Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Prof. Patrick Alois Ndakidemi (41 total)

MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante Sana. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali la nyongeza. Daraja lililopo Jimbo la Moshi Vijijini lilisombwa na maji mwaka mmoja uliopita na daraja hili ni muhimu, linaunganisha kata nne katika Jimbo la Moshi Vijijini. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa daraja hili? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua maeneo yote korofi ambayo madaraja yetu kwa namna moja ama nyingine yameathirika na mafuriko kutokana na mvua ambazo zimeendelea kunyesha hapa nchini. Serikali imeweka mkakati wa kwenda kufanya tathmini ya mahitaji katika maeneo hayo korofi ili kulingana na upatikanaji wa fedha, fedha ziweze kutengwa na madaraja hayo yaweze kujengwa au kufanyiwa marekebisho ili kuwezesha wananchi kupata huduma kama Serikali inavyodhamiria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Moshi Vijijini kwamba eneo hilo Serikali inalitambua na tutakwenda kadri ya upatikanaji wa fedha kutenga bajeti kwa ajili ya usanifu, lakini pia kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo ili tuweze kurahisisha shughuli kwa wananchi.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina swali la nyongeza ambalo lina vipengele viwili.

Mheshimiwa Spika, kwanza, katika Kata ya Uru Shimbwe kuna shida kubwa sana ya huduma ya mawasiliano ya Radio hasa kwa Redio yetu ya Tanzania na Television yetu ya Taifa. Pili, kuna shida ya huduma ya internet na imesababisha Kata ya Uru Shimbwe ishindwe kutuma taarifa kupitia kwenye zahanati yetu kwenye Shirika la Bima la Afya. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba huduma hizi zinaboreshwa kwenye eneo la Uru Shimbwe?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Patrick Alois Ndakidemi Mbunge wa Moshi Vijijini kwa sababu masuala haya tumekuwa tukiwasiliana na jiografia ya eneo husika tayari ameshanieleza jinsi ilivyo. Hata hivyo, kupitia mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba tunafikisha huduma za mawasiliano vijijini zikiambatana na usikivu wa redio katika maeneo husika tayari Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeshaanza kufanya tathmini katika maeneo husika.

Mheshimiwa Spika, vilevile katika eneo ambalo ameongelea kuhusu upatikanaji wa data, Serikali tayari imeshatoa maelekezo kwa watoa huduma wote, sehemu yoyote ambapo tutapeleka mradi wowote ule, lazima mradi huo ukajengwe wa kutoa huduma ya kuanzia 3G maana yake ni kwamba, ni lazima sasa Tanzania tutakuwa na miradi au minara ambayo itakuwa inatoa huduma ya internet. Nasema hivyo kwa sababu hapo kabla tulikuwa tunaangalia tu angalau kila Mtanzania aweze kupata mawasiliano, lakini kwa sasa tunalazimika kwa sababu ya mahitaji ya kuelekea kwenye digital transformation maana yake kwamba mahitaji ya internet ni makubwa zaidi ikiambata na eneo la Mheshimiwa Patrick, Moshi Vijijjini. Nashukuru.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini niseme ukweli kwamba mikopo inayotolewa ni mikopo na si zawadi. Sasa kuna kitu ambacho kimejitokeza kwamba watu wanaosoma shule binafsi au watoto wa watumishi wa Serikali hawapati mikopo huo ndio ukweli tusiseme uongo.

Je, wako tayari kama itajirudia tena hiyo kitu walete sheria Bungeni ibadilishwe ili itamke wazi kwamba watakaopewa mikopo ni watu waliosoma Serikalini na sio waliosoma kwenye shule za watu binafsi au watoto wa watumishi wa Serikali? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimwa Naibu Spika, ahsante na napenda kujibu swali dogo la Mheshimiwa Ndakidemi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi mikopo hii inaratibiwa kwa ile Sheria Namba 178 ya Bodi ya Mikopo ambayo imebainisha vigezo na vielelezo vya mwanafunzi gani na mwenye sifa zipi wa kupata mikopo hiyo na ambayo haibainishi kwamba amesoma shule gani na alikuwa analipa ada gani katika hizo shule za nyuma zilizopita. Lakini kwa vile yeye Mheshimiwa Mbunge amelieleza jambo hili hapa, tunalichukua tunakwenda kulifanyia kazi na kama kulikuwa na mchezo fulani ambao unachezwa nimwahidi tu kwamba katika kipindi hautatokea na mikopo hii itawafikia wote wenye uhitaji wa kupata mikopo hii.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kutokana na jiografia ya Mkoa wa Kilimanjaro, niseme ukweli kwamba changamoto yetu kubwa kule Kilimanjaro ni barabara hasa Jimbo langu la Moshi Vijijini na wakati wa mvua kama huu kuna mafuriko makubwa sana. Naomba nimuulize Naibu Waziri ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya TPC – Mabogini – Kahe yenye urefu wa kilometa 11.4 na kumalizia zile za Kibosho Shine - Kwa Raphael - International School - Kiboriloni - Sudini – Kidia?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Serikali ilishasema ingeanza upembuzi yakinifu wa barabara ya Uru – Mamboleo - Materuni yenye kilometa 10.2, ni lini Serikali itafanya zoezi hilo. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Profesa Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama ulivyoniongoza, umeniomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kuhusu ni lini upembuzi yakinifu utaanza katika barabara ya Uru – Mamboleo – Materuni yenye urefu wa kilometa 10.2.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais makini kabisa Mama Samia Hassan Suluhu, tumesikiliza maombi ya Mheshimiwa Mbunge. Kwa sababu ameomba tu upembuzi yakinifu na nafahamu mpaka muda huu TARURA wananisikiliza ni agizo langu kwao kwamba sasa watenge fedha waanze upembuzi yakinifu kwa ajili ya barabara hiyo ili iweze kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia hizo barabara nyingine zote ambazo ameziainisha, Serikali imesikia tutaziweka katika Mpango kuhakikisha zinakamilika kwa wakati. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante sana kwa kunipa fursa. Shirika la Utafiti wa Kahawa Tanzania Coffee Research Institute limezalisha aina chotara za kahawa ambazo huwa huzaa mara tano zaidi ya zile kahawa za asili zilizokuwa zinaitwa Kent. Wakulima wengi wanalima hizi kahawa za zamani ni lini Serikali itaanzisha program maalum ya kuwafundisha wakulima umuhimu wa hizi kahawa mpya chotara kutoka Lyamungo ili waweze kuongeza tija? Wanahitaji mafunzo sana. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Moshi Vijijini na kwa niaba ya Serikali na Wizara ya Kilimo ni-acknowledge kazi aliyoifanya katika sekta ya kilimo akiwa bado chuoni. Ni kwamba Serikali imekwisha anza kazi na tumeanza kuwatumia wataalam wetu wa TaCRI na tumeshaanza multiplication ya miche la kisasa ambayo tunaanza kuipeleka kwa wakulima. Tumeanza kuigawa miche hii kwa baadhi ya wakulima na kuwapa elimu. Kwa hiyo program hiyo imeshaanza na elimu imeshaanza kutolewa kwa wakulima umuhimu wa kwenda kwenye hybrid ili waweze kuongeza mapato yao.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii na mimi narejea kwenye lile swali la msingi la Hospitali ya Mawenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Hospitali ya Mawenzi ilipandishwa hadhi ikawa Hospitali ya Rufaa na kule Moshi hakuna Hospitali ya Wilaya. Ni lini Serikali itatujengea Hospitali ya Wilaya ili iweze kuhudumia watu wa Jimbo la Moshi Vijijini, Jimbo la Vunjo na Manispaa ya Moshi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu swali la Mheshimiwa ndugu yetu, Profesa Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Wilaya ya Moshi Vijijini haina hospitali ya wilaya na ndio maana hata baadhi ya ambulance kwa ombi la Mbunge ambazo zilikuwepo pale Mawenzi zimetolewa zikapelekwa kwenye vituo vya Moshi Vijijini ili kusaidia wananchi kutokana na hiyo adha ambayo anaisema.

