Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Santiel Eric Kirumba (10 total)

MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Spika, je, Serikali ina mpango wowote wa kuzigawanya fedha hizi katika Halmashauri hususan zile Halmashauri ambazo makusanyo yake yamekuwa madogo katika asilimia 10 ambazo zinatengwa. Halmashauri hizo mfano ni Wilaya yetu ya Shinyanga Vijijini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa nini Serikali isiongeze zile asilimia kutoka asilimia 10 mpaka tano kwa wanawake kutokana na wanawake wamekuwa ni watu wazuri sana katika marejesho? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali inayo mpango wa kuweza kufanya mapitio na kuweza kuweka maboresho zaidi kwenye mifuko hii kwa sababu ni kweli kwamba kumekuwa na changamoto ya Halmashauri nyingine zenye kipato cha chini zile asilimia nne kwa wanawake, nne kwa vijana na mbili kwa watu wenye ulemavu kwenye maeneo mengine wanapata pungufu zaidi ya hapo. Kwa hiyo, hilo nalo ni jambo ambalo tumeshalichukua kama Ofisi ya Waziri Mkuu na limekwisha kuanza kufanyiwa vikao vya tathmini na kuweza kuangalia namna gani tutaweza kuboresha ikiwa ni sambamba na ule mjumuisho wa mifuko hii inayoshabihiana.

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo lingine tumeona kwamba mikopo inayotolewa kwenye Halmashauri tunajaribu kuangalia zaidi tija, vikundi vimekuwa vikijiunga kwa ajili ya lengo la kupata mikopo ile, lakini baada ya hapo vinasambaratika na hawaendi kufikia azma ya kukopea mikopo hiyo na mpaka sasa tukisema katika mifuko tu ya fedha za Halmashauri ni mabilioni mengi ambayo bado hayajaweza kufanyiwa marejesho. Na kwa Ofisi ya Waziri Mkuu peke yake tuliwahi kutoa shilingi bilioni 4.9 lakini katika fedha hizo, ni shilingi milioni 700 tu ambazo ziliweza kurudishwa, zaidi ya shilingi bilioni nne bado hazijaweza kurejeshwa.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili Mheshimiwa Santiel Kirumba, Mbunge wa Viti Maalum kwamba kuona ongezeko la asilimia; hili ni eneo pia nalo ambalo tumekuwa tukilifanyia kazi kuweza kuona namna gani tunaweza tukaboresha Zaidi hasa kwa wale waliokuwa waaminifu katika kukopa kwa sababu lengo la Serikali na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ni kuwawezesha wananchi hawa kiuchumi wanapokopa hizi fedha waweze kuzirudisha ili watu wengine waweze kufanyia biashara zaidi. Na tunategemea waweze ku-graduate kwenye hilo eneo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa kweli tunalifanyia kazi na tunatarajia hivi karibuni hasa kwenye mwaka huu wa fedha, fedha hizi zinazotolewa tuone ile tija na hasa twende hata kwenye kukopesha vifaa kuliko fedha ambapo mara nyingi zimekuwa zinatumika vibaya. Nakushukuru.
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri kwenye Serikali yetu. Je, ni lini bandari hii itaanza kufanya kazi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo ameanza kufuatilia tangu nilipoteuliwa tu, alikuja ofisini kwangu kufuatilia suala la Bandari hii ya Isaka iliyopo Mkoani Shinyanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, anauliza ni lini itaanza hasa. Changamoto kubwa ilikuwa ni kwamba bandari hii ilikuwa haina vitendea kazi. Ilikuwa haina mabehewa, hatuna injini na sasa tumekwishanunua. Nimefanya mkutano jana na Watendaji Wakuu wa Mamlaka ya Bandari pamoja na TRC na nimewaagiza ya kwamba ndani ya wiki hii wanipe ripoti, wafanyabiashara wote ambao wanatumia Bandari ya Dar es Salaam na wanatoka Nchi za Congo, Rwanda na Burundi wakae nao ili waone umuhimu sasa wa kutumia Bandari hii ya Isaka badala ya kuchukulia mizigo yao Dar es Salaam kama ilivyokuwa zamani. (Makofi)
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali; nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na watoto wengi wa kike kukosa masomo siku tano mpaka saba kwa hiyo kunasababisha kwa mwaka kukosa masomo kwa siku 50. Nini commitment ya Serikali katika madarasa haya mengi mapya ambayo hayana mfumo huu wa vyumba maalum?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Santiel Erick Kirumba, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ameianisha hiyo changamoto, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi Ofisi ya Rais – TAMISEMI tunazielekeza halmashauri zote sasa kujenga vyumba ambavyo vinaweza vikawasaidia watoto wa kike kujistiri wakati wa hedhi. Lengo ni kuhakikisha kwamba Watoto hawa hawakosi masomo wanapokuwa katika kipindi chao ili kuweza kuwasaidia kama ambavyo katika michoro yetu mipya ambayo tumeianisha.
