Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Benaya Liuka Kapinga (13 total)

MHE. BENAYA L. KAPINGA aliuliza: -

Je, ni lini barabara ya Kitahi – Lituhi kupitia Ruanda itaanza kujengwa ili kurahisisha usafirishaji wa makaa ya mawe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali lililoulizwa na Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga, Mbunge wa Mbinga Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, magari yote makubwa yanatakiwa yachukue makaa ya mawe katika eneo la Amani Makoro kwa ajili ya kupeleka maeneo mbalimbali nchini. Makaa ya mawe huchukuliwa na magari yenye uzito usiozidi tani 15 kutoka Mgodini (eneo la Ngaka) hadi Amani Makoro.

Ili kurahisisha uchukuaji wa makaa ya mawe kutoka Amani Makoro kwenda maeneo mengine nchini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Ujenzi) kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imeanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kitahi – Lituhi (km 84.5) kwa awamu ambapo mpaka sasa km 5 kuanzia Kitahi hadi Amani Makoro (Coal Stockpile) zimekamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 9,000 katika mwaka wa fedha 2020/2021 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa kiwango cha lami kwa kilometa tano nyingine. Kazi za ujenzi kwa sehemu hii zinatarajia kuanza mwishoni mwa Aprili, 2021. Aidha, ili kuhakikisha barabara yote inapitika kipindi chote cha mwaka, Serikali imetenga kiasi cha shillingi milioni 1,800 za matengenezo mbalimbali katika mwaka wa fedha 2020/ 2021.
MHE. BENAYA L. KAPINGA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha kuanzia Novemba, 2015 hadi Septemba, 2020, Serikali imejenga Hospitali 101 za Halmashauri na kuongeza idadi ya Hospitali za Halmashauri kutoka Hospitali 77 zilizokuwepo mwaka 2015 hadi Hospitali 178 Septemba, 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya kigezo muhimu kwa Halmashauri kupata fedha za ujenzi ilikuwa ni kuandaa eneo la ujenzi. Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ilikosa fedha za ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri kwa kuwa hadi wakati wa tathimini ya Halmashauri zilizotenga maeneo ya ujenzi, Hospitali ya Halmashauri ya Mbinga ilikuwa haijapata eneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 27 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Halmashauri 27 mpya nchini. Aidha, kwa kuwa sasa tayari Halmshauri ya Wilaya ya Mbinga imebainisha eneo la ujenzi, Serikali itaipa kipaumbele sambamba na Halmashauri nyingine ambazo hazina Hospitali za Halmashauri kwenye awamu zinazofuata kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. BENAYA L. KAPINGA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Makamu wa Rais kwa Wananchi wa Mbinga ya kujenga barabara ya Mbinga – Litembo – Kigonsera hadi Matiri kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Liuka Kapinga Beyana, Mbunge wa Mbinga Vijiji kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) tayari imeanza kutekeleza kwa awamu mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara tajwa kwa kuanzia na sehemu ya Mbinga – Mbuji – Litembo yenye urefu wa kilometa 24. Hadi sasa jumla ya kilometa 4.89 zimekwishajengwa kwa kiwango cha lami. Kazi hiyo itaendelea kwa awamu kila mwaka kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, wakati Serikali ikiendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami, barabara hii itaendelea kufanyiwa matengenezo mbalimbali ili iweze kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 jumla ya shilingi milioni 674.896 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu barabara ya Kigonsera – Matiri hadi Kilindi yenye urefu wa kilometa 35.32, Serikali inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali ili iweze kupitika majira yote ya mwaka.
MHE. BENAYA L. KAPINGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza upatikanaji wa maji katika Mji wa Ruanda Wilayani Mbinga?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Liuka Kapinga Benaya, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Ruanda unakua kwa kasi hivyo kuongezeka kwa mahitaji ya maji kufikia wastani wa ujazo wa lita 210,100 kwa siku ikilinganishwa na uzalishaji wa sasa wa ujazo wa lita 162,000 kwa siku. Serikali katika mwaka 2021/2022 imepanga kukarabati Mradi wa Maji Ruanda ambapo kazi zitakazofanyika ni pamoja na kujenga vituo 15 vya kuchotea maji, kujenga chemba moja ya kugawa kwenda kwenye njia kuu, kufanya ukarabati wa chanzo, kulaza bomba njia kuu na njia ya usambazaji umbali wa kilometa 22.9 pamoja na ukarabati wa matanki mawili ya kuhifadhia maji ya ujazo wa lita 50,000 na 75,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 1.39 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maji Wilayani Mbinga ukiwemo ukarabati wa Mradi wa Ruanda kwa ajili ya kuboresha upatikanaji wa maji katika Mji wa Ruanda.
MHE. BENAYA L. KAPINGA aliuliza: -

