Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon Lucy John Sabu (3 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuunga hoja iliyoko mezani. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kunijalia kibali kuwa mahali hapa. Lakini nikishukuru Chama changu Cha Mapinduzi kwa kuniamini hususani Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kiupekee sana Baraza la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Simiyu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hotuba ya Rais imeeleza mambo mengi ambayo yametoa dira na vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imewapa Tanzania matumaini makubwa hususan kwenye sekta mbalimbali za kiuchumi. Mambo haya yote yatafanikiwa endapo sisi tulioaminiwa kuwa wawakilishi wa wananchi wenzetu tutafanya kazi kwa bidii katika kumsaidia Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nijikite zaidi katika hotuba ya Mheshimiwa Rais hususan kwenye suala zima la mikopo itolewayo na Halmashauri zetu. Mikopo hii lengo la Serikali kuwaweza vijana lilikuwa ni nzuri zaidi endapo kama tutaendelea kuwajengea vijana uwezo hususan kwa kutoa elimu ya kutosha, lakini na mafunzo ya ujasiriamali. Kwa sababu kitu kinachotokea vijana wanapounda makundi wanakuwa hawana uzoefu na elimu ya kutosha hususan kwenye ujasiriamali wanakuwa hawana. Hivyo basi kama ambavyo tulivyo na miradi ya maendeleo ya kimkakati basi tulibebe na hili liwe ni fursa ya kimkakati hususan katika kuwaajiri vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ningependa kuishauri Serikali hususan kwenye hii mikopo isiwe ni sehemu muafaka sasa tuunde benki kwa ajili ya vijana ambapo hela zote ambazo zinatoka kwenye halmashauri ziingie kwenye ile benki ambayo tutaifungua lakini pia na mifuko hii ya uwezeshaji mifuko 18 ambayo ipo kwenye Ofisi ya Waziri iingie kwenye benki ambayo tutaianzisha. Nina imani kupitia kuanzisha benki hii itaweza kutoa mikopo kwa mtu mmoja tofauti na ambavyo inatolewa mikopo kwa vikundi. Kwa sababu kwenye vikundi kila mtu ana idea zake tofauti tofauti, unajikuta vijana hao wanashindwa kurudisha marejesho ya pesa wanazopewa Halmashauri zetu. Mwisho wa siku tunakuwa tunapoteza fedha ambazo zinakuwa ni changamoto kwenye Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano na ya Sita kwa kazi nzuri katika Mpango wa Pili wa kuimarisha uchumi wa viwanda ambapo viwanda vingi vimejengwa kati ya mwaka 2015 - 2020 vikiwemo viwanda vidogo, vya kati na vikubwa. Tuna imani kwa dhamira ya Rais wetu wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kazi iendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani kubwa ataendelea kuweka mkazo mkubwa kwenye ujenzi wa viwanda hasa viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini Tanzania. Tunaunga mkono viwanda kwa sababu vinasaidia kuongeza thamani ya mazao yanayopatikana hapa nchini mfano; pamba, alizeti, katani na kadhalika, lakini pia kuboresha bei ya mazao kwa wakulima, kwani inaondoa gharama za usafirishaji kwenda nje ya nchi ambapo fedha inakwenda kumlipa mkulima, lakini pia ajira za wananchi za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo nina mambo machache ya kuishauri Serikali, Simiyu ni mkoa unaoongoza kwa kilimo cha pamba, kutokana na ubunifu wa viongozi wa Simiyu, wakiongozwa na Mheshimiwa Anthony Mtaka na wasaidizi wake waliweza kubuni na kuishawishi Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, NHIF, WCF pamoja na Benki ya Uwezeshaji (TIB), TBS, TIRDO, TMDA kuanzishwa kwa kiwanda cha vifaatiba vitokanavyo na pamba; zaidi ya bidhaa 19 vikiwemo taulo za kike. Mkoa na Wilaya ya Bariadi ilitoa eneo lililoko kwenye maeneo yanayofikika na miundombinu ya maji, umeme, mawasiliano na barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara iliunda kampuni na Bodi ya Wakurugenzi, Serikali iliteua wataalamu waanzilishi wa kiwanda hicho na Serikali iligharamia safari za wataalamu kwenda nje kujifunza teknolojia stahiki kwa ajili ya kiwanda hicho na upembuzi yakinifu ulishafanyika, na gharama zote zilizokwisha kutumika ni shilingi milioni 915.98. Michakato yote ilianza toka mwaka 2016/2017 mpaka sasa hamna kinachoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa mkoa wa Simiyu tungependa kufahamu maelezo ya kina kwa nini kiwanda hicho na ujenzi wake haujaanza?