Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dennis Lazaro Londo (50 total)

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya swali la nyongeza. Kwa kuwa, Serikali imejikita katika umaliziaji wa reli ya mwendokasi kwa jina lingine SGR kutoka Dar-es-Salaam awamu ya kwanza mpaka Morogoro na kutoka Morogoro mpaka Makutupora awamu ya pili; na kwa kuwa, TAZARA ni reli ya kimkakati na TAZARA inaanzia Mlimba inachepuka mpaka Kidatu. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuendelea na hiyo reli mpaka Kilosa kuungana na hii reli ya mwendokasi, ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka reli ya kati na reli ya SGR kutoka Kilosa kuja Kidatu? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Denis Londo, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba, kuna umuhimu mkubwa sana wa kuunganisha reli ya SGR na reli ya TAZARA kuanzia Kilosa hadi Mikumi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Denis Londo kwamba, Serikali ina mpango huo wa kuziunganisha hizo reli, lakini upembuzi yakinifu utafanyika pale tu ambapo Serikali itakuwa imepata fedha, lakini tunaona kabisa ni muhimu kuziunganisha hizi reli kwa ajili ya ustawi wa uchumi wa nchi, lakini pia kuziunganisha hizi reli eneo la Kilosa na Mikumi. Ahsante.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa msamaha ulitolewa kwa wale wote ambao waliondolewa kazini kwa kukosa sifa ya kidato cha nne na baadaye wakajiendeleza kupata sifa hizo; na kuna maeneo ambayo watu hawana mawasiliano ya simu kama Ulingombe, Vidunda, Malolo na Kisanga.

Je, Serikali inatoa tamko gani kwa waajiri kuhakikisha kwamba watu wote ambao wame-qualify kurudishwa na hawana taarifa wanapata taarifa hizi kwa wakati na wanarudishwa kazini bila masharti ya ziada?

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa watumishi hawa ambao walishindwa kujiendeleza kidato cha nne lakini walikuwa na sifa stahiki wakati wanaajiriwa waliondolewa kazini walitumikia hii nchi kwa uadilifu na uzalendo lakini hawakuwa na kosa mahali zaidi ya maelekezo ya Serikali.

Je, ni lini Serikali inaenda kuhakikisha kwamba malipo yao na stahiki zao zinalipwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, msamaha uliotolewa kwa watumishi hawa ambao waliajiriwa baada ya tarehe 20 Mei, 2004 ambapo tangazo la Serikali lilitoka mpaka ifikapo Mei, 2004 watumishi wote wanaoajiriwa Serikalini ni lazima wawe na sifa ya kidato cha nne. Hata hivyo kuna waajiri ambao waliajiri watumishi baada ya tangazo lile la Serikali. Tunatambua kwamba haikuwa kosa la wale watumishi walioajiriwa.

Mheshimiwa Spika, sasa Serikali ilitoa maelekezo kupitia Katibu Mkuu Kiongozi kwamba hawa watumishi wote walioajiriwa baada ya tarehe hiyo wawe wamejiendeleza na kupata sifa ya kuajiriwa Serikalini, yaani cheti cha kidato cha nne mpaka ifikapo Desemba, 2020. Na waliorejeshwa kazini mpaka kufikia Desemba 2020 ni zaidi ya watumishi 4,335 ambao walirudi kwa sababu walikuwa wamejiendeleza.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa wale ambao kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema, kwamba hawakupata taarifa popote ya kwamba wajiendeleza na walijiendeleza kabla ya ile deadline iliyowekwa basi niwaelekeze waajiri wote nchini kuweza kuliangalia hili kuwachukua watumishi hawa kama walijiendeleza tu kabla ya kufikia Desemba, 2020 lakini hawakupata tangazo la kurejea kazini basi waajiri waweze kuliangalia hilo.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la pili aliulizia wale ambao hawakujiendeleza lakini waliajiriwa baada ya Mei 2004. Hawa siku ya Mei Mosi Mheshimiwa Rais wetu mama yetu Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo, kwamba watumishi wote waliokuwa na sifa ya elimu ya darasa la saba walipwe stahiki zao kwa sababu hawa hawakughushi wao waliajiriwa siyo makosa yao basi stahiki zao kama hawakurejeshwa kazini na kama hawakujiendeleza walipwe. Tayari ofisi yetu ilishatoa waraka kupitia Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi kwa waajiri wote nchini kuanza kushughulikia hawa wenye elimu ya darasa la saba ambao hawakurejeshwa kazini, na tayari linafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwa kuwa Serikali inakiri kwamba, uwezo wetu wa kuzalisha sukari ndani hautoshelezi mahitaji ya ndani na tunaagiza kiasi cha takribani tani tani zaidi ya laki moja za sukari kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, na kwa kuwa, miwa ya wakulima katika Jimbo la Mikumi ni zaidi ya tani laki nne zinateketea mashambani. Na kwa kuwa, kiwanda cha Ilovo wakati wanauziwa walikuwa na masharti ya kuongeza upanuzi wa kiwanda hicho na Serikali inasuasua. Je, ni lini Serikali inaenda kuhakikisha kwamba, upanuzi wa kiwanda hicho unakamilika na mazao ya wakulima ya miwa yanaenda kupata soko la uhakika?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kama nilivyosema mahitaji ya sukari hapa nchini ni makubwa ukilinganisha na uwezo wetu wa uzalishaji wa ndani. Suala la wananchi kukosa soko katika Wilaya ya Kilombero ni moja ya maeneo muhimu sana ambayo sisi kama Wizara ya Viwanda na Biashara tumeshayaona. Na moja ya mikakati ya Wizara ya Viwanda ni kuona namna gani sasa tunaongeza uchakataji wa miwa ambayo inakosa soko katika viwanda vilivyopo.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo (TEMDO), tunaenda kuleta mitambo midogo ambayo itaweza kusaidia kuchakata miwa kwa wakulima wadogowadogo ambao wanakosa soko katika viwanda vikubwa kwa sasa, ikiwemo maeneo ya Kilombero.

Mheshimiwa Spika, kuhisiana na viwanda vilivyopo tayari kuna mipango maalum, kwanza kuhamasisha kuongeza uwekezaji kwa kuongeza uzalishaji katika viwanda hivyo, lakini pia kuhakikisha na wao wanaingia sasa, kuna kitu tunaita quail farming, ili waweze kusaidiana na wakulima wadogowadogo kuzalisha miwa mingi, lakini pia na wao wenye viwanda kuwa na mashamba mengine ambayo yatatosheleza mahitaji ya uzalishaji katika viwanda vilivyopo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwanza tutahakikisha miwa ambayo inakosa soko tunaleta hiyo mitambo midogo ambayo itachakata miwa hiyo, ili angalao wakulima wale waweze kupata soko la uhakika.

Mheshimiwa Spika, la pili. Tunaendelea kushirikiana na viwanda vilivyopo ili kuhakikisha wanahamasisha wakulima wadogowadogo kwa maana ya kuingia quail farming katika viwanda vyao.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona kwa ajili ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kivuko hiki cha Mto Malagarasi ni muhimu kama ilivyo barabara ya kutoka Kilosa – Magomeni – Masanze -Zombo – Ulaya - Muhenda – Mikumi. Pia barabara hii ilikuwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi mwaka 2015-2020 na ipo kwenye Ilani 2020-2025 na ipo kwenye bajeti…

NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa.

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, je ni lini ujenzi wa barabara hii unaenda kuanza? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dennis Londo, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyoitaja imeainishwa kwenye Ilani lakini pia ipo kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Dennis Londo kwamba kuanzia bajeti hii tutakayoianza barabara hii itaanza kufanyiwa kazi kwenye mipango yetu kwani viongozi wengi wameahidi barabara hiyo ijengwe. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi yeye na wananchi wa Mikumi kwamba barabara hii ipo kwenye mpango na itatekelezwa katika kipindi hiki cha miaka mitano.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya swali la nyongeza. Kwa kuwa kuna kero kubwa ya maji katika Kata za Ruaha, Mikumi, Ulaya, Tindiga na Malolo; na Serikali inatambua hilo:-

Je, ni lini Serikali itakwenda kutatua shida ya maji katika Kata hizo? Nashukuru. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge, lakini sisi kama Wizara ya maji kwa dhati kabisa tunataka kumaliza tatizo la maji Mikumi pamoja na Morogoro. Hakuna sababu hata moja ya wananchi wa Morogoro na Mikumi kulalamikia suala la maji ilhali wana vyanzo vya maji vya kutosha. Kwa hiyo, sisi kama Wizara ya Maji tumejipanga sasa kujenga miundombinu ili wananchi wako wa Mikumi waweze kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upendeleo mkubwa baada ya bajeti nitafika katika Jimbo la Mikumi ili kuhakikisha kwamba tunakwenda kufanya kitu pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, dhumuni la eneo kinga (buffer zone) siyo kuzuia wanyama kuingia vijijini. Ni kwa jinsi gani Serikali imejipanga kuangalia usalama wa wananchi kwa sababu tembo hawa wanaingia katikati ya vijiji kule Kilangali, Tindiga, Malolo hata Yogo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ikumbukwe tarehe 15 Januari 2019 Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo kwa Wizara saba kukaa chini na kupitia upya mipaka na kuangalia usalama wa watu katika vijiji vinavyopakana na hifadhi. Hata hivyo, mpaka sasa hatujasikia ni vijiji gani vimeshughulikiwa zaidi ya kuona wananchi wakinyanyasika na pia hakuna alama za kudumu ambazo zimewekwa kwenye eneo la kinga (buffer zone) katika vijiji vinavyopakana na mpaka.