Mimi nafikiri Mheshimiwa Mbunge kuna umuhimu wa kukaa sasa na kuangalia jiografia ya Moshi Vijijini kwa sababu ukiiangalia jiografia yake kwanza ni milimani, lakini imezunguka Mji wa Moshi Mjini; muangalie sehemu nzuri kijiografia ambayo inafaa halafu hatua stahiki zianze kufuata sasa kuanzia kwenye Halmashauri yenu kuja Mkoani - RCC, ili iweze kufika TAMISEMI na mwisho wa siku kazi hiyo iweze kufanyika.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nina maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya Ndugu yetu pia:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza nauliza kwa kuwa, tayari barabara ya Mferejini – Narumu – Takri – Lyamungo hadi Makoa imeshatengewa shilingi milioni 500 kwa ujenzi wa kiwango cha lami. Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa hivi kuongeza pesa mwaka huu wa fedha, ili hiyo barabara ikamilike kwa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Mwenyekiti, na swali la pili, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa International School kwa Raphaeli, Umbwe, inayounganisha na hii Barabara ya Mheshimiwa Mafuwe kule Lyamungo kwa kiwango cha lami? Ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa hii barabara inayoishia pale Mto Sere?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Profesa Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ameeleza, kwanza ametambua kwamba, Serikali tumepeleka fedha milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami. Na kikubwa ambacho ameomba tu ni kwamba, je, Serikali ni namna gani tutaongeza fedha kwa ajili ya barabara hiyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, moja, tuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama yetu Samia Hassan Suluhu kwa kutoa fedha milioni 500 kwa majimbo yote nchini kwa ajili ya barabara kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili kwenye jambo hili tuombe Bunge lako tukufu mpitishe bajeti kuu, ili yale mapendekezo yaliyoletwa na Wizara ya Fedha ya kuongezea TARURA fedha katika kile chanzo cha shilingi 100 iweze kupita maana tutapata fedha. Na hizi fedha tutakazopata maana yake tutakwenda kuongeza barabara katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo hili ejeo ambalo mmeliainisha hapo. Kwa hiyo, ombi letu kwenu mpitishe bajeti kuu na sisi tutafanyia kazi maombi yote ambayo Waheshimiwa Wabunge mmeyaleta kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili ameeleza hii Barabara ia International School kupitia Umbwe na hayo maeneo ambayo ameyaainisha ambayo yako katika jimbo lake:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge hivi ninavyozungumza kazi nzuri ambayo ulikuja Ofisini kwetu na ukatuomba tumeanza kwanza kujenga mifereji katika barabara hiyo na itakavyokamilika maana yake tutaipandisha hadhi kwa kuiongezea viwango vile ambavyo vinastahili. Kwa hiyo, ndio kazi ambayo tumedhamiria kuifanya na tutaifanya kwa wakati wote, ahsante sana.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika,
asante sana kwa kunipa fursa na naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba Serikali inatoa kauli gani kuhusiana na bughudha wanazopata wafanyabiashara na wakulima wa soya wa Mikoa ya Ruvuma na Mbeya kwa sababu wanazuiliwa kuuza na kununua wanavyotaka na tunajua zao hili limepata soko huko China sasa hivi. Serikali inatoa kauli gani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Profesa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, position ya Wizara ya Kilimo na Serikali ipo very clear na nitumie Bunge lako Tukufu kusema zao la soya Mkoa wa Ruvuma na mikoa yote inayolima soya halimo kwenye stakabdhi ya ghala. Ninaomba Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wasibughudhi mnunuzi yeyote anayeenda kununua kwa mkulima zao hili. Tumelisema kwa mdomo na tumeandika, tunarudia tena, asibughudhiwe mnunuzi yeyote anayenunua zao la soya, volume ya soya aina economic viability kuingiza kwenye stakabadhi ya ghala, bado volume ni ndogo. Wizara ya Kilimo ndio ina-mandate ya kutangaza zao gani liingie kwenye stakabadhi ya ghala. Tumesema mwaka huu waliondoe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zao lingine ni choroko na dengu yaliyopo katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa hayaingii katika mfumo wa ushirika kwanza, tutayaingiza wakati utakapofika na tutakapoona kwamba sasa ni muhimu kufanya namna hiyo. Tumetoa guidance kwenye price wanachotakiwa Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya ni kufuatilia guided price iliyotolewa na Wizara ya Kilimo as indicated price kwenye masoko na wasiwabughudhi wanunuzi. (Makofi)
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita nane kati ya kilomita 42 inayoanzia Kibosho Shaini – Kwa Rafael hadi International School?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Partrick Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ametaka kujua ni lini Serikali itakamilisha kipande cha kilomita Nane cha barabara yake ya kutoka Kibosho Shaini - Kwa Rafael hadi International School. Barabara hii ina urefu wa kilomita Nane. Serikali ilishaanza na ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatafuta fedha na ikipatikana, kipande hiki cha kilomita nane zilizobaki itakijenga kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa. Shida ya kujengewa hospitali katika Kanda ya Magharibi inafanana kabisa na shida tuliyonayo Wilaya ya Moshi.

