Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Timotheo Paul Mnzava (17 total)

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nitumie nafasi hii kwanza kabisa kumshukuru Mungu ambaye anatupa uzima, pia nitumie nafasi hii kuzishukuru na kuzipongeza Kamati zote mbili ile ya Kilimo pamoja na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Spika, ningeomba kuchangia kwenye maeneo machache. Ningeomba nichangie kidogo kwenye utalii na baadaye nitaenda kuchangia kidogo kwenye eneo la ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la utalii, tulipokuwa kwenye Kamati tumepata taarifa na tumetembelea Mradi huu wa REGROW. Ni mradi mzuri ambao utasaidia nchi yetu kuinua utalii kwenye maeneo ya Kusini mwa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, naomba kushauri tu, ilizungumzwa asubuhi hapa, tunapotaka kuinua watalii kwenye maeneo ya Kusini lazima twende sambamba na kuangalia namna ya kuboresha na kusimamia uhai wa hizi hifadhi zetu. Imezungumzwa kuhusu Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kuhusu ile barabara, barabara ile ina madhara mengi. Kwa haraka haraka kuna changamoto kama nne zinazosababishwa na barabara hii. Changamoto ya kwanza inarahisisha sana shughuli za ujangili na inasababisha uwepo wa takataka ambazo nyingine ni hatari kwa maisha ya wanyama wenyewe. Taarifa tuliyopewa ni kwamba kuna wastani wa kilo 318 za takataka kwa siku ambazo zinazalishwa kutokana na kuwepo na barabara katikati ya hifadhi.

Mheshimiwa Spika, changamoto nyingine ni kugongwa kwa wanyama. Mwaka 2015/2016 wanyama 361 wamegongwa, mwaka 2016/2017 wanyama 218 na mwaka jana Julai mpaka Desemba 2018 ni wanyama 130. Ukichukua mwaka wa fedha wa 2013/2014 mpaka 2017/2018 ni wafanyama 1,062 wamepoteza maisha kwa sababu ya barabara ile. Idadi hii ni kubwa, ni lazima tufanye maamuzi mazito na magumu.

Mheshimiwa Spika, natambua kwamba barabara hii ni ya kimataifa na inawezekana kuna mikataba ya kimataifa ambayo inatuongoza kutumia barabara ile. Lazima ifike mahali Serikali au nchi tuamue na tukapokuja kuamua mambo mazito kwa ajili ya maslahi na ustawi wa nchi yetu haswa maslahi ya hifadhi zetu hatuna haja ya kuangalia sana makele yanayotoka huko nje na maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, tumeona hili kwenye Stiegler’s, watu wamepiga kelele nyingi sana lakini tumesema kama Taifa tunahitaji kuwa na uchumi wa viwanda na ili tuwe na uchumi wa viwanda tunahitaji kuwa na umeme wa uhakika. Tumeamua hakuna namna nyingine lazima nchi kutekeleze mradi huu kwa ajili ya kupata umeme wa kutosha kwa maendeleo ya nchi yetu. Kama Mheshimiwa Rais alivyoamua chini ya Serikali yake kuendesha mradi ule, naishauri Serikali iangalie kwa jicho la haraka na la dharura juu ya barabara hii ili tuendelee kulinda maisha na uhai wa Hifadhi ya taifa ya Miukumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumze kidogo kwenye sekta ya ardhi. Nitumie nafasi kwa dhati kabisa kumpongeza sana Mheshimiwa wa Ardhi na Naibu wake, wanafanya kazi kubwa tunawaona wanavyoangaika kwenye maeneo mbalimbali ya nchi kutatua migogoro ya ardhi. Nachoomba kuwashauri kama Wizara waendelee kutengeneza utaratibu maalumu na mahsusi wa namna gani ya kuondokana na changamoto za ardhi ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kwenye jambo hili la ardhi nilisikia asubuhi watu wanazungumza hapa na ziko dhana na hisia kwamba kuna watu wanaonewa kwenye mchakato wa kufuta mashamba. Kwanza niseme, nilimshangaa sana kumsikiliza ndugu yangu mmoja akisema kwamba tulikubaliana kwenye Kamati lakini anashangaa huko haikusomwa. Mimi ni Mjumbe wa Kamati na kama ndugu yangu yule angekuwa ni Mtumishi wa Mungu kama nilivyo mimi nisingesema hapa tungeenda kuzungumza kiroho lakini kwa sababu si Mtumishi wa Mungu lazima nitumie nafasi hii kusema, hatukukubaliana jambo la namna hiyo kwenye Kamati yetu ya Ardhi, Maliasili ya Utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia Mheshimiwa Rais hafuti tu mashamba kwa kukurupuka, mashamba yanafutwa kwa mujibu wa sheria zilizotungwa na Bunge hili. Bahati nzuri ni Mwanasheria na nimepata nafasi ya kufanya kazi kwenye Wilaya zenye migogoro mikubwa sana ya ardhi na nimewahi kuwa Wakili wa watu waliokuwa na kesi dhidi ya Serikali kwa ajili ya kufutiwa mashamba, nafahamu changamoto ilipo. Kama kuna watu wanaobebembelezwa ni watu wenye mashamba, anapewa onyo, anapewa notice ya siku ya 90 ili ku-remedy breach za conditions za hiyo right of occupancy aliyoipewa, hawafanyi. Technique ambayo inatumika mara nyingi unakuta mtu anakuja dakika za mwisho, siku 90 zimekwisha anaanza kwenda kugusagusa sehemu ndogo anaondoka halafu anasema nimeendeleza, si sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii niseme kwamba nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi aliyoifanya ya kufuta hati za shamba ya baadhi ya wawekezaji kwenye nchi yetu. Ukienda Korogwe leo wananchi wamemwelewa sana Mheshimiwa Rais na wamemshukuru. Bunge hili waliokuwepo muda mrefu ni mashahidi, mtangulizi wangu Profesa Maji Marefu alikuwa kila akisimama analia na mashamba yasiyoendelezwa Korogwe. Leo Mheshimiwa Rais amefuta mashamba watu wanapiga kelele kwa maslahi ya nani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi watu wa Korogwe tunamshukuru Mheshimiwa Rais na tumuombe Waziri wa Ardhi bado kuna mashamba mengine ya akina Chavda yamekaa ni mapori, mpelekeeni Mheshimiwa Rais atafutie wananchi wapate maeneo. Ukienda kule Magoma na Kwa Shemshi kuna ardhi kubwa mashamba yamekaa, hayaendelezwi yamekuwa mapori na wengine wanakodisha, mpelekeni Mheshimiwa Rais atufutie ili wananchi wapate maeneo ya kilimo na makazi. Mimi nawapenda sana wawekezaji lakini lazima tuwe na wawekezaji ambao wanatutendea haki na wanatendea haki masharti ya umiliki waliyopewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia vizuri watu wanalaumu lakini kama kuna mtu anamwelewa Rais ni mimi, ni Rais anayependa haki na ni asiyemuonea mtu. Mimi ninao ushahidi wa baadhi ya mashamba, kwa sababu michakato inaanzia kwenye Halmashauri, yako baadhi ya mashamba ambayo wenzetu kwenye Halmashauri waliwahi kutengeneza na kupeleka kwa Rais yakafutwe. Hata hivyo, yalipofika Wizarani na Mheshimiwa Rais wakaona utaratibu umekiukwa yalirudishwa na Mhesimiwa Rais, tunataka haki ya namna gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nenda Wilaya ya Arumeru, Mheshimiwa Lukuvi anafahamu liko shamba la Karamu Coffee Estate, Halmashauri, Mkoa kote tulipeleka lakini lilipofika juu Rais akasema utaratibu unaonekana hauko sawasawa rudisheni mkarekebishe. Achana na hilo, nenda Kilombero, yuko mtu mmoja alikuwa na nafasi kubwa sana kwenye nchi hii sitamtaja, sasa hivi ni marehemu, Halmshauri walipitisha wakataka yale yafutiwe hati wakapeleka kwa Mheshimiwa Rais akasema hapa kuna uonevu rudisheni, tunataka Rais wa namna gani, tunataka Rais afanye nini tena? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona hapa watu wanasema ooh watu wanaonewa, wanasumbuliwa, wameendeleza, nataka niwaambie ndugu zangu kama kuna Rais tunamshukuru watu wa Korogwe ni Mheshimiwa Rais Magufuli. Sisi watu wa Korogwe hatusimuliwi, tumeona wenyewe, mwacheni Mheshimiwa Rais afanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wote tunawataka wawekezaji lakini waacheni wawekezaji hao wafuate taratibu, sheria na kanuni za nchi yetu na yule ambaye atakiuka achukulie hatua kama ambavyo hatua zimeendelea kuchukulia. Mheshimiwa Lukuvi nakukumbusha tu tunakuomba Korogwe mashamba ya Chavda, Kwa Shemshi na Magoma mwende mkampelekee Mheshimiwa Rais, tufute tuwapelekee Watanzania wakatumie ardhi ile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hakuna mtu anayepewa haki bila kuwa na wajibu. Sheria ya Ardhi inayowapa watu haki ya kumiliki ardhi inawapa na masharti na mtu asipokiuka masharti nimesema anastahili zake, stahili ni pamoja na hizo. Kwenye suala la mashamba, mimi kama Mjumbe wa Kamati, kama Mwakilishi wa watu wa Jimbo la Korogwe Vijijini tuko na Mheshimiwa Rais na tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa jambo kubwa alilolifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeuona ule Mradi wa Kurasimisha na Kumilikisha Ardhi uliokuwa unatekelezwa kwenye maeneo ya kule Malinyi, Kilombero na Ulanga, ni mradi mkubwa. Nimefarijika mradi ule, niliambiwa hata Mheshimiwa Waziri kuwa unasimamiwa na vijana, wamefanya kazi kubwa. Hatusemi kwamba wazee hawafanyi kazi kubwa lakini wale vijana kwenye mradi ule wameutendelea haki wanastahili kupewa pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa Wizara, tuwe na utaratibu wa kuendeleza mradi huu kwenye maeneo mengine. Safari hii tumepata hela za wafadhili hatujui mbele ya safari tutakuwa na hela za wafadhili au tutazikosa. Kwa vyovyote itakavyokuwa mradi ule ni wa muhimu kutusaidia kupunguza migogoro ya ardhi ndani ya nchi.

Mheshimiwa Spika, mwisho naomba nizungumze kidogo kuhusu Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Hifadhi hii ni kubwa, ndiyo hifadhi ya kwanza kwa ukubwa kwenye nchi yetu na Afrika Mashariki. Ni miongoni mwa hifadhi chache ambazo hazijaathiriwa na shughuli za kibinadamu. Kamati imesema kwenye taarifa yake kwamba changamoto kubwa ni kuelekea kukakuka kwa Mto Ruaha Mkuu ambao ndiyo roho ya hifadhi ile. Niiombe Serikali kwenye jambo hili la Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ili tunusuru hifadhi ile tunahitaji kunusuru Mto Ruaha Mkuu.

