Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Jesca Jonathani Msambatavangu (44 total)

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza naomba niulize, je, Wizara hawaoni kwamba sababu mojawapo inayoweza kusababisha malalamiko au kutotekelezeka kwa sera hii ni ile hali ya kuzi-upgrade hii vituo vyetu vya afya na zahanati zetu? Kwa mfano katika Manispaa ya Iringa, hospitali yetu ya Frelimo ilipandishwa hadhi kuwa hospitali ya Manispaa tangu mwaka 2013 lakini mpaka sasa inapokea mgao kama kituo cha afya. Katika hospitali ile tuna takribani akina mama 300 mpaka 350 wanaojifungua pale kila mwezi. Unaweza ukaona hiyo inachangia kwa sababu mahitaji ya watu wanaokuja pale yanakuwa makubwa kuliko mgao wanaoupata.

SPIKA: Yaani Mheshimiwa Hospitali ya Frelimo pale kila siku kumi wanajifungua?

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Ndiyo.

SPIKA: Endelea na swali lako Mheshimiwa.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, kwa sababu hospitali yetu ya Frelimo, kwanza tulikuwa na Hospitali ya Wilaya imepandishwa hadhi na kuwa hospitali ya rufaa, kwa hiyo, wilaya tumepewa ile iliyokuwa kituo cha afya Frelimo kuwa hospitali ya wilaya. Kwa hiyo, ile hospitali yetu iliyokuwa ya wilaya imekuwa hospitali ya rufaa, hivyo, wagonjwa wengi sana wamekuwa wakienda pale na kwa kuwa bado tunapata mgao kama kituo cha afya imesababisha sasa wagonjwa wengi kuwepo pale na akina mama wengi wanaojifungua kukosa ile huduma bure. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka, tangu 2013 jamani kwamba na sisi Iringa tupewe mgao kama hospitali ya Wilaya?

SPIKA: Ahsante sana, swali la pili fupi.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, swali la pili, niombe tena Serikali ione, je, hii migao inayokuwa inakinzana yaani unaipandisha hospitali hadhi halafu unaipa mgao wa kile kiwango cha awali, hawaoni hiyo inaweza kuwa ni sababu mojawapo ya malalamiko kwamba Sera hii haitekelezeki?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza alivyouliza swali lake ni suala ambalo tunahitaji tufuatilie tujue specifically kwamba kwenye hospitali yake mgao wake uko kwa namna gani.

Nikitoka hapa Mheshimiwa Mbunge tutakaa pamoja tuangalie ukweli wa hilo unalosema. Nimekwenda Hospitali ya Mbozi, wanatumia shilingi milioni 415 kwa mwaka kutibu kinamama na watoto, kwa hizi huduma zinazotolewa bure lakini wanapata OC kutoka Serikalini shilingi milioni 485 kwa mwaka, maana yake ukitoa hizo huduma wanabaki na zaidi ya shilingi milioni 60 kwa mwaka ambazo ni zaidi ya matumizi kwa huduma hizi ambazo zinatolewa bure.

Mheshimiwa Spika, hata ukienda Hospitali ya Mkoa wa Mbeya wamepewa dawa za shilingi milioni 53 pamoja na kuhudumia akina mama wakauza wakapata shilingi milioni 157 lakini mwisho wa siku wakaenda kununua dawa za shilingi milioni 29 maana yake ni chini hata ya dawa walizoziuza. Kwa hiyo, kimsingi ukiangalia tunahitaji tupate ushirikiano kwa Wabunge na viongozi wote ili tuhakikishe haya mambo tunaweza tukaya-solve kwa pamoja kwa sababu mengi ni ya kitendaji kule chini.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, lakini tunaenda kwenye bima ya afya kwa wote haya mambo yataweza kutatulika kwa urahisi zaidi.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Wizara, kwanza nawashukuru kwa namna ambavyo wameweza kulifanyia kazi suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la nyongeza ni kwamba je, Wizara inajipanga vipi sasa kuandaa wataalam ili tarehe 1 Agosti tutakapokuwa tumekamilisha mradi huu uweze kuanza kazi mara moja, kwa kuwa mradi wenyewe ni wa muda mrefu; na kwa kuwa tumewekeza fedha nyingi pia, isije kukosa wataalam tukaacha tena, ikakaa muda mrefu sana?

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ina-coordinate vipi na Wizara nyingine, kwa sababu hali ya kwenda kule kwenye machinjio yetu, pamoja na miundombinu tuliyoiweka, bado kuna changamoto kubwa sana ya barabara. Tunaomba hilo pia Wizara watuhakikishie wata-coordinate vipi kwa kuwa ni mradi wa kimkakati? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tunafahamu machinjio hii imekaa muda mrefu na ndiyo maana nimeeleza kwamba fedha ambazo zimetengwa zitakwenda kukamilisha ujenzi ifikapo mwezi Agosti, 2021. Hata hivyo, kipaumbele ambacho kimewekwa, moja ni kuhakikisha kwamba vifaa vinavyohitajika kuiwezesha machinjio ile kufanya kazi vizuri pamoja na watendaji kwa maana ya watumishi, wataalam wanaohitajika ni kipaumbele cha Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, utekelezaji wa mradi huu unakwenda sambamba na ukamilishaji wa majengo na mipango ya kuhakikisha kwamba tunapata vifaa kwa ajili ya kuhakikisha machinjio inafanya kazi vizuri na kuhakikisha kwamba watumishi wanapatikana ili huduma ziweze kuendelea. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mambo haya yote yako kwenye mipango yetu na tutahakikisha inapokamilika, inaanza kutoa huduma kama ilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na barabara, ni kweli ni lazima eneo lile lifikiwe vizuri na barabara kwa sababu tunafahamu machinjio ile ni ya kisasa na lengo letu ni kuboresha huduma katika jamii na kuwezesha Manispaa kupata mapato mazuri. Tutakwenda kuhakikisha tunashirikiana kwa karibu sana na TARURA ili kutenga bajeti ya kuhakikisha kwamba barabara ile inafikika. Barabara hii kama inahudumiwa na TANROADS pia tutawasiliana kwa karibu ili iweze kujengwa, ifike pale ili kuboresha huduma hizo.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na maeneo ya umma kama ambavyo Serikali imeelekeza na kuzielekeza halmashauri kupima lakini migogoro mingine mingi tunapata sana kwenye taasisi kama Majeshi na Magereza. Kwa mfano, Iringa pale Kata ya Isakalilo ina mgogoro mkubwa wa ardhi wa mipaka pamoja na wananchi na Jeshi la Magereza.

Je, Serikali inahusiana vipi na Wizara nyingine kuhakikisha pia inatatua hilo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pia nimshukuru na muuliza swali.

