Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Pius Stephen Chaya (41 total)

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Madini. Nina maswali mawili ya nyongeza. Wewe mwenyewe unatambua kwamba Sekta ya Madini ina mchango mkubwa sana kwenye kukuza ajira kipato na Pato la Taifa. Swali la kwanza, je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka wa kuja na utafiti wa kina ili tuweze kuibua taarifa za kijiolojia zitakayoisaidia Serikali kuwekeza kwenye mambo ya madini?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa tayari Naibu Waziri amesema kuna Taarifa za awali kwenye baadhi ya maeneo ikiwemo Kata ya Makuru, katika Kijiji cha Londoni ambako tayari wachimbaji wa madini wadogo wadogo wanachimba. Sasa, je Serikali imejipanga vipi kuwawezesha wananchi katika maeneo ambayo kuna taarifa za awali ili waweze kujikita kwenye uchimbaji wa madini, tukuze ajira na kipato cha nchi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, nipende kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba utafiti wa kina ndilo jawabu la hatimate kuwezesha uchimbaji kufanyika. Sasa mojawapo ya mabadiliko ya Sheria ya Madini ambayo yanaonesha tumaini na huko mbele ni pamoja na kuziwezesha Taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Madini kwa rasilimali ili ziweze kufanya majukumu yake ipasavyo. Ni katika mtindo huo huo kwamba Taasisi ya Utafiti wa Jiolojia ya Madini - GST imepokea vifaa rasilimali kama wiki mbili zilizopita tulipata magari sita kwa ajili ya kuwawezesha kufanya ugani.

Mheshimiwa Spika, pia STAMICO wamewezeshwa na wao wenyewe kwa pato lao la ndani wamepata mitambo mitatu ya drilling. Sasa hizo ni hatua za kuimarisha Taasisi ili hatimaye ziweze kufanya kazi ya utafiti wa kina na hatimaye kuwasaidia wachimbaji wadogo.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu swali lake la pili linauliza ni lini watawezeshwa; ni katika mtindo huo wa kwamba tutakapokuwa tumeendelea zaidi kuimarisha taasisi zetu kwa uwezo wa kifedha kama ambavyo Serikali imeanza kufanya tunapenda kuamini kwamba tunaelekea mahali ambapo Taasisi ya Jiolojia inaweza ikashirikiana na STAMICO na hatimaye wakawa wanafanya utafiti wa kina mahali fulani na kwa utafiti huo sasa wakapewa wachimbaji wadogo ili waweze kufanya kazi zao kwa tija. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Katika Jimbo la Manyoni Mashariki tuna bwawa la umwagiliaji linalojulikana kama Mbwasa Irrigation scheme. Tayari ilishafanyika upembuzi yakinifu yaani feasibility study zaidi ya miaka 10, tulisaidiwa na watu wa JICA na iligharimu shilingi milioni 200. Napenda kujua sasa commitment ya Serikali ni lini sasa ujenzi wa bwawa hili la umwagiliaji ambalo litasaidia wakulima katika kata zaidi ya tano wa kilimo cha mpunga litaanza kujengwa na Serikali? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tathmini ya mabwawa na maeneo potential mengi ambayo yamefanyiwa usanifu na upembuzi yakinifu kama Wizara sasa hivi tunayafanyia auditing kwa sababu maeneo mengi ukiangalia gharama ambazo zilisanifiwa na hali halisi ya mahitaji ya fedha inayohitajika hazina uwiano.

Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine kwamba watupe nafasi katika bajeti tutakapokuja mwaka huu tutatoa mwelekeo wetu wa umwagiliaji clearly ambao kama Serikali tumeamua kwenda nao.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya eneo ambalo tunalolipa kipaumbele ni kufanya audit kuangalia kweli gharama zinazohitajika katika eneo hili ni halisi na kweli tutapata value for money katika eneo hilo. Njia nyingine ni kwamba miradi mingi ya umwagiliaji tutakayoifanya sasa hivi tutatumia force account na katika bajeti itakayokuja mtaona tutatenga fedha kutokana na Mfuko wa Maendeleo wa Umwagiliaji ambao utakuwa ni chanzo chetu wenyewe kama Wizara bila kutegemea fedha kutoka Hazina katika Mfuko Mkuu. Fedha hizi tutazielekeza katika kununua vifaa ili Tume yetu ya Umwangiliaji iwe na capacity ya kwenda kujenga mabwawa bila kutumia wakandarasi na tutatumia force account kwa kuishirikisha halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge wasubiri, baada ya bajeti tutakuwa tuna mwelekeo sahihi wa sekta yetu ya umwagiliaji.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Hitaji ya chuo cha VETA katika Jimbo la Ludewa linafanana sana na hitaji ya chuo cha VETA katika Jimbo la Manyoni Mashariki.

