Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Timotheo Paul Mnzava (11 total)

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na naishukuru Serikali kwa kazi waliyoifanya. Pamoja na majibu hayo nina maswali madogo mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa barabara hii kwa mara ya kwanza kabisa iliwekwa kwenye Ilani mwaka 2010 na mwaka 2015 na kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hii Serikali haioni iko haja sasa ya kutenga fedha zaidi na kuongeza kasi ya utekelezaji ili tujenge barabara hii isivukwe na muda wa Ilani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wananchi wa Korogwe Vijijini wamekuwa wakisubiri utengenezaji wa barabara hii kwa hamu na kwa muda mrefu, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari baada ya Bunge hili kuongozana nami kwenda Korogwe akaone hali ya barabara hii na kutoa neno la matumaini kwa wananchi wa Jimbo la Korogwe Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Timotheo, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza uniruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Timotheo kwa sababu amekuwa anafuatilia sana mambo mbalimbali kuhusu eneo lake, nampongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maswali yake, kwa ufupi nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kama ilivyo kawaida kwamba Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kufanya maboresho ya barabara katika eneo lake. Kwa hiyo, nimuahidi tu tutaendelea kutenga fedha kadri tunavyopata bajeti ili tuendelee kuboresha barabara katika eneo hili. Niliwahi kutembelea katika eneo hili lakini nakubalia nitakuja kwa sababu zipo changamoto nyingi ili nije kuona pia na maeneo mengine. Ahsante sana.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kazi kubwa inayofanywa na TARURA inapunguzwa faida au kufifishwa faida yake kutokana na ukosefu wa fedha za kujenga madaraja muhimu. Wananchi wa Korogwe wamekuwa wakipata shida ya muda mrefu ya Madaraja yao ya Mbagai, Makondeko na Mswaha. Serikali haioni kwamba iko haja ya kuweka jicho maalum kwenye bajeti inayokuja kwa ajili ya madaraja kwenye barabara ambazo zinatengenezwa na TARURA?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Korogwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge, ni Mbunge mpya lakini anafanya kazi kubwa sana ya kutetea wananchi wake wa Korogwe. Jambo la pili ni kwamba huu mpango mkakati ni wa kudumu na ndiyo maana imeanzishwa TARURA ili wataalam wetu hawa wakilala, wakiamka wafikirie barabara zetu za vijijini na mijini. Kwa hiyo, naomba tu aamini kwamba kazi hii inaendelea kufanyika vizuri na huu ni mwaka wa bajeti na bajeti ya barabara hizi inabidi ianzie katika vikao vyao vya ndani kuanzia kwenye mtaa, kijiji, halmashauri yao na hatimaye hapa Bungeni. Sisi kama Serikali tupo tayari kushirikiana na wananchi wa Korogwe na Mheshimiwa Mbunge wao ili kuhakikisha kazi hii inafanyika vizuri na kuondoa kero zilizopo pale.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kama ilivyo Igalula kumekuwa na changamoto kubwa ya mawasiliano kwenye Jimbo la Korogwe Vijijini hususan kwenye Kata za Kizara, Makumba, Kalalani, Mkalamo, Elewa na Lutindi na Mheshimiwa Naibu Waziri anafahamu changamoto hizi. Ni lini Serikali itatoa utatuzi wa changamoto hizi zinazowakabili watu wa Korogwe Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikiri kwamba nilishatembelea Korogwe Vijijini na hilo eneo alilolitaja Mheshimiwa Mbunge nililiona, ni kweli kwamba kuna mnara wa mawasiliano lakini hauna nguvu ya kutosha. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba nitatuma wataalam kwanza wakaongeze nguvu kwenye hicho kijiji cha kwanza alichokitaja halafu na nitatoa orodha nyingine kesho aangalie vijiji vingine ambavyo tumeviorodhesha kwa ajili ya kuimarisha mawasiliano maeneo hayo.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri alifanya ziara kwenye hili na anazungumza eneo ambalo analifahamu. Pamoja na majibu yake mazuri ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza mradi huu ulibuniwa muda mrefu sana na ni mradi ambao una uwezo wa kuhudumia eneo kwa maana hekta karibu zaidi ya hekta 5000 na tathmini ambayo unasema ilifanyika ya usanifu uliofanyika ulifanyika muda mrefu.

