Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Eng. Kundo Andrea Mathew (7 total)

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Mbulu Vijijini tumepata minara sita ambayo imejengwa. Mwingine umejengwa 2017, mingine inayofuata imejengwa mpaka juzi hapa lakini sasa minara hii sita haifanyi kazi.

Je, Mheshimiwa Waziri ana mpango kuwafuata au kuwaona wakandarasi ili wawashe minara hii sita ambayo sasa wananchi wanaisubiri mpaka leo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa amesema kata hizi atazipelekea mawasiliano na kujenga minara; je, kata zilizobaki lini zinakwenda kupata hiyo minara ambayo amekwishaisema?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kulingana na changamoto ambayo ilikuwepo ya masuala ya ujenzi, kata hizo zilikuwa zimechelewa kukamilishiwa miradi hiyo. Hata hivyo, hivi navyoongea wataalam wetu tayari wameshaanza kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia naomba kutumia fursa hii kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna hatua mbili katika ujenzi wa minara; kuna hatua ambayo inatokana na ujenzi wa mnara wenyewe ambao tunaita passive equipment na hatua ya pili ambayo sasa ni kuweka vile vifaa ambavyo tunaita kwamba ndiyo active equipment.

Mheshimiwa Naibu Spika, vifaa hivi tumekutana na changamoto ya wakandarasi wetu ambao walikuwa wamepewa majukumu ya kukamilisha miradi hii kwa sababu wanatumia sana vifaa kutoka nje na mwaka jana tulikumbana na changamoto ya Corona, hivyo tukaona kwamba tuwaongezee muda ili waweze kukamilisha ujenzi wa minara hii. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, suala hili tayari tunalifanyia kazi na hizi kata ambazo amezisema tayari wataalam wetu wameshafika site kwa ajili ya kujua nini kinafanyika ndani ya muda ambao unatakiwa. Ahsante sana.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nami naomba kuuliza Wizara ya Mawasiliano swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuwa vijiji vitatu katika Kata ya Ziginali, Kisawasawa na Kiberege havina mawasiliano ya simu kabisa. Je, ni lini Serikali itawasaidia wananchi hawa huduma ya mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilijibu katika majibu yangu ya msingi, ni kwamba Serikali iko katika mpango wa kufanya tathmini katika Kata nyingine 1,392 ambazo zimebaki Tanzania Bara ili tuweze kuona namna gani tutaziingiza katika Mpango wa Utekelezaji katika Bajeti ya 2020/2021. Hivyo namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, sambamba na hilo tutahakikisha kwamba tunawasiliana naye kwa ukaribu sana ili kujua changamoto ziko katika maeneo gani ili tuhakikishe kwamba mawasiliano katika Kata hizo yanafika kwa ukamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Tatizo lililopo katika Jimbo la Mbulu Vijijini ni sawa kabisa na changamoto iliyoko katika Jimbo la Kalenga. Kata ya Kihanga, Ulanga, Ifunda katika Vijiji vya Mibikimitali na Kata ya Mgama iliyoko katika Vijiji vya Lupembewasenga, kuna changamoto ya mawasiliano.

Je, ni lini sasa Serikali itahakikisha wananchi hao wanapata huduma hiyo ya mawasiliano ili waweze kufanya shughuli zao za kawaida?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto tuliyonayo kwa sasa, labda nitoe maelezo kidogo. Ni kwamba kuna baadhi ya sehemu ambazo mawasiliano au minara ilipelekwa ambapo uhitaji wake inawezekana walikuwa watu 5,000 ambao walikuwa wanaweza kutumia huduma hiyo. Kwa sababu ya ongezeko la watu katika eneo husika, kwa hiyo, ile minara yetu inashindwa kuwa na uwezo wa kuhudumia watu wengi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, kwa kugundua hilo, tumeagiza mobile operator wote wafanye tathmini, wafanye research za kutosha ili waongeze uwekezaji katika maeneo hayo, aidha kwa kuongeza minara au kwa kuongeza capacity katika minara ambayo tayari ipo katika maeneo husika ili kuhakikisha kwamba wananchi wote wanafikiwa na mawasiliano hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini nina swali la nyongeza ambalo lina vipengele viwili.

