Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mahmoud Hassan Mgimwa (8 total)

MHE. COSATO D. CHUMI (K.n.y. MHE. MAHMOUD H. MGIMWA) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika Kata ya Ikongosi likiwemo na Gereza la Ilupilo, Kata ya Ikweha yenye Vijiji vya Ukelemi, Uyela, Ugenza, Uhambila, Makongomi, Matelefu, Utosi pamoja na Mbugi.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mahmoud Hassan Mgimwa, Mbunge wa Mufindi Kaskazini, lililoulizwa na Mheshimiwa Chumi, Mbunge wa Mafinga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya kufikisha umeme katika maeneo yote nchini ikiwa ni pamoja na maeneo ya Vijiji vya Mufindi Kaskazini. Aidha, Vijiji vya Kata ya Ikongosi likiwemo Gereza la Ilupilo, Kata ya Ikweha, Vijiji vya Ugenza, Makongomi, Matelefu, Mbugi, Uhambila, Ukelemi, Utosi na Uyela vitapatiwa umeme kupitia mradi kabambe wa REA Awamu ya Tatu. Ujenzi wa mradi huu utaanza mwezi Desemba, 2016 na kukamilika katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kupeleka umeme kwenye vijiji hivyo pamoja na Wilaya nzima ya Mufindi itahusisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33, yenye urefu wa kilometa 242, ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 81, ufungaji wa transformer 24, pamoja na kuwaunganishia wateja wa awali 3,533. Kazi hizi zitagharimu shilingi bilioni 11.92
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA Aliuliza:-
Serikali imeweka pesa nyingi sana katika mradi wa umwagiliaji uliopo katika Kijiji cha Ikweha, Kata ya Ikweha, lakini unashindwa kuanza kwa kuwa Serikali imeshindwa kujenga bwawa.
(a) Je, ni lini mradi huu utakamilika ili kutoa ajira kwa vijana walio wengi katika Kijiji cha Ikweha?
(b) Je, Serikali itawachukulia hatua gani wakandarasi waliojenga mradi huu chini ya kiwango?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mahmoud Hassan Mgimwa, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuendeleza Skimu ya Umwagiaji ya Ikweha, Serikali ilitekeleza mradi huo kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza ilitekelezwa kwa gharama ya shilingi milioni 435.9 na awamu ya pili ilitekelezwa kwa gharama ya shilingi milioni 370.7. Baada ya kukamilika kwa awamu hizo kulikuwa na mapungufu mbalimbali ambayo yalibainika na yalitakiwa kurekebishwa ndani ya kipindi cha matazamio ya miezi 12 kilichotarajiwa kukamilika mwezi Agosti, 2016. Hata hivyo, kutokana na ucheleweshaji wa malipo kwa kazi alizokuwa amezifanya iliababisha
ucheleweshaji wa marekebisho wa mapungufu hayo. Kwa sasa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi na mkandarasi wamekubaliana marekebisho hayo yaanze kufanyika mwezi Aprili, 2017.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, endapo mkandarasi atashindwa kukamilisha marekebisho hayo yaliyo kwa muda wa matazamio wa miezi 12, Serikali itamchukulia hatua za kisheria kulingana na mkataba ili kumtoza tozo na kutolipa kazi ambazo ziko chini ya kiwango.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kujenga mabwawa kama hatua muhimu ya kukabiliana na changmoto za mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha usalama wa chakula kupitia kilimo cha umwagiliaji. Serikali katika Bajeti ya mwaka 2017/2018 itafanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa mabwawa mbalimbali ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji likiwemo hili la Ikweha.
MHE. RITTA E. KABATI (K.n.y. MHE. MAHMOUD H. MGIMWA) aliuliza:-
Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipokuwa Waziri wa Miundombinu aliahidi kupandisha hadhi barabara ya kutoka Mtiri – Ifwagi – Mdaburo, Ihanu, Isipi –Mpangatazara – Mpalla Mlimba ambayo inaunganisha Wilaya ya Mufindi na Wilaya ya Kilombero pia Mkoa wa Iringa na Morogoro.
Je, ni lini Serikali itapandisha hadhi barabara hiyo muhimu kwa uchumi wa Wilaya ya Mufindi na Taifa kwa ujumla ambayo Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi imeshindwa kuihudumia wakati wote?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mahmoud Hassan Mgimwa, Mbunge wa Mufindi Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mtili – Ifwagi –Mdaburo, Ihanu, Isipi – Mpangatazara – Mlimba ni barabara ya Wilaya inayohudumiwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu inaifanyia kazi ahadi hiyo ya Serikali ya kuipandisha hadhi barabara hii na barabara nyingine nchini kwa kuzingatia vigezo vilivyoainishwa kwenye Sheria ya Barabara Na. 13 ya Mwaka 2007 na Kanuni za Menejimenti ya Barabara za mwaka 2009. Baada ya taratibu za kisheria kukamilika, Wizara yangu itamjulisha Mbunge pamoja na kutangaza barabara zilizopandishwa hadhi kwenye Gazeti la Serikali.