Mheshimiwa Spika, Wizara katika zoezi zima la utatuzi wa migogoro kila tunapokwenda kwenye zoezi la migogoro utatuzi wake tunashirikisha halmashauri husika na tunashirikisha pande zote mbili. Na unapotaka kutatua mgogoro lazima uwe na lile Gazeti la Serikali linalotangaza mipaka ya eneo husika; na hauwezi kuutatua mgogoro ule unless mmekwenda kwenye site na kuweza kutafsiri. Kwa hiyo kazi kama Wizara tunayoifanya katika migogoro hiyo ya taasisi na wananchi tunaendelea kuitatua kwa kuzingatia sheria zinasema nini na mara nyingi tunapokwenda, Halmashauri husika inahusishwa na pande mbili zinazogombana zinahusika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama Kata ya Isakalilo na Magereza bado kuna mgogoro naelekeza wapimaji wa Mkoa wa Iringa wafike kule site ili waone namna ya kutafsiri mpaka ili kuondoa mgogoro huo.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa ajili ya majibu mazuri ya Serikali, lakini naamini Naibu Waziri yeye mwenyewe ameona namna ambavyo changamoto ni kubwa. Hii ni Hospitali ya Wilaya yenye takriban wakazi 200,000 na kwa mwaka mzima wa fedha tumepewa shilingi milioni 53. Kwa hiyo, anaweza akaona ukubwa wa tatizo ulivyo na kwamba haiwezi kututosheleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, swali langu la nyongeza sasa: Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kutujengea vituo vingine vya Afya katika Jimbo la Iringa Mjini, hasa katika Kata za Kitwilu, Igumbilo, Nduli, Isakalilo na Mkwawa ili angalau kupunguza mzigo katika Hospitali ya Frelimo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, je, ni lini Serikali itaufanyia kazi mpango au ombi letu tulilolileta kama mkoa la kuomba sasa hospitali hizi zibadilishane maeneo; pale ilipo hospitali ya wilaya ijengwe ya mkoa na ile ya mkoa tuachiwe wilaya kutokana na eneo finyu lililopo katika hospitali yetu ya wilaya ili kufanya utanuzi zaidi kwenye eneo la hospitali ya mkoa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jesca Jonathan Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Hospitali hii ya Frelimo ni hospitali ya Manispaa ya Iringa na kama ambavyo nimeeleza kwenye jibu langu la msingi, hospitali hii bado ina upungufu mkubwa wa miundombinu kwa maana ya wodi kwa ajili ya kulaza wagonjwa; wodi ya wanaume, wodi ya watoto lakini pia wodi ya akinamama. Hii imepelekea pamoja na umuhimu wa hospitali hii kuhudumia wagonjwa wachache zaidi ikilinganishwa na hadhi ya hospitali yenyewe. Nndiyo maana kwa vigezo vile vya mgao wa fedha za ruzuku, inapata fedha kiasi hicho ambacho kimsingi lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba tunatenga fedha kwa ajili ya kuongeza wodi katika hospitali ile ili ihudumie wananchi wengi zaidi na mgao wa fedha uweze kuongezeka Zaidi. Katika mwaka ujao wa fedha tumetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunajenga wodi hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusiana na ombi la kujenga vituo vya afya katika kata hizi za Kitwiru, Igumbiru, Mkwawa na nyingine nilizozitaja, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi ni kujenga vituo vya afya katika kila kata na nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge amekuwa mstari wa mbele sana kuhamasisha wananchi kujitolea nguvu zao kuanza ujenzi wa vituo hivi na sisi kama Serikali tutaendelea kumuunga mkono kuhakikisha tunatenga fedha katika bajeti zijazo kuunga mkono nguvu za wananchi katika kujenga vituo vya afya katika kata hizi kwa awamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ni kweli kwamba Mkoa wa Iringa umewasilisha mapendekezo kwa kufuata taratibu zote kuomba Hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa iweze kubadilishana na hospitali ya rufaa ya mkoa. Sisi kama Serikali tumepokea mapendekezo hayo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tutayafanyia kazi na tathmini maombi hayo. Baada ya hapo tutatoa maamuzi ya Serikali ili kuhakikisha kwamba tunaboresha miundombinu ya huduma za afya katika Mkoa wa Iringa.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kwa kuwa utalii unakwenda kwa package na mbuga ya Katavi pamoja na hifadhi nyingine ni sehemu ya utalii kusini na kituo cha utangazaji na taarifa zote kinatakiwa kujengwa Iringa katika sehemu inayoitwa Kisekiroro ni lini Serikali itaanza ujenzi huo?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa kituo hicho unafadhiliwa na Benki ya Dunia katika Mradi wa RIGRO. Mradi huo ulichelewa kidogo kutokana na tatizo la COVID ambalo liliwakuta nchi mbalimbali ikiwemo wafadhili wa Mradi huo. Sasa hivi tayari mradi huo umeshaanza, jana Katibu Mkuu amekabidhi magari 12 kutokana na mradi huo kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Jesca na Wabunge wote wa Iringa na Nyanda za Juu Kusini kwamba kituo hicho kitajengwa haraka iwezekanavyo.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la nyongeza Je, Serikali iko tayari kushughulikia masuala ya bima za afya kwa wauguzi wastaafu wakianzia na Hospitali ya Mkoa wa Iringa ili watibiwe bila usumbufu? (Makofi)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni sahihi kwenye mwelekeo wetu huu wa Bima ya Afya kwa Wote tutachukua makundi yote, hakuna atakayebaki nyuma yakiwepo hayo. (Makofi)
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, ahsante na nashukuru kwa kunipa nafasi ya swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali langu ni je, Serikali inatumia utaratibu gani wa kulipa madeni ya askari ambao unaendelea kwa kuwa wameanza kulipa 2018/2019 na wameacha 2017, lakini pia askari waliopandishwa vyeo kutoka Mainspekta kuwa Warakibu wa Polisi 99, askari 99 ambao walipanda mwaka 2013 mpaka 2017 hawajalipwa mshahara kwa cheo hicho wameanza kulipwa 2018? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali hili la Mheshimiwa Jesca kwamba suala hili ni suala ambalo linahitaji takwimu na linahitaji data za uhakika. Kwa hiyo, kubwa tu nimwambie Mheshimiwa kwamba pamoja na kwamba utaratibu umeshaanza kupangwa, lakini nimuombe tu kwamba, suala hili aendelee kulipa muda ili tukalifanyie kazi halafu tutajua namna ya kuja kumjibu, nakushukuru.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru; ili askari wangu pale Iringa wapate utulivu na kuimarisha ndoa zao na familia wanahitaji makazi bora. Je, ni lini Serikali sasa itatujengea makazi bora ya askari katika Kituo Kikuu cha Polisi Iringa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana na yeye kwa juhudi kubwa ambayo anatusaidia katika kuhakikisha kwamba anawasaidia wananchi, lakini kikubwa nimuahidi kwamba katika mwaka wa fedha ujao tutajitahidi na tutahakikisha kwamba hili eneo ambalo yeye amelizungumza tulipe kipaumbele ili tu wananchi wa eneo hilo waweze kupata na wao huduma za ulinzi na usalama bila ya tatizo lolote, nakushukuru.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa
Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naomba niulize swali.

