Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Michael Mwita Kembaki (18 total)

MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri lakini ningependa kuuliza swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Mtaa wa Kinyambi na Bugosi hawafanyi shughuli zozote katika maeneo yale, na wengi wao walikuwa wanafanya shughuli ndogo ndogo za kujikimu kama kilimo na shughuli zingine na ukizingatia kwamba ni muda mrefu sasa tangu uthamini ufanyike, mwaka 2013 hadi sasa.

Je, wale wananchi wanaweza kuruhusiwa kuendelea na shughuli zile ili waendelee kujikimu badala ya kutaabika na kuendelea kukaa pale bila kufanya shughuli ambazo zinawaongezea kipato? Ahsante.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwita kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza niseme tu kwamba maeneo yote ambayo yanamilikiwa na Jeshi letu ni muhimu na kwa manufaa ya nchi yetu na kwa wananchi kwa ujumla. Lakini niseme tu kwamba uwepo wa maeneo haya umepangwa kistratejia (strategically), tumejipanga kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kazi za jeshi zinafanyika vizuri. Niwaombe tu wananchi waweze kuvuta subira; kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, tunafanyia kazi ili tuweze kuwatendea haki wananchi hawa; hii ni pamoja na kuwalipa fidia zao ambazo zitawawezesha kwenda kufanya shughuli zao zingine.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge kwanza nikupongeze kwa namna ambavyo mara kadhaa tumeweza kuzungumza na Mbunge ili tuone namna nzuri. Kikubwa nachoweza kusema hapa ni kwamba sisi tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba zoezi hili linakamilika mapema na wanachi wanapata haki zao. Tunaogopa kwamba tukiwaruhusu wananchi wakiendelea kutumia maeneo haya wanaweza wakafanya vitu ambavyo vina gharama kubwa na baadaye vikawatia hasara ndugu zetu hawa wananchi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo wavute subira tu, nafikiri tutaendelea kushughulikia suala hili kwa kuwasiliana Serikali zetu za Wilaya na Mkoa ili tuone namna nzuri ya kuwafanya wananachi wasikwame, waendelee kufanya uzalishaji na shughuli zao zingine. Ahsante sana.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kuuliza swali ambalo linafanana na ambalo muuliza swali wa kwanza alivyouliza.

Swali langu ni kwamba katika Mji wetu wa Tarime Mjini lipo korongo maarufu kama korongo la starehe, na korongo hili limekuwa hasa wakati wa mvua linaleta madhara makubwa maana linapitisha maji mengi na hatimaye linahatarisha nyumba za wakazi ambao wanaishi kandokando ya korongo hili.

Je, Serikali ni lini litajenga Korongo hili ili at least wakazi ambao wapo katika mtaa huu waweze kuwa na uhakika wa makazi yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tutatuma wataalam wetu kwenda kuangalia na kufanya tathmini katika Korongo hilo ili kusudi wataalam hao walete tathmini ambayo ni sahihi kwa ajili ya kufanyia kazi ndani ya mwaka wa fedha ujao. (Makofi)
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii kuuliza swali, swali langu ni kwamba mwezi mmoja uliopita daraja lilikatika katika mji wetu wa Tarime na likasababisha vifo vya watu watatu na wengine watatu mpaka sasa hivi hawapatikani na inadhaniwa kwamba walikwenda na maji, na hata sasa hivi ninavyozungumza kuna daraja limekatika kipande kimoja daraja ambalo linatoka mjini kuelekeza Kibaga ambako wanachimba madini na kuna magari makubwa yanabeba makinikia yanapita pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba je, ni lini watarekebisha hili daraja ili lisije likaleta maafa mengine kama ilivyosababishwa na kuvunjika kwa daraja, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine kwamba Serikali inatambua kwamba mwaka huu kumekuwa na uharibifu mkubwa sana wa barabara nyingi na hasa hizi za changarawe na udongo. Na sisi kama Wizara tulishalitambua hilo tuna maandalizi ambayo tulishayafanya ikiwa ni pamoja na kununua madaraja ya dharula lakini imekuwa ni vigumu sasa hivi kutengeneza hizo barabara kwasababu nyingi sio tu zinahitaji kuweka madaraja lakini pia zinahitaji kuweka matuta ambayo yanainuliwa sasa inakuwa ni ngumu kufanya kazi hiyo katika kipindi hiki ambacho mvua inaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine kwamba barabara zote inaainishwa zile ambazo zimepata changamoto hasa kutokana na mvua na mara hali ya hewa itakapokuwa vizuri wakandarasi wapo tayari watazirejesha barabara hizi zote katika hali yake ya kawaida ili ziendelee kutumika ikiwa ni pamoja na barabara ya Mheshimiwa Michael Kembaki Mbunge wa Tarime.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii kuuliza swali la nyongeza.

