Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Deus Clement Sangu (35 total)

MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, siyo kweli kwamba dai la ekari 495 ni jipya, bali ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani mbele ya Mheshimiwa Rais wakati huo alipofanya ziara Mkoa wa Rukwa kwamba watawakabidhi wananchi ekari 495. Lililokuwa linasubiriwa ni kukabidhi kwa maandishi kwa sababu Jeshi la Magereza limekuwa likisema kwamba hatuwezi kufanyia kazi matamko ya wanasiasa mpaka tupewe barua kutoka Wizarani. Ni lini Wizara itawapa barua Jeshi la Magereza ili kukabidhi hizo ekari 495 kwa wananchi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa tamko hili limepelekea Askari Magereza sasa kuingia kwenye mgogoro mkubwa na wananchi na kuwanyanyasa kwa kuwapiga na mara ya mwisho juzi tu hapa nilikuwa huko Jimboni, mama mmoja (na nikikurushia clip utaona) amepigwa na kugaragazwa kwenye matope. Je, Wizara iko tayari kuunda Tume itakayokuja kuchunguza unyanyasaji unaofanywa na hawa Askari Magereza na watakaobainika kunyanyasa wananchi hatua kali za kisheria zichukuliwe iwe fundisho kwa wengine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza tufike wakati tukiri kwamba kuna baadhi ya maeneo bado yana mivutano baina ya wananchi na Kambi za Magereza. Swali kwamba ni lini tutatoa hilo eneo, suala la utoaji wa eneo linahitaji taratibu, siyo suala la kusema tunakwenda na kutoa.

Mheshimiwa Spika, lingine amesema watu wananyanyaswa, wanapigwa, kitu ambacho tunakifanya kupitia Wizara, kwanza tutachunguza, tukiona kwamba kuna Maafisa wetu wa Magereza ambao wanahusika na unyanyasaji huo, hatua kali tutazichukua kupitia Wizara yetu.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii niulize maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; katika operesheni za askari wa Wanyamapori kumekuwa na tabia ya askari kunyang’anya wananchi mali ikiwemo mashine za boti, mikokoteni na mali nyingine za wananchi. Nataka kujua kauli ya Serikali ni nini kwa sababu askari hawa wamekuwa wakizikamata hizo mali, wanakuwa nazo zaidi ya miaka miwili mpaka mitatu, ambayo hiyo ni hasara kwa Serikali na kwa wananchi kuwasababishia umaskini?

Swali la pili; naomba kutokana na unyeti wa tatizo hili na hali kuwa tete katika maeneo haya; je, Naibu Waziri yuko tayari kama Wizara kuja baada ya Bunge hili ili wajionee uhalisia wa jambo hili?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, masuala ya kisheria yanapokuwa yako chini ya kimahakama, sisi kama wahifadhi tunategemea zaidi Mahakama jinsi itakavyoamua. Kwa hiyo, ushahidi mara nyingi lazima ubaki kama kielelezo tosha pale ambapo kesi inapopelekwa Mahakamani, basi ushahidi utolewe ukionyesha na vitu ambavyo amekamatwa navyo mtuhumiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala hili, kwa kuwa mhimili wa Mahakama ni sehemu nyingine tofauti na mhimili wa Wizara ya Maliasili na Utalii, hivyo kwenye masuala ya kisheria tunayaacha yanaendeshwa kisheria na vifaa vyote ambavyo amekamatwa navyo mtuhumiwa inakuwa kama ushahidi, hivyo vinaendelea kutumika mpaka pale ambapo Mahakama inakuwa imeshatoa maamuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lingine la kuamba na Mbunge, Wizara iko tayari na tutaenda kuangalia hiyo migogoro iliyoko katika eneo hilo na tutalisuluhisha kadri itakavyowezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri yanayoleta matumaini makubwa kwa wananchi wa Jimbo la Kwela naomba nitoe alert kwa Serikali, mtaalam wa upembuzi yakinifu ambaye yupo site speed yake ni ndogo sana. Niombe tu close follow-up kuhakikisha anamaliza kazi hiyo ndani ya kipindi cha mkataba.

Mheshimiwa Spika, swali langu la nyongeza; kwa kuwa barabara ya kutoka Mji Mdogo wa Laela kupitia Mnokola, Mwimbi mpaka kuunganisha nchi jirani ya Zambia ni ahadi ya Mheshimiwa Rais alipokuja kwenye kampeni. Wananchi wa maeneo ya Kata hizo zilizopo pembezoni mwa barabara wamekubali kuachia reserve ya barabara ili ijengwe kwa kiwango cha lami kwa sababu ni muhimu kwa uchumi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla. Naomba kupata commitment ya Serikali ni lini barabara hii itafanyiwa upembuzi yakinifu ili baadaye iweze kujengwa kwa kiwango cha lami?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano alipofanya ziara Mkoa wa Rukwa aliahidi ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka katika Kijiji cha Kaengesa - Seminari ya Kaengesa - Kitete kilometa saba na tayari upembuzi yakinifu umekamilika. Ni lini barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kwa kuwa wananchi wanaisubiria kwa hamu na wanataka sana kuipata hiyo barabaa ya lami? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Deus Sangu, Mbunge wa Kwela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tumechukua ushauri wake na tutahakikisha kwamba TANROADS wanamsimamia mkandarasi ili aweze kukamilisha usanifu wa kina unaoendelea ndani ya mkataba.

