Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Benaya Liuka Kapinga (23 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru awali ya yote niungane na wenzangu hasa Mbunge wa Jimbo la Mbozi kwa masikitiko makubwa kusema kwamba sisi wa mikoa ya Kusini hususani Jimbo la Mbinga tumesahaulika sana, wananchi wa Jimbo la Mbinga kwa muda mrefu tukitambua kwamba wao ndio wakulima wakubwa nchi hii,wazalishaji wakubwa wa mahindi wazalishaji wakubwa wa kahawa lakini pia sisi ni wachimbaji wa madini mmesikia habari za mpepo mpepai ni wachimbaji wa madini sasa hivi tunachimba makaa ya mawe lakini kwa muda mrefu sana sana Mbinga imetengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni hivi tu karibuni tumebahatika kupata barabara moja inayotoka Mbambabay inapitita Mbinga inaenda Songea sasa pale inagawika nyingine inaenda Mtwara na unaweza kuja makambako njombe na kuendelea kwa mara ya kwanza lakini tumesubiri tangu kupata uhuru nchi hii. Wananchi wa Mbinga ni watiifu sana katika nchi hii na tangu hapo hawajawahi teteleka wamebaki kuwa watiifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi wa kwanza niliuliza swali hapa kuhusiana na barabara ya kutoka Kitai hadi Lituhi, nikajibiwa hapa majibu vizuri sana, barabara hiyo tutuijenga kwa awamu kuanzia mwezi wa nne majibu yale wananchi wanayasikia nimeenda hivi karibuni hapa wananiuliza mbona kimya imekuwaje kwa bahati nzuri nimepata swali la nyongeza Bunge hili nikaambiwa wako kwenye utaratibu wa tenda tena sio kwa kiasi kidogo tunaitengeneza hii barabara yote kuanzia Kitai mpaka Lituhi ikipitia Rwanda Ndongosi, na maeneo mengine. Lakini sasa lini tunaanza kuitengeneza hii barabara ilikuwa mwezi wa nne hamna kitu hii ni mwezi wa tano tunaenda na humu kwenye bajeti nashukuru nimeona kidogo kwa nini nasema kidogo nimeona hii barabara ina kilometa 90. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hapa nimeona bilioni 11 na milioni 500 lakini maelezo yanasema kuna vipande vipande vya kwenda kulipa madeni kumlipa mkandarasi aliyekamilisha barabara ile ya kutoka Mbinga Mbambabay sijui ni kiasi gani. Lakini inaenda kulipa kipande cha Namtumbo sijui ni kiasi gani inaenda kulipa tena kipande kingine kule juu Masasi sijui sasa najiuliza na nashangaa, ni kiasi gani kinaenda kujenga hizi kilometa 90. Mambo haya ni ya ukweli au ndio yaleyale tunayosema sisi wa kusini sasa tusubirie wenzetu wamalize kujengewa hizo barabara zao kwa kweli kwa mtindo huu naungana na Mbunge wa Mbozi tuko tayari kufanya kitu hapa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani kwani sisi sio watanzania sisi ni watanzania tunalipa kodi na tunazalisha sana kwa nini tusijengewe na sisi barabara kama huko zinakofumuliwa hizo nyingine. Kwa hiyo, ndugu yangu Mbunge wa Mbozi mimi niko tayari kukuunga mkono kichwa miguu kila kitu tukubaliane hapa na sisi tujengewe barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi wa kwanza pia nimeuliza hapa swali Rais wa nchi hii alipokuwa anapita kuomba kura alitoa ahadi ya kujenga barabara kwa kiwango cha lami, kuanzia Mbinga kwenda Litembo. Litembo ndiko sisi tunakotibiwa kuna hospitali ya misheni kule miaka yote tangu uhuru ndio inayotusaidia sisi, namna ya kufika hapo Litembo ni shughuli kubwa. Naibu Waziri Engineer Kasekenya anafahamu lakini pia hata Naibu Waziri wa TAMISEMI nilienda nae mpaka Litembo alishika mikono kichwani kwamba ehh hivi mnapitajepitaje huku tulimpeleka hivyo kwa hiyo yale uliyosema kwamba tuwapeleke.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilijaribu kumpeleka Naibu Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Silinde, halishika mikono kichwani na tulimchangulia kinjia fulani cha kujipenyeza angalau lakini tungempitisha zile njia tunazopita sisi nadhani angemwambia dereva arudishe uongo, ukweli yule pale anasema kweli hali ni mbaya sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa bahati nzuri barabara ile kabla ya awamu hii alifika Rais wa Awamu ya Nne baada ya kuona matatizo kwenye ile barabara akatoa ahadi ya kujenga kwa kiwango cha nini cha lami. Miaka kumi ile imepita tumefika Awamu ya Tano ikatolewa ahadi imepita na bahati nzuri Awamu hii ilikuwa ya Tano imeingiliana hivi Rais wa sasa hivi ndiye aliyepita kule alienda akaja akatupa ahadi.


Mheshimiwa Naibu Spika, nimeuliza swali hapa majibu yale hayaeleweki mpaka sasa hivi sijui nitawaambia nini wananchi wa Mbinga kwamba lini ile barabara itaanza kujengwa na naomba sasa ile ni ahadi ya Rais wa nchi hii. Naomba kupata ufafanuzi lini ahadi ile inaenda kutelezwa ni pamoja na barabara ya kutoka Kigonsera kwenda hadi Matili lakini hiyo barabara inaenda mpaka Hinda kwa Mheshimiwa Eng. Stella Manyanya na yenyewe ipo hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliuliza swali hapa hiyo ni ahadi ya Rais kwamba tunakwenda kujenga barabara hizi kwa kiwango cha lami Mheshimiwa…

NAIBU SPIKA: Ahsante sana muda umeisha Mheshimiwa kengele imeshagonga.

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Sio ya kwanza?

NAIBU SPIKA: Ni ya pili!

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, basi kwa shida sana naunga mkono hoja. (Makofi)

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi asubuhi ya leo siku ya kipekee, siku maalum iliyopatikana kwa maamuzi yako makubwa kwa nia njema kabisa ya kuisimamia Serikali, kwa maneno hayo kwa dhati kabisa nakupongeza wewe na kwa kweli umeonesha kwamba yanapofikia mambo haya mazito your very serious, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakushukuru pia mimi Benaya Kapinga, hivi karibuni umenipeleke kwenye Kamati hii nzito, Kamati ya LAAC, kwa hiyo, nakushukuru kwa uteuzi napata nafasi ya kuisaidia nchi yangu lakini kuona namna gani Watumishi tuliowapa dhamana wanavyokwenda kutuvuruga, wanavyokwenda kuharibu rasilimali ambazo Seirkali imeziweka kwa ajili ya kusaidia nchi. Kwa hiyo, nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimia Spika, nitajielekeza katika maeneo mawili, matatu. Ripoti za Mkaguzi zimetuonesha kuna mapungufu makubwa kwenye utekelezaji wa maagizo na mapendekezo. CAG anasema katika Taasisi za Serikali hizi hususan Halmashauri kuna shida kubwa ya kutekeleza maagizo yanayotolewa. Kwa nini maagizo yanatolewa, au mapendekezo yanatolewa, CAG anapofanya ukaguzi anakutana na vitu tofauti tofatui, anaona dosari tofauti tofauti, ndipo inafikia hatua ya kutoa mapendekezo ili kuondoa hizo dosari. Pia Bunge linapoona kuna dosari hizo ndiyo linakuja kutoa maagizo. Sasa inapofika huyu anayeagizwa hatekelezi yale maagizo inakasirisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, taarifa zinasema mwaka uliotangulia walitoa maagizo zaidi ya Elfu Kumi, kati ya hayo ni maagizo 3,511 tu ndiyo yaliyotekelezwa. Sasa najiuliza wewe ni mwalimu, kule chuo ulikuwa unatoa assignment mwanafunzi harejeshi, unatoa assignment, hivi mwisho wa siku si unajua hatua inayofuata? Nami napendekeza hapa kwa taasisi ama Halmashauri ambazo hazitekelezi haya maagizo kwanza zinaonesha kiburi, jeuri. Kwa nini zinafanya hivyo? Nia ni moja tu Halmashauri za namna hii ni kuzichukulia hatua kali ikiwemo kuziondosha mezani, hakuna haja kuendelea baadhi ya Halmashauri hapa naambiwa zina hoja hizi miaka Kumi, zina hoja hizi miaka saba, kila zinaitwa mezani, zinapigwa maneno zinaondoka, kesho tena…

Mheshimiwa Spika, kwa kweli jambo hili linonesha kupunguza hadhi ya Bunge ambayo inatoa maagizo. Sasa tusikubaliane nalo tuchukue hatua kubwa ikiwemo kuzifukuza hizi Halmashauri na kama zitarejea basi hatua kali zidi ichukuliwe dhidi ya Halmashauri hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee pia suala la upotevu wa mapato, taarifa zinasema kuna upotevu mkubwa sana wa mapato ya Serikali, yako maeneo tofauti tofauti ambayo yanayosababisha upotevu wa mapato ya Serikali ikiwemo wakati wa makusanyo, pia wakati wa matumizi. Katika wakati wa makusanyo, ziko Halmashauri hazipeleki fedha benki, hapa taarifa inasema katika mwaka wa ukaguzi zaidi ya Bilioni 20 hazikupelekwa benki, sasa najiuliza hizi fedha zilienda wapi? Hawa watu wanafahamu sheria iko wazi, ukikusanya ndani ya muda fulani unatakiwa upeleke fedha benki. Sasa kwa vile wanayo mikakati yao na namna yao, Serikali imeanzisha utaratibu mzuri wa makusanyo kupitia POS, inafika baadhi ya sehemu hizo POS zinazimwa, baadhi ya hizo POS zinakusanya fedha hazionekani, baadhi ya hizo POS zinakusanya fedha mtu mmoja ana-ID zaidi ya mbili. Nia hapo ni mbaya sana, nia ovu ya kutaka kutumia hizi fedha za Serikali, sasa Bilioni 20 hazipelekwi benki zinaenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tunaambiwa Bilioni 33.9 hazikukusanywa kabisa, kwenye maeneo ya ushuru wa mazao, kodi za pango, mauzo ya viwanja, leseni za vileo, sokoni, pamoja na ushuru wa hoteli hazikusanywi. Sasa hapa ni mipango inayofanywa na baadhi ya hawa watumishi, wanafanya mipango wanachukua kidogo cha chini cha juu wanamwachia Serikali inapata hasara.

Mheshimiwa Spika, ninaomba sana tuweke maazimio hapa makali, ya kuwataka Wakurugenzi hawa watekeleze Sheria na Kanuni za Fedha, muda mfupi huu wanapokusanya hizi fedha wazifikishe benki na ambaye hajapeleka hizi fedha benki hatua kali ichukuliwe, ikiwemo pia na kumfunga, kwani wezi hawafungwi? Huyu mtu ambaye hapeleki fedha benki kwa maksudi.

Mheshimiwa Spika, nasema nakushukuru kwa sababu ninashuhudia pale tunapofanya mahojiano na Maafisa Masuuli, sababu zingine unaona ni za kawaida mno haifai kabisa. Kwa sababu naona kengele ya kwanza imenigongea na sijui tunachangia dakika ngapi ni dakika Tano ama dakika Kumi? Naona kengele imenigongea Mheshimiwa Spika.

SPIKA: Imegonga ya kwanza, kwa hiyo wewe malizia.

MHE. BENAYA L. KAPINDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Eneo lingine ambalo linatupotezea fedha nyingi ni eneo la uwekezaji. Taarifa hapa imesomwa na Wenyeviti wetu wametuambia, uwekezaji huu kwa baadhi ya Halmashauri wanaufanya na wamelenga kupeleka kwenye maeneo hasa mawili, stendi na soko. Imejidhihirisha maeneo hayo baadhi ya Halmashauri hayana tija. Ningeshauri Sana soko na stendi zijengwe kwenye maeneo labda ya Miji mikubwa na halmashauri za Majiji lakini kule Vijijini tuwe na stendi za kawaida sana ambazo hazina sababu ya kutumia fedha nyingi.

Mheshimiwa Spika, mfano Jiji la Mbeya walikopa fedha kujenga soko la Mwanjelwa, zaidi ya Mabilioni yamewekwa pale na taarifa ya CAG inatuambia deni lile linatakiwa lirejeshwe kufikia 2033, Halmashauri inapaswa kurejesha kila mwaka zaidi ya Shilingi Bilioni Mbili lakini mapato halisi ya pale Halmashauri ni Shilingi Milioni 750 hadi Shilingi Milioni 850, sasa watapata wapi fedha hizo zaidi ya Bilioni na kidogo ili kurejesha benki, tena benki ya kibiashara, hiyo hasara kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, bahati mbaya miradi hii wakati mwingine inafanyika pasipo kufanyika kabisa wanaita tathmini na upembuzi yakinifu, lakini cha zaidi kile kinaitwa project plan - andiko la kibiashara, andiko la kibiashara ndiyo litaonesha mradi huu hapa utakaa kwa namna gani, utatoa faida kiasi gani mpaka mwaka gani, sasa watu wanakwenda wanaweka tu mradi pale hawajafanya chochote wanaleta Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, ninaomba hapa kwamba tusikubali kuruhusu mradi wowote pasipokuwa na tathmini, upembuzi yakinifu wa eneo hilo. Lakini tusikubali kuanzisha mradi pasipo kuwa na hili andiko la kibiashara ambalo litatuonesha faida na muda wa kupata faida huo mradi.

Mheshimiwa Spika, naomba niongelee pia miradi iliyotelekezwa. Taarifa ya CAG inatuambia kwamba ipo miradi ya zaidi ya Bilioni 41.5 imetelekezwa kwa muda mrefu. Miradi hii ukiwauliza Maafisa Masuuli wanasema hii miradi ni ya nguvu za wananchi, mwananchi anapoibua mradi maana yake kaona tatizo anataka kuondokana na lile tatizo, kwa hiyo, hii miradi ni muhimu kuliko hata haya masoko na vingine. Mwananchi kaona hapa tuna shida ya zahanati anaona hapa kuna shida, jambo hili tuitake Serikali itenge fedha nyingi najua inatenga fedha lakini iongeze zaidi fedha ili miradi hii iliyoanzishwa na wananchi ikamilike na lengo la kuanzisha ile miradi kwa wananchi litimie kuliko ilivyo sasa tunawavunja moyo sana wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikupe mfano mmoja.

SPIKA: Utamalizia na huo mfano.

MHE. BENAYA L. KAPINDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Katika Halmashauri yangu kuna ujenzi wa zahanati, zahanati ile imejengwa toka mwaka 1995 imepauliwa mpaka leo ipo hivyo hivyo, yaani imeisha kupauliwa. Sasa ukiona eneo inapotolewa huduma utalia, ni kibanda tu kamepigwa bati hapo ndipo wanakotolea huduma, hapa kuna jengo nzuri, fedha imeenda pale, tena wanasema wananchi walikuwa wanachota maji mbali kweli toka mwaka 1995 hadi leo zahanati ya Kilanga Juu Kata ya Mbuje, lakini Maafisa hawa Masuuli wapo, Afisa Mipango yupo miaka inaenda, miaka inaenda hawaoni hata sababu ya kukamilisha ile miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hii miradi kama nilivyosema Serikali ipeleke fedha nyingi pia hata Halmashauri zenyewe kuliko kuanzisha miradi mingine ikamilishe hiyo miradi iliyopo. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa mchango wangu katika Wizara hii nyeti. Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kuendelea kuaminiwa na Mheshimiwa Rais na Naibu wake. Najua ni wachapa kazi, kwa hiyo niwapongeze sana. Vile vile niwapongeze wataalam ambao wako katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais mwaka jana alirudisha furaha kwa watumishi waliokuwa wameondolewa kazini kwa kusema ile asilimia tano irejeshwe kwa watumishi ambao awali ilionekana hawana haki ya kulipwa chochote. Jambo hili limerudisha furaha kubwa kwa watumishi ndani ya Tanzania hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi wale wameanza kulipwa, baadhi yao wamelipwa, lakini bado kuna watumishi hawajalipwa. Kwa hiyo niiombe Serikali ifanye jambo hili haraka kama agizo lilivyotolewa ili ile furaha ambayo watumishi walianza kuwa nayo iendelee na iwepo, isije sasa ikaonekana jambo hili limesemwa halafu watumishi wanaendelea kusononeka, wanarudisha masikitiko na masononeko kwa Serikali yao ambayo inawapenda sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, nizungumzie suala la ajira. Amezungumza vizuri sana mwenzangu Mheshimiwa Ezra hapa. Ikumbukwe na ifahamike sisi hapa hatusemi maneno yetu wenyewe, yale yote tunayoyazungumza ni maneno ya wale waliotutuma kuja hapa Bungeni. Kule kwenye maeneo yetu ndiko wanakoenda hao watumishi wanaoajiriwa kwa mtindo ule ambao Waziri wa TAMISEMI jana alizungumza hapa. Ni utaratibu mzuri, lakini ule utaratibu una manung’uniko huko kwenye majimbo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, manung’uniko ni mengi sana. Baadhi ya wananchi wanasema ajira hizi zinatolewa upande fulani na wanataja. Naogopa tu kusema hapa, kwa sababu wanawaona mtu fulani kwa jina na majina yanafahamika. Unaona Walimu wameletwa labda 10, katika 10 wale nane majina yanafanana ni ya maeneo fulani. Kwa hiyo, wananchi wanasema kwamba ajira hizi zinatolewa kwa ukanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maneno yale wanatupatia sisi kama wawakilishi wao. Sasa kwa sababu tunakuwa hatuna takwimu, hatuna data pale za kusema kwenye jimbo langu mimi hapa, kwenye halmashauri yangu hii mimi wametoka watumishi wa ngapi? Kwa hiyo, hapa ndio namuunga mkono Mheshimiwa Ezra kwamba idadi ile ikigawanywa kwa halmashauri zote pengine sisi tutakuwa na majibu mazuri kwa wale wananchi tofauti na ilivyo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana jambo hili watusikilize, hatuna nia mbaya na Serikali yetu, tunaipenda sana, najua Serikali zinaongea, Serikali inazungumza, wafanye mawasiliano watusikilize. Kwanza, watoe kwa wale waliokuwa wanajitolea, lakini pili kwa kila jimbo, kwa kila halmashauri basi kuwe na idadi fulani ambayo mimi Mbunge nikienda kuongea nasema hapa bwana kuna orodha ya watu hawa ametoka katika halmashauri hii, itakuwa imekaa vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nilikuwa nataka niongelee suala la ujibuji wa barua. Watumishi wetu hawa wanaandika barua pengine wanakuwa na vikwazo na matatizo fulani kwenye idara husika au eneo fulani analofanyia kazi. Anakuwa amesimamishwa au ana jambo tatizo fulani anaambiwa aandike barua. Anaandika barua, mwisho wa siku anakata rufaa, ipo kwenye Wizara ya Mheshimiwa Waziri, majibu yale hayarudi, inachukua muda mrefu sana watu kujibiwa majibu. Sasa sijajua hiki kitengo hakina watu wa kutosha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama shida ni hiyo, basi waongezewe watu. Mpaka leo nina watu 18 wamepeleka barua toka mwaka 2022. Wale walioondoshwa kwa vyeti fake wamepeleka barua katika Ofisi ya Mheshimiwa Waziri, lakini mpaka leo hawajajibiwa. Sasa kutojibiwa inakuwa kero kwa Serikali, inakuwa kero kwa Mbunge, inakuwa kero kwa Serikali iliyoko pale eneo husika kwa maana ya wilaya na halmashauri, kila siku watu wanahudhuria ofisini hapo. Niombe sana Mheshimiwa Waziri aimarishe hiki kitengo, kijibu zile barua, kama ndio iwe ndio, kama hapana iwe hapana ili lile suala liwe limefungwa. Tofauti na ilivyo sasa kila leo simu, kila leo message, kila leo ofisini, tunakuwa hatujaimarisha utawala bora katika nchi yetu. Naomba sana hili tulifanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la wastaafu na pensheni; wastaafu wetu hawa wamelihudumia Taifa hili kwa uadilifu mkubwa sana. Wanafika sehemu wanastaafu, wengine wanalipwa kwa muda, lakini watu wengine wanapata shida sana kupata mafao yao. Hata hivyo, wanaweza kuwa wamepata mafao, kuja kupata yale mafao ya mwezi hawapati. Vilevile hawapati saa nyingine si kwa sababu yake yeye kuna kitu kinaitwa tozo. Sasa hii tozo mimi nimeifuatilia, haimhusu yule mtumishi aliyefanya kazi akamaliza muda wake, amekwenda pale ale pensheni yake anaambiwa bwana Serikali, sijui taasisi fulani haikulipa hii tozo. Sasa hii tozo inamhusu nini huyu mtumishi? Jambo hili linaumiza sana, jambo hili halikubaliki.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Matiko, taarifa.