Ni lini Serikali inaenda kuweka alama lakini pia inaenda kuanzisha game ranger post pamoja na kuanzisha vikundi vya kuzuia wanyama waharibifu katika vijiji vyetu? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dennis Londo, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpe pongezi Mheshimiwa Mbunge Dennis Londo kwa kuendelea kutoa rai kwa Serikali jinsi ambavyo wanyamapori hasa waharibifu na wakali wanavyoendelea kuathiri wananchi. Hata hivyo, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi ni kwamba sasa Serikali imejipanga kuandaa mkakati ambao utawawezesha hawa wananchi kutambua ni namna gani ya kukabiliana na wanyamapori hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri tumeshaanza kutoa mafunzo katika Mikoa ya Simiyu, tumeshafanya katika Wilaya ya Busega, Wilaya ya Bariadi na maeneo mengine ambayo yanazunguka mkoa huo, lakini pia awamu inayofuata tutaenda katika Mkoa wa Ruvuma, Morogoro na maeneo mengine hapa nchini. Lengo kuu ni kuhakikisha hawa wanyamapori ambao wamekuwa changamoto kwa Tanzania na kwa nchi kwa ujumla wanadhibitiwa kwa kushirikiana na wananchi ambao wanazunguka maeneo ya hifadhi.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri ambayo yanaonyesha jitihada ya wazi ya Serikali kutatua kero ya miwa kwa kulima miwa katika Bonde la Kilombero. Lakini pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri huduma zinaendelea. Kwa mfano, hivi tunavyozungumza, Vyama vya Ushirika vya RCG AMCOS ambavyo vilikuwa na DRD7 mwaka jana, wamepunguziwa kwenda 3. Chama cha Kitete AMCOS ambacho kilikuwa na DRD5 mwaka jana, mwaka huu imepewa 3. Chama cha KIDODI AMCOS ambacho kilikuwa na DRD4 mwaka huu kimepewa 2. Chama cha Mbwade, Msindazi na MIWA AMCOS vyote vimepunguziwa DRD, ambayo inapelekea kupunguza kiasi cha miwa ambacho kinapeleka Kiwandani.

Mheshimiwa Spika, mwaka jana, tulilaza miwa tani 400,000. Mwaka huu wametupunguzia uwezo maana yake nini, maana yake wanajiandaa kuhujumu wakulima wa miwa kwa zaidi ya tani 400,000 ambazo tumelaza mwaka jana. Je, nini tamko la Serikali kwa vitendo hivi ambavyo vinafanywa na Kiwanda hiki? Lakini nini tamko la Serikali kwa makaburu hawa weusi ambao ni watanzania wenzetu wanaowasaidia wawekezaji kuumiza wakulima wetu? Naomba tamko la Serikali. (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, kwanza, Serikali inataka wawekezaji wote nchini, kufanya uwekezaji na shughuli zao zote kwa kuzingatia sheria. Na kama kuna hujuma kama alivyoeleza Mheshimiwa Mbunge, ni kinyume cha sheria na tutafuatilia.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili, suluhu ya kudumu ya miwa ya wakulima wa Kilombero ni upanuzi wa Kiwanda hiki ambao nimeeleza. Kwa sababu, tukishapanua wakulima watauza zaidi miwa yao kwa sababu, kiwanda kitakuwa na uwezo wa kuchukua zaidi ya mara tatu ya miwa ambayo wanachukua sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, lakini la mwisho, kama nilivyoeleza wakati wa bajeti yangu, mwaka huu wenzetu wa SIDO tumewaelekeza na wameshakubali kufanyia kazi. Tutakuwa na mitambo midogo ya kuchakata miwa ya wakulima katika ngazi ya chini.

Kwa hiyo, kutakuwa na wajasiriamali ambao wanaweza wakauza miwa kwa wajasiriamali wadogo wa kuchakata miwa hiyo. Kwa sasa hivi tuna viwanda vikubwa peke yake, sasa tumeona kwamba kuna haja ya kuwa na wajasiamali wadogo wadogo, watasaidia sana kuchukua miwa hii ya wakulima wetu.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara hii swali lilkuwa ni lini ujenzi utaanza. Lakini barabara hii haina tofauti na barabara nyingine ya kutoka Kilosa kuja Mikumi ambayo ipo kwenye Ilani ya mwaka 2015/2020, 2020/2025 na ipo kwenye bajeti hii ya mwaka huu na bado tunaambiwa kwama ipo kwenye maandalizi. Sasa Je, ni lini ujenzi wa barabara hii unaenda kuanza? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nniaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Londo, Mbunge wa Mikumi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti ni kweli barabara ile aliyotaja ya Kilosa Mikumi ipo kwenye Ilani na imetengewa fedha kwa bajeti inayokuja. Kwa hiyo, tunaamini kwamba tutakapoanza utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2021/2022 basi hii barabara itakuwa moja ya barabara ambazo zitaendelea kujengwa kwani tayari barabara hii upande inapoanzia eneo la hapa njia panda barabara ya Morogoro – Dodoma; tayari imeshajengwa mpaka Kilosa na tunaendelea na ujenzi. Kwa hiyo kipande kilichobaki cha Kilosa kwenda Mikumi barabara hii naamini nayo itaanza kujengwa katika bajeti tunayoanza kuitekeleza. Ahsante.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniruhusu kuuliza swali moja la nyongeza.

Kwa kuwa kiwanda hiki kipo katika eneo la kimkakati kwa sababu kimezungukwa na mashamba ya miwa ama eneo ambalo linalima miwa kwa wingi, na kwa kuwa kulikuwa na mpango wa ku-transform kiwanda hiki kwenda kuzalisha sukari.

Je, Serikali inatoa tamko gani ikizingatiwa kwamba sasa hivi kuna mpango wa kuboresha viwanda vidogo vidogo vya kuzalisha sukari?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Dennis Londo, Mbunge wa Jimbo la Mikumi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ukanda huu wa Kilombero ni ukanda ambao tunaweza tukasema ni wa kimkakati kwa uzalishaji wa miwa na sukari kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya hapa nchini. Ni kweli ni moja ya azma ya Serikali kuhamasisha au kuvutia wawekezaji wengi katika kuchakata miwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu la msingi tunatafuta wawekezaji mahiri ambao watajitokeza kuwekeza katika eneo hili ikiwemo wale ambao watataka kuchakata miwa basi na sisi tutawakaribisha ili kutumia nafasi hiyo katika eneo hili la Machine Tools kama sehemu ya kuwekeza viwanda vya kuchakata miwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tupo tayari na tusaidiane na Wabunge ili tuweze kuwekeza katika maeneo haya kwa umahiri zaidi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa hii nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba kuna uchache ama upungufu mkubwa wa hizi mashine za incubator; na anasema kwamba hakuna utafiti wa kisayansi ambao unaonesha kwamba zinaweza kusaidia maisha ya Watoto; je, yuko tayari kuleta utafiti wa kisayansi kuelezea mahusiano ya vifo vya watoto njiti kwa kukosa huduma hasa kwa kutokuwepo kwa hizi incubators?

Mheshimiwa Spika, swali la pili: Kama wametambua kwamba Kangaroo Mother Care imekuwa ni njia mujarabu katika kuokoa maisha ya watoto, ni juhudi gani za Serikali zimechukuliwa kuhakikisha elimu hii inafika vijijini ili kuokoa maisha ya watoto? (Makofi)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ahsante sana Mheshimiwa Londo kwa maswali yako mawili mazuri kabisa. Napenda kujibu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, scientific data au scientific evidence kuhusu eneo hili zipo na sayansi huwa inaendelea kufuatilia mambo mbalimbali kadri muda unavyokwenda na ku-adapt marekebisho ili kuboresha. Hivyo, kwa ridhaa yako, kama tutapata fursa tunaweza tukawasilisha kupitia Kamati ya Huduma za Jamii baadaye ikafika Bungeni, hizi tafiti mbalimbali zilizofikia, tukafanya adjustment siyo tu Tanzania, dunia nzima, kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa elimu kufika vijijini, tayari tulishatoa mwongozo wa maboresho eneo hili, upo; na kupitia Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya tutahakikisha tunasogeza elimu hii kwenye jamii ili waweze kuona umuhimu wa kukaa na mtoto kifuani kwao, hasa anapokuwa amezaliwa na uzito pungufu sana tuendelee kuokoa maisha. Hii imeonesha kwenye data zetu za mwaka 2018 mpaka 2020 vifo vimeendelea kupungua kutoka 11,524 mpaka 8,190. Ni katika mikakati hii ambayo tumeichukua ya kuhakikisha kwamba tunaokoa maisha ya watoto.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa sanaa imekuwa chanzo kikuu cha ajira kwa vijana wetu, je, Serikali haioni kuwa umefika wakati sasa wa kutumia vyuo vyetu vya VETA kama vituo vya kuibua na kuendeleza vipaji vya sanaa kwa vijana wetu?
WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa majibu ya swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Mbunge wa Mikumi, mchapa kazi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ushauri mzuri aioutoa kuhusu matumizi ya vyuo vya VETA, lakini sisi kama Serikali tunakwenda mbele zaidi. Tunategemea kutumia baadhi ya shule tulizonazo kutengeneza academy mbalimbali. Tutatumia shule aidi ya 56 ambazo Serikali imejipanga kuzitumia kwa ajili ya kuendeleza na kukuza vipaji katika maeneo hayo.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, kwanza nishukuru kwa majibu mazuri ya Serikali ambayo yanatoa tumaini kwa vijana wa Jimbo la mikumi. Swali langu la kwanza; kwa kuwa Serikali itaangalia uwekezaji unaofaa katika bwawa hilo, je, mpango huo unahusisha pia uzalishaji wa vyakula vya samaki katika viwanda vidogo na vya kati katika eneo la Jimbo la Mikumi ili kukuza ufugaji wa samaki?