Mheshimiwa Spika, tukisema kunusuru Mto Ruaha Mkuu watu wanafikiria kwenda kuwafukuza watu wanaolima kule kwenye Bonde la Usangu na maeneo mengine. Kama alivyosema mzee wangu, Mheshimiwa Jitu, tunazo teknolojia za kisasa zitumike. Pia changamoto kubwa ukienda kule Mabarali si tu kwamba wanalima mpunga kwa kutumia yale maji, hapana, lakini watu wanashilikia maji kwa kuzua magugu na vitu vingine hata baada ya muda wa kilimo cha mpunga. Wizara ya Maliasili ishirikiane na watu wa Ardhi na watu wa Kilimo tuwe na teknolojia nzuri ili yale maji yakimaliza kufanya shughuli za kilimo basi yaachiwe yaendelee kutiririka kwenye mto ili usiendelee kukauka. Tukifanya hivyo tutakuwa tumeisaidia sana Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja za Kamati zote mbili na mapendekezo yake, ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Awali ya yote, nitumie nafasi hii kukupongeza wewe na viongozi wengine wote wa Bunge kwa namna mnavyotuongoza. Pia nitumie nafasi hii kuzipongeza sana Kamati zote mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma taarifa hizi za Kamati kwenye uchambuzi wao, ukasoma maoni na mapendekezo ya Kamati zote, unaona kabisa kwamba Wajumbe wa Kamati hizi wamelitendea haki Bunge lako Tukufu. Nimezisoma, kazi yao ni nzuri na ni wajibu wangu kuwapongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajadili taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, lakini pia na ile ya Sheria Ndogo. Tunapokuja kwenye uwanja kama huu wa Sheria, kwa sisi tunaoipenda nchi yetu pia lazima tutumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya ya kusaidia utekelezaji na usimamizi mzuri wa sheria ndani ya nchi yetu. Speed, kasi na moyo wa Mheshimiwa Rais kuendelea kuteua Majaji kwa wingi kama anavyofanya sasa hivi ni ishara kwamba Mheshimiwa Rais anataka kuusaidia Mhimili wa Mahakama ufanye kazi zake vizuri na utoe haki kwa wakati jambo ambalo ni wajibu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona ni vyema nichangie mambo machache. Kwa muda mrefu tumekuwa tukisikia na ndiyo msingi wa kuwa na Katiba na kuwa na Sheria, kwamba nchi yetu ni lazima iongozwe na iendeshwe kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu. Hata mchangiaji aliyetoka, kaka yangu Mheshimiwa Lema amesisitiza jambo hilo na ni jambo zuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na kelele nyingi kwenye uhuru wa watu kutoa maoni, uhuru wa watu kushirikiana; na mambo mengine ya namna hiyo. Wote wanaozungumza, wanasema uhuru huu upo kwa mujibu wa Katiba, kwa hiyo, wanataka uhuru huu uheshimiwe. Hilo ni jambo zuri, nami naliunga mkono kabisa; na ndiyo mtazamo wangu, ndiyo msimamo wangu na ndiyo mawazo yangu kwamba kama Taifa, lazima tuheshimu uhuru na haki zilizotolewa kwenye Katiba yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tukumbushane kwamba hata huu uhuru tunaotaka tuuheshimu, tunaotaka ufuatiliwe, tunaotaka utekelezwe; haki za binadamu tunazotaka watu wapate; hakuna haki bila wajibu. Katiba hii hii ambayo inapigiwa kelele kwamba imetoa haki za binadamu, imetoa uhuru kwa watu kufanya mambo, imetoa na namna ya kutekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiisoma vizuri Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na kwamba ziko haki, uko wajibu, lakini ukienda kwenye Ibara ya 30 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa masharti, haiachi tu uhuru ukaenda unavyotaka, kila mtu afanye anavyotaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba inatuambia kabisa, lazima kila mmoja kwenye kutekeleza na kutumia uhuru wake, ahakikishe haingilii uhuru wa mtu mwingine, ahakikishe hautumii katika namna ambayo inakwaza na kuumiza watu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wale ambao tunapigania haki, tuko sahihi kabisa, lakini lazima tukumbushane kwamba uhuru huu una mipaka. Ibara ya 30(2) inaipa Bunge mamlaka ya kutunga Sheria kutekeleza huo uhuru na hizo haki ambazo tunazo kwa mujibu wa Katiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliona kwa kuwa tunajadili taarifa za Kamati hizi ni vyema tukakumbushana jambo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye taarifa ya Kamati ya Sheria Ndogo, kwenye ukurasa wa 36 kama sikosei, Kamati ya Sheria Ndogo imetoa maoni na mapendekezo mazuri sana kuhusu Sheria Ndogo ambazo zinatungwa kwenye nchi yetu; ukurasa wa 36 ile (a), (b), (c), (d) na (e).

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Kamati kwa sababu ushauri walioutoa ni ushauri wa msingi, nami ninauunga mkono na ninaomba ukafanyiwe kazi. Nasema naipongeza Kamati hii kwa sababu gani? Ushauri walioutoa wenzetu kwenye Kamati, umetuonesha pia tofauti ya ile dhana waliyokuwa nayo watu wengine kwenye mawazo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mawazo, dhana na maneno; wako watu ambao wanapinga, wanasema siyo sahihi kuendelea kuiachia Serikali, Taasisi mbalimbali za Serikali kutunga Kanuni. Wako wengine wanasema Kanuni mbalimbali zitungwe ziwekwe ndani ya sheria au zije zijadiliwe Bungeni. Ni dhana zinazungumzwa, lakini ukisoma ushauri huu wa Kamati, unaelewa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba yetu imelipa Bunge mamlaka ya kutunga sheria, ukisoma Ibara ya 64. Ukienda Ibara ya 97(5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inatoa mwanya, baada ya kutunga Sheria inaruhusu kutungwa kwa kutungwa kwa Kanuni na sheria nyingine ndogo ndogo zikiwemo Kanuni, zikiwemo Orders na vitu vingine vya namna hiyo. Kwa hiyo, kwanza, Kanuni kutungwa kwenye Wizara, kutungwa kwenye Taasisi mbalimbali za Umma, kutungwa kwenye vyombo mbalimbali, haikiuki Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hilo ni jambo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, hatuwezi kuacha Bunge likawa linatunga sheria zote, kanuni zote na orders zote. Tutakuwa nchi ya namna gani? Kazi zitafanyika namna gani? Bunge hili tunakutana kwa mwaka mara ngapi? Tunafanya kazi mara ngapi kwenye Bunge hili? Huwezi ukaacha kila sheria ikatungwa na Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili mambo yaende vizuri, tutatunga Sheria ya Bunge, lakini sheria hiyo lazima itoe mwanya kwa Taasisi nyingine au Wizara au Idara kutunga kanuni ili mambo yaweze kwenda vizuri. Hata inapotokea kuna jambo la kurekebisha, pia ni rahisi kurekebisha kanuni kuliko utaratibu wa kurekebisha sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya siyo maneno yangu tu peke yangu. Mwanasheria mmoja mbobezi anaitwa John Alder, ameandika Kitabu kinaitwa “Constitutional and Administrative Law”, edition ile ya saba. Kwenye kitabu chake ukurasa wa 147 anajaribu kueleza huo mkanganyiko na hayo mawazo ya watu, lakini mwisho ana-conclude akasema “however, it is difficult to imagine a complex and highly regulated society that could function effectively if all laws had to be made by the Parliament itself.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema niliseme hili, kwa sababu maoni ya Kamati yamejielekeza vizuri, lakini najua yako mawazo ya watu ya namna hiyo. Mimi nadhani utaratibu uliopo ni mzuri, tuache utaratibu huu uendelee. Sheria zitungwe na kama inavyotukumbusha ile Sheria yetu ya Interpretation of Laws, ukisoma kuanzia section ya 36 inatoa utaratibu, hizi kanuni zitungweje? Ziweje? Zifuatane na kitu gani? Zizingatie vitu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utaratibu uliopo uendele, lakini ushauri wa Kamati uzingatiwe ili kuweza kuboresha utaratibu huu wa kutengeneza Kanuni na Sheria nyingine ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lilitoka kuzungumzwa hapa muda siyo mrefu sana. Tunapokumbushana kuendesha nchi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu, lazima tukumbushane kama nilivyosema, haki na wajibu wa kila mmoja wetu. Sheria zetu na taratibu zetu haziruhusu mambo yaliyoko Mahakamani kujadiliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona imekuwa ni utaratibu wa kawaida na kwa masikitiko makubwa, nimewahi kuona hata kwenye Bunge lako hili, mtu ana kesi Mahakamani, amepewa dhamana, amekiuka masharti ya dhamana, akafutiwa dhamana, ana kesi Mahakamani, ana- challenge uamuzi wa Mahakama kumfutia dhamana, mtu anakuja na jambo hili kulileta Bungeni. Tunakuja kufanya nini kwenye Bunge hili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu uko wazi. Mtu anasema kuna kesi ya Mashehe; ndiyo ipo kesi ya Mashehe lakini iko Mahakamani. Unataka tuilete Bungeni humu kufanya nini? Ni lazima sisi kama Wabunge tuwe watu wa kwanza kuheshimu sheria.

