Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Santiel Eric Kirumba (5 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kushukuru kwa nafasi hii uliyonipatia. Napenda pia kukishukuru Chama changu cha Mapinduzi na UWT kwa Mkoa mzima wa Shinyanga kwa kuniteua kuwa mwakilishi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa ushindi wa kimbunga alioupata kwa mwaka huu. Ilikuwa si kazi rahisi lakini kwa matendo makubwa aliyoyafanya ameweza kushinda na wananchi wakaweza kumwamini na kumpa nafasi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia jinsi Serikali inapaswa katika mpango mpya huu wa kutengeneza ajira milioni nane na uchumi wetu uweze kupanda kwa asilimia nane. Serikali imejikita sana kwa wafanyabiashara ambao kwa sasa hivi tukiangalia kwa hali halisi wako ICU, ukiangalia tunawanyonya sana na wakati tuna lengo kubwa la kutengeneza hizi ajira milioni nane ili kufikia asilimia nane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza, naishauri Serikali iwawezeshe vijana na wanawake kwa kuwapa mitaji ya kutosha kwa sababu hii ndiyo nguvu kazi tuliyonayo. Hawa vijana wakitengenezewa ajira upya, NEMC wakitoa masharti ambayo ni nafuu, nina uhakika kila nyumba ina uwezo wa kuwa na viwanda vidogovidogo vya kuchakata vitu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kwa Mkoa wangu wa Shinyanga kuna vijana wadogo tu wenye miaka 25 wanatengeneza chaki, kuna kina mama wa kawaida tu wamekopeshwa na Halmashauri matrekta makubwa ya kufanyia kazi, mitaji ya milioni 50 wanafanya kazi vizuri. Mheshimiwa Rais aliongelea katika page ya 11 kwamba hii mifuko ya ukopeshaji ikichanganywa na kuwa pamoja itawezesha Halmashauri kutoa kiasi cha pesa cha kutosha. Kwa sasa hivi, hela zimegawanywa katika mifuko mbalimbali, kwa hiyo inafanya kwamba hata zile hela zilizokuwepo kwenye Halmashauri hazitoshi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kama Serikali inaweza ikafuatisha maoni ya Mheshimiwa Rais, hii mifuko ikawa mmoja itasaidia kwa kiasi kikubwa, itaongeza zile asilimia kumi za Halmashauri, itaenda kama ku-boost. Katika zile Halmashauri, wataangalia Serikali ina Halmashauri ngapi watazigawanya kama ni kwa pro rata au kwa ratio ya mikoa au kwa ratio ya wananchi ambao wako katika eneo lile ambao ni wanawake, vijana na walemavu. Hawa wakipewa mitaji ya kutosha watasaidia kui-boost hii ajira kwa kila mtu na tutakuwa tumepata ajira milioni nane na mapato ya nchi yataongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri Serikali hizi certificate zinazotolewa na Halmashauri ziweze kutumika kama dhamana, watu wanateseka sana kwenye dhamana. Kama Serikali inatoa hizi certicate katika Halmashauri ni wakati sasa hizi certicate hata benki wazikubali kwa sababu Halmshauri inazikubali kwa wajasiriamali wadogo wadogo kwa kuwapa mikopo. Ni wakati na benki nazo iviamini hivi vikundi watumie zile certificate kuwapa mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kwa huu Mpango mwingine wa miaka mitano, asilimia za mikopo ya wanawake itoke kwenye asilimia 4 iende kwenye asilimia 7. Ninyi mtaona kwa namna ya pekee wanawake tukiwezeshwa tunaweza. Hata kwenye kura mnatutumia sisi, mnatuita wanawake ni jeshi kubwa lakini wanawake sisi ni jeshi mmetupa asilimia 4, sisi wanawake ndiyo tunaokaa katika jamii tunailinda. Kwa hiyo, naamini kwamba tukitoka kwenye asilimia 4 tukapewa asilimia 7 tuta-boost ajira nyingi za wanawake na mapato ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba Serikali ipokee mchango wangu na naunga mkono hoja na naomba Serikali iunganishe ile mifuko iwe sehemu moja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Spika, wote ni mashaidi kwa muda mrefu ushirika umekuwa ukikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa viongozi wa ushirika wenye uwezo wa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa majukumu ya vyama kwa unafanisi. Hali hiyo imesababisha kukithiri ubadhirifu wa fedha na mali za wanaushirika hivyo kuwakatisha tamaa wakulima kujiunga na vyama hivi.