Ningependa kujua, kwasababu wamesema kwamba wananchi wale ambao walikuwa wanalima katika mlima ule walikuwa wanaharibu mazingira na bado magereza ambao wanapewa eneo lile wameendeleza kilimo kama walivyokuwa wanafanya wananchi. Sasa ningependa kujua kilimo cha wale waliopewa Magereza wao hawaharibu mazingira au wananchi ndio wanaharibu mazingira?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ningependa kujua kama Mlima Nkongole ndio pekee ambao Serikali imeona kwamba uhifadhi lakini ukienda maeneo kama Mwanza wananchi wanaishi mlimani.

Je, ni mlima Nkongole peke yake ndiyo imeonekana ni hifadhi au iutumie au kwa milima yote ambayo ipo katika nchi hii ndiyo inayohifadhiwa na Serikali? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita, Mbunge wa Tarime Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ajenda ya uharibifu wa mazingira, haijalishi mtu ama taasisi kama watu binafsi wanaharibu mazingira, kama Jeshi la Magereza linaharibu mazingira ama taasisi yoyote inaharibu mazingira wote ni waharibifu wa mazingira. Kwa haina excuse ya aina yoyote na kutokana na jibu la msingi Naibu Waziri, Ofisi ya Rais - TAMISEMI alivyokuwa akijibu hapa alieleza wazi kama eneo hilo lipo katika mchakato katika maeneo lindwa. Sio eneo hilo peke yake, isipokuwa kuna maeneo mengine ya fukwe na maeneo mengine ambayo sisi Serikali tumeona kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004 sasa kuna mchakato wa kuainisha maeneo hayo yote.

Kwa hiyo, tuseme kama Jeshi la Magereza licha ya kukabidhiwa wanaharibu mazingira maana yake jambo hilo halifai na ofisi yetu inasema jambo hilo tutaendelea kulisimamia kwa karibu zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa nini maeneo mengine watu bado wanaendelea kujenga nyumba. Tumesema sasa hivi tutakuwa nimetoa maelekezo mahasus katika upande wa mazingira na ndio maana katika suala zima ambalo tutalizindua siku ya tarehe 5 Juni, 2021 Kampeni Kabambe ya Kimazingira miongoni mwa mambo hayo tutakayokwenda kuyaainisha ni suala zima la utoaji elimu katika suala zima la utunzaji wa mazingira.

Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge sote tushirikiane pamoja katika ajenda kubwa ya kulinda mazingira hususan kuilinda nchi yetu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nachukua nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kutupa zaidi ya kilometa 80 ya barabara ya lami kutoka Tarime Mjini, kuelekea Serengeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba kwa sababu tayari wananchi wakazi wale wa Tarime waliopo pembezoni mwa barabara wameshabomoa nyumba zao kwa ajili ya kulima barabara ile, lakini kuna kipande ambacho kulikuwepo na Mkandarasi ambaye alikuwa anajenga kipande pale Lebu Center kwenda Mugabiri na tayari yule Mkandarasi anaendelea…

NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa Kembaki.

MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo najenga hoja ya swali langu.

NAIBU SPIKA: Huna haja ya kujenga hoja, wewe taja barabara unayotaka kuulizia swali.

MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mkandarasi yule anaendelea na ujenzi wa kile kipande na tayari wananchi wamebomoa kwamba ile barabara inajengwa upya kutoka hapo mjini kuelekea…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kembaki uliza swali.

MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni hivi ni kwa nini Mkandarasi yule asingepewa sehemu nyingine ajenge badala ya kujenga sehemu ambayo tayari TANROADS watakuja kujenga?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Kembaki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mkandarasi yupo site na anajenga, namwomba Mheshimiwa Mbunge baada ya hapa nikutane naye kupata maelezo sahihi kwa ajili ya kutatua hiyo changamoto anayosema ili kwa pamoja na Meneja wa TANROADS Mkoa tuone namna ya kuondoa hiyo changamoto. Ahsante.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nimshukuru na nimpongeze Waziri kwa majibu yake mazuri ambayo yametolewa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 45 ya Watanzania wanatumia tiba asili. Tunashuhudia waganga wa tiba asili wakiwapa watumiaji kwa vifungashio ambavyo siyo salama. Vilevile tunaona wanatumia vikombe kupima dawa na mengine ambayo sijayataja. Ningependa kujua, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba dawa wananchi wanazotumia ni salama na vilevile zinasajiliwa kwa ajili ya matumizi sahihi ya wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nijibu swali la Mheshimiwa Kembaki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, alichojaribu kusema ni kwamba asilimia 45 ya Watanzania wanatumia hizi dawa za asili ambayo ni kweli. Pia anajaribu kuonesha kwamba wakati mwingine zinafungwa kwenye vifungashio ambavyo siyo salama. Anataka kujua tunafanyaje ili kuhakikisha sasa hizi dawa zinaweza kuwafikia Watanzania zikiwa salama?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tuna taasisi yetu ya Mkemia Mkuu wa Serikali ambayo kazi yake moja kwa moja ni kwa ajili ya kupima usalama wa dawa hizo; lakini kuwapa maelekezo ni namna gani wanaweza wakazipaki na kufikisha kwa wananchi zikiwa salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakiri ukweli kwamba kwa kipindi hiki cha corona kumekuwa na dawa mbalimbali na mambo mengi ambayo yanaleta shida. Hata hivyo, Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kama nilivyosema nyuma hapa, alishatoa shilingi bilioni 1.2; na leo nimetoka ofisini, imeenda tena shilingi bilioni 1.2, kwa maana ya shilingi bilioni 2.4 kwenye eneo hili la tiba asili kwa ajili ya kwenda kujenga uwezo kwa hawa watu wetu wazalishaji wa tiba ya asili, lakini kujengea taasisi zetu uwezo wa kuangalia hizo tiba asili zinazotolewa.

Je, zina hivyo vitu ambavyo vinaweza kutibu ugonjwa wenyewe unaosemekana? Pia itaenda kununua mashine za kupima na mambo mengine ya kusaidia utafiti na kupima usalama wa dawa hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali imejiwekeza kwenye hilo. Majibu mengine kutokana na hii shilingi bilioni 1.2 ambayo imetoka leo, nayo tutawaletea majibu yake kwa sababu tunaenda kuangalia dawa nyingine 56 ambazo zilikuwa zinatumika wakati huu wa corona. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, katika Mji wetu wa Tarime tunategemea chanzo kimoja kikuu cha maji ya Bonde la Ndurumo, lakini kumetokea baadhi ya watu kuanzisha plant za kuchenjua dhahabu kandokando ya chanzo hiki.

Je, Serikali inatuhakikishiaje watu wa Tarime kwamba maji tunayotumia yapo salama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, maji yote ambayo yanafika kwa mlaji wa mwisho kwa maana ya mwananchi ni maji salama ambayo tayari Wizara kupitia Idara ya Maabara inakuwa imeshafanya kazi yake, hivyo ninapenda kuwatoa hofu wananchi wote wanaoishi kandokando ya wachimbaji kwamba maji yanafanyiwa kazi katika maabara.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi Wizara imekuwa ikitoa tamko la kuzuia masomo ya ziada katika Shule za Msingi na ilhali wakijua kwamba muda wa ukamilishaji wa mtaala unakuwa hautoshi. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba inatenga muda ambao watoto hao watasoma wakamilishe mtaala wao kwa wakati?

