Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita (45 total)

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. DKT. STEPHEN L. KILUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa niweze kuchangia katika hii hoja ya Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuanza kwa kutanguliza shukrani zangu za dhati kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa jinsi ambavyo inaendesha mambo yake katika kupeleka uchumi wa nchi hii mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipokuwa nasoma hiki kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa nimeona kwamba nchi yetu kweli inaelekea kuzuri maana hakuna jua halijageuzwa katika kupeleka maisha ya Watanzania mbele. Sekta za elimu, madini, maji, barabara, usafiri wa anga, you name them, ziko nyingi; kwa hiyo napenda pongezi zangu za dhati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi pia naomba niipongeze Wizara. Mheshimiwa Waziri jina lake ni Dkt. Mpango na jina linaumba na mipango yake ni safi. Nimesoma hotuba yake imepangiliwa kweli kweli, ushauri wangu ni kwamba haya yaliyoandikwa humu tujipange basi sawasawa katika kuyatekeleza.

Mheshmiwa Mwenyekiti, pia naomba niipongeze Kamati, Kamati ya Bunge imefanya kazi nzuri na mahiri kabisa katika kuandika kitabu chake hiki, na yale mapendekezo yaliyopo nayaunga mkono na naomba yafanyiwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo basi naomba nijielekeze katika baadhi ya mambo ambayo na mimi nimeya-note katika hotuba hii na ningeweza kutoa mapendekezo au ushauri wangu. Kwanza naomba pia kuungana na wenzangu ambao wamesifia marekebisho na mapendekezo ya kufutwa kwa kodi mbalimbali, ikiwemo ile ya taulo za kike kwa sababu tunaelewa itawasaidiaje watoto wetu wanaosoma shuleni na wale ambao itawasaidia katika kuzipata kwa bei ambayo naamini itakuwa na punguzo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza pia kuondolewa kwa kodi ya virutubisho kwenye vyakula vya mifugo, isipokuwa nasikitika kwamba hii haitagusa wafugaji wa asili. Sasa huo msamaha usije ukachukuliwa kwamba wafugaji wana kitu kikubwa cha kushangilia hasa wale ambao hawafugi kisasa. Najua dhamira ilikuwa ni kuhamasiha ufugaji bora na wa kisasa, lakini naomba niishauri Serikali kwamba nchi hii kwa asilimia 99.9 bado inategemea mazao ya mifugo ya asili. Nyama inayoliwa ni asilimia 99.9 ya Watanzania ni nyama ya ng’ombe, mbuzi na kondoo
wanaochungwa kiasili. Kwa hiyo bajeti hii ifikirie namna ya kuinua uchumi huo wa mifugo kwa kuiongezea tija na kuiwekea mikakati thabiti ya kuilea hiyo sekta maana bado ni ya muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwa sababu wanajitahidi katika kuwawezesha wafugaji wa asili kupata mbegu bora, lakini mbegu bora itakuwa haina maana kama vitu vingine muhimu vipaumbele vya mfugaji havijazingatiwa na vipo vinne nikivitaja kimoja kimoja. Kwanza ni malisho; malisho ni ya muhimu sana na malisho yabainishwe na kutambulika kisheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni maji, kukiwa na malisho bila maji bado kutakuwa na mgogoro mkubwa wa jamii zetu za kifugaji kulazimika kuacha hata malisho yenye majani hasa katika yale mapori yetu katika wafugaji waliopo Ngorongoro, Longido, Monduli, Simanjiro, Kiteto wakaenda kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na kuleta ile karaha kubwa ambayo tunaona kila siku wakifukuzwa na kupigwa faini kubwa kubwa ambazo zinawadidimiza katika umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, ili kushamirisha hii sekta ya mifugo ni kuhalikisha kwamba wanapatiwa dawa za tiba na dawa za chanjo na Serikali iiweke ruzuku kama inavyoweka katika mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni masoko ya uhakika ya ndani, maana sisi tunaoishi mipakani kule katika Wilaya yangu kama ile ya Longido wafugaji wale hawana sababu ya kupeleka ng’ombe Kenya, wanakwenda kwa sababu hawapati soko la uhakika la ndani; na wanapata karaha kule. Kuna watu wanaitwa middle men, madalali wanachukua wale ng’ombe ndio wanauza sokoni wewe unakaa unangojea, unapewa kile ambacho kitakachopatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, masoko ya ndani yatakapoboreshwa na sisi Watanzania tutaweza kujivunia ufugaji wetu na wafugaji ambao ni jamii kubwa na ambayo inafuga mamilioni ya ng’ombe inayofanya Tanzania iwe nchi ya pili katika ufugaji Afrika hawatakuwa na sababu ya kupeleka ng’ombe nje na watafarijika kuona kwamba Serikali yao inawajali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nilipenda kuchangia ni kwenye hili suala la asilimia kumi zinazotakiwa ziende kwenye miradi ya maendeleo ya akinamama, vijana na walemavu katika mapato ya ndani ya halmashauri zetu. Nimesoma hotuba ukurasa wa 40 nikaona kwamba niishauri Serikali kwamba hiyo asilimia kumi, pamoja na kwamba si kiwango kikubwa sana lakini imesaidia na tumeshaona matokeo yake katika Wilaya zetu, zile Wilaya ambazo hazina mapato ya kutosha ya ndani Serikali iwape ruzuku. Hilo ni la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, naomba basi iongezwe asilimia mbili ili iwe ni asilimia kumi na mbili kwa ajili ya kundi muhimu ambalo limesahahulika, kundi la wazee. Sasa fomula itakuwa kwamba, wanawake watapewa asilimia nne, vijana watapewa asilimia nne, walemavu watapewa asilimia mbili na wazee watapewa asilimia mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri hicho kipengele cha wazee ni cha muhimu sana kwa sababu wazee wetu wanaona kama wao wamenyanyapaliwa, wakati wanawake wamebainishwa tofauti na vijana; na najua katika kundi la vijana kuna vijana wa kike na wa kiume. Katika kundi la wazee inaonekana hatujasema wanawake na wazee, tumesema wanawake tu, kwa maana hiyo wazee wamenyanyapaliwa katika hili, kwa hiyo naomba Serikali izingatie hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kuchangia ni eneo la hii sekta ya utalii. Sekta hii ya utalii ni moja ya sekta muhimu na ni mhimili wa uchumi wa nchi yetu, ukichukulia kwamba ziko tatu za msingi, kilimo chenye mazao na mifugo na uvuvi ndani yake, utalii na
madini; hiyo ndiyo mihimili ya uchumi wetu. Sasa katika hili eneo la utalii ambalo linachangia asilimia 17.7 ya Pato la Taifa na asilimia ishirini na tano ya fedha za kigeni zinaingia katika nchi hii sijaona kwenye bajeti kama wameainishiwa vizuri mikakati iliyowekwa katika kuendelea kuitunza na kuiendeleza zaidi ya kutoa ahueni fulani kwa magari ya kitalii, sijaona mambo mengine ya msingi ambayo nilitegemea kwamba yangeongezwa ili sekta hii iendelee kukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba, ili hii sekta iendelee kuimarika na kuboreka, suala la miundombinu ndani ya parks (National Parks) zetu lipewe kipaumbele. Suala la kutangaza utalii ndani na nje lipewe kipaumbele, suala la kutanganza utalii wa fukwe zetu na liendelezwa lipewe kipaumbele, mambo ya kale, uwindaji, utalii wa kitamaduni, utalii wa usiku...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie pia kwa kusema kuna kero za kodi mbalimbali ambazo wawekezaji wa utalii wanalalamika.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali Wizara ya Maji na Umwagiliaji 2018/2019
MHE. DKT. STEPHEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kutoa mchango wangu katika hoja hii ya bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kutumia pia fursa hii kumpongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya na kuipongeza timu yake ya Baraza la Mawaziri, na Watendaji Wakuu wa Serikali kwa sababu kazi ya Serikali ya Awamu ya Tano inaonekana na inasikika, mwenye macho haambiwi tazama, mwenye masikio pia haambiwi sikiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naipongeza sana kazi kubwa aliyofanya Waziri kuandaa hotuba hii. Napishana na walisema kwamba hotuba hii ni kubwa na haina kitu, hotuba hii ni nzuri ina vielelezo vya kutosheleza, ina details za kutosha kwa wale wanaopenda details na wengine kwa sababu ya haiba zao wanapenda tu kuangalia facts, ina facts za kutosha nimeona viambatanisho ambavyo sijaona katika hotuba nyingine zilizotangulia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia kugusia haya maoni ya Kamati na kwa kweli ninaiunga mkono asilimia mia moja hasa kwenye mapendekezo matatu ambayo bila hayo nafikiri bado tutasuasua sana kama Taifa linalotaka kujenga Taifa lenye uendelevu wa viwanda. Walipotoa maoni kwamba, sekta ya umwagiliaji iongezewe pesa waweze kukuza kilimo cha umwagiliaji hawajakosea, tuzingatie kwamba sasa hivi tuko katika zama za mabadiliko ya tabianchi, mabadiliko ya hali ya hewa, bila kukuza kilimo cha umwagiliaji hatutatoka katika umaskini na upungufu wa chakula katika nchi hii.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono 100 kwa 100 kwamba, hiyo sekta ya umwagiliaji iongezewe pesa, tena ipewe nyingi kwa sababu japo kule Longido hatuna mito mingi ya kumwagilia, lakini kuna mto mmoja ambao unatiririsha maji hadi kwetu Ngarenanyuki na nitaongelea katika muda huu wa dakika chache nilizonazo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia katika maoni haya ya kamati ninaunga mkono hili suala la tozo, hizi tozo kwenye mafuta kwa lita ya petroli na dizeli kuelekezwa katika kusaidia kufikisha maji katika vijiji vingi katika nchi yetu ambavyo bado havina maji ni suala lenye tija. Ninaunga mkono na ninaomba hili lizingatiwe ili tuone kama tutapunguza kero ya maji katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, vilevile ninaunga mkono mapendekezo ya kamati katika suala la kuanzisha Wakala wa Maji Vijijini. Kama vile ambavyo Wakala wa Barabara za Vijijini (TARURA) imeanzishwa tena hivi karibuni, naomba hili nalo lipewe kipaumbele tuone kama tutatoboa katika kupunguza kero ya maji katika vijiji vyetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo basi naomba nidonoe vipengele vichache katika taarifa hii ya hotuba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji. Kwanza napenda kuendelea kuishukuru Serikali kwa mradi mkubwa wa maji ya Mto Simba kuja katika Mji wa Longido ambao unajengwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 15. Mradi huu ambao uligawanywa katika sehemu nne na Waziri amebainisha vizuri katika hotuba yake hii, ulikuwa na hivyo vipengele vinne; ujenzi wa chanzo, ambao kwa masikitiko makubwa nashangaa kuona kwamba umeshatimizwa kwa asilimia 40 tu na muda unazidi kwenda, ulazaji wa mabomba umekamilika kwa asilimia 42 tu, ujenzi wa tenki kwa asilimia 90 na ninashangaa hili tanki likimalizika na maji hayajafika matokeo yake ni nini kama sio kukauka na kupasuka kwa kukosa maji na pia mfumo wa usambazaji wa mabomba ambao umekamilika kwa asilimia 75. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza nasikitika kwamba juzi nilipita Jimboni kwa haraka nikaona kwamba katika huu mfumo wa usambazaji kuna mitaro ilichimbwa ikaachwa wazi maji yakaja yakafukia na sasa hivi pia kwa sababu labda wameshituka tunajadili hii bajeti, nimeona wanaanza kuchimbua na kutoa pipes nyingine kule chini, inawezekana waliweka ambazo ziko chini ya kiwango. Naomba sana wakandarasi wa mradi huu wafuatiliwe kwa makini na Serikali ijaribu kuukaribia huu mradi maana wananchi watakata tamaa kama ahadi ya kupelekewa maji ndani ya mwaka huu tena ilikuwa ni ndani ya mwezi huu haitatimia kwa muda mfupi iwezekanavyo.

Mheshimiwa Spika, pia, nashukuru kwa sababu nimeona kuna fungu la shilingi bilioni sita limetengwa ili kukamilisha mradi huu. Basi naomba Serikali iweke mkono uende kwa kasi zaidi kuliko ilivyo kwa sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, pia ninapenda kujulisha Bunge lako tukufu kwamba maji haya yakifika Longido tu na Orbomba na Engikahet ambapo inakisiwa kwamba itawanufaisha watu takribani 16,712 isije ikachukuliwa kwamba Longido kero ya maji imemalizika. Longido ina vijiji 49 na kutakuwa bado maana hivi ni kama vijiji vitatu tu maji yanafikia hayatakuwa hata yamesambazwa, kuna zaidi ya vijiji 45 bado vina kero kubwa ya maji na hivyo Serikali katika bajeti hii sijaona kama wametupatia kipaumbele katika kuendeleza miradi ya maji, hasa maji ya visima virefu sehemu ambapo hakuna mito ya kupeleka maji karibu vikiweko vijiji vya Wosiwosi, vijiji vya Magadini kule ambako hata sasa hivi nasikitika kusema kwamba baada ya mvua kubwa kunyesha na mafuriko kutokea kumezuka ugonjwa wa kuhara na kutapika ambao dalili zake hazipishani sana na kipindupindu, lakini sina taarifa rasmi niweze kutamka hivyo, ila kuna watu wamepoteza maisha na tusipopeleka maji kwa haraka katika ukanda huo wa Ziwa Natron kuna hatari mara mbili, kuna hiyo milipuko na pia kuna hatari kubwa ya watu kuendelea kuumia mifupa kama alivyosema dada yangu Mheshimiwa Mollel na ninamuunga mkono jana kwa upande wa Arumeru, maji ya Lake Natron nayo ni hatari sana yanapinda hata mpaka miguu ya wanyama wanaokunywa maji yale na watu wale wanaishi tu kama kilometa nane kutoka Mlima Gelai ambako maji ya bomba yangeweza kufikishwa kule tena ni maji masafi kutoka chemchemi, hiyo kero ingeweza kuondoka.

Mheshimiwa Spika, pia nipende kugusia kwa sababu ya muda kwamba katika huu Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji pale Longido hatuna mto, lakini Arumeru ndugu zetu wana maji ya Mto Engarenanyuki. Ule mto ni mkubwa, unapeleka maji mengi tu mpaka kule bondeni katika eneo la Wilaya ya Longido hasa katika Kata ya Tingatinga, lakini wakulima wa Kiholela wanaolima nyanya na ni zao kubwa la biashara wametumia mifumo isiyo ya kisasa, maji mengi yanapotea, maji yanaelekea katika mashamba kwa mifereji.

Mheshimiwa Spika, naomba mto huu ujumuishwe kati ya mito ambayo imebainishwa katika hotuba hii ambayo itafanyiwa usanifu ili kilimo cha kisasa kiweze kutekelezwa, matenki makubwa yajengwe na mabomba yaunganishwe watu walioko Tingatinga hasa vijiji vya Ngereiyani nao waweze kufaidika na kilimo cha nyanya maana maji haya yana floride na chloride kwa wingi kiasi kwamba hayafai kwa matumizi ya binadamu lakini ni maji mazuri sana kwa kilimo cha nyanya.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda ninaomba pia nisiache kusemea kidogo suala la Wakala wa Uchimbaji wa Visima (DDCA). Nimeona kwamba katika bajeti hii hatujaguswa kabisa katika visima ambavyo vitachimbwa, sijaona popote kwamba Longido watachimbiwa visima vya maji ukizingatia kwamba kero ya maji katika zaidi ya vijiji 45 iko palepale na Wilaya ya Longido ni moja ya Wilaya kame sana katika nchi yetu. Tena niombe DDCA pia wapeleke wataalam, wafanye survey ya maji katika vijiji vyote nchi hii ili tuwe tayari tunajua kwamba maji yako wapi, pesa zinapopatikana hasa mkitutengea hizi za mafuta tuweze kuchimba visima na kuondoa kero ya maji.

Mheshimiwa Spika, pia ninapenda kusema kwamba katika huu mradi wa kujenga mabwawa, hatuna bwawa hata moja ambalo limebainishwa. Napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba katika mvua za mwaka huu ambazo zimekuja kwa kasi kubwa baada ya kiangazi cha miaka mingi, tumebomokewa na mabwawa mawili makubwa yaliyokuwa yanasaidia maisha ya wananchi wa Longido. Bwawa la Kimokouwa limepasuka, Bwawa la Emuriatata limepasuka na Bwawa la Sinoniki lilishapasuka tangu mwaka juzi na ningeomba sana katika bajeti hii Mheshimiwa Waziri hebu angalia jinsi ya kutusaidia hayo mabwawa yaweze kufanyiwa ukarabati kwa sababu, ndiyo yanayosaidia maisha ya watu wa Longido.

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna mabwawa yaliyojaa udongo, bwawa la Tingale Sing’ita ambalo huwa halikauki kabisa na linasaidia maisha ya watu wa Kata mbili na Tarafa mbili, Tarafa ya Longido, Tarafa ya Ngaranaibo, ninaomba hili bwawa pia liangaliwe ili liweze kufukuliwa na tuna lingine ambalo liko katika Kijiji cha Ngoswe linaitwa Ngweseiya, pia limejaa udongo.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa nihitimishe hoja yangu kwa kusema kwamba sambamba na harakati za Serikali za kutuletea maji safi, pia kuna ahadi mbili zilishatolewa na Mawaziri hapa, Waziri wa Mifugo na Waziri wa Maji pia kwamba watatuchimbia mabwawa katika Kata ya Tingatinga na katika Kata ya Gilai Lumbwa upande wa Wosiwosi. Ni maeneo ambayo yana kero kubwa ya maji na upimaji ulishafanyika, survey imefanyika, usanifu umefanyika na sijaona kama kuna mradi umewekwa katika bajeti hii ili tupate maji hayo.

Mheshimiwa Spika, mwisho tuna kero kubwa moja ili niweze kumalizia kwa sababu ya muda. Kwamba, katika hii miradi inayotekelezwa Longido, hasa ule wa World Bank uliochukua miaka saba na bado haujakamilika wananchi wanaanza kupoteza matumaini maana miundombinu mingine ilijengwa, kulaza mabomba, kuweka visima sehemu za kunywa watu maji…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, ahsante. Naunga mkono hoja, lakini tusisahaulike katika suala moja la msingi kwamba maji ya World Bank yakafanyiwe uchunguzi na siyo hiyo tu ningeomba pia wananchi hawa wa Longido washirikishwe Halmashauri ishirikishwe katika huu mradi wa maji ya mto Simba maana Halmashauri haihusiki imetoka Wizarani ikaenda Mkoani.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa muda.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA (K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII): Mheshimiwa Spika, ninayo heshima tena kusimama mbele yako na mbele ya Bunge lako Tukufu jioni hii ili niweze kuhitimisha hoja ya Kamati yetu ya Ardhi, Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kutoa muhtasari wa yale ambayo yamejiri katika mjadala ulioendelea hapa, nitumie fursa hii kwa sababu asubuhi nilishikwa na taharuki baada ya kujiandaa kuwasilisha ile ripoti kwa nusu saa nikaambiwa tuna roba saa lakini najua sababu ni nini, kutanguliza shukrani za dhati kwa Kiongozi wa Taifa letu, Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa sababu ya mambo makubwa na ya kupendeza anayoendelea kulitendea Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya jamii ya wafugaji na wakulima, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa tamko lake la juzi la kwamba Wizara husika zikakae ili ardhi zote ambazo zimekaa idle mfano mashamba na maeneo ya hifadhi ambayo yamepoteza hadhi yakapitiwe upya ili wananchi wanaoteseka waweze kupata maeneo ya kulima na kufugia. Kwa kweli amewafariji sana jamii ya wafugaji na wakulima hususani watu wa Kanda ya Kaskazini wamefarijika na wamefurahia sana suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nitumie dakika moja kusema ahsante sana kwa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Umwagiliaji kwa taarifa ambayo nimeisikiliza hapa kidogo na Waziri akanigusa katika maslahi mazuri anayowawekea jamii ya kifugaji ya kuhakikisha kwamba masoko ya uhakika na viwanda yanakwenda kuanzishwa ili tuondokewe na hiyo kero ya kupeleka mifugo Kenya. Nimshukuru Waziri kwa operesheni alizozianzisha ambazo zimeleta kilio kikubwa kwa wananchi wa jamii za kifugaji hasa wa Wilaya ya Longido ambako mifugo yote ya Tanzania inayokwenda Kenya inapitia sasa itakuwa imetokomezwa.

Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri zaidi kwa sababu ameniahidi kwamba tutakwenda kule kujaribu kuwapoza wananchi maana kuna unyanyasaji mkubwa umetokea hivi karibuni kwa namna operesheni ile ya kuzuia mifugo inakwenda Kenya inavyotekelezwa. Kwa sababu nimesimama hapa kutoa shukrani kwa jinsi ulivyotupa matumaini, naomba niishie hapo ili nirejee kwenye hoja yangu ya msingi ambayo nakuja kuhitimisha.

Mheshimiwa Spika, hizi Wizara mbili ambazo Kamati yetu inasimamia, kwanza nianze kuwashukuru wote ambao wamechangia hoja yetu na niwashukuru wajumbe wa Kamati maana wamefanya kazi kubwa na yenye tija ya kuandaa ripoti hii ambayo kwa jinsi mjadala ulivyoendelea inaonekana kwamba kwa kweli kwa asilimia zaidi ya 99 imeungwa mkono hata na wenzetu wa upande huu. Malalamiko yaliyojiri ni madogo sana na nitapitia yale machache ambayo yametamkwa ili nitoe msimamo wa Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kifupi ukiangalia katika Wizara ya Ardhi mambo ambayo yamejiri sanasana ni kuhusu Shirika la Nyumba la Taifa kwamba tulipofanya ziara tulikuta kwamba baadhi ya miradi yake imesimama kwa sababu walizuiwa kukopa fedha na wakawa wameacha miradi viporo. Sisi kama Kamati tulisema kwamba ingefaa sasa Serikali iwaruhusu kama bado wanahitaji hela ya mikopo, maana Waziri hapa ametuambia wana uwezo kabisa wa kulipa wala hakuna tatizo, hiyo miradi viporo imalizwe ili hizo nyumba ziendelee kuleta tija na mapato ya kuwezesha shirika kuendelea kujenga nyumba nyingine hasa zile za bei nafuu ambazo wananchi wanahitaji vijijini.

Mheshimiwa Spika, pia kulikuwa na mjadala ambao umejadiliwa na wengi kuhusu urejeshwaji wa mashamba makubwa yale yaliyotelekezwa. Hapa ndiyo mjumbe wangu mmoja wa Kamati, ndugu yetu Mheshimiwa Mchungaji Msigwa alikwenda katika hatua ambayo sisi hatukufikia kwenye Kamati ya kutaka kuundwa Tume. Kwa kweli sisi tulichofanya kwenye Kamati ni kuunga mkono tamko la Rais la kusema kwamba hayo mashamba yaliyotelekezwa na maeneo ya hifadhi yaliyopoteza hadhi yaende sasa yakafanyiwe mchakato ili warudishiwe wananchi ambao wanateseka. Huu ndiyo msimamo wa Kamati na yale mengine ambayo alisema tumekubaliana, tulichokubaliana sisi yote yameandikwa katika kijitabu cha taarifa yetu ambayo wote mnayo mkononi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kwenye Wizara hiyo ya Ardhi, suala lingine lililojitokeza ni Programu ya Upangaji, Upimaji na Urasimishwaji wa Ardhi na mradi wa mfano ni ule wa Mkoa wa Morogoro ambapo kuna hizo Wilaya tatu za Kilombero, Ulanga na Malinyi ambazo huo mradi umeendelea kutekelezwa. Hoja iliyotokea kwa mmoja wa wachangiaji anaona kama speed ya hiyo kazi ni ndogo sana. Sisi pia mwanzoni tulishikwa na taharuki kwa sababu tuliona kama mradi hauendi lakini baada ya ziara yetu mwezi uliopita tuligundua kwamba ile timu sasa iko imara, wamepata uzoefu na kazi ile inakwenda kwa speed na hofu yetu ikabakia moja tu ambayo kwa niaba ya Kamati naomba niiseme.

Mheshimiwa Spika, hofu yetu ni kwamba fedha za wafadhili katika ule Mradi wa Upimaji na Umilikishaji Ardhi zimekwenda vizuri sana, wao wameshatoa asilimia 90 ya ile shilingi bilioni 28 ambayo ndiyo walitutengea lakini pesa ya Serikali, ile shilingi bilioni 7 mpaka sasa hivi wao wametoa tu asilimia 10. Kwa hiyo, rai yetu kama wajumbe wa Kamati tunaiomba sana Serikali kwamba wajitahidi na wao watimize ahadi yao, watenge fedha za kutosha kwenye bajeti kwa sababu hii misaada ya wafadhili itakapokoma itatukwamisha. Hofu yetu ni kwamba kwa sababu huu mradi unakwenda kufanikiwa kwa kasi na ufanisi mkubwa katika hizi wilaya tatu ni kwamba hatutaweza kunakili au ku- reduplicate katika Wilaya zote za nchi yetu kama sera inavyosema kwamba kila kipande cha ardhi ya nchi hii kitakwenda kupangwa, kupimwa na kumilikishwa. Sambamba na hilo, tulikuwa tunategemea katika zoezi la upangaji wa ardhi ambapo ni mpango wa matumizi bora ya ardhi kila jamii itatenga maeneo mahsusi ya akiba kwa ajili ya vizazi vya baadaye.

Mheshimiwa Spika, hayo ndiyo mambo makuu yaliyojitokeza katika mjadala kwenye Wizara ya Ardhi lakini pia kulikuwa na suala moja ambalo tuliliweka lakini halikuchangiwa ila naomba niseme kwa niaba ya Kamati kwamba, tulipokwenda kutembelea ile mipaka ya nchi yetu na nchi ya Uganda, tulijifunza kwamba alama zilizowekwa tangu enzi za kikoloni (beacons) pamoja na kwamba ni kubwa na zinaonekana kwa mbali, lakini zimefukiwa, ziko mbalimbali na imesababisha raia wa nchi ya kigeni kuvamia ardhi yetu pengine hata pasipo kujua na kuishi kana kwamba wako katika ardhi ya nchi yao.

Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa zaidi ambayo naiomba sana Serikali itilie maanani ni changamoto ya barabara za kuimarisha ulinzi wa mipaka ya nchi yetu. Kwa sababu hakuna barabara ya kuzungukia ile mipaka ili kuiweka madhubuti na kuihakiki na kuwasogeza watu wa nchi za jirani wanaovamia. Kwa hiyo, nimeona kwamba hilo ni pengo moja ambalo wachangiaji hawakuliona lakini sisi kama Kamati tumeliweka katika taarifa yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda, hayo ndiyo mambo ya msingi katika Wizara ya Ardhi lakini kwenye Wizara ya Maliasili mambo yaliyoibuka sana ni ule Mradi wa Kukuza Utalii wa Kanda za Kusini kupitia Mradi wa REGROW na masuala ya misitu. Hoja kubwa nyingine ambayo Wajumbe pia wamechangia na sisi tuliona ni hili la mtawanyiko wa mamlaka zinazosimamia misitu ya nchi yetu. Sasa hivi tuna karibu aina nne za misitu; kuna misitu ya Serikali Kuu, misitu ya Serikali za Mitaa na kuna misitu ambayo iko chini watu binafsi na mamlaka nyingine.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia misitu tuliyonayo asilimia 52 ziko mikononi mwa Serikali za Mitaa na asilimia 35 ndiyo ziko katika Serikali Kuu. Ukiangalia uharibifu katika misitu yetu, asilimia kubwa inatokea katika misitu iliyo katika utawala na usimamizi wa Serikali za Mitaa. Ndiyo maana Kamati katika ripoti yetu imeweka pendekezo kwamba ingependeza na ingefaa sasa na sisi katika Wizara hii tuanzishe mamlaka kamili ya kusimamia misitu badala ya kuwa na Wakala wa Misitu tuwe na Mamlaka ya Misitu kama tulivyo na Mamlaka ya Wanyamapori yaani iitwe Tanzania Forest Authority.

Mheshimiwa Spika, pia wajumbe walichangia kuhusu tozo za utalii na mazao ya misitu. Wazo kubwa ambalo limeungwa mkono ni hili la kusema kwamba tuwe na one stop payment center na kodi zipunguzwe ili kuvutia utalii. Utalii hapa kwetu sasa hivi kwa kulinganisha na nchi za jirani umekuwa ghali na Tanzania as a tourism destination, imeonekana ni ghali ukilinganisha na nchi za jirani kama Msumbiji, Zambia, Afrika Kusini na hata wenzetu hapa Kenya.

Mheshimiwa Spika, pia suala la WMA limeibuka katika mjadala na wachangiaji walikuwa wanasisitiza kwamba WMA zitambulike kama ardhi ya jamii, ambapo jamii ndiyo ina mamlaka nayo juu ya matumizi yake na isiwe na utawala unaofanana na ule wa National Parks wa wananchi kufukuzwa na kusukumwa pale ambapo wamependelea kuishi na kufanyia shughuli zao za kibinadamu. Kubwa zaidi katika WMA, Serikali imekaa mbali nazo hata yale mapato ambayo yanakusanywa na Serikali Kuu inachukua muda sana kurudishiwa na hiyo ndiyo imesababisha WMA nyingi hadhi yake kushuka na pengine baadaye zitakuja kupoteza haki ya uhifadhi na kukosesha jamii mapato.

Mheshimiwa Spika, lakini suala lingine muhimu ambalo limetajwa ni hili la single entry wakati watalii wanapokuja kwenye hifadhi zinazopakana na maeneo ya jamii yenye utalii wa kitamaduni. Kuna malalamiko kwamba wanapoingia wakatamani kutoka na kurudi wanatozwa tena ada nyingine ambayo inawaumiza na inawakatisha tamaa na kuwakosesha wale walioko nje ya parks fursa ya wao nao kupata mgawo wa mkate wanaoleta watalii wanaokuja. Kwa hiyo, tunaomba sana hilo suala ama double entry fee liangaliwe ama uwepo utaratibu wa biometric, zile mashine za kusoma alama za vidole, mgeni akitoka abonyeze ionekane ametoka na ameingia saa ngapi ndani ya zile saa ambazo zinaruhusiwa.

Mheshimiwa Spika, pia hili suala la kuanzisha Utalii Channel tumeliunga mkono sana sisi kwenye Kamati yetu. Napenda tu kusema kwamba kinachohitajika sasa pale ni kutangaza katika lugha mbalimbali za kimataifa pamoja na lugha yetu ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa pia na suala la urudishwaji wa ardhi karibu na maeneo yaliyohifadhiwa. Kuna mwenzetu mmoja katika Wabunge waliochangia ambaye alikuwa anasema kwamba suala hili liangaliwe kwa makini kwa sababu tutakuja ku-block wildlife corridors, yale maeneo au mapito ya wanyamapori. Naungana naye kusema kwamba hilo ni suala la msingi na la muhimu sisi kama wahifadhi kuliangalia. Ni wazi Rais alivyosema kwamba Wizara zikakae ziweke mchakato pamoja na michakato mingine ni kuhakikisha kwamba wamezingatia maslahi ya maeneo ambayo bado yana hadhi ya uhifadhi, yana mapito ya wanyamapori na hawataweza kupangilia makazi ya watu katika maeneo ambayo bado yanatusaidia katika kudumisha rasilimali yetu ya maliasili.