Je, Serikali iko tayari sasa kuharakisha mapitio ya usanifu upya ili kujua gharama halisi kwa mazingira tuliyokuwanayo sasa na kwa namna ya kutekeleza mradi huu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili tunayo Skimu ya Songea na Makalala kule Magoma, lakini pia skimu ya Kwamkumbo pale Mombo ambapo wananchi wamekuwa wakiathirika wakati mvua maji yakiwa mengi yanaenda kwenye mashamba ya wakulima na kuharibu mazao na kusababisha hasara kubwa.

Je, Mheshimiwa Waziri uko tayari, kuwatuma wataalam wa umwagiliaji waende kwenye maeneo haya na kuona namna ya kutatua changamoto hizi za wananchi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anataka kufahamu Serikali kuharakisha mchakato wa kuweza kupitia upya tathmini ya mradii huu. Kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tangu siku zile nilivyofika mimi katika bonde hili na kufika bwawa lile tayari tushawaelekeza viongozi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Kanda ya Kilimanjaro wanalifanyia tathmini upya bwawa lile ili kujua gharama halisi na kuanza utekelezaji kwa mipango ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu athari ya mafuriko katika skimu hizi tatu alizozitaja za Skimu ya Songea na Makalala, kwamba nitumie nafasi hii kwanza kuwaelekeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Kanda ya Kilimanjaro kwenda haraka katika mabwawa haya kufanya tathmini na kuona namna gani tunaweza kujenga miundombinu ile yamatuta kwa ajili ya kukinga mafuriko ya athari ya mabwawa haya.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru halmashauri ya Wilaya ya Korogwe ni miongoni mwa halmashauri ambazo zilielekezwa kuhamisha Makao yake Makuu ya halmashauri kutoka Mjini kwenda kwenye maeneo yake ya utawala, lakini kuna changamoto kubwa sana ya barabara haswa kwa wananchi wa Tarafa ya Bungu barabara ya kutoka Makuyuni Kwemshai na barabara ya Makuyuni, Zege Mpakayi.

Je, Serikali iko tayari sasa kuwa na mkakati maalum wa kusaidia uboreshaji wa miundimbinu ili wananchi hawa waweze kufika kiurahisi kwenye maeneo ya Makao ya halmashauri mpya zilizoanzishwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa kwanza nimpongeze kwa namna anavyohangaika na barabara za eneo lake na nimshukuru alinipa ushirikiano wa hali ya juu nilivyotembelea maeneo haya na maeneo mengine ambayo hakuyataja.