Swali la pili, Mheshimiwa Waziri amesema kwamba Walimu wanapaswa kutafuta muda wa kukamilisha mtaala huu kwa mpango kazi ambao wanao. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapa motisha Walimu hawa ambao wanafanyakazi hii ngumu ya kuhakikisha kwamba elimu inatolewa kwa wakati? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kembaki Mbunge wa Tarime Mjini kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwishajibu kwenye majibu yangu ya msingi kwamba katika mwaka tunazo siku 365, kati ya siku hizo 365 tunatumia siku 194 kwa ajili ya kukamilisha mitaala katika mwaka husika wa masomo. Najua maono ya Mheshimiwa Mbunge kwenye eneo hili, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa vile hivi sasa tunapitia Sheria yetu ya Elimu tunapitia mitaala pia tunapitia sera ya elimu, bado hatujaona changamoto kwa hizi siku 194 kwenye utekelezaji wa mitaala hii kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, kwa vile bado tunaendelea kubeba au kuchukua maoni tunaomba tubebe vilevile maelezo yake haya tuweze kuyaingiza kwenye rasimu yetu ya mitaala inayokuja ili tuweze kuangalia kama hizi siku 194 zitatosheleza au hazitatosheleza au kama kutakuwa na changamoto yoyote tuweze kufanya marekebisho. Hilo eneo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili la motisha, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Bunge lako Tukufu kwamba Serikali imekuwa ikitoa motisha au kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria. Kama tunavyofahamu katika kipindi kilichopita Mheshimiwa Rais aliongeza mshahara siyo tu kwa watumishi kama walimu, lakini kwa watumishi wote. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kufanya hivyo kwa kadri bajeti itakavyokuwa inaruhusu ili watumishi wote waweze kupata stahiki zao kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ninaipongeza Serikali kwa hatua hizi zinazofanya za kuwafikia wakulima, lakini hatua hizi ambazo wamezichukuwa zinalenga hasa wakulima wakubwa. Kama mnavyojua, wakulima wa Tanzania wengi wao wana uchumi mdogo, ni wakulima wadogowadogo ambao wanalima heka moja, nusu heka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni mkakati gani hasa Serikali inao wa kuwafikia wakulima wadogo ambao hawana uwezo wa kununua simu, hawana uwezo wa kununua TV au kuweza kufika kwenye warsha na maonesho ya Nanenane. Je, Serikali ina mkakati gani hasa wa kuwafikia? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu niliyoyatoa kwenye swali la msingi, Serikali inachukuwa hatua mbalimbali: Moja, sasa hivi tumeanza kusajili wakulima, kwa muda mrefu tumekuwa tukihudumia watu tusiowatambua. Kwa hiyo, sasa hivi tumeanza process ya kuwasajili wakulima kuwatambua walipo, kuchukua hadi fingerprints, vilevile tunaenda kuchukua GPS coordinate za mashamba yao, zoezi hili linaendelea.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine tunalolifanya ni kumwezesha Afisa Ugani ili awe na uwezo wa kuwafika wakulima. Tunao upungufu wa Maafisa Ugani katika nchi yetu wasiozidi Elfu Saba, kwa hiyo ili kuhudumia kaya Milioni Saba inakuwa tatizo. Kwa hiyo, Serikali imewekeza kuwapatia pikipiki na sasa tunawapatia nyezo na hivi karibuni tutawapatia vishikwambi ambavyo vitakuwa vinachukua taarifa za kila mkulima aliyemtembelea katika eneo lake. Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge hii extension program itatuchukua kwa kipindi cha miaka mitatu ili kuweza kufika kule ambapo tunapotaka na kutambua mkulima ni nani na kila Afisa Kilimo kukabidhiwa idadi ya wakulima atakaokuwa anawahudumia kwa siku. (Makofi)
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali langu ni kwamba, katika mji wetu wa Tarime Mjini tunacho chanzo cha Nyandurumo ambacho ndicho kinacholisha maji katika Mji wetu wa Tarime, lakini Nyandurumo hii ipo katika Kata ya Kenyamanyori. Wakazi wa Kenyamanyori hawana maji.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba, wakazi wa Kenyamanyori wanapata maji ili waweze kutunza chanzo hiki ambacho ni muhimu sana katika Mji wetu wa Tarime? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, Spika ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael, Mbunge wa Tarime, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nampongea Mheshimiwa Michael, alishaniona katika hili. Sera ya Maji inataka vijiji vyote vilivyopo katika eneo la chanzo wawe wanufaika namba moja. Naendelea kutoa maagizo kwa MD na RMs waweze kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao. Tunakwenda kuhakikisha watu wote wanaopitiwa na mtandao wa bomba wananufaika na maji.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali ningependa kujua maana katika Hospitali yetu Kuu ya Wilaya Bomani, jokofu lake limekuwa likiharibika mara kwa mara.

Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba Jokofu lile linafanya kazi ili watu wapate huduma ambayo inastahili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwita Kembaki Michael, Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli jokofu la Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime ni la siku nyingi ni chakavu na linaleta usumbufu wa kuharibika mara kwa mara, lakini Serikali imeshatenga fedha katika mwaka wa fedha ujao 2023/2024 kwa ajili ya kununua jokofu lingine kwa ajili ya Hospitali ya Mji wa Tarime. Ahsante.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna shule katika Mji wetu wa Tarime inaitwa Bugosi, ina zaidi ya wanafunzi 1,000 lakini ina madarasa Sita na wananchi wamejitahidi sana kujenga lakini jitihada za Serikali kuwatia nguvu inakuwa ni kidogo: -

Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kujenga madarasa ya kutosha katika shule hii? (Makofi)

Swali langu la pili, zipo jitihada za wananchi wanazofanya kuhakikisha kwamba wanajenga shule mpya. Kwa mfano katika Kata ya Kenyamanyori kuna Shule zinaitwa Chira, Nyamitembe na shule nyingine ambazo zimejengwa na zimefika katika hatua ya upauaji lakini Serikali haijapeleka fedha kwa ajili ya kumalizia na shule zile zifunguliwe: -

Je, ni lini fedha zitapelekwa ili majengo yale yakamilike na wanafunzi waweze kusoma? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Kembaki.

Swali lake la kwanza kwenye hule hii ya Bugosi yenye wanafunzi zaidi ya 1,000 na madarasa Sita, kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi, kwamba tunapeleka shilingi bilioni 1.5 katika Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa shule hizi kupunguza msongamano. Kwa hiyo Serikali iko tayari kupeleka fedha na tayari imeshatengewa.

Swali lake la pili, kwenye Kata hii ya Kenyamanyori, nitaa na Mheshimiwa Kembaki tuweze kuangalia upungufu ambao upo katika shule hizi alizozitaja za vijiji vya Kata hii, ili tuone ni namna gani tunaweza tukafanya kuweza kukarabati shule hizi ama kuongeza madarasa.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niishukuru Serikali kwa maamuzi hayo mazuri na jibu zuri ambalo wameweza kutujibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati barabara hii inapanuliwa kuna wananchi ambao walikuwa wamejenga pale na walibomoa nyumba zile ili kupisha ujenzi wa barabara ile; je, ni lini watapata fidia yao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; naishukuru Serikali kwa sababu imeleta taa za barabarani katika barabara hii ya Kenya Road. Lakini taa hizi zimewekwa kwa mbali sana kiasi kwamba hazimuliki vizuri.

