Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Deus Clement Sangu (17 total)

MHE. DEUS C. SANGU Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi ya kukabidhi kwa wananchi wa Vijiji vya Msanda, Muungano, Songambele na Sikaungu shamba lililokuwa limechukuliwa na Jeshi la Magereza Mollo Sumbawanga lenye ukubwa wa ekari 495?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Jimbo la Kwela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza na wananchi wa vijiji vilivyotajwa walikuwa na mgogoro siku za nyuma ambapo mgogoro huo ulimalizwa mwaka 2019 kwa Serikali kutoa eneo la ekari 1,800 kwa lengo la kumaliza mgogoro kama ilivyohitajika.

Mheshimiwa Spika, hitaji la ekari 495 ni dai jipya ambalo Wizara kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza na Ofisi ya Mkoa wa Rukwa, tunaendelea kulifanyia kazi. Ahsante.
MHE. DEUS C. SANGU Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro wa ardhi uliopo katika vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Pori la Akiba la Uwanda?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Jimbo la Kwela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Pori la Akiba Uwanda lenye ukubwa wa kilometa za mraba 5,000 lilianzishwa mwaka 1959 na kutangazwa upya kwa Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori Na.12 ya mwaka 1974 kwa Tangazo la Serikali Na. 275 la tarehe 8/11/1974. Tangu mwaka 1974 hadi 2013 pori hilo lilikuwa likisimamiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na lilikabidhiwa rasmi kwa Wizara ya Maliasili na Utalii tarehe 20/01/2014.

Mheshimiwa Naibu Spika, pori hilo linapakana na vijiji 11 kama ifuatavyo; kuna Kijiji cha Ilambo, Kilyamatundu, Mkusi, Kapenta, Maleza, Kilangawana, Mpande, Legeza, Nankanga C, Liwelyamvula na Kipeta; na vijiji saba ambavyo ni Maleza, Kilangawana, Mpande, Legeza, Nankanga C, Liwelyamvula na Kipeta, ndivyo vyenye mgogoro na Pori la Akiba Uwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia mgogoro huo, orodha ya vijiji husika iliwasilishwa kwa Kamati ya Kitaifa ya Migogoro iliyojumuisha Wizara nane. Utekelezaji wa ripoti ya utatuzi wa migogoro ya ardhi ya Mawaziri nane, chini ya Uenyekiti wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, utaleta ufumbuzi wa mgogoro huu na migogoro mingine kama huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, tunaomba Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Kwela, pamoja na Watanzania wote tuwe na subira wakati utekelezaji wa ufumbuzi wa migogoro hii unaratibiwa. Naomba kuwasilisha.
MHE. DEUS C. SANGU aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya kilometa 200 kutoka Kilyamatundu kupitia Ilemba, Muze, Mfinga mpaka Majimoto?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Kwela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Kilyamatundu – Muze – Mfinga – Kasansa hadi Majimoto yenye urefu wa kilometa 206 ni barabara ya Mkoa inayosimamiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara nchini yaani TANROADS. Barabara hii inaunganisha Mkoa wa Rukwa na Mkoa wa Songwe eneo la Kilyamatundu na Kamsamba katika Daraja la Momba.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hii, Serikali ilianza kuchukua hatua za kuimarisha barabara hii kwa kuanza na kukamilisha ujenzi wa Daraja la Momba lenye urefu wa mita 84 na barabara za maingilio zenye urefu wa kilometa 1.2 ambalo lilikuwa ni kikwazo kikubwa sana cha mawasiliano baina ya Mikoa ya Rukwa, Katavi na Songwe.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Ntendo – Muze – Kilyamatundu ambao unahusisha sehemu ya Kilyamatundu – Muze yenye urefu wa kilometa 142. Kazi ya usanifu imefikia asilimia 50. Mara usanifu wa kina utakapokamilika, maandalizi ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami yataanza kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. DEUS C. SANGU aliuliza:-

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kusambaza Maji kutoka katika mradi wa Maji Kata za
Miangalua na Mnokola katika Jimbo la Kwela?

