Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Godwin Emmanuel Kunambi (4 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, aliyenijalia afya njema hata siku ya leo nikawa hapa. Pia naomba niunge mkono hoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma hotuba zote mbili za Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais kupitia Serikali yake ya Awamu ya Tano anapojenga SGR maana yake anafanya capital investment, anapojenga Bwawa la Kufua Umeme la Nyerere anafanya capital investment; anapojenga na kuimarisha bandari zote anafanya capital investment; anavyonunua ndege anafanya capital investment. Hii tafsiri yake ni nini? Nchi hii miaka ijayo hatuna tena changamoto kwenye suala zima la ukuaji wa uchumi wa nchi yetu kwa sababu Mheshimiwa Rais ameshatuwekea misingi bora ya kukua kwa uchumi wetu na Taifa letu. Kwa hiyo itoshe kusema katika hili nampongeza sana Mheshimiwa Rais na namwombea Mungu amjalie Maisha mema.

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi Serikali ya Awamu ya Tano imefanya mambo makubwa sana kwenye sekta mbalimbali. Ushauri wangu ni eneo moja ambalo linahusu mgawanyo wa huduma hizi kitaifa. Tukifanya tathmini ya ujenzi wa barabara, huduma ya afya, elimu, kitaifa utaona kwamba kuna baadhi ya watu lugha hii hawaielewi. Nikisema tumejenga vituo vya afya kadhaa kitaifa, mwananchi wa Jimbo la Mlimba ambaye hana kituo cha afya haelewi lugha hii. Ukisema tumejenga lami kiwango cha urefu kadhaa, maana yake mwananchi wa Mlimba ambaye tangu azaliwe hajaona lami hawezi kuelewa lugha hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa rai yangu na ushauri wangu na kwa sababu jukumu langu kama Mbunge ni kuishauri Serikali na kwa kuwa tunakwenda kufanya maandalizi ya Mpango wa Taifa, nashauri Wizara husika, hasa Wizara ya Fedha na Wizara nyingine za kisekta, umefika wakati sasa tutazame mgawanyo na uwiano wa huduma hizi kitaifa ili lugha hii kila mwananchi Mtanzania aielewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu kama walipa kodi ni Watanzania wote. Sasa inaleta changamoto kidogo mwananchi wa Mlimba anayelipa kodi ikaenda kujenga Dar es Salaam na yeye kimsingi ni mwananchi ambaye ana haki ya kupata huduma zote mbalimbali. Kwa hiyo nishauri tunapokwenda kuandaa na ni rai yangu na naamini kupitia Mawaziri hawa mahiri kabisa, hii hoja wataichukua, kwamba tunakwenda kupanga mpango wa kitaifa sasa, tutazame mgawanyo wa huduma hizi kitaifa ili Watanzania wote wanufaike na rasilimali za nchi hii, kwa sababu Serikali yetu siyo Serikali ya majimbo, Serikali ya majimbo ndiyo inahamasisha uneven development.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijikite katika eneo lingine la pato ghafi la Taifa. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri mwenye dhamana ya Wizara ya Mambo ya Nje; hakika anafanya kazi kubwa sana. Ana spidi kali sana, lakini jamani wakati sisi wengine we are lagging behind. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unapozungumzia maendeleo ya Taifa letu lazima Wizara zote tuwe na muunganiko wa pamoja, tuzungumze lugha moja, ili tuhakikishe nchi yetu inakuwa kwa maendeleo kwa kasi zaidi. Kwa mfano, Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje anashughulika sana na kuimarisha mahusiano ya nchi yetu na nchi zingine, kupata wawekezaji wa kigeni. Hata hivyo, inapofika Wizara husika kuharakisha mchakato huo ili mwekezaji wa kigeni awekeze kuna masuala ya nenda rudi, njoo kesho, unajua muda pia ni mali; muda ni mali. Leo siyo kesho, siku ya leo haitapatikana tena kesho. Kwa hiyo ni rai yangu kwamba Wizara zingine zina kila sababu sasa ya kuona zinachangia kasi hii ya Wizara ya Mambo ya Nje, hasa kwenye suala zima la uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema nini hapa; ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Rais ukurasa wa tisa utaona ameeleza namna ya ukuaji wa pato la Taifa kutoka trilioni 94.3 kwa mwaka 2015 hadi trilioni 139.9 mwaka 2019. Tunampongeza Mheshimiwa Rais, lakini swali langu na hoja yangu ya msingi hapa, tunapopima ukuaji wa uchumi wa nchi turudi tujikite kuona hasa kwenye suala zima la export na import. Tuone ni kwa kiwango gani tunauza bidhaa zetu nje na kiwango gani tunaagiza bidhaa ndani ya nchi. Kwa mfano, import ikiwa kubwa kuliko export matokeo yake unakuwa na unfavorable balance of payment. Hoja yangu; tuongeze uzalishaji kwenye sekta za kilimo, kwenye sekta za mifugo, kwenye sekta mbalimbali ili tuweze kukuza pato letu la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijikite kwenye Sekta ya Ardhi. Ardhi tuna fursa kubwa; nishauri tu, tuna kila sababu ya kupima nchi hii kwenye halmashauri zote na jambo lenyewe ni dogo sana. Watanzania wakipata hatimiliki Serikali itaongeza tax base na mwananchi wa kawaida anaweza kukopesheka benki na hii ikasaidia uchumi wa nchi yetu kukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapokwenda kuhitimisha naomba niende moja kwa moja kwenye Sekta ya Barabara. Bado nisisitize Mkoa wa Morogoro ni mkoa wa kimkakati, ni mkoa ambao unalisha Taifa letu, hasa Jimbo la Mlimba. Barabara inayounganisha Mikoa ya Morogoro na Njombe kutoka Ifakara, kilometa 125, ni barabara ya muhimu sana kitaifa. Kwa hiyo rai yangu barabara hii ikijengwa itafungua uchumi wa nchi yetu, lakini pia wananchi wa Mlimba watanufaika na barabara hii. Kwa hiyo kwa kuwa barabara hii imeelezwa kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi Ibara ya 76, ombi langu, Wizara husika ya Ujenzi tunapokwenda kwenye Mpango sasa wa Taifa ni vyema kwenye bajeti yetu tukaanza ujenzi wa barabara hii ili Watanzania hawa wanufaike na barabara hiyo kitaifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalize kwenye Sekta ya Elimu. Jana mzee wangu, Mheshimiwa Dkt. Kimei ameeleza hapa, lakini changamoto kubwa hatuwezi kuboresha elimu, hasa kwenye Sekta ya Ufundi kwa kuanzia kwenye tertiary education. Wenzetu Wachina wana kitu kinaitwa industrial culture na kupitia All Chinese Youth Federation, ukisema uanzie kwenye tertiary education kuimarisha elimu ya ujuzi au ufundi mchundo, hatuwezi; tuanze na level ya shule ya msingi. Kuanzia shule ya msingi kuwe na study maalum tuwekeze kwa watoto wadogo, anapokua anakuwa na industrial culture, anavyokua inamsaidia yeye kukuza kipaji chake. Tunapoendelea kuwekeza kwenye sekta ya elimu ya juu, sisemi haina umuhimu, lakini maana yake tunatengeneza Taifa lenye mameneja wengi kuliko wazalishaji. Matokeo yake hawa mameneja hawana wa kuwasimamia.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu kwamba tujikite, Wizara ya Elimu mama yangu yupo hapa, naomba atusaidie. Ikiwezekana vyuo vya VETA nayo iwe elimu bure, wasilipe chochote na ujenzi wa vyuo vya VETA, vijengwe kwenye ngazi ya tarafa, hasa Jimbo langu la Mlimba, Tarafa za Mngeta na Mlimba. Naeleza haya ili kuona namna gani tunaweza kuona Taifa letu linakwenda mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina hoja moja ya mifugo. Ni kweli tumekuwa nchi ya pili kwa ufugaji, lakini Mheshimiwa Rais ameeleza kwenye hotuba yake kwamba hataki kuona wafugaji, wakulima, wanahangaika. Leo hii unaona mfugaji anayefuga mifugo anaambiwa apunguze mifugo badala ya kumpa njia mbadala kwenye mifugo yake anayofuga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kilimo hali kadhalika; kilimo chetu bado kinahitaji kuongezeka thamani.
Kwa mfano pale Mlimba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Kengele ya pili?