Je, ni lini Serikali itatujengea Hospitali ya Wilaya ya Moshi kwa sababu tayari tumeshapata eneo la ekari 38? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge. Mimi mwenyewe nimetembelea eneo hilo ambalo anasema limetengwa, nimeliona. Kikubwa ni kwamba tutashirikiana na wenzetu wa TAMISEMI ili kwenye bajeti ya mwaka huu tuweze kuona ni namna gani utekelezaji wa hilo hitaji lao litafanyika. (Makofi)
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini pamoja na majibu hayo ni ukweli usiofichika kwamba changamoto kubwa kwa uzalishaji wa kahawa ni hayo magonjwa uliyoyataja na mbegu zilizozalishwa bado hazijaweza kupambana na hayo magonjwa mia kwa mia.

Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuanzisha mfuko wa maendeleo ya kahawa ili wakulima waweze kupata pesa za kununua pembejeo wapambane na magonjwa haya?

Mheshimiwa Spika, swali la pili je, kwa kuwa tumehamasisha sana uzalishaji wa kahawa, Serikali haioni pia ni muhimu kuanzisha programu za kuboresha mifereji ya asili ili wakulima waweze kupata maji ya kumwagilia kahawa zao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Profesa Patrick Aloyce Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza sisi tunaona Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo ambao tumeutamka katika bajeti yetu unatosha kwa ajili ya kushughulikia mazoa yote. Nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba zao la kahawa pia ni kati ya mazao ambayo yanashughulikiwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo na hivi sasa utaratibu ambao unaendelea ni kutenga kila shilingi mia moja kwenye zao la kahawa aina ya robusta na shilingi mia mbili kwa arabica kwa ajili ya kuchangia katika mfuko huu, kwa hiyo mwisho wa siku pia utakwenda kuhudumia zao la kahawa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mifereji, nakubaliana na wewe Profesa nami nimefika katika baadhi ya mashamba katioka Mkoa wa Kilimanjaro, hilo tumelichukua tunaendelea kulitekeleza, tutalifanyia kazi ili mwisho wa siku liweze kuleta tija kwa wakulima wetu. (Makofi)
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana; je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba shule zote za kata na za Serikali kwa ujumla zinapata hatimiliki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Profesa Ndakidemi, Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kuhakikisha shule zote zinakuwa na hati iliki na ndiyo mpango uliopo sasa na tumehamasisha halmashauri zote kutekeleza jambo hilo. Kwa hiyo lipo katika mpango wa Serikali. Ahsante.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza. Barabara ya Getifonga - Mabogini hadi Kahe, iko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi kujengwa kwa kiwango cha lami na huko ndiko ilikojengwa hospitali ya wilaya: Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara hii?

Mheshimiwa Spika, barabara ya International School - Kibosho KCU hadi kwa Raphael imebakiza kilomita nane kukamilika kwa kiwango cha lami: Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Profesa Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba barabara aliyoitaja mwanzo ya kutoka Getifonga – Mabogini Kahe, ipo katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge barabara hii kwa sasa iko katika usanifu kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa kiwango cha lami. Usanifu unaofanyika ni wa kilomita 31.25, kwa hiyo, tupo katika hatua nzuri kwenye hiyo.

Mheshimiwa Spika, barabara ya kutoka International School – Kibosho - KNCU mpaka kwa Raphael na yenyewe kilomita 8.42 tayari imeshajengwa kwa kiwango cha lami. Kiwango ambacho kimebakia ni kilomita 5.49, kwa hiyo na yenyewe tunatafuta fedha ili tuanze ujenzi kwa kiwango hicho.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante sana. Kumekuwa na uhaba mkubwa sana wa Maprofesa katika Vyuo Vikuu vya Dar es Salaam, Sokoine, Mandela, Ardhi na Chuo cha Muhimbili. Baada ya kustaafu wakiwa na miaka 65 wanaambiwa waende nyumbani na biashara imeishia hapo, lakini kuna uhaba mkubwa.

