Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Paschal Katambi Patrobas (61 total)

MHE. COSATO D. CHUMI Aliuliza:-

Kituo cha Uwekezaji (TIC) kinampa haki mwekezaji kuajiri wataalam lakini upande wa pili sheria inampa mamlaka Kamishna wa Kazi kufanya maamuzi kuhusu maombi ya vibali vya kazi:-

Je, ni lini Serikali italeta marekebisho ya sheria ili kuondoa mgongano huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuzungumza katika Bunge hili, naomba nichukue fursa hii pia kuwashukuru sana wananchi wa Shinyanga ambao walinichagua kwa kishindo. Pia nikishukuru zaidi Chama cha Mapinduzi, wakiongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi kwa ushindi wa kishindo nchi nzima usio na mashaka yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe pole kwa wananchi wa Shinyanga kwa kupotelewa na Mwenyekiti Mstaafu wa Chama cha Mapinduzi, Ndugu Erasto Kwilasa. Mwenyezi Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu, amina.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kufungua milango kuwavutia wawekezaji kuwekeza nchini. Serikali kupitia Sheria ya Uwekezaji, Sura 38 kama ilivyofanyiwa marekebisho na marejeo yake mwaka 2015 inatoa motisha mbalimbali (incentives) kwa wawekezaji. Miongoni mwa motisha hizo ni kuwaruhusu wawekezaji kuajiri wataalam wa kigeni watano, kwa lugha ya kigeni inaitwa Immigration Quota wakati wa hatua za awali za utekelezaji wa miradi yao (startup period) inapoanza kufanyika chini ya kifungu cha 24 cha Sheria ya Uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kulinda uchumi wetu, ajira za wazawa, maslahi na usalama wa nchi yetu, Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni Na.1 ya mwaka 2015 kupitia kifungu cha 5(1)(b) na 11 kinampa Kamishna wa Kazi mamlaka ya kusimamia ajira za raia wa kigeni nchini kwa lengo la kuhakikisha ajira zinazotolewa kwa wageni ni zile ambazo sifa za kielimu, ujuzi, uzoefu wa kazi ni adimu hapa nchini. Katika kutekeleza jukumu hili, Kamishna wa Kazi hupokea na kuchambua maombi ya vibali vya kazi vya raia wa kigeni kutoka kwenye kampuni/taasisi zinazohitaji kuajiri wageni wanaokidhi vigezo na masharti yaliyowekwa kwa mujibu wa sheria tajwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamishna wa Kazi ameendelea kuzingatia sheria zote, taratibu, sera na kanuni katika kufikia maamuzi yake. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge katika kupokea maoni na mapendekezo yanayolenga mabadiliko ya sheria na sera ili kuimarisha zaidi uwekezaji nchini bila kuathiri matakwa ya sera, sheria, taratibu na kanuni na miongozo iliyowekwa nchini.
MHE. HAJI AMOUR HAJI Aliuliza:-

Kwa kuwa Serikali imeruhusu uwepo wa Mawakala wa Ajira nchini:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani juu ya ajira za nje ya nchi kwa Vijana wetu?

(b) Je, ni upi mchango wa Mawakala wa ajira hapa nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Haji Amour Haji, Mbunge wa Pangawe, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuwasadia vijana wetu kupata ajira za nje ya nchi ikiwa ni pamoja na kubaini nchi za kimkakati zenye fursa za ajira za staha na kuingia makubaliano (bilateral agreement) na nchi husika; kuwajengea uwezo vijana wa Kitanzania kuwa na ujuzi utakaowawezesha kushindania fursa za ajira ndani na nje ya nchi; na kujenga mfumo wa huduma za ajira ambao pamoja na mambo mengine utarahisisha utafutaji wa kazi nje ya nchi; kuweka mwongozo wa kuratibu shughuli za wakala binafsi wa huduma za ajira wanaopeleka watu nje ya nchi; na kufanyia marekebisho Sheria ya Huduma za Ajira ya mwaka 1999 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2014 ili kuweza kuendana na mazingira ya sasa.

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Juni, 2021 Mawakala wa ajira nchini wamechangia mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, jumla ya vijana 39,273 wamepewa huduma ya ushauri nasaha (employment and career counseling). Aidha, vijana 19,509 wamepewa mafunzo ya watafutakazi, vijana 11,371 wameunganishwa na fursa za mafunzo ya utarajali na vijana 10,554 wameunganishwa na fursa za kazi ndani na nje ya nchi. Ahsante sana.
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza:-

Je, ni lini vijana wa Tanzania watapewa stadi mbalimbali za kuwaongezea ujuzi wa maarifa kupitia Mfuko wa Uwekezaji wa Wananchi Kiuchumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali, Mbunge wa Viti Maalum, Tanzania Zanzibar, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa kuwapatia vijana ujuzi wa stadi za kazi na maarifa kama hatua mojawapo ya kuwawezesha vijana kumudu ushindani katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi, Serikali kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi imetoa stadi mbalimbali za kazi kuongeza ujuzi kwa vijana kama ifuatavyo:-

(i) Jumla ya vijana 5,538 wamepatiwa mafunzo ya kukuza ujuzi kwa njia ya uanagenzi (Apprenticeship) katika fani za ufundi stadi katika nyanja mbalimbali kupitia Taasisi ya Don Bosco na Vyuo vilivyoko chini ya VETA;

(ii) Serikali imeingia mikataba na VETA kwa kushirikisha ujuzi kwa vijana katika Mikoa yote nchini katika fani za ufundi wa magari, useremala, uashi, upishi, huduma za vyakula na vinywaji, ufundi umeme, uchomeleaji vyuma, ufundi bomba, uchongaji wa vipuri na ushonaji wa nguo. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 kufikia Februari, 2021 jumla ya vijana 10,178 walikuwa wamerasimishwa na kati ya hao vijana 28 ni watu wenye ulemavu; na

(iii) Vijana wanaohitimu elimu ya juu wanaendelea kupata mafunzo ya uzoefu kazini ambapo Serikali imeendelea na zoezi la kuwashikiza wahitimu kwa waajiri. Kwa mwaka 2020/2021 hadi kufikia Februari, 2021, wahitimu 1,203 wa Vyuo vya Elimu ya Juu na Kati wamekamilisha mafunzo ya uzoefu kazini kupitia viwanda, taasisi na makampuni mbalimbali ya sekta binafsi na umma nchini. Wahitimu 2,037 wanaendelea kupata ujuzi na uzoefu katika taasisi mbalimbali ambazo ni za binafsi na za umma na kati yao, wahitimu 92 ni watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, programu zote za uwezeshaji wananchi kiuchumi zinashauriwa kuhakikisha zinawajengea wadau wake stadi za ujuzi mbalimbali kwa kuzingatia mahitaji ya programu husika.
MHE. AMINA D. HASSAN aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaondoa tatizo la ucheleweshaji wa malipo ya mafao kwa wastaafu wanachama wa NSSF?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Daud Hassan, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikihakikisha kuwa wastaafu wote wanalipwa mafao yao ya pensheni kwa mujibu wa Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini pindi wanapostaafu. Aidha, ili mstaafu aweze kulipwa mafao ya pensheni ni lazima awe amekidhi vigezo vifuatavyo:-

Mosi, awe ametimiza umri wa kustaafu kwa mujibu wa sheria, ambapo ni miaka 55 hadi 59 kwa hiari na miaka 60 kwa lazima. Pili, awe amechangia kwenye Mfuko kwa kipindi kisichopungua miezi 180 au miaka 15.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii yaani NSSF wastaafu wote wanaokidhi vigezo na kuwasilisha taarifa zote zinazohitajika hulipwa mafao ya pensheni kwa wakati pasipo kuchelewa. Mwanachama akiwasilisha maombi ya kuomba kulipwa mafao na akawasilisha nyaraka husika, mwanachama atalipwa mafao yake ndani ya siku 30. Aidha, malipo ya pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu hulipwa tarehe 25 ya kila mwezi moja kwa moja kwenye akaunti za wastaafu na hadi sasa hakuna malimbikizo yoyote ya mafao ya pensheni kwa wastaafu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha Julai, 2020 – Machi, 2021, jumla ya wanachama 93,861 wamelipwa mafao mbalimbali yenye thamani ya shilingi bilioni 377.8. Aidha, tunawasihi waajiri kuwasilisha michango ya watumishi wao kila mwezi kwa wakati na ninawasihi wastaafu kuhakikisha wanawasilisha nyaraka zote zinazotakiwa kwa mwanachama ili kuwezeshwa kulipwa mafao na kuondoa ucheleweshaji unaoweza kujitokeza katika kuandaa mafao ya wastaafu.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kukitumia kikamilifu Kitengo cha Kukuza Tija kilichopo Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi mikubwa nchini unakuwa wa tija na kuwanufaisha Watanzania?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alice Kapungi Kaijage, Mbunge wa Viti Maalum, CCM kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha Kitengo hiki kinatekeleza majukumu yake kikamilifu, Serikali imepanga kutekeleza mipango ifuatayo:-

Moja, kuandaa Sera ya Taifa ya Tija na Ubunifu (National Productivity and Innovation Policy) ambayo itaweka mfumo thabiti wa kupima tija na ubunifu katika ngazi ya taasisi, sekta na Taifa ikiwa ni pamoja na miradi mikubwa ya Kitaifa.

Pili, kuanzisha kanzidata ya makubaliano, matamko na taarifa za Kitaifa, Kikanda na Kimataifa kuhusu tija, ubunifu na ufanisi wa viwanda.

Tatu, kufanya tafiti ya tija katika viwanda vya mfano vilivyopo Mikoa ya Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani.

Nne, kuandaa na kuwezesha Wiki ya Tija na Ubunifu (Productivity and Innovation Week).

Tano, ni kuandaa na kuwezesha Mpango wa Kitaifa wa Tuzo za Tija na Ubunifu (National Productivity and Innovation Award Schemes).

Sita, kuna mpango wa kuendesha programu 24 za kuwajengea uwezo wadau juu ya dhana, kanuni na viwango vipya vinavyotakiwa katika tija, ubunifu na ufanisi wa viwanda.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano wa Tatu (FYDP III) katika kutekeleza katika sekta binafsi, imeelekeza pia sekta binafsi kushiriki katika miradi mikubwa ya Kitaifa kwa kushirikiana na taasisi nyingine ikiwemo Kitengo cha Ukuzaji Tija ili iweze kuboresha ufahamu wa sekta binafsi juu ya masuala ya ufanisi na ushindani na pia utoaji wa huduma zilizo na ubora katika jamii.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-

Wakazi wa Liwale waliathirika na vurugu za Uchaguzi wa mwaka 2020 na mali za wananchi na Serikali zilichomwa moto:-

