Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon Lucy John Sabu (16 total)

MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Ninalo swali moja ambalo kwa kuwa NHIF na WCF walishaomba kibali hususani kwa ujenzi wa kiwanda hiki.

Ni lini sasa Serikali itatoa kibali cha ujenzi wa kiwanda hicho cha vifaa tiba Mkoani Simiyu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Lucy John Sabu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama nilivyosema tayari mkakati huu wa kujenga kiwanda hicho upo na kweli WCF na NHIF ndiyo walikuwa wamepewa kazi hiyo kujenga kiwanda hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Kamati Maalum ambayo inaratibu au inashughulikia sekta ya viwanda vya dawa na vifaa tiba ambao wanaendelea kuchanganua namna bora kama nilivyosema ya kutekeleza mradi huu. Kwa hiyo, kama nilivyosema tukishakamilisha taratibu hizo kiwanda hicho kitaanza kujengwa mara moja kupitia mifuko hii, lakini pia na MSD nao watashiriki kuhakikisha tunakidhi vigezo vya kutengeneza dawa zenye ubora unaotakiwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu.
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Ninalo swali moja dogo la nyongeza; kwa kuwa vijana wengi kutokidhi vigezo na masharti yatolewayo na mabenki.

Je, Serikali haioni haja ya kuweka kigezo cha miradi ama business plan ili vijana wengi waweze kukopesheka? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lucy John Sabu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kabla ya kujibu swali hilo, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi zake za kuwatetea vijana. Ni kweli kwamba vijana walio wengi wanamaliza masomo na wengine ni hodari sana, wana uwezo mzuri wa kielimu, lakini hawakopesheki kwa sababu hawana dhamana. Serikali italichukua hili kulipeleka kwa wataalam wetu kulifanyia uhakiki, ikionekana jambo hili linapendeza, basi business plan itatumika kama ni kigezo cha dhamana katika benki za Serikali.
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.

Kwa kuwa teknolojia inabadilika kila wakati; je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha kuwa hizo CCTV camera na alarm systems zinahuishwa kila wakati?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Serikali imeshachukua hatua ya kuanza kufunga mifumo ya kutambua na kudhibiti majanga kwa majengo mapya; je, Serikali inatoa kauli gani kwa majengo ya zamani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Lucy John Sabu, Mbunge wa Viti Maalumu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tumeshaweka mpango wa kitaifa wa kudhibiti majanga hususani majanga ya moto na tayari tumeshaanza kufanga katika maeneo hayo na tunafahamu kwamba teknolojia ni dynamic, inabadilika mara kwa mara na sisi tumejipanga kuhakikisha tunahuisha mifumo hii ya udhibiti lakini pia ya kutambua changamoto za majanga ikiwepo moto kila mara.