Mheshimiwa Spika, kati ya wachangiaji wa leo, nimepokea michango ya maandishi wachangiaji wane na pia waliochangia kwa kutoa hoja hapa Bungeni wamefikia 16. Napenda kuwashukuru sana wote kwa sababu wamegusia mambo ya msingi ambayo nasi tulikuwa nayo kwenye ripoti yetu na sijapata mawazo yaliyokwenda kinyume na yale ambayo tumeyapendekeza zaidi tu ya kuboresha na kutilia mkazo na sisi tumepokea maoni yenu na naamini kwamba sisi kama Kamati tutakwenda kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, kuna moja ambalo limetokea ambalo sisi hatukuwa nalo kwenye ripoti, kuna mchangiaji mmoja ambaye ameleta kwa maandishi suala la hofu yake kuhusu upimaji wa miji katika ardhi ya wakulima. Akasema kwamba ardhi inapopimwa kwa sababu mji unapanuka na mkulima aliyekuwa anaotesha korosho, mahindi au maharage akaambiwa huwezi kulima tena kwa sababu sasa eneo hili linakwenda kuwa sehemu ya mji linaacha pengo ambapo yule mkulima anakosa mahali pa kuegemea maana mara nyingi anajikuta hawezi kuchukua vile viwanja na hapewi ardhi mbadala. Akasema Kamati katika kazi zake za siku zijazo iliangalie sana kwa makini suala hilo na mimi nalichukua tutaenda kulifanyia kazi. Tungefurahi kujua ni maeneo gani ya mashamba ambayo sasa hivi yanapimwa kuwa miji ambayo wakulima au wakaaji wake wameathirika na jambo hili.

Mheshimiwa Spika, pamoja na maoni mengine yaliyotolewa ambayo yanafanana na yaliyopo kwenye ripoti yetu, naomba nihitimishe hoja yangu kutoka Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa kusema kwamba naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kutoa mchango wangu katika hoja hii iliyoko mezani ya hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Ninapenda kutanguliza shukurani zangu za dhati kwa kazi nzuri inayofanywa na Serikali hii ya Awamu ya Tano na hususan katika mambo mazuri pia yanayofanywa na hii Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Spika, kuna mambo mengi mazuri yanayofanywa na pale mambo mazuri yanapofanywa hatuna budi kutambua na kuunga mkono na kupongeza.

Pia kuna madudu sehemu kadhaa, na hayo pia hayana budi kutolewa maelekezo ndani ya Bunge hili, sisi kutoa ushauri na tutegemee kwamba kuna marekebisho na mabadiliko yatakayofanywa.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote niruhusu pia nitoe shukurani kwa niaba ya watu wa Longido kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa sababu kwa miaka mingi tumekuwa na changamoto ya kutokuwa na gari la kusimamia uhifadhi wa wanyapori na maliasili katika Wilaya yetu. Idara yetu ya Maliasili ya Halmashauri ya Wilaya ya Longido ilikuwa na kilio cha muda mrefu cha kupewa gari la kusaidia doria. Hivi majuzi hata wiki mbili hazijaisha, ndipo gari hilo limepatikana na kwa niaba ya wananchi wa Longido naomba nifikishe shukrani zangu hapa kwa Wizara na kwa Serikali yetu sikivu.

Mheshimiwa Spika, nimepitia hotuba ya Waziri na pia nasimama kuunga mkono maoni yaliyopo katika taarifa ya Kamati kwa sababu nami ni mmojawapo wa wajumbe walioandaa, na maoni yetu tuliyoyatoa ninayasimamia, ninayaunga mkono mia kwa mia na ninaomba yafanyiwe utekelezaji. Bila kusahau lile suala la vigingi vilivyowekwa na TANAPA katika maeneo mbalimbali ya hifadhi za TANAPA ndani ya nchi yetu na yale yaliyogusa maeneo ambayo jamii imekuwa ikiishi kwa miaka mingi bila kuwashirikisha na bila kuwaandaa na kuwafanya watoe ridhaa. Hilo zoezi la kusitisha naomba litekelezwe.

Mheshimiwa Spika, pia nimeona katika hotuba ya Waziri kwamba anafanya overhaul ya vitu mbalimbali, sheria, kanuni na kuna rasimu zimeshaandaliwa. Kwa mfano katika mapitio ya Sera za Taifa kuna rasimu ya Sera ya Misitu na Utalii, anasema imeshaandaliwa.

Mheshimiwa Spika, ningeomba atakapokuja kujumuisha hotuba yake atuambie ni lini itaonekana kwa sababu kuna mapitio mengi ambayo anayafanya na bila sisi kuona na kuridhia inaweza ikawa bado yale mambo ambayo tungependa yabadilishwe yakawa hayatafanyiwa kazi. Kwa mfano, amesema pia kwamba kuna mapitio ya Sheria ya Misitu, kuna utunzi wa Sheria mpya ya Mali Kale, kuna sheria mpya ya uhifadhi wa wanyamapori zinazosimamiwa na TANAPA, Ngorongoro na taasisi mpya ya TAWA, kuna kanuni mpya za usimamizi wa shoroba na maeneo ya wazi yale ambayo wanyamapori wanatawanyikia ambayo kwa asili yake ni maeneo wanamoishi watu.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya uhaba wa muda naomba basi nijikite zaidi katika maeneo matatu katika mchango wangu. Eneo la kwanza niongelee hili suala la WMA’s, eneo la pili nigusie mambo yanayoendelea ya uhifadhi kupitia TANAPA na nipitie pia maeneo yanayosimamiwa na NCAA maana yake ni Ngorongoro Conservation Area Authority, pamoja na taasisi yetu hii ya TAWA.

Mheshimiwa Spika, kuhusu hili la WMA’s, WMA’s ni sera nzuri ya Serikali iliyokuja kubaini kwamba uhifadhi wa wanyamapori nje ya maeneo yaliyohifadhiwa rasmi ni kitu cha muhimu na kisichoweza kuepukwa kwa sababu hatujaweka fence katika hifadhi zetu. Wanyama wanatoka, wanaingia katika maeneo ya jamii na wanapoingia humo maisha yao yanaweza yakawa hatarini, lakini pia wanaleta hatari katika maisha ya watu.

Mheshimiwa Spika, Sera ililenga kuwafanya wananchi wawajibike, kuwatunza hao wanyama na kuwafaidi pia hao wanyama na ndiyo maana WMA’s zilianzishwa. Kwa wale ambao WMA’s zinawaletea kero na hazijawa baraka mimi nawapa pole kwa sababu inategemea mchakato wao waliufanyaje kwa sababu ni mpango shirikishi wa jamii kutunga, kutenga, kupitisha na kuweka utaratibu wa kusimamia rasilimali ya maliasili iliyoko katika maeneo ya jamii.

Mheshimiwa Spika, sisi kule Longido tuna WMA moja ya mfano, WMA ya Enduimet na WMA hii ilitungwa na jamii kwa kushirikiana na Wizara na wadau wa maendeleo ya uhifadhi (African Wildlife Foundation) mimi nilipokuwa Mkurugenzi kule na tuliweka kwamba ni matumizi jumuishi
ambayo yanaruhusu ufugaji na uhifadhi wa wanyamapori ndani ya eneo lile bila vikwazo kwa utaratibu wa mipango ya kanda ambayo imeshawekwa, inafanya kazi na haijafeli hata siku moja.

Mheshimiwa Spika, Ngorongoro iko hivyo hivyo, ule uhifadhi jumuishi ambao unawaruhusu wananchi na wanyama wabaki ndani ya lile eneo la hifadhi halijashindwa, limebaki na limekuwa sahihi na limekuwa salama kabisa kitu ambacho kinakera leo na labda hatujui kama dhana ni nini nafahamu kwamba kuna sensa ambayo imefanyika ya kuhesabu idadi ya watu halali na mifugo iliyoko ndani ya Ngorongoro na inawezekana pia hiyo ikawa ni chanzo cha kutafuta namna ya kuwasogeza watu ndani ya eneo lile.

Mheshimiwa Spika, ninaomba niishauri Serikali kwamba ile dhana ya uhifadhi jumuishi kwa sababu wananchi walitolewa Serengeti wakaambiwa kwamba Ngorongoro wataishi pamoja na wanyamapiri na jamii yetu ya Wamasai kwa asili yao ni wahifadhi wakuu haijashindwa, kinachotakiwa ni mikakati thabiti ya jinsi ya kuendeleza uhifadhi shirikishi bila kuwabughudhi wananchi katika maeneo ambayo wanaishi kihalali na wanaishi sambamba na maliasili ya wanyamapori iliyoko kule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hali kadhalika nikitumia mfano wa WMA ya Makame ambayo pia ilianzishwa mimi nilipokuwa Mkurugenzi wa taasisi ya African Wildlife Foundation ilianzishwa na ikachukua yale maeneo ya muhimu ya wanyamapori ambayo wamekuweko tangu enzi za kale wananchi wale wakiishi katika vile vijiji. Nikisikia leo kwamba kijiji cha Lekuishoibor wako hatarini kupoteza vitongoji vyao viwili, kitongoji cha Lombenek na Enjulah kwa sababu Mkungunero Game Reserve inapanuliwa ije imege yale maeneo ninasikitishwa sana.

Mheshimiwa Spika, ninasikitishwa na kufanya nione kama inawezekana Watanzania tunapotea katika kuhifadhi maeneo yetu kwa kuanza kuhifadhi mpaka maeneo ambayo yalishahifadhiwa tayari na jamii kwa kufikiri kwa kuondoa jamii ndiyo hifadi itafanikiwa. Tunaweza tukashindwa vibaya kwa sababu ya kuwafukuza wananchi katika maeneo waliyohifadhi kwa sababu wao wenyewe ni wahifadhi tayari na tunapowafukuza watapoteza urafiki na wale wanyama, na inawezekana wakawa maadui wa hifadhi badala ya kuwa marafiki wa hifadhi.

Mheshimiwa Spika, nchi yetu haina haja ya kufukuza fukuza watu wanaoishi karibu na maeneo yaliyohifadhiwa, ina haja kubwa ya kutoa elimu, kuwashirikisha, kuwapa manufaa ya uhifadhi ili waweze kuwa wahifadhi sambamba na wale wa taasisi zinazohusika, hatuna uhaba wa maeneo. Naomba ninukuu kwamba kulingana na taarifa zilizopo za Wizara ya Maliasili na Utalii, Tanzania inasemekana imehifadhi asilimia 30 ya ardhi yake. Hata hivyo ukienda katika uhakiki wa kina zaidi, ni zaidi, almost asilimia 40.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, TANAPA wana hifadhi 40 zinazochukua asilimia nne za ardhi ya Tanzania. Ardhi mseto kama ile ya NCAA inachukua asilimia moja. Mapori ya akiba ambayo ziko 28 zinachukua asilimia 13, akiba ya misitu ambayo iko 570 inachukua asilimia 12, mapori tengefu ambayo yapo 44 yanachukua asilimia nane na hifadhi za bahari ambazo ziko nane zinachukua asilimia mbili.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuna iddadi ya maeneo yaliyohifadhiwa 657 ambayo ni sawa na asilimia 40 ya eneo lote la ardhi ya nchi ya Tanzania. Sasa kama tuna hifadhi zote hizi ambazo nchi nyingi za Afrika hazina, kuna haja gani ya kujenga uadui na wananchi wanaoishi karibu na maeneo yaliyohifadhiwa kwa kuwafukuza fukuza na kuwabughudhi? Hakuna haja! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kuna suala lingine ambalo naomba nishauri Serikali. Kuna hili suala la jinsi tunavyoweka enforcement ya kuzuia mifugo isiingie katika maeneo yaliyohifadhiwa. Ni kweli yanahitaji kuhifadhiwa na mifugo inaweza ikaharibu ile ardhi lakini hiyo modality ya kuwapiga fine na kuwakamatia ng’ombe ina kasoro kubwa sana na itazidisha uaduzi miongoni mwa jamii ambayo siku zote wameishi kwa urafiki na wanyapori. Ninaomba na ninaishauri Serikali, wale ng’ombe wote ambao walishashikwa, kesi zikaendeshwa na zikamalizika, ng’ombe waachiwe mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili ninaomba Serikali ifikirie kuondoa hili suala la kupiga watu fine ya pesa kwa sababu kwanza imeleta mazingira mabaya sana ya ufisadi. Wale watekelezaji wa hizi sheria kule chini wengine wamekuwa mamilionea kwa sababu ya hili zoezi. Ninaomba ule utaratibu sasa utumike kwamba hawaruhusiwi kupokea pesa, hawaruhusiwi kutoza faini, ikiwezekana ng’ombe wanapokamatwa kwa sababu wameingia pale, utaratibu tu ufanyike wa kuwa-identify kwamba ni wa nani na wakaandikishwe na mwenye ng’ombe awajibishwe kulingana na sheria zilizopo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja na ninaomba baadaye nipate maelezo kwamba ni kwanini WMA ya Lake Natron haijasajiliwa mpaka leo na wakati mchakato wote ulishamalizika, niko tayari kushika shilingi kama Waziri hataniambia kwa nini WMA ya Lake Natron haijapatikana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa na mimi niweze kuchangia kwenye hoja hii ya Wizara ya Maji. Kwanza nitangulize shukrani za pekee kwa Mheshimiwa Waziri na kwa timu yake yote kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Nitumie fursa hii kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa sababu kati ya watu ambao wameguswa na kujaribu kutatua tatizo la maji nchini ni pamoja na Wilaya yangu ya Longido baada ya ule mradi mkubwa wa maji kutoka Mto Simba kwenye Nyanda za juu za Mlima Kilimanjaro kufikisha yale maji Longido na watu wamefurahia na maji yale kwa kweli yamekuwa ukombozi maana kiangazi ambacho kimekuwa kinaendelea kilipelekea watu wanunue maji mpaka Sh. 1,500 kwa ndoo kutoka katika vyanzo mmbalimbali. Tunaishukuru sana Serikali kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mawazo mazuri yaliyojitokeza katika hotuba hii na nimeona mambo mengi mazuri yanayofanyika, mimi kwanza niwaunge mkono Waheshimiwa Wabunge wanaosema kwamba tuweke miguuu chini leo mpaka Wizara ya Maji watenge fedha za kutosha kuhakikisha kwamba maji yanamfikia kila Mtanzania ili azma yetu ya kumtua mama ndoo kichwani iweze kutimizwa kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwa sababu hii fedha ya Mfuko wa Maji ambayo asilimia 70 imepatikana ikaenda kwenye maji na asilimia 17 tu ndiyo imepatikana kwenye vyanzo vingine, imeonesha kwamba kumbe tungetenga fedha nyingi zaidi kwa vyanzo mbalimbali vya Serikali tungeweza kufikia malengo. Ninaiomba Serikali izingatie suala hili la kuongeza hiyo tozo kwenye mafuta ifike shilingi 100, lakini pia ikamue percent fulani katika kila aina ya tozo inayotozwa kwa huduma mbalimbali katika vyanzo mbalimbali ambavyo Serikali inatoza kodi katika nchi hii. Iwe ni katika Sekta ya Utalii, iwe ni katika Sekta ya madini; sekta zote ambazo Serikali huchukua tozo wekeni percent kidogo iende kwenye kuboresha Mfuko wa Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na tuzingatie kwamba sasa hivi tuna RUWASA, sasa RUWASA kama ni taasisi iliyoundwa ya kuhakikisha kwamba kuna wataalam wa kutosha, kuna vifaa vya kutosha, watapataje kuendesha kwa ufanisi kama hawana fedha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninaomba kwanza kodi zinazokera, za kuumiza hizi tasisi za maji, ziondolewe, kama mitambo ya maji ifutiwe kodi, vifaa vya kuchimba mabwawa vifutiwe kodi na kila namna ifanyike ili kuhakikisha kwamba tunauinua huu mfuko ili tumtoe mama ndoo kichwani na kweli tufikishe huu uhai ambao tunasema maji ni uhai kwa kila Mtanzania. Tukipata maji safi na salama katika nchi hii miradi mingine yote ya maendeleo itawezekana. Afya ya watu itaboreka, muda wa kuwekeza kwenye shughuli nyingine za uchumi utaimarika maana muda mwingi hupotea katika kutafuta maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuunga mkono hiyo hoja na kutoa dukuduku langu la kutamani Wizara iongeze bajeti yake, naomba nijielekeze katika masuala mahususi ambayo yamejitokeza katika hii hotuba, na imegusa miradi ambayo inagusa sana maisha ya wananchi wa Jimbo langu la Longido. Katika ukurasa wa 119 kuna kiambatisho namba 2 kinachoongelea kiwango cha maji katika maziwa, mito mabwawa na vyanzo mbalimbali vya maji nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mto unaitwa Mto Ngarenanyuki, huu mto unatiririsha maji kutoka Arusha National Park unapitia Arumeru unakuja mpaka Longido, Kijiji cha Ngereiyani. Maji yake yana fluoride nyingi, sio mazuri kwa binadamu, lakini yanafaa sana kwa kilimo cha nyanya. Wakulima wengi wamegundua kwamba hayo maji yanaotesha nyanya ya ubora wa kimataifa, nyanya zinauzwa kila mahali nchi hii, Dar es Salaam, mpaka nchi za nje, Mombasa na zinakwenda mpaka Nchi za Uarabuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa kwa matumizi holela ya huo mto mifereji imepasuliwa kila mahali, nyanda za mto zimeharibiwa, huo mto unakwenda kupoteza hadhi yake na mazingira yanaharibika na maji hayafiki tena kwenye nyanda za chini, wananchi wa Ngereiyani hawapati tena yale maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Serikali pia iweke usanifu wapime kiwango cha hayo maji na ikiwezekana wajenge matenki maji yapitie kwenye matenki ndiyo kutoka kwenye mabomba yaende kwenye mashamba ya wakulima wadogo wadogo ili tuhifadhi mto na watu wengi waweze kufikiwa na hayo maji, tuboreshe kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kwa sababu maji ya Mto Simba yanakwenda kusuluhisha tatizo la maji kwa wakazi ambao kwa sasa hivi, hii awamu ikikamilika ni watu kama 18,000 tu wa Kata ya Longido na Kata ya Engikaret na kwa sababu tumetengewa bilioni 2.9 na ninaishukuru Serikali sana kwa sababu ya usambazaji wa hayo maji. Basi huu mradi utakapokuwa umesambaza hayo maji yakatimiza ahadi ya viongozi wakuu wa Serikali akiwepo Rais ya kupeleka hayo maji mpaka Namanga, Kimokowa na kusambaza kule Kiserian, tutakuwa tumetatua kero ya maji kwa wananchi wasiopungua 30,000 wa Longido, lakini bado kuna watu zaidi ya 100,000 ambao hawana chanzo cha uhakika cha maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilishawahi kusema katika Bunge hili kwamba maji ya mafuriko ya mwaka jana yalitupasulia mabwawa ambayo ndiyo yalikuwa yanategemewa na jamii ya wafugaji katika wilaya yangu. Kuna mabwawa yamefukiwa kabisa, kuna mabwawa yamepasiuka, nilitegemea kwenye bajeti hii kwenye ile miradi mingine ambayo Waziri ametaja katika hotuba yake, kuona kuna miradi mingine ya maji ukiacha haya maji ya mito; ningetegemea mabwawa yale yaliyopasuka na yaliyojaa udongo yangetengewa bajeti maana sisi mabwawa hayohayo ndiyo maji ya binadamu ndiyo hayohayo ya mifugo; Bwawa na Kimokowa, Bwawa la Tinga Lesing’ita, Bwawa la Sinoniki, Bwawa la kule Muriatata na mabwawa mengine mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuna ahadi za Serikali za kuchimba pia mabwawa mengine ambayo yatafaa kwa hata umwagiliaji pale katika Kata ya Tingatinga. Kuna ahadi ya Serikali ya kuchimba bwawa la umwagiliaji ili haya maji yanayotiririka ya msimu wa mvua kutoka Kilimajaro yatekwe wananchi wa Tingatinga waweze kuendesha kilimo cha umwagiliaji na maji hayohayo yatafaa kwa mifugo na watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kule Wosiwosi, mwisho wa Wilaya hii ya Longido katika Ukanda unaopakana na Kenya na Wilaya ya Ngorongoro kuna Kijiji kinachoitwa Wosiwosi, wao maji ya kunywa binadamu hakuna kabisa mpaka wanakwenda Kenya kutafuta maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliomba pia bwawa na nilitegemea bwawa hilo lingewekwa kwenye ile miradi mingine ili wananchi wa Longido ambao wako mbali na haya maji ya Mto Simba waweze nao kufarijika na kuona kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inawajali kwa suala la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie fursa hii kuwashukuru baadhi ya wadau ambao wametuunga mkono katika kutatua kero za maji Longido; tuna Shirika la Maisha Bora, wamekuwa wakitusaidia katika miradi ya kuchimba visima virefu katika Kata ya Matale; kuna taasisi ya kiwindaji inaitwa Kilombero Safaris wakishirikiana na Shirika linaitwa World Self International, wamekuwa wakitusaidia kupima maeneo mbalimbali kubainisha maeneo yenye maji ya chini pamoja na wengineo kama Friends for African Development, marafiki zetu kutoka Chuo Kikuu kimoja cha Marekani ambao wametuchimbia visima vitatu. Naomba Serikali itambue juhudi zao na iendelee kututengea fedha za kuchimba visima virefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ambalo ninapenda kuchangia ni suala la umuhimu wa kuvuna maji ya mvua katika nchi yetu. Maji ya mvua yakivunwa, na sheria ipitishwe – maana kabla sijawa Mbunge ilishatengeneza sheria lakini sidhani kama inafanyiwa kazi – na iwekwe kwamba ni kampeni ya kitaifa; kila kaya wahimizwe wawe na mfumo wa kuvuna maji ya mvua, iwe ni sehemu ya requirement katika kusimamia utekelezaji wa ujenzi wa nyumba za makazi ya watu na taasisi mbalimbali nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ya mvua yatatuondolea kero ya maji kwa asilimia kubwa. Inaponyesha hata katika maeneo kame maji mengi yanapotea kwa sababu hatuvuni maji ya mvua na nimeenda katika nchi zingine, kama Jimbo la California kule Marekani, wao hawana mto wowote lakini maji yote ya mvua yanavunwa na wanalimia mpaka wanauza mazao ya matunda nchi za nje; kwa nini sisi Tanzania wenye maji mengi ya mvua ambayo yanafurika kila wakati inaponyesaha, hata katika maeneo kame tusiige huo mfano tukahimiza uvunaji wa maji ya mvua katika mabonde, tuhimize uvunaji wa maji ya mvua katika nyumba zetu za bati kila kaya ihimizwe iwe na mfumo na wataalam wa Serikali wasimamie hiyo kama kampeni mahususi katika shule, katika hospitali, katika taasisi za dini na nyumba za makazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa lakini sio kwa umuhimu, nipende pia kutumia fursa hii kuishukuru Serikali kwa sababu sisi katika Wilaya ya Longido ambayo ni wilaya ya wafugaji kwa asilimia 95, na ni wilaya ya uhifadhi pia wa mazingira ya wanyamapori kwa asilimia hiyohiyo 95, tumeendelea kuona mkono wa Serikali kupitia kile chakula tulichopewa wakati wa ukame. Wananchi wa Longido wamefarijika na wamesema kila wakati ukisimama Bungeni mshukuru Rais kwa sababu tulipolia njaa kwa sababu ya ukame tulipewa chakula, tulitengewa chakula tani 10,000 za mahindi na tani 1,000 ndiyo zinazoendelea kuwalisha watu katika mwezi huu wote tunavyoangalia hali ya hewa itakavyokuwa. Na tumshukuru Mungu mvua imenyesha lakini haitoshelezi.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii haikuangazia utekelezaji wa Dhana ya Hifadhi za Jamii (WMA). Nilitegemea kupata taarifa kuhusu idadi ya WMAs zilizosajiliwa tangu dhana hii ianzishwe chini ya Sera ya Wanyamapori mwaka 2003 hadi sasa (miaka 15) na manufaa ya kiekolojia na uchumi yaliyopatikana. Jamii zenye WMA zimefaidikaje? Serikali imefaidikaje? Serikali ina mkakati gani kuendeleza dhana ya WMAs na WMAs ngapi zinatarajiwa kuanzishwa zaidi katika nchi yetu?
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja zote mbili zilizowasilishwa na Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii pamoja na Kamati ya Masuala ya UKIMWI. Napongeza kazi nzuri walizofanya Kamati zote mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia maoni yangu katika masuala matatu yaliyonigusa katika taarifa ya Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza, katika ukurasa wa 49 hadi mwanzo wa ukurasa wa 50, Kamati imetoa maoni na kupendekeza Serikali ilipe kipaumbele suala la kutoa elimu ya lishe kwa jamii. Naafikiana na mapendekezo haya lakini pia naomba ligusiwe suala la watu au jamii ambayo inakabiliwa na janga la njaa. Pamoja na umuhimu wa kutoa elimu juu ya lishe, Serikali ipange mkakati wa kuwapa chakula jamii zinazokabiliwa na ukame wa muda mrefu katika Wilaya za Kaskazini, Mashariki ya nchi yetu hususan Wilaya za Longido Ngorongoro na Monduli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la pili, linahusu maboresho yanayohitajika kwa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), tazama ukurasa wa 50. TBC Radio ndicho chombo kinachotegemewa kupata habari, elimu na burudani na asilimia kubwa ya wananchi wanaoishi vijijini mahali pasipo na TV wala magazeti au upatikanaji wa Radio za FM. Kwa jamii za pembezoni hasa wale waishio karibu na mipaka ya nchi jirani, wanaishia kupata huduma muhimu ya habari, elimu na burudani kupitia radio za nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maboresho yaliyopendekezwa na Kamati, naomba kipaumbele kitolewe katika kuboresha miundombinu ya kisasa na kuiwezesha Radio ya Taifa isikike katika kila kona ya nchi yetu kupitia mid-wave(MW) na FM frequencies.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu, ninalopenda kuchangia ni kuhusu Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kama ilivyoelezewa katika ukurasa wa 61 wa taarifa ya Kamati. Nakiri kwamba ni kweli Elimu ya Watu Wazima imedorora katika nchi yetu, lakini siafiki taasisi hii kufutwa bali ihuishwe kwani bado kuna watu wengi katika nchi yetu na hasa katika jamii za wafugaji ambao hawajui kusoma na kuandika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile, napendekeza Serikali ianzishe taasisi mahsusi ya Elimu ya Awali nchini. Hili ni kutokana na hali halisi kwamba Kiwango cha Elimu ya Awali ni duni mno katika jamii ya vijiji ambapo umbali wa shule kwa kaya nyingi ni kati ya kilomita kumi hadi kumi na tano hasa Umasaini. Kwa maoni yangu kazi ya Taasisi ya Elimu ya Awali itakapoundwa itakuwa ni pamoja na:-

(1) Kuhakikisha kila kitongoji kwa jamii za vijijini wanakuwa na shule ya awali yenye kukidhi haja ya kuwajengea watoto wetu wachanga msingi bora wa elimu.

(2) Kubeba jukumu la kusomesha na kuajiri Walimu stahiki wenye sifa kamili za kutoa Elimu ya Awali kwa watoto walio chini ya umri wa kuanza elimu ya msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ilivyo kwa sasa utakuta katika vitongoji vilivyo mbali na shule ya msingi kwa watoto wadogo kuweza kutembea, shule za awali zinafundishwa na failures wa darasa la saba ambao ni wanakijiji wa kawaida tu wasio na taaluma yoyote ya ualimu zaidi ya kujua kusoma na kuandika.

(3) Kuandaa na kusambaza mitaala ya Elimu ya Awali katika shule zote za awali nchini pamoja na kuzisimamia shule za awali hadi zile za ngazi ya kitongoji kwamba Wizara ya Elimu inavyosimamia shule za msingi na sekondari.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, kwanza naipongeza Serikali yetu ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri ya kupeleka mbele maendeleo ya nchi yetu. Nampongeza Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu, Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa pamoja na Baraza lote la Mawaziri.

Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa hotuba hii ya bajeti na kazi kubwa anayofanya yeye na Naibu wake kuendeleza sekta ya mifugo na uvuvi.

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizi, naomba nichangie hoja ya bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara izingatie umuhimu wa kuongeza bajeti ya kutekeleza vipaumbele vya sekta ya mifugo kama vile upatikanaji wa maji, majosho, dawa, tiba na masoko.

Mheshimiwa Spika, kutokana na bei ya mifugo kuyumba kila wakati kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa hususani katika Wilaya za Kaskazini Mashariki kwa nchi yetu ikiwemo Longido, Monduli, Simanjiro na Ngorongoro, naiomba Serikali kupanga bei elekezi ya kuuza mifugo kwenye masoko yetu kama mazao mengine mfano zao la pamba na korosho ambazo hupangiwa bei kwa kilo. Ng’ombe nao wapangiwe bei kwa kilo kwa ng’ombe hai na nyama ili wafugaji wapate tija zaidi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu masoko/minada inayoanzishwa mipakani na Halmashauri za Wilaya kama soko la Halmashauri ya Wilaya ya Longido lililopo Eorendeka. Soko hili lilibuniwa na Halmashauri kwa makusudi ya kuinua mapato ya ndani ya Halmashauri na kuwapatia wananchi mnada wa uhakika na kuuza mifugo kwa faida ili kuinua kipato chao. Kwa kuwa Wizara imejitokeza na kuja kunyakua mnada wa Eorendeke na ninatambua kuwa pia Serikali Kuu inahitaji kodi, nashauri Serikali ichukue tu asilimia ndogo ya kodi na kuwaachia Halmashauri ndio wenye jukumu kubwa la kuendelea kuimarisha na kusimamia wafanyabiashara ili mnada/soko la mifugo la ndani liimarike.

Mheshimiwa Spika, kuhusu viwanda vya kuchakata bidhaa za mifugo, napenda kuishauri Serikali iwakopeshe wananchi ili waweze kuanzisha viwanda vidogo vya usindikaji maziwa, nyama na ngozi na pia Serikali ifufue viwanda vilivyokuwepo kwa mfano Kiwanda cha Maziwa kilichotelekezwa na mwekezaji Longido. Kwa kufanya hivyo wananchi watanufaika na mazao ya mifugo.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kuishauri Serikali ianzishe kiwanda kikubwa cha ngozi pamoja na mazao yote ya mifugo na kuwa na viwanda vidogo katika mikoa yote ya wafugaji. Ngozi ni bidhaa ya thamani sana kwa mfano Ethiopia ngozi zina bei kubwa ndani na nje ya nchi hiyo.

Mheshimiwa Spika, kuna tatizo kubwa linalowakabili wafugaji la kupoteza mifugo kutokana na kula mifuko ya plastiki. Licha ya mifuko hii ambayo imetapakaa kila mahali katika nchi yetu kuchafua na kuharibu mazingira, mifugo wengi wanaangamia wakati wa kiangazi na kula karatasi hizo za plastiki. Naomba kuishauri Serikali ipige marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki katika nchi yetu. Rwanda na Kenya majirani zetu wao wamepiga marufuku na wamefanikiwa, sisi pia tuige mfano wao.

Mheshimiwa Spika, hoja kuhusu mnada wa mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido iliyo Kijiji cha Eor Endeke Longido, mnada huu umejengwa kwa juhudi za Halmashauri bila msaada kutoka Wizarani. Lengo la mnada huu ulio karibu na mpaka wa Kenya na Tanzania katika eneo la Namanga lilijengwa kwa kusudi la Halmashauri kujiongezea mapato ya ndani na wananchi kupata soko la mifugo yao.

