Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Pius Stephen Chaya (16 total)

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya utafiti ili kubaini uwepo wa aina mbalimbali za madini katika Jimbo la Manyoni Mashariki hususan Kata za Sasilo, Makuru, Kintinku na Solya?
NAIBU WAZIRI WA MADINI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Taasisi yetu ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (Geological Survey of Tanzania - GST) kwa nyakati tofauti imefanya utafiti wa awali, nisisitize tu utafiti wa awali katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania zikiwemo Kata za Makuru, Solya, Kintinku na Sasilo ambako ndiko Mheshimiwa Mbunge anatoka.

Mheshimiwa Spika, matokeo ya tafiti za awali zilizofanyika katika maeneo hayo zinaonesha kuwa kuna viashiria vya uwepo wa madini kama ifuatavyo:-

(a) Katika Kata ya Makuru – kuna dhahabu kidogo pamoja na ulanga (nickel);

(b) Katika Kata ya Solya – Kuna urani, thorium na madini ya ujenzi;

(c) Katika Kata ya Kintinku – kuna Urani; na

(d) Katika Kata ya Sasilo – kwa utafiti uliofanyika hakukuonekana kwamba kuna viashiria vya uwepo wa madini.

Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha uchimbaji kufanyika, mara nyingi sana tafiti za kina zinahitajika ili kujiridhisha na kiwango cha mashapo iwapo yanaweza kuchimbwa kwa faida au la.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha Mradi wa Maji wa Kintinku – Lisilile ili wananchi wa vijiji 11 vya Kata za Chikuyu, Makutupora, Maweni na Kintinku waanze kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji Kintinku- Lusilile ni mradi mkubwa ambao unatekelezwa kwa awamu nne na hadi mwezi Machi, 2021 utekelezaji wa awamu ya kwanza umefikia asilimia 90 kwa gharama ya shilingi bilioni 2.085. Kazi zilizofanyika ni pamoja na ufungaji wa mitambo ya kusukuma maji, ujenzi wa nyumba ya mtambo wa kusukuma maji, tanki la kukusanya maji la lita 300,000 na ujenzi wa tanki la kuhifadhi na kusambaza maji la lita milioni mbili na ulazaji wa bomba kuu umbali wa kilometa 1.2. Aidha, vijiji vitatu vya Chikuyu, Mwiboo na Mbwasa vinatarajiwa kuanza kupata huduma ya maji mwezi Juni, 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia RUWASA imepanga kukamilisha usambazaji wa maji katika vijiji vyote 11 katika mwaka wa fedha 2021/22 na utahudumia wakazi zaidi ya 55,000.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kwa sababu Hospitali iliyopo haikidhi mahitaji kutokana na uchakavu na ongezeko la watu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Jimbo la Manyoni kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa hospitali 43 kongwe na chakavu za Halmashauri ikiwemo Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni. Serikali inaendelea kufanya tathmini ya miundombinu ya hospitali hizo ili kuona namna bora ya kuziboresha ikiwemo kuzikarabati au kujenga hospitali mpya kulingana na matokeo ya tathmini.

