Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Deus Clement Sangu (7 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia hotuba zote za Mheshimiwa Rais, kwanza kabisa ikiwa mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako tukufu, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijaalia kuweza kufika mahali hapa. Lakini kwa namna ya pekee wananchi wa Jimbo la Kwela kwa kuniamini kuwa Mbunge wao, naomba niwahakikishie nitawatumikia kwa nguvu zangu zote na uwezo wangu kadri Mwenyezi Mungu atakavyonijaalia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mchango wangu nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa namna alivyowasilisha hotuba nzuri sana alipolihutubia Bunge hili la Kumi na Mbili. Kuna mambo mengi mazuri yameelezwa katika hotuba hiyo, lakini mimi kwanza nianze na sekta ya madini. Kweli tupongeze hasa alivyoitendea haki kwa miaka mitano iliyopita ambayo sasa sekta ya madini imeweza kuchangia Pato la Taifa. Kutoka mwaka 2015 ilikuwa ni 3.4% na sasa sekta ya madini inachangia Pato la Taifa kwa 5.2% ni mafanikio makubwa yanastahili pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini katika hotuba yake Mheshimiwa Rais aliongelea jambo kubwa sana na kuutangazia ulimwengu juu ya kuvumbua kwa gesi ya helium ndani ya Bonde la Ziwa Rukwa. Gesi hii inaenda kuleta mapinduzi makubwa katika uchumi wa Tanzania, lakini naomba nitoe rai na juzi nilikuwa nateta na Naibu Waziri wa Madini akanihakikishia kwamba mwezi nne zoezi la kufanya inflation na drilling inaweza ikaanza, changamoto ninayoiona ni maandalizi. Mara nyingi tunakuwa na miradi mikubwa kama hii kwa mfano hii gesi ya helium wasiojuwa ni gesi yenye thamani kubwa na Tanzania tuna ujazo unaokaribia futi za ujazo bilioni 1.38 ambao tunawazidi hadi nchi ya Marekani mara mbili na ambao uchimbaji wa gesi hiyo wao mwaka huu inaelekea kufikia ukomo. Kwa hiyo sisi kama Tanzania tutakuwa tunaweza kuongoza soko hilo la dunia na kuweza kuilisha dunia kwa miaka 20 ijayo na jambo hili liko kwenye Bonde la Ziwa Rukwa ndani ya Jimbo langu la Kwela kuna hekta 3,500. Maandalizi ninayosema ni kuandaa wananchi maana yake huu mradi unaweza kwenda kwao wakaupokea kama tu muujiza kwa kuwa hawakuandaliwa yakatokea mambo kama yale yaliyotokea Mtwara.

Pili, miundombinu naona bado si rafiki sana, nadhani Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wewe ni shahidi siku ya mwaka mpya tulikuwa ndani ya eneo hilo ninalolisema ulijionea hali ya miundombinu ya barabara kuwa ni mibovu, sasa tuna mradi mkubwa kama huu, miundombinu ya barabara ni mibovu kiasi kile na hata Mheshimiwa Waziri Mkuu ni shahidi mwaka juzi ulikuja kule Bonde la Ziwa Rukwa ulijionea mpaka ukaanza kuuliza kuna njia nyingine tutarudi tena tulikotoka, lakini njia ndiyo hizo hizo Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Kwa hiyo, niombe tunapokuwa na mradi mkubwa tufanye maandalizi mazuri ili huu mradi uweze kuleta manufaa makubwa kwa taifa lakini kwa watu wale ambao wanaishi maeneo yanayozunguka mradi mkubwa kama huu.

Mheshimiwa Spika, pili nichukue nafasi hii kuongelea sekta ya kilimo na naomba hapa Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Naibu mnisikilize kwa makini. Katika hotuba yake Mheshimiwa Rais ameeleza wazi kwamba tunaagiza ngano kutoka nje karibu tani 800,000 kila mwaka, lakini nitangaze neema ndani ya Bunge lako tukufu, ndani ya Mkoa wa Rukwa tuna ekta zipatazo zaidi ya 60,000 ambazo zimefanyiwa tafiti na zinafaa kwa kilimo cha ngano. Tukiwekeza huko hakika hata hizi shortage ya tani 800,000 itakuwa historia. Tayari Mkoa wa Rukwa hasa katika Jimbo langu la Kwela eneo hilo lipo, nakuomba Mheshimiwa Waziri wa kilimo na Naibu Waziri kama mtaweza yeyote atakayeweza afike huko twendeni mkajionee jambo hili na pia tuitumie Benki ya Maendeleo ya Kilimo kwa maana ya Benki ya Kilimo waje waweze kuwawezesha wananchi ili hii shortage ambayo inatokea, sisi tumeumizwa sana, tumelima kwa nguvu kubwa, mahindi tumezalisha tani nyingi, tumebaki nayo majumbani yanaoza na mwaka huu tumelima sana hatujui tutapeleka wapi walau hii ujio wa ngano hii na sisi tutapata ahueni kama mkoa na kuachana sasa tuanze kugawa tulime nusu mahindi na nusu ngano kwa sababu mahindi yametutesa, hatujui wapi kwa kupeleka na hali ni nguvu pamoja na hayo uzalishaji huu tunaofanya unategemea tu mvua, umwagiliaji miradi mingi tuliyonayo hasa kwenye Jimbo langu ime-prove failure.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia mawazo yangu kwenye wizara hii muhimu ya Ofisi ya Rais TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu na Manaibu wake pamoja na Katibu Mkuu na timu yake, niwapongeze hakika ni timu ya wachapakazi. Katika mchango wangu wa kwanza nitaongelea mfumo wa ukusanyaji mapato wa kielekroniki, kwa maana ya Local Government Revenue Correction Information system kwa ku-link na pos machines, ni mfumo ambao Serikali ilianzisha kwa nia njema ili kukuza mapato kwenye halmashauri zetu mwaka 2016. Umeenda kwenye processes mbalimbali ya kuziimarisha lakini bado naona kuna changamoto kubwa na gap ninayoiona kwenye huu mfumo ni namna ya ku-entertain collection ya physical cash.

Mheshimiwa Spika, dunia ya leo imeenda mbali sana, mambo ya physical cash yamepitwa na wakati, lazima tutafute namna mfumo huu utakuwa friendly tuanze kukusanya mapato yetu kwa kutumia soft money, na hii ndiyo maana unaona katika ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, halmashauri zetu walikusanya zaidi ya bilioni 18 na hazikwenda benki. Sasa kwa sababu ya ku-entertain cash, ndiyo maana unakuta bilioni 18 haziendi benki.

Mheshimiwa Spika, sasa nikushauri Mheshimiwa Waziri, kama itawapendeza, nendeni mkaupitie huu mfumo kwa undani zaidi, kwasababu umekuwa na loop holes nyingi. Mfano, anayeshika hii pos machine ni mtaalamu wa TEHAMA na huyo anauwezo wa ku-delete transaction, anapigiwa simu anaambiwa bwana hiyo haikuwa laki tano ilikuwa elfu tano na hii imepelekea kwenye Hesabu za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, bilioni nne zilifutwa. Sasa hizi bilioni nne zingeweza kufanya vitu vingapi kwa kuleta maendeleo kwa Watanzania!