Mheshimiwa Spika, la pili, karibu na Zombo kuna reli ya mwendokasi ambako kuna mashimo makubwa ambayo walikuwa wanachimba kokoto wakati wa ujenzi huo. Mashimo haya makubwa yana potential ya kubadilishwa kuwa mabwawa kwa ajili ya ufugaji wa samaki lakini pia kwa ajili ya mifugo. Je, Serikali itakubaliana nami kwamba wakati umefika wa kuyatengeneza mabwawa haya ili kutatua tatizo letu? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Denis Lazaro Londo, Mbunge wa Jimbo la Mikumi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, umuhimu na uhitaji wa vyakula vya mifugo nchini hususan samaki ni mkubwa sana na kwa kadri tunavyoendelea kuhamasisha ufugaji wa samaki umuhimu umezidi kuongezeka.

Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Londo, kwamba tunahitaji uwekezaji zaidi. Katika Mkakati tulio nao ndani ya Serikali ni kuvutia uwekezaji wa uzalishaji wa chakula cha samaki.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mabwawa ama mashimo yaliyotokana na ujenzi wa reli ya SGR, nakubaliana naye na ni wazo jema sana.

Mheshimiwa Spika, sisi katika Wizara tumeanza mazungumzo na wenzetu wa reli ili kuhakikisha kwamba mabwaya yale tunayaongezea thamani kwa kuyatengenezea miundombinu ili yaweze kutumika kwa ajili ya shughuli za ufugaji pamoja na shughuli za ufugaji wa samaki. Ahsante sana.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kama kuna mkoa ambao ulikuwa unasubiri kwa hamu ile Timu ya Mawaziri Nane ni mkoa wa Morogoro. Jimbo la Mikumi, Kata za Zombo, Muhenda, Kisanga na Mikumi zimekuwa katika changamoto ya muda mrefu ya mipaka kati yao na TFS, kati yao na TANAPA.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba kuna timu ambayo imeundwa na Waziri kuorodhesha migogoro hiyo. Je, kata hizo na vijiji hivyo vya kata hizo zinaenda kuingia katika orodha ndefu ya vijiji vyenye migogoro? Nawakilisha.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Londo, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili naomba nilifafanue kwa ufasaha zaidi kuna ile migogoro ambayo inapitiwa na Mawaziri Nane. Hii migogoro Mawaziri Nane watapita kwenye maeneo nchi nzima na watatatua hii migogoro. Hata hivyo, kuna migogoro mipya ambayo haikuwahi kupitiwa na Kamati ya Mawaziri Nane. Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii ameunda Kamati ndani ya Wizara imehusisha na maeneo mengine kwa maana ya watumishi wa ardhi na maeneo ya mazingira kupitia mapori ya hifadhi, kupitia ramani moja baada ya nyingine kuangalia huu mgogoro unatoka wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna migogoro mingine ni ya beacon, kuna migogoro mingine wamesogea kidogo, kwa hiyo kuna mabishano kati ya mipaka na mipaka. Kamati hii itapita tena upya na itaangalia pale ambapo pana mgogoro tutautatua kwa pamoja na tutazisoma ramani tuta- define mipaka na baadaye tutatoa majibu sahihi ili wananchi waridhike na maeneo ya hifadhi, lakini wakati huo huo watendewe haki kuliko ilivyo sasa. Ahsante.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kuna upungufu mkubwa sana wa kada ya uuguzi na madaktari katika vituo vyetu vya afya na zahanati zetu, na kwa kuwa tunaona kuna wimbi kubwa la wastaafu wa kada hizo wanaopewa barua za kustaafu kila siku.

Je, Serikali haioni umefika wakati sasa wa TAMISEMI kukaa na Wizara ya Utumishi ama kuwaongezea mkataba watumishi hawa ama kutoa fursa ya kutoa ajira ku-replace hawa watu ambao wanaondoka kwenye ajira kwa sababu bado wanakuwa kwenye bajeti?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dennis Londo, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na upungufu wa watumishi kwenye vituo vyetu, lakini jitihada za wazi za Serikali zimeendelea kuonekana, kwanza kwa kuajiri watumishi katika vituo hivyo. Kwa mwaka uliopita Serikali iliajiri zaidi ya watumishi 2,726 wa kada za afya na kuwasambaza nchini kote.

Mheshimiwa Spika, lakini upungufu huu wa watumishi pia unatokana na kasi kubwa ya Serikali ya kujenga zahanati, vituo vya afya na hospitali. Kwa sababu idadi sasa ya vituo hivyo imekuwa kubwa na automatically upungufu wa watumishi unaonekana. Kwa hiyo ni hatua nzuri sana kwanza ya kusogeza huduma kwa wananchi, lakini hatua ya pili ni kupeleka watumishi hao.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kuwaongezea mkataba waliostaafu; tunafikiri ni busara kwa sababu kuna vijana wengi wamehitimu masomo ya utabibu, ya uuguzi, ni vyema wakaajiriwa badala ya kuongeza mikataba ya wale ambao wamefika umri wa kustaafu kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, tutaendelea kuhakikisha kwamba fursa za ajira zikitokea vijana wanajiriwa kwenda kupunguza mapengo ya watumishi katika kada za afya. Ahsante.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ardhi ambayo inafaa kwa umwagiliaji ambayo inatumika sasa hivi kwa miradi ya umwagiliaji ni pungufu ya asilimia Tano. Je, nini mkakati wa Serikali kushirikisha sekta binafsi katika kuhakikisha maeneo yote ambayo yanafaa kwa umwagiliaji yanajengewa skimu? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dennis Londo, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, katika Jedwali Na. 6 la Kitabu cha Bajeti cha Wizara ya Kilimo, imeelezwa mahsusi kabisa kwamba Serikali imejipanga kuyafanyia upembuzi yakinifu na usanifu mabonde yote makubwa 22 ndani ya Nchi yetu ya Tanzania kuhakikisha yote yanafanya kilimo cha umwagiliaji, yakiwemo mabonde ya Mto Songwe, Ifakara, Idete, Pangani, Rufiji, Chamanzi na Malagarasi pamoja na Ziwa Victoria.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kuniruhusu kuuliza swali la nyongeza.

Kwanza nikiri kwamba Serikali imefanya kazi kubwa sana Wilayani Kilosa na nimpongeze DC wa Wilaya Kilosa Alhaji Majid Ahmed Mwanga kwa kazi kubwa ya kupunguza na kuondoa kabisa katika baadhi ya maeneo migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na hayo kwa namba hizi ambazo naziona na ripoti nyingi za matatizo ya wakulima kulishiwa mazao yao katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Je, nini mkakati wa Serikali wa kumaliza matatizo haya?

Pili, Serikali haioni wakati umefika sasa wa kulichukulia jambo hili kama janga la kitaifa Wizara ya Mambo ya Ndani ikae na Ofisi ya Waziri Mkuu kuona namna bora ya kulichukulia suala hili kama janga? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Mikumi maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi na vyombo vingine vikiwemo vya Mahakama kwa kweli tumechukua hatua nyingi na tofauti, moja tumegundua kwamba bado kuna watu uelewa wao ni mdogo katika hili. Kwa hiyo cha kwanza ni kuendelea kuwapa taaluma wananchi juu ya suala hili, lakini kingine tunaendelea kutoa maelekezo kwa baadhi ama kwenye vyombo mbalimbali ikiwemo watu wa halmashauri, watu wa miji na majiji ili kuendelea kutusaidia kulilea suala hili ili kuhakikisha kwamba mambo haya yanaondoka kabisa katika jamii.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa upande mwingine nikiri kwamba kweli hili suala ni janga na kwa sababu linarudisha nyuma hali za wananchi zikiwemo hali za kiuchumi na mambo mengine kwa hiyo kutokana na hali hii ndiyo maana sasa tukaona pia bado kuna haja ya kuchukua baadhi ya mikakati na hatua hizi. Kwa hiyo nikiri kwamba hili ni janga na kwa sababu linawaathiri sana wananchi.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, naungana na Wabunge wenzangu, mkandarasi ambaye amepewa Miradi ya REA katika Wilaya za Mvomero, Ulanga, Malinyi, Kilosa mpaka sasa hajawasha umeme katika kijiji hata kimoja. Sasa na hilo nalo wananchi wa Jimbo la Mikumi wanataka kujua nini kauli ya Serikali kwenye hili?