Mheshimiwa Spika, maswali yake mawili ya barabara ya Lahela kwenda nchi jirani lakini pia Kaengesa kwenda Kitete kilometa saba, kama alivyosema hizi ni ahadi za viongozi wetu wa Kitaifa. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo la Kwela, tumesikia na huo ndio ukweli kwamba ahadi zote zilizoahidiwa na viongozi wetu wa kitaifa zitaendelea kama zilivyoahidiwa. Kwa hivyo, Mheshimiwa Mbunge aelewe kwamba tunapoanza upembuzi na usanifu tayari ni hatua ya utekelezaji wa ahadi hizo. Tukishakamilisha basi nimhakikishie kwamba barabara hizo zitajengwa kwa kiwango cha lami kulingana na upatikanaji wa fedha kama viongozi wetu wa kitaifa walivyoahidi. Ahsante.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Wizara, naomba kuuliza:-

Serikali ina mpango gani wa kutanua mradi wa maji wa Mji Mdogo wa wa Laela ili uweze kupeleka katika Kata ya Mnokola na Miangalua kwa sababu hivyo visima vimeshindwa kukidhi mahitaji ya wananchi katika Kata hizo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Serikali inao Mpango wa kusambaza maji kutokana na vyanzo mbalimbali tulivyonavyo, na tutahakikisha tunafanya hivyo hivyo pamoja na chanzo hiki cha Rahela pia tutaenda kukifanyia kazi mwaka ujao wa fedha.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa Serikali imeanza kuwekeza fedha za awali katika scheme za umwagiliaji kama scheme ya Ilemba, Ng’ongo, Sakalilo, Mititi na Bonde la Ilembo; ni lini Serikali itapeleka fedha kumalizia hizi scheme ambazo tayari imeanza na ipo katika mipango yake?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza priority namba moja katika bajeti ya mwaka huu tunayoanza nayo ni kukamilisha scheme ambazo tulishapeleka fedha na ambazo hazijakamilika. Kwa hiyo, scheme zote zipo karibu 1000 na kidogo ambazo zimepelekewa fedha nusu/nusu hazijakamilika. Kwa hiyo, hii ni priority ya kwanza.

Kwa hiyo, nimuhakikikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine kote ambako tulishapeleka fedha na kuanza kuzifanyia kazi, tunafanya tathmini ya mapungufu yaliyopo na ukamilishaji, kwa sababu zipo scheme ambazo tulienda kujenga mifereji wakati hatujatengeneza bwawa la kuweza kuhifadhi maji, kwa hiyo, ni wastage of resources. Kwa hiyo, tunafanya hiyo tathmini na kuitambua na tuta-communicate officially kwa Wabunge kila mmoja kuweza kufahamu scheme zake zilizoko kwenye eneo lake ni lini zitaanza kufanyiwa kazi na zipo kwa sababu tuna-resource ndogo, tutapeleka scale of preference na kuchagua zipi tunaanza nazo kuweza kuzifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, priority ya pili ya bajeti yetu ya mwaka huu kwenye fedha tulizotenga ni kuwekeza fedha kwenye mashamba 13 ya kuzalisha mbegu ili tuondokane na tatizo la mbegu katika nchi kwa sababu tuna mashamba ya kuzalisha mbegu, lakini hatujawekea miundombinu. Serikali inakwenda shambani kuandaa mbegu wakati ambapo mkulima naye yupo shambani. Kwa hiyo, ni jambo la aibu, tumeamua kwamba resource tunaweka namba moja kwenye mbegu; namba mbili kukamilisha scheme ambazo tulipelekeka fedha kidogo kidogo. (Makofi)
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunip nafasi hii kuuliza swali la nyongeza. Kwanza niipongeze Serikali kwa kutupelea hiyo fedha shilingi bilioni moja. Nataka kujua sasa je, ni commitment gani ya Serikali kumalizia hizo fedha shilingi bilioni 1.7 ambazo zimebaki ili jengo hilo likamilike kwa kuwa wafanyakazi wa pale katika Halmashauri yangu wanafanya kazi katika mazingira magumu sana?

Swali la pili, kwa kuwa ujenzi wa Ofisi ya Mkurugenzi ni component inaenda pamoja na ujenzi wa nyumba ya watumishi ikiwemo nyumba ya Mkurugenzi na Wakuu wa Idara. Nataka kujua je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha jambo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Kwela kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nipokee pongezi zake kwa Serikali kwa kupeleka shilingi bilioni moja, lakini commitment ya Serikali tayari imetenga shilingi bilioni moja nyingine kwenye mwaka wa fedha 2021/2022 na shilingi bilioni moja tayari ipo Halmashauri ya Sumbawanga na kazi inaanza siku hii ya leo. Kwa hiyo, nimhakikishie kwa mtiririko huu, Serikali itaendelea kutenga fedha kuhakikisha tunakamilisha jengo la utawala katika Halmashauri ya Sumbawanga.