TAARIFA

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu kumpa taarifa msemaji anayechangia kuhusiana na kadhia wanayoipata wastaafu. Ni kweli alivyosema yaani imekuwa kero. Kwa mfano, mstaafu amepandishwa cheo, alikuwa na cheo fulani amepanda kwenda ngazi fulani ambayo mshahara umepanda, lakini anapostaafu analipwa kikokotoo cha mshahara wa awali sio ambao amepanda cheo. Akiuliza anaambiwa Serikali haikuleta hayo makato. Inatakiwa ulipe kwanza yaani achukue hela pembeni alipe hiyo tozo ya Serikali ili aweze kupewa mafao yakeo. Kwa hiyo, imekuwa ni kero wastaafu wanateseka sana, wengine mpaka wanaweza kufa kabla hawajapata mafao yao.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Benaya Kapinga unapokea taarifa?

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hii tena kwa mikono miwili na ndio ilikuwa hoja yangu ya pili kwamba pamoja na ile ya tozo ambayo nilikuwa naisemea kwamba, hii tozo ni ama taasisi aliyokuwa anaifanyia kazi ama Serikali ilichelewa kupeleka kwenye Mfuko husika. Huyu mtumishi yeye makato yake yalishakwenda, lakini Serikali au taasisi fulani imechelewa kupeleka ile tozo, gharama yake sasa inamrudia mtumishi. Hili jambo si sawa wala sio haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako watumishi sasa hivi katika halmashauri yangu wanahangaika na hilo, hawalipwi mafao yao wana miaka mitano. Hawalipwi pensheni yao ya mwezi kwa sababu tu halmashauri haikupeleka tozo, kwa sababu tu Idara ya Elimu wakati huo haikupeleka tozo. Sasa hii tozo jamani, Serikali si wanaongea? Kwa nini wasizungumze huyu mwananchi raia wa kawaida apate haki yake, aendelee kula. Ameshafika miaka 60, miaka yenyewe ya kuishi mwisho 70, sasa atapata lini hela yake? Kwa kweli jambo hili si zuri na si sawa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ndilo hilo alilosema Mheshimiwa Esther kwamba tunachelewa kuwapandisha vyeo hawa watumishi au anapata barua halafu mshahara hauingii miezi mitano au mitatu. Mwisho wa siku anakuja kupata mshahara wa mwezi mmoja, calculation inayokuja kufanyika inafanyika ile ya kule nyuma sio ile stahiki yake na analipwa hicho, mtumishi huyo anaendelea kuhangaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri, najua yeye ni mchapakazi kweli kweli na ndio maana Mheshimiwa Rais anamwamini na anaendelea kumwamini, naomba hili jambo wakati huu yupo liishe. Vile vile na watumishi kama wananisikia wawasaidie Waheshimiwa Mawaziri hapa, wasikae tu sisi tunasema hapa, tunawasema hawa, wao kule wanafurahia wanafanya mambo yao kama inavyofanyika siku zote. Si jambo jema, wafanyeni kazi kizalendo, waisaidie nchi hii, wamsaidie Mheshimiwa Rais wa Nchi hii kuondoa kero katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulisemea ni suala la Sekretarieti ya Ajira. Tulianza vizuri ilikuwa inaenda vizuri na ilikuwa inafanya kazi vizuri. Najua lengo la Serikali ni kuleta umoja ndani ya nchi yetu. Haya mambo tunayosema ukanda fulani ili yasijitokeze, lakini sasa hivi zimeibuka baadhi ya tasisi zinataka zenyewe sasa ziajiri zenyewe. Jambo hili sio jema tutarudi kule kule ambako tunafikiri sasa ukanda ule ndio utaendelea zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yalikuwepo maneno TRA wamejaa watu wa ukanda fulani, Bandari wamejaa watu wa ukanda fulani wakati fulani, lakini hapa katikati yalipungua sana. Kwa hiyo, niombe tuiboreshe Sekretarieti ya Ajira, badala ya kufikiri kurudisha tena kule hizi taasisi zikawa zinaajiri zenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami niungane na wenzangu kwa dhati kabisa kuipongeza bajeti hii. Ni bajeti ambayo inaenda kuisaidia nchi, inaenda kumkomboa mwananchi wa chini kabisa. Naipongeza Serikali kwa nia ile ya dhati ya kupeleka mikopo kwa vyuo vya kati na pia kuwapeleka wanafunzi kwenye vyuo nao wakasome kwa elimu bure. Suala hili linaoenesha kwa kiasi gani Serikali hii ya Awamu ya Sita ilivyo sikivu. Kwa sababu maoni haya yalitolewa hapa, walishauri Mawaziri hapa, na muda siyo mrefu Waziri wa Fedha amekaa chini, ameshauriana na Mheshimiwa Rais, leo tunaambiwa watoto wataenda kusoma bure, kwa maana ya vyuo hivi, pia na mikopo kwa vyuo hivi vya kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli suala hili litapunguza kero kubwa kwa Mtanzania wa kawaida na kwa sisi viongozi, Wabunge baadhi yetu tulikuwa tunahangaika kusomesha hawa wanafunzi pale ambapo wamekuja maofisini kulia kwamba hawana ada. Serikali hii ya Awamu ya Sita imeliona hili na sasa inaenda kulifanyia kazi. Naipongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naendelea kuipongeza Serikali hii kwa kuendelea kutenga fedha nyingi kwenye kilimo. Tunajua tulianza na shilingi bilioni 294 bajeti ya nyuma kidogo, lakini bajeti ya mwaka 2022 na bajeti hii inaonesha wazi kwamba Serikali hii ina nia juu ya kilimo. Ina nia ya dhati kukitoa kilimo kule kulipokuwa na kukipeleka sehemu nyingine. Safari hii Mheshimiwa Waziri mmekitengea kilimo shilingi bilioni 970. Ni fedha nyingi sana hiyo, itaenda kufanya mambo mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia hapa maoni ya Wabunge wenzangu, nami nina mchango kidogo hapo. Tunapokitoa kilimo kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa kutenga hizi fedha nyingi, tunatarajia uzalishaji mkubwa, tunatarajia wingi wa mazao. Kwa maana ya wingi wa mazao, tunatarajia kuwa na soko zuri. Sasa ziko hofu zinazoonekana hapa kwamba baadhi ya malighafi kutoka nje zimepunguziwa kodi. Kwa kupunguza kodi unasababisha mazao yetu tunayozalisha hapa nayo yashuke bei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo moja kwa Watanzania wenzangu hapa, zao likiwa halina bei hawalimi. Hawatalima. Hofu iliyopo hapa, tutarudi nyuma; watu wataacha kulima. Tunajua kuna maeneo waliacha kulima kahawa, kuna maeneo waliacha kulima mahindi, kuna maeneo waliacha kulima mbaazi, kuna maeneo watu waliacha kulima hata korosho. Sasa kwa nini ifikie huko wakati nia yetu ni njema, Mheshimiwa Rais amefanya kazi nzuri ya kutafuta hata wawekezaji huko nje wa mazao yetu. Kwa nini tukaribishe hizo bidhaa nyingine kutoka nje kwa kuweka kodi? Hata Mheshimiwa Waziri amesema kwamba kodi imebaki vilevile, mapendekezo yangu ni kwamba ingebidi wewe uongeze ili alizeti yetu ipate soko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, jana, juzi na majuzi yaliyotangulia, nimepigiwa simu nyingi sana na wananchi wangu. Sisi kule tunazalisha na tunamshukuru Mungu mwaka huu mvua ilinyesha kiasi cha kutosha. Kwa hiyo, tuna mahindi mengi sana. Mwaka 2022 niliuza swali hapa kwa Waziri Mkuu, na Waziri Mkuu alitoa maelekezo hapa kwamba hatufungi mipaka. Nami sijaona katazo hilo kwamba mazao sasa yasiuzwe nje, lakini sasa hivi ziko hofu huko mitaani, wanasema vibali vya kupeleka mazao nje vimezuiliwa. Hali hii imesababisha mahindi yetu pale jimboni yalikuwa yanauzwa shilingi 75,000 kwa gunia, sasa yanauzwa shilingi 35,400 mpaka shilingi 40,000. Hii inamkatisha tamaa mkulima. Juzi tu hapa tulikuwa tunaongelea mahindi, yalikuwa yanauzwa shilingi 80,000 mpaka shilingi 90,000, leo hii tuna vuna mahindi... (Makofi)

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. BENAYA L. KAPINGA: …kwa kusema yasiuzwe nje, mahindi tunaenda kununua shilingi 35,000 na shilingi 40,000/=…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Benaya, kuna taarifa.

TAARIFA

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kumpa taarifa Mheshimiwa Kapinga ambaye anachangia vizuri sana, kwamba tatizo hili kufungwa kwa soko la mahindi nje, limekuwa ni kero kubwa kwa mikoa yote ya Nyanda za Kusini. Hata Jimbo la Lupembe mahindi yameporomoka bei sana. Tunaomba Serikali itoe kauli, hili jambo likoje? Ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Benaya Kapinga, unaipokea taarifa hiyo ya Mheshimiwa Swalle?

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea hii taarifa kwa sababu ni kweli. Nami hofu yangu ni kwamba sijasikia kauli ya kukataza mahindi yasipelekwe nje, nilichosikia tuwe na hifadhi ya chakula ndani ya nchi, lakini siyo kwamba tusiuze nje. Sasa naiomba Serikali, Mheshimiwa Waziri wakati anakuja kuhitimisha hapa, atuambie, ni kweli kuna katazo la mahindi kutouzwa nje? Ni kweli lipo hilo katazo? Nasema hivyo kwa sababu wananchi wetu wamelima vizuri, waliitikia vizuri wito na kweli uzalishaji ni mkubwa na wala hatutakuwa na njaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo ningependa kuiongelea hapa ni suala la miradi ambayo tunaendelea kuitekeleza katika nchi yetu. Niipongeze sana Serikali hii imekuwa na jitihada kubwa ya kupeleka fedha nyingi katika miradi kwenye kila eneo la nchi yetu na miradi inaonekana na katika Jimbo langu nashukuru sana tulikuwa na shida ya barabara tulipata barabara ya kwanza ya kutoka Songea – Mbinga hadi Mbamba Bay na kipindi hiki tumepata mkandarasi anajenga barabara ya kutoka Kitai kwenda Rwanda hadi Litui lakini barabara hii imesimama kwa muda mrefu. Toka mwezi wa pili barabara hii haiendelei hawajengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii inapitisha magari makubwa makubwa ya makaa ya mawe. Magari zaidi ya 3,000 mpaka 4,000 yanapita lakini barabara hii ni ya vumbi. Sasa hivi tayari tumeanza kupokea taarifa za vifo kwa sababu magari yale yanavyopita vumbi jingi wanagongwa watu, zinatokea ajali watu wanavunjika. Kwa kweli inakuwa ni hatari kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii tuliambiwa ingejengwa kwa miezi 12 lakini sasa miezi 12 kuanzia mwezi wa pili, wa tatu, wa nne, wa tano na huu wa sita miezi mitano kazi haiendelei. Kweli tutaenda kukamilisha hii barabara kwa miezi 12? Shida kubwa anayosema mkandarasi Mheshimiwa Waziri hajalipwa. Hajalipwa tangu, ameleta certificate huko hajalipwa. Kwa hiyo hawezi kufanya kazi ameleta certificate ya kwanza, ya pili, ya tatu. Ombi langu Mheshimiwa Waziri tumlipe huyu mkandarasi ili ile barabara ijengwe ikamilike, itumike kwa sababu ina manufaa makubwa sana kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama makaa ya mawe yote yanayosafirishwa kwenda nje na yanayoletea pato kubwa nchi hii yanatoka pale lakini hayana njia kwa kweli inakuwa shida kubwa sana. Kwa hiyo, niombe sana mkandarasi huyu alipwe ili ile barabara iendelee na ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine niipongeze Serikali kwa mradi huu wa ETS. Mradi huu una manufaa makubwa kwa sababu una faida kwa maana ya kwamba sisi kama nchi tunajua bidhaa zetu. Tunajua idadi ya bidhaa tulizonazo na inatuletea faida kubwa. Kwa hiyo, yapo malalamiko kidogo kwamba huyu mkandarasi huyu charge zake ziko juu. Kwa hiyo, niombe Waziri kaeni na huyu mkandarasi a-charge at a minimum price kiasi kwamba isilete kero kwa wananchi kwa kweli nikupongeze Mheshimiwa Waziri kwa kuendelea na mradi huu una manufaa makubwa kwa nchi yetu. Hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze pia Serikali kwa kazi ile kubwa tuliyoifanya mwaka jana ya sensa na bahati nzuri mwaka huu tumepewa takwimu pale kwamba sasa matokeo ya sensa yako tayari na tumeyaona na kwa kweli ni sensa ya kipekee kwa sababu ina idadi ya watu, ina idadi ya makazi lakini ina idadi ya vituo vya kutolea huduma mbalimbali lakini na mifugo. Kwa kweli wataalamu wanavyotuambia ni sensa ya kipekee. Naipongeza sana Serikali yangu hii ya Awamu ya Sita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo takwimu zile tuzitumie. Tusizitumie kwa idadi ya watu tu. Siku ile pale tumeoneshwa namna huduma zilivyo sambaa. Utakuta concentration ya baadhi ya huduma ziko upande mmoja na upande mwingine una watu wengi hauna huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali kupitia hii sensa tuitumie vizuri, tugawanye mgawanyo wa huduma vizuri. Pale ambapo kuna mapungufu tupeleke huduma siyo kwa sababu tu kwamba labda kuna huduma zigawike kwa idadi kubwa ya watu aah. Hata kwa kuona kwamba zile huduma zingine kwa mfano zahanati au kituo cha afya watu wako sehemu of course ni wachache lakini wanapata huduma mbali sana kwa mujibu wa sensa umeonesha pale kwamba kituo cha afya kipo sehemu fulani na sehemu fulani huku hakuna huduma kwa hiyo watu wanatembea zaidi ya kilometa 20. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Kata yangu ya Ukata idadi ya watu kweli hiyo sifa haina lakini kwa idadi ya umbali na milima ina sifa ya kutosha kabisa. Kwa hiyo, niombe wataalamu wetu wagawanye hizi huduma kwa kutumia hizi takwimu. Wasilenge tu ile kwamba idadi ya watu ni chache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo mwaka jana na mwaka huu pia nilikuja na ombi la kugawanya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga. Ina watu wa kutosha lakini inawezekana pakawa na kigezo cha kwamba aah, huku ni vijijini na huku ni mijini, mjini kuna concentration kubwa ya watu tuka concentrate kugawa halmashauri za mjini. Kijiografia halmashauri hii ni kubwa sana kiasi kwamba mwananchi wa kule chini kuja kupata huduma anatumia muda mrefu, anatumia nauli kubwa, na wengine wanaishia tu kukaa nyumbani na kusema aah, acha tu hilo lipite hivyo lakini anainung’unikia Serikali yake. Kwa hiyo, niombe sana kupitia hii takwimu tugawe hizi huduma vizuri na zitusaidie kwa manufaa ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo ninaunga mkono bajeti hii kwa 100% kwa sababu inaenda kutusaidia sana sana, sana, ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona na kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Awali ya yote na mimi niunge mkono maazimio yote yaliyowasilishwa hapa na Wenyeviti kwani ni maazimio yaliyolenga kuiboresha na kuisimamia Serikali yetu vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishie hapo alipoishia dada yangu Mheshimiwa Salome Makamba, kipengele hiki cha TARURA. Kwanza niwape pole ma-engineer wetu nchi nzima. Wataalamu wetu hawa wako tayari kufanya kazi na wanaipenda kazi yao vizuri sana; na namna unavyoona mnavyoongozana nao mnapokagua matatizo unaona nyuso zao zinavyoumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shida ni kubwa sana kwenye maeneo yetu. Shida hii si mvua tu hizi, yapo maeneo yana mvua karibu msimu mzima wa mwaka. Kwa hiyo maeneo haya yana uharibifu kwa muda mrefu, na ma-engineer wetu hawa mara kadhaa wanaandika maandiko kupeleka TARURA makao makuu ili wapate fedha kunusuru hali iliyopo kwenye maeneo yetu huku lakini kwa bahati mbaya sana fedha hizo hazitoki, na kama zinatoka zinatoka kidogo sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii inatupa wakati mgumu sana sisi Wabunge kwa sababu ni ukweli kabisa tunakaa hapa ndani, tunapitisha bajeti na tunapata ahadi nzuri nzuri lakini utekelezaji unakuwa haupo kabisa. Jambo hili si zuri kwa sababu baada ya vikao hivi sisi Wabunge tunaenda kuwaambia wananchi kule ni nini kinakuja kutekelezwa. Hatimaye bajeti ya mwaka inaisha hali ya barabara zetu inabaki vile vile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi niombe maazimio haya ya Bunge sisi kama Wabunge tunapaswa tuyasimamie kweli kweli pasipo kuoneana aibu, pasipo kuona nani ataniona mimi nasema nini. Lazima tuisimamie Serikali yetu kwa sababu ni Serikali yetu hii. Hakuna mtu mwingine atakayekuja kuisimamia na kuisemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niseme kama walivyosema wenzangu, suala la TARURA kupata fedha lisiwe suala la kusema kwamba sasa ni shukrani, Hapana, ni wajibu wa Serikali. Taasisi hii tumeiunda wenyewe kwa sababu tunataka itusaidie, tuipe fedha ifanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitolee mfano kwenye Jimbo langu la Mbinga Vijijini. Jimbo hili lina mvua nyingi sana, Jimbo hili lina madaraja mengi sana. Nishukuru kwa awamu hii kidogo barabara zinapitika kwa sababu madaraja yamejengwa. Lakini uko ukanda mmoja bado barabara hazipitiki, mvua ikinyesha tu ujue simu kwako. Mbunge huku kuna shida hii, Mbunge hatupiti. Sasa unashindwa kuelewa hii hali itaenda hadi lini? Ifike sehemu, taasisi yetu hii ni kubwa sana, tuipe fedha. Najua uwezo wa kutekeleza na kutatua matatizo yetu wanayo. Kwa hiyo niombe sana fedha tunazotenga hapa Serikali izipeleke kama zilivyopitishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ambayo nataka kuiongelea ni namna tunavyotatua migogoro. Nchi yetu imepangwa vizuri sana; tunaanza kwa mwenyekiti wa kijiji, tunakwenda kata, tunakwenda wilaya, tunaenda mkoa na mpaka huko Wizarani. Maeneo haya yote yalivyotengwa maana yake yana uwezo wa kutatua migogoro. Hata hivyo inashangaza sana, hii migogoro mingine ni ya kawaida sana, lakini wenzetu waliopo kwenye maeneo haya kama walivyoaminiwa hawatatui migogoro hii. Wanasubiri mpaka mtu mwingine atoke huko juu anakuja kutatua ule mgogoro ambao sasa unasababisha mpaka matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mgogoro kwangu kule, maarufu unaitwa “ndika.” Nimeuzungumza hapa mara nyingi sana, ni mgogoro wa ardhi. Mgogoro huu chanzo chake ilikuwa panda miti kibiashara. Pale tuna Mkuu wa Wilaya amehangaika sana kuutatua huu mgogoro sana, ukaja haujaisha. Umefika ngazi ya mkoa haujaisha. Lakini cha kushukuru hivi karibuni Mwenyekiti wetu wa Chama aliingia kati tukaenda mimi, yeye Mwenyekiti, Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya tukaumaliza huu mgogoro. Tukaumaliza kwa kusema wananchi warudishiwe maeneo yao wawe tayari kupanda miti hiyo ya kibiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni wako viongozi wamerudi, wananchi wale wamejipanga kupanda miti kibiashara, viongozi wale wanaenda wanapiga danadana tena ule mgogoro uanze upya. Sasa wewe kiongozi uko hapa umewekwa kufanya nini? Umewekwa ili uendelee kusumbua hao wananchi? Kwa nini usimalize huu mgogoro ambao Mwenyekiti wa Chama wa Mkoa amesema uishe na tumekubaliana wananchi warudishiwe maeneo yao; kwa nini sasa leo hii wewe pekeyako unasumbua wananchi unaleta danadana? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo halikubaliki, halikubaliki kabisa. Viongozi hawa waliopewa dhamana na Serikali ni wajibu wao kumaliza migogoro kwenye maeneo yao. Wasimsubiri Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi aende akamalize migogoro kule, wao wana nafasi zao pale. Wamepewa dhamana na Serikali hii, wamepewa dhamana na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kumaliza ile migogoro. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili jambo kwangu linanisikitisha sana. Ilifika mahali hawa wananchi wako zaidi ya 400 wanasema tunataka kurudisha kadi, tunataka kurudisha kadi za CCM kwa sababu Chama hiki hakitusikilizi. Sasa tumeenda tumewasikiliza, yuko kiongozi mmoja analeta danadana anasema hapana, wasirudishiwe maeneo yao wapewe maeneo mengine. Sasa kwa nini yuko pale? Kwa nini aseme hivi? Kwa nini hakusema wakati tuko pamoja pale? Amesubiri watu tumewaaminisha wananchi kwamba maeneo yenu mnapewa halafu sisi tunaondoka yeye anageuza Kiswahili kule, anamuongopea nani? Nani anayemuongopea? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili halikubaliki na ninalisema leo hapa tukirudi huko lazima tutagombana sana, lazima tutagombana kwa sababu hatutaki kuwa waswahili kiasi hicho. Mgogoro umeonekana wananchi wamechukuliwa maeneo yao si maeneo ya mtu mwingine yaani shamba langu mimi amepewa mtu mwingine. Sasa kwa nini unapata kigugumizi kunirudishia shamba langu? Kwa hiyo hawa viongozi kwa sababu wamepangwa kiutaratibu watimize wajibu wao, wasisubiri watu kuja kuwafanyia kazi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka nilizungumzie hapa ni suala la ujenzi wa vituo vya afya. Nashukuru sana Serikali hii ya Awamu ya Sita kwa sababu kwa upande wa jimbo langu mimi mpaka tunaingia awamu ya sita hatukuwa na kituo cha afya, lakini leo hii nashukuru sana, sana, sana, tuna vituo vya afya tulivyovikamilisha vitano. Viko vituo vya afya vile vya tozo viwili lakini tuna vituo vingine tumejenga kupitia mapato ya ndani vitatu tayari tumevikamilisha lakini uhitaji bado ni mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhitaji ni mkubwa kwa sababu Jimbo lile limetawanyika sana lina kata kubwa 29; kwa hiyo kwa vituo vya afya ni vichache sana. Nishukuru kwa mpango wa Mheshimiwa Rais kwa ahadi ile aliyotupa kwamba kila jimbo litapewa kituo cha afya kimoja. Lakini hapa nataka tu kutoa tahadhari kidogo kwamba yako majimbo yana ukubwa tofauti tofauti. Yako majimbo madogo pengine vituo vilivyopo sasa hivi vimeshatosheleza. Hii kauli ya ujumla ya kwamba kila jimbo linaenda kupewa kituo kimoja kimoja pengine tungeitazama kwa jicho jingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana kabisa tunaweza kurundika sasa vituo vya afya kijiji kwa kijiji kwenye hayo majimbo mengine. Kwa hiyo ningeomba hapa, na ninapendekeza, wazo kama hilo kwenye majimbo yale makubwa makubwa basi tupeleke hata vituo vya afya viwili badala ya kituo cha afya kimoja. Vivyo hivyo hata pamoja na zile shule za SEQUIP yako majimbo sasa hivi wala hawana shida ya shule hizo tayari wameshajitosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ushauri wangu katika maeneo kama hayo; kwa mfano kwa jimbo langu mimi tayari kuna kata tatu hazina shule za sekondari. Wananchi hawa wanakwenda kilometa nyingi sana kupata elimu. Kwa hiyo pengine maeneo kama haya najua kwa namna ilivyo yako majimbo yanayofanana na jimbo langu mimi…