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba baada ya hapa niwasiliane naye ili nijue changamoto hasa kwenye eneo lake ni sehemu gani anasema hakujawasha hata kijiji kimoja. Baada ya hapo tutafuatilia kujua changamoto iko wapi, pengine ni kwa sababu mkandarasi anakuwa na maeneo manne, matano, sita pengine kaanzia kwingine kwake hajafika. Zile hatua za awali za kuhakiki mipaka, kuhakiki maeneo ya kuweka miundombinu na kuhakiki urefu, tayari zimeshafanyika kwenye maeneo yote inafuata kuweka nguzo, kuvuta wires na sasa kuwasha umeme. Kwa hiyo, tukishafuatilia tutajua hatua gani imefikiwa katika eneo lake, lakini kazi hiyo lazima ifanyike na kukamilika.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; ni kweli sheria inataka hivyo, lakini kwa kuwa shughuli za kibinadamu zinaendelea kama uvunaji wa mikaa na kuvuna miti katika misitu hiyo ya TFS, je, Serikali hawezi kuona sasa wakati umfefika wa ku-review sheria hiyo ili kwenda na wakati?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; tunaona hifadhi nyingi ambazo zinachomwa kwa makusudi katika utaratibu wa kuachia muda majani yaote. Je, Serikali haioni kwamba hata utaratibu huo pia umepitwa na wakati, wakati umefika sasa wa kuruhusu watu kuvuna majani ili kutoa suluhisho ya malisho ya ng’ombe ambao sasa hivi wanahangaika hasa katika maeneo ya wafugaji?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Innocent Kalogeris akiwakilishwa na Mheshimiwa Londo, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba nijibu haya maswali mawili kwa pamoja kwamba ni kwa nini tunafanya usafi kwenye maeneo ya hifadhi hususani kuchoma majani na Mheshimiwa Mbunge amesema badala ya kuchoma hayo majani basi yangetumika kwa ajili ya mifugo. Kiutaalam wa kiuhifadhi, wanashauri endapo kuna na mahitaji ndani ya hifadhi, ikiwemo mbolea, lakini pia kuna calcium ambayo wanaitumia wanyama pori, basi huwa kuna maeneo ambayo yameainishwa ambayo yanatengeneza hiyo calcium kwa kuchomwa jivu, ili wanyamapori waweze kupata calcium waendelee ku- survival kwenye maeneo yao ya hifadhi.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo jivu hili huwa linatengeneza mbolea ili iweze kusaidia kuendelea kumea kwenye yale majani ambayo yanatumika kwa ajili ya malisho ya wanyamapori.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umbali wa kutoka Morogoro Mjini mpaka Mikumi ni kilometa 120 na kutoka Mikumi mpaka Iringa ni kilometa 190, kuna ajali nyingi sana ambazo zinatokea katika kipande hiki na wanategemea sana huduma katika Kituo cha Afya na Hospitali hii ya Mtakatifu Kizito pale Mikumi.

(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kupeleka watalaam wa huduma wa utengamao na physiotherapy pale Mikumi? (Makofi)

(b) Je, Serikali haioni wakati umefika sasa kuokoa maisha ya Watanzania wengi kuanzisha centre of excellence ya wataalam wa mifupa kwa ajili ya kujifunza pale Mikumi? Naomba kuwasilisha. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yake mawili moja la kuongeza watalaam. Moja, kwenye eneo la kuongeza watalaam suala tu siyo kuongeza watalaam lakini ni kushirikiana na wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, lakini uchukuzi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunapunguza mambo ambayo yanapelekea ajali zitokee kwenye maeneo hayo, pia kuhamasisha elimu ya magonjwa yasiyoambukiza ili kupunguza idadi ya watu hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na yeye kwamba Mkoa wa Morogoro ukiangalia wanahitajika watalaam 30 na kwa mwaka huu wanaenda kuongezwa watalaam tisa maana yake katika hawa tisa tutaona ni namna gani tunaweza kuhakikisha tunaongeza watalaam kwenye eneo ambalo yeye amelitaja. Lakini kuangalia vizuri zaidi data zilizotumika kuamua wanahitajika Mkoa wa Morogoro hawa 30 kuangalia kama ilitumika data za wakati gani ili kama kunahitajika kuongeza basi tuwaongeze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine la wataalam wa mifupa na vitu vingine tunaenda kufikiria kwenye ajira ambazo amesema Mheshimiwa Waziri wa Utumishi ni 32,000 basi tutaenda kulizingatia eneo hilo wakati tukipata hivyo vibali. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa nia njema Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ilikabidhi Chuo cha VETA pale Mikumi kwa Serikali; na tangu Serikali imekabidhiwa, hakuna ukarabati na Chuo kinaendelea kuchakaa.

Je, ni kanuni au sheria kutowekeza fedha za ukarabati katika vyuo ambavyo Serikali imepewa bure?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Londo, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tuna Chuo cha VETA pale Mikumi ambacho hakijafanyiwa ukarabati na majengo yake ni chakavu. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika mwaka huu wa fedha 2022/2023 tumetenga fedha kwa ajili ya ukarabati pamoja na upanuzi kwenye baadhi ya maeneo ambayo vyuo hivi bado havijakamilika au vina miundombinu ambayo ni chakavu pamoja na hiki Chuo cha Mikumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kituo cha afya cha Kata ya Malolo ni zaidi ya kilomita 150 mpaka hospitali ya Wilaya na kile kituo kimejengwa kwa nguvu ya wananchi na Waziri Mkuu amekichangia sana.

Je, ni lini Serikali itapeleka vifaa tiba ili kituo hiki cha afya kianze kufanya kazi katika ubora wake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) : Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dennis Londo Mbunge wa Jimbo la Mikumi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza ninawapongeza wananchi wa Kata ya Malolo kwa kujenga kituo cha afya kwa nguvu zao na Serikali imeendelea kuhamasisha wananchi kujenga vituo hivi kwa nguvu zao, Serikali ichangie nguvu za wananchi.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie kwamba katika mipango ya kuhakikisha vituo hivi vinapata vifaa tiba, tumeanza na Hospitali za Halmashauri lakini tutakwenda kwenye vituo vyetu vya afya ili vitoe huduma na kituo hicho pia kitapewa kipaumbele.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa, barabara hii ya kutoka Ruaha Mbuyuni kupitia Malolo, Ibanda, Mlunga, Uleling’ombe, Kinusi mpaka Wilaya ya Mpwapwa ndiyo kiungo kati ya Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Dodoma, na kwa kuwa Kata ya Uleling’ombe ndiyo Kata ambayo kiuchumi inalisha maeneo mengi ya Jimbo la Mikumi pamoja na Wilaya ya Mpwapwa.

Je, Serikali haioni kwamba wakati umefika sasa wa kuiweka barabra hii katika vipaumbele vya kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Dodoma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Jimbo la Mikumi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa mwenyekiti, tumetambua umuhimu wa barabara hiyo na ndiyo maana umeona katika mwaka wa fedha unaokuja tumeitengea fedha, kwa sababu awali barabara hii ilikuwa haipo katika mtandao wetu. Kwa hiyo, nimthibitishie Mbunge wa Jimbo la Mikumi, barabara hiyo tutaitengea fedha na itajengwa kama mapendekezo ya Mbunge lakini kutokana na umuhimu wa kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Dodoma. Ahsante sana.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Vijiji vya Changarawe katika Kata ya Masanze na Vijiji vya Malangali, Muungano, Mamoyo, Kibaoni na Maluwi katika Kata za Tindiga na Mabwerebwere mito yake imepoteza mwelekeo, inahatarisha maisha ya watu. Sasa nilikuwa naomba kuuliza Serikali;

Je, ni madhara kiasi gani kwa wananchi wetu yatokee ili Serikali ichukue hatua?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, aaomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Londo (Mb) kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba, ni kiasi gani cha madhara ili Wizara iweze kuchukua hatua. Wizara hatusubiri madhara lakini tayari tunachukua hatua kwa kutimiza majukumu yetu kuhakikisha maji hayawi laana, maji ni neema. Maeneo ambayo maji yanachepuka na kusababisha maeneo ya wananchi kuvamiwa tayari tumeyapa kipaumbele. Kwa maeneo aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge, hasa Mto Miombo ambao unasababisha madhara kwenye kata alizozitaja ya Masaza, Masava na nyingine tayari mkandarasi yupo site anafanya utafiti. Lengo ni kuona maeneo yote ambayo yanaathirika na maji yanapochepuka kwenye mto hasa nyakati za masika tunakwenda kuyadhibiti, yanaenda kutumika vizuri kwa shughuli za kibinadamu. Shughuli ambazo zinafanyika na wananchi hawa za mboga mboga, kilimo kidogo kidogo basi yote yatajengewa miundombinu rafiki ili kulinda mto kwa sababu kulinda vyanzo vya maji ni jukumu letu sote.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, barabara hii ya Londo -Lumecha ni muhimu sana lakini inayofanana na barabara ya Londo ni barabara ya kutoka Kilosa mpaka Ulaya kwenda Mikumi.

Je, ni lini Serikali inaenda kuanza ujenzi wa barabara hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dennis Londo, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii ilishaanza kujengwa na tuna mpango wa kuendeleza. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba azma ya Serikali ni kuunganisha barabara inayounganisha barabara ya Dodoma – Morogoro kwenda Mikumi ili iweze kujengwa yote kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mipango ipo na bado tutaendelea kuikamilisha hiyo barabara kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa shule kongwe zinajumlisha pia shule ya Zombo, shule ya msingi pale Jimbo la Mikumi pamoja na Kidodi. Je, Serikali haioni wakati umefika sasa wa kuona namna bora ya kuboresha shule hizi kwa kuzikarabati.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Londo, Mbunge wa Mikumi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mpango ambao tunao sasa hivi miongoni mwa shule ambazo zitafanyiwa ukarabati ni pamoja na hizi ambazo Mheshimiwa Mbunge ameziainisha.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa walemavu hawa si wote wana uwezo wa kufanya shughuli za kibiashara ama kujiwezesha kiuchumi lakini wanalelewa na babu zao, bibi zao ama baba zao ama wajomba zao ambao hawa-qualify katika hii asilimia kumi.

