Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Boniphace Nyangindu Butondo (5 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. BONIFACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru sana kwa kunipa fursa hii. Kwa mara ya kwanza nasimama katika Bunge lako Tukufu, naomba nimpongeze Mheshimiwa Spika na wewe Naibu Spika kwa kuchaguliwa kuwa viongozi wetu katika Bunge hili Tukufu. Pia nitumie fursa hii kukishukuru Chama changu Chama Cha Mapinduzi kwa kuniteua na kupeperusha bendera ya Chama changu Cha Mapinduzi na hatimaye kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Kishapu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuwashukuru pia wananchi wa Jimbo la Kishapu kwa namna ambavyo wamenipa kura nyingi za kishindo kwa asilimia 87.4. Vile vile niwashukuru sana Wanakishapu kwa ujumla, lakini niishukuru familia yangu, kwa namna ya pekee nimshukuru mke wangu, lakini niishukuru na familia yangu kwa ujumla kwa namna ambavyo wamenipa ushirikiano kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunapata kura za ushindi na hatimaye kufika katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe mchango katika Mpango huu wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka mmoja na miaka mitano. Kwanza nianze kwa kuishukuru sana Serikali yangu kwa jitihada kubwa ambayo imekuwa ikifanya. Sote tuna macho ya kawaida na hatuna macho yenye miwani ya mbao, kwa sababu yako mambo mengi ambayo dhahiri na wazi yamekuwa yakionekana ni mafanikio makubwa kwa Serikali yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Elimu; sote tunafahamu elimu ya sekondari kwamba sasa hivi tuna sekondari katika kila kata na baadhi ya kata zingine tumeanza kuongeza sekondari. Pia shule zetu za msingi zimeboreshwa, ukilinganisha na hali halisi ya kipindi cha nyuma. Yapo mambo mengi vile vile kama vile ujenzi wa Standard Gauge, ambao sasa hivi unaendelea kwa kasi kubwa; uboreshaji wa huduma ya Shirika la Ndege. Shirika hili lilikuwa limekufa na sasa hivi maendeleo ni makubwa, sote tunanufaika na huduma hii ya usafiri wa anga; kuna mradi huu mkubwa wa ufuaji wa umeme wa Mwalimu Nyerere, ni hatua kubwa ambayo Serikali yetu imewekeza na kufanya mradi huu unakwenda vizuri; na suala zima la uanzishwaji wa viwanda vikubwa, viwanda vya kati na viwanda vidogo. Hii ni hatua kubwa ambayo ni dalili tosha kwamba hatua ya kimaendeleo katika nchi yetu tunakwenda vizuri..

Mheshimiwa Mwenyekiti, haitoshi kwa sababu sisi siyo wananchi isipokuwa ni taasisi za kifedha za kimataifa ndizo zilizofikia hatua ya kuiona Tanzania inastahili kuingia katika uchumi wa kati. Kwa hiyo tupo assessed kwa utaratibu wa kitaaluma kabisa kabisa na ndiyo maana tumefika mahali tumeingia katika uchumi wa kati.

Kwa hiyo ni jukumu letu Watanzania kuweka mbele uzalendo ili mradi tuhakikishe uchumi wa kati lakini katika kipato cha juu, sisi wenyewe Watanzania kama wazalendo tuhakikishe kwamba tunapambana na tunakuwa wamoja kuhakikisha kwamba maendeleo ya uchumi wetu yanapaa inavyotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie tu mafanikio haya yanaonekana kwenye Jimbo langu la Kishapu, huwezi ukaamini kwa miaka nane ya nyuma na huko nyuma zaidi coverage ya maji ilikuwa chini ya 20%, lakini leo tunavyozungumza nina Mradi mkubwa wa Maji ya Ziwa Victoria ambao kwasasa hivi coverage ya maji pale iko kwenye asilimia 50. Miradi inayotekelezwa baada ya miezi kama minane nina uhakika nitaweza kufikia coverage ya 70%. Hii ni hatua kubwa sana,