Je, ni lini Vituo vya Afya vya Mapera na Muungano vitaanza kutoa huduma ya upasuaji ambao haufanyiki kutokana na kukosekana kwa baadhi ya vifaa ikiwemo sterilizer?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali katika Mwaka wa Fedha 2019/2020 iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga shilingi milioni 400 kwa ajilii ya ukarabati na upanuzi wa Kituo cha Afya Mapera ambapo ujenzi umekamilika na kituo hicho kimeanza kutoa huduma kuanzia Julai, 2021. Mpaka sasa akinamama wajawazito 11 wamekwishanufaika na huduma ya upasuaji.

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Muungano kilianza kujengwa mwaka 2017 kwa nguvu za wananchi na fedha za mapato ya ndani ya halmashauri. Katika Mwaka wa Fedha 2019/2020 Serikali ilitoa shilingi milioni 60 ili kuendeleza ujenzi wa kituo hicho. Jengo la wagonjwa wa nje (OPD) limekamilika na limeanza kutoa huduma kuanzia Julai, 2021. Ujenzi wa jengo la upasuaji unaendelea na upo kwenye hatua ya ukamilishaji.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kujenga na kukarabati vituo vya afya nchini ikiwemo Vituo vya Afya vya Mapera na Muungano ili kuboresha na kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya, dawa na vifaa tiba kote nchini.
MHE. BENAYA L. KAPINGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga daraja linalounganisha Vijiji vya Kingoli – Litumbandyosi Wilaya ya Mbinga na Machimavyalafu Wilaya ya Ludewa katika Mto Ruhuhu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Liuka Kapinga Benaya, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, daraja la kuunganisha Vijiji vya Kingoli – Litumbandiyosi ni moja kati ya madaraja makubwa ambayo yamepewa kipaumbele na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kingoli hadi mto Ruhuhu yenye urefu wa kilometa 13.0 kwa sasa haipitiki kutokana na kukosekana kwa madaraja madogo ya kudumu katika Mito ya Linyanya na Nyamilola pamoja na daraja kubwa la Mto Ruhuhu. Hata hivyo, TARURA Wilaya ya Mbinga, ilitenga fedha katika Bajeti ya Mwaka wa fedha 2021/2022 ili kujenga madaraja mawili madogo ya Linyanya na Nyamilola na sasa hivi mkandarasi yuko anaendelea na kazi ya ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uhitaji mkubwa wa madaraja katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga na kwa kuzingatia umuhimu wa daraja linalounganisha Mkoa wa Ruvuma na Njombe kupitia vijiji vya Kingoli – Litumbandiyosi, Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini itatenga shilingi milioni 25 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya kufanya usanifu wa daraja linalounganisha Mikoa ya Ruvuma na Njombe lisilopungua urefu wa mita 40 ili kujua gharama halisi na ujenzi wake utaanza kulingana na upatikanaji wa fedha kuanzia bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024. Ahsante.
MHE. BENAYA L. KAPINGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatenga fedha za ujenzi wa Vituo vya Afya Kata za Ukata na Litumbandyosi, Halmashauri ya Wilaya Mbinga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali ilipeleka Shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi Kituo cha Afya cha Kimkakati katika Kata ya Mkumbi iliyopo Tarafa ya Mkumbi. Kituo hiki cha kimkakati kitahudumia Kata sita (6) za tarafa hiyo ikiwemo Kata ya Ukata. Ujenzi wa Kituo hicho cha Afya upo katika hatua za umaliziaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga katika mwaka 2022/2023, imetenga Shilingi milioni 500 fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya katika Kata ya Litumbandyosi.
MHE. BENAYA L. KAPINGA aliuliza: -