Je, Serikali kupitia Mfuko wa Maafa ina mpango gani wa kuwafuta machozi wananchi walioathirika na vurugu hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamedi Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inakiri kupata taarifa za kutokea kwa vurugu zilizosababishwa na wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Liwale na kuleta uvunjifu wa amani, uharibifu wa vitu mbalimbali ikiwemo mali za wananchi na Serikali. Uhalifu huo umefanyika wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba, 2020 katika Jimbo la Liwale na maeneo mengine Mkoani Lindi. Aidha, Serikali ilifanya jitihada mbalimbali za kumaliza vurugu hizo kwa kutumia vyombo vya ulinzi na usalama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, kufanya vurugu za aina hii ni kosa la jinai. Hivyo, matokeo ya madhara ya vurugu hizo yatashughulikiwa kwa mujibu wa sheria zinazohusu masuala ya makosa ya jinai. Sheria ambayo inahusika kwenye masuala ya makosa ya jinai ni Sheria ya Kanuni za Adhabu (Penal Code CAP.16) ambayo imefanyiwa marekebisho mara kwa mara, lakini kwa Sheria ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2015 na Kanuni zake za utekelezaji hazina ufungamanisho wa pamoja na madai ya kijinai na hasa yahusuyo uharibifu wa mali na namna ya kulipa fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua fursa hii kuwapa pole sana wananchi wote walioathirika na kadhia hii kwa sababu si jambo zuri. Serikali pia ililipokea na kulifanyia kazi lakini tunatambua kwamba kuna uharibifu wa nyumba ambao ulifanyika, kuna uharibifu wa mali kama magari, pikipiki na vifaa vinginevyo ambapo hata timu ya mkoa tayari ilikwishakuanza kuchukua hatua za awali za kufanya tathmini ya kujua changamoto hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe wito kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Lindi kuhakikisha uchunguzi kuhusu vurugu hizo unakamilika na hivyo kulifikisha suala hilo katika vyombo vya sheria ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, napenda kuwapa pole wale wote walioathirika na vurugu hizo na kuwaomba wananchi kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili kudumisha amani na usalama nchini.
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA aliuliza:-

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuunganisha mifuko ya mikopo iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuwezesha makundi maalum kupatiwa mikopo kwa urahisi zaidi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia maelekezo yako, lakini pia kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Santiel Eric Kirumba, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ilikwishaona umuhimu na kupitia Mheshimiwa Rais iliagiza na kuelekeza mifuko kuweza kuunganishwa na kufuatia maelekezo hayo, Serikali iliunda kamati ya pamoja iliyohusisha Wizara zote zinazosimamia mifuko hiyo, kwa ajili ya kufanya tathmini ya utendaji wa mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kupima utendaji wa mifuko na programu hizo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilika kwa tathmini hiyo, mapendekezo mbalimbali yametolewa kwa ajili ya kuboresha utendaji wa mifuko na programu za uwezeshaji wananchi ikiwa ni pamoja kuunganisha baadhi ya mifuko yenye majukumu na malengo yanayoshabihiana. Taarifa ya tathmini hiyo inaendelea kufanyiwa kazi ndani ya Serikali kwa hatua zaidi ili hatimaye kuiunganisha na kuongeza tija na ufanisi.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu imekwishatekeleza agizo hilo kwa kukamilisha tathmini ya mfumo wa kiutendaji wa mifuko hiyo na baada ya kuunganishwa, mtazamo mpya wa muunganiko wa programu na mifuko husika na utekelezaji wake utaanza baada ya mamlaka kuridhia, asante.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA aliuliza: -

Je, ni kwa kiasi gani mifuko ya uwezeshaji kiuchumi iliyoanzishwa kwa lengo la kuwaondelea wananchi umasikini na kuwajengea uwezo wa kiuchumi imenufaisha wanawake wa kitanzania kutoka mikoa ya nje ya Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nitumie fursa hii adhimu kulishukuru Bunge lako la Jamhuri ya Muungano kwa kuwapa ruhusa Wabunge kujumuika nasi pale Mwanza katika tukio kubwa la Kitaifa la mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alikuwa akikutana na vijana na changamoto zote za vijana zilizungumzwa na kujadiliwa. Lakini pia alitoa mwelekeo mzuri wa Kitaifa wa namna gani tutakavyoenda kutatua changamoto hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge lakini pamoja na hilo sambamba Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuratibu vizuri shughuli hiyo lakini sambamba na hilo tunaenda kwa kweli kupitia Waheshimiwa Wabunge hawa kuwasaidia vijana wote nchi nzima hasa kwa kuwasikiliza, kuwapokea na kutatua changamoto zao katika maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini zaidi katika kufanya hivyo kwa kweli tutahakikisha kwamba vijana hawa wanapewa kila wanachostahili kwa Serikali kutengeneza mazingira wezeshi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa muda huo lakini pia sasa nitumie fursa hii kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia mwezi Desemba, 2020, mifuko na programu za uwezeshaji zimetoa mikopo, ruzuku na dhamana yenye thamani ya shilingi trilioni
4.34 kwa wajasiriamali 6,037,462. Kati ya hao, wanawake ni 3,079,105 sawa na asilimia 51 na wanaume ni 2,958,357 sawa na asilimia 49. Aidha, jumla ya ajira 10,844,589 zimetengenezwa kupitia uwezeshaji huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya wanawake 3,079,105 walionufaika na mikopo, ruzuku na dhamana kupitia mifuko na Programu za Uwezeshaji, wanawake 1,046,896 sawa na asilimia 34 wametokea Mkoa wa Dar es Salaam na wanawake 2,032,209 sawa na asilimia 66 wametokea katika mikoa mingine nje ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi litaendelea kuweka mikakati ambayo itaimarisha utendaji wa mifuko na programu hizi ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi na tija.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia watumishi waliostaafu kupata mafao yao kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ulianzishwa rasmi tarehe 1/ 8/2018 kwa Sheria Namba 2 ya Mwaka 2018. Mfuko huu ni matokeo ya kuunganisha mifuko minne ya awali (LAPF, GEPF, PPF na PSPF) ambayo ilikuwa ikihudumia watumishi mbalimbali wa Umma na kuufanya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kubaki ukihudumia sekta binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati, mipango na utekelezaji wa Serikali katika kuhakikisha watumishi waliostaafu wanapata mafao yao kwa wakati ni kama ifuatayo: -

(i) Kutengeneza mifumo mbalimbali ya TEHAMA ili kuweza kuwatambua wanachama wake na kulipa mafao stahiki pale wanapodai mafao;

(ii) Kulipa malimbikizo mbalimbali ya mafao ya wanachama yaliyopaswa kulipwa na mifuko iliyounganishwa na yale yaliyopokelewa kipindi ambacho mchakato wa kuunganisha mifuko huo ulikuwa unaendelea; na

(iii) Kuandaa ofisi mbalimbali nchini kote na kuweka misingi bora itakayowezesha utoaji wa huduma bora kwa wanachama wake ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya malipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha wastaafu wanalipwa kwa wakati, waajiri wanakumbushwa kufuata kikamilifu utaratibu ulioainishwa katika Sheria namba 2 ya Mwaka 2018 ambapo inaelekeza ipasavyo maandalizi ya taarifa za wastaafu kabla ya malipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mifuko imeendelea kuboresha mifumo yake ambapo matarajio ni kuwa waajiri nao wafuate vizuri utaratibu ulioainishwa kisheria ili kupunguza ucheleweshaji wa kulipa mafao kwa wastaafu.
MHE. ESTER A. BULAYA K.n.y. MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza ajira kwa wahitimu wa Vyuo Vikuu hasa katika sekta ya kilimo kwa kuwa mikopo ya elimu ya juu imewezesha wanafunzi wengi kuhitimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha ajira kwa wahitimu wa Vyuo Vikuu zinaongezeka hususan katika sekta ya kilimo, Serikali imetekeleza mipango ifuatayo: -

(i) Kutoa mafunzo ya kilimo cha kisasa kupitia programu ya kukuza ujuzi nchini, ambapo jumla ya vijana 12,580 katika Mikoa 17 nchini, wakiwemo wahitimu wa fani ya kilimo wamepatiwa mafunzo ya kilimo cha kisasa na sasa wapo tayari kuanza biashara ya kilimo na kutumia teknolojia na ujuzi wa kitalunyumba.

(ii) Kuwezesha wahitimu kupata uzoefu wa kazi nje ya nchi (internship), ambapo Serikali kwa kushirikiana na Ushirika wa Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUGECO), wamewezesha wahitimu 703 kwenda nchini Israeli na Marekani. Kati ya hao, wahitimu 311 wamerudi nchini na wamejiajiri katika maeneo mbalimbali nchini.

(iii) Kupitia Benki ya TADB na mikopo ya Halmashauri, baadhi ya wahitimu waliopatiwa mafunzo nje ya nchi wamepatiwa mikopo ya jumla ya Shilingi Milioni 170 na wanaendelea na shughuli hizo.

(iv) Kupitia Vituo vya Uatamizi kwa wahitimu (Incubator Centres) katika Mikoa ya Morogoro na Pwani, wahitimu 1,000 wamepatiwa mafunzo ya uanzishaji shughuli za kilimo na ujasiriamali na;

(v) Kupitia kilimo cha vizimba (block farming), wahitimu 39 wamepatiwa fursa ya kuanzisha shughuli za kilimo. Kati ya hao, wahitimu 30 wamepatiwa fursa ya kushiriki katika shamba la hekari 1,500 lililopo Mkoani Morogoro Mvomero. Aidha, wahitimu Tisa wamepatiwa fursa ya kushiriki katika shamba la kahawa Mkoani Songwe.

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha wahitimu wengi zaidi wanaendelea kuwezeshwa kuajirika lakini pia kujiajiri, kupitia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa, Serikali imetenga zaidi ya Shilingi bilioni 54 ili kuwawezesha wahitimu 1,500 kupata mafunzo ya uzoefu wa kazi ikiwemo fani ya kilimo. Ahsante. (Makofi)
MHE. ZAYTUN S. SWAI K.n.y. MHE. ALI HASSAN OMAR KING aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawatambua watoto wenye ulemavu ambao wanaishi kwenye mazingira magumu ili kuwasaidia kwa matibabu na kimaisha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ali Hassan King, Mbunge wa Jang’ombe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuwatambua na kuwapatia huduma stahiki watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na waishio katika mazingira hatarishi zaidi kwa kuzingatia aina ya ulemavu walionao na hitaji la msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utambuzi huo umekuwa ukifanyika kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2004. Kwa kuzingatia sera hiyo, Serikali imeanzisha Rejesta ya Utambuzi wa Watoto Waishio katika Mazingira Hatarishi zaidi. Serikali imeweka pia mfumo wa ulinzi na usalama wa watoto. Aidha, Serikali imekamilisha Mwongozo wa Utambuzi wa Mapema wa Afua na Stahiki za Watoto wenye Ulemavu wa mwaka 2021 unaoainisha namna sahihi ya kumtambua mtoto mwenye ulemavu na afua anazostahili kupatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wenye ulemavu waishio katika mazingira hatarishi zaidi hupatiwa huduma kupitia afua mbalimbali ikiwemo kupatiwa elimu kupitia shule zenye vitengo maalum na jumuishi; kuwapeleka katika hospitali kwa ajili ya kupatiwa afua za matibabu, kupatiwa stadi za maisha kwa lengo la kuwajengea uwezo ili waweze kujitegemea na kujilinda; kupatiwa uchangamshi wa awali na huduma za utengamao; kuwarejesha katika familia zao na kuwaweka katika familia za kuaminika (fit family); utoaji wa vifaa saidizi; kuwaunganisha na vyuo maalum vya watu wenye ulemavu kwa ajili ya kupatiwa ujuzi na huduma za marekebisho na kwa wale ambao hawana walezi au wazazi hupelekwa kwenye makao ya watoto kwa ajili ya huduma mbalimbali.
MHE. ALI JUMA MOHAMED aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwatafutia ajira na fursa mbalimbali nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ali Juma Mohamed, Mbunge wa Shaurimoyo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza mpango mikakati ifuatayo ili kuunganisha vijana na fursa za ajira nje ya nchi: -

(i) Imeingia makubaliano (bilateral agreements) na baadhi ya nchi zenye fursa za ajira duniani.

(ii) Imeweka mwongozo wa kuratibu shughuli za Wakala Binafsi wa Huduma za Ajira ili kuwezesha shughuli za kuunganisha Watanzania na fursa za ajira nje ya nchi kufanyika kwa kuzingatia haki za msingi za wafanyakazi na viwango vya kazi vinavyokubalika na Shirika la Kazi Duniani (ILO). Hadi sasa jumla ya Wakala 58 wamesajiliwa na kupewa leseni, kati ya hao Wakala watano wanajishughulisha na kuwaungaunisha watafuta ajira nje ya nchi.