MBUNGE FULANI: Endelea.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kaka yangu, Mheshimiwa Bashe nisikilize hapa kidogo…

NAIBU SPIKA: Muda wako umeshaisha Mheshimiwa.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Umeisha?

NAIBU SPIKA: Ndiyo. Ahsante sana.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naomba kuwasilisha. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na 2) wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze mchango wangu kwa kutoa pongezi za dhati kabisa kwa Wizara ya Katiba na Sheria lakini pia kwa Wizara ya Ardhi, kuna eneo hapa wamenifurahisha ku-address changamoto moja kwa wananchi na nitaieleza baadaye.

Mheshimiwa Spika, naomba niaze mchango wangu moja moja kwa kujielekeza kwa mchango alioutoa hapo awali dada yangu Mheshimiwa Dkt. Pindi Chana, ningekuwa mimi ile Taarifa nisingeipokea, sio Taarifa sahihi, yeye alikuwa sahihi zaidi kuliko mtoa taarifa.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu alichokisema yeye naomba Regional Advocates Ethics Committee, niseme vizuri there is establishment in each region, the Regional Advocates Ethics Committee, end of quote. Ninamaanisha nini? Yeye alichokuwa anasema hiki kipo hapa kwenye regional level anaomba pia neno ethics litumike kwenye National level.

Mheshimiwa Spika, lakini akasema kwenye schedule of amendment ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali bado ameondoa ethics, amebaki na mtazamo wa kuwa naomba nieleze basii…

SPIKA: Umsikilize Mheshimiwa namlinda, ongea na mimi Mheshimiwa.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, kwenye schedule of amendment ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameondoa neno ethics, ethics ameondoa, ameondoa maana yake nini? Hatuna neno ethics kwenye Regional Level au National Level. Ndiyo hivyo, kwa hiyo yeye anasema mchango wake neno hili litumike pande zote mbili. Kwa hiyo, amempa taarifa ya uongo tu. (Makofi)

SPIKA: Tukifika kipengele hicho mtatukumbusha enhee tuone vizuri.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, nilikuwa naona taarifa sahihi kwenye eneo hilo, naomba niende kwenye mchango wangu.

Mheshimiwa Spika, naomba nijielekeze moja kwa moja kwenye mchango wangu kwenye eneo la marekebisho hasa kwenye eneo la Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya. Changamoto kubwa zitatukuta kwenye eneo hili huko mtaani kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, la kwanza, lilikuwa ni ucheleweshwaji wa mashauri haya kwenye level za Mabaraza ya Kata. La pili, ambalo nadhani nitoe ushauri kwa Serikali wakati ujao litazamwe hili pia. Changamoto ya pili, ni kutofika eneo la mgogoro kwa wenyeviti wetu wa Mabaraza haya ya Wilaya ya Ardhi. Changamoto ya tatu, ni mawanda ya ushahidi wa mashauri haya ya Ardhi.

