Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Pius Stephen Chaya (7 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, nami nachukua nafasi hii nikushukuru wewe, lakini kipekee sana namshukuru Mwenyezi Mungu na nimshukuru sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa kazi kubwa ambayo ameifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wote ni mashahidi kwamba wakati Mheshimiwa Dkt. Magufuli anaingia, nchi yetu ilikuwa inakusanya mapato machache sana. Hivi sasa tuna uwezo wa kukusanya zaidi ya shilingi trilioni mbili kwa mwezi. Haya ni mafanikio makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya maombi yetu yote ambayo tunayatoa hapa ya maji, elimu na barabara hayawezi kutokea iwapo hatutamuunga mkono Rais katika kusimamia ukusanyaji wa mapato. Kwa hiyo, nawaomba Wabunge wenzangu, tutakapofika Bunge la Bajeti, tuweke mikakati ya kuisaidia Serikali ili tuwezekuongeza mapato, ili haya mahitaji ya Watanzania ambayo wote tuna azma kubwa ya kuitimiliza, yaweze kufanikiwa.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ya Rais, lakini pia nampongeza kwa kuja na approach ya kuanzisha Mamlaka ya Maji yaani RUWASA. Sisi sote ni mashahidi, kabla hatujaanzisha Wakala wa RUWASA, maji na upatikanaji wa maji katika vijiji vyetu ilikuwa shida sana.

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu la Manyoni Mashariki, tuna mradi mmoja mkubwa wa shilingi bilioni 11 wa Kitinku/Lusilile. Huu mradi una-cover vijiji 11 na tayari tumeshapata takribani shilingi bilioni mbili. Mbali ya kwamba tumeanzisha hizi Wakala, bado nina ushauri kwa Wizara ya Maji. Ushauri wa kwanza ni kwamba nadhani tusiwe na utitiri wa miradi ya maji. Tujitathmini kwa miradi ambayo tumeianzisha, tutengeneze acceleration plan, kwamba kwa kipindi gani tutamalizia ile miradi ambayo tayari tumeshaianzisha.

Mheshimiwa Spika, Rais wetu ni mtu wa matokeo, anataka kuona matokeo kwa kitu alichokianzisha. Kwa hiyo, naishauri sana Wizara ya Maji, kwa miradi ambayo tumeianzisha, tusikimbilie kuanzisha mradi mpya, tutengeneze acceleration plan ya lini tutamalizia ile miradi, halafu tuangalie ni jinsi gani tunaweza ku-scale up hii approach ambayo tumeanza nayo kwenye maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, vilevile naomba Wizara ya Maji iongeze wigo wa financing ya Mfuko wa Maji. Kutegemea chanzo kimoja ku-finance miradi ya maji, bado naona tunaipa mzigo sana Serikali. Naomba wakati Bunge la Bajeti likifika Wabunge tuangalie jinsi gani tutaisaidia Wizara ya Maji, tuje na options mbalimbali za kupanua wigo wa kuongeza financing mechanism ya miradi ya maji.

Mheshimiwa Spika, suala la TARURA, vilevile namuunga mkono Rais hasa kwa kuanzisha Wakala wa Barabara (TARURA). Sote ni mashahidi, kulikuwa na tatizo kubwa sana la ujenzi wa barabara za TARURA, lakini wachangiaji wengi wameelezea suala la kuongeza na kubadilisha allocation formula ya 70 kwa 30.

Mheshimiwa Spika, nina hoja mbili; hoja ya kwanza, nadhani tatizo ni ile fixed approach, kwa sababu tunatumia 70 kama ilivyo na 30 kama ilivyo. Nashauri tuwe flexible. Mahitaji ya utengenezaji wa barabara yanategemeana na demand ya mwaka huo. Kuna kipindi demand ya barabara ya vijijini ni kubwa kuliko demand ya barabara za mjini ambazo zinasimamiwa na TANROADS. Nashauri sasa kwamba inapofika kipindi ambacho tunahitaji kupeleka bajeti TARURA na TANROADS, basi mfuko wa barabara usikilize mawazo ya TARURA na TANROADS, wa-present waone kwamba je, kweli TARURA wanahitaji asilimia 30 au wanahitaji zaidi ya asilimia 30? Hiyo ndiyo hoja yangu.

Mheshimiwa Spika, lingine nashauri kwamba, tuna- depend sana kwenye chanzo kimoja cha ku-finance TARURA. Tuna-depend sana kwenye fuel levy, ambacho nadhani kimelemewa. Nashauri Bunge lako tukufu tutafute options nyingine za ku-finance TARURA. Badala ya kusema tuongeze asilimia 30, nadhani kuna haja sasa ya kuhakikisha tunaongeza wigo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Chaya.

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii nikushukuru sana kwa nafasi uliyonipatia. Pia nimshukuru sana Dkt. Mwigulu pamoja na timu yake kwa kuja na huu Mpango mzuri sana. Mapendekezo yangu yatajikita kwenye usimamizi wa miradi ya kimkakati. Wewe mwenyewe unatambua kwamba tumefanya mambo makubwa sana katika nchi hii katika miradi ya kimkakati ukiwepo ununuzi wa ndege zaidi ya 10, ujenzi wa reli ya kisasa, lakini vile vile tunategemea kuanza ujenzi wa bandari mbalimbali hapa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, hapa Dodoma tumekuwa na miradi ya kimkakati mingi sana. Hivi karibuni wenzetu wa Jiji la Dodoma wamemaliza ujenzi wa hoteli kubwa sana ambayo itakuwa five star haya yote ni maendeleo makubwa sana ambayo yameletwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi. Sasa hoja yangu ni kwamba, katika hii miradi ya kimkakati ambayo ni uwekezaji mzuri sana kwa nchi yetu, lakini nalitazama katika upande wa usimamizi. Kwa sabbau tayari tuna sera ya Public Private Partnership, Sera ya Ubia kati ya Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo hususan Private Sector, lakini tuna sheria ya ubia kati ya Public Sector and Private Sector. Nadhani ni muda muafaka sasa sisi kama Serikali tuangalie jinsi gani tunaenda ku-capitalize kwenye hii sera ili tuweze kuisadia Serikali.