Kipi bora, je, tuongeze miaka yao ifike angalau 70 waendelee kuhudumia nchi yetu? Kwa sababu kuna ombwe kubwa sana la ngazi hizi kwenye Vyuo Vikuu. Naomba Serikali ifikirie hawa watu waendelee mpaka miaka fulani hivi ili vijana wetu wapate elimu ya uhakika. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Profesa Ndakidemi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli anayozungumza Mbunge kwamba tumekuwa na changamoto sana ya Wahadhiri katika kada hii ya Maprofesa kutokana na wao kustaafu. Naomba nimweleze tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kustaafu kwa upande wa Utumishi wa Umma ilikuwa ni miaka 60 kwenye maeneo mengine yote, lakini kwa upande wa wenzetu hawa Maprofesa au Wahadhiri wa Vyuo Vikuu ilipandishwa kutoka miaka 60 kwenda miaka 65. Sasa hivi Mheshimiwa Profesa Ndakidemi anasema kwamba angalau tungeongeza ifike miaka 70.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tulibebe wazo hili, ingawa vilevile nimeeleza kwenye majibu yangu ya msingi kwamba katika mradi wetu wa HEET, unakwenda kufundisha katika level ile ya Ph.D ambapo tunaamini wengi sasa wataenda kuwa Maprofesa, ambao tutahakikisha katika eneo hili tunaenda kufanya coverage kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuchukue wazo lake Mheshimiwa Prof. Ndakidemi twende tukalifanyie kazi ili tuweze kuona mtu akifikisha miaka 70 atakuwa na uwezo wa kusimama darasani akafundisha au akasimamia watu kwenye kazi zao? Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa. Wananchi wa kata za Mbokomu na Uru-Shimbwe katika Jimbo la Moshi Vijijini wamejenga Vituo vya Polisi na bado havijakamilika.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi hawa waliotumia nguvu zao kujenga hivi vituo na kuwajengea nyumba Polisi wa Kata?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Prof. Patrick Ndakidemi, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze yeye na wananchi wake kwa kuanza ujenzi wa vituo hivi kwa kutumia nguvu zao na jitihada zao Mbokomu na Uru. Kama nilivyojibu kwenye swali lililoulizwa na moja ya Wabunge hapa tutawatuma Askari wetu upande wa Kilimanjaro ili wafanye assessment ya kiwango kilichofikiwa, kiasi gani kinatakiwa ili vituo hivi viweze kukamilishwa hatimaye tuviingize kwenye mpango wa ujenzi. Nashukuru. (Makofi)
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika,
ahsante sana kwa kunipa fursa.

Kituo cha afya cha Umbwe ambacho ni ndio kituo pekee cha afya katika Tarafa ya Kibosho hakina gari la kubeba wagonjwa; je, Serikali ina mpango gani wa kutupatia gari la kubeba wagonjwa katika kituo hiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Profesa Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimia Spika, ni kweli kwamba Kituo cha Afya cha Umbwe ni kituo pekee katika tarafa hiyo na kinahudumia wananchi wengi na hakina gari la wagonjwa. Mheshimiwa Ndakidemi amekuwa akifuatilia mara kwa mara, lakini naomba nikujulishe Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote kwamba Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mwaka huu wa fedha tutapeleka magari ya wagonjwa katika halmashauri zote 184, lakini pia tutapeleka magari ya huduma za afya kwa maana usimamizi katika halmashauri zote 184, ikiwemo Halmashauri hii ya Moshi Vijijini, na hivyo ni maamuzi ya halmashauri kuona inakipa kipaumbele kituo hiki cha afya cha Umbwe ili kiweze kupata gari hilo, ahsante.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na ninamshukuru sana Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Nina swali moja la nyongeza.

Kwa kuwa, biashara hii huwa inahusisha upandaji na utunzaji wa miti. Je, Serikali haioni umuhimu wa kusukuma hii biashara iende katika maeneo ya Kilimanjaro inayopakana na Mlima Kilimanjaro ili kwanza tutunze ule msitu ili Mlima usiharibike na wananchi wa Kilimanjaro wajipatie kipato?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Patrick Ndakidemi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri na niseme kwamba ipo haja ya mradi huu kwenda Kilimanjaro kwa lengo na madhumuni ya kuhifadhi na kutunza mazingira.

Mheshimiwa Spika, pia kuna haja ya mradi huu kupelekwa Kilimanjaro na tutakwenda kuhakikisha tunapeleka ili lengo na madhumuni wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro na vijiji vilivyomo ndani ya Mkoa huo waweze kunufaika, kwa sababu mradi huu si kwamba tu unanufaisha Serikali Kuu lakini hata vijiji vidogo vidogo vinanufaika kupitia mradi huu, kwa sababu kuna asilimia maalum huwa inapangwa kwenye mradi huu.

Mheshimiwa Spika, tayari tumesha-practice katika Mkoa wa Katavi, Manyara na Mikoa mingine. Tumeona tayari zipo shule, yapo maji safi, zipo zahanati zilizojengwa kutokana na asilimia ya mradi huu. Ninakushukuru. (Makofi)
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, tunamshukuru sana Waziri kwamba tumepata mradi wa maji katika Kata ya Mabogini. Lakini baada ya manunuzi ya vifaa havijatosha kufikisha maji Umasaini eneo la Remiti. Je, Serikali ina mpango gani wa kutusaidia?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya, lakini kikubwa nataka nimhakikishie maeneo yote ambayo panaishi watu na wanahitaji maji Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan imetoa maelekezo kuhakikisha tunawafikishia maji na wananchi waweze kupata huduma hii muhimu sana ya maji.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika,
ahsante sana kwa kunipa fursa; je, Serikali ina mpango gani kuboresha mawasiliano ya simu ya katika Kata za Urushimbwe, Kibosho Kati na Mabogini, zilizopo katika Jimbo la Moshi Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya katika wananchi wake wa Jimbo la Moshi, lakini vilevile katika kata ambazo amezitaja Urushimbwe, Kibosho Kati pamoja na Mabogini, tayari tumeziingiza kwenye mradi wa Tanzania kidigitali. Vilevile Mheshimiwa Mbunge wiki mbili zilizopita alifika ofisini kwetu tukakaa tukaongelea kuhusu suala la kata hizi tatu na alihakikisha kabisa kwamba tayari tumeshaziweka kwenye utekelezaji wa mradi wa Tanzania kidigitali. Nakushukuru sana.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa. Kumekuwepo na ongezeko kubwa la kima, ngedere na nyani kwa vijiji vinavyopakana na Mlima Kilimanjaro na wanyama hawa wamekuwa wanasababisha uharibifu mkubwa sana wa mazao ikiwa ni pamoja na kula kuku na kusababisha umaskini.