Je, ni lini sasa Serikali itakuja na mpango wa kuhakikisha kwamba Jimbo la Manyoni Mashariki hususan Wilaya ya Manyoni inakwenda kujengewa chuo cha VETA? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mbunge wa Manyoni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimeeleza mara kadhaa katika Bunge lako hili Tukufu kwamba hivi sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa vyuo 29 katika Halmashauri mbalimbali nchini, ambapo jumla ya shilingi bilioni 48.6 zimeweza kutengwa na zinaendelea kutumika kwa ajili ya ujenzi huo. Serikali inaendelea na utaratibu wa kutafuta fedha kwa sababu lengo kuu ni kuhakikisha kwamba katika kila Wilaya na Mkoa tunakuwa na VETA.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge mara tu fedha zitakapopatikana tutahakikisha kwamba tunakwenda kujenga VETA katika Halmashauri ya Manyoni lakini na Halmashauri zote ambazo bado hazijafikiwa na VETA nchini. Ahsante.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, natumia nafasi hii kumshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa huu mradi umechukua muda mrefu sana, zaidi ya miaka kumi, kukamilika, na kwa kuwa Waziri ameahidi kwamba ndani ya huu mwaka mmoja huu mradi unakuja kukamilika; ninapenda kujua sasa Wizara inakuja na mikakati gani ndani ya huu mwaka mmoja kuhakikisha maji yanafika katika vijiji 11.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa huu mradi vilevile unanufaisha kata tatu ambazo zina miradi mikubwa ya kimkakati ukiwepo mradi wa ujenzi wa reli lakini vilevile na kituo cha afya. Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa haraka kupeleka maji katika Kata ya Kintinku na Maweni?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Naibu Waziri wangu kwa kazi kubwa na nzuri namna anavyojibu maswali yake, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilifanya ziara katika Mradi wa Kintiku-Lusilile, ni mradi ambao umechukua muda mrefu sana na mkandarasi alikuwa akidai kiasi cha pesa. Tumeweza kumlipa kiasi cha shilingi milioni 500, lakini pia tumepokea fedha shilingi bilioni 25, kwa ajili ya kuwalipa wakandarasi. Nataka nimhakikishie mmoja wa wakandarasi ambao watalipwa fedha ni Mradi huu wa Kintiku-Lusilile. Kwa hiyo maelekezo ya Wizara na wakandarasi wote watakaopata fedha ni kuhakikisha wanakamilisha miradi kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako nataka niliambie Bunge lako Tukufu jana Mheshimiwa Rais ametoa maelekezo mahususi katika Wizara yetu ya Maji, na sisi kama viongozi wa Wizara ya Maji tumeyapokea na tutayafanyia kazi kikamilifu. Lakini naomba nitume salamu kwa wahandisi wa maji pamoja na wakandarasi; wakae mguu sawa, na sisi tutafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha Watanzania wanapata huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; je, ni lini sasa tathmini ya uchakavu wa miundombinu ya Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni itaenda kukamilika?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa hii hospitali ilianza mwaka 1973 na mwaka 1992 ilipandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya na kwa kuwa bado inaendelea kutoa huduma katika Wilaya ya Manyoni na kwa kuwa tuna upuungufu mkubwa sana wa wataalam katika hospitali na Jimbo zima la Manyoni Mashariki, nini commitment ya Serikali ya kupeleka wataalam katika Jimbo la Manyoni Mashariki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Manyoni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekwishaweka utaratibu wa kufanya tathmini katika hospitali zetu zote kongwe na chakavu 43 ambazo tumekwishazitambua ikiwemo hospitali hii ya Manyoni na kazi hiyo tayari imeanza na inaendelea. Tunatarajia ifikapo mwezi wa tatu mwaka ujao tutakuwa tumekamilisha na kufanya maamuzi wapi tutajenga hospitali mpya na wapi tutakwenda kuzikarabati zile hospitali ambazo bado zinahitaji ukarabati.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna changamoto ya upungufu wa watalaam katika huduma za afya katika vituo vyetu na Hospitali za Halmashauri ikiwemo Manyoni na Serikali imeendelea kuomba na kutoa vibali bvya ajira na katika mwaka huu wa fedha tumeomba vibali vya watumishi 12,000 lakini kipindi hiki tunaendelea na mchakato wa kuajiri watumishi 2,796 wa kada mbalimbali za afya. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Manyoni pia itapewa kipaumbele cha kupata watumishi hawa wa afya.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Manyoni Mashariki chumvi inapatikana katika Vijiji vya Mpandagani, Majiri na Mahaka.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi wa vijiji hivyo vitatu ili waweze kuwekeza katika viwanda vidogo vidogo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Chaya, Mbunge wa Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli sisi Tanzania tumebahatika kuwa na madini ya chumvi mengi kwa maana ya maeneo mengi, lakini uzalishaji wetu bado ni mdogo, ni wastani wa takribani tani 330,000 ambazo tunazalisha kwa mwaka. Kwa hiyo, kama nilivyosema, lengo la Serikali ni kuona sasa tunahamasisha viwanda vingi ili tuweze kuzalisha zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, na takwimu zinatuonesha kwamba tunaweza kuzalisha mpaka uwezo wa tani milioni moja kwa mwaka. Kwa hiyo tani 330,000 ambazo zipo ni kidogo. Kwa hiyo, jimbo la Mheshimiwa Dkt. Chaya ambao nao pia wana deposit nyingi za chumvi, basi nako pia tutaona namna gani ya kuona sasa tunahamasisha viwanda vingi ili viweze kujengwa katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Chaya kwa kuwa amekuwa akifuatilia sana suala hili na mimi nimuahidi kwa niaba ya Serikali kwamba tunafanya kila liwezekanalo ili tuweze kuwa na viwanda katika Mkoa huu wa Singida, Jimboni kwa Mheshimiwa Chaya kule Manyoni Mashariki. Ahsante sana.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ulishafanyika wa daraja la Sanza.

Je, nini commitment ya Serikali kuhakikisha kwamba inaanza kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa kipande cha barabara ambacho kitaunganisha daraja hilo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, ni lini Serikali itawamalizia kuwalipa fidia wananchi wa vijiji vya Sanza Chicheho na Ikasi ili ujenzi wa daraja uweze kuanza? Ahsante sana (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jibu langu la msingi, ni kwamba tayari tumeshakamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa daraja na ujenzi huo utaanza mara moja, ikiwa ni pamoja na approach roads zenye urefu wa kilometa tisa upande wa Singida na kilometa tano nukta kadhaa upande wa Dodoma kwa ajili ya kuondoa changamoto iliyokuwepo kwa sababu hilo daraja liko chini. Kwa hiyo ujenzi utaanza mara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la fidia; daraja hili limehamishwa mahali lilipokuwa na barabara inajengwa upya sehemu ya hilo daraja. Tayari fidia, atakubaliana nami Mheshimiwa Mbunge, Wizara na Serikali tumeshalipa zaidi ya milioni 300.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya wananchi kulalamika tumefanya tathmini upya na kuona kwamba zinahitajika si zaidi ya milioni 65. Tayari mchakato wa kupata hizo fedha unaendelea ili kabla ya kuanza ujenzi tumalize kwanza kuwalipa wananchi fidia halafu tutaanza ujenzi wa daraja hilo. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Manyoni kwamba fidia tayari tumeshafanya tathmini upya, tutawalipa, halafu tutaanza ujenzi wa hilo daraja na hizo barabara zake. Ahsante.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza; ni lini sasa Serikali itatoa huo mwongozo mpya ili tuweze kusaidia zile halmashauri ambazo zina uhitaji mkubwa wa kuwekeza kwenye miradi ya kimkakati?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; katika Jimbo la Manyoni Mashariki hatuna stendi ya mabasi. Sasa nini commitment ya Serikali kuhakikisha kwamba kwa kupitia huu mfumo itakuwa tayari kusaidia Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kujenga stendi ya mabasi ili itumike kama kitega uchumi kwa halmashauri?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na mwongozo mpya ilitokana na mapendeezo ambayo Mheshimiwa Mbunge amewasilisha. Kwa hiyo pale ambapo utakuwa umekamilika kwa kuzingatia haya mapendekezo ambayo ametupatia tutampatia. Hata hivyo, kwa huu mwongozo ambao tunaendelea nao na tunadhani mpaka sasa hivi haujaleta changamoto kubwa, ninao hapa na nitampatia baadaye.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili; niwapongeze kwanza yeye Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wake wa jimboni kwake kwa jitihada ambazo wameanzisha, lakini nimhakikishie kwamba kama ambavyo tumekuwa tukifanya siku zote kuhakikisha tunasaidia ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri zetu mbalimbali ikiwemo miradi ya stendi za mabasi, basi na jimbo lake na lenyewe tumelichukua tutaangalia tuingize katika mpango wetu wa utekelezaji pale tutakapofanya upembuzi wa kina kubaini kwamba ni utaratibu gani muafaka wa kuweza kuendelea na mradi huo na bajeti itakapokuwa imeruhusu.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; katika Jimbo la Manyoni Mashariki hususan Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, tuna upungufu mkubwa sana wa Watendaji wa Vijiji na tayari tulishapeleka maombi ya kupata kibali cha kuajiri Watendaji wa Vijiji na Watendaji wa Kata. Je, ni lini Serikali itatupatia kibali sasa cha kuwaajiri Watendaji wa Vijiji?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; katika Jimbo la Manyoni Mashariki tuna kilimo kikubwa sana cha korosho kwa kutumia block farming. Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kusaidia kupeleka wataalam wa kilimo ili kuchochea uwekezaji huo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Pius Chaya Mbunge wa Manyoni Mashariki, lakini pia Mheshimiwa Massare Mbunge wa Manyoni Magharibi na Mheshimiwa Aysharose Ndogholi Mattembe kwa kazi kubwa sana wanazozifanya kwa pamoja, kuhakikisha wananchi wa Manyoni na Singida kwa ujumla wanapata miradi ya maendeleo kwa ustawi wa jamii.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tuna changamoto ya upungufu ya Watendaji wa Vijiji na Kata katika halmashauri zetu zilizo nyingi. Serikali inaitambua changamoto hii na tathimini na mpango mkakati unaendelea kuandaliwa, hatua nzuri ili tuone namna gani tunakwenda kujaza nafasi za Watendaji wa Vijiji na Kata katika maeneo yetu ili waweze kusimamia kwa ufanisi zaidi shughuli za maendeleo. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaendelea kulifanyia kazi hilo na litapatiwa ufumbuzi kwa awamu na kwa hatua stahiki.