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali. Nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Barabara hii imekuwa ikiahidiwa na viongozi wengi wakubwa wa Serikali tangu mwaka 2010 na haijatekelezwa mpaka sasa kwa kilometa hizo 148 kwa kiwango cha lami. Nini kauli ya Serikali kuikamilisha barabara hii kwa sababu imekuwa kero kwa watumiaji wake?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; ni lini pia Serikali itaanza ujenzi kwa kiwango cha lami kutoka Kahama – Nyandekwa – Nyamilangano (kilometa 148)? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Santiel Kirumba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Mwanangwa – Mwakitolyo
– Bulige hadi Kahama ni kweli imekuwa ikiahidiwa na ndiyo maana tumeanza kuijenga kwa hatua na hasa maeneo ambayo tunajua ni ya mjini wakati Serikali ikiendelea kutafuta fedha kuijenga barabara yote kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nia ya Serikali ipo na ndiyo maana tumefanya usanifu barabara yote na tumeanza kujenga maeneo yale muhimu kwa hatua tukitafuta fedha yote.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa barabara aliyotaja ya pili kutoka Nyandekwa – Wogo, barabara hii ipo kwenye mpango na tumeipangia fedha kwenye mwaka huu wa fedha ikiwa ni maandalizi kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Spika, huduma hii tangu izinduliwe ni mwaka mmoja sasa na Mheshimiwa Rais alishatoa maelekezo kampuni nyingine kuweza kujiunga kutoa huduma hii ya usafiri wa dharura kwa mama mjamzito na watoto.

Nini kauli ya Serikali kukamilisha mchakato huu kwa haraka? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kutokana na huduma hii kupatikana hasa maeneo ya mjini; je, Serikali imejipangaje kutoa elimu na matangazo ya kutosha kwa maeneo ya vijijini kuhusu huduma hii ya bure ya usafiri wa dharura wa mama mjamzito na mtoto? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Santiel, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba huduma hii toka imezinduliwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni karibia mwaka sasa, na maagizo yake yalikuwa mawili; moja, kuhakikisha tunapeleka nchi nzima. Hivi tunavyoongea, tumeshapeleka nchi nzima kasoro mikoa mitatu na kufikia tarehe 22/9/2023 tutakuwa tumewasha nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, la pili, lilikuwa hili la kutoa wito kwa wadau wengine kuendelea kuungana na Serikali katika kuhakikisha mfumo huu unafanya kazi. Wadau wameendelea na mazungumzo na Serikali lakini waliopo wameendelea kuongeza fedha na ndiyo ambayo imetupa uwezo wa kuendelea kusambaza huduma hii maeneo mengine ya nchi.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni kweli kwamba huduma hii ni ngeni kwa baadhi ya maeneo na kwa hiyo, kutambulika kwake hakuwezi kwenda kwa mara moja. Tunachokifanya, kila tukipeleka mahali, tunaanza kutoa elimu kwa watendaji na hasa wale wa huduma za afya.

