Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Abdulhafar Idrissa Juma (4 total)

MHE. ABDUL- HAFAR IDRISSA JUMA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kukifungua Kituo cha Polisi cha Betrasi kilichopo katika Jimbo la Mtoni Zanzibar ambacho kimefungwa kwa zaidi ya mwaka sasa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI, Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdul-Hafar Idrisa Juma Mbunge wa Mtoni Zanzibar, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Polisi cha Betrasi ni kituo kidogo cha polisi ambacho kilijengwa mwaka 1994 na kilikuwa kinafanya kazi kwa masaa 12, kutwa na kilikuwa kinawahudumia wananchi wa eneo la Mtoni na kilijengwa na mdau wa ulinzi kwa wakati ule Ndugu Noushad Mohamed. Kituo hiki kilifungwa mwaka 2018 kutokana na uhaba wa askari. Wananchi wa eneo hilo pia wanapata huduma za polisi katika Kituo cha Polisi cha Bububu na pindi pakipatikana ongezeko la askari kituo hicho pamoja na vituo vingine vya aina hiyo vitafunguliwa ili kuhudumia wananchi. Nakushukuru.
MHE. IDRISSA JUMA ABDUL-HAFAR aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupambana na visababishi vya maradhi yasiyoambukiza?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Idrissa Juma Abdul-Hafar, Mbunge wa Jimbo la Mtoni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga shilingi milioni 725 kwa ajili ya kutekeleza Mpango Mkakati wa Tatu wa Kitaifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza (2021 – 2026) ambao umeainisha mikakati mahsusi ya udhibiti wa visababishi vya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo:-

(1) Kuimarisha uratibu na ushirikishwaji wa sekta mtambuka;

(2) Kuimarisha miundombinu ya utoaji wa huduma;

(3) Kuwajengea uwezo watumishi katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza;

(4) Kuimarisha na kusimamia shughuli za utafiti; na

(5) Kuhamasisha wananchi kuhusu njia za kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.

Njia hizi ni pamoja na kufanya mazoezi, pamoja na kuzingatia kanuni bora za lishe.
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA aliuliza:-

Je, kuna mpango gani wa kusaidia upatikanaji wa Bima ya Afya kwa watoto wasio na wazazi ambao walikuwa wakilipiwa bima na wahisani?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdul-Hafar Idrissa Juma, Mbunge wa Mtoni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa mfumo wa kulipia watoto kupitia Toto Afya Kadi umebadilika na kwa sasa unafanyika kupitia utaratibu wa shule na vifurushi vya bima ya afya vya najali, wekeza na Timiza.

Mheshimiwa Spika, suluhisho la kudumu la tatizo hili, ni kukamilika kwa Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambao tunaamini utawezesha watoto wengi zaidi wasio na changamoto ya kiafya na wenye changamoto za kiafya kulipiwa Toto Afya Kadi. Hatua hii itasababisha kuwepo kwa uhai na uendelevu wa Mfuko wa Bima ya Afya, naomba kuwasilisha.
MHE. ABDUL-HAFAR IDRISSA JUMA aliuliza: -

Je, ni lini majimbo ya Zanzibar yatapata fedha za Mfuko wa Jimbo kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdul-Hafar Idrissa Juma, Mbunge wa Mtoni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, fedha za Mfuko wa Jimbo kwenda Majimbo ya Zanzibar hupelekwa kwa wakati na kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za fedha, ambapo fedha hizo huamishwa moja kwa moja kutoka Wizara ya Fedha na Mipango ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Aidha, katika mwaka 2021/2022 fedha za mfuko kiasi cha Shilingi Bilioni 1.4 zimeshatolewa kwa ajili ya Majimbo ya Zanzibar. Ahsante.