Mheshimiwa Spika, leo hii kuna kero kubwa imejitokeza baada ya Wizara kuja kuingilia mnada huo na kupanga kodi kubwa ya ushuru wa Serikali wa shilingi 20,000 kwa ng’ombe na shilingi 5,000 kwa mbuzi na kondoo. Kodi hii si rafiki kwa wananchi na hali hii imewakatisha tamaa na kupelekea kuanza kurudi tena kupitishia mifugo maporini kuvusha Kenya ili kuendeleza biashara zao. Hivyo kupelekea Serikali Kuu na Halmashauri kupoteza mapato.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hii, naomba kuishauri Wizara na Serikali izingatie kufanya yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ipunguze kodi kwa kushauriana na wananchi, itoe huduma za export permit palepale mnadani badala ya kwenda hadi Arusha au Wizarani. Wizara ya Mifugo wakae na Halmashauri waafikiane jinsi ya kuendesha mnada huu ili uweze kuleta tija kwa wananchi, Halmashauri na Serikali Kuu.

Mheshimiwa Spika, mwisho wajasiriamali wa mifugo (wachuuzi) na wananchi wa Longido wanaiomba Serikali yetu sikivu iwatafutie soko la ndani la uhakika kwani wasingetamani kupeleka mifugo kwenye minada na masoko ya nchi jirani kama siyo ni kutokana na kutokuwepo mnada wenye bei nzuri nchini ukilinganisha na nchi ya jirani.

Mheshimiwa Spika, changamoto ya wafugaji waliopoteza ardhi kwa ajili ya uwekezaji na uhifadhi; mfano wa mashamba yaliyoko Kanda ya West Kilimanjaro, wafugaji walikuwepo West Kilimanjaro kabla ya Bara la Afrika kugawanywa na wakoloni mwaka 1884. Wajerumani ndio
wakoloni wa kwanza kuitawala Tanganyika na ndio waliowatoa wafugaji kutoka katika nyanda za juu zenye rutuba, mvua za uhakika, malisho na maji kwenda katika maeneo ya mbugani ambayo ni makavu na yasiyo na maji wanapoishi hadi leo.

Mheshimiwa Spika, baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia mwaka 1945 Serikali ya Uingereza baada ya kukabidhiwa koloni la Tanganyika na Umoja wa Mataifa wakati huo ukiitwa The League of Nations, waliwazawadia wanajeshi waliopigana Vita ya Pili ya Dunia yale maeneo. Wafugaji wakaendelea kubaki bila ardhi yenye maji na malisho ya mifugo yao nyakati za kiangazi.

Mheshimiwa Spika, mwaka 1968 baada ya Serikali kutangaza Azimio la Arusha na kutaifisha yale mashamba, Rais wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Mungu ampe heri ya milele) alipotembelea Wilaya ya Maasai kama ilivyojulikana wakati huo alisikitika alipobaini kuwa wafugaji hawana ardhi inayofaa kwa malisho na maji ya mfugo yao nyakati za kiangazi. Akaagiza wapewe ekari 5,500 kwa ajili ya malisho ya mifugo yao. Tarehe 13/3/1973 Bunge liliridhia wafugaji kurudishiwa hizo ekari 5,500 na tarehe 16/3/1973 Serikali ilitenga rasmi ekari 5,500 za malisho kupitia GN No. 59.

Mheshimiwa Spika, TANAPA ilipopitisha operation ya kubaini na kuweka alama mipaka ya Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro miaka ya karibuni eneo hilo lilijumuishwa katika Hifadhi ya KINAPA (Kilimanjaro National Park).

Mheshimiwa Spika, naomba kuishauri na kuiomba Serikali iwape wafugaji hawa ardhi mbadala katika mashamba pori ya NDC, NARCO na NAFCO yaliyoko katika ukanda huo wa West Kilimanjaro.

Mheshimiwa Spika, aidha kuna mashamba mawili ambayo matumizi yake yamekuwa yasiyo na tija, hususani West Kilimanjaro Ranch yenye jumla ya ekari 95,000 na ng’ombe wa NARCO wasiofika 200 na Endarakwai Ranch yenye ekari 11,000 ambayo mwekezaji mmoja wa kiingereza, Peter Jones, analitumia kufugia wanyamapori na mifugo hawaruhusiwi kuingia.

Mheshimiwa Spika, mwaka 1982 Rais wa Awamu ya Kwanza, Hayati Mwalimu Nyerere alimwagiza aliyekuwa Waziri Mkuu wakati huo, Hayati Edward Moringe Sokoine (apumzike kwa amani) kuanzisha Ranchi ya Jamii ya Larkarian. Ardhi husika iliainishwa, Mbunge na Waziri Mkuu wa wakati huo, Hayati Sokoine aliwahamasisha wafugaji wakachanga mitamba 1,500. Lakini baada ya kifo chake, mradi wa Ranchi ya Jamii nao ukafa. Baada ya Hayati Sokoine na Mradi wa Ranchi ya Jamii kufa, wawekezaji wakapewa ardhi hiyo ambayo inajumuisha mashamba nane yafuatayo; Ndarakwai Ranch, Roselyn Farm, Tilonga Farm, Simba Farm, Mountain Side Farm; Engushai Farm, Mawenzi Farm na Leghumushira Farm.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa baadhi ya mashamba haya yamekuwa mashamba pori. Kwa hiyo, naomba kuishauri na kuiomba Serikali iwarejeshee wafugaji wa Kanda ya West Kilimanjaro ardhi hiyo au wepewe mbadala kwa ajili ya shughuli zao za ufugaji na hasa kufufua Mradi wa Ranchi ya Jamii.

Mheshimiwa Spika, Ndarakwai Ranch yenye ukubwa wa ekari 11,000 ilikuwa ni mojawapo ya maeneo muhimu ya jamii ya Kimasai ya kulisha mifugo yao hadi wakoloni walipojimilikisha. Ni baada ya Azimio la Arusha mwaka 1967 ndio Serikali ilitaifisha shamba hili na kuikabidhi TBL.

Mheshimiwa Spika, mwaka 1992 TBL ilibinafsisha shamba la Endarakwai kwa Kampuni ya Tanganyika Film and Safari Outfitters inayomilikiwa na Bwana Peter Jones, raia wa Uingereza. Mwekezaji huyu aligeuza shamba hili kuwa pori la kufugia wanyamapori na amekuwa na ugomvi mkubwa na wafugaji wanapojaribu kwenda kulisha katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, wafugaji wa West Kilimanjaro wanaiomba Serikali iwarejeshee ardhi hii.

Mheshimiwa Spika, naomba kuhitimisha kwa kutoa kilio cha wafugaji, wafugaji wana matatizo mengi lakini kubwa zaidi ni la kunyang’anywa ardhi yao ya asili katika sehemu mbalimbali za nchi yetu ikiwemo eneo hili la West Kilimanjaro nililojadili, Serengeti, Tarangire, Mkungunero na maeneo mengine mengi ndani ya nchi yetu. Maeneo haya yalibadilishwa kuwa ya matumizi mengine yenye maslahi mapana kwa Taifa lakini tatizo ni kuwaacha wenyeji bila ardhi inayofaa ya mbadala kwa malisho na maji ya mifugo yao na watu.

Mheshimiwa Spika, naiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi ichukue hatua za kizalendo na watatue migogoro ya ardhi ya wazawa iliyotwaliwa kwa jina la uwekezaji na kugeuzwa kuwa mashamba pori yasiyo na faida kwa Serikali wala wananchi na badala yake, yamekuwa chanzo cha ufilisi kwa wafugaji maskini ambao kila wanapokanyaga mashamba pori hayo wakitafuta malisho na maji wakati wa kiangazi wanakamatwa, wanapigwa na kutozwa faini kubwa zinazozidi kuwakandamiza kiuchumi na kuwaacha katika umaskini mkubwa zaidi.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha na ninaunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia kwenye hoja hii iliyopo mezani, ya Bajeti yetu Kuu ya Serikali. Nitumie fursa hii kuipongeza sana Wizara hii chini ya uongozi wa ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na Naibu wake Mheshimiwa Hamad Masauni na watendaji wote, kwa sababu kazi mliyofanya kutuletea bajeti hii iliyofurahisha taifa hili lote, na inawezekana hata mataifa ya jirani sio kazi ndogo, hongereni sana. Lakini pia nimpongeze Rais wangu, Mheshimiwa mama yetu, Mama Samia Suluhu Hassan, kwa sababu bajeti hii imeakisi maono yake; na nadhani ndiyo maana Mheshimiwa Waziri kila wakati ulisema mama amesikia kilio chenu akafanya hiki, amesikia kilio chenu akafanya kile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamshukuru sana kwa sababu amesikia kilio cha Watanzania ambao tunawawakilisha hapa Bungeni na amefanya mambo makuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sina haja ya kuangalia mambo mazuri yaliyofanywa kwenye bajeti hii kwa sababu mengi yameshasemwa. Mimi nadhani kazi yangu hapa ni kutoa tu ushauri katika maeneo madogo madogo ambayo nadhani yangeweza kuboreshwa ili Watanzania waendelee kuneemeka na bajeti hii ambayo miongoni mwa vipaumbele katika miradi ya maendeleo ni kuwawezesha wananchi kiuchumi. Kuna mambo ambayo tusipoyazingatia tukayaweka sawa tutakuwa hatujawatendea haki baadhi ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, katika eneo la mifugo kuna changamoto kubwa kwa sababu, kwanza bajeti yao ni ndogo, bilioni 16, kwa sekta ambayo ina rasilimali ya mifugo ambayo ni ya pili katika Bara la Afrika na malengo waliyojiwekea?

Ninaunga mkono kabisa maoni ya Kamati wamesema kwamba miongoni mwa malengo makuu ambayo wamependekeza Wizara ya Mifugo ifanye ni kuwezesha upatikanaji wa maeneo ya malisho, kuwezesha upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo, kutenga na kupima maeneo ya malisho, kusimamia suala la utafiti wa mifugo, kutatua migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, kuimarisha vikundi, kuboresha mbegu na mambo kama hayo. Sasa, kwa bilioni 16 utafanya nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi nilikuwa napenda tu kuwashauri basi wasimamiaji wa utekelezaji wa bajeti hii katika sekta husika na Wizara yenyewe kwa ujumla, Wizara ya Fedha, kwamba tuangalie maeneo mahususi ya kipaumbele ili basi tuone kama na mfugaji naye atakwamuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, hili suala la migogoro ya ardhi kati ya watumiaji wengine wa ardhi ni suala nyeti sana. Napenda kuishauri Serikali kwamba, Wizara ambazo zinaguswa moja kwa moja na migogoro inayozuka zikae pamoja, zipitie sheria na kanuni na taratibu, zije na mfumo sahihi ambao utasaidia kutatua migogoro hiyo ili upatikanaji wa ardhi ya malisho iweze kubainishwa na maeneo ya watumiaji wengine yaweze kuwekwa wazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Wizara ya Ardhi ambao ndio wapimaji wa ardhi, Wizara ya TAMISEMI ambayo ndiyo wenye vijiji, Wizara ya Maliasili ambao ndio wananyakua nyakua hati za watu bila hata kuwashirikisha wengine, wakae pamoja na Wizara ya Mifugo, ili kumaliza migogoro ya ardhi ambayo inajitokeza kila wakati na kupunguzia wafugaji maeneo yao. Na nina-reference nzuri kwa sababu kumbukumbu tuliyonayo sisi watu wa Longido kuna eneo linalotaka kutwaliwa la malisho. Eneo mahususi la malisho wakati wa kiangazi, eneo la Lake Natron na milima yote inayozunguka huo uwanda wa Longido. Haiwezekani Wizara moja ikachomoka ikaenda kutangaza eneo kwamba wanataka kulifanya pori la akiba, na ni la wafugaji na Wizara ipo, TAMISEMI waliotambua vijiji wenye hiyo ardhi wapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hayo ni masuala ya msingi ambayo lazima tuishauri Wizara ya Fedha na Mipango, waangalie wanapotenga fedha ielekezwe kwenye yale masuala ya msingi ambayo yatatusaidia kusonga mbele na kupata maendeleo ya Watanzania wote kama yalivyokusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo pia, ningependa kushauri Serikali katika maeneo mengine mahususi; kama kwenye hii sekta ya maliasili ambayo Mbunge mwenzangu wa Arusha ameshasemea na kutoa takwimu. Mimi napenda tu kuiomba Serikali, kwamba itoe kitu kinachoitwa incentive package ya kuchochea utalii ili uweze kurudi; kwenye sekta zote, utalii wa kuona wanyama, utalii wa uwindaji, wapunguze bei ili watalii warudi. Maana sasa hivi pamoja na corona South Africa wao wanapata watalii kwenye maeneo yao ya kiwindaji mpaka milioni tisa kwa mwaka. Namibia wanapata mpaka milioni nane, na hata Zambia ambao wote kwa pamoja hawana maeneo mengi ya uhifadhi kama sisi na ya uwindaji lakini kwa sababu, sisi bei zetu tumeziweka juu na hatuna mpango wa kupunguza bei ili kuvutia tumeendelea kuathirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuchochee utalii wa ndani. Utalii wa ndani utaimarika pale ambapo packages zitatangazwa, ziwekwe bayana kabisa kwamba watoto wa shule, watu wazima, ma-group yanapoungana wakienda kutalii kwa bei ndogo kabisa, hapo kila mtu atataka kuona hifadhi zetu na mapato yatapanda kwa njia hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Sekta ya madini. Napenda kuishauri Serikali kwa sababu watu waliposikiliza hii bajeti wakaanza na wao wananchi ambao tunawakaribisha kurusha kero zao. Kwa mfano, Ninalo andiko hapa watu wa madini wanasema kuna kitu kinaitwa kodi ya pay as you earn na kuna kodi inayoitwa SDL ambayo nadhani hiyo inahusika na masuala ya Skills Development Levy, sijajua Kiswahili chake. Wanasema kwamba TRA hasa kwenye migodi ya madini haya ya Tanzanite, wanawalazimisha wale wachimbaji wawalipe watu mishahara, wakaweka na viwango na kumbe makubaliano yao huwa ni kwamba wanalipana baada ya mali kupatikana na ni mfumo ambao ulishakubalika. Kwa hiyo ingebidi TRA wasiwalazimishe watu hawa wa madini kulipa fedha ambayo wenzao wanaochimba bado hawajapata na watambue kwamba kuna utaratibu waliokwishajiwekea tayari.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni tozo la huu Wakala wa Meli Tanzania inaitwa TASAC. Wao huwa wana- charge fedha tu lakini hawa-track ule mzigo, wao wakishapokea tu wakishalipwa basi hawana taarifa ya ku- track huo mzigo mpaka umfikie mnunuzi katika nchi aliyopo. Watu wa sekta ya madini hawa nao wanaotuma madini nje, wanaomba kwamba hilo Shirika la TASAC halina msaada wowote kwao, charge hizo wanazo-charge hazina maana kwa hiyo ziachwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu eneo la ongezeko la thamani kwenye biashara kati ya wafanyabiashara wa ndani, kwenye soko lile kuna watu wanaouuza na kununua mlemle. Wenzao wale wanaowauzia wanatoza VAT na VAT ilishaondolewa, kwa hiyo nalo pia liondolewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa, kuna kitu napenda kuongeza kabla ya muda wangu haujakwisha, kwamba Madiwani walivyowaongozea maslahi yao na Watendaji wa Kata imekuwa ni nderemo, vifijo na furaha kwa nchi nzima. Hata hivyo, kuna watu ambao ndio wako kwenye ground, kule ambako ndio tyre inagusa lami. Watendaji wa Vijiji hawajafikiriwa katika kuwawezesha. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kiruswa kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Francis. Karibu.

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba Madiwani hawajaongezewa fedha bali wamewekewa kulipwa na Serikali Kuu kwenye Akaunti zao. Posho zao sio kwamba wameongezwa, ili taarifa zikae vizuri.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Kiruswa, unapokea taarifa hiyo?

