Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Jesca Jonathani Msambatavangu (2 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi na nawashukuru wote kila mmoja kwa nafasi yake aliyechangia uwepo wangu mahali hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kupokea Hotuba ya Rais kwa mikono miwili na nampongeza sana kwa sababu sisi kama Wabunge, tumepokea dira na tumepata kitendea kazi cha kufanyia kazi katika uwakilishi wa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, naanza na sekta ya utalii, katika ukurasa wa 46, Mheshimiwa Rais ameongea kwamba ni sekta ambayo itawekewa mkazo mkubwa kutokana na umuhimu wake katika Taifa letu; kwanza, katika mchango wake mkubwa katika kuongeza pato la Taifa, pia ni sekta ambayo itatoa ajira kwa vijana wetu kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza upande wa Serikali; wenzetu hili wameshalianza, nasi watu wa Kanda ya Kusini au Southern Socket Tourism tunawashukuru sana kwa sababu tumeletewa mradi mkubwa wa REGROW ambao umetengewa dola milioni 150 kwa ajili ya kuendeleza utalii kusini; Iringa pia haikuachwa, itakuwa hub ya utalii huo, nasi tumepewa dola milioni sita kwa ajili ya kuanzisha Tourist Resource Center pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunawashukuru sana kuhusu msitu wa Kihesa Kilolo. Namshukuru Waziri wa Maliasili, tumeongea hili na amelifanyia kazi kwa haraka sana. Naamini ujenzi unaanza pale mara moja ili nasi southern socket au ukanda wa kusini tuwe sehemu ya kuchangia pato la Taifa kupitia utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba, ili utalii uweze kuwa mzuri, tunahitaji kuboresha huduma zetu kwa watalii. Kwanza, naomba tuboreshe huduma ya upatikanaji wa ubadilishanaji wa fedha za kigeni. Watalii wetu wengi wanapokuja kwenye zones za utalii wanakosa huduma hii kutokana na mchakato ambao ulipitishwa kwenye maduka yetu ya kubadilisha fedha za kigeni. Kwa hiyo, tunaomba Serikali iangalie hasa kwenye hizi nyanda za utalii, ni namna gani inalegeza masharti ili tuweze kuwahudumia watalii na lile neno lao, watakaporudi tutapata watalii zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuhusu kuboresha huduma za miundombinu, tunaomba barabara. Tumeshaanza kuboreshewa kiwanja cha ndege, sasa tunaomba barabara ile ya National Park, watakaposhuka pale ile barabara ya kutoka Iringa mpaka Ruaha National Park ya kilometa 104 basi nayo iboreshwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja kwenye suala la elimu. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa ukarabati mkubwa uliofanyika kwenye Shule za Sekondari kongwe, tunaomba juhudi zile zile zielekezwe kwenye shule zetu za msingi kwani nazo zimechakaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mtaala haliepukiki, tunaomba Wizara ya Elimu tujipange kubadilisha mtaala kwa watoto wetu ili watoto wetu waweze kuajirika na kujiajiri nje na ndani ya nchi yetu. Tunaomba sana elimu ya kujitegemea irudishwe kwenye shule zetu ili watoto hawa wanapotoka waweze kujifunza kujitegemea. Vile vile tunaomba kuwe na masomo compulsory kama ya ujasiriamali kuanzia kwenye level ya shule ya msingi ili watoto waweze ku-develop visions zao wenyewe tangu wakiwa wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru sana kwamba kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais pia amesema kutakuwa na program mbalimbali za mafunzo ya ujuzi na maarifa ili kukuza uchumi. Tunaomba sasa vyuo vikuu vilivyoko kwenye zones zetu na mikoa yetu, kama kile Chuo Kikuu cha Mkwawa, kiwe independent, kiweze kusimama chenyewe ili kisaidie kutengeneza program zao kwenye kanda zetu zile ili kuwasaidia watoto wetu waweze kupata maarifa ya kufaidika na mazingira yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tusiendelee kuwa ni Vyuo Vikuu Shirikishi halafu vinaendelea kupokea program zinazopangwa Dar es Salaam wakati kule kule zinge-scan mazingira ya kule, zingepanga program za kule kule, zitawasaidia wananchi wetu. Tunaomba sana hili lichikuliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la uchumi, tunashukuru kwa ajili ya uzalishaji, lakini tunaomba sana mafunzo ya ujasiriamali yatiliwe mkazo kwa sekta binafsi lakini kwa informal sector na formal sector. Tunaomba makundi yale ya Madereva, Wamachinga, makundi ya bodaboda, yapewe mafunzo ya ujasiriamali ya kimkakati kutokana na kazi zao. Mafunzo ya ujasiriamali yasiandaliwe tu kwa ujumla, lakini yaende specific. Kwamba hawa ni Mama Ntilie, katika sekta yao tunawaboresha vipi? Hawa ni madereva wa bajaji, katika sekta yao tunawaboresha vipi? Tusitafute kupeleka mafunzo ambayo ni mafunzo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kengele imeshagonga.