Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita (7 total)

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA aliuliza:-
Upungufu wa maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu na mifugo ni moja ya kero kubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Longido. Vyanzo vya maji vilivyoko ni vichache na ni vya muda (seasonal) na mahali pengine hakuna kabisa:-
(a) Je, utekelezaji wa mradi mkubwa wa kuleta maji ya bomba kutoka Mto Simba ulioko Siha, Mkoani Kilimanjaro hadi Mji wa Longido kilometa 64 unaogharimu shilingi bilioni 16 umefikia hatua gani?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuendeleza usambazaji wa maji hayo ili yawafikie wananchi wapatao 23,000 waishio katika Kata Kimokouwa na Namanga pia Kiserain ambazo zipo umbali wa kuanzia kilometa 15 - 25 tu toka Longido Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Steven Kiruswa, Mbunge wa Longido, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza mradi wa uboreshaji wa huduma ya upatikanaji wa maji katika Mji wa Longido. Mradi huo umegawanyika katika vipande vinne. Utekelezaji wa kipande cha kwanza unagharimu shilingi bilioni
• Hadi mwezi Machi 2018, utekelezaji wa kipande hicho umefikia asilimia 15. Utekelezaji wa kipande cha pili unagharimu shilingi bilioni 2.54.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi mwezi Machi 2018 utekelezaji wa kipande hicho umefikia asilimia 40. Kipande cha tatu kinagharimu shilingi milioni 276.36. Hadi mwezi Machi 2018 utekelezaji wa kipande hicho umefikia asilimia 90. Kipande cha nne kinahusu ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji katika Mji wa Longido kwa gharama ya shilingi bilioni 2.09 ambapo utekelezaji wa kipande hicho umefikia asilimia 85.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu umesanifiwa kutoa huduma kwa Kata za Longido, Engikaret na Orbomba zenye jumla ya wakazi 16,712 kwa takwimu ya sensa ya watu wa makazi ya mwaka 2012, ambapo Kata ya Longido ina wakazi 2,285; Kata ya Orbomba 7,900; na Engikaret ya wakazi 6,527; na inatazamiwa idadi ya watu ikafika 26,145 kwa Kata zote tatu ifikapo mwaka 2024 kwa ongezeko la asilimia 3.8 kwa mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, Kata za Kimokouwa, Namanga na Kiserian zitaingizwa katika mpango wa awamu ya pili ya uzambazaji maji baada ya mradi huu kukamilika.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA aliuliza:-
Ubora wa elimu wanayopata watoto wa jamii ya kifugaji wanaosoma shule za kutwa vijijini unaathiriwa sana na umbali mrefu wanaotembea wanafunzi kutoka makazi yao (maboma) hadi shuleni.
(a) Je, ni kwa nini Serikali isijenge mabweni katika baadhi ya shule zilizo kwenye vijiji vyenye mtawanyiko mkubwa wa maboma?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi wa Longido kujenga vyumba 177 vya madarasa, nyumba 291 za walimu na matundu 561 ya vyoo?
(c) Je, Serikali imepanga lini kuziba upungufu wa walimu 234; Waratibu Elimu Kata 18 na maafisa ngazi ya Wilaya 12 katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali refu la Mheshimiwa Dkt. Steven Lemomo Kiruswa, Mbunge wa Longido, lenye vipengele (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua changamoto inayowakabili watoto wa jamii ya kifugaji ndivyo maana katika kipindi cha kuanzia Julai, 2017 hadi Aprili, 2018 imekamilisha ujenzi wa bweni la wasichana na matundu 14 ya vyoo na inaendelea na ujenzi wa bweni la wavulana na nyumba tatu za Walimu katika Shule ya Msingi Sinya.
Vilevile nyumba ya Walimu two in one na madarasa matatu yanaendelea kujengwa katika Shule ya Msingi Kitumbeine ambao yatakamilika Juni, 2018.
Aidha, katika Shule ya Msingi Longido, ujenzi wa vyumba nne vya madarasa uko katika hatua ya msingi. Shule hizo tatu zina uwezo wa kuhudumia wanafunzi 1,323. Utekelezaji huo unafanyika ili kuwapunguzia adha watoto wa jamii ya kifugaji ambao kwa wastani hutembea zaidi ya kilometa 15 kutoka nyumbani hadi shuleni.
