Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Neema Kichiki Lugangira (13 total)

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA Aliuliza:-

Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi wa Manispaa ya Bukoba kuwa wanufaika wa TASAF ni wananchi wenye uwezo badala ya kaya maskini:-

Je, hayo ndiyo malengo ya kuanzishwa kwa TASAF?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nami ndiyo mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu, napenda kuanza kwa kumshukuru Mungu kwa mema yote ambayo anaendelea kutujalia hadi kufika siku hii ya leo. Pili, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa imani yake kwangu na kuniteua kuwa Naibu Waziri katika ofisi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, malengo ya Mpango wa TASAF ni kuzinusuru kaya maskini katika Halmashauri zote za Tanzania Bara na Unguja na Pemba kwa upande wa Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya kwanza ya Mradi wa Kunusuru Kaya Maskini ulianza rasmi mwaka 2000 hadi 2005; awamu ya pili ilianza mwaka 2005 hadi 2012; na awamu ya tatu, kipindi cha kwanza ilianza kutekelezwa mwaka 2013 hadi Desemba, 2019; na kipindi cha pili cha awamu ya tatu kilianza Februari, 2020 hadi Septemba, 2023 ambapo jumla ya kaya maskini 1,100,000 zimeweza kuandikishwa na wanufaika kunyanyua hali yao ya kimaisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Kagera jumla ya kaya maskini 68,915 zimeandikishwa na kuingizwa kwenye Mpango huu wa TASAF. Katika utekelezaji wa kipindi cha kwanza walengwa wamepokea ruzuku kwa takribani miaka mitano. Hali hii imechangia walengwa hawa kuwa na miradi mikubwa ya uzalishaji mali kama mashamba, mifugo na shughuli za ujasiriamali ambazo zimewawezesha wao kuboresha maisha na kujiimarisha kiuchumi. Walengwa kama hao ndio wanalalamikiwa kuwa TASAF inasaidia watu wenye uwezo badala ya kaya maskini. Ukweli ni kwamba kaya hizo ziliingia kwenye mpango zikiwa na hali duni na ziliweza kujikwamua kiuchumi.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA Aliuliza:-

Je, ni kwa nini Mahakama isipewe jukumu la kugharamia chakula cha mahabusu ambao wapo gerezani kutokana na ucheleweshaji wa kesi kupatiwa hukumu?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Magereza wapo kwenye wajibu wao wa kisheria wa kutoa huduma ya chakula kwa mahabusu. Hivyo kwa mujibu wa Sheria ya Magereza Sura ya 58 (105) ambacho kinatoa mamlaka kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kutunga Kanuni (The Prison Management Regulations) ambapo Kifungu cha 23 cha kanuni iliyotokana na sheria hiyo kimemuelekeza Mkuu wa Magereza kusimamia chakula kwa wafungwa na mahabusu wanapokuwa gerezani kama sehemu ya wajibu wa Magereza.

Mheshimiwa Spika, naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Mahakama haijawahi kuchelewesha utoaji wa maamuzi ya mashauri mbalimbali bila uwepo wa sababu muhimu zinazochangia kucheleweshwa kwa kesi husika. Wote tunafahamu kuwa vipo vyombo mbalimbali vinavyohusika katika suala la kesi. Vyombo hivi ni kama Polisi, Magereza, TAKUKURU, Ofisi za Mashtaka, Ofisi ya Mkemia Mkuu na kadhalika, kabla ya kuifikia Mahakama.

Mheshimiwa Spika, hivyo katika sura ya kawaida huonekana kuwa Mahakama ndizo zinazochelewesha utoaji wa hukumu, lakini ukweli ni kwamba kesi huchakatwa na vyombo nilivyovitaja; na wakati mwingine mchakato huchukua muda mrefu kabla ya kutoa nafasi kwa Mahakama kutoa maamuzi. Hata hivyo ninatoa wito kwa vyombo husika kuharakisha michakato inayopita kwenye vyombo vyao ili kufanya Mahakama kutoa hukumu kwa wakati na hivyo kufanya wananchi kupata haki zao kwa wakati. Ahsante. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA aliuliza:-