Je, Serikali ina mpango gani wa kutumia wazawa katika kukuza utalii wetu hasa cultural tourism? Kwa mfano kutumia wazee wa kimila kama wazee wa kihehe ambao walianza kutunza Mbuga ya Ruaha wakati wa Chief Mkwawa na kutumia wazee wengine kama Wamasai, ili kuhakikisha kwamba utalii wetu unakua, kwa kuwa wao wenyewe wanakuwa tayari ni kivutio?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jesca, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli sasa hivi Serikali ina mpango wa kutumia watu maarufu, wazee wa kimila kama ambavyo amewaainisha Mheshimiwa Mbunge na watu maarufu wakiwemo wasanii ambao tutawatumia kama mabalozi wa hiyari. Kwa hiyo nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, suala hili Serikali inalishughulikia; na tulishukuru sana Bunge hili limetupitishia bajeti nzuri ambayo sasa mwaka wa fedha 2021/22 tunaenda kutekeleza maeneo yote haya. Ahsante.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.

Ni lini Serikali itakamilisha barabara ya Iringa bypass kwa kilometa 6.8 zilizobaki?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara uliyoitaja ya kilometa
6.9 ni barabara muhimu ambayo itatuondolea adha pale ambapo changamoto ikitokea kati ya Ruaha na Mjini pakikwama basi mji unakuwa umefunga. Na Mheshimiwa Mbunge anajua kwamba tayari tumeshaanza na katika bajeti tunayoanza, barabara hii utaendelea; lengo ikiwa ni kukamilisha hizo kilometa zilizobaki kwa ajili ya kuondoa hizo changamoto, ahsante.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa majimbo ya mijini mitaa ndio kama vijiji. Swali, je, ni lini sasa Serikali itapeleka umeme kwenye mitaa yetu kwa mfano Jimbo la Iringa Mjini kata ya Isakalilo, Mtaa wa Kitasengwa Mkonga, Majengo Mapya; Kata ya Mkwawa, Mtaa wa Wahe na Hoho, Kata ya Igumbilo Mtaa wa Ulonge…

MWENYEKITI: Sio zote tena wewe taja moja tu.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia umeme katika mitaa. Sasa naomba nijibu swali lake la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumetenga mitaa 637 kwa nchi nzima ikiwemo mitaa kwa Mheshimiwa Jesca na mitaa yote itaanza kupelekewa umeme kuanzia mwezi Novemba mwaka huu ndani ya miezi 18. Tumetenga fedha hizo kwa awamu tunaanza na mitaa yote ambayo inafanana na hali ya kivijiji, lakini na mitaa mingine ambayo ipo katika majiji makubwa pamoja na manispaa kwa nchi nzima. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na mimi nilitaka niulize swali. Serikali ilikuwa na programu ya kukarabati shule kongwe nchi nzima ikiwepo Shule ya Sekondari Iringa Girls na Lugalo Secondary zilizopo Iringa ambazo ni za bweni kwa watoto wa kike na hasa watoto wenye ulemavu wa ngozi, viungo na wasioona. Pale hapakufanyika ukarabati wa mabweni mawili; moja katika shule ya Iringa Girls na nyingine Lugalo Secondary.

Je, ni lini sasa Serikali itatukamilishia mabweni yale ili watoto wale wenye ulemavu wasiendelee kupata shida ya mahali pa kulala? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Jesca Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri anazungumza kitu ambacho anakifahamu kwamba hizi shule alizozitaja ziko katika mipango yetu. Kwa hiyo, aondoe wasiwasi tu kwamba tutatekeleza ahadi ya kuwasaidia wanafunzi wote sio Iringa Girls na Lugalo ni shule zote kongwe tulizozikusudia zitafikiwa. Ahsante sana.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nilikuwa nina maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza, Serikali ina mpango gani pia kuendelea kutoa vibali kwa ajili ya wale wawindaji waliokuwa wakifanya uwindaji katika mbuga zetu za nyanda za juu kusini?

Mheshimiwa Spika, pia Serikali ina mkakati gani wa kushirikiana na Wizara ya Fedha ili kuboresha huduma za upatikanaji wa fedha za kigeni ili kuwarahisishia watalii nchini hasa kwa kuruhusu maduka ya kubadilisha fedha za kigeni?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jesca Jonathan Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameulizia kuhusu vibali vya uwindaji. Vibali vya uwindaji vimeendelea kutolewa na Wizara kama kawaida na wafanyabiashara kwa maana ya wawekezaji wote ambao wanatamani kuja kuwekeza kwenye eneo hili la uwindaji, tumekuwa tukitoa vibali kupitia mbinu mbalimbali ikiwemo ya kupitia manunuzi ambayo tunatangaza kwa njia ya kieletroniki. Kwa hiyo, ninawaalika tu wawekezaji ambao wanataka kuwekeza katika sekta hii ya uwindaji waje na kila baada ya muda tunapokuwa tumefanya matangazo haya kuna ambao wanapata lakini wanaochelewa, tunaendelea kutangaza kila baada ya muda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye upande wa kubadilisha fedha kwenye maduka haya ya fedha za kigeni, mpaka sasa Serikali imeendelea kushirikiana na hao wafanyabiashara ikiwemo kuandaa mazingira mazuri kwa ajili ya kuendelea na biashara hii ya kubadilisha fedha. Tunawaomba tu wale wafanyabiashara wote ambao wanafanya biashara hizi waendelee kufuata taratibu wa Serikali kama ambavyo imeendelea kuelekezwa na Wizara ya Fedha. Nasi Sekta ya Maliasili na Utalii tutaendelea kuungana nao pamoja ili kuhakikisha kwamba biashara hii inaendelea kufanyika ili tuweze kukuza utalii katika nchi yetu. Ahsante.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nilikuwa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza je, Serikali iko tayari sasa kuweka utaratibu wa muda maalum kwa ajili ya kuhakikisha kwamba hizo moving expenses zinalipwa ili kuondoa usumbufu kwa watumishi wa umma?

