Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Miraji Jumanne Mtaturu (2 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika hoja ambayo iko mezani. Kwa sababu leo itakuwa ni siku ya kwanza kuchangia naomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi na uhai wa kuweza kuchangia hoja hii ambapo naishauri Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake ya Wizara nzima, Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu na watendaji wote kwa kuandaa na kutuletea Mpango huu ambao kwa kweli ni Mpango ambao umeendelea kutuonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuwaletea Watanzania maendeleo. Naomba nichukue nafasi hii kuwapongeza na naomba niseme tu kwamba tutaendelea kutoa ushauri ambao utakuwa na tija kwa ajili ya kuleta maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba Mpango wenyewe huu unakwenda kumalizia katika Mpango wa Miaka Mitano ninajua mambo mengi yako dhahiri ambayo yameonekana yameshafanyika. Zaidi niseme tu kwamba kuwa na Mpango ni jambo moja lakini kuusimamia na kuutekeleza ni jambo la pili. Kwa hiyo, sisi kwenye hili tunawapongeza kwa sababu tumekuwa na Mpango na sasa tunaona namna ambavyo kwa muda huu unaenda kumalizika mwaka wa tano mafanikio makubwa katika maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kwa kweli kwa dhati kabisa kumpongeza sana Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna ambavyo ameonesha dhamira ya dhati katika kuhakikisha kwamba anawaletea wananchi maendeleo. Najua kwamba utashi wake ndiyo ambao unatupa hata jeuri au inaipa jeuri Serikali kuhakikisha inafanya kazi vizuri kwa sababu tumekuwa tukipata fedha ya kuweza kutekeleza miradi hiyo. Tunaweza tukawa na mipango mizuri sana isipowezeshwa itakuwa ni kazi bure na itakuwa inabaki kwenye vitabu kama ambavyo tumekuwa tukiona baadhi ya maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba maeneo mengi ambayo naweza kuyasema ni yale ambayo nasema kwamba tumeanza kuona dhamira ya Serikali katika kukusanya mapato. Unaweza ukawa na mpango mzuri lakini ukawa hauna fedha lakini ukiwa na mpango mzuri ikiwa ni pamoja na kukusanya mapato inakusaidia wewe kuhakikisha kwamba unatimiza malengo ambayo yako mbele yetu. Jambo kubwa ambalo ni vizuri tukalisema ni dhamira ile ya kusimamia na kuzuia mianya yote ya kukwepa kodi katika nchi yetu. Siyo hivyo tu ni pamoja na kusimamia na kutokomeza kabisa rushwa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika baadhi ya maeneo ambayo tulikuwa tunateseka sana ni pale ambapo baadhi ya watumishi ambao hawana dhamira njema wamekuwa hawafanyi vizuri sana katika kusimamia mapato yetu. Kwenye hili, naomba niipongeze Serikali kwa namna ambavyo imesimamia na imeendelea kuongeza mapato katika nchi yetu yanayonifanya tuweze kutekeleza mipango ambao tunajipangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo yote nieleze sasa yale ambayo yanaonekana waziwazi. Tumeona namna ambavyo tunaboresha sana miundombinu ya barabara ambayo kwa kweli imekuwa ndiyo nguzo kuu ya uchumi wa nchi yetu. Niseme hapa katika mpango nimeona namna ambavyo mwaka huu ambapo tunaelekea kwenye bajeti tutaenda kujikita katika kuongeza fedha ambazo zinakwenda kuongeza uwezo wa kujenga barabara zetu ikiwa ni barabara za lami na madaraja makubwa na kadhalika. Niombe tu kwamba haya ambayo yamepangwa basi yawekwe vizuri kwa ajili ya kutoa fedha ili tuweze kuona miradi hiyo inaweza kufanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, si hivyo tumeona reli ya SGR inajengwa. Ni dhamira ya dhati tuliamua kama Taifa na leo tunavyoona speed ni kubwa sana tuko zaidi ya asilimia 60 ya utekelezaji wa mradi. Kwa hiyo, niseme tu kwamba hii nayo itakuwa ni kichocheo muhimu katika uchumi na usafirishaji wa mizigo ikiwa ni pamoja na kupunguza bei ya bidhaa sokoni. Bei ya bidhaa ikipungua maana yake itamsaidia mwananchi wa kawaida kuweza kupunguza mfumuko wa bei kwa sababu bei itakuwa chini katika usafirishaji wa mizigo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo yote hatutaacha kusema maneno machache kwenye sehemu