Mheshimiwa Naibu Spika, na niseme tu labda ni kwa kutoa kumbukumbu sahihi kwa mvua ambazo ambazo ziliathiri Mkoa wa Tanga zilikuwa ni kubwa sana kiasi kwamba urejeshaji wa maeneo ambao tumeyafanya hadi sasa tumetumia bilioni 7.8 kurejesha eneo la Tanga peke yake kwa mvua za mwezi Octoba peke yake na nikubaliane na yeye kwamba sasa tumefanya tena kwenye uratibu huu wa mvua zilizonyesha kuanzia Octoba kuja Januari kwa upande wa Tanga pia kumbukumbu kwamba kuna mahitaji makubwa ikiwepo maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge umeyataja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumetambua maeneo yote yenye shida hizi ikiwepo maeneo uliyoyataja na tunafanya utaratibu wa kuwa na fedha tena kama tulivyofanya Awamu ya I ya mvua za mwezi Octoba tutakwenda kufanya kazi kubwa kufanya marejesho ya maeneo haya ambayo nayataja kwa sababu nafahamu eneo la kwako pia ndiyo limekumbwa na maporomoko ya udongo wananchi wamepata athari kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunatambua hivyo na tutakuja kufanya uharaka wa kurejesha maeneo hayo uliyoyataja,ahsante sana.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kabla sijauliza maswali ya nyongeza, niruhusu niendelee kuwapa pole wananchi wa Jimbo langu la Korogwe Vijijini na Mkoa mzima wa Tanga kwa mafuriko makubwa yaliyotupata siku chache zilizopita. Tunaendelea kutumaini juhudi ya Serikali kurejesha miundombinu yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; moja ya sababu ya nchi tunazoshindana nazo kwenye soko la mazao ya viungo na mazao ya bustani kufanya vizuri ni wao kuwa na mamlaka za kusimamia mazao haya. Je, ni lini Serikali yetu itaona umuhimu wa kuanzisha Mamlaka ya Kusimamia Mazao ya Viungo na Mazao ya Biashara?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; wananchi wa Tarafa ya Bungu, Wilaya ya Korogwe, ni wakulima wakubwa na wazuri sana wa mazao ya viungo na zao la chai, lakini tumekuwa na changamoto kubwa sana ya bei kwenye zao la chai. Je, ni upi mkakati mahususi wa Serikali wa kuhakikisha kwamba wanaboresha bei ya zao la chai ili kuweza kuwaletea tija wananchi na wakulima wa zao la chai nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mnzava kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kutumia nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwamba Wizara ya Kilimo inafahamu umuhimu wa kuanzishwa kwa taasisi itakayosimamia mazao ya horticulture na mazao ya viungo. Hivi sasa tunapitia mfumo na muundo wa Wizara kupunguza idadi ya bodi na kuanzisha mamlaka chache ambazo hazitazidi tatu, mojawapo ikiwa ni Mamlaka ya Maendeleo ya Mazao ya Horticulture.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwenyezi Mungu akijaalia hivi karibuni Bunge hili litapokea sheria ambayo itaonesha mabadiliko ya muundo wa taasisi mbalimbali ndani ya Wizara ya Kilimo ili kuipa sekta hii nafasi inayostahili kwa sababu ni subsector ndogo katika Sekta ya Kilimo inayokua kwa kiwango kikubwa sana na inahitaji attention inayostahili. Kwa hiyo nimtoe hofu kwamba tuko katika hatua za awali na kabla ya kufika Bunge lijalo la Bajeti tutakuwa tumeshaanzisha Mamlaka ya Mazao ya Horticulture.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la chai; ni kweli kama Serikali hatua tunazochukua mojawapo sasa hivi tuko katika hatua za mwisho za kuanzisha a primary market katika eneo la Dar es Salaam ili tuwe na mnada wa kwetu hapa Tanzania. Tumesha-earmark eneo na sasa hivi tuko katika hatua za awali kutengeneza utaratibu ili chai yetu badala ya kwenda kuuziwa katika soko la Mombasa sasa ianze kuuziwa katika soko la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tutatumia mfumo wa TMX ili kuwaruhusu wanunuzi duniani waweze ku-bid. Mchakato huu unawahusisha Sekta Binafsi ambao wamewekeza katika chai ili kuhakikisha kwamba zao la chai linapata soko na bei ya uhakika. Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge tunaamini kwamba ndani ya muda mfupi tutaanzisha soko la kwetu ndani ya Tanzania na chai yetu itauziwa hapa na itapunguza gharama na kumpatia mkulima bei nzuri.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni Wilaya ya Korogwe zimeathiri kwa kiasi kikubwa miundombinu ya maji na kusababisha shida ya upatikanaji wa maji.