Lakini swali langu la pili je, ni lini sasa Serikali pia itafanya marekebisho kwa yale madaraja ya watumishi wa umma yaliyofutwa mwaka 2016 na 2017. Hasa katika Manispaa yangu ya Iringa wapo watumishi zaidi ya 300 ambao hawajafanyiwa marekebisho pamoja na kazi nzuri ambayo imefanywa na Serikali ya kupandisha madaraja. Ni lini itafanya kazi hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, na pia tumeshaleta sana hili ombi mara nyingi sana kwa Waziri lakini halijafanyiwa kazi, tunaomba commitment ya Serikali? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la kwanza kama nilivyosema kwenye majibu ya msingi. Waajiri wote wanatakiwa kuhakikisha wanatekeleza matakwa ya Kanuni za Kudumu za Kudumu za Utumishi wa Umma na tayari Kanuni hizo zipo kwamba ni Mtumishi yoyote anapokoma utumishi wake wa umma au mtumishi pale anapohama anastahili kulipwa moving expenses.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nitumie fursa hii kuwataka tena Waajiri kuhakikisha wanatenga bajeti ya moving expenses kwa sababu wanajulikana wale watumishi ambao wanakaribia kustaafu. Sasa ni wajibu wa mwajiri kuangalia wale wanaokaribia kustaafu mwaka unaofuata wa fedha na kuweza kutenga bajeti hiyo. Kwa hiyo, nirudie tena kuwataka Waajiri wote si tu wa local government, si tu wa Iringa Mjini, lakini taasisi zote za umma kuhakikisha wanatenga bajeti kwa ajili ya watumishi wao katika hii moving expenses.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye swali lake la pili, la madaraja ya 2006. Madaraja haya yalisimama kuanzia Mei, 2016 lakini madaraja haya yalianza tena kutolewa mwezi Novemba, 2017 ambapo Serikali ilipandisha jumla ya watumishi 55,000 Novemba, 2017. Hii ya kutoka 2016 madaraja haya yalikoma kupisha uhakiki uliokuwa ukiendelea, lakini sasa tunaangalia ni namna gani bora ya kuweza kuleta msawazo ili kulindi ile Seniority katika eneo la kazi na Serikali bado inalifanyia kazi suala hili na litakapokuwa tayari tutatolea maelezo zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. kwa kunipa nafasi. Pamoja na maelezo mazuri ya Mheshimiwa Waziri, moja ya changamoto kubwa anayoanza nayo kwenye Wizara hii ni mauaji ambayo yanaendelea katika jamii hasa katika yanayosababishwa na jinsia, ikiwepo wanawake kuwaua wanaume, wanaume kuwaua wanawake, watoto kuwaua wazazi wao kwa ajili ya kupata mali: -

Je, Wizara imejipangaje sasa kabla ya kufikia kwenye vyombo vya usalama kuhakikisha kwamba wanazuia hali hii inayoendelea katika jamii?
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jesca Msambatavangu, kuhusu vitendo vya ukatili vinavyoendelea kwenye jamii yetu. Ni kwamba tunao mkakati wa kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto mpango wa Taifa uliozinduliwa mwaka 2017/2018 na unakwenda mpaka mwaka 2021/2022, ambao umeandaa Kamati kwenye ngazi ya Kijiji zinazoongozwa na Wenyeviti wa Serikali za Kijiji, Mtaa, Kata, Halmashauri mpaka Taifa na mkoa ukiwemo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati hizi tumeshazipelekea maelekezo na leo tunakwenda kuazimisha Siku ya Kupinga Ukeketaji tarehe 6 Februari, 2022. Hii ni Fursa ya kuziamsha hizi Kamati zote zifanye kazi yake. Zikitekeleza majukumu yake yaliyomo kwenye huo mwongozo, tutaweza kudhibiti ukatili huo unaotokea kwenye jamii kwa kuona viashiria husika na kuvitolea taarifa katika vyombo husika vinavyoshughulika na uhalifu.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Je, ni lini zile mashine ulizokuja kukagua mwaka jana ukaniahidi baada mwezi utaleta Wataalam wa dialysis zitaanza kufanya kazi katika Hospitali ya Mkoa ya Iringa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, nalipokea swali lake na kwa sababu tulienda wawili tukalitembelea eneo, naomba tukutane tukae pamoja tuhakikishe hiyo kazi inaanza mara moja.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mepesi ya Serikali naomba nitoe ushauri mmoja lakini pia niwe na swali moja la nyongeza. Kwanza tuwaombe Wizara ya Maliasili, pamoja na dhamana kubwa waliyopewa ya kulinda maliasili za Taifa letu, lakini wajue wana wajibu pia wa kuruhusu Watanzania wahudumiwe bila wao kuwa kikwazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, eneo la Hifadhi ya Msitu Kihesa, Kilolo ni eneo ambalo limepitia mchakato mkubwa mpaka kutengwa kwa ajili ya kujenga Kituo cha Utalii Kusini. Nilikuwa nataka kuuliza, maana swali hili tunaliuliza tangu Januari, 2021 na tunapata majibu yasiyokuwa straight; naomba leo Mheshimiwa Naibu Waziri atuhakikishie hapa: Ni lini hasa ujenzi wa Kituo cha Utalii Kusini Kihesa, Kilolo utaanza chini ya mradi wa REGROW kwa sababu miradi mingine yote ya REGROW inaendelea na imeanza, kasoro Kituo cha Utalii Kusini cha Kihesa, Kilolo.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Jesca Jonathani Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Jesca kwa namna ambavyo anaendelea kufuatilia mradi huu wa ujenzi wa Kituo cha Information Center ambacho kitasaidia upatikanaji wa ofisi mbalimbali na pia kuwezesha masuala ya utalii ili yaweze kuendelea vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba natambua kwamba wananchi wa Iringa wana hamu kubwa sana ya ujenzi wa jengo hili ambalo linatarajiwa kujengwa ghorofa tano pamoja na jengo lingine la Kituo cha Utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba ujenzi huu unatarajiwa kuanza mwezi Mei na sasa hivi tulikuwa tuna mkandarasi ambaye alikuwa anaangalia michoro, na michoro tayari imeshakamilika, na kulikuwa kuna marekebisho kidogo na utaratibu sasa wa kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi umeshaanza. Hivi ninavyoongea, tunatarajia kumpata na mwezi wa Tano ujenzi unaanza. Pia nimhakikishie kwamba tuko ndani ya muda, na ujenzi huu unatarajiwa kukamilika mwaka 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine amesema ni ushauri, tunaupokea lakini nataka nimkumbushe tu kwamba utaratibu wa utoaji wa vibali kwenye maeneo ya misitu ambapo unatarajiwa miti kukatwa, unategemea hasa hasa mteja anayetarajia kupitisha nguzo za umeme awe amekamilisha kulipa tozo zote zinazotakiwa.

Mheshmiwa Mwenyekiti, misitu hii inasimamiwa na Serikali Kuu kupitia Wakala za Huduma za Misitu Tanzania, lakini kuna misitu mingine inasimamiwa na Halmashauri na mingine ni misitu ya vijiji. Kwa misitu ya Halmashauri na Vijiji, tuna kamati za uvunaji ambazo zinasimamiwa, ziko chini ya Wilaya. Kamati hizo pia zinatoa vibali baada ya kuwa mteja amekamilisha taratibu zote za ulipaji wa tozo. Tozo hizi zinasimamiwa na Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nafahamu pamoja na kwamba sheria hiyo ipo na sisi ndio tunaosimamia utawala wa sheria, lakini nafikiri pia makampuni haya yanasimamiwa kwa regulation za taratibu zetu za nchi.