Mheshimiwa Spika, huduma hii inasimamiwa kwa pamoja kati yetu Wizara ya Habari kama watoa teknolojia lakini Wizara ya Afya na TAMISEMI ambao kwa kweli wanafanya kazi nzuri, na idadi inaendelea kuongezeka siku hadi siku. Tunaamini tukishirikiana na Waheshimiwa Wabunge na hasa Wabunge wa Viti Maalum kupeleka hii elimu kwenye maeneo yetu ili akina mama watumie huduma hii kuokoa maisha ya mama na mtoto, itasaidia uelewa lakini pia itaongeza watumiaji wa huduma hii. (Makofi)
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali. Nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Je, kutokana na viwanja vingi vya Serikali kujengwa na makampuni ya nje. Nini kauli ya Serikali kuwajengea uwezo makampuni ya ndani ili yaweze kujenga viwanja hivi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kutokana na mkataba huu kusainiwa tangu umesainiwa ni miaka Mitano. Nini kauli ya Serikali itawalipa fidia lini hawa wananchi wa Shinyanga kwa sababu tangu mwaka 2017 mpaka sasa 2022 miaka mitano imepita, itawalipa fidia ya mwaka 2017 au mwaka 2022, kutokana na bidhaa nyingi kupanda?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Santiel Eric Kirumba, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Shinyanga, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mbunge Santiel kwa jinsi anavyofuatilia ujenzi wa uwanja huu. Suala la Wakandarasi wa ndani. Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imekuwa mara kwa mara ikihimiza na ikiwajengea uwezo Wakandarasi wote wa Tanzania ili waweze kufanya miradi mikubwa. Hii siyo tu kwa viwanja vya ndege ni pamoja na miundombinu mingine ikiwemo majengo makubwa na hata barabara. Kwa hiyo, kinachofanyika kwanza ni kuwapa elimu ya kuwaunganisha pamoja ili waweze kuwa na mitaji mikubwa pia kuwawezesha ili waweze kupata mikopo kwa taasisi mbalimbali za fedha ikiwemo mabenki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ipo inafanya kazi hiyo na tunaamini kwa kuwawezesha Wakandarasi wa ndani maana yake fedha yetu nyingi itaendelea kubaki na kukuza uchumi pia kuwezesha uwezo wa hawa Makandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusu fidia. Serikali ilikwishawalipa fidia wananchi ambao wamepisha ujenzi. Kwa mujibu wa sheria zetu tunapolipa fidia tunaondoa kitu kinachoitwa uchakavu na hasa uchakavu wa majengo. Masharti ya wenzetu hawa ambao wanatoa fedha wana sharti moja kwamba ni lazima fedha ya uchakavu pia ilipwe. Kwa hiyo, Serikali imeshafanya tathmini ya uchakavu wa yale majengo na tayari yameshawasilishwa Wizara ya Fedha ili wakalipwe zile fidia za nyongeza kwa uchakavu wa yale majengo. Kwa hiyo, tayari tuko kwenye process na hawa watu wataongezwa fidia kwa maana ya ile ambayo sheria yetu ilikuwa inasema tusiwalipe lakini wanaotufadhili wanatuambia ni lazima pia walipwe. Kwa hiyo wananchi hawa watapata nyongeza ya fidia tofauti na waliyopata ile ya awali. Ahsante. (Makofi)
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Je, Mheshimiwa Waziri uko tayari kuambatana na mimi ili ukaweze kunidhibitishia mradi huu utakamilika mwaka huu wa fedha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili kutokana na changamoto nyingi wanawake wanazozipitia kipindi wanachokuwa wajawazito; Je, Serikali haioni haja kushusha huduma hii Wilayani ili tuweze kupata huduma hii kwa Mkoa wa Shinyanga kwa Watoto Njiti? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Santiel Erick Kirumba Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, moja niko tayari kuandamana naye kwenda Shinyanga na nitafurahi tukiwa wawili tu peke yetu. Ahsante. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni kwamba Je, Serikali haioni kuna umuhimu wa kupeleka kwenye hospitali za Wilaya huduma hizi. Kwenye bajeti yetu Mheshimiwa Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alisema kwamba, kwa mwaka huu unaokuja wa fedha tunaenda kujenga sehemu za Watoto Njiti 100 na siyo tu kwenye hospitali za Wilaya na kwenye Vituo vya Afya. Kwa hiyo, fedha zimeshapatikana sasa imebaki kuwasiliana na Waziri wa TAMISEMI ili kupanga sehemu za vipaumbele vya kuanza na kwa jiografia ya Mkoa wa Shinyanga ni mojawapo ya maeneo yataenda kufaidika na huu ujenzi. Ahsante sana.