Je, Serikali ipo tayari kupitia Sera na Sheria ya Uvuvi nchini ambayo inaonekana kutokidhi mahitaji ya wavuvi wadogo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ipo tayari kupitia Sera na Sheria ya Uvuvi nchini na katika kulitekeleza hilo, Wizara imekuwa ikifanya mapitio ya Sera, Sheria na Kanuni za Uvuvi ili ziweze kuendana na mahitaji halisi ya wakati husika na imekuwa ikifanya hivyo mara kwa mara. Kwa mfano, Wizara ilifanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Uvuvi na Mikakati yake ya Mwaka 1997 na kutunga Sera ya Taifa ya Uvuvi ya Mwaka 2015 ambayo imezingatia mahitaji ya wadau wa Sekta ya Uvuvi na Uendelevu wa Rasilimali za Uvuvi.

Mheshimiwa Spika, aidha, Wizara ilifanya mapitio ya Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania Na. 6 ya Mwaka 1980 na kutunga Sheria Na. 11 ya Mwaka 2016 ili kuimarisha shughuli za utafiti nchini. Pia, katika mwaka 2020 Wizara ilifanya marekebisho madogo kwa maana Miscellaneous amendments kwenye Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya Mwaka 2003 ili kuimarisha shughuli za ulinzi na usimamizi shirikishi wa rasilimali za uvuvi nchini.

Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kufanya maboresho makubwa kwenye Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya Mwaka 2003 ili iweze kuendana na mahitaji halisi ya sasa ya kisekta ikiwemo kutatua kero mbalimbali za wadau wa Sekta ya Uvuvi hususan wavuvi wadogo na wakuzaji viumbe maji.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwakomboa wanawake wanaobebeshwa mzigo mkubwa wa kugharamia matunzo ya watoto bila msaada wa baba?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. MWANAIDI ALI KHAMISI) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu maswali la Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Viti Maalum kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kulithibitishia Bunge lako tukufu kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wanaotoa wanawake tangu enzi za kupigania uhuru na maendeleo ya nchi kwa ujumla hadi kufikia hapa tulipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuwakomboa wanawake hawa wanaobebeshwa mimba na kuachwa bila matunzo, Serikali imeandaa Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 ambayo pamoja na masuala mengine inatoa maelezo kuhusu matunzo kwa mtoto kutoka kwa wazazi wote wawili. Sheria hii kupitia kifungu cha 7(1), kifungu cha 8(1)(a) mpaka (g), kifungu cha 8(2) na kifungu cha 9(3)(a) na (b) imetoa maelezo kwa wazazi kuhakikisha kuwa watoto wanapata mafunzo yote ya stahiki ili kuhakikishiwa kuwa haki sawa na ustawi wake vinatimizwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria hii pia kupitia kifungu cha 44 (a) mpaka (e) na kifungu cha 45(1) pia imetoa maelezo endapo wazazi wa mtoto kama hawaishi pamoja na kama mtoto atakuwa anaishi na mzazi wake wa kike yaani mama, basi mzazi wa kiume atawajibika katika kugharamia malezi ya mtoto kulingana na kipato alichonacho na mazingira anayoishi mtoto husika. Aidha, sheria hii pamoja na kanuni zake imekuwa ni msaada mkubwa katika kuhakikisha kuwa mzigo wa kugharamia malezi ya watoto unawagusa wazazi wa pande zote mbili yaani baba na mama wa mtoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe rai kwa wananchi wote kuwa jukumu la kutunza familia ni la lazima watu wote wawili na asitokee mmojawapo kutegea kwa kutotoa matumizi. Nashukuru. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA aliuliza: -