Mheshimiwa Spika, Serikali imepanga kukamilisha kwanza ujenzi wa Hospitali za Halmashauri 28 na hivyo baada ya ujenzi huo kisha hospitali chakavu zitawekewa mpango.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza ujenzi wa barabara ya kutoka Manyoni - Sanza - Chipanga - Bahi hadi Dodoma kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ninapenda kujibu Swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Manyoni East – Heka - Iseke - Sanza - Chipanga katika Wilaya ya Bahi; Chidilo Juction – Bihawana Juction Dodoma yenye urefu wa kilometa 194 ni barabara ya mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania TANROADS ambapo ni Mkoa wa Singida na Dodoma. Kati ya hizo kilometa 126 zinasimamiwa na TANROADS Mkoa wa Singida na kilometa 68 ni Mkoa wa Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii kiuchumi, Serikali imeanza na hatua ya kwanza ya ujenzi wa daraja la Sanza ambapo kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa daraja lenye urefu wa mita 75 na barabara unganishi zenye jumla ya urefu wa kilometa 14.5 kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami umekamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, jumla ya Shilingi milioni 1,500, sawa na bilioni 1.5 zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Daraja la Sanza ambalo ni kiungo muhimu kwa barabara hii inayounganisha Mkoa wa Singida na Dodoma. Aidha, mipango ya ujenzi wa sehemu ya barabara inayobaki kwa kiwango cha lami itaendelea kufanyika kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhuisha vigezo vya mfumo wa miradi ya kimkakati kupitia maandiko ya miradi ili iweze kusaidia Halmashauri kubuni miradi ya kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejikita katika kutoa huduma bora na zenye uhakika kwa wananchi wake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba Mamlaka za Serikali za Mitaa zinaendelea kujiongezea mapato kwa kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao ili kutoa huduma bora kwa lengo la kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka Serikali Kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kufikia lengo hili, Serikali iliandaa mkakati maalum wa kuwezesha halmashauri kujitegemea kimapato. Katika kutekeleza mkakati huo, Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatakiwa kuhakikisha zinatumia kwa ukamilifu fursa za kimapato zilizopo katika maeneo yao na kuongeza uwezo wa kujitegemea kimapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za kugharamia miradi ya kimkakati hutolewa kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa na Wizara ya Fedha Mipango. Hivyo, hoja ya Mheshimiwa Mbunge kuhusu uboreshaji wa vigezo vilivyowekwa kwenye uchambuzi wa miradi ya kimkakati imechukuliwa na kwa sasa Serikali inaangalia njia bora itakayosaidia kuboresha utaratibu wa maombi na vigezo vya uandaaji wa miradi ya kimkakati kabla ya utoaji wa fedha.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza upembuzi yakinifu wa ujenzi wa kiwango cha lami barabara ya Manyoni East – Heka – Isseke - Sanza hadi Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GEOFREY G. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Manyoni East – Heka – Isseke – Sanza – Chali – Igongo hadi Bihawana Junction Dodoma ni barabara ya Mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS). Barabara hii ina urefu wa kilometa 193 na kati ya hizo kilometa 124 ziko Mkoa wa Singida na kilometa 69 ziko Mkoa wa Dodoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, Serikali imekamilisha usanifu wa kina na maandalizi ya nyaraka za zabuni kwa daraja la Sanza lenye urefu wa mita 75 lililopo kwenye barabara hii. Kazi hii ilikamilika mwaka 2018. Kwa sasa Serikali inatafuta fedha za kulijenga. Kazi za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara hii zitafuata kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili kuhakikisha kuwa inaimarika na kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka huu wa fedha wa 2021/2022, jumla ya Shilingi milioni 1,513.284 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara hii. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo cha VETA katika Wilaya ya Manyoni?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Jimbo Manyoni Mashariki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inayo azma ya kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka huu wa fedha Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni mia moja kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi katika Wilaya 62 kwa Wilaya ambazo zilikuwa hazijajengewa Vyuo vya Ufundi Stadi. Aidha, Wilaya ya Manyoni ni miongoni mwa Wilaya hizo 62 ambazo zipo kwenye mpango wa kujengewa Vyuo vya Ufundi Stadi kwa mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa ambapo Serikali inaendelea na hatua hizi, nashauri wananchi wa Wilaya ya Manyoni wakiwemo wa Jimbo la Manyoni Mashariki waendelee kutumia Chuo cha Ufundi Stadi cha Mkoa wa Singida, na Chuo cha Wilaya ya Ikungi, Pamoja na Vyuo vya Singida vya FDC na vyuo vingine vya ufundi stadi vilivyopo hapa nchini. Ahsante.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza: –

Je, kuna mpango gani wa kujenga Kituo cha Polisi Tarafa ya Kintinku Manyoni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na Kituo cha Polisi pamoja na nyumba za makazi ya askari katika Tarafa ya Kintinku. Kwa sasa wakazi wa eneo hilo hupata huduma toka Kituo Kidogo cha Polisi kinachotumia jengo lililokuwa ghala la mazao ya kilimo waliloazimwa na Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni.

Mheshimiwa Spika, Serikali inamshauri Mheshimiwa Mbunge, ashirikiane na Uongozi wa Wilaya na Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, kutenga eneo mahsusi kwa ajili ya kujenga kituo na nyumba za askari ili Serikali iweze kukiingiza kituo hicho katika mpango wake na kukitengea fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Mradi wa Maji wa Kintinku- Lusilile katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji Kintinku-Lusilile ni mradi uliopangwa kuhudumia Vijiji 11 vya Chikuyu, Mwiboo, Mbwasa, Makutupora, Mtiwe, Chilejeho, Maweni, Mvumi, Ngaiti, Kintinku na Lusilile. Mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ilikamilika mwezi Oktoba, 2021 na Vijiji vitatu vya Chikuyu, Mwiboo na Mbwasa vinapata huduma ya maji. Katika mwaka wa fedha 2022/ 2023, utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi unaendelea na unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2022 na kuboresha huduma ya upatikanaji wa maji katika vijiji vyote 11.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza: -

Je, ni lini barabara ya kutoka Kintinku hadi Makanda inayounganisha Mkoa wa Singida na Dodoma itahamishiwa TANROADS?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007, kifungu cha 11 na Kanuni za Usimamizi wa Barabara ya mwaka 2009 kifungu 43(1) na (2) na kifungu 44(1) kupitia Tangazo la Serikali Na. 21 ya tarehe 23 Januari 2009, zimeainisha vigezo na utaratibu wa kuhamisha barabara ili iwe chini ya TANROADS ambapo barabara inaweza kupandishwa au kuteremshwa toka daraja moja kwenda daraja lingine.

