Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Miraji Jumanne Mtaturu (3 total)

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nianze kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kunijalia kuingia kwenye Bunge lako Tukufu na kuweza kuwawakilisha ipasavyo Wananchi wa Jimbo la Singida Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Ikungi pamoja na Jimbo la Singida Mashariki ni kama ambavyo swali la msingi lilivyouliza lina matatizo yanayofanana na jimbo lililoulizwa katika swali la msingi. Pamoja na matatizo hayo zimefanyika jitihada, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya kipenzi chetu Dkt. John Pombe Magufuli, wameshatuletea takribani bilioni 1 na milioni 500 kuchimba visima virefu 28.

Mheshimiwa Spika, sasa nimekuja hapa kuomba kwa kupitia Waziri, wako tayari, tumeshafanya tathmini ya kutosha tuweze kupata, maana kuchimba maji na kuyapata ni jambo moja na kutoka maji ni jambo la pili. Kwa hiyo, ninaomba Mheshimiwa Waziri anihakikishie kwamba, kupitia tathmini iliyofanyika na iko Wizarani tunahitaji jumla ya bilioni 2 ili tuweze kutengeneza miundombinu ya maji Wananchi wa Singida wapate maji. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, kwanza namfahamu vizuri alikuwa Mkuu wa Wilaya, lakini nataka niwahakikishie wana-Singida Mashariki hili ni jembe wembe walitumie vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, katika kuhakikisha kwamba, tunatatua tatizo hili la maji tumeshafanya jitihada za uchimbaji. Nimuombe baada ya Bunge Saa saba tukutane tupange mikakati ya kwenda kutatua tatizo la maji kwa haraka kabisa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wilaya ya Ikungi ni Wilaya iliyoanzishwa mwaka 2013; na hivi tunavyoongea, ofisi au OCD anakaa kwenye majengo ambayo yalikuwa ni maghala ya mkoloni. Kwa sababu ulishaanzwa ujenzi wa kujenga jengo la OCD kwa maana ya wilaya, ni lini sasa Serikali itamaliza, kwa sababu limesimama muda mrefu, miaka mitatu iliyopita?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mimi na Mheshimiwa Mtaturu tulishazungumza pembeni kwamba niende Jimboni kwake, nimhakikishie kwamba moja katika mambo ambayo tutafanya ni kwenda kukitembelea kituo hiki kwa pamoja halafu tushauriane juu ya utaratibu muafaka wa kukimaliza kituo hiki kwa haraka.
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona.

Matatizo ambayo ameyaeleza Mheshimiwa Kiula yamefanana na Wilaya ya Ikungi ambayo ndiyo Jimbo la Singida Mashariki lilipo. Wakati nauliza swali hili naomba niwahakikishie wananchi wa Jimbo la Singida Mashariki, niko imara kuwawakilisha katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilitaka niseme tu, kwa kuwa barabara au miundombinu ya barabra ndiyo inayosaidia kukuza uchumi wa wananchi; na kwa kuwa barabara ya Njiapanda – Makiungu – Kwamtoro mpaka kule Handeni ni barabara ambayo imekuwa ikifanyiwa upembuzi muda mrefu: Ni lini sasa Serikali itaanza kuijenga na kuweza kusaidia kukuza uchumi wa wananchi wa Wilaya ya Ikungi na Mkoa wa Singida? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mtaturu na nimhakikishie tu kwamba tutampa ushirikiano wa hali ya juu katika kutekeleza majukumu yake ya kibunge katika eneo lake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba, barabara anayoitaja Mheshimiwa Mbunge kutoka Njiapanda kupitia Makiungu kwenda kwa Mtoro, itatoka Chemba kwenda mpaka Handeni, kilometa 461; ni kweli kwamba usanifu umeshakamilika na kwa kadri tutakavyopata fedha tutaanza kujenga barabara hii. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi kwamba mradi huu mkubwa wa Kilometa 461 utawanufaisha sana wananchi wa eneo lake na kwa kweli tumejipanga kama Serikali kuona kwamba tunawahudumia vizuri wananchi katika eneo lake.nnAhsante. (Makofi)