Mheshimiwa Spika, naomba Serikali kuweka mazingira rafiki wezeshaji kwa ajili ya upatikanaji wa masoko ya mazao ya uhakika ndani na nje ya nchi. Najua Serikali ilianzisha Kitengo cha Masoko (Agricultural Marketing Unit) katika Idara ya Maendeleo ya Mazao inayosimamia utafutaji wa masoko na tafiti za masoko na bei za mazao pamoja na kufuatilia mifumo ya uuzaji, pia Serikali inapaswa kuweka bajeti ya kutosha kufanya haya majukumu ili kusaidia hawa wakulima wetu wanapata shida.

Mheshimiwa Spika, naomba Serikali ya Awamu ya Sita kuendelea na utekelezaji wa programu ya kuendeleza kilimo awamu ya pili (ASDP II) hii itasaidia sana sekta ya kilimo. Serikali inapaswa kuboresha mifumo ya taasisi, bodi na sheria za kilimo kwa ajili ya usimamizi wa maendeleo ya mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, Serikali inapaswa kuunganisha wakulima wadogo na mashamba makubwa ili kuendeleza kilimo biashara, kupata ujuzi na maarifa ya kilimo. Wizara inapaswa kuharakisha upatikanaji pembejeo na masoko.

Mheshimiwa Spika, naiomba Wizara pia kuwekeza nguvu katika ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji, maghala, masoko na miundombinu bora ya kuhifadhi mazao ya kilimo. Pia naiomba Serikali kuimarisha uzalishaji wa mbegu bora na upatikanaji wa pembejeo nyingine za kilimo na kuzisambaza kwa wakulima.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote ningependa kukushukuru kwa kunipa nafasi hii. Ningependa kumpongeza Waziri wa Elimu kwa jinsi anavyofanya kazi yake vizuri, ni mama ambaye anajitoa sana kwenye hii kazi na hata ukimuita kwenye Kamati yoyote ni mwepesi kuhudhuria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini matatizo yanayowakabili wanafunzi hayana tofauti sana na matatizo ambayo yanawakabili walimu. Walimu unakuta kwa mfano natokea Jimbo la Msalala, Kata ya Bulyankulu walimu ni wachache. Walimu wana changamoto nyingi, wakitoka kazini wanaenda kuchota maji, kule unaweza ukakuta walimu wale labda wakang’atwa na nyoka. Kingine napenda kusema kwamba walimu hawa wamekuwa wakipitia changamoto nyingi sana apart from sisi Wabunge kuwasemea na watu wengine kuwasemea, walimu hawa wana chama chao. Chama chao hiki kimekuwa sio msaada kwa walimu kabisa, walimu wanakatwa asilimia mbili katika mishahara yao kila mwezi lakini mwalimu hata akipata ajali hawezi kusaidia na chama chake. Zaidi kwamba anaonekana atatibiwa na Bima ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, walimu hawa nimechukua tu kwa ratio ya kawida, walimu 5,000 Tanzania hii ambao wanakatwa shilingi 25,000 kwa mwezi wabachangia milioni 125,000. Kwa mwaka chama cha UWT kwa walimu 5,000 kipanata bilioni 1.5 lakini mwalimu anapostaafu chama hiki kinampa mabati. Kweli kwa miaka yote anayochangia ni kweli anastahili mwalimu kupewa mabati? Tufike mahali sisi wenyewe tunawafanya hawa walimu wanashindwa ku-perform katika kazi zao vizuri. Chama hiki wanalazimishwa automatically kujiunga lakini katika ya CWT inamwambia kwamba mwalimu kujiunga ni hiari yake lakini automatically wanashirikiana na utumishi kuwafanya walimu hawa kuingia na kuwakata hiyo asilimia mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachoomba Serikali chini ya Wizara ya Elimu, walimu wasilazimishwe kujiunga na hiki chama kwasababu sio msaada kwao. Walimu wana changamoto nyingi lakini CWT haiwasemei chochote zaidi ya kukusanya. CWT ina mabenki, lakini walimu hawanufaiki. Wana kila hela wanazochukua, mahesabu yao hayako wazi. Sijawahi kusikia CWT inatoa mwongozo wowote kwamba mapato na matumizi yaliyotumika mwaka huu yako hivi.