Kwa hiyo nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na nimpongeze kwa ufuatiliaji wake mzuri kwamba Serikali imeweka mfumo ambao utakuwa mara kwa mara unapitia na ku-update mifumo hiyo ili iweze kufanya kazi vizuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu majengo ya zamani ni kweli kwamba mifumo hii sasa kwenye majengo mapya imekuwa sehemu ya michoro kuhakikisha kwamba inazingatia uwepo wa vifaa na miundombinu hiyo. Lakini tumetoa maelekezo katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa katika mikoa kote nchini kuhakikisha katika majengo yale ya zamani yakiwemo masoko, Ofisi za Serikali na maeneo kama hayo wanafunga mifugo ya kutambua na kudhibiti majanga ya moto, ahsante.
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa fursa hii, naomba kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itajenga, barabara ya Maswa – Kadoto, kupitia Mnadani kwa kiwango cha lami? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lucy Sabu, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimuondoe hofu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba bahati nzuri maeneo aliyoyataja yapo katika mipango yetu na kadri tutakavyoweka fedha maana yake tutayajenga na yatakamilika. Ahsante sana.
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa fursa hii ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka vifaa tiba ikiwemo mtambo wa kuzalisha oxygen katika hospitali ya Wilaya Meatu katika jengo la mahututi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lucy John Sabu, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka huu wa fedha imetenga Shilingi Bilioni 69.95 kwa ajili ya kununua vifaa tiba na kuvipeleka katika vituo na hospitali zetu kote nchini. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwanza bajeti ya vifaatiba katika hospitali ya Wilaya ya Meatu tayari ipo, lakini tutakwenda kufanya tathmini kuona uwezekano wa kuwa na mtambo wa kuzalisha oxygen kulingana na mahitaji ili tuweze kuona namna ya kutekeleza wazo hilo.
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba niulize swali dogo la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itapeleka mtaalam wa meno katika Hospitali ya Somanda Wilaya ya Bariadi kwa kuwa aliyekuwepo amestaafu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sabu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, anachohitaji ni mtaalam wa meno na ninaamini tunapokuwa tunaajiri, tunazingatia maeneo yenye upungufu. Kwa hiyo, ninaamini pamoja na eneo analolitaja, litakuwa katika hizo sehemu za ajira ambazo zitatangazwa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, ni lini hasa magari mapya ya Wilaya zingine za Mkoa wa Simiyu yatapelekwa ili kuweza kusimamia miradi ya maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa Mkoa wa Simiyu una changamoto kubwa ya vyanzo vya maji, je, RUWASA wamejipangaje, kupeleka mitambo ambayo itasaidia katika kunusuru changamoto kubwa ya maji huku tukisubiri Mradi Mkubwa wa Maji wa Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa ameuliza lini haswa, mara baada ya magari kufika Mheshimiwa Mbunge magari yatafika sisi ni watu wa kuahidi na kutekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu vyanzo vya maji Mkoa wa Simiyu, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Mbunge, kwa Mkoa wa Simiyu tuna mradi mkubwa zaidi ya bilioni nne ambao unatekelezwa kwa mabadiliko ya tabia nchi. Kwa hiyo, Mkoa wa Simiyu tayari umeshatupiwa jicho la kipekee kabisa na tayari miradi hii imeanza kutekelezwa. Vilevile vyanzo vya maji na kwa kutumia magari haya ambayo Mheshimiwa Rais ametupatia fedha nyingi, tayari ni tarehe 11 magari yatazinduliwa na tayari utaratibu wa kufika katika mikoa mbalimbali utaendelea.
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada zinazochukuliwa na Serikali za kupunguza vifo vya wajawazito, lakini kasi ya upunguaji hairidhishi: Je, Serikali imefanya tathmini ya sababu zake?

Swali la pili; kwa kuwa vifo vingi vya wajawazito vinatokana na uzazi pingamizi na majengo mengi yaliyojengwa hususan majengo ya upasuaji hayana wataalamu na vifaa tiba: Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya jambo hilo? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Lucy Sabu kwa suala hili kubwa na nyeti ambalo lote linatugusa wanawake, akina baba na wanaume. Kwa suala la vifo vitokanavyo na uzazi ni kipaumbele cha Serikali kuhakikisha tunavipunguza kadiri inavyowezekana. Sababu za vifo hivi tunazifahamu Mheshimiwa Lucy, ni pamoja na uchungu pingamizi, kutokwa na damu kabla, wakati na baada ya kujifungua. Pia kuna suala la kifafa cha mimba na kuna maambukizi pia ya bakteria.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Lucy pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inayo mikakati mingine ya ziada ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi. Kuanzia Julai tutatekeleza mradi mkubwa chini ya ufadhili wa World Bank wa Shilingi bilioni 460 ambazo tunazielekeza kwenye huduma za akina mama wajawazito na watoto wachanga.

Mheshimiwa Spika, tutajenga vyumba vya wanawake wajawazito mahututi katika hospitali za wilaya, tutawajengea uwezo watumishi wa afya ili waweze kutoa huduma bora za uzazi wakati wa kujifungua, tutaweka vifaa tiba pamoja na dawa za kuzuia vifo vya akina mama wajawazito ikiwemo dawa ya oxytocin pamoja na dawa ya kuzuia kifafa cha mimba Magnesium Sulphate.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba taarifa rasmi kuhusu vifo vitokavyo na uzazi tutazipata mwezi Oktoba, 2022 baada ya Tanzania National Bureau of Statistic kukamilisha taarifa au utafiti kuhusu hali ya afya na demografia nchini Tanzania. Ndiyo tutaona vifo vinapungua kwa kasi ya aina gani. (Makofi)
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza nishukuru Serikali kwa kupeleka fedha katika majengo ya OPD na upasuaji lakini Hospitali ya Mji wa