Mheshimiwa Spika, suala la kupandisha hadhi barabara ni la kisheria na kuzingatia vigezo. Ili barabara iweze kupanda kutoka daraja la barabara ya Wilaya kwenda daraja la barabara ya Mkoa (kusimamiwa na TANROADS) inatakiwa barabara hiyo ijadiliwe kwenye Kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa husika na ikionekana inakidhi vigezo, Bodi hiyo kupitia kwa Mwenyekiti itamshauri Waziri mwenye dhamana na barabara kuwa barabara husika imekidhi vigezo na hivyo ipandishwe daraja na kuwa chini ya TANROADS.

Mheshimiwa Spika, hivyo, nashauri utaratibu wa kuhamisha barabara kwenda TANROADS uzingatiwe ikiwemo kwa hii ya Kintinku - Makanda kwenda TANROADS.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Vituo vya Afya Kata za Chikola na Makanda katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ilipokea vipaumbele vya ujenzi wa vituo vya afya katika Kata za Sanza, Chikola na Makanda zilizopo katika Jimbo la Manyoni Mashariki. Katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali ilipeleka Shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kimkakati cha Sanza ambapo ujenzi wa awamu ya kwanza kwa OPD na maabara umekamilika. Ujenzi wa awamu ya pili, unaohusisha wodi ya wazazi, chumba cha upasuaji na laundry upo kati hatua ya ukamilishaji.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Afya vya kimkakati nchini ikiwa ni pamoja na kwenye Kata za Chikola na Makanda kadri fedha zitakavyopatikana.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga campus ya Chuo Kikuu Mzumbe katika Mkoa wa Singida?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na mpango wa kupeleka huduma ya elimu ya juu katika mikoa isiyokuwa na Chuo Kikuu au Taasisi ya Elimu ya Juu ukiwemo Mkoa wa Singida. Kwa sasa Serikali kupitia Mradi wa Higher Education for Economics Transformation (HEET) imetenga jumla ya Dola za Kimarekani milioni nane kwa ajili ya upanuzi na ukarabati wa Kampasi ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) katika Mkoa wa Singida. Maandalizi ya shughuli za ujenzi yameshaanza ambapo hadidu za rejea za kumpata Mshauri Elekezi na Mkandarasi, Michoro na Mpango kabambe wa Ripoti ya Tathmini ya mazingira na Jamii (Environmental and Social Impact Assessment) vimeshaanza kuandaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jitihada hizo za kusogeza elimu ya juu kwenda mikoa ambayo haina taasisi hizo, Chuo Kikuu cha Mzumbe pia kupitia mradi wa HEET kimepangiwa kujenga kampasi mpya katika Mkoa wa Tanga katika Wilaya ya Mkinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanzisha Mamlaka ya Kuratibu na Kupambana na Magonjwa Yasiyoambukiza?

NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Manyoni Mashariki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Afya imekwishaunda programu maalum ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza ndani ya Idara ya Tiba ambayo ina jukumu la kuandaa miongozo na mikakati ya kisekta kwenye mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu imekwishatekeleza jukumu hili kwa kukiongezea jukumu Kitengo cha Afya Moja (One Health) kusimamia magonjwa yasiyoambukiza chini ya Kurugenzi ya Menejimenti ya Maafa, naomba kuwasilisha.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Jengo la OPD katika Kituo cha Afya cha Kintinku ambacho kimeanza kutumika bila kuwa na jengo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 Serikali ilitenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa Kituo cha Afya Kintinku. Aidha, majengo matano yalijengwa ikiwa ni pamoja na jengo la Wazazi, jengo la Upasuaji, jengo la Kufulia, jengo la kuhifadhia maiti na nyumba ya mtumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni imetenga shilingi milioni 20 katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo la OPD.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu msingi katika vituo vya afya kote nchini kikiwemo Kituo cha Afya Kintiku.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Ukaguzi wa Magari cha Muhalala – Manyoni?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Manyoni Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Kituo cha Ukaguzi wa Pamoja cha Muhalala Manyoni ulisimama kutokana na mkandarasi kusitisha utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kituo hicho tarehe 11 Septemba, 2018 ukiwa umefikia 60.1%.

Mheshimiwa Spika, kusitishwa kwa ujenzi wa mradi huo kulisababisha mkandarasi kuingia katika mgogoro wa kimkataba na Serikali. Hivi sasa Serikali iko katika hatua ya kukamilisha makubaliano ya stahili za pande zote mbili kati ya Serikali na mkandarasi. Aidha, kwa kuwa Mkataba wa Ufadhili chini ya Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU) bado unaendelea, Serikali itaendelea na mchakato wa kutafuta mkandarasi mwingine atakayemalizia kazi zilizobaki mara baada ya makubaliano ya stahili kukamilika, ahsante.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi katika Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni imekwishaandaa wazo mradi (concept note) kwa ajili ya ujenzi wa Mradi wa kimkakati wa stand ya mabasi. Kazi inayoendelea kwa sasa ni kutafuta msanifu wa mradi kwa ajili ya kuandaa michoro ambayo itawezesha kujua gharama halisi za mradi huo. Kazi hii ya usanifu inatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 Juni, 2022.

Mheshimiwa Spika, baada ya kupata gharama halisi za mradi huo na kukidhi vigezo vya mradi wa kimkakati, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuutekeleza. Ahsante.