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara zinazojengwa kwa kasi kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza haya nataka niseme kwamba, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa sababu ameendelea kutujalia afya. Pia naomba niendelee kukushukuru wewe sana kwa sababu nimepata nafasi ya kuchangia jioni hii katika bajeti hii muhimu ya Wizara ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu hasa nitajielekeza katika eneo la TARURA pamoja na elimu na kidogo nitagusia upande wa afya. Kwanza, naungana mkono kabisa na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba ipo haja ya kuitizama TARURA kwa macho mawili na hasa katika eneo zima hili la kuongeza hii percentage ya kiasi ambacho TARURA wamekuwa wakipewa fedha kwa ajili ya kushughulikia barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo kubwa lenye mtandao mkubwa unaohitaji kutengenezwa ama kulipa kipaumbele ni eneo la barabara zilizopo vijijini. Eneo la Kishapu tuna jumla ya kilometa 1,030 ambazo zinahitaji kutengenezwa lakini zikiwa katika mazingira magumu kweli kweli. Yapo maeneo mengine yapo katika mbuga hasa lakini vile ni vijiji na kuna maeneo ya kiutawala ya kata.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa vyovyote vile huduma ya barabara ni ya msingi sana kwa sababu bila huduma ya barabara huduma hizi zingine; kwa mfano huduma ya afya wananchi hawawezi wakayafikia maeneo kwa ajili ya kwenda kupata huduma iwe katika health centre au dispensaries lakini hata katika sekta ya elimu kuna wakati watoto wanashindwa kufika maeneo ya shule kutokana na matatizo ya maji na hasa panapokuwepo na matatizo ya vivuko kadhaa kuharibika Zaidi, kwa hiyo, lipo tatizo kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia usafirishaji wa mazao kila mmoja hapa anafahamu Mkoa wa Shinyanga ni Mkoa ambao unalima sana pamba. Tunapozungumza zao la pamba ni Wilaya ya Kishapu ndiyo inayoongoza kwa kulima pamba. Tafsiri yake Wilaya ya Kishapu ni moja kati ya wilaya na inawezekana ikawa ya kwanza ama ya pili nchini kwa uzalishaji wa pamba. Sifa ya zao la pamba katika kuchangia uchumi wa nchi hii unaweza ukawaona hawa wana Kishapu ndiyo wanaongoza kwa adha ya barabara, hapa hakuna haki kabisa. Nataka niishauri sana Serikali na hasa Wizara yetu ione umuhimu wa Wilaya ya Kishapu kuhakikisha kwamba barababara zinatengenezwa na inaongezewa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu niyataje baadhi ya maeneo ambayo yana hali mbaya kabisa, zikianza tu kunyesha mvua safari za kuelekea Kata za Itilima, Kiloleli, Mwaweja na Mwamalasa inakuwa ni shida, hizi ni kata ambazo hazipitiki kabisa. Hili ni tatizo ambalo kwa kweli tusipoliangalia tunaweza tukawakatisha tamaa sana wananchi. Zipo Kata za Uchunga, Mwataga na Somagegi, hizi ni kata ambazo na zenyewe zinakuwa kisiwani pale mvua zinapoanza kunyesha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna haja ya Serikali kulitazama eneo hili na kuona haja ya kupeleka fedha za kutosha. Wenzangu wameshauri sana katika masuala ya simu, hili jambo tunaweza tukaliangalia na Serikali ifike mahala iwe serious, tuwahurumie wananchi. Bunge limekuwa likitoa mawazo hata katika eneo la mafuta, kwa nini tusifike mahali tukajifunga mkanda lakini lengo tuwafungulie njia wananchi? Nasema hivi kwa sababu Watanzania kwa ujumla wanahangaika na masuala ya barabara. Kwa hiyo, mimi naamini kwa sababu Serikali ya CCM ni sikivu kupitia mMwaziri wetu na hususani Mheshimiwa Ummy Mwalimu pamoja na wasaidizi wake ndugu yangu Mheshimiwa Silinde na Mheshimiwa Dkt. Dugange mfanye hili jambo ili mradi tuwapunguzie adha wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepata habari kwamba kuna kama shilingi bilioni 100 zimeongezeka kidogo na wengine wameshaanza kupata taarifa, zimeshaanza kutumwatumwa kule, mimi naomba Kishapu tuikumbuke. Tuikumbuke Kishapu kwa jicho la huruma kwa sababu wananchi hawa wanateseka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nataka nizungumzie ahadi za viongozi wetu wakuu. Kipindi cha Uchaguzi aliyekuwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli alifika Kishapu na bahati nzuri aliweza kuahidi kilometa nne. Ahadi hii alikuja kusisitiza kwa sababu alishaiahidi awamu ile ya kwanza, maana yake miaka mitano barabara hiyo ilikuwa haijatekelezwa lakini imeanza kutekelezwa kwa mwaka fedha uliopita.