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kapinga, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa; Mheshimiwa Jackson Kiswaga, taarifa.

TAARIFA

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Mheshimiwa Kapinga ni rafiki yangu naomba nimshauri akazane kuomba kwenye jimbo lake asitaje majimbo ya wengine na sisi tuna mahitaji yetu. Akazane kuomba vituo vingi kwake aache na sisi wengine tuendelee na ya kwetu, ni taarifa tu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kapinga, taarifa unaipokea? Malizia mchango wako.

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siwezi kuipokea taarifa kwa sababu hafanyi utafiti yule. Hafanyi utafiti kwa sababu nilivyomwambia yako majimbo makubwa makubwa. Jimbo lake ni dogo kweli kweli sasa unaipeleka tena shule pale inaenda kufanya nini? (Makofi)

MWENYEKITI: Malizia mchango wako.

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo jimbo langu mimi ni kubwa ndiyo maana nimesema hapa sasa hivi nakosa shule tatu, yeye kwake zote zimetimia. Kwa hiyo Jimbo kama la Kalenga zile shule zinazopaswa kupelekwa kule zirudi kwenye jimbo la mimi. (Makofi/ Vicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ombi langu lilikuwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia, muda wako umeisha.

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu lilikuwa hasa kwenye upande huu wa vituo vya afya na shule tuangalie ukubwa wa maeneo halafu tuvigawe hivyo vituo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Na mimi niungane na wenzangu kwanza kabisa kumpongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na wasaidizi wake. Tunatambua Wizara hii amekabidhiwa muda mfupi, lakini anachanja mbuga kweli kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Jimbo la Mbinga Vijijini amezungumza ndugu yangu Mheshimiwa Judith, sisi wa Mbinga Vijijini kama inavyoitwa vijijini tuna changamoto kidogo ya mawasiliano. Tuna kata 29 na miongoni mwa kata hizi, baadhi ya Kata hazina mawasiliano kabisa. Mheshimiwa Judith alijaribu kuzitaja, nami naomba nirudie kwa Kata ambazo hazina mawasiliano kabisa. Kata ya Ukata, Kata ya Kipololo, Kata ya Kitura, Kata ya Kiyangimauka, Kata ya Muhongozi na Kata ya Kitumbalomo. Kata hizi ili wananchi waweze kuwasiliana lazima wasogee kata jirani ndiyo wanaweza kuwasiliana, ama wategeshe simu maeneo fulani fulani; akitikisika kidogo tu, basi hana mawasiliano tena. Sasa kwa karne hii tunawanyima fursa wananchi hawa, wanakosa fursa nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwenye randama hapa Mheshimiwa Waziri ameonesha baadhi ya kata hizi zinaenda kupata mitandao na kwa bahati nzuri katika hii taarifa anaonesha kwanza baadhi ya Kata zilipata wakandarasi muda mrefu, lakini toka mwaka 2018 baadhi ya kata hizi hao wakandarasi bado hawajaenda kujenga minara. Namwomba Waziri akija kuhitimisha hapa atueleze sisi wananchi wa Mbinga, lini na sisi sasa tunaenda kupata mawasiliano?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kizuri nimeona pia hapa kuna baadhi ya kata saba zimejengewa minara; na ile minara ni ya muda mrefu, lakini hadi leo haijawashwa. Kuna mnara upo Lunolo Kata ya Kipololo haujawashwa; kuna mnara upo Litoho Kata ya Ukata, haujawashwa; kuna mnara upo Kitura, Kata ya Kitura, haujawashwa; na pia kuna mnara upo Muhongozi, Kata ya Muhongozi, haujawashwa. Minara hii ikiwashwa angalau hizi kata nazo zitapata mawasiliano japo siyo kwa kutosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie kwamba wananchi wa Mbinga wako vizuri. Nami nashangaa haya makampuni ya kibiashara yana hofu na Wilaya ya Mbinga; sisi ni wakulima wa Kahawa, tunalima kweli kweli. Kama tuliweza kununua mashine za kusaga kila nyumba, hivi tutashindwa kununua Airtime hii! Nashangaa kweli kweli wanapofikiri uchumi wetu ni wa chini. Uchumi wetu ni mkubwa kweli kweli! Kwa hiyo, nawaomba na ni-encourage haya makampuni yasiwe na hofu na Wilaya ya Mbinga; wananchi wa Mbinga wapo vizuri kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kata moja ina uwezo wa kuingiza shilingi bilioni nane, sasa kuna shida gani hapo? Kwa kweli nawaomba sana watu wa mitandao kwa Wilaya ya Mbinga na hususan Mkoa wa Ruvuma kiujumla, kiuchumi tupo vizuri, kwa hiyo, msihofu kwamba mkipeleka mitandao kule hamtafanya biashara. Siyo sawa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sisi kule tupo mpakani. Kuwa na mtandao wa mawasiliano ni ulinzi kwa nchi. Sasa hivi tunapokea mawasiliano ya Malawi, ya Msumbiji, inakuwa haipendezi kidogo. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie kwa hilo; na anapokuja kuhitimisha hapa atueleze hizi kata ambazo hazina mawasiliano kabisa ni lini sasa na zenyewe zinaenda kuingia kwenye mawasiliano?

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha pili, yale maeneo ambayo kidogo yana mawasiliano, yanakosa mawasiliano ya Internet; hatuna kabisa mawasiliano ya Internet. Amezungumza mwenzangu hapa, ku-download kitu ni lazima ufike mjini, lakini sasa kipindi hiki kama manavyotambua mambo sasa hivi ni ya kimtandao tu; unataka kusoma, unasoma online; Serikali yenyewe inafanya kazi na kutoa maelekezo online; sasa mtu yupo kijijini kule, Afisa Mtendaji ametumiwa kitu na Mkurugenzi, hawezi ku-download. Ni lazima aende sehemu nyingine huko akatafute mawasiliano hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana, kuna baadhi ya maeneo mliweka siku kadhaa, baadaye wakatoa. Sasa sijajua kwa nini watoe? Kwa kweli naomba sana sana nasi tupate nawasiliano haya ya Internet.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, zile kata sita nilizozitaja ambazo zimeshafungiwa minara, pengine Waziri unapokuja kutoa hitimisho hapa utuambie kwa nini imechelewa? Cha msingi zaidi, ni lini sasa tunaenda kuwasha ile mitandao? Nakushukuru sana, ahsante sana kwa muda. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nami niunge mkono hoja kwa asilimia 100.

Mheshimiwa Spika, nitachangia eneo la Mradi wa Umeme Vijijini (REA). Katika jimbo langu utekelezaji wa mradi huu hauendi vizuri. Nimekwenda mara kadhaa kwa Mheshimiwa Waziri, nimemuomba afanye ziara aje ashuhudie kinachoendelea. Bahati nzuri aliniahidi mwezi wa pili tungeenda naye lakini bahati mbaya mambo yaliingiliana hakufanikisha. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri afanye ziara hiyo kwa sababu haiwezekani hapa kila Mbunge anayesimama anampongeza ameenda mara mbili, tatu au nne kwenye jimbo au wilaya yake, sasa mimi nashindwa kusema. Kwa hiyo, naomba na mimi nataka nije hapa kusema alikuja jana, juzi na siku nyingine.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa ni vijiji 34 tu ndivyo vilivyofungiwa umeme kati ya vijiji 117, kata 16 zote hazina umeme ziko gizani. Hata hivyo vijiji 34 ni kituko, utakuta kijiji kimoja ni nyumba sita tu ndiyo zimeingiziwa umeme. Sasa hivi kuna wananchi 2,100 waliomba kufungiwa umeme katika nyumba zao, wameshafanya kila kitu na wamelipia mita, ni zaidi ya miaka mitatu baadhi ya wananchi hawa hawajafungiwa umeme. Navyomuomba twende akashuhudie tafadhali afanye hivyo.

Mheshimiwa Spika, wiki iliyopita Baraza la Madiwani limekaa kikao na lilitoa maazimio. Azimio mojawapo ni la kunitaka mimi nishike shilingi mpaka Waziri aende kule akawaambie ni lini watafungiwa umeme hawa wananchi 2,100 ambao zaidi ya miaka miwili, mitatu wamelipia umeme lakini hawafungiwi; mita hazipo, vifaa fulani havipo, sasa tunafanyaje?

Mheshimiwa Spika, siyo hivyo tu kuna Kata tatu za Matili, Mkumbi na Litembo tulisema miradi ingekamilika Desemba lakini haikukamilika. Miradi hii mingine ni ndani ya miaka mitano ya kipindi kilichopita leo zinakuja nguzo, kesho wanaleta nyaya, keshokutwa wanachimba mashimo mpaka leo miradi hii wananchi hawajaona umeme. Kwa hiyo, ni kero kubwa sana mpaka wanasema hivi sisi tunachagua CCM kwa nia ipi? Wanakuwa na mawazo mengine, sasa si vizuri Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni ukatikaji wa umeme, Wilayani Mbinga umeme unakatika sana yaani usipokatika chini ya mara 15 siku hiyo kuna umeme, ni mara
20 mara 40 na kuendelea. Hali hii imesababisha wafanyabiashara kupoteza mali zao na mitaji yao na sasa hivi wengi hawafanyi biashara, shida ni nini Mheshimiwa Waziri?

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri sisi pale tuna vyanzo vya umeme pale pale; kuna watu binafsi wanazalisha umeme wa kutosha lakini unaenda kwenye Gridi ya Taifa hapa Mbinga kilometa 2 tu hamna umeme. Kuna mwingine anazalisha mjini pale lakini hamna umeme. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kutoa majumuisho hapa atuahidi anakuja lini lakini hizi kata ambazo zina mradi sasa hivi umekaa miaka mitano hauishi lini tunaenda kuwasha umeme? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa na mengi lakini naona muda huu hautoshi, niseme tu naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuwa mzungumzaji wa mwisho wa session hii ya asubuhi. Niungane na wenzangu kwa dhati kabisa, kumpongeza mtani wangu mla kale kanyama katamu, Mheshimiwa Lukuvi, hongera sana pamoja na Naibu Waziri, lakini na wataalam kule. Kwa kweli mmefanya kazi nzuri na hii inaonesha wachangiaji wamekuwa wachache tofauti na pale nyuma Wizara hii ilikuwa na wachangiaji wengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nachangia eneo moja eneo la migogoro. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Jimboni kwangu kumekuwa na matatizo mengi ya migogoro kwa muda mrefu kuanzia mwaka 2017, nina orodha hapa zaidi ya watu 3,000, hawa wananchi wa Kata ya Maguu, Kijiji cha Mkuwani na vijiji vingine vya Jirani. Hawa wananchi kwa miaka zaidi ya minne wanahangaika na maeneo yao ambayo yalikuwa mashamba sasa yamechukuliwa na Wilaya ya Nyasa kufanya mradi wa panda miti kibiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu ni mzuri sana, lakini utaratibu uliotumika ni wa hovyo mno, umesababisha tumefika mahali sasa hivi wanapigana risasi pale kijijini. Tumefika mahali wananchi hawa wanachukuliwa mali zao, tumefika mahali wananchi hawa hawawezi kufanya shughuli ya kiuchumi kwenye hayo, maeneo ambayo walikuwa wanayamiliki tangu wengine walivyozaliwa na wengine sasa hivi ni wababu, wana wajukuu na vitukuu, lakini imefika mtu mmoja tu ameamua huu mradi uanzishwe na kuwafukuza hawa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2019 alienda Waziri Mkuu, wananchi wale walishika mabango tunadhulumiwa ardhi yetu, tunadhulumiwa ardhi yetu. Waziri Mkuu alitoa maelekezo kwa viongozi ambao leo pia Mheshimiwa Waziri ametoa maelekezo hapa kwamba, viongozi waliopo huku watatue kero za wananchi. Kwa bahati mbaya sana yale maelekezo viongozi wale hawakuyafanyia kazi, wananchi hawa wamehangaika ngazi zote katika mkoa wetu hawakupata masuluhisho, mwisho wa siku waliamua kuja hapa. Namshukuru sana sana Waziri, alipiga simu na sasa hivi angalau wanapumua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri ile ahadi aliyoisema kwamba atakwenda kule kwenda kuona naomba aitekeleze, kwa sababu bila yeye hatutapata masuluhisho, kwa nini nasema hivi? Shida kubwa hao viongozi aliowaelekeza hapa na wao wana interest na maeneo hayo. Nimefuatilia nimegundua kwamba, maeneo yale viongozi wa maeneo ya kule nao wameamua kujiingiza kwenye hii miradi, sasa mwananchi akilalamika eneo langu linaporwa, hana masuluhisho hawezi kutoa utatuzi wa ile shida ikiwa yeye pia ni mmiliki wa mradi ule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, inahitaji mtu mwingine kama alivyofanya Waziri. Nimesikia hapa wenzangu wanasema tuwaachie Mwenyekiti wa Kijiji, sijui na nani anayefuata na mwingine, wengine ndio wanufaika wa hii miradi sasa atatoaje masuluhisho? Kwa hiyo, mgogoro huu umeleta shida sana sana sana, leo hii ukifika Mbinga Mheshimiwa Waziri watakupa jogoo, mbuzi na ng’ombe kwa majibu aliyoyatoa hapa siku ile kwa wale wananchi wachache waliokuja kumwona. Kwa hiyo, nimpongeze sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri, ninachosema ule mradi ni mzuri sana, ingewezekana kabisa. Kwa sababu, kwa maneno yao wanasema kwamba wameshauriwa kimazingira kwamba sasa eneo lile linatunza maji ya Ziwa Nyasa, kwa hiyo, ni lazima liwekwe vizuri, lipandwe miti, sawa. Kwa nini hawakufikia kuwashirikisha hawa wananchi wamiliki wa yale maeneo na kuwaambia sasa jamani mmekuwa hapa kwa muda mrefu, sasa hivi imefika mahalI hapa tunataka tupaboreshe tufanye mradi wa kimazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa badala ya sisi wa eneo fulani au watu fulani kuwanyang’anya ninyi maeneo yenu, basi muwe sehemu ya huu mradi, kwani hili haliwezekani? Lingefanyika hili, pengine lisingeleta usumbufu ambao sasa hivi zaidi ya miaka minne wale watu hawana sehemu ya kulima. Kwa hiyo, ninachoshauri Mheshimiwa Waziri aje na maelekezo mazuri kuhusiana na hawa wananchi kwenye ardhi ambayo wamekuwa nayo, wamekufa nayo na wengine wanaendelea kuzeeka nayo mpaka leo hii, lakini sasa hawana haki nayo kabisa. Imefika mahali wamepigwa risasi watu pale kabisa kabisa, sasa unampigaje mtu mwenye haki yake risasi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ni kweli Watanzania tuko hivyo? Kilichofanyika ni kwamba, kabla ya mwaka 2012, eneo lile lilikuwa Wilaya moja, sasa hivi Wilaya ile imegawanyika iko Wilaya ya Nyasa na Wilaya hii ya Mbinga.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Stella Manyanya.