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA aliuliza:-
Mwaka 2013 Waziri Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Mizengo Kayanza Pinda, aliahidi kutoa shilingi 295,000,000 kwa ajili ya kusaidia ukamilishaji wa mradi wa umwagiliaji uliopo katika Kijiji cha Nundwe, Kata ya Ihalimba.
Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi hii ya Waziri Mkuu Mstaafu ili vijana walio wengi wapate ajira?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza napenda nimshukuru sana Mwenyezi Mungu. Lakini la pili, nimshukuru sana Rais wangu, Dkt. John Pombe Magufuli, lakini pamoja na wewe na Waheshimiwa Wabunge wote, kwa ushirikiano wote mnaonipa kipindi ambacho nipo Bungeni hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mahmoud Hassan Mgimwa, Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ahadi ya Waziri Mkuu Mstaafu, Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda, ilianza kutekelezwa mwaka 2014 kwa Serikali kutoa kiasi cha shilingi milioni 101 ikiwa ni sehemu ya ahadi ambapo fedha fedha hizo zilitumika kujenga banio la Skimu ya Umwagiliaji ya Nundwe. Wakulima wa skimu hiyo waliweza kuchangia nguvukazi kwa kuchimba mfereji mkuu wenye urefu wa mita 1,500. Hata hivyo, usakafiaji wa mfereji mkuu kwa lengo la kudhibiti upotevu wa maji haujafanyika kwa sababu ya ufinyu wa bajeti.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa mradi huu, Wizara yangu hivi sasa inafanya mapitio ya mpango kabambe wa umwagiliaji wa mwaka 2002 ambapo miradi yote iliyoanzishwa na haijakamilika na ile inayohitaji ukarabati imepewa kipaumbele katika utekelezaji. Hivyo basi, mradi huu utaingizwa katika bajeti ya mwaka 2018/2019 kwa hatua zaidi ya utekelezaji.
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA aliuliza:-
Mheshimiwa Mizengo Pinda akiwa Waziri Mkuu mwaka 2013 aliahidi kuchangia shilingi 295,000,000 katika mradi wa umwagiliaji uliopo kijiji cha Nundwe, kata ya Ihalimba.
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo ili wananchi wa eneo hilo waweze kujikwamua kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mahmoud Hassan Mgimwa, Mbunge wa Mufindi Kaskazini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2013 alitoa ahadi ya kuchangia kiasi cha shilingi 295,000,000 katika ujenzi wa mradi wa umwagiliaji wa kijiji cha Nundwe kata ya Ihalimba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari serikali ilishaanza utekelezaji wa mradi huo kwa kuwezesha upimaji wa ulalo wa ardhi, usanifu wa banio, ujenzi wa banio, ujenzi wa mfereji mkuu wenye urefu wa mita 2000 na ujenzi wa maumbo ya mashambani. Kazi zote hizo zilikamilika mwaka 2015 na kugharimu kiasi cha shilingi 101,000,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa mradi huo kwa wananchi wa Kijiji cha Nundwe na Taifa kwa ujumla Serikali itaendelea kutafuta na kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji iliyobaki kwa lengo la kuongeza uhakika wa usalama wa chakula na kipato na hivyo kujikwamua kiuchumi.
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD (K.n.y. MHE. MAHMOUD H. MGIMWA) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya mawasiliano katika Kata za Mpanda, Mpangatuzara, Ihanu na Ikweha?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mahmoud Hassan Mgimwa, Mbunge wa Mufindi Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa huduma ya mawasiliano nchini, Serikali kwa kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, uliyaainisha maeneo ya Kata za Mapanda na Ikweha na kuyaingiza katika zabuni ya awamu ya pili ‘A’ kwa ajili ya kuwekewa huduma za mawasiliano. Kata hizo mbili zilipata mzabuni wa kufikisha huduma ambaye ni Vodacom. Kazi ya kufikisha huduma ya mawasiliano ilishakamilika ambapo vijiji vya Ugenza, Ukelemi na Uyela katika Kata ya Ikweha vinapata huduma hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, baadhi ya maeneo ya Kata hiyo hususan Kijiji cha Ikweha hakina mawasiliano. Kwa upande wa Kata ya Mapanda, huduma inapatikana katika baadhi ya maeneo ya Kata hii lakini mengi ya Vijiji vya Mapanda, Chogo, Ukami, Uhafiwa na Ihimbo havina huduma hii muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote itayaainisha maeneo ya Kata za Ihanu zenye Vijiji vya Isipii, Lulanda, Ibwanzi na Kilosa; Kata ya Mpanga yenye Vijiji vya Mpanga, Tazara; Kata ya Ikweha, Kijiji cha Ikweha; na Kata ya Mapanda yenye Vijiji vya Mapanda, Chogo, Ukami, Uhafiwa na Ihimbo na kuyaingiza katika miradi ya mfuko ambayo itakayotekelezwa siku za usoni kwa kadri ya upatikanaji wa fedha hususani kuanzia mwaka huu wa fedha 2018/2019.
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA aliuliza:-