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi kilometa nne tumepata jumla ya shilingi milioni kama 114, shilingi milioni karibu 380 zilikuwa hazijafika. Naomba sana fedha hizi ziweze kufika na kusaidia wananchi hawa ili mradi Mji wa Kishapu na wenyewe uweze kufanana. Kwa sasa hivi kazi iliyopo kwenye ile kilometa moja kuna asilimia kama 94, lakini nachoomba Wizara iweke msukumo na kuhakikisha fedha zile zinafika Kishapu na kuhakikisha kwamba mradi huo tunaukamilisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna upungufu wa walimu 1,611 katika shule za msingi, hapa kuna tatizo kubwa sana. Kwenye nyumba za walimu na penyewe pana shida kubwa. Kuna tatizo kubwa sana upande wa madarasa, wananchi wamejitahidi sana kutoa nguvu zao kuhakikisha kwamba wanasukuma mbele na kutoa mchango upande wa madarasa. Hata hivyo, kuna haja Serikali kuweka mpango maalum kuhakikisha kwamba ina-support nguvu za wananchi, yako magofu mengi ambayo yanahitaji support na hii ni katika shule za msingi na sekondari. Naomba sana Wizara hii iweze kutazama maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna Kata mpya za Shagihilu, Mwaweja, Bupigi, Mwasubi, Mwadui, Luhumbo na Mwamala tumeshaanzisha sekondari mpya na bahati nzuri Serikali imekuja na mpango wa kuhakikisha inapeleka fedha kwa ajili ya sekondari hizi. Naomba sana Wilaya ya Kishapu ipewe kipaumbele na wananchi hawa tusiwakatishe tamaa tuhakikishe tunawapelekea fedha kwa ajili ya kuhakikisha maeneo haya yanafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni upande wa Waheshimiwa Madiwani na nataka nizungumzie maslahi yao. Nimekuwa Diwani kwa zaidi ya miaka 20 na nimekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa zaidi miaka 10. Nataka nizungumze Madiwani wana shida kubwa sana na kusema ukweli hawa Madiwani ndiyo wanaosimamia shughuli za maendeleo, ndiyo wanahamasisha shughuli za maendeleo. Hawa Madiwani ndiyo wanaotoka jasho kwa ajili yetu sisi Wabunge ili mradi tupate ushindi pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuna kila sababu Mheshimiwa Ummy, Mheshimiwa Silinde, Mheshimiwa Dkt. Dugange oneni huruma kwa hawa viongozi wenzetu waongezeeni posho, laki tatu na siyo hela. Jamani tuangalieni majukumu waliyonayo na wananchi wanaowahudumia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine hawa watu posho zao za vikao ni matatizo makubwa sana, ipo shida kubwa. Pengine na mimi nilikuwa naungana mkono tuhamishe posho hizi za madaraka ziwe zinalipwa na Serikali Kuu tubaki na hizi posho za vikao kwa sababu mzigo kwa baadhi ya Halmashauri unakuwa ni mkubwa na Halmashauri zinashindwa kulipa. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi iliniweze kuchangia katika Wizara hii muhimu inayoshughulikia masuala ya miundombinu na hasa barabara zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naomba niwapongeze Mawaziri; kwa maana ya Waziri pamoja na Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote katika Wizara hii. Kazi wanayoifanya ni kubwa lakini kusema kweli changamoto bado ni nyingi. Tunahitaji kuongeza nguvu zaidi kuhakikisha kwamba barabara zinapitika kwa sababu msingi wa uchumi wetu unahitaji sana kuimairisha miundombinu na hasa barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kama Tanzania hii tumeamua kusimama na kuamua Tanzania yetu iwe ni Tanzania ya viwanda. Viwanda hivi bila kuwa na barabara nzuri, uhakika wa viwanda vyetu kuzalisha na kuwa na ufanisi bado utaendelea kuwa ni hadithi. Pia tunafahamu kwamba bila barabara nchi yetu inategemea kilimo na kilimo ndiyo uti wa mgongo, wakulima wetu wataendelea kupata shida ya kusafirisha mazao na hivyo na wao wataendelea kutokupata tija katika shughuli yao ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla shughuli zote za kijamii, ziwe huduma za afya na maeneo mengine kama hatujajipanga vizuri katika eneo hili la miundombinu bado Tanzania tutaendelea kusuakusua kwenda mbele katika shughuli za kimaendeleo. Kwa hiyo eneo hili ni eneo muhimu sana, hivyo Serikali nchi nzima bila kujali eneo fulani ama maeneo ya mijini, iwe vijijini ni lazima igawanye sawa hii keki kama Waheshimiwa Wabunge wenzangu ambavyo wamechangia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka nizungumzie katika bajeti ya hii ambayo tunaijadili, kusema ukweli katika eneo langu na hasa Kishapu unaweza ukaona ni kana kwamba hakuna barabara yoyote mpya ambayo imeweza kuwekewa fedha hapa. Kuna barabara ambayo hapa imeainishwa ni Barabara ya Kolandoto yenye urefu wa kilometa 