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuwa mimi ni Mbunge ninayetoka Nyasa na kwa mchango huu unaotolewa na Mheshimiwa Mbunge, jirani yangu kuhusu mgogoro huu uliodumu kwa muda mrefu kidogo, ambao nakubaliana kwamba, mpango na mradi unaoendelea pale wa miti ni mzuri na kwa sababu mwekezaji sio lazima atoke sehemu za mbali tu na asiwe Jirani yetu. Kwa hiyo, jambo jema ni kwamba hata wao wanaweza kuendeleza katika misingi ya mradi ule lakini bila kuwa na migogoro. Kwa hiyo ninachoomba ni kwamba siku ikitokea Mheshimiwa Waziri anaenda huko, basi mimi Mbunge wa Nyasa niwepo pia, ili kuhakikisha kwamba haki zinatendeka katika pande zote mbili. Ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Benaya Kapinga, malizia mchango wako.

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na taarifa yake naipokea, nilikuwa nasubiri aongee vile alivyosema, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kugawanyika kwa mipaka hakumwondolei mtu haki ya kumiliki mali, sisi wote ni Watanzania, tuna haki ya kufanya shughuli eneo lolote ili mradi hatuvunji sheria. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri, sikuwa na maneno mengi nilitaka nimwambie hili ili aendelee kutusaidia kama alivyotatua maeneo mengine na sisi akatutatulie huu mgogoro wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi uliyonipa. Kwanza kabisa naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali ya Awamu ya Sita, kwa muda mfupi ililyoanza kufanya kazi imefanya mambo mazuri sana, imewatia moja sana Watanzania. Tulifika mahala watu walikuwa na hofu totauti tofauti lakini sasa kwa awamu hii ya sita matumaini yamerudi kwa kasi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Waziri Dkt. Mwigulu Nchemba, nimpongeze engineer Masauni pamoja na wataalamu wa Wizara hii, mmefanya vizuri sana, niwapongeze sana sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru Serikali kwa fedha waliyotowa. Kwa muda huu mfupi fedha nyingi imekwenda kwenye majimbo yetu. Tumepata fedha kwa ajili ya madarasa pamoja barabara na vilevile tutapata fedha za shule mpya. Kwa jimbo langu mimi niseme tu kata sita hazikuwa shule kabisa, lakini sasa tunamatumaini ya kwenda kupata shule hizi mpya. Ahsanteni sana Serikali hii ya Awamu ya Sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nishukuru sana kwa wazo lile la kuwalipa Madiwani moja kwa moja kutoka Serikali Kuu ilikuwa ni kilio kikubwa sana cha Madiwani, hasa Madiwani wa halmashauri yangu ambao waliniletea kero nyingi sana. Na kabla sijapeleka kwa Waziri, Waziri ameliona hilo na tayari ametoa ufumbuzi. Ombi la Waheshimiwa Madiwani, wanasema tunashukuru sana lakini wafikiriwe kuongezewa kidogo, waongeze kidogo pale. Tunafahamu Madiwani wana kazi kubwa, wakiamka asubuhi wale ndio wanaokuwa na wapiga kura wetu, muda wote wanao shida zote wanazo, lakini wanafanya hivyo kwa namna mungu anavyowasaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nishukuru sana sana Serikali kwa maamuzi haya ambayo Mheshimiwa Waziri kupitia bajeti hii alituambia hapa. Ninamatumaini makubwa sana kwamba zahanati zangu, maana tutulikuwa na maboma ya zahanati zaidi ya 34; kwa maneno aliyosema Waziri hapa sasa yanaenda kukamilika. Nilivunjiwa madaraja zaidi ya 24 wakati mvua hizi zilizopita. Sasa kupitia mpango ule wa TARURA ninauhakika yanaenda kujengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunashida ya kero ya hospitali sisi tulikuwa hatuna hospitali sasa hivi tumepokea milioni 500 ujenzi umeanza nina uhakikia kwa mipango hii hospitali ile inaenda kukamilika mapema iwezekanavyo; pamoja na mambo mengi mazuri, kama vile mikopo kwa wanafunzi, tulikuwa tunashida na wanafunzi, na mimi kama Mbunge nasomesha baadhi ya wanafunzi, lakini sasa najua kupitia mikopo hii aliyotuambia Mheshimiwa Waziri hapa sasa na mimi Mbunge hapa nitapumua, nitafanya mambo mengine. Niishukuru sana Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivi naomba nishauri kidogo. Tumefanya vizuri kwa upande wa Madiwani lakini kiko kilio kikubwa kwa upande wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Wenyeviti wa vijiji. Niliona mahala fulani kwenye halmashauri zenye uwezo, ziliwahi kufanya kitu wakati fulani. Ninafahamu Serikali yetu, Serikali Sikivu, inaweza kufanya kitu kwa wenyeviti hawa wa vijiji. Kama halmashauri za manispaa ziliweza kulipa 50,000 kwa mwezi kwa wenyeviti wa mitaa ninauhakika tukipanga tukiamua tunaweza kuwalipa kitu fulani wenyeviti hawa wa vijiji, Kwa hiyo nikombe Mheshimiwa Waziri utakapohitimisha basi wape matumaini wenyeviti wetu wa vijiji nawao wapate kitu fulani, inawezekana kwa mwezi hata kwa miezi mitatu mitatu kwa kuanzia ikibidi tufanye kitu fulani kwao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kwa upande ule wa fedha za majumuisho; tumepeleka fedha milioni 500 kwa kila halmashauri kwa kila jimbo. Hata hivyo, yapo majimbo yenye ukubwa wa kipekee. Inatakiwa majimbo haya pamoja na kuwapa hizi milioni 500 tuyafikirie Zaidi, kwa sababu hatuwezi kufanana, hata vidole hivi havifanani. Yako maeneo yamefika mahala pazuri, lakini yako yana majimbo makubwa sana. Tukisema tumetoa tu milioni 500 na tukapiga makofi kwa kweli zile fedha zinaweza zisionane kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kwa mfano ile milioni 500 naenda kuendeleza ujenzi wa barabara ya kutoka Mbiga – Litoo hadi Ngumbo kwa Mheshimiwa Stella Manyanya, ni barabara ya TARURA, tulipata msaada pale tumejengewa kilometa 34 34 kwa kiwango cha lami, lakini sasa zimebaki kilometa 14, kwa hiyo tunaenda kuendeleza kilometa moja; unaweza ukano. Na hii ni barabara yenye kilometa nyingi sana ndani ya jimbo. Kwa hiyo ombi langu kwa Serikali, pamoja na kutoa fedha hizi tuyaangalie majimbo makubwa, tuyaongezee fedha ili zikafanye vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo hivyo kwa upande wa…

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Benaya Kapinga kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jacqueline Msongozi.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara anayozungumzia Mheshimiwa Benaya ambayo imebakiza kilometa 14 kujengwa kwa lami inayopita kwenye Ukanda wa Ziwa Nyasa ambako kuna vivutio vingi vya utalii na vivutio vingi vya asili; mimi nilikuwa tu nataka nimuongezee mchangiaji kwamba, ni vizuri sasa Serikali ikatenga pesa kwa ajili ya kumalizia kilometa 14 badala ya kutoa kilometa moja. Kwa sababu kilometa moja inakuwa haina tija labda wangetoa pesa za kilometa 14 ingeleta tija zaidi. Ahsante. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Benaya, malizia mchango wako.

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naipokea taarifa yake kwa mikono miwili, nakushukuru sana dada yangu Msongozi.

Mheshimiwa Naibu Spika, na barabara hii mwezi wa kwanza tulipokwenda hata Mheshimiwa Waziri Mkuu aliitolea maelekezo, kwamba ikamilike kwa sababu ina muhimu mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nitoe ushauri upande wa kilimo. Wananchi wa nchi wamefanya vizuri sana kufikia hapa tulipofikia, kiasi kwamba kwa kiasi kikubwa Tanzania haina njaa. Wakulima wetu wamefanya kazi wenyewe kwa nguvu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukifuata taarifa za bajeti hapa upande wa huu wa kilimo hatukufanya vizuri sana, tuwe wa kweli, hatukufanya vizuri sana. Fedha zinatengwa lakini zinazokwenda ni kidogo sana, na hii ipo tofauti na nchi Jirani. Hata kwa bajeti hii tunayoijadili nchi za wenzetu kwa upande wa kilimo zimefanya vizuri zaidi kuliko sisi. Unaweza kuona Kenya wao wametenga trilioni 1.2 kwenye kilimo, Uganda wametenga almost hela ya kwao trilioni 45…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie dakika moja tu.

NAIBU SPIKA: Sekunde thelathini.

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Rwanda pia wametenga fedha nyingi, sisi Tanzania tupo chini kuliko nchi za wenzetu. Kwa hiyo nikuombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kwamba bajeti inayokuja tufanye mambo makubwa, fanya, weka alama kwenye kilimo ili taifa hili likukumbuke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii ya kuchangia Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niungane na Wabunge wenzangu kutoa pongezi nyingi sana kwa Serikali hii ya Awamu ya Sita kwa namna inavyofanya kazi. Siyo kwa kufanya kazi tu lakini kwa namna inavyosikiliza kero, inavyosikiliza hoja za wananchi kupitia sisi Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni tu yamefanyika mambo mengi na mabadiliko makubwa na Serikali hii ya Awamu ya Sita ilipokwenda kusikiliza hoja za Waheshimiwa Wabunge naipongeza sana Serikali hii ya Awamu ya Sita. Kipekee nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa namna anavyofanya kazi. Karibuni tu tulikuwa na mgogoro mkubwa kule Ngorongoro, lakini kwa utulivu mkubwa suala hili limeshughulikiwa nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo tuwe wakweli, Waheshimiwa Wabunge naomba tuwe wakweli na wa wazi kabisa katika suala hili la mfumuko wa bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumza wenzangu hapa ni kweli kabisa kuna vita ya Ukraine na Urusi ambayo hadi leo ina siku 36, lakini suala hili la mfumuko wa bei halikuanza siku hizo. Amesema hapa Injinia Ezra mwaka jana Disemba, 2021 vitu vilianza kupanda bei, malalamiko yalianzia kwenye mbolea, yakafika kwenye vifaa hivi vya ujenzi, yamefika mafuta ya kupikia vita hakuna. Vita imeanza Februari hapa!

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo kweli tukajivika kwenye suala hili la mafuta na vita ya Ukraine, hapa pana jambo Serikali inapaswa kufanya kitu! siyo tu kukimbilia kwamba sasa mafuta yamepanda basi na vitu vitakwenda kupanda, nasema siyo sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunakumbuka vizuri Waziri Dkt. Ashatu aliwahi kusema hapa tumeunda Tume inapitia huko itakuja na taarifa, hivi wenzangu ile taarifa mliipata? Kwa hiyo, lazima tuende vizuri, tukubaliane vizuri. Serikali ina jambo la kufanya hapo pamoja na vita hii ina jambo la kufanya.

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa wapi? Mheshimiwa Waziri wa Fedha.

T A A R I F A

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba Serikali ina fursa ya kujibu lakini ni vizuri majibu ambayo wananchi wangetamani kuyapata muda ule ule yatolewe muda ule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo ningependa na Wabunge wote pamoja na wananchi waelewe, hakuna mtu Serikalini aliyesema jambo lililosababisha bei za bidhaa kupanda ni vita peke yake hakuna! Hakuna mtu aliyesema hivyo!

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtiririko wa vitu zaidi ya kimoja ambavyo vimesababisha bei za bidhaa ziweze kupanda. Jambo la kwanza ambalo lilitangulia kabla ya yote ilikuwa ni COVID-19 na madhara ya COVID-19 kiuchumi siyo ya siku ile ile jamani hiki ni kitu cha kawaida. Usipozalisha leo utakula ulichozalisha jana ila siku ambapo unatakiwa ule kile ambacho ulizalisha jana kwa kuwa jana hukuzalisha ndiyo hakitakuwepo. Madhara ya COVID yasingetokea mwaka 2019, madhara ya COVID lockdown ya mwaka 2019 inatokea mwaka 2020/2021 hivyo ndivyo uchumi unavyokuwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hapa mtu asipolima mwaka jana hapati njaa mwaka jana ule ambao hakulima, anapata njaa mwaka ambao unafuata. Kwa sababu, ndiyo unapotakiwa kuvuna. Kwa maana hiyo, madhara ya bei kupanda siyo tu vita peke yake yamelundikana kuanzia COVID hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili; kwetu hapa Tanzania wengine wanasema sasa mbona imetokea vita kule mbona na alizeti mafuta yake yamepanda bei? Tukumbuke mwaka jana Wabunge angalieni Hansard zetu hapa mwaka jana Mikoa yote haikupata mvua katika kipindi ambacho kinatakiwa kiwe hili wala siyo vita ni ukame. Mikoa yote, kote mnakotokea mvua hazikuanza kama ambavyo huwa zinatakiwa kuanza.

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.

WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la tatu sasa ndiyo imekuja hiyo ya vita, baada ya vita imepandisha vitu vingine vyote kwa sababu ya masuala ya mafuta, lakini hata ile demand tu imekuwa kubwa katika maeneo mengine yote yale. Baada ya demand kuwa kubwa ndiyo inasababisha pressure ya bidhaa zingine zote, hiyo inakuwa spiral yaani inaongezeka inaji-fuel.

MWENYEKITI: Ahsante sana kwa ufafanuzi Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Benaya Kapinga endelea kuchangia.

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na nashukuru kwa maelezo mazuri ya Serikali na mimi sikatai lakini nasema tuna jambo la kufanya zaidi ya tulivyofanya sasa hivi. Kama nilivyosema mwezi Januari Serikali ilisema kuna Tume imeundwa inafuatilia hayo malalamiko ya bei ya bidhaa kupanda, nimehoji hapa ile taarifa ilipatikana na ilifanyiwa kazi ipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilindie muda wangu kwa sababu dakika kadhaa zimekwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Jimboni kwangu kuna shida nimempongeza hapa Mheshimiwa Waziri Mkuu kafanya kazi nzuri Ngorongoro, Serikali imejipanga vizuri, wananchi sasa kwa utaratibu mzuri kabisa wanahamishwa au watahamishwa kutoka Ngorongoro kuja maeneo mengine yaliyopangwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Jimboni kuna mradi wa panda miti kibiashara, mradi huu ni mzuri sana. Mradi huu utekelezaji wake niliusema hapa mwaka jana na ninaendelea kuusema leo, mradi huu ulipotekelezwa ni maeneo ya wananchi ni maeneo ya wakulima. Wakulima wale walikuwa wanamiliki maeneo yale kihalali kabisa kwa miaka yote ya nchi hii, lakini bahati mbaya sana imefika sehemu sasa umeanzishwa mradi ukawapuuza wale wananchi. Wananchi wale wamebaguliwa hawana chao, wamekalishwa tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo hawana haki tena, hivi sasa hivi kuna risasi zinapigwa pale, hivi sasa hivi kuna mapanga yanapigwa pale, wananchi wale hawana haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuomba unilindie muda sijui hiyo ni kengele ya ngapi?

MWENYEKITI: Nimekuongeza dakika moja, malizia hoja yako.

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa hiyo naiomba Serikali kama ilivyofanya Ngorongoro, naiomba Serikali vivyo hivyo iende pale Jimboni eneo la Ndika ikasuluhishe hili. Kwa sababu maeneo yale ni haki ya wakulima wale. Wamepanda miti sawa sijui ni ya nani haieleweki kwa sababu kila mtu anasema mara ya Kijiji, mara ya mtu fulani, mara ya TFS hakuna anayejulikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamshukuru sana Mkuu wa Wilaya ameunda Tume na sasa hivi wanaendelea na mchakato, lakini bahati mbaya sana kasi yake sio ile ya kutoa majibu haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni suala la Madiwani. Madiwani hawa wana kazi nyingi sana pale wanapokuwa katika maeneo yale lakini malipo yao hasa kwenye eneo la posho za kujikimu. Upo Waraka wa tarehe 02 Januari, 2019 unaosema fedha za kujikimu atapewa Diwani anayelazimika kulala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina hakika Wabunge Waraka ule nasi unaweza ukafanya kazi, sina hakika. Kama sivyo kwa nini kwa Madiwani kuwe na Waraka unaosema fedha ya kujikimu apewe yule anayelazimika kulala, wakati maeneo ya vijijini ulazima wa kulala upo tu. Mtu anaweza akaja sasa hivi kwenye kikao, kikao kikaisha Saa 10 hakuna usafiri wa kurudi kwenye eneo lake lazima atalala. Lakini tafsiri ya wale wanaotafsiri ule Waraka wanasema posho ya kujikimu atalipwa yule Diwani anayelazimika kulala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waraka huu ni wa kibaguzi kama kwa upande wetu hautumiki ningependekeza Serikali ifute Waraka huu, kwa sababu unawabagua. Wote ni viongozi wa kisiasa Madiwani ni wanasiasa na Wabunge ni wanasiasa na viongozi wengine. Kama hautumiki hapa kwa maana ya kwamba, kwa sababu kuna Wabunge wanaolazimika hata wasilale, lakini kama hautumiki hapa basi hata kwa Madiwani Waraka huu ufutwe. Madiwani wale walipwe posho zao za kujikimu kama wanavyolipwa wengine wanaolazimika kulala. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza Serikali kwa bajeti nzuri yenye matumaini makubwa kwa nchi yetu. Nina mapendekezo yafuatayo nikianza na ujenzi wa vituo vya afya. Jimbo la Mbinga Vijijini mpaka sasa lina kituo kimoja cha Mapera kinachofanya kazi. Ikiwa jimbo hili lina Kata 29 na Tarafa tano. Nashukuru kupata vituo viwili vya kimkakati katika Kata ya Mkumbi na Muungano ambavyo vinajengwa lakini bado kuna vituo vya kimkakati vya Mbuji, Ukata na Litumbandyosi naomba vianze kujengwa.