Je, Serikali haioni wakati umefika sasa wakuangalia wazazi ama walezi wanaoangalia walemavu ambao wenyewe hawajiwezi lakini wanaweza kuwezeshwa kwa ajili ya kuangalia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dennis Londo, Mbunge wa Jimbo la Mikumi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna walemavu ambao hawana uwezo wa kufanya shughuli hizo na wangehitaji kupata mikopo ili wajikwamue kiuchumi. Naomba tuchukue wazo la Mheshimiwa Mbunge, tukalifanyie tathmini na kuona uwezekano wa kuwapa mikopo hiyo wazazi au walezi wa hao wenye ulemavu ili waweze kuwasaidia. Ahsante.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya kutoka Kilosa kwenda Mikumi inaungana na Mji wa Kilosa ambako kuna uwekezaji wa mabilioni ya hela station ya SGR lakini kipande hiki kimekuwa kimeingia kwenye bajeti kwa miaka mitano mfululizo bila utekelezaji. Sasa kwa kuwa sisi wengine hatujui kuruka sarakasi ndani ya Bunge, ni lugha ipi ambayo unataka tutumie kuwaeleza Serikali barabara hii ni muhimu kutengenezwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Londo, Mbunge wa Mikumi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba Serikali ilishaanza kuijenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami hadi Kilosa na tumetenga na tumeendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuendelea kwenda Ulaya hadi Mikumi na ni azma ya Serikali kuunganisha hii Barabara ya Morogoro kutoka Dodoma kwenda Morogoro na Morogoro kwenda Iringa kupitia Kilosa hasa tukitambua umuhimu wa hiyo barabara kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inafahamu na ndiyo maana imeanza kutenga fedha na hata kwenye kipindi hiki cha bajeti nina hakika hiyo barabara itaendelea kutengewa fedha ili kuijenga japo siyo yote lakini kwa awamu.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kama alivyozungumza kwenye majibu yake Mheshimiwa Naibu Waziri kwa suala la FDC na VETA, kwamba lengo ni kupeleka katika kila Wilaya.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri haona sasa wakati umefika wa ku-engage TAMISEMI katika mlolongo huu wa kwenda kusimamia ili hivi vyuo kuwa endelevu? Serikali haioni wakati umefika wa kumshirikisha TAMISEMI katika usimamizi wa hivi vyuo vya ufundi? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Londo, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ametoa ushauri wa kwamba tushirikiane, lakini tumekuwa tukishirikiana kwenye eneo hili la utoaji wa elimu kuanzia shule hizi za msingi, sekondari mpaka vyuo. Kwa hiyo, nimwondoe wasiwasi kwamba ushirikiano upo, lakini kwa vile ametoa ushauri, ushauri huo tumeuchukua tunaenda kuufanyia kazi. Kwa maana ya ushirikiano, bado tunaendelea kushirikiana na TAMISEMI kwa sababu vyuo hivi viko kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, idadi ya watanzania ambao wako diaspora milioni 1.5 ni sawasawa na idani ya wananchi wote ambao wanaoishi katika Mkoa wa Mtwara. Pia ni zaidi ya wananchi ya wananchi wote ambao wanaishi katika Mkoa wa Pwani, Songwe, Iringa, Lindi, Njombe na Katavi.

(a) Mheshimiwa Spika, kwa ukubwa wa idadi ya wananchi hawa; je, Serikali haioni wakati umefika sasa kushirikiana nao kuwa na uongozi rasmi ambao utakuwa daraja kati ya diaspora na Serikali yetu hapa nyumbani?

(b) Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, Serikali imekiri mchango mkubwa wa diaspora, sasa Serikali haioni kwamba wakati umefika wa kuondoa vikwazo na kulieleza Bunge hili mchakato wa uraia ama hadhi maalum umefikia wapi? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu uongozi Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na diaspora ambazo ziko organized katika nchi mbalimbali, kwa kutambua hilo Mabalozi wetu wote katika nchi wanazotuwakilisha ndio Walezi wa Jumuiya hizi za diaspora na wamekuwa wakipata ushirikiano mkubwa sana katika Balozi zetu.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la kuondoa vikwazo, hili ni kweli kwa kutambua mchango mkubwa wa diaspora katika maendeleo ya nchi yetu, tayari Serikali imeamua kutoa hadhi maalum kwa diaspora, hivi sasa Serikali inakamilisha taratibu za kuwapa hadhi maalum na muda si mrefu diaspora watapatiwa hadhi maalum. Ninakushukuru sana. (Makofi)
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikumi idadi ya malori ni kubwa msongamano ule unasababisha hatari na usalama wa maisha ya raia na mali zao. Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imetoa Milioni Mia Moja kwa ajili ya kutatua tatizo hilo la malori kwa kutenga eneo na kusaidia ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nini commitment ya Serikali kusaidia Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa katika kutatua tatizo la malori ambalo linasababishwa na mizani pale Mikumi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F.
MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli eneo la Mikumi kuna msongamano wa malori mengi na Mheshimiwa Mbunge ninakupongeza kwa kufatilia jambo hili, alipolileta Serikalini tukawapa eneo ambalo ni la TRC kwamba waendelee kulitumia na tayari tulishatoa kibali hicho kama Serikali, kinachosubiriwa sasa ni wao kama Halmashauri kulifanyia hilo eneo ukarabati ili malori yaliyoko pale barabarani yahamie eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo ninakupongeza Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi zako hizo. Ahsante.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. lakini barabara inayofanana na Gairo kwenda Nongwe ni barabara ambayo inaanzia Ruaha Mbuyuni – Malolo – Mlunga – Reli Ng’ombe mpaka Kibakwe – Mpwapwa. Barabara hii imeshapitishwa na RCC kwa miaka miwili sasa; Je, nini kauli ya Serikali?

Mheshimiwa Spika, kutokupitisha barabara hii kwa kadiri ya maombi ya RCC mkoa wa Morogoro; Je, Serikali haioni kwamba inawapotezea haki wananchi hawa ambao wanasafiri mwendo zaidi ya kilomita 400 kufika Mpwapwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kwa pamoja ya Mheshimiwa Londo Mbunge wa Mikumi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara hii inaunganisha mikoa ya Morogoro, Iringa na Dodoma na Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba kwa sasa barabara hii inahudumiwa na wenzetu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini, na atakuwa pia anaelewa kwamba baada ya kupokea maombi kuipandisha barabara hii ili ihudumiwe na TANROADS, wataalamu wameshaitembelea ili kufanyia tathmini na kuona kama inakidhi vigezo vya kuhamishiwa TANROADS. Kwa hiyo tayari maombi yameshafika Wizarani kwa ajili ya kufanyiwa tathmini na maamuzi, na baada ya hapo tutawajulisha kama imekidhi vigezo ili iweze kupanda hadhi, ahsante. (Makofi)
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nishukuru kwa majibu mazuri ya Serikali lakini tunazungumzia maisha ya watu kwa idadi ya watu 863 ambao wameonekana hawana hatia ni asilimia 41.8 ni watu wengi sana katika utendaji wa umma na watu hawa wamepitia mateso, wamedhalilika katika jamii ambayo tunaishi ambapo tuhuma tayari ni uhalifu sasa swali. Serikali inachukua jitihada gani kuwasafisha watumishi ambao wamepelekwa Mahakamani kwa tuhuma za rushwa asilimia 41.8 wameoneka hawana hatia kutumia nguvu ile ile ya kuwatangaza ni wahalifu, wanatumia nguvu gani kuwasafisha watumishi hao? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa madhara ni makubwa ya kisaikolojia, kijamii na haiba yao imechafuka kwenye macho ya umma. Kwa muda gani Serikali itaendelea kuvumilia kuwaona watumishi hawa wanaendelea kuhangaika na nini jitihada za Serikali katika kuhakikisha kwamba wanarudi katika utumishi wakiwa wana haiba njema na safi?

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Mikumi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Dennis Londo utaratibu wa utumishi wa umma umeelezwa ndani ya sheria kama nilivyozitaja pamoja na sheria nyingine lakini pia utaratibu wa kuwarudisha watumishi kazini nao pia umeelezwa katika sheria hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Dennis Londo utaratibu wa kuwaandikia wale ambao wamekwisha safishwa na Mahakama na kuonekana kwamba hawana makosa utaendelea kufanyika. Pamoja na hilo pia Mheshimiwa Rais, ameelekeza na ndiyo tunayo yafanyia kazi kwamba lazima tuhakikishe kwamba hawa watu ambao wanakutwa hawana makosa tunawafanyia haki la kwanza, lakini pili wanarudishwa kazini mapema iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo lote Mheshimiwa Rais ameendelea kuhakikisha kwamba kupitia Tume yake wa Utumishi wa Umma taratibu na haki zote wa watumishi hawa zinafuatwa na kusimamiwa. (Makofi)
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya jitihada za kuongeza watalii dunia nzima ni kurahisisha miundombinu, hasa barabara na mageti kutokea kila upande. Kuna maelekezo ya Serikali pale Mbuga ya Mikumi kufungua geti lingine kwa upande wa Kilangali na Tindiga ili kurahisisha usafiri wa watalii kutokea Kilosa kwenye station ya SGR itakapokamilika.

