Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Dr. Adelardus Lubango Kilangi (3 total)

MHE. FAIDA MOHAMMED BAKARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri niko na maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa hizi sheria naona kama zitakuwa zimepitwa na wakati; na kwa kuwa Mheshimiwa Rais wetu amekuwa mfano mzuri wa kuhamasisha utumiaji wa lugha ya Kiswahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni je, Mheshimiwa Waziri atakubaliana nami kwamba sasa umefika wakati muafaka wa kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa matumizi ya Kiswahili katika Mahakama, katika kuandika maamuzi yake kwa lugha hii ya Kiswahili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa hata hapa Bungeni unaletewa hii Miswada hii unaiona hii kwa lugha ya Kiingereza, hii ni Tanzania tunaletewa Miswada kwa lugha ya Kiingereza na humu Bungeni kuna watu tofauti na elimu zetu tofauti, watu wanaweza wakajadili wakawa hawapati muafaka mzuri kwa sababu hawaelewi hii lugha iliyomo katika Miswaada mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakubaliana nami sasa kwamba ni wakati muafaka katika nchi yetu ya Tanzania tutumie lugha yetu ya Kiswahili, Lugha ya Taifa katika Mahakama na katika Mabunge na katika sehemu zote? Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie katika majibu ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameshayatoa. Kuhusiana na lile suala la kwanza la kuendesha mashitaka kwa Kiswahili halafu hukumu zinatolewa kwa lugha ya Kiingereza ametoa maelezo ya kutosha na nafasi ipo kwamba kama mashtaka yanaendeshwa Hakimu au Jaji anaweza kuruhusu yaendelee kwa Kiswahili au kwa Kiingereza; na sababu nadhani amezitoa za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kuhusu Miswada na pengine sheria kuandikwa kwa lugha ya Kiswahili hilo lipo katika mpango wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuanza na kutafsiri karibu sheria zote ziwe na zisomeke kwa lugha ya Kiswahili kwa sababu ndiyo lugha inayozungumzwa na kueleweka na watu wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, suala hili linahitaji rasilimali na tuna changamoto kidogo za rasilimali lakini pia hata utaalam wa kutosha kwa sababu kuna hatari, sheria ina lugha yake unapoitafsiri tu moja kwa moja kwenda Kiswahili kuna hatari kubwa pia ya kupoteza mantiki iliyokusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuna changamoto pia ya kuwa na wataalam wanaoweza kutufanyia kazi hii kwa usahihi. Hata hivyo, hilo ni kati ya mambo ambayo tumeyawekea mipango tuanze kuyafanyia kazi sheria zote ziandikwe kwa Kiswahili. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana tukaona mambo haya ya uchaguzi ni mepesi lakini amani ya Taifa hili itapotea ama itaathirika kama tukipuuza masuala ya uchaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, subsidiary legislation zozote zinazotungwa katika nchi hii leo, lazima kwa njia moja au nyingine ziwe ratified na Bunge. Sheria ndogondogo tunazozitunga kabla hazijaanza kutumika kimsingi zinastahili kuletwa kuwa ratified na Bunge. Vikao vya wadau vinavyokaa ni maoni wala vikao vya wadau vinavyokaa kujadili subsidiary legislation ama legislation yote haviwezi kuwa mbadala wa Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Sheria Ndogo ya Bunge haijawahi kuona kabisa au kupitia na kuthibitisha ama kuzi-accept ama kutoa maoni kanuni hizi zilizotungwa na TAMISEMI. Ninachouliza Mheshimiwa Waziri atueleze katika utamaduni huo ambako tayari kanuni zimeshaingizwa kazini, Kamati ya Sheria Ndogo ya Bunge haikuzipitia kwa kisingizo kwamba wadau walizipitia ambao sio Bunge. Je, jambo hili ni sahihi? (Makofi)
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe maelezo kidogo kuhusu suala ambalo ameliibua Mheshimiwa Mbowe, amesema kwamba sheria ndogondogo zinapotungwa lazima kuletwa Bungeni kabla ya kuanza kutumika, hiyo kwa mujibu wa utaratibu siyo sahihi na bahati nzuri Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo yupo hapa ataeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria Ndogo huwa zikishatayarishwa zinapelekwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchambuzi yaani vetting na baada ya hapo Mwanasheria Mkuu wa Serikali humrudishia Waziri husika na Waziri yule anazi-gazette halafu baada ya hapo zinapelekwa kwenye kikao kinachofuata cha Bunge kwenye Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo kwa ajili ya kuchambuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongeze kusema mtu anaweza kusema labda mchakato huo hautoi nafasi ya kuweza kuziangalia vizuri zile sheria ndogo, kimsingi sheria ndogo zote zinatungwa chini ya sheria mama na ipo misingi ya kisheria inayoelekeza namna gani sheria ndogo zitungwe na mojawapo ya misingi hiyo ni kwamba isipingane kimsingi na sheria mama. Na inapotokea kuna changamoto moja au mbili ile Kamati ya Bunge kuhusu sheria ndogo kutoa maoni na maelekezo yake na kama kuna changamoto yoyote inarekebishwa, kwa hiyo, hakuna tatizo kabisa katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza na namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri yenye tija.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa baadhi ya mashirika ya umma yanaendelea kutumia mawakili binafsi katika kuendesha kesi am bazo imeshtakiwa na wadai. Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya mashirika ya umma na taasisi zake zinazoendelea kutumia mawakili binafsi katika kuendesha kesi za umma?