Pia naiomba Serikali iunge mkono juhudi za Wanambinga Vijijini ya kukamilisha maboma ya zahanati, shule ya msingi na ofisi za vijiji na kata ambapo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga wananchi wameitikia wito wa ujenzi wa miundombinu hii, ombi lao ni kuwaunga mkono!

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu TARURA; napendekeza mgao wa fedha uendane na hali halisi ya maeneo yetu. Mfano Jimbo la Mbinga Vijijini lina mtandao mkubwa wa barabara wenye sura ya nchi ya milima na mabonde na mvua nyingi, kiasi cha kuhitaji maraja na mifereji. Hali hii inahitaji bajeti kubwa tofauti na ya ujenzi wa barabara tu. Hivyo napendekeza kwa majimbo ya aina hii yapewe bajeti ya ziada ili kukabilina na mazingira hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala; Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga pamoja ukubwa wa kijiografia ikiwa na umbo la mwezi ina kata 29 zenye uwezo wa kuzaa kata nyingine na tarafa tano, tayari tumekamilisha mchakato katika ngazi ya Wilaya na mkoa la kugawa Halmashauri hii na kata, maombi haya yapewe kipaumbele muda ukifika ili kusogeza huduma kwa wananchi tofauti na ilivyo sasa mwananchi wa upande mmoja ili kupata huduma analazimika kupita Halmashauri nyingine ndipo azifikie ofisi za Halmashauri.

Kuhusu Mfuko wa Jimbo, napendekeza utolewe zaidi ya mara moja tofauti na ilivyo sasa kwa miaka hii miwili umetolewa mara moja kwa mwaka kiasi cha kuchelewa kuchochea baadhi ya shughuli za maendeleo za wananchi hususani za msimu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, nianze kuhusu ukubwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga/Jimbo la Mbinga Vijijini; Halmashauri hii ni kubwa, ina kata 29, naomba kuleta maombi ya kuigawa, jambo ambalo tayari vikao vya ushauri Wilaya na Baraza vimeridhia. Kugawanya kwa Halmashauri hii kutasogeza huduma karibu na wananchi tofauti na ilivyo sasa wananchi wanafuata huduma hii mbali kiasi cha kutumia gharama kubwa za usafiri na kutumia muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, maombi ya mgawanyo wa Halmashauri yaende sambamba na mgawanyo wa Kata za Litembo, Litumbandyosi, Langiro, Maguu, Linda, Nyoni, Matiri, Ngima, Mkumbi na Maguu. Kata hizi ni kubwa kimaeneo lakini pia na idadi kubwa ya wakazi kiasi cha kuleta ugumu kwa watumishi na watoa huduma zingine kuwafikia wananchi kwa wakati. Ikiwa hoja hizi zitakuwa na ugumu katika utekelezaji wake niombe huruma ya Serikali ya kuongeza fedha kwa ajili ya Mfuko wa Jimbo na mafuta ya kuwezesha kuwafikia wananchi kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, kuhusu maombi ya vituo vya afya vya kimkakati; naleta ombi la vituo vya afya vya kimkakati kutokana na maeneo haya kufuata huduma hiyo mbali au nje ya wilaya yaani Wilaya ya Nyasa. Hivyo naomba Kituo cha Afya Mbuji, Tarafa ya Mbuji ambayo inakata za Mpapa, Nyoni, Mbuji, Litembo na Kitura haina kituo cha afya hata kimoja, pamoja na Kituo cha Afya Ukata, Kata ya Ukata ambayo pia iko mbali na huduma na eneo ambalo pia lina mlipuko wa magonjwa mara kwa mara.

Mheshimiwa Spika, ajira; naomba kipaumbele kitolewe kwa wanaojitolea na wale waliohitimu mafunzo vyuoni miaka ya nyuma, maana ikiwa yupo mwombaji wa ajira amemaliza chuo mfano mwaka 2015 na mwingine mwaka 2020 basi yule wa mwaka wa nyuma kumaliza apewe kipaumbele ikiwa na kigezo cha umri wa mwombaji tukitambua ajira Serikalini unataka umri usiozidi miaka 45.

Mheshimiwa Spika, maombi ya watumishi; Halmashauri ya Wilaya Mbinga ina upungufu mkubwa wa watumishi katika sekta ya afya na elimu. Upungufu ni mkubwa zaidi katika afya kiasi cha zahanati kubaki na mhudumu mmoja tu. Mfano kuna upungufu wa zaidi 80%; waliopo ni 20% Idara ya Afya, hivyo ombi langu katika ajira hizi mpya tupewe kipaumbele kuongezewa watumishi katika sekta ya afya na elimu.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa TARURA; naomba waongezewe fedha hususani TARURA Halmashauri ya Mbinga DC kutokana na ukubwa wa eneo, lakini hali ya milima na mabonde kiasi cha kuhitaji madaraja na mifereji mingi. Niombe waongezewe fedha kwa kutekeleza miradi ya barabara zitakazoweza kupitika msimu mzima wa mwaka tofauti na ilivyo sasa barabara nyingi zinapitika kiangazi na kufunga kupitika wakati wa masika kutokana na kukosa madaraja na tope kuwa jingi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kufunga dimba siku ya leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote na mimi niungane na Wabunge wenzangu kuishukuru sana Serikali hii ya Awamu ya Sita kwa kazi nzuri inayoendelea kufanya katika nchi yetu. Ninamshukuru sana na nimpongeze Waziri Dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama, amekuja muda mfupi katika Wizara hii lakini sasa hivi amejenga matumaini makubwa kwa watumishi. Watumishi wengi wanayo imani sana, ninamshukuru Naibu wake lakini nimshukuru pia Katibu Mkuu Dkt. Laurine Ndumbaro pamoja na Wasaidizi wake wanafanyakazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kuishukuru na kuipongeza Serikali kwa kibali kile cha ajira 32,000. Nina uhakika wamsema wenzangu hapa na hasa wale wa Majimbo ya vijijini na mimi natoka kijijini, hali yetu kule tunaijua watumishi wako pungufu sana, tuna uhaba mkubwa sana wa watumishi. Nitolee mfano tu, iko shule ina Walimu Watatu na miongoni wao mmoja anaondoka, shule hiyo inabaki na Walimu Wawili. Kwa hiyo, nina uhakika sasa kwa kibali hiki cha watumishi 32,000 na mimi shule zangu kule zitapata watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia na zahanati zangu zitapata watumishi, lakini pia na hospitali itapata watumishi, naishukuru sana na ninaipongeza Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na Mheshimiwa Kasinge, nchi yetu inaongozwa kwa Katiba na Katiba hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa haki kwa Watanzania wote, haki ya kushiriki siasa, kwa maana ya kuchagua na kuchaguliwa, vilevile imetoa haki ya kufanya kazi na imetoa haki ya kuajiriwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2020 tulikuwa na Uchaguzi Mkuu katika nchi yetu, kuna Watumishi ambao walienda kushiriki kwenye uchaguzi ule, baadhi ya watumishi hawa walikuwa wateule wa Rais, kulikuwa na Wakuu wa Mikoa, kulikuwa na Wakuu wa Wilaya, lakini kulikuwa na watumishi wasiokuwa wanasiasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Katiba hii hakuna raia wa Tanzania aliyezuiwa kushiriki siasa hakuna! Wananchi wote wameruhusiwa kwa mujibu wa Katiba hii kushiriki siasa. Kwa bahati mbaya sana mwaka ule wako wananchi raia wa nchi hii baada ya kuingia kwenye siasa walisitishwa haki yao ya kufanya kazi. Utaratibu ule haukubaliki kabisa kwa mujibu wa Katiba hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru sana Serikali hii ya Awamu ya Sita ilichukua hatua baada ya kusikia kilimo cha Wabunge wa Bunge hili kwamba utaratibu ule ulikuwa siyo sahihi, watumishi wale wengi kama siyo wote wamerejeshwa kwenye nafasi na sasa wanaendelea na kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uko Waraka wa mwaka 2014 unaosema uko wazi kabisa kwamba, mtumishi wa umma ataondolewa kwenye utumishi atakapoteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwamba yeye ni nani sasa anashiriki uteuzi au uchaguzi wa katika maeneo yake ya siasa. Upo ule waraka umeeleza vizuri sana, lakini lililofanyika mwaka ule limeenda tofauti sana na waraka ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu kuchukua fomu tu alisitishiwa ajira, alisitishiwa kufanyakazi, tulikiuka sana Katiba hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watumishi wale wamerudi, walirudi baada ya kukaa nje ya kazi kwa zaidi ya miezi wengine Saba, wengine Sita, wengine Nane. Mwenzangu amehoji hapa wale watumishi walikuwa likizo ipi? Kwa sababu bado wana haki zao, kushiriki siasa hakumuondolei mtu haki ya kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami naungana na mwenzangu Serikali kwa vile tayari tumewarudisha wale watumishi kazini, tunafahamu miezi kadhaa walikuwa hatuelewi kama walikuwa likizo au ilikuwa ni kitu gani lakini miezi kadhaa wana madai yao, kwa hiyo ningeomba maelezo yatolewe hapa na Serikali ule muda ulikuwa ni kitu gani. Nadhani kwa sababu Serikali hii sikivu na Mheshimiwa Jenista wewe ni msikivu utakuwa na majibu mazuri yanayoenda kuwatia moyo wale watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ni suala la hii recategorization. Recategorization ni kitu kizuri sana kina manufaa pande zote. Kina manufaa kwa mtumishi lakini kina manufaa pia kwa upande wa Serikali. Imekuwa hivyo vizuri inafanyika lakini kwa bahati mbaya sana kuna baadhi ya Taasisi inapofanyika hii recategorization ina wanyanyasa au inawaonea watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mtumishi ameenda kusoma, mtumishi yuko kwenye nafasi fulani mahala Fulani, Taasisi inaona upungufu wa Idara Fulani, inamtoa mtumishi kutoka Idara aliyokuwa anafanyia kazi, anarudi kufanyakazi hapa kuimarisha ile Idara lakini mwisho wa siku anapunguzwa mshahara anakuja kuanza as if anaanza leo ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili siyo sahihi sijui, lakini ikibidi kama kweli mtumishi yule ameomba mwenyewe sawa, lakini sasa Idara au Taasisi inamhamisha kutoka Idara fulani inamrudisha hapa ili aendane na muundo wanamuondolea mshahara aanze tena upya! Ningependa Serikali itoe tamko hapa watumishi ambao Idara au Taasisi ndiyo iliyohitaji abadilishwe mfumo basi wale wasianze upya wasianze katika level ile ya kwamba anaanza ajira, wahame na mishahara yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Waziri atakapokuja kusema hapa na mimi nitashika shilingi kama hiyo kauli sitaisikia. Kuna orodha ya watumishi wako hapa, wameondoka kwenye Idara fulani wamepelekwa kwenye Idara fulani wakaenda wakawashushia mishahara yao. Leo hii yule mtumishi alikuwa na mkopo, ana mkopo wa Loan Board anaenda kufanyakazi anarudi hana kitu kabisa! Si ndiyo tunafundisha watu kuiba hapa, tunafundisha watu ufisadi si ndiyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Serikali tuliangalie hili, suala hili la recategorization ni zuri mno likifanyika na mtu akahama na kamshahara kake hivi nani anaumia? Hakuna kitu cha kuumia hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona niseme hili na nalisema kwa uchungu sana kwa sababu lina maumivu mno. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine ni ile ya uhakiki wa wale watumishi Darasa la Saba na hii naomba niliseme kwa upole. Ninatambua tuliwaondoa baadhi ya watumishi kwenye ajira, lakini ukienda kuwasikiliza baadhi ya watumishi hao sababu inayoonekana kwamba wali-forge vyeti, baadhi ya watumishi hawa ni Walinzi, anakuambia kabisa mimi sikuwahi sign hicho kitu, mimi nimekikuta tu kwenye file yangu mimi sihusiki, ninaorodha ya watumishi 12 wana malalamiko hayo kwamba wao kama wao na ukiangalia zile documents zao unaona kabisa miandiko iko tofauti, sasa ni nani alibadilisha taarifa zile?

Ninaomba Serikali kwa unyenyekevu mkubwa na kwa sababu Rais wetu anasimamia haki na mara kadhaa amesema yeye ni mpenda haki, ningeomba sana kwa unyenyekevu mkubwa, tufanye uhakiki wa watumishi hawa, ikithibitika siyo basi warejeshwe kazini, yapo malalamiko ya wazi kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, naunga mkono hoja.(Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi nami niweze kuchangia Wizara hii muhimu katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na wataalam katika Wizara hii. Nampongeza Mheshimiwa Waziri kipekee kabisa na Naibu wake, watu hawa ni wasikivu sana. Mwaka 2022 nilipata malalamiko jimboni kwangu. Nilipoenda kuwaona, walinisikiliza vizuri na baadaye wakapanga safari. Kwanza nilienda na Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini baadaye akaja mwenyewe Waziri. Kwa kweli tulifanya Mkutano mkubwa sana sana wa Wadau wa Makaa ya Mawe. Kwa hiyo, kwa namna ya pekee nampongeza Waziri na Naibu wake, wanaitendea haki sana Wizara hii wanayoiongoza. Hongereni sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika kikao kile ambacho Waziri alikuja kwa wito wangu, kulikuwa na mambo mengi yamezungumzwa. Kwanza, tulizungumzia suala la CSR; na pili, tulizungumzia suala la local content. Mheshimiwa Waziri kwenye mkutano ule alitoa maelekezo mazuri sana, kwamba lazima madini haya yawanufaishe maeneo yanamochimbwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni sisi tumeanza uchimbaji huu wa makaa ya mawe. Nawapongeza sana wenzetu wa dhahabu, wameanza muda mrefu, na sasa hivi angalau manufaa kwenye maeneo yale yanaonekana wazi wazi, lakini maeneo yetu, bado wananchi walikuwa na manung’uniko na masononeko kwamba tunaona tu magari makubwa makubwa yanapita katika maeneo haya, lakini hamna kitu tunachokiona sisi hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika tunaona Serikali sasa na Mkoa wetu wa Ruvuma kipato kimeongezeka sana sana. Tunaishukuru sana Serikali. Ila pale yanapochimbwa madini, bado wananchi wale hawajaridhishwa kabisa na namna ile inayobaki pale. Kwa hiyo, mwaka 2022 Mheshimiwa Waziri alitoa maelekezo pale na nadhani mliongelea suala kwamba mnatengeneza kanuni. Sasa pengine ni wakati muafaka Mheshimiwa Waziri ukasema ni hatua gani imefikiwa ya kanuni ile ili sasa na sisi wa makaa ya mawe tuanze kunufaika sawa na wenzetu wa dhahabu kama walivyonuifaika ikiwepo pia na lile suala la local content. Ni masuala muhimu sana katika uchimbaji wa haya madini, hususan madini ya makaa ya mawe. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri najua unafahamu hiki kikao na maelekezo uliyotoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine Mheshimiwa Waziri alilozungumzia pale ni suala la leseni. Katika maeneo haya, ziko leseni zilizokwisha muda wake. Wapo wamiliki wamekaa na leseni hizi lakini hawafanyi kazi na muda wake umekwishwa. Kwa hiyo, kupitia kikao kile, Mheshimiwa Waziri alitoa maelekezo kwa wachimbaji wadogo. Nina orodha ya wachimbaji wadogo wadogo wanaendelea kufuatilia utekelezaji wa yale maelekezo yako. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, basi kama ziko hizo leseni, tuwatangazie wale wachimbaji wadogo wadogo nao wapate maeneo waweze kuchimba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina uhakika, kwa uwezo pamoja na Naibu wako na Wizara kwa ujumla, mtalifanyia kazi hili haraka ili wananchi wale wa Mkoa wa Ruvuma nao wanufaike na rasilimali iliyopo katika mkoa wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ninalotaka kuliongea ni la Kitaifa zaidi, ni suala la uchimbaji wa madini haya ya chuma (metallic minerals). Nchi yetu imebarikiwa sana na madini haya. Bahati nzuri yapo, na bahati nzuri yanatumika sana ndani ya nchi hii. Madini haya ndiyo yanayoenda kwenye viwanda hivi vya cement. Kwa wale ambao hawajui, utaona kama mawe hivi yamekaa humo barabarani, hayo ndiyo madini yanayoitwa metallic minerals, na kazi yake kubwa ni kwenda kutengeneza clinker kwenye viwanda hivi vya ciment.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wako wachimbaji waliokuwa wanaendelea kufanya hii kazi, lakini wanakatishwa tamaa na tozo zetu. Wanaochimba hii metallic minerals tumewawekea loyalty ya 6% pamoja na ushuru wa inspection wa 1%. Ukijumlisha wachimbaji hawa kwa jumla wanatoa 7%. Hii inakuwa tofauti na wachimbaji wengine wa madini kama ya gypsum, na madini mengine ya namna hiyo. Wao pamoja na makaa ya mawe, wao wanatoa 3% na inspection yao 1%. Kwa hiyo kule wanakuwa na 4% lakini wale kule wanakuwa na 7%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiasi hiki ni kikubwa sana, nina ushahidi wa baadhi ya maeneo wachimbaji hawa wameacha uchimbaji, wameona sasa bora tufanye shughuli nyingine kuliko kuchimba na kuendelea kuumia wakati faida inayopatikana humu ni kidogo sana. Nikuombe Mheshimiwa Waziri unalijua hili vizuri sana, lifanyie kazi ikiwezekana basi wote twende kwa, iende flat rate kwa sababu wote hawa wanachimba ni minerals hizi za viwandani, wote hawa wanachimba raw materials za viwandani kwa hiyo kwa vile hawa tumewa-charge kwa 3% basi na wale nao wa metallic minerals basi tuwapige nao kwa 3%. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine hapo hapo kwenye hizi metallic minerals, nchi yetu hii ina viwanda vingi sana vinavyotumia hii metallic materials lakini kinachoonekana sasa hivi hivi karibuni kuna kitu kimefanyika ndani ya nchi yetu. Ninakumbuka sisi miaka mitano iliyopita na hadi sasa hivi tulikuwa tuna-promote viwanda vyetu vya ndani. Sasa kupitia hiki kinachoenda kuendelea sasa hivi kinaenda kuharibu utaratibu huu wa kulinda viwanda vyetu vya ndani na wazalishaji wetu wa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema nini? Viwanda vyetu vinavyotumia hizi metallic minerals zimeingia na mpango wa kutumia copper slug. Copper slug naweza kusema labda kwa lugha ya Kiswahili ni pumba, pumba za copper. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani copper ile inachimbwa huko inakochimbwa, inapelekwa huko nje, inaenda inachakatwa huko, yale mabaki mabaki yale yanarudishwa ndani ya nchi wanayatumia tena kwenye viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa vile viwanda vilivyokuwa vinatumia hizi metallic minerals hizi, vinakwepa sasa kununua metallic minerals hizi chuma hizi, haya mawe unayoyaona na wewe unapita hii njia ya kwenda kama unaenda Manyara, kuna mawe yanapatikana kuanzia hapa Maya Maya unaenda mpaka unapita Chemba hivi kuna mawe yanapatikana hapo. Yale mawe ni muhimu sana na ndicho chuma chenyewe kinachotumika watu wa viwanda vya cement wanayatumia haya kwa ajili ya uzalishaji wa cement.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wanakwepa kuyanunua haya, wanakwenda kuchukua hiyo copper slug mbadala wa hii metallic minerals. Athari yake ni nini? Athari yake tunaenda kupoteza hadhi kwa hawa wananchi wetu, tunaenda kupoteza ajira, tunaenda kupoteza mali zetu ambazo tunazichimba humu humu nchini. Hawa wanaenda kuchukua haya na bahati mbaya sana sina uhakika Mheshimiwa Waziri kama tuna uchimbaji mkubwa wa hii copper hapa nchini. Najua copper zinazalishwa nje zaidi kuliko sisi wenyewe na pale jimboni kwangu copper ninayo lakini hatujaanza kuchimba lakini hii inayotumika sasa ni ya wenzetu, tuna wanufaisha wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri kwa nia ile ile ya local content hapa tutakuwa tunaenda nje ya utaratibu wa local content kwa sababu tunajua lazima tuwape kipaumbele watu wetu na tunapowapa kipaumbele watu wetu ndipo tunapozalisha zaidi. Ndipo tunapotumia rasilimali zetu lakini pale tunapotumia hizi kutoka nje maana yake uchumi wote tunaupeleka wapi, nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri sijajua hili limetoka hivi vibali vimetoka kwako? Kwa sababu pale nyuma tulidhibiti hili hivi vibali vilikuwa havitolewi. Sasa aliyetoa hiki kibali kwa kweli sisemi kwamba haitendei lakini siyo sawa sawa. Lazima twende tuvilinde viwanda vyetu. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana naunga mkono hoja lakini nikuombe sana Waziri suala hili ulitolee maelezo na ufafanuzi ili tunufaike ndani ya nchi hapa. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi kupata nafasi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu kwa maendeleo ya Nchi yetu. Kwanza kabisa nianze kwa kuipongeza Serikali hii ya Awamu ya Sita kwa kazi nzuri inayofanya katika kuwekeza viwanda ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunafahamu namna Mheshimiwa Rais anavyopambana kuifungua nchi, kukaribisha wawekezaji lakini pia ku-promote vitu vyetu vya ndani. Kwa hiyo niipongeze sana sana sana Serikali hii ya Awamu ya Sita.