62.4. Barabara hii ya kutoka Kolandoto ambayo inakwenda mpaka Mwanuzi hizi kilometa 62 sote ni mashahidi ni kilometa nyingi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza ukaona labda ni fedha ambazo zimewekwa kwa ajili ya kushika kifungu ni bilioni mbili, bilioni mbili hizi zinakwenda kutengeneza kilometa ngapi? Ni mambo ambayo unaweza ukashangaa. Barabara hii ni barabara ambayo imekuwepo hata katika Ilani ya mwaka 2015 - 2020, lakini barabara hii haikuweza kutengewa fedha, lakini katika kipindi hiki imetengewa peke yake, jumla ya shilingi bilioni mbili peke yake. Fedha hizi ni kwa ajili ya kufanya nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine wananchi wetu wanaweza kufika mahali wakasema hii ni habari ya utani. Walikuwa wanataka majibu sawasawa katika hatua ile ya majumuisho ya mwisho ya Mheshimiwa Waziri kwamba nini mpango wa Serikali kwa sababu fedha hizi ni fedha za ndani lakini kama pengine kuna mikakati ya kupata fedha za nje nataka nipate majibu sawasawa na vinginevyo naweza nikaona kwamba wananchi wetu wanaendelea kuvunjika imani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais, aliyekuwa Rais wetu Marehemu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alisema kwamba barabara hii ni lazima tuitekeleze na akawakumbusha wananchi tuliweka kwenye mpango katika kipindi kilichopita hatukutekeleza tunawahakikishieni tunakwenda kuitekeleza. Kwa hiyo hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, lakini kwa sababu imo kwenye Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi ni lazima tujipange tuhakikishe kwamba barabara hii tunaitekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza ukaona katika barabara nyingine ya Mwigumbi kwenda Maswa, hii ni barabara ya lami ambayo ipo tayari. Kitu ambacho kinasikitisha pengine labda nipate majibu katika, ukiangalia kwenye bajeti hii barabara hii imetengewa bilioni 50.3, sasa bilioni 50.3 hizi sijajua ni kwa ajili ya nini kwa sababu barabara hii ilishakamilika na kuna maeneo ambayo yalikuwa mabovu yalishafanyiwa matengenezo. Kwa nini fedha hizi zisingepelekwa kwenye barabara hii ya kutoka Kolandoto kwenda Mwanuzi kuja Kishapu. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, sasa haya ni mambo ambayo pengine nataka nijue hizi bilioni 50 ni kwa ajili ya kufanya nini? Kwa sababu tunaendelea kutoa pesa nyingi tunazipeleka kwenye barabara ambayo tayari ilishatengenezwa. Wakati mwingine inaweza ikaleta tafsiri ni mianya rahisi ya kuweza kutumia fedha bila kuwa na maswali mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilitaka nataka nizungumze hili, nipate majibu mazuri kwamba hii bilioni 50 kwa barabara hii ya Mwigumbi kwenda Maswa ni kwa ajili ya nini wakati barabara hii imekamilika. Juzi ilipata matatizo ikafanyiwa maintenance, lakini bado imewekewa fedha nyingi huku barabara ya Kolandoto kwenda Kishapu imewekewa bilioni mbili, nataka tafsiri na maelezo kuhusiana na hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka nizungumzie ni suala zima la uwanja wa ndege wa Shinyanga. Mkoa wa Shinyanga tuna shughuli za madini pale Mwadui, lakini tuna wachimbaji wadogo katika Mji wetu wa Maganzo pamoja na eneo lingine, eneo lote linalozunguka maeneo ya Maganzo na wananchi wanazo fedha, lakini Shinyanga tunalima pamba, habari ya fedha kwetu siyo tatizo. Kwa hiyo, habari ya usafiri wa ndege wala hata sisi kwetu siyo habari mpya kwa sababu ni watu ambao tunazo fedha bwana. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Uwanja wa Ndege wa Shinyanga imekuwa ni hadithi, hadithi. Kila mwaka kipindi kilichopita ilikuwemo kwenye Ilani, ilikuwemo sijui kwenye bajeti mbalimbali, uwanja wa Shinyanga unaenda kukarabatiwa, kila mwaka ni habari ya hadithi hizi. Jamani katika Wizara hii kuna matatizo gani? Uwanja huu mimi niwaambieni hata kipindi kile ambacho kiwanja hiki kilikuwa kinafanya kazi, kati ya viwanja ambavyo vilikuwa na abiria wengi sana kipindi cha nyuma, kimojawapo ni Kiwanja cha Shinyanga. Sasa sijajua kama wanapiga hesabu ama tunaendelea kujenga viwanja vingine tu bila kuangalia uhalisia na historia ya viwanja vipi ambavyo vinakuwa na wateja wengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nipate majibu mazuri kwamba kiwanja hiki kinakwenda kutengenezwa kweli? Unaweza ukaangalia fedha zilizowekwa peke yake ni bilioni 3.6, naziona ni fedha kidogo na kiwanja kile tumekiacha kwa muda mrefu, kilikuwa na uharibu mdogo, lakini viwanja vya aina hii vimeendelea kuharibika, kwa rafiki yangu kule Mhata kule…