Bariadi bado ina majengo mengi chakavu ikiwemo jengo la wagonjwa mahututi pia na majengo ya wodi;

Je, Serikali ina mpango gani wa kuyakarabati ili yaweze kutoa huduma bora kwa wananchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Hospitali ya Mji wa Bariadi ina changamoto ya upungufu wa wauguzi na madaktari; je, Serikali inatoa tamko gani juu ya upungufu huu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Lucy John Sabu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Hospitali ya Mji wa Bariadi ni hospitali kongwe na ndiyo maana Serikali iliona umuhimu wa kupeleka shilingi milioni 900 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa majengo ya upasuaji, na jengo la OPD. Zoezi hili la ukarabati na upanuzi wa hospitali ile ni endelevu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kila mara Serikali itakuwa inatenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa hospitali kongwe basi Hospitali wa Mji wa Bariadi pia itapewa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni kweli kumekuwa na upungufu wa watumishi wa sekta ya afya katika Halmashauri wa Mji wa Bariadi. Hata hivyo, mwaka uliopita Serikali ilipeleka watumishi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba zoezi la kupeleka watumishi kila kibali cha ajira kinapotoka Halmashauri ya Bariadi pia itapewa watumishi hao, ahsante.
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa fursa hii. Naomba kuuliza swali la nyongeza: -

Mheshimiwa Spika, je, ni lini barabara ya kutoka Itilima kwenda Meatu itajengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja Mheshimiwa Sabu, Mbunge wa Viti Maalum, Simiyu, ipo kwenye mpango na ndio maana sasa hivi tunachofanya ni kufanya review ya usanifu, ili Serikali iweze kujua gharama yake kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami.
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Spika, ahsante; je, ni lini barabara ya Bariadi – Ngulyati kwenda Magu itajengwa kwa kiwango cha lami kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sabu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, pia hii barabara ni kati ya barabara ambazo zimeongelewa sana. Namwomba Mheshimiwa Mbunge tusubiri, tutakapoleta bajeti yetu watupitishie, na ninaamini itakuwa ni moja ya barabara ambazo zitakuwepo kwenye mpango, ahsante.
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.

Je, Serikali imejipangaje katika kupunguza gharama za huduma hii ya dialyisis, kwani kwa sasa ni shilingi 200,000 hadi shilingi 350,000 kwa mgonjwa anapoenda kuhudumiwa kwa mara moja?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kutokana na majibu ya Serikali, napenda kufahamu, ni utaratibu upi mgonjwa ambaye ana kipato kidogo afuate ili aweze kupata msamaha wa huduma hii ya usafishaji wa figo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge, lakini niseme, moja ni kwamba kwenye bajeti hii ambayo tunaiwasilisha sasa, mpaka jana tulikuwa tunakaa kuangalia maeneo mawili. Waziri wetu ameangalia kwenye eneo la mama na mtoto na eneo hili, na tumegundua kuna uwezekano badala ya tiba hii kuwa shilingi 350,000, inawezekana kabisa mtu akatibiwa kwa shilingi 90,000 hadi shilingi 150,000. Kwa hiyo, tuna mpango huo wa kushusha gharama hizi.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni kwamba, mtu afuate utaratibu gani? Moja, akishakuwa na barua ya Mtendaji wake wa Kata, hiyo inatosha kumfanya aweze kupewa exemption, ndivyo utaratibu unavyosema.
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa fursa hii, naomba sasa niulize swali dogo la nyongeza.

Kwanza naipongeza Serikali kwa majibu mazuri, kwa kuwa katika mkutano wa vijana Mkoa wa Mwanza na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliahidi kwamba tutaanzisha Benki ya Vijana Wajasiriamali.

Je, ningependa kufahamu ni hatua zipi zimefikiwa katika mchakato wa uanzishwaji wa benki hiyo. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante, awali ya yote naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Lucy pamoja na Wabunge wengine wote kwa kufuata nyanyo za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutaka kujua au kuona hali ya vijana wetu kiuchumi inaimarika.

Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sabu kwamba suala hili lipo katika hatua ya majadiliano katika kikao kazi cha Makatibu Wakuu, litakapokamilika tu hatua iliyopo sasa, basi tutajulishwa ili wananchi wote wajue na hatua nyingine ziweze kuendelea.
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa zoezi hili ni endelevu, je, Serikali imejipangaje sasa kuhakikisha kwamba wanafunzi ambao hawajasajiliwa wanasajiliwa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Pili; kwa kuwa utekelezaji wa zoezi hili si kwa takwa ama kwa mujibu wa sheria. Je, Serikali sasa ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba sheria hii inawekwa kuhakikisha kwamba wanafunzi wote wanasajiliwa katika Bima ya Afya? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri.

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ni nini tutafanya ili kusajili wanafunzi wengi zaidi, kikubwa ni kuendelea kuhamasishana kuwaomba wakuu wa shule na wazazi kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu wote kwa pamoja tuone umuhimu wa watoto wetu kuwa na bima ya afya kwa sababu ugonjwa hauji kwa kusema, ugonjwa unakuja kwa ghafla na vizuri kujipanga wakati wote, hilo ni moja.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu mpango gani, kwa sababu hili suala haliko kisheria, tunafanya nini. Mheshimiwa Mbunge ni kwamba ndiyo maana Serikali ilikuja na Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote ili kulifanya hili jambo liwe sasa la kisheria. Kikubwa ambacho nawomba Watanzania, nawaomba ninyi Wabunge tuendelee kuelewa na kupigana kwa pamoja kuhakikisha Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote unarudi hapa ili tuweze kufanya hili suala la kisheria kwa sababu masuala ya afya ni muhimu na afya ni uchumi wa nchi. (Makofi)
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Spika, ahsante, Mkoa wa Simiyu una jumla ya vitongoji 2,649 lakini vitongoji 1,713 havijafikiwa na umeme; je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika vitongoji hivyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu wa vitongoji vyote 36,101 vya Tanzania Bara ambavyo havina umeme, na tayari mradi umetengenezwa tunaouita kwa kifupi HEP – Hamlet Electrification Project na tunatarajia mwaka wa fedha wa 2024/2025 tutaanza kuutekeleza na utaigharimu Serikali jumla ya kama shilingi trilioni 6.7.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa kuanzia katika mwaka wa fedha unaokuja Mkoa wa Simiyu, lakini kwenye majimbo yote mbalimbali yatapata vitongoji angalau 15 kwa kila jimbo. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Lucy kwa kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Bariadi anakotokea washirikiane ku-identify vile vitongoji 15 vya kuanzia ili kupunguza changamoto, lakini katika ule mwaka mwingine tutaanza sasa kupeleka umeme katika vitongoji vyote ambavyo vinahusika.
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; je, ni vigezo vipi vinatumika kwa ajili ya kibali maalum kutolewa kwa shule za bweni?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Waraka wa Elimu Na. 2 wa mwaka 2023 umetoa maelekezo wamiliki kuwa na kibali kwa ajili ya shule za bweni: -

Je, ni hatua zipi zimechukuliwa kwa shule ambazo zimekiuka agizo hili? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Lucy John Sabu, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyokwisha eleza kwenye majibu ya swali la msingi, kwamba vipo vigezo ambavyo Kamishna wa Elimu anatumia, lakini hivi sasa tunahuisha vigezo hivyo. Na nimesema kuwa Wizara kwa kushirikiana na wadau inakamilisha kuandaa vigezo vitakavyotumiwa na Kamishna wa Elimu katika kutoa vibali hivi maalum. Kwa hiyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, tunaendelea kufanya uhuishaji wa vigezo hivi na mara vitakapokuwa tayari basi Umma utajulishwa juu ya vigezo hivi ili iweze kufwata wakati wa kuomba vibali hivyo maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili, anataka kujua hatua zipi zilizochukuliwa; naomba nimhakikihsie Mheshimiwa Mbunge wale wote ambao walikuwa wanaendesha shule hizi kinyume na utaratibu wameweza kupewa notice, lakini vilevile wadhibiti ubora wetu wameweza kutembelea maeneo hayo na kuweza kujiridhisha juu ya huduma ambazo zinatolewa hapo, na baada ya kuona hali ilivyo basi tutachukua hatua mara moja, nakushukuru sana.