Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dennis Lazaro Londo (16 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika,hii ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge lako tukufu, nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye imempendeza mimi kiumbe wake kuwa sehemu ya Bunge lako hili la Kumi na Mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwa namna ya kipekee nikishukuru Chama changu chini ya uongozi wake Mwenyekiti wetu Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kunipa imani, lakini kwa namna ya kipekee pia nishukuru familia yangu na wananchi wa Jimbo la Mikumi kwa imani yao juu yangu kuwakilisha katika Bunge lako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Bunge lako la Kumi na Moja lilifanyakazi kubwa, kazi ambayo imemsaidia Rais wetu na Serikali yetu kwenda kwenye uchumi wa kati. Jukumu la Bunge hili la Kumi na Mbili naamini ni kwenda kutoa tafsiri chanya ya uchumi wa kati katika maisha ya Mtanzania mmoja mmoja. Hotuba ya Mheshimiwa Rais inatupa dira na mwangaza wa nini ambacho anataka kutoka kwetu, lakini pia anatuonesha ni jinsi gani tunaweza kuipeleka Tanzania katika uchumi wa viwanda ili Mtanzania mmoja mmoja aone matunda ya nchi yake kuwa katika uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hili tunapoenda kuzungumzia uchumi wa kiwanda sekta ya kilimo hatuwezi kuiacha nyuma kilimo ndiyo uti wa mgongo kilimo ndiyo kila kitu. Kuna mengi ambayo naamini yako nje ya uwezo wetu ambayo Serikali bado inayafanyia kazi. Lakini kuna mengi ambayo yako ndani ya uwezo wetu naamini tukisimama pamoja tunaweza kumkomboa mkulima na mkulima akawa sehemu ya uti wa mgongo katika Tanzania ya viwanda ambayo wengi tunaitarajia na wengi tuna matumaini nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna changamoto naomba nichukue kilimo cha miwa kama mfano. Jimbo la Mikumi wakulima wa miwa katika Bonde la Kilombero wanauwezo wa kuzalisha tani 900,000 za miwa, mnunuzi ni mmoja tu kiwanda cha sukari Kilombero ambaye uwezo wake kila mwaka ni kununua tani 600,000 tu. Maana yake tunaenda kupoteza tani 300,000 kila mwaka. Hakuna namna ambayo tunaweza kuelezea zaidi ya wananchi kukosa matumaini na hujuma kuwa sehemu ya maisha ya wakazi ama wakulima wa bonde lile.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe mfano msimu huu zaidi ya ekari 1,300 ama zaidi ya tani 30,000 za miwa zimeteketea kwa moto, hasara hii kubwa ambayo wakulima hawa wa miwa wameipata inaelezea ndwele ambayo inaelezea changamoto wakulima wanaipitia. Katika hali hii mimi naamini Tanzania haipaswi kuwa na nakisi ya sukari ama kuagiza nje sukari kama tunaweza kujiweka vizuri na kujipanga pamoja na nakisi ya sukari ambayo tunayo viwanda hivi ambavyo kazi yake ni kuzalisha sukari vimekuwa na jukumu la kuagizia sukari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu kwanza jukumu la kuagiza sukari lisiachiwe wazalishaji wa sukari, kwa kuwafanyia hivyo maana yake wanakosa incentive ya kuhakikisha miwa ya wakulima inaenda kusangwa katika viwanda vyao. Jukumu hili libebwe na Bodi ya Sukari ama Serikali yenyewe na viwanda hivi vijikite katika suala zima la uzalishaji wa sukari ndani. Tukifanya hivi maana yake tunaondoa incentive kwao. Lakini la pili miwa ya wakulima isiuzwe kwa tani za miwa, tuuze kwa suclose, kwa kufanya hivi mkulima anaenda kupata thamani ya zao ambalo amelitolea jasho lake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiondoka hapo kwa namna ya kipekee nilikuwa naomba kuzungumzia suala zima la utalii. Tunaambiwa watalii 20 kati ya 100 ndiyo ambao wanarudi Tanzania kwa ajili ya kutalii. Tuna swali la kujiuliza kwanini hawa 80 hawarudi? Wakati tunaendelea kutafakari hili naamini majibu mazuri ya Serikali yanaweza yakaboresha sekta ya utalii na kuhakikisha kwamba tunaongeza idadi ya watalii kwa kuhoji maeneo ambayo tuna changamoto nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni kuhusiana na hii barabara ambayo inahudumia SGR…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi ya kuchangia mpango huu wa maendeleo. Naomba nimshukuru Waziri wa Fedha na Mipango kwa taarifa nzuri ya mpango huu wa maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nitakuwa sijatenda haki kama sitachangia mawili matatu ambayo naona kuna umuhimu wa kuyazungumzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ambalo ni muhimu ni kwamba mpango huu wa maendeleo ni makakati wa kuendelea kuwaondoa wananchi wetu katika umaskini. Ni kweli mpango uliopita umeweza kutufikisha katika uchumi wa kati lakini uchumi huu bado umekosa tafsiri chanya katika maisha ya mtu mmoja mmoja, bado umebakia kwenye Takwimu. Kwa hiyo katika utekelezaji wa mpango huo wa maendeleo naomba uende ukatoe tafsiri chanya katika maisha ya mtu mmoja mmoja ili mabadiliko ya uchumi huu tuyaone kwa macho na si kwa takwimu tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kubwa kuliko yote mpango huu ni lazima ujikite katika ukuaji wa uchumi mpana na jumuishi wenye kupunguza umaskini kwa kiwango kikubwa na kuwanufaisha watu wengi hasa wanaoishi katika mazingira ya pembezoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili jitihada za ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, ufufuaji wa bandari na meli kubwa kubwa na ndogo kwa kweli umeweza kuonyesha ni jinsi gani uchumi ambao tunataka uwe unakuwa jumuishi. Lakini reli hii ya mwendo kasi ambayo tunaijenga inaambatana pembezoni mwake na barabara ambayo inatumika kwa ajili ya ujenzi wa reli hii. Barabara hii imeweza kufikia vijiji vingi ambavyo awali kabla ujenzi wa reli hii vilikuwa havifikiki. Vijiji hivi ni muhimu sana katika uzalishaji wa bidhaa za mashambani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba Waziri wa Fedha na Mipango ashirikiane na Wizara nyingine kama za Ujenzi na Uchukuzi kuona barabara hii inaenda kuwa ya kudumu, kwasababu tukiiacha barabara hii tutakuwa tumepoteza kitu kikubwa na cha thamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kutoka hapa Makutopora kwenda Kilosa ni pa fupi sana ukipita kwa barabara hii ya SGR ambapo awali ilikuwa uende mpaka Dumila. Lakini kutoka Kilosa kwenda Morogoro pamekuwa karibu sana kwa kutumia barabara hii, lakini miaka minne ya nyuma ulikuwa huweze kufikia baadhi ya vijiji hata kwa pikipiki lakini kwasababu za ujenzi wa Reli hii vijiji vyote vinafikika, na unaweza kuona mabadiliko chanya katika maisha ya mtu mmoja mmoja katika vijiji hivi kwasababu ya uwepo wa barabara hizi ambazo lengo lake si kurahisisha usafiri wa wananchi ilikuwa ni ujenzi reli hii. Kwa hiyo tuiangalie barabara hii kwa jicho la kipekee kwa nia ya kubadilisha maisha ya wananchi wetu katika maeneo ya pembezoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia hatuwezi kuepuka kilimo. Kilimo tunasema ni uti wa mgongo kilimo tunazungumzia kwamba ndiyo dhana ambayo inaweza kututoa katika umaskini, na kilimo ndicho kitu ambacho kinaajiri watu wengi kupita kiasi, lakini tuna changamoto ya masoko. Masoko haya ambayo tunayazungumzia mengine yanatokana na uzalishaji ambao hauzingatii mahitaji ya soko, lakini kuna maeneo ambayo kwa Sheria ama kwa taratibu ambazo tuliziweka ni kwamba zinamnyima fursa Mkulima kuwa na soko la uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano katika Jimbo la Mikumi kilimo cha miwa ndio uti wa mgongo. Katika bonde lile kuna zaidi ya tani laki nne kila mwaka zinaharibikia mashambani kwasababu mnunuzi ni mmoja ambaye ame- monopolize soko la Miwa. Miwa hii ambayo inaharibika tunaweza tukai - convert kwenda kwenye tani 40 elfu za sukari ambazo ndizo tunazoagiza kila mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mzalishaji huyu ambaye alikuwa anapaswa kutafuta suluhisho la kudumu la wakulima hawa kuangalia jinsi gani anaenda kununua miwa yao yeye anapewa kibali na Serikali kwa ajili ya kuagiza Sukari ambayo ni rahisi kuingiza kuliko kuzalisha, kwa hiyo tunajikuta kama Serikali tunaumiza wakulima wetu wenyewe badala ya kuwa - encourage ama kuwapa incentive ya kuzalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunataka tumkomboe mkulima kikweli kweli basi ni lazima tuhakikishe tunamuwekea mazingira rafiki ya uzalishaji, lakini pia kumuwekea mazingira ya uhakika wa soko. Kama mzalishaji huyu ameshindwa kununua miwa hii basi tuanze kuangalia utaratibu wa kuwawezesha wananchi kupitia vyama vya Ushirika ama mmoja mmoja kupitia Benki ya Kilimo kuanzisha viwanda vidogo na vya kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeishi nchi ya Asia kwa zaidi ya miaka minne, huwezi kukuta viwanda vikubwa vya sukari. Viwanda ni vidogo vidogo na watu wanashiriki katika kilimo cha miwa lakini uzalishaji wa sukari ya miwa na viazi katika uwezo mdogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika hili, ili tuongeze mnyororo wa thamani na kukuza stadi za uzalishaji wa bidhaa za kilimo basi ni vyema tukajikita katika taasisi zetu za fedha kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wakati kujiingiza kikamilifu katika uzalishaji wa sukari katika maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine kubwa kuliko yote ni uboreshaji wa miundombinu. Tunapozungumzia miundombinu maeneo mengi ya uzalishaji wa kilimo ni mabonde na maeneo haya wakati wa masika hayafikiki. Nchi za Asia zimepata kuendelea kwasababu kwanza walihakikisha barabara zao zote ambazo zinaenda katika maeneo ya uzalishaji zinapitika mwaka mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi kama China ambayo tunaweza kuichukulia kama model ya maendeleo yetu ni kwamba wenyewe walijikita katika kuhakikisha barabara zote zinapitika kwa changarawe kwasababu uwezo wa Lami hawakuwa nao. Sisi tunaweza tuka - copy model hiyo ya maendeleo kwa kuhakikisha kwamba barabara zetu zinaweza zikapitika katika maeneo yote uzalishaji wa kilimo na kuunganisha na barabara kuu. Hilo litapunguza gharama za uzalishaji lakini litafikisha bidhaa masokoni katika bei ambayo inauhalisia na kuongeza ushindani wa bei ya soko na kuongeza tija kwa maisha ya mkulima mmoja mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia taasisi zetu za fedha ni lazima zisiseme tu kwamba zinashiriki katika kumwezesha mkulima bali pia zionekane zikifanya hivyo. Riba yetu bado ni kubwa na riba sio rafiki kwa wakulima wetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni dakika sita tu nimeweka stop watch hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo katika hili tunaweze kuangalia ni jinsi gani tunaweza kuweka sera rafiki kwa taasisi zetu za fedha ili kuhakikisha kwamba zinapunguza Riba lakini pia zinamwezesha mkulima mmoja mmoja katika kuongeza tija ya mazao yake pamoja na kuongeza uzalishaji wa bidhaa za kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, na katika hili kwakweli hatuwezi kuacha utalii pembeni. Sekta ya utalii ni muhimu mno na ni uti wa mgongo. Kwa Jimbo langu la Mikumi sekta ya utalii imeajiri wengi, lakini tafiti na stadi mbalimbali zinaonyesha kwamba ni asilimia 20 tu ya watalii wanaokuja Tanzania ambao wanarudi tena, kiasi hiki ni kidogo, na hasa ukizingatia kwamba utalii ni moja ya maeneo muhimu katika ukuaji wa uchumi wetu. Kwa hiyo nilikuwa naomba Serikali iangalie ni vitu gani ambayo vinafanya watalii wasirudi hapa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tuangalie tena jukumu la Bodi ya Utalii na taasisi zake ambazo zina jukumu la kuhakikisha kwamba mtalii anakuja Tanzania. Wanaboresha huduma zao wanatangaza vivutio vyetu lakini pia wanashirikisha wananchi wetu katika suala zima la sekta hii ya utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, na katika hili miundombinu katika mbuga zetu na hifadhi zetu hatuwezi kuliweka kando. Pale Kilosa ama katika Mbuga ya Mikumi kuna geti moja tu la kuingilia mbugani; lakini tunasema tuna reli ya SGR ambayo inakuja mpaka Kilosa. Unaposhuka Kilosa kwa SGR maana yake unaenda kuongeza idadi ya watalii ambao wangependa kuja Mikumi lakini mtalii huyu angeweze kuja akaingilia katika geti la hapa Tindiga ama Mabwelebwele ama Kilangali ambako ni kilomita 15 kutoka stesheni ya reli ya SGR. Sasa kwa sababu ya kutokuwa na geti pale na kwa kutokuwa na barabara ya kuingilia pale mbugani unamsababisha mtalii huyu atembee kilometa zaidi ya 120 kabla hayakutana na geti.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunapozungumzia miundombinu ni pamoja na kurahisisha usafiri kwa watalii lakini pia kumpunguzia muda na kuongeza thamani ya fedha zake kwa kulinda muda wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo si kwa umuhimu wake ni suala zima la kwanini tulishindwa katika mipango yetu ya maendeleo huko nyuma. Mipango ya awali ilishindwa kufanikisha malengo yake mengi ilhali Serikali ilikuwa imedhamiria katika ukuzaji wa viwanda kama kipaumbele chake cha miaka mitano iliyopita.