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea hiyo taarifa, nashukuru kwa sahihisho lakini kile kitendo cha wao kulipwa moja kwa moja kimewaondolea adha na kero kubwa sana. Kile kitendo cha Watendaji wa Kata kupewa dhana, vitendea kazi, mafuta pia imewaongezea ari ya kufanya kazi kwa bidii sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kundi ambalo limesahaulika, Watendaji wa Vijiji na wao wanafanya kazi kubwa, ingefaa katika bajeti hii na wao wafikiriwe. Kwanza katika vijiji vingi katika nchi hii likiwemo Jimbo la Longido, sisi asilimia 75 hawajaajiriwa wana kaimu kwa miaka mingi sana, sijajua bajeti wanawaweka wapi na kama shida ilikuwa ni fedha itafanyika nini ili Watendaji wa Vijiji waajiriwe katika nchi nzima ambapo kuna Makaimu wasiohesabika na kwa miaka na muda mrefu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuchangia hoja yangu ya mwisho kwamba katika kupanga haya maendeleo ambayo hii bajeti inakwenda kutekelezwa, wananchi wanaoishi katika maeneo ya uhifadhi jumuishi kama Ngorongoro kuna haja kubwa ya Wizara ya Maliasili hata Wizara ya Fedha wasaidie ili fedha inayotolewa kwa ajili ya miradi kama shule, hospitali, barabara, wakati wa mchakato wa kutafuta namna sahihi ya kufanya uhifadhi jumuishi au wa mseto zikiendelea, wale wananchi nao waangaliwe maendeleo yao yasirudi nyuma. Nasema hivyo kwa sababu kuna vikwazo vikubwa na watu Ngorongoro hawapati maendeleo kwa ajili hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo basi, ili kuleta umoja kati ya wahifadhi na wafugaji kuna haja sasa ya kusahau sera za zamani za kuona kwamba mifugo na wanyamapori ni maadui. Sio maadui ni kuweka tu mpango wa matumizi bora ya ardhi ili wanyamapori na mifugo kwa utaratibu wa matumizi bora ya ardhi ambayo yanaweza yakapangwa wakashirikiana nyanda za malisho katika maeneo mahsusi kama Ngorongoro ama katika maeneo ya uwindaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile hizi tozo ambazo watu wanatoza watu wa maliasili ile Sh.100,000; ningeomba hata sasa leo wakati baadaye hii hoja inajumuisha, tuambiwe ni sheria gani hiyo ilipitishwa na Bunge gani linaloruhusu mfugaji atozwe 100,000 kwa kila ng’ombe anapokutwa ameingia katika eneo la hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, kuna pia kero kubwa kwa sababu bajeti haijazingatia matakwa ya wafanyabiashara wa mifugo. Kodi yao haijaguswa popote kupunguzwa. Naomba kodi yao iangaliwe hasa kupeleka mifugo nje maana bado soko la ndani ni hafifu, ni duni ili na wao wapate punguzo, wapate ahueni na maisha yao yaboreke kutokana na bajeti hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nawapongeza Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro, Naibu wake, Mheshimiwa Mary Masanja, Katibu Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Allan Kijazi, pamoja na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa na muhimu wanayofanya ya kusimamia maliasili yetu kwa manufaa ya kizazi cha leo na vizazi vijavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, naomba sasa nijielekeze kwenye hoja kwa kuchangia katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ni ushauri kwa Serikali kuhusu haja ya kuinusuru Tasnia ya Uwindaji wa Kitalii katika Taifa letu. Tasnia hii ni moja ya vyanzo vya mapato kwa Taifa letu ambayo kwa muda wa miaka 10 sasa imekuwa katika hali tete na inaendelea kushuka zaidi hasa katika kipindi hiki cha janga la ugonjwa wa Corona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na takwimu za Chama cha Wawindaji wa Kitalii (Tanzania Hunting Operations Association - TAHOA), idadi ya watalii wa uwindaji wanaokuja nchini kwetu imekuwa ikishuka kwa kasi sana. Idadi imepungua kutoka wawindaji 1,503 mwaka 2010 hadi 519 mwaka 2019. Mapato nayo yameshuka kutoka Dola za Kimarekani milioni 23.5 mwaka 2010 hadi kufikia Dola milioni 11.5 mwaka 2018, sambamba na kushuka kwa umiliki wa vitalu vya uwindaji kwa asilimia 51 kutoka vitalu 157 mwaka 2010 hadi 87 tu ambavyo ndivyo vyenye wawekezaji kwa sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamiliki waliviacha vitalu vyao kwa hiari tangu mwaka 2018 kwa sababu ya kushuka sana kwa faida na ongezeko kubwa la gharama ya ada na kodi wanazotozwa na Serikali, jambo ambalo linalifanya Soko la Tanzania la biashara ya Utalii wa Uwindaji kuwa la bei ya juu zaidi kuliko washindani wetu Afrika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Zimbabwe kwa mfano, hupokea wastani wa wawindaji wa kitalii 800 japo wao wana vitalu 16 tu vya Serikali ikilinganishwa na Tanzania yenye zaidi ya vitalu 150. Zambia ambayo ina vitalu 26 tu, kulingana na takwimu za mwaka 2019, ilipokea wawindaji 446 ikilinganishwa na Tanzania ambayo ilipokea wawindaji 541 tu kwenye vitalu vyake 76, na zilizobaki hazikupata wawindaji kabisa. Afrika ya Kusini wao hupokea wastani wa wawindaji 9,000 kwa mwaka ikifuatiwa na Namibia ambayo hupokea watalii wa uwindaji 8,000 kwa mwaka licha ya kuwa maeneo yao ya uwindaji ni machache ukilinganisha na idadi na maeneo tuliyonayo sisi Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mojawapo ya tozo zinazolalamikiwa sana na TAHOA kwamba imechangia kuongezeka kwa gharama ya utalii wa uwindaji ni Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya asilimia 18 kwenye mauzo yao yote ambayo ilianza kutozwa mwaka 2016; na kufikia mwezi Machi mwaka 2020, pigo kubwa zaidi liliikumba tasnia ya uwindaji baada ya asilimia 80 hadi 100 ya watalii kuahirisha safari zao kutokana na kuzuka kwa ugonjwa wa corona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kufuatia kushuka kwa biashara ya utalii wa uwindaji, nashauri, Serikali iridhie mambo mawili muhimu ambayo yasipozingatiwa, tasnia hii itazidi kuathirika sambamba na kushuka kwa mapato yanayotokana na utalii wa uwindaji pamoja na ulinzi na uhifadhi wa maliasili yetu katika maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba VAT irejeshwe kwenye mfumo wa ugawaji kama ilivyokuwa kabla ya mwaka 2016. Kulingana na taarifa za TAHOA, tangu VAT ianze kutozwa kwa kiwango cha asilimia 100 ya pato lao, Tanzania imeshindwa kushindana na nchi nyingine za Afrika zenye uwindaji kama Zimbabwe, Zambia, Msumbiji, Namibia, Afrika ya Kusini, Botswana, Uganda, Ethiopia, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Gabon na Benin. Nchi hizi wao hutoza VAT ya kati ya asilimia 10 hadi 18, lakini ni kwa baadhi ya bidhaa tu kama vyakula, malazi na ada ya uwindaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya mwaka 2016, TAHOA ilikuwa inalipa VAT kwenye vyakula na malazi tu na hizi zilikuwa zinahesabiwa kama asilimia10 ya ada za safari na asilimia 90 iliyobaki ilikuwa haihesabiwi ama ilipewa msamaha, kwa sababu TAHOA walikuwa wanatambulika kama wauzaji wa nje (exporters).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli TAHOA ni exporters kwa sababu hakuna mtalii wa uwindaji atakayekuja Tanzania kuwinda kama hatasafirishiwa nyara zake kwenda nchi aliyotoka aweze kwenda kufurahia. Hata Kimataifa, uwindaji wa kitalii unatambulika kama export industry, na hata Tanzania tuliitambua hivyo mpaka mwaka 2016 VAT ilipoanza kutozwa kwa asilimia 100 ya mauzo na mapato ya makampuni ya uwindaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wadau wetu wa Tasnia ya Utalii wa Uwindaji wanailalamikia Serikali kuwa pamoja na kulipia VAT kwenye mapato yao yote, kampuni hizi pia zinawajibika kubeba gharama kubwa za kudhibiti ujangili, kuendeleza vitalu, kuchangia miradi ya maendeleo ya jamii, kulipa ada za mwaka za vitalu (Block Fees), mambo yote ambayo yanawapunguzia kwa kiwango kikubwa faida wanayopata na wakati mwingine hujikuta zikijiendesha kwa hasara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba kutokana na kudorora kwa utalii wa uwindaji, nashauri Serikali isamehe kampuni za utalii wa uwindaji kwa muda au kupunguziwa Ada ya Vitalu vya Uwindaji. Kwa sasa, kwa mwaka kitalu cha uwindaji hulipiwa Dola za Kimarekani 60,000 kwa vitalu vya daraja la kwanza, USD 30,000 kwa vitalu vya daraja la pili, na USD18,000 kwa vitalu vya daraja la tatu. Katika kipindi hiki cha janga la Corona, wenye vitalu wengi wanashindwa kulipia ada ya vitalu kutokana na kukosekana kwa wateja wa uwindaji. Kwa hiyo, kutokana na hali hii, makampuni ya uwindaji wanashindwa pia kufanya doria na ulinzi wa wanyamapori kudhibiti ujangili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mwaka 2020, hadi tarehe ya mwisho kulipia ada ya vitalu, ni vitalu 64 tu ndivyo vilivyolipiwa na vitalu 48 hawakuweza kulipia kwa wakati hata baada ya kuongezewa muda wa ziada wa siku 30. Hii inaonyesha hali ilivyo tete kwa sasa katika tasnia hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri ili kuinusuru tasnia hii yenye faida kiuchumi na kiuhifadhi, Serikali ifanye mapitio ya sera kuhusiana na tasnia hii na kufanya mabadiliko muhimu ili kuzidi kuboresha mazingira yake ya uwekezaji. Kuna haja ya kufanya marekebisho kwenye viwango vya kodi na ada ya vitalu, pamoja na tozo mbalimbali ikiwemo VAT ya asilimia 18 kwenye huduma na mauzo yote ili kuchochea ukuaji na uwekezaji katika tasnia ya uwindaji na hivyo kuongeza mapato kupitia kuongezeka kwa watalii watakaovutiwa na punguzo la bei kuja kuwinda nchini kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia kubwa ya mapato yanayotokana na uwindaji hayatokani na ada ya vitalu kwani huchangia asilimia 15-20% tu na asilimia 80 - 85 hutokana na ada za nyara pamoja na ada za leseni. Hivyo naishauri Serikali ipunguze kodi ya vitalu ili kampuni ziweze kumudu kupunguza bei kwa wateja wao na hivyo kuvutia idadi kubwa zaidi ya watalii wa uwindaji. Kwa njia hiyo, wataweza kuinua mapato yanayotokana na tasnia hii ambayo kwa sasa yameshuka kwa zaidi ya asilimia 50.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni ushauri kwa Serikali kuhusu kufuta pendekezo la kutaka kuanzisha Pori la Akiba katika katika Wilaya ya Longido Ukanda wa Ziwa Natron.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilijulishe Bunge lako Tukufu na wewe mwenyewe kuhusu mchakato wa Wizara ya Maliasili ulioanzishwa mapema mwaka 2020 wa kutaka kuanzisha Pori la Akiba katika maeneo ya vijiji vya wafugaji wa wilaya ya Longido na ambayo wao wenyewe wameyatenga na kuyahifadhi mahususi kwa ajili ya malisho ya akiba kwa mifugo yao misimu ya kiangazi na nyakati za majanga ya ukame ambayo hutokea mara kwa mara katika wilaya yetu ya Longido.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na hali ya kijiografia na maisha ya wakazi wa Wilaya ya Longido ambao kwa asilimia 95 ni wafugaji, kutakuwa na athari kubwa sana kijamii na kiuchumi endapo Pori la Akiba lililopendekezwa litaanzishwa katika maeneo ya malisho ya mifugo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo basi, naomba niishauri Serikali yetu sikivu ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mama yetu jasiri, mpendwa wetu, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, isitishe mchakato huu kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamii ya wafugaji wanaoishi katika eneo husika wanatunza mazingira na tayari eneo hilo ni Pori Tengefu (Game Control Area – GCA) na linatumika kwa uwindaji wa kitalii tangu miaka ya 1950. Sambamba na shughuli ya ufugaji kwa Jamii ya Kimasai ambayo ndiyo wakazi Wakuu wa Wilaya ya Longido, kuna azma ya Serikali yetu kuongeza maeneo ya wafugaji na siyo kuyapunguza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lililopendekezwa la Ukanda wa Ziwa Natron, milima ya Gelao, Ketumbeine, Matale na nyanda za malisho ya vijiji zaidi ya 17 za Tarafa ya Ketumbeine na Engarenaibor ambazo zitamezwa na Pori hilo la Akiba, linategemewa sana na wafugaji ambao ni asilimia 95 ya wakazi wa Longido na mifugo ndiyo njia kuu ya uchumi wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo cha kufanya eneo husika Pori la Akiba litaleta mgogoro kati ya wananchi na hifadhi na itaongeza migogoro ndani ya Wilaya ya Longido na maeneo ya jirani Wilayani Ngorongoro ambako tayari hali ya uhifadhi na jamii imekuwa tete.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan akiwa Makamu wake, walizirudishia zaidi ya vijiji 900 ardhi ya hifadhi ili wananchi wapate maeneo ya kuishi na kufanyia shughuli za kiuchumi; na kwa Vijiji vya Wilaya ya Longido, hazikuwa kwenye orodha yoyote ya vijiji vyenye mgogoro na hifadhi. Hivyo, siyo vizuri sasa kuongeza tena eneo la hifadhi kwa wananchi ambao tayari wanaishi vizuri na wanyamapori na bila kuwa na migogoro na hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Pori la Akiba linalopendekezwa litaathiri vijiji vyote 19 vya Tarafa ya Ketumbeine; Vijiji 11 vya Tarafa ya Engarenibor na Kijiji kimoja cha Kiserian katika Tarafa ya Longido. Hili ni eneo lenye zaidi ya watu 90,000. Vilevile Pori hilo litaathiri baadhi ya vjiji vya Wilaya ya Ngorongoro na ikizingatiwa kuwa eneo la Ngorongoro tayari kwa sehemu kubwa ni hifadhi na hivyo ikifanyika hivi wananchi hawatakuwa na mahali pa kuishi na kufuga; hivyo kuongeza migogoro katika wilaya husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Longido tuna kiwanda kikubwa na cha kisasa chenye uwezo wa kuchakata nyama ya mifugo zaidi ya ng’ombe 1,000 kwa siku, mbuzi na kondoo 4,000 kwa siku; na hivyo eneo kubwa zaidi ya hili tulilonalo kwa sasa linahitajika kwa ajili ya kufuga na kunenepesha mifugo yetu kwa ajili ya viwanda vyetu vya ndani. Hivyo pendekezo la kumegua sehemu ya ardhi ya Longido haliendani na azma ya Serikali ya kuongeza maeneo ya malisho ili kuinua sekta ya mifugo na kukuza uchumi unaotokana na mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Hotuba ya kwanza ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa Bunge letu ya tarehe 22 Aprili, 2021 Dodoma, alikazia dira ya Taifa letu la kuendelea kuongeza maeneo ya ufugaji. Wilaya ya Longido ni moja ya wilaya kame sana nchini na ambayo hukabiliwa na majanga ya ukame mara kwa mara, hivyo milima inayotaka kutwaliwa pamoja na eneo la nyanda za Ziwa Natron ndiyo huwa kimbilio la kupatia malisho na maji wakati wa majanga ya ukame.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamii katika ngazi zote (Kijiji, Kata kupitia WDC, Halmashauri ya Wilaya kupitia Baraza la Madiwani, wala DCC na RCC) hawakuwahi kushirikishwa katika mchakato wa pendekezo la kuanzishwa kwa Pori hili ili kupata mawazo yao. Hivyo jambo hili siyo shirikishi. Pori linaloonekana kama liko wazi kwa wageni ni maeneo ya asili ya wafugaji waliyopangilia matumizi ya malisho na maji kwa misimu tofauti ya mwaka ili kutunza ekolojia na upatikanaji wa malisho bora ya mifugo kwa majira ya mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya milimani ndiyo hunusuru mifugo kwa malisho na maji wakati wa kiangazi na nyanda za chini hufaa nyakati za mvua na masika tu kutokana na ukosefu wa vyanzo vya maji misimu ya kiangazi katika Wilaya ya Longido. Hivyo kuyatwaa maeneo hayo ni sawa na kuwaangamiza wafugaji wa Wilaya ya Longido.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, naomba Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii isikilize kilio cha wananchi wa Jimbo langu la Longido na ichukue hatua sahihi bila kusita kusitisha na kulifutilia mbali pendekezo la kutaka kutwaa eneo hili la wafugaji na kulifanya kuwa Pori la Akiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja na ahsante kwa kupokea mchango wangu.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ili nami niweze kuchangia katika mpango huu. Nianze kwa kuipongeza Serikali yetu ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuendelea kupeleka mbele maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuelekeza pongezi zangu za dhati katika maeneo kadhaa ambayo ni dhihirisho la uhakika kinyume na hoja walizotoa wenzetu wa Kambi ya Upinzani kwamba maendeleo ya nchi yetu yanarudi nyuma. Napingana nao kwa sababu hata ukiangalia katika upande wa ukuaji wa uchumi nchi yetu iko katika mstari wa mbele inaongoza katika Ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuwa na ukuaji wa asilimia 7.1 mwaka 2017 na mwaka huu asilimia 7.2. Inaonekana kwamba uchumi wetu unakua na hakuna sababu ya kutilia mashaka hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuipongeza Serikali yetu kwa sababu nimeangalia katika baadhi ya mambo yanayotekelezwa nikaona kwamba kuna mapinduzi makubwa katika sekta ya madini. Mabadiliko makubwa yamefanyika katika sera na sheria na mapato yameongezeka, sawasawa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Wizara ya Ardhi na hata Uhamiaji. Nimesoma katika mpango, nami napenda kupongeza hilo na kuishauri Serikali kwamba tuendelee katika kutumia hii teknolojia ya kielektroniki kwani ndiyo imekuwa chanzo cha makusanyo ya Serikali kuongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningetamani kuona hili likichukuliwa kama kipaumbele cha kwanza na Wizara yetu ya Maliasili na Utalii kwa sababu kuna tozo nyingi ambazo zimetawanyika na zinawakera wateja wetu ambao ni watalii. Natamani kuona kitu ambacho napendekeza kiitwe One Stop Payment Centre ambapo mtalii kwa kutumia mifumo ya mitandao ambayo itaanzishwa anaweza aka- book parks anazotaka kwenda akiwa kwao, akalipia kwa credit card yake fees zinazohusika, akalipia hata visa, akifika airport anaonesha tu kwamba ameshalipia na anaongozwa mpaka kwenye parks zetu akatalii kwa raha zake na kuondoka bila kubugudhiwa. Tukifanya hivyo, naamini sekta ya utalii itaongeza mapato kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuipongeza Serikali katika sekta ya elimu. Ukiangalia sekta hii sasa hivi kuna sera ya elimu msingi bila malipo ambayo imeongeza idadi ya watoto wanaosoma. Pia napenda kuipongeza Wizara kwa sababu wameonesha jitihada katika kuchapisha vitabu vya kiada na rejea hata katika ngazi ya chini kuanzia elimu ya awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri kwamba kwa sababu tuna azma kubwa ya kufundisha wataalam wa fani mbalimbali katika nchi yetu, hatutaweza kuwa na wataalam wabobevu na wenye msingi imara tusipowekeza katika elimu ya awali kwa kuhakikisha kwamba hizi shule zinazoitwa shule shikizi ambazo jamii ndiyo inawatafuta walimu, tena ambao hawajasomea, naiomba Serikali iweke katika huu mpango wa mwaka huu unaokuja mkakati kabambe wa kuhakikisha kwamba shule shikizi zinasimamiwa na Serikali ama kwa kuwapelekea walimu au kwa kuhamasisha jamii waaajiri walimu ambao wamesomea jinsi ya kutoa elimu ya awali. Ni katika kutoa elimu bora katika ngazi ya awali ndiyo tunapata watoto ambao wameiva kwenda elimu ya msingi, sekondari, vyuo na kuwapata wataalam katika fani mbalimbali zinazohusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nilipokuwa napitia hii taarifa ya Kamati wameelezea baadhi ya miradi mikubwa ambayo ingeiletea faida Serikali yetu lakini inaonekana haijawekwa katika mpango wa mwaka 2019/2020. Wametaja mradi mmoja unaoitwa Mradi wa Magadisoda wa Bonde la Engaruka, nafikiri wamekosea na wakasema upo katika Ziwa Manyara, ni ukurasa wa 22 lakini Bonde la Engaruka haliko katika Ziwa Manyara liko katika Wilaya ya Monduli na Bonde hilo lina ziwa kwa lugha yetu ya Kimasai linaitwa Orboloti Langaruka, ni eneo la mpakani mwa Longido na Monduli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba katika kuangalia kwa kina manufaa ya mradi huu kwa jamii zinazozunguka eneo hilo, watakapokuwa wanafanya usanifu na naamini umeshafanyika, ili kuepusha migogoro wabainishe uhalisia wa maeneo yaliyopo katika Wilaya ya Monduli maana asilimia kubwa ya ziwa liko katika Wilaya ya Monduli lakini kuna maeneo pia ya bonde hilo ambayo yanaangukia katika Wilaya ya Longido. Napenda kutoa ushauri huo ili kuepusha migogoro ambayo inaweza ikazuka baadaye wananchi watakapokuwa wanadai manufaa yatakayotokana na mradi huo wa magadisoda katika Bonde la Engaruka kwenye hilo Ziwa la Orboloti na haliko katika Ziwa Manyara na naomba hilo liangaliwe na kusahihishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na suala ambalo Kamati imeleta kuhusu ukamilishaji wa miradi ambayo inaonekana inakwenda kuwapatia wananchi nguvu za kiuchumi na maendeleo. Kwa mfano, wananchi siku hizi wanahamasishwa waanzishe miradi mbalimbali, waanzishe majengo ya zahanati yajengwe mpaka lenta; waanzishe majengo ya shule, madarasa na nyumba za walimu wajenge mpaka lenta na nyumba za madaktari. Inapofikia mahali ambapo wananchi wamekamilisha ile miradi na Serikali ikaendelea kuchelewesha kuja kuwaunga mkono na kumalizia inawavunja wananchi moyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Kamati kwa sababu ni maoni yao na kuisihi Serikali iwekeze katika kuweka bajeti ya kutosha kumalizia miradi ambayo imeanzishwa kwa nguvu za wananchi. Tuna miradi mingi ya mfano ambayo ningeweza kutoa katika Jimbo langu, lakini kwa sababu tunachangia mpango kwa ujumla wake katika kuielekeza na kuishauri Serikali, naomba nisiende huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dakika zilizobakia naomba nielekeze maoni yangu katika kuchangia hili suala la Wakala wa Maji Vijijini. Kwa kweli kama tulivyoanzisha TARURA, naishauri Serikali ifanye haraka kuanzisha wakala huu. Ningefurahi kujua ni lini Wakala wa Maji Vijijini utaanzishwa kwa sababu moja ya vyanzo vya migogoro katika Taifa letu na hata dunia kwa sasa hivi vinatokana na masuala ya ardhi na maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala ya maji ndiyo yamesababisha kuwa na mgongano mkubwa kati ya jamii zinazoishi katika maeneo yaliyohifadhiwa ambayo ndiyo yenye maji nyakati za kiangazi na maeneo mbalimbali kama Hifadhi za Taifa au Ranchi za Kitaifa. Tukipata wakala huu ukaharakisha kasi ya kupeleka maji katika maeneo mahsusi ya wafugaji, tutaepusha migogoro mingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, katika hili suala la ardhi, naomba pia nidokeze kwa kusema kwamba hii Sera ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambayo inasema kwamba kuna sera ya kupanga, kupima na kusajili ardhi ipewe kipaumbele katika huu mpango wa mwaka wa fedha unaokuja ili kila kipande cha ardhi basi kiweze kupimwa; maeneo ya uwekezaji yaweze kubainishwa na maeneo ya wafugaji na wakulima yaweze kutenganishwa ili kupunguza migogoro ambayo inaendelea kutukabili kila wakati na huenda ikawa ni changamoto moja ya kutopeleka mbele maendeleo ya Taifa letu. Sasa hivi kuna migogoro mingi kati ya vijiji na vijiji, wilaya na wilaya na hata mkoa na mkoa na nafikiri hii sera ya kupima, kupanga na kurasimisha usajili wa ardhi, ingepewa kipaumbele katika mpango wa 2019/2020 tutaweza kupiga hatua kubwa katika kuharakisha kasi ya maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa muda ulionipa, basi naishia hapo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia katika hotuba hii ya bajeti ya Waziri Mkuu. Nitangulize pongezi zangu za dhati kwake yeye Waziri Mkuu na timu yake yote kwa kazi nzuri wanayoifanya na kwa jinsi walivyoiratibu na kuangazia masuala chanya ya maendeleo yanayoendelea katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nitumie fursa hii kwa niaba ya wananchi wa Longido kutoa shukurani zangu za dhati kwa sababu ya maendeleo chanya yaliyoonekana na kushangiliwa na wananchi wa Longido katika Serikali hii ya Awamu ya Tano ambapo mradi mkubwa kabisa wa maji kutoka Mlima Kilimanjaro uliogharamiwa kwa jumla ya shilingi bilioni 15.9 hatimaye umefika Longido, watu wamepata maji safi na salama na mengi na ya kutosha. Wananchi wa Longido wamesherehekea na wanaendelea kufurahia, sasa watu wanaweza wakaoga hata mara tatu kwa siku kwa sababu yale maji yamekuja kwa wingi wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa sababu kulikuwa na ahadi za Serikali za kuendeleza maji haya yawafikie na majirani waliko pembezoni mwa bomba hilo kubwa katika vijiji mbalimbali kuanzia kule maji yanapotokea Kata ya Olmolog Kijiji cha Elerai; Kata ya Sinya, Kijiji cha Sinya; Kata ya Tingatinga, Kijiji cha Ngereyani na hivi vijiji vya pembezoni mwa Longido hadi Kimokouwa na Namanga ambapo hata Rais mwenyewe alipokua kuzindua ule mpaka wa pamoja alitolea tamko kwamba nao wamepelekewe maji hayo. Kwa kweli Longido wameona haya maji kama ni uzima, wamepewa maisha na mimi nakumbuka kila nikipita pale Moshi kuna mnara wa Askari ambapo kuna slogan chini yake inasema “maji ni uhai” nikawa najiuliza kwa nini Askari anashika bunduki anaelekeza Mlima Kilimanjaro kumbe analinda uhai. Maji ni uhai, ni ya kulindwa, ni ya kuenziwa na wananchi wa Longido wamefarijika sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia wananchi wa Longido kwa mwaka huu wamepata mgao mkubwa wa fedha za kujengewa hospitali ya Wilaya ambayo hatukuwahi kuwa nayo. Hospitali ya Wilaya imetengewa bilioni moja na nusu bila kuhesabu vituo vya afya viwili ambavyo vimejengwa viko katika hatua ya umaliziaji, japo bajeti imekwisha lakini naamini bajeti hii itawapa watu wa Eworendeke na Engarenaibor fedha za kumalizia na moja ambayo wananchi kwa ari kabisa wa Tarafa ya Ketumbeine nao wameanza kuijenga kwa nguvu yao wenyewe mpaka wamefikia hatua ya kupaua.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya shukrani hizo kwa sababu nataka tu kuonyesha ni kwa jinsi gani Serikali hii inawaenzi wananchi wake tena watu wa Wilaya za pembezoni kama Longido, sasa napenda kuchangia katika hotuba hii ya Waziri Mkuu kwa kudonoa baadhi ya mambo machache ambayo nime-note. Kwa suala la ardhi kuna hii sera ya Serikali inayosema kwamba Mpango wa Taifa kufikia mwaka 2033 ni kuhakikisha kila kipande cha ardhi ya Tanzania kimemilikishwa na kinamilikishwa baada ya kupangwa na kupimwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa angalizo kama Mjumbe wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwamba tulivyofanya ziara katika baadhi ya mikoa inayopakana na nchi za jirani tumeona ardhi yetu inavamiwa hovyo kabisa na sisi Watanzania naona ardhi yetu ni kubwa hatujakaribia sana ile mipaka kama wenzetu. Tumetembelea mipaka yetu na Rwanda, Uganda, Kenya upande wa Tanga maeneo ya Horohoro tukashangaa nchi za jirani zimejenga mpaka zimeiinga katika ardhi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiunganisha suala hilo na hili la barabara, wao wametengeneza barabara za kuzunguka mipaka yao lakini sisi hatuna. Kwa sababu tumedhamiria kufanya hilo zoezi la kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi, naomba kuiasa Serikali ilipe kupaumbele zoezi hilo ili twende kwa kasi kubwa tuweze kuimarisha mipaka yetu na kuilinda hiyo rasilimali muhimu ya ardhi ambayo ndiyo chimbuko letu sisi sote.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hili suala la barabara ni la muhimu sana katika kuzunguka hii mipaka yetu maana tulikuwa tunaenda mpaka nchi ya jirani ndiyo tuone beacon. Hili jambo siyo salama na ni lazima Serikali sasa ione umuhimu wa kutenga fedha za kutosha ili kuimarisha hiyo yetu mipaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye suala lingine la msingi la mawasiliano, katika hotuba ukurasa wa 51 yameongelewa mawasiliano ya Mkongo wa Taifa lakini kuna kipengele muhimu ambacho sijakiona mawasiliano ambayo nafikiri ni sehemu ya huduma za jamii, mawasiliano ya simu za mkononi. Sasa hivi simu ni kama sehemu ya uhai wetu, ukitaka kujua hebu Waheshimiwa Wabunge wote waambiwe waache kutumia simu kuanzia asubuhi mpaka jioni. Biashara zinaendeshwa kwa simu, mawasiliano na kila kitu kinafanyika kwa simu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wengi katika baadhi ya maeneo nchi hii bado hawana hiyo huduma ya simu. Naomba zaidi Serikali itilie mkazo maeneo ya mpakani. Tumezungumza hiyo mipaka niliyoitaja kila mpaka wenzetu wa nchi tunayopakana nao wao wana minara ya simu na watu wetu wanatumia minara ya simu ya nchi nyingine wakati suala hilo pia ni la kiusalama. Naomba Serikali yetu iwekeze katika kusimamia ule Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, wawekezaji au wadau wa mitandao ya simu minara ijengwe katika vijiji vinavyopakana na mipaka ili kuimarisha ulinzi na ili wananchi wetu walio katika hii mipaka wapate minara.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukianzia katika Wilaya yangu ambayo kilomita 300 tumepakana na nchi jirani ya Kenya ukienda Kata ya Kamwanga nusu ya watu wanatumia minara ya Kenya. Ukienda Kata za Matale, Wosiwosi na Kilailungwa wote wanatumia minara iliyoko Kenya na kuna Kata ndani ya Wilaya yangu ambazo hazina mawasiliano na Watanzania wale nao wanaona kwamba sasa ifike wakati wapewe minara ya simu kwambabu tuko karne ya teknolojia ya mawasiliano ya kielektroniki.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kugusia suala la mifugo. Ni kweli mifugo ni sekta ambayo haijapewa kipaumbele katika nchi hii. Kwa masikitiko niseme kwamba kuna zoezi lilifanyika la kuwadhibiti watu wanaovusha ng’ombe kupeleka Kenya katika mipaka ya Wilaya yangu, wale watu kweli walionewa. Sheria tumeweka sisi tukaweka na faini ambazo siyo za kiulihalisia na wananchi wale walikuwa wanakwenda kule kwa sababu hatuna masoko. Sasa hivi sisi tuna kiwanda cha mwekezaji kinajengwa mpakani kitakamilika mwezi Oktoba basi naomba Serikali
ijihusishe na kuweka mikakati thabiti ya kuhakikisha kwamba masoko ya uhakika yatapatikana. Serikali itoe bei elekezi kama inavyotoa katika mazao ya kilimo, waangalie minada ya nje wapange kabisa bei ambayo itawafanya wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo wasipate sababu ya kutaka kuvusha ng’ombe na kuuza kwenye masoko ya ndani. Kwa kufanya hivyo, zile bidhaa nyingine kama ngozi, pembe, mifupa, kwato zitaweza kuongeza mnyororo wa thamani kwa sekta hii ya ufugaji.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa muda wako umekwisha.

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niwe mchangiaji wa kwanza wa hoja hii ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa siku hii ya leo.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabla sijaanza kutoa mchango wangu, naomba nitumie fursa hii kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa usikivu wake wa kujali mahitaji ya wananchi wanapomlilia katika shida zao.

Mheshimiwa Spika, ni wiki moja tu imepita tulipotoa kilio kwamba hali ya chakula ni tete katika Kanda ya Kaskazini na wananchi waliouza mifugo yao hata hawana pa kununulia chakula maana bei ya mahindi ilipanda mpaka shilingi 20,000/= kwa debe, lakini Mheshimiwa Rais alitoa tamko kwamba kwa kuwa tuna maghala ya Serikali yanayoweka chakula, wananchi waliouza mifugo yao, wapelekewe chakula kwa bei ya Serikali na chakula hicho kimefika. Naomba niishukuru Serikali, nimshukuru Waziri wa Kilimo na timu yake yote kwa ushirikiano waliotoa. Wanalongido wamefurahi, chakula kimewafikia, na hata wale walanguzi sasa wameshusha bei baada ya kuona kwamba Serikali sikivu imewaletea wananchi wake chakula. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa pongezi na shukrani hizo, nitasema mambo machache sana kuhusiana na hotuba ya Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa sababu mengi yameshasemwa na sipendi kurudia yaliyosemwa, lakini nina machache ya kusema kuhusu Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza na Jeshi la Zimamoto.

Mheshimiwa Spika, kwa Jeshi la Polisi, naungana na wenzangu waliotangulia kusema kwamba mazingira yao ya kuishi na kufanyia kazi ni duni. Serikali iwaangalie kwa jicho la karibu. Ukija kwa mfano katika Jimbo langu la Longido ukaenda katika Kituo cha Polisi kilichopo Kamwanga, wale Polisi wanaishi katika shacks; shacks ni kama banda la kuku. Kwa kweli sisi kama wananchi wa Longido pia tunajali hivyo vyombo vya usalama na hata tulijitolea kabisa tukajenga na Kituo cha Polisi ambacho kinakaribia kumalizika, lakini Polisi wetu hawana makazi.

Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri; na nilishaongea naye kwamba atuunge mkono kumalizia kile Kituo cha Polisi kipya kilichojengwa kupisha barabara ya lami inayounganisha Wilaya za Rombo na Siha na baadaye Longido.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Jeshi la Magereza, napongeza sana kazi wanayoifanya na uzaishaji ambao wameonesha. Pia nategemea kwamba baada ya kuanzishwa kwa Mobile Courts msongamano wa wafungwa utapungua. Pia nitoe rai kwamba kama zilivyoundwa na Serikali yetu sikivu, tume mbalimbali za kuhakiki masuala ambayo yalikuwa hayaendi sawa katika nchi hii, kwa mfano uhakiki wa watumishi hewa, wale wenye vyeti feki na watu wengi wakabainishwa, naomba pia tume iundwe na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhakiki wafungwa waliosahauliwa ndani ya Magereza.

Mheshimiwa Spika, wako wafungwa ambao wametuhumiwa tu, ni mahabusu. Wamekamatwa kwa tuhuma za kuhujumu uchumi. Kwa mfano, katika Jimbo langu la Longido, kuna waliotuhumiwa tu kwamba wanajihusisha na biashara ya ujangili kwa sababu sisi ni Wilaya ya Wanyamapori na wanatupwa kule Gerezani, wengine wana mpaka miaka miwili; wanaitwa tu Mahakamani wanarudishwa, wanasema uchunguzi bado unaendelea.

Mheshimiwa Spika, naamini kwamba suala hili litapewa kipaumbele baada ya Mahakama kuongezewa wigo wa kuwa na Mobile Courts na Vyombo vya Usalama vifanye uhakiki wa uhalifu wao kwa haraka, wasikae Gerezani pasipo sababu kama mahabusu ambao hata hawajahukumiwa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Jeshi la Zimamoto; ni ukweli usiopingika kwamba bado tuko nyuma sana katika kuendeleza Sekta ya Zimamoto na kunusuru maisha na mali za Watanzania wanaoweza kuathirika kwa majanga ya moto; na wilaya nyingi nchi hii ambazo nimeshazipita hazina miundombinu kabisa ya uzimaji moto; na katika Wilaya yangu ya Longido pia hatuna hata gari la Zimamoto.

Mheshimiwa Spika, naomba katika bajeti hii iongezwe fedha ya kuhakikisha kwamba kila Wilaya angalau inapata gani moja la Zimamoto maana tunapata majanga ya moto kila wakati.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, sisi katika Shule yetu ya Sekondari ya Longido karibu kila baada ya mwaka mmoja au miwili tunapata janga la moto. Hata Kituo cha Polisi Longido mwaka 2018 nyumba ya Askari iliungua moto tukishuhudia; tunazima kwa mchanga na udongo, hatuna chombo chochote cha kuzimia moto. Naomba hilo liangaliwe.

Mheshimiwa Spika, pia nikienda katika huduma za uhamiaji, napongeza Serikali kwa sababu ya huduma ya kielektroniki na kwa kutengeneza passports zilizokidhi hadhi ya Kimataifa na kuwa moja ya passports bora duniani; lakini niombe kutoa rai kwamba hizi paspoti za kielektroniki zitengenezewe mazingira ya kuwa rafiki kwa waombaji na Watanzania wote wenye haja ya kupata passport.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi kwa sababu Watanzania wengi uwezo wao wa kutumia mitandao bado uko chini, hizi passports za muda mrefu ambazo mtu ukitaka kupata, mpaka ujaze fomu iende kanda, iende Makao Makuu; nasi watu tunaoishi mipakani tumekuwa tunategemea zaidi hizi hati za dharura tu. Unaona katika taarifa na hotuba ya Mheshimiwa Waziri ameonesha kwamba idadi ya wasafiri wa dharura ni kubwa mno ukilinganisha na wasafari wa aina nyingine. Siyo kwamba kuna dharura ni kwamba ndiyo hati ya pekee ambayo ni rahisi kuipata mtu unapotaka kusafiri nchi ya jirani.

Mheshimiwa Spika, naomba kwa sababu sasa hivi adha wanayopata wananchi wanaotaka kusafiri nchi ya jirani kwa biashara au kwa shughuli za kifamilia au kwa matibabu ni kubwa, maana kila akienda akirudi ile passport inayoitwa hati ya dharura ina-expire; akitaka kuomba nyingine labda ameambiwa arudi ndani ya wiki hiyo hiyo, mpaka apeleke tena zile nyaraka zote; apeleke birth certificate, apeleke sijui barua ya mtendaji na akirudi tena wiki ijayo anaitishwa tena back up ya zile documents zote.

Mheshimiwa Spika, nia ya Serikali najua kwamba ni njema, Waziri wa Mambo ya Ndani alishakuja akatoa elimu katika Jimbo langu, lakini naomba passport za muda mrefu, angalau zile za East African Community zirahisishwe wananchi waweze kupata katika ngazi ya Wilaya. Mtu akija, ajaze fomu, atoe vielelezo vyake, apewe passport ya muda mrefu kwa sababu naamini haki ya kuwa na passport ni haki ya kila Mtanzania mwenye kuwa na haja nayo.

Mheshimiwa Spika, pia naomba niongelee kidogo suala Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, vitambulisho hivi kasi yake ya kutoa ni ndogo mno, wananchi wangu wa Longido kuna waliopigwa picha za kupewa hivyo vitambulisho tangu mwezi wa Kumi mwaka jana lakini mpaka leo hawajapata.

Mheshimiwa Spika, pia niunganishe hapa kwa sababu ya ufinyu wa muda suala zima la kupatiwa hivi vitambulisho ili mtu aweze kuhakikiwa na line yake ya simu. Naomba kuuliza na Waziri anijibu baadaye atakavyohitimisha hoja, Mheshimiwa Waziri atusaidie kwa wale raia ambao siyo raia wa Tanzania lakini wapo nchini kihalali aidha kwa work permint au huku kwa sababu ni dependants, wao ni vitambulisho gani watahitajika kuonyesha ili line zao za simu zisifungiwe itakapofika wakati wa kuzifunga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, niipongeze Wizara, Waziri wenyewe ambao ni mmoja ya Mawaziri wasikivu sana ambao mimi nimewafahamu katika Bunge hili, yupo tayari usiku na mchana kukuhudumia ukimpigia simu, nimpongeze yeye na timu yake yote kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kuandaa hotuba ya bajeti na pia katika utendaji wao tunaouona katika vyombo vya kitendaji wanavyovitumia. Kazi yao ni nzuri, Mheshimiwa Waziri aendelee hivyo hivyo, tupo nyuma yake kum-support kwa sababu kazi anayofanya inawasaidia Watanzania kubaki salama, lakini tuendelee kuongeza bidii katika kupunguza urasimu na hasa rushwa katika Jeshi letu la Polisi.

Mheshimiwa Spika, polisi bado wanakula rushwa, naomba hata kwa sababu tumekuwa electrified hizo electronic agency zitumike tu kumsoma mtu anayefanya uhalifu kwa mfano barabarani akakutane na faini yake mbele ya safari na sio polisi kuanza ku-negotiate naye. Teknolojia imeendelea, kuna nchi ukienda unapigwa picha tu barabarani unatumiwa kwenye barua kwa sababu gari yako inajulikana, ni ya nani, unatumiwa barua ya madai na usipopeleka gari yako inataifishwa. Kwa hiyo, naomba pia sera hiyo ya kufanya Electronic Traffic Monitoring System iweze kuboreshwa zaidi, maaskari waondokane na hadha ya kusamisha wasafiri barabarani na kuanza kuwahoji na kupatana na hatimaye kudaiwa rushwa ndipo mtu aweze kwenda au vinginevyo atapigwa faini kubwa.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Kiruswa.

MHE. DKT. STEPHEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kusema naunga mkono hoja na ahsante kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika hoja iliyoko mbele yetu ya Mpango wa Taifa kwa Mwaka wa 2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia kwenye Mpango na nimetazama baadhi ya maeneo mahususi kama maeneo ya vipaumbele na hasa nikavutiwa na mirdi mikubwa ya kielelezo, ni mingi, lakini napenda kutaja umeme wa maji wa Nyerere National Park, reli ya standard gauge, Shirika la Ndege kuimarishwa, bomba la mafuta, gesi asilia na huu mradi wa makaa ya mawe ya Mchuchuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi ambayo sasa hivi yanasababisha kuweko kwa upungufu mkubwa wa rasilimali ya nishati mbadala kama kuni na uhalisia wa kuhitaji uhifadhi mazingira na haja ya sisi kupiga marufuku ukataji wa mkaa hovyo, napenda kuishauri Serikali kwamba, hii miradi miwili mikubwa ya nishati mbadala, gesi asilia pamoja makaa ya mawe ingepewa kipaumbele kikubwa kabisa. Serikali ingefanya kila liwezekanalo hata kama ni kukopa fedha hii miradi itekelezwe kwa kasi Watanzania waanze kubadilika sasa na kutumia gesi kwa wingi zaidi na makaa ya mawe ili tuondokane na athari za kuharibu mazingira, kuchangia katika hali mbaya ambayo tayari tunayo inayoletwa na mabadiliko ya tabianchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipengele kingine nilipoangalia ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, nimeguswa sana kutaka kusemea maeneo mawili; eneo la kilimo cha mazao na mifugo na eneo la wanyamapori. Kwa upande wa kilimo cha mazao, katika karne hii ya 21 tuliyopo kwa kweli matamanio yangu ni kuona Tanzania ikiondokana na kutegemea kilimo cha jembe la mkono na jembe la kukokotwa na wanyama. Tuondokane sasa katika hiyo sayansi ya karne zilizopita tuwekeze na Serikali ifanye kila liwezekanalo katika kilimo cha kisasa zaidi kinachotegemea matrekta na power tillers.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kuishauri Serikali waanze tena kama zamani nilipokuwa mdogo, kuna wakati matrekta ya vijiji yalikuwa yanatolewa. Wapeleke matrekta vijijini hata wakopeshwe vijiji matrekta na power tillers tuweze ku-phase out kilimo cha jembe la mkono na jembe la kukokotwa na wanyama ili kilimo chetu kiweze kuwa na tija zaidi tuzalishe kwa wingi zaidi. Sambamba na hilo, Serikali iwekeze kwa kila hali katika kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika sekta ya mifugo nimeona kwamba kuna mipango mizuri inayowekwa ya kuongeza tija, masoko, uzalishaji, maeneo ya malisho, lakini naomba suala la maji lizingatiwe. Asilimia kubwa ya mifugo ambayo ndiyo inabeba uchumi wa wafugaji katika nchi hii ni mifugo ya asili ambayo mingi ndiyo ambayo inaiingizia Serikali mapato kwa mifugo inayouzwa ndani na nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta hii ya mifugo, naishauri Serikali kwamba, waangalie katika zile nyanda za malisho za wafugaji, waweke kabisa nguvu katika kuweka maji; maji ya mabwawa, visima virefu, sambamba na kuhakikisha masoko yetu ambayo nimeona wameweka mkazo kwamba, kuna uboreshaji wa masoko na viwanda vya kuchakata nyama na bidhaa za mifugo, masoko yetu yahakikiwe yaweze kutoa bei yenye tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi mifugo mingi ya nchi yetu inapelekwa nchi za jirani na hasa Kenya. Endapo tutakuja kutengeneza viwanda, tusipokuwa na mkakati wa kuweka bei inayofanana na ile ambayo wenzetu wanaopeleka mifugo Kenya wanaipata, tutaendelea kupoteza mazao ya mifugo kwa sababu wafanyabiashara wa mifugo wataendelea kutamani kupeleka nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali itendee Sekta ya Mifugo kama kile kinachofanyika kwenye Sekta ya Mazao ya nafaka kama korosho, kahawa na chai, wawe wanawekewa bei elekezi ambayo ninaamini huwa inatengenezwa kitaalam kwa kuangalia hali halisi ya bei za mazao hayo katika Soko la Dunia. Mifugo pia ifanyie hivyo ili mfugaji aweze naye kupata bei ambayo inamvutia, apende kuuza kwenye masoko ya ndani na apate faida ambayo ataipata tu popote atakapokwenda na asiwe na hamu ya kutaka kupeleka mifugo nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nilikuwa nimeangalia katika suala la kufungamanisha uchumi na maendeleo ya watu, nikatamani sana nitoe maoni kwa Serikali na ninaomba niishauri Serikali kwenye suala la ardhi. Ardhi ndiyo mama yetu sisi wote, ndiyo chimbuko la kila kitu; na ardhi ya Tanzania haiongezeki, sisi tu binadamu ndio tunaongezeka na viumbe wengine walioko katika hii ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itilie mkazo sana suala la upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi kuhakikisha kwamba tunawasomesha wataalam wa kutosha, tunawekeza katika kuweka vifaa vya kutosha na kuhakikisha kwamba hii ardhi inapangwa na ipangwe mapema kuepuka adha tunayopata ya makazi holela na migogoro ya ardhi isiyoisha. Hii itatusaidia sana kuondokana na migogoro na katika kuhakikisha kwamba Watanzania wa kesho watakuta ardhi iliyopangiliwa na ambayo matumizi yake yameshabainishwa na tutaondokana na adha kubwa tuliyonayo kwa sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa suala la wanyamapori, kwa kuwa naona muda wangu umeisha, nilikuwa naomba kwa sababu wanyamapori wameongezeka baada ya uhifadhi kuimarika, Serikali sasa iwekeze katika kuweka packages, mafungu yenye kuvutia ya kufidia au kutoa vifuta machozi na vifuta jasho vitakavyowafanya Watanzania waendelee kuthamini rasilimali yawanyamapori tuliyonayo. Hilo likifanyika, uhifadhi wa wanyama utaweza kuwa guaranteed. Kwa sababu sasa hivi mgongano wa wanyamapori na binadamu unazidi kwa sababu wanyama wamehifadhiwa na sisi pia tunaongezeka; na suluhisho la hilo ni kuwafanya wananchi wawe wavumilivu kwa kuwapa mafao mazuri kutokana na hifadhi ya wanyamapori.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, napenda kusema kwamba naunga Mpango mkono na ninaipongeza Serikali yangu kwa kazi kubwa inayoendelea kufanya katika kutekeleza Mpango wetu wa Miaka Mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. DKT. STEPHEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili name niweze kuchangia hoja zilizopo mezani za Kamati ya Ardhi Maliasili na Utalii pamoja na kamati ya Kilimo Mifugo na Maji.