Aidha, ujenzi wa madarasa 24 kwenye Shule za Ranch, Imatiani Sokoni, Olmoti, Olmolog na Engurusai vimekamilika wakati ujenzi wa madarasa 18 katika shule mbalimbali unaendelea. Ujenzi wa bweni katika Shule ya Msingi Ngerenyai umekamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 515. Kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo, vyumba vya madarasa na nyumba za walimu. Serikali kwa kushirikisha nguvu za wananchi na wadau itaendelea kujenga mabweni kwenye maeneo ya wafugaji na maeneo mengine yenye uhitaji kadri ya upatikanaji wa fedha utakavyowezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Longido ina Kata 18 ambazo kwa sasa Kata zote zina Maafisa Elimu Kata. Katika ngazi ya Halmashauri ya Wilaya kuna upungufu wa Afisa Elimu vielelezo baada ya aliyekuwepo kuhamishwa kwenda Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC). Serikali itaziba pengo hilo hivi karibuni, sambasamba na kupunguza upungufu wa walimu katika Shule za Msingi na Sekondari.
MHE. DKT. STEPHEN L. KIRUSWA aliuliza:-
i. Je, Serikali ina mikakati gani ya kuboresha elimu ya awali?
ii. Kwa kuwa msingi mzuri wa elimu huanzia katika shule za awali. Je, Serikali haioni kuwa ni jambo la muhimu kuanzisha shule za awali na kuajiri walimu waliofuzu kutoa elimu hiyo katika shule za vitongoji hasa vijijini tofauti na ilivyo sasa ambapo jamii ndiyo inayozianzisha na kuziendesha shule hizo kwa kutumia walimu wasio na taaluma?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Steven Lemomo Kiruswa, Mbunge wa Longido kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa elimu ya awali kabla ya mtoto kuanza darasa la kwanza na kwa kutambua umuhimu huo Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuboresha elimu hiyo ikiwemo kutenga vyuo 18 ambavyo vinatoa mafunzo kwa ajili ya kuandaa walimu wa elimu ya awali ili kuongeza idadi ya walimu wa kufundisha wanafunzi hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali inaboresha mtaala na muhtasari wa elimu ya awali na kutoa mafunzo kwa walimu kwa ajili ya utekelezaji wa mtaala huo na kuandaa vitabu vya kiada vya aina sita pamoja na vitabu vya ziada 12 vya hadithi kwa ajili ya elimu ya awali ambavyo tayari vimekwishaandaliwa na sasa viko katika hatua ya uchapaji. Pia Serikali imehakikisha kuwa kila shule ya msingi inakuwa na darasa la elimu ya awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taratibu za elimu zinaelekeza watoto wa elimu ya awali wanapaswa kufundishwa na walimu waliosomea elimu ya awali au kupata mafunzo kazini kuhusu ufundishaji wa elimu ya awali. Hivyo Serikali itaendelea kuimarisha mafunzo ya ualimu wa elimu ya awali sambamba na kuendelea kuimarisha madarasa ya elimu ya awali.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA aliuliza:-
Asilimia 95 ya eneo lote la Wilaya ya Longido hutumika kwa ufugaji wa wanyamapori. Aidha, asilimia tano ya eneo hilo ndiyo hutumika kwa shughuli za kilimo.
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuendeleza sekta ya mifugo kwa kuzingatia kuwa mifugo ndio shughuli kuu ya uchumi wa wananchi wa Longido na Wilaya nyingine za ufugaji nchini?