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Mheshimiwa Rais imefungua maeneo mengi ambayo yanahitaji mjadala wa kina. Moja ambalo ni kubwa mazingira yetu ya uwekezaji si rafiki kwa sababu hatuangalii Watanzania kama sehemu muhimu ya wawekezaji, lakini pia masharti yetu yakufungua biashara yamekuwa magumu mno. Tuna taasisi nyingi ambazo mfanyabiashara ama Mwekezaji anapaswa kuwasiliana nazo kabla ya kufungua biashara yake; matokeo yake uwekezaji umekuwa ni wa gharama kubwa mno Tanzania ukilinganisha na washindani wetu katika maeneo ya Maziwa Makuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika uwekezaji Watanzania wote lazima wapewe kibaumbele bila kujali maeneo yao ya kijiografia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiangalia mpango wa maendeleo haujazungumzia diaspora. Diaspora ni eneo kubwa na muhimu sana katika uwekezaji wa ndani. Ninaamini kabisa hapo awali tulishindwa kutumia kikamilifu rasilimali watu hasa ndugu zetu wa diaspora ambao wana skills lakini pia wana access ya mitaji katika maeneo ambayo wapo. Naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango anapohitimisha hotuba yake atuelezee ama alielezee Bunge lako ni jinsi gani wanaenda kuangalia Watanzania kama significant players katika uwekezaji, hasa hawa ndugu zetu za diaspora.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara nyingine nishukuru kiti chako kwa kunipa nafasi hii ya kuzungumza mbele ya Bunge lako Tukufu likiwa limeketi kama kamati. Kimsingi kwa sababu muda hautoshi, naomba nijielekeze zaidi kwenye sekta ya utalii. Sekta ya Utalii katika nchi yetu bado hatujaitendea haki, kwa sababu pamoja na kwamba tuna vivutio vingi vya asili, lakini bado tumeshindwa kuhakikisha kwamba sehemu kubwa ya vijana wetu hasa ambao wanaweza wakaenda kwenye elimu ya kati ama vyuo vyetu vya VETA wakapata elimu ambayo inaweza kuwasaidia kujikita katika tasnia ya utalii na kujiajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi nimepata nafasi ama bahati ya kuishi kwenye nchi mbalimbali zinazotegemea sana utalii. Gharama ya utalii kwetu ni kubwa mno na hata tafiti zinaonesha kwamba kati ya watalii mia moja ambao wanatembelea Tanzania ni 20 tu ambao wanarudi. Idadi hii ndogo mno, ni lazima sasa kama Serikali tujikite kutafuta sababu kwa nini watalii hawa mia hawarudi wote ama hawawi mabalozi kwa wengine kwa ajili ya kuvutia vivutio vyetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo naomba kujikita ni eneo la kilimo; tumekuwa na slogan nyingi; kilimo kwanza, kilimo uti wa mgongo, lakini kimsingi Mtanzania hahitaji hizi kauli mbiu, kilimo kwake ndio kila kitu, amezaliwa anategemea kilimo, amesomeshwa na kilimo, anaishi kwa kilimo, haitaji mtu kumpa kauli mbiu, anahitaji mazingira rafiki ya yeye kujikita kwenye kilimo. Mazingira ambayo tumemwekea sasa hivi si rafiki. Naomba nitumie mfano wa wakulima wa miwa katika Bonde la Kilombero, nilizungumza mwanzo kwamba kati ya tani 900,000 ambazo mkulima wa miwa anazalisha pale Kilombero, ni tani 600,000 tu ambazo zinaweza kununuliwa na kiwanda pekee cha Ilovo, tani 300,000 zinaharibikia mashambani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazingira hayo bado tunasema miwa ni zao la kimkakati, lakini ni zao la kimkakati hakuna mazingira wezeshi ya kuhakikisha kwamba mkulima wa miwa ana soko la uhakika. Matokeo yake sasa hivi watu wamekata tamaa, pendekezo langu naomba Serikali iwe inaagiza sukari kwa sababu jukumu la kuagiza deficit anaachiwa mzalishaji ambaye ndiye mwenye jukumu la kuhakikisha ananunua miwa ya kulima; na kwa kuwa sukari ya kuagiza ni bei rahisi ukilinganisha na sukari ya kuzalisha; mzalishaji huyo wa sukari badala ya kum-encourage mkulima kuzalisha amekuwa kikwazo kwake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, naomba Serikali ihakikishe kwamba inaenda kumsimamia Ilovo kukamilisha upanuzi wa kiwanda ili kuhakikisha kwamba mkulima ana soko la uhakika…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa kengele imegonga.

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wananchi wa Mikumi nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze mchango wangu kwa kumnukuu mwanafalsafa Frantz Fanon ambaye anasema kwamba kila kizazi kina jukumu la kihistoria. Ni jukumu la kizazi hicho kutafuta na kulifahamu jukumu lake. Aidha, ni jukumu la kizazi hicho kubeba hilo jukumu na kulitekeleza ama kulisaliti. (Makofi)

Mheshimwia Naibu Spika, Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli akisaidiana na Makamu wake ambaye sasa ni Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, wanaingia kwenye historia ya nchi yetu kama wazalendo na viongozi ambao walitambua jukumu lao la kihistoria, walilibeba na walilitekeleza. Maamuzi ambayo walichukua kuongoza Taifa letu katika vita dhidi ya wahujumu uchumi, vita za kiuchumi duniani, kurejesha imani ya wananchi kwa Serikali yao, kurudisha nidhamu ya utumishi Serikalini, ujenzi wa miundombinu ya barabara ya reli, ununuzi wa ndege, ujenzi wa vituo afya na miundombinu ya elimu, ni mambo ambayo yatawafanya waendelee kukumbukwa kwa vizazi vingi vijavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ameshaonyesha dira yake, ameonyesha azma ya Serikali yake katika kutekeleza miradi yote ya kimkakati na miradi ya kimaendeleo. Azma yake ni njema na azma hii sisi kama Bunge tunapaswa kuiunga mkono kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni jukumu la Bunge lako kuhakikisha kwamba kila mmoja ndani ya Bunge hili anatimiza jukumu lake la kihistoria katika kuhakikisha kwamba tunaenda kuisaidia Serikali chini ya Rais Mama Samia Suluhu Hassan kutekeleza majukumu yake, lakini pia kuhakikisha kwamba anafanya kila linalowezekana ili Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi itekelezwe. Ni jukumu la Bunge lako kuhakikisha kwamba tunaenda kutoa kila support ambayo Rais wetu anastahili ili nchi yetu itekeleze yale yote ambayo tumewaahidi wananchi katika ilani ya chama chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu siyo kisiwa, ni sehemu ya ulimwengu mkubwa ambao unaingia sasa kwenye mapinduzi ya nne ya viwanda. Mapinduzi haya si lele mama, mapinduzi haya yanaenda kuwa katili kuliko mapinduzi yoyote ya viwanda. Tumejiandaaje kuingia katika uchumi shindani na shirikishi katika mazingira ambayo bado vijiji vyetu vingi havijafikiwa na umeme lakini pia tuna tatizo kubwa la mawasiliano? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, katika Jimbo la Mikumi katika vijiji 57 vya Jimbo langu, ni vijiji 23 tu ambavyo unaweza kupata mawasiliano ya simu ya uhakika. Maeneo makubwa ya Kata za Uleli Ng’ombe, Vidunda, Masanze, Kivungu, Kisanga na Tindiga hayana mawasiliano ya uhakika. Hata kwa upande wa umeme, ni vijiji 17 tu katika vijiji 57 ambavyo unaweza kupata umeme katika Jimbo la Mikumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali hii, tunapoenda katika uchumi shindani na shirikishi, hatuwezi tukahakikisha watu hawa wanashiriki kikamilifu katika uchumi huu wa mapinduzi ya nne ya viwanda bila kuhakikisha kwamba tunawaunganisha wananchi hawa kupitia mawasiliano na pia kuhakikisha kwamba tunawapa umeme. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, mengine ambayo…

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa. Kengele imegonga.

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala Za Mikoa Na Serikali Za Mitaa
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine tena nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa. Ofisi au Wizara hii ni muhimu san ana tunajadili bajeti ambayo imebeba hatma ya wengi kwenye nchi yetu. Kwa umuhimu wake ina mafungamano ya karibu san ana Wizara nyingi na Taasisi nyingi za Serikali.

Mheshimiwa Spika, tunapojadili Wizar aya Ofisi ya Rais Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa kuna kilimo humo ndani, kuna afya humo ndani, kuna uvuvi humo ndani, kuna barabara humo ndani, kuna afya na vitu vingi humo ndani. Kimsingi kwa muundo wa Ofisi hii ya Rais Tawala za Miko ana Serikali za Mitaa ndiyo ambayo inashuka mpaka chini kwa wananchi. Kwa hiyo, tunapoizungumzia Serikali kwa mwananchi wa kawaida tunazungumzia Halmashauri za Vijiji, Mtendaji wa Kijiji na Mwenyekiti wa Kijiji ambaye anaangukia katika Wizara hii. Kwa hiyo, tunazungumzia bajeti muhimu sana na utendaji kazi wa Wizara hii pamoja na majukumu yake kama yalivyoainishwa kutoka ukurasa wa tisa mpaka wa 15 inaonesha uzito na dhamana ambayo inaangukia katika Wiara hiyo.

Mheshimiwa Spika, wananchi wetu hawakumbani na Serikali mara kwa mara. Mwananchi wa kawaida kule kijijini anakutana na Seriali pale ambapo anahitaji huduma katika kituo cha afya, katika Ofisi ya Mtendaji Kata, katika Ofisi ya Afisa Elimu Kata ama Mwalimu Mkuu na hawa wote wanaangukia katika Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kule kwetu kwenye majimbo yetu ambako tunatokea, wananchi wana imani kubwa sana na Serikali hii lakini hiyo haiondoi ukweli kwamba kuna nakisi ya imani kwa Serikali za vijiji ama kwa kiingereza tunaweza tukasema kwamba public trust deficit kwa wananchi kitu ambacho kinatuweka kwenye dilemma kwa kiasi kikubwa. Kuna migogoro mingi ya ardhi, viwanja, mashamba yanagawiwa bila kufuata taratibu wala sheria. Kuna changamoto kubwa ya watu kuonewa kule bila kufuata sheria lakini hayo yote ukija kufuatilia kwa makini yanatokana na uwezeshwaji wa hawa watu. Je, wana elimu ya kutosha kulingana na majukumu ambayo wameyaomba? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu wamechaguliwa katika nafasi zao kama Wenyeviti wa Serikali za Vijiji. Je, wamepata seminar ya jinsi ya kuongoza watu, sheria ambayo inaongoza mamlaka za vijiji na vitu vingine. Kwa hiyo, vitu hivi vinatusababisha katika migogoro mingi ambayo tungeweza kuitatua kama tungeangalia jinsi gani ya kuwawezesha hawa walau kuwapa elimu.

Mheshimiwa Spika, lakini pia hata uwezeshwaji wa posho. Imekuwa shida sana kwa Wenyeviti wetu wa vijiji kwa hiyo naomba wakati tunapitisha bajeti hii tuangalie ni jinsi gani tunaenda kuwaangalia hawa watu ambao ni muhimu sana. Mheshimiwa Chiwelesa amezungumzia kuhusiana na jinsi gani tumejiandaa na wimbi kubwa la watoto ambao ni graduates wa elimu bila malipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka huu watoto ambao wameingi akidato cha kwanza ni 800,872 ukilinganisha na watoto ambao wameingia darasa la kwanza 1,500,000. Sasa udahili wa watoto hawa ambao wanaingi akidato cha kwanza 800,000 haufanani san ana hawa watoto ambao wameingia darasa la kwanza 1,500,000. Kwa hiyo, ni rai yangu kwa Wizara ya Ofisi ya Rais TAMISEMI kuangalia ni jinsi gani tunajiandaa na hii influx kubwa ya watoto ambao ni zao la elimu bila malipo ambalo linatokea 2022 ambapo ni mwakani tu. Kwa hiyo, tuna bajeti moja tu ya kujadili lakini bajeti ya 2022 tutakuwa na kazi kubwa ya kuangalia watoto hawa wanaenda wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo nilikuwa naomba kutoa rai Ofisi za Vijiji na Kata uendeshaji wake unategemea sana asilimia 20 ya ruzuku ambayo inatoka Serikali Kuu. Lakini wote sisi ni mashahidi vijiji vimekuwa vikihangaika jinsi ya uendeshaji wa ofisi zao lakini hata kata pia na kuna kata ambazo ziko mbali sana kimiundombinu na ofisi za Halmashauri lakini Watendaji hawa Kata, Watendaji wa Vijiji hivi wanaitwa kwenye mikutano inabidi wahangaike watoe hela zao za mifukoni lakini kuna fedha za ruzuku za Serikali Kuu ambayo asilimia 20 inapaswa kwenda lower level.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni rai yangu kwa Ofisi ya Rais TAMISEMI kuangalia namna bora ya kuhakikisha fedha hizi asilimia 20 za ruzuku zinaenda kule katika ngazi za vijiji na kata kurahisisha uendeshaji wa ofisi hizi ili kuondoa manung’uniko kwa watendaji wetu ambao ni muhimu sana katika utekelezaji wa maagizo na maelekezo ya Serikali Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo nilikuwa naomba niunge mkono hoja ya Wabunge wenzangu ambao wametangulia kuhusiana na suala zima la barabara. Tunazungumzia kuhusiana na suala zima la uzalishaji wa viwandani lakini kimsingi unapozungumzia uzalishaji wa viwandani unazungumzia kilimo na katika majimbo ya pembezoni kama Mikumi, kilimo ndiyo uti wa mgongo na kuna maeneo mengi ya uzalishaji na ninaomba kupitia Bunge lako nitoe mfano wa Kata moja inaitwa Vidunda.