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Butondo kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe taarifa Mheshimiwa mzungumzaji kwamba ni kweli kabisa nakubaliana naye kwamba Serikali haiangalii viwanja ambavyo vina; mosi, vinakuwa vina historia lakini pia vinaweza kuchangia pato kubwa kwenye uchumi wa Taifa, mfano uwanja wa ndege wa Musoma ambapo anatoka Baba wa Taifa, tuna madini kule, tuna ziwa, tuna Mbuga za Wanyama na vitega uchumi kibao lakini mpaka sasa hivi unasua sua tu, nilikuwa naomba nikupe hiyo taarifa Mheshimiwa. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Butondo unapokea taarifa hiyo.

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli kwa sababu hoja ya Mheshimiwa Matiko ni ya maslahi mapana kabisa ya Taifa letu nimeipokea taarifa yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nataka nizungumzie kwa Mheshimiwa Mhata, Kiwanja kile cha Masasi ni aibu, ni moja kati ya maeneo ambayo nilitaka nizungumze kwa uwazi. Kiwanja kile kilifikia hatua mbaya, hata kile kipindi tunakwenda kumhifadhi cha mzee wetu, ilifanyika kazi ya kuchoma nyasi zile, ndiyo ile helikopta ikatua pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunavisahau viwanja vikongwe na viwanja ambavyo tumekuwa tukisema mwaka kila baada ya mwaka kwamba vitakwenda kukarabatiwa. Hii ndiyo habari ambayo wanazungumza wenzangu, Mheshimiwa Mwenisongole amezungumza kwamba keki hii