Je, Serikali ina mpango gani kusaidia wananchi wetu kukabiliana na changamoto hii?
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Moshi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna changamoto ya ngedere, nyani na kadhalika katika maeneo ya Mlima Kilimanjaro; lakini tumeanzisha utaratibu wa kugawa miti ambao tunatarajia kuanza ili kuwepo na upandaji wa miti katika maeneo ambayo tunaamini haya tukiweza kuyazuia na kuyahifadhi vizuri basi wanyama hawa wataweza kuishi maeneo salama zaidi kuliko ilivyo sasa ni kweupe zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa wakati huo huo tulishaahidi kwamba hawa ngedere tutatafuta namna ya kwenda kuwapunguza na kupeleka katika maeneo mengine ya hifadhi. Hilo nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutalitekeleza. Ahsante.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa. Wananchi wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka Mlima Kilimanjaro hushindwa kuripoti changamoto za kiusalama kule mlimani kama kukata miti na moto kutokana na uhaba au uhafifu wa mawasiliano. Je, Serikali ina mpango gani kusaidia kuboresha mawasiliano katika vijiji vinavyozunguka Mlima Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Profesa Ndakidemi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hii changamoto kweli tumeiona, sometimes unafika wakati kunatokezea majanga ya moto na mambo mengine, wananchi wanashindwa kuweza kutoa taarifa na sisi kama Serikali tukachukua hatua kwa wakati. Nimuambie tu Mheshimiwa kwamba hili jambo tunalichukua na tunakwenda kulifanyia kazi ili matukio yakitokea tuhakikishe kwamba sisi yanatuletea taarifa mapema na tunayachukulia hatua zinazofaa kwa mujibu yaani kwa wakati unaohusika.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa. Swali la kwanza; je, Serikali ina mpango gani wa kufungua VIP route ya Kibia ambayo hupeleka watu maalum kupanga Mlima Kilimanjaro ili tuweze kupata fedha za kigeni kama ambavyo tume-plan.

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili mti mrefu kuliko yote Barani Afrika wenye mita 81.5 upo katika msitu wa Mlima Kilimanjaro katika Kijiji cha Pema, miundombinu ya kufika katika eneo hili na mazingira ya eneo hili ni mabaya. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha eneo hili ili tuweze kupata fedha za kigeni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Profesa Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba tu nimtaarifu Mheshimiwa Profesa Patrick pamoja na wananchi wa Moshi kwamba kwa sasa hivi tayari Wizara imeshaanza ukarabati wa lango hili la VIP route ambapo lipo takribani asilimia sabini na kwa sasa tunatafuta Wawekezaji kwa ajili ya kujenga huduma za malazi na chakula. Pia kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024, tutajenga lango kuu linalopitia katika hiyo VIP route ambayo itawasaidia wageni kuingia katika Hifadhi ya KINAPA.

Mheshimiwa Spika, kwenye suala hili lingine mti mrefu zaidi hapa Afrika tumeshaanza kutenga kutenga fedha kwa ajili ya kuweka miundombinu sahihi katika eneo hilo ili Wataliii waweze kufika kwa urahisi. Kwa hiyo, kwa bajeti hii ambayo itapitishwa na Bunge lako hili tunatarajia kwamba zoezi hili litaanza kwa mwaka wa fedha unaokuja, ahsante. (Makofi)
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara ya Kibosho Shine, Kwa Raphael hadi International School kwa kiwango cha lami kwani ni kipande kidogo kimebakia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema kipande kilichobaki kidogo nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua kazi kubwa imeshafanyika na tunatafuta fedha kuweza kukikamilisha hicho kipande kilichobaki cha barabara ili wananchi waweze kupata huduma ambayo imekusudiwa na Serikali. Ahsante.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini Serikali itakuja na bei elekezi ya kuunganisha maji nchi nzima kama ilivyo kwenye umeme?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, Profesa Ndakidemi kuhusu bei elekezi nchi nzima kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, uunganishaji wa maji tunazingatia umbali kwa sababu ya mabomba na miundombinu ambayo inatumika. Tunaangalia kutokea kwenye main line kuja kwa wewe mtumiaji pale ulipo ndivyo ambavyo gharama inakwenda.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuniona. Je, Serikali ina mpango gani kujenga au kuboresha vituo atamizi katika vyuo vyetu vikuu au taasisi za elimu ya juu, kwani hivi vituo ndio chachu ya kutengeneza viwanda hapa nchini?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Ndakidemi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kwamba vituo atamizi ni muhimu sana kwa ajili hasa ya kuunganisha juhudi za taaluma na maendeleo ya viwanda na maendeleo ya nyanja nyingine mbalimbali hapa nchini, nguvu kubwa tunazielekeza huko. Naamini hata baadhi ya Wabunge watakuwa wamepata fursa ya kuangalia wiki ya ubunifu ambayo inaendelea kwenye viwanja vya Jamhuri leo na juhudi ambazo tumezifanya na baadhi ya matokeo ambayo tayari tumeshazifanya. Kwa hiyo, tunalichukulia suala hili kwa umuhimu mkubwa na tutajitahidi sana kuongeza juhudi ya kuwa na vituo vyakutosha atamizi katika vyuo vikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kesho tunazindua Industrial Advisory Council ya Sokoine ambayo vilevile ni kwa ajili ya kuunganisha juhudi za maendeleo ya viwanda na Chuo Kikuu cha Sokoine na vyuo vingine vyote hapa nchini.
MHE. PROF. PATRICK ALOIS NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika,
Nakushukuru kwa kunipa tena fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Je Serikali ina mpango gani wa kushirikisha jamii ya vijiji vyote vinavyozunguka mlima Kilimanjaro ili kutunza rasilimali ambazo zipo katika mlima huo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Maporomoko ya Materu au Materu water falls iliyopo katika mto Kware katika viunga vya Mlima Kilimanjaro ni kivutio kikubwa cha watalii;

Je, Serikali ina mpango gani kusaidia juhudi za wananchi katika kuboresha maporomoko hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa
Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Patrick Alois Ndakidemi Mbunge wa Moshi Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, namna gani tunaweza tukawashirikisha wananchi; Ushirikisho wa kwanza ni kuendelea kuwapa elimu, kwa sababu tunaamini kwamba moja ya miongoni mwa mambo ambayo yanaweza yakahifadhi hili eneo au yakatoa huo ushirikiano wa kuwashirikisha wananchi au wanakijiji ni kuendelea kuwapa taaluma.