Mheshimiwa Spika, nataka kushauri kwa mfano, tuna mradi mkubwa hapa Dodoma wa hoteli, hoteli ya five star, je, tunaenda kutumia business modal gani kuhakikisha kwamba ile hoteli inaenda kufanya kazi vizuri. Kwa nini tusiingie kwenye huu ubia sasa wa Private Sector na Public Sector tukaangalia ni maeneo gani ambayo Private Sector wana uwezo nayo tukawaachia, halafu yale maeneo ambayo sisi tuna uwezo nayo tukayafanyia kazi. Hilo ni la kwanza ningependa kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Spika, lingine, tuna miradi mingine ambayo ni mikubwa tunaifanya. Sasa hivi tunasisitiza suala la Public Private Partnership, naomba nimshauri Waziri kwa nini wasiunde task force ikaenda kupitia miradi yetu yote ile mikubwa wakaja kuishauri Serikali kuja na business modal ya jinsi gani tunaweza ku-manage hii miradi. Kwa nini tusiende kwenye ile management contract kwamba eneo ambalo Serikali tuna uwezo nalo tutalifanyia kazi, lakini yale maeneo ambayo Serikali hatuna uwezo nayo, nashauri tunahitaji kuchukua maamuzi magumu ili kuhakikisha kwamba Private Sector na yenyewe ili iweze kukua tunahitaji kuigawia sehemu ya ile miradi ili waweze kuisimamia. Kuna faida nyingi katika hili.

Mheshimiwa Spika, kwanza, tunaenda kukuza ajira; Pili, tunaenda kukuza mahusiano kati ya Public Sector na Private Sector; na Tatu, itatufanya sisi tulale. Badala ya Waziri wa Fedha kulala anawaza kwamba sijui mradi huu haufanyi vizuri, una-transfer risk, unampelekea mtu mwingine, kazi yetu inabaki kukusanya kodi lakini vile vile kuangalia gawio letu mwisho wa mwezi.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii, naomba kwamba Serikali ichukue haya maoni yangu na iyafanyie kazi. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa nafasi hii lakini nimshukuru sana Waziri kwa kuleta Mpango huu. Nimeupitia Mpango huu ni mzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nishukuru kwa miradi mikubwa ambayo tumeiwekeza kwa miaka mitano. Huo ndiyo mwelekeo sahihi wa nchi, lazima tuwe na capital investment. Kama tunataka hili Taifa baadaye liwe lenye heshima lazima tuanze kuwekeza sasa hivi kwenye miradi ya muda mrefu; miradi ya umeme, barabara, reli na ununuzi wa ndege. Bila kufanya hivyo litakuwa taifa lenye aibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite kwenye tatizo la ajira kwa vijana wetu wanaomaliza vyuo vikuu. Watu wengi wameongelea kero mbalimbali upande wa elimu kwamba elimu yetu ni mbovu na kadhalika. Mimi naomba niwatoe mashaka kwamba ingekuwa mbovu mimi leo nisingekuwa Daktari hapa wa Policy, ingekuwa mbovu Mwigulu leo asingekuwa Daktari pale wa Uchumi. Nadhani kuna maeneo ambayo sisi kama wataalam tunahitaji kuishauri Serikali, ni case by case na tusi-generalize. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia Mpango huu kwa kweli naomba niseme tunahitaji kuja na chapter ya pekee ni jinsi gani tunakwenda kutatua tatizo la ajira kwa vijana wetu waliomaliza vyuo vikuu. Mimi naomba nijikite kwa vijana waliomaliza vyuo vikuu tu kwa ngazi ya cheti, diploma na digrii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa Mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dodoma na nimefundisha Chuo cha Mipango, nina vijana wangu ninaowafahamu wamemaliza wana miaka 8 bado wapo mtaani. Wanaoathirika zaidi ni watoto wa maskini ambao hawapo aggressive, hawajui wapi pa kuanzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashauri nini Serikali? Kwanza, natambua kuna program ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inaendeshwa na ndugu zetu wa TAESA, wengi tumepiga kelele hapa kwamba vijana wanamaliza vyuo hawana uwezo, huwezi kupata uwezo chuoni, uwezo tunaupata kwa kupitia on job training. Kule tunafundisha theory lakini lazima tuje na programu ambayo itawahamisha wale vijana kutoka kwenye theory kwenda kwenye practice na ndiyo kitu ambacho Ofisi ya Waziri Mkuu wamefanya kupitia program hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamefanya nini? Wamechukua vijana kama internship program wamewaweka pale kwa mwaka mmoja wakawapa token ya 150,000 then wakawasaidia kuwa-groom, wanawapitisha kwenye zile life skills, interpersonal skills, communication skills, computer skills na kadhalika, aki-graduate pale wanam-link na job seekers au wale supplier wanaotaka watu kwa ajili ya kuwaajiri. Hiki ndiyo kitu ambacho mimi nashauri huu Mpango ujikite kwamba tuendeleze ile program ambayo imeshaanza, financing yake ambayo bado ipo weak vijana wanapomaliza vyuo wajiunge pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka tuje na Sera ya Internship. Tuna vijana wengi wapo mtaani tunalalamika kwenye vituo vya afya hakuna watoa huduma wa afya, tunalalalmika kwenye sekondari hakuna walimu lakini tuna vijana wengi mtaani. Ile program ambayo Waziri alikuja nayo wanawapa shilingi 150,000 kwa mwezi kwa nini tusiifanye hiyo program tuajiri vijana wale tuwaweke kwenye health facilities, tuwalipe shilingi 150,000. Kwanza itakuwa tumewapunguzia stress ya maisha, tumepunguza stress ya wazazi kuwatunza na tumepunguza stress ya watoto wa kike kuolewa tukawaweka pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kuja na hiyo program kwenye huu Mpango kwamba sasa internship program iwe compulsory, tutengeneze sera na sheria kijana yeyote akishamaliza ile miaka mitatu anakuwa mainstreamed kwenye internship program. Akishamaliza pale, hapa sasa uhusiano kati ya TAESA na Sekretarieti ya Ajira, nitashangaa kuona Sekretarieti ya Ajira unamuacha kijana ambaye Mheshimiwa Waziri amem-groom mwaka mzima kupitia internship program unaenda kumchukua mtu hajapita kwenye program hiyo. Tunapiga kelele vijana hawana skills, hizo skills tutazijenga kwa kupitia internship program na Sekretarieti ya Ajira sasa fanyeni kazi na TAESA ili kuhakikisha kwamba vijana wanaokuja kule hatutakuwa na malalamiko hawawezi kujieleza, tayari tumeshawa-groom kwa mwaka mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine hili ni la Wizara tofauti. Tunapoenda kutumia hii program ya internship, nataka tuje na kitu kinaitwa policy maximum, hebu sisi kama nchi tujiwekee ukomo wa kisera, kijana asikae zaidi ya miaka miwili tangu amemaliza chuo. Tunajisikia aibu vijana wanakaa miaka mitano mtaani wanatembea na vyeti, sisi wenyewe tumewafundisha, tumewekeza na tunataka warudishe zile kodi. Hebu tuje na sera ambayo nimei-propose tuweke kiwango cha ukomo kwamba sasa Viwanda, Uwekezaji na watu wengine ambao sisi ndiyo creators wa kazi tukae pamoja tutengeneze modeling ya vitu gani ambavyo tunahitaji kuvifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kitu kimoja, kwa mfano, kwenye huu Mpango sijaona zile ajira milioni 8 ambazo tumeahidi tunaendaje kuzifikia? Tunahitaji kufanya modeling mwaka wa kwanza tutahitaji kufikia labda watu milioni mbili, mwaka wa pili milioni 3. Halafu pia tunawapataje hawa, ni kutoka private sector au public sector? Hicho kitu natamani kifanywe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni Mfuko wa Kuchochea Ajira kwa Vijana. Nashukuru Mheshimiwa Waziri ameliweka vizuri kwenye Mpango wake na namuunga mkono lakini naomba niboreshe kwenye ….