Mheshimiwa Spika, kata hii ni kilometa 5 tu kutoka pale Kidodi ambapo ni barabara kuu lakini ndiyo Kata ambayo inalisha bonde lote la hapa chini Ruaha, Mikumi, Kidodi mpaka Morogoro na Dar es salaam. Kilometa hizi tano huwezi kwenda kwa gari. Tangu nimezaliwa nilikuwa nashuhudia watu wakishusha mizigo na matenga toka enzi hizo mpaka sasa. Hali hii inafanana sana na kata nyingine za pembezoni kama Malolo, Ulening’ombe, lakini kuna kata za chini kama Tindiga ambao ni wazalishaji wakubwa sana wa zao la mpunga. Jan anilirusha clip kwa Mkurugenzi Mkuu wa TARURA na Maafisa wengine wa Wizara ya Ujenzi waone hali ilivyo. Ni umbali wa barabara kilometa mbili haipitiki hata kwa pikipiki, hali ni mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia uchumi wa viwanda tunazungumzia bidhaa za kilimo, unapozungumzia bidhaa za kilimo unazungumzia suala zima la uzalishaji, usafirishaji, na ufikishaji wa mazao sokoni. Unapomnyima barabara mtu ambaye kazi yake kubwa ni kuzalisha kilimo maana yake tunahujumu uchumi wetu sisi wenyewe lakini unapandisha gharama katika uzalishaji na mwisho wa siku unampandishia gharama mlaji. Tunazungumzia hali ni ngumu, hali ni ngumu kimsingi inatokana na gharama ya bidhaa za kilimo masokoni ambayo tungeweza kuipunguza kama tungeweza kuboresha miudombinu. (Makofi)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Dennis Londo.

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. Nashukuru. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hotuba ya bajeti na ninaomba niaze kwa kuchangia bajeti kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa yale yote ambayo yametokea tangu Bunge hili lilipoanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niishukuru Serikali ya Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameifanya katika kipindi hiki kifupi lakini kubwa kuliko yote ni kuendelea kutunza imani ya Watanzania kwa Chama cha Mapinduzi, kutunza imani ya Watanzania kwa Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi yamefanywa katika kipindi hiki kifupi lakini kwa uchache suala la kupeleka fedha za ujenzi wa miundombinu ya shule hasa maabara na kuongeza vyumba vya madarasa katika Halmashauri mbalimbali wananchi wa wanashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia upelekaji wa shilingi milioni 500 kwa kila Jimbo kimsingi imeweza kwenda kujibu kero nyingi hasa za miundombinu ya barabara na Mikumi tumeamua kupeleka milioni hizi 500 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Mto wa Ruhembe, mto ambao umeuwa watu wengi, wananchi wengi katika lile eneo lakini ni daraja ambalo kimsingi ni la kimkakati katika uzalishaji wa miwa na usafirishaji katika kiwanda cha Illovo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, daraja hili linaenda kupunguza gharama ya uzalishaji kwa wakulima pia usafirishaji wa mazao yao kutoka mashambani katika Kata za Mikumi, Kidodi, Ruhembe, Ruaha na hata vidunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hotuba nzuri ya bajeti ambayo imejaa ubunifu mkubwa lakini pia inaongozwa na uzalendo wa hali ya juu, hotuba ambayo imechukua maoni ya Wabunge kikamilifu ni hotuba ya bajeti imeonesha uzalendo katika kulinda viwanda vyetu vya ndani na bidhaa ambazo zinazalishwa na viwanda vyetu vya ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupunguza tozo na kodi mbalimbali hili siyo tu kwamba linavutia wawekezaji kuja kuzalishia hapa ndani lakini linaenda kuongeza ajira na linaenda kuamsha uwekezaji wa ndani na hivyo kuboresha uchumi wetu katika namna mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii pia kuipongeza Serikali kwa ubunifu na kubuni njia bora zaidi ambazo hazimsumbui mwananchi lakini ni katika kuongeza tax base hasa kupitia kukusanya kodi ya majengo na viwanja kupitia simu lakini pia kupitia LUKU.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya principal za kodi ni kupunguza gharama ya ukusanyaji pia kuongeza kiasi cha ukusanyaji, shida kubwa ya makusanyo yetu ya kodi ni kwamba tunatumia gharama kubwa kukusanya kodi ndogo lakini pia kumsumbua yule mlipa kodi kiasi ambacho mlipa kodi anatakiwa kutumia mara nyingine shilingi 5,000 ama Shilingi 10,000 kwa ajili ya kwenda kulipa shilingi 7,000.

Kwa hiyo, hali hii inapelekea wananchi wetu wengi kutojitoa kikamilifu katika kutimiza majukumu yao ya kiraia hasa katika eneo hili la kulipa kodi. Kwa ubunifu huu naamini kabisa wananchi watajitoa kimasomaso katika kuunga mkono jitihada za Serikali katika kutimiza wajibu wao wa kizalendo katika kulipa kodi ambayo ndiyo msingi wa ujenzi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie nafasi hii pia kuishukuru Serikali kwa maamuzi ya upanuzi wa kiwanda cha sukari cha Kilombero, upanuzi huu siyo kwamba unaenda kutatua tatizo la soko la miwa kwa wakulima wa Kilombero, unaenda kutatua tatizo la sukari katika nchi yetu ya Tanzania. Uwekezaji huu mkubwa ambao haujapata kutokea katika ukanda huu wa Afrika siyo tu ni mfano wa kuigwa kwa sababu unaenda kuongeza ajira ya wananchi wetu lakini unaenda kupanua soko la ajira la vijana wetu ambao wanamaliza shule hawana kazi ya kufanya ama ajira ambayo ina tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo linaenda kuongeza kipato cha vijana wetu lakini inaenda kuwawezesha wananchi wetu uwezo wao wa kuweka akiba ambayo inaweza kuwasaidia katika kuwekeza katika maeneo mbalimbali na hivyo kupambana na jitihada za kupiga vita umaskini, haya yote yatachochea uchumi wetu ili ukuwe kwa kasi, hata hivyo naomba maboresho machache yafanyike:

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja; wananchi wetu hasa wa pembezoni siyo tu wanatumia simu kama chombo cha mawasiliano lakini kwao ni muhimu sana, wengi siyo kwamba wanatumia kwa sababu wana fedha, kwa hiyo hii tozo kwa wananchi naomba tuwe na kima cha chini. Kwa mfano, unaweza kusema mwananchi yoyote consumption yake ama matumizi yake ya simu hayazidi shilingi 5,000 huyo hatakiwi kutozwa, lakini zaidi ya 5000 pengine ndiyo atozwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili litasaidia sana wananchi wetu hasa wenye kipato cha chini kuendelea kuhamasika kutumia mawasiliano kwa ajili ya jitihada za kupambana na hali yao. Pia naomba Wizara ya Fedha iangalie njia bora za kupanua wigo wa kodi (tax base) katika kuangalia haya makampuni ambayo yanafanya biashara kimtandao wanaita e-commerce. Biashara nyingi sasa hivi zimeamia katika mfumo wa biashara mtandao, biashara hizi zinafanywa kwa kiasi kikubwa lakini hatujui VAT wanalipia wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, makampuni makubwa yanafanya biashara hizi za mitandaoni tunaona Amazon, tunaona Alibaba na wengine, mtu anaponunua bidhaa kutoka kwenye makampuni haya VAT analipa wapi, lakini hata corporate tax inaenda wapi? Nani anatoza? Kama tunaweza kuangalia eneo hili tunaweza kuongeza uwezo wetu mkubwa wa ukusanyaji wa kodi na hivyo ku-contribute katika miradi yetu ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili naomba nizungumzie Tanzania kwa Geografia lakini kwa historia hegemonic power, hegemonic power katika ukanda wetu, lakini hegemonic power katika siasa za Afrika. Ni wakati sasa umefika kwa Serikali yetu, Wizara zetu kuzungumza kwa pamoja kuangalia nafasi yetu, influence yetu katika Ukanda wa Maziwa Makuu lakini katka Ukanda wa Kusini na Bara zima la Afrika. Katika hilo tuangalie ushiriki wetu katika mashirika ya Kikanda Kama SADC, kama East Afrika, Cooperation lakini pia katika African Union. Je, nafasi yetu ni ile ile kama tumelegalega ni wapi? Nini kifanyike ili Tanzania irudi katika nafasi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili ni lazima tutumie fedha, Wizara ya Fedha lazima tushirikiane na Wizara ya Mambo ya Nje kuhakikisha kwamba zile business center ambazo tulikuwa nazo lazima zirudi na tuzitangaze kikweli kweli. Pia tusitengemee sana watumishi wa Mambo ya Nje katika Balozi zetu kunadi vivutio vyetu, kunadi sekta mbalimbali za uwekezaji. Wakati umefika sasa wa kampuni mashirika na taasisi nyingine kuanza kuajiri watu wao na kuwa station katika Balozi zetu, Wizara ya Mambo ya Nje iwe ni coordinator ama mratibu wa hawa watu kutoka Bodi ya Utalii na kituo cha uwekezaji lakini pia Taasisi mbalimbali ambazo zinapaswa kutangazwa huko nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ilivyo sasa wanadiplomasia wetu ambao wanaenda kwenye Balozi zetu ndiyo tunawatumia kufanya kazi zote ikiwemo kutanganza utalii wetu kitu ambacho naamini tumeona matokeo yake na hatuhitaji mwalimu wa kutueleza wapi ambapo tumeangukia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia kilimo ni uti wa mgongo na Bunge hili limejipa jukumu la ajenda la kufanya mapinduzi ya Kilimo. Kilimo hiki ambacho tunasema ni uti wa mgongo tunakichukulia poa kwa kiasi kikubwa, kilimo ni sayansi na kilimo kinagusa kuanzia natural, social na hata economics na ndiyo maana uwezi kuzungumzia uzalishaji bila kuzungumzia kilimo. Nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumteua ndugu yetu Prof. Mkenda kuwa Waziri wa Kilimo, yeye ni Mchumi na kwa sababu kilimo ni uchumi basi tunaamini kabisa anaenda kufanya mageuzi makubwa na mapinduzi katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza kuona ni jinsi gani kilimo chetu bado hatujakitendea haki kwa sababu hata sera zetu za maliasili, sera zetu za ardhi, za uwekezaji bado zinaji- contradict unapozungumzia sera yetu ya kilimo. Kwa hiyo nilikuwa naomba kuwe na mafungamano kati ya sekta ya kilimo na sekta nyingine, tatizo hapa unakuta ile concept ya ceteris paribus kwa Wachumi, ambayo inaanzia kuangalia kilimo na kuangalia uchumi wetu kutokea kwenye jicho la viwanda na huduma. Lile linatuonesha ni jinsi gani tunakosea ni lazima hiyo concept ya ceteris paribus ianzie kuangalia kilimo na kuangalia kwa sababu kilimo ni uzalishaji lakini kilimo kinaenda mpaka kwenye ulaji. Tuangalie sheria zetu zinaangalia vipi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza kuona kwamba hata mikopo ya benki inatolewa katika rate ambazo mtu anatakiwa kulipa kila mwezi, mkulima wa miwa ambaye anavuna kwa season anawezaje kulipa kila mwezi? Lakini mkulima huyu ukimwambia alipe baada ya msimu wa mauzo anaweza akafanya. Unaweza ukampa mortgage ya nyumba unaweza ukampa mortgage ya mashine na anaweza akatumia vitu hivyo na akalipa kwa msimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja nashukuru sana (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza kabisa, ningependa kumshukuru sana Rais wetu mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Pia, yeye akiwa kama Rais wetu tunaona nia njema ambayo anayo kwa nchi yetu kwa kumpa maelekezo CAG, kwamba afanye uchambuzi wa kina, asipepese macho, aandike ripoti yenye kueleweka ili tuijenge nchi yetu. Ripoti hii ya CAG ambayo tunaiangalia leo sisi kama Wabunge tunapaswa kutimiza jukumu letu la kuisimamia na kuishauri Serikali kwa niaba ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mengi ambayo yameelezwa ndani ya Ripoti ya CAG, lakini mawili makubwa ambayo ningependa kuyaangalia; kwanza ni uwekezaji wenye tija, lakini pia kuangalia sehemu ya matumizi. Tunazungumzia Mitaji ya umma, kwangu mimi moja ya mitaji mikubwa ya umma ni nguvu kazi, ni rasilimali watu. Katika ripoti hii ya CAG, tunaona kuna watoto 53,755 ambao waliandikishwa kuanza darasa la kwanza kati ya mwaka 2018 na 2021 ambao hawakumaliza elimu ya msingi. Tunafahamu nchi yetu inawekeza fedha nyingi sana kwenye elimu ya watoto wetu, kile ambacho kinaitwa elimu bure sio bure, mlipakodi wa nchi hii analipa fedha nyingi kama capitation kwa ajili ya watoto wetu waende shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto hawa ambao wanaandikishwa darasa la kwanza hawafiki la saba, maana yake uwekezaji mkubwa ambao unafanywa na nchi hii na walipa kodi wa nchi hii unapotea bure. Ningeomba kwa unyenyekevu kabisa, Bunge na Serikali kuchukulia ripoti hii kwa umakini mkubwa. Watoto 53,755 si idadi ndogo, watoto hawa wanaondoka katika mfumo katika elimu ya msingi. Tunapozungumzia elimu ya msingi huko ndiko tunapojenga Taifa, zile manners ndogondogo, raia mwema anatakiwa ku-behave vipi, kuheshimu wakubwa na wadogo, kuheshimu mamlaka, zote zinafunza katika katika shule ya msingi na ndiyo maana inaitwa msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapokuta watoto hawa wanaondoka katika mfumo huu wa elimu ya msingi, maana yake sio tu tunapoteza Watoto, lakini ni suala la security ya nchi yetu. Watoto hao wako wapi? Wanafanya nini? Wamekwenda wapi? Nani ambaye anasumbuka kujua watoto hawa wapo wapi? Watoto 53,755 si watoto wachache na hili ni suala la security ya nchi yetu na ni lazima tulichukulie kwa uzito ambao unastahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia kuwekeza kwa wananchi wetu, kama ilivyo kwenye elimu tunavyowekeza kwa hawa Watoto, lakini pia Serikali imekuja na mpango maalum kabisa wa kuwezesha makundi maalum ya vijana, wanawake na walemavu. Fedha ambazo zinatengwa kwa ajili ya makundi haya, kuyakwamua katika hali ya umaskini ni fedha nyingi sana ukilinganisha na mahitaji ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukua bajeti yetu ya nchi, fedha ambazo tunalipa madeni, fedha ambazo tunalipa mishahara ya watumishi wa umma, fedha kidogo ambayo inabaki kwa ajili ya maendeleo, hatuna anasa ya kupoteza hata shilingi tano. Hatuna anasa hiyo, kwa sababu tunapambana kukusanya hela ambayo inaishia kwenye mahitaji ya lazima, hatuna fedha za kufanyia anasa. Unaposikia fedha zinapotea, fedha za umma zinapotea, inaumiza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, hesabu ambazo CAG amewasilisha kati ya mwaka 2020/2021, zaidi ya bilioni 75 za mikopo zilitoka katika mwaka huu mmoja wa bajeti. Katika hizo zaidi ya bilioni 47 hazijarejeshwa. Fedha hizi ni nyingi sana, fedha hizi zinaweza zinaweza kubadilisha maisha ya watu wengi katika nchi hii, kutengeneza barabara za vumbi kuwa za changarawe kilometa za kutosha; kutengeneza lami nyepesi, kutengeneza shule za msingi, shule za sekondari, zikakarabati vyuo vya ufundi, zikapeleka hata vifaa tiba katika hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaposikia kuwa fedha hizi zimepotea na hatuoni jitihada za kweli za kuzikusanya fedha hizi, Bunge lako haliwezi kunyamaza. Ningeomba kwa namna ya kipekee, kwanza kabisa nishukuru Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kuna jitihada za wazi ambazo imezichukua kuhakikisha kwamba wanaenda kusimimamia suala zima la utoaji wa mikopo lakini pia ukusanyaji wake. Ni hatua nzuri lakini jitihada pia zifanyike, kuhakikisha kwamba zile fedha ambazo zimetoka kimichongo wahusika wanachukuliwa hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kutoa mkopo ni suala moja na suala la haki kwa makundi ambayo yanastahili kupata mkopo ni suala lingine. Wote ni mashahidi, juzi tulikuwa na mjadala mrefu sana kuhusiana na haki ya mikopo kwa wale ambao wanastahili elimu ya juu. Vijana wetu ambao wameomba mikopo na wanastahili kupata mikopo lakini hawajapata mikopo, hali si tofauti kwa mama zetu kwa vijana na walemavu katika halmashauri tunazotoka. Kuna makundi mengi ambayo yanastahili kupata mikopo hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la uwazi kwenye ugawaji wa fedha hizi, linafanya makundi mengi ambayo yanastahili kupata fedha hizi wasizipate. Matokeo yake, Wabunge na Madiwani wamekuwa wahanga wa lawama kutoka kwa makundi haya na wenyewe wanabakia kulalamika kwa sababu hata ushirikishwaji wao si mkubwa ukilinganisha na majukumu waliyonayo hasa kuwa sehemu ya majibu ya changamoto kwa wananchi wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado naomba tena, nilizungumza mwaka jana, lakini nazungumza tena leo, rasilimali za halmashauri kutumika kwa uwazi, kutumika kwa haki na wale wote ambao wana haki ya kupata fedha hasa hizi za ten percent, basi wajulikane na taratibu zijulikane na wao wanufaika wapate fedha hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni mgawanyo wa fedha za asilimia 40 kwa 60. Kwa maana fedha za matumizi mengineyo, lakini pia fedha za maendeleo. Haiyumkiniki na sijadili busara ya hawa ambao walitengeneza vigezo hivi, lakini napata shida sana kuona kwamba kuna halmashauri ambayo inapata bilioni 30, inaambiwa itenge asilimia 40 kwa ajili ya matumizi mengineyo na halmashauri nyingine ambayo inapata milioni 800 ama bilioni moja na yenyewe inaambiwa itenge asilimia 40 kwa ajili ya matumizi mengineyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiziangalia hizi halmashauri, utakuta huyu ambaye anaingiza bilioni moja anajitahidi kulipa malimbikizo ya posho za watumishi wake, Wauguzi na Walimu, lakini utakuta huyu ambaye anapata bilioni 30 hajishughulishi na madeni ya watumishi wake. Pia, hata kupeleka fedha ambazo kisheria anapaswa kupeleka, kwa maana ya asilimia 10 hapeleki. Sasa, rai yangu kwa Serikali tujaribu ku-review mgawanyo wa fedha za matumizi mengineyo na fedha za maendeleo. Ikiwapendeza waone mgawanyo wa haki ili fedha nyingi ziende kutibu matatizo na changamoto ambazo Serikali kuu haiwezi kuzibeba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka nilizungumze hapa, ni suala la matumizi ya hii akaunti ya Amana. Ripoti inaonyesha kwamba kimekuwa ni kichaka cha kufichia fedha, lakini pia kufanyia ubadhirifu. Ni rai yangu, hatua zichukuliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile matumizi ya bakaa, fedha za bakaa kwa maana ya salio ambalo halmashauri inaingia nalo katika mwaka mpya wa fedha. Sheria ya Matumizi ya Fedha za Serikali za Mitaa zinaitaka halmashauri kuripoti kwenye vikao katika robo ya kwanza, lakini haizungumzii baada ya robo ya kwanza wanaripoti wapi na chenyewe ni kichaka cha matumizi mabaya ya fedha za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni rai yangu kwa Serikali na ikipendeza Bunge lako, ripoti ya matumizi ama kuchunguza akaunti za amana kwenye halmashauri zetu, lakini pia matumizi ya fedha za bakaa, ripoti hiyo ije kwenye Bunge tuijadili, kuona uhalali na matumizi sahihi za fedha hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia suala la uwekezaji wenye tija; halmashauri nyingi zimewekeza kwenye kile ambacho kinaitwa miradi ya kimkakati. Kwa mfano, stendi za malori na za mabasi lakini pia masoko. Pia, kuna halmashauri ambazo hazina wataalam wa kuandika maandiko, hazina utaalam huo, nyingi zimeishia kuwa wahanga wa mfumo wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kuna ajenda ya kuzisaidia halmashauri hizi, ikiwemo Kilosa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kukushukuru kwa kiti chako kuniona walau niwe miongoni mwa wachingiaji wa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora. Mimi naomba nichangie maeneo mawili; moja umuhimu wa dhamana ya utumishi katika Serikali yetu, lakini la pili nakisi ya imani ya wananchi wetu katika utumishi wa umma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli tunapozungumzia utumishi ni dhana ambayo inahitaji tafsiri mpya na hasa ukizingatia katika Taifa ambalo sekta binafsi imeajiri watu wengi ambao wanautumikia umma kiasi ambacho tafsiri ya utumishi umma inakosa maana ama inayumba yumba hapa katikati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utakuta watu wengi katika sekta binafsi wanatumikia umma kuliko watumishi wenyewe, utakuta watu wanapata shida katika ofisi ya umma kiasi ambacho wanapata huduma bora zaidi ambazo zilikuwa zinapaswa kubebwa na ofisi ya umma katika taasisi binafsi. Na ndio maana mfumuko huu wa mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yanahudumia watu yamechukua sana majukumu ya watumishi wetu Serikalini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilikuwa naomba watu ambao wanaomba ajira Serikalini na wale ambao watumishi walipoko Serikalini wajue dhamana waliyonayo, kwamba wao ndio kioo cha Serikali wanapoenda kuhudumia watu wao ndi Serikali, mwananchi anapofika katika ofisi ya umma kwenda kuomba ama kusiliza shida yake yule ndio Serikali, na dhamana hii ni ya muda ni lazima watumishi wetu wafahamu kwamba hatma ya nchi yetu ipo mikononi mwa mtumishi wa umma. Lakini watumishi hawa wanahitaji pia maandalizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni mjumbe wa Kamati ya USEMI ya Utawala na Serikali za Mitaa kilio kikubwa cha Chuo cha Utumishi pale Magogoni ni kwamba hawana wanafunzi wa kutosha ambao ni watumishi wa Serikali. Wanafunzi wengi ambao wanasoma katika chuo hiki wanalipiwa na wazazi na wengine wanatoka majumbani. Tunapoteza lengo la msingi la chuo hiki kuwanoa na kuwafundisha watumishi wa Serikali hili kuboresha utumishi wao kwa umma wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni ambalo nilikuwa naomba kuchangia ni dhana ya uzalendo; kwa wenzetu kazi za kujitolea ndio msingi wa uzalendo katika Taifa lao. Sisi hapa pia tuna vijana wengi ambao wanajitolea kwenye sekta mbalimbali hasa elimu, lakini vijana hawa ajira inapotoka miongozo ya utumishi haiwatambui. Sasa ni wakati, wakati tunaboresha teknolojia, watu sasa hivi wana apply kazi kwa mitandao tuwe na vigezo vya kuangalia vijana ambao wanajitolea katika mazingira mbalimbali na kujitolea kuwe sehemu ya mahitaji ama sehemu ya masharti ya watu ambao wanaweza wakapata added advantage pale wanapoomba kazi Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wetu wana malalamiko mengi hasa watumishi wa umma, kuna wengi ambao walisimamishwa kinyume cha sheria wakati ule wa mjadala wa vyeti fake na wafanyakazi hewa na baadae wakarejeshwa kwenye ajira zao. Lakini naomba kuchukua nafasi hii kuwasikitika mpaka sasa wengine hawajalipwa malimbikizo yao na wengine waliachishwa kazi barua zimetoka za kuwarudisha kazini, hawarejeshwa kazini mpaka sasa hivi. Nilikuwa naomba kutumia nafasi hii kutoa rai kwa ndugu zetu wa Utumishi, kuona ni jinsi gani wanaenda kuhakikisha kwamba wale watumishi ambao waliondolewa kimakosa basi wahakikishe kwamba malimbikizo yao ya mishahara yanaenda kurejeshwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo linazungumzia suala malimbikizo ya mshahara ni watumishi wale wahanga 2,000 wa Ilovo. Wakati tunabinafsisha mashirika ya umma, kuna Watanzania wengi waliachishwa kazi na malimbikizo yao mpaka leo hawajalipwa na wengine walilipwa pungufu na hawajui mahali pakwenda kulalamika PSRC wanasema watalipwa na mwajiri, mwajiri anasema watalipwa na Hazina. Kwa hiyo watu hawa bado wana kilio kikubwa naomba sana Wizara ya Utumishi iwaangalie hasa hawa wahanga 2,000 kule Ilovo ambao mpaka sasa hivi wana kesi mahakamani lakini kuna wengine ambao hawana kesi mahakamani wanaagaikia malipo yao.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti ya maji. Kwanza nianze tu kwa kusema kwamba naipongeza Wizara, nampongeza Waziri ndugu yetu Mheshimiwa Aweso; Naibu Waziri, Mheshimiwa Maryprisca Mahundi na timu yake. Kwa kweli, wanafanya kazi kubwa nasi tunaiona. Nashukuru kwa jinsi ambayo ameweza ku-transform Wizara yake katika kipindi hiki kifupi. Kwa kweli, ni mwakilishi mzuri wa vijana nasi tunashukuru kwa uwakilishi huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuzunguka sana katika miradi mbalimbali ya maji, sisi bado hatujakuona Jimbo la Mikumi kwa sababu hakuna mradi wa kuja kuutembelea. Hatuna mradi wa kichefuchefu wala mradi wa maji ambao unaendelea. Shida ya maji kwenye Jimbo la Mikumi ni kubwa na ninaomba niweke kwenye rekodi zako kwamba Jimbo lile linaongozwa na Mbunge ambaye anawakilisha wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu la kuwaangalia wanyama tumewaachia TANAPA, kwa hiyo, sasa hivi tunaangalia shida za wananchi wetu. Wananchi wetu kule shida kubwa ambayo wanayo ni maji. Kuna miji mikubwa kama Mikumi ambayo huwa unapita ukielekea Jimboni kwako kutokea Dodoma ama kupitia Dar es Salaam. Shida kubwa ya Mji ule ni maji. Usanifu umefanyika, lakini hakuna mradi wa maji na watu wana shida sana ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, kwenye mji wa Ruaha ambao una watu wengi sana ambao wanafanya kazi katika Kiwanda cha Sukari Kilombero, watumishi na vibarua wale kazi kubwa ambayo wanaifanya muda wao mwingi ni kutafuta maji. Mheshimiwa Waziri, huwezi kuamini kwamba muda ambao watumishi wa kiwanda kile wanatafuta maji katika Mji ule ni mwingi kuliko muda ambao wanautumia mashambani na viwandani. Hapo hatuzungumzii wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mji mkubwa wenye uzalishaji mkubwa kama huo unapokuwa na shida ya maji unashindwa kuelewa shida ikoje katika maeneo ya pembezoni kama Ruhembe, Tindiga, Mabwelebwele, Ulaya, Malolo na hata Zombo. Kwa kweli, Jimbo la Mikumi limesahaulika kama yalivyo Majimbo mengi Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, aliangalie Jimbo hili kwa namna ya kipekee sana kwa sababu kuna vyanzo vingi vya maji ambavyo havitumiki kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wetu kuondokana na adha ya maji ambayo inawakumba.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ningependa kuchangia ni mahusiano ya Taasisi zetu ama wakala wetu wa maji kwa mfano MOROWASA na RUWASA. Kwa kweli mahusiano yao yanatuchanganya na hatujui nani ni nani na nani anafanya lipi? Kwa mfano, katika Mji mdogo wa Mikumi wamechukua MOROWASA na katika maeneo yote mengine wako RUWASA. Yote haya tunazungumzia ni maeneo ya pembezoni ambayo RUWASA walikuwa wanapaswa kuwa wasimamizi wa miradi hii ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuelewi ni vigezo gani ambavyo Mikumi Jumuiya ya Maji imechukuliwa kwa MOROWASA na hasa ukizingatia kwamba ilikuwa inafanya vizuri na ilikuwa Jumuiya ya mfano katika Jumuiya zote za maji hapa Tanzania na imekuwa ikichukua cheti cha ubora kwa miaka mitatu mfululizo. Tangu wamechukua ile jumuiya wamepeleka MOROWASA, Mheshimiwa Waziri anaweza akatuthibitishia hapa performance ya maji na shida ya maji imeongezeka maradufu. Hata hayo madogo ambayo yalikuwa yanapatikana sasahivi yanapatikana kwa mgao ambao haumithiliki. Kwa hiyo, tunaomba wakati wanaanzisha maeneo mapya ya kuyagawa kati ya Mamkala ya Maji ya Mijini na Vijijini waangalie vilevile katika kuboresha hali ya upatikanaji wa maji katika maeneo hasa haya ya pembezoni. Pia hata hizi mamlaka mahusiano yake na halmashauri za miji, zinaripoti kwa nani?