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, dakika moja. Kulinda tunu za Taifa, naomba hili niliseme. Hapa yameongelewa masuala…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Jesca kuna majina mengi hapa mbele. Ahsante sana.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Mpango wa Tano wa Maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo ya msingi tunapotaka kufanya mabadiliko ya kiuchumi na kwenye biashara. Ukichukua mfano wa nchi ya China ilipotaka kufanya mabadiliko yake kwenye masuala ya uchumi na biashara zaidi ya miaka 40 walikuwa wakiendelea kusuguana na sheria na sera zao. Mipango na mikakati yao ilikuwa imekaa vizuri; ilikuwa ikijali muda, lakini ukienda kwenye mambo ya sheria na sera zao zilikuwa zinawarudisha nyuma na zikafanya uchumi wao kuendelea kuwa duni, ulishindwa kuendelea kukua, tegemezi na usiozingatia ushindani wa kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadaye walipoamua sasa kuanza kubadili sera na sheria zao ndipo walipoanza kuleta maendeleo makubwa na ndani ya miaka nane kwa ripoti za Benki ya Dunia, walikuwa wanakua mara mbili zaidi ya GDP ambayo ilikuwa ni kwa asilimia 9.5. Ndipo walipoweza sasa kutoa umaskini kwa watu wao zaidi ya milioni 800 maana tunapoongelea China ni watu zaidi ya milioni 1,400.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sasa Mpango huu wa kwetu wa Maendeleo wa Miaka Mitano ni mzuri na umezingatia standard na spidi au umejikita katika muda lakini kikwazo kikubwa kitakachokuja kutukuta, katika ukurasa wa tano wa maeneo ya muhimu ya kuzingatia ambao Mpango unaeleza, umeeleza mambo mazuri lakini haukuweka msisitizo katika kuhakikisha kwamba tunabadili na sisi sheria na sera zetu ambazo huwa zinatusababisha tusiende kwa spidi au tusiende kwa wakati ule ambao tumeupanga, hicho kipengele hakijawekwa. Kwa hiyo, tunaomba tushauri kwamba katika Mpango huu tujaribu kuangalia namna gani tutabadilisha sheria na sera zetu ili ziweze kuendana na muda ili tuweze kuutekeleza huu mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi sana tumekuwa tukipanga vitu vingi lakini unakuta kuna sheria zinakinzana. Tunakwenda kwa spidi tunataka kuinua utalii, Mpango unatuambia kwamba tutoke katika watalii 1,500,000 mpaka itakapofika 2025 tuwe tumefika watalii 5,000,000, lakini kuna sera nyingine ambazo zipo sasa zinahusiana na masuala ya kutoa vibali au permit za kuishi, unakuta zinakinzana na ile sera ya sisi kuboresha spidi ya kuendeleza utalii wetu au kuboresha spidi ya uwekezaji. Mwekezaji anakuja katika taifa letu, amekuja na mtaji, anakuja kupambana na Sheria ya Labour ambapo yeye anataka kuja na mke wake lakini sheria inamkatalia asije na mke wake au anapata usumbufu kupata permit ya kuishi na mke wake. Sasa unakuta vitu kama hivi vinakuwa vinakinzana, tusipoziangalia sheria na sera zetu, bado hatutaweza kuutelekeleza huu Mpango kwa wakati kama ambavyo tunatarajia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza tukajifunza kutoka kwenye Sekta ya Madini, namna ambavyo madini yamechangia kwenye maendeleo yetu katika Mpango wa Pili, ni kwa sababu pia yalifanyika mabadiliko makubwa ya kisheria kwenye sheria za madini na ile ikatusababisha tukaenda vizuri. Kwa hiyo, ushauri ni kwamba tunaomba sheria na sera nazo ziangaliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kujua kwamba tuna mkinzano wa kisheria na mipango yetu utaona mara nyingi sana mambo yetu mengi yanakwenda kwa waraka, matamko, yanakuwa kama ya zimamoto hivi. Kwa sababu kama sheria ingekuwa inakwenda sawasawa na mipango, hivi vitu vya zimamoto, kwenda kwa matamko na nyaraka visingekuwa vinakwenda namna hii. Hii inaonesha namna gani sheria yetu inawezekana haiko sawasawa na mipango ile ambayo tunaiweka. Kwa hiyo, tujitahidi kubadilsiha sheria zetu na tujitahidi kuangalia mabadiliko makubwa kwenye sera zetu ili tuweze kwenda sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi wetu unatakiwa ujengwe sasa kwa misingi ya soko. Tusitengeneze tu mpango kwamba tulime mazao haya zaidi, tulime kitu hiki au kile zaidi, hebu tuangalie soko lina uhitaji gani. Kama tunasema tuna uhitaji mkubwa wa mafuta ya alizeti, huko ndiko sasa tutengeneze mpango namna gani tunawashawishi wakulima ili waweze kulima alizeti na namna gani tunatengeneza sheria ambayo itazuia uingizaji wa mafuta ya alizeti kwenye nchi yetu ili soko letu la ndani lenyewe lianze kuwa ni soko kabla hatujategemea soko la nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu, lazima …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Kengele imeshagonga Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. (Makofi)