Mheshimiwa Spika nitumie fursa hii kuwapongeza Kamati kwa kazi kubwa walizozifanya na Wizara husika kwa kazi kubwa wanaoifanya kupeleka mbele maendeleo ya watanzani.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe dondoo chache katika sekta ya ardhi, maliasili na mifugo; na kama muda utaniruhusu nitaongelea pia suala la maji kwa kifupi sana.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ardhi; napenda kuipongeza Serikali kwa dhana nzuri muhimu sana ya kupanga kupima na kuradhimisha kila kipande cha ardhi ya nchi yetu; kwakweli hii dhana ni muhimu sana. Ninachelea kusema kwamba kwa ufinyu wa bajeti ambayo mapato ya ndani inatenga kila mwaka kuwapa Wizara, na kwa uhaba wa fedha za wafadhili na hata za mikopo tunayopata hatutakaa tufanikishe zoezi hili. Ningependa kuishauri Serikali kwamba twende sasa kwenye hatua ya kujiongeza, twende nje ya box kidogo. Tutafute namna nyingine ya kuongeza mapato ili tuweze kukamilisha zoezi hili kwa sababu migogoro ya ardhi haitakaa iishe kama kasi tutakayoendelea kwenda nayo ni hii ya kuhangaika ya urasimishaji wa makazi ambayo yalishazuka kiholelea katika sehemu mbalimbali za nchi yetu. Badala yake twende proactively mbele na kupima ardhi yote ya Tanzania na kumilikisha; tuwahi maeneo kabla hayajavamiwa na watu ambao nao wanazidi kuongezeka na kila siku wanahitaji kujenga.

Mheshimiwa Spika, ingependeza kama ambavyo imeshawahi kufanywa na Bunge hili tukaongeza hata tozo zingine katika baadhi huduma za kijamii na mazao au bidhaa mbalimbali kwa ajili tu ya kuongeza mfuko wa upangaji umimaji na urasimishaji wa ardhi ya nchi yetu .

Mheshimiwa Spika, mimi nilikuwa napenda kuishauri Serikali kwamba Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi ambao unahitajika kwa kasi zaidi kuliko inavyokwenda sasa usipofanya kwa kuweka fedha za ziada katika Wizara hatutafika na migogoro haitapungua. Ndiyo maana migogoro iko kila siku kati ya vijiji na vijiji kata na kata wilaya na wilaya, mkoa na mkoa na hata nchi na nchi.

Mheshimiwa Spika, kwahiyo naomba sana Serikali iende hatua ya ziada ya kutafuta fedha hata katika kuongeza kodi katika baadhi ya bidhaa zinazotengenezwa au kuuzwa au kuletwa nje ili tuweke kodi kama ile ya TDL ambayo iko katika mazao mengine ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kwenye sekta ya maliasili. Ninapenda kuipongeza kwa kweli wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya na kwa kuongezeka utalii nchini na kuimarika kwa hifadhi ya wanyamapori; na ndiyo maana hata sasa wanyama wamezidi mpaka wanakuja kurandaranda kwenye makazi ya watu na adha inazidi kuongezeka na kuwa kubwa katika mgongano unaotokea kati ya wanyama na binadamu.

Mheshimiwa Spika, mimi naomba, kwa sababu Wizara sasa hivi inafanya marejeo ya kanuni mbalimbali, katika marejeo inayohusika na suala la kifuta machozi pamoja na suala la kifuta jasho; pamoja na kwamba tunaamini package itaongezeka ili itie matumaini kuna kipengele muhimu ambacho hakipo; suala la majeruhi. Mtu anaweza akajeruhiwa akalipwa laki mbili na nusu lakini majeraha aliyopata anahitaji matibabu ya gharama kubwa na ambayo kile kifuta machozi hakiwezi kugharamia. Kwa mfano katika jimbo langu la Longido mtoto wa darasa la nne aliyekuwa anachunga tu wakati wa likizo aliparamiwa na tembo akaaribiwa mfumo wa mzima wa sehemu zake za siri katika ya miguu. Yule mtoto angekufa, lakini Wizara ya Maliasili na Utalii ilimpeleka Hospitali ya Rufaa ya Seriani; akatibiwa takribani miezi mitatu, gharama ikapanda mpaka ikafika milioni kumi na sita. Mtoto yule angezuiliwa pale mpaka alipe lile deni, lakini kwa sababu ya ubinadamu uliotumika na penda kuishukuru wizara ili bidi wamzamini mtoto akatoka na wizara ikatafuta kila namna tukasaidiana ili yule mtoto alipiwe ile bill.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa sababu hakuna sheria na wala haiko kwenye kanuni, ningeomba kanuni ya mafao ya kumtimu majeruhi iongezwe kwenye zili kanuni ili mtoto au mtu anapojeruhiwa lakini hajafa ile 250 tu ya kumfuta machozi haitoshi; ahudumiwe na Wizara wananchi waweze kuthamini hifadhi ya wanyamapori kwa sababu unalipa.

Mheshimiwa Spika, lingine ni kwa upande wa sekta ya mifugo. Sekta ya mifugo kwa kweli; nimeona kwenye ripoti yao; wametia mkazo zaidi kwenye suala la kuaharakisha uwekezaji kwenye viwanda. Tukiwekeza kwenye viwanda ilhali hatujawekeza kwenye malisho, maji, majosho, dawa za tiba na za chanjo pamoja na kuimarisha bei ya masoko ya mifugo tutakuwa hatujafanya kitu. Sawa, viwanda vinaweza vikajengwa lakini, je, kama hatujaweka mbele maslai ya ubora wa mifugo tunayofuga haijawekewa mkazo tutafika kweli? Ninaomba kwamba Serikali ijitahidi kuweka mkazo katika uboreshaji wa afya ya mifugo kwa kuwekeza kwenye maji, malisho tiba na vitu kama hivyo ili tuweze kufanikisha kuvipatia viwanda hivyo rasilimali inayostahili. Ikitokea kwamba viwanda vimekwisha na hatuna ng‟ombe wenye tija ambao viwanda vile vinahitaji wafugaji wetu wataendelea kuwa na adha kubwa ya sehemu ya kuuza mazao yao ya mifugo.

Mheshimiwa Spika, na sambamba na hilo pia niombe Wizara hii ya Mifugo, zile tozo ambazo sisi Wabunge wafugaji tumelalamikia kila wakati ni kubwa. Kabla hatujapata soko la ndani hizo tozo zipunguzwe ili hawa wafugaji waendelee kuuza hata nchi ya jirani wapate hela ya kuendelea ku-support familia zao.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, hivi viwanda vitakavyomalizika na vikaanza kuwa ndio watumiaji wakubwa wa bidhaa ya mifugo tunayozalisha hapa nchini ningeomba bei yenye ushindani itolewe; tusije tukaweka bei bei chini hao wawekezaji wa viwanda wakalaza bei ikawa ni kichocheo cha watu kuendelea kutamani kupekeka mifugo nje ya nchi Tanzania. Tuangalie masoko ya nje, nchi za jirani, tuweke bei ambayo ni sawia ili tuweze kutumia rasilimali ya mifugo kwa utaratibu huo na sisi tukapata faida.

Mheshimiwa Spika, kwenye sekta ya maji mimi nilikuwa nimeona kero moja kubwa sana ambayo iko katika miradi ya maji inayoanzishwa na Serikali; katika wilaya yangu kuna ile ya World bank; unakuta visima virefu vimechimbwa, watu wamewekewa miundombinu stahiki na mashine kubwa za kusukuma maji ku-pump maji lakini wanaachwa wananchi wasio na ujuzi wakaendesha zile mashine; na ndani ya miaka michache generator la milioni 20 unakuta limekufa kwa sababu hawajuwi ni lini oil inabadilishwa.

Mheshimiwa Spika, ningeomba Serikali iwe makini kukaribia hiyo miradi ambayo imeanzishwa waendelee kuwapeleka wataalamu na wawasimamie wanakijiji kamati zile za majizisiachiwe jukumu la kuendasha mitambo ambayo hawana ujuzi nayo maana wanaingia hasara. Sasa hivi sisi katika wilaya yangu tuna visima vingi mwaka huu na mvua imearibu mabwawa yote. Watu watakaa bila maji kwa sababu mashine zimearibika na hakuna utaalamu wa kuzitengeneza na wananchi hawana uwezo wa kununua mashine kama zile zilizowekezwa na Serikali mara ya kwanza.

Mheshimiwa Spika, sambamba hili na mwisho kabisa nipende pia kusema kwamba sisi jamii ya Wana Longido ni wafugaji na asilimia 99 ya maji ya mifugo ni yanatokana na mabwawa, na mabwawa yetu yote; tulikuwa na mabwawa 25 takriban yote ama yamejaa udongo ama yamepasuka. Wizara ya Maji na Wizara ya Mifugo kwa sababu sisi tukipata maji ya mifugo binadamu watatumia hayo hayo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana…

MHE. DKT. STEPHEN L. KIRUSWA: …tukipata maji ya binadamu mifugo watatumia maji hayo hayo wafanye bidii warudi Longido watusaidie kurekebisha miundombinu ya maji maana hali ni mbaya kweli kweli.

Mheshimiwa Spika ninakushukuru kwa kunipa nafasi, ninaunga mkono hoja zote za Kamati zote.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, natanguliza shukrani na pongezi kwa Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri inayofanyika. Nampongeza Rais, Mheshimiwa John Pombe Magufuli; Makamu wa Rais, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu; Waziri Mkuu na Baraza lote la Mawaziri, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Naibu Mawaziri kwa kazi nzuri na kubwa wanayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa mambo ninayojivunia anayoyafanya Rais wangu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ni pamoja na kujenga uchumi wa viwanda; kujenga nidhamu ya watumishi; kukemea uzembe; kuendesha vita dhidi ya ufisadi na dawa za kulevya; kufufua Shirika la Ndege Tanzania; kujenga reli ya kisasa (SGR) na barabara; kuongeza vyanzo vya umeme ikiwemo miradi ya gesi ya Stiegler’s Gorge Hydro Elecricity Power na kusambaza umeme hadi vijijini; kujenga bomba la mafuta kutoka Hoima (Uganda) – Tanga (Tanzania); kuimarisha huduma za afya; kutoa elimu ya msingi hadi kidato cha nne bila malipo; kujenga miradi ya maji; kuandaa mifuko ya maendeleo ya vijana, akina mama na walemavu; na kuhamishia makao makuu ya nchi Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee naishukuru Serikali kwa kuipatia Wilaya ya Longido miradi ya maendeleo kama ifuatavyo:-

(i) Mradi wa maji safi na salama kutoka Mto Simba Mlimani Kilimanjaro hadi Longido Mjini wenye jumla ya shilingi bilioni 16;

(ii) Ujenzi wa vituo vitatu vya afya katika Kata za Longido, Engarenaibor na Kimokoukwa/Namanga zinazogharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.5;

(iii) Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ambayo imetengewa fedha za kujengwa katika mwaka huu wa fedha wa 2018/ 2019;

(iv) Umeme wa REA Awamu ya Kwanza na Pili ambayo ulifikia vijiji 19 kati ya vijiji 49 vya Wilaya ya Longido; na

(v) Barabara inayosimamiwa na TANROADS kutoka Sanya Juu hadi juction ya barabara ya Mto wa Mbu Ngaresero yenye zaidi ya kilometa 200.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nijielekeze katika kuiomba Wizara iangalie orodha ya miradi ya maendeleo itakayotekelezwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018/2019 kama ifuatavyo:-

(i) Ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Sanya Juu, Wilayani Siha, Mkoa wa Kilimanjaro hadi Mjini Longido, Mkoa wa Arusha (kilometa 64). Barabara hii ilibainishwa kwenye Ilani ya CCM ya 2015-2020;

(ii) Kuendeleza mradi wa REA ili umeme ufike katika vijiji 30 vilivyosalia ndani ya Wilaya ya Longido. Kati ya kata 18 za Wilaya ya Longido ni kata 10 tu ndizo ambazo zimeshafikiwa na umeme wa REA. Kati ya vitongoji 176 za Wilaya ya Longido ni 36 tu ndizo vimefikiwa na umeme.

(iii) Katika Wilaya ya Longido bado tuna vijiji vingi ambavyo bado havina mitandao ya mawasiliano ya simu. Mbaya zaidi baadhi ya vijiji hasa kama Kata nzima ya Matale, Gelai - Wosiwosi na Kamwanga zinalazimika kutafuta mawasiliano ya simu kwa kutumia mitandao ya nchi jirani ya Kenya. Maeneo mahsusi ambayo bado hayana mawasiliano ya simu ni pamoja na Kata ya Matale, Gelai, Meirugoi, eneo la Wosiwosi, Kata ya Lumbwa, Elang’ata Dapash, Noondoto, Engikaret eneo la Kiserian na Kata ya Kamwanga.

(iv) Kutokana na kupanuka kwa eneo la jiografia na la kiutawala hasa kwa kuongezwa vijiji, kata na tarafa mpya Wilayani Longido, kuna vijiji kadhaa ambavyo bado vina changamoto kubwa ya miundombinu ya barabara. Naziomba TARURA na TANROADS zitusaidie kufikisha huduma ya barabara katika vijiji vya Meirugoi – Magadini (kilometa 34); Gelai Lumbwa – Wosiwosi (kilometa 54); Ketumbeine – Elang’ata Dapash (kilometa 18); barabara ya Ketumbeine hadi Iloirienito (kilometa 24); Meirugoi – Nadaare (kilometa 14); Engarenaibor – Matale C (kilometa 15); Namanga – Sinonik na Kimwati (kilometa 40); Sinya – Namanga (kilometa 30) na Engikaret – Kiserian (kilometa 14).

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kuna barabara nyingi za kuunga vijiji na vitongoji vyake zinazoendelea kujengwa kwa nguvu za wananchi Wilayani Longido, naiomba TARURA itenge fedha za kuwaunga mkono wananchi kwa kupitisha greda katika barabara hizo ili zipitike kirahisi. Miongoni mwa barabara zinazojengwa kwa sasa kwa nguvu za wanachi ni pamoja na barabara ya Mundarara – Orpukel – Gelai (kilometa 20); barabara ya Mundarara – Ingokiin – Engarenaibor (kilometa 15); barabara ya Mundarara – Injalai (kilometa 8); barabara ya Mairowa – Ing’ong’wen (kilometa 12); na barabara ya Matale A – Emurutoto – Mesera (kilometa 16).

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naomba niishauri Serikali kuhusu kuboresha huduma za usafiri wa anga na barabara kuja mji mkuu wa makao makuu ya nchi, Dodoma. Nashauri ATCL waanzishe safari za kutwa asubuhi na jioni kutoka Dar es Salaam – Dodoma; Dodoma – Arusha/ Kilimanjaro; Mwanza – Dodoma na Dodoma – Mbeya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri vilevile barabara za Mji wa Dodoma ziboreshwe, vibao viwekwe na kuwe na parking ya uhakika nje ya eneo la Bunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Rais wetu Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kazi kubwa na nzuri anayofanya kwa maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Waziri Profesa Ndalichako na Naibu wako Ole Nasha kwa hotuba yako nzuri iliyosheheni mambo mengi mazuri kuhusu elimu nchini mwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachangia hoja katika masuala matatu; kwanza, elimu ya awali (tazama hotuba ukurasa 78), pili; elimu maalum (tazama hotuba ukurasa 81) na tatu; Programu ya Lipa kwa Matokeo (EP4R) ukurasa wa123 – 124.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza elimu ya awali, Serikali iweke kipaumbele katika uanzishwaji wa shule za chekechea, shule za awali kabla ya darasa la kwanza (pre- schools). Kwa kuwa msingi mzuri wa elimu huanzia katika shule za awali, nashauri ijihusishe rasmi katika uanzishwaji wake na kuajiri walimu waliofuzu kutoa elimu kwa ngazi hiyo (early childhood development).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iandae mitaala ya elimu ya awali. Nashauri Serikali ianzishe taasisi mahsusi ya elimu ya awali kama ilivyo Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siri ya mafanikio katika shule za binafsi ni kwa sababu wamezingatia kumuendeleza mtoto kuanzia umri mdogo kabisa (3 -5 years) kabla ya kuanza elimu ya msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuelekeza juhudi za kuboresha elimu nchini kuanzia ngazi ya elimu ya awali, naomba Serikali izingatie kuwa shule za awali zilizoko ndani ya shule za msingi nchini haziwasaidii watoto wadogo walio chini ya umri wanaotoka au kukaa mbali na shule, hususan kwa jamii za wafugaji wanaoishi mbali na shule. Hivyo Serikali izingatie haja ya kusogeza huduma za elimu bora ya awali hadi kwenye vitongoji. Elimu hii itolewe na walimu waliosomea tofauti na sasa ambapo elimu hii ndani ya vituo vya ngazi ya vitongoji hutolewa na walimu wasio na ujuzi (failures wa darasa la saba au kidato cha nne) wanaoajiriwa na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu maalum; ukienda ukurasa wa 81 wa kitabu cha hotuba ya Waziri kifungu cha 80(i) na (ii) utapata maelezo yasiyojitosheleza kuhusu usimamizi wa elimu maalum. Natoa rai kwa Serikali/Wizara ijipambanue kwa ufasaha zaidi kuhusu elimu maalum. Naunga mkono suala la elimu jumuishi lakini nashauri kuwepo kwa vitengo mahsusi ndani ya shule zetu kuanzia chekechea hadi vyuo kwa ajili ya nyanja mbalimbali za elimu maalum. Mbadala wake zianzishwe shule mahsusi kwa ajili ya ulemavu wa aina tofauti. Shule za viziwi (chekechea – vyuo), vipofu (chekechea – vyuo), wenye mtindio wa ubongo (chekechea – vyuo).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu programu ya lipa kulingana na matokeo katika elimu (EP4R), huu mpango ni mzuri sana. Naomba uongezewe bajeti na wigo wa miradi ya kutekelezwa upanuliwe kulingana na mahitaji ya shule husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba katika Wilaya yangu ya Longido fedha hizi pamoja na mambo yameshaelekezwa, lakini pia zielekezwe katika kununulia gari la shule. Sekondari zetu saba zilizo katika remote areas ambapo huduma muhimu na dharura ikitokea ziko mbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za sekondari za bweni Wilayani Longido ambazo zinastahili kuwa na gari la shule ni pamoja na shule ya wasichana Lekule iliyoko Gelai Lumbwa umbali wa kilometa 90 kutoka barabara ya lami na makao makuu ya Wilaya, Flamingo sekondari Kata ya Meirugoi ambayo ipo zaidi ya kilometa 90 kutoka barabara ya lami, shule ya sekondari Ketumbeine iliyoko umbali wa kilometa 60 kutoka lami, shule ya Enduimet sekondari kilometa 110 kutoka Longido Mjini na barabara ya lami, sekondari ya Tingatinga kilometa 50, sekondari ya Engeremibor kilometa 40, sekondari mpya tarajiwa ya Matale kilometa 60.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote naunga mkono hoja. Pili, nampongeza Waziri, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu na watendaji wote wa Wizara kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuleta mapinduzi ya kiuchumi katika Sekta ya Mifugo. Sekta hii ya Mifugo ilikuwa imedorora kwa miaka mingi pamoja na kuwa ni sekta muhimu kwa uchumi wa Taifa letu. Sera ya Mifugo ya mwaka 2006 na Sheria ya Nyanda za Malisho ya Mwaka 2010 zinasisitiza kwamba uchumi wa mifugo una nafasi muhimu na ya kipekee katika kujenga uchumi imara wa Taifa letu. Ili mifugo iwanufaishe wafugaji na kuliletea mapato makubwa Taifa ni lazima mifugo ipate maeneo ya malisho, maji, tiba na masoko sambamba na miundombinu ya barabara, viwanda vya nyama na mazao ya mifugo.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hotuba ya Waziri imeagiza haya yote naomba atekeleze aliyoyasema kwa kuhakikisha kuwa wafugaji hasa wa asili wanapimiwa na kutengewa maeneo yao mahsusi ya kufugia. Kwa mfano, katika Jimbo langu la Longido, sisi tuna nyanda za malisho zaidi ya 20 ambazo zikiendelezwa kwa kuchimba mabwawa na visima virefu vitawezesha ufugaji wenye tija ili viwanda vya nyama vinavyoendelea kujengwa nchini ipite rasilimali ya kutosha na yenye ubora unaohitajika. Baadhi ya maeneo yetu ya malisho yanayohitaji kuendelezwa ni pamoja na Loorboro, Oldenja na Engasurai.

Mheshimiwa Spika, tiba, chanjo na uogeshaji izingatiwe. Tatu, masoko mpaka masoko ya ndani ya uhakika yapatikane, masharti na tozo za kuuza mifugo na bidhaa zake nje zilegezwe ili wafugaji wasiendelee kuumia. Mwisho naomba Wizara izingatie na kuongeza suala la jinsi ya kukab iliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kwenye suala zima la uendelezaji wa Sekta ya Mifugo hususan nyanda za malisho na vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi ya kuchangia na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Waziri, Mheshimiwa Dkt. Augustine Mahiga na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Suzan Kolimba na Watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuendelea kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia kwa masuala ya uhusiano wa Kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, napenda kuendelea kuipongeza Serikali yetu ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, kwa kazi nzuri na kubwa ya kuijenga Tanzania ya viwanda na maendeleo ya uchumi wa kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizi naomba sasa nichangie hoja ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali ipatie kipaumbele haja ya kurekebisha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuruhusu raia wake kuweza kuwa na uraia pacha (Dual Citizenship). Nionavyo kuna faida kubwa kuliko hasara kama Watanzania wanaopenda kuwa na uraia wa nchi mbili watahalalishwa kufanya hivyo, kwani kwa kufanya hivyo, tunajiongezea fursa za kiuchumi na kijamii, hasa kwa Watanzania wenzetu wanaoishi na kufanya kazi nchi za nje (The Diaspora Community).

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la Itifaki ya Soko la Pamoja la Afrika ya Mashariki. Ingawa hotuba ya Waziri inatamka bayana katika ukurasa wa 28, aya ya mwisho kuwa, wananchi na hasa vijana washiriki katika kuchangamkia fursa zilizoko kwenye soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki, hali ilivyo sasa kwa wasafiri wanaotumia Hati za Dharura za kusafiria siyo rafiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, zamani Hati za Dharura za Kusafiria zilikuwa zinatolewa kwa kuruhusu kutumika kwa multiple entries kwa muda wa mwaka mmoja, lakini kwa sasa na kwa sababu ambazo wananchi wanaosafiri mara kwa mara kwenda na kurudi katika nchi jirani zetu Afrika Mashariki hupewa hati za dharura ambazo zinaruhusu single entry visa tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni kumaanisha kuwa, mara msafiri anapopita kwenda nchi ya jirani, mfano Kenya, kwa wajasiriamali wa mpaka wa Kenya na Tanzania, Namanga, ambao hufanya biashara katika masoko ya nchi jirani kila wiki hulazimika kukata hati mpya ya dharura ya kusafiria kila trip hata kama atasafiri kwenda na kurudi kila siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili siyo rafiki kwa uchumi wa wananchi na vijana wanyonge ambao Itifaki ya Soko la Pamoja ililenga kuwasaidia. Gharama ya hati kwa kila safari ni wastani wa Sh.20,000/= na kama msafiri atahitaji kwenda Kenya mara tano kwa mwezi, kwa mfano, atalazimika kutumia hadi Sh.100,000/= kwa hati ya kusafiria.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri na kuiomba Serikali watengeneze mazingira rafiki ya ama kurejesha Hati za Dharura ambazo ni valid for multiple entries for one year au utoaji wa Pasi za Afrika Mashariki urahisishwe na kuwezekana kutolewa mpakani tofauti na sasa ambapo ni mpaka maombi yapelekwe Dar-es-Salaam na kuchukua zaidi ya miezi sita mpaka msafiri apate pasi hiyo, au ikubalike sasa kuwa, Watanzania waruhusiwe kusafiri nchi za Jumuiya yetu kwa kutumia vitambulisho vyao vya Kitaifa tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Baada ya kuunga mkono hoja hii muhimu ya Wizara ya Nishati, naomba pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu wake pamoja na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuitoa Tanzania gizani na kutupatia nishati ya kuendeshea viwanda.

Mheshimiwa Spika, pia naomba kuishukuru Serikali kupitia Waziri kwa kututengea fedha kutoka fungu la TANESCO kwa ajili ya kupeleka umeme Makao Makuu ya Tarafa ya Ketumbeine yenye vijiji 20 ambavyo tangu mradi wa REA kuanzishwa nchini hadi leo hawajafaidika bado kupata umeme.

Mheshimiwa Spika, kwa ajili ya ufanisi na uendelevu wa mradi mkubwa wa Stiegler’s Gorge, naomba kushauri Serikali iwekeze kwa makini katika zoezi la kuhakikisha kuwa vyanzo vyote vya kupeleka maji kwenye Bwawa la Stiegler’s Gorge yahifadhiwe na kutunzwa kwa gharama yoyote.

Mheshimiwa Spika, pili, katika usanifu unaoendelea na ujenzi wa Stiegler’s Gorge Dam, ni vizuri Serikali izingatie na kujipambanua namna ya kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi. Serikali iwekeze katika kuwatafutia wananchi wanaotegemea maji ya vyanzo vinavyopeleka maji hadi Bwawa la Stiegler’s Gorge vyanzo vya mbadala ili maji yote yaelekezwe katika mradi huu wa kuzalisha umeme kwa ajili ya utoshelevu na uendelevu wake majira yote ya mwaka hata katika majira ya ukame.

Mheshimiwa Spika, mwisho naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja yake ayajibu maswali mawili yafuatavyo; moja, ni lini vijiji 30 vya Wilaya ya Longido ambavyo bado havijafikiwa na umeme wa REA; watapata nishati hii? Ni vijiji vingapi vimeingizwa katika bajeti ya mwaka huu wa 2019/2020?

Mheshimiwa Spika, kuna vijiji ambavyo vimeshafikiwa na umeme lakini makazi yameongezeka na kuna vitongoji vingi havijapelekewa umeme bado. Mwaka huu wa fedha 2019/2020 Serikali imetenga fedha za kufanya ujazilizi katika vijiji vya Wilaya yangu ya Longido. Kati ya maeneo ambayo yana uhitaji mkubwa wa mradi wa ujazilishi ni pamoja na vijiji vya Mundarara kwenye machimbo ya madini ya Ruby, Mairowa (Kata ya Engarenaibor), Namanga, Longido, Olmolog, Elerai, Kamwanga na vijiji vyote 20 vya Tarafa ya Ketumbeine ambavyo bado havijafikiwa na umeme wa REA.

Mheshimiwa Spika, kwa haya machache, nashukuru na natamka tena kuwa naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali ya Awamu ya Tano ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kazi kubwa na nzuri ya kulinda na kudumisha amani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba na Waandamizi wake kwa hotuba nzuri ya kiwango na kwa kazi nzuri wanayoifanya. Baada ya pongezi, naomba sasa nichangie hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kuhoji yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hati za dharura za safari, naomba Mheshimiwa Waziri anifafanulie kwa nini hati za dharura za safari kwa sasa zinatolewa kwa single journey badala ya multiple trips kwa muda wa mwaka mmoja kama zamani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wengi wa wasafiri wanaokwenda nchi za jirani hususani Kenya kwa upande wa mpaka wa Namanga Wilayani Longido ni Watanzania maskini na wajasiliamali. Je, Serikali haioni inawakandamiza na kuwasababishia usumbufu usio wa lazima wananchi ambao watahitaji kufanya safari kadhaa kwenda na kurudi nchi ya jirani ndani ya muda mfupi au mara kwa mara, kwa mfano wanaokwenda kwenye masoko ya County ya Kajiado na Nairobi kila wiki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali ilivyo sasa hivi kwa wananchi wenye haja ya kwenda Kenya angalau mara moja kila wiki na ambao ni maskini tu wasio na pesa kubwa wanalazimika kuomba mpya kila wiki na wanalazimika kuwasilisha upya viambatisho lukuki (Vyeti vya kuzaliwa vya Mwombaji na wazazi, vitambulisho na kadhalika) ambavyo mara nyingi hawana na hasa kwa jamii yetu ya Kimasai ambao wengi hawana vyeti vya kuzaliwa. Utaratibu wa sasa unaleta adha kubwa kwa wasafiri maskini na hivyo naomba Serikali irejeshe Multiple Trips Travel Documents.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa kutoa hati za dharura za safari mpakani. Naomba kuishauri Serikali iboreshe mazingira ya wananchi wanaohitaji kusafiri nchi za jirani kwa kutumia hati za dharura waweze kupewa pale mipakani tofauti na sasa ambapo wanalazimika kusafiri kwenda Makao Makuu ya Wilaya kupata Hati hizo ambazo uhai wake ni kwa safari moja hata kama atahitajika kurudi mara kadhaa ndani ya wiki moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kurahisisha upatikanaji wa Pasi za Afrika Mashariki; kwa kuwa hati za dharura za safari ina adha kubwa na gharama kwa wasafiri wanaohitaji kusafiri na kurudi ndani ya muda mfupi, watengenezewe mazingira ya kuweza kupata pasi za Afrika Mashariki zenye uhai wa muda mrefu palepale mpakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ilivyo kwa sasa upatikanaji wa pasi Afrika Mashariki ni mgumu kwani ni mpaka upeleke maombi Makao Makuu ya nchi na inachukua muda mrefu kabla ya kutoka. Kwa kuwa, Wilaya ya Longido ni ya mpakani na kuna haja ya kuiwekea ulinzi wa kutosha, naomba Serikali itujengee angalau kituo kimoja cha Polisi katika kila Tarafa hasa zile zinazopatikana Kenya ikiwemo Tarafa ya Katumbeine na Engarenaibor.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Wilaya ya Longido ina vituo vitatu vya Polisi kimoja mpakani Namanga, kimoja Mjini Longido na Kata ya Kamwanga. Kwa uhaba uliopo wa vituo vya usalama wa raia, katika Tarafa ya Ketumbeine, karibu kila mwaka majambazi huteka watu na kuwapora mali. Hivyo, kuna haja kubwa ya kujenga kituo cha Polisi katika Tarafa hiyo hasa Kata ya Mairugoi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ni kuhusu Sekta ya Kilimo; kwa kuwa mwaka huu Kanda ya Kaskazini hasa Mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro inakabiliwa na ukame kufuatia mvua za masika kutonyesha, nashauri Serikali iandae bajeti ya kutosha na kuweka utaratibu wa kuwaletea wananchi chakula cha bei nafuu toka mikoa yenye chakula cha kutosha mwaka huu.