Sasa tunaomba kujua Serikali ina mpango gani sasa wa kuitisha taarifa za mashirika hayo ili kujua wametoa gawio kiasi gani na tangu walipoanza kuuza hisa wametoa gawio kiasi gani na kuwapa wananchi taarifa nini hatma yao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jesca, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni shauri na shauri lake tumelichukua, tunaenda kulifanyia kazi.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona REA wanayo miradi mbalimbali lakini tunaotoka Majimbo ya Mjini na tunayo mazingira ya maeneo ambayo yana sifa za vijiji ingawa yako Mjini. Je, ni lini mtatupelekea umeme kwa sababu hata miradi hakuna huko, tunaona tu ya REA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Iringa Manispaa mtaa wa Ugele, Mtaragara, Msisina, Kagrielo na Wahe, ni lini mtatuletea umeme maeneo ya pembeni?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jesca Msambatavangu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wenye Majimbo ya Vijijini wamekuwa na miradi ya REA na densification na mingine, sisi ambao tuko kwenye Majimbo ya Mjini na mimi nikiwemo Jimbo la Bukoba Mjini, tumepata mradi unaoitwa peri-urban ambao kama nilivyotangulia kujibu kwenye siku zilizopita, mradi huu sasa umeenda kwenye awamu ya pili na tutakwenda kwenye awamu nyingine zinazokuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilianza Mkoa wa Pwani na Kigamboni, awamu ya pili ikaja Mkoa wa Arusha, Dodoma na Mwanza, Awamu ya tatu imepata Mikoa mingine kama mitano au sita, sasa tutaenda awamu ya nne nimhakikishie Mheshimiwa Msambatavangu kwamba na Iringa pia itaingia kwenye awamu inayokuja kwa sababu pesa inapatikana taratibu lakini kila mmoja lazima apate pesa katika kufanya miradi hii kwenye maeneo yake.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Swali langu ni: Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba tunashirikiana na nchi nyingine ambazo zimeendelea katika sekta hii ya ufundi stadi hasa kwa masuala ya Exchange Program kuwapeleka watoto wetu Internship ili waweze kujifunza zaidi ufundi?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nashukuru sana kwa swali la Mheshimiwa Jesca kwa sababu pamoja na swali alilouliza hapa, tunafanya jitihada pamoja kuhakikisha kwamba tunaunganisha nguvu kupeleka vijana kwenda kusoma nchi za nje ikiwa ni pamoja na nchi ya Uturuki ambapo wameendelea vizuri sana katika masuala ya ufundi stadi na elimu ya ufundi.

Mheshimiwa Spika, Serikali inakusudia kuhakikisha kwamba tunaanzisha taratibu kwanza za kuwa na staff exchange ya walimu wetu wa ufundi kwenda nchi nyingine kuangalia wanafundishwa vipi na kuleta walimu kutoka nje kuja kukaa kwa muda katika vyuo vyetu ili kuboresha elimu ya ufundi. Vile vile kupeleka wanafunzi wetu katika nchi ambazo zimeendelea vizuri zaidi katika elimu za ufundi ikiwa ni pamoja na Uturuki. Namwahidi Mheshimiwa Jesca kwamba jitihada ambazo ameshazianza tutazifanya pamoja mpaka tutazikamilisha. Ahsante sana.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumWuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, hiyo barabara ya Iringa Bypass ni mwaka wa tatu sasa tangu imejengwa na imeanza kubomoka.

Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Iringa Bypass?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jesca Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii yenye urefu wa kilometa saba tumeshaanza kuijenga. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Iringa na watu wote wanaopita hiyo barabara, Serikali inatambua ni barabara muhimu sana kwani, pale kwenye barabara pakifunga, hatuna njia. Namwomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira, kwenye bajeti hii tuna hakika tutaendelea kuijenga kwa awamu ili tuweze kuikamilisha na tuwe na barabara ambayo ni bypass kwa Mji wa Iringa, ahsante.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, ahsante, nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza, nashukuru kwa majibu yaliyotolewa.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza. Katika Hospitali yetu ya Mkoa wa Iringa imefungwa mashine ya CT-scan na inatoa huduma kwa wagonjwa wote isipokuwa wagonjwa wa bima ya afya kwa sababu NHIF wameshindwa kutoa kibali cha wagonjwa kupata huduma hizo. Swali langu ni kwa nini hawataki kutoa kibali?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; gari ya chanjo ya Manispaa ya Iringa ni ya mwaka 1998, imekwenda zaidi ya kilometa 380,000 na zaidi na hatuna gari, gari imechakaa kabisa. Ni lini tutapata gari hiyo ili wananchi waendelee kupata huduma za chanjo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kusema kwamba Rais wetu alipopokea nchi kwenye Tanzania nzima ni hospitali mbili tu za mikoa zilikuwa na CT-scan na kwa sasa hospitali zote za mikoa zimepelekewa CT-scan na zimebaki nne za ziada maana yake Rais wetu amefanya kazi kubwa mno. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tusingefurahi mtu yeyote awakoseshe Watanzania hiyo huduma ambayo Rais wao amepeleka. Kwa hiyo, niseme tu kwa niaba ya Waziri wa Afya nimuagize DG wa Bima kwamba mpaka kesho saa mbili watu wa Iringa ambao wanastahili kupata huduma na waliotimiza vigezo waanze kupata huduma.

Mheshimiwa Spika, swali lako la pili ni kwamba gari; tumezungumzia hapa tukasema zimenunuliwa Ambulance zaidi ya 727 maana yake hata Iringa itaenda kupata gari na tutaenda kuwekeza kwenye eneo hilo ambalo unasema ambalo ni muhimu sana la chanjo.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, ahsante, scheme ya umwagiliaji ya Mkoka ni moja ya scheme ambazo zimeharibiwa na mvua zilizokuwa zinaendela na hivyo kuleta kero kwa wakulima; Mheshimiwa Waziri unatusaidiaje kwa ghafla au kwa dharula?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika,napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nitaelekeza timu yangu ya wataalam kuangalia athari iliyojitokeza na tuweze kukarabati scheme hiyo ili wananchi waendelee na kilimo cha umwagiliaji.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Barabara ya Iringa – MR – Itunundu iko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi zaidi ya miaka 30. Ni lini itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge, kwanza itatakiwa iingizwe kwenye usanifu wa kina, baada ya hapo tukishafanya hiyo kazi, ndiyo tutaanza kuijenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, tunatambua kwamba iko kwenye Ilani, ifanyiwe usanifu na ninaamini kazi hiyo tutaifanya katika kipindi hiki cha miaka mitano, ahsante.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Mheshimiwa Waziri ulituahidi mwaka jana kwenye Bunge la Bajeti ungetuchimbia visima katika shule za Kata ndani ya Manispaa ya Iringa, ulipokuja kwenye Wizara Rais mwezi wa Agosti uliahidi kuleta gari katika Mkoa wa Iringa ili tuweze kupata huduma hiyo ya visima, sasa hatijachimbiwa visima mpaka leo.

Swali langu ni; kwanza, huogopi kwenda motoni?

