Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Eng. Christopher Kajoro Chizza (8 total)

MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Spika, kwanza niruhusu niipongeze Serikali kwa siku za karibuni imeongeza kiwango cha usimamizi wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara kutoka Nyakanazi kuelekea mpaka Kabingo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sasa barabara hiyo inajengwa na inaishia katika kijiji cha Kabingo; na kwa kuwa kipande cha kutoka Kabingo kwenda mpaka Kibondo, Kasulu hadi Kidahwe bado ni vumbi. Je, kwa muendelezo huohuo ambao Serikali imetuonyesha, ina mpango gani sasa kipande cha kutoka Kabingo kwenda Kibondo, Kasulu mpaka Kidahwe kiweze kutekelezwa ili Mkoa wa Kigoma uweze kufunguka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Chiza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, uniruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Chiza kwa kuchaguliwa na wananchi wa Buyungu kuwa Mbunge na Mwakilishi wao na namkaribisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na utaratibu wa kujenga barabara katika Mkoa wa Kigoma. Nafahamu na Mheshimiwa Chiza anafahamu pia kwamba barabara ya kutoka Nyakanazi kuja eneo lake ujenzi unaendelea, lakini utaratibu ule wa manunuzi unafanyika na hivi karibuni kilomita karibu 87 hivi zitaanza kujengwa zikipita katika eneo hili la Kabingo kama alivyolitaja. Pia kilomita zote 300, Serikali iko katika hatua nzuri ya kujenga kwa maana ya kutoka sasa upande wa Kakonko, Kibondo kwenda Kasulu na viunga vyake vinavyoenda kuunganisha nchi ya Burundi kwa maana ya Manyovu na kipande kile cha Mabamba.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hatua iliyofikiwa ni nzuri na kwa vile Mheshimiwa Mbunge yupo nafikiri itakuwa ni vizuri sasa tuzungumze ili angalau nikupe picha ili uweze kuona na kutimiza wajibu wako kama Mbunge wakati ukiwawakilisha wananchi wako kwamba Serikali imejipanga vizuri kujenga barabara hizi.
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Naishukuru pia Serikali kwa kututengea Sh.500,000,000 za kujenga kituo cha Afya cha Gwanumpu na nimetoka Jimboni kazi sasa imeanza, ahsanteni sana.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo sasa nina swali moja tu. Pamoja shukrani hizo, Mheshimiwa Waziri kwa kuwa anajua kabisa Ubunge wangu bado mbichi; sasa ananiahidi nini kwa awamu hii inayofuata; kwamba itaanza lini ili Kata za Kiziguzigu, Kasanda, Rugenge, Gwarama na Nyamtukuza nazo zipate fedha za kujenga vituo vya afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, kama ambavo tumeainisha kwenye ilani yetu ya CCM kwamba kila kata tutajenga kituo cha afya na kila Wilaya ambako hakuna Hospitali ya Wilaya tutaenda kujenga, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, miongoni mwa maeneo ambayo tutahakikisha yanajengwa vituo vya afya ni yale ambayo yana upungufu mkubwa ikiwa ni pamoja na Wilaya yake ya Kakonko.
Mheshimiwa Spika, naomba nimuhakikishie, hakika pale ambapo bajeti itaweza kupatikana ikaongezeka hatutawasahau Kakonko na hasa tukiwa tunajibu fadhira ambazo wananchi wa Kakonko na hasa Buyungu walitoa kwa Chama cha Mapinduzi.
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kuniona. Serikali imejenga miradi ya maji ya Kakonko mjini Gwanu, Mbuki, Dudu A, Nyagwijima, Mamuhange katika Wilaya ya Kakonko. Lakini miradi hii ambayo imetumia takribani shilingi bilioni mbili mingine haifanyikazi hata iliyokamilika haifanyikazi na mingine haijakamilika.