(b) Je, ni lini Serikali itapatia Hati ya Idhini ya kutumia na kusimamia (User Rights Certificate) Jumuiya ya Uhifadhi wa Wanyama Pori (WMA) wa Kanda ya Lake Natron?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Steven Kiruswa, Mbunge wa Longido lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imeandaa mkakati wa kuboresha sekta ya mifugo nchini unaolenga kuongeza tija na uwekezaji katika mifugo, kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali yatokanayo na biashara ya mifugo na mazao yake ili kuongeza mchango wa mifugo katika Pato la Taifa. Aidha, mikakati ya kuendeleza sekta ya mifugo katika Wilaya ya Longido inahusisha ujenzi wa mnada wa kimkakati wa Eworendeke ambao umekamilika na unatarajiwa kuzinduliwa rasmi Julai, 2018. Mnada huu utasaidia wafugaji kupata soko la uhakika la mifugo. Pia, Halmashauri ya Longido imepata mwekezaji ambaye atajenga kiwanda cha kusindika nyama katika eneo la Eworendeke ambacho kinatarajiwa kukamilika mwezi Disemba, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na Wilaya ya Longido kuwa na Hali ya Ukame Halmashauri imejenga mabwawa, vibanio vya kunyweshea mifugo pamoja na kusambaza madume bora ya ng’ombe kwa lengo la kuboresha mifugo ya asili ilikupata mifugo bora inayostahimili mazingira ya Longido na kukua kwa haraka. Pia Halmashauri itaendelea kutoa huduma za ugani kwa wafugaji kwa lengo la kuboresha ufugaji ikiwamo kutoa mafunzo kuhusu mabadiliko ya tabia ya nchi na uboreshaji wa maeneo ya malisho.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Ziwa Natron ni pori tengefu kwa mujibu wa Kanuni za Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) za mwaka 2012 kifungu cha 8(1)(a)- (c). Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori huanzishwa katika maeneo yaliyo nje ya maeneo yaliyohifadhiwa kisheria. Aidha, hati ya matumizi ya rasilimali za wanyama pori kwa maana ya User Rights Certificate hutolewa kwa Jumuiya ya Hifadhi za Wanyama pori iliyoanzishwa na kusajiliwa kisheria. Kwa kuwa eneo hilo bado ni Pori Tengefu, limeendelea kupangiwa vitalu vya uwindaji wa kitalii ambapo wananchi na Halmashauri ya Wilaya wananufaika na asilimia 25 ya mapato yatokanayo na ada za wanyamapori wanaowinda.
MHE. DKT. STEPHEN L. KIRUSWA aliuliza:-

Seikali ina mkakati gani wa kujenga Kiwanda cha Kusindika Nyanya katika maeneo ya Mto Ngarenanyuki?
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kufanya marekebisho kidogo ya Kiswahili sanifu kwenye majibu yangu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Stephen Lemomo Kiruswa, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa eneo la Mto Ngarenanyuki katika Wilaya za Arumeru na Longido ni miongoni mwa maeneo yanayolimwa nyanya kwa wingi nchini. Ndiyo maana kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo tumeendelea kuweka mazingira wezeshi sambamba na kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kusindika nyanya. Kwa kuwa ni muhimu kwa kiwanda kuwa na uhakika wa malighafi za kutosha mwaka mzima namwomba Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana kuhamasisha uzalishaji zaidi wa nyanya ikiwezekana zipatikane kwa mwaka mzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu kupita SIDO imekuwa ikitoa mafunzo ya aina mbalimbali kuhusu ujasiriamali na usindikaji wa mazao ya kilimo. Naomba wananchi wa eneo wa Mto Ngarenanyuki katika Wilaya hizo mbili na Wilaya nyingine nchini waitumie fursa hiyo kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kusindika mazao ikiwemo nyanya.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA aliuliza:-

Halmshauri ya Longido inatakiwa kuwa na watumishi 1,660 wa kada mbalimbali lakini kwa sasa wapo 1atumishi 1,117 tu, hivyo, kuna upungufu wa watumishi 543 na wengi wao ni Watendaji wa Vijiji, Kata, Madereva na Makatibu Muhtasi:-

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa vibali vya kuajiri watumishi wanaohitajika ili kuondoa upungufu uliopo?