Namba Mbili; mnatuchimbia lini visima?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, tuliomba kuwa na magari kwa ajili ya uchimbaji visima katika kila Mkoa, magari yale tumekwishayapata na katika kila Mkoa tumekwishayapeleka. Ninamuomba Mheshimiwa Mbunge katika yale maeneo ambayo anaona tunahitaji uchimbaji visima, kwa sababu vitendea kazi tunavyo, hatuna kisingizio chochote. Kwa hiyo, jukumu letu ni kuhakikisha maeneo ambapo panatakiwa kuchimbiwa visima tunakwenda kuchimba visima. Ahsante sana.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kikokotoo, issue siyo elimu, issue ni ile percent inayotolewa. Watu wanalalamikia percent inayotolewa kwamba hawajakubaliana nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; tuna malalamiko kutoka kwa kundi muhimu la wafanyakazi ambao wote tunajua historia ya wafanyakazi ndiyo hasa kundi kubwa lililokuwa likifanya mapinduzi mbalimbali, sehemu mbalimbali duniani. Sasa ni lini Serikali pamoja na majibu iliyoyatoa, itafanya ile ujumuishi? Kwa sababu wafanyakazi waliostaafu pia wanasumbuka sana. Wapo ambao walikuwa NSSF wakahamishiwa PSSSF, wanapokwenda kudai mafao yao wanalipwa kidogo na PSSSF na wanatakiwa tena kuanza kufuatilia NSSF; imeleta usumbufu mkubwa. Ninyi kama Serikali mmejipangaje kuwasaidia ili walipwe kwa pamoja?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Askari wetu au Jeshi la Polisi, wao ni kama majeshi, lakini kikokotoo hiki kinaoneka kwamba hakiwahusu majeshi mengine, isipokuwa askari wameingizwa kwenye kikokotoo hiki, nao hawakubaliani na hiyo. Wanasema kwa nini wao wasiwe regarded kama majeshi mengine yalivyokuwa regarded? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Msambatavangu alivyoeleza, ni kwa sababu tu ya pengine taarifa kuwafikia watu vizuri na ndiyo maana wakati wote kumekuwa na mkakati wa kutoa elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali watumishi waliokuwa wakichangia kwa asilimia 25, kama alikuwa anapata shilingi milioni 46, kwa sasa malipo ya mkupuo analipwa shilingi milioni…; wakati huo alikuwa analipwa shilingi milioni 44 na katika pensheni ya kila mwezi alikuwa analipwa shilingi 800,000. Kwa mabadiliko haya ya sasa ambayo yalikubaliwa na wadau wote pia wakiwemo vyama vya wafanyakazi, katika asilimia 33, ukiangalia mkupuo umeongezeka. Ukiangalia mchango wake ule wa milioni 46 sasa hivi analipwa milioni 58. Pia ongezeko lingine kwenye pensheni ya kila mwezi, analipwa zaidi ya shilingi 700,000. Kwa hiyo, unaweza ukaona utofauti ambao umekuwepo hapo katika hiyo. Umekuwa na faida. Zaidi ya asilimia 81 kwa sasa wananufaika na mpango huu. Lilifanywa hili baada ya kushirikisha wadau, kwa sababu asilimia 31 ndio wamekuwa wanufaika wa kikokotoo hiki kipya. Kumbuka tulikuwa asilimia 25, tumekuja asilimia 33.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna faida nyingine ya kutengeneza uendelevu wa mifuko. Hii mifuko utakumbuka, awali kulikuwa kuna mifuko mingi; LAPF, tulikuwa tuna PSSF, na mifuko mingine mingi. Wajibu wa Serikali na agizo lililotolewa ilikuwa ni kuangalia ile faida kwamba hii mifuko itakuwa inaendeshwa lakini mwisho wa siku wanachama wake wapya hawawezi kunufaika nayo kwa sababu ya kutokuwa na ustahimilivu au stability ya mifuko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kilichofanyika ni kuunganisha mifuko ili kutengeneza utaratibu ambao utawasaidia zaidi wanachama kuweza kunufaika na ndiyo maana tukawa na skimu hizo mbili. Moja ya upande wa wafanyakazi wa Serikali ambapo ni PSSSF na pili NSSF inashughulika na wale ambao ni watumishi katika kada za kawaida. Kwa hiyo, faida ni nyingi kuliko hasara kwa kipindi hiki. Walioongezeka hapo ni asilimia 81 ambao wanapata faida zaidi hasa kwenye mkupuo ule wa mwisho, imekuwa fedha wanayolipwa kwenye mkupuo ni kubwa zaidi, ahsante.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, ahsante, Miji wa Iringa ni kivutio cha utalii Kusini na katikati ya mji tumeboresha sana majengo yetu. Kuna jengo la TANESCO la Ofisi ya Mkoa ambalo limetelekezwa muda mrefu, ni lini mtalimalizia ili liendelee nalo kuchangia uvutiaji wa Kusini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Katika maeneo yote ambayo majengo hayajakamilika ni swala la kibajeti na tunaendelea kujikusanya kwenye fedha na kutanguliza vipaumbele lakini nimhakikishie Mheshimiwa Jesca kwamba jengo hilo pia litakamilishwa ili liweze kuwahudumia wananchi lakini kama ulivyosema liwe kivutio cha utalii Iringa.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kituo cha Afya Mkoga, kimejengwa kwa nguvu za wananchi na Mfuko wa Jimbo, tumefikia hatua ya boma: Je, Serikali inawezaje kutusaidia ili tumalizie kwa sababu tunahitaji sana huduma kwa eneo lile? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie Mheshimiwa Mbunge, kama ambavyo Serikali imekuwa ikitoa fedha shilingi milioni hamsini hamsini kwa ajili ya kumalizia vituo kama hivyo, navyo tutaenda kuviangalia na tutahakikisha na kituo chake kinakuwepo kwenye orodha ya vituo ambavyo vitamaliziwa.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, ahsante, Mji wa Iringa ni mji ambao barabara kubwa zote zinapita katikati ya mji; je, ni namna gani Serikali itatusaidia kwa dharura ili kupanua barabara za pembeni kwa kuwaongezea TARURA bajeti?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali lengo lake ni kuhahikisha kwamba barabara zetu zinapitika vizuri zaidi. Pia ni jukumu la halmashauri kuainisha maeneo ambayo wanadhani ni muhimu barabara zipanuliwe vizuri zaidi. Mameneja wa TARURA wa Mkoa na Wilaya wanatakiwa kufanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitumie fursa hii kutoa wito kwa Meneja wa TARURA Mkoa wa Iringa, wa Wilaya ya Iringa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, kuainisha barabara hizo, kutambua gharama zinazohitajika ili tuweze kuweka mpango kazi wa utekelezaji kwa awamu, ahsante. (Makofi)
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya makazi ya polisi katika Kituo Kikuu cha Iringa Mjini ni mbaya sana na majibu ya Naibu Waziri ni kwamba mpaka fedha zitafutwe. Nilitaka kujua wale askari wataendelea kuishi wapi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu la ulinzi na usalama katika Tanzania yetu ni jukumu la kila mtu na jukumu la kusaidia kuona kwamba huduma zinapatikana ni jukumu la Serikali lakini pia ni jukumu la viongozi. Namwomba basi angalau Mheshimiwa Mbunge naye aanze kuonesha mfano halafu sisi kama Serikali tutakuja kuongezea ili tuone namna ambavyo wananchi wanaweza kupata huduma hizo, nakushukuru. (Makofi)

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Hifadhi ya Msitu wa Kihesa - Kilolo pia imekutana na athari hizo. Je, Serikali iko tayari kutusaidia na sisi kuja kupanda miti ili kuendela kuhifadhi eneo lile?