Mheshimiwa Spika, lakini namshukuru Mheshimiwa Waziri Mbarawa amesikia kilio chetu na amekuja, ameikagua miradi hii tarehe 26 Novemba. Sasa kwa kuwa Mheshimiwa Waziri alitoa maelekezo kwa ma-engineer ili wafanye usanifu pamoja na makadirio ya kuikarabati miradi hii kuokoa gharama iliyokwishatumika na akawaelekeza waweke utaratibu wa kubadilisha mfumo wa kusukuma maji kutoka Nishati ya mafuta kwenda nishati ya jua. Je, sasa shughuli hiyo imefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge. Lakini la pili nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wetu Mheshimiwa Mbarawa anafanyakazi kubwa sana na nzuri katika kuhakikisha tunamtua mwanamama ndoo kichwani. Sasa kwa yale ambayo aliyoagiza Mheshimiwa Waziri kwetu ni utekelezaji, tunamuagiza Katibu Mkuu aweze kutatua tatizo hilo kwa haraka ili wananchi wa Kigoma waweze kupata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, majibu yanaleta matumaini. Nina swali moja tu kwa Mheshimiwa Naibu Waziri; kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri Bunge lililopita aliniahidi yeye mwenyewe jua linawaka kwamba angefuatana na mimi kwenda kuwasaidia wananchi hawa ambao tayari wameanza kuchimba madini haya, lakini bahati mbaya mambo yakawa mengi.

Sasa kwa kuwa wananchi hawa wameanza kuchimba madini kwa kutumia nyenzo duni, utaalam duni na wakati mwingine hata hawajui uzito wala purity ya madini; je, sasa anawaahidi nini wananchi hawa ambao wameanza kuchimba madini ili waweze kutumia sasa fursa hii na fursa za masoko ya madini ambayo yamefunguliwa kama lile la Geita ambalo amezindua Waziri Mkuu juzi, anawaahidi nini hasa katika uwezeshaji waweze kufanya shughuli hii kwa ufanisi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Engineer Chiza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikubaliane na yeye kwamba nilimuahidi kweli nitakwenda Kigoma, hasa maeneo ya jimbo lake. Mimi tu nipende kusema kwamba nitashiriki naye, nitakwenda, tutakwenda hadi kwa wachimbaji, tutakwenda kufanya kazi na tutakwenda kuwaelimisha na kuwapa maelekezo ya Serikali yanavyostahili. Kwa hiyo kwa hilo mimi sina tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusiana na suala la wachimbaji wadogo. Kweli tuna matatizo makubwa sana ya kimitaji, teknolojia, maeneo, tafiti kwa wachimbaji wadogowadogo. Sisi kama Wizara ya Madini tumejipanga vizuri na tumeamua sasa hivi kupitia Geological Survey of Tanzania pamoja na STAMICO tutaendelea kufanya tafiti mbalimbali ambazo zitawasaidia wachimbaji wadogowadogo ili tuweze kuwapa yale maeneo ambayo tukiwapa tunakuwa na uhakika kwamba wataweza kupata madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ninapozungumza STAMICO tayari tumekwisha kununua rig machine ambayo inaweza kufanya kazi ya drilling kwa wachimbaji wadogo kwa gharama ndogo. Kwa hiyo tunawaomba wachimbaji wadogowadogo waje waombe maombi yao katika Wizara yetu tuwafanyie tafiti mbalimbali kwa gharama ndogo kwa sababu kufanya tafiti ni gharama kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tunaendelea kutoa elimu ya uchimbaji, uchenjuaji, na uwepo wa masoko haya ambalo Mheshimiwa Waziri Mkuu amelifungua kule Geita na lingine juzi nimekwenda kufungua pale Kahama na maeneo mengine, tunaendelea na mikoa yote ambayo inakwenda kufungua masoko ya madini. Tunakwenda kuhakikisha kwamba wachimbaji wadogo wanapata ile tija ambayo wanadhamiria kuipata tofauti na sasa hivi walikuwa wanakwenda kuuza katika masoko ya pembeni wanadhulumiwa, wanauza kwa bei ndogo, vilevile wanaibiwa. Sisi kama Wizara ya Madini tumejipanga kuwasaidia wachimbaji wadogowadogo kwa kuhakikisha kwamba wanapata tija. Ahsante sana.
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina kila sababu za kuishukuru Serikali si kwa majibu tu, lakini kwa utekelezaji wa vitendo. Kwa mfano katika Skimu ya Itumbiko, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Kakonko, Ndugu Masumbuko, ameshirikiana sana na wananchi na mimi mwenyewe na tayari maji yameanza sasa kuingia katika mfereji mkuu na banio limetengenezwa, lakini bado tunahitaji miundombinu mingine ikiwemo barabara za kutoa mazao mashambani zitengenezwe.

