima hicho kutoka lita 40,000 kwa saa hadi lita 65,000 kwa saa. Kukamilika kwa kazi hizi kutaboresha upatikanaji wa huduma ya maji katika mji wa Mpwapwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mpango wa muda mrefu, Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Mpwapwa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji ya Dodoma (DUWASA) inaendelea kufanya usanifu unaotarajiwa kukamilika mwezi Mei, 2021 na kubainisha maeneo ambayo yana upungufu mkubwa wa maji katika Mji wa Mpwapwa ambapo vitachimbwa visima virefu vinne na kuongeza mtandao wa mabomba katika Mji wa Mpwapwa na viunga vyake. Aidha, katika mwaka 2021/2022, Serikali itakarabati mradi wa maji wa mtiririko wa Mayawile na Kwamdyanga.
MHE. GEORGE N. MALIMA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutengeneza kingo za korongo linalopita katikati ya Mji wa Mpwapwa lisiendelee kutanuka ili kunusuru maisha na makazi ya wananchi wa maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa George Natany Malima, Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa naomba kutoa maelezo yafuatayo kuhusu Korongo lililoko katikati ya Mji wa Mpwapwa:-

Mheshimiwa Spika, Mji wa Mpwapwa umejengwa pembezoni mwa mto ambao ni maarufu kwa jina la Mto Shaaban Robert, ambao sasa unaonekana kama Korongo linalopita katikati ya Mji. Kutokana na wananchi kufanya shughuli zao mbalimbali za kijamii na kiuchumi kwenye kingo za mto huo, kumekuwa na kubomoka kwa kingo hizo. Hali ambayo imeleta athari kubwa kwenye miundombinu na makazi ya watu walioko karibu na kingo za mto huo.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa George Natany Malima, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na uharibifu huo wa mazingira, Serikali imefanya upembuzi wa awali kwenye mto kiasi cha urefu upatao kilometa mbili ambazo ziko jirani na makazi ya watu ili kufahamu gharama za kudhibiti kingo zake. Katika upembuzi huo, inakadiriwa kwamba zinahitajika kiasi cha shilingi bilioni 2,170 kwa ajili ya ukarabati huo. Fedha hizo zitatumika kwa ajili ya kufanya yafuatayo:-

(i) Kuweka gabioni kiasi cha mita za ujazo 8,870;

(ii) Kujenga vizuri mmomonyoko kwa zege kiasi cha mita za ujazo 52;

(iii) Kujaza udongo maeneo yote yaliyoporomoka kiasi cha mita za ujazo 9,000; na

(iv) Kurudisha mto kwenye mkondo wake wa asili ambapo kinahitajika kifusi kiasi cha meta za ujazo 6,000. Serikali imetenga fedha ili kuweza kutekeleza mradi huo.

Mheshimiwa Spika, pia, napenda kuchukua fursa hii kuwasihi wananchi kuacha shughuli zinazosababisha uharibifu wa mazingira katika kingo za mito na badala yake wajitahidi kupanda miti, kupanda majani ambayo yatazuia mmomonyoko wa kingo hizo. Ahsante.
MHE. GEORGE N. MALIMA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafanya ukarabati wa Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Natany Malima, Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga Shilingi bilioni 16.55 kwa ajili ya kufanya ukarabati mkubwa wa hospitali kongwe za Halmashauri 19 kote nchini. Hospitali ya Halmashauri ya Mpwapwa ni miongoni mwa Hospitali hizo ambapo imetengewa Shilingi milioni 900 kwa ajili ya kazi hiyo. Ahsante.
MHE. GEORGE N. MALIMA aliuliza: -