(iii) Kujenga mfumo wa kielektroniki wa huduma za ajira utakaorahisisha na kuweka uwazi katika kuratibu upatikanaji wa fursa za ajira nje ya nchi; mchakato wa kuandaa Watanzania wenye sifa pamoja na kufuatilia hali za Watanzania wakiwa wanafanya kazi nje ya nchi. Mfumo unatarajiwa pia kukamilika na kuanza kutumika kabla ya mwezi Juni, 2022.

(iv) Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu katika mpango huo ni kutekeleza Programu ya Taifa ya Mafunzo ya Ujuzi hususani kupitia mafunzo ya uanagezi pamoja na utarajali ili kuwezesha vijana husika kuwa na ujuzi stahiki kufanya kazi nje ya nchi.

(v) Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tano baadhi ya machache hayo nikiyataja kwa sababu ya muda kufanyia marekebisho Sheria ya Huduma za Ajira ya mwaka 1999 pamoja na Kanuni za mwaka 2014 ili ziweze kuendana na mazingira ya sasa ahsante.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza ajira kwa Wahitimu wa Vyuo Vikuu hasa katika Sekta ya Kilimo kwa kuwa mikopo ya Elimu ya Juu imewezesha wanafunzi wengi kuhitimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa ajira kwa wahitimu wa Vyuo Vikuu zinaongezeka hususan katika sekta ya kilimo, Serikali inatekeleza mipango ifuatayo: -

(i) Mpango wa Taifa wa Kukuza Ujuzi nchini ambao unatoa mafunzo ya ujuzi na uzoefu katika kilimo cha kisasa cha kutumia teknolojia ya vitalu nyumba. Kupitia mpango huo, hadi sasa jumla ya vijana 12,580 wakiwemo wahitimu wa fani ya kilimo wamepatiwa mafunzo ili waweze kujiajiri;

(ii) Mpango wa mafunzo ya uzoefu wa kazi (internship) kwa wahitimu wa elimu ya juu nchini kupitia waajiri wa ndani na nje ya nchi, ambapo jumla ya wahitimu 6,624 wamepatiwa mafunzo husika;

(iii) Mpango wa Vituo vya Uatamizi kwa Wahitimu (Incubation Centres) ambao tayari umeanza kutekelezwa katika Mikoa ya Morogoro na Pwani. Hadi sasa, jumla ya wahitimu 1,000 wamepatiwa mafunzo ya uanzishaji wa shughuli za kilimo na ujasiriamali;

(iv) Mpango wa kilimo cha vizimba (Block Farming), ambapo tayari wahitimu 39 wamepatiwa fursa ya kuanzisha shughuli za kilimo katika mashamba mbalimbali nchini;

(v) Mpango wa mafunzo ya uzoefu wa kazi kwa wahitimu, ambapo Serikali kwa kushirikiana na Ushirika wa Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUGECO) imewawesha wahitimu 703 kwenda nchini Israel na Marekani kupatiwa mafunzo katika kilimo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na mipango hiyo, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo imeanzisha Mpango mpya uitwao ‘Building a better Tomorrow’’ unaowalenga vijana wahitimu na wasio wahitimu. Katika mpango huu, Ofisi ya Waziri Mkuu itakua na jukumu la kuwapatia mafunzo vijana hao na Wizara ya Kilimo itakua na wajibu wa kutoa ardhi, mitaji, kuweka miundombinu katika mashamba tengwa ya Agro Parks/Blocks pamoja na kuwaunganisha na masoko. Ahsante.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza: -

Je, Serikali inachukua hatua gani ya kuwawezesha Wahitimu wa Vyuo Vikuu ambao hawana ajira kulipa mikopo yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu mojawapo la msingi la Serikali ni kuandaa mazingira wezeshi kuhakikisha Watanzania wanapata maarifa na ujuzi wa kuwawezesha kujiajiri na kuajirika ili kukuza uchumi wa Taifa na vipato vyao. Kutokana na msingi huo, Serikali kupitia Bunge lako Tukufu ilitunga Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Na. 9 ya Mwaka 2004 ambayo inawezesha kutoa mikopo au ruzuku kwa wanafunzi wahitaji waliokidhi vigezo.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, wazazi au wadhamini wanatakiwa kuhakikisha mikopo inarejeshwa ili iweze kunufaisha Watanzania wengine wanaohitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wanufaika wa mkopo ambao baada ya kumaliza vyuo wanachukua muda mrefu kupata ajira au kujiajiri, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuwawezesha kuajiriwa au kujiajiri. Miongoni mwa hatua ambazo Serikali imezichukua ni pamoja na zifuatazo: -

(i) Kutoa mafunzo ya uzoefu wa kazini (internship) kwa wahitimu wa elimu ya juu nchini kupitia waajiri wa ndani na nje ya nchi ambapo jumla ya wahitimu 6,624 wamepatiwa mafunzo ya uzoefu wa kazini na wahitimu 11,475 wamepatiwa mafunzo ya kushindania fursa za ajira katika sekta mbalimbali za kiuchumi;

(ii) Kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, jumla ya Shilingi bilioni 3.3 katika Serikali hii ya Awamu ya Sita, zimetolewa katika kipindi cha miaka ya nyuma mitano kwa ajili ya kuwapatia vijana mikopo nafuu wakiwemo wahitimu wa vyuo vikuu.

(iii) Kupitia mikopo inayotolewa na Halmashauri ya asilimia 10, jumla ya shilingi bilioni 145.8 zimetolewa kwa ajili ya mikopo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu;

(iv) Kutoa mafunzo ya ujasiriamali, kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, hadi sasa programu hii imewafikia vijana 8,736 wa elimu ya juu nchini;

(v) Kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwa sekta binafsi ambayo Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan ametilia mkazo sana eneo hili kuhakikisha kwamba tunapokuwa na uwekezaji na private sector kwa sababu ndiyo inaandaa watu wengi zaidi, vijana waweze kupata fursa ya kuajirika, kuajiriwa na kujiajiri. Ahsante.
MHE. AMINA ALI MZEE aliuliza: -

Je, Serikali inatumiaje Chuo cha Bahari cha DMI kuendeleza vijana wa Kitanzania ili kukabiliana na changamoto za ajira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PATROBAS P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Ali Mzee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) ni Chuo cha Serikali ambacho kimeanzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 22 ya mwaka 1991 Chuo kinatoa elimu na mafunzo katika sekta ya usafiri wa njia ya maji na hivyo kina mchango mkubwa katika kukuza ajira nchini.

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto za ajira, Chuo cha DMI kina kitengo maalum cha uwakala wa ajira za mabaharia (DMI Crewing Agency). Kitengo hiki kilianza kazi mwaka 2018. Kina usajili Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa ajili ya kutafuta ajira na mafunzo melini kwa vijana wa Tanzania kwa meli za ndani na nje ya nchi yetu hususan kwenye mashirika mbalimbali ya meli ikiwemo Azam Maritime, Zan Fast Ferry, TPA Kyera, Greece Marine Company na Verba Shipping Company.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa kuwawezesha wahitimu wa Chuo cha DMI na mabaharia wa Tanzania kupata ajira katika meli za Kimataifa, Serikali inaendelea na taratibu za kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Kusimamia masuala ya Bahari duniani (IMO Convention
– Maritime Labour Convention). Kuridhiwa kwa mkataba huu, kutawezesha kutoa mafunzo na ajira kwa mabaharia takriban 150 ambao ni sawa na 25% ya wahitimu kwa mwaka. Ahsante. (Makofi)
MHE. ANTON A. MWANTONA aliuliza: -

Je, nini mchango wa Serikali katika kuwawezesha vijana zaidi ya 100 waliomaliza Vyuo vikuu ambao wapo tayari kwa ajili ya kujiajiri katika kilimo Wilayani Rungwe kupitia Ofisi ya Mbunge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU (MHE. PATROBASS P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anton Albert Mwantona, Mbunge wa Rungwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua umuhimu wa vijana katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo ya jamii nchini, imeendelea kuweka mazingira wezeshi ili vijana waweze kuanzisha na kuendesha shughuli zao za kujitegemea kwa kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali. Baadhi ya fursa hizo ni kama ifuatavyo: -

(i) Utengaji wa maeneo maalumu kwa ajili ya shughuli za vijana za kiuchumi zikiwemo shughuli za kilimo. Halmashauri zote nchini zimeagizwa kutenga maeneo hayo, ambapo Halmashauri ya Rungwe imetenga Ekari 88.9 kwa ajili ya shughuli za kilimo, viwanda na masoko.

(ii) Mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba kwa ajili ya mazao ya muda mfupi (mbogamboga). Mafunzo hayo yamenufaisha vijana 98 wa Halmashauri ya Rungwe kati yao 15 wamejifunza namna ya kujenga vitalu nyumba.

(iii) Mikopo isiyo na riba ya 4% iliyotengwa na Halmashauri hiyo ya Rungwe kwa mwaka wa fedha 2021/ 2022 imetenga zaidi ya shilingi milioni 133.7 kwa ajili ya vijana.

(iv) Mikopo yenye riba nafuu ikiwemo Mifuko na Program za uwezeshaji wananchi kiuchumi, ukiwemo Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ili kuwawezesha vijana kuanzisha na kuendeleza miradi mbalimbali katika sekta ya kilimo katika eneo hilo la Jimbo la Rungwe.

(v) Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo imeanzisha Mpango uitwao “Building a Better Tomorrow” unaowalenga Vijana wahitimu na wasio na kazi wajiingize katika kufanya shughuli katika sekta ya kilimo. Katika mpango huu, Ofisi ya Waziri Mkuu itakuwa na jukumu la kuwapatia mafunzo vijana. Vile vile Wizara ya Kilimo itakuwa na wajibu wa: kwanza, kutoa ardhi; pili, kuweka mitaji na kuwatafutia mitaji vijana hawa; na tatu, kuweka miundombinu katika mashamba ambayo yatakuwa yametengwa ya Agro Parks/Blocks pamoja na kuwaunganisha na masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Mbunge kupitia ofisi yake awashauri na kuwahimiza vijana wa Rungwe waliohitimu Vyuo Vikuu kuzingatia fursa zinazotolewa na sisi tutaendelea kumpa ushirikiano popote atakapohitaji ili kuweza kuwaunganisha vijana na kuwaweka katika kazi. Ahsante.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa muongozo kwa Vyama vya Wafanyakazi hasa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na kupunguza ada ya uanachama au kuondoa kabisa mfumo wa asilimia ili kuweka kiwango kitakachokubaliwa na wanachama wenyewe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Vyama vya Wafanyakazi kikiwemo Chama cha Walimu Tanzania (CWT) vimeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004 ambayo ndiyo inayoongoza vyama vya wafanyakazi, vyama vya waajiri na mashirikisho vikiwa na lengo la kusimamia haki na maslahi ya wanachama wake ambao ni wafanyakazi walio katika sekta ya elimu.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu 47(c) cha sheria hiyo kimetoa sharti kwamba katiba za vyama lazima zieleze kuhusu ada ya uanachama au njia yoyote ya kuamua ada hiyo. Kwa mantiki hiyo, chama kupitia katiba yake na wanachama ndio wenye mamlaka ya kujadili na kukubaliana masuala ya ada za uanachama katika chama husika na siyo Serikali.