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge tuwe watu wa kwanza kuheshimu misingi na taratibu na Katiba ya…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mnzava, ahsante.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja za Kamati. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Awali ya yote, nitumie nafasi hii kwanza kabisa kumshukuru Mungu mwingi wa rehema aliyenijalia uzima na kuweza kuwepo humu ndani leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kumpongeza kwa dhati kabisa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya kutuletea maendeleo watu wa nchi ya Tanzania. Pia nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na Waziri wa Utumishi wanafanya kazi kubwa na wasaidizi wao wote kwenye Wizara, tunaona kazi wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa niruhusu nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa jambo moja kubwa ambalo amelifanya kwenye nchi yetu. Baada ya kuingia kwa Serikali ya Awamu ya Tano Mheshimiwa Rais amekuja na namna tofauti ya kuwapata Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya, Halmashauri za Miji, Majiji na vile vile Makatibu Tawala wa Wilaya na watumishi wengine wa maeneo mengine, tofauti na utaratibu uliokuwa umezoeleka mwanzoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili limetusaidia kuondoa utendaji wa mazoea kwenye Halmashauri zetu. Kama kuna mtu ambaye analipiga vita, atakuwa na matatizo, lakini tunaojua tunaona kwamba jambo hili limetusaidia sana kupunguza urasimu na mazoea kwenye Halmashauri ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kwenye eneo la afya. Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, tunaishukuru sana Serikali sisi watu wa Korogwe. Mlichukua Hospitali ya Wilaya ya Korogwe ikaenda Halmashauri ya Mji lakini mmetupa shilingi bilioni 1.5 kutengeneza Hospitali ya Wilaya na inajengwa pale Makuyuni na ujenzi umeanza. Tunaishukuru sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tukumbuke jambo moja, unapotoa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya au shilingi milioni 400 au 500 kwa ajili ya kituo cha afya halafu gharama za kuingiza umeme kwenye hospitali shilingi milioni 200, gharama za kuingiza maji shilingi milioni 150 na hakuna fedha nyingine nje ya hiyo inayotoka, hiyo shilingi bilioni 1.5; inatupunguzia majengo ambayo tungeweza kujenga kwenye hospitali hizi za wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba TAMISEMI itusaidie kukaa na Wizara nyingine kama ya Nishati na Wizara ya Maji. Sisi Korogwe alipokuja Mheshimiwa Waziri wa Maji nilimwomba kutusaidia kusogeza huduma ya maji kwenye hospitali ya wilaya tunayoijenga sasa hivi na alikubali. Bado tunapata shida kwenye upande wa umeme na zaidi ya shilingi milioni 190. Naomba sana Mheshimiwa Waziri aangalie namna ya kuwasiliana na Wizara nyingine kuweza kutusaidia kwenye jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kwenye kitabu humu ndani Mheshimiwa Waziri ametengea Korogwe shilingi milioni 200 kwa ajili ya kituo cha afya Kerenge, tunakushukuru sana. Wewe ulikuja Korogwe unajua shida iliyokuwa Korogwe kulingana na eneo la kujenga hospitali ile ya wilaya, pamoja na shilingi milioni 200 kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Kerenge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyo vituo vya afya vingine vitatu Korogwe. Mwaka wa fedha uliopita hatujapata fedha yoyote kwa ajili ya kituo cha afya. Kuna Vituo vya Afya vya Bungwe na Kituo cha Afya Magoma, vina hali mbaya. Ni vya muda mrefu. Mwaka 2018 aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya TAMISEMI anayeshughulika na afya, mama yangu Zainab, alikuja Korogwe na aliwaahidi watu wa Korogwe kwamba watapata shilingi milioni 500 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa Kituo cha Afya cha Bungu. Kwenye kitabu hiki sijaona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana kaka yangu, Ubunge wenyewe ndiyo kwanza nimekuja juzi, namwomba, Kituo cha Afya cha Bungu chonde chonde tusaidie tupate hela tukatanue kile Kituo cha Afya. (Makofi/ Kicheko/Kigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kidogo upande wa TARURA. Kwanza tuwapongeze TARURA, wanafanya kazi nzuri. Pamoja na changamoto za kibajeti, lakini wanajitahidi wanafanya kazi nzuri. Sisi Korogwe tuna Jimbo kubwa, jiografia yetu ni kubwa na siyo nzuri. Hela tunayotengewa ukilinganisha na maeneo mengine havilingani. Tunaomba mtupe kipaumbele watu wa Korogwe. Mwaka wa fedha uliopita tumetengeneza barabara 11 tu tena ni kwa vipande, lakini ziko barabara muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale tunapojenga hospitali ya wilaya alipokuja Mheshimiwa Waziri, ukiangalia kwa upande wa juu kuna mlima, ndiyo inapatikana Tarafa ya Bungu. Ili ile hospitali ya wilaya iweze kuwa na faida kwa watu wa Tarafa ya Bungu ya mlimani, iko barabara inaitwa Makuyuni - Zege - Mpakani, Kwemchai – Makuyuni lazima itengenezwe. Bajeti ya kuitengeneza ni zaidi ya shilingi milioni
140. Kabla ya bajeti hii, nimekwenda TARURA zaidi ya mara tatu, nimekwenda ofisini kwa Mheshimiwa Waziri zaidi ya mara nne nikiwaomba ili hospitali ile ya wilaya iweze kutusaidia watu wa Korogwe. Tusaidieni barabara hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya kwenda Kizara; huko mahali mvua ikinyesha kuna eneo la Kizara na Foroforo ni kisiwani kwa sababu barabara ni mbovu. TARURA ukizungumza nao kwamba matengenezo yanahitajika; wanasema yanahitaji hela nyingi na hela tunayopewa ni ndogo, tunawaomba muwaongezee TARURA hela iweze kutusaidia kufanya hii kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumekuwa na shida kwenye upande wa madaraja. Ukiangalia hela wanayopewa watu wa TARURA kutengeneza barabara inakuwa ngumu sana kwa wao kutengeneza madaraja. Ninalo daraja kule Korogwe linaitwa Daraja la Mswaha, ni zaidi ya shilingi milioni 180 kutengeneza lile daraja, lakini utakuta TARURA wanapewa shilingi milioni 400 kwa mwaka mzima wa fedha. Hawawezi kutengeneza daraja kama hilo. Wananchi wanapata shida, wanapata taabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo daraja kule kwa Lukongwe, liko daraja linalotuunganisha watu wa Korogwe na wenzetu wa Bumbuli kule Mbagai, yamesimama kwa muda mrefu, wananchi wanashindwa kuvuka, wanapata shida ya kupita kwa sababu ya hela ndogo ambayo wanapata watu wa TARURA. Mheshimiwa Waziri, nakuomba sana hebu tuangalieni, ili ile hospitali iweze kuwa na faida, tusaidie kwenye hizo barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kwamba Serikali imeweka msimamo. Yapo maelekezo kwamba hakuna kutoa maeneo mapya ya utawala; lakini kuna Halmashauri ya Mji wa Mombo imepewa Mamlaka ya Mji Mdogo tangu 2004. Miji mingine yote iliyopewa Mamlaka ya Miji Mdogo pamoja na Mji wa Mombo ilishakuwa Halmashauri za Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo tu kwa ajili ya kupewa muda mrefu, jioghrafia ya Korogwe Vijijini ni ngumu. Mheshimiwa Waziri ndiyo maana hata kwenye eneo la kujenga hospitali tulipata shida kwa sababu ya aina ya jiografia ya Wilaya ya Korogwe. Pamoja na hayo maelekezo ya Serikali, naomba sana muangalie uhalisia wa jiografia za Wilaya zilivyo, ukubwa wa wilaya zilivyo kuweza kutafuta maeneo mapya ya utawala kwenye maeneo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa jambo hapa kuhusu Ofisi za Wakuu wa Wilaya kuingilia Ofisi za Halmashauri. Zimepigwa kelele nyingi sana. Natambua kwamba Ofisi za Wakuu wa Wilaya zimeanzishwa kwa mujibu wa sheria. Sheria ya Tawala za Mikoa, ukisoma kifungu cha 13 (1) na (2). Ukisoma kile kifungu cha 14, kinasema Mkuu wa Wilaya ndio principle representative wa Serikali na wanasema all executive functions zitafanywa na Mkuu wa Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tujue tunasema Rais wetu ana sehemu tatu; kwanza, ni mkuu wa nchi; pili, ni mkuu wa Serikali; tatu, ni Amirijeshi. Mkuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa ndio Wawakilishi wa Mheshimiwa Rais. Wanaonjaonja na haka kaharufu. Huwezi ukawa Mkuu wa Wilaya ukaona kwenye Halmashauri ndani ya Wilaya yako, Halmashauri inafanya vitu vya ovyo halafu ukaviacha. Ni lazima ufuatilie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi ni mashahidi. Ziko Halmashauri ambazo Wakuu wa Mikoa walizuia ziara za Madiwani za zaidi ya mamilioni ya shilingi na wakasaidia kuokoa hela za wananchi. Tunachokitaka hapa ni tuweke tu utaratibu mzuri wa namna gani hawa Wakuu wa Wilaya watashiriki kuzisimamia vizuri hizi Halmashauri zilizokuwa chini yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kwamba TAMISEMI mlitoa Waraka Na. 2 wa 2010, unaonyesha ushirika wa Ofisi za Wakuu wa Wilaya kwenye Halmashauri. Kuna mahali kuna upungufu kwenye ule waraka. Unasema Katibu Tawala wa Wilaya ambaye ndiye technical person kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya; naomba ni-declare interest, kabla sijawa Mbunge nilikuwa Katibu Tawala wa Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waraka unasema, ataingia kwenye vikao vya SMT, unasema ataingia kwenye Baraza la Madiwani, lakini kikao cha kila mwezi cha kufanya maamuzi ni Kamati ya Fedha. Katibu Tawala wa Wilaya haingii, anapata wapi taarifa za kumpelekea Mkuu wa Wilaya ili kujua wapi pana shida aweze kuingia hapo? Naomba sehemu hii ifanyiwe marekebisho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Makatibu Tawala wa Wilaya na Makatibu Tarafa wamesahaulika. Yako maeneo Katibu Tawala wa Wilaya anakuwa MC wa kusherehesha kwenye shughuli wanapokuja wageni. Hii kitu siyo sawasawa. Naomba wapewe heshima yao, naomba wakumbukwe na wasaidiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiiti, ukienda kwenye Halmashauri za Upinzani kwa mfano, ziko Halmashauri ambazo Mabaraza ya Madiwani yanataka kufanya maamuzi kinyume hata na maelekezo ya Serikali, kinyume hata na sera za nchi. Huwezi ukaacha Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa kuingilia kwenye Halmashauri za namna hiyo. Ni lazima uingie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze kidogo kwenye eneo la utawala bora. Kwanza nilimsikia ndugu yangu, baba yangu Mheshimiwa Ally Saleh asubuhi alisema, ni kweli tuna uhuru, kila mtu ana uhuru na uhuru upo kwenye Katiba…

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba hii inayotoa huo uhuru, kwa mujibu wa haki za binadamu…

MWENYEKITI: Taarifa.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ulinde muda wangu

T A A R I F A

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba siyo wajibu wa Wakuu wa Mikoa wala Wakuu wa Wilaya kuingilia Halmashauri. Ofisi za Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya kazi yao ni kuIshauri Halmashauri. Kwa hiyo, wao hawana hiyo mamlaka wanayotaka kupewa na Bunge lako Tukufu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mnzava.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei hiyo taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mnzava kwanza pokea hiyo taarifa ya mwanzo.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza siipokei hiyo taarifa kwa sababu sheria iko wazi kwamba Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa ndio wenye jukumu la kusimamia; na hiyo iko kwa mujibu wa sheria siyo kwa matakwa ya mtu. Huwezi kusimamia, halafu mtu unayemsimamia afanye mambo ya ovyo halafu usiingilie, haiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kwenye utawala bora. Ibara ya 30(2) inaweka utaratibu wa hizo haki tunazozisema. Unaposema huna haki ya kusema, una haki ya kukusanyika; ibara hii imetoa mwanya kwa nchi kutengeneza Sheria ya Kusimamia Utaratibu huo. Huwezi ukakusanyika kama hali ya usalama inahatarishwa, huwezi ukakusanyika kama kuna jambo haliendi vizuri. Hiyo ni katiba na hakuna katiba inayovunjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona hoja ya mama yangu, namheshimu sana mama yangu Mheshimiwa Ruth Mollel, kuna hoja mbili kwenye ukurasa wake wa 17 na 18 kwenye hotuba yake, anasema TAKUKURU iache kupeleka watu Mahakamani…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: …mpaka itakapoweza kupata ushahidi wa kutosha.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Pia anasema kwamba kushindwa kwa kesi nyingi za TAKUKURU mahakamani ni ishara…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa mwenyekiti, umenipa ruhusa au!

MWENYEKITI: Taarifa kuhusu nini? Kwa sababu anazungumza kitu ambacho kiko kwenye kitabu.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, si kawaida kupiga taarifa!

MWENYEKITI: Ananukuu kitabu kilichoelezea. Hebu endelea Mheshimiwa Timotheo.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa mwenyekiti, taarifa.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, anasema kwenye kitabu chake kwamba kushindwa kwa kesi nyingi za TAKUKURU Mahakamani ni ishara kwamba kesi hizo siyo za haki.

