Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Paschal Katambi Patrobas (1 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nianze kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, lakini zaidi nami nitumie fursa hii kuwapa pole Watanzania kwa msiba mkubwa uliotufika wa kumpoteza aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Zaidi ya hapo nimpe pole Mheshimiwa Rais, lakini sambamba na hilo nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini tena katika nafasi hii.

Mheshimiwa Spia, kwa sababu ya ufinyu wa muda, niende moja kwa moja na kujielekeza katika wasilisho la bajeti la Mheshimiwa Waziri Mkuu katika ofisi yake hasa kwenye maeneo ambayo Waheshimiwa Wabunge, lakini pia Kamati zimegusia. Nianze katika eneo moja la ajira, mchango wa ajira au nafasi zinazopatikana katika ajira.

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2019 kwa maana ya kipindi cha mwaka 2015 - 2020 taarifa na maswali mengi yalikuwa yanaulizwa kuhusiana na ajira millioni nane ni kama hazipo. Sasa niwape taarifa rasmi kwamba, kwa idadi ya ajira zilizopatikana kwa awamu ya kwanza vijana kati ya umri wa miaka 15 hadi 35 ni 11,891,057 ambayo ni sawa na asilimia 52.96.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia upande wa wenye umri zaidi ya miaka 36 kwenda juu ni sawa na 10,560,488 sawa na asilimia 47.4, hii inatokana na ripoti ya taarifa ya mchanganuo wa ajira kwa shughuli na umri ya mwaka 2019 ambapo pia katika upande wa Wizara ya Fedha Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa wakati huo ambaye sasa ni Mheshimiwa Makamu wa Rais wetu, aliziandikia Wizara zote barua kuweza kutoa taarifa za kuhusiana na ajira. Hizi ndio takwimu kama zinavyojionesha hapo, kwa maana hiyo kwa kipindi hicho chote tulifanikiwa kupata ajira ya zile ambazo zilikuwa zimekusudiwa.

Mheshimiwa Spika, taarifa nyingine pia ambayo ni muhimu katika upande wetu maeneo ambayo mengi yameuliziwa zaidi ni kuhusiana na fursa ambazo vijana wetu wamekuwa wakipewa chini ya Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Katika kipindi hicho tumekuwa tukitoa mafunzo yaani internship kwa graduates zaidi ya 5,975 walikuwa wanufaika, program ya mafunzo ya ufundi stadi zaidi ya wanufaika 28,941 waliweza kupatiwa mafunzo hayo ya kujenga ujuzi na kuongeza stadi za kazi kupitia mafunzo ya uanagenzi. Pia katika program ya urasimishaji ujuzi, zaidi ya wanufaika 19,462 nao pia waliweza kunufaika na mpango huo.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni mafunzo ya kilimo cha kisasa, hapa Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ilifanikiwa kupeleka vijana 136 nchi ya Israel kujifunza namna ya kuweza kufanya kilimo cha kisasa. Hao tunakwenda kuwatumia pia kama trainer, training ilikuwa kama training of trainers ambao nao pia tutawatengenezea utaratibu wa kuweza kupata ajira kwa maana ya kujiajiri na kupewa vifaa au mikopo ili waweze kujiendeleza.

Mheshimiwa Spika, vile vile katika mafunzo ya greenhouse nchini kote kati ya mikoa ambayo ilinufaika, mikoa 12 zaidi ya Watanzania vijana 8,980 nao waliweza kupatiwa mafunzo hayo. Program hizi ni endelevu ikiwa sambamba na Mfuko wa Kukuza Ujuzi (skills development) zaidi ya wanufaika 1,550 wamepata mafunzo hayo.

Mheshimiwa Spika, katika upande wa pili kwa kujali zaidi muda nijielekeze katika eneo hili la fursa ambazo zilipatikana za moja kwa moja. Fursa za moja kwa moja za ajira zilipatikana kwa mujibu wa taarifa iliyotoka Wizara ya Fedha, baada ya kuwasiliana na Wizara zote, ni zaidi ya 11,891,772 ikiwa ni ulinganifu wa fursa za ajira zisizo za moja kwa moja 881,354…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Spika, nashukuru.