Je, Serikali ina kauli gani? Lini geti hili linaenda kufunguliwa kuheshimu maelekezo ya Makamu wa Rais, lakini wewe pia Naibu Waziri ulipoitembelea Mikumi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, tunatambua kwamba, geti hili ni la muhimu sana kwa ajili ya uchumi wa nchi, hususan katika masuala mazima ya utalii na tayari tulishaanza mpango wake. Kwa hiyo, nimuondoe shaka Mheshimiwa Mbunge wa Mikumi kwamba geti hili tutalifungua na pale tu ambapo mchakato wa reli utakavyoanza tayari na sisi utekelezaji wake utakuwa umekamilika.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali imekiri kwamba kuna idadi ndogo sana ya usajili kwa maana ni asilimia 16 tu ya nguvu kazi ya walipa kodi: Je, Serikali haioni wakati umefika sasa kwa Wizara ya Fedha, TAMISEMI na Wizara ya Viwanda na Biashara kukaa pamoja na kuona namna bora ya kusajili wafanyabiashara na walipa kodi katika ngazi ya vijiji badala ya kugombania leseni kwa maana ya leseni B?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo ya kimkakati, mfano Jimbo la Mikumi ambalo siyo wilaya wala siyo halmashauri, lakini ni maeneo ya kimkakati ya biashara na kodi: Serikali ina mpango gani wa kuchechemua maeneo haya ili wafanyabiashara washiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa letu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ni kweli kama nilivyosema, bado idadi ya walipa kodi ni ndogo na tayari Serikali ina mikakati mbalimbali ili kuhakikisha tunaongeza idadi ya walipa kodi kulingana na nguvu kazi iliyopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, ni kuendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Ufanyaji Biashara nchini (MKUMBI), na hili tumeendelea kutoa elimu na hatua mbalimbali ambazo zinapelekea kuvutia wafanyabiashara na wazalishaji mbalimbali kurasimisha biashara zao ikiwa ni pamoja na kuondoa kodi, tozo na ada ambazo ni kero kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumeendelea kuweka mazingira ambayo yanarahisisha usajili wa biashara kwa wananchi wote. Kwa hiyo, tayari Serikali inafanya kazi kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha, TAMISEMI lakini pia Wizara ya Viwanda. Sasa hivi tunataka tuone namna ya kuhakikisha tunapeleka maelekezo kwenye ngazi ya vijiji ili kuwa na dirisha la pamoja la kuratibu masuala ya biashara kutoka ngazi ya Kijiji, lakini tayari tumeshafika kwenye halmashauri ambako tunaweka Idara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji ambao watafanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, maeneo mkakati, ni kweli tunaona umuhimu wa kuhakikisha maeneo ya kimkakati ambayo yana fursa nyingi za kibiashara kuyawekea miundombinu wezeshi ikiwemo masoko na kuweka vituo maalum vya kuhamasisha wananchi kusajili biashara zao. Tayari Wizara kupitia BRELA tumeshaanza kupeleka elimu na kuhamasisha wananchi kusajili biashara zao katika maeneo husika kwa maana ya halmashauri na hata katika maeneo yale ya kimkakati ambayo tunaona yana biashara ambazo zinaweza kuleta tija kwa uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, Sera ya Ugatuaji ni Sera ya Kitaifa. Suala la mapato ya taasisi zetu na maduhuli ya Serikali kwenda moja kwa moja hazina inaenda kinyume na hii Sera ya ugatuaji. Ndio inayosababisha miundombinu muhimu kwenye hifadhi zetu kutotengenezwa mara kwa mara. Je, Serikali haioni wakati umefika sasa wa kurudisha walau asilimia 20 ya mapato kwenye hifadhi zetu, ili washughulikie miundombinu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, Serikali inakiri kufunguliwa kwa geti hili katika Kata ya Kilangali na Tindiga kunaenda kufungua fursa za kiuchumi. Je, wamewaandaa vipi wananchi wa Kata za Tindiga, Dhombo, Masanze na Kilangali, ili wasije kuwa wageni wakati fursa hizi ambazo zitatokana na kufunguliwa kwa lango hili zitakapowadia? Nashukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na changamoto ya kukamilika kwa miundombinu kwenye maeneo yetu kutokana na kukosekana kwa fedha na mabadiliko tuliyokuwa tumefanya ya mfumo wa kukusanya mapato na kuyapeleka moja kwa moja kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina. Hata hivyo, baada ya jambo hili kujadiliwa kwa kina ndani ya Bunge lako Tukufu na jambo hili kufikishwa Serikalini tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuridhia kurejesha tozo ya maendeleo ya utalii ambapo tayari Mheshimiwa Rais ameridhia asilimia tatu ya fedha hizi iweze kutumika kwa ajili ya shughuli hizi.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali la pili; jukumu la kutoa elimu kwa wananchi wetu sio jukumu la Serikali Kuu peke yake ni pamoja na halmashauri zetu. Nitoe rai kwa halmashauri husika ziweze kutoa elimu kwa wananchi, tukiwepo sisi Waheshimiwa Wabunge, ili wananchi waweze kuchangamkia fursa za kimaendeleo zinazokuja katika maeneo yetu.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kuna ongezeko kubwa la thamani ya bidhaa zinazotokana na ubunifu, kwa mfano, kutoka mwaka 2002 kulikuwa na shilingi bilioni 208, kufikia mwaka 2020 zaidi ya shilingi bilioni 700 kwa takwimu za Umoja wa Mataifa. Je, Serikali imejipangaje kulinda hakimiliki za wabunifu wa Kitanzania ili washiriki kikamilifu katika uchumi bunifu wa dunia?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa uchumi bunifu na bidhaa bunifu ni utajiri wa kibiashara na kiutamaduni. Je, Serikali haioni wakati umefika sasa Wizara ya Elimu kushirikiana na Wizara ya Utamaduni, Wizara ya Fedha na taasisi nyingine za kibiashara kuona kwamba Tanzania inashiriki kikamilifu katika uchumi bunifu katika dunia yetu? Nashukuru.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Londo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inajitahidi kwanza kuchochea bunifu mbalimbali hapa nchini na kuanzia mwaka 2019, Serikali imekuwa ikiendesha Mashindano ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu maarufu kama KISATU kwa ajili ya kualika watu mbalimbali walete bunifu zao, washindanishwe, zitambuliwe na ziendelezwe. Baada ya kuendelezwa ziweze kulindwa kwa kupata hakimiliki. Tangu tuanze mashindano hayo tayari bunifu 283 zimeshahakikiwa, 38 tayari ziko sokoni nazo hizo zinalindwa kwa ajili ya kuingia sokoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla wake Serikali inaona umuhimu sana wa kuchochea bunifu kwa ajili ya maendeleo ya uchumi, ndiyo maana vile vile tunasaidia vijana wetu ambao wanaenda na bunifu mbalimbali katika mashindano ya Kimataifa na baadhi yao wameshinda tuzo mbalimbali na sisi tunachochea waingie sokoni kwa ajili ya kubiasharisha bunifu zao.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniruhusu kuuliza swali la nyongeza. Juzi kulikuwa na ajali ambayo imepoteza maisha ya watu watano na majeruhi hali zao ni mbaya; jana kulikuwa na ajali ambayo imejeruhi majeruhi wanane ambao hali zao ni mbaya; na hizi namba ambazo tunapewa na Serikali 128 ni namba za ajali ambazo ni kubwa mno, zina madhara makubwa:-

Mheshimiwa Spika, Swali langu kwa Serikali:-

(a) Serikali haioni wakati umefika sasa kwa sababu ajali hizi zina athari kubwa na pana kwa jamii yote, kutangaza eneo hili kama ni janga?

(b) Serikali haioni wakati umefika sasa Wizara ya mambo ya ndani kukaa pamoja na TAMISEMI na Wizara ya Afya kuangalia Kituo cha Afya Mikumi na Hospitali ya Mtakatifu Kizito kama maeneo ya kimkakati ya uokozi wa majeruhi ambao unatokana na ajali hizi, badala ya kukichukulia kama wanavyokichukulia sasa hivi?

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni kweli ajali hutokea na kadiri alivyosema, katika kipindi cha miaka hii 12 zimetokea ajali 128. Kwa takwimu zetu, ajali hizi zimekuwa zikishuka kadiri Serikali inavyoimarisha usimamizi wa sheria. Kwa mfano, mwaka 2010 tulikuwa na ajali 16 na majeruhi wakawa saba, vifo vinane; 2011 tulikuwa na ajali 14, vifo vitano na majeruhi 10, lakini kadiri miaka ilivyoongezeka ajali hizo zilipungua. Kwa mfano, mwaka 2021 ajali tano, vifo vitatu na majeruhi watatu; na mwaka 2022 ni ajali tano, vifo vitatu na majeruhi wawili.

Mheshimiwa Spika, kiukweli hata kama atakufa mtu mmoja, kwetu tusingependa kumpoteza kwa jambo ambalo lingeweza kuzuilika. Kwa hiyo, pamoja na dhamira yake kwamba litangazwe janga, sijaona kama kiwango hiki kinatufikisha mahali pa kutangaza kama hili ni janga.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, tutaendelea kuimarisha doria kama inavyofanyika kwa wenzetu wa Iringa, Askari hufuatilia magari haya, na kwa kweli kule ajali zimepungua sana. Kwa hiyo, kupitia Bunge lako Tukufu, tumwelekeze RPC Morogoro aanzishe utaratibu kama uliofanywa na mwenzie wa Iringa kuona kwamba magari yanafuatiliwa kwenye maeneo ambayo ni prone, yenye mwelekeo mkubwa wa ajali.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kukaa pamoja kwa Wizara husika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaangalia kupitia ushirikiano wetu kwenye vikao vyetu vya Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, wadau wote aliowataja ni Wajumbe ili kuona namna ya kuimarisha huduma za uokozi katika Kituo cha Afya Mikumi na Hospitali ya Kizito iliyopo pale Mikumi. Nashukuru sana.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Je, Serikali haioni kwamba ni busara kukamilisha barabara ya Kilosa kwenda Mikumi ili kuongeza tija kwenye uwekezaji mkubwa wa reli ya SGR pale Kilosa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge wa Mikumi, siyo tu busara, lakini kwa kweli ni barabara ambayo ni muhimu, ambayo sasa itakuwa inaunganisha barabara ambayo tunaijenga kwa EPC kuanzia Namtumbo – Malinyi – Mikumi ambayo tunaona busara badala mtu kwenda Morogoro, itoke Mikumi kuja Kilosa. Kwa hiyo, hiyo mipango ipo kuhakikisha kwamba tunapafungua kati ya Kilosa na kuunganisha na Mikumi, ahsante.