Mheshimiwa Spika, lakini pili, mpango wa ujenzi wa majengo ya utawala unaenda sambamba na mipango ya ujenzi wa nyumba ya watumishi kwa maana ya Mkurugenzi na Wakuu wa Idara. Kwa hiyo, safari ni hatua nimhakikishie wakati tunaendelea na ujenzi wa jengo la utawala pia tunakwenda kuweka mipango ya kuanza ujenzi wa nyumba za Mkurugenzi na Wakuu wa Idara kwa awamu, ahsante sana.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu hayo yenye matumaini makubwa nataka kujua: Je, ni lini mtaanza ujenzi wa Skimu ya Ilembe ambayo usanifu wa kina uko hatua za mwisho, ikiwa ni pamoja na kumalizia skimu ya Ng’ongo na skimu ya Sakalilo ambazo zimetelekezwa kwa muda mrefu sana? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, nataka kujua pamoja na kutambua skimu ya Mititi, Ilembo na Itela, ni lini mtaanza upembuzi yakinifu kwenye skimu hizo muhimu kwa wananchi wa Kata hizo nilizozitaja?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sangu, Mbunge wa Kwela kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba skimu hizi kwa muda mrefu zimekuwa idle na hazijafanya kazi yake kwa kiwango ambacho kinatarajiwa. Matatizo mengi ya mifumo yetu ya umwagiliaji imekuwa kwamba skimu nyingi zinajengwa na zinaishia njiani ama zinajengwa mifereji bila kuwa na vyanzo vya uhakika vya maji. Kwa hiyo, hatua ya kwanza ambayo nilitaka nimwahidi kwamba skimu ambazo tumeshazifanyia usanifu, tutaanza kuzitengea fedha kuanzia bajeti ya mwaka 2022/2023.

Mheshimiwa Spika, nimpe commitment; nilimwahidi tulipokuwa wote Rukwa na ninamwahidi tena mbele ya Bunge lako kwamba skimu hii ambayo usanifu wake upo kwenye hatua za mwisho, ni moja kati ya skimu za Mkoa wa Rukwa ambazo tumeshaziweka katika bajeti ya mwaka kesho. Kwa sababu, usanifu tulioufanya ni usanifu kamili kuanzia chanzo cha maji na mifereji mikuu na mifereji ya primary na secondary canals.

Mheshimiwa Spika, la kuhusu kwa ujumla, nataka niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwamba sasa hivi kama Wizara na wiki hii iliyopita Waziri wa Kilimo alituagiza tukae na Tume ya Umwagiliaji. Tumeanza utaratibu mpya kabisa kwenye mifumo ya umwagiliaji kwamba hatujengi skimu nusu nusu, ni heri tujenge skimu moja katika Mkoa kwa ukamilifu, badala ya kupeleka hapa shilingi milioni 50 pale shilingi 100. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, watusubiri tunavyoleta katika bajeti yetu itakayokuja, tutahakikisha Ofisi za Mikoa za Umwagiliaji zinapewa uwezo. Vile vile tutakwenda kufungua Ofisi za Umwagiliaji katika kila Wilaya ili ziweze kusimamia skimu na kuzitambua skimu zote ambazo zipo katika Wilaya zetu. (Makofi)
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Katika Jimbo langu la Kwela Serikali ilileta fedha shilingi bilioni 2.9 kwa ajii ya mradi ndani ya kata ya Ikozi, lakini mpaka sasa mradi huo haujakamilika ni kama umetelekezwa. Nataka nijue commitment ya Serikali ni namna gani ambavyo watawahakikishia ndani ya muda mfupi wananchi wa kata ya Ikozi wanapata maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sangu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, miradi yote ambayo tayari utekelezaji unasubiriwa ama umeanza Mheshimiwa Waziri ameshaagiza watendaji wetu mikoani wote kuhakikisha hii miradi inakamilika hivyo Mheshimiwa naomba nikutoe hofu kazi zinakuja kufanyika mradi lazima utekelezwe. Mama Samia anasema kumtua ndoo mama kichwani siyo option, ni lazima. (Makofi)
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza. Pamoja na nia njema ya Serikali kutaka kujenga mialo kwenye Forodha ya Nankanga na Ilanga, lakini kumekuwa na mgogoro wa muda mrefu ndani ya Ziwa Rukwa kati ya Hifadhi ya Uwanda Game Reserve na ile Rukwa Lukwati.

Je, Serikali mna mpango gani wa kuweka alama za kudumu zitakazowafanya wavuvi wafanye shughuli zao za uvuvi bila kubughudhiwa na askari wa wanyamapori wa Uwanda Game Reserve pamoja na wale wa Rukwa Lukwati?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili: Ziwa Rukwa ni moja kati ya maziwa ambayo yana mamba wengi hapa Tanzania na imesababisha wavuvi wengi kupoteza maisha. Nataka kujua, ili kuwalinda wavuvi wetu ndani ya Ziwa Rukwa, Serikali mmejipangaje kuleta vyombo vya uokozi ndani ya Ziwa Rukwa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Deus Sangu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza anataka mpango wetu juu ya kuweka maboya. Hili tutashirikiana na wenzetu wa Wizara ya Maliasili na Utalii ambayo ndiyo inasimamia hizi game reserves kwa ajili ya kuweza kuona namna tunavyoweza kutekeleza jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, halikadhalika, lile la mamba wanaokula wavuvi; kwa kuwa mamba pia ni rasilimali na inasimamiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, naomba nirejee tena katika jibu la mwanzo kwamba tutashirikiana na wenzetu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na tutafanya mkutano wa pamoja ili tuweze kutafuta suluhu ya jambo hili, ikiwemo kupata vifaa vitakavyowawezesha wavuvi hawa kuweza kuokolewa. Ahsante sana.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza kwa niaba ya Mheshimiwa Vicent Paul Mbogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu ya Serikali, lakini nina jambo moja ambalo nataka nimwambie Naibu Waziri; kwamba pesa hizo shilingi milioni 25 zilizotengwa kwa ajili ya ku-repair hizo boti na magari ni kidogo. Kwa sababu hizo boti mbili ziko beyond repair na zimekuwa grounded kwa miaka mitatu. Nataka kujua, Serikali inawaambia nini wananchi wa Jimbo la Nkasi kusini; kwamba itawapelekea lini boti mpya ili waachane na huu mpango wa kutenga shilingi milioni 25 ambazo hazitoshelezi kurekebisha hizo boti? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sangu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa matengenezo ya magari na vifaa mbalimbali katika Halmashauri kwanza ni jukumu la Halmashauri kutenga kwenye bajeti zao; kufanya preventive maintenance ya vifaa pamoja na magari. Ikiwa Halmashauri haina uwezo wa kutosha wa kifedha wa wa kufanya matengenezo makubwa kama hizi boti ambazo ziko beyond repair, wanatakiwa kwanza kufanya tathmini ni kiasi gani cha fedha kinatakiwa kufanya matengenezo yale; na pili, kuomba maombi maalum ya kupata vifaa hivyo kwa ajili ya kutoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge, kwanza wafanye tathmini, hizo boti zinahitaji kiasi gani kufanya matengenezo? Pili, Halmashauri katika vyanzo vyao wana uwezo wa kiasi gani? Kisha wasilishwe sehemu ile inayobaki ili Serikali iweze kuona namna ya kuongeza nguvu kwa ajili ya matengenezo hayo. Ahsante.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu yenye matumaini kutoka Serikalini, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, utambuzi wa Bonde la Mititi na Ilembo ndani ya Jimbo la Kwela kwa ajili ya kuanzisha skimu umefanyika muda mrefu. Sasa nataka kujua, ni lini Serikali mtaleta fedha kwa ajili ya usanifu kuanzisha skimu hizo?

