Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Eng. Christopher Kajoro Chizza (6 total)

MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA aliuliza:-
Sera ya Serikali ni kuwa na Hospitali za Wilaya na Vituo vya Afya katika kila Kata:-
• Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kakonko?
• Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Vituo vya Afya katika Kata za Kiziguzigu, Kasanda, Gwarama, Rugenge, Nyamutukiza na Kata nyingine ambazo hazina Vituo vya Afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Christopher Kajoro Chiza, Mbunge wa Buyungu, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, hatua za awali za kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kakonko zimeanza ambapo limetengwa eneo lenye ukubwa wa ekari 32 katika Mtaa wa Kanyamfisi karibu na yanapojengwa Makao Makuu ya Wilaya.
Mheshimiwa Spika, Serikali inajenga Hospitali za Wilaya kwa awamu ambapo katika awamu ya kwanza zimetengwa shilingi bilioni 100.5 kuanza ujenzi wa Hospitali 67 za Wilaya. Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko itapewa kipaumbele cha kujenga Hospitali ya Wilaya katika awamu inayofuata.
Mheshimiwa Spika, Serikali imetoa shilingi bilioni 4.2 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa vituo tisa vya afya katika Mkoa wa Kigoma. Kati ya fedha hizo, halmashauri ya Wilaya ya Kakonko imetengewa Sh.500,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Gwanumpu. Maeneo yaliyobaki zikiwemo Kata za Kizuguzugu, Kasanda, Rugenge, Gwarama na Nyamtukuza yatapewa kipaumbele kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA aliuliza:-

Katika Wilaya ya Kakonko kuna wachimbaji wadogo wa madini aina ya dhahabu katika Vijiji vya Myamwilonge, Nyakayenzi, Ruhuru na kuna dalili za kuwepo madini hayo katika sehemu nyingine. Aidha, kuna madini ya chokaa katika Milima ya Nkongogwa ambayo yana matumizi mengine ya viwandani:-

Je, Serikali imejipangaje kufanya utafiti wa uwepo wa madini na kuwasaidia wachimbaji ili wayachimbe na kujipatia kipato?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda sasa nijibu swali la Mheshimiwa Engineer Christopher Kajoro Chiza, Mbunge wa Buyungu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania ilifanya tafiti zifuatazo:-

(i) Upimaji na utafiti wa jiolojia uliofanyika mwaka 1960 na kuchora ramani ya jiolojia ya QDS (Quarter Degree Sheet) namba 43 pale Kakonko.

(ii) Utafiti wa pili ulifanyika mwaka 1978 – 1980 Serikali ilifanya utafiti wa jiofizikia kwa kutumia ndege na kufanya uchakataji wa takwimu zilizochukuliwa na hatimaye kuainisha maeneo yenye mipasuko ya miamba inayoashiria uwepo wa madini mbalimbali katika maeneo ya Kakonko na taarifa hizo zipo katika Ofisi ya GST (Geological Survey of Tanzania).

(iii) Utafiti wa tatu ulifanywa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ikiwemo Mradi wa Nordic Fund, Kampuni ya Beak Consultants ya Ujerumani na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kati ya mwaka 2003 na 2014 walifanya utafiti wa jiosayansi na kubainisha yafuatayo:-

(a) Uwepo wa madini ya dhahabu katika Kata ya Muhange, Kijiji cha Mwiluzi, Nyamtukuza, Nyamwilonge, Msekwa/ Galama, Kasela na Kata ya Kasuga katika Kijiji cha Nyakayenzi; na;

(b) Madini ya agate katika Kata za Kasanda, Kijiji cha Nkuba, Kata ya Gwanumpu katika Kijiji cha Kabingo na Kata ya Nyamtukuza katika Vijiji vya Nywamwilonge na Kasela.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kupitia Geological Survey of Tanzania inakamilisha uandaaji wa kitabu cha madini yapatikanayo katika toleo la nne ambacho kinaonesha uwepo wa madini katika mikoa, wilaya na vijiji, hivyo kitasaidia wananchi na wachimbaji wadogo katika kutambua madini yaliyopo katika maeneo yao na matumizi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali kupitia Geological Survey of Tanzania itaendelea kufanya tafiti zaidi za kijiosayansi katika mwaka 2019/2020 kwenye maeneo ya Ruhuru na Nkongogwa katika Wilaya ya Kakonko ili kubaini madini yaliyopo katika maeneo hayo. Pia itatoa elimu kwa wachimbaji wadogo kuhusu njia bora za uchimbaji na uchenjuaji ili waweze kuelewa kuhusu jiolojia na madini yaliyopo kwenye maeneo yao na kuwashauri namna bora ya kufanya uchimbaji na uchenjuaji salama wenye tija kwa lengo la kuhakikisha kuwa wananchi wanafaidika na rasilimali ya madini iliyopo katika maeneo yao.
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA aliuliza:-