Mheshimiwa Spika, lakini cha pili ni kuanzisha na kuendeleza vikundi shirikikishi. Vikundi ambavyo vitasaidia katika kulinda haya maeneo. Lakini kingine, tumeona moja miongoni mwa njia ya kuweza kunusuru maeneo haya ni kuhakikisha kwamba tunawasisitiza wananchi wanaendelea kupanda miti kwa wingi. Kikubwa zaidi tunaendelea kuwaomba wananchi wa maeneo yale waache kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo yale ya Mlima Kilimanjaro, zikiweno shughuli za Kilimo, shughuli za ukataji miti lakini mwisho wa siku wanakwenda kuchoma miti pale na hatimaye inapelekea majanga makubwa. Kwa hiyo hiyo ni sehemu kubwa ambayo tumeichukua kama hatua ya kuwashirikisha wanakijiji.

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili katika suala la kuboresha na kutunza hichi chanzo cha maji cha Materu Water Falls, cha kwanza tunaendelea kutoa elimu kama kawaida yetu kwa sababu tuna amini elimu ndiyo itakayokitunza kile chanzo. Cha pili tumesisitiza watu waendelee kuipanda miti pale kwa sababu kisayansi miti ile ndiyo inayokwenda kuvuta mvua ile na tayari kile chanzo kina imarika. Kikubwa tunaendelea kusisitiza Wananchi wasifanye shughuli za kibinadamu kwenye maeneo ya vyanzo vya maji mwisho wa siku wanaharibu hivyo vyanzo.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Katika bajeti hii tunayomalizia ya 2022/2023 Serikali ilikuwa imepanga kujenga minara ya mawasiliano katika Kata za Urushimbwe, Mabogini na Kibosho Kati. Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusiana na ujenzi wa minara hii?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Profesa Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kulikuwa na changamoto hii na Mheshimiwa Mbunge, aliwasilisha changamoto hii mara kwa mara lakini Serikali ilijitahidi sana kutafuta fedha na hatimae Mheshimiwa Rais, ametoa fedha na tunakwenda kuingia mkataba na kampuni ya Vodacom na TIGO kwa ajili ya Urushimbwe, Mabogini pamoja na eneo la Kibosho kati. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, baada ya Bunge hili tuna uhakika kwamba kati ya Mwezi wa Sita au wa Saba tayari ujenzi wa mnara huo utaanza rasmi.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa fursa. Nina maswali mawili ya nyongeza. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na kwamba mmeanza kugawa miche ili tuboreshe uzalishaji wa Kahawa. Kwa kuwa mmegawa miche; je, sasa Serikali ina mikakati gani ya kuboresha zile skimu za umwagiliaji za asili ili tuweze kuongeza tija kwenye kuzalisha kahawa, kwani bila maji hata hiyo miche haitakuwa inafanya vizuri sana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Je, Serikali ina mkakati gani wa kusindika kahawa aina ya Arabica kwa sababu kahawa hii ina soko zuri sana katika soko la Dunia na kuna teknolojia nyingi za kawaida tu ambazo zinaweza zikatumika tukapata chapa au brand yetu: Je, Serikali ina mkakati gani wa kutusaidia kusindika kahawa hizi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza la kuhusu skimu za umwagiliaji wa mifereji ya asili, tunao wakandarasi ambao wako katika Mkoa wa Kilimanjaro, wanaotekeleza miradi ya umwagiliaji, wameshapata maelekezo watakwenda kukarabati na kujenga mifereji yote ya asili inayogusa jimboni kwa Mheshimiwa Ndakidemi, kwa Mheshimiwa Saashisha pamoja na kwa Mheshimiwa Dkt. Kimei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, Serikali inao mkakati wa dhati kabisa kuhakikisha kwamba tunaendelea kusindika kahawa yetu na tusiuze kahawa ambayo haijasindikwa. Hivi sasa Bodi ya Kahawa imeshatoa zaidi ya leseni 20 kwa ajili ya wasindikaji ili kuchochea usindikaji wa zao la kahawa na mwisho wa siku tutengeneze masoko ya uhakika. Hivi sasa tumepata nafasi kahawa yetu inauzwa sana na kupekekwa Japani ikiwa ni sehemu ya kazi nzuri ambayo imefanywa katika hatua ya awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, kazi hii inaendelea.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha bei ya zao la kahawa kwa wakulima wanaolima kahawa aina ya Arabika na Robusta? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Prof. Ndakidemi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli moja ya maeneo ambayo Serikali inaangalia kwa ukaribu sana ni kuona namna gani tunaboresha bei ya mazao ya kilimo ikiwemo Kahawa katika nchi hii. Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunaendelea kuongeza uwekezaji. Mosi, uwekezaji wa viwanda vya kuchakata zao la Kahawa. Pili, kuona tunafungua masoko ili wananchi hawa ambao wanazalisha, hata wale ambao hawajaongeza thamani waweze kuuza popote. Kwa hiyo, maana yake kupitia hiyo najua bei yake itaongezeka kwa sababu mahitaji yatakuwa makubwa kwa hiyo bei nayo itapanda. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa.