Je, Mheshimiwa Waziri anasema ni upi mkakati maalum na wa dharura wa Serikali kurekebisha miundombinu hii na kurudisha miundombinu hii na kurudisha huduma ya maji kwa wananchi wa Korogwe Vijijini kama wanavyofanya wenzenu kwenye upande wa barabara?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ni uhai. Namwomba Mheshimiwa Mbunge tukutane leo saa 7.00 ili tujue namna ya kuweza kuwasaidia wananchi wa Korogwe.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, pamoja na majibu ya matumaini ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, moja ya changamoto kubwainayochelewesha kukamilika kwa wakati kwa miradi yah ii ya REA ni tofauti ya size ya transfoma iliyopo kwenye mikataba ya kVA 33 na ukubwa na laini ambazo wanachukulia ule umeme. Jambo hili limesababisha kuchelewa kwa Miradi ya REA ya kukamika kwenye Jimbo la Korogwe Vijijini, kwenye vijiji vya Kulasi na vijiji vya Mswaha Majengo, nguzo zimesimama kwa zaidi ya miezi sita.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali itatoa maelekezo kwa REA kuharakisha utatuzi wa changamoto hizi ili wananchi hawa waweze kupata umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika Jimbo la Korogwe Vijijini zipo kata tano ambazo vijiji vyake vyote katika kata hizo havijafikiwa na huduma ya umeme. Kata za Kizara, Foroforo, Kararani, Mpale na ya Mswaha. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, uko tayari kuwahakikishia wananchi wa kata hizi kuiwapa kipaumbele na kupata umeme kwenye mwaka wa fedha unaoanza Julai mwaka huu?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali la msingi la Mheshimiwa Mnzava, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Mnzava, pampja na kwamba si Mbunge wa muda mrefu, lakini kafanya mambo makubwa sana kwenye jimbo lake hata nilizotembelea. Baada ya kusema hayo basi napenda nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mnzava.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, ni kweli, katika Kijiji cha Kurasi Kibaoni pamoja na Mswaha Majengo, kuna transfoma zilifungwa za kVA 33, lakini tumeshamwelekeza mkandarasi kuanza kushusha kutoka kVA 33, kwenda kVA 11 kuanzia Jumamosi iliyopita. Kwa hiyo, vijiji viwili vya Kulasi pamoja na Mswaha vimeshaanza kupelekewa umeme na vitapata umeme mwisho wa wiki hii. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Mnzava katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kweli zipo kata tano ambazo zilikuwa hazijapata umeme katika Jimbo la Korogwe Vijijini na kati ya kata tano tayari kata moja ya Mswaha- Majengo imeshaanza kupelekewa umeme. Zimebaki kata nne ya Foroforo pamoja na Kirarani ambazo nazo zinaanza kupelekewa umeme kuanzia Julai mwaka huu na kufikia Juni, mwakani nafikiri zitakuwa zimepatiwa umeme. Nimpongeze sana Mheshimiwa Mzava, aendelee kutupa ushirikiano.

Mheshimiwa Naibu Spika, na nilipotembelea tarehe 22 kwa Mheshimiwa Mnzava, Kijiji cha Mkalekwa pamoja na Welei vilipelekewa umeme na nikaagiza Kijiji cha Kulasi nacho kiwashwe umeme. Kimeshawashwa umeme tangu tarehe 28 mwezi uliopita. Kwa hiyo, nashukuru sana Mheshimiwa Mnzava tuendelee kushirikiana. Ahsante sana.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kama ilivyo kwa barabara hii ya Lupiro – Malinyi, barabara ya Korogwe – Dindira – Bumbuli mpaka Soni iliahidiwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, lakini pia kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ilikamilika. Napenda kujua, ni lini sasa kazi ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami itaanza ili kuwasaidia wananchi wa Korogwe na Lushoto kwenye eneo la usafiri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mbunge ambaye ameuliza barabara ya Korogwe hadi Soni ni lini itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wabunge wawe na imani na Serikali hii ya Awamu ya Tano kwani kwanza ni ahadi za viongozi wetu wa kitaifa Mheshimiwa Rais lakini pia zimetajwa katika Ilani. Naomba tuanze bajeti na nina hakika hizi barabara ambazo tunaziulizia zimo, kwa sababu tumeahidi tutatengeneza hizi barabara kwa kiwango cha lami. Nashauri Waheshimiwa Wabunge wawe na imani kwamba barabara hizi zitajengwa ikiwa ni pamoja na barabara ya Korogwe kwenda Soni. Ahsante.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na Serikali kwenye ujenzi wa hospitali na vituo vya afya, kama alivyokiri Mheshimiwa Naibu Waziri, ni kweli bado kuna uchakavu mkubwa wa vituo vyetu vya afya.