ni lazima tuigawanye katika usawa. Kwa hiyo nataka niiombe sana Wizara, tusije tukajenga tafsiri ya kwamba kwa kweli kuna baadhi ya maeneo watu wengine wanapendelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata katika hotuba hii maeneo mengine tusingependa kuyafungua na kuzungumza, baadhi ya maeneo yamepewa fedha tena fedha nyingi, lakini baadhi ya maeneo mengine hatuna fedha, pengine inaweza ikaleta tafsiri nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nataka hili nilizungumze naikumbusha Wizara kwamba iwe makini kuhakikisha kwamba maeneo yote hasa ya msingi yanatazamwa na fedha zinapelekwa kwa ajili ya kusaidia wananchi katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nataka nilizungumzie, ni kuhusiana na daraja. Lipo daraja moja ambalo limejengwa katika Jimbo langu la Kishapu. Daraja la Buzinza, Kishapu - Buzinza na daraja lile linaunganisha pia Wilaya ya Igunga. Daraja hili limejengwa kwa thamani ya shilingi bilioni 2.3, lakini tangu daraja hili litengenezwe leo ni zaidi ya miaka mitatu daraja hili limekamilika, lipo katika Mto Manonga, lakini baada ya kukamilika daraja hili halifanyi kazi kwa sababu nyakati za masika kushoto na kulia yaani unapokuwa unavuka na unapokuwa unavuka upande mwingine mto ule unatakiwa ujengelee sasa barabara. Kivuko cha kutoka huku na kivuko cha kutoka huku, kwa sababu ule ni mto.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni sawa na kwamba Serikali imekwenda kutupia zile fedha halafu barabara hiyo haina maana yoyote. Niombe sana Wilaya ya Igunga na Wilaya ya Kishapu iunganishwe kupitia daraja hili vinginevyo ni sawa na kwamba tumezimwaga zile fedha na hakuna maana yoyote ya kupeleka hizo fedha. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele ya pili imegonga.

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, ilikuwa ya kwanza.

NAIBU SPIKA: Imeshagonga ya pili, ahsante sana.

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia. Kwanza nami naomba nimshukuru sana na nimpongeze sana Mheshimiwa Biteko pamoja na Naibu Waziri wake kwa namna ambavyo wamekuwa wakisimamia vizuri sana sekta hii ya madini na Watanzania wote wanaona mafanikio na sote kwa ujumla tunanufaika kwa kuongeza pato la Taifa kwa asilimia zaidi ya tano kutokana na sekta hii ya madini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la kwanza nataka nizungumzie kuhusiana na suala la Mgodi wa Mwadui. Mgodi wetu wa Mwadui sote tunafahamu kwamba, Serikali ina asilimia 25 na mwekezaji asilimia 75, lakini Mgodi huu tangu tarehe 8/4/2020 umesimamisha uzalishaji, lakini suala hili limetokana na kwanza kulikuwepo na kuporomoka sana kwa bei ya Soko la Dunia la Almasi na sote tunafahamu soko lile la almasi liko Ubelgiji peke yake.

Mheshimiwa Spika, baada ya tatizo hilo, muda ule ule palitokea tatizo la Covid 19 na tangu kipindi kile mgodi wa Mwadui hadi sasa tunavyozungumza; tangu tarehe 8 ya mwezi wa Nne, mpaka sasa mgodi huu haufanyi kazi.

Mheshimiwa Spika, tunaweza tukajua pale katika eneo lile kuna watumishi zaidi ya 1,200, sasa Serikali inaweza ikaona tu kwamba kuna watumishi wengi sasa ambao wanapata shida na mahangaiko makubwa. Tatizo kubwa hili la kuteremka kwa bei ya almasi, bado ni changamoto hadi sasa, lakini angalau kuna improvement; na juzi waliamua kuanzisha uzalishaji, tatizo linalosumbua pale ni mtaji kwa ajili ya kuhakikisha mgodi ule sasa unaanza kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, ziko taratibu ambazo wameanzanazo ili mradi waanze ku-run huo mgodi na waanze kuzalisha, lakini tatizo kubwa ni mtaji wa kuanzia kwa sababu, zinatakiwa dola milioni 25 ambazo unaweza ukaona ni karibu shilingi trilioni tatu. Fedha hizi ni fedha nyingi. Kuna wakati wamezungumza na CRDB na NMB. CRDB walionesha mwelekeo wa kutaka kusaidia Mgodi wa Mwadui ili mradi uanze kuzalisha, lakini baadaye walirudi nyuma. Wameanza mazungumzo na NMB, lakini NMB mpaka sasa hivi hawaja-respond sawa sawa.