Mheshimiwa Spika, kwanza, katika Kata ya Uru Shimbwe kuna shida kubwa sana ya huduma ya mawasiliano ya Radio hasa kwa Redio yetu ya Tanzania na Television yetu ya Taifa. Pili, kuna shida ya huduma ya internet na imesababisha Kata ya Uru Shimbwe ishindwe kutuma taarifa kupitia kwenye zahanati yetu kwenye Shirika la Bima la Afya. Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba huduma hizi zinaboreshwa kwenye eneo la Uru Shimbwe?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Patrick Alois Ndakidemi Mbunge wa Moshi Vijijini kwa sababu masuala haya tumekuwa tukiwasiliana na jiografia ya eneo husika tayari ameshanieleza jinsi ilivyo. Hata hivyo, kupitia mpango wa Serikali wa kuhakikisha kwamba tunafikisha huduma za mawasiliano vijijini zikiambatana na usikivu wa redio katika maeneo husika tayari Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeshaanza kufanya tathmini katika maeneo husika.

Mheshimiwa Spika, vilevile katika eneo ambalo ameongelea kuhusu upatikanaji wa data, Serikali tayari imeshatoa maelekezo kwa watoa huduma wote, sehemu yoyote ambapo tutapeleka mradi wowote ule, lazima mradi huo ukajengwe wa kutoa huduma ya kuanzia 3G maana yake ni kwamba, ni lazima sasa Tanzania tutakuwa na miradi au minara ambayo itakuwa inatoa huduma ya internet. Nasema hivyo kwa sababu hapo kabla tulikuwa tunaangalia tu angalau kila Mtanzania aweze kupata mawasiliano, lakini kwa sasa tunalazimika kwa sababu ya mahitaji ya kuelekea kwenye digital transformation maana yake kwamba mahitaji ya internet ni makubwa zaidi ikiambata na eneo la Mheshimiwa Patrick, Moshi Vijijjini. Nashukuru.
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote una jukumu kubwa la kuboresha mawasiliano hususan kwenye sehemu za vijijini ambazo hazina mawasiliano ya simu ya kutosha, lakini juzi juzi tumeshuhudia hapa Mfuko huu ukizindua studio za kisasa za TBC wakati bado kuna sehemu hususan za vijijini hazina mawasiliano ya simu ya kutosha.

Mheshimiwa Spika, nataka kujua ni nini hasa vipaumbele vya Mfuko wa huu wa Mawasiliano kwa Wote?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Zaytun Swai, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa ni jukumu la Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kuhakikisha kwamba tunafikisha mawasiliano maeneo ya vijijini, lakini sio maeneo ya vijijini peke yake maeneo yote ambayo hayana mvuto wa kibiashara, kwa sababu kuna maeneo ambayo watoa huduma wengine hawawezi kwenda kuwekeza kwa sababu zao za kibiashara.

Mheshimiwa Spika, vilevile tunapoongelea kufikisha mawasiliano ni pamoja katika maeneo ambayo ni ya mipakani. Pamoja na maeneo ya mipakani, kuna maeneo ya hifadhi, kuna maeneo ambayo kwa kweli ukiangalia katika ramani vizuri ni kwamba hakuna wakazi wengi, lakini hao wakazi waliopo pale wana haki ya kupata huduma ya mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo, kwa sababu huduma ya mawasiliano tunaichukulia kama ni sehemu ya usalama, sehemu ya huduma ya msingi ya kila Mtanzania na kubwa zaidi ni uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu mawasiliano yanaenda kuwa moja ya njia kuu ya uchumi wa nchi yetu. Hivyo Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote utaendelea kufanya tathmini katika maeneo yote ambayo bado yamebaki nyuma kimawasiliano ili yaweze kufikishiwa mawasiliano. Nakushukuru sana.
MHE. AMINA ALI MZEE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, hatua zipi zinachukuliwa na Serikali kuwawezesha vijana wanaofanya biashara mtandao ili kuwezesha mapato ya Taifa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu na mikopo ili kuwezesha upatikanaji wa ajira ya ndani na nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Serikali kazi yake ni kuhakikisha kwamba inaweka mazingira wezeshi kwa vijana ili waweze kufanya biashara hiyo. Sambamba na hilo kupitia biashara zozote za kimtandao Serikali imeweza kurasimisha shughuli hizo kwa kuanzisha sheria ya makosa ya kimtandao maana yake kwamba kijana ili aweze kujua mipaka ya namna gani biashara yake akaifanye.