Mheshimiwa Spika, katiba ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kupitia kifungu cha 23.1(c) kimetoa mamlaka kwa Mkutano Mkuu kufanya mabadiliko ya katiba kwa uamuzi wa theluthi mbili za wajumbe walio na haki ya kupiga kura. Hivyo kupitia mkutano huo, wanachama ndiyo walioamua kuhusu njia ya ukataji wa ada kwa asilimia mbili. Hivyo, kwa kutumia chombo hicho hicho wanachama wanaweza kuamua kuweka utaratibu mwingine wa ukataji wa ada husika bila kuvunja sheria. Ahsante.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA aliuliza: -

Je, ni lini wastaafu ambao waajiri wao walikuwa hawatoi michango katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii watalipwa haki zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mafao ya pensheni hulipwa kwa mstaafu kwa kuzingatia kipindi kilicholipiwa michango yake. Kumekuwepo na changamoto kwa baadhi ya waajiri kushindwa kuwasilisha michango ya watumishi wao katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa wakati. Kutokana na changamoto hiyo, mifuko imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwapeleka Mahakamani waajiri ambao hawawasilishi michango kwa wakati ili kuwezesha wastaafu hao kupata haki yao.

Mheshimiwa Spika, hatua zilizochukuliwa na mifuko kukabiliana na changamoto hii ni pamoja na kutoa elimu kwa waajiri, kutengeneza namba ya kumbukumbu ya malipo (control number) kupitia Mfumo wa Malipo ya Serikali (GePG) na kupunguza tozo zinazotokana na ucheleweshwaji wa michango hiyo. Aidha, mifuko imeingia makubaliano maalum na waajiri 63 ya namna ya kulipa madeni yao.

Mheshimiwa Spika, waajiri ambao wameendelea kukaidi kuwasilisha michango ya wanachama kwa wakati, Mfuko kwa kushirikiana na Wakili Mkuu wa Serikali (Solicitor General) imechukua hatua ya kuwapeleka Mahakamani kwa mujibu wa sheria. Aidha, waajiri 123 tayari wamefikishwa Mahakamani, ahsante.
MHE. KHADIJA S. TAYA aliuliza: -

Je, Serikali inatoa kauli gani kwa waajiri ambao wanasuasua katika kuwaajiri watu wenye ulemavu wenye sifa stahiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa niaba ya Wazir Mkuu naomba kujibu swali namba 135 lililoulizwa na Mheshimiwa Khadija Shaaban Taya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mnamo mwaka 2010, Serikali ilitunga Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 kwa lengo la kusimamia masuala mbalimbali ya watu wenye ulemavu. Katika kifungu cha 31(1) kinaeleza kuwa kila mwajiri wa umma au binafsi, endapo kutatokea nafasi ya ajira na mtu mwenye ulemavu aliyekidhi viwango vya chini vya ajira hiyo akaomba atalazimika kumwajiri. Aidha, kifungu 31(2) cha Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya 2010 kinaeleza kuwa kila mwajiri mwenye waajiriwa kuanzia 20 na kuendelea anatakiwa kuwa na watu wenye Ulemavu wasiopungua asilimia tatu ya waajiriwa wake.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia takwa hili la sheria naomba kuwakumbusha waajiri wote kuzingatia viwango hivyo vya ajira kama vilivyoelekezwa katika sheria na tutaendelea kufanya kaguzi na kuchukua hatua kwa wasiotekeleza takwa hilo la msingi la kisheria na kibinadamu.
MHE. HUSNA J. SHEKIBOKO K.n.y. MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kurasimisha vijana waliopata ujuzi nje ya mfumo rasmi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. PATROBAS P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inao mkakati kupitia Mpango wa Taifa wa maendeleo wa miaka mitano wa kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo kwa vijana 100,000 ifikapo mwaka 2025/2026. Aidha, katika utekelezaji wake hadi kufikia Juni, 2022 kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi jumla ya vijana wapatao 22,296 (kike 3,349 na kiume 18,947) kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara wamerasimishwa ujuzi ikiwemo Singida zaidi ya watu 1,138.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo fani kumi zinazohusika katika urasimishaji ambazo ni uashi, useremala, ufundi magari (makenika), upishi na uhudumu wa hoteli, baa na migahawa, ufundi bomba, unyooshaji bodi za magari, umeme wa majumbani; ushonaji nguona uchomeleaji vyuma. Aidha, kutokana na manufaa wanayoyapata vijana, katika mwaka wa fedha 2022/2023 jumla ya vijana 18,445 (wa kiume 13,873 na wa kike 4,572) wamejitokeza na kukuziwa uchuzi na kuchukua fomu kwa ajili ya kurasimishwa ujuzi wao kupitia programu hii ambapo taratibu zinakamilishwa ili waweze kupatiwa fursa hiyo. Ahsante.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuwapatia warithi wa mstaafu asilimia 67 ya michango yake pindi anapofariki?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Ulyankulu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii hutoa mafao kwa wanachama wake kwa mujibu wa Sheria ya Hifadhi ya Jamii Sura Na. 135 kama ilivyorejewa kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria Na. 6 ya Mwaka 2019 ambapo fao la warithi ni mojawapo ya mafao yanayotolewa pindi mwanachama anapofariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Mfuko wa PSSSF, kupitia Kifungu cha 39(1) cha Sheria ya Mfuko, mstaafu anapofariki Mfuko hulipa mafao ya mkupuo ambayo ni jumla pensheni ya miezi 36 (sawa na miaka mitatu) kwa wategemezi. Kwa upande wa NSSF pia, kwa mujibu wa Kifungu cha 37(1)(2)(3) cha Sheria ya Mfuko, mstaafu anapofariki Mfuko hulipa mafao ya mkupuo sawa na pensheni ya miezi 36 kwa wategemezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ulipaji wa mafao huzingatia Sheria ya Hifadhi ya Jamii ya Mwaka 2018 na Marekebisho yake ya Mwaka 2019 na Kanuni za Mafao kama zilivyorejewa mwaka 2022. Mafao yanayolipwa hayazingatii asimilia ya michango isipokuwa wastaafu na wategemezi hulipwa mafao kwa mujibu wa kanuni zinazoongoza ulipaji wa mafao.
MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. BONNAH L. KAMOLI aliuliza: -

Je, nini mpango wa kuhakikisha Madereva wa magari ya abiria na mizigo wanapewa mikataba ya kazi ili kupata mafao na Bima za Afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bonnah Ladislaus Kamoli, Mbunge wa Segerea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kusimamia Sheria za Kazi na kuwahimiza waajiri wote nchini kuwapatia wafanyakazi wao mikataba ya ajira kwa kuwa hili ni takwa la kisheria na ni haki ya wafanyakazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhimza hili Serikali ilitoa tamko na maagizo kwa wamiliki wa mabasi na malori tarehe 12 Juni, 2022 na tarehe 22 Julai, 2022, kwamba ifikapo tarehe 30 Agosti, 2022, wafanyakazi madereva wote wawe wamepewa mikataba kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa taarifa katika Bunge lako Tukufu kuwa waajiri wengi wametekeleza na baadhi bado wanaendelea kutekeleza mikataba hiyo kwa ajili ya kuwapatia madereva, lakini pia wafanyakazi wote katika sekta rasmi nchini. Aidha, Ofisi imejipanga na inaendelea kufanya ukaguzi maalum katika Sekta ya Usafirishaji na kuchukua hatua stahiki kwa waajiri wanao kiuka takwa hilo la kutoa mikataba kwa wafanyakazi madereva na Sekta nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua na kulinda haki za wafanyakazi madereva, imeweka utaratibu wa kukaa Vikao vya Mashauriano na Majadiliano na Viongozi wa Vyama vya Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji (Malori na Mabasi) pamoja na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi Madereva kwa lengo la kupeana taarifa kuhusu changamoto zinazowakabili madereva na kuzitafutia ufumbuzi. Aidha, utaratibu huu ni endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti mbali na kaguzi hizo, nitoe rai na kumwomba Mheshimiwa Mbunge na Watanzania wote kutoa taarifa endapo watapata taarifa za kutokuwepo kwa mwajiri katika sekta hii ambaye bado hajatekeleza maagizo haya ya Serikali kwa kutoa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi madereva, hatua stahiki zitaendelea kuchukuliwa pia kwa mujibu wa sheria kwa kutambua kwamba sekta hii ni muhimu na ina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi yetu. Ahsante.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaridhia Mkataba Na.189 wa Kazi za Staha kwa Wafanyakazi wa Majumbani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCAL P.
KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Mkataba huu wa Kimataifa wa kuhusiana na haki za wafanyakazi wa majumbani haujaridhiwa ambapo Serikali inafanya tathmini ya kina kuona kama kuna umhimu wa kuridhia na kuwa masuala mengi yaliyoko katika Mkataba huu yanatekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Sura 366 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019. Aidha, siyo kila Mkataba wa Kimataifa unaridhiwa. Tunaridhia mikataba ya msingi (Core Conventions) ambapo kwa Mikataba isiyo ya lazima (Other Conventions) uridhiaji wake utazingatia mila, desturi na hali ya uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kushauriana na wadau katika suala hili. Nitumie fursa hii kuwaomba wadau kuendelea kutoa maoni ya njia bora ya kuendelea kuboresha maslahi na haki za wafanyakazi wa majumbani kwa kuzingatia mila, desturi na hali ya nchi yetu. Ahsante.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza: -

Je, ni lini Wazee watapata nafasi ya uwakilishi Bungeni kama ilivyo kwa Vijana na Wanawake ili waweze kusikilizwa na kutoa ushauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PATROBAS P KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ibara ya 66(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, imeweka sharti la aina sita za Wabunge ambao ni Wabunge wa kuchaguliwa kuwakilisha Majimbo ya Uchaguzi, Wabunge Wanawake wasiopungua asilimia thelathini ya Wabunge wote, Wabunge watano kutoka Baraza la Wawakilishi, Mwanasheria Mkuu pamoja na Wabunge wasiozidi 10 wa kuteuliwa na Rais na Spika iwapo hatakuwa amechaguliwa kutoka miongoni mwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Ibara ya 67(1)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeainisha moja ya sifa ya mtu kuwa Mbunge ni lazima awe mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa. Hivyo tunatoa wito kwa Vyama vya Siasa nchini kutenga nafasi za uwakilishi wa wazee kama ilivyo kwa watu wenye ulemavu na vijana ili waweze kupata nafasi ya uwakilishi Bungeni.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kuzungumza na taasisi za kifedha ili mikopo kwa watu wenye ulemavu itolewe kwa mtu mmoja mmoja badala ya vikundi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Elias Mahawanga, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, taasisi mbalimbali za kifedha ikiwemo mabenki zimekuwa zikitoa mikopo kwa mtu mmoja mmoja na makundi mbalimbali wakiwemo watu wenye ulemavu. Aidha, wananchi wa kipato cha chini wakiwemo makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu wanashindwa kunufaika na mikopo inayotolewa na taasisi hizo kutokana na mikopo hiyo kuambatana na vigezo vinavyowekwa ikiwemo waombaji kuwa na dhamana au mali isiyohamishika kama viwanja, mashamba na nyumba.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua changamoto hiyo, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI imekuwa ikisimamia utoaji wa mikopo ya uwezeshaji kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa mujibu wa kifungu 37A cha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa na Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu za mwaka 2019 na marekebisho yake ya mwaka 2021. Sheria na Kanuni hizi zimeelekeza kuwa mikopo hii itatolewa kwa vikundi vya wajasiriamali wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa uwiano wa asilimia nne kwa wananwake; nne kwa vijana na mbili kwa watu wenye walemavu kwa lengo la kuwawezesha kuanzisha na kuendeleza shughuli zao za ujasiriamali ili kujiongezea kipato na kupunguza umaskini.