Swali la pili; skimu ya umwagiliaji iliyopo Kata ya Ilemba kwa maana ya Kijiji cha Sakalilo, imetumia muda mrefu sasa, imetumia zaidi ya Bilioni Moja, na bado fedha karibia Milioni 800 kukamilisha skimu hiyo. Nataka kujua ni lini wataleta fedha hiyo ili iweze kukamilisha skimu hii ya Sakalilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Kwela, kwa pamoja kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mipango hiyo tumeiweka katika Mwaka wa Fedha 2023/2024 na imekuwa ni kilio cha Mheshimiwa Mbunge. Ahadi yetu ni kwamba tutafanya utekelezaji katika mwaka huu wa fedha na kuendelea.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa ya swali dogo la nyongeza.

Kwa kuwa katika orodha aliyotoa Mheshimiwa Waziri ya usambazaji wa minara vijijini kata zangu za Kaengesa, Mfinga, Izimba na Milepa hazimo; je, Serikali mna mpango gani wa kupeleka minara katika kata hizo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo uliagiza Wizara yetu tulete orodha hapa Bungeni, orodha hiyo ina segments mbalimbali; ina borders and special zone, phase six, miradi 763, vijiji ambavyo vimeshafanyiwa tathmini 2,116. Kama ukiangalia kwenye kata 763 haupo, basi tunaamini kabisa katika vijiji 2,116 unaweza ukawemo. Na kama utakuwa haupo basi tunaamini kwamba katika hatua za kuendelea kufanya tathmini tutaviingiza vijiji hivyo ili vipate mawasiliano, ahsante.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi ya maswali madogo ya nyongeza.

Swali langu la kwanza, kwanza niipongeze Serikali kwa nia ya dhati ya kutatua kero kwenye Mji wa Mpui na Laela kwa kutumia chanzo cha Ziwa Tanganyika na Mto Momba.

Je, ni lini mkandarasi anayefnaya Mradi wa Kaoze Group ataripoti kuanza kazi kwenye Kata ya Kaoze, Kilanga One na Kipeta?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa tatizo la maji kwenye Mji Mdogo wa Mpui ni kubwa sana na mmesema mnaenda kuchimba kisima kimoja.

Je, Serikali hamuoni kuna haja ya kuendeleza mpango wenu wa kutumia Mto Kazila kupeleka maji katika Mji Mdogo wa Mpui?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deus Sangu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimepokea pongezi, nikupongeze nawe pia kwa sababu ufuatiliaji wako katika suala hili umekuwa ni mzuri.
Mheshimiwa Spika, lini mkandarasi atakwenda, ni mwezi wa tatu mwanzoni; wiki ya kwanza ya mwezi wa tatu tunatarajia mkandarasi huyu atafika site na kuanza kazi ya mradi.

Mheshimiwa Spika, matumizi ya Mto Kazila, ni kweli usanifu ulifanyika. Mto huu upo mbali kodogo wa kilometa 21 na ipo kwenye Wilaya tofauti na ambapo mradi upo. Kwa hiyo, tutachimba kisima kwa sababu tuna uhakika tutapata maji ya kutosha kama tulivyochimba maeneo mengine katika jimbo lako Mheshimiwa Mbunge. Itakapobidi kutumia Mto Kazila kwa sababu Wizara tunahitaji kuona tunatumia vyanzo vyote ambavyo vinatuletea miradi endelevu, Mto Kazila pia tutautumia.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Swali la Kwanza; kwa kuwa, Rais wa Awamu ya Tano Dokta John Pombe Magufuli Hayati, alipotembelea eneo la Kaengesi aliahidi ujenzi wa kilomita Saba za lami kutoka Kaengesa junction mpaka Chitete. Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kuanza ujenzi wa barabara hiyo ya lami ambao usanifu na utambuzi wa barabara hiyo umekamilika?

Swali la pili; kwa kuwa, Jimbo langu la Kwela lina Miji mingi midogo, ukianza Mji wa Laela, Mpuyu, Kaengesa, Mji Mdogo wa Muze, Ilemba na Kilyamatuni, Miji hiyo ina barabara za mitaa ambazo hazijatambuliwa bado.