ya uboreshaji wa ununuzi wa ndege. Hili jambo tusipolisema na dhamira ya dhati ikaonekana maana wengine wamekuwa wakipotosha eti wanathaminisha ndege wanasema vingejengwa vituo vya afya kadhaa. Niseme tu kama Taifa lazima tuamue nini cha kufanya, huwezi kusema unaogopa kununua shati jipya kwa sababu huna utoshelevu wa kubadilisha kula mboga, huwezi kuogopa hilo, lazima uamue kwamba ndege zinazonunuliwa zinaenda kuongeza uwezo wetu wa kuweza kuhudumia sekta ya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tumekuwa tukiona na tukilalamika na mimi nimekuwa nikiwaona Waheshimiwa Wabunge wanasema ndani ya Bunge kwamba haiwezekani watalii washukie Kenya waletwe kwa magari kuja kwenye mbuga zetu na baadaye warudi wakapandie Kenya kwa shirika lingine la ndege. Leo tunapata ndege maana yake tuna uwezo sasa wa watalii wale wote kushuka kwenye viwanja vyetu ndani ya nchi yetu na wanakwenda moja kwa moja kwenye utalii. Utalii ndiyo sekta ambayo inaongoza katika mapato katika nchi yetu. Kwa hiyo, tunapoboresha Shirika la Ndege maana yake moja kwa moja tunaiboresha hii sekta ya utalii ambayo ndiyo inaleta fedha nyingi ambapo mwisho wa siku itajenga vituo vya afya, shule, itaboresha elimu bure pamoja na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Taifa lazima tujivunie kwa sababu lazima nchi isonge mbele kwa kuwekeza kwenye mambo makubwa. Kwa hiyo, hatuwezi kuwa sisi wenyewe tunafanya mambo makubwa lakini hatujui kama tunafanya mambo makubwa. Hii haitatujenga kama Taifa, Watanzania tuipende nchi yetu kwa yale makubwa mazuri tunayoyafanya. Tofauti ya vyama vya siasa isitufanye tuondoke kwenye reli, lazima tujivunie na sasa hivi tunaona ATCL wanafanya vizuri, Mheshimiwa Waziri anayehusika na sekta hii yupo pale kwa kweli kazi inafanyika vizuri na sisi kama Waheshimiwa Wabunge ni lazima tuunge mkono juhudi kubwa hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kueleza maelezo haya, kabla muda wangu haujaisha, nitoe maneno machache ya ushauri kwenye suala la kilimo. Waheshimiwa Wabunge wengi wamesema, lakini naomba na mimi nieleze kidogo, asilimia 80 ya wananchi wetu wanafanya kilimo. Kama kweli tutaweza kuwekeza kwa dhamira ya dhati katika kilimo itasaidia sana kutuongezea pato la Taifa lakini itasaidia uchumi wa mwananchi mdogo kule chini chini, wakati wa kutegemea msimu wa mvua umepitwa na wakati, tuongeze nguvu katika kilimo cha umwagiliaji na zaidi tuongeze uwezo wetu wa kusimamia miradi hiyo na itoe matokeo, katika baadhi ya maeneo tuweze kuvuna zaidi ya mara mbili ili tukipata mapato ya kutosha kwenye eneo hili itasaidia hata mapato ya ndani katika halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halmashauri zetu nyingi zinategemea mazao katika mapato, tukiwekeza kwenye kilimo naamini kabisa tutaenda kuongeza uwezo wa wananchi wetu na kipato chao katika kaya. Kipato cha kaya kikifanikiwa ndiyo tutasaidia kwenda kwenye huo uchumi wa kati ambao tunausema kwa sababu tunaangalia na tunatathimini namna ambavyo mwananchi anajipatia kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiondoka kwenye eneo hilo, niende sasa kwenye eneo la pili la miundombinu. Tunaamini zile barabara kubwa zile trunk roads zinajengwa kwa kiwango cha lami, lakini nieleze kidogo kwenye barabara ambazo ziko chini ya TARURA. TARURA wamekuwa wakitengewa fedha kidogo sana naamini wanataka kujenga madaraja, wanataka kuongeza uwezo wa ujengaji wa barabara zao, lakini fedha wanazopata ni ndogo sana hazina uwezo wa kututoa pale na ile dhamira ya kuanzisha hii agency haitakuwepo kama hatutawapa fedha za kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana kwenye mpango huu naona imeguswa na imewekwa, lakini naona kabisa namna ambavyo mfano kama Wilaya ya Ikungi pale, zipo barabara ndevu lakini nyingi hazijawahi kutengenezwa, ni barabara za asili kama mapalio, naamini kabisa Mheshimiwa Waziri ananielewa ninavyoeeleza hayo, kwa sababu TARURA huwa wanaleta maombi yao na yamekuwa wakipata fedha kidogo sana, wakati ambapo barabara hizi zikijengwa zitasaidia kusogeza mbele suala la kuleta maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikimalizia kwenye eneo la umeme juhudi naziona ni nzuri sana, nipongeze sana Serikali kwa namna ambavyo wizara imeendelea kusimamia upatikanaji wa umeme kwa kupitia miradi ya REA, tatizo kubwa ambalo naliona lipo kwa wakandarasi, wakandarasi wamekuwa hawatekelezi miradi kulingana na mikataba yao, wakandarasi wengine wanalalamikiwa hata na wafanyakazi wao, hivyo inasababisha kufifisha juhudi za kuwapelekea wananchi umeme, kwenye eneo hili ni vizuri Serikali kupitia Wizara husika waweze kusaidia kuhakikisha kwamba wananchi wanapatiwa umeme mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ndogo ambayo ipo pia ni maeneo yale ambayo wanasema kwamba wanapelekewa umeme kwenye vijiji lakini wanapelekewa vijiji ambavyo viko pale pale centre, umeme hauendi mpaka kwenye vitongoji. Inawezekana dhamira ya Serikali ni hiyo, lakini imekuwa tunavuka baadhi ya vitongoji, jambo hili linatuweka kwenye wakati mgumu ambapo tunakosa majibu, wakati hamu ya wananchi ya kupata umeme ni ya hali ya juu. Baada ya maneno haya, naomba tu niendelee kusema CCM hatujakataa kuingia uwanjani, tuko tayari, lakini naomba pia na wao wafuate mwongozo uliowekwa ili waingie uwanjani wakiwa salama. Huwezi kuingia uwanjani huna viatu wakati wenzako wanaingia na viatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hoja katika Kamati hizi mbili ambazo zimewasilisha taarifa zao, nami nipo kwenye Kamati ya Miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumshukuru sana Mungu ambaye ni mwingi wa rehema kutujalia uzima na kuweza kuendelea kufanya majukumu haya kwa ajili ya Watanzania wenzetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nitumie nafasi hii kwanza kumshukuru sana Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ambaye kwa hakika mwelekeo na dhamira yake imekuwa inarahisisha sana utendaji wa Serikali. Hii yote ni kwa sababu wananchi wa Tanzania wamekuwa na imani naye na ndiyo maana basi naye amekuwa akifanya kazi hii kama ambavyo wananchi wanatarajia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapongeza kwa namna ambavyo tumeendelea kupata bajeti kwenye hii Wizara yetu ya Ujenzi kwa maana ya kutekeleza majukumu yaliyopo ndani ya Wizara hii. Kama alivyoeleza Mwenyekiti wetu pale asubuhi, ni kwamba tumepata fedha za kutosha kutekeleza miradi mbalimbali ambapo haya mashirika mbalimbali na taasisi yalileta taarifa zao kwenye Kamati yetu na kuona namna ambavyo Serikali iliendelea kuleta fedha. Najua bado kuna changamoto lakini ninaamini zitatatuliwa kulingana na muda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushahidi pekee ni pamoja na maeneo mbalimbali ikiwemo ununuzi wa ndege, ujenzi wa barabara za lami katika nchi yetu, mawasiliano mbalimbali, kwa maana minara inajengwa na hata juzi tumesaidi mkataba kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunapeleka minara kwenye vijiji vipatavyo 555 nchi nzima. Yote hiyo ni dhamira ya dhati ya Serikali kuhakikisha kwamba inaboresha mawasiliano na huduma mbalimbali zinazotokana na Wizara yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili nitumie nafasi hii kuendelea kumshukuru sana Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Selemani Kakoso pamoja na Makamu wake Mheshimiwa Hawa Mchafu ambao wamekuwa wakiongoza vizuri Kamati hii. Vile vile Wajumbe kwa pamoja tumekuwa tuna ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha kwamba tunahoji mambo ya msingi kwa ajili ya maslahi ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yetu tulipata fursa ya kukutana na taasisi mbalimbali zilizopo chini ya Wizara hii ya Ujenzi, Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Mawaziri wake walituletea wataalam hao na tumeendelea kuhojiana kwenye Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia sekta mbili ambazo nilidhani niweze kuzitolea maelezo ndani ya Bunge lako Tukufu. Nianze na wenzetu wa Wakala wa Huduma za Meli. Kama ambavyo tunajua kwamba sisi kijiografia katika ukanda huu tumekaa vizuri sana katika biashara kwa maana ya bandari na