Mheshimiwa Mweyekiti, sisi tutakuwa nchi ya ajabu kweli. Hivi ni lazima kila anayeenda Mahakamani ashinde? Hilo ni swali l a kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine hebu tuulizane, hivi ni nchi gani ambayo eti mpaka ushahidi wote ukipatikana ndiyo unaenda kumpeleka mtu Mahakamani. Hili ni jambo endelevu, wakati mwingine unaweza ukamkamata mtu, ukampeleka mahakamani…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Ukaendelea kuafuta ushahidi…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mnzava, malizia.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza TAKUKURU, nataka waendelee kufanya kazi vizuri…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: …waimarishe Kitengo cha Uchunguzi, waimarishe Kitengo cha Prosecution ili wafanye kazi nzuri kwa ajili ya kutetea nchi yetu na kupingana na mafisadi wanaoifisadi nchi yetu. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema aliyetujalia uzima, aliyenipa uwezo kuwepo Bungeni leo na kuweza kuchangia bajeti ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji na Naibu wake, wanafanya kazi nzuri Mheshimiwa Waziri ni msikivu sana tunampongeza sana anafanya kazi kubwa na kazi nzuri. Pia tumpongeze Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, kwenye Wizara hii siyo kwa Waziri na Katibu peke yake hata wataalam wao wale watu wa Idara ya Maji Vijijini Mkurugenzi na Msaidizi wake wanafanya kazi nzuri, wanatoa ushirikiano wa kutosha huwa nawasumbua wakati mwingine mpaka usiku nikiwa na changamoto za maji kule kwetu Korogwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niishukuru sana Serikali, kwa muda mrefu watu wa Korogwe tumekuwa tukiangaika na vibali vya mradi wa Vuga, Mlembule, na mradi wa Lusanga, lakini mwezi wa pili hatimaye tumepata vibali vile na miradi ile tayari taratibu zimeanza manunuzi kwa ajili ya wakandarasi kuendelea na kazi zile, tumesubiri kwa muda mrefu kwa hiyo tunaishukuru sana na kuipongeza sana Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Waziri nikushuku sana kwa ile kazi ya ujenzi wa tenki pale Mombo tulikuwa na changamoto ya mtambo kwa ajili ya kutibu maji, tumeshamaliza michoro, imeshaletwa Wizarani tunaomba mtusaidie ile kazi ifanyike kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana dada yangu Mheshimiwa Mboni, alizungumza kwa uchungu sana kuhusu kero ya maji kule Handeni; na ni kweli Handeni kuna shida kubwa sana ya maji, na miongoni mwa njia za kutatua kero ya maji Handeni ni mradi ule wa HTM, na Wizara ilishafanya mpaka usanifu wa kupanua na kuboresha ule mradi. Sasa ukienda kule Korogwe kuna Kata inaitwa Kata ya Mswaha, ina vijiji vitano, kijiji kimoja kinaitwa Kijiji cha Tabora, ndipo kwenye chanzo cha maji cha mradi huu wa HTM na kuna vijiji vingine vinne Kijiji cha Mswaha Darajani, Mswaha Majengo, Kijiji cha Mafuleta, na Kijiji cha Maulwi Rutuba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji hivi vilifanyia usanifu pia kwamba vitafaidika na mradi huu wa uboeshaji na upanuzi wa mradi huu wa HTM ni muda mrefu wananchi wale wanasubiri Mheshimiwa Waziri tunakuomba sana kazi hii ifanyike na itakapofanyika msiwasahau watu wa Korogwe kwenye Vijiji hivyo maana Kata hiyo ndiyo kilipo chanzo cha maji cha HTM.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kule Korogwe kuna eneo linaitwa Bungu, tuliwahi kuwa na mradi wa maji tulipata ufadhili wa watu World Division, tukawa na mradi wa shilingi milioni 969, na ule mradi ulikamika na ulinufaisha vijiji tano, lakini maji yale ni mengi yana uwezo wa kunufaisha vijiji vingine vitatu, Kijiji cha Mlungui, Kijiji cha Kwemshai na Kijiji cha Ngulu. Tunaiomba sana Wizara tuko kwenye maandalizi ya mwisho ya kuleta maombi kwenu ili mtusaidie tuweze kupata fedha za kusambaza na kupeleka maji kwenye maeneo hayo ambayo nimeyataja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi wa maji wa Mwanga, Same, korogwe, mradi huu umesemwa muda mrefu ni mradi muhimu sana unanufaisha Wilaya za Same, Wilaya ya Mwanga na Wilaya ya Korogwe, nimeona kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri kwenye mwaka wa fedha unaokuja tunasema tumetenga bilioni 29 sijaona kama ndiyo tunakwenda kukamilisha ule mradi au bado tutaendelea kusubiri kwa miaka mingine na awamu nyingine zijazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa shida ambayo tunaipata watu wa Korogwe ambao na sisi tumesubiri kwa muda mrefu mradi huu sisi ndiyo tuko mwishoni, tuna Vijiji vitano kwenye Kata ya Mkomazi, Kijiji cha Manga Mikocheni, Kijiji cha Manga Mtindilo, Kijiji cha Mkomazi Kijiji cha Bwiko na Kijiji cha Nanyogie. Vinanufaka na mradi huu na sisi ndiyo tuko mwishoni na tunaambiwa kuna bilioni 29, je mradi huu unakwenda kukamilika? Maana sisi watu wa Korogwe ambao ndiyo tuko mwishoni tunanufaika na mradi huu ukiwa umekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri ukumbuke kwamba tumeusubiri kwa muda mrefu, na changamoto ya maji kwenye vijiji hivyo ni kubwa sana tunakuomba sana utakapokuja kufanya majumuisho utuambie maana mwanzoni pia kwenye vikao vya maandilizi na utekelezaji wa mradi huu watu wa Korogwe tulikuwa tunahusishwa, lakini baadaye kumekuwa na kama sintofahamu hivi hatujui hata kinachoendelea ni nini. Utakapokuja utuambie ni kweli bado watu wa Korogwe ni wanufaika kwenye mradi huu? Na kama ndivyo matumaini yetu yale lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepeleka Wizarani taarifa ya usanifu wa mradi wa maji wa Kijiji cha Mgwashi na kwa Kibomi tangu mwezi wa tatu, hatujapata taarifa yoyote kwamba tutapa lini kibali. Nilikuwa namuomba sana Mheshimiwa Waziri najua watu ni wasikivu kule Wizarani tusaidie tuweze kupata kibali ili mradi huu angalau ukaanze tutekelezwa kwenye maeneo ya Mgwashi na Kwakibomi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hizi fedha za PBR, sisi ni miongoni ambao tulikuwa tunatumaini kwamba tutanufaika na fedha hizi, lakini kwa mwaka huu wa fedha tulikokuwa nao mpaka sasa hatujapata hizi fedha, na sisi tulikuwa tumelenga kwenda kutatua changamoto za maji kwenye baadhi ya maeneo ndani ya Jimbo letu kwa kwenda kufanya ukarabati mdogo wa vyanzo vya maji. Tulikuwa tunategemea kupata fedha hizi kwa ajili ya ukarabati vyanzo vya maji kule Magoma, tulikuwa tunategemea kupata kwa ajili ya kukarabati chanzo cha maji kule Mazinde, tulikuwa tunategemea kwenda kukarabati chanzo cha maji Kerenge na baadhi ya Vijiji vya Kata ya Mashewa. Lakini mpaka leo hatujapata hizi fedha nimejaribu kuuliza Wizarani sijapata majibu ambayo yamekaa vizuri, naomba sana Mheshimiwa Waziri utusaidie tupate hizi fedha twende tukatekeleze hayo mambo kwenye hayo maeneo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ulikuja Korogwe tulikuomba fedha kwa ajili ya kupeleka maji kwenye eneo tunalojenga Hospitali ya Wilaya na tunashukuru kwamba ulikubali na tuliandika ikaja Wizarani baadaye mkaturudishia tulete mchanganuo tukaandaa, tukaleta mchanganuo Wizarani na ukatuhaidi kutupa shilingi milioni 95.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa bahati mbaya sana maji tuliyokuwa tunataka kuyatumia pale chanzo chake ilikuwa ni maji ya kisima, lakini tumegundua chanzo kikubwa na kizuri cha maji ambacho kitakuwa na maji ya mtiririko kwa ajili ya hospitali, pia kwa ajili ya maeneo na Makuyuni na maeneo ya kwa Sunga Mpirani. Kama utaridhia Mheshimiwa Waziri pamoja na kwamba ulikubali, na ukahaidi kutoa milioni 95 nakuomba sana kwa unyenyekevu najua wewe ni msikivu, wewe ni muungwana sana hebu ukubali tukuletee haya marekebisho ili badala ya kutumia chanzo kile cha kisima tutumie chanzo hiki kingine cha maji ya mtiririko na vijiji vingine vya karibu na maeneo yanayojengwa hospitali na vyenyewe viweze kunufaika na maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu Bunge limeanza la bajeti tangu bajeti ya kwanza nilikuwa nataka kuchangia naenda uhamishoni, lakini leo sijaenda uhamishoni nachangia nikiwa kwenye kiti hiki, kwa sababu maji ni jambo muhimu ndiyo maana hata humu unaona kumetulia. Ukisoma vizuri hata kitabu hivi vitabu vya hotuba vya rangi hii nadhani mnanielewa nikisema vya rangi hii kwa mara ya kwanza nimeona hotuba ambayo imegusa vitu tofauti na nyingine utakuta Wizara tatu, Wizara nne hotuba ni hiyo hiyo, lakini leo nimeona hotuba nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba tumesema hapa na nimesema Mheshimiwa Waziri kila mahali nasema tunaomba tunaomba niliposoma hutuba yako kwenye kitabu hichi ukurasa wa 106 changamoto ya kwanza unaionesha ni ukosefu wa fedha. Kwa hiyo, pamoja na maombi yote haya ambayo tunayaweka kama hatuna fedha bado changamoto ni kubwa ni miradi hii itakuwa na shida kwenye kutekeleza, yamekuwepo mawazo humu kwamba iongezwe shilingi 50 na wengine wamesema kwenye mafuta, pia iko hofu kwamba inaweza ikasababisha mfumuko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nishauri tunahitaji kweli ongezeko la fedha kwa ajili ya miradi ya maji kwenye nchi yetu. Ukiangalia lengo tulilokuwanalo la kufika upatikanaji wa maji mwaka 2020 na asilimia tuliyokuwa nayo sasa bila kuwa na mkakati madhubuti wa kupata fedha kwa ajili ya miradi ya maji tutapata shida kwenda kufikia lengo letu. Niombe tu kuishauri Serikali wametusikia Waheshimiwa Wabunge hebu ufanyieni kazi huu ushauri wa Wabunge uliotolewa, ungeniambia kwenye mafuta kunakuwa na mfumuko wa bei nikasema bado yako maeneo mengine, kuna maeneo kwenye mawasiliano kuna watumiaji wengi, tunaweza kuangalia namna ya kuongeza huko ili tupate fedha ajili ya kuweza kusaidia kugharamia miradi ya maji, baada ya kusema hayo nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri na timu yake yote, hotuba yangu kwa ujumla imelenga kwenye maombi, naomba sana maombi yangu myapokee, naomba myafanye kazi naomba muwasaidie watu wa Korogwe ili tuondokane na changamoto hii ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja, kwa asilimia 100. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake, wanafanya kazi nzuri, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitumie nafasi hii kuzungumza mambo machache; kule Korogwe tuna barabara inaitwa Korogwe – Dindira – Bumbuli – Soni, ni barabara ya kilometa 77. Kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010 ambayo ninayo mkononi hapa, kwenye ukurasa wa 48 kulikuwa na ahadi ya kufanya usanifu kwenye barabara hii. Kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015, kwenye ukurasa wa 58 kuna ahadi ya chama chetu kwenda kutengeneza barabara hii kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilipoingia kwenye Bunge lililopita, kwa maana ya Mkutano wa Kumi na Nne, niliuliza swali, Mheshimiwa Waziri akaniambia wametenga shilingi milioni 130 kwa mwaka huu wa fedha unaoisha Juni kwa ajili ya usanifu, lakini mpaka sasa hivi hela zile hazijafika, na usanifu umeshafanyika kwenye kilometa 20 za kutoka Soni kwenda Bumbuli, bado kipande cha kutoka Bumbuli – Dindira – Korogwe na ahadi hii imekuwa ni ya muda mrefu kwa watu wa Korogwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepitia kitabu cha Mheshimiwa Waziri, nimeona kwenye ukurasa wa 181 kuna hela, bilioni sita, wametenga kwa ajili ya barabara pale, wamesema kuanza matengenezo ya lami. Hata hivyo, nilipokwenda ndani zaidi kwenye kitabu, kwenye ukurasa wa 275 wametenga shilingi milioni 770 kwa ajili ya ukarabati, lakini wameweka kwenye ukurasa wa 317 wametenga shilingi milioni 140 kwa ajili ya usanifu. Kwa ukubwa wa kilometa zilizobakia, shilingi milioni 140 haiwezi kutosha kukamilisha shughuli ya usanifu kwenye barabara ile, hata ile 130 ambayo bado haijafika ikija haiwezi kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kwamba matengenezo ya barabara hii ni muhimu, lakini kwa kuwa watu wa Korogwe wamekuwa na kiu ya barabara hii kwa muda mrefu na ni ahadi ya chama chetu; ni ahadi ya viongozi wa Serikali akiwemo Mheshimiwa Rais, akiwemo Mheshimiwa Waziri Mkuu, nimwombe Mheshimiwa Waziri, kama hatuna mahali pengine pa kupata fedha ya kukamilisha usanifu ili tuanze kujiandaa kwenda kujenga, basi hizi 770 tupeleke kwenye usanifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka huu tumefanya matengeneo na nimpongeze Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Tanga, Enineer Ndumbaro, anafanya kazi nzuri sana, sisi Wabunge wa Mkoa wa Tanga tunaisifia kazi yake, anafanya kazi nzuri sana. Mwaka huu tumefanya matengenezo, sehemu iliyobakia ni maeneo machache yaliyobaki, nina hakika hizi milioni 140 na zile milioni 60 nyingine wametenga zinaweza kutosha kumaliza hii kazi. Hebu hizi milioni 770 tupeleke kwenye usanifu ili kazi ya usanifu ikamilike, halafu tuendelee na kutafuta hela kwa ajili ya kutengeneza barabara kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara ya Old Korogwe kwenda mpaka Magoma ambayo inakwenda kuunganisha mpaka na wenzetu wa Mkinga, ni barabara muhimu, lakini haijawahi kufikiriwa kuwekwa kwenye kiwango cha lami. Tunaomba sana Serikali iikumbuke hii barabara. Pia nawakumbusha watu TANROADS wameweka alama za X kwenye nyumba za watu na kuna wengine wamekaa miaka mingi kama watu wa pale maeneo ya Kerenge Kibaoni waende wakapewe elimu juu ya hatma ya makazi yao pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilipongeze sana Shirika la Reli kwa kazi kubwa ya kufufua hii reli, reli ya kutoka Tanga kwenda mpaka Moshi na sehemu ya Tanga- Same imeshakamilika. Ninachoomba tu, SGR wakati ukifika watukumbuke, lakini kwa sasa hivi yale maeneo ambayo kuna makazi ya muda mrefu, watuwekee vivuko ili wananchi waweze kuvuka kutoka upande mmoja wa reli kwenda upande mwingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Nditiye na kaka yangu Engineer Ulanga wamefanya kazi kubwa kule Kizara tulikuwa na shida ya mawasiliano, lakini bado yako maeneo nimeyapeleka kwao maeno ya Lewa, Lutindi, Makumba na Kata ya Mkalamo, tunaomba watupelekee huduma ya mawasiliano kwa ajili ya watu wetu pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, muda sio rafiki sana. Kuna jambo limezungumzwa hapa na kiti chako kimeshalisemea. Tunazungumza yapo malalamiko kwamba kwa nini Wakala wa Ndege amehamishwa kwenda kwenye Ofisi ya Mheshimiwa Rais? Lazima tukumbuke nchi yetu inaongozwa kwa mujibu wa sheria za nchi yetu aliyepewa dhamana ya kuongoza Taifa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hawa walio chini yake wanamsaidia na hata ukiosoma Presidential Affairs inaeleza, hakuna dhambi kwa Rais kuamua kazi ipi ya Serikali isimamiwe chini ya Wizara ipi au ofisi ipi siyo dhambi. Ni vibaya kusema kwamba Rais amefanya makosa au ana nia ovu, sheria inamruhusu, hakuna sheria inayovunjwa ni utaratibu wa kawaida. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, aliyetujaalia uzima. Pia nitumie nafasi hii kwa dhati kabisa kuipongeza Serikali, kumpongeza Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni mara yangu ya kwanza kuchangia bajeti ya Serikali. Tangu nimekuwa Mbunge hii ni mara yangu ya kwanza kuchangia bajeti. Nafarijika sana kuona kwamba nakwenda kuchangia bajeti ambayo ukiisoma unaiona bajeti inayogusa maisha ya watu wa Tanzania. Yanaweza yakasemwa maneno mengi, kunaweza kuwa na hadithi nyingi, lakini ukweli ni kwamba bajeti iliyowasilishwa inakwenda kugusa maisha ya wananchi wetu kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Serikali. Hii miradi mikubwa tunayofanya, inawezekana matokeo yake yasionekane kwa haraka leo, lakini ni miradi ambayo inakwenda kutuvusha kama Taifa kutoka hapa tulipo tuweze kwenda kwenye hatua nyingine. Unapoona mtu analalamika anasema hali ya uchumi ya watu wetu siyo nzuri, mtu analalamika anasema tume-import sana kuliko ku-export, lakini wakati huo huo miundombinu ya kusaidia tuwe na viwanda vya kutosha kwenye nchi yetu watu wanaipiga vita. Ni vitu vya ajabu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unapotaka kuwa na umeme wa uhakika ni kwa ajili ya kusaidia viwanda, unapotaka kuwa na miundombinu ya barabara ya uhakika, kuwa na bandari ya uhakika ni kwa ajili ya kusaidia viwanda, ukipata viwanda vingi ukazalisha vizuri, tutafika huko tunakotaka kufika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, nimeona tangu mjadala huu umeanza tumekuwa tukipigana kelele, mtu anasema, Serikali hii hakuna kitu ilichokifanya. Pia tumefika mahali tunahukumiana kwa kutumia Ilani za Vyama tulizotumia kwenye uchaguzi wetu wa mwaka 2015. Sisi wote tunajua, Vyama vinapokwenda kwenye uchaguzi, Ilani tunazozinadi tunazinadi kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania kwa miaka mitano, ndiyo muda tuliojiwekea kwa uongozi kama Taifa kwa mujibu wa Katiba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, muda wa kutekeleza Ilani ni miaka mitano. Miaka mitano haijaisha, pressure hizi zinatoka wapi?mtu anaongea kana kwamba leo ndiyo tunamaliza, Serikali inakwisha, muda wa uongozi umekwisha, tunakwenda kwenye uchaguzi. Hii siyo sawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wamezungumza kuhusu shilingi milioni 50, mtu anapiga kelele anasema mliwaahidi Watanzania shilingi milioni 50, ziko wapi? Kwanza nikubaliane kabisa na dada yangu Mheshimiwa Gekul. Tunapoahidi vitu, Serikali iliyopo madarakani iliahidi vitu vingi, kila kitu kinafanyika kulingana na nafasi na wakati ambao tunao. Hizo shilingi milioni 50 za kwenye vijiji, yako mambo yamefanyika makubwa kwenye maeneo ya watu wetu na yanayogusa maisha ya Watanzania, tofauti hata na hiyo shilingi milioni 50 ingekwenda moja kwa moja kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Serikali, tumefanya vizuri kwenye maboma ya shule za sekondari na za msingi, tupeleke na huo moyo kwenye zahanati kwenye vijiji ambavyo watu wetu wapo. Wananchi wetu wanajitoa sana kwenye ujenzi wa zahanati, tumefanya vizuri kwenye maboma shule za sekondari na za msingi, hebu twende tukasaidie na kwenye zahanati. Huyo anayesema kwamba bajeti haigusi maisha ya watu, akaangalie maji, zahanati na barabara, atasema kama bajeti inagusa maisha ya watu au haigusi maisha ya watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri mambo machache kwa ajili ya kusaidia kuongeza mapato kwenye nchi yetu. Mheshimiwa Waziri wa Fedha unafahamu, inawezekana kabisa wakati mwingine kuongeza kodi kukakupunguzia idadi ya watu wanaoweza kuwa walipa kodi. Inawezekana kabisa kuongeza kodi kukakupunguzia idadi ya watumiaji wa huduma ambayo ingesaidia kupata kodi. Sasa naomba sana Mheshimiwa Waziri hili jambo tuliangalie vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, mimi nilikuwa naangalia tu barabarani mle, miaka michache iliyopita watu waliokuwa wanatumia magari ambayo yamesajiliwa kwa majina yao, ninavyoona kama idadi ile inapungua. Ukiangalia vizuri, inawezekana imesababishwa na kuongezeka kwa kodi ile, lakini kodi ile ingekuwa angalau kwenye kiwango kizuri, ni rahisi kupata watu wengi zaidi na kupata kodi nyingi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili lipo pia kwenye Sports betting. Tunachukua kodi kule, wale waendeshaji wanalipa asilimia 25 ya mapato ghafi wanayopata, lakini na yule mtu ambaye anashinda kwenye ile zawadi anayopata analipa asilimia 20. Wako watu ambao kwa kuona kwamba wanalipa kodi, wengine wameamua kuacha hizo, wameamua kufanya za online, inasababisha kwenda kukosa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshauri Mheshimiwa Waziri, tuangalie namna ya kupunguza kodi hasa kwa wale ambao wanashinda ili ku-encourage watu wengi zaidi waweze kushiriki ili kutengeneza kodi zaidi kwa wale wanaoendesha lakini pia wanalipa kodi kwenye huduma nyingine kama wakifanya matangazo wanatoa ajira kwa watu wetu na vitu vingine vya namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye upande wa utalii. Juzi hapa tumefanya mnada wa vitalu. Katika vitalu 26 naambiwa tumefanikiwa kuuza vitatu saba. Hii imechangiwa sana na ongezeko la gharama za kununua vile vitalu. Naiomba Serikali, vitalu hivi vikikaa kwa muda mrefu bila kuwa na watu waliovichukua tunapata hasara sisi kama Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati yako ya Bunge, Ardhi Maliasili na Utalii. Tuliishauri sana Serikali, tunaweza tukaweka makadirio yetu lakini tusiyatangaze, lakini pia tusiwe rigid kwenye hayo makadirio ambayo tumeyaweka, lakini pia tusiongeze sana ili kuweza kusaidia watu wengi waweze kujitokeza na kuja kuomba kununua vitalu ili tufanye biashara na Serikali iweze kupata fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kwenye upande wa utalii ni kwenye hoteli. Miaka ya nyuma Serikali yetu iliamua kubinafsisha baadhi ya hoteli. Ziko baadhi ya hoteli nyingine ambazo ziko chini ya Serikali pia ziliuzwa. Watu waliobinafsishiwa hoteli hizi, ukienda vizuri, hoteli nyingi zilizobinafsishwa hazifanyi kazi vizuri na kwa kutokufanya kazi vizuri hazitengenezi vizuri ajira, hazitengenezi vizuri mapato kwa maana ya kulipa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunahangaika sana kukuza utalii na utalii ni eneo ambalo tunaweza kutusaidia kama Taifa kupata fedha nyingi, lakini tunakuza utalii, lakini ili tuwaalike watalii wengi zaidi waweze kuja kwenye nchi yetu, wakati huo huo miundombinu tuliyokuwa nayo haiendani na hii kasi ya uingizaji wa watalii kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye nchi yetu ukilinganisha vitanda ambavyo tunavyo vinavyoweza kulipiwa kodi, ukilinganisha na nchi jirani za wenzetu, sisi bado tuko nyuma sana. Tungeweza kutatua tatizo hili kwa kwenda kuziboresha hoteli ambazo ziko ndani ya nchi yetu. Cha kusikitisha zaidi, ziko hoteli ambazo tulizibinafsisha, watu wakachukua zile hoteli, wakachukua mikopo, wakafungua biashara nyingine za namna ile kama hoteli na wakafanya kazi na wanafanya kazi vizuri. Zao zinakwenda vizuri, walizobinafsishiwa na Serikali haziendi vizuri. Naishauri sana Serikali, tuna jambo la kuangalia hapa. Tuangalie namna ya kuboresha hizi huduma za hoteli ili tuweze kuwasaidia watu wetu, tuweze kusaidia nchi yetu kuweza kupata mapato zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakubaliana kwamba kilimo ni miongoni mwa maeneo muhimu katika kutafuta malighali kwa ajili ya viwanda vyetu. Naiomba sana Serikali, tuendelee kuweka mkazo kwenye kilimo, hasa kilimo cha umwagiliaji ili kuhakikisha kwamba watu wetu wanazalisha zaidi na wapate soko la kuweza kulisha viwanda vyetu na waweze kupata fedha, lakini pia viwanda viweze kwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kule Korogwe tunalo bonde ambalo likitengenezwa mradi wa umwagiliaji, tunaweza kulima hekta 5,000. Kwa karne tuliyonayo hekta 5,000 ni eneo kubwa sana. Ukiwa na wananchi 5,000 wamejiingiza kwenye kilimo cha uhakika wanaweza kulima kwa zaidi ya mara mbili kwa mwaka mmoja. Ni kuwa na misimu ya kilimo zaidi ya miwili kwa mwaka mmoja. Ni jambo kubwa sana. Tunatengeneza uchumi mzuri kwa ajili ya maisha ya watu wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilisema nichangie hayo machache kuishauri Serikali namna ya kuongeza mpato, kubwa nasema bajeti hii ni nzuri, bajeti hii inafaa, bajeti hii inagusa maisha ya wananchi wetu moja kwa moja, watu wamepiga kelele tulikuwa tunaomba sana tozo zipunguzwe tusiwe na mtiririko wa kodi na ndiyo spirit ya Mheshimiwa Rais, bajeti hii iliyowasilishwa inajibu hoja hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono bajeti hii. Ahsante sana. (Makofi)
Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya Eneo la Pori la Akiba Kigosi Kuwa Hifadhi ya Taifa Kigosi pamoja na Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji wa Hadhi Sehemu ya Eneo la Pori la Akiba la Igalla Kuwa Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki (Minamata Convention on Mercury)
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru sana kunipa nafasi niweze kuchangia na kwa ujumla mambo mengi yameshazungumzwa na Wabunge wengine waliochangia, lakini nitumie nafasi hii kwanza kabisa kusema naunga mkono maazimio yote yaliyoletwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuunga mkono maazimio yaliyoletwa na Serikali, pia nitumie nafasi hii kuipongeza sana Serikali kwa kazi kubwa wanayoifanya hasa watu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ulinzi mkubwa wa rasilimali zetu, hata ongezeko la tembo mpaka wanakuja kwenye makazi ya watu sasa hivi ni matokeo ya kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya kazi kubwa mliyoifanya ya kuhifadhi na tembo wamekuwa wengi basi mtusaidie kwenye yale maeneo kama kule Korogwe tumeathiriwa sana na tembo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaunga mkono, nichangie kwa upande wa maazimio haya mawili ya kubadilisha hadhi Mapori ya Akiba ya Ugalla na Kigosi kuwa Hifadhi za Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ziko faida nyingi sana kupandisha hadhi mapori haya na tunajua kwamba Hifadhi ya Taifa ni hatua ya juu kabisa ya uhifadhi kwa maana kwenye Hifadhi ya Taifa haturuhusu shughuli nyingine za kibinadamu, kwa hiyo kwa mapori haya kupandishwa hadhi kuwa Hifadhi ya Taifa tutakuwa tumeimarisha ulinzi wa rasilimali zetu, ikiwemo wanyama na baionuwai nyingine kwenye maeneo haya ya mapori.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaipongeza sana Wizara na tunaunga mkono azimio hili kwa sababu ni jitihada za kwenda kuongeza na kuimarisha ulinzi wa rasilimali zetu, lakini pia iko faida nyingine ya kupandisha hadhi mapori haya na kuwa Hifadhi ya Taifa. Faida nyingine kubwa ni kwenda kusaidia kuongeza mchango kwenye Pato la Taifa, lakini pia kwenda kugusa maisha ya watu wetu, hasa kwenye maeneo ambayo yanapakana na hifadhi hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo nyuma tulikuwa tunapiga kelele kidogo baadhi ya watu kwenye mambo kama ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Chato, sasa kwa kazi kubwa inayofanywa na Serikali sasa hivi ya kuimarisha miundombinu kama ujenzi wa viwanja wa ndege, kama reli ya SGR, kama ujenzi wa barabara, lakini pia kufufuliwa kwa shirika letu la ndege ni sehemu ya kutusaidia kwenda kuongeza pato kwa maana inakwenda kuchocheo utalii kwenye hifadhi hizi ambazo zitakwenda kuanzishwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi naunga mkono maazimio hayo, lakini naomba nishauri kwenye maeneo mawili, TANAPA ina hifadhi 19 na jambo hili limesemwa sana na tunaomba tuliweke msisitizo kidogo, tukichukua azimio tulilopitisha jana na haya mawili ya leo na yakienda kupita na hifadhi hizi zikianzishwa tutakuwa na jumla ya hifadhi 22 na hifadhi zinazoweza kujiendesha ni hifadhi tano. Kwa hiyo, unaweza ukaona huo mzigo wa kuendesha hifadhi nyingine ulivyokuwa mkubwa kwa TANAPA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yale majibu mazuri sana ya kitaalamu aliyoyatoa Mheshimiwa Waziri wa Maliasili jana, lakini tunaomba tushauri vitu viwili, kitu cha kwanza, ni lazima Wizara iisimamie TANAPA vizuri na iwaelekeze waongeze Mkakati madhubuti wa kutangaza masoko ili kusaidia hifadhi hizi mpya zinazoanzishwa tusichukue muda mrefu sana zikaendelea kuwa tegemezi, ziweze kuanza kuingiza mapato vizuri na ziweze kuweza kujiendesha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili ni kwenye mzigo wa kodi, lilisemwa jana, lakini hata mama yangu Mheshimiwa Lulida amelizungumza hapa. TANAPA wanalipa kodi nyingi, TANAPA wanalipa asilimia 15 wanatoa asilimia 15 ya gawio kwenda Serikalini, malipo ya asilimia tatu kwenda kwenye tourism development levy, wanalipa skills development levy, lakini pia wanalipa cooperate tax, lakini hayo yote siyo shida ile miradi wanayofanya kwa ajili ya kusaidia jamii ambazo zinapakana na Hifadhi za Taifa na yenyewe inakuwa inatozwa kodi kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimuombe sana Mheshimiwa Waziri tunaunga mkono azimio hili, ni azimio zuri litatusaidia kuimarisha maliasili zetu, litatusaidia kuongeza pato la Taifa lakini...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: ...salama nipongeze mkakati wa kuweza kutangaza vivutio vyetu ili waongeze utalii kwenye maeneo yetu, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri, lakini na kazi wanayoifanya yeye na Manaibu Waziri.