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Je, Mheshimiwa Waziri uko tayari kuambatana na mimi ili ukaweze kunidhibitishia mradi huu utakamilika mwaka huu wa fedha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili kutokana na changamoto nyingi wanawake wanazozipitia kipindi wanachokuwa wajawazito; Je, Serikali haioni haja kushusha huduma hii Wilayani ili tuweze kupata huduma hii kwa Mkoa wa Shinyanga kwa Watoto Njiti? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Santiel Erick Kirumba Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja niko tayari kuandamana naye kwenda Shinyanga na nitafurahi tukiwa wawili tu peke yetu. Ahsante. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni kwamba Je, Serikali haioni kuna umuhimu wa kupeleka kwenye hospitali za Wilaya huduma hizi. Kwenye bajeti yetu Mheshimiwa Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alisema kwamba, kwa mwaka huu unaokuja wa fedha tunaenda kujenga sehemu za Watoto Njiti 100 na siyo tu kwenye hospitali za Wilaya na kwenye Vituo vya Afya. Kwa hiyo, fedha zimeshapatikana sasa imebaki kuwasiliana na Waziri wa TAMISEMI ili kupanga sehemu za vipaumbele vya kuanza na kwa jiografia ya Mkoa wa Shinyanga ni mojawapo ya maeneo yataenda kufaidika na huu ujenzi. Ahsante sana.
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kutokana na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, amesema inategemea na busara; je, haoni kwamba Serikali inahitajika kuweka mkazo kwenye suala hili, kwa sababu siku 90 zile mama hazimtoshi kwa kipindi kile anapomlea mtoto njiti? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Je, Serikali pia haioni haja ya kuweka mkazo kwa wanaume pia kuwasaidia wanawake kwa kuwaongezea likizo ya uzazi wanaume wanaopata watoto njiti? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza kuhusu kuweka utaratibu, nataka nilihakikishie Bunge lako kwamba maelekezo ya Bunge lako yalishatoka, lakini pia ni nia ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye alituelekeza sisi aliotupa dhamana ya kusimamia Ofisi ya Rais, Utumishi, kuyaangalia mazingira yote yatakayomwezesha mtumishi wa Umma kufanya kazi yake akiwa yupo na furaha ya kutimiza hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufanya hivyo, Serikali imeandaa mwongozo wa ujumuishwaji wa jinsia katika Utumishi wa Umma mwaka 2023 ambao pamoja na masuala mengineyo tunazungumzia jambo la kutoa likizo kwa wazazi wanaopata watoto njiti likiwemo pia jambo hili la kuingiza wanaume katika sehemu ya watu watakaochukua likizo katika kipindi hicho cha kusaidiana kulea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo Serikali italeta mwongozo huu mbele ya Bunge lako, tutajadili kwa pamoja na tukubaliane kimsingi ni njia gani nzuri au ni kipindi gani kizuri cha kuwawekea wazazi hawa ili tuweze kufikia ulezi ulio bora usiochosha kwa mzazi mmoja au kwa mzazi mwingine, ahsante. (Makofi)
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali, licha ya hivyo nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; mradi huu umekuwa ukikabiliwa na changamoto ndogo ndogo ambazo ni ukosefu wa miundombinu, maji safi na salama, ongezeko la shule mpya nyingi ambazo haziko kwenye mradi, zimepelekea watoto wetu wanapokuwa shuleni kukosa chakula.

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Wadau hawa wa Sekta ya Elimu wameelekeza watoto wanapokuwa shuleni wafundishwe namna bora ya kupanda mbogamboga na kupanda matunda ili yaweze kuwasaidia kupata mlo bora ambao utawatoa wasiweze kushindwa kupata udumavu, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Santiel Kirumba; la kwanza, hili la ukosefu wa miundombinu mbalimbali hasa katika shule mpya ambazo zimejengwa hivi karibuni miundombinu kama maji na kadhalika. Tunashirikiana na Wizara ya Maji, Wizara ya Nishati na kadhalika katika kuhakikisha miundombinu muhimu inafika katika Taasisi zetu za Serikali kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo shule na tutaendelea kufanya hivyo ili kuhakikisha huduma bora inatolewa katika shule zetu zote hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili; Kuna club mbalimbali katika shule zetu katika kuhakikisha kwamba upandaji wa mbogamboga unafanyika na kuendelea kufundishwa kwa wanafunzi wetu katika shule zile na Serikali itaendelea kutilia mkazo uwepo wa club hizi. Hivyo basi, nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kuwaelekeza ma-REO wote na ma-DEO wote nchini (Maafisa Elimu Mkoa na Maafisa Elimu Wilaya) kuhakikisha kwamba club hizi za upandaji wa mbogamboga zinaendelezwa katika shule zetu za sekondari na shule zetu za msingi nchini kote.