tumekuwa tukifanya hivyo kwa miaka mingi na tumekuwa tukipata faida kubwa ya fedha tunapotoa mizigo hapa kwenda kwenye nchi mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri inayofanywa, changamoto moja kubwa sana ambayo tumeigundua; tumefanikiwa kukutana na wadau wa sekta hiyo ambao ni wasafirishaji mbalimbali wanaoleta mizigo kupitia bandari yetu, wamekuwa na malalamiko mbalimbali ikiwemo ucheleweshaji wa mizigo yao kutolewa kwenye bandari. Hii imesababisha baadhi ya wafanyabiashara kuhamisha mizigo yao na kushushia kwenye bandari nyingine ikiwemo Beira pamoja na pale Mombasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ukilisikiliza kwenye Kamati tumeenda kwa kina sana. Kwa kweli ni jambo ambalo tusipolifanyia kazi, wafanyabiashara wataondoka wengi wataenda kushushia mizigo eneo ambalo siyo hapa kwetu. Hii itakuwa ni athari kubwa kwenye uchumi wetu; na haya ambayo tunampongeza leo Mheshimiwa Rais na Serikali yake hawawezi kufanya bila kuwa na fedha za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la storage limekuwa ni tatizo kubwa lakini pia kumekuwa na urasimu mkubwa sana katika utoaji wa mizigo. Kuna manung‟uniko makubwa kwa wadau. Tunaiomba Serikali ikakae na wadau iwasikilize na watoe ushauri wao namna ya kuenenda. Wao hawana tatizo na ulipaji, wana tatizo na urasimu mkubwa uliopo ndani ya mamlaka hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivi, tutakuwa tunaitendea haki nchi yetu na kwa hakika tutakuwa tuna uwezo wa kuongeza mapato ya kutosha kwa ajili ya kuwa na uhakika wa kutekeleza miradi ya kimaendeleo ambayo tunayo katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wametueleza wenzetu pale kuhusu uchakavu wa bandari nchini. Ni ombi letu kupitia Bunge lako Serikali iende ikaboreshe miundombinu iliyopo kwenye bandari zetu. Najua juhudi zinaendelea, lakini kwa sasa wao wenyewe kama mamlaka walituambia kwamba changamoto kubwa ilikuwa ni uchakavu wa bandari zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ushindani. Chombo hiki kinachosimamia biashara hii ni vizuri ikajua kwamba wenzetu wanafanyaje? Maana leo hii baadhi ya wengine wanaona wanakuwa na comfort kubwa kuwa kwenye bandari nyingine kuliko kwenye bandari yetu ya hapa Dar es Salaam. Tukifanya hivyo, tutakwenda kuongeza nguvu kubwa ya kuvutia wafanyabiashara kushushia mizigo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwenye sekta moja ya ujenzi ambayo ni wenzetu wa TBA. TBA ni wakala, anafanya kazi nzuri. Lengo la kuanzishwa kwake ilikuwa ni kusaidia eneo la ujenzi katika majengo mbalimbali ya Serikali yaliyopo hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumegundua pamoja na juhudi wanazofanya, wenzetu wa TBA wana upungufu mkubwa wa rasilimali watu, hawana wafanyakazi wa kutosha katika kutekeleza miradi yao. Kwa hiyo, ombi letu wahakikishe kwamba wanaongezewa rasilimali watu ili waweze kufanya kazi yao vizuri na lile lengo la kuanzishwa kwao liwe limetimia kwa sababu wanakwenda kufanya kazi ambayo inaenda kusaidia Sekta ya Ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, ni namna ambavyo menejimenti yao, flow ya fedha na vitu kama hivyo nayo imekuwa ni changamoto katika usimamizi. Ombi letu ni kwamba kupitia Kamati tuliishauri na hapa ninaomba niongezee tena kwamba TBA wakiwezeshwa wanaweza kuwa wanafanya kazi nzuri sana na wakaingia kwenye soko la ushindani katika Sekta ya Ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tena kusema kwamba sisi wote ni Watanzania, tuendelee kwa pamoja kuwa kama Taifa moja, tofauti zetu za kimitazamo zisianze kutuingiza kwenye machafuko ambayo hayana sababu. Ninaamini kabisa wote tuna nia njema ya kuwatumikia Watanzania, lakini kila mmoja ana views zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ombi langu ni hilo tu kama ambavyo leo asubuhi tumejadili baadhi ya wenzetu wanapotuchonganisha na Jumuiya za Kimataifa, nadhani inatuweka katika hali ambayo siyo salama sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya, naomba kuunga hoja mkono kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)