Mheshimiwa Spika, naomba the way CAG anavyopambana na watu wengine naomba sasahivi akaifanyie kazi CWT. Kwasababu haiwezekani walimu wanateseka kiasi hiki, CWT iko kimya! Kuna walimu wamefukuzwa vyeti feki, CWT ni chama tu kilitakiwa kiwape hata washirika wake pesa zozote hata kile kifuta jasho kwa ambao wamefukuzwa lakini CWT imekaa kimya! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kwa kweli Waziri wa Elimu hiki chama kifutwe kwasababu walimu wengi wanakuambia hakina manufaa, wanalalamika. Elfu 25,000 kwa mwalimu mmoja kwa mwaka ni 200,000. Mimi kule ninapotoka chumba mwalimu ni shilingi 10,000 kwa hiyo hii kodi ya karibu mwaka mzima.

SPIKA: Mheshimiwa Santiel, kwa hiyo unataka walimu wasiwe na chama.

MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Spika, wajiunge kwa hiari lakini sio kwa kulazimisha kwasababu walimu nao wana changamoto. Nakupa mfano kuna mwalimu Shinyanga alipata ajali, chama kama chama anachangia, kweli leo ukistaafu upewe bati mbili na shughuli zote hizi unazowafanyia wananchi wako? Bundle mbili za bati kweli ni sawa? Tuongee kwa hali halisi. Mwalimu anachangia, ni walimu wangapi wamechangia? Kwa nini hiki chama hakiko wazi? Waache watu wajiunge kwa hiari sio kuwalazimisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, walimu nao wana haki sidhani hapa kama sisi Wabunge tungelazimishwa kuchangia hela…

SPIKA: Mheshimiwa Santiel kuna mambo mengi inabidi ujifunze bado. (Kicheko)

MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Spika, sijakataa lakini naangalia. Nimechukua changamoto ambazo walimu wanapitia…

SPIKA: Nafikiri hilo siku moja ulinyanyue kwenye Kamati ya Chama upate elimu kidogo ya mambo haya yakoje na nini. Kuna haja ya ku-improve kama kuna improvements lakini ukisema kufuta sasa wabakie empty ndiyo watakuwa wamekwenda, wamerudi nyuma hatua 100? Lakini kama kuna areas of improvement, ndiyo kazi yetu Wabunge lakini kwamba kundi la wafanyakazi wasiwe na, yaani does it… ila kama kuna mapungufu ni areas za ku-improve.

MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Spika, samahani… hoja yangu ilikuwa…

SPIKA: Mheshimiwa waziri ulisimama, Waziri wa Nchi.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, nilikuwa tu nataka kusaidia kwenye eneo hilo kwamba sisi ni wanachama wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) na tumesharidhia mikataba na katika mikataba tuliyoridhia iko mikataba ambayo inatutaka tutoe uhuru wa majadiliano kwa wafanyakazi. Uhuru wa majadiliano ndiyo unaojenga uwepo wa vyama vya wafanyakazi kwenye maeneo ya kazi. Na wajibu wa vyama vya wafanyakazi ni kuhakikisha kwamba wao wanakuwa ni daraja la mahusiano kati ya mwajiri na wafanyakazi.