Je, ni kwa kiasi gani mifuko ya uwezeshaji kiuchumi iliyoanzishwa kwa lengo la kuwaondelea wananchi umasikini na kuwajengea uwezo wa kiuchumi imenufaisha wanawake wa kitanzania kutoka mikoa ya nje ya Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nitumie fursa hii adhimu kulishukuru Bunge lako la Jamhuri ya Muungano kwa kuwapa ruhusa Wabunge kujumuika nasi pale Mwanza katika tukio kubwa la Kitaifa la mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alikuwa akikutana na vijana na changamoto zote za vijana zilizungumzwa na kujadiliwa. Lakini pia alitoa mwelekeo mzuri wa Kitaifa wa namna gani tutakavyoenda kutatua changamoto hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge lakini pamoja na hilo sambamba Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuratibu vizuri shughuli hiyo lakini sambamba na hilo tunaenda kwa kweli kupitia Waheshimiwa Wabunge hawa kuwasaidia vijana wote nchi nzima hasa kwa kuwasikiliza, kuwapokea na kutatua changamoto zao katika maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini zaidi katika kufanya hivyo kwa kweli tutahakikisha kwamba vijana hawa wanapewa kila wanachostahili kwa Serikali kutengeneza mazingira wezeshi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa muda huo lakini pia sasa nitumie fursa hii kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia mwezi Desemba, 2020, mifuko na programu za uwezeshaji zimetoa mikopo, ruzuku na dhamana yenye thamani ya shilingi trilioni
4.34 kwa wajasiriamali 6,037,462. Kati ya hao, wanawake ni 3,079,105 sawa na asilimia 51 na wanaume ni 2,958,357 sawa na asilimia 49. Aidha, jumla ya ajira 10,844,589 zimetengenezwa kupitia uwezeshaji huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya wanawake 3,079,105 walionufaika na mikopo, ruzuku na dhamana kupitia mifuko na Programu za Uwezeshaji, wanawake 1,046,896 sawa na asilimia 34 wametokea Mkoa wa Dar es Salaam na wanawake 2,032,209 sawa na asilimia 66 wametokea katika mikoa mingine nje ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi litaendelea kuweka mikakati ambayo itaimarisha utendaji wa mifuko na programu hizi ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi na tija.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA Aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kuja na mpango mkakati wa kuwezesha NGOs kupata rasilimali fedha kupitia njia mbalimbali ikiwemo ruzuku katika maeneo mahsusi kama ambavyo inafanyika kwa Vyama vya Siasa, hasa baada ya uamuzi wa Serikali kuanzisha Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ambayo inahusisha Asasi za Kiraia katika malengo yake?
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM Alijibu: -

Mheshimwa Mwenyekiti, ahsante sana. awali ya yote kwa ridhaa yako naomba niseme maneno machache tu kwa sababu hii ni Wizara mpya.

Mheshimwa Mwenyekiti, kwanza, naomba kutoa shukrani zangu za pekee kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa maono yake makubwa ya kuunda Wizara hii mpya itakayoshughulikia masuala ya maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum.

Mheshimwa Mwenyekiti, hakika maono yake yamekuja kwa wakati ambapo kwa sasa kasi ya maendeleo kupitia msukumo wa teknolojia ni kubwa na changamoto za nchi yetu ni nyingi katika makundi mbalimbali ya jamii zetu, jambo ambalo linahitaji chombo mahususi cha kuangalia kwa kina zaidi changamoto hizi na fursa zilizopo ili kuweza kuiendeleza jamii yetu.

Mheshimwa Mwenyekiti, aidha, namshukuru kwa imani yake kwangu kuendelea kuniamini na kuniteua niweze kuisimamia Wizara hii. Mimi na timu yangu yote ambayo ametuamini tunaahidi hatutamuangusha. Tutaungana na jamii na wadau wote kuhakikisha tunaleta msukumo wenye tija kuendeleza maono aliyonayo na jamii yetu kuweza kuendelea na kuwa na ustawi.