Mwaka 2005 Serikali ilikamilisha ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Itumbiko, lakini banio lake limeharibika na kusababisha Skimu nzima kushindwa kufanya kazi; aidha, Serikali kupitia Mfuko wa Food Aid Counterpart Fund ilipata shilingi milioni 300 ili kujenga miundombinu ya umwagiliaji katika Kijiji cha Gwanumpu lakini mradi huo hauendelei licha ya kutengenewa fedha za utekelezaji.

(a) Je, lini Serikali itakarabati banio la Skimu ya Umwagiliaji ya Itumbiko ili kuokoa miundombinu inayoendelea kuharibika na kuwasaidia wananchi kuendelea kulima ?

(b) Je, ni kwa nini Serikali imeshindwa kuwasiliana na Mkurungenzi Mtendaji wa Wilaya ya Kakonko ili kufuatilia fedha za Food Aid Counterpart Fund ambazo zimekosa wafuatiliaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Christopher Kajoro Chiza, Mbunge wa Jimbo la Buyungu, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Skimu ya Umwagiliaji ya Itumbiko ina jumla ya hekta 230 na inategemewa na wakazi zaidi ya 339. Skimu hiyo imejengwa mara ya kwanza mwaka 2004 kwa fedha kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Umwagiliaji Wilaya kwa kiasi cha shilingi milioni 340 ambazo zilitolewa kwa awamu mbili. Aidha, kutokana na uharibifu wa miundombinu uliotokana na mafuriko mwaka 2017/2018 Serikali itatuma wataalam wake kufanya tathmini ya kina ili kubaini athari zilizotokea na kuainisha gharama za ukarabati zinazohitajika kwa ajili ya ukarabati na uendelezaji wa Skimu hiyo ya Itumbiko.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Kakonko Serikali inatekeleza ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Gwanumpu iliyopo Kijiji cha Gwanumpu, Kata ya Gwanumpu, yenye hekta 139 kwa kushirikiana na Serikali ya Japan, kupitia shirika lake, kupitia Mradi wa Food Aid Counterpart Fund kwa gharama ya Sh.358,302,000. Aidha, jumla ya Sh.248,570,000 zimetolewa katika awamu ya kwanza na ya pili na Sh.109,732,000 zitatolewa kutegemeana na utekelezaji wa mradi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inafuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa ujenzi wa Skimu ya Gwanumpu kwa ushirikiano na Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko. Mwezi Disemba mwaka 2019 wataalam wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wakishirikiana na wataalam wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko walipitia upya tathmini ya awali iliyofanyika na kubainisha gharama za ujenzi kwa wakati huu na kuziwasilisha katika shirika la Food Aid Counterpart Fund kwa ajili ya kupata fedha za ujenzi huo.
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA Aliuliza:-

Serikali ilitoa zaidi ya shilingi bilioni mbili kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji ya Nyabibuye, Gwanumpu, Muhange, Kiduduye, Nyangwijima na Kakonko Mjini. Miradi hiyo sasa inahitaji ukarabati mkubwa hata kabla ya kuanza uzalishaji na mingine utekelezaji upo chini ya asilimia 10:-

(a) Je, ni kasoro gani zimesababisha miradi yote sita kutotekelezwa kwa mwaka uliopangwa?

(b) Serikali imechukua hatua gani kuhakikisha miradi hiyo inakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Christopher Chiza Mbunge wa Buyungu, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa miradi ya Muhange, Kiduduye na Nyangwijima ulikamilika lakini ulishindwa kuwanufaisha wananchi kutokana na kasoro mbalimbali zilizojitokeza ikiwemo eneo la kisima cha pampu cha mradi wa Muhange kujaa tope; na pia kwa mradi wa maji Nyagwijima na Kiduduye eneo la chanzo kushindwa kuzuia maji kuyapeleka kwenye kisima chenye pampu hii imetokana na matatizo ya usanifu yaliyojitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha miradi hii inatoa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa, Serikali imechukua hatua mbalimbali kwa miradi ya Muhange, Kiduduye na Nyagwijima, Wizara imefanya mapitio ya usanifu ambapo kiasi cha shilingi milioni 300 kimekadiriwa ili kurekebisha kasoro zilizojitokeza. Tayari Serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 120 kwa ajili ya maboresho ya mradi wa maji Muhange ambapo utekelezaji unaendelea na umefikia asilimia 45. Serikali itaendelea kutenga na kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha pia miradi ya Nyagwijima na Kiduduye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya maji Gwanumpu, Nyabibuye na Kakonko Mjini utekelezaji wake ulichelewa kutokana na wakandarasi kujenga miradi hiyo kwa kasi ndogo kutokana na uwezo mdogo wa kifedha. Hali hii ilisababisha baadhi kusitishwa mikataba yao. Mkandarasi wa Mradi wa Gwanumpu yupo eneo la mradi na anaendelea na kazi ambapo amefikia asilimia 40. Kwa Mradi wa Maji wa Nyabibuye na Kakonko Mjini taratibu za kusaini mikataba na wakandarasi wapya zinaendelea ili waweze kukamilisha utekelezaji wa miradi hiyo.
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA aliuliza:-