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na changamoto tulikuwa tunazungumzia kuhusiana na mahusiano ya TARURA na halmashauri zetu, lakini changamoto hiyo bado ipo hata kwa RUWASA. Hatujui ni nani ambaye anapanga vipaumbele? Nani anashiriki katika usimamizi wa utekelezaji wa miradi? Wananchi wanawakilishwa na nani katika Serikali za Mitaa kwenye miradi ambayo inahusiana na maji? Kwa hiyo, naomba hilo Mheshimiwa Waziri aliangaliwe kwa namna yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo chetu cha Maji cha Rwegarulila kilikuwa ni chuo maarufu sana katika miaka ya 80 na 90, lakini chuo hiki kinahitaji maboresho makubwa. Naomba kupitia Bunge lako kwamba, Mheshimiwa Waziri aangalie ni jinsi gani mitaala ya chuo hiki inaendana na changamoto zilizopo. Vile vile aangalie ni jinsi gani anaweza akashirikisha vyuo vingine vya ufundi kushirikiana na Rwegarulila katika kuzalisha wataalam wabobezi katika kusimamia, ku-design na ku-implement miradi ya maji katika maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumza kwamba, maji ni uhai, lakini ni kwa kiasi gani kauli hii ina-reflect ama inaakisi uhalisia katika maeneo ya pembezoni? Kodi katika vifaa ambavyo vinahusiana na miradi ya maji bado ni kubwa.

Kwa sababu tunaamini kwamba, maji ni uhai sioni busara ya kuweka kodi kubwa katika vifaa, hasa pump za maji kwa sababu, pump za maji zinaenda kuhudumia watu. Pump za maji ni huduma, pump za maji zinaenda kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi wetu hasa katika maeneo ya vijijini. Kwenda kutoza kodi ama kufanya pump za maji kuwa chanzo kikubwa cha kodi ni kumuumiza mwananchi ambaye tunataka twende kumtua ndoo kichwani, hasa mwanamke wa vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Wizara yetu na Taasisi za Serikali zizungumze. Zione ni jinsi gani zinaenda kutekeleza ilani ya chama chetu ambayo inasema kwamba, tunaenda kumtua mama ndoo kichwani. Hatuwezi kwenda kumtua mama ndoo kichwani kama vifaa ambavyo ni muhimu katika uzalishaji na usambazaji wa maji tunaenda kuvitoza bei kubwa, hatutafikia malengo haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kwamba, kwa moto ambao Mheshimiwa Waziri anaenda nao na akishirikiana na Wizara nyingine kama Fedha na Wizara ya Maendeleo ya Jamii naamini kabisa tunaenda kutengeneza jumuiya za uhakika ambazo zinaenda kusimamia miradi ya maji katika maeneo yetu ya pembezoni, hasa vijijini. Miradi hii ambayo inatengenezwa ikawa na ownership ya wananchi, lakini pia ikawa endelevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa ambayo tunayo ya miradi yetu ya maji huko vijijini ni kwamba, Serikali hata inapoweka fedha haiwi endelevu kwa sababu, hata jumuiya za maji kule haziwezeshwi, hazielimishwi, hazipatiwi msaada wa uwezeshaji, ili wajue majukumu yao, lakini pia wangalie miradi ambayo inawekezwa kwa fedha nyingi za Serikali kuwa endelevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha na naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Bajeti ya Wizara hii ni muhimu sana kwa Taifa hili kwa sababu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ndiyo roho ya kile ambacho tunaita mapinduzi ya nne ya viwanda ama uchumi wa kati ama uchumi wa viwanda. Hatuwezi kuzungumzia uchumi wa viwanda bila kuzungumzia miundombinu hasa ya barabara ambazo zinapitika mwaka mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mengi ya nchi yetu bado barabara ni changamoto. Ni muhimu wakati tunajadili bajeti ya Wizara hii, kuangalia ni jinsi gani Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi inakuwa na mafungamano ya karibu sana na Wizara zote ambazo tunazitegemea katika ku-transform uchumi wetu hasa Viwanda na Biashara, Wizara ya Kilimo, Afya, Uvuvi na Mifugo; hizi zote zinategemea sana mipango ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ili ipange mipango ya muda mfupi na muda mrefu ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi pamoja na dhana nyingine ya kuwa na mafungamano ya karibu na Idara nyingine ama Wizara nyingine, zina umuhimu sana wa kuangalia ni jinsi gani inaenda kuunganisha wananchi wa Tanzania hasa wanaoishi katika maeneo ya pembezoni.


Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna kasi ambayo inaendelea katika ujenzi wa standard gauge. Pembeni ya standard gauge kuna barabara ambayo inahudumia ujenzi wa reli hizi ambazo imeunganisha vijiji vingi sana katika nchi yetu. Barabara hizi sasa hivi ukipita zimesahaulika, ni barabara ambazo zinaokoa maisha ya watu, lakini zinakuza uchumi sana katika maeneo ya vijijini. Kwa hiyo, ni muhimu Wizara hii ikaziangalia barabara hizi kwa jicho la pekee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo kule Wilaya ya Kilosa kila mwaka tunakuwa na mafuriko. Kuna mabwawa yanaitwa mabwawa ya punguza, mabwawa haya yalitengenezwa enzi ya Mjerumani na miaka yote yalikuwa chini ya Shirika la Reli, tangu yamepelekwa katika Wizara ya Kilimo yamejaa na maji ya Mto Mkondoa yanashindwa kuwa na mahali pa kufikia, matokeo yake yanasababisha maafa kwa wananchi wetu siku zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapozungumzia dhana ya mafungamano kati ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi hapa ndipo ninapoanzia. Kuna umuhimu wa Wizara hii kukaa na Wizara ya Kilimo na Wizara ya Maji kuona ni jinsi gani maji ya mito kama haya ambayo yanachukua reli kila siku, reli ya kati kule Godegode inabebwa kila siku kutokana na mafuriko ya mto huu. Ni lini Wizara hii itakaa pamoja na Wizara ya Maji na Wizara ya Kilimo kuona kwamba maji haya badala ya kuwa dhahama na balaa kwa reli yetu ambayo ni miundombinu tunayotegemea inakuwa baraka kwa kutengeneza mabwawa ambayo yanaenda kuhifadhi maji, hivyo kuepusha vifo vya wananchi katika Wilaya ya Kilosa na maeneo ya Jimbo la Mikumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba wakati Waziri anahitimisha hoja atuelezee Wizara yake imejipanga vipi kuhakikisha kwamba inazungumza na Wizara nyingine kuhakikisha mabwawa haya ambayo yalikuwa chini ya Shirika la Reli yanarudi huko na yanatunzwa na kuangalia ni jinsi gani maji yake yanaenda kuzuiwa yasilete athari kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusiana na suala zima la uwezeshaji wa wakandarasi wetu wazawa. Kuna miradi mingi mikubwa ambayo tunaigharamia kama Standard Gauge, lakini kuna bwawa la Mwalimu Nyerere na miradi mingine mikubwa ya barabara. Ni kwa jinsi gani miradi hii tunaitumia kama fursa ya kuwafundisha vijana wetu kuiba teknolojia ama kutumia teknolojia ambayo wenzetu wanaitumia katika ujenzi huu kama sehemu ya masomo ama mafunzo kwa vijana wetu wa ndani. Hii itasaidia miradi hii inapokamilika, basi vijana wetu wanatoka na ujuzi ama wanatuachia ujuzi ambao kesho hautatulazimisha kuagiza ama kuwapa tender makampuni ya nje kwa kisingizio kwamba wakandarasi wetu hawana ujuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona jitihada za makusudi ambazo Wizara ya Ujenzi inafanya katika kuwawezesha wakandarasi wetu wazawa. Pale Kilosa kuna Barabara ya Kilosa - Mikumi ambayo Kampuni ya Umoja ambayo ni ya wazawa wamepewa kama sehemu ya majaribio ama sehemu ya kujifunza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule Tabora kuna Barabara ya Kaliua - Urambo ambayo wamepewa wakandarasi wazawa. Pamoja na kuwawezesha wakandarasi hawa wazawa, bado mradi huu ambao tunauona ulikuwa ni sehemu nzuri ya wao kujifunza unakwazwa na nia njema ya baadhi ya watu. Pamoja na kwamba nia ni kujenga barabara hii, lakini vijana hawa unaweza kuona kwamba wanashindwa kutekeleza mradi wao kwa wakati kwa sababu ya GN, fedha haziji kwa wakati, malipo yao hayaji kwa wakati na hivyo kupelekea faida ndogo ambayo ingeweza kutumika kwa wao kuongeza uwezo wa kudai miradi mingine unapotea…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa kengele imegonga.