Mheshimiwa Spika, ni kweli tunahitaji wataalam wa kilimo lakini pia wa kada mbalimbali. Nalo pia linafanyiwa kazi na kwa kadri ya uwezo wa Serikali na upatikanaji wa wataalam hao tutaendelea kuajiri ili wakafanye kazi hizo. Nakushukuru sana.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Barabara ya Bihawana, Chali, Sanza, Manyoni ambayo imeulizwa na Mheshimiwa Nollo ili iweze kukamilika inahitaji ukamilishaji wa ujenzi wa Daraja la Sanza; na kwa taarifa yako upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ulishakamilika na fidia ilishatolewa kwa wananchi wa Kijiji cha Sanza: -

Je, nini commitment ya Serikali ya lini ujenzi wa daraja la Sanza utaanza? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pius Chaya, Mbunge wa Manyoni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli daraja analosema limeshafanyiwa usanifu na litagharimu pamoja na barabara zake za kuingilia shilingi bilioni 23 na barabara zitakazojengwa ni kilomita kama 14.5. Tunavyoongea, tayari tumetenga shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuanza hiyo kazi. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kutokana na majibu ya Naibu Waziri ni kwamba tangu mwaka 2018 tayari upembuzi yakinifu ulishafanyika.

Swali la kwanza, ni lini sasa Serikali itamalizia kuwalipa fidia wale wananchi wa vijiji vya Ikasi, Sanza na Chicheho ambao wanadai takribani shilingi milioni 60 ili kupisha ujenzi wa lile daraja? (Makofi)

Swali la pili ni kwamba, barabara hii ya kutoka Manyoni - Heka - Sanza mpaka Dodoma inaunganisha Halmashauri Nne; Halmashauri ya Itigi, Halmashauri ya Manyoni, Halmashauri ya Bahi na Halmashauri ya Dodoma Mjini. Kwa mantiki hiyo, hii ni barabara muhimu sana kwa sababu inaleta watu kwenye Makao Makuu ya nchi: Je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka kuhakikisha kwamba tunatafuta vyanzo vya fedha ili kufungua hii barabara kukuza Mji wa Dodoma? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GEOFREY G. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Manyoni Mashariki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Daraja la Sanza ambalo litakuwa na urefu wa barabara kilomita 14.5 pande zote mbili limeshafanyiwa usanifu na tunavyoongea hivi, kama Wizara tayari tulishapeleka maombi ya fedha Wizara ya Fedha ili tuweze kuwafidia wananchi wote ambao watapisha ujenzi wa barabara. Baada ya hapo, kama Mheshimiwa Mbunge alivyouliza, tayari tumeshatenga shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ni muhimu kama alivyosema, lakini haitapitika kama daraja lile halitajengwa. Kwa hiyo, Serikali iliona ni busara kwanza tujenge hilo daraja ili kuwe na mawasiliano ya moja kwa moja mwaka mzima. Ndiyo maana kama nilivyosema, kwa umuhimu huo ambao unaunganisha Halmashauri nne alizozitaja, tunaamini baada ya kukamilika daraja usafiri utakuwa na uhakika na baadaye tutaanza kutafuta fedha kujenga kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Manyoni Mashariki tuna mradi mkubwa wa shilingi bilioni 10 unaojulikana kwa jina la Kintinku-Lusilile. Kwanza naishukuru Serikali mpaka sasa hivi tayari chanzo cha maji kimepatikana. Lakini ningependa kusikia majibu ya Serikali ni lini sasa mkandarasi wa kusambaza maji, katika mradi huo katika Kata za Kintinku, Maweni na Makutupora ataanza kazi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Pius Chaya; ni kweli mradi huu una vijiji 11 na tayari vijiji vitatu vimeshaanza kufanyiwa kazi na wiki ijayo tunatarajia kusaini mkataba wa kukamilisha vijiji nane vilivyobaki na tayari tumetenga fedha zaidi ya shilingi bilioni 3.3 ili mradi huu uweze kuendelea katika utekelezaji wake. (Makofi)
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi hii. Kwa kuwa vijana wanaoenda chou kikuu ni wachache, hasa wale wanaomaliza kidato cha nne, ukilinganisha na wale wanaobaki. Je, ni nini mpango wa Serikali sasa wa kujenga chuo cha VETA cha ufundi katika Wilaya ya Manyoni? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Chaya, Mbunge wa Manyoni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza katika majibu ya swali la msingi na maswali mawili ya nyongeza, pamoja na yale maswali ya Dkt. Kimei; dhamira na nia ya Serikali na Sera yetu inazungumza kwamba, kila wilaya angalau tuwe na chuo kimoja. Tumeanza tayari mkakati huu na tumeanza kutekeleza katika wilaya 29 nchini. Namwomba Mheshimiwa Dkt. Chaya awe na Subira katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea kutafuta fedha, tutaifikia Manyoni, tumeanza na pale Ikungi na tukitoka Ikungi tutakwenda Manyoni kwa Mheshimiwa Dkt. Chaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Chanya aondoe shaka, Serikali hii ya Awamu ya Sita iko hapa kwa ajili ya kutekeleza mahitaji yao. Tukitoka hapo tutaenda kwa Mheshimiwa Katambi kule Shinyanga kuhakikisha na Shinyanga nayo inapata chuo hiki. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie fursa hii kuishukuru sana Serikali kwa ajili ya kuingiza Wilaya ya Manyoni katika mpango wa kujenga Chuo cha VETA mwaka huu, lakini ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa tuna vijana wengi wanamaliza kidato cha nne hawaendelei kidato cha tano na vijana wengi wanamaliza kidato cha tano na sita hawaendelei vyuoni; je, nini mpango wa Serikali kuifanya elimu ya ufundi kuwa basic education yaani elimu ya msingi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa sasa hivi tuna uhitaji mkubwa sana wa elimu ya ufundi hasa hasa kwa ajili ya uzalishaji viwandani; nini mpango wa Serikali na Wizara kutoa mikopo kwa vijana ambao wanaenda kusoma elimu ya ufundi? Ahsante sana.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Chaya, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Serikali inakusudia kama nilivyosema kujenga vyuo vya ufundi katika Wilaya zote hapa nchini na sasa hivi zimebaki wilaya hizo 62. Kwa hiyo, ujenzi utaendelea na kuhakikisha kwamba vyote vinafanya kazi kwa ajili ya wanafunzi kuweza kusoma humo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwa sababu sasa hivi tunapitia mitaala na kazi mojawapo kubwa ya kupitia mitaala ni kuongeza elimu ya ujuzi, ujuzi ikiwa ni pamoja na ufundi, tunaamini tutakapokamilisha kazi hii rasimu zitakamilika mwisho wa mwaka huu maamuzi mwakani, tunaamini kwamba tutakuja na mkakati ambao utaongeza mafunzo ya ufundi na ujuzi katika shule zetu kuanzia darasa la kwanza kwenda mpaka elimu ya kidato cha sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali lake la pili kuhusu mikopo. Kwa sasa hivi kwa kweli Serikali haitoi mikopo kwa ajili ya kwenda kwenye vyuo vya VETA, lakini tumefanya mazungumzo na Benki ya NMB kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunaweza tukatoa mikopo kwa wale ambao wana miamala inayopitia kwenye benki hiyo kwa ajili ya kusaidia wanafunzi kusoma kwenye vyuo vyote ikiwa ni pamoja na vyuo vya ufundi.