Mheshimiwa Spika, na nionge with very serious note, kwenye halmashauri yangu zaidi ya milioni 400 zilitoka huko nje mpaka leo tunavutana na tunakaa tunang’ang’ana tuwapeleke polisi, tuwafunge tutawamaliza watendaji woote, wa kata na wa vijiji na wote wanaoshika pos machine, bila kuja na solution ya kuondoa physical cash tukawa na ile ambayo ni soft cash, tutawamaliza na hii defaulters itafutika, itakuwa historia tena mwaka huu mki-test, mtaona na kama mnataka muone cash management solution, nendeni kwenye benki watakupa, ni gharama ndogo tuna vijana wetu waliosomea IT watatupa ujuzi huu ni namna gani tunaweza kufanya cash management solution kwenye halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa spika, kwa hiyo, nikuombe with due respect Mheshimiwa Waziri, nendeni mkaone namna ya kufanya jambo hili ni jambo jema sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia mchango wangu wa pili, naomba kuongelea mahusiano kati Wakurugenzi wa halmashauri, Madiwani na Wabunge.

Mheshimiwa Spika, nitaanza msemo mmoja kwa ruhusa yako ya kilatini, unasema Helius Beneficum cum servire regnire est maana yake ni kwamba, ni jambo jema sana na lenye baraka kuchagua wale ambao unawatumikia ni kutawala pamoja nao. Sisi wanasiasa tulivyoenda kuomba kura kwa wananchi wakiwepo Waheshimiwa Madiwani, Waheshimiwa Wabunge, tulichagua kuwatumikia, ambao kuwatumikia ni kutawala pamoja nao, lakini kuna baadhi ya halmashauri huu msemo umekuwa ni tofauti kabisa, na nitolee mfano wa halmashauri yangu.

Mheshimiwa Spika, nimebahatika kuhudhuria vikao vya finance mara mbili, nimekutana na mambo ya ajabu kabisa! Inafikia Mkurugenzi anasimama na kuwatukana Waheshimiwa Madiwani, anamtukana Mbunge, anaitukana Kamati za Hesabu za Serikali LAAC kwamba hawezi kumfanya kitu chochote, ameteuliwa na Rais, hii dharau ni ya kiwango cha juu haiwezi kuvumilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na leo hii ninavyoongea Madiwani wangu walikuwa na kikao cha baraza la Madiwani wiki hii, Mkurugenzi kwa kujisikia tu akawaita anavyotaka, wao wameenda pale wanasubiri na hivi Kamati ya Usalama na Ulinzi iko pale kesho atafanya kikao, aje asije huko ndiyo tulikoenda.

Nikuombe sana Mheshimiwa Ummy ili uweze kutusaidia sisi hasa wananchi wa Jimbo la Kwela walituchaguwa wanataka wakaone tunavyo-deliver, tunavyowaletea maendeleo, hatuwezi kuwa na halmashauri ambayo ina mgogoro, Mkurugenzi ana kiburi, kama anafikia hatua ya kuweza kumtukana Mkuu wa Mkoa, anamtukana RC, anamtukana Mkuu wa Wilaya, kuna maisha hapo tena!

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, halmashauri imebaki kama kijiwe tu pale, na nikuombe, fedha ambazo umepeleka juzi, nililikufua sana mkatupelekea bilioni 2.5, kazifuatilieni fedha hizi za mradi kwa sababu pale kumebaki kama kijiweni with very serious note. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi sikuongea kwa hiyo, nilimwambia, mimi ninaenda kwenye platform yangu Bungeni nikaeleze na Tanzania nzima isikie, kwamba sitaki mchezo, wanananchi walinichaguwa na hili nimekuomba mama, tutakutana tena kwenye shilingi ya mshahara wako, ili nihakikishe limefanyiwa kazi, halmashauri yangu imerudi kati ya halmashauri ambazo zinaheshimika na Waheshimiwa Madiwani wapewe heshima yao. Hivi kweli mtu unaitukana Kamati ya Bunge, kwamba mimi niliteuliwa na Rais, mtu anayeweza kunioji ni Rais tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na ninaomba kwa kweli tuangalie hata Walaka wa Mwaka 2011, mliwapa pawa sana wakurugenzi wakabaki kwenye loop hole ya ku-hang, mwishowe wanaanza matusi, kunidharau Mbunge, kumdharau Diwani, umedharau wananchi. Kwa hiyo, nikuombe sana, nimeongea kwa uchungu mkubwa, nadhani ndugu yangu Silinde wewe classmate wangu umenielewa, nimekueleza mara nyingi, Mkuu wa Mkoa ameleta barua nyingi RC, kumekaa kimya, nendeni mkainusuru Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niungane na wenzangu pia kuongelea jambo la TARURA, TARURA wameongea, sihami sana kwenye concept yao, twendeni tuka-review mgawanyo wa fedha hizi, huu mgawanyo umekuwa unfair! Baadhi ya halmashauri zina kilometa chache zinapewa triple au twice kuliko halmashauri zenye network kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huu ni kuumiza wengine, kuna baadhi ya kata tangia watoe, halmashauri iache kuudumia barabara, wana maisha magumu, hawajawahi kuona hata greda. Nina Kata kama Mnangalua, Kata ya Mnokola, Kata ya Nankanga, Kata ya Kalambanzite, Kata ya Kaengesa, Kata ya Kanda, ninaweza nikazitaja kata hapa, wanalia, naombeni nendeni mka-review upya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuongeza fedha TARURA ni jambo la kwanza, lakini jambo la pili, wajitahidi kuhakikisha mgawanyo unakuwa fair kwa kila halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe pia nichangie kuhusu huduma ya afya, na hii ndugu yangu Silinde utakuwa unamnong’oneza hapo Mheshimiwa Waziri. Wewe tunatokea jirani pale na Tarafa yangu ya Kipeta ni jirani pale na wewe, ile Tarafa tangia uhuru haina kituo cha afya na ina wakazi wanakaribia laki moja, wala haina miundombinu yoyote ya maji, wao wako kama wapo jangwani, ni kama wana ambao wametelekezwa. Nikuombe sana, wamekuwa wakija pale Kamsamba napo huduma zinaenda kwa kusua sua kwa ndugu yangu Conchesta pale.

Mheshimiwa Spika, nikuombe sana, angalieni namna tutaanza kuisaidia hii Tarafa ya Kipeta, ipate kituo cha afya kwa haraka. Kwasababu maisha ya wananchi hawa ni hatari, juzi watu walikuwa wanakwenda pale kijijini kwenu Mkulwe, wameliwa wananchi 15 wamedumbukia kwenye mto, tumeishia kuzika wananchi wanafuata huduma ya afya huko ng’ambo. Nikuombe sana ndugu yangu tushirikiane kwa pamoja, tuhaikishe haya mambo yanaenda ili kuweza kuleta ufanisi ndani ya halmashauri yangu na Taifa la Tanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa na hayo tu, niwaombe sana mkayafanyie kazi, hakika wananchi wangu wa Jimbo la Kwela na Waheshimiwa Madiwani wangu wao tu hawalii kilio tu cha stahiki, na kutukanwa matusi juu, na wamerudi nyuma, Mkuu wa Mkoa leo alikuwa ananipigia simu anasema, sasa tutaendaje Mheshimiwa Mbunge, nikasema hapana, wananchi walipanga mstari kutupigia kura, hili jambo lazima Serikali itatusikia na itafanya hatua ya haraka sana.