Mheshimiwa Spika, kipekee nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake na watendaji. Wamejipanga vizuri, sasa hivi husikii makelele makelele mengi ya kuongezeka kwa bei za bidhaa, nchi imetulia na kazi inaendelea. Hongereni sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi hiyo nzuri. Kipekee niishukuru Serikali na nimshukuru pia Mheshimiwa Waziri. Mwaka jana nilienda kumwona pamoja na wadau kuhusiana na viwanda vya ukoboaji wa kahawa pale katika jimbo langu. Kulikuwa na malalamiko yanajitokeza mara kwa mara kuhusiana na curing loss. Kwamba wakati kahawa inakobolewa, kuna taarifa za upotevu wa kahawa, inaitwa curing loss.

Mheshimiwa Spika, sasa ilikuwa inatofautiana kati ya kiwanda kimoja na kiwanda kingine. Kahawa hiyo hiyo imetoka kwenye chama kimoja ikipelekwa kwenye kiwanda hiki curing loss inakuwa kubwa lakini ikipelekwa kiwanda kingine inakuwa ya kawaida. Nilikuja na wadau kumwona Mheshimiwa Waziri tatizo lile limeshughulikiwa sasa hivi pako shwari. Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ameunda tume juzi imefanya kazi nzuri, imehoji baadhi ya AMCOS, zimejibu kwamba sasa hivi kelele ile sasa imekwisha. Kwa hiyo nishukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kulishughulikia hilo. Niombe usiishie hapo endelea kuchunguza chunguza, maana hawa watu wajanja wanaweza wakawa wamefanya leo vizuri kesho wakafanya tofauti ili wakulima wetu wanufaike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili nimpongeze pia Waziri katika kipindi hiki ndipo tunaposhuhudia ulipwaji wa fidia wa Mchuchuma na Liganga, mradi ambao kwa kweli una historia kubwa na ndefu kweli kweli. Sisi wengine hata tulizaliwa suala la Mchuchuma na Liganga lilikuwa inazungumzwa. Leo watu wamekufa masuala haya yalikuwa yanazungumzwa; lakini leo kipekee tunashuhudia watu wanalipwa fidia. Ni hatua ya kupongeza sana kwamba tunatoka hatua moja kwenda hatua nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu, sasa tukilipa fidia tusikae, tusikae tuanze kutekeleza ule mradi. Nimeambiwa aliyeshinda hii tender hayupo tena duniani lakini watu wapo wa kuendeleza hii kazi. Nikuombe sana Waziri simama kama ulivyosimama, sasa hizi fidia zinalipwa, mradi huu uanze kutekelezwa.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi duniani ndiko kwenye malighafi ya makaa inahitajika. Watu sasa hivi wanavuna makaa pamoja na chuma kwa nguvu na kwa speed kubwa sana. Kwa hiyo nimuombe sana Mheshimiwa Waziri kipindi hiki ndicho cha kunufaika na huu mradi. Tusikae tena tunalipa fidia halafu tunaenda kutulia. Hatutai tendea haki nchi yetu, hatutawatendea Watanzania hawa haki. Mimi nina uhakika na Mheshimiwa Waziri suala hili ataenda nalo kwa speed kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine niishukuru pia Serikali. Pale kwangu kulikuwa na Mgodi wa TANCOAL kwa muda mrefu ulifanya kazi lakini ukasimama kwa muda pia mrefu sana kwa sababu tu ya migogoro ambayo pengine ilikuwa haina hata manufaa kwa nchi yetu lakini kwa Watanzania ambao walikuwa wanafanya kazi pale. Kulikuwa na mgogoro kati ya NBC, Milambo na Taifa Mine. Taarifa njema sasa hivi kupitia watu wetu wa FCC mambo haya yamezungumzwa vizuri na muda si mrefu kwa maelezo niliyopewa kuna muwekezaji mpya anakabidhiwa huu mradi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu ni kwamba suala hili nalo liende kwa speed ile ile, lisije likakawia tuakona tena kizungumkuti. Kwa sababu limeshaisha linakaribia sasa huyu muwekezaji mpya ku-take off pale; na wamesema baada ya kukabidhiwa, pale tu mkataba utakapo sainiwa basi wale watumishi, wafanyakazi waliokuwepo pale wataanza kunufaika na mafao yao ya huko nyuma kwa sababu kulikuwa na kelele nyingi sana za malipo yao ya huko nyuma, lakini pia kulikuwa na madai tofauti tofauti pale. Mara kadhaa ilikuwa nikienda pale unasikia kelele za wafanyakazi, kelele za waliowekeza pale kwa maana ya kwa sababu migodi hii ya makaa ya mawe inakuwa na wawekezaji wengi wengi. Kwa hiyo kila mtu alikuwa anadai kupitia kwenye hii Kampuni ya TANCOAL.

Mheshimiwa Spika, sasa nina uhakika Mheshimiwa Waziri baada ya kusainiwa huu mkataba hawa wote watalipwa na sasa hatutapata tena kelele. Lakini shughuli ya uchimbaji ya makaa ya mawe ambayo sasa yanahitajika sana sana duniani itaanza kwa kasi sana. Kwa hiyo nikuombe sana Mheshimiwa Waziri hili lishughulikiwe. Lakini nikupongeze kwa hatua hii ya awali ambayo imefikiwa, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine nitoe ombi. Kwa sababu wakati tunaambiwa tumegundua makaa ya mawe katika jimbo letu, wananchi hawa waliaminishwa kwamba sasa viwanda vitakuwepo, maendeleo yatakuwepo. Hata hivyo mpaka leo hatujapata kiwanda hata hiki, kimoja. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, kwa sababu tuna malighafi zetu pale, naomba sasa na sisi tupate kiwanda ili sasa wananchi wale waone manufaa ya kuwa na haya makaa ya mawe pale na malighafi nyingine. Niombe sana hilo Mheshimiwa Waziri; najua pengine utalitolea ufafanuzi hapo baadaye.

Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la kulinda viwanda vyetu. Nilisikiliza baadhi ya michango hapa jana ya namna tunavyo- promote viwanda vilivyopo ndani ya nchi yetu. Tuna viwanda vingi, mimi hapa niwe specific kuzungumzia Kiwanda cha Magari cha GF Motors Limited. Kwanza tumshukuru sana huyu mtu mzawa huyu kwa kuwa na wazo hili la kiwanda ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunafahamu watu kadhaa walijaribu kuanzisha viwanda hapa Tanzania wakashindwa, lakini huyu ndugu yetu kaanza muda si mrefu na sasa hivi progress yake ni nzuri sana. Ameshafikia kuzalisha magari mpaka 700 na malengo yake mwaka huu anaenda kuzalisha magari 1,200. Kwa kweli watu wa namna hii wanapaswa kupongezwa lakini cha ziada wanapaswa kulindwa ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu sasa hivi ninavyokwambia mimi nilipata nafasi ya kutembelea pale. Tayari anawafanyakazi 115 wako pale wanafanya kazi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde 30 malizia.

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ombi langu watu wa namna hii wanapaswa kulindwa kwa sababu wanai-promote nchi yetu, wanakuza uchumi wa nchi yetu na wanatoa ajira kwa nchi yetu. Kwa hiyo tuombe sana Mheshimiwa Waziri watu hawa walindwe kwa nguvu zote.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa nafasi na kuwa mchangiaji wa kwanza siku hii ya leo. Jimbo la Mbinga Vijijini, kama inavyotamkwa vijijini ni wakulima. Kwa niaba ya wakulima wote na mimi mwenyewe ni mkulima wa Mbinga, tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita kwa mpango ule wa mbolea za ruzuku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbinga bila mbolea hatuvuni. Mwaka uliotangulia kabla ya msimu huu tulipata shida sana kupata mbolea, lakini tunaishukuru Serikali, tunamshukuru Mheshimiwa Waziri, tunamshukuru Naibu Waziri, kwa mpango huu wa ruzuku ya mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu hii kupitia hizi mbolea za ruzuku kila mkulima alipata mbolea na amelima vizuri, shida ndogo tu kwamba mbolea hizi awamu hii kwa sababu ulikuwa ni mpango wa awamu ya kwanza haukufika kwa wakati, kulikuwa na ucheleweshaji wa baadhi ya mbolea. Kwa hiyo, ninakuomba sana Mheshimiwa Waziri kwamba msimu huu unaokuja, najua mpango huu bado upo, nimepitia kwenye bajeti, lile lililotokea msimu uliopita basi tusilione safari hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na shida ya baadhi ya mbolea, mbolea za ya CAN na SA hazikuwa zinapatikana, kama zinapatikana basi ni kwa shida sana, ninashukuru ulinialika kwenye kikao chako cha maandalizi ya msimu ujao kupitia watu wa TFS na wale wengine wanaoagiza hizi mbolea, nimeona maandalizi yanakwenda vizuri. Hivyo, Mheshimiwa Waziri ninakuomba na ninakuamini sana, uko vizuri kwenye kupanga na kusimamia, msimu huu ile mipango niliyoishuhudia kwa watu wa TFC basi isimamie vizuri kusiwe tena na wimbi la wananchi kulalamikia baadhi ya mbolea kutopatikana ndani ya nchi yetu. Hili nina uhakika Mheshimiwa Waziri utalitekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la ushirika. Ni ukweli kabisa umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu. Nimesikiliza baadhi ya michango jana, watu wanasema tuachane na ushirika tukaribishe mnunuzi mmoja mmoja. Kwetu Mbinga habari hiyo ya kuachana na ushirika hatuitaki, tunajua wanunuzi hawa wana nia tofauti tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mfanyabiashara mwenye lengo la kumsaidia mkulima, hayupo. Mfanyabiashara yeyote anayefanya biashara nia yake ya kwanza ni kupata faida, kwa hiyo hatakuwa na nia ya kuwasaidia wakulima, lakini wakulima hawa wakiwa pamoja ninajua watajenga nguvu ya pamoja na watauza kwa pamoja, watauza kwa bei nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, anaweza akaja mfanyabiashara mmoja akajifanya ananunua vizuri kwa mtu mmoja rafiki yake, akapandisha bei ataenda ku-substitute kwa wakulima wengi kwa kununua bei ya chini. Kwa hiyo, najua kuna matatizo kwenye ushirika, lengo hapa liwe kuboresha siyo kwenda kubomoa kabisa na kwamba tuanze upya, hapana. Hata mimi mambo yangu hayajawa vizuri sana kwenye ushirika lakini nashukuru vyama vingi msimu huu uliopita vimelipa vizuri, vichache havijalipa, nami najua kwa nini havijalipa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ushirika hapa upo utaratibu wa hizi AMCOS kukopa kwenye mabenki. Hapa Mheshimiwa Waziri mimi nikushauri kwamba utaratibu huu ulisumbua sana kwenye korosho, kwamba AMCOS inakwenda kukopa halafu inakuja kuwalipa wakulima malipo ya awali, inalipa malipo ya pili na inalipa malipo kule kwenye korosho walikuwa wanaita majaliwa. Ilikuwa ni shida sana kwa wakulima hawa kulipwa malipo ya pili na yale ya majaliwa, lakini malipo ya awali kwa sababu wanakwenda kuchukua benki wanalipa, ikifika yale ya pili ni ngumu sana kulipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ninakuomba korosho sasa hivi wanalipa kwa mkupuo, mkulima akipeleka korosho zake kwenye AMCOS zikaja zikauzwa analipwa malipo yake yote, sasa hivi hakuna kelele, lakini huu mfumo wa benki kuruhusu AMCOS ikakope waje walipe mara ya kwanza, waje walipe mara ya pili, fedha zote zinaishia kulipa kwenye benki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitolee mfano Mahenge AMCOS ni chama kizuri sana lakini kimeshindwa kulipa malipo ya pili hata mkulima mmoja, milioni zaidi ya 89 wanadaiwa, hawajamlipa hata mkulima mmoja. Siyo kwamba hawana uwezo, walikusanya mazao wakauza kwa milioni 480 lakini huku nyuma kwa sababu walikopa benki milioni 500 ikabidi malipo yale yote yaingie benki na wakulima sasa hawajalipwa, wanabaki wanalalamika mpaka leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nikuombe, vyama vile ambavyo vinalipa malipo kwa mkupuo safari hii hawana kelele, lakini vyama vile ambavyo vimeenda kukopa benki halafu wakalipa malipo ya awali halafu wanakuja walipe tena malipo ya pili wengi wamepata matatizo kwa sababu kiasi wanachouza kinakwenda kuishia kulipa benki. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ninakuomba sana toa kauli vyama hivi vilipe kwa mkupuo, hatutakuwa na shida wala malalamiko kama yale waliyosema Songwe, nasi Mbinga tutakuwa na furaha zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, mwaka jana au mwaka juzi tulisherehekea hapa kwa kauli ya Waziri Mkuu ya kupunguza makato kwenye kahawa. Sasa hivi karibuni msimu huu ulioisha Mheshimiwa Waziri mmeweka makato pale ya shilingi 200 kwa kilo bila makubaliano na mkulima, ninakuomba utakapokuja hapa utoe ufafanuzi yale makato kwa nini umeyaweka, yana manufaa gani kwa mkulima na kwa nini akatwe mkulima?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kama huku tunapunguza kwa nini huku tena tunaongeza kwa njia nyingine? wakulima wangu wanalalamikia sana hilo. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri utakapokuja hapa utoe majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, hivi kwa nini kwenye vikao hivi vya wadau wa kahawa hamuwaaliki Wabunge…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Benaya Kapinga.

MHE. BENAYA L. KAPINGA: …ambao ndiyo wanapokea kero zote za wakulima?

MWENYEKITI: Ahsante sana, muda wako umekwisha.