Je, Serikali mna mpango gani wa kuzitambua hizo barabara ili ziweze ku-qualify kupata bajeti kutoka Serikalini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Deus Clement Sangu Mbunge wa Jimbo la Kwela kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ahadi zote za Viongozi Wakuu wa nchi yetu ambazo zimeainishwa zote zipo katika mipango yetu ikiwemo barabara ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha ya kilomita Saba ambayo Hayati Dokta John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Awamu ya Tano alitoa. Kwa hiyo, ipo katika mipango yetu na tunatafuta fedha ili utekelezaji wake uanze.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la barabara ili ziweze kutambuliwa jambo hilo nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa Miji hiyo inakuwa kwa kasi na bahati nzuri ni maeneo ambayo hata mimi mwenyewe nayafahamu, basi nikuahidi tu kwamba tutatuma wataalamu wetu ili waweze kuzitambua na kuzisajili ili sasa zianze kupatiwa huduma. Ahsante sana.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga mpaka sasa tuna uhaba wa watumishi wa kada ya afya 660. Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta watumishi katika kada hii ya afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deus Sangu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kipaumbele cha Serikali kwenye vituo vyote vya afya vilivyokamilika vinavyotoa huduma na ambavyo vinatarajiwa kuanza kutoa huduma ni kupeleka watumishi ili viweze kutoa huduma. Ndiyo maana kuna ajira ambazo zimetangazwa. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge mkakati wa Serikali ni kuhakikisha watumishi wanakwenda kwenye kituo hicho pia na tutahakikisha watumishi wanakwenda kutoa huduma za afya pale. Ahsante. (Makofi)
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa ya swali dogo la nyongeza. Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa REA ndani ya Mkoa wa Rukwa speed yake ni ya kusuasua sana, hususani ndani ya Jimbo langu la Kwela kufikia mwezi Machi katika vijiji 54 alikuwa amewasha vijiji tisa. Nataka kujua comittment ya Serikali leo ili wana Rukwa na Jimbo la Kwera wajue nini hatima yao kupata umeme? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deus Sangu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe comittment ya Serikali kwamba ile mikataba yote ambayo ilitakiwa kwisha Desemba mwaka huu kwa wale wakandarasi ambao wanaendelea na kazi hizi, tutaendelea kuwasimamia kwa karibu zaidi. Tumeshawekeana deadline na timeline za mambo mbalimbali na wale ambao wanaendelea kuzikiuka taratibu ambazo tunazichukua za kisheria watazipata muda si mrefu. Kwa hiyo niwahakikishie kwamba watapata umeme kabla ya muda wa mkataba kwisha na wale ambao watashindwa tutachukua hatua mapema ili tuweze ku– rescue situations kupata wakandarasi wengine ambao watakamilisha upelekaji wa umeme katika miradi ambayo tumekubaliana.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kituo cha Polisi Mji Mdogo wa Mpui na Kaengesa vimechakaa sana na vinahudumia kata 11.

Je, ni lini Serikali inakarabati vituo vya polisi katika mji mdogo wa Kaengesa na Mpui?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deus kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake ameliuliza kwa ujumla, kwamba ni lini Serikali itakarabati vituo vilivyochakaa kama ilivyo cha kwakwe cha mji mdogo alioutaja. Nimuahidi tu kwamba pale tutakapokuwa tunapata fedha na vituo hivi vikiingizwa kwenye bajeti basi vitafanyiwa ukarabati. Atakumbuka kwamba mwaka huu maeneo mengi ikiwemo hata Zanzibar na Bara baadhi ya vituo vimekarabatiwa. Kwa hivyo nimwahidi tu kwamba kadri hali ya fedha itakavyoruhusu kituo chake pia kitafanyiwa ukarabati, nashukuru.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa ya swali dogo la nyongeza. Kutokana na mvua kubwa inayonyesha Bonde la Ziwa Rukwa, madaraja takribani sita yamesombwa na mafuriko: Je, ni lini kauli ya Serikali juu ya kurudisha mawasiliano kwa dharura katika eneo hili la Bonde la Ziwa Rukwa ambalo na Mheshimiwa Naibu Waziri unalijua fika?
NAIBU WAZIRI UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sangu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba katika kipindi cha mvua, barabara nyingi huharibika na madaraja mengi kusombwa likiwemo daraja la Mheshimiwa Sangu ambalo ni eneo la bondeni. Naomba tu nichukue nafasi hii kumjulisha ama kumpa maelekezo Meneja wa TANROADS Mkoa wa Rukwa ahakikishe kwamba anapeleka timu ya wataalam kuanza kufanya tathmini na ikiwezekana kurudisha mawasiliano ya muda na pia aweze kuleta taarifa Makao Makuu kuomba uwezesho wa fedha ili kurejesha mawasiliano haya ya kudumu, ahsante.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa fursa ya maswali madogo ya nyongeza. Kwanza, naishukuru Serikali kwa kukubali ombi hili na nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu aliahidi, wananchi wa Laela wanamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza la nyongeza; Kata ya Ilemba ina wakazi wapatao 30,000 na ni miaka kumi sasa wanajenga kituo chao cha afya, hakijakamilika: Je, Serikali ina mpango gani wa kuunga juhudi za wananchi kukamilisha kituo hiki cha afya?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; Kata ya Msandamuungano kuna kituo cha afya ambacho kinajengo moja tu la OPD; Serikali ina mpango gani wa kuongeza majengo ili kiweze kutoa huduma zote zinazohitajika katika kituo cha afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Jimbo la Kwela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata hii ya Ilemba ambayo ameitaja Mheshimiwa Mbunge ambayo wananchi wameanza ujenzi wa kituo cha afya; kwanza nitumie fursa hii kuwapongeza wananchi wa Kata hii kwa kuongeza nguvu zao katika ujenzi wa kituo hiki cha afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwahakikishie kwamba Serikali imeweka mpango mzuri wa kuunga nguvu za wananchi katika ukamilishaji wa majengo ya vituo vya afya na zahanati na tutaendelea kutenga bajeti na mara tukiwa na fedha hiyo, tutaona uwezekano pia wa kuchangia kukamilisha hicho kituo cha afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusiana na Jengo la OPD lililopo katika kituo hicho, ni kweli tuna vituo vingi vya afya vyenye majengo machache na vinahitaji kuongezewa majengo mengine, na mpango wa Serikali ni kuendelea kutafuta fedha na kupeleka kwenye majengo haya kikiwemo kituo hiki ili majengo yakamilike na kutoa huduma bora kwa wananchi, ahsante. (Makofi)
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Wananchi wa Jimbo la Kwela wamejitahidi kuanza kujenga mabweni katika Sekondari za Mpui, Mzindakaya, Milenia na Vuma. Je, ni lini Serikali mtaunga mkono jitihada hizi kwa kuwapelekea fedha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Kwela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali itapeleka fedha kuunga mkono juhudi za wananchi wa Kwela kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha. Ni kipaumbele kuhakikisha kwamba tunajenga mabweni katika shule hizi ambazo hasa ni za A- Level katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa ya maswali madogo ya nyongeza. Nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa maneno yenye matumaini kwa wananchi wa Kata ya Msanda Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Serikali imetumia fedha takribani shilingi 500,000,000 kujenga kituo cha afya katika Kata ya Kipeta, Tarafa ya Kipeta lakini mpaka sasa haijapeleka vifaa tiba;