Mheshimiwa Spika, ombi langu ni Serikali kuweka mkono wake ili mradi waone kwamba mgodi huu unaanza kuzalisha. Faida kubwa ya mgodi huu iko kote kote; kwenye Halmashauri kuna Service Levy ambayo Halmashauri Halmashauri ya Kishapu itaweza kupata, lakini kuna CSR ambayo inaweza ikasaidia mambo mengi sana kusukuma mbele shughuli za maendeleo, lakini na Serikali inapata mapato makubwa kutokana na mgodi huu. Kwa hiyo, naiomba Serikali iweke jitihada za karibu sana, pengine wazungumze na waweke mkono wao ili CRDB ama NMB waweze kutoa fedha na mgodi huu uanze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kuna tatizo lingine katika mgodi huo. Kulikuwepo na suala zima la almasi ambazo ziliweza kukamatwa zilizokuwa na matatizo, Serikali imeshughulika na baadhi ya watumishi wetu walihusika katika kuhujumu. Tatizo hilo nadhani lilienda Mahakamani likazungumzwa likafikia hatua za mwisho.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naiomba Serikali iweze kutoa maamuzi, ikiwezekana kama sehemu hiyo ingefaa kurudishiwa sehemu ya zile mali Mgodi wa Mwadui waweze kurejeshewa, lakini hatua zile za kisheria kwa watumishi wetu ambao walikiuka ziweze kuchukuliwa, lakini mgodi uweze kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, kuna masuala yale ya VAT kabla ya sheria haijaweza kubadilishwa, Serikali iweze kuangalia. Kwa sababu, kuna VAT ambazo zilipaswa kurejeshwa katika mgodi huo, hizi nazo pamoja na mali zitakazorejeshwa zinaweza zikasaidia mgodi ukaweza kufanya kazi yake…. (Sauti ilikatika)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine nataka kuzungumzia suala la migogoro ya mipaka kati ya Nyenze na Ng’wang’holo. Kuna mwekezaji aitwae El-hilal ambaye eneo lile la Mwan’gholo na Nyenze kabla ya miaka miwili huko nyuma wananchi walikuwa wanalitumia kwa kilimo, kuchunga na mambo mengine, lakini juzi wachimbaji wadogo wakaja kuibua madini ya almasi, lakini huyu mwekezaji aliibuka na kusema eneo lile ana hati.

Mheshimiwa Spika, kipindi cha uchaguzi, aliyekuwa Rais wetu mpendwa Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli alielekeza jambo hili kwamba anakwenda kulishughulikia kwa sababu alitambua kwamba wananchi ndio waliogundua kule, lakini akaona ukubwa wa eneo hilo na akasema kwamba ipo haja ya wachimbaji wadogo kukatiwa sehemu ya eneo hilo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Boniphace!

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba Serikali iweze kuchukua uamuzi na kuweza kufidia ili mradi…

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: …wachimbaji wadogo waweze kupewa eneo hilo, lakini pia Wizara ya Ardhi waweze…

SPIKA: Mheshimiwa Butondo.

MHE. BONIPHACE N. BUTONDO: … katika eneo hilo… (Sauti ilikatika) (Kicheko/Makofi)