Mheshimiwa Spika, nina mambo machache sana leo ya kuzungumza, mambo kama mawili tu. Jambo la kwanza ningeomba kuchangia kwenye kilimo cha mkonge, kwa mwaka 2014 - 2018 kwenye mkonge tumezalisha tani 190,649. Katika hizo Mkoa wa Tanga peke yake umezalisha tani 106,221 na katika Mkoa wa Tanga Wilaya inayoongoza kwa kuzalisha mkonge ni Wilaya ya Korogwe hasa Halmashauri ya Korogwe. Hata hivyo, tumekuwa na changamoto kadhaa kwenye zao la mkonge, changamoto kubwa ya kwanza ni usimamizi usioridhisha wa taasisi inayosimamia zao la mkonge. Pia ushiriki mdogo wa taasisi zetu za utafiti kama ile ya pale Mlingano kwenye kusaidia kuendeleza zao la mkonge.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tumekuwa na wakulima wadogo wengi kule Korogwe na Mkoa mzima wa Tanga, lakini tuna changamoto kubwa sana. Wakulima walio wengi hata mbegu wanaokota kutoka kwenye mashamba ya mkonge ya muda mrefu kwenda kupanda kwenye mashamba yao. Mbegu hizi zinafanya mkonge huu usiweze kuwa na muda mrefu wa kuvunwa lakini tungeweza kuvitumia vizuri vyuo vyetu vya utafiti na taasisi za utafiti kama pale Mlingano tungeweza kuwa na mbegu bora na wakulima wetu wangelima na wangeweza kuvuna mkonge kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, inawezekana changamoto kubwa inayotusumbua ni fedha. Kwenye zao la mkonge kwa miaka mingi tunapata service levy ya 0.3%, lakini kwa mujibu ya Sheria ya Fedha kwenye mazao haya ya biashara tunapaswa pia kuwa na ushuru wa mazao produce cess lakini kwa mujibu wa Sheria ya Fedha produce cess anayepaswa kuilipa ni mnunuzi.