T A A R I F A

MBUNGE FULANI: Taarifa.

SPIKA: Taarifa, nimekuona Mheshimiwa.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mchangiaji kwamba vijana wanaomaliza vyuo vikuu akiona zizi la ng’ombe, akiona kinyesi anakimbia, akiona banda la kuku anakimbia. Vijana hawa wanaomaliza chuo kikuu hawajapata mahali popote pale pakwenda ku- practice hata kama ni kilimo kidogo. Shule zetu kuanzia sekondari tumeondoa mashamba darasa, hakuna mahala ambapo mwanafunzi anaenda ku-practice.

Mheshimiwa Mwenyekiti, graduate anawazungumzia mchangiaji hawajawahi ku-practice hivyo vitu kuanzia wanaanza darasa la kwanza mpaka wanamaliza hiyo degree. Mimi napigiwa simu kama Mbunge, Mheshimiwa Mbunge tunaomba utusaidie kazi, nawauliza kazi gani? Wanasema kazi yoyote hata kufagiafagia. Hii inaonesha kwamba mpaka anamaliza chuo kikuu haja-define exactly na kile kinachofanyika nyumbani kwake ufugaji na kilimo haoni kama ni kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimpatie taarifa mwalimu ambaye amefundisha chuo kikuu muda mrefu kwamba watoto kwa upande wa ku-practice vitu ambavyo tunataka viendeleze taifa kwenye kilimo hawa graduates hawajapata fursa hiyo na ni weupe kabisa. Ukimwambia chips kuku anakimbilia kuila ila mchakato wa kupatikana kwa mayai na viazi hataki kusikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Dkt. Chaya muda wako ulishapita, nilikuvumilia tu.

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nachukua nafasi hii nikushukuru sana kwa kunipa hii nafasi. Kipekee namshukuru sana Profesa pamoja na timu yake ya Wizara ya Elimu kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi leo naenda kujikita kwenye mfumo wa elimu. Nimefanya uchambuzi wa mfumo wa elimu na nimejikita kwenye zaidi ya nchi 15 ambazo nimefanya uchambuzi. Nimepitia mfumo wa elimu wa Tanzania, Japan, America, UK, Kenya, China na vile vile nimepitia mfumo wa elimu wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina hoja takriban nne ambazo ningependa kuziwasilisha. Baada ya kupitia mifumo yote hii ya elimu, hoja ya kwanza niliyogundua inaleta utofauti kati ya elimu yetu na elimu nyingine duniani ni suala la muda wa kuanza Darasa la Kwanza na pili suala la umri wa kuanza darasa la kwanza. Vile vile ni aina ya elimu ambayo tunaitoa katika ngazi ya vyuo vikuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili ambayo nimeigundua baada ya kupitia mifumo mbalimbali ya elimu duniani ikiwepo ya Zanzibar na ya Tanzania, kuona ni stage gani ambayo elimu yetu inatakiwa iwe academic, lakini ni stage gani ambayo elimu yetu inatakiwa iwe technical na ni stage gani ambayo tunahitaji kuwa na mixture ya technical na academic? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya tatu ambayo nimepitia nikagundua ni suala la miundo ya mitaala. Katika miundo ya mitaala nimegundua vitu viwili; ya kwanza, ukipitia mitaala yetu kuna tatizo kubwa sana la masaa ya kukaa darasani na vile vile masaa ya kufanya practical, (field work).

