Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon Lucy John Sabu (9 total)

MHE. LUCY J. SABU Aliuliza:-

Je, ni lini ujenzi wa kiwanda cha vifaa tiba vinavyotokana na zao la pamba Mkoani Simiyu utaanza kwa kuwa upembuzi yakinifu ulishafanyika?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy John Sabu, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya viwanda vya dawa hapa nchini ina jumla ya viwanda 17 ambapo viwanda 12 vinatengeneza dawa za binadamu, viwanda viwili vinatengeneza vifaa kinga na viwanda viwili vinatengeneza dawa za mifugo na kimoja vifaa tiba. Viwanda 17 hivyo vinauwezo wa kuzalisha dawa chini ya asilimia 12 tu ya dawa zote zinazohitajika nchini. Hivyo zaidi ya asilimia 88 ya dawa za binadamu zinazotumika zinaagizwa kutoka nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka mkakati na mbinu za makusudi kuwezesha uwekezaji wa viwanda vya dawa vilivyopo na kuongeza ufanisi ili kufikia asilimia 60 ya uzalishaji wa dawa na vifaa tiba hapa nchini ifikapo mwaka 2025. Mikakati na mbinu hizo inahusisha pia kuongeza idadi ya viwanda vya vifaa tiba nchini. Aidha, Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwenye sekta hiyo ili kuvutia wawekezaji wengine katika sekta hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada hizo, kuna umuhimu pia wa kuanzisha Kiwanda cha Vifaa Tiba Simiyu ambapo malighafi ya pamba inayolimwa kwa wingi nchini itatumika. Taratibu zote za kuanzisha kiwanda husika zimekamilika ikiwa ni pamoja na upembuzi yakinifu kama alivyobainisha Mheshimiwa Lucy John Sabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa kiwanda hicho unategemea kuanza mara tu baada ya Serikali kukamilisha utaratibu bora wa kugharamia mradi huo. Nashukuru.
MHE. LUCY J. SABU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka Dirisha Maalum la Vijana kwenye kila Benki za Serikali nchini ili kuwawezesha vijana kupata mitaji na mikopo yenye riba nafuu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy John Sabu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania inatekeleza sera na mikakati mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha kuwa riba za mikopo zinashuka ili kuwezesha makundi yote likiwemo kundi la vijana yanapata mikopo yenye riba nafuu na kuweza kushiriki vyema katika shughuli za kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Benki za Serikali zinatoa huduma za mikopo kwa makundi yote likiwemo kundi la vijana kwa kuzingatia taratibu za utoaji mikopo za mabenki ambapo kwa wale wenye vigezo hupatiwa mikopo bila usumbufu wowote.

Mheshimiwa Spika, aidha, kwa kutambua umuhimu wa kundi la vijana katika suala zima la upatikanaji wa mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kuwawezesha kufanya shughuli za kiuchumi, Serikali ilianzisha programu maalum ya utoaji mikopo ya uwezeshaji yenye riba nafuu kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2019 ambapo halmashauri zote zinatakiwa kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya kutoa mikopo kwa makundi hayo. Vijana wengi nchini wameendelea kunufaika na mikopo hiyo hadi sasa.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha vijana wote wanaokidhi vigezo na masharti ya kupata mikopo wanapatiwa mikopo ili kuendesha shughuli zao na hatimaye waweze kuwa na mchango kwenye ukuaji wa uchumi na pato la Taifa letu. Ahsante.
MHE. LUCY J. SABU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka CCTV camera na alarm systems katika masoko, shule na sehemu za wazi zenye mkusanyiko?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy John Sabu, Mbunge wa Viti Maalumu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ili kudhibiti majanga mbalimbali katika taasisi, Serikali imekwishachukua hatua mbalimbali ambapo kupitia Mpango wa Uendelezaji Miji ya Kimkakati Tanzania na Mpango wa Uboreshaji wa Miji jumla ya miji 26 iliyotekeleza miradi ya kimkakati ya ujenzi wa masoko, stendi, na bustani za kupumzikia zimefungiwa vifaa vya utambuzi ikiwemo CCTV camera na alarm system. Aidha, ukarabati wa shule 89 kongwe na chakavu uliofanyika umezingatia miundombinu ya kujikinga na majanga hususani majanga ya moto.