Mheshimiwa Spika, sasa wakulima hawa wakubwa wa mikonge ambao wanazalisha singa wenyewe mnunuzi wanamkuta nje, ambapo kule nje wanamkuta wakala hakuna nani ambao; kwa hiyo ni vigumu sana kupata produce casse wanapoleka mkonge kule nje; na hata halmashauri zetu zimekuwa zikikosa sana mapato kwa sababu hii.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia vizuri kama tungekuwa tunapata produce cess 2014 mpaka 2018 tungepata zaidi ya bilioni tisa kwenye produce cess peke yake. Kwenye service levy tumepata takriban shilingi milioni sita na kitu. Nilikuwa naiomba sana Serikali tuangalie namna, hapa hatuombi kuibua kodi mpya, hii kodi ipo kwa mujibu wa sharia. Changamoto tuliyonayo ni namna ya kupata fedha hizi; kwa sababu mnunuzi anayepaswa kulipwa yuko nje ya nchi na hajumo ndani ya nchi.

Mheshimiwa Spika, tuna mfumo mpya sasa hivi; na ninampongeza sana Mheshimiwa Mkuu wetu wa Mkoa wa Tanga, ametusadia sana na ametusaidia kupata haki na faida kwa wakulima wadogo wa mkonge. Tuna wakulima wadogo wa mkonge ambao wanauza mazao yao ya mkonge kupitia vyama vyao vya ushirika na mnunuzi anapatikana kwa kushindanishwa kwenye mnada. Sasa tunapopata mnunuzi anayeshindanishwa kwenye mnada ananunua mazao ya wakulima hawa wadogo wa mkonge yule mnunuzi analipa produce cess kwa sababu yeye anakuja kununua ndani; lakini hawa wakulima wakubwa wanaopeleka nje hawalipi, hatimaye hii ita-discourage hawa wanunuzi wanaokuja kununua mazao ya wakulima wadogo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mnzava.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara ya Elimu kwa kazi kubwa wanayoifanya. Elimu; iko haja ya kuangalia au kupitia upya mitaala yetu na Sera ya Elimu ili kuwaandaa wanafunzi kwa level mbalimbali kujiajiri na sio tu kutegemea kuajiriwa, elimu ya stadi za maisha iwekewe mkazo zaidi. Katika maeneo mengi mwananchi wamejitahidi kujenga mabomba kwa ajili ya madarasa na maabara, Serikali iangalie namna ya kuwasaidia wananchi hawa kumalizia majengo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukarabati wa shule kongwe. Serikali imefanya ukarabati wa shule kongwe za sekondari, zipo shule za msingi kongwe na zenye hali mbaya zinahitaji ukarabati mfano kwenye Jimbo la Korogwe vijijini ipo Shule ya Msingi ya Madela Ratuba, shule hii ilijengwa mwaka 1952 na haijafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu. Niombee Wizara isaidie ukarabati wa shule hii pia ipo Shule ya Msingi Ng’anzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya ufundi; naiomba Serikai imaarishe elimu ya ufundi. Kwenye Jimbo la Korogwe Vijijini tuna Chuo cha Ufundi Mnyuzi, chuo hiki kikipanuliwa, kikapewa vitendea kazi na kuongeza aina ya course zinazotolewa kitasaidia sana wanafunzi wanaoshindwa kuendelea na masomo kwa mfumo wa elimu ya shule. Chuo hiki kinaweza kusaidia wanafunzi wengi sana wa Wilaya za Korogwe, Lushoto, Muheza na hata Handeni. Naomba sana Wizara itusaidie kuboresha, kupanua na kuimarisha chuo hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Mikopo; bado kuna manung’uniko ya baadhi ya Watanzania maskini kukosa mikopo kwa ajili ya kugharamia elimu ya juu. Ni vyema Bodi ya Mikopo ikaangalia hili lakini pia tayari kufanya marekebisho hata katikati ya masomo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kama kijana wa Kitanzania kiongozi nasimama kwa uchungu sana kwa yanayoendelea ndani ya Bunge letu. Tunapofanya siasa na kuchafua sura ya Taifa letu badala ya kulitetea na kuliweka vizuri Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, muda ni mchache, nizungumze mambo machache. Jambo la kwanza nizungumze nafasi ya haki za binadamu kwenye mahusiano ya Kimataifa. Nakubaliana kabisa kwamba haki za binadamu zina nafasi kubwa kutuweka kama Taifa kwenye sura nzuri kwenye ulimwengu huu, kwenye mahusiano yetu na nchi nyingine na Mataifa mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu ambacho tunasahau, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache sana ambazo zinatii na kufuata haki za binadamu. Ni miongoni mwa nchi chache sana ambazo haki za binadamu hazitajwi tu, tumeziweka kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sura ya Kwanza, sehemu ya tatu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika…

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Taarifa.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi ya hayo…

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Taarifa.

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Kwenye nchi yetu tunazo sheria zilizotuwekea utaratibu, tunayo institutional and legal framework ya namna… (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, muda hautoshi.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Hakuna mtu ametoa taarifa, Mheshimiwa Salome naomba unyamaze. Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa naomba ukae nimeshasimama, naomba ukae. Waheshimiwa Wabunge tujifunze kuheshimu mamlaka…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Nasema hivyo kwa sababu, nisikilizeni. Mheshimiwa Susan Lyimo amechangia dakika zake tano hakuna mtu nimemruhusu kusimama, Mheshimiwa Lulida amechangia hakuna mtu amesimama na huyu mchangiaji wa CCM atachangia bila mtu kusimama. Mheshimiwa Timotheo Mzava. (Makofi)

MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa hoja yangu ni hii, kwamba kwenye nchi yetu tunayo Katiba na tunazo Sheria za Haki za Binadamu na namna ambavyo mtu atakuwa anahisi haki za binadamu zimevunjwa, aende kwenye vyombo vya sheria kwenda kufuata haki hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kushauri vitu viwili; cha kwanza niishauri Serikali. Niiombe Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje semeni juu ya haya mambo, tusiache watu wakachafua nchi yetu. Mheshimiwa Kabudi ameenda Geneva, ametoa taarifa nzuri na amesifiwa lakini huku ndani watu hawajui.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili nataka kushauri, kwa kuwa tunayo legal na institutional framework ya namna ya ku-deal na mambo ya haki za binadamu, niwashauri wenzangu, Watanzania wote twende kwa namna hiyo, tuache kuzunguka kwenye maofisi huko mara kwenye Mabalozi, tunao utaratibu wa kisheria na kikatiba wa namna ya ku-deal na vitu vya namna hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze jambo la pili kwenye diplomasia ya uchumi. Diplomasia ya uchumi ni dhana pana na inawezekana tunapata shida sana kuielewa, niwapongeze sana Mabalozi wa nchi yetu ambao wanatuwakilisha kule nchi. Balozi wetu wa China, Balozi wa Urusi wanafanya kazi kubwa, matokeo tunayoyaona kwenye utalii sasa hivi ni matokeo ya kazi kubwa wanayoifanya kwenye diplomasia ya uchumi. Hata kitendo cha Zimbabwe kukubali tupeleke mahindi tani zaidi ya 700,000 kwenye ziara ya Mheshimiwa Rais ni matokeo ya diplomasia ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wasichoelewa ni kitu kimoja, Sera yetu ya Mambo ya Nje, Toleo la Mwaka 2001 imejisimika kwenye diplomasia ya uchumi, lakini haina maana kwamba kwa sababu ya diplomasia ya kiuchumi tumeacha vitu vingine na hata sera ile imesisitiza kwamba tunaendelea kuimarisha misingi na kanuni za sera yetu ya asili ile ya mwanzo ambayo ilitokana na Serikali ya Awamu ya Kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa kanuni za kwenye Sera yetu ya asili ya Mambo ya Nchi za Nje pamoja na kwamba ilikuwa ni kwa ajili ya kuangalia ukombozi wa nchi nyingine, ilikuwa ni kulinda uhuru wa Taifa hili. Kuja kwa sheria za kwenye Sekta ya Madini, mabadiliko tuliyoyafanya ni ishara ya kulinda uhuru wa Taifa kwenda kutafsiri diplomasia ya uchumi ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri tu Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje iendelee kutoa ushirikiano mkubwa kwenye mikataba na Mataifa mengine, kwenye mikataba ya wawekezaji ili katika kufanyia kazi mambo hayo, tujitahidi kuhakikisha kwamba na zile dhana zote zinazohusiana na mambo ya diplomasia na uhusiano wa mambo ya nje zinazingatiwa vizuri kwa kuondoa mikwaruzano na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze sana Serikali, tangu 2015 mpaka sasa tumeanzisha Balozi zaidi ya saba, mpaka juzi tumeanzisha Balozi nyingine ya Cuba. Kukubaliwa kuanzisha balozi kwenye nchi nyingine, yenyewe ni ishara kwamba tuna mahusiano mazuri na nchi nyingine. Hii dhana inayojengwa kwamba tuna mahusiano mabaya, watu wanatupotosha. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sana Serikali, waendelee kusimamia mahusiano na nchi nyingine, waendelee kusimamia diplomasia ya Tanzania kwenye Mataifa mengine. Sisi tunamwamini Mheshimiwa Profesa Kabudi, Mheshimiwa Dkt. Ndumbaro na tunamwamini Mheshimiwa Rais, wafanye kazi kwa niaba ya Watanzania, nchi yetu ipate sura nzuri mbele ya ulimwengu na dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Nitumie nafasi hii kwanza kabisa kumshukuru Mungu lakini pia kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Naibu Waziri na Watendaji wao Wizarani wanafanya kazi kubwa, wanafanya kazi nzuri sana hongera sana kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja kwa mujibu wa tafiti mbalimbali duniani moja ya njia bora kabisa ya kuondoa kama sio kupunguza migogoro ya ardhi ni kupima na kupanga matumizi bora ya ardhi. Hii ndio moja ya njia bora kabisa pamoja na kwamba tunakubaliana kwamba kwa mujibu wa sheria zetu Planning Authority ni kule kwenye Serikali za Mitaa, lakini Wizara ndio yenye jukumu la kusimamia kutekeleza sera kwenye Sekta ya Ardhi. Naomba sana pamoja na changamoto za kifedha na za kibajeti watutafutie mkakati maalum wa kupima na kupanga maeneo yetu. Tume ya Mipango ya Ardhi inafanya kazi nzuri, lakini bado uwezo wake ni mdogo na imebaki kuwa kama waratibu tu.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kwenye mashamba yasiyoendelezwa. Nitumie nafasi hii kwa dhati kabisa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, tangu ameingia amefanya kazi ya kufuta hati za mashamba ya baadhi ya wawekezaji ambao hawayaendelezi vizuri na hata kule kwetu Korogwe, hili pia limefanyika pamoja na maboresho yaliyofanyika kwenye mashamba yale sita ambayo yalifutwa, bado alichokifanya Mheshimiwa Rais kinawasaidia sana watu wetu na sisi watu wa Korogwe tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, ninayo mashamba mengine kule na nimeshamwambia Mheshimiwa Waziri zaidi ya mara moja na namwamini sana baba yangu na naikubali sana kazi yake, kama pale Wizarani kuna watu wanakwamisha yasifike kwa Mheshimiwa Waziri hebu aingie ndani aangalie kuna nini huko, kuna shamba la pale Mwakinyumbi, Hale. Nimekuja juzi kwenye Bunge lakini hii nazungumza ni mara ya tatu kama sikosei.

Mheshimiwa Spika, kuna shamba linaitwa Kwashemshi, kuna mwekezaji anasema yeye ni mwekezaji wa Mkonge, anakodisha kwa watu wengine, miaka miwili iliyopita alikuwa anakodisha kwa wananchi walime mahindi kule ndani kwa sababu eneo kubwa halijalimwa mkonge. Mwaka huu ameamua mpaka na kuwafukuza wananchi amechukua mtu binafsi amekuja analima mahindi kwenye shamba hilo, wananchi hawana maeneo.

Mheshimiwa Spika, mimi ni muumini ambaye naamini kabisa sio sawasawa kila ardhi ya mwekezaji tukaichukua tukagawa kwa wananchi, hatuwezi kuwa nchi ya namna hiyo, lakini lazima tukubaliane kama mtu amepewa ardhi haitumii kwa mujibu wa masharti aliyokabidhiwa masharti yake ya umiliki, wahukue hatua. Hili suala nimelisema muda mrefu, namwomba sana Mheshimiwa Waziri aingie, najua kwake mara naambiwa halijafika, mara limefika likarudi, sielewi kinachoendelea hapo, hebu aangalie Mheshimiwa Waziri hapo kwenye Wizara, kuna mtu atakuwa anacheza na hivi vitu, kuna shamba linaitwa shamba la Mwakinyumbi.

Mheshimiwa Spika, huu ni mwaka sijui wa ngapi tunalalamika na hili jambo. Marehemu Profesa Majimarefu amepiga kelele sana humu ndani mpaka Mwenyezi Mungu amemchukua, hatujui kinachoendelea kwenye mashamba haya. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kwa unyenyekevu mkubwa na kwa kazi yake anayoiamini awasaidie watu wa Korogwe waweze kupata maeneo, lakini pia kazi zifanyike vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri jambo lingine hasa kwa niaba ya vijana wote lakini na Watanzania kwa ujumla, sasa ni wakati muafaka wa kuwa na sera ya nyumba. Ni wakati muafaka kama Taifa kuwa na sera ya nyumba, hebu Wizara walifanyie kazi hili jambo tuweze kufikia mahali pazuri.

Mheshimiwa Spika, yamesemwa hapa na nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi anayoifanya, ile kazi tuliyoikuta inafanyika Kilombero, Ulanga na Malinyi ilikuwa ni kazi nzuri sana nimpongeze yeye lakini niipongeze na ile timu iliyokuwa inasimamia ule mradi. Mheshimiwa Waziri kwenda kugawa hati ni sehemu ya namna ya kusadia kutatua changamoto za migogoro ya ardhi kwa watu wetu, hakuna kosa. Korogwe pia tukipima tutamwita Wziri aje atugawie hati na sisi tutapokea.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri anafanya kazi nzuri, sina maneno mengi, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Wizara ya Afya kwa juhudi inazofanya za kuboresha Sekta ya Afya nchini. Katika Jimbo la Korogwe lenye tarafa tatu na kila tarafa ikiwa na kituo cha afya, tuna gari moja tu la kubebea wagonjwa. Gari ambalo na lenyewe limechakaa sana maana ni la muda mrefu, naiomba sana Wizara kwa unyenyekevu mkubwa watusaidie tupate gari la wagonjwa maana vituo vya afya viko mbali na hospitali.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulipokea fedha za ujenzi wa Kituo cha Afya kipya katika Kata za Mkumbara, kituo kimekamilika. Tunaiomba Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI kutupatia vifaa ili kituo hiki kianze kufanya kazi ya kutoa huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu wa watumishi katika Wilaya ya Korogwe kwa zaidi ya 46%; tunaiomba Wizara kusaidia upatikanaji wa watumishi hawa ili kuboresha huduma za afya wilayani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha na kuratibu vizuri huduma za wazee, ni vyema Serikali ikaandaa Sheria ya Wazee kama ilivyo kwa watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, viko vituo vya afya vya muda mrefu kama Kituo cha Afya cha Magoma na Bungu ambavyo vinahitaji ukarabati na upanuzi. Pamoja na uhitaji wa ukarabati na upanuzi, pia vifaa kama vitanda vimechakaa sana vinahitaji kubadilishwa kama siyo kuongezwa. Naiomba Wizara ianzishe utaratibu wa kuongeza vifaa kwenye vituo vya afya kwa awamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ustawi wa Jamii; viko vituo vya kulelea watoto/makao ya watoto ambavyo havina hadhi ya kuwa makao ya watoto na vingine vinatuhumiwa kwa kashfa mbalimbali kama unyanyasaji na ukatili wa kijinsia na Maafisa Ustawi walioko wilayani baadhi yao siyo waaminifu, ni vyema Wizara iimarishe utaratibu wa ukaguzi wa makao ya watoto.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nami nitumie nafasi hii kukishukuru sana Chama changu cha Mapinduzi na wananchi wa Jimbo la Korogwe Vijijini kwa kura nyingi na za heshima walizotoa kwa chama chetu na kuniwezesha nami kuwa mwakilishi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma vizuri mapendekezo ya Mpango, nimesoma vizuri mpango huu, naipongeza Serikali kwa kazi kubwa na hatua kubwa ambayo tumepiga mpaka sasa. Ila nilipokuwa nasoma Mapendekezo ya Mpango huu wa Awamu ya Tatu kwenye ukurasa wa 87 nimekutana na vipaumbele pale viko vitano. Ukisoma kuanzia kipaumbele cha kwanza, cha pili na cha tatu, huoni namna ambavyo unaweza ukaikwepa sekta ya kilimo kwenye kuendeleza na kukuza uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri sana Serikali, kwenye suala la kilimo, tunayo mambo mengi sana ya kufanya na mengi yameshazungumzwa, mimi naomba nizungumzie sana eneo la soko. Ni lazima Serikali ijitahidi kuweka uhakika wa masoko kwa wakulima wetu wanaolima kwenye nchi yetu hii. Tukiweka uhakika wa masoko tutasaidia viwanda vyetu, tutatengeneza ajira, tutaongeza pato kwa wale wakulima wanaolima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tulikuwa tunamwuliza Waziri Mkuu kuhusu mkakati tulionao kwenye mazao ya kimkakati, nikatoa mfano wa zao la mkonge. Wananchi wameitikia na wanalima sana, lakini tusipokuwa na uhakika wa soko kwa ajili ya mazao haya, mwisho wa siku wananchi watakuja kuishia kupata hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya njia ya kuweka uhakika wa soko ni kutengeneza viwanda na kushawishi wawekezaji kuwekeza kwenye sekta ya viwanda. Tunavyo viwanda kwa mfano kwenye zao la mkonge, tulikuwa na viwanda vya magunia, sasa hivi havifanyi kazi vizuri. Asubuhi kuna mtu amezungumza hapa kwamba wale wawekezaji ikiwezekana wanyang’anywe lakini ni lazima tujiulize hivi viwanda vya magunia vilikwama wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya magunia ni makubwa sana, lakini uzalishaji wa magunia ni mdogo, kwa nini? Ni gharama za uzalishaji. Siyo hivyo tu, pia magunia yetu yanakumbana na ushindani kutoka kwenye magunia yanayozalishwa kwa kutumia mazao mengine na bidhaa nyingine kama jute. Ukiangalia India na Bangladesh, wao wana subsidy kwenye jute na wanajitahidi sana kuwekea mfumo mzuri wa kununua mazao yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia East Africa Community, Sheria za Ushuru wa Forodha zinatoa nafuu ya kodi kwa bidhaa ambazo zinaingia kwa ajili ya kuchukua mazao na kutoa bidhaa na kuzipeleka nje kwa ajili ya ku-export. Haya yote ukiangalia yanafanya magunia ya jute yanakuwa na bei rahisi wakati magunia yanayozalishwa na mkonge yanakuwa na bei kubwa. Ukienda kwenye ushindani hatuwezi kupata faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze jambo linguine, tumejiwekea malengo, tumepiga hatua kidogo kwenye umwagiliaji na tumejiwekea malengo mpaka 2025 tufike hekta 1,200,000. Naiomba Serikali, lazima tuangalie miradi mikubwa ya umwagiliaji itakayotusaidia kuweza kuhudumia eneo kubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo tulikuwa nao Tanga, Bwawa la Mkomazi, mradi mmoja tu una uwezo wa kuhudumia hekta zaidi ya 6,000, lakini kwa zaidi ya miaka 10 wananchi wamekaa na matumaini wanasubiria miradi hiyo haitekelezwi. Naomba tuweke nguvu kwenye maeneo ya namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni la miundombinu. Kilimo kinafanyika vijijini, lakini miundombinu ni mibovu sana. Leo tunasema tuongeze uzalishaji kwa kuongeza maeneo ya kulima, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo na Waziri wa Kilimo wanajua, kwenye chai peke yake kwa mwaka, zaidi ya kilo milioni nne tunazipoteza, zinachelewa kufika kiwandani kwa sababu ya miundominu na zinapotea. Thamani yake ni karibu shilingi bilioni 2.8 kwa sababu ya miundombinu. Naungana na Mheshimiwa Nditiye, tunahitaji kuwa na nguvu na mkakati wa ziada kwenye suala la miundombinu, kutafuta fedha kuiongezea TARURA ili wananchi wetu wapate uhakika wa kupeleka mazao kwenye masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, mkonge; pamoja na mchango wangu wa kuzungumza naomba nishauri Serikali kwa Wizara ya Kilimo na Fedha kukaa pamoja ili kuweka kwenye Finance Bill kipengele cha namna ya kutoza produce cess kwa wakulima wote wakubwa wanaosafirisha nje mkonge ili tusiwavunje moyo wanunuzi wanaokuja kununua mkonge wa wakulima wadogo. Pia fedha hizi zitasaidia utatuzi wa changamoto za zao la mkonge.