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nimeangalia mfumo wa assessment. Katika mfumo huu nilichojifunza, hususan mfumo wetu wa Tanzania, unawaandaa vijana kuwa na exam fear ambayo ni mbaya sana. Katika hili wasiwasi wangu uliopo ni kwamba tumeweka uzito mkubwa sana kwenye mitihani. Unakuta mitihani ya mwisho ina takriban asilimia 70 lakini yale mazoezi ambayo yanaenda kumjengea uwezo yana asilimia 30. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya mwisho ni hoja ambayo Waziri wa Elimu alisema kwamba wanakuja na mfumo wa ku-review sera yetu ya elimu ya Taifa, lakini vile vile kupitia mitaala yetu ya Elimu ya Taifa. Hoja yangu ni kwamba wakati Wizara inajipanga kwenda kufanya mapitio ya hii sera, nadhani ni muda muafaka sasa wa kujikita kikamilifu kuhakikisha kwamba tunakuwa na comprehensive review ya sera. Tuwe na muda wa kutosha katika ku-review and then tuje tujikite katika ku-review mitaala. Maana yake ni nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yangu ni kwamba tunahitaji kuwa na sera ambayo itakuja ku-inform hiyo curriculum ambayo tunaitaka, lakini tunahitaji kuwa na sera ambayo itakuwa customized kulingana na case studies mbalimbali tulizokutana nazo katika nchi mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali baada ya kutoa hoja zangu hizo takriban tano, la kwanza, kama nilivyotangulia kusema, naomba nimshauri Waziri kuwa suala la mapitio ya Sera ya Elimu ni suala la msingi sana. Naomba tunavyopitia Sera ya Elimu ya Taifa, tufanye harmonization na wenzetu wa Zanzibar. Zanzibar elimu ya msingi wanaenda miaka sita, lakini tuna labour mobility ya kutoka Zanzibar kuja Bara, Bara kwenda Zanzibar. Ni muda muafaka sasa tufanye harmonization ya hii mifumo yetu ya elimu ili kuhakikisha kwamba tunapokuwa na wenzetu wa Zanzibar tunaongea lugha moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali ilifanyie kazi. Tunahitaji kuwa na mfumo mmoja wa elimu kwa sababu Bara na Zanzibar ni nchi moja, nasi hatuna restrictions zozote kwenye masuala ya elimu. Kwa hiyo, hilo naomba tulifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, ni suala la kuondoa ile tunaita exam fear. Katika kuondoa exam fear mimi nina hoja ifuatayo: Nimefanya kazi vyuo vikuu. Nimefundisha Chuo Kikuu cha Dodoma muda mrefu na pia nimefundisha Chuo cha Mipango muda mrefu. Kitu nilichojifunza na nimekisema, nadhani kuna tatizo kwenye curriculum zetu. Tumeweka weight kubwa sana kwenye mitihani ya mwisho ambayo inatengeneza exam fear. Mwanafunzi anahangaika ili aweze kupata A na B, badala ahangaike kupata competency. Nataka kushauri kwamba katika hili naomba sasa unapopitia mitaala na sera, punguza weight ya mitihani, peleka weight kwenye practicals, vijana tuwa-expose kwenye mazingira ya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la nne, naishauri Serikali tuanzishe kitu kinaitwa integrated education system. Tuje na combination ya academic na technical. Wabunge wengi wameelezea. Mheshimiwa Waziri wewe unafahamu, tumesoma huko nyuma kwenye shule ambapo tulikuwa tunafundishwa sayansikimu, elimu ya kilimo na vitu vingine, lakini ile elimu ilikufa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapotaka kuandaa vijana waweze kujitegemea, ni muda muafaka sasa kuhakikisha kwamba tuna-impart hizi competences kuanzia huko chini shule ya msingi, sekondari na ile inawajengea palatability ya kupenda, kwamba baadaye niende nikasomee mambo ya kilimo, baadaye nikasomee ufundi na kadhalika. Huwezi kujenga palatability ya mtu akiwa level ya juu, unataka aende akasomee ufundi VETA. Tunahitaji ku-instill kuanzia chini shule za msingi na sekondari ili wale vijana anapotoka pale anasema mimi nataka niwe fundi wa bomba.

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Kuna taarifa, sijajua inatoka wapi? Mheshimiwa Mwita Getere.

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, hapa. Nilitaka nimpe msemaji hapa…

NAIBU SPIKA: Ngoja ngoja. Kulikuwa na taarifa kutoka pale, ndiye niliyemwita. Kwa hiyo, wewe subiri kidogo.

Mheshimiwa Mwita Getere.

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nataka kumpa taarifa Mheshimiwa anayeongea kwamba rushwa siyo lazima iwe kwenye pesa peke yake. Corruption of mind ni jambo kubwa sana katika nchi za Kiafrika na hasa Tanzania. Kuna haja gani ya kutomwekea mtoto maarifa ya kufundishwa namna ya kufuga kuku, namna ya kufuga ng’ombe, namna ya kulima, ukamshindilia ma-pai, ma-triangle na mambo mengi ambayo watoto wengi wanaotoka primary siyo kwamba wote wanaenda sekondari, wengi wanabaki vijijini. Wanaobaki vijijini wanabaki na nini?

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwita Getere, tafadhali naomba ukae kidogo. (Kicheko)

Waheshimiwa Wabunge, taarifa tunazozitoa inabidi ziendane na Kanuni zetu. Mbunge anayeruhusiwa kusema kuhusu taarifa ni pale ambapo Mbunge mwenzake halafu kuna jambo anataka kumpa taarifa iliyo sahihi. Pengine kile anachokisema kimekaa namna fulani hivi. Sasa nimeona Wabunge wanasimama kusema taarifa, wakati anataka kuchangia yeye wazo lake. Sasa hiyo ni kinyume na kanuni zetu, ndiyo maana huwa kuna nafasi ya kuchangia. Usiwe na wazo lako unataka kumpa mwenzako ili na yeye alifanye wazo lake, hapana. Unampa taarifa kwenye kile kile anachokizungumza.

Mheshimiwa Dkt. Pius Chaya, taarifa kutoka kwa Mheshimiwa…

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Hamna Taarifa juu ya taarifa. Kwa hiyo, uwe unasubiri kidogo, tutaenda vizuri tu, hamna shida.

Mheshimiwa Dkt. Chaya unapokea taarifa ya Mheshimiwa Getere?

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Napokea Taarifa ya Mheshimiwa Mbunge na nadhani alikuwa anaunga mkono hoja na mawazo ambayo nilikuwa nayatoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ambacho ningependa kuishauri Serikali ni upande wa vyuo vikuu.

NAIBU SPIKA: Kuna taarifa nyingine. Sasa kwa utaratibu kwa sababu tunajifunza, akishazungumza mmoja akitoa taarifa, lazima mzungumzaji azungumze ndiyo mwingine anaomba tena taarifa. Kwa hiyo, kwa sasa kwa sababu hilo tulikuwa hatujalielewa vizuri, nitakupa nafasi Mheshimiwa Saashisha, lakini kwa kawaida ukikaa chini namna hiyo, akishasimama kuzungumza akaongea, unaomba upya taarifa.

Mheshimiwa Saashisha.