Mheshimiwa Spika, Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kutoa mchango wangu niliotumwa na wananchi wa Jimbo la Kwela na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla, kuhusu sekta hii muhimu ambayo inagusa maisha ya wananchi wa Mkoa wa Rukwa. Sitakuwa nimewatendea haki wananchi wa Jimbo la Kwela na Mkoa wa Rukwa kwa ujumla kama sitaongelea hali halisi ya zao la mahindi ndani ya mkoa wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini Mheshimiwa Aida amesema hapa na naomba nisisitize kwa umuhimu wake, leo hii inaonekana Mkoa wa Rukwa tumekuwa kama kichwa cha mwendawazimu. Mwaka jana nilipata masikitiko makubwa katika hotuba yake alivyokuwa anahutubia Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI wakati huo Mheshimiwa Jafo, akawa anasema kati ya mikoa ambayo yamechangia na kupata mapato ghafi kidogo sana na ya mwisho katika mikoa yote Tanzania ulikuwa Mkoa wa Rukwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sababu kubwa iliyopelekea tukae mkiani, sio kwasababu sisi hatufanyi shughuli, ni wavivu, hatulimi wala hatujielewi, hapana, wananchi wa Mkoa wa Rukwa wanajituma sana, tunalima na sisi ndio katika top two katika kilimo cha mahindi nchi hii, Mkoa wa Rukwa ni mmojawapo. Nimekuwa nikifuatilia sana mijadala hapa Bungeni, mwezi Februari nilisimama katika Bunge hili Tukufu, nikaongelea suala la zao la mahindi, lakini pia kuna Wabunge mbalimbali akiwepo Balozi Dkt. Pindi Chana aliuliza swali katika Wizara hii, lakini majibu ya Naibu Waziri yalikuwa ya kukatisha tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakumbuka wakati huo katika Bunge la Kumi na Moja mtu ambaye nilikuwa ninam-rank kama the best of Rukwa Region alikuwa ni Mheshimiwa Naibu Waziri Bashe, alikuwa ni front liner na champion mkubwa wa kupigania zao la mahindi, alikuwa anatoa takwimu unit cost ya production per heka na mauzo anayouza mkulima kwa heka moja. Alikuwa anasema gross loss ilikuwa ni Sh.150,000 kwa mkulima kila msimu. Bahati mbaya wakati huu hiyo gross loss anayopata Mkulima kwa heka moja imeenda mpaka Sh.300,000 yaani unapofika wakati wa mavuno, akijumlisha gharama zake za uzalishaji mkulima wa Mkoa wa Rukwa anapata hasara ya Sh.300,000, hapo hajatunza mazao, afanye hedging asubiri bei itakapopanda, hivi ninavyoongea Sh.18,000 gunia moja, heka moja Sh.700,000…

SPIKA: Mheshimiwa Deus Sangu mimi shahidi yako, nilikuwa nikikaa hapa Mheshimiwa Bashe yupo pale nyuma anashuka jinsi wakulima wa mahindi ambavyo hawatendewi sawasawa kwa hesabu kwa takwimu, sasa leo yupo wapi? (Makofi)

MHE. DEUS C. SANGU: Yuko hapa.

SPIKA: Haya endelea kuchangia Mheshimiwa.

MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniunga mkono. Kwa hiyo Mheshimiwa Bashe ni msalaba wake huu, is your baby, naomba leo wakiwa wa Waziri hapa Profesa waje watuambie wananchi wa Mkoa wa Rukwa na Nyanda za Juu Kusini, wanawapa habari njema. Habari ya kusema kwamba mipaka ipo wazi, hiyo sio stori brother, lazima waanzishe marketing intelligent system waende kwenye nchi hizo ambao wanadhani ni masoko, mpaka unaweza ukawa wazi, lakini sio wazi kwa Tanzania pekee, Zambia wanaangalia hiyo mipaka iliyo wazi; Kenya wanaangalia mipaka iliyo wazi; DRC wanaangalia mipaka iliyo wazi na Burundi hivyo hivyo.

Mheshimiwa Spika, sasa wakikaa kwenye madawati huko Wizarani wanasubiria tu kwamba mipaka iko wazi you will wait until the next coming of Jesus Christ. Kwa hiyo namwomba sana Mheshimiwa Waziri kwa Mkoa wetu wa Rukwa, leo hii halmashauri zetu zime-paralyze, hazina mapato, sisi hatuna migodi ya dhahabu, hatuna jambo lolote tunalotegemea zaidi ya zao la mahindi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bahati mbaya hadi mpunga sasa umeshuka bei. Mwaka jana hali ilikuwa ngumu. Halmashauri zetu zote katika Mkoa wa Rukwa zimeshindwa kukusanya mapato. Tumeshindwa kujenga madarasa, tumeshindwa kujenga zahanati, tumeshindwa kuboresha vituo vyetu vya afya, maisha ni magumu watuonee huruma wananchi wa Mkoa wa Rukwa, tumechoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna solution zinatolewa kwamba substitute, twende tupeleka mikorosho na wakituletea mikorosho its good initiative, lakini haitoshi, wakileta mikorosho ina maana tuache kulima mahindi. Tukiacha mahindi maana yake nchi itaenda kwenye baa la njaa, baadaye wataanza kuhangaika kutafuta mahindi sehemu nyingine. Kwa hiyo, hatutaki korosho iwe ni replacement ya mahindi, tunataka iwe ni alternative tu, anayetaka ku-jump kwenye korosho ataenda, anayetaka ku-jump kwenye mazao mengine ya kimkakati ataenda, lakini hatutaki mahindi yawe replaced, tunataka mahindi yabaki kuwa pale pale, kwa sababu wakati wa njaa sisi ndio mkombozi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi ikiingia kwenye matatizo ya njaa, Wizara inakimbilia Rukwa, sasa hivi mazao tumefanya over production wanaanza kutukimbia wanatukwepa na sababu ndogo ndogo. Nilienda front line, tukaenda mpaka wa Waziri Mkuu tukamwambia huu ni mwezi Februari Mheshimiwa Waziri Mkuu tunaomba na akaja kusema ndani ya Bunge hili Tukufu kwamba tayari tutaunda timu itakayoenda huko Kongo na Burundi ili ku-secure hayo masoko.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuwa na dhamira njema na safi, lakini naona watendaji wake hawaendi na sauti ile, ilitakiwa tamko la Waziri Mkuu hapa liwaamshe, waje tukae Wabunge wa Mkoa wa Rukwa na management ya Mkoa wa Rukwa, twende huko, baadaye tutakuta yale masoko yameenda, hatuna soko la mahindi, confidence ya wakulima imepotea, wamekata tamaa.