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, tumelichukua, wataalam wetu wataenda kufanya tathmini na kuona jinsi ambavyo tunaweza kusaidia.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Mkoa wa Iringa una potential kubwa ya madini ya chuma pamoja na madini ya viwandani, je, Wizara ya Fedha iko tayari kutuunganisha na wadau ili tuweze kutumia potential hiyo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mkoa wa Iringa pia umekuwa ukikusanya maduhuli kila mwaka takribani bilioni moja kutokana na madini. Sasa Wizara ya Fedha ipo tayari kuwa na mpango mahususi kuisaidia GST na STAMICO kufanya utafiti wa kijiolojia ili tuongeze mapato hayo na yenyewe inufaike? (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la kwanza, Wizara ya Fedha tuko tayari na Mheshimiwa Mbunge kabla ya kurudi Jimboni tufanye kikao ili tuweze kumuunganisha na Idara inayosimamia hiyo ili aweze kuwaunganisha na wadau aliowataja kwa ajili ya kufanikisha hilo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu lile la pili, GST pamoja na taasisi zingine kuhusu kuongeza utafiti zaidi, tulishaongea na Wizara ya Kisekta na tuko tayari kuongeza fedha ili utafiti zaidi uweze kufanyika, kwa sababu potential ya kugundua maeneo mengine ya uchimbaji bado ipo na inaweza ikatuletea tija zaidi. (Makofi)
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza naishukuru Serikali kwa hatua tuliyofikia. Pia namshukuru Naibu Waziri kwa juhudi kubwa aliyoifanya mpaka mahali tulipofika. Naamini hatakata tamaa, tumalizie kabisa.

Mheshimiwa Spika, maswali yangu mawili ya nyongeza: La kwanza, kwa kuwa sasa Iringa inakwenda kuwa lango la utalii kusini. Ni namna gani Serikali imejipanga kuhakikisha kwamba tunaingiza tamaduni, mazingiira ya Iringa, watu wa Iringa, vivutio vya Iringa ili viwe sehemu ya kutoa taarifa au picha halisi kwa watalii watakaokuja kusini?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Mmejipanga vipi kuhakikisha kwamba viongozi wakiwepo Waheshimiwa Madiwani wanapewa semina kuhakikisha kwamba wanaupokea utalii kusini? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza niwataarifu tu wananchi wa Iringa hususan mikoa yote iliyoko kusini mwa Tanzania, kwamba malengo ya Serikali ni kuhakikisha tunatanua wigo kwa masuala mazima ya utalii. Ujenzi wa kituo hiki unaendana sambamba na kutanua wigo wa masuala mazima ya utalii. Kwa hiyo, tuna Hifadhi ya Ruaha katika maeneo yale ya jirani, lakini tutahakikisha tunaunganisha package zote za masuala ya utalii ikiwemo masuala ya utamaduni, masuala ya kihistoria, tunaunganisha na utalii wa wanyamapori. Haya yote yatakuwa yanaunganishwa kwenye package moja ambayo tutaisaidia sasa sekta hii iweze kukua katika maeneo mazima yaliyoko kusini mwa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kwenye suala lingine hili la viongozi wa kisiasa hususan Waheshimiwa Madiwani, kwa kuwa tunaanzisha kituo mahususi hiki, lazima tutatoa elimu kwa wananchi na viongozi ili nao watusaidie kutoa promotion katika maeneo hayo na pia waweze kutembelea vivutio hivi, kwa sababu tunaamini kiongozi anapofika katika eneo hilo, tayari anawahabarisha hata wengine ambao hawajawahi kufika katika eneo hilo. (Makofi)
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, ahsante. Yaliyotokea Mtwara Mjini kwa PRIDE pia yametokea ndani ya Iringa Manispaa. Je, zoezi hilo Julai mtalifanya kwa wote nchi nzima pamoja na Iringa Manispaa walioathirika?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jesca kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tuliposema kwamba Kampuni hii ya PRIDE tayari imefanyiwa taratibu na Sheria ya Ufilisi, tunaenda kulipa fedha hiyo kwa wadai walioko Mtwara nina maana kwamba ni nchi nzima wale ambao wana madai Julai tutaanza kulipa fedha hiyo. (Makofi)
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kituo cha Afya cha Ipogolo ni kati ya vituo vikongwe vya afya na vinahudumia zaidi ya wanawake 600 kwa mwezi lakini hakina combined ward.

Je, Serikali inaweza kutusaidia kutujengea combined ward katika kituo hiki ili kupunguza msongamano?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, tutatuma timu kwenda Halmasahuri ya Manispaa ya Iringa kwa ajili ya kufanya tathimini ya kituo hiki cha afya cha Ipogolo na kuona kama eneo linaruhusu kuweza kujenga maeneo haya ambayo Mheshimiwa Mbunge ameomba na kama inaruhusu tutaweka katika mipango yetu ya kutafuta fedha ili kuweza kujenga kituo hiki cha afya ambacho ni kongwe.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, ahsnate. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali langu la kwanza, mmesema Serikali imejipanga kuipa kampuni yetu ya TFC mtaji wa bilioni 40 na sasa hivi tumebakiwa na miezi mitatu tu tufike kwenye high season ya kuhitaji mbolea. Je, mtatumia muujiza gani kuhakikisha mmeagiza mbolea na mnaisambaza nchi nzima?

Swali langu la pili, ni kwa nini CPB hawataki kuwarudishia wakulima fedha, walizoahidi kuwapa mahindi wakati Serikali imezuia CPB isitoe mahindi, na fedha zao hamtaki kuwarudishia ni kwa nini na mnarudisha lini hizo fedha?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nilitoa taarifa humu ndani Bungeni na naomba leo nirudie ya kwamba Serikali imejipanga kuhakikisha ifikapo mwezi wa saba mbolea zote za kupandia na kukuzia ziwe zinapatikana kwa wakulima ili waanze msimu na mbolea zikiwemo.