Napenda kujua kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, ni upi sasa mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba tunamaliza kabisa ukarabati wa vituo vyote vichakavu na vikongwe vikiwemo Vituo vya Afya vya Mombo, Bungu na Magoma katika Wilaya ya Korogwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mnzava, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Serikali imefanya kazi kubwa sana katika ujenzi wa hospitali, vituo vya afya na zahanati na pia imefanya kazi kubwa sana katika kukarabati vituo vya afya ili kuwezesha kutoa huduma bora kwa wananchi. Ni kweli pia kwamba bado kazi ipo na inahitajika kufanyika zaidi na Serikali inatambua kwamba bado kuna vituo vya afya ambavyo ni chakavu na vinahitaji kukarabatiwa vikiwemo vituo vya afya vilivyopo katika Jimbo la Korogwe Vijijini kwa Mheshimiwa Mnzava.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka huu, Serikali imetenga shilingi bilioni 11 na imeshaainisha hospitali 43 za Halmashauri kwa ajili ya ukarabati na kuongeza majengo ambayo yanapungua ili yaweze kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi. Pia mchakato wa kuandaa na kuainisha vituo vya afya chakavu vikiwemo vya Korogwe Vijijini, unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mnzava kwamba vituo vyake pia vitaingizwa katika orodha hiyo ili kadri ya upatikanaji wa fedha viweze kukarabatiwa na kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake lakini nina nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ahadi ya ujenzi wa bwawa na miundombinu ya umwagiliaji kwenye eneo hili ni ya muda mrefu tangu wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne. Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano aliuhisha ahadi hiyo wakati wa kampeni zake za mwaka 2020. Eneo hili lina maji mengi ambayo yanaleta mafuriko kwenye Kata zaidi ya tano. Kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri kwenye majibu yake ni sehemu ya mpango kabambe, swali langu nataka kujua, ni lini ahadi hii itatekelezwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Wilaya ya Korogwe inaongoza kwa fursa na mazingira mazuri ya kilimo cha umwagiliaji. Serikali haioni sasa ni wakati sahihi kuboresha skimu zilizopo kwenye Tarafa za Magoma na Mombo ikiwemo Skimu ya Kwamkumbo ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri waliitolea ahadi wakati wa ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu Februari, 2021?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili madogo ya Mheshimiwa Mnzava, Mbunge wa Korogwe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini tutaijenga Skimu ya Mkomazi, commitment ya Wizara na Serikali ni kwamba katika kipindi cha miaka hii mitano kwa maana ya plan ya 2025, Skimu ya Mkomazi ni moja kati skimu ambazo Serikali itazijenga. Nataka nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba hii ni moja kati ya skimu tutakayoipa priority kwa sababu kila mwaka maafa yanayotokea na upotevu wa maji katika eneo hilo ni makubwa sana kuna potential kubwa ambayo na sisi tunafikiri kwamba ni muhimu tukaifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahadi tuliyoitoa tukiwa katika ziara na Mheshimiwa Waziri Mkuu ipo palepale. Tuliahidi kwamba baada ya mvua hizi wataalam wetu wa Wizara ya Kilimo kwa maana ya wataalam wa Tume ya Umwagiliaji watapeleka vifaa kwa ajili ya kwenda ku-repair ile skimu ambayo ilikuwa imeathirika. Ahadi ile ipo palepale, naomba avumilie, Inshaallah, hivi karibu wataalam wetu watakwenda.