Pili ni kuhusu Sekta ya Mifugo na Uvuvi; nashauri Serikali iwekeze katika uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo na uanzishwaji wa masoko ya ndani ya uhakika. Pia nashauri Serikali ipange bei elekezi kwenye bidhaa za mifugo na ipange bei ya kishindani kwa kulinganisha na bei ya bidhaa husika katika masoko ya nchi jirani kama vile Kenya. Vile vile nashauri bei ya nyama ya mbuzi, kondoo na ng’ombe kwa kilo ipangwe na Serikali na mifugo minadani iuzwe kwa kupimwa kwenye mizani na bei ya mifugo kwa mnyama hai (live weight) ipangwe na Serikali kama ilivyo kwa mazao ya kilimo (mazao ya biashara).

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, ni Sekta ya Utalii; nashauri Serikali ipanue wigo wa biashara ya utalii kwa kuunganisha utangazaji wa vivutio vya utalii nchini ili pamoja na wanyamapori ambao ndio kivutio kikuu, pia tutangaze utalii katika misitu yetu ya asilia (Nature reserves) sambamba na utalii wa utamaduni (cultural tourism). Pia nashauri channel yetu ya utalii itangaze kwa lugha mbalimbali za mataifa yanayopenda utalii. Sambamba na hilo tuombe airtime space kwenye channel za Serikali za mataifa yanayopenda utalii na vivutio tulivyonavyo. Baadhi ya Channels hizo ni pamoja na PBS ya Marekani (Public Broadcasting Service), BBC, DW na National Geographic Society.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika, utitiri wa kodi uunganishwe ili kuwa na kituo kimoja (one stop center) na kodi moja jumuishi ili kuondolea wawekezaji na wateja usumbufu na urasimu usio wa lazima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, Sekta ya Ardhi; nashauri Serikalli iongeze bajeti na rasilimali fedha, vifaa na wataalam wa kutosha hadi ngazi ya Halmashauri za Wilaya nchini ili kuongeza kasi ya kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi ya nchi yetu kulingana na Sera na Mpango wa Taifa wa Ardhi 2013 – 2033.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano ni Sekta ya Barabara; katika kufungua barabara zenye kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi, naomba Serikali itoe kipaumbele mwaka huu wa fedha kumalizia kipande cha barabara chenye urefu wa kilomita 41 zilizobaki kwenye barabara ya Sanya Juu hadi Kimwanga kuzunguka Mlima Kilimanjaro. Pia barabara ya Siha/Sanya juu – Longido (kilomita 56) ipewe kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, kuhusu Kazi, Ajira na Vijana; nashauri Serikali mgawo wa 10% ya mapato ya ndani ya Halmashauri zetu za Wilaya ambapo akinamama na vijana hupewa mikopo isiyo na riba kwa uwiano wa 4% kwa kila kundi na watu wenye ulemavu 2%. Nashauri watu wenye ulemavu wasikopeshwe hiyo 2% wanazogaiwa bali wapewe kama msaada (seed fund) wa kuwawezesha kuanzisha miradi ya kujikimu kimaisha. Kwa kuwa watu wenye ulemavu huwategemea ndugu na jamaa na watu wenye mapenzi mema kuwazungushia mitaji yao, mara nyingi kasi ya miradi huwa ndogo na pia uwezo wa kurejesha mikopo yao kwa wakati kuwa hafifu. Hivyo basi nashauri iwe sehemu ya social welfare na uwajibikaji (CSR) wa Serikali yetu kuwapa watu wenye ulemavu hiyo 2% kama msaada na siyo mikopo ya kurudishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira za moja kwa moja katika Utumishi wa Umma; nashauri Serikali iongeze bajeti ya kutoa ajira za moja kwa moja ili kuondoa upungufu mkubwa wa watumishi wa kada mbalimbali unaozikabili Halmashauri za Wilaya zetu na sekta mbalimbali za Serikali. Kwa kutoa ajira za moja kwa moja Serikali itaondoa changamoto kubwa iliyopo ya kuwa na utitiri wa watumishi wanaokaimu nafasi mbalimbali na kwa muda mrefu. Jambo hili linaathiri utendaji (performance) katika Halmashauri ya Wilaya yangu ya Longido ambapo zaidi ya 50% ya Watendaji wa Vijiji (VEDS) ni watumishi wanaokaimu nafasi hizo na kwa miaka mingi.

Pia kwenye idara za halmashauri tuna upungufu mkubwa na lundo la watumishi wanaokaimu nafasi kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, naomba kutamka kuwa naunga mkono hoja! Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote natoa pongezi kwa Waziri Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako, Naibu Waziri Mheshimiwa William Ole Nasha, Katibu Mkuu na timu nzima ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kazi nzuri na kwa hotuba hii nzuri iliyosheheni miradi mingi iliyotekelezwa mwaka huu 2018/2019. Baada ya pongezi hizi naomba sasa nichangie hoja kwa kutoa maoni na ushauri wangu kwa Serikali, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Miundombinu; ukarabati wa Taasisi za Elimu; naishauri Serikali isiishie kukarabati vyuo na shule kongwe tu bali itenge fedha za ukarabati wa shule zake zote kila mwaka wa fedha. Kwa suala la shule kongwe, Wilayani Longido sisi tuna shule kongwe za msingi zilizojengwa tangu enzi ya ukoloni. Kwa mfano tuna shule ya bweni ya msingi ya Longido ambayo ilijengwa mwaka 1947 na majengo yake yamekuwa chakavu, hivyo inastahili kukarabatiwa na Serikali. Hii ndiyo shule ya msingi aliyosoma hayati Edward Moringe Sokoine, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mitaala; Taasisi ya Elimu Tanzania; suala la Mitaala, Miongozo na Vitabu; Serikali ijumuishe shule za awali katika mipango yake ya kuandaa mitaala, miongozo na kuchapa vitabu vya kiada na rejea. Msingi wa elimu bora huanzia ngazi ya elimu ya awali na si darasa la kwanza na kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA); nashauri Serikali iongeze kasi ya kuanzisha VETA katika kila wilaya nchini. Kwa kuwa, Wilaya ya Longido hakuna chuo chochote cha Serikali na tuna ardhi ya kutosha na kwa sasa tuna maji safi na salama ya kutosha pamoja na umeme Makao Makuu ya Wilaya na vijiji jirani, naikaribisha Wizara watujengee VETA ya Taifa inayolenga fani zifuatazo: Mifugo (livestock production & livestock products), wanyamapori (wildlife nature conservation & tourism), madini (small scale mining skills), huduma za kitalii (Hospitality & Hotel Management), Uashi na useremala, TEHAMA na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na uanzishwaji VETA kila wilaya, nashauri Serikali ianzishe chuo mahsusi cha Walimu wa sayansi, ili kuziba pengo la uhaba mkubwa tulionao wa Walimu wa sayansi katika shule zetu za sekondari na vyuo. Kwa kuwa, sisi Longido tuna ardhi, maji na umeme naikaribisha Serikali ijenge chuo hicho Wilayani Longido na kiitwe Tanzania Science Teachers’ College. Chuo hiki kitakuwa ndio kiwanda cha kuzalisha Walimu wa fani zote za sayansi kwa ajili ya mahitaji ya nchi yetu katika ngazi zote husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu; naipongeza Serikali kwa ongezeko la wanafunzi wanaopewa mikopo ya elimu ya juu. Naomba kuishauri Serikali itoe elimu ya jinsi ya kuzaja fomu kwa usahihi katika kila shule yenye wanafunzi wanaostahili kupewa mkopo ili kuondoa tatizo lililopo la baadhi ya wanafunzi wenye sifa kukosa mikopo kwa sababu ya kutojua jinsi ya kujaza fomu za maombi kwenye mitandao kwa usahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba niiangalize Serikali kuhusu suala la uwepo wa vijiji vichanga nchini ambavyo bado havina shule za msingi sambamba na huduma zingine muhimu za kijamii kama zahanati, barabara, mawasiliano ya simu, maji na umeme. Kwa mfano, katika Wilaya ya Longido yenye jumla ya vijiji 49, tuna vijiji kadhaa ambavyo havina shule na hivyo, kuna idadi kubwa ya watoto ambao hawaendi shule. Baadhi ya Vijiji hivyo katika Wilaya ya Longido ni pamoja na Engusero (Kata ya Naondoto), Nadaare (Kata ya Iloirienito), Wosiwosi (Kata ya Gelei Lumbwa), Leremeta (Kata ya Sinya) na Loondolwo (Kata ya Meinigoi). Naiomba Serikali itenge fedha za kuwaunga mkono wananchi kwa kuwachochea kuanzisha shule za awali na msingi katika vijiji hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naunga mkono hoja, lakini pia naomba kumpongeza Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanayofanya. Pamoja na kazi nzuri zinazofanywa na Wizara, naomba kuchangia hoja kwa kuangazia maeneo machache kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, uhamasishaji wa akinamama kujifungulia zahanati, vituo vya afya na hospitali. Kuna changamoto kubwa ya wodi za kujifungulia, wataalam na vifaa katika facilities tulizonazo katika Wilaya ya Longido. Vijiji vingi havina zahanati na kwa vichache viliyonavyo nafasi na huduma hazitoshelezi kulingana na uhitaji.

Naomba Serikali iongeze kasi katika kujenga zahanati na vituo vya afya katika vijiji na Kata za Ketumbeine, Kimokouwa/Namanga na Tarafa ya Enduiment.

Mheshimiwa Naibu Spika, Suala la Afya kwa Umma (Public Health); Wilaya ya Longido tuna changamoto kubwa ya kutokuwa na gari la kuzoa taka kwenye miji yetu midogo na pia gari la kunyonya maji machafu vyoo vinapojaa. Naomba kumuuliza Waziri kuwa Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa watu kila wilaya (Halmashauri) imepata gari la taka na la kunyonya maji machafu kwenye vyoo hasa vya Taasisi za Umma kama hospitali, shule na kwingineko?

Mheshimiwa Naibu Spika, upatikanaji dawa kwenye zahanati na vituo vya afya; katika Wilaya ya Longido, tuna kata ambazo zinategemea zahanati moja tu kama Namanga ni kuwa Idadi ya Wakazi ni kubwa sana (zaidi ya wakazi 12,000) mgao wa dawa wanayopata kila baada ya miezi mitatu toka MSD hazimalizi hata mwezi mmoja kabla ya kwisha na wananchi hulazimika kwenda kununua madawa kwenye maduka ya binafsi. Hali hii imepelekea wananchi kutoona manufaa ya kujiunga na Mfuko wa Bima ya Jamii (CHF) kwa sababu hawapati dawa nyakati zote. Naomba kuishauri Serikali kugawa dawa kulingana na idadi ya watu na wanaohudumiwa katika kituo husika badala ya kuangalia kiwango kuwa ni zahanati au kituo cha afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mandatory Health Cover, ulazima wa kila mtu/Mtanzania kuwa na Bima ya Afya); naunga mkono hoja ya kutaka kila Mtanzania kuwa na Bima ya Afya, lakini nashauri kuwa kabla ya kupitisha Sheria ya kusimamia zoezi hili, Serikali ihakikishe kuwa kila kituo cha huduma ya Afya (Zahanati, Kituo cha Afya, Hospitali) kinakuwa na dawa zate za msingi wakati wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, Uhaba wa nyumba za Wahudumu wa Afya hasa vijijini; katika Wilaya ya Longido tuna changamoto kubwa ya nyumba za Wauguzi hasa katika Zahanati zetu za vijijini. Kwa mfano katika Kijiji cha Losirwa, Kata ya Iloinenito, Tarafa ya Longido, Madaktari na Nesi wanaishi ndani ya zahanati kutokana na ukosefu wa nyumba za kuishi na kijiji kilichoko katika eneo lenye mazingira magumu kwa barabara, mawasiliano na hata maji. Naomba Serikali itenge bajeti ya kusaidia maeneo kama hayo katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumalizia ujenzi wa vituo vitatu vya afya, naomba kushukuru Serikali kwa kuwa ilitutengea fedha mwaka uliopita kwa ajili ya ujenzi wa vituo viwili vya Afya – Kata ya Engiromibor shilingi milioni 400 na Kata ya Kimokouwa shilingi milioni 700. Kwa Vituo hivi viko katika hatua za umaliziaji na fedha tulizopewa zimemalizika, naomba Serikali itenge tena fedha katika bajeti hii ili tuweze kumalizia Kituo cha Engareneibor kinahitaji shilingi milioni 269 kumalizika ni Kimokouwa tunahitaji shilingi milioni 310 kumalizia.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tuna Kituo cha Afya kipya tulichoanza kujenga kwa nguvu za wananchi katika Tarafa ya Ketumbeine, Kata ya Ketumbaine. Tumeweza kujenga hadi kupaua na sasa naomba Serikali ituunge mkono ili kumalizia kituo hicho mwaka huu wa fedha ili kianze kutoa huduma kwa wananchi wa vijiji 20 vya Tarafa ya Ketumbeine ambao kwa miaka yote wamekuwa wakifuatilia huduma za afya Longido ambavyo kwa vijiji vingine ni zaidi ya kilomita 110 kwenye barabara mbovu za vumbi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba tena kusema naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naunga mkono hoja na nampongeza Waziri wa Viwanda na Biashara pamoja na Naibu wake na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri wanayofanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi sina, naomba nimpongeze Rais wangu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya kuhamasisha ujenzi wa uchumi wa kati wa viwanda. Miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu inayoendelea ikijumuisha njia za reli, umeme, barabara, viwanja vya ndege na bandari ni ishara tosha kuonyesha dhamira njema ya Rais ya kujenga uchumi wa viwanda inakwenda kutekelezwa kwa vitendo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa msingi huu, nashauri sasa Serikali iwekeze juhudi za dhati za kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa viwanda vya aina mbalimbali nchini kwa kuondoa au kupunguza kodi zisizo za lazima, kuharakisha utoaji wa vibali na kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika nchi yetu. Hizi fursa ni pamoja na kuanzisha na kufufua viwanda vya mazao ya kilimo, mifugo, madini na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe hoja kuhusu mradi wa Magadi Soda Engaruka. Mradi huu umezungumziwa katika kitabu cha hotuba ya Waziri ukurasa wa 17. Pamoja na utafiti wa kina ambao umeanza kufanyika kubaini upatikanaji wa rasilimali ya magadi, maji safi, athari za mazingira na kijamii, naomba nitoe angalizo kuhusu masuala yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ingawa eneo kubwa la mradi wa magadi liko katika Wilaya ya Monduli, vilevile kuna sehemu ya ardhi iliyopimwa ambayo imeingia ndani ya eneo la Wilaya jirani ya Longido (Kijiji cha Sokon). Hivi sasa tunavyojadili bajeti ya Wizara hii, wananchi wa Kijiji cha Sokon wanaoishi katika eneo ambalo limeingia ndani ya ardhi iliyopimwa na kufanywa sehemu ya viwanda wameshapewa notisi ya kuhama ndani ya wiki mbili na huku bado hawajafidiwa. Nashauri wananchi wasibughudhiwe mpaka wafidiwe kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, faida za mradi kwa wananchi ama Wilaya husika. Kwa kuwa mradi huu wa magadi umetwaa vipande vya ardhi vilivyoko ndani ya Wilaya ya Monduli na Longido, ni vyema Wizara itambue hilo na ibainishe kuwa kiko katika wilaya zote mbili ili jamii zote wapate faida na kuepusha migogoro isiyo ya lazima ya kugombania rasilimali husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, miundombinu. Kwa kuwa eneo la mradi ni mbali (remote area) na lenye mazingira magumu na lisilo na barabara inayopitika, nashauri Serikali iwekeze kwanza katika kufungua barabara za kufikia eneo la mradi. Kuna njia mbili za kufika katika eneo la mradi: Barabara ya kutoka Mto wa Mbu (km 70); na barabara ya kuunga barabara ya moram inayotoka Longido – Oldonyo Lengai (km 14).

Mheshimiwa Naibu Spika, nne, umuhimu wa kuanzisha kiwanda cha kuchakata nyama. Kwa kuwa eneo la Bonde la Engaruka na maeneo yote yanayopakana nalo ni ya wafugaji ikijumuisha Tarafa nzima ya Ketumbaine, Wilayani Longido, Engaresero, Wilayani Ngorongoro na Tarafa ya Ngorongoro, Wilayani Monduli. Napenda kuishauri Serikali kuwa kijengwe kiwanda katika eneo hili cha kuchakata nyama. Eneo hili ni tajiri kwa mifugo na lina nyanda pana za malisho kasoro maji safi na kwa kuwajengea wafugaji kiwanda cha kuchakata nyama na mazao mengine ya mifugo itakuwa ni faida ya ziada ya kufunguliwa uchumi wa viwanda katika Bonde la Engaruka.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, naomba kuhitimisha kwa kutamka tena kuwa naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hoja iliyopo mezani ya taarifa hizi zilizoletwa na Kamati zetu. Nikijielekeza kwenye Kamati ya Nishati na Madini, nitumie fursa hii kuwapongeza sana Wanakamati kwa kazi nzuri mno na ripoti nzuri ambayo wametuletea sisi kama Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika taarifa waliyoileta wameleta mapendekezo na maoni yao mbalimbali. Nitumie fursa hii kusema kwamba sisi kama wizara tumeyachukua yote na tutakwenda kuyafanyia kazi na tutaleta mrejesho unaoeleweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwenye mapendekezo ya taarifa hii ya Kamati masuala mbalimbali yamejitokeza. Kwa mfano, wameelezea suala la STAMICO kwamba STAMICO ijikite katika uwekezaji wa mambo machache lakini yenye tija. Hili sisi tunalichukua kama Wizara tutaenda kulifanyia kazi kwa sababu tayari STAMICO ni moja ya taasisi zetu muhimu sana katika kufanikisha ukuzaji wa sekta ya madini. Hivi sasa STAMICO wanaendelea kujikuza kuongeza mitambo ya kisasa zaidi, kuongeza ujuzi zaidi na wameleta hata kuwekeza katika kutafuta mitambo ya kuwasaidia wachimbaji wadogo. Kwa hiyo, hili tunalibeba kwa uzito wake na tutalifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na suala lingine la mambo ya PPRA kwamba Kamati kweli imeona umuhimu wa STAMICO kuongeza kasi ya utendaji iweze kuwa shindani katika soko; maana yake kuna kampuni za binafsi pia zinafanya kazi za uchorongaji, utafiti, ni kweli na sisi tunalipokea hili na kama Wizara tutaendelea kuijengea uwezo na kwa sababu mfumo wa PPRA unahusika na ununuzi wa umma procurement, nadhani hili ni suala nyeti ambalo tutahitaji kukaa na wenzetu wa Wizara husika tuangalie namna ambavyo watawasaidia STAMICO nao waende kwa kasi. Maana procurement zingine zinachukua muda na wanapitwa na kandarasi ambazo zingewaongezea mapato na Shirika letu la STAMICO liendelee kuonekana kama ni shirika la kibiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia taarifa ya Kamati tunapokea tu yale ambayo wameleta tutayafanyia kazi nataka tu wajue kwamba tumeyapokea yote, lakini kwa upande wa utitiri wa tozo mbalimbali, ada zinazotozwa hasa kwa wachimbaji wadogo. Sisi tumelipokea hilo na Wizara tayari imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kwamba tutakaa na wenzetu wa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na taasisi yao TRA tuangalie ni tozo zipi, kodi zipi ambazo zinakwenda kukwamisha ukuaji wa sekta ya uchimbaji wa madini hasa wachimbaji wadogo. Hilo pia tumelipokea kwa uzito wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano tu wa kwamba Serikali inasikiliza. Katika awamu iliyopita kabla mimi sijaingia kwenye nafasi hii, kuna wakati hata baadhi ya kodi ziliondolewa, kama ile VAT ya asilimia 18 kwa wachimbaji wadogo iliondolewa, ikaondolewa pia kodi ya zuio, withholding tax ya asilimia tano na kuna utitiri wa kodi nyingine ambazo bado tutakwenda kuendelea kuzifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kupokea hii Taarifa ya Kamati walipendekeza kwamba Tume ya Madini iendelee kuongezewa uwezo au tuseme tu taasisi zote za Wizara ya Madini maana tuna Tume ya Madini, STAMICO, TEITI, Geological Survey of Tanzania – GST na hawa wote wana changamoto za upungufu wa wafanyakazi, kuna watu wanaokaimu, wanahitaji kuongezewa bajeti. Haya yote tumeyachukua na tunakwenda kuyafanyia kazi na taarifa ya Wizara itatoka na hoja za Waheshimiwa Wabunge zitajibiwa kikamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine muhimu ambalo limejitokeza ni hili la TASAC. TASAC kwa sababu ni Taasisi ya Uwakala ambayo ndiyo inayopitishiwa madini yanayokwenda nje ya nchi. Ni kweli taarifa ya Kamati imethibitisha kwamba watu wanapokuwa wametoa madini yao kule migodini wanakuwa wameshalipia kodi nyingi nyingi inapofika kwenye port of exit iwe ni uwanja wa ndege, bandarini basi unakuta wanalazimika tena kulipia kodi. Hili nalo tumelichukua na tutakwenda kulifanyia kazi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Madini
NAIBU WAZIRI MADINI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kutumia dakika zangu tano kuchangia kwa kifupi kuhusu hoja yetu ambayo imepokelewa na kujadiliwa na Bunge lako Tukufu.

Mhehimiwa Spika, kabla sijasema mambo mawili, matatu kwa hizi dakika tano, niruhusu kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kunipa nafasi hii ya kuwa Naibu Waziri wa Madini. Leo ni mara yangu ya kwanza kusimama kuchangia kwenye hoja ya bajeti yetu kwa mwaka huu 2022/ 2023 na nikiwa chini ya Waziri wangu mahiri Dkt. Biteko, niseme tu kwamba kazi tuliyopewa na Mama Samia tunaisimamia usiku na mchana kwa uadilifu mkubwa na kwa umahiri mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikushukuru pia wewe Mheshimiwa Spika pamoja na Naibu wako kwa ushirikiano mnaotupa na niwapongeze kwa sababu na ninyi mmeingia kwenye nafasi hizi hivi karibuni, lakini mnavyotuongoza tutafika salama. Mungu azidi kuwaongoza katika kutuendesha katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo yaliyosemwa katika mjadala wa bajeti yetu ni mambo ya msingi ambayo kwanza Kamati yetu ya Nishati na Madini imeyafunika kwa asilimia kubwa kupitia kwenye taarifa yake na nipende tu kusema kwamba haya yote yaliyosemwa na Kamati na sisi tumekuwa na desturi ya kusikiliza ushauri wao na kufanyia kazi kila aina ya ushauri na mwongozo wanaotupatia kwa kuchambua kila hoja na kuifanyia kazi. Haya yote tumeyapokea na kwa kumsaidia waziri tunakwenda kuyafanyia kazi na baadhi ya mambo yameshaanza kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, kwa maoni ya Waheshimiwa Wabunge katika maeneo mbalimbali ya ushauri waliotupa pia tumeyapokea na kuna eneo moja mahsusi ambalo nilipenda kuligusia zaidi nimwachie Waziri wangu atahitimisha yale mengine, ni eneo la wachimbaji wadogo. Ni kweli wachimbaji wadogo ndiyo kundi kubwa ambalo likiwezeshwa watakwenda kuinyanyua sekta ya madini ili iweze kuleta tija zaidi ya hapa tulipokwishafikia.

Mheshimiwa Spika, katika kutambua hilo sisi tumechukua juhudi za ziada kama Wizara na tutaendelea kuzifanyia kazi ya kuhakikisha kwamba tunaziwezesha hizi taasisi zetu zilizo chini ya Wizara hasa GST na STAMICO kwa kuwapa vifaa na kuendelea kuwaongezea rasilimaliwatu ili wafanye utafiti wa kina katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu yanapopatikana madini. Katika kufanya hivyo wataweza kubainisha maeneo mahususi yanayofaa kupewa wachimbaji wadogo, kwa sababu moja ya malalamiko ambayo yanajitokeza hapa ni kwamba mitaji inapotea wanawekeza katika maeneo ambayo ni ya kubahatisha.

Mheshimiwa Spika, sisi katika kutambua hilo STAMICO sasa hivi wao wameagiza mitambo mipya ambayo inakwenda kusaidia kwa bei punguzo, kuwasaidia wachimbaji wadogo kubaini madini yanayopatikana katika maeneo ambao wanapendelea kuchimba kwa aina ya madini ili waweze pia kupata dhamana katika mabenki yetu ambapo tumeshapata benki zaidi ya nne ambazo zimekubali kutoa mikopo ama ya fedha ama ya vifaa kwa wachimbaji wadogo; mabenki hayo ni NBC, KBC na CRDB. Hawa wote wameshasaini maridhiano na Wizara kupitia taasisi ya STAMICO kwamba wako tayari kutoa mikopo. Wachimbaji wadogo wanapoungana na kuunda vikundi vya uchimbaji wao wako tayari wakizingatia vigezo vya kuhakikishiwa na kudhaminiwa na Wizara kwamba wanayo maeneo yenye mashapu ya dhahabu au maeneo yenye madini ya vito, wapo tayari kuwakopesha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baadhi ya wachangiaji wanasema kwamba masharti ni magumu. Masharti siyo magumu ni suala tu la kufuata utaratibu, ni suala la tukufuata vigezo vya kawaida kabisa ambayo wakivifuata kimoja baada ya kingine na sisi tukiwa tumewapa taarifa za viashiria vya uwepo wa madini katika eneo husika watakwenda kupata hiyo mikopo.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu naona muda ni mfupi sana nimalizie pia kwa hili suala Local Content na CSR.

Miongozo ya Wizara imewekwa bayana inadhihirisha kabisa kila mwekezaji anatakiwa aje na mpango wake wa CSR aje na mpango wake wa Local Content kwamba katika aina ya uchimbaji wanaofanya vifaa gani vinapatikana nchini na ataweka katika orodha ya database ambayo inaandaliwa na Wizara ataweka yaani ata- float yale mahitaji yote ambayo yeye anahitaji katika uchimbaji wake na watu wa ndani ndiyo wanaopewa kipaumbele na wale wengine yale yasiyopatikana nchini ndiyo yanayokwenda kuagizwa nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, CSR ni mwongozo ambao namshukuru Mheshimiwa Salome amelitolea ufafanuzi mzuri, ndivyo ilivyo, ni wao wenyewe ndiyo wanapambana kule katika halmashauri zao kwa sababu hawazingatii…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa mchango wako.

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya eneo la Pori la Akiba la Selous kuwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hoja hii ya hili Azimio lililoko mezani. Kwanza ni- declare interest kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati na moja ya mambo ambayo tumeyachekecha katika kupitia na kutolea maoni Azimio hili ni uhalisia wa eneo ambalo limependekezwa limeguliwe na sehemu fulani ibakie kuwa Hifadhi ya Taifa na sehemu nyingine ibakie kama Pori la Akiba.

Mheshimiwa Spika, katika uchambuzi wetu kwenye Kamati ambayo maoni yetu nayaunga mkono asilimia 100 pamoja na wazo la Mheshimiwa Rais la kupanua wigo wa maeneo yaliyohifadhiwa nchini na kuweka sehemu ya Selous kuwa mojawapo, tumeona kwamba kuna faida mara mbili endapo eneo hili litachukuliwa katika ujumla wake na kuhifadhiwa kama mamlaka sawa na ile ya Ngorongoro. Kwa maana hiyo sasa tutakuwa na mamlaka mbili ya maeneo yaliyohifadhiwa yenye matumizi ya aina mbalimbali badala ya kuwa matumizi ya aina moja tu kwa maana ya tofauti ya National Park na Conservation Area ni kwamba kwenye National Park ni exclusive use ya matumizi ya kupiga picha tu utalii wa picha, lakini kwenye conservation area kuna matumizi mseto ndiyo maana kwa sababu eneo hili lilikuwa ni eneo la akiba la uwindaji, tutakapokuwa tumekubaliana kwamba sasa na yenyewe liwe mamlaka kama Ngorongoro, tutakuwa na hiyo fursa ya kuwekeza kwenye utalii wa picha katika yale maeneo ambayo utalii wa picha unawezekana hasa eneo la Kaskazini maana nimeangalia katika kumbukumbu zilizopo hili pori linaweza likatengwa katika maeneo manne.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la Kaskazini ambalo limepakana na Hifadhi ya Mikumi ni eneo safi kabisa kwa utalii wa picha na eneo la Mashariki na eneo la Kusini na eneo la Magharibi haya ni mapori ambayo hata leo tukisema yote iwe National Parks itatuchukua miaka mingi sana kuyaendeleza, kuwekea miundombinu, kuna milima kuna misitu kuna maeneo oevu na ningefikiri kwamba tunapochukua kama ni eneo la hifadhi kama la Ngorongoro tunakuwa tumepata faida ya kuwa na maeneo ya utalii wa picha na yale matumizi mengine ya uwindaji wa kitalii ambayo yatafanya yale mapato yawe maradufu.

Mheshimiwa Spika, tutapata mapato kutokana na utalii wa picha katika eneo ambalo lina hadhi ya kama National Park na tunapata matumizi ya ule uwindaji wa kitalii ambao pia utatuletea manufaa makubwa.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo katika Kamati tuliona kwamba mapendekezo ya Mheshimiwa Rais ambayo tunayaunga mkono asilimia 100, yalitamka Nyerere National Park, tukasema tusipoteze jina la Mwalimu wetu kwa sababu Mwalimu ni cheo ambacho mtu hata ukipandishwa hadhi ukawa Rais bado utaendelea kuitwa Mwalimu na ndiyo maana Mwalimu anaitwa Mwalimu milele.

