Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon Haji Makame Mlenge (7 total)

MHE. HAJI MAKAME MLENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali ambayo yametolewa, lakini bado nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; kwa sababu ni muda mrefu sasa toka marehemu alipofariki na hadi leo hajapata na alikuwa ni mtendaji wa Jeshi la Polisi. Je, ni lini sasa Serikali itawapatia mafao yao hawa wahusika?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; naamini changamoto hii haiko kwa hawa tu, iko kwa watu wengi. Sasa je, Serikali inawaahidi nini wananchi wa Tanzania ambao wana matatizo kama haya juu ya kutatua tatizo hili? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, sasa naomba nijibu swali la Mheshimiwa Haji Makame Mlenge, Mbunge wa Jimbo la Chwaka, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, je ni lini warithi wa marehemu watapata urithi wao. Baada ya kukaa na kupekua, kwanza tumegundua kwamba kweli marehemu alikuwa ni mtumishi wa Jeshi la Polisi, lakini changamoto kubwa ambayo tulifika tukakutana nayo, tulifika wakati tukakosa kujua ni nani anayesimamia mirathi ya marehemu. Sasa hii kwa kweli kwetu ikaja ikawa ni changamoto. Kwa kuwa tayari msimamizi wa mirathi hii tumeshampata, kikubwa tumwahidi tu Mheshimiwa Mbunge, tutashirikiana tuhakikishe kwamba mirathi au mafao haya yanapatikana kwa wale ambao wanasimamia mirathi hii.

Mheshimiwa Spika, kikubwa nimwambie binafsi niko tayari kwenda kukutana na huyo msimamizi wa mirathi na wengine wanaohusika na mirathi hii ili tuone namna ambavyo tunahakikisha watu hawa wanapata mafao yao au mirathi yao kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, lakini je ni nini sasa kauli ya Serikali katika suala hili au tuna mpango gani? Kikubwa ambacho nataka nimwambie Mheshimiwa cha mwanzo linapojitokeza jambo kama hili kwa wananchi wengine basi cha kwanza kabisa wateue au wafanye uchaguzi wa kuteua msimamizi wa mirathi, kwa sababu sisi la mwanzo tukutane na msimamizi. Yeye ndiye atakayesimamia na kutupa taarifa zote zinazohusika.

La pili, tuhakikishe kwamba wanawasilisha vielelezo kwa sababu hatutaweza kujua nini shida yake kama hakuna vielelezo vilivyowasilishwa vikiwemo vya taarifa ya kifo, vikiwemo labda kituo ambacho alikuwa akifanyia kazi, mkoa na kadhalika. Hivyo ni vitu ambavyo vitatusaidia sisi katika kuhakikisha kwamba anapata mirathi yake kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, kingine wakati wanawasilisha hivyo vielelezo viende kwa watu husika. Wengine huwa wanawapa tu kwa sababu jirani yake ni askari atampa nipekee. Sasa pengine sio mhusika, matokeo yake sasa lawama zinakuja kwenye Serikali, Wizara au kwa Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Spika, kikubwa ambacho nataka niseme, ufuatiliaji wa mara kwa mara, kwa sababu na sisi tutakuwa tunalifuatilia lakini na wao sasa wawe wanalifuatilia kuhakikisha kwamba hii mirathi inapatikana kwa wakati. Nakushukuru.
MHE. HAJI MAKAME MLENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Naomba kuuliza swali moja tu la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Jimbo la Chwaka lina kituo kingine kidogo cha Polisi kilichopo Jozani: Je, Serikali haioni kwamba kuna sababu ya kukipelekea usafiri angalau wa ma-ring mawili? Ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Haji Makame Mlenge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tunayo changamoto kubwa sana katika vituo vingi vya Polisi, shida kubwa ikiwa usafiri. Yapo maeneo hata ya wilaya nzima kabisa ikiwemo Wilaya ya Kongwa, gari pale ni mbovu na iko moja.