Pia nashukuru Tume ya Umwagiliaji imenipa taarifa kwamba, shilingi milioni 109 kutoka Food Aid Counterpart Fund zimepatikana kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Umwagiliaji wa Gwanumpu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa hiyo, nina swali moja tu la nyongeza; kwa kuwa, wakati tunaanzisha miradi hii ya Itumbiko na Gwanumpu kwenye package hiyo tulikuwa na Mradi wa Umwagiliaji wa Nyamtukuza ambao uko katika mpaka wa Wilaya ya Kakonko na Ngara na mradi huu ulitarajiwa kunufaisha Kata za Kumbuga katika Wilaya ya Ngara na Kata ya Nyamtukuza katika Wilaya ya Kakonko na tayari Serikali imeshaweka fedha nyingi, lakini mradi umetelekezwa hautekelezwi na sababu zinazotolewa hazitoshelezi kwa sababu ni zile za mabishano tu kwamba, nani autekeleze, ni Ngara au Kakonko? Ni Kagera au ni Kigoma? Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari sasa kuingilia kati ili mradi huu nao utengewe fedha ili utekelezwe na wananchi wa Ngara na wa Kakonko waweze kunufaika na mradi huu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Christopher Chiza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kwa niaba ya Serikali, tunampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi zake kutekeleza miradi hii. Alitenga fedha za Jimbo kwa ajili ya kushirikiana na wananchi wake kusaidiana na Serikali kuendeleza skimu hii aliyoisema.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili kwenye swali lake la msingi nataka nimweleze kwamba, niko tayari kuingilia kati kwa sababu, nia ya Serikali ni kupeleka maendeleo kwa wananchi wake, mradi cha muhimu kwamba, watu wa Kagera ni Watanzania, watu wa Kigoma ni Watanzania, ilimradi mradi huu tuumalize kwa wakati upeleke maendeleo kwa wananchi wetu na waweze kunufaika na Serikali yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la mwisho, sio kwa umuhimu, nataka nimwombe Mheshimiwa Mbunge, hela kama alivyosema ziko tayari, lakini kuna changamoto ndogo tu kutoka wale viongozi wa skimu, waharakishe mchakato ule wa kupata watia saini, ili hela zile ziweze kuingizwa kwenye akaunti yao haraka iwezekanavyo.
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza niishukuru sana Serikali kwa kuanza kutekeleza ahadi yak. Baada ya Waziri kutembelea na kusikia kilio cha wananchi imetenga shilingi milioni 300 na tayari wamepeleka shilingi milioni 20 na wataalam wameanza kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza. Katika lot ya miradi ya Kiduduye, Nyagwijima na Muhange, kwa kuwa tayari mradi wa Muhange unatekelezwa: Je, ni lini sasa Serikali itapeleka wataalam na fedha kwa ajili ya miradi miwili ya Nyagwijima na Kiduduye kuanza kutekelezwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Wakati Mheshimiwa Waziri wa Maji akihitimisha hotuba yake ya Bajeti ya mwaka huu, alituhamasisha Wabunge wote kupeleka orodha ya visima vinavyofaa kuchimbwa katika Majimbo yetu, nami nilikuwa wa kwanza kumkabidhi orodha ya visima 15 vilivyofanyiwa utafiti: Je sasa, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kuniambia au kuwaambia wananchi wa Buyungu ni lini sasa ligi itapelekwa katika Jimbo la Buyungu kuanza kuchimba visima hivi 15? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kwa muda mfupi tangu amechaguliwa na wananchi wake. Kikubwa amekuwa mfuatiliaji, nasi kama Wizara hatutakuwa kikwazo kum- support kuhakikisha tunatatua tatizo la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya changamoto kubwa sana kusuasua kwa miradi ya maji kulikuwa kunatokana na wakandarasi wababishaji. Sisi kama Wizara ya Maji, tumejipanga, sasa hivi tumeanzisha Wakala wa Maji kwa maana ya RUWASA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie, kwa miradi ile ambayo imekuwa ikisuasua, tutaitekeleza kwa kutumia wataalam wetu wa ndani ili kuweza kukamilisha miradi ile kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, miradi hiyo tutaifanya kwa wataalam wetu na tutawa-support kuwapatia fedha ili miradi iweze kukamilika na wananchi wako, waweze kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la ahadi ya visima, ahadi ni deni. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tukutane tufanye mazungumzo na wenzetu wa DDC ili tuwatume waende kuchimba visima kwa wananchi wake waweze kupata huduma hii muhimu ya maji safi na salama.