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ahsante pia kwa mwongozo mzuri. Nataka kumpa msemaji taarifa kwamba hapo awali kabla ya mwaka 1919 Wizara ya Elimu ilikuwa na mfumo rasmi kabisa wa shule za msingi za ufundi na kwetu kule Hai tulikuwa na shule tano zenye muundo huo. Yaani watoto wakiwa shule ya msingi walikuwa wanafundishwa pia masomo ya ufundi na kulikuwa na walimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka ninavyozungumza sasa hivi, shule ya msingi ya ufundi Mshara kuna walimu ambao waliandaliwa kwa ajili ya mitaala hii kufundisha rasmi masomo ya ufundi. Tatizo ni kwamba shule hizi zimeachwa hazijaendelezwa. Kwa hiyo, nampa taarifa kwamba kulikuwa na mfumo huu, ila umelala. (Kicheko/Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, nawakumbusha kwenye vishkwambi vyenu zimo Kanuni mle. Tuzipitie vizuri. Huko tunakoelekea kwenye hili Bunge ni mwisho mwisho wa kujifunza Kanuni. Baadaye itakuwa ni mtu kaa chini, sogea kidogo, futa ulichosema. Sasa hivi tunaenda taratibu.

Mheshimiwa Dkt. Chaya malizia mchango wako.

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubali vile vile taarifa ya Mheshimiwa Mbunge na bado naendelea kuishauri Serikali kwamba tunahitaji kuhuisha mitaala yetu hususan katika ngazi ya shule za msingi na sekondari.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho upande wa vyuo vikuu. Kwa uzoefu wangu ambao nimekaa kwenye vyuo vikuu, unakuta kwa mfano wale wanaosoma certificate, diploma, na degree tuna wa-subject kwenye kufanya research. Mwanafunzi gani wa certificate anaweza kufanya research ikatumika katika maisha yetu? Mwanafunzi gani katika level ya diploma anaweza akafanya research ikatumika katika maisha yetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kushauri, Wizara ya Elimu, mje na mfumo unaoitwa capstone project system; huu mfumo unaweza ukatumika kwa ngazi za chini ambao unawajengea uwezo wale watu, tunawa-expose kwenye mazingira ya kazi, wanakuja na ubunifu, innovations. Unaweza ukamchukua mtu ukampeleka kwa mfano TANESCO, anaenda kubuni mradi fulani na ile inakuwa na weight kubwa kama nilivyotangulia kusema huko. Badala ya kuweka weight kubwa kwenye mitihani tunatengeneza fear of exams. Tupeleke weight kubwa kwenye hizi capstone projects ambazo zitasaidia kuwajengea competences na skills. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, namwomba Waziri, katika Jimbo langu la Manyoni Mashariki sina Chuo cha VETA na nina vijana wengi sana waliomaliza sekondari wanahitaji kuwa na Chuo cha VETA.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nichukue nafasi nikushukuru sana kwa hii nafasi. Vile vile nichukue nafasi hii kipekee kumshukuru sana Waziri wa TAMISEMI, dada yetu Mheshimiwa Ummy pamoja na timu yake kwa kazi nzuri ambayo anaifanya.

Mheshimwa Naibu Spika, tunamfahamu vizuri sana dada yetu Mheshimiwa Ummy, hatuna wasiwasi kabisa na utendaji wake. Pia tunawafahamu Manaibu wake vizuri sana, hatuna wasiwasi kabisa na utendaji wao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nina mambo matatu ambayo nahitaji kuishauri Serikali. Jambo la kwanza nitashauri kwa upande wa afya ya msingi, jambo la pili nitashauri upande wa barabara na madaraja na jambo la tatu nitashauri kuhusu suala la ugatuzi wa madaraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natoka katika Jimbo la Manyoni Mashariki. Jimbo langu la Manyoni Mashariki lina zaidi ya vijiji 60. Katika vijiji vile 60 nina vijiji 29 ambavyo vina Zahanati. Vile vile nina Kata 19 na katika Kata hizo, nina Kata mbili ambazo zimejengewa Vituo vya Afya. Kwanza nachukua nafasi hii kuishukuru sana Serikali kwa kutujengea Vituo vya Afya viwilli; Kituo cha Afya cha Kintinku ambacho tayari kimeanza kutumika na Kituo cha Afya cha Nkonko ambacho tayari kilishakamilika, lakini bado kuna changamoto za hapa na pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa hiyo, nachukua nafasi hii kumshukuru sana Waziri, lakini naomba nimkumbushe mambo mawili. Jambo la kwanza, kwenye Vituo vya Afya viwili ambavyo vimejengwa hususan Kituo cha Afya Nkonko tayari kimekamilika, lakini bado hatuna wataalam. Tulipeleka mtaalam mmoja ambaye ni Daktari (Medical Doctor), hakuweza kuripoti. Kile Kituo cha Afya ni kikubwa sana, kinahudumia zaidi ya Kata sita. Naishukuru tena Serikali kwa kutupa hiyo nafasi, lakini bado kile Kituo cha Afya hakitumiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba niishauri Serikali, kwa sababu tuna tatizo la hao wataalam kwenda kwenye Vituo vyetu vya Afya, nadhani tunahitaji kuja na mbinu mbadala. Naishauri Serikali husasan Wizara ya TAMISEMI tuangalie jinsi gani tunaweza tukafanya mapping ya wale vijana waliomaliza Shahada za Udaktari kwenye kanda husika, kwa mfano, Kanda ya Kati ili tunapowapangia vile vituo, tupange kulingana na kikanda. Hii itapunguza kasi ya vijana kutowasili au kutoripoti kwenye vituo vyao. Naomba nilishauri hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nawaza kuhusu balance kwamba, kati ya kujenga Kituo cha Afya na Zahanati kipi kianze? Natambua kwamba Sera yetu ya Afya inatambua kila Kata lazima iwe na Kituo cha Afya, kila Kijiji lazima kiwe na Zahanati, lakini katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi vile vile imebaini kwamba kila Kata inatakiwa iwe na Kituo cha Afya, lakini kila Kijiji kiwe na Zahanati.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu nini? Ni wakati gani sasa tunahitaji kuanza kujenga Kituo cha Afya na ni wakati ambapo tunahitaji kuanza kujenga Zahanati? Hoja yangu inajikita kwenye eneo langu la Jimbo la Manyoni Mashariki ambapo nina vijiji zaidi ya 60 lakini nina Zahanati 29 tu; nina Kata zaidi ya 19 na Vituo Afya viwili. Nadhani Mheshimiwa Waziri unahitaji kuangalia zaidi jinsi ya ku- balance unapofanya maamuzi aidha uanze ku-exhaust Zahanati kwenye Kata then twende kwenye kujenga Kituo cha Afya, badala ya kujenga Kituo cha Afya kwenye Kata ambayo haina Zahanati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nalisema hili? Kuna vijijij vipo mbali sana na kupata huduma za afya. Ningetamani kuona kila Kijiji kinapata Zahanati, then ile Kata ambayo tayari ina Zahanati i-qualify kupata Kituo cha Afya. Lengo letu ni kupunguza umbali wa watu kupata huduma za afya, lakini vilevile ku-promote suala health seeking behavior ili watu wasikimbilie kwenye dawa za kienyeji.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni suala la barabara. Naishukuru Serikali kwanza kwa Kuanzisha TARURA, nilishasema huko nyuma; na kwa Jimbo la Manyoni Mashariki tuna mtandao wa barabara zaidi ya kilomita 1,000 na bajeti yetu kwa mwaka tunapata takribani milioni 600. Mwaka huu tumekumbwa na matatizo makubwa sana ya kuharibika kwa barabara, barabara ya Kintinku Makanda takribani kilomita 30 imejifunga kuanzia Januari mpaka sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Makanda kuna mnada mkubwa sana ambao unachangia pato la Wilaya yetu ya Manyoni, lakini tuna barabara ya kutoka Iseke - Mpapa - Simbanguru – Mangori, ilijifunga kwa muda mrefu sana. Vile vile tuna barabara ya kutoka Chikuyu - Chibumagwa - Mahaka kwenda Sanza, nayo ilijifunga kwa muda mrefu sana. Tunahitaji kufanya nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani ni muda muafaka, watu wengi wamesema tunahitaji kuipa nguvu TARURA, naunga mkono hilo. Kwa upande wa Manyoni Mjini ningemshauri Mheshimiwa Waziri hasa kwa mijini, wilaya ambazo tunazo, Makao Makuu ya Wilaya, sidhani kama bado TARURA wanahitaji kuendelea kukarabati kwa kiwango cha vumbi.