Ni lini sasa zile sehemu ambazo hazina taa za barabani zikiwemo za Masara, barabara ya Musoma pamoja na Magena watawekewa taa za barabarani? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Michael Mwita Kembaki, Mbunge wa Tarime Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la fidia kwa wale waliobomolewa kupisha ujenzi wa barabara hii ni kweli kwamba wale wote waliobomolewa ni kwa mujibu wa sheria ya mwaka 1967 na marekebisho yake ya mwaka 2007 Na. 13, kwamba waliokuwa ndani ya hifadhi ya barabara kwa maana ya mita 22.5, hawa ndio walioguswa, lakini waliokuwa nje ya hifadhi ya barabara, mpaka mita 30 hawakuguswa. Kwa hiyo hapa hakutakuwa na fidia kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa suala la taa za barabarani; tumewaelekeza managers wote wa TANROADS nchi nzima kwamba lazima watenge fedha kwa ajili ya kuweka bajeti za taa barabarani na kwa maana hiyo kwenye mwaka wa fedha ujao katika eneo hili la Tarime Mjini, tumetenga shilingi milioni 270 kwa ajili ya kusimika taa za barabani na mitaa yake yote. Na hata hivyo, kuna taa nyingine ambazo zimeshasimikwa lakini tutaongeza zaidi ili huu mji uweze kupendeza zaidi, ahsante.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba kuuliza swali la nyongeza. Ni lini Serikali itapeleka fedha kwenye miradi ya Itununu, Tabweta ili iweze kukamilika na wananchi wa Tarime wapate maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Michael Mwita, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, miradi hii aliyoitaja ipo katika mpango wa kulipa fedha katika miezi hii ya Julai na Agosti. Fedha zimechelewa kufika, lakini kuanzia wiki hii wakandarasi wapo kwenye utaratibu wa kuweza kulipwa kwa lengo la kuendelea na utekelezaji wa miradi hii.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Nishukuru Serikali kwa majibu mazuri lakini napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, ni lini Serikali itapeleka fedha kukamilisha ujenzi wa mabweni katika Shule ya Sekondari ya Mogabiri? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, katika Shule ya Sekondari Tarime mabweni yana uwezo wa ku-accommodate watoto 750 lakini wanafunzi waliopo katika shule ile ni zaidi ya 1,500. Je, ni lini Serikali itajenga mabweni zaidi ili kutoa huduma ya mabweni mazuri katika Shule ya Sekondari Tarime?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kembaki. La kwanza kuhusu mabweni katika Shule ya Sekondari Mogabiri kwamba ni lini Serikali itapeleka fedha kumalizia ujenzi wa mabweni.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba Serikali Kuu ilipeleka shilingi milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni na madarasa mawili katika shule hii. Walibadilisha eneo ambalo lilikuwa limewekwa mwanzo kwa ajili ya ujenzi wa mabweni haya hivyo kupelekea gharama za ujenzi kuongezeka.

Mheshimiwa Spika, tathmini imeshafanyika na Halmashauri ya Tarime Mji na imefahamika kwamba inahitajika shilingi milioni 120 kwa ajili ya ukamilishaji wa mabweni haya. Serikali iko katika mchakato wa kutafuta fedha hizi kupitia mapato ya ndani ya halmashauri yenyewe na Serikali Kuu ili kuweza kumalizia ujenzi wa mabweni haya. Mkurugenzi wa Halmashauri hii tayari ameshaleta maombi hayo Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili la Shule ya Sekondari ya Tarime kuwa na wanafunzi wengi, ni kweli kwamba shule hii ina wanafunzi wengi. Kwa kulitambua hilo, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI katika kupanga wanafunzi wa kidato cha tano mwaka huu shule hii ilipelekewa wanafunzi wachache kulingana na miundombinu ambayo ipo. Tunaendelea kutafuta fedha ili kuona ni namna gani ambavyo tunaweza tukapeleka kwa ajili ya kuongeza mabweni katika shule hii ya Tarime Sekondari.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, katika Mgodi wa Kebaga wachimbaji wadogo ambao wanachimba pale wanapata wakati mgumu wa kuuza dhahabu kwa sababu wataalam wanaokwenda kufanya tozo zile za dhahabu wanachelewa kwenda pale, hawana siku maalum ya kwenda kufanya tathmini.

Je, lini Serikali itaweka utaratibu mzuri wa siku zile za kwenda kuhakiki ili kutoa nafasi kwa wachimbaji wale kuuza madini yao? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, upo ushuru unaokusanywa pale na hakuna risiti za EFD ambazo zinatolewa, wanapewa risiti za kawaida; je, huu ni utaratibu ambao unakubalika na sheria?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza kuhusu kuchelewa kununuliwa kwa madini ya wachimbaji wadogo, ninapenda kurejea majibu yangu ya msingi kwamba kwa kufahamu umuhimu wa shughuli za uchimbaji wa madini pale, tumeanzisha kituo kidogo cha ununuzi wa madini na mchimbaji yeyote ambaye ameshachimba madini yake akifika pale tathmini hufanyika na biashara hufanyika.