Kwa hiyo, tunaamini kwamba itasaidia kupunguza adha ya wanafunzi kutopata mkopo lakini tutaendelea kutafuta mikakati mizuri zaidi kuhakikisha kwamba tunatoa fursa ya mikopo.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa hii nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Manyoni Mashariki tuna Kituo cha Afya cha Kintiku ambacho tayari Serikali ilishajenga jengo la maabara, jengo la x-ray, wodi ya mama na mtoto na mochwari, lakini hatuna jengo la OPD. Ni nini kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba wanatupatia jengo la OPD?
NABU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dokta Chaya Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ameainisha kwamba katika Kituo cha Afya cha Kintiku kinachokosa tu ni jengo la OPD na nimhakikishie tu kwamba maeneo yote ambayo yana mapungufu na sisi tulipeleka fedha tutamaliza majengo, kwa sababu maeneo mengine yanakosa mochwari, maeneo mengine yanakosa maabara, mengine yanakosa wodi za akina mama, kwa hiyo lipo katika mpango ikiwemo katika eneo hili la Kintiku ambalo Mheshimiwa Mbunge ameliainisha. Ahsante.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Serikali iliahidi kufanya ukarabati wa Skimu za Chikuyu na Udimaa: Je, ni lini sasa Serikali itatekeleza ahadi hii? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pius Chaya, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Skimu za Chikuyu na Udimaa ni skimu ambazo kama Naibu Waziri nimeshakwenda kuzitembelea, nimeziona na tumebaini changamoto yake. Ninavyozungumza hivi sasa, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Umwagiliaji na timu yake wanaelekea katika maeneo hayo kwa ajili ya kukamilisha kazi ya kupitia upya michoro na kuanza utekelezaji wa miradi ambayo itawafanya wananchi waendelee na kilimo cha umwagiliaji.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru sana kwa majibu mazuri kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa tayari wananchi wa Tarafa ya Kintinku wameshatenga eneo la zaidi ya hekari nne katika Kijiji cha Lusilile kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi. Je, Naibu Waziri yuko tayari kuambatana nami kwa ajili ya kuona hilo eneo kama linafaa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi?

Mheshimwa Spika, swali la pili; katika Makao Makuu ya Polisi ya Wilaya ya Manyoni, tuna upungufu mkubwa sana wa nyumba za watumishi hususani OCD na Mpelelezi wa Wilaya.

Je, nini commitment ya Serikali kuhakikisha kwamba tunawajengea watumishi hawa nyumba za kuishi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chaya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza niwapongeze wananchi wa Tarafa ya Kintinku kutenga hizo hekari nne ili kujenga Kituo chao cha Polisi, nami nitaungana na Mheshimiwa Mbunge wakati wowote atakapokuwa tayari kwenda kujiridhisha juu ya kituo hicho. Hata hivyo, hata kabla mimi sijaenda, niutake Uongozi wa Polisi Mkoa wa Singida waanze kutembelea eneo hilo na kama wanaona linafaa waweze kuwashauri ipasavyo wananchi hawa ili nitakapofika basi ni uamuzi uwe unafanyika.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la ukosefu wa nyumba za watumishi akiwemo OCD Manyoni, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge, tumeripoti hapa wakati wa bajeti kwamba tunao mpango wa ujenzi wa vituo vya polisi na makazi ya askari na tutakwenda kujenga kwa awamu kwa kutegemea upatikanaji wa fedha. Ni matarajio yetu kabla ya mwaka 2025 Manyoni pia watakuwa mmefikiwa. Ahsante sana.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kuishukuru sana Serikali, lakini nimshukuru Waziri kwa majibu mazuri na kwa juhudi ambazo wanaendelea kuzifanya kuhakikisha kwamba huu mradi unakamilika.