Mheshimiwa Spika, habari njema ni kwamba Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imefanya marekebisho ya Kanuni mwaka 2021 ambayo yametoa fursa kwa mtu mmoja mmoja mwenye ulemavu kuomba mkopo. Hivyo, niombe Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote kwamba tufikishe taarifa hii ya mabadiliko ya kanuni za mikopo hiyo ambayo imetoa fursa kwa mtu mmoja mmoja mwenye Ulemavu kuomba mkopo.
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kutoa mwongozo wa upandishaji mishahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mshahara katika sekta binafsi unapanda baada ya Bodi ya Kima cha Chini cha Mishahara katika sekta binafsi ambayo inaundwa kwa mujibu wa Sheria ya Taasisi za Kazi, Sura ya 300 kufanya utafiti na kupanga viwango vya mishahara katika sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, ninapenda kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa Bodi hiyo tayari imekamilisha kazi ya kupanga kima cha chini kipya na kumshauri Waziri mwenye dhamana na masuala ya kazi ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kutangaza kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi. Kwa ujumla, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha suala hili na itatangaza rasmi kima cha chini cha mshahara katika sekta binafsi mwezi huu wa Novemba, 2022. Ahsante.
MHE. JUDITH S. KAPINGA K.n.y. MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza: -

Je, ni lini marekebisho ya sheria yataletwa Bungeni ili mwanamke anayejifungua mtoto njiti aongezewe likizo ya uzazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mkataba wa Kimataifa wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Na.183 kuhusu haki ya uzazi unaelekeza nchi wanachama kuweka utaratibu wa kuwalinda mtoto na mama kutokana na changamoto za uzazi.

Mheshimiwa Spika, haki ya likizo ya uzazi kwa mwanamke mwajiriwa ipo kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Sura ya 366, Marejeo ya Mwaka 2019 kifungu cha 33 ambapo mwajiriwa mwanamke akijifungua mtoto mmoja anapewa likizo ya uzazi ya siku 84 na akijifungua watoto mapacha hupewa siku 100, kadhalika akijifungua mtoto njiti hupewa siku 84 katika mzunguko wake wa likizo.

Mheshimiwa Spika, uzoefu unaonesha kuwa wafanyakazi wanawake wanapewa likizo ya uzazi kwa mujibu wa sheria na endapo likizo itamalizika na bado kuna uhitaji wa kumlea mtoto njiti, mwajiriwa anapaswa kujadiliana na mwajiri wake na kukubaliana kuhusu nyongeza ya likizo.

Vilevile mzazi anapokuwa amelazwa hospitalini na mtoto anapaswa kupewa Exemption from Duty (ED) ambayo itamwezesha mwajiriwa huyo kuendelea kulea mwanaye bila kupoteza haki ya kulipwa mshahara wake endapo atawasilisha cheti cha daktari kwa mwajiri wake.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sheria haijaainisha utaratibu mahususi wa kumwezesha mwanamke mwajiriwa kupewa likizo ya uzazi baada ya kujifungua mtoto njiti, ninapenda kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imelipokea suala hili na italifanyia kazi kwa kufanya maboresho katika kanuni za sheria husika kuwawezesha waajiri kuandaa sera za ajira ambapo pamoja na mambo mengine suala la likizo kwa mwanamke atakayejifungua mtoto njiti litaanishwa kwa lengo la kumlinda mtoto njiti na mzazi wake. Ahsante.
MHE. STELLA I. ALEX aliuliza: -

Je, ni Mikoa mingapi, Wilaya, Vijiji na Vitongoji wameunda Kamati za Watu wenye Ulemavu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Ikupa Alex, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, uundwaji wa Kamati za Watu Wenye Ulemavu katika Ngazi ya Mkoa, Wilaya, Vijiji na Vitongoji ni kwa mujibu wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na.9 ya mwaka 2010 kifungu cha 14(1) ambacho kimeelezea juu ya uundwaji wa Kamati za Watu Wenye Ulemavu katika ngazi ya Kijiji, Mtaa, Wilaya, Mkoa pamoja na majukumu ya kila Kamati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, imetekeleza kwa kiwango kikubwa uundwaji wa Kamati hizo. Mchanganuo wa idadi ya Mikoa, Halmashauri na Vijiji/Mitaa ya Tanzania Bara iliyounda Kamati za Watu wenye Ulemavu ni kama ifuatavyo: -

(i) Mikoa yote 26;

(ii) Halmashauri zote 185;

(iii) Vijiji 7,483 kati ya 12,319; na

(iv) Mitaa 2,284 kati ya 4,263.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha na kufuatilia Vijiji na Mitaa yote inaunda Kamati za Watu Wenye Ulemavu, Serikali imeandaa mikakati mbalimbali ikiwemo kuingiza masuala ya Kamati za Watu Wenye Ulemavu kwenye Mwongozo Kabambe wa Upangaji wa Mipango na Bajeti ya Huduma za Ustawi wa Jamii kwenye Halmashauri (Council Comprehensive Social Welfare Operation Plan – CCSWOP) ambapo utekelezaji wake utaanza mwaka ujao wa fedha 2023/2024. Aidha, Serikali itaendelea kufuatilia Watendaji wa Vijiji au Mitaa ili kuhakikisha Kamati za Watu Wenye Ulemavu zinaanzishwa katika maeneo yao.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatangaza kima cha chini cha mishahara kwa Wafanyakazi wa Serikali na mashirika binafsi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, Mbunge wa Viti Maalum kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ninapenda kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa kima cha chini cha mshahara kwa sekta ya umma kilitangazwa tarehe 13/5/2022 na utekelezaji wake ulianza tarehe 1 Julai, 2022. Kwa upande wa sekta binafsi kima cha chini cha mshahara kilitangazwa tarehe 25/11/2022 kwenye Gazeti la Serikali Na. 687 baada ya Bodi ya Kima cha Chini cha Mishahara kukamilisha utafiti na kutoa mapendekezo ya viwango kwa Sekta Binafsi ambayo yaliridhiwa na Baraza la Ushauri kuhusu Kazi, Uchumi na Jamii (LESCO). Utekelezaji wake unaanza rasmi Tarehe 1 Julai, 2023.
MHE. JERRY W. SILAA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawalipa mafao waliokuwa Wafanyakazi wa Viwanda vya Kilitex na Sunguratex Gongo la Mboto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jerry Silaa, Mbunge wa Ukonga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia mwaka 1989 Serikali kupitia Mifuko ya NSSF uliokuwa PPF iliwalipa mafao waliokuwa wafanyakazi wa viwanda vya Kilitex na Sunguratex Gongo la Mboto baada ya ukomo wa ajira zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Aprili, 2022 Mfuko wa PSSSF ulipokea malalamiko ya waliokuwa wafanyakazi wa kiwanda Sunguratex wapatao 644 wakidai kuwa hawakulipwa mafao kikamilifu na uliokuwa Mfuko wa PPF. Baada ya Mfuko kufanya uchambuzi wa madai hayo, imeonekana kuwa wafanyakazi hao walishalipwa mafao kikamilifu isipokuwa baadhi yao wanasubiri kufikisha miaka 55 ili waanze kulipwa pensheni ya mwezi. Kuhusu wafanyakazi wa kiwanda cha Kilitex Mfuko haujapokea malalamiko yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ipo tayari kuendelea kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine kama wafanyakazi hao wapo ili kutatua changamoto ya waliokuwa wafanyakazi wa viwanda vya Kilitex na Sunguratex Gongolamboto. Ahsante.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa vijana walio mashuleni juu ya kujikinga na dawa za kulevya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeandaa na kuzindua Mwongozo wa Utoaji Elimu Kuhusu Dawa za Kulevya nchini ambao ulizinduliwa tarehe 2 Julai, 2022 na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwenye kilele cha siku ya Taifa ya Kupinga Dawa za Kulevya, Jijini Dar es Salaam. Mwongozo huo tayari umeanza kutumika kuelimishia walimu wa shule za msingi na sekondari pamoja na asasi za kiraia zinazojihusisha na utoaji wa elimu kwa makundi mbalimbali ya jamii wakiwemo vijana waliopo mashuleni, juu ya tatizo la dawa za kulevya nchini.
MHE. LUHAGA J. MPINA aliuliza: -

Je, ni Vijana wangapi hawana ajira nchini na Serikali imewaandaaje kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Kisesa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi wa mwaka 2021 unaonesha kuwa vijana wenye umri wa miaka 15-35 ambao wana ukosefu wa ajira ni 1,732,509. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 12.2 ya nguvu kazi, maana ya vijana walio katika umri huo na wapo katika mfunzo au hawana ulemavu unaosababisha wasijishughulishe na shughuli za kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Katika kuhakikisha kwamba Vijana wanaendelezwa ipasavyo kushindana katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeweka mkakati wa kitaifa wa kukuza ujuzi wa miaka 10 mwaka 2016/2017 – mwaka 2025/2026. Kupitia mkakati huu, Serikali imefanya maboresho ya miundombinu ya mitaala katika ngazi za Elimu ya Juu, Elimu ya Kati, na Mafunzo Stadi ya Ufundi.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, sambamba na maboresho hayo, Serikali imetoa mafunzo ya kuwezesha vijana walio nje ya mafunzo rasmi ili kumudu ushindani katika soko la ajira, yakiwemo mafunzo ya uanagenzi, mafunzo ya uzoefu wa kazi (internship) kwa wahitimu, mafunzo ya urasimishaji ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu (RPL), na mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya vitalu nyumba. Ahsante.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kutoa elimu kwa watumishi juu ya ukokotoaji wa mafao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alice Karungi Kaijage, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha watumishi wanapata elimu juu ya ukokotoaji wa mafao na elimu ya hifadhi ya jamii kwa ujumla, Serikali kupitia Mifuko ya PSSSF na NSSF imekuwa ikitoa elimu kwa watumishi.

Mheshimiwa Spika, kuanzia mwezi Julai hadi Desemba 2022 mifuko imeweza kutoa elimu kwa jumla ya waajiri 318 ambapo wanachama 19,656 walihudhuria mafunzo hayo kutoka katika sekta ya umma na sekta binafsi. Kazi ya kuwafikia waajiri na wanachama wengine ili kuwapa elimu husika inaendelea.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kusimamia, kuratibu na kuhakikisha elimu kwa watumishi wa umma inatolewa kupitia makundi mbalimbali yanapokuwa na vikao kama Mabaraza ya Wafanyakazi, semina, warsha na makongamano. Aidha, mifuko inaendelea kuwatembelea watumishi katika maeneo yao ya kazi, kuandaa na kuwashirikisha katika vipindi kwenye luninga na kurusha vibango katika mitandao ya kijamii, ahsante.
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza: -

Je, ni vikundi vingapi vya vijana wa Zanzibar vimenufaika na mikopo au uwekezaji kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana Taifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Maendeleo ya Vijana umeanzishwa kwa Sheria ya Fedha Namba 6 ya 2001 (The Public Finance Act, 2001) chini ya kifungu namba 45, ikisomwa sambamba na kifungu namba 12 cha sheria hiyo, ambapo Mfuko wa Maendeleo ya Vijana hutoa huduma ya mikopo yenye masharti nafuu kwa vijana Tanzania Bara tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Zanzibar upo Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambao pia unahudumia vijana na wana mpango maalum unaowahudumia vijana wa Zanzibar chini ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni, na Michezo na unaendeshwa kwa mujibu wa taratibu na sheria za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hivyo, kwa pande zote mbili za Muungano tuna ushirikiano wa karibu katika masuala yote ya maendeleo ya vijana na kubadilishana uzoefu, lakini pia masuala ya utatuzi wa changamoto kwa ajili ya kuwajenga vijana katika kuweza kupata fursa za ajira na mitaji. Ahsante.
MHE. BONNAH L. KAMOLI aliuliza: -

Je, ni Watanzania wangapi wamejitokeza na kupata fursa ya mafunzo maalum ya ujuzi yaliyotangazwa kupitia VETA kote nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bonnah Ladislaus Kamoli, Mbunge wa Segerea kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tangu kuanza kutekeleza Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi mwaka 2016/2017, kupitia Vyuo vya VETA, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) na Vyuo Binafsi, jumla ya vijana walioomba mafunzo ni 215,233 na waliopatiwa mafunzo ya ujuzi ni 96,894 ambapo kati yao vijana 74,578 wamepatiwa mafunzo kwa njia ya uanagenzi na vijana 22,296 wamepatiwa mafunzo kupitia njia ya urasimishaji ujuzi (RPL).

