Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Timotheo Paul Mnzava (5 total)

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza:-

Katika Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 wananchi wa Korogwe waliahidiwa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Korogwe - Dindira – Bumbuli.

Je, ni lini ujenzi huo utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara ya Korogwe - Dindira hadi Bumbuli inayopita kwenye maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya biashara na matunda imeanza kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa lengo la kujenga kwa kiwango cha lami barabara yote ya Soni – Bumbuli – Dindira - Korogwe yenye urefu wa kilomita 77 ikiwemo sehemu ya Bumbuli - Dindira - Korogwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina sehemu ya Soni - Bumbuli yenye urefu wa kilomita 21.7 imekamilika mwezi Juni mwaka 2018. Hivi sasa Serikali ipo katika hatua ya ununuzi wa kumpata mtaalam mshauri wa kufanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa sehemu iliyobaki ya Bumbuli-Dindira-Korogwe yenye urefu wa kilomita 5.3. Kiasi cha shilingi milioni 130 zimetengwa katika bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya kuanza kazi hiyo. Usanifu utakapokamilika na gharama za ujenzi kujulikana, fedha za ujenzi zitafutwa ili ujenzi wa kiwango cha lami uanze kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza:-

Wananchi wa Tarafa ya Mombo wamekuwa na hitaji la kuwa na skimu kubwa ya umwagiliaji katika Bonde la Mto Mkomazi na mara kadhaa viongozi wa Serikali wamekuwa wakitoa ahadi ya kukamilisha jambo hilo.

Je, ni lini Serikali itatekeleza mradi wa umwagiliaji katika Bonde la Mto Mkomazi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Timotheo Mnzava Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijiji kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka 1980 Serikali kupitia na washirika wa maendeleo, yaani Wakala wa Ushirikiano wa Kitaalam wa kimataifa wa Serikali ya Ujerumani (Germany) Agency for Technical Cooperation Limited) ulifanya upembuzi yakinifukwa ajili ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji katika Bonde la Mkomazi katika tarafa ya Mombo, Halmashauri ya Korogwe. Hata hivyo taarifa ya upembuzi yakinifu na usanifu zilibaini kuwa ujenzi wa bwawa hilo ungesababisha kuongezeka kwa maji katika Ziwa Manga na kupelekea kuzama kwa Kijiji cha Manga Mikocheni pamoja na mashamba ya wakulima.

Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto hiyo katika mwaka 2014/2015 wataalam wa Ofisi ya Kanda ya Umwagiliaji ya Kilimanjaro walifanya mapitio ya upembuzi yakinifu upya na usanifu wa kina uliofanywa katika eneo hilo kwa lengo la kuepusha uwezekano wa kufurika kwa Ziwa Manga, kuzama kwa Kijiji ca Manga Mikocheni na mashamba ya wakulima kutokana na ujenzi wa bwawa hilo. Mapitio hayo yalibaini uwezekano wa ujenzi wa bwawa na mradi wa umwagiiaji katika eneo hilo bila kuathiri wakazi wa eneo hilo. Mapitio ya usanifu huo yalibaini kuwa ujenzi wa bwawa pekee utagharimu shilingi bilioni 1,543,736,877.

Mheshimiwa Spika, Serikali iko katika mchakato wa kufanya ukaguzi na tathmini ya kina ya miradi yote ya umwagiliaji nchini ili kufanya uhakiki wa eneo la umwagiliaji kwa lengo la kubaini ubora wa miradi, thamani ya fedha, gharama za miradi na mahitaji halisi ya sasa ya kuboresha, kuendeleza na kuongeza miradi mipya ya umwagiliaji. Aidha, baada ya tathmini hiyo Serikali itaendelea kutafuta fedha ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha mabwawa na skimu za umwagiliaji nchini ikiwemo mradi wa umwagiliaji katika Bonde la Mkomazi zinaendelezwa na kuwanufaisha wananchi wa Mombo na taifa kwa ujumla.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza:-

Katika Jimbo la Korogwe Vijijini bado vijiji vingi havina umeme.

Je, ni lini usambazaji wa umeme kupitia REA utakamilika katika vijiji vya Jimbo la Korogwe Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kutekeleza mradi wa kupeleka umeme katika vijiji vyote nchini hadi ifikapo mwezi Juni, 2021. Katika Jimbo la Korogwe Vijijini jumla ya vijiji 71 vitaunganishiwa umeme. Aidha, vijiji 14 vya Hamashauri ya Wilaya ya Korogwe Vijijini vinatarajiwa kupatiwa umeme kupitia Mradi wa REA III mzunguko wa kwanza unaoendelea kutekelezwa. Hadi kufikia mwezi Juni, 2019 Mkandarasi Kampuni ya DERM Electrics ameshawasha umeme katika vijiji vinne vya Nkalekwa, Magila, Kwasunga na Welei pamoja na kuunganisha umeme kwa wateja wa awali zaidi ya 112.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa mkandarsi anaendelea na kazi ya kusimika nguzo, kuvuta nyaya na kufunga transifoma katika vijiji kumi vitakavyopatiwa umeme kupitia mradiwa REA lll mzunguko wa kwanza. Kazi za mradi katika Jimbo la Korogwe Vijijini zinahusisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 9.45, njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 48 na ufungaji wa transfoma 18 za kVA 50 na 100, pamoja na kuunganisha umeme kwa wateja wa awali 825 na gharama za mradi ni shilingi bilioni moja na milioni 600.

Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vilivyosalia 57 vitapatiwa umeme kupitia mradi wa REA III mzunguko wa pili, unaotarajiwa kuanza mwezi Julai, 2019 na kukamilika mwezi Juni, 2021.
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza:-

Barabara ya Msambiazi - Lutindi – Kwabuluu ni muhimu kwa uchumi na maisha ya watu wa Korogwe hususan Kata za Tarafa ya Bungu, lakini barabara hii ni mbovu na korofi sana.

(a) Je, ni lini Serikali itajenga barabara hii kwa kiwango cha lami?

(b) Je, ni lini barabara hii itapandishwa kuwa ya mkoa hasa ikizingatiwa kuwa inakwenda kuunganisha Bumbuli na Lushoto?
WAZIRI WA NCHI, OFISI WA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, barabara ya Msambiazi – Lutindi – Kwabuluu ni barabara ya Mkusanyo (Collector road) yenye urefu wa kilometa 17.5. Kuanzia Mwaka wa Fedha 2017/2018 hadi 2019/2020 Serikali imeifanyia matengenezo kwa gharama ya shilingi milioni 43. Katika Mwaka wa fedha 2020/2021 Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Korogwe umeomba kutengewa shilingi milioni 50 kwa ajili ya matengenezo ya barabara hii. TARURA Wilaya ya Korogwe inaendelea kufanya upembuzi wa kina wa mtandao wa barabara zake utakaobaini vipaumbele vya ujenzi wa mtandao wa barabara Wilayani Korogwe kwa viwango vya lami, changarawe na vumbi.

(b) Mheshimiwa Spika, kabla ya kuanzishwa kwa TARURA, barabara hii iliombewa kuingizwa kwenye orodha ya barabara zinazohudumiwa na TANROADS kupitia Baraza la Madiwani ambapo baada ya kuanzishwa kwa TARURA imepewa jukumu la kuendelea kuihudumia barabara hiyo. Aidha, Serikali imeshatoa maelekezo kwa Makatibu Tawala wa Mikoa yote nchini kuhusu utaratibu wa Bodi za Barabara za Mikoa, Wabunge au Kikundi cha watu kutuma maombi ya kupandishwa hadhi barabara. Utaratibu huu umetolewa na Kamati ya Kitaifa ya Kupanga Barabara katika Hadhi Stahiki (National Roads Classification Committee- NRCC).
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya muda mrefu ya Mhe. Rais ya ujenzi wa Bwawa la umwagiliaji kwenye Bonde la Mto Mkomazi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali Mheshimiwa Timetheo Paul Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Skimu ya Umwagiliaji ya Mkomazi ipo katika Kijiji cha Manga Mikocheni, Kata ya Mkomazi, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe. Skimu hiyo ina jumla ya hekta 5,000 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ambapo kati ya hizo, hekta 200 zimeendelezwa kwa kujengewa miundombinu ambazo zilifadhiliwa kutokana na fedha za ndani za halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Kilimo kupitia Ofisi ya Tume ya Umwagiliaji ilifanya mapitio ya upembuzi yakinifu ya awali na kubaini hitaji la Sh.3,379,000,000 ili kuendeleza bonde hilo. Kati ya fedha hizo Sh.4,041,000,000 ni kwa ajili ya ujenzi wa bwawa na Sh.2,337,999,000 ni za ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji. Ujenzi wa Skimu ya Mkomazi pamoja na bwawa lake upo katika Mpango wa Umwagiliaji wa mwaka 2018 (National Irrigation Master Plan). Mkakati mpana wa Serikali ni kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji ili ifikapo mwaka 2025 tuwe na uwezo wa kumwagilia hekta milioni 1.2 ambapo Skimu ya Mkomazi ni mojawapo ya skimu zitakazotekelezwa katika mkakati huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara imeanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Umwagiliaji wenye lengo kufanya matengenezo ya miundombinu na kujenga miradi mpya. Pia Wizara imeelekeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kuanzia sasa kujenga miradi kwa kutumia wataalam wa ndani kwa utaratibu wa force account kwa Mfumo wa Usanifu na Ujenzi (Design and Build).