Je, ni lini Serikali itapeleka vifaa tiba kwenye kituo hiki ambacho kilisubiriwa kwa muda mrefu na wananchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Serikali ilipeleka fedha takribani shilingi milioni 100 kwa ajili ya kujenga zahanati katika Vijiji vya Nderema, Mpembano, Mpona na Lyapona, lakini mpaka sasa zahanati hizo zimekamilika na hazina vifaa tiba;

Je, ni lini sasa Serikali mtapeleka vifaa tiba?
NAIBU WAZIRI, 0FISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii mbele ya Bunge lako Tukufu kumpongeza Mheshimiwa Sangu, kwa sababu ni majuzi tu alikuja ofisini kwa ajili ya kuangalia zahanati hizi katika Jimbo lake la Kwela. Tayari kuna milioni 150 ambayo imetengwa. Kwenye swali lake la kwanza imetengwa shilingi milioni 150 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwenye bajeti hii ya 2022/2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile nikienda kwenye swali lake la pili; kwenye zahanati zilizokamilka vilevile imetengwa shilingi milioni 50 kwa jili ya ununuzi wa vifaa tiba. Na fedha hizi mtakaponunua vifaa tiba pale Sumbawanga DC ninyi ndio mtaamua viende kwenye vituo vipi; lakini priority iwe katika hivi ambavyo vimekamilika na vinasubiri kutoa huduma kwa wananchi.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza mpango wake wa kujenga reli kutoka Tunduma mpaka Bandari ya Kasanga na Kabwe?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, reli hii ya kutoka Tunduma mpaka Rukwa, katika mwaka wa fedha ujao tutaanza kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa awali, ahsante.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Vijiji vya Kapewa na Mtetezi vilivyopo Kata ya Mpui vina changamoto kubwa ya mawasiliano. Nataka kujua ni lini Serikali mtapeleka minara katika vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, vijiji ambavyo Mheshimiwa Mbunge amevitaja vipo katika utekelezaji wa Mradi wa Tanzania Kidigitali. Ahsante sana.

MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, Serikali ilifanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika Mradi wa Kalole Group utakaohudumia Kijiji cha Skaungu, Kazi, Katonto na Kalole: Je, ni lini Serikali itaanza kujenga mradi huu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Serikali iliahidi kupitia Mradi wa MAU kuchimba visima kwenye mji mdogo wa Laela na Mpui ambapo kuna changamoto kubwa ya maji. Nataka kujua, hivyo visima vya dharura mtaanza kuchimba lini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Deus Sangu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mradi wa Kaole sisi kama Wizara tumeshajipanga kwa mwaka ujao wa fedha tutakwenda kuutekeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, maeneo haya mawili ya Laela na Mpui, Mradi wa MAU unaendelea kufanya kazi kwa maana taratibu zinaendelea kukamilishwa na tayari kwa pale Laela utaratibu umekamilika na mwezi huu wa Juni mwishoni tutaanza kuutekeleza kwa kuchimba kile kisima. Pale Mpui mkandarasi ambaye ataenda kufanya usanifu ameshapatikana na mwezi huu Juni anakwenda kufanya kazi. Mara baada ya kumaliza usanifu, tutachimba visima hivi tulivyoahidi kwa wananchi. (Makofi)
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kampuni yetu ya Mbolea ilikopesha wananchi, watu binafsi, vyama vya ushirika na Serikali zaidi ya Shilingi bilioni 18 ambayo ilisababisha kampuni ikawa na mtaji hasi: Je, Serikali ina mpango gani wa kukusanya haya madeni ili kuiongezea nguvu Kampuni yetu ya Mbolea?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la madeni ni kweli na moja kati ya kazi ambazo tumeipa management hivi sasa ni kuhakikisha inafuatilia madeni yote na kuhakikisha kwamba madeni haya yanalipwa ili kuongeza mtaji wa Kampuni ya TFC.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na mkakati wa jumla wa Serikali wa kukarabati zahanati 18 ndani ya Jimbo la Kwela lakini katika Kijiji cha Kavifuti, Kata ya Miangalua na Kijiji cha Kiandaigonda zahanati zake ni kama magofu kabisa zimechakaa. Je, Serikali wana mpango gani wa dharura kunusuru walau wananchi wapate huduma sehemu iliyo salama?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; wananchi wa Kijiji cha Kapewa, Mtetezi, Mumba pamoja na Mtapenda wametumia nguvu kubwa kujenga zahanati ambayo imebaki fedha kidogo kumalizia. Je, Serikali haioni haja ya kupeleka fedha ili wananchi wapate huduma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge, kwa kuwa anafanya kazi nzuri sana kuwasaidia wananchi wa Jimbo lake la Kwela hususan katika kufatilia haya masuala ya zahanati. Bahati nzuri maeneo haya ambayo Mheshimiwa Mbunge, anayataja hata mimi binafsi nimewahi kufika na nimeona hiyo changamoto na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilishaahidi kuyafanyia kazi. Katika sehemu ya mpango wa dharura hususan katika maeneo ya Miangalua, maeneo ya Mpui hayo yapo katika mpango wa Serikali. Kwa hiyo kikubwa sasa ni kuendelea kuyafuatilia ili yaweze kutekelezeka.

Mheshimiwa Spika, maeneo ya Mtapewa ambapo kuna nguvu kubwa ya wananchi moja ya mpango wa Serikali ni kuhakikisha maeneo yote ambayo wananchi wameweka nguvu yao, itapeleka fedha kwa ajili ya kumalizia maboma hayo, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii ya swali la nyongeza. Barabara ya Chombe, Kaoze ni barabara muhimu sana na mvua za mwaka jana zilipelekea uharibifu mkubwa na ombi maalum lipo tayari Wizarani. Nataka kujua je, ni lini Serikali itaijenga barabara hii ya Chombe, Kaoze ambayo ni muhimu kwa uchumi wa Kata ya Kaoze?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sangu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kufuatia mvua barabara zetu nyingi zimeathirika na Serikali imefanya tathmini, lakini wataalam wote Mameneja wa Mikoa na Halmashauri wameelekezwa kuleta maandiko maalum ya mapendekezo, lakini na gharama ya utengenezaji wa barabara hizo. Niwapongeze halmashauri hii wameshaleta andiko hilo, tunalifanyia kazi na mapema iwezekanavyo tutaona uwezekano wa kwenda kufanya matengenezo ili barabara ipitike vizuri. Ahsante.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa ya swali la nyongeza.

Mchakato wa mkandarasi wa kujenga barabara ya Ntendo – Muze imechukua muda mrefu takribani miezi 11 mpaka sasa. Nataka kujua ni lini mkandarasi anaripoti site kuanza ujenzi wa lami katika barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deus Sangu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Ntendo – Muze – Kiliamatundu ina package mbili; mkandarasi tayari ameshasaini kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami kilometa za awali na kilometa zingine zinazoongezeka zipo kwenye taratibu za manunuzi. Kwa hiyo, muda wowote nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge mkandarasi atakuwa site kwa ajili ya kuijenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya swali dogo la nyongeza.

Kwa kuwa, skimu ya umwagiliaji wa Ilemba usanifu wa kina umekamilika kwa asilimia 100. Je, ni lini Serikali mtaanza ujenzi wa skimu hii ambayo ni muhimu sana kwa uchumi wa wananchi wa Kata ya Ilemba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deus Sangu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mradi ambao Mheshimiwa Mbunge ameusema upo katika utekelezaji wa mwaka wa fedha unaokuja, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba mradi huo utatekelezwa.

MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii ya maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nishukuru na kuipongeza Serikali kutenga hiyo fedha ambayo itakuwa na matumaini makubwa kwa wananchi wa Mtowiso wanaosubiri barabara hiyo ya Ng’ongo.

Mheshimiwa Spika, swali langu la kwanza la nyongeza; kwa kuwa Serikali mmetumia shilingi milioni 900 kujenga barabara ya Msia - Mawezuzi, kwenda Sumbawanga Mjini na bado haijakamilika.

Je, ni lini mtaleta shilingi bilioni 1.5 zilizobaki ili kukamilisha barabara hii ipitike?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili la nyongeza; kutokana na mvua nyingi mwaka huu barabara za Kijiji cha Kamsamba ambayo inaunganisha Kijiji cha Kavifuti na Miangalua ilibebwa na maji na mpaka sasa tumeandika andiko liko Wizarani. Nataka kujua je, ni lini fedha hizo za dharura zitakuja ili kutengeneza Daraja hilo la Kamsamba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Jimbo la Kwela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali ilikuwa imetoa fedha milioni 900 na mpaka sasa tunahitaji kuongezea fedha ambapo ziko katika mchakato na mchakato ukikamilika fedha ile itapelekwa ili barabara hiyo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameianisha hapa iweze kumalizia hicho kipande kilichobakia.