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. NG’WASI D. KAMANI K.n.y. MHE. LATIFA K. JUWAKALI aliuliza: -

Je, upi mkakati wa Serikali wa kukuza ujuzi na stadi kwa vijana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Latifah Khamis Juakali Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukuza ujuzi na stadi za kazi kwa vijana, Serikali imeandaa Mkakati wa Taifa wa Kukuza Ujuzi wa miaka 10 (2016/2017 na 2025/2026) ambapo umelenga kuhakikisha nguvu kazi ya vijana inashiriki katika kujenga uchumi wa Taifa. Mkakati huu unatekelezwa kupitia program na mipango mbalimbali ya kukuza ujuzi na stadi kwa vijana inayotekelezwa na wadau mbalimbali wakiwemo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Baadhi ya programu na mipango hiyo ni pamoja Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi inayotekelezwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ambayo tangu kuanza kutekelezwa mwaka 2016/2017 imetoa mafunzo ya ujuzi na stadi za kazi kwa jumla ya vijana 118,415 na Mpango wa Mafunzo na Uwezeshaji wa Vijana kushiriki kilimo unaotekelezwa na kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu lakini kutekelezwa na Wizara ya Kilimo, ahsante.
MHE. STELLA I. ALEX aliuliza: -

Je, lini Mfuko wa Taifa wa Watu wenye Ulemavu utaanza kufanya kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Ikupa Alex, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mfuko wa Taifa wa Watu Wenye Ulemavu umeanzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 57 cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010. Katika kutimiza azma ya Serikali ya uanzishwaji wa Mfuko huu, hatua mbalimbali zimeshachukuliwa na Serikali ikiwemo uandaaji wa Mwongozo wa Usimamizi, Uratibu na Uendeshaji wa Mfuko husika pamoja na kufunguliwa kwa akaunti ya mfuko.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kukamilika kwa hatua zote muhimu za mfuko kuanza kutekeleza majukumu yake, mfuko huu haujaanza kutoa huduma kutokana na maelekezo ya kuunganisha mifuko yote ya uwezeshaji wananchi kiuchumi yaliyotolewa mwaka 2020. Zoezi hili liliambatana na tathmini ya ufanisi wa utendaji wa mifuko. Aidha, tathimini hii itakapokamilika, wadau wote wataarifiwa juu ya uanzishwaji wa mifuko hiyo ukiwemo Mfuko huu wa Taifa wa Watu wenye Ulemavu, ahsante.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE K.n.y. MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali italipa kiinua mgongo kwa wazee ambao hawajawahi kuajiriwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniventura Destery Kiswaga, Mbunge wa Magu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kiinua mgongo ni malipo ambayo hulipwa na mwajiri pindi mfanyakazi wake anapostaafu kufanya kazi. Hata hivyo, kutokana na kuwepo kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambapo mwajiriwa na mwajiri huchangia, mfanyakazi hulipwa pensheni badala ya kiinua mgongo na hupokea mafao ya mkupuo mara anapostaafu na badaye kuendelea kulipwa pensheni ya kila mwezi kwa maisha yake yote. Hivyo, kwa sasa hakuna mfumo wa kulipa kiinua mgongo kwa mzee ambaye hajawahi kuajiriwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza: -

Je, Serikali imejipanga vipi kushughulikia malalamiko kuhusu kikototoo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathan Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilitangaza matumizi ya kanuni mpya ya mafao ya kikokotoo ya pensheni kuanzia tarehe 1 Julai, 2022 kupitia Gazeti la Serikali Na. 357 Toleo la Tarehe 20 Mei, 2022. Kanuni hiyo iliandaliwa kwa kuzingatia haja ya kuboresha, kuwianisha mafao ya wanachama na kuifanya Mifuko ya Pensheni kuwa endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua wajibu wa kuwaelimisha wananchi hususan waajiri na wanachama wa Mifuko ya Pensheni kuhusu Kanuni mpya ya Mafao ya Pensheni, elimu imeendelea kutolewa na Mifuko ya Pensheni kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA). Hadi kufikia tarehe 28 Februari, 2022, Mifuko iliweza kutoa elimu kwa jumla ya waajiri 2,927 (PSSSF), waajiriwa 318 na NSSF waajiriwa 2,609 ambapo wanachama 71,836 wa PSSSF wakiwa 19,656 na NSSF 52,180 walifikiwa na mafunzo hayo. Mifuko inaendelea kutoa elimu kama sehemu ya majukumu yao ya kila siku, ahsante.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza: -

Je, lini Serikali itahakikisha Watanzania wanaofanya kazi kwenye Kampuni za Kichina wanalipwa vizuri kwa mujibu wa sheria?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninaomba kujibu swali kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria za Kazi ili kulinda haki za wafanyakazi. Aidha, katika kuendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi wa sekta binafsi, Serikali kupitia Bodi ya Kima cha Chini cha Mshahara cha Sekta Binafsi imefanya utafiti na kuboresha kima cha chini cha mishahara ya sekta binafsi, viwango hivyo vipya vya mishahara vilitangazwa kupitia Gazeti la Serikali Namba 687 la tarehe 25 Novemba, 2022 na utekelezaji wake umeanza rasmi tarehe 01 Januari, 2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na taasisi nyingine zinazohusika na masuala ya kazi itaendelea kuhakikisha kuwa waajiri wanatekeleza ipasavyo viwango vya mishahara vilivyotangazwa kwa kufanya kaguzi za mara kwa mara katika maeneo ya kazi na kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi ili uelewa wao katika kutekeleza Sheria za Kazi unafanyika. Aidha, ofisi imeendelea kuchukua hatua dhidi ya waajiri wanaobainika kukiuka Sheria za Kazi hususan ulipaji wa mishahara kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria.
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza: -

Je, tangu kuanzishwa kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ni kiasi gani cha fedha kimewekezwa na nini faida na hasara za uwekezaji huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2022 kwa hesabu zilizokaguliwa na CAG, thamani ya uwekezaji wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ilikuwa imefikia jumla ya shilingi trilioni 14.4 ambapo Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ulikuwa umewekeza jumla ya shilingi trilioni 6.03, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ulikuwa umewekeza jumla ya shilingi trilioni 7.49 na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Workers Compensation Fund ulikuwa umewekeza jumla ya shilingi bilioni 521.94.

Mheshimiwa Naibu Spika, faida ya uwekezaji huu ni kulinda thamani ya michango ya wanachama na kuhakikisha Mifuko inakuwa endelevu ili kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kulipa mafao. Aidha, uwekezaji huu huchangia na kuongeza ajira, mapato ya Serikali kupitia kodi na kuchochea shughuli za uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo katika uwekezaji wowote kuna vihatarishi (risk) ambavyo vinaweza kusababisha hasara kwa baadhi ya uwekezaji. Hasara zilizojitokeza kwa uwekezaji uliofanywa na Mifuko ni pamoja na kutolipwa kwa wakati kwa mikopo iliyotolewa kwa wanufaika mbalimbali na baadhi ya miradi kutofanya vizuri ikilinganishwa na matarajio yaliyokuwepo wakati wa kubuni miradi hiyo, ahsante.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwawezesha kimaendeleo vijana wa skauti nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kwa vijana wengine wote wa Tanzania wakiwemo vijana wa Skauti ambao wapo kati ya miaka 15 hadi 35, Serikali kwa kushirikiana na Chama cha Skauti Tanzania, imeendelea kutekeleza programu mbalimbali kama vile Klabu za Skauti katika shule za msingi na sekondari ambapo vijana hupatiwa mafunzo ya ujasiri, kutatua matatizo katika jamii, kujitolea na uzalendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, vijana wa skauti ni miongoni mwa vijana ambao hunufaika na programu mbalimbali zinazosimamiwa na Serikali ikiwa ni pamoja na fursa za mikopo yenye masharti nafuu ili kuanzisha miradi ya uzalishaji mali inayowawezesha kujiajiri pamoja na mafunzo ya fani mbalimbali kupitia programu ya kukuza ujuzi nchini, ahsante.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza: -

Je, Serikali imefikia wapi kuhusu mchakato wa pensheni kwa wazee wote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, pensheni kwa wazee wote inajumuisha wazee ambao walikuwa katika ajira ambao kwa sasa wanalipwa pensheni na Mifuko waliyochangia wakati wanafanya kazi na pili, wazee ambao hawajawahi kuajiriwa kwa sasa hawalipwi.

Mheshimiwa Spika, mchakato wa kuwalipa pensheni wazee wote ambapo utajumuisha wazee ambao hawajawahi kuajiriwa ni utaratibu mpya ambao utahitaji kugharamiwa na bajeti ya Serikali. Hivyo, itahitaji kufanyika utafiti wa kina ili kuona uwezo wa Serikali katika kulipa pensheni kwa wazee wote. Hata hivyo, kwa sasa Serikali imekuwa inahudumia wazee kutoka katika familia au kaya zenye umaskini uliokithiri kupitia Mradi wa TASAF ambapo wazee ni sehemu ya familia hizo, ahsante.
MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza: -

Je, nini mpango wa Serikali kuhusu malalamiko ya wastaafu juu ya kikokotoo kinachotumika kupiga mahesabu na kulipa mafao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ilitangaza matumizi ya kanuni mpya ya mafao (kikokotoo) ya pensheni kuanzia tarehe 1 Julai, 2022 kupitia Gazeti la Serikali Na. 357 Toleo la tarehe 20 Mei, 2022. Kanuni hiyo iliandaliwa kwa kuzingatia haja ya kuboresha na kuwianisha mafao ya wanachama na kuifanya Mifuko ya Pensheni kuwa endelevu.

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuendelea kuwaelimisha wananchi hususani waajiri na wanachama wa Mifuko ya Pensheni wakiwemo wastaafu kuhusu faida ya kanuni mpya ya mafao ya pensheni. Hivyo, Serikali kupitia Mifuko ya Pensheni na kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) imejipanga na inaendelea kutoa elimu ya Kanuni hiyo. Hadi kufikia Tarehe 30 Juni, 2023, Mifuko iliweza kutoa elimu kwa jumla ya waajiri 5,580 kati ya waajiri 6,200 waliopangwa kufikiwa kipindi hicho. Aidha, wanachama 131,497 walifikiwa na mafunzo hayo. Mifuko itaendelea kutoa elimu kama sehemu ya majukumu yao ya kila siku, ahsante.
MHE. NICODEMUS H. MAGANGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha pesheni za wastaafu zinalipwa kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nicodemus Henry Maganga, Mbunge wa Mbogwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwneyekiti, pensheni ni mafao wanayolipwa wanachama waliostaafu kwa kila mwezi katika kipindi chote cha maisha yao. Katika kuhakikisha wastaafu wanalipwa pensheni zao kwa wakati, Serikali kupitia Mifuko ya Pensheni ya PSSSF na NSSF imeweka utaratibu mahsusi wa kufanya malipo kwa njia ya kielektroniki kupitia kwenye akaunti zao za benki kila au ifikapo tarehe 25 ya kila mwezi. Hadi kufikia mwezi Machi, 2023 idadi ya wastaafu wanaolipwa pensheni katika Mifuko ya PSSSF na NSSF imefikia 186,605 ikijumuisha PSSSF wastaafu 158,735 na NSSF wastaafu 27,870.