Mheshimiwa Spika, sasa nilichokuwa nataka kukisema hapa ni kwamba CWT iko kwa mujibu wa sheria na taratibu za vyama vya wafanyakazi nchini. Kwa hiyo, kama kuna walimu wanaona kuna matatizo kwa kuzingatia Katiba waliyonayo na miongozo inayoongoza uwepo wa vyama vya wafanyakasi wana fursa na nafasi ya kufanya majadiliano kwa kupitia utaratibu ambao umewekwa kisheria na wakafikia muafaka na vyama hivyo vikaendelea kuwepo. Uwepo wa vyama vya wafanyakazi ni muhimu sana kwenye maeneo ya ajira kuliko kitu kingine chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni ushauri tu kama Taarifa. Niseme kwamba, kama yako matatizo iko fursa ya majadiliano na huo ndiyo msingi wa kisheria na sheria za kazi na ajira zinaweka msingi huo wa majadiliano ya pamoja.

SPIKA: Ndiyo maana nikasema Mheshimiwa Santiel kwamba bado kuna mengi ya kujifunza kwa sababu hawa wako kila Wilaya. Kila jimbo mlipo wapo CWT na wanafanya kazi pale na Mkurugenzi ambaye ndiyo mwajiri wa walimu katika wilaya ile. Ule uonevu wote n.k wanafanya kazi huko huko kimya kimya.

Mkitaka hicho chama kiwe ni cha kupiga kelele mtatoka jasho hasa ninyi Chama Tawala. Kumbuka kundi la walimu ndiyo kundi kubwa kuliko kundi lolote lile la wafanyakazi. Kwa hiyo, hawa watu wanaofanya kazi kubwa ambayo ninyi wengine hamuijui mkafikiri kwamba zawadi yao ni kupigwa tu humu ndani n.k ndiyo maana nikasema there is a lot to learn sometimes. Bado una dakika mbili au ziliisha? Wanasema moja lakini nakuongeza ya pili.

MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Spika, kikubwa nilichokuwa naomba kwasababu kuna Tume ya Utumishi wa Walimu, lakini ninachoomba walimu kwenye chama hiki wasilazimishwe kujiunga. Wajiunge kwa hiari kwasababu Katiba yao inawaambia kwamba watumishi hawa wajiunge kwa hiari na sio kama hivi inavyopitia kwa utumishi kwamba automatically anakuwa amejiunga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimepitia kuwauliza walimu wengi, ni kweli wanakwambia hawajawahi kuandika barua yoyote ya kujiunga kwa hiyo inaenda automatically, kwasababu Katiba ipo…

SPIKA: Si umeshaambiwa ni sheria?

MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: … mimi naomba kwamba…

SPIKA: Sasa kaa chini!