(b) Je, ni lini Serikali itapeleka Pesa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Kwela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa maji katika Kata za Miangalua na Mnokola ni asilimia 51.2. Kata hizi ya Miangalua inapata huduma ya majisafi kupitia mradi wa Maji wa Skimu ya Miangalua ya visima virefu vinavyohudumia vijiji vya Miangalua, Tunko, Movu, Kavifuti na Nampako vya Kata hiyo na kijiji cha Mnokola kilichopo katika Kata ya Mnokola.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha hali ya upatikanaji wa maji Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga inazidi kuimarika, Serikali imeendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji ambapo kwa mwaka wa fedha 2020/ 2021 jumla ya miradi mitano ya maji imetekelezwa na kukamilika katika Vijiji vya Nankanga na Sakalilo (Kata ya Ilemba), Milepa na Kisa (Kata ya Milepa), Kizungu (Kata ya Muze) na miradi minne ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji katika Kata za Mtowisa, Ikozi, Msandamuungano na Mufinga.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/ 2022, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 2.76 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 18 ya maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga. Aidha, Serikali itatoa fedha kwa kuzingatia miongozo ya kupeleka fedha za utekelezaji wa miradi itakayopangwa katika bajeti husika.
MHE. DEUS C. SANGU aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Ofisi za Makao Makuu ya Halmashauri ya Sumbawanga katika Mji wa Laela baada ya agizo la Serikali la kuhamisha Makao Makuu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Jimbo la Kwela kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ni miongoni mwa Halmashauri 30 zilizohamia kwenye maeneo mapya ya utawala mwaka 2019.

Mheshimiwa Spika, ili kuwezesha Halmashauri kutoa huduma bora kwa wananchi, Serikali imeweka mpango wa ujenzi wa jengo la utawala utakaogharimu shilingi bilioni 2.7.

Mheshimiwa Spika, mwezi Mei, 2021 Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuendelea na ujenzi huo. Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga imesaini mkataba wa ufundi na Chuo cha Sayansi Mbeya kwa ajili ya ujenzi utakaoanza tarehe 22 Juni, 2021.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha za ukamilishaji wa jengo hilo, ahsante sana.
MHE. DEUS C. SANGU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha Miradi ya Umwagiliaji ya Ilemba, Ng’ongo, Maleza, Mititi, Itela, Ilembo na Nkwilo katika Jimbo la Kwela?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Kwela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mpango wa Kuendeleza Kilimo cha Umwagiliaji Wilayani (DIDF), kwa mwaka 2008/2009 na mwaka 2009/2010 ilitenga jumla ya shilingi milioni 650,000,000/= kwa ajili ya kuendeleza skimu ya umwagiliaji ya Ng’ongo, yenye ukubwa wa hekta 650 ambazo ujenzi ulianza kutekelezwa mwaka 2012 na kukamilika mwaka 2013. Fedha hizi zilitumika kujenga banio na mfereji mkuu wenye urefu wa mita 1,725 pamoja na miundombinu yake.

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kupitia (ASDP II) imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwenye skimu ya umwaguliaji ya Ilembe yenye ukubwa wa hekta 800. Aidha, kazi ya kupima mashamba imekamilika na usanifu wa kina upo hatua za mwisho katika skimu ya umwagiliaji ya Ilembe.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeanza kufanya tathmini ya kina katika miradi yote ya umwagiliaji katika Mikoa ya Rukwa na Katavi. Tathmini hiyo ni pamoja kuangalia kwa kina upungufu kwenye skimu hizo na kutambua maeneo mapya na pia kufanya usanifu wa kina na kutathmini gharama za ujenzi wa miundombinu hiyo ili kuanza kutenga fedha katika bajeti zijazo.
MHE. DEUS C. SANGU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga mialo katika Forodha za Nankanga na Ilanga zilizopo ndani ya Ziwa Rukwa ili kurahisisha shughuli za Uvuvi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Kwela, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango mkakati wa Serikali ni kuhakikisha inajenga na kuboresha mialo katika maeneo mbalimbali nchini yanayojishughulisha na shughuli za uvuvi ikiwemo maeneo yanayozunguka Ziwa Rukwa kama vile forodha za Nankanga na Forodha ya Ilanga. Aidha, utekelezaji wa mkakati huu unategemea upatikanaji wa rasilimali fedha.
MHE. DEUS C. SANGU aliuliza: -

Je, nini mpango wa kujenga Skimu ya umwagiliaji Kata za Kaoze, Kipeta na Kilangawana kwa kutumia Mto Momba Kwela?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Kwela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Vijijini kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kupima mabonde ya umwagiliaji yaliyopo katika Kata za Kaoze, Kipeta na Kilangawana ili kubaini eneo halisi linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, pia ulalo wa ardhi, kiasi cha maji kwa ajili ya umwagiliaji na aina ya mioundombinu itakayohitajika.