Mheshimiwa Spika, nakata nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba TFC walianza maandalizi haya mapema na hivi sasa tuko katika hatua za mwisho kuanza kupokea shehena za meli ambazo tutashusha mzigo huo, pia tunayo mbolea ya kutosha kuanzia kwa wakulima katika msimu unaoanza hivi karibuni. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba jambo hilo litafanyika.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, nimesikia hoja yake ya CPB na wakulima, naomba nikae na Mheshimiwa Mbunge nipate hayo madai ya wakulima, mimi na CPB tutakaa tuone namna ya kuweza kutatua jambo hili, ili mwisho wa siku tuweze kuhakikisha kwamba wakulima wanapata haki yao.
MHE. JESECA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa viongozi wa Wizara ya Mambo ya Ndani wana afya nzuri ya akili, ni lini sasa watatujengea nyumba za askari katika Kituo Kikuu cha Polisi pale Iringa Manispaa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru Balozi wa Afya ya Akili anatambua jinsi tulivyo timamu. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi yangu ni hiyo, kwamba katika ujenzi wa vituo vya Polisi huenda sambamba na ujenzi wa nyumba za Maaskari, Wakaguzi na Maofisa. Kwa hiyo, Iringa kama alivyosema ni mjini, ukiangalia kwa vipaumbele, pale angalau watu wanaweza wakapata nyumba zenye hadhi za kupanga, lakini kuna maeneo ya vijijini kabisa ambayo uwezekano wa kupata nyumba za kupanga ni changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwenye ujenzi wa nyumba, vipaumbele tutaweka kwenye maeneo ambayo yana changamoto kubwa za kupata makazi. Kwa hiyo, wale wa Iringa watasubiri, lakini kadri fedha zitakapopatikana na wao pia watajengewa.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, ahsante. Katika Hospitali yetu ya Mkoa wa Iringa tuna kitengo cha Watoto Njiti na tuna upungufu mkubwa wa mashine na dawa inaitwa Lung surfactant ambayo dozi moja inauzwa Shilingi Laki Tano na mtoto ili a-survive anahitaji dozi tatu. Serikali ina mpango gani kuangalia kwamba dawa hizi angalau zinawekewa ruzuku ili kupunguza gharama hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, moja kwanza sioy dawa kuwekewa ruzuku kwa taratibu na sheria na taratibu za Wizara ya Afya ni kwamba huduma ya mtoto chini ya miaka Mitano including hawo Watoto Njiti na Mama na Mtoto ni bure. Kwa maana kwamba tunaposema mlitupitishia bilioni 200 kwa ajili ya kununua dawa na vifaatiba. Hilo eneo tutakwenda kulielekeza nguvu nyingi kuhakikisha kwamba Watoto njiti hawawezi kukutana na matatizo hayo.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, ahsante. Katika Hospitali yetu ya Mkoa wa Iringa tuna kitengo cha Watoto Njiti na tuna upungufu mkubwa wa mashine na dawa inaitwa Lung surfactant ambayo dozi moja inauzwa Shilingi Laki Tano na mtoto ili a-survive anahitaji dozi tatu. Serikali ina mpango gani kuangalia kwamba dawa hizi angalau zinawekewa ruzuku ili kupunguza gharama hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, moja kwanza sioy dawa kuwekewa ruzuku kwa taratibu na sheria na taratibu za Wizara ya Afya ni kwamba huduma ya mtoto chini ya miaka Mitano including hawo Watoto Njiti na Mama na Mtoto ni bure. Kwa maana kwamba tunaposema mlitupitishia bilioni 200 kwa ajili ya kununua dawa na vifaatiba. Hilo eneo tutakwenda kulielekeza nguvu nyingi kuhakikisha kwamba Watoto njiti hawawezi kukutana na matatizo hayo.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Je, ni lini Serikali itaanza kujenga barabara ya MR – Pawaga kwa kiwango cha lami kuanzia MR – Iringa Mjini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge atakuwa shahidi kwamba katika bajeti ya mwaka huu kuna kiasi kimetengwa kwa ajili ya kuanza kilomita kama sikosei ni kilometa kama 20 kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, kadri tutakavyokwenda taratibu zikishakamilika barabara hizo zitatangazwa kwa ajili ya kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni lini Serikali itatekeleza mpango wake wa peri urban kupeleka umeme katika mitaa yenye sura za vijiji katika miji yetu ikiwepo katika Manispaa ya Iringa Mtaa wa Ugere, Mosi, Msisina na Mtalagala.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Msambatavangu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango wa kupeleka umeme kwenye maeneo ya miji yenye sura za vijiji (peri urban) na kazi hiyo inaendelea kwa sasa. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge awe na Subira, kazi hii itakamilika, maeneo haya yatapatiwa umeme.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, naomba sasa niwe na swali moja tu la nyongeza. Kwa kuwa maelezo ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri umeyaeleza, vikundi vingi vilivyopewa mizinga hiyo ni vya Wilaya ya Iringa lakini kutoka Iringa Vijijini na Iringa Manispaa ni lango la utalii Kusini.

Je, mpo tayari sasa kutupatia na Iringa Manispaa ili angalau uoto wa asili urudi kwa kufuga nyuki? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jesca Msambatavangu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mara tutakapopata orodha ya vikundi vilivyoanzishwa kwa jambo hili, Wizara itaona jinsi ambavyo inaweza kushirikiana na hamashauri ili kuweza kuwapatia mizinga. (Makofi)
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza naishukuru Serikali kwa majibu mazuri ambayo wametupatia, nami nakubaliana nayo na wala hatuna shida kwenye majibu hayo, isipokuwa tu, tutakapokuja kujadiliana nafikiri tunaweza tukafikia muafaka.

Mheshimiwa Spika, kwanza tunawashukuru kwa watumishi mliotuletea 26 ndani ya Manispaa ya Iringa wanaokwenda kwenye zahanati zetu na vituo vya afya na kwa ajili ya ujenzi wa wodi pale Frelimo. Ili kupunguza changamoto ya hiyo Hospitali ya Mkoa, Serikali ina mpango gani sasa wa kutujengea wodi ya watoto katika Hospitali ya Frelimo na wodi ile ya Internal Medicine kwa ajili ya wagonjwa wa kawaida katika Hospitali ya Frelimo pamoja na kututengenezea zile rooms za reproductive health pharmacy na CT katika Hospitali ya Frelimo ili kupunguza changamoto ya Hospitali ya Mkoa wa Iringa?

Mheshimiwa Spika, pia ule mgao tulioomba kwa Hospitali ya Mkoa wa Iringa; je, tumepata Madaktari? Maana tulikuwa tuna upungufu wa watumishi karibu 200; ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwenye suala lake la kwanza la ujenzi wa wodi ya akina mama na Watoto, kama ambavyo Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu alisema, katika ununuzi wa vifaa na manunuzi yote ambayo yamefanyika kwa ajili ya vitu mbalimbali kwenye fedha ambazo Rais wetu alitupa, shilingi trilioni 1.3, imeokolewa shilingi bilioni 13, kwa maana tumenunua kwa bei rahisi zaidi kuliko ilivyotegemewa.

Mheshimiwa Spika, sisi na Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo tumezoea kukaa pamoja, tunaweza tukakaa tuone kipaumbele tushirikiane na Waziri wa TAMISEMI ili anachokisema kiweze kufanyika.

Mheshimiwa Spika, suala lako la pili linazungumzia masuala ya Hospitali yake ya Mkoa. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, wakati tunakuja na ile timu, mimi naye tutakuwa pamoja na nina uhakika kwamba anachokifikiria kitakwenda kutekelezwa, ahsante.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, Serikali ina kauli gani kwa barabara ya Iringa (MR) – Pawaga Road (Itunundu) ambayo mkandarasi ametelekeza vitu na haendelei na wakati alikuwa ameichimbachimba, hivyo wananchi kupata shida?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Mbunge, baada ya hapa tuweze kukutana naye ili niweze kujua changamoto ya huyo mkandarasi na tuweze kuondoa hiyo changamoto ambayo mkandarasi anaileta kwa wananchi. Ahsante.