Mheshimiwa Naibu Spika, natamani kuona katika bajeti ya Mheshimiwa Waziri wanatenga angalau kilomita moja kwa ajili ya kujenga barabara za mijini, Makao Makuu ya Wilaya kwa kiwango cha lami, kuliko kuja na barabara za vumbi kwenye Makao Makuu ya Wilaya. Hizi barabara za changarawe na vumbi tuzipeleke vijijini, Natamani kuona tunaboresha Makao Mkuu yetu ya Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, sanjari na hilo, vile vile natamani kuona mnapokuja na mpango wa kujenga barabara za lami kwenye maeneo ya Makao Makuu ya Wilaya tuangalie jinsi gani tutaweka taa za barabarani kwa ajili ya kuboresha miji yetu na vilevile kuwafanya wafanyabishara weweze kufanya kazi kwa muda mrefu na pia itaboresha usalama wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho ni suala la ugatuzi wa madaraka. Mimi ni muumini wa ugatuzi wa madaraka, nimehusika sana katika mchakato wa kuandaa Sera ya Ugatuzi Madaraka. Wote mnatambua kwamba suala la ugatuzi wa madaraka lilianza miaka ya 1998 ambapo tulianza na D by D Policy Paper, ambayo imekaa kwa zaidi ya miaka 20, lakini hatujawahi kuwa na Sera ya Ugatuzi wa Madaraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, D by D Policy Paper ndio ilitumika kama sera ambayo tumeitumia sana kuja na program ya kwanza ya maboresho ya Serikali za Mitaa na program ya pili ya maboresho ya Serikali za Mitaa ambayo iliisha 2014. Kuanzia mwaka 2019, natambua TAMISEMI walianza mchakato wa kutengeneza Sera ya Taifa ya Ugatuzi wa Madaraka. Hoja yangu ni nini? Napenda kujua kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, mchakato wa ile sera ya ugatuzi wa madaraka imefikia wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, namshukuru Mheshimiwa Waziri, katika bajeti yake ameweza kutenga fedha kwa ajili ya program ya kuimarisha Serikali za Mitaa na Mikoa, yaani Regional and Local Government Strengthening Program. Napenda kujua kwamba ni kwa jinsi gani sasa Wizara inakuja kuwahusisha wadau wa maendeleo?

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kwamba katika kuandaa hii program na hata hii Sera ya Ugatuzi wa Madaraka, wadau mbalimbali walihusika sana wakiwepo USAID, UNICEF, EU, DFID, JICA na wengine: Je, Mheshimiwa Waziri amejipangaje kuhakikisha anawahusisha hao wadau ili kiasi cha one point five billion ambacho tumekipanga kwenye bajeti yetu tuweze kupata nguvu vilevile ya wadau ambao walihusika sana katika kuhakikisha kwamba suala la ugatuzi wa madaraka linaenda kupata kipaumbele?