Mheshimiwa Mwneyekiti, mifuko inaendelea kuimarisha mifumo ya ndani ya ulipaji wa mafao ili kuhakikisha maombi ya wastaafu wapya yanafanyiwa kazi kwa haraka na kuanza kulipwa pensheni ndani ya kipindi kisichozidi siku 60 kama sheria inavyotaka, ahsante.
MHE. NANCY H. NYALUSI aliuliza:-

Je, lini Serikali itaboresha mafao ya Wastaafu kwa kuongeza kiwango cha pensheni anayopata Mstaafu kwa mwezi?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA. VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nancy Hassan Nyalusi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii huongeza kiwango cha pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu mara baada ya kufanya tathmini na kujua uendelevu na uwezo wa kulipa mafao kwa wanachama wake. Tathmini hiyo hufanyika kila baada ya miaka mitatu kwa kipindi kifupi, miaka mitano kwa kipindi cha kati na tathmini ya kipindi kirefu kwa miaka kumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kanuni za ulipaji mafao Namba 11(1) za mwaka 2018, zinaelekeza Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuongeza pensheni kwa kuzingatia mfumuko wa bei na uendelevu wa Mfuko kila baada ya miaka mitatu. Hata hivyo, ninayo furaha kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa hadi sasa wastaafu wa Serikali waliboreshewa pensheni zao za kila mwezi ambapo imefikia kiwango cha chini cha shilingi laki moja na kuendelea, tofauti na hapo awali, ahsante.
MHE. NG'WASI D. KAMANI aliuliza:-

Je, Serikali inatumia mfumo gani kuhakiki ubora na matokeo chanya ya programu mbalimbali zinazotolewa kwa vijana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ng’wasi Kamani, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ya miradi na programu zote zinazotekelezwa ikiwemo programu za vijana. Katika kutekeleza hilo mwezi Januari, 2022 Serikali ilitoa Mwongozo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Miradi mbalimbali na Programu za Maendeleo. Kwa kuzingatia mwongozo huo, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imekuwa ikifanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa programu mbalimbali kila robo mwaka. Aidha, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu imekuwa ikifanya tafiti ili kupima matokeo ya utekelezaji wa programu mbalimbali, ikiwemo utafiti wa nguvu kazi ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano.

Mheshimiwa Spika, matokeo ya utafiti wa nguvu kazi uliofanyika mwaka 2020/2021unaonesha kuwa kutokana na programu za vijana zinazotekelezwa ikiwemo Programu ya Kukuza Ujuzi, kiwango cha ujuzi cha juu kimeboreka. Kiwango cha ujuzi cha kati kimeongezeka kutoka asilimia 16.6 mwaka 2014 hadi kufikia asilimia 19.9 mwaka 2021, na kiwango cha ujuzi wa chini kimepungua kutoka asilimia 79.9 mwaka 2014 hadi asilimia 76.9 mwaka 2021.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaendelea kusimamia utekelezaji wa programu hizo ili ziweze kuleta tija kwa Taifa. Sambamba na hatua hiyo, mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali imepanga kufanya tathmini mahususi (tracer study) ya mafunzo yanayotolewa kupitia programu mbalimbali za kuwawezesha vijana kubaini mafanikio yaliyopatikana kwa kuwezesha kujiajiri na kuajiriwa, ahsante.
MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza:-

Je, ni mafunzo ya aina gani yanatolewa kwa vijana wa Tanzania kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu inatoa mafunzo ya ujuzi Stadi na stadi za kazi kwa nguvu kazi ya vijana iliyopo katika soko la ajira, yaani kwa vijana walio nje ya mfumo rasmi wa elimu na mafunzo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mafunzo yanayotolewa ni: -

(i) Mafunzo ya kukuza ujuzi wa ufundi katika fani mbalimbali kwa njia ya Uanagenzi yaani Apprenticeship training ambapo kijana anatumia zaidi ya 60% ya muda wa mafunzo katika maeneo ya kazi;

(ii) Mafunzo ya kurasimisha ujuzi unaopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu na mafunzo yaani Recognition of Prior Learning Skills ambapo vijana wanafanyiwa tathmini ya mapungufu waliyonayo, kupatiwa mafunzo na hatimaye kupatiwa vyeti ambavyo vitawasaidia kuendelea na mafunzo ngazi zinazofuata kwa ajili ya kuajiriwa au kujiajiri;

(iii) Mafunzo ya Uzoefu wa Kazi kwa wahitimu yaani Internship Training ambapo wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu wanapelekwa maeneo ya kazi kujifunza kazi;

(iv) Mafunzo ya kukuza ujuzi kwa wafanyakazi waliopo makazini yaani Skills Updating and Upgrading ili kuziba mapengo ya ujuzi yanayotokana na mabadiliko ya teknolojia na utendaji wa kazi na utoaji wa huduma;

(v) Mafunzo ya ujasiriamali, usimamizi wa biashara, miradi, Urasimishaji na Uendelezaji. Mafunzo haya huenda sambamba na utoaji mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana;

(vi) Mafunzo ya Stadi za Maisha kwa Vijana hasa wale walio nje ya mfumo wa shule ili kuwawezesha kujitambua, kuwa na uzalendo na kufanya maamuzi sahihi kuhusu maisha yao, ahsante.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU aliuliza: -

Je, Serikali inatambua utaratibu wa Mgodi wa GGML wa ku-blacklist vijana nchini na ni vijana wangapi wapo blacklisted?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, Mbunge wa Geita Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imewahi kupata malalamiko kuhusu Mgodi wa GGML ku-blacklist vijana ambao wamesitishiwa ajira zao na Mgodi huo kwa sababu mbalimbali. Ufuatiliaji uliofanyika haukubaini suala hili. Kilichobainika ni kuwa mgodi umeweka utaratibu wa kutunza taarifa za kiutendaji na mienendo ya wafanyakazi wake ikiwemo matendo/matukio ya ukiukwaji wa kanuni na taratibu ambayo mfanyakazi anakuwa amefanya katika kipindi cha ajira yake.

Mheshimiwa Spika, katika utaratibu wa kuajiri, Kampuni/Waajiri karibu wote hufuatilia taarifa za utendaji wa waombaji wa kazi kwa waajiri wao wa awali. Hivyo, GGML imekuwa ikitoa taarifa za utendaji na mienendo ya wafanyakazi waliowahi kufanya kazi nao pale inapoombwa kufanya hivyo. Aidha, pamoja na kutoa taarifa hizo, GGML haizuii kwa namna yoyote Mgodi husika kuwaajiri waombaji.

Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwataka vijana ambao wana uhakika utumishi wao katika Mgodi wa GGML haukuwa na dosari na wanaweza kuthibitisha kuwa wamekuwa black-listed katika kampuni hiyo kuwasiliana na Ofisi yangu ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa. Aidha, nichukue nafasi hii kuwasihi vijana wote kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu ili kujiepusha na athari za kuwa kwenye kumbukumbu mbaya za utumishi wao hali inayokwamisha jitihada zao za kujikwamua kiuchumi na kushiriki katika Ujenzi wa Taifa letu.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itashughulikia kuboresha ujira wa madereva wa magari ya IT?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua mchango wa sekta mbalimbali katika uchumi ikiwemo sekta ya usafirishaji, tayari imepanga kima cha chini cha mshahara kilichoboreshwa ambacho kimeanza kutumika tarehe 1 Januari, 2023. Hivyo mishahara na maslahi kwa madereva imeboreshwa kupitia amri ya kima cha chini cha mshahara kipya.

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa kazi kwa madereva wanaoendesha magari ya IT unafanyika kwa kuingia makubaliano ya kazi kati ya mmiliki wa gari na dereva husika ambapo malipo hufanyika baada ya mhusika kufikisha gari linapokwenda. Kwa muktadha huo, mahusiano yaliyopo si ya ajira bali ni makubaliano/mikataba binafsi ya kibiashara (independent contractor) kwa ajili ya contract for service.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, natoa rai kwa madereva wa magari ya IT kuingia mikataba ya kazi ya kibiashara na pale ambapo atatokea mwajiri au kampuni ambayo itaajiri madereva kwa ajili ya kuendesha magari ya IT atapaswa kuzingatia Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ambayo inaelekeza ulipaji wa ujira kulingana na sekta hiyo, ahsante.
MHE. COSATO D. CHUMI K.n.y. MHE. BONNAH L. KAMOLI aliuliza:-

Je, Serikali imejipangaje kushirikiana na Sekta Binafsi kuhakikisha vijana wanaohitimu wanapata ajira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bonnah Ladislaus Kamoli, Mbunge wa Segerea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha vijana wanaohitimu wanapata ajira, Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi imejipanga kufanya yafuatayo:-

(i) Kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili kuwezesha Sekta Binafsi kuwekeza kwenye sekta zinazoweza kuzalisha fursa nyingi za ajira na hivyo kuwezesha vijana wengi wahitimu kupata fursa za ajira;

(ii) Kuendelea kutekeleza programu ya mafunzo ya uzoefu wa kazi (Internship) kwa vijana wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu na mafunzo ili kuwawezesha vijana husika kuwa na ujuzi unaohitajika na waajiri wa Sekta Binafsi wa ndani na nje ya nchi;

(iii) Serikali inaendelea kufanya majadiliano na Nchi za kimkakati kwa lengo la kuwezesha kuwa na Hati za Mashirikiano ya Uwili (Bilateral Agreements) ili kuwezesha Watanzania kunufaika na fursa za ajira zinazotokana na utangamano wa kikanda pamoja na ushirikiano wa kidiplomasia;

(iv) Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inaendelea kutekeleza Programu ya kuwezesha vijana kushiriki katika Kilimo Biashara (Building a Better Tomorrow Youth Initiative for Agribusiness – BBTYIA);

(v) Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendelea kutekeleza programu ya mafunzo ya vitendo (Atamizi) kwa wahitimu wa fani za uvuvi na ukuzaji viumbe maji; na

(vi) Serikali kupitia Wizara ya Madini imeendelea kuwezesha wachimbaji wadogo wa madini kwa kuwatengea maeneo pamoja na kufanya utafiti ili kuwa na uhakika wa kupata madini, kuanzisha vituo zaidi ya 93 na Ofisi za masoko 42 za kuuzia madani na hii inawapa fursa za ajira, ahsante.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaongeza mafao kwa askari wastaafu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii huongeza kiwango cha pensheni ya kila mwezi ya wastaafu mara baada ya kufanya tathmini na kujua uendelevu wake na uwezo wa kulipa mafao kwa wanachama wake. Tathmini hiyo hufanyika kila baada ya miaka mitatu kwa kipindi kifupi, miaka mitano kwa kipindi cha kati na miaka kumi kwa kipindi kirefu.