Je, ni lini visima viwili vilivyochimbwa katika Mji wa Mpwapwa Mwaka 2021 vitaanza kufanya kazi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Natany Malima, Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka fedha 2022/2023, Serikali imepanga kutekeleza ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji kutoka kwenye visima viwili vilivyochimbwa katika Mji wa Mpwapwa mwaka 2021. Kazi zilizopangwa kufanyika ni pamoja na ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilometa 48.8, ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita 200,000 na ujenzi wa vituo 18 vya kuchotea maji. Taratibu za manunuzi kwa ajili ya kumpata Mkandarasi wa Ujenzi zinaendelea na ujenzi wa mradi unatarajiwa kuanza mwezi Aprili, 2023 na kukamilika mwezi Aprili mwaka 2024. Kukamilika kwa mradi huu kutanufaisha wananchi wapatao 21,360 waishio kwenye Kata za Vihangwe na Mpwapwa Mjini.
MHE. GEORGE N. MALIMA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaweka taa za barabarani katika Mji wa Mpwapwa ili kuongeza usalama nyakati za usiku?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Natany Malima, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga kiasi cha Shilingi milioni 350 kwa ajili ya kuweka taa za barabarani katika Mji wa Mpwapwa kwa urefu wa kilometa 2.5. Kazi za uwekaji wa taa umeanza na inatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2023, ahsante.
MHE. GEORGE N. MALIMA aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga vituo vya afya katika Kata za Mlembule, Godegode, Chunyu na Berege – Mpwapwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Natany Malima, Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mahitaji ya vituo vya afya katika Kata za kimkakati kote nchini. Katika kipindi cha miaka mitano Serikali imetekeleza ujenzi wa vituo vipatavyo 2,406 vya kutolea huduma za afya ambavyo bado vina uhitaji wa baadhi ya miundombinu ikiwemo vifaa tiba na watumishi.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga kwa awamu fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya kwenye maeneo ya kimkakati kote nchini ikiwemo Kata za Godegode, Chunyu na Berege katika Halmashauri ya Mpwapwa, ahsante.
MHE. GEORGE N. MALIMA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua tatizo la kukatika kwa umeme katika Mji wa Mpwapwa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa George Natany Malima, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, awali Mji wa Mpwapwa pamoja na maeneo ya Wilaya za Mpwapwa, Kibaigwa na Kongwa zilikuwa zinapata huduma ya umeme kupitia njia ya ya umeme ya Mpunguzi yenye msongo wa kilovoti 33 na urefu wa kilometa 660.4 kutoka katika kituo cha kupoza umeme cha Zuzu, Dodoma Mjini. Kutokana na urefu na uchakavu wa njia hiyo, kulikuwepo na tatizo la kupungua kwa nguvu za umeme yaani low voltage katika maeneo ya Wilaya za Kongwa na Mpwapwa. Hata hivyo, Serikali kupitia TANESCO ilikamilisha ufungaji wa kifaa kiitwacho AVR yaani Automatic Voltage Regulator katika eneo la Kibaigwa na hivyo kufanikiwa kupunguza tatizo hilo.

Mheshimiwa Spika, tarehe 3 Agosti, 2021 Serikali kupitia TANESCO ilikamilisha ujenzi wa njia mpya ya kusambaza umeme ya msongo wa kilovoti 33 inayohudumia maeneo ya Wilaya za Kongwa na Mpwapwa. Kukamilika kwa ujenzi wa njia hii kumefanya njia iliyokuwepo awali kuendelea kuhudumia maeneo ya Kibaigwa pekee na hivyo kufanya maeneo ya Kongwa na Mpwapwa kuwa na umeme wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TANESCO inaendelea kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme nchini ikiwemo Wilaya ya Mpwapwa na katika mwaka wa fedha 2022/2023 TANESCO itatengewa shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya kufanya matengenezo na kuboresha nguvu za umeme katika njia chepushi za umeme yaani spur lines ikiwa ni pamoja na kubadilisha nguzo za miti kuweka za zege hasa katika maeneo korofi, kubadilisha vikombe na nyaya zilizochakaa pamoja na kufunga vikata umeme vinavyojiendesha vyenyewe yaani auto reclosers. (Makofi)