Mheshimiwa Spika, katika utaratibu wa kawaida wa kusikiliza mashauri haya kwenye level za Mabaraza ya Kata, yakishasikilizwa sasa hoja yangu ambayo ningependa nipate ufafanuzi, hii sheria ilivyoleta ime-address changamoto moja ya kuharakisha ucheleweshaji kwamba wakichelewa ndani ya siku 30 huna sababu ya kusubiri Baraza la Kata tena nenda wilayani, jambo jema ambalo nalipongeza kwa Wizara na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wizara ya Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Spika, ninachoomba kwa Serikali wakati ujao na hili wanaweza kulitazama upya, kwamba namna gani liwe takwa la kisheria kwamba Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi la Wilaya atakwe lile takwa la Kisheria kwenda kwenye eneo la mgogoro. Sasa hivi ana hiari ya kwenda au kutokwenda, sasa tatizo na mgogoro wa ardhi changamoto ni eneo la mgogoro. Anaweze akaamua tu akiwa mezani lakini asione upana wa tatizo lenyewe. Kwa hiyo, nadhani Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Wizara ya Katiba na Sheria lakini kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi mlitazame hili katika kipindi kijacho.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni suala la ushahidi, sasa hapa pia nahitaji ufafanuzi Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Imeelezwa tu kwamba ikicheleweshwa ndani ya siku 30 anapaswa kukata rufaa siyo kukata rufaa anakwenda ku-proceed anaanza kama fresh complaints au anakwenda kama rufaa yaani isiposikilizwa anakwenda kuanza upya, lakini je nikisikilizwa na sijaridhika na haki yangu katika ngazi ya Baraza la Kata inakuwaje? Inakwenda kama rufaa au nakwenda kuanza upya na kama inakwenda kama rufaa, hoja yangu ya msingi hapa mawanda ya ushahidi yanafungwa.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu kesi ya msingi kama ikishaikilizwa kwa level ya Baraza la Kata, nikikata rufaa kule Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi la Wilaya yeye hana nafasi ya kufokea tena ushihidi, kwa hiyo ataendelea tu kwa maamuzi yaliyofanyika kwa watu ambao hawana taaluma ya sheria.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ombi langu kipindi kijacho kama hilo pia litatazamwa kwa upande wa Serikali waje na utaratibu ambao unaeleza kwamba mgogoro ule kwenye level ya kata kuamuliwa, sasa sijui utaratibu gani utumike yaani kule uende mgogoro upya ili ufungue mawanda ya ushahidi kwa wale wataalamu wa sheria ngazi za mabaraza wa pale.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni eneo hili la Regional Advocates Ethics Committees. Utamaduni wa leo katika mahakama za kawaida za wilaya, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wamekuwa Wenyeviti wa Kamati za Nidhamu ngazi ya wilaya kwa mahakimu na ngazi ya mikoa kwa Wakuu wa Mikoa kwa mahakimu ndani ya mkoa.

Mheshimiwa Spika, ombi langu katika hili ambalo linahusu mawakili, niiombe Serikali kama itaona inafaa kwa nini Wakuu wa Mikoa hata wawe tu co-opted member inawezekana siyo mwenyekiti, mwenyekiti anaingia kuwa Registrar lakini Mkuu wa Mkoa kwa sababu ana dhamana ya upande wa maeneo hayo ya migogoro ya ardhi awe kama sehemu ya mjumbe yaani co-opted member. Kama siyo co-opted member, siyo mjumbe kamili kwenye eneo hilo lakini Registral aendelee kuwa mwenyekiti ili asije akafanya intervention kwenye maamuzi. Kwa hiyo, ombi langu kwenye ngazi ya mkoa kwa sababu inaishia kwenye level ya mkoa basi, Wakuu wa Mikoa wapate fursa ya kuwa wajumbe kwenye haya Mabaraza yanayohusu Mawakili.

Mheshimiwa Spika, kengele ya pili? Ya kwanza!

Mheshimiwa Spika, eneo la lingine nijielekeze kwenye marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira. Nimeona hapa kuna eneo linaelekeza kwamba anaruhusiwa, inasema hivi; naomba ninukuu:-

“Notwithstanding the provision of sub-section one the Director General may in addition to the fine in cause under sub-section one applies to the court pursuant to the section 193 for feature of any instrument article vehicle or other thing if any respect of which the offence has been committed.”