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara muhimu ya Maliasili na Utalii. Kimsingi nikiangalia michango ya Waheshimiwa Wabunge, pamoja na kwamba, wote tunakiri kuna kazi kubwa sana ambayo imefanywa na Wizara hii katika ku-transform sekta ya utalii kwa maana ya kuongeza idadi ya watalii, lakini pia kuongeza pato la Taifa, lakini bado kuna kutokuridhishwa kwa Wabunge wengi kwa jinsi hali inavyoenenda katika sekta ya utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia michango ya Waheshimiwa Wabunge unaweza kuona kwamba, wengi wanaona kwamba, sekta hii haijatendewa haki kwa maana kwamba, kuna fursa nyingi za utalii ambazo bado hazijaguswa. Tumejikita sana kwenye utalii wa wanyamapori, lakini kuna talii za fukwe kuanzia Tanga mpaka Mtwara ambazo hazitumiki kikamilifu, tuna talii za kwenye visiwa ambazo hazitumiki kikamilifu, lakini tuna talii za kiutamaduni ambazo hazitumiki kikamilifu. Kwa hiyo, sekta hii ya utalii ikigusa maeneo yote haya naamini kabisa tunaweza kupata tija ambayo tunaitarajia.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado tunaona kwamba, pato ambalo linatokana na utalii kama tunaenda ku-adapt sera ya ugatuaji wa madaraka ya D-by-D, kama tunaenda kushirikisha wafanyabiashara wadogo katika sekta ya utalii, tunaweza kwenda kuona makubwa katika sekta hii. Tatizo la sekta yetu ya utalii imehodhiwa na wafanyabiashara wachache wakubwa na hawa ndio ambao wana-drive hii sekta kwa kuweka masharti magumu ambayo wafanyabiashara wadogo katika sekta ya utalii kushindwa kuingia na kufanya biashara. Matokeo yake vijana wachache ambao tunawaelimisha kwa gharama kubwa katika sekta ya utalii wanaishia kuwa watumishi na vibarua katika sekta ya utalii na sio kama wajasiriamali katika sekta hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakuomba kupitia Bunge lako wananchi wetu, hasa vijana wetu ambao wamesomea utalii wawekewe mazingira wezeshi ya kuingia katika sekta ya utalii kama wajasiriamali na sio kama vibarua. Ninachokiona kuna cha kujifunza kwa wenzetu, hasa nchi za Asia, kule wenzetu utalii mwingi uko katika ngazi ya familia katika ngazi ya vijiji. Huwezi kukuta mahoteli makubwa makubwa katika maeneo mengi ya vivutio, utakuta kuna bed and breakfast, utakuta kuna vi-lodge, kuna vihoteli ambavyo vinaitwa boutique kule Myanmar, Laos, Thailand hata Cambodia. Unaona kabisa jinsi gani utalii ulivyoenda kuajiri watu wengi kwa mpigo ukilinganisha na kwetu ambapo tunategemea wawekezaji wachache kuajiri vijana wengi kama vibarua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya yote yanahitaji fedha. Kitendo cha kuondoa fedha za Mfuko wa Utalii kupeleka katika Mfuko Mkuu wa Hazina, kwa kweli kwa namna mona ama nyingine imeuwa sekta ya utalii. Naomba Serikali ilitafakari tena upya kwa sababu, tuna maoni mengi ambayo tunataka Wizara hii isimamie mabadiliko katika sekta ya utalii, lakini swali, fedha wanapata wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha inabidi waombe kama wengine wanavyoomba kutoka katika Mfuko Mkuu wa Hazina. Hali hii haitatupelekea sababisha kuona mabadiliko yale ambayo tunayatarajia katika sekta hii ya utalii. Ombi langu, ni Serikali kuona jinsi gani inarejesha Mfuko huu wa Utalii na ili Wizara isimamie mapato haya kwa ajili ya kuwekeza kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika ku-transform utalii wetu, lakini pia katika ujenzi wa miundombinu katika mbuga zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mawasiliano katika mbuga zetu ni suala la muhimu. Mtalii anayeingia Mikumi anaweza akaingia toka asubuhi mpaka jioni asitume status kwenye WhatsApp kwa sababu hakuna simu, lakini pia hata akitaka kutoka pale Mikumi kwenda Ruaha atapita pale Ng’apa, atapita Msimba, atapita Ruaha hana mawasiliano hata ya simu. Halafu tunataka mtalii huyu aende akatangaze utalii kwao? Hakuna utalii mzuri kama watu kushuhudia nini ambacho kinaendelea katika mbuga za wanyama, lakini kama hawawezi wakajirusha wenyewe kwenye status kuonesha kwamba, nini wanachokiona katika mbuga zetu, si rahisi kushawishi wengine kuja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nchi yetu kama ilivyo katika nchi nyingine, kasheshe la corona liliathiri sekta yetu ya utalii, lakini ilifungua fursa ya watalii kutoka nchibya Urusi ambao walikuja kutokea Zanzibar. Sasa naomba Serikali iione hii kama fursa kwa nchi za Baltic na Russia kama sehemu ya kuhamasisha utalii wa kuja moja kwa moja kutokea Zanzibar kuja Mikumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Bajeti yetu. Awali ya yote, pamoja na kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia naomba nitoe pongezi nyingi kwa Serikali yetu ya Awamu ya Sita, hasa kwa mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi ambavyo ameweza kusimamia uendelezaji wa miradi yote mikubwa ambayo imeanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Pia nampongeza sana kwa jinsi ambavyo ameweza kutusimamia na kutupelekea miradi mikubwa hasa ya vituo vya afya na ujenzi wa miundombinu ya madarasa. Kwa kweli wananchi wanashukuru sana na hili limepunguza adha na maswali mengi kwetu sisi Waheshimiwa Wabunge. Kwa kiasi kikubwa imeturahisishia kazi, hasa tunapojiandaa kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwezi Januari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa bajeti iliyopita michango mingi sana ilijikita kwenye ujenzi wa miundombinu, hasa barabara. Kwenye mapendekezo ambayo tumeyasoma kupitia Mpango huu wa Serikali tumeona kwamba kuna barabara nyingi ambazo zilikuwa zimeshafanyiwa upembuzi yakinifu na nyingine zilishatangazwa, bado ujenzi haujaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya barabara hizo ni ya kutoka Kilosa kupitia Ulaya kwenda Mikumi, barabara ambayo ni muhimu sana kiuchumi na naamini kuna barabara nyingi za aina hiyo. Sasa ombi langu ni kwamba mipango hii inapokuja mipya inapaswa kuzingatia barabara zile ambazo zilikuwa kwenye mpango uliopita zinakamilika kabla haijajikita katika maeneo mapya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, Mpango huu haujazungumza kilio cha Wabunge wengi hasa kuhusiana na hii service road ambayo inahudumia ujenzi wa barabara ya SGR. Barabara hii ambayo kazi yake ni ujenzi na kusafirisha vifaa vya ujenzi kwa ajili ya SGR imefungua vijiji vingi sana vya nchi hii kuanzia Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma, Tabora mpaka kule Mwanza. Kuna maeneo ulikuwa huwezi kufika hata kwa pikipiki, lakini kwa sababu ya ujenzi wa reli yetu barabara hii imefungua vijiji vingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote hayo, lakini hatujaona mpango wa uhakika wa Serikali, unakwenda kuihudumia vipi barabara hii kuwa moja ya njia za uhakika ambazo zitapitika mwaka mzima bila kujali masika au kiangazi. Tunajua kwamba reli hii inakwenda kukamilika, lakini nini future ya barabara ambayo inahudumia reli hii? Itaendelea kutumika kwa wananchi; Serikali inaichukua au ina mpango gani na hii barabara?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu moja ya vitu ambavyo tunavizungumzia ambavyo Bunge letu hili limejipa jukumu ni kwenda kufanya mapinduzi ya kilimo. Barabara hii inasaidia sana katika mapinduzi haya ya kilimo kwa kuunganisha vijiji vyetu na barabara kuu na masoko. Kwa hiyo pamoja na mpango mzuri, naomba kupata uhakika ni kwa jinsi gani Serikali inakwenda kuichukulia barabara hii kama maeneo ya vipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu maendeleo vijijini. Vijiji vyetu vingi ambavyo vinajikita kwenye kilimo havihitaji barabara ya lami, vinahitaji kufikika mwaka mzima, masika na kiangazi. Shughuli zinazofanyika kule ni nyingi na ni kubwa na ni muhimu kwa uchumi wetu. Kikwazo chao ni kimoja tu; wana uwezo wa kuzalisha, lakini hawana uhakika wa kufikisha bidhaa zao sokoni kwa sababu tu barabara hazifikiki. Kwa hiyo naomba huu Mpango wa Maendeleo au Mpango wa Bajeti ujikite katika kuhakikisha barabara zetu za vijijini ambazo zinakwenda kwenye maeneo ya uzalishaji zinapitika mwaka mzima, siyo kwa lami, kwa kiwango cha changarawe tu kwa kuanzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini mchango wake ni mkubwa sana kwenye uchumi wa hii nchi na tukifanya hivyo naamini kilimo chetu kinakwenda kuongeza thamani yake, lakini pia umuhimu wake katika kuzalisha ajira za vijana wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kulizungumzia hap ani umuhimu wa kilimo chetu na hasa kuweka mafungamano na sekta binafsi. Benki Kuu imejitahidi, imetoa fedha zaidi ya trilioni moja kwa mabenki ya biashara na lengo hapa ilikuwa ni kusisimua sekta binafsi, na hasa sekta ya kilimo. Hata hivyo, tunaona kwamba pamoja na fedha zote hizi ambazo zimewekwa kwenye mabenki ya biashara kusisimua kilimo chetu, bado ukuaji wa kilimo ni wa kusuasua kwa maana hakikui zaidi ya asilimia tatu mpaka nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii siyo ishara nzuri katika nchi ambayo zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wake wamejiajiri katika sekta ya kilimo. Hii ni mbaya zaidi ukilinganisha na ukuaji wa sekta nyingine kama ujenzi ambayo inakuwa kwa zaidi ya asilimia 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu; kwanza tusiishie tu kuzungumza kwamba, kilimo ni uti wa mgongo, kilimo kwanza, kilimo ni siasa; hizi slogans haziwezi kutufikisha tunakotaka. Kilimo chetu kinahitaji mkakati wa kweli, kwanza wa kuboresha miundombinu kwa maana ya barabara, lakini pia pembejeo, viuatilifu, mbegu na mwisho uhakika wa soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukivifanya hivi vyote kwa uhakika naamini mkulima wa Kitanzania hahitaji kuamshwa asubuhi, atakwenda kulima, atajituma kwa sababu ana uhakika wa kupata pembejeo kwa wakati, ana uhakika wa kupata viuatilifu kwa wakati na ana uhakika wa kupata masoko ya bidhaa zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kwamba kuna maeneo mengi tumefanikiwa kwenye uwekezaji, lakini eneo la pembejeo za kilimo siyo eneo ambalo tunapaswa kujisifia. Naomba mapendekezo ya Mpango wetu yaje na mkakati ni namna gani tunakwenda kuhamasisha wawekezaji wadogo, wa kati na wakubwa katika uzalishaji mkubwa wa mbolea na viuatilifu ndani ya nchi na makampuni binafsi ya uzalishaji wa mbegu. Haya yakifanyika yatasaidia katika kuhamasisha kilimo chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la usalama wa chakula. Waswahili wanasema adui yako mwombee njaa, kwa sababu tumbo lenye njaa huwa mara nyingi halina busara. Katika hilo wakati Taifa letu tunasema kwamba tunaweza kwenda kukutana na ukame mwakani, ni vyema tukajiandaa kuhakikisha kwamba tuna hifadhi ya kutosha ya chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili tumezungumza kwenye mapendekezo kwamba tunahitaji kuiwezesha NFRA. Naomba kusema kwamba hatuhitaji kuiwezesha NFRA, tunahitaji kuilipa madeni yake. Serikali inadaiwa na NFRA, ni lini inakwenda kulipa madeni haya kwa NFRA ili itumie fedha hizi katika kuwekeza maghala na kuwekeza katika ununuzi wa mazao ya wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naomba kulizungumzia ni suala zima la Serikali kuwekeza kwenye innovation kwa maana ya vijana wetu kujiajiri katika kuendeleza technology ndogondogo, lakini pia kuwekeza kwenye viwanda vidogovidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawekeza sana kwenye viwanda vikubwa, lakini wananchi wetu hawana mitaji mikubwa, wanahitaji msaada wa Serikali ku-facilitate kuwekeza katika viwanda vidogovidogo ili viwanda vikubwa viwe facilitator wa viwanda vidogo, viwanda vikubwa vitegemee viwanda vidogo katika uwekezaji wake. Najua hili liko ndani ya uwezo wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nazungumzia maendeleo ya kilimo, ni lazima tuzungumzie sekta ya maji. Hifadhi yetu ya maji siyo nzuri, vyanzo vyetu vinateketea. Wakati tunazungumzia maendeleo yetu ni vyema tukaja na mkakati wa Kitaifa kuona ni jinsi gani tunakwenda kulinda vyanzo vya maji yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ingawa siyo kwa umuhimu, Jimbo la Mikumi ni jimbo la giza, halina mawasiliano. Sisi tunaomba minara midogo kwa kimo cha Mheshimiwa Mchungahela ambayo hatuna. Afadhali ya yeye ana minara mifupi, sisi hatuna kabisa kule katika Jimbo la Mikumi, kwa hiyo ikiipendeza Serikali wakati tunakwenda katika mapinduzi ya tano ya viwanda ni vizuri wakafikiria umuhimu wa mawasiliano katika kuwezesha wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuanza kuchangia Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa ninaomba nijielekeze kwenye kuipongeza Serikali ya mama Samia kwa kazi nzuri ambayo imefanya ya ujenzi wa madarasa, vituo vya afya na zahanati. Lakini kuna kazi kubwa ambayo inaendelea chini ya TARURA. Pamoja na kazi hii kubwa, lakini pia tunaona impact ya hii mikopo ya asilimia 10 kwenye halmashauri zetu. Ni kazi nzuri ambayo inahitaji uungwaji mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata hivyo fedha ambazo zinakwenda kwenye mikopo kwa ajili ya makundi maalum ya hiyo asilimia kumi ni nyingi sana. kwa mfano kwenye bajeti ya mwaka huu ni zaidi ya bilioni 69 na kitu ambazo zinakwenda kwenye mikopo kwa ajili ya makundi haya maalum. Fedha hizi ni nyingi, ni vizuri tuka-review uendeshaji na usimamizi wa fedha hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungependa kujua ni kiasi gani ambacho kipo kwenye mikono ya vikundi ambavyo vimekopeshwa; ni kiasi gani ambacho kimerejeshwa na nini mpango endelevu wa hizi fedha? Kwa sababu hatuwezi kuendelea kutoa fedha hizi kwa maisha yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tujue ni kiasi gani ambacho kipo ambacho kinaweza kikawa mtaji wa kutosha tukaingiza kwenye revolving fund ikazunguka yenyewe bila ya kuendelea kuchota tena kwenye bajeti kuu. Kwa hiyo ni vizuri tukajielekeza namna bora ya kuangalia uendeshaji wa hizi fedha za asilimia kumi ya mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, halmashauri zetu kimsingi zinahitaji mipango endelevu, hasa ujenzi wa miundombinu ambayo inaweza kwenda kutoa ajira endelevu kwa wananchi wetu. Ukiangalia reli ambayo inatengenezwa ya SGR kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza, Makutupora, unaweza kuona mashimo makubwa ambayo yanatumika kama chanzo cha kokoto za ujenzi wa reli hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mashimo haya makubwa yanaweza sana kutusaidia kutengeneza mabwawa ambayo yanaweza kwenda kutumika kwa ajili ya shughuli za uvuvi, mifugo na kilimo kwa ajili ya umwagiliaji na ika-save fedha nyingi sana za Serikali. Ninapenda kujua ni kiasi gani cha mashimo ambayo yamechimbwa ambayo tunaweza tukabadilisha kuwa mabwawa na ikawa sehemu nzuri ya kutengeneza miundombinu kwa ajili ya wavuvi, wakulima na umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili linahitaji mahusiano ya karibu kati ya halmashauri zetu (TAMISEMI), Wizara ya Kilimo na Wizara ya Maji na huku kwenye mifugo. Kazi nzuri ambayo inafanyika katika Serikali za Mitaa inahitaji mahusiano ya karibu kati ya TAMISEMI, Wizara ya Kilimo na Mifugo ili kuleta matokeo chanya kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ambayo ipo sasa hivi na mahusiano yaliyopo hayatoshi kwa sababu ukiangalia idara ya mifugo kwenye halmashauri zetu, ukiangalia uvuvi kwenye halmashauri zetu ukiangalia kilimo kwenye halmashauri zetu, haziakisi umakini katika suala zima la kuhakikisha kwamba sekta hizi zinakwenda kutoa ajira ya maana kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu; tutengeneze mfumo madhubuti ambao Wizara hizi zinaweza zikakaa pamoja kuona namna bora ya kuboresha masoko na biashara zetu. Kwa mfano unaweza ukaangalia suala zima la ghala au stakabadhi ya ghala jinsi gani ilivyo sensitive katika uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado hatujui role ya halmashauri katika usimamizi wa maghala; hatujui role ya Wizara ya Viwanda na Biashara katika usimamizi wa maghala; hatujui role ya Wizara ya Kilimo katika usimamizi wa maghala. Tunahitaji kujua nani ambaye ana dhamana ya kusimamia maghala na biashara, hasa katika suala zima la bidhaa na usambazaji wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kadhia ambayo imetokea kwenye soda inaweza ikatokea kwenye pembejeo, inaweza ikatokea kwenye viuatilifu, inaweza ikatokea hata katika usambazaji wa mazao. Hii scarcity ama deficit inaweza ikawa created kwa sababu hatuna taasisi ambayo inakwenda kusimamia maghala. Tunahitaji kuwa na sheria ambayo inatoa majukumu ya nani anakwenda kusimamia na kuratibu haya maghala.