Wafanyabiashara wa Wilaya ya Kakonko wanapenda kujisajili BRELA ili kurahisisha biashara zao na kulipa kodi stahiki lakini wengi wanashindwa kufanya hivyo kwa kukosa Vitambulisho vya Taifa

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuharakisha zoezi la kutoa Vitambulisho vya Taifa ili wananchi waweze kuvitumia katika shughuli za maendeleo?

(b) Kuna wananchi wanaokaa katika mipaka kati ya Tanzania na nchi nyingine; je, Serikali imewawekea utaratibu gani wa kuwapa vitambulisho wananchi hao kwa haraka bila kuathiri malengo ya zoezi la utoaji wa Vitambulisho vya Taifa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Christopher Kajoro Chiza, Mbunge wa Buyungu, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inaendelea kukamilisha usajili wa watu wote wenye sifa kwa matarajio ya kukamilisha zoezi la uchukuaji wa alama za vidole, picha na saini za kielektroniki ifikapo tarehe 31 Desemba, 2019. Lengo la Serikali ni kununua mashine mpya za uzalishaji wa vitambulisho zenye uwezo mkubwa zaidi ili kuharakisha upatikanaji wa Vitambulisho vya Taifa. Aidha, Mamlaka imefungua dawati Maalum la usajili katika ofisi ya BRELA, usajili huu unafanyika kwa kuzingatia sifa bila kuathiri masharti ya kisheria na kikanuni yaliyowekwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kuwapa vitambulisho vya taifa kwa haraka wananchi wanaokaa mikoa ya mipakani, utaratibu wake hautofautiani na utaratibu wa kawaida wa usajili ambapo mamlaka kuhakikisha kuwa taratibu zote za usajili zimezingatiwa na hatua zote za uhakiki na ufuatiliaji wa mapingamizi zimefuatwa kikamilifu. Natoa rai kwa wananchi wote nchini kuanza taratibu za usajili mapema ili kuepusha usumbufu.
MHE. ENG. CHRISTOPHER K. CHIZA aliuliza:-

Kumekuwa na dalili za upatikanaji wa madini ya dhahabu katika Vijiji vya Kabingo, Ruhuru, Nyakayenzi, Nyamwilonge na Muhange Wilayani Kakonko na katika baadhi ya vijiji uchimbaji umeanza:-

Je, Serikali inatoa ushauri gani kwa vijana ambao wapo tayari kujishughulisha na uchimbaji wa madini?
WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Christopher Kajoro Chiza, Mbunge wa Jimbo la Buyungu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwa na dalili za upatikanaji wa madini ya dhahabu katika Vijiji vya Kabingo, Ruhuru, Nyakayenzi, Nyamwilonge na Muhange, Wilayani Kakonko.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa katika Kijiji cha Nyamwilonge uchimbaji unaendelea na Serikali imekwishakutoa leseni saba kupitia Tume ya Madini, leseni za uchimbaji mdogo (primary mining licence) kwa madini ya dhahabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mnamo mwezi Mei, 2017, Wizara ya Madini kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ilifanya utafiti wa awali ambao uliombwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko kubaini maeneo yenye madini ya dhahabu. Katika ripoti yake ilibainika uwepo wa dhahabu katika Vijiji vya Nyakayenzi, Nyakahura na Nyamwilongo. Pia ripoti hiyo ilishauri utafiti wa kina ufanyike ili kujua kiwango cha wingi na upatikanaji wa dhahabu katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Madini inashauri vijana wote wanaotaka kujishughulisha na shughuli za uchimbaji madini kwenye maeneo hayo, wafike kwenye Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Kigoma ili waweze kupewa ushauri wa kitaalam pamoja na kuelimishwa kuhusu utaratibu wa kufuatwa kupata leseni ya uchimbaji madini ili waweze kufanya shughuli zao kwa mujibu wa sheria.