Mheshimiwa Spika, naona hapa kama kuna adhabu mara mbili, sijui, lakini naona kama kuna adhabu mara mbili, kwamba capitally kuna fine pale juu halafu tena juu hapa bado anaweza akachukuliwa mali zake, nadhani hii itazamwe kwenye Serikali. Kwamba tayari umemtoza mtu faini wakamuhukumu kwenye compound offences aka-clear kila kitu lakini bado kuna fursa ya mtu mwingine Director General anapata fursa ya kuomba hatamu zile mali zake tena anyang’anywe. Hii sidhani kama linaweza kuwa na afya kweli kwenye jamii zetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, michango yangu ni hiyo kwa siku ya leo. Lakini ningeomba pia Serikali initolee ufafanuzi kwenye maeneo haya mawili muhimu ili la Wakuu wa Mikoa lakini na hili la hizi compound offences pale ambapo tunaona kuna adhabu mara mbili. Ahsante.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aliyenijalia afya njema hata siku ya leo ikampendeza niwepo hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nimshukuru Mheshimiwa Rais lakini eneo kubwa nimpongeze, kwa kiwango kikubwa sana amefanya uwekezaji kwenye mtaji kama taifa. Mheshimiwa Rais anavyoelekeza jitihada kubwa katika ujenzi wa reli ya SGR anafanya capital investment (uwekezaji wa mtaji), anavyoimarisha bandari anafanya capital investment, anavyonunua ndege pamoja na jitihada za ujenzi wa Bwawa la Umeme la Nyerere anafanya uwekezaji katika mtaji. Maana yake nini? Maana yake Mheshimiwa Rais anatuandalia taifa ambalo miaka hamsini ijayo sisi akina Kunambi vijana wa leo na vijana wa kesho tutanufaika na mtaji huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme tu kwamba nimesoma mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano. Nianze kwa kusema mpango ni zao la malengo, unavyotengeneza mpango lazima uanze na lengo ambalo litakupa mpango, mpango utakupa mkakati, mkakati unakupa mbinu, mbinu zinakupa mafanikio. Unavyokuwa na mpango lazima ujiandae na mikakati na mbinu za kutekeleza mpango ili tuweze kufanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite kidogo kwenye sekta ya kilimo na kaka yangu Mheshimiwa Bashe ni msikivu sana na naomba katika eneo hili anisaidie kidogo. Ukisoma ukurasa wa 88 mpaka 89 unaeleza habari ya sekta ya kilimo. Sote tunafahamu asilimia 65 ya Watanzania tunapata kipato kutokana na kilimo. Kama hiyo haitoshi kilimo kinachangia takribani 27% kwenye pato la Taifa na kati ya asilimia 27, asilimia 24 ni mauzo ya nje ya nchi na haya yameelezwa kwenye mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado tuna kazi kubwa kwenye sekta ya kilimo, lazima tukubali. Kilimo chetu tunafanya subsistence agriculture, ni kilimo kwa ajili ya kula, not for surplus is for consumption kitu ambacho bado tuna safari ndefu sana. Nchi kama Tanzania yenye ardhi kubwa yenye rutuba lakini bado hatujaitumia vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipata fursa ya kwenda training ya quality structure system ya mwezi mmoja nchini Japan, nilishangaa sana. Nilikutana na Vice President wa JICA alinieleza maneno haya kwamba Japan kwa mwaka mzima wananunua chakula kutoka nje ya nchi ikiwemo Afrika lakini aliitaja Zimbabwe, why not Tanzania? Kama kuna nchi imebarikiwa ukiondoa Kongo inafuata South Africa na Tanzania ni nchi ya tatu kwenye rasilimali za nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, itoshe kusema pamoja na kwamba tuna changamoto ya funding kwenye sekta ya kilimo, lakini tatizo siyo funding inawezekana tukafanya mageuzi makubwa sana kwa kumuunga mkono Mheshimiwa Rais. Changamoto kwa Watanzania kuu ni tatu na siyo tu kwa level fulani, Watanzania wote tuna changamoto kuu tatu. Ya kwanza ni mindset. Marcus Garvey alisema neno moja, ukiwaza juu ya jambo lolote umeshindwa. Ukianza kwa kuwaza tu, mmh, nitaweza kweli umeanza kushindwa mapema na hutashida. Ni mindset kwa maana ya positive thinking. Ndiyo challenge tuliyonayo kwamba inawezekana, yes it can be done, kwa Mtanzania hiyo ni changamoto, unaanza kuwa na hofu kabla hujaanza safari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ya pili ni uzalendo, tulio wengi hatuipendi nchi yetu. Ndiyo maana utaona hata kwenye Utumishi wa Umma watu hawawajibiki. Ile OPRAS ningetamani iende kwa nafasi zote hata kwenye teuzi za Mheshimiwa Rais, kila mtu awe na OPRAS. Kama mtu anateuliwa apewe miezi sita hamna matokeo aondolewe tu. Unakuta kama ni Mkurugenzi, Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa anafika anakuta kiti kilekile na analazimika kukaa kiti kilekile mpaka anaondoka hata kubadilisha kiti hawezi, hata kubadilisha mkao wa kiti hawezi, wengi tuna changamoto hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni commitment, utayari juu ya jambo fulani. Itoshe kusema I am not speaking from without, I am speaking from within, nazungumza mambo ambayo nayafahamu. Naomba niseme hapa bayana lengo ni kujenga nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya kilimo kwenye suala zima la umwangiliaji bado tuna changamoto.