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha na ninaomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi pia ya kuchangia hotuba ya bajeti ya Waziri Mkuu. Awali ya yote naomba nianze kwa kumpongeza Rais wetu mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa kazi kubwa ambayo inafanywa hasa katika Majimbo ya pembezoni kama Mikumi. Kuna kazi kubwa inaendelea kuna mambo mengi ambayo yalikuwa yameshindikana lakini sasa yanafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kule Ruhembe kuna daraja kubwa ambalo linaenda kuunganisha Kata za Ruhembe, Kidodi na Ruaha zinaenda kupunguza umbali wa wananchi na wakulima kutoka kilometa 30 mpaka kilomita mbili. Pia kuna kata inaitwa Vidunda ambayo ilishatengwa na haikuwa na mawasiliano ya barabara lakini sasa hivi inaenda kuwa na mawasiliano ya barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Kata za pembezoni kama Malolo, kama Uleling’ombe, Kilangali hata Kisanga ambazo sasa hivi zinaenda kuunganishwa na barabara kuu lakini pia uzalishaji wake wa bidhaa za kilimo unaenda kuunganishwa na masoko. Jitihada zote hizi zinaendana pamoja na uboreshaji mkubwa wa vituo vya afya, shule na maeneo mengine ya huduma za kijamii. Tafsiri yake ni kwamba huko tunakoenda wananchi wengi watabakia vijijini na migration kutoka vijijini kuja mjini itaendelea kupungua kwa sababu ya uboreshwaji wa miundombinu lakini pia huduma za kijamii katika kata na vijiji vya pembezoni. Maana yake nini tunaenda kushuhudia rural transformation ambayo haijawahi kuonekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali hapa je ni kwamba elimu inayotolewa na vyuo vyetu inaakisi maendeleo haya ambayo yanaendelea vijijini? Kozi ambazo zinatolewa na vyuo vyetu zinaandaa vijana wetu kurudi vijijini na kwenda kutumikia maisha katika kata na maeneo ya pembezoni? Ninapoona tunaendelea ku-admit wanafunzi katika vyuo vyetu vikuu katika kozi ambazo hazitoi ajira, sioni kama kuna seriousness katika ku-transform vijiji vyetu na hasa katika kata za pembezoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye hili kwa sababu Ofisi ya Waziri Mkuu inasimamia sera, lakini pia ajira vijana na hata walemavu, ningependa sana kuona uratibu katika huu Mfuko 10% za wanawake, vijana na walemavu za TAMISEMI zinaratibiwa vizuri kuwa sehemu ya kutoa majibu ya changamoto katika maeneo yetu ya pembezoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Ofisi ya Waziri Mkuu na Serikali yetu, mwaka 2014 ilifanya study ya kuangalia kiwango cha ujuzi wa nguvu kazi na katika study hiyo tulikuwa tumeona kwamba lengo ilikuwa ni kuangalia namna ya kujenga uwezo unaohitajika katika soko la ajira, watu kujiajiri na kuajiriwa. Tuliona matokeo ya utafiti ule, asilimia 79.9 ya nguvu kazi ilikuwa chini ya kiwango cha ujuzi, kwa maana low skilled, 16.6% ni semi skilled kwa maana kiwango cha ujuzi katika soko la ajira kilikuwa ni kiwango cha kati. Tuliona 3.6% ya nguvu kazi katika ajira na ujuzi wake ni chini ya 3.6% ambao walikuwa ni higher skilled na ndiyo matokeo yake Ofisi ya Waziri Mkuu na Serikali ikaja na mikakati minne ya kukuza ujuzi kwa maana utarajali internship, lakini pia urasimishaji wa ujuzi ambao umepatikana nje ya mfumo kukuza ujuzi wa wafanyakazi na wale waliojiajiri lakini pia uanagenzi kwa maana ya friendship.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hizi program zilikuwa ni muhimu sana na kwa kweli kwenye baadhi ya maeneo tumeona matokeo chanya. Ombi langu ni vyema sasa tukafanya study kuona ni jinsi gani tunaenda ku-transform hizi program nne kuona kwamba zinaenda kutatua tatizo la ujuzi kwenye nguvu kazi ya vijana wetu katika soko la ajira. Hapa tunaweza tukajifunza kutoka katika Nchi kama za Ujerumani ambazo zilifanikiwa sana, Nchi ya Finland, Korea lakini hata China juzi hapa tuliona wameamua kubadilisha Vyuo vyao Vikuu zaidi ya 600 kuwa polytechnics na vocational kwa ajili ya kufunza ama kutoa ujuzi kwa vijana wao ili waende kuzalisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa katika hili tuna la kujifunza, kama wenzetu wana Vyuo Vikuu 600 na wameona kabisa module ya elimu wanayoitoa pale ni nadharia zaidi, haiendi kujibu changamoto ya ajira, wamebadilisha kwenda kutoa ujuzi, kuna jambo kubwa la kujifunza kwao. Je, tunavyobadilisha vyuo vyetu vya kati kwenda kuwa Vyuo Vikuu na kutoa degree za nadharia, tunapotoa graduates 5000, 10,000 ambao wamesomea procurement wanaenda kuajiriwa na nani wanaenda kufanya kazi wapi hawa? Tunapoenda kutoa ajira ama graduates 10,000 wanasheria. Je, wahalifu wameongezeka kwenye hii nchi? Mahakama zimeongezeka? Shughuli zao ni nini wanaenda kuwaajiri wapi, je, kuna mkakati wa kuenda ku-absorb hili kundi kubwa ambalo lina graduate kutoka kwenye vyuo vyetu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mambo haya tukiyatafakari kwa kina, tunaona kwamba kuna umuhimu wa ku-review elimu tunayoitoa kwenda kujibu changamoto za ajira zetu. Study hii ambayo imefanyika 2017 leo ni 2022 ni miaka mitano utekelezaji wake umefikia wapi kuna umuhimu wa kuifanyia tena study ili kujua je, asilimia hizi ambazo zilitajwa 2014 zimebakia kama zilivyo ama vipi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu Ofisi ya Waziri Mkuu inashughulikia pia majanga, majanga mengi ukiondoa yale ya kiasili kama matetemeko na mafuriko, mengi tunaweza tukayadhibiti. Migogoro ya wakulima na wafugaji ni moja ya majanga ya Taifa hili ambayo tunaweza tukayadhibiti kama tunajipanga. Vyuo Vyetu vya Ufundi vyuo vyetu vya kati, vinaweza vikawa sehemu ya suluhisho la changamoto hizi kama vitaenda kutoa elimu ama ujuzi kwenye kilimo, kwenye ujenzi, kwenye miundombinu na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili ningeomba kusisitiza vyuo vya ufundi na vyuo vya kati vipewe jicho la kipekee. Tuna sheria ambayo 4% ya private sector inatoka ama inalipwa kwenye skill development levy. Bunge lako hatujui zinatumikaje ni vizuri tukajua kwa sababu lengo la skill development levy ni kuendeleza ujuzi wa nguvu kazi yetu. Je, fedha hizi zinaenda kwenye lengo lililokusudiwa na sheria? Tunajua 2% inaenda kwenye mikopo ya higher learning, lakini hizi 2% zinatumikaje katika kujenga na kuendeleza ujuzi wa vijana wetu? Ni swali ambalo tunatakiwa kulijibu na katika jibu lake linaweza kutupa changamoto ambazo tunazo lakini majibu ya kukosekana kwa ajira kwa vijana wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili ninapozungumzia 2% ya skills development levy, ni zaidi ya shilingi bilioni 150. Bilioni 150 inaweza ikatumika sehemu kwa ajili ya kuwanunulia vifaa vijana 90,000 ambao wanasoma katika vyuo vyetu vya VETA, wakatoka pale na vifaa vya kuanzia kazi, wakajiajiri na wakaajiri vijana wenzao na sisi tukapunguza mzigo wa vijana wetu kukosa ajira katika soko la ajira. Katika hili tunahitaji uratibu taasisi zetu za SIDO, VETA, TIRDO wana wajibu wa moja kwa moja ku-incubate vijana ambao wana ari ya kujiajiri na kuajiri wengine. Changamoto ya bureaucracy katika leseni na vitu vingine imekuwa ni zuio kwa vijana wengi kujiajiri. Sasa taasisi hizi zinapaswa kubeba jukumu la kulea vijana wajasiriamali ambao wanatumia ujuzi wao ambao wameupata kwenye vyuo vyetu vya ufundi kujiajiri na katika kuwalea wanapaswa kuangalia hizi compliance kama TBS, OSHA, Weight and Measures wanazi- meet katika kipindi cha uangalizi. Hilo linaweza likatusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, suluhisho la…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango wetu ambao uko hapa mezani. Kwanza niishukuru Serikali yetu kwa kazi kubwa ambayo inaifanya chini ya Rais wetu, mama yetu Samia Suluhu Hassan. Pia nimshukuru Spika wetu, dada yetu Mheshimiwa Tulia Ackson na wewe mwenyewe msaidizi wake kwa jinsi mnavyoliongoza Bunge letu. Tumepata wakati wa kutosha wa kuchangia Mpango huu ambao naamini kabisa mchango wa Wabunge unaenda kuakisi katika ule Mpango Mkuu ambao utawasilishwa hapa kwenye Bunge la Januari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa ni kawaida kwetu kuchangia huu Mpango wa Miaka Mitano na sasa tuko kwenye Mpango wa Tatu. Bado sijaona ni kwa jinsi gani maoni ya Wabunge ambao tunajadili hapa yanaakisi katika mipango hiyo. Nilipenda sana kuona Mpango unapowasilishwa uelezee waziwazi ukiainisha mchango wa Wabunge umechukuliwa kwa kiasi gani katika bajeti, lakini pia katika utekelezaji wa Mpango huu ambao unawasilishwa kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kuna maendeleo chanya, ukuaji chanya katika uchumi wetu. Kwa mfano, ongezeko la asilimia 5.4 katika mwaka 2021, kwa sasa hivi tumeenda zaidi ya ongezeko la asilimia 5.5. Hii ni indication nzuri kwetu, lakini tunaona kabisa ongezeko hili limetokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika maeneo ya maji safi na taka, ambao ongezeko lake ni asilimia 11.9, fedha bima asilimia 10, uchimbaji wa madini na mawe asilimia 8.5, huduma za jamii asilimia 8.5 na umeme asilimia 8.3. Tunaona kabisa hapa maeneo yote haya ambayo yametajwa yanagusa sekta binafsi ambazo katika Mpango Mkuu wa Miaka Mitano, sekta binafsi ilikuwa inatarajiwa kuchangia uchumi wa Taifa kwa takribani trilioni 9.8 na kati ya hizo trilioni 5.1 zilikuwa zinategemewa kuzalishwa na sekta binafsi za ndani wakati hicho kiwango kilichobakia kuchangiwa na sekta binafsi za nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa umakini ushirikishwaji wa sekta binafsi kwetu bado ni changamoto. Kwanza kabisa inaanza na definition ya sekta binafsi, sekta binafsi ni nini? Kwa sababu, inavyoonekana na jinsi tunavyoichukulia kiwepesi tunaona kabisa kwamba, sekta binafsi ni taasisi za watu binafsi ambazo hazina mahusiano na Serikali, lakini wenzetu walishaondoka huko, sekta binafsi ina mahusiano chanya na Serikali na sekta za umma. Sekta ya umma haiwezi kuendelea bila ya mahusiano chanya na sekta binafsi. Ndio maana wakati wenzetu wanajitahidi ku- out source kila kitu kushirikisha sekta binafsi, sisi tunakimbilia Force Account katika kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wale Watanzania ambao walipata kufanya kazi nje wanafahamu. Kule wenzetu mpaka simu ya kampuni ambayo unatumia imekodishwa kutoka kwenye kampuni binafsi, computer unayotumia imekodishwa kutoka kwenye kampuni binafsi, photocopy ambayo unachapisha imekodishwa kutoka kampuni binafsi. Hivyo ndivyo wanavyoshirikisha sekta binafsi katika ukuaji wa Serikali, katika biashara za Serikali na ndivyo wanavyotengeneza matajiri wa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kila kitu tunaenda kwenye Force Account. Sina hakika tutaishia wapi, lakini nina hakika kwamba, kama tunaweza tukafanya research kuna maeneo ambayo tunaweza kabisa kuona tumeshindwa. Wakati umefika sasa kuangalia ni jinsi gani tuna-engage watu wetu katika uchumi mpana wa nchi yetu katika kuwashirikisha aidha, moja kwa moja ama kupitia shughuli zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la sekta binafsi unaweza kuona kwamba, hata mikopo ambayo imetolewa kwa sekta binafsi, pamoja na kwamba, imeongezeka kutoka trilioni 20.6 mwaka 2021 mpaka trilioni 24.5 mpaka Juni, 2022, lakini tujiulize mikopo hiyo imekwenda wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiasi kikubwa cha fedha ambazo zimekopeshwa sekta binafsi, asilimia 38 zimeenda kwenye shughuli binafsi. Unaposikia shughuli binafsi unashindwa kuelewa ni zipi katika uzalishaji. Hakuna kitu kinachoitwa shughuli binafsi katika uzalishaji. Asilimia 16 imeenda kwenye shughuli za kibiashara, asilimia 10.7 zimeenda kwenye viwanda, lakini ukienda kuangalia riba on average unakuta riba ni asilimia 16.4.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uchumi wa kisasa katika dunia hii ambayo tunaishi huwezi ukaenda kumlipisha riba mwananchi wako ya asilimia 16, ukategemea kwamba, inaenda kuchochea uchumi. Huwezi kwenda kumtoza riba mjasiriamali kwa asilimia 16, ukategemea kwamba, anaenda kuwa competent katika dunia ambayo inakimbia sasa hivi kwenye single digits. Ndio maana wawekezaji wote ambao wanatoka nje wanafanya vizuri sana hapa Tanzania ukilinganisha na Watanzania kwa sababu, taasisi zetu za kifedha hazijatimiza wajibu wake wa kuhakikisha kwamba, zinamwezesha Mtanzania katika kuhimili mikikimikiki ya kiuchumi, ya kibiashara na yeye anakuwa full participant badala ya kuwa subordinate wa wageni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ukweli kabisa, jukumu la kuwatengenezea mitaji wananchi ni la Serikali, ku-facilitate matajiri, kutengeneza matajiri ni la Serikali na jukumu hili hatuwezi kulikaimisha kwa watu. Tunatengenezaje mitaji? Kwa kuwapa mikopo ambayo ina nafuu, kuwatengenezea ruzuku, kutengeneza miundombinu ambayo unamwachia mwananchi nafasi ya kushiriki kikamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri sasa umefika wakati wa Bunge lako, hii michango ya Wabunge kuichukulia kikamilifu na umefika wakati wa kuanza kutafakari kuwa hata na Kamati ya Bunge ambayo kazi yake ni kufuatilia maazimio ya Bunge na utekelezaji wa Serikali. Tukifanya hivyo tutajua tumetoka wapi? Tuko wapi na tunaenda wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukishindwa kufanya hivyo ndio utakuta kwamba, tunapanga bajeti ya mwaka huu ya fedha. Kwa mfano, pale Dumila kuna barabara imetengenezwa mpaka Kilosa, Kilosa pale tunaizungumzia Mikumi, kuna Kiduku pale ambacho hatujui lini kimeshakaa kwenye bajeti ya Serikali zaidi ya miaka mitano na hivi tunavyozungumza ipo kwenye bajeti ya Serikali na hatujui lini itatengenezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia Mpango wa bajeti, tunazungumzia jinsi ya kutengeneza framework ambayo inaweza kwenda kusaidia kutengeneza fedha za Serikali kwa ajili ya kuhudumia jamii nyingine. Kuna uwekezaji mkubwa pale Ilovo, bilioni 571 zinaenda kuwekezwa pale Ilovo, lakini kuna SGR ambayo inapita Kilosa, lakini kuna reli ya TAZARA kutoka pale Kidatu kwenda Mlimba kwenda mpaka Zambia. Kipande cha reli kutoka Kilosa kuja Ilovo kimekufa na sasa hivi tunawekeza bilioni 571 pale Ilovo lakini hakuna mechanism ya kusafirisha sukari tukikamilisha kile kiwanda kutoka Ilovo kuja Kilosa kuungana na SGR kupeleka nje ya nchi na mikoani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili hatuhitaji mawazo ya wageni kuja kutuambia, linaonekana kwa macho, lakini hata ujenzi wa barabara ambayo itabeba bidhaa za sukari kutoka kwenye kiwanda hiki ambacho tunawekeza inahitaji kuingizwa kwenye mpango, sio tu kwa sababu, Mbunge amesema, lakini ni kwa sababu inaenda kwenye eneo la uzalishaji ambalo tunahitaji kwa ajili ya kukuza uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali sasa inapaswa kujielekeza katika maeneo ya uzalishaji. Utalii Kusini ni jambo ambalo haliepukiki. Utalii kuunganisha Hifadhi ya Nyerere na Mikumi haliepukiki, kuna zaidi ya dola milioni 120 zimewekezwa pale, lakini ukiangalia nje ya zile hifadhi kuna uwekezaji gani ambao unaenda kusisimua wananchi kushiriki katika shughuli za kitalii, haupo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kusema kwamba, kuna zile bilioni 260 za CSR ambazo zinatokana na Bwawa la Mwalimu Nyerere…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili sisi hatuna la kusema zaidi ya kusema inna Lillah wa inna ilayhi raji’un. Ahsante. (Makofi)
THE WRITTEN LAWS (MISCELLANEOUS AMENDMENTS) (NO. 5) ACT, 2021
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwanza kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Naomba nijielekeze sana kwenye haya mabadiliko ambayo yanapendekezwa katika Sheria, Sura ya 432 katika marekebisho ya sheria, ambayo inazungumzia kuzuia usafirishaji wa binadamu. Katika Kifungu cha 3 tafsiri za baadhi ya misamiati inapendekezwa kufutwa na badala yake kuweka tafsiri mpya na tafsiri za misamiati mingine zinazopendekezwa, ili kuboresha kwa lengo la kuondoa mikanganyiko.