Mheshimiwa Spika, Zanzibar kule vituo hivi viko karibu karibu sana. Katika kugawa magari haya tutaangalia sana hata ukubwa wa jiografia, tutaangalia pia maeneo yenye changamoto kubwa zaidi hasa ya mipakani. Vile vile niseme tu, kwa maeneo ambayo vituo viko karibu karibu, huduma ile wanaweza kuipata katika wilaya, kwa sababu setup yetu katika vituo vya Polisi, bado ni ya kiwilaya zaidi, siyo vituo vile vidogo vidogo. Kwa hiyo, niseme tu tutakwenda kuangalia tuone umbali kati ya kituo hiki anachokisema na kituo cha wilaya halafu tuone kama hilo analolisema litawezekana. Ahsante sana.
MHE. HAJI MAKAME MLENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali hata hivyo na maswali mawili ya nyongeza.

Je, Wizara yako inayo mpango wowote wa kutengeneza bustani kando kando ya barabara hasa maeneo ya Mjini?

Swali la Pili, kwa kuwa mazingira ni muhimu. Je, Wizara yako inashirikiana vipi na Wizara ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira katika kuratibu mazingira, hasa bustani katika maeneo ya pembeni ya barabara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Makame Mlenge Haji, Mbungwe wa Chwaka, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria na Kanuni zimetoa maelekezo kwa watu wote ambao wanataka kutumia hifadhi ya barabara bila kuathiri matumizi wafike kwenye mamlaka husika ili waweze kuendeleza na kupendezesha Miji. Suala hili linafanyika kwa barabara za TANROADS, vilevile barabara za TARURA kwa maana ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu kushirikiana na hifadhi ya mazingira ni kwamba taratibu na sheria inayoongoza iko chini ya Wizara ya Ujenzi. Kwa hiyo, tunahakikisha kwamba tukishampa mtu kazi, kwa maana ya kumpa kibali, basi anafanya kazi kulingana na miongozo na taratibu ambazo zimewekwa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni ambayo inalinda kutumia hifadhi ya barabara. Ahsante.
MHE. HAJI MAKAME MLENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuweza kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini pia naomba kuuliza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa baadhi ya viwanda au baadhi ya wadau mbalimbali hutengeneza bustani nzuri tu kandokando ya barabara, lakini hulipishwa fedha nyingi na Wizara yako.

Je, huoni sasa ni muda muafaka wa kuondoa tozo hizo ili wadau hao waendelee kutengeneza bustani nzuri hasa katika maeneo ya majiji yetu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Wizara yako ina mkakati gani wa kuwatia moyo wale wote wanaotengeneza bustani nzuri kando kando ya majiji badala ya kuwalipisha fedha nyingi pale wanapofanya hivyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Haji Makame Mlenge, Mbunge wa Chwaka kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tuna kitu kinachoitwa road maintenance manual ambacho ni kama mwongozo wa watu wote ambao wanaomba kutumia hifadhi ya barabara na kule ndiyo tumetaja gharama ya kila shughuli ambayo mtu anaifanya ikiwepo ni pamoja na kuweka bustani kando kando ya barabara.

Kwa hiyo, tuna mwongozo ambao upo, lakini kama bei ni kubwa, tutalichukua na kuliangalia kama limekuwa ni changamoto kwa watu ambao wanatumia eneo la kandokando ya barabara kwa ajili ya kutunza mazingira na kupendezesha mji.

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la pili kama alivyosema, sisi tuko tayari kukaa na hao watu ili tuwatie moyo na bado nafasi huwa zinatangazwa, yaani kwamba barabara ikishajengwa unaruhusiwa kwenda kuomba na kupewa kibali cha kuweka shughuli ambazo siyo za kudumu kandokando ya barabara ikiwa ni kutunza mazingira na kupendezesha miji, na kwa miji tunashirikiana sisi na wenzetu wa TAMISEMI ambao wana barabara nyingi katika miji, majiji na manispaa, ahsante.
MHE. HAJI MAKAME MLENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mbali na majibu mazuri ya Serikali naomba niulize masuala mawili ya nyongeza. Kwa kuwa watoa hati ni wanadamu na wanadamu wana kawaida ya wakati mwingine kukosea. Inapotokea kukosea wakati wa kutoa hati (printing error) na wakati huo wale wapewa hati wanakuwa wameshalipa. Kwa nini idara inawalipisha tena watu wale wakati wao Uhamiaji ndiyo wamekosea?