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja lakini ninaomba Waziri ujibu haya maswali niliyokuuliza hapa mwisho, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii niweze kuchangia katika Wizara hii ya Afya. Awali ya yote niungane na wenangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, kumpongeza sana Naibu wake, lakini kuipongeza wizara kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, wanafanya kazi kweli kweli. Hakuna asiyejua ndani ya nyumba hii kwamba watu hawa ukiwaambia neno wanakukimbilia, ukiwapa changamoto wanaisikiliza na kuitatua lakini ukiwaita kwenye jimbo lako wanakuja. Leo niwaombe, najua hamjafika Jimbo la Mbinga vijijini, kwa hiyo, niwaombe sana kupitia nafasi hii, tukimaliza hotuba hii au baada ya Bunge hili basi mpate nafasi mfike Mbinga vijijini. Karibu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze sana na nitoe shukrani kwa Serikali hii ya Awamu ya Sita, imefanya kazi kubwa katika jimbo langu. Nitoe shukrani kwa shilingi milioni 400 kwa ukarabati wa Kituo cha Afya Mapera. Sio hivyo tu, hivi karibuni wametoa milioni 350 vifaa tiba, kituo hiki cha afya sasa hivi kiko full full. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepewa ahadi kupitia mradi wa Global Fund kwamba naenda kupata ambulance. Kwa hiyo, kwa kweli tunashukuru sana. Tukijumlisha na ile ya COVID maana yake tunakwenda kuwa na ambulance hizi mbili. Ahsanteni sana Serikali hii ya Awamu ya Sita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maombi, tumejenga sasa hivi na kukamilisha vituo vya afya, Muungano, Matili na Mkumbi lakini pia kuna kituo cha Afya Magagula kwa Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Jenista Mhagama, niombe sana tupeleke maeneo haya vifaa tiba lakini na madaktari wakafanye upasuaji katika maeneo haya. Kwa sababu Jimbo la Mheshimiwa Jenista Mhagama na la kwangu yako Jirani. Kwa hiyo, hata wananchi wanaingilia na wanalima kule upande wa Msonga na Magagula yenyewe. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri, kama ulivyofanya hapa juu fanya pia na pale kupeleka hivi vifaa tiba ili wananchi hawa wapate huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo langu la pili, utoaji wa huduma na huduma hizi za kibingwa. Kama nilivyosema hapo awali, nchi yetu sasa hivi kila mahala kuna majengo mazuri ya kutolea huduma hizi za afya. Tuna zahanati, tuna vituo vya afya, tuna hospitali za wilaya na tuna hospitali za rufaa kwa maana za mikoa na hizi za kanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, huwa ninaumizwa sana na ninasikitika sana pale wananchi wetu wanaposema siendi hospitali hii naenda hospitali fulani. Hapa niwe specific, kwa kule kwetu sisi sasa hivi habari ya mjini ni Ikonda iko Makete. Sasa mwananchi anakuja hana hela anaomba nauli ya kwenda Makate. Unamwelekeza kwa nini usiende hapa hospitali ya wilaya hii? Hakuelewi. Kwa nini usiende usiende pale mkoani kuna hospitali pale General? Hakuelewi anakwambia huduma nzuri zinatoa? Makete. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa kwa kweli niwapongeze kwanza madaktari wetu wanafanya kazi nzuri katika mazingira haya tuliyokuwa nayo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, nikuombe hebu tutafute majibu na utujibu hapa ni majibu gani yatakayowafanya wananchi waliopo huko wakaacha vituo vya afya na hospitali zilizopo maeneo haya waende sasa kwa mfano nilivyosema Ikonda? Sisemi kwa nia mbaya kwamba naichukia Ikonda, hapana naomba mnielewe sana. Hoja yangu tumejenga, tuna vituo vya afya vizuri na majengo mazuri na tuna madaktari maeneo haya. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, niombe utupe maelezo mazuri namna gani wananchi wetu hawa wataviamini hivi vituo na kupata huduma? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, ni utoaji wa fedha za dawa. Upo ucheleweshaji mkubwa sana wa utoaji wa fedha hizi za dawa na hasa pale kituo kinaposajiliwa. Inachukua muda mrefu sana kituo kikisajiliwa kuingia kwenye mfumo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitolee mfano katika halmashauri yangu, kuna vituo vimesajiliwa muda mrefu vimechukua miezi mitano mpaka sita kuingia kwenye mfumo. kwa hiyo, niombe Waziri tubadilishe huu utaratibu, kwa sababu sasa hivi Serikali inasomana kwa nini ichukue muda mrefu? Tumesajili labda zahanati, tumesajili kituo cha afya, tumesajili hospitali lakini inachukua miezi mitano mpaka sita kituo hiki kuingia kwenye mfumo. Hawa watu wanafanyaje kazi? Sasa wanaanza kuwa omba omba, wanakwenda kituo fulani wanaomba, wanaenda kituo fulani wanaomba dawa. Hii inaleta shida hata kwenye kile kituo wanachoomba dawa. Nikuombe Mheshimiwa Waziri, tutafute namna ya kurahisisha mambo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia fedha hizi za basket fund, hapa naomba tuwe na utaratibu mzuri. fedha hizi nadhani zinatoka Wizara ya Afya zinakwenda TAMISEMI halafu ndio zinakwenda eneo la kutolea huduma, lakini zinachukua pia muda mrefu sana. Sasa tatizo hapa sijui wapi wanapochelewesha kati ya Wizara ya Afya au TAMISEMI? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitolee mfano, fedha za mwezi wa saba katika halimashauri yangu, yaani quoter ya kwanza na ya pili zimekuja kutoka Desemba mwishoni. Sasa maana yake kazi yake zinakwenda kufanyiwa Januari. Hapa kutakuwa na ucheleweshaji wa mambo mengi yaliyopangwa kwenye ule mpango. Hata hivyo, tunasababisha hoja kwa hawa watu wa halmashauri. Kwa sababu, kwa nini hawakutekeleza huu mradi kwa wakati husika? Kwa hiyo, niombe sana kama ni Wizara ya Afya na mimi siamini, lakini pia siamini pia kule kwa Mama yangu Kairuki kama ndiko wanakochelewesha. Sasa niombe mkae mzungumze ni wapi hizi fedha zinacheleweshwa? Lakini tuzitoe kwa wakati zikafanye ile miradi iliyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kama nilivyosema pale awali, tumejenga vituo vya afya na vituo hivi vya kutolea hudma za afya ni vingi sana. Iko shida mpaka sasa sealing inayotumika ni ile ile ya miaka mitano. Maana yake ni nini? Kama eneo limejengwa sasa hivi vituo vya afya vitano au zahanati tano mpaka kumi, zahanati hizi zinatumia bajeti ile ile ya miaka mitano iliyopita. Hii inapelekea watu hawa kupata mgao mdogo tofauti na uhalisia uliopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu tupeleke hizi dawa, tupeleke hizi fedha kulingana na hali halisi iliyopo kwenye mazingira hayo. Tunajua na mnajua kwamba Serikali sasa hivi inafanya kazi, kila siku tunajenga, kila siku tunasajili basi tunaposajili tuingize kwenye mfumo na sealing isomeke na dawa ziende kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yangu yalikuwa haya naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ningependa sana niende kwenye kipengele hiki cha migogoro. Si kizuri, lakini sasa inabidi tu tukisemee, ilipaswa tuje hapa tuchangie maeneo mengine ya kuboresha zaidi, lakini sasa inabidi turudi nyuma tusemee migogoro. Wamesema wenzangu hapa, na tayari wamesema chanzo cha migogoro ni sisi kutopima maeneo yetu kwa ukubwa wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naliongea hili jambo leo hapa kwa mara ya tatu; ni mgogoro wa mashamba ya wakulima Ndika. Wako wananchi Kijiji cha Mkuani, Makuka pamoja na sasa mgogoro unakua unaenda mpaka Kata nyingine ya Kipapa. Mkuani iko Kata ya Maguu, wananchi hawa tangu mwaka 2017 walichukuliwa mashamba yao na mradi unaoitwa Panda Miti Kibiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hapa mimi niombe sana Serikali msomane. Maana tunaisema Wizara ya Ardhi lakini kumbe ndani yake kuna watu wengine Wizara ya Maliasili na Utalii na wengine wako humo ndani lakinimambo yanaenda Wizara ya Ardhi tu. Niombe sana Wizara hizi zisomane na mambo haya muyapange kwa pamoja, ili tuwe na amani katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Panda Miti Kibiashara sidhani kama Waziri wangu wa Ardhi anahusika nao hivyohivyo, huu uko upande wa Wizara ya Maliasili na Utalii; lakini ardhi ile imechukuliwa ni ya wananchi waliokuwa wanaimiliki kwa halali kabisa. Wananchi wale wamekaa pale tangu kupata uhuru nchi hii, lakini kwa bahati mbaya sana anakuja mtu mmoja leo anasema anataka kuanzisha hili shamba ninyi ondokeni, lakini la pili kwa sababu, sijui umepatikana wilaya nyingine, zamani tulikuwa wilaya moja, sasa ninyi ni wilaya nyingine ondokeni, mkitaka mkaombe kule. Nani anasema tukigawa mipaka hii ya kiutawala inanyima uhuru na umiliki wa ardhi wa mtu Mtanzania huyu, ni nani anasema hivyo? Si sawa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wananchi wale wanapata shida kuanzia mwaka 2017 mpaka leo. Wanakufa njaa ilhali wana mashamba yao pale kwa sababu tu ya mambo haya, mtu anakuja analianzisha hili jambo kirahisi tu hivi. Sasa niombe Waziri, wakati fulani Mheshimiwa Waziri Lukuvi alianza kulishughulikia hili na pakawa na amani, lakini ilifikia hatua pale maeneo yale, sisi hatujazoea, sisi Wamatengo kule mambo ya vita haya hatujazoea, lakini watu wametupiga risasi pale. Mgogoro, unapiga mtu risasi. Wanapigwa mapanga pale, kwa nini iwe hivyo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Waziri, tutatue huu mgogoro kwa sababu mashamba yale ni ya watu walikuwa wanaishi pale miaka yote. Kuanzisha huu mradi kama kweli wanataka hawa watu kuchukua yale mashamba, mbona sheria ziko wazi, walipe fidia. Walipe fidia ili wananchi wale waondoke pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nimshukuru sana Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, Mheshimiwa Aziza Mangosongo. Amefika anajitahidi kupambana na huu mgogoro, ili ufike mahali, lakini sasa kwa sababu uko na wilaya nyingine anashindwa. Sasa niwaombe, Mheshimiwa Rais wa nchi hii anafanya kazi nzuri ya kumaliza migogoro, siyo mpaka mgogoro huu wa Ndika tumsubiri Rais aje kutamka maneno pale, Waziri upo na viongozi wengine wapo, njooni mmalize huu mgogoro, tusimsubiri Mheshimiwa Rais, tunampa mzigo mkubwa, ana mambo mengine ya kutuletea fedha na maendeleo mengine ndani ya nchi hii. Hii migogoro ndiyo maana mpo nyie mtusaidie uishe, pale mahali wala si mahali pakuchukua muda mrefu; ukifika Waziri kwa sababu, maeneo ni ya watu utatamka tu neno, wananchi wale watasherehekea na ng’ombe watakupa, si rushwa, lakini ni sadaka kwa ajili ya shukrani; sisi wamatengo tunatoa shukrani. Uje ututamkie ili wananchi wa Ndika, wananchi wale kutoka Kipapa wawe na amani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna kijiji kingine kipo pale, Kijiji cha Kata ile ya Burma, Kata ile ya Mpapa. Na kwenyewe tuna kijiji muda mrefu, kiko pale, lakini wamekuja watu sasahivi eneo lile lote wamelihamisha. Tumejenga mpaka shule, mpaka sasahivi wanafunzi wanatoka maeneo mengine mbali wanakuja kusoma kwenye shule ile ambayo ilikuwepo pale na kijiji kilikuwepo. Lakini ni kama nilivyosema suala hili si lako peke yako, zungumza na Wizara hii ya Maliasili na Utalii, mipango hii wanapofanya basi waifanye vizuri, ili kwamba mwisho wa siku tusilete hii mivutano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro huu wa Ndika sasahivi wananchi wameamua kwenda kulima wenyewe. Wanasema hivi, kule kulikuwa ni kwetu, tuliondoshwa, sasa mtu kurudi kwao nani atakayemfukuza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamerudi pale, lakini kilichofanyika pale ni kama wametengeneza, yaani mgogoro wenyewe sasa ndio unaenda kuwa mkubwa. Kwa sababu wananchi wamesema sisi tunarudi kwetu. Tumeisubiri Serikali itoe maamuzi haijatoa, sasa sisi tunarudi kwetu kwenye mashamba yetu. Kwa hiyo hofu yangu tunakoenda huku kutakuwa kubaya zaidi kuliko huku tulikotoka. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri twende tukalimalize hili suala pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili. Nikushukuru sana kwa huu mpango wa hii fedha ya mkopo maana na mimi Mbinga ni mnufaika. Wananchi wetu katika vijiji vya Mbinga tutapata, japo ni vichache, tutapata na sisi kupimiwa viwanja vyetu. Ombi langu sasa, kama si kitu kibaya, Kamati hapa imeshauri kwa nini zile fedha nyingi zile bilioni 47 zikatumike kwa matumizi mengineyo na si kupima ardhi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama si kuvunja sheria, basi Mheshimiwa Waziri chukua huu ushauri wa Kamati. Kwamba, zile fedha nyingi tukapime vijiji vingi. Na hesabu zimetolewa hapa na Mheshimiwa Komredi Kunambi hapa, ametoa hesabu vizuri sana. Ametoa hesabu kwamba, tukipima vizuri fedha hizi tunaweza kupima vijiji vingi zaidi, ili kuvifikia hivi vijiji na lengo likiwa kupunguza hii migogoro. Maeneo haya yakipimwa mengi maana yake migogoro itapungua sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine nilikuwa napendekeza; maeneo yetu haya, ardhi yetu hii kwa sababu hatujaipanga wananchi wanajichukulia hatua ya kwenda kukaa kila eneo. Kila eneo wanaenda kukaa, kila eneo wanaanzisha kijiji, kila eneo wanaanzisha mji, suala ambalo linasababisha hata Serikali kupata ugumu wa kupeleka huduma kwenye hayo maeneo. Sasa tukipanga, utoaji wa huduma na kupeleka huduma nyingine kwenye maeneo haya utakuwa ni rahisi sana, lakini pia tutaitunza ardhi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke tulipopata uhuru tulikuwa wangapi? Na mwaka huu tuko wangapi? Na miaka ijayo inayokuja tutakuwa wangapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ardhi yetu imebaki ni ileile. Kwa hiyo, tukiipanga hii, kama wananchi watakaa maeneo fulani na maeneo mengine yatakuwa kwa shughuli nyingine itakuwa ni jambo jema zaidi na ardhi yetu itakuwa nyingi na kubwa kuliko, hiataisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona niseme haya kwa nafasi hii. Nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. Asante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuzungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote na mimi niungane na wenzangu kwa dhati kabisa kuunga mkono bajeti hii kwa mipango mizuri ambayo Mheshimiwa Waziri amekuja kutuonesha hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuunga mkono nizungumzie utekelezaji wa mradi wa REA katika Jimbo la Mbinga Vijijini. Ninaipongeza Serikali kwa nia ya dhati kabisa kwamba ina lengo la kutekeleza mradi huu ifikapo mwaka wa fedha ujao, kwamba ifikapo mwaka wa fedha ujao basi vijiji vyote vitakuwa na vimefikiwa na umeme kupitia mradi huu wa REA. Ninaipongeza sana Serikali na kwa kweli imeonesha dhati hiyo kwa sababu vijiji vingi katika Majimbo mengi asilimia ya utekelezaji ni kubwa sana, lakini napata shida kubwa sana mradi huu namna unavyotekelezwa katika Jimbo la Mbinga Vijijini, na napata hofu kubwa kama lengo hili la Serikali litafikiwa kwa namna Mheshimiwa Waziri alivyolisema hapa wakati anatuhutubia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mbinga Vijijini lina vijiji 117, vijiji 44 tu mpaka leo ndivyo vilivyofikiwa na umeme wa REA, vijiji zaidi ya 70, mahala pengine ni Majimbo mawili haya, hawajafikiwa na umeme huu. Vijiji 30 hata nguzo hazijafika, kilichofanyika katika vijiji hivyo ni survey tu. Naomba nikusomee hapa Mheshimiwa Waziri usifikirie natamka tu, vijiji 30 havijafanyiwa kazi kilichofanyika ni survey tu, hamna nguzo hamna mashimo, hamna chochote, vijiji hivyo ni Kijiji cha Mkalite, Kijiji cha Mkoa wa Asili, Kijiji cha Langiro, Kijiji cha Makonga, Kijiji cha Ndanga, Liyombo, Ukombozi, Kizota, Kitumbi, Muhilo, Matuta, Lingomba, Mkoha, Langilo Mkaoni, Mkuka, Kihongo, Kitesa, Ugano, Tunolo, Njombe, Ndembo, Ulorela, Silo, siyo wewe Mwenyekiti, hiki ni Kijiji chetu kule. Kijiji cha Mpawa, Sara, Kihumboburu, Mapipili, Liwii na Kiangimauka. Vijiji hivi hata nguzo hazijafika huko sasa napata shida sana ikiwa lengo hili linaweza kufikiwa kama alivyotamka Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu, Mheshimiwa Waziri mimi nakuamini sana wewe namuamini pia Naibu Waziri, pia na wataalam wa mradi huu REA nawaamini wako vizuri, uzuri nimefika kwako ulinikutanisha na hao wataalamu tukapanga mkakati mzuri wa namna ya utekelezaji wa huu mradi, lakini nikuambie Mheshimiwa Waziri tangu tulivyokutana naye mwaka jana mwezi wa nane amewasha vijiji viwili tu, pamoja na mpango mzuri aliousema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tuliongea na Mheshimiwa Waziri na hivyo vijiji vimewashwa baada ya mimi kuja kwako, vijiji viwili tu vya Charukalasi na Kijiji cha Lihale. Vijiji hivyo vingine vyote havijawashwa, sasa huu toka mwaka jana mpaka mwaka huu na anasubiri pengine bajeti inakuja ndiyo wanafanya fanya hizi kazi ikiisha hii bajeti kimya. Ombi langu la kwanza, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana, hebu njoo Jimbo la Mbinga Vijijini, najua kufika kwako wanasema mgeni aje mwenyeji apone, inawezekana kabisa ukifanya ziara katika Jimbo hili mabadiliko yanaweza kutokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili niombe Mtendaji wa REA amenihakikishia, hapa naipongeza Serikali kwa sababu fedha zipo shida siyo fedha, kama shida ni huyu Mkandarasi basi ifanyike namna kuliko tunakaa maeneo mengine miradi inaenda mpaka hii kilomita mbili hizi watu wametekeleza sisi kule kilomita mbili hatujaanza, hatujui tutaanza lini bado tunahangaika na ile kilomita moja hivi vijiji 70 vyote havina kitu. Kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri na niko chini ya miguu yako nyumba yangu inaungua moto kule njoo uizime. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine niombe Wilaya ya Mbinga kunakatika sana umeme na hapa yamezungumzwa sana. Nilisema mwaka jana lakini niliuliza swali hapa, Serikali iliahidi itafanya utekelezaji bajeti inayokuja ya 2024/2025, sasa kwa sababu mipango yetu ni mizuri na inaenda vizuri, mimi niombe ule mpango muurudishe uanzie mwaka huu kwa sababu hali inavyokatika umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shida ni kwamba ile lane ni ndefu sana ukianzia Songea, ije Mbinga mpaka Nyasa lane ni moja. Kwa hiyo, ninaomba sana ile mipango ya ujenzi wa substation basi na sisi awamu hii mtufikirie tuwe na substation pale, kwa sababu ukuaji wa Mbinga ni mkubwa sana, sasa hivi tuna Uchimbaji wa makaa ya mawe watu wameongezeka sana na tuna viwanda vingi sana viko pale vya kahawa na viwanda vingine vya maji, kwa hiyo wanahitaji umeme kwa ajili ya uzalishaji. Nikuombe Mheshimiwa waziri utufikirie tupe substation ili na sisi tusahau shida hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ninampongeza sana Mheshimiwa Rais wa nchi hii, nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake kwa kufanikisha mazungumzo haya ya LNG, kwa sababu mazungumzo haya kwa kweli yalikwama muda mrefu sasa yanaonesha njia kabisa kwamba tunaenda kupata mradi huu mkubwa wa kuingizia pato kubwa nchi yetu. Hongereni sana, hongereni sana hongereni sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee lile suala la hofu ya mradi ule wa Songas, mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri wakati tunaenda na miradi hii mikubwa hata ile miradi midogo midogo ambayo ilikuwa inatusaidia wakati tuna crisis ya umeme tusiisahau, tusiiache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbukumbu zangu kama niko sawa sawa mradi huu ni wa PPP na unaunda na wabia wa nchi tatu, Tanzania ikiwemo Norway na Uingereza. Sasa nikuombe Mheshimiwa Waziri, ule mkwamo uliopo wa hofu iliyopo katika kampuni hii, kwamba mkataba inawezekana Serikali haina haja ya kuendelea na mkataba, kwamba TANESCO ndio inaweza kuendesha huu mradi. Aah! mimi nikuombe Waziri fanya mambo, kama kuna vipengele katika ule mkataba havifai na mimi najua wewe uko makini pengine linaloonesha hapa kukwamakwama kidogo ni vipengele vya mikataba wa ule mkataba, ikiwemo Naibu Waziri ni Mwanasheria mzuri sana lakini najua una wanasheria wazuri sasa hivi katika Wizara yako, kaeni chini mjadili, wekeni vipengele kwa manufaa ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua huu mradi umetusaidia sana, sasa hivi pale Lindi pamechangamka sana, sasa huu mradi ukiwa unaondoka kwa kweli tutaparudisha nyuma na mimi niko eneo hilo la Mikoa ya Kusini ya Ruvuma, Lindi na Mtwara ni Mikoa inayoingiliana, kuchangamka kwa Lindi, kuchangamka kwa Mtwara ndiko kuchangamka kwa Ruvuma. Tukuombe sana Mheshimiwa Waziri endeleza mazungumzo hayo, kwamua huu mradi uendelee kuwepo, wananchi waendelee kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la mwisho nizungumzie suala la mradi huu mkubwa wa Bwawa la Nyerere. Hatua iliyofikiwa na maneno aliyotuambia hapa Mheshimiwa Waziri yamenitia faraja kubwa sana na wananchi wangu Mheshimiwa Waziri wamenipigia simu kwamba walikuwa wanasikia hadithi. Sasa maneno uliyoyasema hapa wamefarijika sana, wanakupongeza sana Mheshimiwa Waziri, pia wanampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa sababu hakurudi nyuma alikwenda mbele kutoa fedha na sasa tunaambiwa baada ya wiki moja bwawa lile lina uwezo wa kuzalisha umeme, lina uwezo wa kuanza kuzalisha umeme. Hongera sana Mheshimiwa Waziri lakini hongera sana kwa Awamu ya Sita kwa kutenda kazi hii njema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi, naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi. Kwanza nampongeza Waziri, Naibu Waziri na timu nzima ya Wizara naona wamejipanga vizuri, na tumeona mwanzo umekuwa mzuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda nitaongelea hoja moja ya Kahawa. Nampongeza sana Waziri, kwa muda mfupi ametoa taarifa, ameanza kusambaza miche ya kahawa katika maeneo yale yanayolima kahawa. Kwa bahati mbaya, sisi wana Mbinga tunalima kahawa na kwa bahati mbaya hatukupata miche. Nina uhakika kwa sababu ulikuwa mwanzo, sasa hivi ataenda kutoa miche Wilayani Mbinga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Mbinga wamenipigia simu hapa, wana imani kubwa sana na Mheshimiwa Waziri. Wanaomba kwamba akimaliza bajeti hii, basi apange muda akawatembelee. Wako tayari kumpokea na wana mashamba wameandaa, wanachosubiri sasa hivi ni miche ya kahawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, suala la Bodi ya Kahawa. Mimi sifahamu, Bodi nyingine unasikia zimechangamka zinafanya hivi, lakini Bodi ya Kahawa sisikii chochote. Kwani wao siyo Bodi kama Bodi ya Pamba? Kwani wao siyo Bodi kama Bodi ya Korosho? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ongea na huyu Bwana wa Bodi ya Kahawa, kwa sababu tunataka tuone nchi inachangamka. Kama Korosho Bodi inafanya hivi, Pamba inafanya hivi tunataka kuona na Kahawa pia mtu wa Bodi anafanya kitu fulani. Mpaka saa hizi sijaona Bodi inafanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, waliweka malengo ya kuongeza uzalishaji kwenye kahawa, lakini sijaona mikakati hasa ya nini kinaenda kufanyika. Kama Bodi, wao wanafanya nini? Kwa hiyo, nakuomba Mheshimiwa Waziri, najua umejipanga vizuri kwenye hili na ulininong’oneza pembeni kwamba Mbinga watapata miche mingi kwa sababu Kahawa ya Mbinga ni nzuri zaidi halafu tamu na inapendwa zaidi duniani huko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la mbolea. Sisi wana-Mbinga bila mbolea hatujavuna. Tunamshukuru Mungu safari hii tulitumia miujiza. Maana yake mfuko mmoja tumetumia zaidi ya ekari mbili mpaka tatu. Kwa hiyo, tunashukuru mazao yamekua lakini uzalishaji hautakuwa kama ule tuliouzoea miaka yote. Kwa hiyo, uzalishaji kidogo utapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa lile wazo la ruzuku ya mbolea. Nami nikuomba suala hili kama ulivyosema jana, uko tayari ukose vingine vyote lakini tupate ruzuku ya mbolea. Mbinga ni wazalishaji wakubwa wa mahindi, lakini hatuwezi kuzalisha bila mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda huu mfupi, nashukuru sana. Nilikuwa na mambo hayo mawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote niungane na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake lakini na wataalam kwa ujumla. Nampongeza Waziri kwa dhati kabisa kwa hii operation ya postcode, Mheshimiwa Waziri amekuja muda mfupi tu, lakini kazi aliyoifanya kila mtu ameiona. Kwa kweli hongera sana kwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Mbinga, pamoja na pongezi hizi, kwa upande wa Mbinga nina masikitiko kidogo. Kazi imefanyika vizuri, kwa bahati mbaya tumekwenda kuvuruga miradi iliyokuwa inaendelea. Wilaya ya Mbinga ina shida sana ya barabara, barabara hizi za TARURA na unajua Halmashauri ya Mbinga Vijijini ni milima na mabonde. Kwa hiyo, kwa muda mrefu barabara zetu zinapitika kwa shida sana. Zipo barabara tulizitengea fedha kwa bahati mbaya sana barabara zile fedha zimeondolewa zimepelekwa kwenye postcode. Sasa sijajua kama na katika maeneo mengine kumefanyika hivyo. Kama maeneo mengine haijafanyika hivyo kwa nini sisi Mbinga; Barabara ya Ngima kwenda Litembo ambako kuna hospitali, Barabara ya Mitawa kwenda Ilela na Daraja la Linyani, fedha za miradi hii imeondoshwa imepelekwa kwenye mradi wa postcode.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kati ya yale mabao na barabara kipi muhimu zaidi, hivi ni nani anaweza kuvumilia kukosa kuona kibao na kukosa kupita njia nzuri kwenda hospitali? Litembo nilisema hapa ndipo tunapotibiwa sisi, barabara hii inapitiwa na Kata nne za Ngima, Mkumbe, Ukata na Kipololo, lakini pia Kata ya Ukilo zote hizi zinatumia barabara hii. Hali ya barabara hii ni mbaya sana. (Makofi)