Mheshimiwa Spika, nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa tayari vijiji vitatu vimeanza kupata maji, ni nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba zile Jumuiya za Watumia Maji zinakuwa jumuiya endelevu zenye uongozi imara hususani kuweka mafundi katika ngazi ya kata ili waweze kusaidia?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kuna maeneo ambayo Wizara imechimba visima mara tatu wamekosa maji, kwa mfano; Kijiji cha Mpapa, Igwamadete na hata Mazuchii. Nini mpango wa Serikali kuja na njia mbadala kunusuru vijiji hivi? Ahsante sana.
MHE. NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Dkt. Pius Chaya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nipende kupokea pongezi zake, lakini ni kwa sababu ya mashirikiano aliyonayo Mheshimiwa Mbunge na tuendelee kushirikiana lengo ni kuona tunapeleka maji kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na jumuiya kuwa na mafundi ngazi ya kata tayari hili ni agizo limeshatolewa na Mheshimiwa Waziri na maeneo mengi yameshafanya. Hivyo nipende kutoa agizo kwa watendaji waliopo katika jimbo lako kama hawajafanya hivyo wanapaswa kufanya hivyo haraka iwezekanavyo kuwa na fundi ngazi ya kata.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na njia mbadala; sisi kama Wizara maeneo yote ambayo yana changamoto ya maji ardhini, tunaendelea kuona chanzo kilicho karibu kiweze kuleta maji safi na salama. Mheshimiwa Mbunge hili tuendelee kushirikiana kama ambavyo tumekuwa tukishirikiana, lengo hivi vijiji ambavyo maeneo haya maji ardhini ni shida, basi nao tuweze kuwapelekea kupitia njia nyingine.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza: Je, ni lini ujenzi wa Daraja la Ntumbi ambalo linaunganisha barabara ya Ntumbi - Nangongo utaanza kufanya kazi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Nini mpango wa Serikali wa kuweka taa za barabarani katika Mji wa Manyoni ili kuweza kuboresha ulinzi na usalama wa Mji wa Manyoni?

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Pius Chaya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa daraja la Ntumbi, tayari bajeti ilikuwa imeshatengwa shilingi milioni 496 na tayari usanifu ulikuwa umeshafanyika na sasa wapo katika hatua za kutangaza ili daraja hili liweze kujengwa na wananchi wa Mheshimiwa Chaya pale na Watanzania wale wa Manyoni waweze kupata huduma ya barabara hiyo kupitika.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili kuhusu taa za barabarani, katika mwaka huu wa fedha tayari bajeti ilikuwa imetengwa kwa taa 15. Kwenye hili pia nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kulifuatilia sana. Tayari katika bajeti ya mwaka wa fedha unaofuata zimetengwa taa 28 pale Manyoni Mjini ambapo tutaenda kutekeleza.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa hii nafasi kuuliza swali la nyongeza. Katika halmashauri ya Wilaya ya Manyoni tulitenga kujenga Zahanati katika Kijiji cha Udimaa ambacho hakina Zahanati kupitia mradi wa TASAF.

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Zahanati ya Udimaa kwa kupitia mradi wa TASAF? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Chaya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi mingi inaibuliwa na wananchi, na sisi kama Wizara au Ofisi ya Rais inayosimamia miradi ya TASAF majukumu yetu ni kuchukua miradi hiyo na kuingiza kwenye mipango ya bajeti. Pale itakapopatikana bajeti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi wake huo tutakwenda kuufanyia kazi.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika jimbo la Manyoni Mashariki kuna Barabara ya kutoka Sorya kwenda Hika – Makulu – Londoni na Ikungi Singida.

Je, ni lini Serikali itaanza kufanya upembuzi na usanifu wa kina kwa ajili ya kuijenga katika kiwango cha lami ? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika,naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hiyo tumeipendekeza ifanyiwe usanifu mwaka wa fedha tunaoanza kama bajeti yetu itapitishwa, ahsante.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza: -

Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Maweni, wananchi walijenga boma la kituo cha afya, miaka ya 2012, lakini mpaka sasaivi halijakamilishwa; je, nini kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba boma hilo linaenda kukamilishwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Serikali ilitoa shilingi milioni 50 kwa ajili ya kukamilisha Zahanati ya Mhalala, Sasajila, Igose, Magasai na Mahaka; bahati mbaya zile fedha hazijatosha: Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba zile zahanati zinakamilishwa ili ziweze kuanza kutoa huduma? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, la kwanza; kwenye Kata ya Maweni, ujenzi wa kituo cha afya ambapo boma limekamilika toka mwaka 2012, Serikali itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma haya ambayo yamejengwa na wananchi kwenye vituo vya afya na zahanati.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge, ameleta orodha hii ya zahanati ambazo anazitaja, na alinikabidhi mimi mwenyewe juzi hapa. Tutaendelea kutafuta fedha kwa ajili ta umaliziaji wa zahanati hizi, lakini kwa sasa kuna tathmini ambayo inafanyika kwa ajili ya ramani zile ambazo zilipelekwa mwanzoni kwenye majimbo mbalimbali hapa nchini kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ili kuweza kujua ni kiasi gani sasa kinahitajika kwa ajili ya kumalizia.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa hii nafasi. Kwa kuwa Serikali imekuja na mfumo mpya wa kukusanya mapato unaojulikana kama TAUSI, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba madiwani wote wanapata elimu ya huu mfumo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI):
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali kwenye mfumo huu wa TAUSI, kwanza ni Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilitoa technical specification kwa halmashauri zote za aina ya POS ambazo zinatakiwa kununuliwa ambazo zitaendana na mfumo huu. Kadri tunavyokwenda tunatoa mafunzo kwa wale wanaohusika na POS hizi kule kujua ni namna gani wanatumia POS hizi ambazo zinaendana na mfumo huu wa TAUSI.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; katika Wilaya ya Manyoni tuna uhitaji mkubwa sana wa chuo ambacho kinaweza kikatoa elimu ya afya katika ngazi ya cheti na diploma. Je, nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba, sasa wanasogeza kampasi ya chuo cha afya cha ngazi ya certificate and diploma katika Wilaya ya Manyoni?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa, kuna uhitaji mkubwa sana wa Wahadhiri katika vyuo vikuu vyetu na vyuo vya kati; na kwa kuwa, hivi karibuni Serikali imekuwa ikitumia mfumo wa usaili kuwapata Wahadhiri, hususan Tutorial Assistants, je, Serikali haioni haja ya kurudi kwenye mfumo wa zamani ambapo vijana waliokuwa wakipata first class walikuwa wakibakizwa vyuoni na kuendelezwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Chaya, Mbunge wa Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na jambo la kwanza, swali lake la kwanza analozungumzia suala la chuo cha afya. Naomba tuubebe ushauri wake tuweze kuangalia namna gani ya kufanya upande wa hivi vyuo vya afya, tukishirikiana na wenzetu wa Wizara ya Afya au na taasisi nyingine binafsi, tuweze kuangalia namna bora ya kufanya katika upatikanaji wa vyuo hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Dkt. Chaya, pale katika jimbo lake katika wilaya yake tayari sisi kama Wizara ya Elimu, kama Serikali, tumeshapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha VETA ambavyo huenda baadaye tukatohoa tu na hizo kada za afya vilevile zikaweza kufundishwa katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, anazungumzia suala la wahadhiri. Ni kweli zamani tulikuwa na utaratibu katika vyuo vikuu, wale wanafunzi wanaofanya vizuri huwa wanabaki palepale chuoni kwa ajili ya kuwa Wahadhiri. Utaratibu huu hapa katikati ulisitishwa ili kuweza kuweka ushindani kwanza, lakini vilevile kuondoa upendeleo kwa namna moja au nyingine. Kwa hiyo, mamlaka yale sasa yalikasimiwa au yalipelekwa moja kwa moja kwenye Tume ya Utumishi wa Umma kwa lengo la kutoa vibali vya kuajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapokea ushauri huo hata wakati tunakusanya maoni wakati wa mapitio ya mitaala suala hili lilizungumzwa sana. Kwa hiyo, tuachie kama Serikali twende tukalifanyie kazi, ili tuweze kuangalia namna bora ya kurudisha utaratibu ambao utakuwa mzuri na kutoa fursa kwa kila Mtanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa hii nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Manyoni Mashariki kuna Daraja la Sanza ambalo upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na ulipaji wa fidia wananchi ulishakamilika. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Daraja la Sanza? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli daraja la Sanza ni kati ya madaraja makubwa ambayo yanaunganisha Mkoa wa Singida na Mkoa wa Dodoma na Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba tulitangaza tenda lakini bahati mbaya sana, Mkandarasi aliyepata hiyo tenda alijitoa na sasa tunaendelea na negotiations na Mkandarasi wa pili kwa maana ya kulijenga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo daraja lilikuwa limepangwa actually liwe limeanza kujengwa katika mwaka huu wa fedha. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira hiyo ipo, tunaendelea na negotiations na yule mshindi wa pili ili aweze kuanza kulijenga hilo daraja. Ahsante.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Katika Wilaya ya Manyoni tuna kata tatu za Majiri, Maweni na Kijiji cha Kibumagwa ambako kuna uvuvi wa Samaki: Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba, tunaboresha uvuvi huu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Manyoni ambako na kwenyewe wanaendesha uvuvi wa samaki, anachotaka ni sisi kwenda kuboresha. Jukumu letu kubwa ni kwamba, moja, tutaendelea kuleta elimu pamoja na kuongeza vifaa vya kisasa kupitia hii mikopo ya masharti nafuu. Kwa hiyo, tutafika katika kila eneo ambalo watu wetu wanajishughulisha na hizi shughuli za uvuvi pamoja na mifugo, ahsante sana.