Mheshimiwa Spika, nawaheshimiwa sana Mheshimiwa Bashe na Mheshimiwa Waziri, sitaki kesho niendeshe mgomo wa Wabunge wa Nyanda za Juu Kusini, tuwawekee mgomo wa Bajeti yao mpaka waje na kauli thabiti, kauli ambayo sasa tukirudi mwezi Julai kwenye ziara kwa wananchi, tuwe tunawaambia jambo linaloeleweka sio stories. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda, naomba tu niseme hayo kwa uchache, ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia kutoa mawazo yangu katika Bajeti Kuu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nichukue nafasi hii kufikisha salamu za wananchi wangu wa Jimbo la Kwela. Wamenituma nisimame ndani ya Bunge hili Tukufu nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Rais kwa mambo makubwa aliyotufanyia. Mwanzoni mwa Bunge hili nilikuja kulalamika, tulikuwa na maafa makubwa; madaraja karibia 18 yaliondoka katika Jimbo langu. Nashukuru Mheshimiwa Rais katika Awamu hii ya Sita ametutizama kwa jicho la huruma, ametuletea fedha takribani shilingi bilioni 3.6 za kwenda kurekebisha madaraja haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haitoshi katika barabara ya Kata 13 za Bonde la Ziwa Rukwa, Mheshimiwa Rais ametukumbuka katuletea shilingi bilioni 4.8. Kwa kweli wananchi wamesema tufikishie pongezi kupitia Bunge hili Tukufu ili Mheshimiwa Rais ajue Wana-Kwela wanathamini jinsi anavyowajali na anavyowakumbuka wakati wa matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, isitoshe ametuletea shilingi bilioni moja kujenga ofisi ya Makao Makuu katika Mji Mdogo wa Laela na shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya miradi ya afya na elimu. Wananchi wa Jimbo la Kwela ndani ya kata zote 27 wanampongeza Mheshimiwa Rais, wanamwombea afya njema na siha, aendelee katika speed hii hii aliyoionesha ndani ya miezi hii mitatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, isitoshe, shilingi milioni 500 ambazo tumetangaziwa neema na Waziri, dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu, pia shilingi milioni 600 za barabara; na wananchi wa Jimbo la Kwela pia wanamshukuru Mheshimiwa Rais na timu yake ndani ya Serikali kwa namna ambavyo amekuja kwa kasi ya ajabu kuwaletea wananchi maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna shukurani ambazo nimetumwa na Waheshimiwa Madiwani wa Jimbo langu kwamba katufikishie salamu kwa kutukumbuka. Nasi tunaanza kulipwa kutoka kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina. Shukrani ya pekee wanaomba, angalau hii isiishie hapa, iwekewe sheria maalum ili kesho asije mtu mwingine akabadilisha kwamba hii ilikuwa batili. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, nakuletea hii habari ya Madiwani wangu, naomba uisikilize na mkaifanyie kazi, muifanyie reinforcement. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nitoe pongezi kwa Wizara hii ya Fedha. Nakupongeza ndugu yangu, First Class Economist, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, kwa kweli unaitendea haki hiyo First Class yako ya uchumi. Ndugu yangu kwenye Kamati yangu tulikuwa naye PAC, tulikuwa tunamwita Engineer wa Kamati ya PAC. Kweli kazi mnayoifanya kwenye Wizara hii ya Fedha mna- deserve sifa kubwa sana, mmetuletea bajeti ambayo ni realistic, ambayo inakuwa communicated. Tunai- communicate vizuri kwa wananchi na wameielewa. Naomba kwa spirit mliyokuja nayo mwendelee hivi hivi. Kweli Watanzania wanaanza kupata matumaini makubwa kutokana na bajeti hii ya kwanza katika Awamu hii ya Sita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa pongezi zangu, nina mambo ya kuishauri Serikali. Naomba hapa tusikilizane vizuri kwa umakini mkubwa sana. Ni-declare interest kwamba, nisipoona mkulima wangu au wakulima ndani ya nchi hii wanatetewa, nakuwa mnyonge kwa sababu kwanza mimi binafsi ni mtoto wa mkulima. Nimekuja niongelee jambo moja kwa umakini mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, NFRA - Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula, ndiyo instrument pekee ya Serikali ambayo inaweza ikawa na touch au DNA na wakulima wetu kwa sababu hili ndilo soko la uhakika la wakulima kwa mazao yetu ya nafaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilikuwa napitia bajeti hapa. Tumewatengea bajeti ya shilingi bilioni 14. Mwaka wa fedha uliopita ilikuwa shilingi bilioni 15; kwa hiyo, kila mwaka tunapunguza kidogo. Miaka minne back hapo, tulikuwa tunawatengea shilingi bilioni 100. Sasa tunapoi-cripple hii NFRA maana yake tumeamua tuwazike wakulima wetu na hawa ndio wata-participate vizuri katika ku-implement bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tukafikirie, NFRA ina vyanzo vingi, achana na grant ya Serikali, wao pia walikuwa na room ya kwenda kukopa kwenye Commercial Bank. Mwaka 2019/2020, nina story naisikia kwamba mmewazuia Wizarani kwako Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, fieldmarshal, nasikia hamtoi vibali, wakakope. Wamekopa shilingi bilioni 35, lakini wamerudisha kwa uaminifu mkubwa, mpaka Commercial Bank nyingine wamethamini kwamba NFRA ni wateja wazuri. Hizi hela hawaendi kulipana posho, zinaenda kununua mazao hata kwa dada yangu, Mheshimiwa Jenista Mhagama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana, nendeni mkatoe hicho kibali NFRA wakachukue hizo bilioni nyingi, warudishe kwa wakulima, wanunue mazao; na kwa sababu jukumu lao ni kutafuta masoko nje, wataenda kuuza huko, tutafanya recycling ya ile, itarudi tena kwenye mzunguko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa construction industry imefanya vizuri tume-invest mabilioni ya pesa; na ndiyo inafanya vizuri, ime-contribute asilimia 13 katika uchumi; kilimo 4.8; lakini investment kwenye kilimo ni short term investment ambayo impact yake tunaiona kwa haraka. Msiwanyime, waende kwenye Commercial Bank na ziko willing kutoa hiyo mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba kabisa, ndugu zangu naamini ninyi ni wasikivu, naombeni msikilize ili mkawakomboe wakulima. Kwa sababu mtapopeleka fedha ile tunaongeza purchasing power yao na ndio hao wataweza kuonja kwamba tuko kwenye uchumi wa kati, kwa sababu ya fedha zile tulizowapelekea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja ambalo limekuwa likisikitisha na hili naomba niongee nikutwishe mzigo dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama. Kutokana na ripoti ya CAG, inaonesha NFRA ilikopwa na Kitengo cha Maafa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, shilingi bilioni 167. Hizi zinanunua karibia tani 365,000. Sasa miaka 12 hamjarudisha hata senti moja, nendeni mkaweke utaratibu mzuri tukawalipe walau kwa installment 12 years, hawarudishiwi kitu chochote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutai-paralyse hii institution ya NFRA ambayo ni muhimu sana kwa wakulima wetu masikini wakiwemo wakulima wa Mkoa wa Rukwa, Ruvuma, Njombe na Iringa wanaitegemea sana NFRA. Nawaomba mwende kama Wizara, m-discuss jambo hili muone ni namna gani ambayo mtarudisha hizi fedha kwa wakulima. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULAMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULAMAVU: Namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kukumbusha hilo deni ambalo anasema limejitokeza kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu. Naomba tu kumpa taarifa kwamba deni hilo ni yale mahindi ambayo yanakwenda huko huko kwenye Halmashauri za Waheshimiwa Wabunge ili kushughulikia matatizo mbalimbali wakati wa maafa na vitu vya namna hiyo, lakini hasa wakati wa maafa, ndiyo yale mahindi tunayowaletea huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote, ulizaneni kwenye Halmashauri zenu; Halmashauri ambazo hazijalipa zirudishe hiyo fedha haraka sana ili iweze kufanya hiyo kazi ambayo Mheshimiwa Mbunge anaishauri.

Kwa hiyo, naomba nitoe hiyo taarifa, nadhani Mbunge atakubaliana nami Halmashauri waharakishe kurudisha hizo fedha. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Mbunge unapokea taarifa hiyo nzuri?

MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Taarifa hiyo naipokea, lakini mzigo mzigo tunawakabidhi Wanyamwezi kwa maana Ofisi ya Waziri Mkuu watusaidie kulibeba hili. Huko Halmashauri ni wadogo, likiwa kwa mkubwa, Waziri Mkuu naamini litafanyiwa kazi kwa umakini mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme jambo moja. Nchi yetu kama Tanzania tuna advantage kubwa. Kwenye uzalishaji; productionwise na locationwise katika nchi zilizopo kwenye ukanda wa Maziwa Makuu, tuna faida kubwa. Sasa NFRA walishapewa mandate; katika dhima yao mojawapo ni kuhakikisha usalama wa chakula nchini kwa kununua, kuhifadhi na kuzungusha chakula. Kwa hiyo, wanaruhusiwa kufanya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Waziri Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na Naibu hapo, tusaidieni, kaiwezesheni hiyo ofisi ika-capitalize hayo masoko yaliyopo katika nchi za Maziwa Makuu ili tukawanusuru wakulima wetu. Kama tukiwa serious kweli kuiwezesha hii NFRA, nawahakikishieni nchi yetu tutaenda vizuri katika sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuwa mchangiaji wa kwanza jioni ya leo. Katika hoja tatu kubwa zilizowasilishwa jioni ya leo. Hoja ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Hoja ya Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma na ile Kamati ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, katika fursa hii niliyopata mimi mjadala wangu utajikita katika taasisi kubwa mbili. Leo nitajadili Fungu Namba 28 – Jeshi la Polisi na Fungu Namba 93 – Jeshi Uhamiaji. Katika ripoti ya CAG na ripoti iliyowasilishwa leo na Kamati ya PAC kuna mambo muhimu ambayo yamezungumzwa; na mimi katika uchambuzi wangu nitaanza na Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Jeshi la Polisi, katika ripoti ya CAG na ripoti ya Kamati imeonesha ndani ya Jeshi la Polisi kuna mfuko ambao ulianzishwa na Jeshi la Polisi unaoitwa Reward and Fine Fund ambao kwa jina lingine unaitwa Tuzo na Tozo. Mfuko huu ulianzishwa kwa nia njema. Nia ya Serikali au Jeshi la Polisi ilikuwa ni kwa ajili ya ustawi wa Polisi ili kuwawekea mazingira mazuri, ikiwemo ujenzi wa nyumba zao na miradi mbalimbali. Lakini uanzishaji wa mfuko huu ulikuwa na sheria yake, na sheria ile ilitungwa; na kulingana kufuatana na taratibu na mahitaji ya sheria ya fedha na kufuatana na kuanzishwa kwa mfuko huu miaka 10 ilitakiwa kwanza ipate idhini, kwa maana kanuni zitungwe na Waziri mwenye mfuko husika.

Mheshimiwa Spika, lakini cha ajabu mpaka hivi ninavyoongea ni zaidi ya miaka kumi na CAG amebaini kwamba mfuko huo umekuwa ukipokea ela na unafanya matumizi lakini Waziri hajawai kutunga kanuni zinazoelekeza namna fedha zitumike. Tafsiri yake ni kwamba mfuko umekuwa ukijiendesha kienyeji.

Mheshimiwa Spika, nataka kusema, kwamba fedha zimekuwa zikikusanywa na chanzo kikubwa cha fedha kwenye mfuko huu ni huduma ambazo wamekuwa wanazitoa kwenye ulinzi wa taasisi za fedha, migodi na sehemu nyingine. Mfuko huo una fedha nyingi na Jeshi la Polisi linaweza kukusanya bilioni 10 hadi bilioni 15 kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, lakini fedha hizi hazina mwongozo wa kanuni uliotungwa na Waziri, hakuna Mhasibu wa kusimamia mfuko huu na haujawahi kukaguliwa tangu uanzishwe na CAG, na, hakuna hesabu zilishawahi kufanywa kwenye mfuko huu. Bahati mbaya huu mfuko kuna ukiukaji mkubwa sana. Kwa mfano mkataba unaingia na taasisi ya fedha, let us say wanaingia mkataba wa milioni 80 kwa mwezi; sasa mchezo unaofanyika ni kwamba, wale Askari wanaopangiwa kwenda kufanya majukumu wanalipwa posho kutokana na hizo fedha, na baadaye Jeshi la Polisi likihitaji malipo wanakata kulingana na ile fedha waliolipa kwanza wale Polisi waliotoa huduma.

Mheshimiwa Spika, maana yake ni kwamba kunafanyika matumizi ya fedha mbichi. Yaani ina maana wanafanya invoice discounting wanachukua ela yao mapema. Hapa pana-create mwanya, fedha zinaweza zikachukuliwa nyingi. Kama Jeshi la Polisi lilitakiwa kukusanya milioni 80 unaweza ukakuta mwisho wa siku invoice wanayo peleka ni milioni 20, milioni 80 zimechukuliwa zikiwa mbichi.

Mheshimiwa Spika, mimi sipingi askari wetu wanapofanya kazi ya kulinda malindo haya kupewa risk allowance, lakini risk allowance lazima iwe na utaratibu wake kwa miongozo ya Sheria ya Fedha. Huwezi ukachukua tu huko benki unakolinda kwamba wanakulipa huko huko. Benki au migodi imeingia mkataba na Jeshi la Polisi, kwa hiyo ilibidi fedha zote ziingie kwanza kwenye mfuko halafu Jeshi la Polisi lifanye arrangement ya kuwalipa askari kule kule na si kule wanapofanya kazi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jambo hilo limeendelea na haijulikani sasa utaratibu upi wanafanya ili kufanya reconcialiation ya fedha hizo. Hivyo, Kamati iliona na CAG aliona kupitia mazingira haya kunaweza kukawa na upotevu wa fedha nyingi kwa sababu control yake ni ngumu.

Mheshimiwa Spika, CAG alielekezwa kwenda kufanya ukaguzi maalumu kwenye mfuko huu ambao umekaa zaidi ya miaka kumi haujafunga hata hesabu zake. Mpaka sasa hivi kuna kigugumizi na ushirikiano wanaopata ni mdogo. Sasa nashindwa kuelewa ni kwa nini CAG hapewi ushirikiano wa kufanya hii special audit ili sasa umma ujue na sisi Wabunge kwa niaba ya wananchi tujue, fedha hizo zilizokusanywa kwenye mfuko huo ni kiasi gani, matumizi yake yalikuwa yapi na kwa nini kanuni ya kuongoza na kuguide namna ya matumizi ya mfuko huo hazijatungwa mpaka leo? Sipati majibu ya mambo haya na mabo yanaendelea.

Mheshimiwa Spika, Mfuko huu ni mfuko ambao una fedha nyingi, na umesikia mara nyingi hata Mheshimiwa Waziri akiwa anajibu maswali ya Waheshimiwa Wabunge, wakiomba kituo cha Polisi anawaambia tutaenda kuchukua kwenye tozo na tuzo. Lakini hiyo, tozo na tuzo haina control yoyote, ni kama kichaka fulani hivi. Sasa hatuwezi katika nchi hii, na hizo fedha hazipitishwi wala haziidhinishwi na Bunge, zinaishia huko. IGP anamwandikia Pay Master General; anataka bilioni 10, zinakuja kwa IGP zinaenda kwenye matumizi moja kwa moja, hakuna utaratibu wa namna hiyo. Hivyo, kuna ukiukwaji wa Sheria ya Fedha maana hakuna control yoyote wala hesabu zinazowekwa.