Kwa hiyo, ibakie kwamba Mwalimu Nyerere Conservation Area kama ndiyo moja ya majina ambayo tunapendekeza kama Kamati nami naunga mkono, pia lisimamiwe na TAWA.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu unaweza ukajiuliza hapo ulipo kwamba Ngorongoro ndiyo waje wasimamie? Jibu ni hapana TAWA tayari walikuwa wanalisimamia kama pori la akiba nasi katika maoni yetu na maoni yangu binafsi naona kwamba TAWA nao wapewe fursa ya kusimamia eneo la hifadhi inayofanana na Ngorongoro, wakachukue somo kule Ngorongoro wamefanikiwaje na wawekewe kabisa bajeti ya kutosha kwa sababu lile pori ni kubwa waweze kuli-manage likiwa na sehemu mbili. Sehemu ambayo ina utalii wa picha, linalofanana kabisa na Mbuga yoyote ya Taifa na eneo lingine lililobaki ambalo litaendelea na yale matumizi ambayo yalikuwa yameshabainishwa.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nilikuwa najiuliza na naomba hili nitoe kama maoni binafsi kwamba huku sasa tunaelekea kuwa na taasisi mbalimbali za uhifadhi hapa nchini, tunayo TAWA, tunayo Misitu, tuna TANAPA, na sasa pia tuna Ngorongoro, kwanini tusifikirie tuunganishe hivi vyombo vyote tukawa na chombo kimoja? Kwa mfano Kenya, wao wanayo ‘Kenya Wildlife Service’, Uganda wanayo ‘Uganda Wildlife Service’ nasi labda tuje na pendekezo nilikuwa najisemesha mwenyewe hapa kwa kufikiria nikasema kwanini tusiwe na Tanzania Wildlife and Nature Conservation Authority ikachukua hizi Taasisi zote pamoja zikaunganishwa tukawa na mamlaka moja inayosimamia uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yake katika Taifa letu la Tanzania.

Mheshimiwa Spika, tukija na huo model basi tutakuwa tunaya-manage maeneo yote bila kuwa na utengano na kuwa na moja ambayo inajiona kwamba ni dhaifu, nyingine ni bora kuliko nyingine na kwa njia hiyo tutakuwa tumehifadhi rasilimali yetu ya Tanzania katika upeo na mtizamo mpana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema kwamba maono ya Mheshimiwa Rais na hekima yake tumepokea kwa furaha kabisa na tunampongeza kwa kuwa na maono ya kuhifadhi Selous kama National Park na tunamuongezea maoni yetu kwamba iwe ni mamlaka ambayo inasimamiwa kwa ujumla wake bila kugawanywa na isimamiwe na taasisi moja ambayo ni TAWA.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana naomba kuwasilisha na naunga Azimio mkono asilimia 100. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye hoja hii ya Wizara ya Mifugo. Nitangulize pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Waziri wa Mifugo, ndugu yangu Mheshimiwa Luhaga Mpina, Naibu wake Mheshimiwa Abdallah Ulega, Makatibu Wakuu, ndugu yangu Profesa Elisante Ole-Gabriel na Dkt. Rashid Adam kwa kazi kubwa wanayofanya kama Wizara katika kuleta mapinduzi ya sekta ya mifugo ambayo kwa miaka mingi imesahauliwa na kuwekwa pembeni kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa mtoto mdogo wakati nilipokuwa nasikia jinsi Wizara ya Mifugo inavyobebwa na Serikali ya awamu ya kwanza. Wakati ule na nimepitia nyaraka zilizopo, kulikuwa na Sheria inayoitwa The Ranch Development and Management Act, ya mwaka 1964.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyakati hizo nyanda za malisho zilipewa hadhi yake, ziliundwa Commissions, zikagawanya Kanda, zikaanzishwa na kuhamasishwa Jumuiya za Kifugaji na Ranch za Ufugaji, ndiyo wakati ule pia hata katika ukanda mkubwa wa Masai Steppe iliyokuwa Wilaya ya Maasai, ambayo leo ina Wilaya karibu sita ndani yake ikiwemo Longido, Monduli, Simanjiro, Ngorongoro, kukawa kuna Masai Ranch. Ile taasisi ilikuwa imewezesha, ina mitambo ya kuchimba mabwawa, ina magari, inatoa tiba ya chanjo, dips za kuongesha na kwa kweli hata wafugaji wa wakati ule walipoambiwa walipe kodi ya kichwa cha ng’ombe hawakulalamika maana yake wanajua Serikali inawatunzia mifugo na walilipa kwa furaha, kulikuwa na upungufu wa kitu kimoja tu, masoko, lakini Serikali haikujali wanauza wapi ili mradi wanahudumiwa ili uchumi wao uweze kuimarika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipoangalia nyaraka zilizofuatia, kuna hii Sera ya Mifugo ya Mwaka 2006, halafu ikaja na Sheria ya Nyanda za Malisho ya Mwaka 2010. Hizi zote zinasisitiza kabisa na kuweka mkazo kwamba, ili mifugo iwanufaishe wafugaji na kuliletea Taifa mapato makubwa, ni lazima mifugo wapewe maeneo ya malisho, maji, tiba, masoko, sambamba na kuimarisha miundombinu ya barabara na viwanda vya kuchakata nyama na mazao ya mifugo. Hivi vitu vyote vimekuwa ombwe kubwa katika kukuza na kuimarisha sekta ya mifugo, lakini katika hotuba hii, iliyoandaliwa kwa makini na mambo ambayo Waziri amebainisha kwamba anakwenda kufanya, imenijaza matumaini na naamini kwamba akiyasimamia tutaona mapinduzi katika sekta hii ya mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba Waziri basi azingatie katika suala la malisho, hata yale maeneo ambayo hayana migogoro kama Longido. Sisi tuna maeneo lukuki ya malisho lakini yana uhaba mkubwa wa maji; na ninakushukuru kwa sababu kwenye ziara yako ya juzi ulipopita ulitujaza matumaini ukatambua mabwawa yaliyovunjika, mabwawa yaliyojaa udongo na ukasema kwamba utatusaidia kukarabati, yatawekwa kipaumbele katika bajeti hii, sambamba na kutujengea yale mabwawa nane yaliyobomoka ukijua na kutilia maanani kwamba sisi wananchi tumetengeza kwa nguvu zetu kupitia wadau na halmashauri yenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikutajie tu baadhi ya nyanda za malisho ili ujue ni kwa jinsi gani Longido ina maeneo ambayo yakiboreshwa na yakawekezwa tuna maeneo ya kutunza mifugo yatakayokuwa na tija kubwa; na sisi tumeimarisha mifugo kweli kweli kwa ajili ya hivi viwanda ambavyo pia vitajengwa na Longido pia ikiwa ni mnufaikaji wa kiwanda kimoja kitakachochinja ng’ombe 500 kwa siku na mbuzi 2,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna nyanda za malisho, sisi tunaita Ngaron, nikutajie tu baadhi. Kuna Loorboro, Oldenja, Engasurai, Naambala, Leleki, Ildonyo-dapashi, Loomunyi, Ngurmausi, Lookinyoyo, Loosikitok, Olesulenge, Kitang’a- engutak, Idonyo-oonyokioo, Ang’ata-eopir, Endonyo- nanyokie, Loolwaa, Ndashat, Orkiloriti, Orpelela, Lekuruki, Kelembusi, Endonyo-emali, Endarakwa, Kitenden, Ndiakakati, Endapitipit, Kesertet, Emesera na Molonjoni. Hizo zote ni nyanda ziko wazi ni maeneo mahususi yanayopata majani kwa haraka, mvua hata wiki moja ikinyesha lakini mara nyingi wakati ule bado hali ya tabianchi haijabadilika ni moto tu na mchwa ndiyo anakula yale majani kwa sababu hakuna maji katika nyanda hizo. Mheshimiwa Waziri tupatie kipaumbele kuweka mabwawa, kuweka visima virefu, mifugo watashamili, mbuzi, ng’ombe, kondoo na hivi viwanda havitatindikiwa malighafi vikapokuwa vimekamiliaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la mwisho ni kero. Kwa kweli kwa miaka yote hii Tanzania haijawa na soko la uhakika la mifugo na kwa miaka yote hii hatujaona nguvu ya Serikali katika kutusaidia kutunza hii mifugo. Kwa hiyo hii operesheni iliyoanzishwa inayoitwa Zagamba ambayo imezagaa kule kwetu Longido imewaumiza wafugaji na wachuuzi wa mifugo kutoka sehemu mbalimbali ya Tanzania waliokuwa wanatumia mpaka huu wa Kenya kupeleka mifugo Kenya kwenye soko lenye tija. Kwa sababu licha ya kwamba walikuwa wanasimamia Sheria lakini pia kwa kanuni ulizoweka. Kwamba akipatikana mtu anayekwenda kuvusha mifugo au akituhumiwa tu anapigwa faini 500,000, hata kama alikuwa anapeleka mbuzi wawili maskini ya Mungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwingine bado mifugo haijalipiwa kwenye masoko; nadhani zile tozo zinazojulikana; unakuta yule mtu anawekewa na faini. Kwa mfano kuna watu walikamatwa walikuwa ni watatu wenye ng’ombe kila mtu 500,000, mbuzi 30,000 kwa sababu sasa faini ng’ombe 50,000 halafu bado akifika kule mpakani wanatozwa kodi zingine za kupeleka ng’ombe nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi wamefilisika kwa sababu ya operesheni, rushwa pia imetumika na kuna pia msimamizi wa kikosi huko amekuwa na unyama wa hali ya juu. Mimi siwezi kumtaja kwa jina lakini ile operesheni Mheshimiwa Naibu Waziri alipokuja tulikaa tukasema kama wafugaji hatukushirikishwa katika kuweka hizi taratibu. Kama tungelishirikishwa tungeulizwa mnaenda kupata faida kiasi gani mkipeleka mifugo Kenya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakasema kama tungelitozwa hata hizo kodi, kwa mfano kodi ya kupeleka ng’ombe Kenya ni 30,000 ya kupeleka mbuzi ni 7,500, ukiweka na kodi za halmashauri inafika 9,000 na sasa hivi ukiwaambia wafugaji wanawenda kupata faida kiasi gani hawapati. Wakaililia kabisa Serikali wakasema ng’ombe awe 15, 000, mbuzi awe 4,500, wao wenyewe wapewe kazi ya kusimia operesheni ya wanaotaka kutosha mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanatoroshwa kwa sababu hawapati faida tena wakilipa hizo tozo; na mbaya zaidi ni hizo faini ambazo zina wafilisi wengi. Mheshimiwa Waziri nakuomba, kwa sababu hizo ziko ndani ya kanuni, ukiacha Sheria ambayo naomba pia Bunge hili tubadilishe, tuweke kodi zinazoendana zipunguzwe mpaka pale Serikari itakapokuwa imetuwekea masoko ya uhakika na viwanda ndipo sasa wafugaji wetu waweze kuwekewa faini kubwa wakitaka ng’ombe Kenya kwa sababu hawa sababu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamwomba Mheshimiwa Waziri abadilishe hizo kanuni zake. Haiwezekani mtu anayekamatwa akipeleka mbuzi watatu alipe 500,000 halafu mtakuwa mmemfilisi hata hao mbuzi wenyewe hawafiki 300,000 wakiwauza laki moja moja…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri usipofanya hilo mimi niko tayari kushika shilingi kwa sababu kwa kweli tuna kero kubwa ya watu ambao wamefilisika kwa sababu ya kanuni ulizotunga ambazo zimekuwa kandamizi na za kuumiza wafugaji wetu wanaotafuta riziki kwa sababu hapa nchini kwetu bado hatuna masoko ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DKT. STEPHEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia hii hoja muhimu ya Wizara yetu ya Maliasili na Utalii ambayo na mimi ni mjumbe wa kamati yake ya kudumu. Kwa hiyo mambo mengi ambayo ningependa kuyasemea bahati nzuri yapo katika ripoti ya makini tuliyoandaa kama kamati. Kwa sababu nimepewa dakika 5 sina muda wa kuyapitia hayo ila nina maswali machache ambayo nitamuomba Waziri na kweli azingatie ayatolee ufafanuzi baadaye atakapokuja kuhitimisha hoja yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kwanza ni kwenye haya maeneo ya jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori ambayo tunaita WMAs na nitatumia mfano wa WMA ya Jimbo langu ya Enduimet. Naomba Mheshimiwa Waziri utakapokuja kuhitimisha hoja yako baadaye unipatie ufafanuzi kuhusu hili suala la kucheleweshwa kwa mgao wa fedha za WMA zinazotokana na upigaji picha (photographic safaris) na hizi za uwindaji. Maana kwenye mfumo zinapokelewa, na tulitegemea kila mwezi baada ya watalii kupita, wanapewa mgao wao, baada ya msimu wa uwindaji kufanyika wanapewa hela yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, uhalisia ni kwamba haiji kwa wakati na ukweli ni kwamba hii inaathiri sana shughuli za uhifadhi kuwalipa ma-game scouts na kufanya shughuli nyingine za kulinda rasilimali lakini pia inachelewesha miradi ambayo vijiji vilivyotenga maeneo yao yahifadhiwe yalishabuni na walikuwa wanategemea hayo mapato ili waweze kujiletea maendeleo waone manufaa ya eneo walilolitenga.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo Mheshimiwa Waziri nitakuomba utoe ufafanuzi baadaye ni kuhusu utaratibu usiwafurahisha wanajamii wa WMA, labda zote lakini mimi naseme ya Enduimet ambayo ndiyo ya pekee tuliyonayo ambayo imeshasajiliwa ya uwindaji. Hawa jamii ya WMA wanao watu wao waliondaliwa tayari wamefunzwa, wapo village game scouts wanajua kusimamia, kukagua na kusaini vibali; lakini uhalisia ni kwamba wanapokuja wale viongozi wa idara ya wanyamapori wanawaleta wawindaji wanawa-bypass, hawawashirikishi, na wanasahau kwamba hawa ni watu waliajiriwa na jamii yenyewe waliopewa mamlaka kamili na ambao wanaaminika, wanalalamika kwamba kulikoni mamlaka yao yanaporwa wakiangalia mbona hawashirikishwi. Mheshimiwa Waziri utakapokuja baadaye naomba utolee ufanunuzi hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo linahitaji ufafanuzi maana nimejikita kwenye WMA kama eneo nyeti, ni hili la hii Jumuiya ya Enduimet ambayo imetokea sintofahamu baada ya eneo lao la uwindaji lenye hadhi ya grade A, grade namba I kushushwa hadi kuwa grade namba II bila kuwashirikisha wanajumuiya na kusababisha kupoteza mapato yanayotokana na uwindaji katika eneo la grade A kwa asilimia 50. Jamii imeshikwa na taharuki wanashangaa kwa nini hawajashirikishwa, pengine kuna vigezo vya msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri utakapokuja hapa hebu uwaambie wananchi wa Enduiment kulikoni maana wamejipanga kuja kukuona ofisini lakini waliposikia leo nitachangia hapa, wakaomba nilisemee mbele ya Bunge zima ijulikane kwa sababu wao walishaingia mkataba na muwekezaji kwamba wamemsainisha grade A lakini wameshalipwa kwa mara ya kwanza malipo ya grade II ambayo ni nusu ya malipo ya grade A.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo nilipenda kulisemea kwa haraka haraka kwa sababu dakika zangu zinaisha, ni oparesheni za kudhibiti wawindaji haramu. Mimi naunga mkono asilimia 100 kudhibiti wawindaji haramu kwa sababu kizazi hiki na vijavyo vitategemea rasilimali hii ya wanyamapori. Lakini kuna utaratibu unaotumika ambao unawasababishia watu na raia wasio na hatia kutiwa hatiani na kuumia karibu yote magerezani.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninavyoongea, nina barua hata hapa ya mmoja lakini sitaweza kusoma kwa sababu ya muda, wapiga kura wangu waliopo mahabusu wananiandikia. Kuna mmoja hapa sitaki kumtaja hata jina namhifadhi, lakini amewekwa mahabusu takriban miaka miwili sasa, tangu mwaka 2017 na kosa alilolifanya niliamini kwamba vyombo vilivyopo vinavyobaini watuhumiwa vina uwezo wa kuwadadisi, kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria, kuwahukumu na kuwafunga wasio na hatia na kuwaachia wasio na hatia. Kuna watu wanatumika kuwarubuni watu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kiruswa, kengele imegonga, lakini naona una barua ya huyo mtu; nadhani unaweza kuwaona watu wa Serikali, utawaona wao na orodha yako yote wewe wakabidhi ili sasa uweze kuwafuatilia, kwa sababu hata ukitaja hapa na wao watahitaji muda wa kuifuatilia.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa niwezeuwa wa kwanza kuchangia alasiri hii kwenye hoja hii yetu muhimu ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mheshimiwa Spika, mimi ni mjumbe wa kamati ya Wizara hii, ninakiri na kuungana na wezangu wote wanaowapongeza watendaji wakuu wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya. Mheshimiwa William Lukuvi, Mheshimiwa Angelina Mabula, Waheshimiwa Katibu Mkuu, Doroth Mwanyika na Naibu Mathias Kagundugulu, kazi mnayoifanya pamoja na watendaji wengine wote wa idara mbalimbali, tukiwa nyuma yenu ni kazi iliyotukuka, nawapongeza sana. (Makofi)

Pamoja na hayo kazi yenu ni kubwa, haijafika hata nusu, bado mna kazi kubwa sana mbele yetu na nifananishe kazi mnayoifanya na uhalisia kwamba ninyi ni Wizara ya Ardhi au sisi ni Wizara ya Ardhi; na ardhi ni kitu cha kipekee sana katika masha ya mwanadamu na uumbaji. Kwa wale wanaosoma Biblia, mnaweza mkarejea katika kitabu cha Mwanzo kwanza Mungu alioiumba hii dunia, akaweka vitu vyote na mwishoni akamweka mwanadamu alimpa wajibu wa kuitunza, akamweka katika Bustani ya Edeni aitunze.

Mheshimiwa Spika, na baada ya watu kuongezeka, tukatawanyika duniani kote; na sasa nasema mwenyewe siyo kwenye Msahafu tena; tulijikuta kwamba kila sehemu ya dunia ni sehemu ya hiyo bustani na sisi Watanzania tukajikuta tuko Tanzania ndiyo bustani yetu ya edeni ambayo tuna wajibu wa kuitunza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika muda mufupi ambao nimetumikia kwenye kamati ya Wizara hii na nikiwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nimeweza kutembea maeneo mbalimbali nikashuhudia jinsi ambavyo watanzania tumejisahau katika suala zima la kutunza hii bustani yetu ya edeni, nchi yetu ya Tanzania. Mipaka yake imeingilia kuanzia mpaka wa Uganda, Rwanda, Burundi, Kenya, kila moja ina mgogoro kwa sababu imeingiliwa, na ni kwa sababu watanzania sijui tulifikiri kwamba ardhi haina ukomo, tukaachia mpaka majirani zetu wakaingilia mpaka kwenye mipaka yetu.

Mheshimiwa Spika, mimi naiomba Serikali, kwa sababu sasa tumezinduka na tumeoa Sera nzuri ya Ardhi tuliyonayo, ielekeze nguvu ya kipekee katika kuiwezesha Wizara hii kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi ya nchi yetu, ipewe nguvu sana inayopewa sekta ya ukuzaji wa viwanda, uchumi wa kati. Namuomba Mheshimiwa Rais aibebe Wizara hii, aifanye moja ya Wizara mahsusi ya kushughulikiwa ili tuweze kuipima hii ardhi yetu na tuondokana na hii migogoro ambayo itazidi kuongezeka tusipochukua jukumu. Mipaka inagombaniwa katika ngazi za vijiji, kata, tarafa, wilaya, kati ya mkoa na mkoa na sasa hata katika ngazi ya nchi na nchi.

Mheshimiwa Spika, nafikiri tukiendelea kuiona Tanzania iliyojaa migogoro isiyowahikuisha ya ardhi.

Nashukuru sana kazi nzuri aliyofanya Mheshimiwa Rais ya kuteua Wizara za kushughulika na migogoro ya ardhi. Nimeona umeshika ile dossier ya Mheshimiwa Waziri, likitabu ambalo umesema ni mwarobaini wa hizo kero zetu. Ninakwenda kuamini kwamba itakwenda kutumalizia kero ya migogoro tuliyonayo ya muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano sisi Longido kule wasiwasi kuna migogoro ya miaka 20, kijiji na kijiji tu, kata na kata, Matale na Gelai Lumbwa. Mipaka yetu na Mwonduli upande wa Engaruka, mipaka yetu na Arumeru upande wa Oldonyo Sambu na Engikaret, mipaka yetu na NARCO Ranch na kila sehemu. Hii basi ifanyike sera; ambayo hata katika bajeti hii mimi ningeomba Wizara na Serikali kwa ujumla tengeni mafungu muwape Halmashauri na ofisi za ma-DC ili hii migogoro ya ngazi ya wilaya waimalize wao wenyewe na muwape deadline. Wakati mwingine wanakwama kwa sababu zinahitaji resources kwenda kuhakiki, kupima na kushirikisha pande zote.

Mheshimiwa Spika, naomba hilo lizingatiwe ili tuondokane na hii kero ya migogoro ya ndani, na tukiwa kuendelea kurasimisha makazi yale ambayo yalishavamiwa zamani tulipokuwa hatujijui nayo iweze kuendelea. Tumejiachia mpaka mabonde yasiyofaa kuishi watu wakaishi, milima isiyofaa kuishi watu wakaishi na ndiyo maana leo tuna sera ya urasimishaji.

Mheshimiwa Spika, naomba pia nielekeze kauli mbiu yangu katika kuishauri Serikali. Ukienda kule katika mwisho wa Wilaya ya Longido inapopakana na Rombo, kuna kamwanya ka nchi kali mwisho wa mpaka wa Tanzania na Kenya pale na Rombo kuna watu, nina orodha yao hapa, watu 196 bao waliorodhesha mwaka 2016 ambao wameishi hapo miaka nenda miaka rudi, wamezaliana, hawana pa kwenda. Zoezi la kuhakiki mipaka lilipopita wakaonekana hawastahili kuwa pale, wameiandikia Serikali barua kuomba watafutiwe mahali pa kwenda kuishi. Walikuwa 196 mwaka 2016, sasa hivi wameendelea kuongezeka na ninaamini watakuwa zaidi ya 200. Wengine wamezaliwa palepale, hawajuwi pa kwenda, hawana ardhi, wanaishi kwenye strip ya no man’s land. Wanakodisha mashamba ya kulima Kenya na wakati mwingine idara ya misitu upande wa Mlima Kilimanjaro wanapovuna misitu, ndiyo wanakwenda kulima pale. Wananchi wale hawana ardhi na hivyo wanaililia Serikali kwamba watafutiwe mahali pa kwenda kuishi.

Mheshimiwa Spika, vilevile nipende tu kuiasa Serikali, kwamba tunapokwenda kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi ya nchi yetu tuzingatie suala la kuweka benki ya ardhi; kila kijiji iwekwe benki ya ardhi kwa ajili ya matumizi ya baadaye ya vizazi vijavyo na maendeleo yatakayozidi kujitokeza. Sambamba na hilo, kwa sababu naona kama tunasubiri mpaka mazingira ya mahali paive, sijui idadi ya watu ifikie watu wangapi, ndipo tunapoingia kufanya mipango miji; tuanze kupanga miji yetu mpaka ile inayotarajiwa baadaye, maeneo ya wazi yasiyo na migogoro yapimwe, Serikali iwe na kazi moja tu ya kumuonyesha kila mtu sehemu iliyopimwa anapokuwa tayari kuhitaji eneo la kujiendeleza na kujenga makazi yake.

Mheshimiwa Spika, kwa ajili hiyo basi niangalize kwamba sisi wafugaji wa Wilaya ya Longido, tulishabainisha mpaka nyanda zetu za malisho, zinafika 27 kwa sasa hivi. Tunaomba mkono wa Serikali katika kutusaidia kupima, kurasimisha, tuweze kusimamia kama maeneo ya malisho na benki yetu ya ardhi ya vizazi vijavyo; na kwa ajili hiyo wakati huo tutakuwa tunaingezea Serikali mapato maana najua kila ardhi iliyopimwa, tunalipia kodi. Tuko tayari, tunakata ku-secure ardhi yetu na Watanzania wote wanahimiza waweke benki ya ardhi, maeneo ya malisho na kilimo na makazi ya watu na tufuate sera hiyo hiyo.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa muda huu mfupi ulionipa, mawazo yangu ni hayo pamoja na kuungana na maoni yetu ya Kamati ambayo tumeyaandika na kubainisha na yamewasilishwa leo asubuhi. Naunga mkono hoja asilimia 100. (Makofi)
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa hii nafasi ili na mimi niungane na Wabunge wenzangu katika kuchangia hii hotuba madhubuti, imara iliyojaa kila aina ya maelezo sahihi ya dira ya taifa letu kwa miaka mitano ijayo. Lakini nikiri pia kwamba baada ya kuangalia hotuba zote mbili kuna kitu kimoja ambacho Wabunge wengi hawajakiongelea mimi kimenigusa sana. Ni kwamba Rais wetu katika kupanga vipaumbele ametanguliza katika hotuba zote haja ya kuendelea kulinda na kusimamia tunu za Taifa ambazo ni amani, umoja, mshikamano pamoja na kuimarisha Muungano wetu na Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, mimi hivi vitu hasa amani imenigusa sana kwa sababu ni rahisi sana watu kuchukuwa for granted kitu ambacho wanacho kizuri bila kujuwa dhamani. Uki-imagine nchi ambazo zina vita katika dunia hii, nchi ambazo hazina, amani, umoja, mshikamano halafu sisi Watanzania tangu Uhuru tume-enjoy hivyo vitu na Rais alivyoji- commit kwamba moja ya kipaumbele chake namba moja ni kuendeleza amani ya nchi hii na umoja na mshikamano mimi nawiwa kusema kwamba tumpigie Rais makofi kwa sababu amelinda kwa dhati hayo mambo yanayohusu umoja wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia kwa sababu ametoa dira ya vipaumbele mbalimbali na muda huu wa dakika tano hautoshi kupitia vyote acha nichukue ya sekta inagusa roho ya wapiga kura yangu sekta ya mifugo. Napenda kumpongeza Rais kwa sababu ameelekeza kabisa na ameona umuhimu wa sekta hii ya mifugo kwa uchumi wa nchi yetu na ndiyo maana amekusudia kuongeza hekta zinazopatikana kwa ajili ya ufugaji kutoka milioni 2.8 mpaka zifike hekta milioni sita.

Mheshimiwa Spika, hivyo kwa kweli kwa jamii ya wafugaji wa nchi hii na uhakika ni faraja kubwa sana na niombe kuishauri Serikali basi kwa sababu Rais ameshaonesha dira kwamba tunahitaji kukuza sekta ya mifugo kama moja ya vyanzo vikuu vya kuongeza mapato ya nchi hii na kutuelekeza kwenye uchumi wa kati, ningeomba sera zingine za Serikali kama za uhifadhi kwa mfano basi waangalie vizuri hili suala kwa maana Rais ameshaonesha nia ya kuongeza maeneo ya malisho.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa masikitiko kuna maeneo mengine ambayo Wizara zingine niki-refer Wizara ya Maliasili wao wako katika harakati ya kupunguza maeneo ya malisho ili waongeze maeneo ya uhifadhi na wakati kiutamaduni au sijui kiasilia mifugo na wanyamapori vinarandana. Wilaya kama Wilaya yangu ya Longido ambayo asilimia 95 ni eneo la ufugaji na ni eneo pia la wanyamapori, tangu kuanzishwa kwa dunia imekuwa hivyo na ndiyo maana walioanzisha game controlled areas walianzisha tu wakijuwa kwamba ni maeneo ya wafugaji, lakini kulikuwa na proposal ya kutaka kumegua lile eneo la Longido asilimia isiyopungua 30 kwa sababu ni vijiji 14 kuvifanya viwe ni game reserve.

Mheshimiwa Spika, sasa mimi nikafikiri kwamba hiyo itakuwa inaenda kinyume na azma ya Rais ya kuongeza maeneo ya malisho, maana ukishatengeneza game reserve maana yake mifugo hawana nafasi na bahati mbaya sana katika eneo kama lile la Longido yale maeneo ambayo game reserve ingetengenezwa ndiyo yale maeneo ya kimbilio ya wafugaji wakati wa kiangazi, milima kama ya Gelai, Ketumbeine, milima ile ya … ambayo inatokeza mpaka upande wa Namanga na maeneo ya Lake Natron. Kwa hiyo, ningefikiri hiyo dhana ya game controlled pamoja na sheria iliyopo ambayo napendekeza pia ifanyiwe marekebisho ili mifugo na wanyamapori pale ambapo matumizi mseto yanaendelezeka yanaendelee kuachwa hivyo hivyo maana sasa hivi game controlled areas kwa sheria iliyopo ndiyo watu wasiishi ndani lakini zimekuja tu sheria zimeweka wakati watu mule na maeneo ya wafugaji tu, hakuna shughuli nyingine na mimi naomba kwamba hii azma ya Rais ya kupanua maeneo ya malisho ya mifugo iendelee kuungwa mkono asilimia mia moja kuhakikisha kwamba Wizara zingine haziingilii Wizara nyingine katika kuhakikisha kwamba maeneo haya yapo, yanahifadhiwa maana yanahifadhiwa kwa ajili ya mifugo na siyo kwa matumizi mengine.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hiyo nigusie eneo la kilimo, kwa kweli linahitaji nalo tuangalie namna ya kuondokana na kilimo duni cha jembe la mkono twende kwenye kilimo cha kisasa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Dkt. Kiruswa.