Mheshimiwa Spika, sisi ni Waafrika na jamii zetu sisi tunasema kwamba, ziko kwenye extended families. Sasa katika haya maboresho ya misamiati naona kuna maneno badala ya lile unyonyaji (exploitation) kuna maneno mengine yamewekwa kwa mfano, wanasema: -

(a)keeping a person in a state of slavery;

(b) subjecting a person to practices similar to slavery;

(c) involuntary servitude;…

(f) forced labour;…

(h) forced marriage; or

(i) forced begging.

Mheshimiwa Spika, sasa jamii zetu zinategemeana sana, kuna watoto wa mjomba, kuna watoto wa shangazi ambao wanahamia kwa shangazi, wanahamia kwa mjomba, wanahamia kwa jirani. Hawa unategemea wanapokaa kwenye hizi familia zetu wawe kama sehemu ya familia, kwa maana ya kushiriki katika shughuli zote za kifamilia; iwe shughuli za uzalishaji, mashambani, biashara na kadhalika. Hatuna mfumo wa kuandikishiana mikataba tukiamini kwamba, kwa sababu ni sehemu ya familia, huyu mtoto ama kijana anapaswa kushiriki katika hizi shughuli mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, sasa wasiwasi wangu, sheria hii itasababisha migogoro ndani ya familia kwa maana mtoto wa mjomba ambaye amekaa miaka mitatu kwa shangazi ametumikishwa anadai, sio kutumikishwa, ameshiriki katika shughuli za uzalishaji pale akadai kwamba, yeye ni muathirika wa hizi shughuli za usafirishaji wa binadamu kwa maana kwamba, amenyonywa.

Mheshimiwa Spika, nikiangalia kwa mapana yake naona tuna changamoto sana hasa kwa huu mtindo wa familia zetu kuagiza watumishi wa ndani, mayaya. Kwa sababu, sheria hii inazungumzia sio tu namna alivyochukuliwa kule, lakini namna ambavyo anashiriki katika shughuli za uzalishaji mali, lakini bila ya kuangalia stahiki za mfanyakazi. Stahiki za mfanyakazi tunazijua kuna kima cha chini cha mshahara, tunajua bima, tunajua pension, lakini tunajua aina ya familia zetu, watumishi wetu na jinsi gani hawa mayaya wanaishi katika hizi familia. Sasa tusije tukapitisha sheria ambayo inaenda kusababisha migogoro ndani ya familia mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, mimi nina bahati mwaka…

SPIKA: Hebu rudia tena, inasemaje? Inasemaje hii kitu maana…

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, huu msamiati mpya katika hii Sura ya 432 unazungumzia suala la forced labour, involuntary servitude, lakini kuna Kifungu (b) wanasema, subjecting a person to practices similar to slavery. Ukiangalia katika tafsiri unaweza ukasema kwamba, mtu ambaye halipwi mshahara wa mwezi, kwa mfano, inaonekana kwamba, huyu mtu anatumikishwa na inaweza ikatafsiriwa kwamba, huyu mtu ni mtumwa.

Mheshimiwa Spika, katika familia zetu sisi kuna vijana ama ndugu ama marafiki ambao wanakuja mjini kutafuta fursa kwa ndugu, ama wengine kwa sababu maisha yamewashinda wanakuja kukaa kwa ndugu zao. Sasa hawa wanapokaa na kama umesoma Kitabu cha Bulicheka wanazungumzia kabisa mgeni siku ya kwanza umfanyie nini, siku ya pili, siku ya tatu mpe jembe aende akalime. Sasa isije ikawa siku ya tatu anapewa jembe aende akalime, akaja jirani na kwa sababu, sheria hii inatusababisha kwamba, mtu yeyote anaweza akapeleka taarifa, mtu yeyote yule, anaweza akaenda na wako wengi mjini, anaweza akasema kwamba, unachokifanya hicho ni utumikishwaji na ni kinyume cha sheria na ukapelekwa mahakamani ukashitakiwa.

Mheshimiwa Spika, hiki kitu kinaweza kikaparaganyisha familia nyingi tusipokuwa waangalifu. Sasa comfort yangu nataka tuone ni kwa jinsi gani sheria hii ime-take into context mazingira yetu halisi ya kiafrika.

SPIKA: Ahsante. tukifika kipengele hicho nitakupa nafasi, Mwanasheria Mkuu atakufafanulia.

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nina bahati 2007 wakati kuna Global Forum Against Trafficking pale Vienna nami pia nilishiriki. Moja ya vitu ambavyo vilituwekesha mpaka usiku mkubwa ni tafsiri.

Mheshimiwa Spika, kuna Taifa moja ambalo siwezi kulitaja kwa jina, lenyewe lilikataa kabisa kupitisha ile protocol kwa sababu ya neno moja tu, sexual tourism; wanakwambia kwamba, wao in their context hilo neno halipo na kwenye sheria zao halipo. Sasa sisi tunavyoleta maneno kama ya involuntary servitude ama forced labor wakati TANU ama CCM ilikuwa na msemo kwamba, watu wasiwe nzige, kwa maana unapoenda kwa familia lazima uwe unachangia, unashiriki katika shughuli za uzalishaji. Katika mazingira kama hayo katika context yetu, sheria hii inazungumzia vipi?

Mheshimiwa Spika, nachelea kusema kwamba…

SPIKA: Umeeleweka, litapata ufafanuzi baadaye na nitakupa nafasi nimesema ya kuchangia, unless una lingine. Kama ni hilo…

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, la mwisho ni hili suala la forced marriage na forced begging…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. (Makofi)