Mheshimiwa Spika, sasa niombe nishauri mambo yafuatayo; mfuko huu una fedha nyingi, pamoja na kutumika hadi anapoondoka CAG zipo fedha kwenye akaunti yao huko BOT, bilioni 35 karibia na milioni 300 na kidogo, na bado wanaendelea kukusanya. Niombe, kama tuna nia njema na tunataka kuweka transparency kwenye matumizi ya fedha za umma, niombe mambo yafuatayo: -

i. Wa-suspend matumizi kwenye mfuko huu mpaka kanuni ziundwe na Waziri mwenye dhamana.

ii. Serikali ijikite kwenda kumpa CAG ushirikiano afanye audit ili tujue kuna nini na fedha hii imetumikaje kwenye mfuko huu.

iii. Tuombe wakaandae hesabu, inakuwaje mfuko ambao hauna mhasibu upo tu na billions of money zipo tu zinachukuliwa kiholela. Waende pale wakatuandalie hesabu na sisi tuweze kujua ni jambo gani linaendelea kwenye mfuko huu wa tozo na tuzo.

Mheshimiwa Spika, Kuna njia rahisi, tuwasaidie Serikali, tunahangaika tunashida na vituo vya polisi nchi nzima. Tengenezeni arrangemet kwani kile chanzo kina fedha ambazo ni stable and sustainable, nendeni kwenye financial institution mkaombe mortgage mjenge kwa wakati mmoja Vituo vya Polisi nchi nzima. Halafu, kwa kuwa ile fedha kwa kuwa source iliyo stable mtaenda kulipa huo mkopo na tutakuwa na Vituo vya Polisi nchi nzima bila upendeleo na kila mtu ataona manufaa ya mfuko huu, kuliko wakati huu ambapo IGP akiwa huru ataona sasa hivi nina interest na sehemu gani ngoja nikajenge majengo hapa. Akiondoka IGP huyo ana-abandon majengo yale anakuja IGP mwingine anaanzisha uelekeo wake.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hatuna direction kwenye mfuko huu. Kama nchi tutafakari kwa pamoja, twende tukafanye jambo la muhimu kwenye mfuko huu, ili uletwe. Na kwa kuanzia mwaka wa fedha ujao tupitishe hapa makadirio ya mapato na matumizi ya mfuko huu ndani ya Bunge hili na hapo ndipo tutakuwa tumefanya kazi. Tumekosea sana tumevunja Sheria ya Fedha, hatujali tunaenda tu.

Mheshimiwa Spika, niombe sana, Serikali ipo hapa, hili jambo mkiendelea ni bomu kubwa sana, kuna ubadhirifu mkubwa upo hidden kwenye huu mfuko. Mkiuacha bila Kwenda kuufanyia hatua za haraka bomu litakuja kulipuka, tusije tukalaumiane.

Mheshimiwa Spika, hilo nimemaliza. Nadhani watakuwa wamenielewa juu ya mfuko huu wa tozo na tuzo. Niwaombe kabisa tena mambo mengine ya kuja kutuambia tutakwenda tutaenda kuchukua; m-suspend huo mfuko mpaka mfuate taratibu zote zinazo wahitaji kama Serikali ili kusiwe na mkanganyiko. Hiyo nimemaliza naomba niende kwenye fungu lingine la uhamiaji Fungu Namba 93.

Mheshimiwa Spika, hii ni taasisi nyingine iliyo ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Mambo ya kusikitisha kabisa, nitatoa literature moja juu ya kilichotokea pale Uhamiaji. Alisema hapa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, kuna habari ya stickers za visa. Hizi stickers za visa ni kichaka ambacho kinagharimu Taifa letu hasara kubwa. Wale Maafisa wa Uhamiaji ulikuwa ni mradi wao wa kujitengenezea mabilioni.

Mheshimiwa Spika, walikuwa na mambo mawili; mwaka 2019 CAG alienda pale kufanya special audit tena ilikuwa ya interval ndogo ya miezi sita, kuanzia Januari mpaka Juni, 2019, kukagua namna ya utoaji wa stickers za visa kwa wageni wanaokuja ndani ya nchi. Alikutana na maajabu makubwa sana. Alikuta kwanza kuna visa zaidi ya 33,500 zilizotolewa ni fake. Yaani wale Maafisa Uhamiaji walienda kujitengenezea hizo stickers, wakagawa, wakachukua hela, wakaweka mfukoni zaidi ya Shilingi 3,800,000,000/=, maisha yakaendelea business as usual.

Mheshimiwa Spika, walipoendelea kukagua wakakuta zaidi ya visa 21,705; zilipokelewa fedha zikaingizwa kwenye database ya Uhamiaji, baadaye wale Maafisa wakaenda kufuta zile taarifa zote kwenye database, wakachukua zaidi ya Shilingi 2,516,000,000/= wakagawana wafanyakazi 40, maisha yakendelea, business as usual. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kilichokuja kutokea sasa, Maafisa saba wakapelekwa Mahakami wakafunguliwa kesi ya Uhujumi Uchumi kwenye Mahakama Kuu Moshi. Wakakaa pale gerezani miaka miwili, baadae DPP akafanya nolle prosequi kwamba sina nia ya kuendelelea na kesi hii. Wakarudi kazini, wakaendelea kupiga maisha. Tuki-audit mwakani tutakuta wametupiga tena Shilingi bilioni sita, business as usual. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, lazima kama Taifa tutafakari. Watu 40 wamekula vituo vya afya sita peke yao, na wamerudishwa kazini, wameingia kwenye payroll na maisha yanaendelea. Sisi tunakuja kupiga kelele hapa, tutawasadiaje Watanzania masikini tuliowaacha huko Vijijini, waliotutuma ndani ya Bunge hili? Watu wachache wananufaika na fedha za Umma.

Mheshimiwa Spika, nawaomba sana watu wa Serikalini, ninyi mliopewa dhamana na Mheshimiwa Rais, katusaidieni katika mambo haya. Kuwaachia watu wanakula fedha, wamerudi wako ofisini na hiyo audit ilikuwa ni trend a miezi sita, just imagine kama unge-audit ya miaka mitano, si ungekuta karibia bajeti ya Wizara nzima watu saba wamekula, business as usual na maisha yanaendelea! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili la Uhamiaji nadhani message mmeipata vizuri kitu gani nakusudia kusema. Nendeni mkafanye upya, mrudie na ule mfumo, hao watu walienda kufuta vitu kwenye database. Ule mfumo mmeuanzishaa upya, nendeni pia mkafanye reconciliation baada ya ku-abandon ule mfumo wa zamani: Je, huu mfumo mpya una-address yale matatizo? Au mme-create mfumo mpya ambao ni loophole nyingi kutupiga zaidi na zaidi! Kwa hiyo, nawaomba watu wa Serikali mkawe makini kuangalia hasara tuliyosababishwa, lakini watu hawa waliosababisha wizi wa namna hiyo kuwarudisha ndani ya Uhamiaji ina-send message mbaya kwa wale waliopo mle, kwamba, kumbe unaweza ukapiga hela! Mimi napokea mshahara wa Shilingi 800,000/=, mwenzangu kapiga Shilingi bilioni mbili kaenda kupumzika kidogo gerezani mwaka mmoja amerudi, tumeendelea na Shilingi bilioni mbili na hakuna chochote! Naye atakuwa attempted, atachukua naye Shilingi bilioni tano, naye ataenda kukaa gerezani mwaka mmoja atarudi nolle prosequi, maisha yataendeleea. Ndugu zangu, haya ni mambo ya kusikitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna jambo kubwa ambalo pia niwaombe watu wa Serikali, nimepitia sana ripoti ya CAG katika area ya compliance kwenye Public Procurement Act. Yaani taasisi hii, ile sheria ni kama wameiweka huko kwenye kabati wanajiendeshea mambo. Nimeona Jeshi la Polisi pale, hata issues zao za procurement, 70% ya issues zote walizozifanya ni non-compliance na sheria. Wanaenda kulipa fedha wakandarasi bila hata kazi kukamilika, Auditor anaenda kukuta fedha zimelipwa na mradi haupo.