Mheshimiwa Spika, lakini suala la pili, wameomba fedha kwa ajili ya barabara ambayo imeharibika kutokana na mvua na fedha hizo ni za dharura, na ni kweli hilo andiko lipo Ofisi ya Rais, TAMISEMI (TARURA) na sisi tuko katika hatua za mwisho kuhakikisha kwamba hiyo fedha tunaipata ili tulete na turekebishe barabara hiyo, kwa hiyo, hayo ndiyo majibu.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana; Daraja la Mto Mlokola ambalo lipo ndani ya Kata ya Mlokola ni daraja ambao lina hali mbaya sana na juzi tu limesababisha ajali kubwa iliyogharimu maisha ya wananchi wangu ndani ya Jimbo la Kwela.

Je, ni lini Serikali itatengeneza daraja hilo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante na napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deus Sangu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba nimuagize Meneja wa TANROADS aende kwenye daraja hili akafanye tathmini ili tujue changamoto na tuone gharama ili tuweze kurejesha mawasiliano ya daraja hili ambalo Mheshimiwa Mbunge amelitaja, ahsante. (Makofi)
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, Kituo cha Afya Msandamuungano ni kati ya vituo vya afya vilivyoko ndani ya Jimbo la Kwela na kina miundombinu chakavu kimekuwa cha muda mrefu; je, Serikali mna mpango gani wa kuboresha hiki kituo cha afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deo Sangu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tumefanya tathmini ya vituo vyote kote nchini, vituo chakavu, hospitali chakavu ambazo zitapangiwa bajeti kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Tumeanza na hospitali za halmashauri, lakini tutakwenda na vituo vya afya ili kuvikarabati au kuviongezea majengo. Kwa hiyo naomba nichukue hoja yako Mheshimiwa Sangu ili tufanye tathmini pia katika kituo hicho na kutafuta fedha kwa ajili ya ukarabati na kuongeza majengo ya maeneo hayo, ahsante sana.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Serikali imejenga vituo vya afya vitatu katika Kata ya Kaegesa, Kipeta na Kaoze: Je, ni upi mkakati wa kupeleka vifaatiba na watumishi katika vituo hivyo vya afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka wa fedha huu imetenga jumla ya shilingi bilioni 69.9 kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba kwa ajili ya kupeleka kwenye vituo vya afya. Mwaka wa fedha uliopita, halmashauri zote zilipata vifaatiba. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba zoezi hili ni endelevu na tutapeleka vifaa tiba kwa ajili ya vituo hivi vya afya lakini na pia tutapeleka watumishi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba vituo hivi vinaanza kutoa huduma, ahsante.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa ya swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, katika Bunge la Bajeti lililopita Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata aliuliza swali juu ya mgogoro huu na ulitoa maelekezo kwamba Waziri afanye utaratibu wa kuja kuangalia mgogoro huu na umalizike. Hata hivyo, nashukuru Naibu Waziri alikuja, jambo lililofanyika ni kutoa maelekezo kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wahakikishe wanashughulikia tatizo hili. Mheshimiwa Naibu Waziri hakupata fursa ya kwenda field kuona tatizo na uhalisia wake.

Mheshimiwa Spika, naomba tena nirudie, naomba tena kupitia Bunge lako, niombe Waziri aje Mkoa wa Rukwa, aende akafuatilie aone uhalisia wa tatizo hili kwa sababu suala la kumuachia Mkuu wa Mkoa limekuwepo tangu miaka 13 iliyopita ambapo Mkuu wa Mkoa, mama yangu Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya analijua vizuri. Ninataka Waziri aje na timu ya wataalam wajifunze vizuri kuliko haya majibu ambayo yanaweza yakachochea hasira na mgogoro zaidi, nakushukuru. (Makofi)
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini niungane na Mheshimiwa Mbunge kwa concern yake ya kupambania wananchi wake.

Naomba nimuahidi tarehe 17 Novemba, baada tu ya Bunge hili nitafika jimboni kwake, nikiambatana na timu ambayo tumeunda task force ya wataalam kwa ajili ya kutatua migogoro mikubwa kama hii, kwenda uwandani kuona hali halisi na kutatua tatizo hili mara moja, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa fursa ya swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, nataka muuliza Mheshimiwa Naibu Waziri; je, ni lini mtamaliza mgogoro uliopo kati ya Kata ya Nankanga, Kipeta na Kilangawani kwa Pori la Akiba lile la Uwanda na wewe mwenyewe ulikuja ukajionea mgogoro ule ambavyo unawatesa wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Deus Sangu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli nilifika katika eneo hili ambapo kulikuwa kuna changamoto kati ya hifadhi kwa maana ya maeneo ya Ziwa Rukwa pamoja na wananchi wanaoishi maeneo hayo. Lakini nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba ufafanuzi tuliutoa na tutaendelea kuutoa, na tutafika pale kuendelea kutoa ufafanuzi kwa sababu maeneo yale tunayahifadhi kwa ajili ya kuzuia wavuvi kusogea kwenye maeneo ambayo ni mazalia ya samaki.

Mheshimiwa Spika, wananchi wengi wanataka wafike wavue kwenye maeneo ambayo mwisho wa siku watajikuta wanakosa mazao ya samaki. Hivyo, hata wananchi tunapaswa kuwaeleza ukweli kwamba kuna maeneo ambayo yanahifadhiwa kwa ajili ya faida yao wenyewe. Tutafika, tutatoa ufafanuzi, lakini wananchi wanatakiwa wafahamu tunatunza kwa ajili ya matumizi ya wao wenyewe wananchi, ahsante.