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. LUCY J. SABU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hoja iliyopo mezani. Nami nitajikita katika uwezeshaji wa wananchi kiuchumi hususan katika ujuzi kwa vijana na ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa juhudi mbalimbali ambazo imekuwa ikizifanya hususan kwa vijana kupitia Programu ya Kukuza Ujuzi Kitaifa. Kupitia programu hii, nafahamu kwamba Serikali imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kukuza ujuzi kwa vijana na ili waweze kujiajiri na kuajiriwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nikiri kuwa mnufaika wa vijana hawa ambao wamekuwa wakipatiwa ujuzi kupitia vyuo vya VETA hususan kwenye kurasimisha ujuzi lakini pia VETA wamekuwa ni watu ambao wanawasaidia vijana hawa kuwashikiza hususan kwa waajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la vijana hawa kupatiwa ujuzi na kujiajiri ni vitu viwili tofauti. Nikichukulia mfano, tulipokuwa na ziara ya Kamati tulitembelea TIRDO (Tanzania Industrial Research and Development Organization) ambapo tulikutana na vijana ambao wana ujuzi ama ubunifu wameweza kutengeneza taa ambapo zina uwezo hata kama ukiwa nje ya nyumba yako, wame-install program kwenye simu ukai-request kwamba zima ama washa taa hata kama ukiwa nje ya nchi. Changamoto inakuja kumekuwa na vijana wengi ambao wana ujuzi wa aina mbalimbali lakini wanashindwa kujiajiri kwa kukosa mtaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi napenda kuiomba Serikali yangu na kuishauri kwa kuwa tuna Programu ya Kukuza Ujuzi kwa Vijana ije na utaratibu wa kutengeneza fursa za kimkakati. Kwa mfano, tunao vijana ambao wana ujuzi wa ufundi seremala na kuna baadhi ya maeneo ambayo yana upungufu wa madawati, Serikali inaweza ikatengeneza fursa kwa vijana hawa wenye ufundi wa useremala kwa kutengeneza kambi rasmi na kuweza kuchukua vijana hawa kuwapa tender ya kutengeneza madawati kwa kuwapa materials na vitendea kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu Serikali imekuwa ikitoa mikopo kwa ajili ya vijana hususan kwenye Halmashauri zetu. Tunaishukuru Serikali yetu Sikivu, kipindi cha nyuma tulipiga kelele sana Waheshimiwa Wabunge, kwa sababu makundi yalikuwa yakiundwa na watu kumi kumi lakini tarehe 26 Februari, kupitia Ofisi ya Wizara ya TAMISEMI ililegeza masharti ya mikopo na kuboresha zaidi kutoa nafasi kwamba hata wakiwa vijana watano wana uwezo wa kukopa mkopo huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini matamanio ya vijana wenzetu ni kuwa mkopo huu uwe ni wa mtu mmoja mmoja. Kama Serikali imeweza kutoa mikopo kwa mtu mmoja mmoja hususan kwenye mikopo ya vyuo vikuu, naomba na hili Serikali ilifanyie kazi. Hii ni kwa sababu mikopo ya watu kwenye makundi inakuwa ina mambo mengi, kila mtu anakuwa ana interest zake kwenye ideas ambayo wanafanya kwenye biashara husika. Niiombe sana Serikali yetu sikivu iweze kutusaidia kwenye jambo hili ili liweze kuwa la manufaa zaidi kwa vijana wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo yote, niiombe Serikali yetu iendelee kutoa elimu kwa vijana wote ambao wanachukua mikopo kwenye Halmashauri. Nasema hivi kwa sababu vijana wanakuwa na interest tofauti tofauti, hivyo, mkopo unavyochukuliwa bila elimu ya kutosha matumizi yanakuwa tofauti na marejesho yanashindwa kufikiwa kwa wakati muafaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja iliyopo mezani. Ahsante sana. (Makofi)