Mheshimiwa Spika, kuna Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa walinunua magari, magari yenyewe hayo yalilipiwa zaidi ya Shilingi bilioni mbili na milioni mia saba na kidogo, lakini magari yenyewe hayapo. Kwa maana hayo magari yalilipiwa hata kabla hayajawa delivered. Yaani you pay before delivery of goods. Katika bajeti hiyo, tena wame-exceed. Bajeti iliyokuwa approved na budget approving authority ilikuwa ni Shilingi milioni 388. Kwa bahati mbaya, unakuta wamefanya expenditure ya Shilingi 2,400,000,000/= bila budget approving authority.

Mheshimiwa Spika, sasa variance unayoiona hapo kwenye Shilingi 2,300,000,000/= iliyokuwa approved, variance ni kubwa sana. Sasa tuki-entertain mambo haya na tukaona hii ndiyo culture ya kuendesha mambo yetu ndani ya Serikali, tuta-create vacuum kubwa kwenye Taifa hili. Watu wataacha ku-comply, tutakuwa na hizi documents kama urembo tu na watu watakuwa hawa-comply. Kwa sababu tunaweka wenyewe sheria, badala ya kuzifuata, tunaweka kwenye makabati, tunaanza kutumia sisi wenyewe tunavyofikiria. Haiwezi kutusaidia.

Mheshimiwa Spika, nimeona pale TTCL kwenye manunuzi, yaani ni wezi. Tuombe PPRA ikafanye special audit kwenye mashirika haya ambayo tumeona. Compliance kwenye Sheria ya Manunuzi ni mbaya. Compliance siyo ile ambayo, inaishia tu kwamba tume-comply, ni compliance ambazo zina impact kwenye finance. Kwa sababu unakuta umesaini mkataba na mtu, hakuna power of attorney, kwa maana ule mkataba is null and void. Mmempa kazi, kesho na kesho kutwa asipo-perform hamwezi kumshitaki. Hakukuwa hat ana mtu aliyepewa power ya kisheria ya kusimamia mkataba wa Shirika. Shirika kubwa kama TTCL yanafanyika mambo ya ajabu kama haya. Nawaomba ndugu zangu, kuna issues nyingi sana kwenye compliance ya manunuzi. Nendeni mka-scrutinize document ya CAG muone weight ilivyo na significant impact itakayotupelekea. Kutakuwa na issue za litigation, tusipoona hapa tutashtakiwa.

Mheshimiwa Spika, kuna mkataba mmoja nimekuta pale TTCL wa Shilingi bilioni tano. Wamesaini ule mkataba na Mkandarasi alitakiwa amalize ndani ya miezi ya mitatu, ilikuwa ni kutengeneza ule mfumo wa short sms, lakini mpaka leo una zaidi ya miaka tisa hajawahi kumaliza. Nikawauliza sasa position ya mkataba kama huu ni upi? Yaani yeye alitakiwa awakabidhi kazi ndani ya miezi mitatu, lakini amechukua zaidi ya miaka mitano na mnaendelea na maisha na mnasema this is good, let us live, business as usual.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kutoa mawazo yangu niliyotumwa na wananchi wa Jimbo la Kwela katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu kwa kazi nzuri wanayochapa katika Wizara hii, wataalam wa Wizara hii pamoja na Kamati ya Bunge inayosimamia Wizara yao kazi ni nzuri, niwape pongezi zangu za dhati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi zangu, naomba niwakumbushe Mheshimiwa Naibu Waziri na Waziri hapo. Mnamo tarehe 12 Februari niliuliza swali kuhusu mgogoro wa Uwanda Game Reserve kule katika Jimbo langu la Kwela. Huu mgogoro umetutesa sana wananchi, hasa wa Kata ya Kapenta, Nankanga, Kilangawani na Kipeta baada ya hili pori kuchukuliwa na askari wa TAWA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwanzo lilikuwa linamilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, mwaka 2013 walipochukua ndio matatizo yalipoanza, maisha ya wananchi yamekuwa ya mateso miaka saba. Naibu Waziri ni shahidi, kila wiki nampigia simu zaidi ya mara mbili nampelekea migogoro, nashukuru ananisaidia, wananchi wangu juzi walinyang’anywa mipunga na askari, wamerudishiwa. Pia wavuvi wale wa Forodha ya Nankanga waliokuwa wamelazimishwa walipe shilingi milioni nane, Waziri ameingilia kati hawakulipa zile shilingi milioni nane. Nawapongeza kwa jitihada hizo ni nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hii ni ad hoc solution, tunatakiwa tuwe na permanent solution. Baada ya askari wa TAWA kuchukua pori lile mipaka ilivurugwa, haieleweki, kwa hiyo, wananchi wamebaki dilemma kwa miaka saba. Wamekuja Mawaziri waliowatangulia wanaahidi na wakawaambia wananchi tumeunda timu ya Mawaziri saba tutawapa majawabu, mimi nimekuwa nikifuatilia hayo majawabu sijayasikia, wananchi wako hawajui kinachoendelea. Kwa bahati mbaya hii Uwanda Game Reserve hata wanyama wenyewe sio wengi, wako tembo wanne na nyati wawili tu na kwa miaka minne iliyopita tumepata watalii wawili tu, for four years watalii wawili. Kwa hiyo, imekuwa ni cost generation centre rather than revenue generation centre. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri, kutokana na mabadiliko ya tabianchi Ziwa Rukwa linakua, limekua mpaka limeingia kwenye hifadhi, wavuvi wakiingia kuvua kwenye hili wanawakamata…

T A A R I F A

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Cecil Mwambe.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nampa Taarifa mzungumzaji kwamba kilichopo kwenye hiyo game reserve anayoitaja, tuna game reserve pia nyingine iko Masasi DC inaitwa Misyenjesi. Wananchi wanatamani waachiwe lile eneo wafanye shughuli zao za kilimo kwa sababu haina manufaa yoyote kwao na hakuna wanyama pale ndani.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Deus Sangu, unapokea Taarifa hiyo?

MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naipokea hiyo Taarifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nitoe ushauri kwa Wizara hii, waliniahidi kwamba, tutaenda kutembelea hili pori. Nashukuru, nasubiri hiyo ahadi yao na aliniahidi Waziri kwamba, tukimaliza bajeti hii tunaenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, wavuvi wanakamata vifaa vyao. Boti ukilichukua ukalitoa kwenye ziwa ukaweka nchi kavu miaka mitatu, baada ya hapo wakifanya mnada inakuwa ni kuni, inakuwa hasara kwa mvuvi pia inakuwa hasara kwa Serikali, hakuna kitu kiinachozalishwa pale. Kwa hiyo, niwaombe sana ili tuondoe migogoro hii na kufanya ile Uwanda Game Reserve tutoe vibali kwa wavuvi wakavue kwa vibali, kwa sababu kitendo cha kutotoa vibali mmewahalalishia askari waanze kuchukua rushwa. Mvuvi anatoa shilingi milioni moja, hela zinaenda kwa mtu binafsi, Serikali hawapati chochote, si bora watoe vibali ili waingize fedha katika Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaombe sana Wizara hii. Migogoro hii hata Rukwa Lukwati kule kuna mgogoro wa aina hii, wavuvi wananyanyasika sana. Wavuvi wanakuwa charged mpaka shilingi milioni tatu, hizo fedha wanachukua askari binafsi, Serikali haipati hata senti moja, mateso ni makubwa, wananchi wameumizwa sana. Niwaombe sana watakapokuwa wana-wind up watoe kauli, migogoro ile wataimaliza lini ili la wananchi wa Kata ya Nankanga, Kapenta, Kipeta, Kilangawane, wafurahie kwamba, kuwepo kwa ile Uwanda Game Reserve kuna faida kwa sababu, wanatusaidia katika bio diversity conversation. Wamekuwa wakitusaidia pamoja na kwamba hamna watalii, lakini pia utunzaji wa mazingira, lakini wananyanyasika sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia kwenye hoja zilizopo hapo mezani. Kwanza kabisa niungane na wenzangu kukupongeza kwa nafasi hii ya kuwa Spika wa Bunge pia nimpongeze Naibu Spika. Lakini kwa namna ya pekee nizipongeze oversite committee zote kwa maana ya PAC na LAAC kwa presentation ya Wenyeviti wake wamefanya presentation nzuri sana niwapongeze sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nitajikita kuchangia hasa kwenye benki zetu za Serikali nataka nielezee going concern ya benki zetu za Serikali. Serikali kuwa na benki zake yenyewe ni jambo muhimu sana, lakini kuanzia mwaka, 2017 Serikali ilichukua uamuzi wa kuunganisha benki zake. Kwanza, ilianza kuichukua TWIGA kuiunganisha na Benki ya Posta; baadaye ikaja kuchukua Benki ya Wanawake ikaiunganisha mwaka, 2018 na Benki ya TPB. Shida kubwa hizi major mbili hazikuwa na tatizo kubwa shida kubwa ilikuja pale ambapo, Serikali iliamua kuchukua benki ya TIB Corporate na kuiunganisha na Benki ya TPB ili kuunda Benki ya TCB ambayo ni Benki ya Biashara ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lengo lilikuwa ni zuri labda tulikuwa tuna-revert will yetu ya kubinafsisha Benki ya NBC ili tuwe na Benki ya Biashara ya kwetu ya Serikali, lakini kitendo cha kuileta TIB Corporate tayari ilikuwa na mikopo chechefu ya Shilingi bilioni 130, hii imekuja kuharibu mizania ya vitabu vya, Benki hii ya TPB ambayo ilikuwa tayari ipo kwenye top ten ya benki zinazofanya vizuri hapa nchini. Kwa sababu, tuna benki sasa zaidi ya 50 lakini benki yetu ya Serikali ya TPB ilikuwa ina- perform vizuri. Kuleta kwa mikopo chechefu na pia ikaleta mzigo wa wastaafu kwa maana ya staff management team ile ambayo ilikuwa na mishahara mikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpaka leo kutokana na ofisi ya Treasurer kuto-solve huu mtanziko pale ndani ya benki ni kama kuna management mbili. Kuna wale waliotoka TIB Corporate ambao wage bill yao kwa mwezi inakwenda, 1.7 billion shillings ambao kazi kubwa inayokwenda pale ni kusoma magazeti. Unalipa shilingi 1.7 billion kwa mwaka fedha za walipa kodi hawajapangiwa majukumu, sasa inaonekana Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina hawakujipanga wakati wanafanya hii merger. Ilitakiwa watumie approach ile waliyofanya wakati wanabinafsisha ile Benki ya NBC, walichukua madeni na mali zile ambazo, wale makaburu hawakuzitaka, wakaunda Shirika pembeni tanzu la CSC kwa ajili ya ku-deal na yale mambo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa huku approach ilikuwa wakapeleka madeni mabaya Shilingi bilioni 130 na Treasurer aliji-commit kwamba huu mzigo nitaubeba. Tangu Juni, 2020 ameweza ku-recover Shilingi bilioni tatu tu, kwa hiyo itamchukua zaidi ya miaka 40 ku-recover ile mikopo chechefu. Ile mikopo mingi, ukiiona haina future yoyote, mikopo ile yote yawezekana hata Serikali isiweze ku-recover zile fedha. Sasa, naomba kuishauri Serikali kuna approach mbili ambazo unaweza kutumia kuisaidia benki hii, ambayo ina matawi 83 na ina wakala wa benki zaidi ya 3,500 nchi nzima na ni benki ambayo tunaitegemea kama Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza; wakubali kuchukua ile mikopo iondoke kwenye mizania ya vitabu vya Benki ile ya TCB. Pili, hawa management ambao wanalipwa Shilingi 1.7 billion na wapo tu wanasoma magazeti, watafutiwe sehemu nyingine ndani ya Serikali, kuna mamlaka nyingi, wakafanye kazi, kuliko kutumia fedha za walipa kodi hawafanyi kazi yoyote. Hii contradiction tu ni basi tu katika making decision, ilitakiwa siku ile tu ya merger wawe wameamua hili jambo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatu, tuna benki yetu nyingine kubwa kabisa Benki ya Maendeleo ambayo ni TIB Development katika nchi yoyote ile kwa mfano China Development Bank. Hii China Development Bank ndio ina- finance miradi yote mikubwa ya kimkakati ndani ya nchi ya China, lakini sisi hii TIB Development alipoianzisha Mwalimu Nyerere mwaka 1970 alikuwa na nia njema. Kukaingia ulaghai na ujanja ujanja mpaka ninaposema leo hii mikopo chechefu imefika Shilingi bilioni 327 na kila mwaka wakijitahidi wanakusanya labda shilingi bilioni mbili au tatu. Maana yake hata benki hii leo hii ukienda wame-stop lending hawakopeshi, kwa sababu, fedha ina liquidity crisis maana yake ni nini kinachoweza kutokea hapo?

Mheshimiwa Spika, wamesema watatoa non cash bond. Noncash bond ni kwenda tu kuweka mizania ya vitabu ikae vizuri, lakini hai-address tatizo la mtaji la benki hii. Ina mtaji wa Shilingi bilioni 38, lakini requirement ya Benki Kuu inatakiwa Benki aina ile ya TIB Development iwe na mtaji wa shilingi bilioni 50. Sasa, leo hii unakwenda kufanya non cash bond ambayo pia inakwenda na impact kwenye deni la Taifa, tayari hata TCB wanasema, wanakwenda kuweka non cash bond, yes ni initiative ya kuweka mizania ya vitabu, isome vizuri, lakini hai-address matatizo ya benki zetu hizi za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali kama inataka kweli twende mbele kwenye financial sector na hapa sijaongelea Benki ya Maendeleo ya Kilimo nayo hali ni hii hii. Maana yake sisi ndio tuna-prove failure; Benki Kuu inasema asilimia tano ya non-performing loan against assets zako ndio inatakiwa, lakini sisi kwa mfano, TIB leo mikopo chechefu ni zaidi ya asilimia 50 wakati inatakiwa iwe asilimia tano, tunakwenda wapi tumeamua kuua benki zetu wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa sababu ya muda niishie hapa. Ahsante sana. (Makofi)