(b) Je, ni lini Serikali itatoa vibali vya kuwathibitisha maafisa wanaokaimu wenye sifa za kuajiriwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Steven Kiruswa, Mbunge wa Longido, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inakiri kuwepo kwa tatizo la upungufu wa watumishi kwa waajiri mbalimbali hapa nchini na siyo kwa Halmashaui ya Wilaya ya Longido pekee. Upungufu huu umesababishwa kwa kiasi kikubwa sana na zoezi la kuwaondoa katika Utumishi wa Umma watumishi waliobainika kutumia vyeti vya kughushi katika ajira zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na upungufu wa watumishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Serikali imetoa kibali cha ajira mbadala nafasi tano (5). Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Longido itapatiwa nafasi za Walimu na Fundi Sanifu Maabara kutoka kwenye mgawo wa nafasi 4,549 za Ajira Mbadala za Walimu ambazo mchakato wake unaendelea chini ya Ofisi ya Rais - TAMISEMI.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hatua nyingine, Halmashauri ya Wilaya ya Longido imetengewa jumla ya nafasi 177 za kada mbalimbali zikiwemo Watendaji wa Vijiji, Kata, Madereva na Makatibu Muhtasi katika mwaka wa fedha ule 2018/2019. Katika kuhakikisha suala la upungufu wa watumishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido linapatiwa ufumbuzi wa kudumu, Serikali itaendelea kutenga nafasi za ajira mpya pamoja na kutoa vibali vya Ajira Mbadala kwa kada za kipaumbele katika mwaka wa fedha 2019/2020 na kuendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika sehemu (b) ya swali la Mheshimiwa Dkt. Steven Kiruswa, Mbunge wa Longido, naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba watumishi wa umma wanaothibitishwa katika nafasi za uongozi kwa maana ya madaraka ni wale walioteuliwa rasmi katika nafasi hizo baada ya taratibu za upekuzi kukamilika. Aidha, hakuna utaratibu wa kuthibitisha watumishi wa umma wanaokaimu nafasi za uongozi kwa maana ya madaraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hufanya upekuzi kwa watumishi wa umma wanaokaimu nafasi za madaraka ili kubaini iwapo wanafaa au la. Uamuzi iwapo mtumishi husika anafaa kuteuliwa kwenye nafasi anayokaimu hutegemea na matokeo na upekuzi. Hivyo, pamoja na kuwa na sifa za kitaaluma, Serikali hailazimiki kumthibitisha mtumishi iwapo anakosa vigezo vingine vya uongozi.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa rai kwa watumishi wa umma wote nchini wanaokaimu nafasi za uongozi wafanye kazi kwa bidii, weledi, umahiri, uzalendo kwa kuzingatia maadili ya kazi ili waweze kukidhi vigezo vya kuteuliwa na kisha waweze kuthibitishwa kwenye nafasi za uongozi ambazo ni madaraka wanazoteuliwa kuzishika. Ahsante.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatoa Hatimiliki kwa Vijiji vilivyopimwa na kusajiliwa ambavyo bado havijapewa Hati?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Steven Kiruswa, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya mwaka 2001, vijiji vilikuwa vinapimwa na kupatiwa Hatimiliki ambayo ilikuwa inatolewa kwa Halmashauri za Vijiji kwa kuzingatia Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1923. Baada ya Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na.5 ya Mwaka 1999 kutungwa na kuanza kutumika mwezi Mei, 2001, ilielekeza kuwa vijiji vilivyotangazwa na kusajiliwa vitapimwa na kupatiwa cheti cha ardhi ya kijiji badala ya Hatimiliki iliyokuwa inatolewa hapo awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cheti hicho hutolewa kwa mujibu wa Kifungu cha 7(7) cha Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya Mwaka 1999 ili kuipatia Halmashauri ya Kijiji majukumu ya kusimamia ardhi pamoja na kuwapatia haki ya ukaaji na utumiaji wa ardhi ya kijiji wanakijiji wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Cheti cha Ardhi ya Kijiji kinathibitisha mamlaka ya Halmashauri ya Kijiji kusimamia ardhi ya kijiji tofauti na Hatimiliki ambayo ilimaanisha Halmashauri ya Kijiji kumiliki ardhi ya kijiji na hivyo kuwanyima fursa wanakijiji kumiliki ardhi kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, cheti hiki hutolewa na Kamishina wa Ardhi kwa kijiji husika kikiwa kinaonyesha mipaka ya ardhi iliyowekwa na kukubaliwa na pande zote zinazopakana na kijiji husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi Julai, 2019 Wizara imewezesha uandaaji na utoaji wa vyeti vya ardhi ya vijiji 11,165 kati ya vijiji 12,545 vilivyosajiliwa. Serikali inaendelea na utaratibu wa utatuzi wa migogoro ya mipaka ya vijiji kwa maeneo ambayo bado hayajapatiwa vyeti ambayo haizidi asilimia 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa rai kwa Halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa zinashirikiana na wadau wengine katika kusimamia utatuzi wa migogoro ya mipaka baina ya vijiji kwa njia ya maridhiano ili taratibu za upimaji na utoaji wa vyeti wa vijiji ufanyike.