SPIKA: Ahsante sana. Wachimbaji wadogo leo wana watetezi kweli kweli.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. BONIFACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nami naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu kabisa ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Kalemani pamoja na Naibu Waziri wake, niwapongeze pia na watendaji wote katika Wizara hii. Sababu kubwa kwa nini nampongeza Mheshimiwa Kalemani ni kwa namna ambavyo amekuwa mfano wa kuigwa kwa Mawaziri na hasa katika jambo kubwa la kutusikiliza sisi lakini pia kufika kwa wakati katika majimbo yetu na kuona changamoto na matatizo yaliyopo katika maeneo yetu. Kweli wewe ni kiongozi wa kuigwa na Mawaziri wengine ningependa waige mfano na mwenendo wa Kalemani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kishapu ina jumla ya vijiji ya 127 lakini vijiji 75 vina umeme na vijiji 52 bado vina tatizo kubwa la umeme. Hivi navyozungumza kata tano hazina kabisa umeme kati ya kata 29 hata Kata nakotoka ya Lagana. Kata hizo ni Lagana, Bunambiu, Mwasubi, Itilima na Masanga, hizi kata hazina kabisa umeme hata katika kijiji kimoja. Kwa hiyo, hili bado ni tatizo kubwa sana katika eneo langu. Naomba sana Wizara katika hii REA III Awamu ya Pili vijiji hivi vyote viweze kupata umeme.

Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri mwaka 2017 aliweza kufika katika Jimbo la langu katika Kata za Ukenyenge, Mwamashele na bahati nzuri aliahidi kwamba maeneo hayo yatapatiwa umeme. Kata ya Mwamashele nguzo zimefika lakini mpaka sasa hatujapata umeme, kwa hiyo, bado wananchi wanasubiri umeme. Mimi ninahakika kwa jinsi ambavyo Waziri ameahidi atakwenda kutekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna changamoto kubwa ya kukatika umeme katika Mji wa Munze ambao ni Makao Makuu ya Wilaya yangu ya Kishapu, liko tatizo kubwa na kwa kweli jambo hili linasikitisha. Pengine wakati una-wind up naomba ueleze tatizo ni nini kwa sababu maelezo yako mengi. Kwa kutwa nzima umeme unapatikana kwa wastani wa asilimia 30 ama 40 asilimia 60 unakatika; kwa siku unaweza ukakatika mara tatu, mara nne ni tatizo kubwa sana. Tunaomba kujua tatizo ni ni linalosababisha kukatika kwa umeme katika maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka nizungumzie ni masuala mazima ya watumishi. Wilaya ya Kishapu tuna watumishi 12 peke yake na Mheshimiwa Waziri anafahamu watumishi katika sekta hii muhimu ni kubwa. Pale inapotokea emergency, kwanza katika emergency gang inatakiwa watumishi 12 waende haraka kwa ajili ya kutatua tatizo sasa unapokuwa na watumishi wilaya nzima 12 panapotokea emergency unafanya nini pia kuna maeneo yanayotakiwa kutolewa huduma za kila wakati, kwa hiyo, hili ni tatizo kubwa.

Mheshimiwa Spika, pia nizungumzie suala zima la wakandarasi. Nchi nzima wakandarasi wametolewa katika kila wilaya, Wilaya ya yangu ya Kishapu haijapata mkandarasi, hili ni tatizo sijajua sababu ni nini. Wakati Mheshimiwa Waziri ana-wind up aeleze nini tatizo. Nimeendelea kufuatilia mchana huu Mkoa mzima wa Shinyanga hatujapata wakandarasi. Kwa hiyo, hili bado ni tatizo na pengine nataka nipate majibu tatizo ni nini. Juzi Waziri alisema atakapowaita hao wakandarasi pamoja na mameneja wa TANESCO kutoka katika kila wilaya atawapa maelekezo wawasiliane na Waheshimiwa Wabunge ili waweze kuona maeneo gani ambayo yana changamoto na ya kufanyia kazi kwa haraka, kwa hiyo, kwangu hili ni tatizo kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumzie pale panapotokea matatizo ya moto. Mwezi Machi palitokea tatizo la kuungua nyumba tatu katika Kata ya Mwaweja Wilayani kwangu Kishapu kutokana na short za umeme. Tumepata tatizo kubwa sana kuzima moto katika nyumba zile lakini pia hata TANESCO wenyewe kuwahi kufika ilikuwa ni tatizo kubwa. Tatizo hili limechangiwa pakubwa sana kutokana na kutokuwa na magari na watumishi wa kutosha. Kwa hiyo, naomba sana mjaribu kuitizama Kishapu na watusaidie ili tuondokane na tatizo hilo.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)