Mheshimiwa Spika, Serikali imekwishatoa maelekezo katika Mikoa yote nchini kuzingatia ufungaji wa vifaa vya kutambua na kudhibiti majanga mbalimbali katika taasisi. Ahsante sana.
MHE. LUCY J. SABU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza magari RUWASA – Simiyu ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy Sabu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuijengea uwezo RUWASA, Mkoa wa Simiyu ili iweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu. Katika mwaka wa fedha 2021/2022, jumla ya magari 37 yalinunuliwa ambapo gari moja lilikabidhiwa RUWASA, Mkoa wa Simiyu na gari nyingine ilipelekwa Wilaya ya Itilima.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika jitihada za kuendelea kuboresha mazingira ya kazi ya RUWASA nchini, Serikali itanunua jumla ya magari ya 86 kwa ajili ya RUWASA na magari hayo yatapelekwa kwenye wilaya mbalimbali nchini ikiwemo Mkoa wa Simiyu.
MHE. LUCY J. SABU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza vifo vya akina mama wajawazito?
WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, niruhusu kwa kuwa leo ni siku ya Wauguzi Duniani, nitumie Bunge lako Tukufu kuwashukuru wauguzi wote nchini Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaifanya katika kuwahudumia wagonjwa. Tunafahamu kwamba asilimia 80 ya huduma katika hospitali zinafanywa na wauguzi, na tunatambua kwamba wana mzigo mkubwa. Tutaendelea kuajiri watumishi wauguzi wengi tutaendelea kuboresha mazingira ya kufanya kazi kwa wauguzi wote Tanzania. Tunawaomba watimize wajibu wao kwa kuzingatia viapo vyao ambao ni kuokoa maisha.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy John Sabu, Mbunge wa Viti Maalum, Vijana, Mkoa wa Simiyu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatoa elimu kwa Umma hususan kwa akina mama wajawazito kuhusu viashiria vya hatari kupitia njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari na wakati wa mahudhurio ya kliniki. Aidha, Serikali inasomesha wataalam mbalimbali wa afya ya uzazi katika ngazi ya ubingwa na inaendelea kuimarisha miundombinu katika vituo vya kutolea huduma za afya na kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaatiba pamoja na kuhakikisha huduma za mama wajawazito zinatolewa bure.
MHE. LUCY J. SABU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya ukarabati wa miundombinu ya Hospitali ya Mji wa Bariadi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy John Sabu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ukarabati wa hospitali kongwe nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga fedha shilingi bilioni 17.1 kwa ajili ya ukarabati wa hospitali 19, ikwemo Hospitali ya Mji wa Bariadi. Aidha, hadi kufikia mwezi Februari, 2023 kiasi cha shilingi bilioni 12.95 zimekwishatolewa kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya hospitali kongwe 14 ambapo hospitali ya Mji wa Bariadi imepelekewa shilingi milioni 900 na kazi za ujenzi zinaendelea, ahsante.
MHE. LUCY J. SABU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha huduma za dialysis kwa Wagonjwa wenye kipato cha chini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy John Sabu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoa huduma za matibabu ikiwemo huduma ya kusafisha figo (dialysis) kwa wagonjwa wote bila kujali kipato cha mgonjwa husika. Huduma hizi kwa sasa zinatolewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali za Rufaa za Kanda, Mikoa na Hospitali Maalum, ikiwemo Hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa wito kwa wananchi wenye kipato kidogo kufuata taratibu zinazopelekea wao kupata misamaha ya huduma ikiwemo huduma hii ya usafishaji wa figo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. LUCY J. SABU aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanzisha Benki ya Vijana Wajasiriamali?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy John Sabu, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa uwezeshaji vijana kiuchumi, Serikali ipo katika hatua ya kuandaa mkakati wa upatikanaji wa mitaji kwa wajasiriamali wadogo na wa kati, ambao utawezesha vijana kupata mitaji kupitia benki, taasisi za huduma ndogo za fedha, masoko ya mitaji, mifuko na programu za Serikali za uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, katika hatua ya utekelezaji wa mkakati huu, Serikali inatarajia kuanzisha taasisi mahsusi ya fedha itakayosimamia upatikanaji na utoaji wa mikopo kwa makundi maalum wakiwemo vijana, wanawake, watu wenye ulemavu na wafanyabiashara wadogo wadogo wakiwemo wamachinga. Ahsante.
MHE. LUCY J. SABU aliuliza:-

Je, kuna mpango gani wa kuwasajili wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo vya kati kwenye utaratibu wa Bima ya NHIF?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lucy John Sabu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya imeanzisha mpango wa bima ya afya kwa wanafunzi wa ngazi zote kwa kuchangia shilingi 50,400 kwa mwaka ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma za matibabu wakiwa masomoni, likizo na wakati wa mafunzo kwa vitendo.

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Machi, 2023 mfuko umeshasajili jumla ya wanafunzi 342,933 ikiwemo wa Shule za Msingi, Sekondari, Vyuo vya Kati na Vyuo Vikuu. Zoezi hili la kusajili wanafunzi ni endelevu kupitia shule na vyuo.