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la pili kwamba kunakuwa na ucheleweshaji katika kuwahudumia hawa wachimbaji wadogo na wanatoa risiti ambazo ni za karatasi, kama changamoto hiyo ipo, nitamwomba Mheshimiwa Mbunge baada ya kipindi hiki tukutane na tuwasiliane na RMO kule tujue changamoto hiyo hutokana na nini ili tuweze kuishughulikia kikamilifu.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nina maswali mawili ya nyongeza. Lakini Shirika letu la Umeme TANESCO Ta rime linafanya kazi nzuri ya kusambaza umeme ingawa wanafanya kwa mazingira magumu hawana gari. Ningeomba Serikali wawapatie gari ili warahisishe usambazaji wa umeme katika Mji wetu wa Tarime.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kumekuwepo na utamaduni wa kurundika nguzo katika mitaa na nguzo hizo zinakaa muda mrefu kwa mfano katika Mtaa wa Ugete kuna nguzo zimekaa pale miaka miwili sasa na mpaka sasa hazijasambazwa. Je, ni lini nguzo hizi zitasambazwa ili wananchi waweze kupata umeme? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kumekuwepo na utamaduni wa kupeleka umeme katika kaya moja katika mtaa. Kwa hivyo kaya nyingi katika mitaa hiyo inayofata haina umeme. Ni lini Serikali itasambaza umeme katika kaya hizi ambazo hazijapata umeme katika mitaa hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Michael Kembaki Mbunge wa Tarime Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikubali kwamba, miundombinu na vitendea kazi tulivyokuwa navyo havitoshi lakini Serikali inaendelea kujihimu na katika bajeti inayokuja tunataraji kupata magari na vitendea kazi vingine na kuvisambaza katika maeneo yenye uhitaji kwa ajili ya kuweza kuwezesha utendaji wa kazi nzuri. Naamini na Tarime Mjini pia itanufaika na matengenezo na mafanikio hayo ambayo tutakuwa tumeyapata.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye maswali mawili ya nyongeza nimwakikishie Mheshimiwa Kembaki kwamba katika bajeti inayokuja tumetengewa fedha za kutosha na Mheshimiwa Rais ametuhakikishia kuzipata kwa ajili ya kukamilisha hiyo miradi ambayo imekuwa ni viporo kama inaonekana nguzo zimelala miradi haijakamilika lakini na kuongeza wigo wa kupeleka umeme katika maeneo yetu kuanzia kwenye maeneo ya vijiji pia kwenye maeneo ya mitaa. Kwa hiyo, tutakuwa na nafasi nzuri ya kupanua wigo wa kupeleka umeme kwenye maeneo mbalimbali kuanzia mwaka ujao wa fedha kwa sababu tunatarajia kupata fedha nyingi zaidi.
MHE. MICHAEL M. KEMBAKI: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika korongo lile zipo nyumba ambazo ziko jirani sana, wananchi na wakazi wa Mtaa ule wangependa kujua wale wananchi waliopo karibu na korongo zile kaya, je, Serikali ina mpango gani, watawafidia au itakuwa namna gani?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; korongo hili ni hatarishi sana; je, ni lini hasa Serikali itaanza ujenzi wa korongo hili? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kembaki; la kwanza hili la nyumba zilizopo jirani na korongo hili. Kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi kwamba Serikali itatenga fedha katika mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja hili kwenye korongo.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba nichukue nafasi hii mbele ya Bunge lako Tukufu kumwelekeza Meneja wa TARURA, Mkoa wa Mara kwa kushirikiana na Meneja wa TARURA, Wilaya ya Tarime kwenda kufanya tathmini katika eneo hili na kuona hizi nyumba ambazo Mheshimiwa Kembaki amezitaja zipo umbali gani kutoka kwenye road reserve ambayo imewekwa na kisha kuwasilisha taarifa hii TARURA Makao Makuu.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili, nirejee tena majibu yangu ya msingi kwamba Serikali itatenga fedha mwaka wa fedha 2024/2025 na fedha hii itakapotengwa ndipo kazi hii itatangazwa na kuanza kujengwa daraja hili katika Bonde hili la Mto Starehe.