Mheshimwa Mwenyekiti, baada ya hayo, naomba nijielekeze kwenye swali la Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum. Majibu ya swali hili ni kwamba: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa sasa haijatenga fungu maalum kwa ajili ya ruzuku kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. Hata hivyo, Serikali kwa kutambua umuhimu wa mashirika hayo kuwa uendelevu, tarehe 30 Septemba, 2021 Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliagiza Wizara kwa kushirikiana na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na wadau mbalimbali kuandaa Mpango Mkakati wa kuwezesha mashirika haya kupunguza utegemezi. Rasimu ya andiko la awali la Mpango huu imeandaliwa ambayo imeainisha njia mbalimbali za kuwezesha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuweza kupata rasilimali za kutekeleza shughuli zao. Ahsante.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA aliuliza: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kupitia upya mfumo wa haki jinai ili kupunguza changamoto ya idadi kubwa ya mahabusu kuliko wafungwa magerezani?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria naomba kumjibu Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhakikisha maboresho ya mfumo wa haki jinai nchini yanafanyika ili kuimarisha upatikanaji wa haki jinai nchini ikiwemo kuondokana na mlundikano wa mahabusu katika magereza yetu. Kutokana na umuhimu huo, Wizara imeandaa andiko la mapendekezo ya maboresho ya mfumo wa haki jinai ikishirikiana na Taasisi Zisizo za Kiserikali, Taasisi za Dini na Vyuo vinavyotoa elimu ya sheria ili kuhakikisha kwamba Mfumo wa Haki Jinai unafanyiwa marekebisho na kuwekwa sawa. Ahsante.

SPIKA: Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali nakuona umesimama.

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu wa Waziri wa Ardhi kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria ningependa kurejesha kumbukumbu sahihi za kazi ya Bunge hili kwamba Sheria Namba 1 ya mwaka 2022 iliyotungwa na Bunge hili mwezi wa pili ilizuia kufikishwa mahakamani kwa kesi ambazo upelelezi bado isipokuwa kwa makosa yale makubwa. Hiyo ni hatua moja kubwa sana na iliyolenga kupunguza msongamano wa mahabusu. (Makofi)
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA aliuliza: -

Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha mbegu za asili zenye virutubisho zinatambulika kisheria, zinalindwa, zinahifadhiwa na kusajiliwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanzisha Kitengo cha Taifa cha Hifadhi ya Nasaba za Mimea chini ya Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kwa ajili ya kuzitambua na kuzihifadhi nasaba za mimea ikiwemo mbegu za asili za mazao ya kilimo zilizopo nchini. Hadi kufikia Desemba, 2022, sampuli 10,000 ya nasaba za mimea zimekusanywa kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini na kuhifadhiwa katika Benki ya Taifa ya Kuhifadhi Nasaba za Mimea iliyopo Makao Makuu ya TPHPA - Arusha. Serikali imeanza kutekeleza taratibu za kuandaa mapendekezo ya kutunga Sheria ya Hifadhi ya Nasaba za Mimea ambayo itabainisha taratibu za kisheria za kuzitambua, kuzisajili, kuzihifadhi na kutumia mbegu za asili za mazao zilizopo nchini.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA aliuliza: -

Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha shule zote nchini zinapata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali ni kuhakikisha huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza inapatikana kwenye shule na vituo vya afya kote nchini. Katika kutimiza azma hiyo, Wizara inaendelea na zoezi la kubainisha shule na vituo vya afya vyenye changamoto ya huduma ya maji, kazi itakayokamilika mwezi Juni, 2022. Baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, kuanzia mwaka 2022/ 2023, Serikali itatekeleza mpango maalum wa miaka mitatu wa kupeleka huduma ya maji kwenye taasisi hizo.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA aliuliza: -

Je, Serikali imejiandaaje kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji nchini?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha kuna mazingira wezeshi Serikali imeendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya kufanya Biashara Nchini (MKUMBI) lakini pia kuboresha sera na sheria mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge lako tukufu, Serikali ilitunga Sheria mpya ya Uwekezaji Tanzania ya mwaka 2022 ambayo pamoja na masuala mengine imeboresha na kulinda maslahi ya wawekezaji na uwekezaji, kuboresha huduma kwa wawekezaji katika kupata vibali na leseni mbalimbali kupitia mfumo unganishi wa kielektroniki katika kuhudumia wawekezaji, kuboresha utoaji wa vivutio vya kikodi kwa wawekezaji kwa kuongeza muda kutoka miaka mitatu hadi mitano na kutoa vivutio katika miradi ya upanuzi na ukarabati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia inaendelea kuboresha miundombinu wezeshi kama barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege na umeme, nakushukuru.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA aliuliza: -