MWENYEKITI: Bado la tatu, umetutajia mawili.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu ni commitment (utayari). Tuna changamoto ya uzalendo, pili mindset kwa maana fikra chanya, tatu ni commitment, haya mambo matatu ndiyo changamoto ya Mtanzania siyo fedha, hatuna shida ya fedha hii nchi ni tajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta ya kilimo tunatakiwa kufanya mageuzi makubwa sana. Kaka yangu Mheshimiwa Bashe pale Mlimba, Kata yangu ya Mgeta ina shamba ya hekta 5,000 mpaka leo zimetekelezwa. Serikali imewekeza kuna miundombinu ya umwangiliaji ndani ya hekta 3,000 na hekta 2,000 ndiyo bado na huu mradi hadi Baba wa Taifa miaka ya 1985 alipewa msaada na Serikali ya Korea lengo ni kuifanya Tanzania ipate uwezo wa kujikimu kwenye chakula. Ule mradi wamekwenda wajanja wajanja fulani mpaka leo umetelekezwa, Serikali imewekeza hekta 3,000 zina miundombinu ya maji ya kumwangilia hekta 2,000 ndiyo bado, hiyo ni fedha ipo pale, tungeenda kule tungefanikiwa. Kaka yangu Mheshimiwa Bashe naomba nimpeleke pale Mgeta, Jimbo la Mlimba akaone jinsi gani Serikali inapata hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni sekta ya ardhi, tuna changamoto ya kodi lakini ardhi ya Tanzania inaweza kutupa fedha nyingi sana. Bado sekta ya ardhi haijafanya kazi. Naomba niseme bayana na Mheshimiwa Waziri au Naibu Waziri naomba mnisikilize. Nchi hii inaweza kupimwa, tuna halmashauri 185 lakini leo hii Wizara ya Ardhi hata kupima halmashauri 50 hatuwezi, kuna haja ya kuendelea kuwepo hapo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina mfano bora, Dodoma hii tunayoona leo, ndiyo maana nimesema naeleza nachokifahamu, Dodoma hii miaka mitatu iliyopita ilikuwa haijapimwa. Mimi ni mfano, Jiji la Dodoma tumepima viwanja 2,000 bila kupata fedha benki wala ya Serikali Kuu. Tukipima nchi hii kwenye halmashauri zote kazi ndogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaeleze jinsi gani wanaweza kupima nchi nzima, Naibu Waziri ananisikiliza. Umesajili kampuni za vijana wa Kitanzania ambao wamesoma, wakajiajiri, ukizipeleka zile kampuni zaidi ya 180, unazo Mheshimiwa Naibu Waziri kwenye ofisi yako, zikapime kwenye halmashauri zote, ardhi ikipimwa ni mtaji tunaongeza wigo wa kodi. Nitasema kweli daima, kuna pesa tunaiacha kwenye ardhi. (Makofi)

MWENYEKITI: Ndiyo maana nchi jirani, si mnajua tuna jirani nchi moja tu, tunazo nchi nyingi lakini moja ndiyo jirani zaidi, yule pale Kaskazini, ndiyo maana bajeti yao ni twice comparing with ours kwa sababu ardhi ya Kenya all most yote imepimwa ukiacha lile jangwa. Kwa hiyo, wanalipia every year ardhi yetu haijapimwa, nakuunga mkono. (Makofi)

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Anachoweza kufanya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi ni jambo moja tu, kuna vijana waliosoma land management na amewasajili, anazo kampuni zaidi ya 180, leo hii ana- discourage kampuni zisipime nasikitika sana. Namshauri aruhusu kampuni za vijana hawa wakapime kwenye halmashauri zote nchini. Yeye kazi yake wale vijana wakipima ardhi ile mwananchi atapata hati miliki, atakopesheka, uchumi wake utakua, kama ni shamba atakopa mkopo benki atalima. Vilevile wigo wa kodi unaongezeka yaani tax base ya nchi inaongezeka. Hizi kodi tunazokusanya ni ndogo sana sekta ya ardhi peke yake inatupa utajiri wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalize kwa kusema, leo nimesema maneno haya Mheshimiwa Naibu Waziri ikimpendeza kuna ule mfumo wa ILMIS awekeze pale, atafuta fedha awekeza kwenye mfumo, hizi kampuni binafsi ziende kwenye halmashauri zikapime. Waziri hana haja ya kupeleka fedha pale, hakuna haja ya hela, nimepima Dodoma viwanja 2,000 bila hela ya Serikali Kuu na kila mtu amepata ardhi hapa Dodoma viwanja bure inawezekana.