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri na timu yake na ninaomba niseme kwamba naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nachukua nafasi hii kukushukuru sana wewe, nimshukuru kipekee kabisa Waziri, Mheshimiwa Eng. Dkt. Chamuliho na vile vile nawashukuru manaibu wake wawili. Nachukua nafasi hii niwashukuru sana ndugu zangu wa TANROAD Mkoa wa Singida, wamekuwa proactive sana tunapopata matatizo sisi Wilaya ya Manyoni hususan panapotokea matatizo ya kuharibika kwa barabara. Kwa kweli hili naomba niwashukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina hoja tatu ambazo zinaendana na ujenzi wa barabara, lakini vile vile nina hoja ambayo itahusiana na suala la ujenzi wa daraja na hoja nyingine ambayo nataka kuchangia inahusu Kituo cha Pamoja cha Ukaguzi wa Magari (One Stop Inspection Station) ambacho kipo katika Jimbo la Manyoni Mashariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natoka katika Jimbo la Manyoni Mashariki. Kwanza nichukue nafasi hii nimshukuru sana Waziri, katika bajeti hii ambayo ameiwasilisha kuna daraja ambalo linajulikana kama Daraja la Sanza ambalo limekuwepo ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa miaka 10. Nafurahi na namshukuru sana Waziri kwa sababu tayari upembuzi yakinifu ulishafanyika, tayari usanifu wa kina ulishafanyika na tayari zaidi ya 90% ya wananchi walishalipwa fidia zao. Namshukuru sana Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sanjari na hilo, kwa mwaka huu wa fedha, Waziri ametutengea takribani shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hili daraja. Hoja yangu ya msingi, nataka kupata majibu haya wakati Waziri anakuja kuhitimisha kwa sababu hili daraja limekuwa likipangiwa hela kila mwaka lakini haliendi kutekelezeka. Nitapenda kusikia sasa kutoka kwa Waziri: Je, ni lini sasa huo ujenzi wa daraja utaanza? Wamejipangaje kuhakikisha kwamba wanatangaza hizo tenda ili Wakandarasi waanze hiyo kazi ya kujenga daraja? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nina barabara ambayo Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliiahidi alipokuja wakati wa kuninadi wakati wa kampeni. Barabara ya kutoka Manyoni - Heka - Sanza ambayo inaenda mpaka Chaligongo barabara inaenda mpaka Mbabala - Bihawana inatokea Dodoma. Hii barabara ina umbali wa takriban kilomita 200. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii barabara ina umuhimu mkubwa sana. Kwanza hii barabara inagusa Halmashauri nne. Inagusa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, inagusa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, inagusa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi na Halmashauri ya mji wa Dodoma. Kwa maana nyingine, hii barabara inaunganisha mikoa miwili; Mkoa wa Singida na Mkoa wa Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi, hii barabara ni muhimu sana kwa ukuaji wa uchumi wa mikoa miwili hususan Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Singida. Tuna wakulima wengi sana ambao wapo katika Jimbo langu la Manyoni Mashariki, Jimbo la Bahi na Jimbo la Dodoma Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya hilo tuna Game Reserve ya Kizigo ambayo ni maalum kwa Utalii wa Uwindaji. Hiki ni kitega uchumi muhimu sana ambapo kwa kweli tunahitaji kuhakikisha hii barabara tunaiimarisha, nini hoja yangu? Ni muda muafaka sasa kwa sababu Rais Hayati John Pombe Joseph Magufuli alituahidi na tayari ipo ndani ya hii bajeti, lakini haijatengewa fedha. Sasa napenda kusikika kutoka kwa Waziri ni lini tunakuja kujipanga kufanya upembuzi yakinifu (feasibility study), lakini tunakuja kuanza kupanga na kuweka bajeti kwa ajili ya detail design na vile vile, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa hii barabara angalau kwa awamu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu Wabunge wengi wameeleza kilio chao cha barabara mbalimbali, wote tunatambua hizi barabara ambazo zinaunganisha zaidi ya halmashauri mbili, lakini barabara ambazo zinaunganisha mikoa zaidi ya miwili, ni barabara muhimu sana kwa uchumi wa Taifa letu. Kubwa zaidi ndugu zangu wa kutoka kwenye haya majimbo manne wanapata huduma zao nyingi za kiafya Dodoma, hususani katika hospitali ya Mkapa lakini hospitali ya Uhuru na hata Hospitali yetu ya General hapa Dodoma. Kwa hiyo, utaona ni kwa jinsi gani Serikali inahitaji ku-invest kwenye hii barabara ili tuweze kukuza uchumi wa maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni hiki Kituo cha Pamoja cha Ukaguzi wa Magari ambacho kinajulikana kama One Stop Inspection Station na kipo katika Kijiji cha Muhalala. Hiki kituo kimefikia asilimia 50 ya ujenzi wake yaani execution rate na kwa mwaka huu tumetengewa milioni 120 kwa ajili ya ujenzi wa hiki kituo na tayari pale kuna magofu ya majumba zaidi ya miaka miwili yamekaa mradi ulikuwa umesimama. Hoja yangu ni nini? Kwanza nitapenda kujifunza kutoka kwa Waziri je, hii milioni 120 imewekwa kwa ajili ya vitu gani? Ningependa kupata narrative ya hii milioni 120 inaenda kukamilisha asilimia ngapi? Nasema hivi kwa sababu amesema kwamba ni asilimia 50 tu ambayo tayari tumeshakamilisha, bado asilimia 50. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ya pili ningependa kujifunza kutoka kwa Waziri vilevile, atuambie kwamba, je, anategemea huu mradi utaenda kukamilika lini? kama umekaa miaka miwili Serikali haijapeleka fedha, then mwaka huu anatuwekea milioni 120 na tayari ni asilimia 50 tu ndiyo ambayo imeshakamilika, je, hiyo milioni 120 itaenda kukamilisha hiyo asilimia 50. Kwa hiyo, ningependa kupata majibu haya kutoka kwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nirudie tena kumshukuru sana Waziri, lakini vilevile, niwashukuru sana ndugu zangu wa TANROADS Mkoa wa Singida, wamekuwa na mchango mkubwa sana. Tuna barabara yetu ya kutoka Solya kwenda Londoni kwenda Ikungi kwa muda mrefu hii barabara ilikuwa haipitiki kipindi cha masika, lakini hawa ndugu zetu wa TANROADS wa Mkoa wa Singida kwa kweli walikuwa very proactive, tulikuwa tukiwapigia simu wanakuja kutoa ushirikiano mkubwa sana kwa ajili ya kutengeneza

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hii barabara ya kutoka Manyoni kwenda Heka kwenda Sanza kipindi cha masika ilikuwa haipitiki. Hawa ndugu zetu wa TANROAD wa Singinda walitusaidia sana, tulikuwa tunawakuta wamefika site wanakuja kurekebisha. Kilio chetu kikubwa ni hii barabara ya kutoka Manyoni kwenda Heka kwenda Sanza inakuja kutoka Mbambala inakuja kuingia Dodoma, Rais Hayati Magufuli alituahidi kuweka kiwango cha lami, nitapenda kusikia kutoka kwa Waziri anawaambia nini wananchi wa Manyoni sasa hii ahadi ambayo Rais wetu mpendwa hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naomba niishauri Wizara, kuna ahadi nyingi sana ambazo zimetolewa na viongozi wetu wakubwa, wengi wamesema kuna ahadi kuanzia Awamu ya Tatu, ya Nne na Tano. Ningeishauri Wizara wafanye mapping ya ahadi zote, unajua hawa wenzetu wakubwa wakishaahidi wananchi wetu wanakuwa na imani kubwa sana. Hivyo, ni vizuri tukatengeneza mapping na tukatengeneza planning ya jinsi gani kila mwaka wataenda kupunguza zile ahadi. Hawa ni viongozi wakubwa, wametumikia hili Taifa, tunahitaji kuwapa heshima, lakini tukumbuke ahadi ni deni. Mbaya zaidi…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele imeshagonga.