Je, Serikali ina mkakati gani kukamilisha barabara ya Kiboroloni – Kichudini mpaka Kidia, kwa sababu barabara hii itakuwa inapandisha watalii kupitia Lango la Kidia. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara hii ya Kiboroloni sasa hivi inasimamiwa na TANROADS kupitia Meneja wa Mkoa na imepangiwa fedha ya maendeleo kwenda kwa awamu. Sasa pengine tutaangalia ukubwa wake ili kama inawezekana tuweze kuongeza fedha ili kipande kile kidogo kilichobaki kiweze kukamilika na ijengwe yote kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana; je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha lango la kuingia Mlima Kilimanjaro la Kidia kwani lango hili litakuwa linatumiwa na watu maarufu kupanda Mlima Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, sekta ya utalii ina mchango mkubwa katika kuongeza mapato katika nchi yetu. Kwa hiyo, ni makusudio ya Serikali kuboresha malango katika hifadhi zetu zote za Taifa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, katika hili la Kidia, tayari Serikali inaendelea na kuboresha eneo lile. Tayari tunavyozungumza barabara ya kilometa karibu 28 ya watembea kwa miguu kwenye eneo lile imeboreshwa. Barabara karibu kilometa tisa inajengwa kwa kiwango cha changarawe na katika bajeti ya mwaka huu kupitia TANAPA zimetengwa karibu milioni mia tisa kwa ajili ya kujenga mageti kwenye eneo hilo.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri yenye matumaini kutoka Serikalini na nina hakika wananchi wangu wa Mabogini na Kahe watakuwa wamepata faraja kubwa sana. Pamoja na hayo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza tunaishukuru Serikali ilitenga shilingi milioni 475 kutengeneza barabara ya TPC, Samanga hadi Chemchem lakini tamanio la wananchi hawa ilikuwa ni kutengeneza daraja kwenye mto Ronga unaounganisha vijiji vya Samanga na Chemchem.

Je, Serikali ina mpango gani kutengeneza daraja hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili barabara ya International School Kibosho KNCU hadi kwa Raphael haijakamilika kwa kiwango cha lami.

Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa barabara hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya Profesa Ndakidemi, kwanza ni hii barabara ya Samanga – Chemchem kuhitaji daraja katika mto unakopita.

Kwanza kama alivyosema yeye mwenyewe Mheshimiwa Mbunge Serikali ilitenga shilingi milioni 475 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii na tutaangalia katika bajeti tunayoenda kuanza hii ya TARURA ya mwaka 2023/2024, kuona imetengewa kiasi gani kwa ajili ya ujenzi wa daraja hili na tutamwelekeza Meneja wa TARURA Mkoa wa Kilimanjaro kuweza kuelekeza fedha mara moja kwa ajili ya ujenzi wa daraja hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili hili la International School hadi Kibosho barabara hii. Serikali itaendeleza ujenzi wa barabara hii kadri ya upatikanaji wake wa fedha na tutaangalia Mheshimiwa Mbunge katika bajeti hii inayokuja kuona ni namna gani ambavyo tunaweza tukatenga fedha kwa ajili ya kwenda kuanza ukarabati wa kiwango cha lami kwenye barabara hii.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa. Je, Serikali ina mkakati gani wa kukamilisha barabara ya Kibosho Shine hadi kwa Rafael kwa kiwango cha lami?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Prof. Ndakidemi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara aliyoitaja ya Kibosho Shine kwenda kwa Rafael ina hudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania lakini kuna kipande ambacho pia kinahudumiwa na wenzetu wa TARURA. Kwa upande wa barabara ambayo kwa sasa inahudumiwa na TANROADS ni mpango wetu kuhakikisha kwamba tunaijenga yote kwa kiwangio cha lami, na hadi sasa mkandarasi yuko site. Na katika mwaka unaokuja pia tumetenga fedha kuendelea na ujenzi kwa awamu kwa kiwango cha lami ili kuikamilisha barabara yote hiyo kuijenga kwa kiwango cha lami.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa. Serikali imepeleka Polisi Kata kwenye kila Kata katika nchi hii kwenye rank ya inspector, lakini mapolisi hawa hawana ofisi wala makazi kwenye haya maeneo. Je, Serikali ina mpango gani kuwapelekea vijana wetu hawa kuwajengea Ofisi na nyumba za kuishi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni kweli tunatambua kwamba kuna baadhi ya Ofisi zimekuwa zimechakaa kwa sababu ni za muda mrefu, lakini vilevile tunatambua kwamba kuna maeneo mengine hata hizo Ofisi zinakuwa changamoto, lakini nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutajitahidi, kama ambavyo tumejibu katika majibu yetu ya msingi, tutajitahidi kuhakikisha kwamba kila mahali wanapata Vituo vya Polisi, lakini kila mahali wanapata nyumba za makazi kwa ajili ya Askari Polisi, nakushukuru.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa. Je, Serikali ina mpango gani wa kuendelea kugawa miche bora ya kahawa yenye ukinzani dhidi ya magonjwa sugu ya kahawa kwa wakulima wa Jimbo la Moshi Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mibuni tuliyonayo asilimia kubwa imeshakaa zaidi ya miaka 25 na hivyo kupunguza uzalishaji, hivi sasa Serikali kupitia TAKRI na wadau wengine kama bodi ya kahawa tutahakisha kwamba tunazalisha miche ya kutosha na hasa kupitia teknolojia ya chupa ili wakulima wengi zaidi wapate miche iwafikie kwa urahisi na waweze kuongeza uzalishaji ikiwemo wa kulima wa jimboni kwa Mheshimiwa Prof. Ndakidemi.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa.

Je, Serikali ina mpango gani kusaidia wagonjwa wanaohitaji viungo bandia kama vile miguu bandia, kwani gharama zake ziko juu sana kwa mgonjwa wa kawaida. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, alichokisema Mheshimiwa Ndakidemi ni kweli na kuna tatizo hilo na ndiyo maana bado tulikuwa tunasisitiza, mwarobaini wa tatizo hili la uwezo wa kulipia tiba ni Bima ya Afya kwa wote hilo ndiyo la kwanza. Kumekuwepo na utaratibu wa Serikali kusaida Watanzania wasiojiweza, wale ambao watathibitika hawana uwezo wa kujilipia basi kuna utaratibu unakwenda kwa Mtendaji wako wa Kata anaandika barua na kuna social welfare kwenye hospitali zetu wanazipitia basi anapata exemption anaweza kuhudumiwa. (Makofi)
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa. Tunaishukuru sana Serikali kwa kutujengea Kituo cha Afya cha Uru Kusini na kinakaribia kinakamilika;