Mheshimiwa Spika, upimaji huo utahusisha hekta 16,000 katika Kata ya Kaoze, hekta 5,000 katika Bonde la Kata ya Kipeta na hekta 7,000 katika Bonde la Maleza, Kata ya Kilangawana. Kukamilika kwa upimaji huo kutawezesha maeneo hayo kuingizwa kwenye mpango wa uendelezaji wa miundombinu ya umwagiliaji kwa kipindi cha mwaka 2023/2024 na kuendelea.
MHE. DEUS C. SANGU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo la maji kwenye Mji Mdogo wa Laela na Mpui katika Jimbo la Kwela?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deus Sangu, Mbunge wa Jimbo la Kwela kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Mji Mdogo wa Laela ni 51%. Ili kuboresha huduma ya maji Laela kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imeendelea na upanuzi wa Mradi wa Maji wa Laela na kazi zinazofanyika ni pamoja na ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilometa 2.6 na ukarabati wa tenki lenye ujazo wa lita 225,000.

Aidha, kwa upande wa Kata ya Mpui yenye vijiji vya Mpui A na Mpui B wananchi wanapata maji kupitia chanzo cha mserereko na kisima na hali ya huduma ya maji ni 36%. Ili kupunguza kero ya maji Kata ya Mpui katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali itachimba kisima kirefu kimoja.

Mheshimiwa Spika, mpango wa muda mrefu wa kumaliza tatizo la maji katika Mji Mdogo wa Laela na Kata ya Mpui, kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali itajenga mradi mkumbwa utakaotumia chanzo cha Ziwa Tanganyika au Mto Momba. Kwa sasa usanifu wa mradi huo unaendelea.
MHE. DEUS C. SANGU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga walau KM Tatu za barabara ya lami katika Mji wa Laela - Sumbawanga ambao hauna barabara ya lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu Mbunge wa Jimbo la Kwela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Ujenzi wa barabara za lami katika Mji mdogo wa Laela ambazo zitachochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa Wananchi wa Mji huo. Aidha, katika Mwaka wa Fedha 2022/ 2023 Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini inatarajia kufanya zoezi la kuainisha na kuzifanyia usanifu barabara zenye urefu wa kilomita Tatu kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hizo ili kupata gharama halisi za ujenzi.

Mheshimiwa Spika, baada ya utambuzi na usanifu wa barabara hizo kukamilika, TARURA itaweka katika vipaumbele vyake barabara hizo kwa ajili ya kuanza ujenzi katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024.
MHE. DEUS C. SANGU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupanua Kituo cha Afya cha Laela na kuwa katika hadhi ya Hospitali ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Jimbo la Kwela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya Laela kinamilikiwa na Kanisa Katoliki ambapo Mwaka 2004 kiliingia mkataba wa kutoa huduma na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ili kuhakikisha wananchi wa Kata ya Laela wanapata huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Serikali itatenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya kipya katika Kata ya Laela ambacho kitakuwa na uwezo wa kutoa huduma za afya pamoja na huduma za upasuaji za dharura.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga imeshajenga Hospitali ya Wilaya, Kituo cha Afya cha Laela kitatoa huduma kwa ngazi ya kituo cha afya, ahsante.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA K.n.y. MHE. DEUS C. SANGU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatatua changamoto za mawasiliano ya simu Kata za Milepa, Zimba, Kaengesa na Lusaka?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI, alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Kwela kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilibaini kuwepo kwa changamoto katika Kata za Lusaka, Milepa, Kaengesa pamoja na Zimba. Hata hivyo, Kata ya Lusaka imepata mtoa huduma wa kufikisha huduma za mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata za Milepa, Zimba pamoja na Kaengesa zitafikishiwa huduma za mawasiliano kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. DEUS C. SANGU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati Kituo cha Afya cha Msanda Muungano katika Tarafa ya Mpui?
NAIBU WAZIRI, 0FISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Jimbo la Kwela, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kukarabati vituo vya afya vikongwe nchini kikiwemo Kituo cha Afya Msanda Muungano kwa kutenga bajeti kwa ajili ya kuongezea miundombinu ili kuviwezesha kutoa huduma muhimu ikiwemo upasuaji wa dharura kwa mama wajawazito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa vituo vya Afya ikiwemo kituo cha Msanda Muungano katika Tarafa ya Mpui.
MHE. DEUS C. SANGU aliuliza:-