Uwe unaelewa. Ukiona unakwenda mahali unatafuta kaa na Waheshimiwa Mawaziri n.k upate elimu Mheshimiwa Santiel.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote napenda kuipongeza Wizara ya Fedha kwa bajeti hii ambayo imekuwa ni rafiki kwa maendeleo ya nchi hii, bajeti ambayo ieonesha dhima nzima ya Mheshimiwa Rais ambayo siku ile alikuwa ana hotubia hapa. Pia, bajeti hii imelenga hasa katika suala kamilifu la kutekeleza kuboresha mazingira ya kibiashara. Tumeona kwamba katika bajeti hii kodi nyingi zimefutwa. Mama amejitahidi kwa kiasi kikubwa kuonesha nchi hii ni sehemu salama kwa kwa ajili ya watu kuja kuwekeza. Viel vile bajeti hii imeweza kurahisishwa ulipaji wa kodi. Kwa hiyo, napenda kuipongeza sana Awamu ya Sita kwa kazi kubwa inayoifanya na Wizara ya Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuchangia kwenye kitu kingine na kutilia mkazo katika Halmashauri zetu. Halmashauri zetu zinafanya kazi vizuri, lakini kuna nyingine ambazo makusanyo yake ni madogo. Sijui Wizara ya Fedha imejipangaje katika kwa Halmashauri ambazo vipato vyake ni vidogo, makusanyo hayo ambayo yanakwenda kuathiri zile asilimia 10 ambazo tumewaahidi wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikichukulia mfano kama Halmashauri ya Shinyanga Vijijini, Ushetu, kwa kweli kwa mwaka hawa watu mapato yao ni madogo. Unakuta makusanyo kwa mwaka ni shilingi milioni 137, watu waliokopeshwa unakuta ni vikundi 10. Sasa fikiria kwa haraka haraka, ni vikundi vingapi vitakuwa vimefikiwa ili kuwezesha hawa vijana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnaona huku kwenye Serikali ajira bado ni ngumu kupatikana na pia huku tumeweka katika Ilani yetu kwamba tutawezesha vijana, wanawake na walemavu kupata mikopo. Ukija huku nako bado mapato yanayopatikana ni machache kiasi kwamba hawawezi kukopesheka na hawawezi kupata fedha za kutosha kwa ajili ya kutenga ile asilimia 10, vijana wote na wanawake wote wakaweza kufikiwa. Licha ya hivyo, bado fedha nyingi zipo mikononi. Sijaelewa kwa jinsi gani Wizara ya Fedha itaweka msisitizo katika hizi Halmashauri zile fedha ziweze kurudishwa ili zikawasaidie wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nakuja kwenye suala lingine la TRA. Mmeona kabisa tulivyokuwa kwenye semina imeonesha kwamba walipa kodi ni 5% katika nchi hii ambayo ina watu milioni 60 ambapo walipa kodi almost milioni tatu. Utafikiria kwamba kwa kiasi kikubwa wananchi hawalipi kodi. Vilevile Serikali haijaweka mazingira rafiki kwa ajili ya watu kulipa kodi. Unaweza kufikiria kwamba kwa kipindi kilichopita kuna watu walikuwa wanabambikiziwa kodi kitu ambacho kinaweza kikawafanya wale wafanyabiashara wakaingia hofu na kutufanya tupoteze mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali itaweza kujipanga na ituoneshe kwamba katika bajeti hii imejipangaje kwa wale watu ambao walibambikiziwa kodi? Maana kuna watu walibambikiziwa kodi mpaka wamefunga maofisi. Je, haioni kwamba ni wakati sahihi sasa hivi ya kukaa tena na wale wafanyabiashara na kuzitoa zile kodi ambazo zilikuwa siyo sahihi? Wali-double charge kwenye VAT katika mapato yao ya kipindi cha nyuma. Naona Wizara ya Fedha ingekuja na mkakati mpya wa kupitia wale wafanyabiashara ambao walikuwa wamefanyiwa huo mchezo. Nami nakuomba Mheshimiwa Waziri, nakuona hapo, mimi nitakufuata kwa sababu nami ni muhanga wa suala hili, kwa sababu hiyo inamfanya mtu akwepe kabisa kulipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine, kuna hizi Agency Notice zinawekwa. Unakuta kuna wafanyabiashara wanafanya kazi on credit bases; thirty days, sixty days of invoice. Sasa unakujakuta hata yale malipo hajayapata, ameshatumiwa Agency Notice kwa mteja wake. Ile inamfanya huyu mlipaji kodi ashindwe kulipa hii kodi. Kwa hiyo, naomba kabisa Wizara ya Fedha ifanye mkakati wa kufanya hii Taasisi ya TRA, walipa kodi walipe kwa hiari, siyo kwa kutumiwa task force, siyo walipe kodi kwa kulazimishwa. Mtu afike mahali aone ni hiari kuichangia Serikali yake, siyo Serikali itumie nguvu kum-force mtu alipe kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka kuchangia sehemu nyingine ambayo ni ya mwisho, nayo ni sekta ya afya. Nimeona kwenye sekta ya afya mmetenga bajeti kwa ajili ya kumaliza maboma 8,000. Hiki ni kitu muhimu sana. Haipendezi tena tunaporudi kule kwa