Barabara ya kutoka Kinyanambo A – Isalavamu – Igombavanu – Sadani hadi Madibira ilikuwepo kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2005 – 2010 na 2010 – 2015 lakini hadi sasa haijajengwa kwa kiwango cha lami:-

(a) Je, ni sababu zipi zilizofanya Serikali kutoanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami, hasa ikizingatiwa kuwa barabara hiyo ni muhimu kwa uchumi wa Wilaya za Mbarali na Mufindi?

(b) Je, ni lini sasa ujenzi wa barabara hiyo utaanza?

(c) Je, ni lini Serikali itaanza uthamini kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi wanaopisha ujenzi wa barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mahmoud Hassan Mgimwa, Mbunge wa Mufindi Kaskazini, lenye Sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Kinyanambo (Mafinga) – Madibira ni barabara ya Mkoa inayosimamiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na inajulikana kama Barabara ya Rujewa – Madibira – Kinyanambo yenye urefu wa kilometa 152. Barabara hii ambayo kwa sasa ipo katika kiwango cha changarawe, ikiunganisha Mkoa wa Iringa, sehemu ya Kinyanambo na Mkoa wa Mbeya sehemu ya Madibira, imepita maeneo muhimu yenye kilimo cha mahindi na mpunga.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) tayari imefanya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na kuandaa nyaraka za zabuni kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Kazi hii ilikamilika mwaka 2009 ikiwa ni pamoja na kufanya uthamini kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi watakaopisha ujenzi wa barabara hiyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara hiyo kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Hata hivyo, wakati Serikali inatafuta fedha za ujenzi barabara hiyo, itaendelea kufanyiwa matengenezo mbalimbali kila mwaka ili iweze kupitika majira yote ya mwaka.
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA aliuliza:-

Barabara ya Mtiri - Ifwagi - Mdaburo - Ihamu - Mpangatazara hadi Mlimba inaunganisha Wilaya ya Mufindi na Kilombero, na ni muhimu sana kiuchumi na kijamii kwa mikoa hiyo miwili. Aidha, Mheshimiwa Rais aliahidi kuipandisha hadhi barabara hii kuwa chini ya TANROADS.

(a) Je, ni lini Serikali itapandisha hadhi barabara hiyo ili kuwa chini ya TANROADS?

(b) Je, kuna mkakati gani wa dharura kuhakikisha barabara hiyo inapitika kwa wakati wote?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mahmoud Hassan Mgimwa, Mbunge wa Mufindi Kaskazini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mtiri – Ifwagi - Mdaburo – Ihamu – Mpangatazara hadi Mlimba ni barabara ya Wilaya inayohudumiwa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Mufindi. Kufuatia kuundwa kwa TARURA mwaka 2017 maombi ya kupandishwa hadhi barabara za Wilaya kuwa za Mkoa au kusimamiwa na TANROADS kwa kigezo cha kukosa fedha limesimamishwa kwa muda ili kuipatia TARURA fursa ya kutekeleza majukumu mahsusi ya kuundwa kwake.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hii inayopita kwenye maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya biashara na chakula pamoja na kuendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali, barabara hii imewekwa kwenye mpango wa kukarabatiwa kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia mradi ujulikanao kama Road Inclusion and Social Economic Opportunities (RISE). Ahsante sana.