Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Maryam Azan Mwinyi (4 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsnate sana kwa kunipa nafasi hii ambayo ni ya upendeleo, hasa kutoka Pemba. Kwa kuchangia hotuba ya Ofisi ya Makamu wa Rais ya Muungano, mimi hasa najikita katika mazingira.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano imetoa mwongozo kufanya vikao katika taasisi mbili kutoka Zanzibar na kutoka Tanzania Bara ili vikao hivi viweze kuleta tija kwa Watanzania wote. Sasa tatizo ni hili ambalo vikao vinachelewa sana kufanywa katika Serikali zetu hizi mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vikao hivi vitasaidia kujadili pamoja mambo mengi na fursa nyingi za Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, hasa kwenye miradi ya mazingira. Pia kuwe na ushirikiano wa kupatiwa taarifa ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar, vipi inanufaika katika mikataba ya mazingira inayoridhia ili taarifa hizo ziweze kuwasaidia wananchi wa Tanzania yote; Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara.

Mheshimiwa Spika, wananchi hao waweze kufahamu fursa ambazo Serikali zetu zinaimarisha Muungano kwenye sekta ya mazingira. Kwa hiyo, tunamwomba Mheshimiwa Waziri katika Wizara hii alichukulie kuwa ni muhimu sana katika sekta hiyo ya kufanya vikao na kutoa taarifa katika nchi yetu kwa Tanzania Bara na Tanzania Visiwani ili Muungano huu uzidi kudumu na kuimarishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, naomba kuchangia bajeti ya Wizara ya Maji na ninaomba nianze kwa kumpogeza Mheshimiwa Rais kwa jitihada zake za kumtua mama ndoo kichwani kwa kuipatia shilingi 709,361,607,000 kwa maendeleo ya miradi ya maji katika Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya jitihada kubwa za kuchimba visima maeneo oevu ili kuboresha hali ya upatikanaji wa maji. Ninaiomba Serikali iongeze fedha kupitia bajeti hii ili visima vingi vichimbwe nchini ili kuzidi kutatua changamoto ya maji katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nchi yetu ina miradi mingi ya maji ambayo haijakamilika, niombe Serikali ikamilishe miradi yote ambayo imeshaanza ili kuweza kuwatua akimama ndoo kichwani katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, niendelee kuishukuru Serikali kwa jitihada zake za kuhakikisha tatizo la maji linamalizika hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Spika, ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa hai na salama. Ninapenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anazozifanya katika Taifa letu hili, kwa kuzidi kuiongeza bajeti ya Wizara ya hii ya Kilimo kwa mwaka wa 2023/2024. Haya yote ni kwamba Mheshimiwa Rais anawapenda wananchi wake wa Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, pia ninapenda kumpogeza Waziri na Naibu wake, uongozi wote wa Wizara hii. Hakika maneno ya wazee wetu kwamba pumu imepata mkohozi Wizara hii imepata mtendaji hodari sana.

Mheshimiwa Spika, tunaomba Wizara ya Fedha itoe pesa kwa Wizara hii ili mipango yote mizuri iliyoletwa iweze kutekelezwa kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, tunaomba Wizara kuimarisha masoko na huduma za masoko kwa wakulima na kuwasogezea masoko, sambamba na kuimarisha miundombinu ya kuyafikia masoko.

Mheshimiwa Spika, kuimarisha usafirishaji kutoka mashambani na kwenda katika maeneo ya masoko hasa barabara za vijijini zifanyiwe matengenezo ili ziweze kupitika kipindi chote.

Mheshimiwa Spika, ninaomba Wizara iwajengee uwezo zaidi Maafisa Ugani ili kufanya shughuli zao na kumudu majukumu yao.

Mheshimiwa Spika, Serikali iendelee kuongeza mashamba darasa ili kuwawezesha wakulima kuendelea kujifunza kupitia mashamba hayo.

Mheshimiwa Spika, pia wakulima wapatiwe ujuzi na maarifa baada ya mavuno ili waweze kutunza na kuhifadhi mazao yao wakati wakisubiri kupata soko la mazao hayo.

Mheshimiwa Spika, Serikali kuimarisha wigo wa kuongeza thamani ya mazao ili kuongeza tija kwa wakulima kwa kupata masoko ya ndani na nje.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwa wananchi wengi wanazalisha mazao ya chakula, tunaomba Serikali izidi kuhamasisha wananchi wetu waweze kuzalisha mazao ya biashara ili waweze kupata kipato cha kujikimu katika maisha yao.

Mheshimiwa Spika, Serikali kuhakikisha inatafuta masoko ya kutosha kwa mazao ya wakulima ili kuepusha kupata hasara, mfano alizeti, ufuta, mbaazi na mbogamboga.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. MARYAM AZAN MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuchangia bajeti ya Wizara ya Mifungo na Uvuvi ya mwaka 2022/2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumshukuru Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi zake nzuri anazozifanya katika Taifa letu. Aidha, napenda kuwapongeza Waziri, Naibu Waziri na Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Wizara hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania tuna wavuvi wengi wadogo wadogo lakini bado hali za maisha sio nzuri na kwa vile wameshavua muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu, ni lazima tuanzishe viwanda vya Samaki ili kuweza kuwatengezea mazingira bora wavuvi wetu na wale wadogo wadogo ambao watavua bahari kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Serikali iweke cold room (majokofu) ya kuhifadhia samaki kwa vile tunajikita katika uvuvi wa bahari kuu. Tukiwa na sehemu hizi tunavutia meli nyingi kuja kuvua nchini kwetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali iweke mikakati endelevu ya muda mfupi wa kuimarisha na kuwasaidia wavuvi ili kuwa na uwezo kamili na kuvua kwenye bahari kuu, kwa kufanya hivi kutasaidia ajira katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inapaswa kutoa mafunzo kwa wavuvi wetu wadogo ili kuimarisha uvuvi wa bahari kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunaiomba Serikali kuimarisha upatikanaji wa masoko ya kimataifa ya kuuza samaki. Jambo hili ni muhimu na litasaidia kuitangaza zaidi nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.