Mheshimiwa Spika, Kanuni ya Ulipaji Mafao Namba 11(1) za mwaka 2018 zinaelekeza Mfuko wa PSSSF kuongeza pensheni kwa kuzingatia mfumuko wa bei na uendelevu wa mfuko kila baada ya miaka mitatu. Hata hivyo, ninayo furaha kukuarifu na kuarifu Bunge lako tukufu kuwa hadi sasa wastaafu wote wa Serikali walishaboreshewa pensheni zao za kila mwezi ambapo kiwango cha chini ni shilingi 100,000 inaendelea kulipwa tofauti na hapo ilivyokuwa awali, ahsante.
MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza: -

Je, nini hatma ya madai ya maslahi ya waliokuwa wafanyakazi wa Kiwanda cha Sukari Kilombero?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Jimbo la Mikumi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, taarifa zilizopo katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii zinaonesha kuwa hakuna madai ya mafao ya malimbikizo ambayo yapo kwa waliokuwa wafanyakazi wa Kiwanda cha Sukari Kilombero. Wafanyakazi wote waliofungua madai wamelipwa. Iwapo kuna mfanyakazi yeyote ambaye hajafungua madai, ninashauri afungue madai yake ili aweze kulipwa mafao yake kwa mujibu wa sheria na kanuni za mifuko zilizopo, ahsante.
MHE. LUHAGA J. MPINA aliuliza:-

Je, ni vijana wangapi hawana ajira nchini na Serikali imewaandaaje kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali namba 216 lililoulizwa na Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi wa mwaka 2021 unaonesha kuwa vijana wa umri wa miaka 15 – 35 ni 17, 712,831 ambapo kati yao, vijana 14,219,191 wana uwezo wa kufanya kazi na vijana 3,493,640 hawana uwezo wa kufanya kazi kutokana na sababu mbalimbali kama vile masomo, ugonjwa na kadhalika. Kati ya vijana wenye uwezo wa kufanya kazi, vijana 12,486,682 sawa na asilimia 87.8 wana ajira na vijana 1,732,509 sawa na asilimia 12.2 hawana ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha vijana wanaandaliwa ipasavyo kushindana katika soko la ajira, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa maana ya Serikali imekuwa ikiandaa programu mbalimbali za kuweza kuhakikisha kwamba kunakuwa na mikakati ya kuwapatia vijana fursa za ajira na kuwaandaa kuweza kupata fursa ikiwemo mafunzo mbalimbali kwa maana ya uzoefu kazini, internship kwa hitimu wa vyuo vikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo imekuwa na scheme mbalimbali ya kuweza kuwapatia mikopo, mafunzo, ya utarajali na mafunzo ya kilimo cha kisasa kutumia teknolojia ya vitalu nyumba kupitia mafunzo haya, zaidi ya vijana 84,245 wamenufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Elimu pia Wizara ya Kilimo, kuweza kuhakikisha zinatolewa program mbalimbali ikiwa ni pamoja na mikopo, mafunzo na kutengeneza fursa mbalimbali zaa jira kutokana na Wizara hiyo.
MHE. MIRAJI J. MTATURU aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamaliza changamoto ya kuchelewesha mafao kwa wastaafu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Miraji Jumanne Mtaturu, Mbunge wa Singida Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya jitihada mbalimbali za kulipa Deni la Mfuko wa PSSSF ikiwa ni pamoja na kutoa Hatifungani ya Shilingi Trilioni 2.17 ambazo zitaimarisha mtiririko wa mapato na kuwezesha kutoa mafao kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia Julai Mosi, 2021 hadi Tarehe 30 Aprili, 2022, wastaafu na wanufaika 24,757 wa Mfuko wa NSSF wamelipwa jumla ya Shilingi Bilioni 78 na wanufaika 42,427 wa Mfuko wa PSSSF wamelipwa jumla ya Shilingi Trilioni 1.99. Serikali inawahakikishia wastaafu wote nchini kwamba, itaendelea kuwalipa mafao yao kwa wakati.
MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y MHE. STELLA I. ALEX aliuliza:-

Je, upi mkakati wa Serikali kufanya Marekebisho ya Sheria Na. 9 ya mwaka 2010 ya Watu Wenye Ulemavu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nikushukuru na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi hii, lakini uniwie radhi kwamba nataka kutumia fursa hii kukupongeza sana, kwa kuwa Rais wa Mabunge Duniani, hii inadhihirisha uwezo mkubwa lakini weledi mkubwa ulionao katika kuongoza Bunge letu lakini pia kuaminika katika Dunia.

Mheshimiwa Spika, pia nimpongeze sana Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukupa fursa hiyo lakini zaidi pia kuweza kuwezesha jambo hili kufanikiwa. Haya ni mafanikio makubwa kwa nchi yetu na kwamba, imekuwa kielelezo wewe pamoja na Dkt. Samia Suluhu Hassan cha kufanya sasa leadership tourism katika nchi yetu ya Tanzania, wanaweza kuja kujifunza masuala ya uongozi kupitia Dkt. Samia Suluhu Hassan pia uongozi wako mzuri.

Mheshimiwa Spika, mimi najivunia kuwa wa kwanza kujibu swali leo mbele ya Rais wa Mabunge Duniani. Hili siyo jambo rahisi, najivunia sana hilo lakini pia ni Mbunge wa kipekee kwa sababu hata Waziri Mkuu wa Uingereza anatoka Jimboni kwangu, kwa hiyo ahsante kwa kuniongezea rekodi.

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo naomba nijibu swali kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu la Mheshimiwa Stella Ikupa Alex, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mkakati wa Serikali kwa sasa ni kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2004 ambapo utekelezaji wake umeanza. Baada ya kukamilika kwa mapitio ya Sera ya mwaka 2004, ndipo hatua za Marekebisho ya Sheria ya Watu wenye Ulemavu (Na. 9) ya mwaka 2010 itaanza kwa kuzingatia mapungufu yatakayobainishwa katika tathmini ya utekelezaji wa Sera ya mwaka 2004. Ahsante.
MHE. RASHID A. SHANGAZI K.n.y. MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza:-

Je, Serikali imefanya tathmini ya mafunzo wanayopatiwa vijana chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu baada ya kumaliza mafunzo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali, lililoulizwa kwa niaba yake na Mheshimiwa Rashid Shangazi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Waziri Mkuu inatekeleza Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi nchini ambayo iliandaliwa baada ya kufanya utafiti wa nguvu kazi wa mwaka 2014 ambapo ulionesha kiwango cha ujuzi wa nguvu kazi ya Taifa ni asilimia 3.6 kwa ujuzi wa juu, asilimia 16.4 kwa ujuzi wa kati na asilimia 79.9 ujuzi wa kiwango cha chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2021/2022 Serikali ilifanya tena utafiti wa nguvukazi na kuonesha kiwango cha ujuzi wa nguvukazi kimeanza kuwa bora na nguvukazi yenye kiwango cha chini cha ujuzi ilifikia asilimia 76.9 ya nguvu kazi kutoka asilimia 79.9 na kiwango cha kati kimefikia asilimia 19.9 ya nguvukazi kutoka asilimia 16.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kujiridhisha na ubora wa mafunzo yanayotolewa kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi, Serikali imepanga kufanya tathmini ya mafunzo yanayotelewa kwa kufanya tracer study katika mwaka wa fedha 2024/2025, ahsante.
MHE. RASHID A. SHANGAZI K.n.y. MHE. LATIFA KHAMIS JUWAKALI aliuliza:-

Je, Serikali imefanya tathmini ya mafunzo wanayopatiwa vijana chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu baada ya kumaliza mafunzo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamis Juwakali, lililoulizwa kwa niaba yake na Mheshimiwa Rashid Shangazi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Waziri Mkuu inatekeleza Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi nchini ambayo iliandaliwa baada ya kufanya utafiti wa nguvu kazi wa mwaka 2014 ambapo ulionesha kiwango cha ujuzi wa nguvu kazi ya Taifa ni asilimia 3.6 kwa ujuzi wa juu, asilimia 16.4 kwa ujuzi wa kati na asilimia 79.9 ujuzi wa kiwango cha chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2021/2022 Serikali ilifanya tena utafiti wa nguvukazi na kuonesha kiwango cha ujuzi wa nguvukazi kimeanza kuwa bora na nguvukazi yenye kiwango cha chini cha ujuzi ilifikia asilimia 76.9 ya nguvu kazi kutoka asilimia 79.9 na kiwango cha kati kimefikia asilimia 19.9 ya nguvukazi kutoka asilimia 16.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kujiridhisha na ubora wa mafunzo yanayotolewa kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi, Serikali imepanga kufanya tathmini ya mafunzo yanayotelewa kwa kufanya tracer study katika mwaka wa fedha 2024/2025, ahsante.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itathibitisha Mkataba Na. 189 wa Wafanyakazi wa Majumbani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Thea Medard Ntara, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya kuridhia Mkataba Na. 189 ulianza mwaka 2011 hadi 2016 ambapo ulifika hatua ya kuridhiwa kwa kuwasilishwa Bungeni. Hata hivyo, kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi na utekelezaji wa Mkataba tajwa, iliamuliwa kuwa wadau waendelee kupewa elimu kuhusu Mkataba huo kabla ya hatua za uridhiaji kuendelea. Hivyo, Serikali kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyakazi wa Majumbani CHODAWU imetoa elimu kuhusu Mkataba husika kupitia Makongamano na vikao 90 ambao ni wafanyakazi wa majumbani, Viongozi wa vyama vya wafanyakazi na waajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2023/2024, Serikali imeanza hatua ya uchambuzi wa Mkataba Na. 189 kwa kupitia Sheria na Kanuni zinazosimamia wafanyakazi wa majumbani. Baada ya hatua hizo na mapitio kukamilika, hatua inayofuata ni ya kushirikisha wadau kwa lengo la kupokea maoni yao kuhusu maeneo ambayo Serikali inapendekeza kuridhia katika mkataba husika. Aidha, Serikali itazingatia umuhimu wa vipengele vya mkataba ambavyo vitazingatia mila, desturi na uwezo wa nchi katika kutekeleza Mkataba husika, ahsante. (Makofi)
MHE. MRISHO M. GAMBO aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya mapitio ya malipo ya mkupuo (kikokotoo) ya asilimia 33 kwa wafanyakazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mrisho Mashaka Gambo, Mbunge wa Arusha Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilitangaza matumizi ya Kanuni mpya ya mafao ya pensheni kuanzia tarehe 1 Julai, 2022. Kanuni hiyo iliandaliwa kwa kushirikisha wadau wote (Serikali, wafanyakazi na waajiri) kwa lengo la kufanya maboresho ya pensheni ili kuwianisha mafao ya wanachama na kuifanya mifuko kuwa endelevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuboresha mafao ya pensheni ikijumuisha malipo ya mkupuo kwa wafanyakazi. Sheria inaitaka Mifuko kufanya tathimini ya kupima uhimilivu kila baada ya miaka mitatu na kutoa ushauri na mapendekezo mbalimbali ikijumuisha maboresho ya mafao ya wanachama na kuifanya Mifuko kuwa endelevu. Kwa kuwa Mifuko itafanya tathmini kwa hesabu zinazoishia mwezi Juni 2023, Serikali itazingatia ushauri wa mtaalam ambaye atafanya tathimini hiyo ili kuongeza Pensheni ya Wastaafu ambayo inajumuisha malipo ya mkupuo wa asilimia 33, ahsante.
MHE. KHADIJA S. TAYA aliuliza: -

Je, kwa nini Baraza la kushauri masuala ya Watu Wenye Ulemavu linashindwa kufanya kazi kama ilivyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Shaaban Taya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Baraza la Ushauri la Taifa la Watu wenye Ulemavu limeundwa kwa mujibu wa Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010 sehemu ya tatu Kifungu cha 8 hadi 12. Aidha, Sheria hiyo imefafanua majukumu ya Baraza hili ikiwa ni pamoja na kumshauri Waziri anayehusika na Watu Wenye Ulemavu juu ya utekelezaji wa Sheria za Watu wenye Ulemavu na Sheria Na. 9 ya mwaka 2010 hususani katika utoaji wa haki, usawa baina ya Wanawake na Wanaume wenye Ulemavu, masuala ya afya, marekebisho, elimu, ajira, miundombinu, mafunzo ya ufundi stadi na haki nyingine kama zilivyo katika Sheria hiyo.

Mheshimiwa Spika, Baraza limekuwa likiendelea kutekeleza majukumu yake ya kuishauri Serikali kama nilivyoeleza katika aya ya kwanza.