Mheshimiwa Spika, chai; kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa pembejeo kwenye zao la chai. Jambo linalowalazimisha wakulima kukopa pembejeo kwa wenye viwanda na kuwaathiri kwenye bei. Ushirika katika chai uimarishwe , pia tuanzishe soko au mnada wa chai hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, umwagiliaji; ili kuwaondoa katika umaskini wananchi wa kata 10 za Tarafa ya Mombo ni kutekeleza Mradi wa Umwagiliaji wa Bonde la Mto Mkomazi. Bwawa linaloweza kusaidia kilimo cha umwagiliaji kwenye hekta zaidi ya 5,000.

Mheshimiwa Spika, Bodi ya Mkonge, kumekuwa na udhaifu mkubwa wa usimamizi wa mkonge kwa sababu ya uwezo mdogo wa Bodi ya Mkonge. Nashauri bodi iangaliwe upya. Pia Serikali ifuatilie utaratibu uliotumika kutoa mashamba ya mkonge. Pia namna mali za Bodi ya Mkonge zilivyouzwa au kugawanywa ili kujua Bodi ilikuwa na mali gani, zimekwenda wapi na kwa utaratibu upi?
Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nipate fursa ya kuchangia maazimio haya mawili yaliyoletwa mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa nami niungane na wenzangu kutoa pole kwa Mheshimiwa Rais na Watanzania kwa ujumla kwa msiba mzito ambao ulitufika kama taifa wa kuondokewa na mpendwa wetu Dkt. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, maazimio haya yamekuja kwa wakati sahihi na ni jambo sahihi na ni jambo muhimu na kubwa sana kufanywa na Bunge lako Tukufu. Katika miaka sita ambayo Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amehudumu kama Rais wa nchi hii amefanya mambo makubwa, amefanya mabadiliko makubwa sana kwenye taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukisema tuanze kueleza kazi nzuri na njema alizofanya Dkt. Magufuli, hata muda huu haunitoshi kusema yote mazuri aliyoyafanya. Lakini kama Mbunge na kama Mbunge kijana, nianze kabisa kwa kutambua mchango na thamani kubwa ambayo Dkt. Magufuli aliitoa kwa vijana wa taifa hili kwa kuwateua kwenye nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya nchi yetu. Mheshimiwa Dkt. Magufuli aliwaamini sana vijana, aliwapa nafasi za kufanya kazi na kuitumikia nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika,inawezekana yako maeneo tumemuangusha kidogo lakini kwa sehemu kubwa vijana aliowateua walifanya kazi nzuri ya kumsaidia na kuleta uongozi kwenye taifa letu. Sisi kama vijana tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli kwa imani hiyo kubwa kwa vijana. Amewatengeneza watu wengi kuwa viongozi na kuweza kutoa mchango kwenye taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kubwa zaidi alilofanya Dkt. Magufuli ni kutusaidia kukamilisha ndoto kubwa tulizokuwa nazo kama taifa kwa miaka mingi. Kwa muda mrefu tumekuwa na ndoto ya kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi yetu lakini tulikuwa tukisuasua kwenye utekelezaji wa jambo hili. Dkt. Magufuli kwenye kipindi chake amesimama imara jambo hili limefanikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuishia kuhamishia tu makao makuu, alihakikisha kwamba Wizara za Serikali zinapata majengo mazuri na ya kudumu kwenye eneo la Dodoma ili Serikali iweze kufanya shughuli zake vizuri hapa Dodoma. Ni muhimu sana kuendelea kuenzi mchango huu. Pia amefanya kazi kubwa kwenye kusimamia rasilimali za taifa letu. Tulibadilisha sheria kwenye usimamizi wa madini na nchi yetu imeongeza thamani na imeongeza mapato kutoka kwenye rasilimali tulizokuwa nazo kama taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi nzuri alizofanya Dkt. Magufuli, lakini kwa mara ya kwanza kama kijana wa Kitanzania nimeona na kusuhudia kitu cha tofauti. Nimeona na kushuhudia baadhi ya watu wakifurahia kifo na kusema maneno yasiyokuwa mazuri. Kwa umri wangu mdogo, kwa nilivyolelewa kwa utamaduni wetu si jambo zuri sana kufurahia kifo cha mtu mwingine. Lakini pia si jambo zuri kukosoakosoa mtu akiwa ameshatangulia mbele ya haki. Ninawaomba Watanzania, Dkt. Magufuli ameifanya kazi yake vizuri, ameimaliza safari yake, amefunga kitabu chake. Tumpe heshima anayostahili, tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu amhifadhi mahali pema peponi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuondoka kwa Dkt. Magufuli tumempata mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kipekee kabla ya kumpongeza Mheshimiwa Samia ni lazima Watanzania tujipongeze kama taifa. Tumepita kwenye kipindi ambacho pengine kuna watu walikuwa wanatuangalia kama tutavuka salama au hatutavuka salama. Lakini leo tunapozungumza kwa uimara wa Katiba iliyotengenezwa na waasisi wa taifa letu, kwa uimara wa sisi Watanzania na kupendana kwetu, kwa uimara wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, kama taifa tunavuka salama na tunavuka vizuri. Tunayo sababu ya kujipongeza na kujivunia Watanzania, ni jambo kubwa ambalo tunaweza tukaliona kama ni jambo la kawaida, lakini ni jambo kubwa sana kuvuka kwenye kipindi kama hiki tukiwa salama na tukiwa tumeendelea kushikamana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kuendelea kumpongeza sana Mheshimiwa Samia kwa kupata nafasi ya kuwa Rais wa Nchi yetu. Mheshimiwa Samia ana uzoefu mkubwa kama ilivyosemwa na aliyewasilisha hoja ya Azimio la Kumpongeza. Ana uzoefu mkubwa kwenye kuongoza Serikali ya nchi yetu, ana uzoefu mkubwa kwa uongozi wa Serikali kwa pande zote mbili za Muungano, na hili ni jambo la kipekee na muhimu sana. Tunampongeza kwa kupata nafasi ya Urais. Tuna matumaini kwamba ataifanya kazi hii vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Samia ni mchapakazi. Kama wako watu ambao wanafikiri baada ya kuondoka kwa Dkt. Magufuli mambo yatalegalega, wanafikiri watapata nafasi ya kuja kuiibia na kuifisadi nchi yetu, kwa mama Samia nafasi hiyo haipo. Ni mama mwadilifu anayependa taifa lake, mama mzalendo anayeichukua rushwa na mchapakazi wa kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 15 ya mwezi Februari tulikuwa Korogwe kwenye ziara na Mheshimiwa mama Samia akiwa Makamu wa Rais. Tulikuwa na daraja linasumbua akiwa mama kwa muda mrefu, tulipomueleza akatoka palepale akafanya mawasiliano na Wizara na TARURA wakasema hawana fedha. Akawaambia hata kama hakuna fedha jengeni kivuko ambacho akina mama wanaokwenda kupata huduma za afya hawatateseka. Leo ninapozungumza mkandarasi yuko site ameshashusha vifaa na kazi inafanyika; ni ufuatiliaji wa mama Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema kwamba mama Samia Suluhu Hassan si mtenda miujiza. Kama ambavyo tumetoa ushirikiano kwa Dkt. Magufuli, nawaomba Watanzania tumuunge mkono Mheshimiwa Rais, nawaomba tumuombee, nawaomba tushirikiane naye ili mama huyu aweze kuifanya kazi vizuri aende mbali zaidi kuanzia pale alipotuacha Dkt. John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na ninaunga mkono maazimio yote mawili. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, hoteli zote zilizokuwa za Serikali zilizopewa, zilizokodishwa au zilizouzwa zifuatiliwe mikataba yake na utekelezaji wa mikataba kwa kuangalia hali za hoteli hizo na utendaji kazi wake kwani hoteli nyingi zinaonekana kuwa na hali mbaya na haziingizii faida Serikali na nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, TFS iendelee kuimarisha ushirikiano wake na jamii kwa kuondoa migogoro iliyopo kati yake ni vijiji kama kule Korogwe kwenye Hifadhi ya Nilo na Msitu wa Chang’andu, Kata ya Kwalukonge.

Mheshimiwa Naibu Spika, TFS na Wizara kuendelea kuacha kiwanda cha mazao ya misitu cha TAMISO CHIPBOARD ambacho bado kina mashine nzuri kimeendelea kuchezewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, utetezi wa TFS na Wizara kuwa kiwanda hicho kinaangaliwa na Msajili wa Hazina sio sawasawa kwani hata uanzishwaji wa kiwanda hiki ulikuwa maalum kwa ajili ya mazao ya misitu ya shamba la miti la Shume na Gologolo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuendelea kukitelekeza kiwanda hiki ni matumizi mabaya ya fedha za nchi na kufifisha nia na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na kazi nzuri ya kupambana na ujangili kumekuwa na ongezeko kubwa la tembo na wanyama wakali. Je, mamlaka zinazohusika zimejiandaaje kupambana na ongezeko hilo?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, naipongeza Wizara ya Nishati kwa kazi kubwa wanayofanya hasa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini (REA). Hata hivyo kasi ya utekelezaji wa mradi huu hasa kwenye Wilaya ya Karagwe na Jimbo la Korogwe Vijijini sio ya kuridhisha. Kwenye mradi huu kwenye Awamu III mzunguko wa kwanza Korogwe ilipangiwa vijiji 16 mpaka sasa umeme umewashwa kwenye vijiji saba tu.

Mheshimiwa Spika, tulileta maombi ya kupelekewa umeme kwenye vijiji 67 katika Mradi wa REA, awamu ya tatu, mzunguko wa kwanza. Ni vyema Wizara ituambie baada ya bajeti hii tutapata umeme kwenye vijiji hivyo vyote au hapana?

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na shida ya kuunganisha umeme kwa wakati, viko Vijiji vya Kulasi, Kibaoni na Mswaha Majengo vimesimikwa nguzo tangu mwaka 2018 mwezi Oktoba, lakini mpaka sasa umeme haujafika katika vijijji hivyo. Mkandarasi anasema tatizo ni tofauti ya transformer kati ya size inayotamkwa kwenye mkataba ambayo ni 33 kv na size ya line iliyopo ambayo ni 11 kv. Tofauti hii haijafanyiwa kazi muda mrefu na kusababisha malalamiko.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri alipofanya ziara Korogwe tarehe 19 Mei, 2019 alitoa maelekezo kuwa Kijiji cha Mahenge kipelekewe umeme. Umeme huo unatoka Kijiji cha Kerenge Kibaoni, Jimbo la Korogwe Vijijini lakini kuna vitongoji viwili vya Antakae na Mianzini vinapitiwa na umeme huo ukienda Mahenge. Naomba sana vijiji hivi visirukwe.