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniruhusu kuuliza swali la nyongeza. Hifadhi za Taifa na Mapori ya Akiba imekuwa ni moja ya chanzo cha migogoro mikubwa kati ya wananchi na taasisi za Serikali, lakini kutokushirikisha wananchi kupitia sera hiyo ya uwajibikaji kwa jamii imekuwa ni moja ya vyanzo vya migogoro hii. Je, Serikali inaweza ikatoa tamko ni kwa nini fedha za CSR hazijaenda kwa wananchi ambao wanapakana na Hifadhi ya Mikumi kwa miaka sita mfululizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali hilo la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la fedha hizi ambazo kama ambavyo tumeeleza zinazotoka kwenye taasisi zinazosimamia uhifadhi. Lengo na madhumuni moja kwa moja ziende kwa wananchi, lakini changamoto iliyokuwepo ni moja kwamba fedha hizi haziwezi kutosheleza kupeleka kwenye Halmashauri zote kwenye maeneo yote. Kwa hiyo nimwambie tu Mheshimiwa, moja ni kwamba tunawashirikisha na ndiyo maana tukamjibu Mheshimiwa pale kwamba fedha hizi ni bora ziende moja kwa moja kwa wananchi ili tuwashirikishe na tuweze kujua wanachokitaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutakapopata fedha, tutahakikisha kwamba kwenye Halmashauri yake na maeneo yake fedha hizi zinafika na zinatekeleza miradi ya wananchi.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya kutoka Dumila kwenda Kilosa, kutoka Kilosa kwenda Mikumi kupitia Masanze – Zombo – Ulaya na Muhenda mpaka Mikumi ni uti wa mgongo kwa uchumi wa Mkoa wa Morogoro: Nini Kauli ya Serikali kuhusiana na hali ya barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dennis Londo, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakubaliana na Mheshimiwa Londo kwamba, kwa kweli hiyo ni barabara muhimu sana na hasa tutakapokamilisha hii barabara ya kutoka Lumecha – Malinyi – Kidatu hadi Mikumi. Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba, kwa sababu ya umuhimu wake, katika bajeti inayokuja tumeitengea fedha ili kuendelea kuijenga kwa kiwango cha lami ili kuunganisha Kilosa na Mikumi kwa kiwango cha lami, ahsante.

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, madai ya watumishi wa kilichokuwa Kiwanda cha Sukari Kilombero na process nzima ya ubinafsishaji limebaki kuwa kovu kwenye kidonda kwa wananchi hawa.

Swali langu kwa Serikali; kuna mkataba wa hiari kati ya watumishi hawa na kilichokuwa Kiwanda cha Sukari Kilombero ambao haujatekelezwa mpaka sasa; je, nini hatua za Serikali katika utekelezaji wa hilo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuna kauli ya Serikali ambayo ilitolewa na Waziri Kusila pamoja na Waziri Kimiti walipokutana na watumishi hawa mwaka 2000.

Nini utekelezaji wake ili kutibu majeraha ambayo yametokana na ubinafsishaji wa kiwanda hiki cha sukari?

SPIKA: Mheshimiwa Londo, hilo la pili Mheshimiwa Naibu Waziri anajua kweli ama unazo hizo taarifa hapa?

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, suala hili lipo katika Ofisi ya Waziri Mkuu.

SPIKA: Hilo ni la nyongeza.

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, ni la nyongeza, ndiyo.

SPIKA: Ndiyo, sasa ili yeye aweze kuwa na majibu lazima ajue hao wawili uliowataja walisema nini, ndiyo nauliza Mheshimiwa Waziri hizo taarifa za walichosema anazo? Maana swali lako ni la msingi, lakini sasa nataka kujua yeye anayo? Maana asije akatupa majibu ambayo wale hawakusema.

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, Serikali iliahidi kuwapatia mshahara wa miezi kumi kati ya 40 ambayo ilikuwa ni kifuta jasho kwa watumishi hawa. Sasa utekelezaji mpaka leo hawajatekeleza, nini kauli ya Serikali.

SPIKA: Ahaa, kwa hiyo hicho ndicho walischosema hao wawili?

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, ndiyo.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dennis Lazaro Londo, Mbunge wa Jimbo la Mikumi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, la kwanza, kuhusiana na mkataba wa hiari aliousema, unaitwa mkataba wa hali bora kwa mujibu wa sheria. Katika mkataba huu wa hiari, bado ni sawa na mikataba mingine kwa mujibu wa Sheria yetu ya Mikataba Cap. 345, na kama kutakuwa kuna utekelezaji ambao haukufanyika, hilo ni eneo la kwenda kufuatilia na kuweza kushughulikia.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, mtakumbuka kwamba katika kesi hii ilikuwa ni suala ambalo lilihitaji majadiliano katika upande wa wafanyakazi, Chama cha Waajiri, lakini pia uongozi wa kiwanda wakati wanabinafsisha kiwanda hicho. Na katika kipindi hicho mbali na yale ambayo yalizungumzwa kama utatuzi ya mgogoro, kulikuwa kuna mashauri ambayo yalikwenda mahakamani, sasa katika mashauri yaliyokwenda mahakamani kuna uamuzi wa mahakama ambao ulifanyika, kama malipo yatakuwa hayajafanyika, utaratibu wa kisheria ni kufanya execution of decree. Kwa hiyo enforcement of the execution of decree kama haikufanyika, nitawasiliana na Mheshimiwa Mbunge tuweze kuona, kwa sababu mahakama ilifanya maamuzi mahususi, niwasiliane naye, na kama kesi hiyo itakuwa kubwa kwa kiwango chake tutaona namna ya kwenda kushirikiana na kukutana na wafanyakazi hao ili haki yao iweze kupatikana kwa mujibu wa sheria na maamuzi ya mahakama, ahsante.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, Barabara ya kutoka Iyombwe – Kisanga – Malolo mpaka Kilolo ni barabara ambayo inahudumiwa na TAZAMA lakini ni barabara muhimu sana ya kuunganisha Mkoa wa Morogoro na Iringa.

Je, Serikali ina kauli gani kutumia barabara hii kama mbadala wa barabara kuu ya kutoka Mikumi kwenda Mbeya?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, barabara aliyotaja ni kweli ni muhimu na kwa sasa Serikali inachofanya ni kuhakikisha kwamba inakarabatiwa kwa kiwango cha changarawe wakati Serikali ikiendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuifanyia usanifu ikiwa ni maandalizi ya kuijenga kwa kiwango cha lami, ahsante. (Makofi)
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, changamoto ya tembo kwenye vijiji ambavyo vinazunguka hifadhi ya Mikumi ni kubwa na Serikali imetoa ahadi nyingi; nini kauli ya Serikali kwa madhara makubwa ambayo wananchi wanayapata kutokana na uvamizi wa tembo katika vijiji vya Kilangali, Zombo, Ulaya na Iyombo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, nimepokea maswali tisa ya nyongeza kwa Waheshimiwa mbalimbali na naomba niyajibu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la Mheshimiwa Londo; ameuliza ni nini kauli ya Serikali? Kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi. Ni kwamba sasa hivi tunaangalia njia mbadala wakati huo huo tunaendelea kutatua migogoro hii ya wanyama wakali na waharibifu. Tunajenga vituo, tunaajiri VGS, lakini wakati huo huo tumeshaweka sasa mipango kwenye baadhi ya maeneo tuanze kuweka fence ya umeme ili kupunguza hii athari ya wanyama wakali na waharibifu.

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la Mheshimiwa Anne Malecela, naomba niahidi mbele ya Bunge lako hili Tukufu kwamba baada ya Bunge hili tutaongozana naye katika maeneo yale. Lakini pia tumeshaanza kuongeza nguvu kwake, tumepeleka askari na tutaendelea kuajiri VGS katika maeneo hayo ili tuweze kushirikiana pamoja. Kwa hiyo, wananchi wa Same kilio chenu kimeshasikika Bungeni na tutaongozana na Mheshimiwa Mbunge (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye suala hili la Mheshimiwa Vita Kawawa, ni kweli Mheshimiwa Waziri alitoa ahadi ya ujenzi wa madarasa katika jimbo lake, na huu ulikuwa ni mpango wa CSR si kwa ajili ya fidia ya wanyama wakali na waharibifu. Ni kwamba Mheshimiwa Waziri alifanya ziara katika jimbo hilo na akatoa ahadi ya ujenzi wa madarasa ili kuwafanya wananchi wanaoishi katika maeneo hayo tushirikiane pamoja katika uhifadhi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niendelee tu kuahidi kwamba ahadi ni deni, Wizara itatekeleza. Na kwa kuwa ilikuwa ni kauli ya Mheshimiwa Waziri basi tutafuatilia ili ahadi hii iweze kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dunstan, Mbunge wa Mkinga, yeye ameongelea kuhusu kituo; niahidi tu kwamba katika mpango wa fedha wa 2023/2024 uliopitishwa katika Bunge lako hili, tutapeleka kituo katika Jimbo la Mkinga ili tuongeze nguvu ya kudhibiti wanyama wakati na waharibifu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Justin Nyamoga, madhara makubwa; naomba niahidi tu kwamba tutaendelea kufuatilia katika maeneo haya ili wananchi waweze kulipwa fidia inayotokana na wanyama wakali na waharibifu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Grace Tendega; naomba tu nilitaarifu Bunge lako, na kwa ridhaa yako, nipe tu nafasi kidogo nitoe ufafanuzi. Tumekuwa na changamoto nyingine imejitokeza katika Mkoa wa Iringa; kuna uvamizi wa simba kwenye baadhi ya maeneo, lakini naomba niwataarifu wananchi, nadhani wameona juhudi za Serikali toka uvamizi huu umejitikeza tumekuwa karibu na wananchi, tunatoa elimu.