Mheshimiwa Spika, pili, kwa kuwa moja ya malengo ya kubadilisha kuagiza kesi binafsi, kesi zilizoshtakiwa Serikali zisimamiwe na mawakili wa Serikali ni kupunguza gharama za uendeshaji wa kesi. Sasa gharama za kuendesha kesi nchi za nje zimekuwa kubwa sana na sababu moja inayosababisha Serikali ishtakiwe nje ni pamoja na kuvunja mikataba kiholela.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha inalipa wadai wote, wakandarasi wote ambao wamei-supply Serikali kwenye mikataba ya Kimataifa ili kuiondoa Serikali na mzigo mkubwa wa madeni na kushtakiwa nchi za nje? (Makofi)
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kubenea.

Mheshimiwa Spika, la kwanza, baadhi ya Mashirika ya Umma kuendelea kutumia mawakili binafsi hii inawezekana ni kwamba wakati maelekezo haya ya kesi zote kusimamiwa na Wakili Mkuu wa Serikali yanatolewa yale mashirika yalikuwa tayari yameshawa-engage wale lawyers, lakini kwa vyovyote vile kwa sasahivi wanafanya kazi pamoja na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na kuanzia pale lilipotolewa lile agizo kwamba kesi zote za haya mashirika ya umma zisimamiwe na Wakili Mkuu wa Serikali hakutakuwa na kesi yoyote ambayo itasimamiwa tena na Mawakili binafsi isipokuwa katika mazingira ambayo Mheshimiwa Waziri ameyaeleza. Kama iko kesi nje ya nchi na iko katika mahakama ambayo kuna taratibu ambazo haziwezi zikawaruhusu wanasheria wetu kusimama katika zile mahakama basi tutapata mawakili binafsi wa kusimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili ambalo linagusa kesi mbalimbali zilizoko na zinazotokana na kuvunjwa kwa mikataba na kadhalika, nimueleze tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa hivi tunao umakini mkubwa sana tunapoingia hii mikataba kiasi kwamba hatutaingia katika mazingira ya kuweza kushtakiwa kwa sababu ya kuvunja mikataba.

Kwa hiyo sasa hivi tunazingatia mambo yote ya muhimu, maslahi ya nchi na kadhalika na kuhakikisha kwamba mikataba yetu inategengenezwa vizuri kabisa kiasi kwamba hatutakuwa na matatizo ya kesi hizi mbalimbali. Na kwa kesi ambazo ziko tayari kwa kiasi kikubwa tumeingia katika majadiliano na mashauriano tuone namna gani tunaweza tukazimaliza kesi hizo kwa njia ya mashauriano badala ya kuendelea na njia ya mahakama. Naomba kuwasilisha.