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, tuna Skimu ya Udimaa na Skimu ya Ngaiti ambazo zimechakaa sana, lakini zipo kwenye bajeti ya mwaka huu: Je, ni lini Serikali itaanza utekelezaji wa kujenga hizi skimu mbili ambazo nimezitaja? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ni kweli tunajua katika baadhi ya maeneo skimu nyingi zimechakaa, kwa maana ni za muda mrefu. Ndiyo maana kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, tayari tumeshaweka fedha kwenye mwaka huu wa 2023/2024. Kwa hiyo, muda wowote tutaanza kutekeleza skimu hizo ikiwemo ya kwa Mheshimiwa Mbunge kule Manyoni ili kuhakikisha skimu hizo zinaboreshwa ili ziweze kutoa faida kwa wakulima na kuweza kuhakikisha kilimo cha kisasa kinaendelea, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; kwa kuwa tafiti zinaonyesha magonjwa yasiyoambukizwa yanakua kila siku; je, Serikali haioni haja sasa ya kuanzisha mchakato wa kuanzisha Mamlaka ya Kusimamia Magonjwa Yasiyoambukizwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni tuna Hospitali ya Kilimatinde inayoendeshwa kwa ubia kati ya Serikali na Kanisa la Anglikana, lakini hospitali hii haifanyi vizuri; je, nini mkakati wa Serikali wa kuiboresha hospitali hii iweze kusaidia katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza la kwamba magonjwa haya ya kuambukizwa yanaongezeka, ni kweli yanaongeza na hasa Kusini mwa Afrika yanaongezeka sana. Sasa hata ukiangalia leo kwenye UKIMWI, wewe ni shahidi tunatoka kwenye suala la kuuangalia UKIMWI peke yake kama UKIMWI, lakini tunaangalia magonjwa kwa ujumla na data zinaonyesha kwamba unapomchukua mgonjwa wa matatizo ya UKIMWI ukaangalia suala la pressure wakati huohuo sukari na ukatibu yote kwa pamoja, matokeo yanakuwa mazuri kuliko unapotibu ugonjwa mmoja na kumwangalia kama ugonjwa mmoja.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nafikiri pamoja pia na kuanzisha Taasisi kama alivyoshauri Mheshimiwa Mbunge ambayo itashughulikia hilo moja, tunaweza tukatumia fedha nyingi ambazo bora tu hizo fedha tungepeleka kuenga vituo vya afya kule kwenye jimbo lako.

Kwa hiyo, nafikiri Mheshimiwa Mbunge aendelee kukubaliana na Serikali kwa namna hii ambayo itatumia rasilimali vizuri, lakini wakati huo huo mgonjwa huyo akaangaliwa kwa ujumla wake, kwa sababu mgonjwa anapokuja huwezi tu kusema ni mgonjwa wa pressure au mgonjwa sukari unamwangalia kwa ujumla wake kuanzia saikolojia na mambo mengine ambayo yanafuatana na hilo. Kwa hiyo tukiyaangalia kwa pamoja namna hiyo tutapata matokeo mazuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili la hospitali hiyo ambayo Serikali iko pamoja na Kanisa. Mheshimiwa Mbunge mwenyewe ni shahidi kwenye hii hospitali kwamba Serikali imepeleka watumishi, lakini vilevile Serikali inatoa dawa, pia wanapewa ile asilimia ya basket fund kwa maana ya kuboresha mambo yao. Sasa ninachofikiri kama Serikali imefanya yote hayo na bado Mheshimiwa Mbunge kama mwakilishi wa wananchi bado wananchi wake wanalalamika kwamba huduma inayotolewa bado ni ya chini maana yake inawezekana kuna suala sasa la kiutawala.

Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Mbunge, Manyoni Mashariki ni karibu hapa, saa nne zinatutosha mimi na yeye twende site, tukae kwa saa nne tuangalie mambo mengi ili tuweze kuhukumu kwa haki na kutoa maamuzi ya kuboresha hiyo hospitali kwa namna ambayo tutakuwa tuko site, ahsante.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza. Katika Wilaya ya Manyoni, tuna Gereza la Wilaya na gereza hili wanajishughulisha sana na kilimo, lakini kuna changamoto sana ya zana za kilimo za kisasa. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba tunaliwezesha Jeshi la Magereza la Manyoni ili waweze kujikita kwenye kilimo cha kisasa hususan kupeleka matrekta?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Katika Gereza hilo hilo la Wilaya ya Manyoni tuna upungufu mkubwa sana wa nyumba za watumishi. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba sasa tunawajengea Maafisa Magereza nyumba za kisasa ili nao wajione ni sehemu ya Tanzania? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu umuhimu wa kuwa na zana za kilimo za kisasa ikiwemo matrekta, huo ndio mwelekeo mpya wa Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Jeshi la Magereza kuimarisha vikosi vyake ili viweze kulima kwa tija. Kwa kufanya hivyo tumeimarisha Shirika la Uchumi la Magereza kwa maana ya SHIMA ili lianze kuzalisha kwa tija hatimaye magereza mengine ambayo hayajaingizwa katika utaratibu huu yaweze kuiga kutokana na kazi inayofanywa na SHIMA na moja ya vitendeakazi wanavyotumia ni matrekta. Kwa hiyo, Mheshimiwa atupe muda tu, tutakapokuwa tumeboresha, Gereza la Manyoni litafikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu umuhimu wa kuwa na nyumba bora za watumishi pia ni kipaumbele cha Jeshi la Magereza na kwa sasa wanatumia nguvukazi ya Jeshi la Magereza ili kujiimarisha kwa kujenga nyumba zinazofaa. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kumwomba Mkuu wa Magereza Mkoa wa Singida awasiliane na wenzie wa Magereza yake ndani ya mkoa waanze miradi ya kujenga nyumba za maafisa ili Serikali kwa maana ya Magereza Makao Makuu yaweze kuwa–support vifaa vya kukamilishia majengo hayo, nashukuru. (Makofi)
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ni lini sasa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni nayo itaingizwa kwenye Mradi wa TACTIC? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, tukimaliza tathmini ya hizi tier tatu za miji hii 45, ndipo tutaangalia kama Serikali kuona uwezekano wa kuongeza Miji, Halmashauri za Manispaa na Halmashauri nyingine DC ambazo zipo nchini, ikiwemo ya Manyoni. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge avute subira, na pale ambapo tutakamilisha mchakato huu, kama nilivyokuwa nimemjibu Mheshimiwa Chumi, basi tutaangalia na maeneo mengine ya nchi yetu.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali kwanza nitumie fursa hii kuipongeza Serikali na kuishukuru wametupatia bilioni moja kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Mkoa. Ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya cha Kintiku kinahudumia takribani Halmashauri tatu, Halmashauri ya Bahi, Halmashauri ya Chemba na baadhi ya vijiji vya Halmashauri ya Manyoni. Kituo hiki kipo kwenye high way ya kutoka Dodoma kwenda Mwanza. Je, lini Serikali itapeleka gari la wagonjwa (ambulance) ili iweze kusaidia kwenye kituo hicho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili katika Kata ya Nkonko kuna kituo cha afya ambacho kilijengwa, vilevile walijenga jengo la x-ray ambalo bado halijakamilika. Je, lini Serikali itakamilisha jengo hilo la x-ray katika Kituo cha Afya cha Nkonko ili kiweze kuanza kutoa huduma? ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, kwanza kuhusu hichi Kituo cha Afya cha Kintiku. Ni kweli ninakiri kwamba kituo hiki cha afya ni muhimu sana kwa sababu kipo barabarani na kama alivyosema Mheshimiwa Chaya ni kituo kinachohudumia Wilaya ya Chemba, kinachohudumia wakazi wa Wilaya ya Bahi na Wilaya ya Manyoni yenyewe na kipo kilometa takribani kama 26 ama 27 kutoka mpakani mwa Dodoma na Mkoa wa Singida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hivi sasa imetenge bilioni 93 kwa ajili ya ununuzi wa magari 316 ya wagonjwa nchi nzima na kwa kuanzia kila Halmashauri itapata walau magari mawili ya wagonjwa. Tayari magari 117 yameshanunuliwa mpaka kufika mwezi Mei mwaka huu na tutahakikisha tunaweka kipaumbele kwenye vituo vya afya vya maeneo ya kimkakati kama Kituo cha Afya cha Kintiku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali lake la pili la Kituo cha Afya Kata ya Nkonko ambacho kinahitaji jengo la x-ray. Tutaangalia katika mwaka wa fedha 2023/2024 kuona ni namna gani Serikali Kuu itaongeza nguvu kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kuweza kukamilisha ujenzi wa jengo hili la x-ray katika Kituo cha Afya cha Nkonko ili wananchi wa maeneo haya waweze kuanza kupata huduma za x-ray.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Jimbo la Manyoni Mashariki, Shule ya Msingi ya Iseke, Makanda na Sasagila ni kongwe sana. Je, nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba wanapeleka madarasa kwenye hizi shule kongwe? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Pius Chaya, Mbunge wa Manyoni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hili lini Serikali itapeleka fedha katika shule hizi kongwe. Tayari Serikali kupitia mradi wa BOOST imetenga zaidi ya bilioni 230 kote nchini kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa shule kongwe hapa nchini na shule mpya katika halmashauri mbalimbali ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni. Hizi shule za Iseke, Makanda na Sasajira nazo tutazifanyia tathmini kuona uhitaji uliopo na baada ya hapo tutaziweka katika mipango yetu kwa ajili ya ofisi kutoa fedha.
MHE. DKT. PIUS STEPHEN CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa hii nafasi kuuliza swali la nyongeza. Katika Jimbo la Manyoni Mashariki kuna mradi wa maji wa Kintiko wa vijiji 11 Mkandarasi alisaini Mkataba mwezi Februari mwaka huu lakini mpaka sasa hivi kazi haijaanza. Nini kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba Mkandarasi anaanza kazi ya kumalizia huu mradi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Chaya Mbunge wa Jimbo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huo anaongelea Mheshimiwa Mbunge ni kweli lakini nampongeza kwanza Mkandarasi ameanza kufanya kazi zile za awali na kinachosababisha hajaanza anasubiria advance payment lakini ninamsihi pale anapoweza kuendelea kufanya aendelee kwa sababu malipo haya yako mwishoni na yeye pia atalipwa kwa sababu tumeshapokea andiko lake.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali, na kwa kuwa mradi huu umechukua miaka sita sasa tangu ulipositishwa, ninayo maswali mawili ya nyongeza: -