wananchi wetu tuwakute tena wanalalamika na wameweza kupandisha mabomba maboma hayo 8,000 mpaka kufika hapo. Serikali inabidi sasa mkafanye mpango kama mlivyofanya kwenye barabara na pia kujenga shule. Mheshimiwa Ummy umefanya jambo moja zuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nakuomba sana, wanawake wakasaidiwe kupata sehemu salama za kujifungua kwa sababu haya maboma 8,000 yanaweza kufanya ushawishi mkubwa sana kwenye Sekta ya afya, itafanya mapinduzi makubwa sana kwa sababu kuna yale maeneo ambayo kweli yana mwendo mrefu mtu kukuta Kituo cha Afya. Nina imani kwamba hili nalo likitekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, sisi Wilaya ya Kishapu ina maboma 20 ambayo hayajakamilika. Ukienda Wilaya ya Shinyanga Vijijini, ina maboma 39 ambayo haijakamilika. Sasa utaona kwa jinsi gani kukiwa na mama mjamzito atapata shida, ambao ni wanawake wenzangu; kuna Watoto na wazee ambao wanaenda mwendo mrefu kupata huduma ya afya. Nina imani hilo nalo linaenda kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, hayo ndiyo yangu, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa katika Mkutano wa Tatu wa Bunge na Mkutano wa Nne wa Bunge pamoja na Kanuni za Uvuvi za Mwaka 2009
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kukushukuru kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia katika hii Kamati ya Sheria Ndogo nikiwa kama Mjumbe. Kuna mambo madogomadogo, kwanza katika sheria hizi zinazotungwa ni sheria ambazo zinaweza kutuingizia mapato sisi katika halmashauri zetu na sheria hizi zinagusa mwananchi directly. Kwa hiyo tunapozitunga lazima tuangalie sheria hizi zinaendana na uhalisia wa maisha ya mwananchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapenda kuishauri Serikali iwe inapitia kwa karibu sheria hizi kabla hazijafika mbali na kabla hazijaanza kutumika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia suala moja; katika GN ya tarehe 9, Julai, Na. 589 ya The Wildlife Conservation, sheria hii kifungu cha 12(4) hakimpi mamlaka Waziri kutunga sheria na badala yake kinakinzana na sheria mama ambayo imemruhusu katika Kifungu cha 121(a) ambayo Waziri anapewa mamlaka kutunga sheria zozote ambazo zinamhusu. Kwa hiyo tunapenda kama Waziri husika afanye marejeo anapotunga sheria zake, aangalie kifungu hicho mama kinamwelekeza nini ili aweze kufanya kazi yake hii kwa ufasaha. Hata hivyo, ni watu ambao wanafanya kazi vizuri na tumeshirikiana nao vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hiyohiyo GN ya Julai 9, 2021 Na. 589, hili ni jambo lingine la kushangaza, The Wildlife Conservation Act inaelezea kwamba mtu yeyote aliyeajiriwa katika Jeshi Usu haruhusiwi kufanya kazi nyingine yoyote, unapomaliza kazi uende ukapumzike. Wanaelewa kabisa hawa watu tulivyowaajiri vipato vyao ni vidogo, unapomwambia asijihusishe na kazi yoyote, ile sheria uliyotunga inakinzana na sheria mama ya Labour Act, unless uwe na conflict of interest katika lile jambo, lakini hakuna, unamwambia anapomaliza kazi yake asiende kufanya shughuli yoyote, sidhani kama hili liko sawa. Wabunge wanaelewa vipato vyetu ni vidogo, uambiwe usijihusishe na jambo lolote au na shughuli yoyote, unapomaliza shughuli zako za Bunge uende ukapumzike; kweli itaweza kufaa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri arudie tena hiki kifungu, akipitie. Unless kama haipingani, haina conflict of interest, awaruhusu hawa watu waweze kuendelea kufanya kazi zao nyingine. Kwa sababu mnaelewa hawa Jeshi Usu mishahara yao jinsi ilivyo midogo. Tukiendelea kufanya sheria ambazo zinawabana wananchi wetu wasijiingizie kipato, wasifanye shughuli nyingine, hiki kitu ni changamoto sana. Halafu kingine, inatengeneza hali ya uchonganishi na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vitu ambavyo vinaongeleka, ni vitu ambavyo vinasaidika na ni vitu ambavyo vinawezekana. Naomba Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wako hapa na tulikuwa nao kwa pamoja, waipitie hii kanuni ya 24 iweze kuwapa uhuru hawa Jeshi Usu kufanya kazi nyingine. Naelewa wanaelewa kazi ngumu ambayo wanaifanya na hawa watu wanafanya kazi ngumu sana, lakini kama haiathiri sheria zao, naomba waruhusiwe hawa watu kufanya shughuli nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ya kwangu ni hayo, nashukuru sana. (Makofi)