Mheshimiwa Spika, naniendelee kutoa elimu kupitia Bunge lako hili, kwamba wakati huu ambapo tunawasaka hawa simba, wananchi wawe na tahadhari ya kutotembea usiku. Lakini pia wenye mifugo wawashe moto kuzunguka maeneo yale ya mifugo ili kuepusha simba wasisogee katika maeneo hayo tunajitahidi sana kulinda maisha ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaombe Wanairinga, Serikali iko kazini na tumeshapeleka helikopta inazunguka usiku na mchana kuhakikisha tunawasaka hawa simba. Tuendelee kushirikiana pamoja ili kuhakikisha zoezi hili tunalikamilisha na simba hawa tunawachukua na kuwarudisha katika maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la Mheshimiwa Charles, Mbunge wa Mwibara; kumekuwa na changamoto ya viboko na tembo. Naomba niendelee tu kuahidi, nakumbuka tuliwasiliana na Mheshimiwa Mbunge na tukaongeza nguvu ya askari katika maeneo hayo. Tuendelee tu kuwasiliana, nguvu tutaongeza lakini pia tutaendelea kuajiri VGS ili waweze kusaidia pale inapotokea dharura katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na ombi la Mheshimiwa Jimbo la Tunduru kwamba tuongeze VGS (askari wa vijiji). Tunaomba tulipokee hili na tutaweka priority katika eneo hili, tunajua hii changamoto ya wanyama wakali.

Mheshimiwa Spika, pia kulikuwa kuna shida moja ya mratibu ambaye alihamishwa. Nadhani maelekezo yameshatoka, atarudishwa katika eneo hilo ili aweze kushirikiana na wananchi kudhibiti wanyama wakali na waharibifu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Matiko tayari nimeshalijibu, kwamba tuko kwenye process ya ku-review hizi sheria na kanuni kuangalia sasa angalau tusogeze kiwango fulani ili wananchi nao waweze kuona umuhimu wa namna ya uhifadhi.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya kutoka Kilosa – Ulaya kwenda Mikumi ambayo inapitia Masanze - Zombo na Ulaya ni barabara muhimu sana kwa kuchukua watalii kutoka SGR Station pale Kilosa kuja Mikumi mbugani na barabara hii ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010, 2015 na 2020.

Sasa kwa kuwa mimi siwezi kuruka sarakasi, nifanye nini ili Serikali ijue kwamba barabara hii ni muhimu kutengenezwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dennis Londo, Mbunge wa Mikumi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba barabara hii ilishaanza kujengwa ila bado haijakamilika nani azma ya Serikali kuikamilisha barabara hii na ni barabara ambayo inaunganishwa na barabara ya Mikumi – Kidatu hadi kwenda Songea.

Kwa hiyo, katika mipango ambayo Serikali inaendelea nayo kama alivyowasilisha Mheshimiwa Waziri wakati wa bajeti barabara ambazo zinafikiriwa pengine kujengwa kwa mpango wa EPC ili kuikamilisha barabara yote. Ahsante.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Chuo cha VETA Mikumi ni chuo ambacho kilijengwa na Irish people kwa ajili ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa na kwa nia njema kabisa Chuo kile tuliikabidhi Serikali. Tangu tumeikabidhi Serikali hakuna jitihada zozote za kujenga ama kukarabati miundombinu ya chuo kile hasa ukizingatia kwamba hali yake ni mbaya na hakina mabweni. Sasa nini kauli ya Serikali kuhusiana na ujenzi wa miundombinu hasa mabweni katika Chuo cha VETA?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la kaka yangu Mheshimiwa Londo, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Londo kwa ufuatiliaji wa karibu wa chuo hiki, siyo mara moja wala mara mbili tumeshawahi kukutana.

Mheshimwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Londo aridhie baada ya kikao hiki tuweze kukutana ili kuangalia kitu gani cha kufanya na vilevile tuweze kutuma timu kwenye eneo hili kwa ajili ya kufanya tathmini kama tutakavyofanya kwa Mheshimiwa Kimei, tuweze kufanya vilevile na kwake, kuangalia thamani ya ukarabati pamoja na uongezaji wa miundombinu kwenye eneo lile ili tuweze kutekeleza kwa wakati.

Mheshimwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa, Mheshimiwa Naibu Waziri, amezungumza kwamba moja ya vigezo vya kupata Halmashauri ni maombi ya Halmashauri husika kufika TAMISEMI. Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imeshaomba kwa miaka mitano mfululizo kuanzisha Halmashauri katika Jimbo la Mikumi, tuna vigezo vyote ambavyo vingine vimepitiliza.

Je, ni nini kauli ya Serikali kwa wananchi wa Jimbo la Mikumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dennis Londo, Mbunge wa Jimbo la Mikumi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Halmashauri ya Kilosa ina Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mikumi, na ninafahamu kwamba vikao vya awali vya kuomba kupandishwa hadhi kuwa halmashauri ya Mji vimeanza, kwa ngazi ya DCC, lakini nafahamu kwamba RCC bado haijakaa kupitisha maombi hayo. Kwa hiyo, nimwelekeze Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kufanya mapema suala hili ili tuweze kuona kama inakidhi vigezo hivyo baada ya kuwasilishwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kuboresha barabara kwa kiwango cha lami katika Kata za Mikumi na Ruaha ambazo ni Kata za kimkakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, Serikali itatekeleza ahadi hii ya kuboresha Barabara za Mikumi na Ruaha kwa kiwango cha lami kadri ya upatikanaji wa fedha. Nitakaa na Mheshimiwa Londo kuona ni namna gani ambavyo tunaweza tutaratibu hili kupitia Ofisi ya Meneja wa TARURA Wilaya ya Kilosa na Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro ili tuweze kutekeleza ahadi hiyo.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, treni ya mwendokasi kutoka Dar es Salaam ndani ya miezi michache itaanza kufanya kazi na kuna uwekezaji mkubwa kwenye kituo cha treni pale Kilosa, wakati huo huo kuna uwekezaji zaidi ya dola milioni 120 kwenye Hifadhi ya Taifa ya Mikumi ambayo inaenda kuongeza ndege mpaka 50 kwa siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokukamilika kwa barabara ya kutoka Kilosa kuja Mikumi kuunganisha miundombinu hii miwili muhimu sana kwa Taifa letu; je, ni amri, taaluma au utaalamu?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Londo, nimhakikishie barabara hii ni muhimu na Serikali inafanya kila jitihada lakini yote haya yanategemeana na upatikanaji wa fedha. Kwa hiyo, nimhakikishie fedha zitakapopatikana tutaweka barabara hii kuijenga kwenye utaratibu aliouomba. Nakushukuru sana.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, treni ya mwendokasi kutoka Dar es Salaam ndani ya miezi michache itaanza kufanya kazi na kuna uwekezaji mkubwa kwenye kituo cha treni pale Kilosa, wakati huo huo kuna uwekezaji zaidi ya dola milioni 120 kwenye Hifadhi ya Taifa ya Mikumi ambayo inaenda kuongeza ndege mpaka 50 kwa siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokukamilika kwa barabara ya kutoka Kilosa kuja Mikumi kuunganisha miundombinu hii miwili muhimu sana kwa Taifa letu; je, ni amri, taaluma au utaalamu?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Londo, nimhakikishie barabara hii ni muhimu na Serikali inafanya kila jitihada lakini yote haya yanategemeana na upatikanaji wa fedha. Kwa hiyo, nimhakikishie fedha zitakapopatikana tutaweka barabara hii kuijenga kwenye utaratibu aliouomba. Nakushukuru sana.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mamlaka ya Mji Mdogo wa Mikumi ina zaidi ya umri wa miaka 20 na mchakato wa kuomba halmashauri ulishapita katika ngazi ya wilaya, mokoa na TAMISEMI na kwa kuwa Jimbo la Mikumi au Tarafa ya Mikumi siyo halmashauri wala siyo makao makuu ya wilaya imepitwa na fursa zote za miradi ya kimkakati. Je, nini mpango wa Serikali katika kukumbuka miji hii ambayo haina hadhi ya wilaya au halmashauri katika miradi mikubwa ya kimkakati kama TACTICs na miradi mingine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dennis Londo Mbunge wa Jimbo la Mikumi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, uanzishwaji wa mamlaka za miji midogo ikiwemo Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mikumi ulianzishwa kwa dhamira njema ya Serikali kuhakikisha kwamba inasogeza huduma za jamii karibu zaidi na wananchi. Hiyo ndiyo sababu ya msingi Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mikumi ilianzishwa lakini pia na mamlaka za miji midogo maeneo mengine kote nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mikumi kwa kuwepo kazini kwa zidi ya miaka 20 lakini pia kwa kuwasilisha maombi ya kuomba kuwa Halmashauri ya Mji wa Mikumi kwa kufuata taratibu zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunatambua kwamba Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mikumi ishawasilisha maombi yao na taratibu zinazoendelea sasa ni kujiridhisha na vigezo hivyo. Pale wakati utakapofika kwa ajili ya kuanzisha Halmashauri ya Mji wa Mikumi basi hatua hizo zitachukuliwa kwa manufaa ya wananchi wa Mikumi, ahsante.