Mheshimiwa Spika, je, ni lini sasa Serikali itakamilisha mchakato wa kupitia hasara zilizosababishwa na kusimamishwa kwa mkataba huu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni lini Serikali itakamilisha mchakato wa kumpata mkandarasi mpya ili kazi ya ujenzi wa mradi wa Mhalala uweze kuanza? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyonyeza ya Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Manyoni Mashariki kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, suala la kwanza, Benki ya Maendeleo ya Ulaya iko tayari, na fedha zipo kwa ajili ya kuendeleza. Kilichokuwa kinachelewesha ni kwamba baada ya kuingia mgogoro wa kimkataba ilikuwa ni lazima Serikali ihakikishe kwamba wanakaa pamoja na mkandarasi huyu ili waweze kukamilisha changamoto zote zilizokuwepo, wakishakubaliana sasa ndiyo waingie mkataba kutafuta mkandarasi mwingine wa kukamilisha.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni imani ya Serikali kwamba kwa mwaka tunaoanza wa fedha tutahakikisha kwamba mkandarasi anapatikana, na kazi iliyobaki, Kituo cha Ukaguzi hiki cha Muhalala pamoja na kile cha Nyakanazi, kwa sababu vyote vilisimama kwa pamoja vinaanza kujengwa na kukamilika kwa sababu ni muhimu sana kwa ajili ya kulinda barabara zetu, ahsante.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa hii nafasi. Katika Jimbo la Manyoni Mashariki, tuna araja la Sanza ambalo tayari upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ulishafanyika na hilo daraja liliingizwa kwenye bajeti hii inayoishia. Sasa nini kauli ya Serikali kwamba ni lini ujenzi wa hili daraja utaanza?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Chaya, Mbunge wa Manyoni, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, daraja hili ni kati ya madaraja makubwa ambayo yameainishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, nasi kama Wizara, daraja hili tayari limeshapata kibali cha kuanza kujengwa pamoja na barabara zake za maingilio.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, katika Jimbo la Manyoni Mashariki kuna Kata ya Makutupora ambayo ilipangiwa kujenga shule mpya, lakini mpaka sasa hivi fedha ya kujenga shule mpya katika Kata ya Makutupora haijapelekwa. Je, ni lini sasa Serikali itapeleka fedha hii ili shule ianze kujengwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa utoaji wa elimu ya awali katika Mkoa wa Singida bado ni hafifu; je, nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba sasa tunaajiri walimu wa elimu ya awali hususani katika maeneo ya vijijini ya Mkoa wa Singida? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Chaya, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki kama ifuatavyo;-

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi ya Serikali na ujenzi wa shule ya sekondari katika Kata ya Makutupora iko pale pale na tutajenga kata hiyo kwa sababu fedha zipo katika bajeti yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili kuajiri walimu wa awali katika ajira hizi zilizotangazwa moja ya kigezo ambacho tumezingatia ni kuajiri walimu wapya ambao wana shahada ya elimu ya awali na stashahada ambao tutawapeleka katika shule zote nchini ili kusaidia hii elimu ya awali nchini.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kwa kuwa kumekuwa na changamoto nyingi sana kwenye huu mfumo wa stakabadhi ghalani; je, nini mpango wa Serikali sasa kutoa elimu kwa wakulima wa choroko na dengu kabla ya mfumo haujaanza?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, mfumo wa stakabadhi ghalani unahitaji uwepo wa warehouse (maghala); nini mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba wanaanzisha maghala katika halmashauri zote ambazo huu mfumo unakwenda kufanyakazi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Chaya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la kwanza la kuhusu elimu, Wizara tumejipanga kutoa mwongozo ambao ndani yake pia unajumuisha masuala ya elimu na masuala yote ya muhimu kabla ya kuingia katika Mfumo wa Stakabadhi za Ghala. Lengo letu ni kutatua changamoto ambazo zimekuwepo na hivyo kupitia mwongozo huu utakuwa umetibu tatizo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili kuhusu maghala, tunafahamu kwamba moja kati ya requirement kubwa ya stakabadhi za ghala lazima kuwepo na maghala. Katika bajeti yetu ambayo tumeisoma kupitia Wizara ni kwamba katika mwaka wa fedha unaokuja tunakwenda kujenga maghala mengi katika maeneo ya uzailishaji, lengo letu ni kuhakikisha kwamba nchi yetu inakuwa na maghala kuanzia katika ngazi za vijiji ambapo wanazalisha kwenda juu. Kwa hiyo katika eneo hilo, Serikali imeona imeona umuhimu na tumetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa maghala.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nakushukuru kwa kunipa hii nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa nimeliuliza hili swali mara mbili hapa Bungeni na majibu ya Serikali yamekuwa kwamba Halmashauri bado haijawasilisha andiko; na kwa kuwa tayari Waziri ana taarifa kwamba kuna andiko ambalo limeshaandikwa, lakini limechukua muda mrefu.

Sasa je, nini kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba inaweka mkakati wa kuzisaidia Halmashauri zote nchini ambazo zinahitaji kuja na hii miradi ya kimkakati ili ziwasilishe hii miradi kwa wakati?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Waziri yupo tayari kuambatana nami kwenda katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni ili akajionee hali halisi ya stendi ya mabasi ambayo ipo? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Chaya amekuwa akifuatilia sana sana miradi ya maendeleo kwa wananchi wa Jimbo la Manyoni Mashariki ikiwemo stand hii na ni kweli ameuliza hapa mara pili. Na nitoe maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kwamba andiko hili limekuwa likisubiriwa kwa muda mrefu na sasa tunatoa maelekezo kwa tarehe hiyo ambayo wameji-comment tarehe 30 Juni, lazima andiko liwe limefikishwa hapa ili Serikali ifanye tathmini na kuona namna ya kuwaletea wananchi wa Manyoni maendeleo.

Mheshimiwa Spika, niko tayari kuambatana na Mheshimiwa Mbunge kwenda Manyoni, tutakubaliana baada ya Bunge hili tuweze kwenda kuona stand hiyo.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipata nafasi hii. Kituo cha Polisi cha Sanza, ni chakavu sana ambacho kipo katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni. Nini mkakati wa Serikali wa kuwasaidia Wananchi wa Sanza kujenga kituo kipya cha Polisi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uchakavu wa Kituo hiki na Mheshimiwa ameomba tujenge Kituo Kipya. Naomba anikubalie tufanye tathmini ya kiwango cha uchakavu wa kituo kilichopo. Tutakapobaini gharama za kufanya ukarabati ni kubwa au zinakaribia kulingana na ujenzi wa kituo Kipya. Basi tutaunga mkono juhudi zako kwa kujenga kituo kipya, nashukuru sana. (Makofi)
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali la nyongeza.

Katika Jimbo la Manyoni Mashariki tuna Bwawa la Mbwasa ambalo tayari upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ulishafanyika. Je, nini kauli ya Serikali kuhusu lini itaanza ujenzi wa bwawa hilo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Chaya, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bwawa la Mbwasa liliwekwa katika mpango kupitia Benki ya BADEA na hivi sasa tunajiandaa kwa ajili ya ujenzi wa bwawa lenyewe, lakini vile vile na skimu za umwagiliaji katika bajeti ya fedha ya mwaka 2023/2024.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa hii nafasi. Kwa kuwa Naibu Waziri amesema upembuzi yakinifu wa ujenzi wa minara umeshafanyika na katika Kata ya Iseke tayari walishafika: Je, ni lini sasa ujenzi wa mnara wa mawasiliano utaanza katika Kata ya Iseke? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Dkt. Chaya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Iseke kama ambavyo nimejibu katika majibu mengine ni kwamba, vifaa vikishaingia nchini na hatua za kiufundi na za kiutaratibu na za kisheria zikishakamilika, tutahakikisha kwamba Kata ya Iseke tunaanza ujenzi mara moja na kuhakikisha kwamba Wananchi wa maeneo hayo wanaendelea kufurahia matunda ya nchi yao, ahsante sana.