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri nina swali moja tu la nyongeza. Kwa kuwa Mheshimiwa Kuchauka ameuliza maswali ambayo yanahusiana na utendaji kazi wa Jeshi la Polisi, na kwa kuwa yamo masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu. Je, Mheshimiwa Waziri uko tayari sasa ukutane na Mheshimiwa Kuchauka ili aweze kukupa maelezo kama yapo specific uweze kuyafanyia kazi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze kwa swali lake zuri ameuliza suala kitaalam sana na nimuahidi kwamba huo ndiyo utaratibu mzuri kwa pale ambapo wawakilishi wa wananchi kama Wabunge wanapoona kuna tatizo Specifically limejitokeza kwa wananchi wao Serikali tupo kwa sababu hiyo. Kwa hiyo, wakati wowote Mheshimiwa Kuchauka atakapokuwa amerejea tutakuwa tayari kukaa naye tuweze kujua kama anakusudia kuna tatizo mahsusi ambalo analifahamu na uthibitisho wa tatizo hilo ili tuweze kusaidiana kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vitambulisho hivi vya Taifa ni muhimu kwa maendeleo na vinatambuliwa, hata mtu akiwa nje ya nchi vitambulisho hivi vinatabuliwa. Sasa kwa sababu vitambulisho hivi ni muhimu lakini ukitazama zoezi linaloendelea linasuasua na hususan kwa wananchi wa kawaida, maana watu ambao wamevipata ni watu kama sisi Wabunge na watumishi wa Serikali, wananchi wa kawaida kwa kweli hawajavipata.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu, Mheshimiwa Waziri amesema Serikali inaendelea kukamilisha usajili wa watu wenye sifa kwa kuchukua alama za vidole, picha na saini za kielektroniki. Kwa kuwa katika Wilaya ya Kakonko takribani kata tano kati ya 13 wamekwishakamilisha zoezi hili, kwa nini sasa vitambulisho hivi hawavipati? Swali la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ninapenda kujua sasa, mara ya mwisho Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani alisema Watanzania takribani milioni 16 wamekwishapata vitambulisho, je, hivi sasa ni wananchi wangapi wa Tanzania wakiwemo wale wa vijijini, wote kwa ujumla wamekwishapata vitambulisho hivi muhimu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Chiza, ni miongoni mwa Wabunge ambao wamekuwa wakiuliza maswali yao kwa umakini wa hali ya juu. Lakini kuhusiana na hoja zake mbili kwa pamoja, nataka nimjibu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Nabu Spika, moja, nina mashaka juu ya takwimu ambazo amezitoa akimkariri Mheshimiwa Waziri kwa sababu uhalisia uliopo ni kwamba mpaka sasa hivi tumeshatoa vitambulisho takribani milioni tano huku vitambulisho takribani milioni 13 vikiwa vipo katika hatua za mwisho kutolewa, wakati malengo yetu mpaka itakapofika mwezi Desemba ni kama milioni 24.2. Kwa hiyo utaona kwamba tupo vizuri kwa sababu milioni 18 ni kama vile tayari process yake imekamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nikijibu swali lake la mwanzo sasa kwamba inawezekana miongoni mwa watu ambao wananchi wake wa Kakonko ambao hawakupata vitambulisho ni hawa ambao vitambulisho vyao ni hivi milioni 13 ambavyo vinafanyiwa kazi. Kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Mbunge avute subira, muda si mrefu vitambulisho hivi vitatolewa na wananchi wake wengi nina uhakika watakuwa wamepata vitambulisho hivyo kama watakuwa wamekamilisha, kama nilivyosema, processes zote za kuweza kujisajili.