Mheshimiwa Spika, swali la pili Je, Serikali ipo tayari kutoa tamko kupitia Waziri la kwamba suala hili wapewa hati hawatalazimika kulipishwa mara ya pili badala yake gharama hizi wachukue Idara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Haji Makame Mlenge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna wakati makosa hufanyika lakini makosa yakichunguzwa yakionekana aliyechangia kufanya makosa haya ni yule mwombaji kwa sababu ya taarifa alizojaza basi mwombaji huyo lazima atalipa. Lakini ikiwa itathibitika kwamba makosa hayo yanatokana na waandaaji ambao ni watumishi wa Idara ya Uhamiaji basi tutaangalia uzito wake ili waweze kufidia wenyewe utoaji wa hati hizo mpya. Nashukuru.
MHE. HAJI MAKAME MLENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mbali na majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa benki hii haikufilisika bali ilifilisiwa na inasemekana walikuwa na fedha za kulipa waathirika wa benki hii. Je, Serikali inajua maumivu wanayoyapata waathirika wa benki hii?

Swali la pili, kwa kuwa Serikali ndiyo dhamana wa mabenki yote Tanzania na Watanzania wengi wameathirika na benki hii. Je, haioni haja hivi sasa Serikali ikachukua jukumu la kuwalipa Watanzania wlioathirika katika benki hii na wao wakasubiri jibu la Mahakama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Haji Mlenge kwa namna anavyofuatilia kwa karibu sana suala hili la benki ya FBME. Naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inajua kadhia hii na ndiyo maana Serikali inafuatilia kwa karibu sana siku hadi siku, mpaka kutoa wataalam wetu hapa kwenda kusimamia kesi hiyo kule Cyprus.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, naomba Mheshimiwa Mlenge uwe na subira mara tu maamuzi ya Mahakama yatakapotolewa na taratibu kukamilika nakuhakikishia kwamba Serikali itawalipa wateja hao bila pingamizi yoyote.
MHE. HAJI MAKAME MLENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza niipongeze Serikali kwa kufikia hatua hii ya kusema Mei, mwezi huu watalipwa warithi wa Marehemu Makame Haji Kheir aliyefariki toka mwaka 2003 lakini kwa sababu ni muda sasa na mwezi Mei ukiisha hajalipwa, ikifika mwezi Agosti nitauliza tena swali hili ndani ya Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la msingi, kwa kuwa tatizo hili naamini kwamba liko kwa wingi sana Nchini Tanzania. Je, Serikali ina mkakati gani au inawaambia nini Watanzania wenye tatizo kama hili la mirathi ambao hawajalipwa mpaka leo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu ambayo tumempa Mheshimiwa Mlenge ndio majibu ambayo tunakwenda kuyafanyia kazi. Kwa maana ya kwamba huu mwezi Mei huyu mtu ambaye anadai mafao yake kupitia warithi, atapata mafao yake kwa sababu kila kitu kipo na vielelezo vimekamilika na fedha zimeshatengwa na zipo tayari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna changamoto pamoja na kwamba tunachowaambia Watanzania kwamba madai yote na hiki tunataka tuwaambie, itakapofika Oktoba mwaka huu tutahakikisha kwamba warithi wote wameshapatiwa mafao yao ili lengo na madhumuni sasa changamoto hizi zisiendelee kujitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyojitokeza na ndiyo maana tunachukua muda mrefu halafu wananchi wanailaumu Serikali ni kwa sababu ya kuchelewa kuleta vielelezo vitakavyotupa sisi uhalali wa kuweza kuwapatia wananchi ile stahiki. Kwa hiyo niwaombe tu wananchi kwamba likishatokea hili walete vielelezo haraka iwezekanavyo ili na sisi tuweze kuwafanyia haraka waweze kupata haki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.