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naomba niunge mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii, lakini naomba nimshukuru Waziri, Profesa Mkenda pamoja na Naibu Waziri, Mheshimiwa Bashe na Watendaji wote wa Wizara.

Mheshimiwa Spika, nina hoja mbili kubwa, hoja ya kwanza ni kuhusu Mfuko wa Umwagiliaji na hoja ya pili ni kuhusu kilimo cha korosho Manyoni. Kwanza, niishukuru sana Serikali tulianzisha Tume ya Umwagiliaji, kuna Kanuni za Umwagiliaji za 2015, lakini kuna Sheria ya Umwagiliaji na vilevile kuna Mwongozo wa Tozo na Ada za Umwagiliaji, hii ni hatua kubwa sana kwenye sekta ya umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini niseme kwamba hatuwezi kuendeleza kilimo cha Tanzania iwapo Profesa hutaweka mkazo na uwekezaji kwenye umwagiliaji. Hiyo itabaki kuwa ndoto, naomba tuige nchi za wenzetu Egypt, Somalia, Sudan na nchi zingine ambazo zimeendelea.

Mheshimiwa Spika, hoja yangu ni nini? Katika Jimbo langu la Manyoni Mashariki nina skimu zaidi ya 8, nina skimu za Udimaa, Ngait, Mawen, Chikuyu, Saranda, Msemembo, Kintinku na Mtiwe. Hata hivyo, nikipitia bajeti hii, sijaona sehemu ambako Profesa unaenda kuwekeza kuhakikisha kwamba ule uharibifu ambao ulisababishwa na mvua kubwa tunaenda kuwakomboa wakulima.

Mheshimiwa Spika, nina masikitiko makubwa kwa sababu kama hatutawekeza kwenye umwagiliaji…

SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Chaya sekunde moja tu, Waheshimiwa Wabunge sasa tumpe nafasi Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mbunge yeyote asiende pale ili apate kusikiliza masuala ya kilimo kwa sababu ni muhimu sana. Anayemhitaji Waziri Mkuu tuna ofisi hapa Administration kuanzia saa 7.00 mchana mpaka saa 11.00 jioni mnaweza mkaenda kumuona. Sasa hivi muacheni ili asikilize hoja za Waheshimiwa Wabunge kuhusu matatizo halisi ya wananchi maana yeye ndiye Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni. Mheshimiwa Dkt. Chaya, endelea. (Makofi)

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, hoja yangu ni nini? Mwaka jana katika hizi skimu nyingi za umwagiliaji ambazo ziko katika Jimbo la Manyoni Mashariki zilipata adha kubwa sana ya mvua. Niliwasiliana sana na wenzetu wa Tume ya Umwagiliaji nawashukuru, waliahidi kuja kuturekebishia.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Mfuko wa Umwagiliaji, nina hoja kadhaa ambazo napenda kulishauri Bunge. Kwanza huu mfuko ambao tumeuanzisha na umeanza kufanya kazi mwaka jana unategemea ada na tozo za wanachama. Sasa tunategemea huu mfuko uje ujenge skimu kubwa hapa Tanzania lakini unategemea skimu ambazo hazijaendelezwa. Profesa naomba uliangalie hili, tunahitaji kwanza kuwekeza kwenye skimu hizi, kuzirekebisha ili huo mfuko wako utune. Bila kuwekeza kwenye hizi skimu Profesa hizi skimu zitabakia kuwa ndoto na mfuko utabakia kuwa ndoto na umwagiliaji Tanzania utabakia kuwa ndoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine hivi vyama vya wamwagiliaji vimeanzishwa lakini havijapewa mafunzo na utendaji wake wa kazi upo chini sana. Napenda kujua Profesa umejipangaje kwenye bajeti yako kuhakikisha kwamba, kwa mfano kwenye zile skimu zangu 8, umeweka bajeti ya kuja kuviwezesha vile vyama vya umwagiliaji, uwape mafunzo, wajue jinsi ya kusimamia mifuko hiyo, jinsi ya kuchanga na hata jinsi ya kuchukua hizo tozo na kurudisha kwenye mfuko wa Serikali. Kwa hiyo, naona hii ni hoja ya muhimu na ningemshauri Waziri aweze kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni suala la kilimo cha korosho. Mimi naishukuru sana Serikali tumeanzisha kilimo cha korosho na baadhi ya Wabunge wetu humu wengi mna mashamba ya korosho kule Manyoni. Tunatumia block farming system ambapo wakulima wengi wameungana na nimshukuru sana Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kuhakikisha kwamba kilimo cha korosho kinaenda kuwa na tija.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tumeanza uvunaji wa awamu ya kwanza wa korosho kule Manyoni. Hoja yangu hapa, nitatamani kusikia kutoka kwa Profesa kwenye bajeti hii, amejipangaje sasa kuhakikisha kwamba Manyoni kilimo cha korosho kinakuwa chenye tija? Je, mnawasaidia vipi watu wa Manyoni kwa kuja na mfumo rafiki sasa kwenye masuala ya masoko, maghala na kuwa na mfumo rafiki kuhakikisha kwamba wale wakulima wawe sasa na matumaini ya zao la korosho?

Mheshimiwa Spika, kuna sintofahamu kubwa sana kuhusu suala la korosho. Nimesikia ndugu zangu wa Mtwara na Lindi wakilalamika, hatutaki hayo makosa yatokee Manyoni na ningetamani kuona sasa Waziri anakuja kwenye bajeti yake na bajeti ambayo Manyoni itakuwa ni sehemu ya kipaumbele kwenye suala la korosho na hasa kipindi hiki ambapo tumeshaanza kuvuna ili wananchi na wakulima wetu wapate matumaini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la miundombinu. Tutatamani kuona Waziri unakuja na bajeti ambayo kwa Manyoni ambapo Bodi ya Korosho inafanya kazi ni jinsi gani mnaenda kuwasaidia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Chaya, dakika tano ni ndogo.

MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)