Je, Serikali ina mpango gani kupeleka vifaa na wahudumu ili wananchi waanze kupata huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika mwaka huu wa fedha 2022/2023 imeajiri watumishi wa afya wapatao 8,000 ambapo wengine watapangiwa katika Halmashauri ya Moshi Vijijini anapotoka Prof. Ndakidemi kule. Lakini vile vile katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imeweka kwenye bajeti shilingi bilioni 112 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba. Vitakapo nunuliwa tutahakikisha na Moshi Vijijini napo kwa Mheshimiwa Profesa Ndakidemi nao wanapata vifaa tiba hivi.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na niishukuru Serikali kwa majibu ya kutia moyo. Nina maswali mawili ya nyongeza: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kaya nyingi kule Uchaggani na maeneo mengi ya Tanzania, kaya zote zina wanyama kama vile ng’ombe, mbuzi na kondoo: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwekeza kwenye gesi endelevu kwa mfano tupate nishati ya kupikia na kuwasha taa kutoka kwenye kinyesi cha wanyama ili kuzuia matumizi ya kuni?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; je, Serikali haioni umuhimu wa kuhamasisha wananchi watumie majiko bunifu na mikaa ya tofali inayotokana na pumba za mpunga na masalia mengine ya mimea ili kupunguza matumizi ya kukata miti na kuwapatia wananchi nishati?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Profesa Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mheshimiwa Prof. Ndakidemi, kwa ufuatiliaji wa eneo hili ambalo ni eneo jipya ambalo Serikali imetilia mkazo kuhakikisha kwamba tunatumia nishati safi, hasa ya kupikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali yote mawili kwa pamoja kwa kutoa maelezo yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mwaka jana Mheshimiwa Rais alizindua mjadala wa Kitaifa wa nishati safi ya kupikia, na ni azma ya Serikali kupitia Wizara ya Nishati, mmeona tukijikimu kuelekea sasa kwenye nishati safi ya kupikia. Na katika eneo hili tunahamasisha utumiaji wa gesi ya mitungu, lakini gesi asilia, lakini pia maeneo mengine waliyoyasema ya kutumia biomass, kwa maana vinyesi vya wanyama, na mikaa hii ambayo ni ya kutengeneza ambayo haitoi moshi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Nishati kupitia REA inawezesha na ku-facilitate wale wagunduzi na watengenezaji wa majiko banifu na hii mikaa ya asili, kama mlivyotembelea mabanda yetu mliwakuta pale wabunifu wa namna hiyo. Kwenye Serikali itakuwa siyo rahisi sana kutumia nguvu ya Serikali kuzalisha umeme au gesi ya kupikia kwa pesa ya Serikali kutumia vinyesi vya wanyama na maeneo mengine. Kwa hiyo, Serikali inatoa pesa lakini pia tunapata mifuko mingine kama Green Fund ambayo ina-facilitate wananchi na wawekezaji binafsi katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Prof. Ndakidemi kwamba tutaendelea kusimamia eneo hili kuhakikisha kwamba tunawawezesha wananchi na kuwapa fedha za mitaji ili waendelee kupata vitendea kazi vya maeneo hayo kuweza kuzalisha gesi asilia na kuweza kutumika katika kuwasha umeme, lakini pia katika nishati safi ya kupikia. (Makofi)
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa. Je, Serikali ina mkakati gani kusaidia wabunifu kuhatamia teknolojia zao au ku-incubate wakati wakijiandaa kuanzisha viwanda vidogo vidogo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa kaka yangu, Profesa Ndakidemi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimejibu katika majibu yangu ya nyongeza kwenye maswali yaliyopita kwamba, katika kipindi cha miaka minne iliyopita Serikali ilianzisha mashindano ya MAKISATU ambayo tulianza mwaka 2019 na mwaka huu sasa ni awamu ya nne. Katika mashindano haya zaidi ya bunifu elfu moja mia saba na themanini na kitu yaliweza kuibuliwa na zaidi ya bunifu 200 zimeweza kuendelezwa au kuatamiwa na zaidi ya bunifu 26 tayari zimeshapelekwa sokoni, sasa kitu gani tunachofanya?

Mheshimiwa Spika, baada ya kuwapata hawa wagunduzi au wabunifu tunawapeleka kwenye zile hub zetu, tuna center mbalimbali nchini kote ambazo zinawalea na Serikali sisi tumeweza kupeleka fedha katika maeneo haya. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tumeweza kupandisha bajeti ya kuwalea hawa wabunifu wetu kutoka bilioni 3.0 mpaka bilioni 9.0 katika mwaka ujao wa fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali tayari imeshafanya eneo leke na katika kipindi hiki hizi bunifu tulizozipata katika mashindano haya yaliyopita, zaidi ya milioni 700 tumeshazipeleka tayari kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, hawa tunakwenda kuwaendeleza ili bunifu hizi ziende kuwa biashara na bidhaa ambayo tunaweza tukaipeleka sokoni.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa, Kata za Kibosho, Kilima, Kibosho Kati, na Kibosho Magharibi katika Jimbo la Moshi Vijijini lina tatizo la low voltage.

Je ni lini Serikali itatusaidia kutatua changamoto hii kwa sababu umeme uwa unawake kuanzia saa tano usiku?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Moshi Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa katika Mkoa wa Kilimanjaro na Wilaya ya Moshi Mjini na Moshi Vijijini kumekuwa na changamoto ya kufifia kwa umeme na nguvu ndogo ya umeme na Serikali imelibaini hilo na ndio maana imeanzisha programu kubwa kabisa ya National Grid Stabilization Project. Na maeneo haya ya Kata alizozitaja Mheshimiwa Mbunge yamo katika miradi ya kuimarisha Gridi ya Taifa. Kwa hiyo napenda nimpe faraja, na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutatekeleza mradi wa kuimarisha upatikanaji wa umeme katika kata zake za Jimbo la Moshi Vijijini.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa. Hospitali mpya ya Wilaya ya Mabogini imeshaanza kutoa huduma, je, Serikali ina mpango gani kupeleka umeme katika Hospitali yetu hii mpya?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Hospitali ya Mabogini tayari tumeshaifanyia tathmini na tupo katika mchakato wa kupata fedha ili ifikapo Januari, 2024 tuweze kuhakikisha Hospitali hii ambayo tayari inafanya kazi iweze kupatiwa umeme wa uhakika, ahsante. (Makofi)