Je, ni lini Kata za Kiangamanka, Ukata, Kipololo na Kijiji cha Kiwombi zitapelekewa mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI, alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari na Teknolojia ya Habari napenda kujibu swali la Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga, Mbunge wa Mbinga Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kata ya Kipololo inapata huduma za mawasiliano kutoka kwa Kampuni ya Halotel iliyojenga mnara katika Kijiji cha Lunoro. Kata ya Ukata inapata huduma za mawasiliano kutoka kwa Kampuni ya Vodacom iliyojenga mnara katika Kijiji cha Ukata na vile vile kutoka Halotel iliyojenga mnara katika Kijiji cha Litoho. Minara hii imejengwa kati ya mwaka 2017 na 2019 kwa ruzuku ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Kata ya Kiangamanka na Kijiji cha Kiwombi, Serikali itafanyia tathmini ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano kata hii na kijiji hiki Katika mwaka huu wa fedha wa 2022/2023. Tathmini hiyo vile vile itahusisha uhakiki wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo yote yaliyopo katika Kata za Ukata na Kipololo, ahsante.
MHE. BENAYA L. KAPINGA aliuliza: -

Je ni lini Kituo cha Afya Mapera kilichopo Mbinga Vijijini Kitaanza kutoa huduma za Mionzi na Ultra sound?
NAIBU WAZIRI , OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya cha Mapera kilipokea fedha Shilingi Milioni 400 mwaka wa fedha 2019/ 2020 kwa ajili ya ukarabati mkubwa na upanuzi wa Kituo. Kituo hicho kimekamilika na kuanza kutoa huduma za upasuaji toka Julai 2021 na jumla ya Wakinamama 114 wamekwisha pata huduma ya upasuaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Wananchi wa Kata ya Mapera wanapata huduma ya X- Ray kwenye Kituo cha Afya cha Maguu kilichopo kilometa tatu kutoka kwenye Kituo cha Afya Mapera. Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga inashauriwa kutenga fedha kutoka kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya kujenga jengo la X-ray ili Serikali ikipatie Kituo hicho mashine ya X-ray. Ahsante.
MHE. BENAYA L. KAPINGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya ujenzi wa kiwango cha lami barabra ya Kigonsera hadi Matiri na Mbinga hadi Litembo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imetangaza zabuni kwa ajili ya kupata Mhandisi Mshauri wa kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina barabara ya Mbinga – Litembo – Mkiri sehemu ya Mbinga – Litembo/Mbuji kilometa 22 kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami ambapo zabuni zimefunguliwa tarehe 19 Aprili, 2023 na uchambuzi wa zabuni unaendelea. Baada ya usanifu kukamilika na gharama za ujenzi kujulikana Serikali itatafuta fedha za kuanza ujenzi.

Mheshimiwa Spika, aidha, kwa barabara ya Kigonsera – Matiri – Mbaha kilometa 55, Serikali inaendelea kutafuta fedha za kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. BENAYA L. KAPINGA aliuliza: -

Je, lini Serikali itapitia upya mipaka na kuweka alama za Hifadhi katika Vijiji vya Ndongosi, Mtunduaro, Litumbandyosi na Kiwombi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vya Ndongosi, Mtunduaro, Litumbandyosi na Kiwombi vinapakana na Hifadhi ya Msitu wa Litumbandyosi katika Wilaya ya Mbinga. Kwa sasa Serikali inaendelea na utaratibu wa kuhakiki msitu huo wa Hifadhi wa Litumbandyosi kwa kuwashirikisha wananchi, baada ya kukamilika kwa uhakiki huo zitawekwa alama za mipaka zinazoonekana ili kuwezesha wananchi kutambua eneo la hifadhi na hivyo kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza kutokana na kutokuwepo kwa mipaka inayoonekana wazi.
MHE. BENAYA L. KAPINGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka watumishi wa sekta ya afya kufikia asilimia 50 ya mahitaji katika Halmashauri ya Mbinga?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mahitaji makubwa ya watumishi wa afya katika Mamlaka za Serikali za Mitaa yaliyosababishwa na maboresho ya miundombinu yaliyofanyika katika ngazi ya afya ya Msingi.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 na 2022/2023 Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ilipata kibali cha ajira na kuajiri watumishi wa kada ya afya 12,653 ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga imepangiwa watumishi 68.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuajiri watumishi wa kada ya afya kadri Bajeti ya Serikali itavyoruhusu.
MHE. BENAYA L. KAPINGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Unyoni hadi Maguu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Benaya Liuka Kapinga, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali tayari imekamilisha kufungua barabara yote kuanzia Unyoni hadi Maguu yenye urefu wa jumla ya kilometa 25 kwa kiwango cha changarawe. Aidha, jumla ya kilometa 4.22 katika eneo la Mapera zimejengwa kwa kiwango cha lami nyepesi katika sehemu korofi. Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuijenga barabara yote kwa kiwango cha lami. Ahsante.