Je, kwa kiasi gani ushiriki wa Tanzania katika mikutano ya Kimataifa unazingatia upatikanaji wa fursa za kiuchumi na utekelezaji wake?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ushiriki wa Tanzania katika mikutano ya Kimataifa unalenga kupata na kutumia fursa za kiuchumi ikiwa ni pamoja na kupata mitaji, uwekezaji, masoko ya bidhaa na huduma, kukuza utalii, miradi ya kisekta, mikopo ya masharti nafuu na misaada, kujengewa uwezo wa kitaalamu na upatikanaji wa teknolojia.

Mheshimiwa Spika, ushiriki wa Tanzania katika mikutano ya Kimataifa umewezesha Tanzania kupata masoko ya bidhaa mbalimbali, kama vile mbogamboga, matunda, korosho, nafaka, utalii, malumalu na bidhaa za kioo. Vilevile nchi yetu inanufaika kwa kupata wawekezaji katika sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na utalii, viwanda, kilimo, uvuvi, mifugo, madini na nishati anuwai.

Mheshimiwa Spika, kadhalika katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Sita, ushiriki wa Tanzania katika mikutano ya Kimataifa umeiwezesha Tanzania kupata misaada mbalimbali ikiwa ni pamoja na fedha kutoka Shirika la Fedha Duniani kiasi cha shilingi trilioni 1.3 kwa ajili ya kukabiliana na janga la UVIKO- 19.

Mheshimiwa Spika, Benki ya Dunia kutenga kiasi cha dola za Marekani bilioni 2.1 (sawa na shilingi trilioni 4.8) kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kipindi cha mwaka 2023/2024 na 2024/2025, na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) kutoa dola za Marekani milioni 58.5 kwa ajili ya miradi ya kilimo kwa mwaka 2021/2022. Aidha, kupitia ushiriki katika Mkutano wa 27 wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi (COP 27), Benki ya Dunia ilizipatia Nchi za Afrika ikiwemo Tanzania, kiasi cha dola za Marekani bilioni 18 kwa ajili ya miradi ya nishati jadidifu, ahsante sana.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA aliuliza:-

Je, ni lini Sheria ya Makosa ya Mtandao na Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Pamoja na Malabo Convention vitahuishwa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha utungwaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (Personal Data Protection Act, 2022) iliyosainiwa Novemba, 2022 na kutangazwa katika gazeti la Serikali tarehe 2 Desemba, 2022. Sheria hiyo imeanza kutumika rasmi tarehe 1 Mei, 2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuweka mazingira wezeshi zaidi ya utekelezaji wa masuala mbalimbali yanayohusiana na TEHAMA nchini ikiwemo kufanikisha kufikia azma ya uchumi wa kidijitali, Serikali kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali (DTP) inaendelea na zoezi la mapitio ya Sera, Sheria, na Mikataba mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa inayohusu TEHAMA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria zinazofanyiwa mapitio kwa ajili ya kuhuishwa ni pamoja na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015. Vilevile mikataba ambayo utaratibu umeanza kwa ajili ya kuridhiwa ni pamoja na Mkataba wa Malabo.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupitia sheria zinazokinzana na Sheria Namba 4 na 5 juu ya umiliki wa ardhi kwa wanawake?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Ibara ya 24 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inampatia kila mtu bila kujali jinsia yake, haki ya kumiliki mali ikiwemo ardhi na haki ya kuhifadhi kwa mali yake aliyonayo kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, kama kuna Sheria inayokinzana na Katiba na Sheria za Ardhi Na. 4 na Na. 5 ya mwaka 1999 kuhusu umiliki wa ardhi kati ya mwanaume na mwanamke, Serikali itaanzisha mchakato wa kuzifanyia mabadiliko Sheria hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu umiliki wa ardhi kwa watoto chini ya miaka 18 wanaweza kumiliki ardhi kwa kupitia waangalizi wao kwa mujibu wa sheria.