WABUNGE FULANI: Tunanunua.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Ndiyo unanunua lakini nimepima Dodoma karibia asilimia zaidi ya 50, kama kuna mbishi asimame hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihitimishe kwa kusema kama kweli tunataka kumsaidia Mheshimiwa Rais Wizara ya Ardhi ijitathimini. Kwa kiwango kikubwa tunataka nchi hii iwe tajiri. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, aliyenijalia afya njema hata siku ya leo nikawa hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja zote mbili, kwa maana ya maazimio yote mawili; lakini pili nijielekeze kwenye azimio la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hayati aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli sisi, ulimwengu wa kimwili tunaona ametangulia mbele za haki lakini bado yu hai. Bado yu hai kwasababu matendo yake, aliyotutendea watanzania yatadumu milele. Na watu wenye vitendo vya namna hii, wenzetu waingereza wanasema immortality ni mtu ambaye anaweza kuishi angali amekufa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kazi kubwa ambayo mimi naomba nilishauri Bunge letu Tukufu; amefanya mambo makubwa ndani ya nchi yetu lakini kukumbukwa kwake kutakuwa ni jambo la msingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda South Africa pale Johannesburg, utaona kuna mnara pale lakini pia kuna sanamu nzuri sana ya Mandela, wanapaita Mandela Square. Kwa kazi kubwa aliyoifanya kuhamisha Makao Makuu yetu ya Nchi kuja Dodoma. Hapa Dodoma kuna eneo tengwa la Serikali na lina haki miliki maeneo ya Chimwaga; na Chimwaga tunafahamu kihistoria. Zaidi ya heka 100 zimetengwa pale kwa ajili ya recreational park, eneo la mapumziko. Niombe kushauri Serikali, ingefaa tujenge monument pale ambayo wajukuu, watoto wetu na kizazi kijacho kitakuwa kikisema Magufuli ni nani? Wanakwenda pale, na hii itatusaidia kumjengea heshima kubwa aliyotutendea Watanzania. Eneo lipo, zaidi ya heka 100 na lina hati ya Serikali na ni mali ya Jiji la Dodoma, kwahiyo hakuna mashaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini baada ya kuzungumza haya nijikite kwenye eneo hili la Rais tuliyenaye Mama yetu mpendwa Samia Suluhu Hassan. Waingereza wanasema, all starts well ends well, all starts well ends well, mama ameanza vizuri, ametuonesha Watanzania kwamba kazi anaiweza. Mfano mzuri leo hii tumeona jina hapa la Makamu wa Rais. Ukitazama unaona matarajio yetu Watanzania, kwamba sasa yale yote yalioachwa na Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli yatakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema haya. Ukiangalia makamu wa Rais yeye amekuwa Waziri wa Fedha, lakini haitoshi, ni bigwa na mbobezi wa kukusanya mapato ya nchi haitoshi pia kubana matumizi. Kwahiyo hii chemistry ya Mheshimiwa Rais, mama yetu Samia Suluhu Hassan na Mheshimiwa Makamu wa Rais ni sawa na oxygen; yaani hydrogen mbili ukijumlisha, wale wana kemia ukichukuwa, ukichukuwa hydrogen mbili ukijumlisha na oxygen moja unapata maji. Kwa hiyo chemical reaction hii hatuna mashaka nayo, lazima maji yatapatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nisichukue muda mrefu, itoshe tu kusema kwamba aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ametubadilishia fikra Watanzania. Kuna watu tulikuwa tunaamini bila rushwa huwezi kupata huduma ya afya, lakini leo hii Watanzania tunaamini utapata huduma ya afya bila rushwa. Kuna watu tulioamini hakuna uwajibikaji ndani ya Taifa hili, lakini leo hii tunaona Taifa letu uwajibikaji umekuwa wa kutukuka na utawala bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nisiseme sana lakini itoshe tu kusema nionge mkono maazimio yote mawili. Ahsante sana.