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta ya Mwaka 2010, hii yote inatoa guidelines za namna gani kijana anaweza kuingia katika biashara hiyo.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo kwa sababu unapofanya biashara lazima kuna transactions zitakuwa zinafanyika, ili sasa kumlinda katika zile transactions Serikali pia ilichukua jukumu la kuanzisha Sheria ya Miamala ya Kieletroniki ambayo sasa transaction yoyote inakuwa inatambulika, anapokuwa anafanya hizi biashara.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo kupitia Wizara yetu kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia vijana hawa, Serikali ina mpango mzuri wa kutoa elimu ambapo vijana watakuwa wanajua namna gani na sehemu zipi wanaweza kuwa wanapata mikopo kwa ajili ya kujiongezea kipato na hatimaye tunaongeza pato la Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza, nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri, kwa kweli nimehakikisha mwenyewe kwamba kazi inaendelea.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kama unavyojua jiografia ya Wilaya ya Lushoto ni ya milima na mabonde ambayo husababisha kutopata huduma katika maeneo mbalimbali hasa Makanya, Mavului, Mbwei na maeneo mengine ya Mazumbai. Je, ni lini sasa Serikali itaenda kujenga minara ile ili kuondoa kadhia wanayoipata wananchi wa Wilaya ya Lushoto?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Wilaya ya Lushoto ina changamoto ya usikivu wa Radio ya Taifa yaani TBC na hili suala nilikuwa naliongelea mara kwa mara lakini mpaka leo hii hakuna majibu yoyote wala hakuna mnara wowote uliojengwa. Je, ni lini Serikali itaenda kujenga minara ya habari ndani ya Wilaya ya Lushoto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hatua ambazo Serikali inazichukua kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kwanza kabisa ni kujiridhisha na ukubwa wa tatizo wa eneo husika. Ukubwa huo unaweza ukategemea na tatizo lenyewe, inawezekana katika maeneo fulani mawasiliano hakuna kabisa; maeneo mengine mawasiliano ni hafifu; lakini kuna maeneo mengine ambapo unakuta kwamba mawasiliano yako hapa hayako hapa; kunakuwa na dark sport za kutosha. Sasa Serikali inapofanya tathmini ni kujiridhisha pia na ukubwa wa tatizo ili kujua teknolojia gani ambayo tunaweza kwenda kuitumia pale ili kutatua tatizo la eneo husika kulingana na tathmini iliyofanyika.

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri tumekuwa na mawasiliano mazuri na amekuwa akiwapambania kweli wananchi wa Jimbo lake na sisi kama Serikali kwa sababu ndio jukumu letu na kupitia Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi, ibara ya 61(f) na (g) inaeleza kabisa kwamba ni jukumu la Serikali kwenda kufikisha mawasiliano kwa wananchi wote, kwa hiyo, suala lake litaangaliwa baada ya tathmini kufanyika.

Mheshimiwa Spika, vilevile suala la usikivu ni jambo lilelile ambalo pia kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wanaendelea na kufanya tathmini katika maeneo yote pamoja na maeneo ya mipakani kuhakikisha kwamba palipo na changamoto ya usikivu basi Serikali inafikisha mawasiliano katika maeneo husika.