TAARIFA

MHE. ENG. STELLA M MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nimshtue kidogo kaka yangu, Mheshimiwa Benaya nadhani kwa uchungu wa zile barabara zilizokosa fedha amesema hata yale mavibao yana haja gani. Kimsingi kwa kweli anuani za makazi ni muhimu na vile vibao ni muhimu, kwa hiyo ningeomba tu kwamba pamoja na uchungu huo lakini tujiweke vizuri kidogo. Ahsante sana.

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei hii taarifa yake kwa sababu ananipotezea muda wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naomba unilindie dakika zangu. Namheshimu sana dada yangu Injinia Stella Manyanya na ndiyo Mwalimu wangu; lakini kwenye hili sijakaa mradi ule ni mradi mzuri, nafikiri kwenye maelezo yangu ya mwanzo sijui hakunisikia, ni mradi mzuri, lakini nilikuwa nahoji hapa, hivi mtu akikosa kusoma kibao na akakosa barabara, yupi ataumia hapa? Ndiyo hoja yangu ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii mwaka 2020/2021 iliondolewa fedha; tukaitengea fedha 2021/2022 inaondolewa tena fedha, hivi kweli kwa sababu zipi za msingi kiasi hicho? Pia nilikuwa nahoji hapa, hivi ilivyofanyika Mbinga ndivyo yalivyofanyika kwenye Majimbo mengine? Kama sivyo, kwa nini sisi tufanyiwe hivyo. Barabara hii inakwenda kwenye Hospitali pekee ya Halmashauri ya Wilaya Mbinga kwa maana ya Hospitali ya Misheni tunayoitumia sisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hapa zaidi ya kata tano zinapita hii barabara na barabara hii utafikiri ni palio la ng’ombe, mashimo mashimo, mawe mawe, haipitiki.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge, muda wa Mheshimiwa unakaribia kwisha, ngoja amalizie hoja yake anayoongea.

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi wananchi wanalazimika kwenda Mbinga ndiyo waende Hospitali ya Litembo, wanalazimika kwenda Mbinga kilometa zaidi ya 30, wakati pale kuna kilometa 10 tu wanafika hospitalini. Mama Mjamzito anaongezewa safari ya kilometa ya zaidi 30, kwa kweli jambo hili limenisikitisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uzuri wa mradi huu pamoja na mimi naheshimiana sana na Mheshimiwa Nape, lakini nataka kwenye majumuisho anieleze fedha hizi zitarejeshwaje na miradi hii itatekelezwaje, bila hivi mimi nitaondoka na Siwa hii. Haiwezekani hili Siwa mimi nitatoka nalo ni lazima aniambie Mheshimiwa Nape miradi ile inakwenda kuishaje? (Makofi) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kapinga.

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naam!

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kapinga hebu kaa chini, hebu kaa chini kwanza.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kuhusu Utaratibu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge.

KUHUSU UTARATIBU

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanuni ya 71(j) lugha inayotumika ambayo kwa kiasi fulani inakera. Mheshimiwa Kapinga ninamheshimu sana na ninafahamu bado ni kijana ni Mbunge wa mara ya kwanza, kwenye record zetu hakuna mtu amewahi kuondoka na Siwa, kwa hiyo, wewe utakuwa ni Mbunge wa kwanza kuondoka na Siwa. Hili Siwa ndilo Bunge lenyewe. Kwa mujibu wa utaratibu wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola Siwa hili limewekwa ndiyo heshima yetu, ndiyo tunalolisalimia hapo na ndiyo inayoshika mamlaka ya Spika. Kwa hiyo, wewe ukiondoka na hili Siwa maana yake umeondoka na hili Bunge lote umekwenda nalo Mbinga. Kwa hiyo, ninakuomba tu ama ufute maneno hayo ili uendelee kutoa mchango wako mzuri na mimi naamini wewe ni Mbunge mzuri sana. (Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kapinga.

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kufuta maneno hayo. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi. Awali ya yote na mimi niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri Dkt. Angeline umefanya kazi kubwa sana katika Wizara hii, hongera sana. Mimi nakumbuka ukiwa Naibu Waziri tumefika hadi huko Masasi kwenye vitongoji huko kutatua migogoro, ukiwa na nguvu timamu kabisa kwakweli hongera sana mama yetu. Lakini pia nampoingeza pia Naibu Waziri, kwa muda mfupi tu ame-cope na Wizara hii, hongera sana Naibu Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza makatibu na naibu katibu. Pia naipongeza Serikali kwa kufanya uamuzi ule wa kumrejesha Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba. Uamuzi ule ni wa manufaa sana kwa nchi yetu. Waswahili wanasema uchungu wa mwana anaujua ni mzazi. Tunajua mkurugenzi yule ndiye aliye lihuisha lile Shirika, kwa hiyo mambo mengi na miradi mingi alikuwa anaifahamu. Kwa hiyo nawapongeza sana nakupongeza Waziri lakini naipongeza Serikali kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niungane na wenzangu pamoja na Bunge hili kwa uzito mkubwa kumpongeza Rais wetu kwa ushindi Mkubwa wa hii Tuzo ambayo ameipokea. Ushindi huu ni mkubwa kwa nchi yetu lakini kwa maendeleo ya Taifa letu. Kwa niaba yangu mimi mwenyewe lakini kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mbinga Vijijini natoa hongera sana sana sana kwa Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitajikita kwenye maeneo mawili. Eneo la kwanza ni eneo hili la maduhuli ya Serikali. Ninaipongeza Serikali, naona wanafanya jitihada mbalimbali za makusanyo lakini bado tupo nyuma sana kama taarifa ya Waziri inavyosema na hata taarifa ya Kamati imeeleza hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka uliopita tulitarajia kukusanya kwa asilimia 100, lakini kwa bahati mbaya sana tumefikia asilimia 42. Hata hivyo bado mwaka huu nimeona tumejiwekea malengo ya ongeleko la asilimia 11. Mimi hofu yangu tu ni kwamba, ikiwa mwaka jana hatukufikia malengo hata kwa nusu kwanini awamu hii tumejiwekea malengo yanayozidi tena kwa asilimia 11? Ipo mikakati gani, mikakati ipi tumejiwekea ya kwenda kuyafikia haya malengo ya mwaka huu? Kwa hiyo niombe Wizara kwa dhati kabisa, wenzangu wamesema hapa, na mzungumzaji aliyetangulia amesema hapa; sisi kule vijijjni wananchi wetu wapo tayari kumiliki ardhi lakini tunanyimwa fursa hii wananchi wetu hawana hati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa hawana hati tunawanyima fursa nyingine lakini pia sisi Serikali tunajinyima fursa ya kupata haya maduhuli ambayo pengine tungefikia haya malengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niiombe niiombe sana sana sana Serikali, kama tumejiwekea ongezeko hili la asilimia 11 basi tuone na mikakati ya dhati kabisa, kabisa kabisa; na mimi nawaamini, ninamuamini Mheshimiwa Waziri lakini ninamuamini Mheshimiwa Naibu Waziri, uwezo huo mnao, nawaomba sana tufanya mabadiliko. Tumeona kwenye kilimo mambo yanakwenda, tuone pia hapa kwenye ardhi; hili ongezeko hili la asilimia 11 tuweze kulifikia. Na hatuwezi kulifikia kwa kuzungumza tu hapa, tunataka tuone mikakati ya dhati. Hivyo nikuombe Mheshimiwa Waziri utakapokuja kuhitimisha hoja hapa kesho utueleze mikakati inayowezesha kufanikisha mpango huu kwa sababu fursa zipo kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni kuhusu migogoro. Ninaiona jitihada ya Serikali ya kutatua hii migogoro ya ardhi, ipo, lakini migogoro hii utatuzi wake unachelewa sana. Tumesikia kuna Tume, kuna Kamati lakini majibu mpaka leo hakuna. Na tutambue ndugu zangu, kucheleweshwa kwa haki hizi tunawachelewesha Watanzania fursa nyingine; tunawachelewesha sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na wanasema haki iliyocheleweshwa ni sawa na haki iliyopotea. Kwa hiyo niwaombe sana ndugu zangu, niombe Wizara tufanye juu chini migogoro hii itatuliwe kwa wakati. Nitaomba pia Mheshimiwa Waziri utupe hatua gani utachukua ili kuharakisha utatuzi wa migogoro hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitolee mfano kwenye jimbo langu pale upo mgogoro tangu miaka iliyopita na mimi nimeukuta. Wamekuja viongozi, upo, mpaka leo hii, katika Kijiji cha Ndika. Ndika hii niliisemea mwaka jana, na naishukuru Wizara, kwa sababu mlikuwa wote na Mheshimiwa Lukuvi, alijaribu kutoa maelekezo yalipunguza migogoro zaidi kwa sababu ilifikia hatua watu walikuwa wanarushiana risasi pale. Risasi zilipigwa na mapanga yalipigwa kwasababu maeneo ya watu ya kulima yamechukuliwa bila hata yakufuata utaratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi hapa niombe sana mnisaidie mgogoro huu huishe, kwa sababu mpaka ninavyosema sasa hivi wananchi wamejipanga kuacha kupeleka watoto shule wakisema tutapelekaje watoto shule wakiwa wana njaa? Kwa sababu maeneo yao waliyokuwa wanalima siku zote hawalimi tena, ni miaka zaidi ya mitano hawalimi wanakaa tu kusubiri Serikali itatuondolea kero hii, Serikali itatatua mgogoro huu, mgogoro hautatuliki mpaka leo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana Wizara. Jitihada mwaka jana ilionekana lakini haijafikia mwisho. Kwa hiyo niombe sana Kijiji cha Mkuka, Kijiji cha Mkuani lakini pia kata ya Jirani ya Langilo na kata ya Kipapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi inafika sehemu, kwa sababu watu wa TFS wao ndio wanaoonekana kufanya ulinzi eneo lile, wananchi hata kupita njia wanahofu. Na ni kweli ukipita wanakufanyisha mazoezi ya kichurachura sijui na nini! Kwa kweli niombe Wizara tutatue migogoro hii haraka haraka. Kwa kuchelewesha kutatua migogoro hii, kama nilivyosema pale mwanzo, watu wanakosa fursa ya kimaendeleo kwa sababu hawazalishi. Watu wanakosa chakula, na ndiyo maana sasa wamesema Mheshimiwa Mbunge sisi hatutapeleka watoto wetu shule, hatuwezi kupeleka watoto shule wakiwa na njaa. Miaka mitano hadi sita mgogoro tu wa eneo la wakulima hautatuliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nimshukuru Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, amekuja naye muda mfupi pale ameanza kuchukua hatua. Kwa ushirikiano wetu, kwa maana ya Wizara naye pengine tutayafikia haya majibu haraka au kwa wepesi zaidi. Kwa hiyo, nawaomba sana Mheshimiwa Waziri utakapokuja kujumuisha hapa, unipe majibu ya namna ambavyo tunaenda kumaliza huu mgogoro. Kwa leo nilikuwa sina mengi, nilitaka nisema haya, nawashukuruni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa dakika tano ulizonipa, ahsante sana. Nami niungane na wenzangu kuipongeza Wizara na Serikali kwa ujumla. Kwa dakika tano hizi naomba nizungumze jambo moja suala la REA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza michango ya Wabunge wenzangu humu ndani wamezungumza kwa hisia sana na wamezungumza kwa hisia kwa namna mradi wa REA unavyotekelezwa kwenye Majimbo yao. Pamoja na hisia hizo baadhi ya Wabunge wenzangu atakwambia vijiji vilivyobaki katika Jimbo lake 10, 11, 12.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa jimbo langu linavijiji vikubwa vipo 117, kati ya vijiji hivyo vijiji vilivyopata umeme ni vijiji 34 na kwa bahati mbaya kati ya vijiji hivyo 34 vijiji Tisa zimesimikwa nguzo tu lakini tunasema vimepata nini umeme, vijiji 86 vyote havina umeme, Kata 15 hazina umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemuomba sana Roho Mtakatifu anishukie hapa nizungumze kwenye kona zile za Mheshimiwa Spika. Kwa sababu wenzangu wamezungumza hapa kwa hisia kali sana ni vijiji 10,15, 20, mimi vijiji 86 ongeza Tisa ni vijiji vingapi havina umeme? Kwa hiyo, kwa masikitiko makubwa sana, nashukuru sana Mheshimiwa Waziri nakuheshimu sana na bahati nzuri nilikuja kukuona umenipa ushirikiano mzuri, ukanikutanisha na Mkurugenzi REA naye alinipa ushirikiano mzuri akanikutanisha na Wakurugenzi wake, Wasaidizi wake na bahati nzuri akamuita na Mkandarasi. Kwahiyo, niombe yale tuliyokubaliana yale tuliyozungumza na moja ulilolisema ni kuja Mbinga kuangalia hali ya utekelezaji wa huu mradi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua ujio wako utatoa push sasa tunasema vijiji 23, vijiji 9 zimesimikwa nguzo tu, nguzo imesimikwa hivyo vijiji vingine mwenzangu alisema hapa jana kwamba utekelezaji wa huu mradi ni 0.5, maana yake ni kama wameenda ku-survey tu, yaani wamefanya survey tu na pengine wamelaza nguzo. Kwa hiyo, kwa ujumla mradi huu Jimbo la Mbinga na nilimwambia waziri sehemu itakayokuonesha wewe umeshindwa kutekeleza mradi huu kwa asilimia 100 ni Mbinga na kama si Mbinga basi Mkoa wa Ruvuma kwa sababu hata Tunduru kuna vijiji 86 havijaingiziwa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana Waziri atakapofanya majumuisho hapa atueleze namna ya kasi itakavyokwenda katika Jimbo la Mbinga Vijijini ili ifikapo Desemba kama walivyoahidi nasi vijiji vyetu vyote viingie kwenye umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine napata faraja kidogo wanasema kawia ufike, nimeona kwenye hiki kipeperushi kwamba tunaenda kusambaza umeme sasa kwenye vitongoji hasa kwa vile mimi vijiji vyangu 86 havipo kwenye mradi huu vimechelewa kuingia kwenye mradi wa umeme; 86 sasa tunaenda kwenye vitongoji ninauhakika tutaanzia huko na vitongoji kwamba sasa vitongoji vyote na vijiji vyote vitapata umeme ninauhakika huo najua hautaniangusha hapa kwasababu tumechelewa kusubiri umeme sasa tuna bahati sasa tunaaanza vitongoji na kwasababu sisi tulichelewa zaidi basi tutaanzia hapo ndiyo maana nimefarijika kusema kawia ufanye nini? ufike na kutangulia sio kufanya nini? kufika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona niseme hilo tu kwa hizo dakika na nashukuru sana kwa kuniruhusu. Ahsante. (Makofi)