Je, lini Serikali itapeleka fedha za utekelezaji wa Miradi ya Maji katika maeneo ya Mkunda Kaengesa, Kaoze Group na Ilemba Kwela?

NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Jimbo la Kwela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza utekelezaji wa miradi ya maji ya Mkunda Group, Kaoze Group na Ilemba. Miradi hiyo inatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2023/2024 na kunufaisha wananchi wa vijiji vya Mkunda, Kaengesa A, Kaengesa B, Kianda, Ilemba A, Ilemba B, Kaswepa na Kaoze.
MHE. DEUS C. SANGU aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati zahanati 18 katika Tarafa za Laela, Mpui, Mtowisa na Kipeta?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Jimbo la Kwela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, inaendelea kufanya tathmini ya majengo yote chakavu yanayohitaji ukarabati ili yaweze kukarabatiwa na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ukarabati wa zahanati kongwe kote nchini zikiwemo zahanati 18 katika Tarafa za Laela, Mpui, Mtowisa na Kipeta katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga.
MHE. DEUS C. SANGU aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami inayounganisha Mji Mdogo wa Mtowisa na Sumbawanga Mjini kupitia Mlima Ng’ongo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Jimbo la Kwela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, awali barabara hii ilisanifiwa kujengwa kwa kiwango cha changarawe kabla ya ahadi ya Mheshimiwa Rais kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami ambapo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga shilingi milioni 875 kwa ajili ya kujenga urefu wa kilometa 25 kwa kiwango cha changarawe.

MHE. DEUS C. SANGU aliuliza:-

Je, lini Serikali itamaliza mgogoro wa ardhi kati ya mwekezaji wa Shamba la Malonje na wananchi wa Kata ya Muungano na Mollo Kwela?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dues Clement Sangu, Mbunge wa Kwela, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Shamba la Malonje linalojulikana kama Shamba Namba 48/1 Malonje katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga na Manispaa ya Sumbawanga lenye ukubwa wa hekta 10,002 liliuzwa na Serikali kwa mwekezaji ambaye pia ni Bodi ya Wadhamini wa Efatha Ministry. Mgogoro wa ardhi katika shamba hili unasababishwa na baadhi ya wananchi kutoka katika vijiji vya Msanda Muungano, Sikaungu na Songambele Azimio katika maeneo ya shamba hili yaliyo ndani ya mipaka kutwaliwa kinyume cha utaratibu.

Mheshimiwa Spika, katika kushughulikia suala hili, Serikali iliwasilisha maombi kwa mwekezaji kumega sehemu ya shamba ili igawiwe kwa wananchi na vijiji vinavyozunguka shamba hilo kwa ajili ya shughuli za kilimo. Pamoja na mwekezaji kuridhia kumega sehemu ya shamba lenye ukubwa wa ekari 3,000 ili angalau kila kijiji kipate ekari 1,000 bado wananchi wameendelea kuvamia shamba la mwekezaji.

Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa uongozi wa Mkoa na Wilaya kusimamia upangaji na ugawaji wa ardhi iliyotolewa na mwekezaji kwa vijiji hivyo ili kuondoa mgogoro uliopo. Aidha, uongozi wa Mkoa na Wilaya uwaelimishe wananchi juu ya kuheshimu mipaka ya ardhi ya mwekezaji kwa kuwa anamiliki eneo hilo kisheria.