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi hii naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ili niweze kuchangia kwenye huu Mpango wetu wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano pamoja na Mpango wa mwaka wa fedha unaokuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilijipanga kuchangia katika maeneo yaliyotamkwa na kuelezewa kwa kina kwenye Mpango katika sekta za kilimo, mifugo, maji na madini, lakini kwa kutambua ufinyu wa muda nitaomba nichangie maeneo mengine kwa maandishi ila nijikite katika hoja inayohusu sekta ya mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba Mpango umeweka bayana mikakati sahihi na safi kabisa ya kuijenga sekta ya mifugo kwa kuhakikisha kwamba maeneo ya malisho yanaongezwa, upatikanaji wa maji, upatikanaji wa madawa ya tiba na chanjo na maendeleo mengine ya miundombinu ya mifugo, lakini kuna changamoto nyingine moja kubwa ambayo bado tunakabiliwa nayo kama Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ni kwenye upande wa masoko; hali halisi ilivyo sasa hivi kwa wafanyabiashara wa mifugo katika nchi yetu ni kwamba hakuna masoko yenye tija ya ndani wala nje. Naomba nichukue mfano na naipongeza sana Serikali yetu kwa kutengeneza mazingira safi ya wawekezaji kwenye sekta ya bidhaa za mifugo kuja kuwekeza nchini na azma kubwa iliyojitokeza ya ujenzi wa viwanda mbalimbali vya mazao ya mifugo nichukue mfano wa kiwanda kikubwa kilichojengwa katika Wilaya yangu ya Longido Kiwanda cha Elia Foods Oversees Limited. Kiwanda kile kimejengwa kwa gharama kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda kile kimejengwa kwa gharama kubwa, kina uwezo wa kuchinja mpaka ng’ombe 500 kwa siku na mbuzi pamoja na kondoo 4,000 kwa siku. Baada ya mwekezaji kumaliza kujenga kiwanda kile na akaanza uzalishaji mwezi wa 11 akakutana na changamoto kubwa ambayo hata sisi kama wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo tumeona kwamba itakuwa ni kikwazo kikubwa kwa ufanisi wa viwanda vinavyojengwa katika sekta ya mifugo katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna utitiri wa kodi ambazo bahati nzuri Mheshimiwa Kingu alishatolea ufafanuzi juzi akatoa ulinganifu mzuri kabisa wa jinsi Tanzania tunavyofanya vibaya kwa kuwekeza tozo mbalimbali katika viwanda vyetu kiasi cha kufanya vile viwanda ili viweze kuwa endelevu. Kuna zaidi ya tozo 11 lakini ukiangalia madhara anayopata mwekezaji ya kutoona namna nyingine ya kutengeneza faida, anayahamishia kwa muuzaji ambaye sasa ni mfanyabiashara wa mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika hiki kiwanda cha mfano tu ambacho nimekitaja cha Longido, mwekezaji huyu amepanga bei ya kununua mbuzi Sh.6,500 kwa kilo na wafugaji ambao wamekuwa wakitegemea soko la nchi ya jirani hawaoni tija kwa sababu hata kama wakilipia ushuru wa Serikali wakifisha mbuzi zao Kenya wanauza kilo kwa Sh.8,500. Kwa hiyo, kwa ajili ya kodi zilizoko maana nilishafanya kikao kati ya wafanyabiashara wa mifugo wa wilaya yangu na Tanzania kwa ujumla wanaotumia soko la Namanga na mwekezaji tukatafuta chimbuko la shida iko wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji akatupa changamoto zake akasema kuna hizi regulatory fees ndiyo zinafanya yeye asiweze ku-compete na masoko ya nchi jirani na asiweze kutoa bei yenye tija. Yeye kila akichinja na kuweka consignment moja akifisha bandarini asilimia moja ya thamani ya ile consignment inachukuliwa na Meat Board. Mwekezaji huyu anapopeleka bidhaa yake sasa kuuza sokoni, Wizara inachukua Sh.50 kwa kila mbuzi na kondoo kwa kilo na Sh.100 kwa ng’ombe. Mfanyabishara huyuhuyu mwenye kiwanda anachajiwa na BAKWATA kwa ajili ya kukagua nyama shilingi milioni 2 kwa mwaka ambayo sasa hivi wanabishania nao wawe wanalipwa kwa kila kilo ya nyama wanayosafirisha kwenda kuuza kwenye masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, akajikuta kwamba hakuna namna anaweza akaongeza bei kwenye bidhaa na yeye akaweza kukiendesha kiwanda kile. Kwa sababu hiyo basi tukajikuta ile adhima iliyotamkwa kwenye Mpango ya kuendesha uchumi wa viwanda na shindani hatuko anywhere karibu na kufanikiwa kwa kuwa washindani katika biashara ya bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na viwanda vya hapa nchini kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda kuishauri Serikali ili tutoke na wafugaji wetu wasiwe na sababu ya kupeleka mifugo Kenya tukapoteza bidhaa mbalimbali inayotokana na mifugo, ni vizuri sasa kodi hizi ama zifutwe au zifanyiwe marekebisho ili ziweze kutoa tija kwa wafugaji wetu na mwekezaji naye aone kwamba kiwanda chake kinamuletea faida na aweze kukiendeleza.

Pia kama kuna uwezekano kuwe na tax holiday ya mpaka mwaka mmoja maana huyu mwekezaji alisema kwamba mkinipunguzia kodi nitatoa bei shindanishi na ya Kenya ili ateke soko wale wafugaji wote wanaopeleka mifugo Kenya walete bidhaa pale pale Longido wauze kwenye kiwanda chetu na ajira ziongeze na faida zingine tunazopata kwa sababu kiwanda kile kinatumia kila kitu mfano kwato, pembe, mifupa na mbolea zinatoka finished product ambazo zinaendelea kuingia sokoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwekezaji huyu akasema kwamba kama Serikali ikimuondolea kodi yuko tayari kushindana. Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie suala la kupunguza kodi katika bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na viwanda vyetu vya ndani ili tuweze kujenga huo uchumi na biashara shindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa yale mengine ambayo nilitamani kuchangia, nitawasilisha kwa maandishi na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye

hii hoja ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Nianze kwa kumpongeza Waziri na timu yake yote, Naibu Waziri na Watendaji katika Wizara hii kwa kazi nzuri na muhimu wanayoifanya.

Mheshimiwa Spika, Wizara hii ya Mambo ya Ndani ya Nchi ni nyeti na ukiangalia maslahi ya watenda kazi katika Wizara hii yanasikitisha na kutia huruma. Kwa mfano, katika Wilaya yangu ya Longido sisi ni wilaya ambayo karibu ina miaka 25 sasa tangu ianzishwe lakini hakuna Kituo cha Polisi cha Wilaya, kuna kituo kidogo kilichojengwa tangu enzi ya ukoloni na nyumba za maaskari pale ukiziangilia zinatia huruma. Naomba katika bajeti hii Waziri hebu aangalie kule Longido atatusaidiaje.

Mheshimiwa Spika, lakini pia ukienda Kwamwanga kuna Kituo cha Polisi ambacho zamani kilikuwa barabarani, barabara ya lami ikafika pale kutoka Rombo, wananchi wakajiongeza wakajenga kituo kingine pembezoni, imebakia finishing tu. Waziri aliyepita nilishamuomba angetuchangia tu kama milioni 20 tunafanya finishing nzuri.

Mheshimiwa Spika, pia maaskari pale wanalala nje, ukiona nyumba wanazolala zinatia huruma. Naomba sana pia katika bajeti hii hebu muangalie hali ya usalama katika Wilaya ya Longido inayopakana na nchi ya jirani yenye kilometa zaidi ya 350.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tulishahamisha wananchi kwa sababu alisema kwenye hotuba yake kwamba na sisi tunaweza tukachangia ili tupate vituo vingine zaidi vya polisi, tumefanya hivyo. Kule Mndala tumeanzisha kituo, Serikali haiweki hata mkono. Tarafa ya Kitumbene yenye vijiji zaidi ya 19 tulishapendekeza tuwe na kituo lakini hamna juhudi yoyote ya Serikali katika kuhakikisha kwamba tuna vituo hivyo vya polisi.

Mheshimiwa Spika, naomba suala hili la miundombinu ya polisi kuwafanya wafanye kazi katika mazingira rafiki na makazi yao lizingatiwe sana nchi nzima lakini katika Wilaya yangu ya Longido basi nilisemee maana ndiyo nyumbani kwamba kwa kweli hali ni mbaya, hata ya magari ni mbaya. Kila wakati mimi kama Mbunge ndiyo nachangia tairi, matengenezo ya gari na unakuta kuna magari mengine yamekaa juu ya mawe kwa sababu hamna bajeti inayotolewa kutoka Wizarani kusaidia uendeshaji wa operesheni za polisi katika wilaya yangu. Hata Zimamoto lakini ni jina tu, hawana hata gari ya kukimbia kwenye matukio yakitokea kwenda kushuhudia licha ya gari ya kuzima moto unapotokea mahali popote. Naomba haya masuala yazingatiwe.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu dakika ni chache naomba nijielekeze kwenye suala la wafungwa na mahabusu. Tunashida kubwa sana na sijui Wizara ya Mambo ya Ndani itatusaidiaje. Kuna kikosi kinachodhibiti ujangili wa nyara za Serikali kinachofanya kazi katika wilaya hizi zenye wanyamapori, kuna vitendo viovu vinafanyika. Naomba tu nimjulishe Waziri na ajue namna ya kufanya kwa sababu ndiyo wanaolinda mali na raia wa nchi yetu kwamba watuhumiwa wanapokamatwa kuna mazingira ya rushwa na kuna mahabusu wanaokaa magerezani mpaka miaka mitano hawahukumiwi.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe mfano, kuna mtu anaitwa Taraiya Paulo alikamatwa kwa sababu tu kwenye simu yake alikutwa amefanya mawaliano na mtu ambaye anafanya biashara ya ujangili lakini alikuwa anamfuata kwa deni lake la mbuzi aliyomuuzia. Akakaa mahabusu miaka mitatu, ametoka juzi tu ndiyo anaeleza kwamba yeye alikamatwa kwa sababu simu yake imekutwa na mawasiliano ya mtuhumiwa.

Mheshimiwa Spika, kuna mwingine anaitwa Luka Olokwen, yeye alikamatwa na mguu wa swala ambaye ameliwa na chui akabakiza, kwa sababu sisi jamii ya kifugaji hatuli nyama pori akabeba ule mguu ampelekee mbwa wake nyumbani, akakamatwa akaambiwa usipotoa milioni tano hatukuachii. Familia ikauza tena walewale ng’ombe aliokuwa anachunga akalipiwa milioni tano baada ya mwaka mmoja amekuja amechukuliwa juzi amefungwa miaka 20, kwa sababu tu alikutwa na mguu wa swala aliyeliwa na mnyama pori. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mwingine anaitwa Daniel Saitot, yeye alikamatwa tangu tarehe 1/9/2018. Kesi yake haijasikilizwa mpaka leo, alikutwa sijui ana ngozi ya chui. Hiyo ni kusema kwamba hebu Wizara hii ya Mambo ya Ndani iangalie mazingira ya kusaidia raia wa Tanzania wasio na hatia wanaopewa kesi mbalimbali za uhujumu uchumi. Sambamba na hilo, mimi naomba hizi kesi za uhujumu uchumi ziwekwe kwa category, ziwekwe ambazo zinadhaminika watu wadhaminiwe waendelee na kesi zao wakiwa majumbani ili kupunguza msongamano katika magereza yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, kuna hili suala la uhamiaji, kipengele kinachotukera kidogo sisi watu wa mipakani ni ile hati ya kusafiria ya Single Entry Permit. Mtu ana shida kubwa labda anamuuguza mgonjwa yupo Nairobi anahitaji kwenda kila wiki anadaiwa akate hiyo permit kila wiki. Naomba passport za muda mrefu zitengenezwe na kuwa zinapatikana pale pale mpakani kuwaondolea raia wetu adha ya kulazimika kununua passport mpya ya muda wa dharura kila wakati wanapohitaji kusafiri.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. DKT STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye hoja iliyoko mezani ya Wizara yetu ya Maji. Nitangulize kwanza pongezi zangu za dhati kwa Wizara hii kwa jinsi ambavyo wamedhihirisha kwa matendo uchapakazi wao katika kupunguza kero ya maji nchini. Kwa kweli wamefanyakazi kubwa na nielekeze pongezi za kipekee kwa Waziri wetu Mheshimiwa Aweso pamoja na timu yake yote, Naibu Waziri na watendaji wa Wizara hii kwa sababu kwa kweli tumeona matokeo ya kazi yao. Hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, kwa sababu ya uhaba wa muda, naomba nijielekeze moja kwa moja kwenye baadhi ya dondoo nilizotoa katika hotuba yake. Ukiangalia kiambatisho namba moja miradi 355 ya maji vijijini ambayo imekamilika katika mwaka wa fedha unaoisha ambayo iko katika ukurasa wa 91, Wilaya ya Longido nayo imepata miradi miwili ambayo imekamilishwa. Moja uko Kijiji cha Noondoto na mwingine ulikuwa Kijiji cha Magadini. Naomba kwa hii miradi niishauri Serikali kwamba inapomaliza miradi na kuiachia jamii ambayo haijaelimishwa, Kamati za Maji hazijui wajibu wake hii miradi itarudi tu kuharibika na tutakuwa tumefanya kazi bure.

Mheshimiwa Spika, kwa huu wa Noondoto naomba niishauri Serikali kwamba kuna upungufu. Ule mradi wa kutoa maji juu ya Mlima Kitumbeine kupeleka mpaka Kitongoji cha Ordoko ulihitajika uwe pia na tenki la maji, hakuna tenki la maji pale. Kwa hiyo naomba huo upungufu ukazingatiwe. Naomba nishukuru kwa kule Magadini maji yaliyotoka juu ya Mlima Gilayi yamefika mpaka Shule ya Msingi ya Magadini na inaonekana kwamba ule mradi umekamilika kwa asilimia 100, naishukuru sana Serikali.

Mheshimiwa Spika, nilipoangalia kiambatisho namba tatu kwenye miradi 67 ya maji iliyokamilika katika maeneo ya mijini, ukurasa wa 130 nikaona kwamba Longido nayo ni miongoni mwa wilaya ambazo zimeguswa na hiyo miradi na ule mradi wa maji safi na salama kutoka Mlima Kilimanjaro uliogharimu zaidi ya bilioni 15, uliweza kusambazwa katika mji wetu wa Longido. Upungufu kidogo upo kwa sababu bado pia kuna nyumba nyingi hazijasambaziwa maji.

Mheshimiwa Spika, naomba pia katika kuendelea kusambaza maji majumbani hilo lizingatiwe maana pale Longido sasa hivi tukitaka kuoga baada ya breakfast wakati wa lunch na wakati wa chakula cha jioni tunayo maji ya kutosha, tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano na Awamu ya Sita kwa sababu Longido ni moja ya Wilaya kame nchini, lakini sasa shida hiyo imekuwa ya historia katika maeneo ya Makao Makuu ya Wilaya.

Mheshimiwa Spika, nipende pia kuishukuru Serikali kwa sababu mradi ule, yale maji ni mengi pale Longido, umeanza kuelekezwa Mji wa Mpakani Namanga na utakapofika Namanga tutakuwa tumetimiza ahadi ya Hayati ya Dkt. John Joseph Magufuli aliyoitoa alipokuja kuzindua ule mpaka wa pamoja, akawaahidi watu wa Namanga kwamba maji ya Kilimanjaro lazima yafike mpaka Namanga. Napenda pia kutoa hizo shukrani.

Mheshimiwa Spika, nikiangalia katika kiambatisho namba 4a, kipo katika ukurasa wa 132, maji vijijini mradi ambao utatekelezwa katika huu mwaka wa fedha tunaojadili bajeti yake. Naishukuru sana Serikali kwa sababu kuna miradi saba imeorodheshwa inaenda kugusa Wilaya yangu ya Longido na ambayo itatupatia jumla ya shilingi bilioni 2.08 ambayo naamini tukiisimamia vizuri Vijiji hivi vya Leremeta, Olmolog, Orkejuloongishu, Lopolosek, Ermanie na Vijiji vingine kama Kiseriani, Meirungoi, Elangadabash, Lerangwa na Olmolog watakwenda kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunashukuru sana kwa sababu hivi vijiji vina shida kubwa ya maji, lakini niiombe pia Serikali iangalie katika yale maeneo ambayo nilitaja jana kwenye swali langu…

SPIKA: Watu wangu wa Hansard sijui watapata hivi vijiji sawasawa? Endelea Mheshimiwa Kiruswa (Kicheko).

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, katika Kijiji cha Olmolog, Kijiji cha Orkejuloongishu, Lopolosek, Ermanie Kiseriani, Meirungoi, Elangadabash, Lerangwa na vijiji vingine vingi kuna zaidi ya shilingi bilioni mbili ambayo Serikali ya Awamu hii ya Sita imetutengea ili tukajaribu kupunguza kero ya maji.

Mheshimiwa Spika, naomba pia niishauri Serikali na kuiomba kwamba yale maji ya bomba la Mto Simba basi yakasambazwe nayo sasa yale matawi yafike Vijiji vya Tingatinga, Ngereiyani, Sinya na Elerai ambapo ndiyo kijiji cha kwanza ambacho kimeguswa, hasa na eneo la Motooni. Ila kuna vijiji vimesahaulika na vina shida kubwa ya maji sana. Namwomba Mheshimiwa azingatie Wosiwosi ndiyo mwisho wa Wilaya tunapopakana na Kenya karibu na Ziwa Natron. Maji ya chini yana chumvi, lakini kuna maji mengi na mazuri kule Ngaresero upande wa Ngorongoro, naomba mradi wa maji safi kwenda Wosiwosi uangaliwe na maji hayo yapitie Magadini yaongezee yale yaliyotoka Mlima Kilai tuweze kupata maji toshelevu na masafi kwa wananchi wa mwisho wa wilaya yangu upande wa magharibi. Pia niiombe Serikali na kuishauri kwamba katika maeneo ambayo maji yameletwa na mita zinafungwa bei ya maji ya mifugo iangaliwe tofauti na unit zinazochajiwa kwa matumizi ya binadamu.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo kwa sababu muda umeisha naomba maintenance, mashine zinafungwa za ma-borehole, maji yanaharibika ndani ya mwaka mmoja, mashine inakufa watu hawajui, wekeni wataalamu wa maji.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja iliyoko mezani ya Wizara yetu ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na watendaji wote wa Wizara hii mpya ambayo kazi wanayoifanya ni muhimu na ni kazi nyeti sana katika kuweka Taifa letu kwenye chart ya hiki kitu kinachoitwa mawasiliano ya kisasa ICT. Kwa sababu mawasiliano ndiyo nyenzo muhimu ya kufanyia biashara ya kipesa, ya kielimu, sasa hivi kuna haja kubwa sana ya kudhibiti masuala ya mawasiliano katika maeneo yaliyo pembezoni mwa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatolea mfano Jimbo langu la Longido ambalo lina takriban kilomita 350 za mpaka ambao tunashiriki na nchi ya Jirani ya Kenya kuanzia Rombo mpaka kule tunapopakana na wilaya ya Ngorongoro karibu na Ziwa Natron. Katika ukanda huo wananchi wake wanategemea kwa asilimia zaidi ya 90 mitandao ya nchi Jirani kupata mawasiliano. Hili siyo jambo jema kwa sababu hata wanapotaka kutoa taarifa kwa viongozi wao kama sisi tukiwa Bungeni inabidi afanye roaming atumie safaricom ndiyo aweze kupiga simu hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisiwe mtovu wa shukrani kwa sababu katika kipindi kifupi ambacho Wizara hii imeundwa, kulikuwa na kata kama mbili ambazo hazikuwa kabisa na namna ya kupata mawasiliano ya Lang’atadapash na Nondoto, lakini mnara wa Vodacom umeshaanza kufanya kazi unasubiri tu kuzinduliwa rasmi na hivyo sasa hivi katika katika kata hizo mbili wananchi wamefarijika japo zile kata ni kubwa, kwa hiyo mnara mmoja hautoshi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimeona katika ukurasa wa 47, kiambatisho Na.3 kwamba Waziri ametaja kwenye hotuba yake kata ambazo zimeshapata huduma ya mawasiliano kufikia mwezi Aprili na kweli akatamka hiyo la Elang’ata Dapash na Noondoto ambayo Vodacom wameshatoa huduma lakini pia ametamka ya Engarenaibor akimaanisha mnara wa TTCL ulioko katika Kijiji cha Ngoswak kwamba umewashwa. Nipende kutoa taarifa kupitia Bunge hili kwamba huo mnara haujawashwa na wananchi wanasubiri kwa hamu sana mnara wa TTCL wa Kijiji cha Ngoswak ambao ulitegemewa kutoa huduma katika Vijiji vya Mairowa, Sinonik mpaka Kimwati utakapowashwa utakua umeondoa kero na kupunguza huo utegemezi wa minara ya nchi ya Jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Gelai Lumbwa pia hotuba ya Waziri inaonyesha kwamba mnara wa airtel unahudumia Kijiji cha Lumbwa na Alaililai ni kweli, lakini kuna kijiji kingine kinaitwa Ilchangitsapukin ambacho kinaenda mpaka Kenya na wao pia bado hawana kabisa mawasiliano katika Kata ya Gelai Lumbwa. Hivyo hivyo katika Kata ya Gelai Meirugoi kuna mnara wa TTCL ambao Waziri alionyesha kama unawasha mpaka Magadini lakini kweli Magadini hawana mtandao kabisa na ukitaka wapate mawasiliano bora uweke Ngaresero upande wa Ngorongoro mnara mkubwa ambao utasaidia upande wa Ngorongoro na upande wa Magadini kwa ukanda huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika kiambatisho Na.4 ukurasa wa 69, hotuba ya Waziri inatamka maeneo ambayo yanakwenda sasa kuwekewa minara ya mawasiliano. Kwenye Kata ya Engaranaibo, Kijiji cha Mairowa, Ngoswak na Sinonik TTCL watakwenda kuweka minara, tunaomba hiyo minara ipewe kipaumbele kwa sababu hiyo ni kata inayopakana na mpaka wa nchi jirani moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Engikaret kuna Kijiji cha Kiserian hiki kijiji kwa kweli ni kama kisiwa kwa barabara ni ngumu kufika, mitandao hakuna na umeme haujafika. Naomba pia hilo lipewe kipaumbele kwa sababu Waziri ameorodhesha lakini kuna maeneo zaidi ya 14 katika mpaka mzima ambayo bado hayana minara ya mawasiliano. Baadhi nimeshayasema Kijiji cha Magadini, Wosiwosi, Matale B, Matale A, Kitongoji cha Irngong’wen, Kimwati, Sinonik, Eworendeke, Kimokouwa, Leremeta, Elerai, Kitenden, Irkaswa na maeneo Lerang’wa hivi ni vijiji vyote vilivyoshikamana na mpaka na hakuna mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nipende kutoa angalizo kwamba kuna baadhi ya maeneo ambayo wameshapata minara kama Matale A, lakini mnara ule unawaka mchana tu, ikifika jioni maana unategemea solar, hivyo mawasiliano hukatika. Naomba sana kwa kampuni yoyote itakayoweka mnara, waweke backup generator pale ambapo umeme haujafika. Hali hiyo inajitokeza katika Kijiji cha Kamwanga inayopakana na Rombo na Kijiji cha Matale A, lakini mbaya Zaidi minara huko ni ya 2G.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa taarifa mzungumzaji anayeongea Mheshimiwa Kiruswa kwamba nadhani umefika wakati sasa Wizara hii kuangalia kwamba hatuwezi kuwa na minara sijui 300 nchi nzima, tufike wakati tuongee na makampuni kama kuna mnara mmoja kwenye eneo moja kama ni mnara wa airtel, basi makampuni yote ya-share kwenye mnara huo ili kuweka mtandao wa pamoja. Haiwezekani tukajenga minara mingi katika nchi nzima kwa sababu minara na yenyewe ni magonjwa kutokana na mionzi yake.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kiruswa taarifa umeikubali?

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa yake na sina ubishi kabisa kwamba ikiwezekana basi ikafanyika collaboration kati ya makampuni, minara ipunguzwe, lakini mawasiliano yawafikie wananchi wote ambao wanahitaji huduma ya mawasiliano ya simu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipengele kingine ni eneo la redio; vijiji hivi vya mpakani pia vina uhaba mkubwa wa kupata usikivu wa redio na television za nchini kwetu. Nishukuru Wizara kwa sababu wamejaribu kuweka booster za kuleta Redio Tanzania mpaka mpakani kule Namanga na Longido, lakini bado usikivu ni hafifu mno. Kwa hiyo, naomba katika mipango ya Mheshimiwa Waziri atambue tu kwamba bado usikivu wa TBC maeneo ya Namanga, Longido na vijiji vya pembezoni ni sawa na hakuna, kwa hiyo wafanye kitu ili tuweze kupata mawasiliano hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kwa sababu nimeshasemea hili la 2G kwamba ndiyo liko katika minara mingi na ningeomba sana iongezwe na wengine wengi wameshalisemea. Kuna hili suala la hii channel ya utalii inaitwa Safari Channel. Naona hii channel ina maudhui mazuri sana ya kuhamasisha biashara ya utalii kama ingeweza kununua hata segment ya dakika chake katika TV kubwa kubwa duniani, wakarusha zile clips.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua hii linaenda kugusa Wizara ya Utalii, lakini pia inaweza ikasaidia sekta hii ambayo inatakiwa isaidie katika kukuza utalii wa nchi yetu kwa kutafuta nafasi CNN, BBC na channel nyingine kubwa kubwa za Kimataifa kama hizo ili tuweze kutangaza utalii wa nchi yetu na kuongeza mapato ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, nashukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hii hoja ya Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuishukuru Wizara, kwa sababu katika kipindi cha mwaka wa fedha unaoisha, wameweza kutukarabatia bwawa moja kati ya mabwawa 27 ambayo ndiyo tegemo la Wanalongido katika Kata ya Kimokouwa. Ahsanteni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kwanza kuwapongeza kwa sababu najua kazi kubwa wanayoifanya na ugumu wa kazi hii, kwa sababu Wizara hii imeunganisha sekta mbili ambazo zote zinahitaji rasilimali kubwa sana katika kusimamia ili kuweza kufikia malengo ya kiuchumi kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kufanya ulinganifu kidogo wa bajeti iliyotengewa Wizara hii kwenye fedha za maendeleo. Nimeangalia bajeti ya mwaka huu unaoisha; mwaka jana wa fedha (2020/2021) ambao ndiyo unaisha mwezi wa Sita, fedha za maendeleo zilikuwa ni shilingi bilioni 23.4 na mgawanyo wake katika sekta zake mbili; Fungu 64 ambalo ni Uvuvi na Fungu 99 ambayo ni Mifugo ni kama ifuatavyo: mifugo walipewa shilingi bilioni 10.3 na uvuvi walipewa shilingi bilioni 13.05; na walijitahidi kufanya kazi walizozifanya na hizi ni fedha za maendeleo. Returns au maduhuli yaliyokusanywa katika hizo fedha walizowekeza mpaka mwezi huu wa Tano, mifugo wanakaribia kufikia shilingi milioni 40, nadhani wameshafika shilingi milioni 40 kufikia sasa, lakini uvuvi wako chini ya shilingi milioni 18. Sasa utaona kwamba ni kwa jinsi gani hizi sekta zinaweza zikazalisha lakini haziwekezewi mtaji wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu wa fedha bajeti ambayo Waziri amewasilisha leo hotuba yake hapa, jamii yote ya wafugaji Tanzania pamoja na mimi tuna masikitiko makubwa. Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu mwaka huu mmeongeza bajeti ya maendeleo kwa asilimia 80 kutoka shilingi bilioni 23 mpaka shilingi bilioni 116.01, lakini katika mgawanyo kwenye mafungu yake yote mawili, mmeipendelea Sekta ya Uvuvi mkawapa shilingi milioni 99 ambayo ni sawa na asilimia 76 ya fedha yote ya maendeleo mkiaibakizia Sekta ya Wafugaji ambayo nayo ndiyo uti wa mgogo wa watu wengi katika nchi hii, asilimia 14 tu ambayo ni shilingi bilioni 16.8. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni masikitiko makubwa sana kwa sababu katika ukusanyaji wa maduhuli, bado mmeiweka sekta hii kwamba mnatarajia iwape shilingi bilioni
50 na uvuvi iwape shilingi bilioni 33 na wakati huo huo mmeshaona kwamba hata katika fedha kidogo za mwaka unaoisha wa fedha sekta hii ya mifugo ndiyo iliyokuwa inaleta returns zaidi kuliko uvuvi. Sasa imenifanya niungane na mwenzangu Mheshimiwa Olelekaita leo asubuhi akisema, kama mnaona kwamba hii Sekta ya Uvuvi ndiyo ina umuhimu mkubwa, basi ni bora Sekta ya Mifugo ipewe Wizara yake ijisimamie yenyewe ili tuweze kutafuta rasilimali za kuiendesha kwa ufanisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimeangalia katika ilani ya CCM ya mwaka 2020 mpaka 2025 ambayo ndiyo iliyounda Serikali inayoongoza nchi hii wameshabainisha vipaumbele na kwa masikitiko makubwa sidhani kwa bilioni hizi bilioni 16 tunaweza tukafanikisha masuala ya ugani na utafiti masuala ya uzalishaji wa mifugo na kutafuta masoko ya maziwa na nyama biashara ya nyama biashara ya mifugo na mazao yake soko landani na la nje ukarabati wa miradi mbalimbali ya minada mambo ya kimkakati ya mpakani na mapitio ya ada na tozo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, hata wizara yenyewe waliweka malengo ambayo sijui watayatekelezaje na bilioni 16 kwenye hii sekta ya mifugo maana ndio ninayoisemea. Walisema kwamba tutasimamia kuimarisha afya ya mifugo ambayo ni mambo ya chanjo madawa majosho walisema watasimamia mambo ya vyakula vya mifugo na maji na wakati wilaya kame ndizo zenye wafugaji wengi kuliko wote nchi hii unakuta hawana vyanzo vingine wanategemea mabwawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Olelekaita yeye anahitaji mabwa 40 mimi nahitaji 27 wametengeneza moja tu na fedha sizioni hapa, lakini basi kwa masikitiko makubwa nipende tu kusema kwamba wizara imetuangusha katika kugawa hizi rasilimali na ninamuomba waziri atueleze ni utaratibu gani au ni kwa sababu gani ameamua kuwapatia uvuvu asilimia 75 ya fedha zote za maendeleo akawapatia wafugaji asilimia 15 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kwa sababu ya uhaba wa muda nilimsikia Mheshimiwa Spika, asubuhi hii akiongea kwamba NARCO imeferi kweli imeferi, lakini mimi ninaomba tu nishauri Serikali sisi kama kamati niseme kwamba naunga mkono hoja ya kamati yangu yote na kazi tuliyoifanya. Tulishapendekeza kwamba ifanyiwe review kwa ajili ya kujua ilianzishwa kwa nini, kwani ni imeferi na kama malengo yako bado yanahitajika wakati huu miongozo na kanuni zilizoianzisha zipitiwe kabla ya kufikia hatua ya kusema tuifutilie mbali maana yake nadhani ndio shamba darasa la kuzalishia mbegu bora za kuendeleza wafugaji wa nchi kwa hiyo naomba wapewe nafasi ya pili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la mwisho, napenda kuongelea huu mtafaruku ulioko wa migogoro ya ardhi kati ya wafugaji na wakulima na watumiaji wengi, katika jimbo langu la Longido sisi hatukuwahi kuwa migogoro na wakulima kwa sababu sisi ni wafugaji kwa asilimia 95 na maeneo ya hifadhi lakini pia hatujawahi kuwa na migogoro na hifadhi. Isipokuwa katika kipindi hiki kililchopo kuna pendekezo nadhani liko mezani halijaingia katika Bunge hili lakini limeshapita kwenye Baraza la Mawaziri la kutaka kumegua eneo la Wilaya ya Longido kuwa pori la akiba na ile ni ardhi prime land ya wafugaji ndio inaenda kuchukuliwa kuwa pori la akiba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati marais wote wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Joseph Magufuli na wa Awamu ya Sita mama yetu mpendwa Samia Suluhu Hassan wana tuahidi kwamba ardhi ya ufugaji inakwenda kuongezwa ifikie hekta milioni sita sasa inakuwaje leo kuna wizara inanyemelea tena nyanda zetu za malisho na kuzipunguza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Waziri wa Mifugo ebu angalia kutana na mwezako wa maliasili kwamba utaratibu huo wa kwenda kutwaa ardhi ya wafugaji ,ardhi ambayo imepimwa ni ya vijiji, na maeneo ambayo yametenga ili kuyafanya hifadhi iangaliwe upya kwa sababu inaenda kinyume na matarajio katika maeneo ya wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hii hoja ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Naomba nianze kwa kuipongeza Wizara kwa kazi muhimu ya kuhifadhi rasilimali yetu ya Taifa wanayoifanya, lakini specifically nimshukuru pacha wangu Waziri Dkt. Ndumbaro na Naibu wake Mary Masanja kwa kitu kizuri nilichojifunza kutoka kwao. Tangu waingie katika Wizara hii wameanzisha mtindo mzuri wa kusikiliza kero za wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa sababu Mheshimiwa Waziri alisikiliza kero ya wananchi na mwekezaji wa Green Miles akaja mpaka uwandani kushuhudia mwenyewe na matokeo yake yamewafariji wale wananchi. Sasa kilichobaki tu ni yule mwekezaji naye kwa sababu alimpa kibali cha kurudi katika lile eneo, akajipatanishe na wananchi maana yeye ndiye aliwakosea na ndiyo chanzo cha ule mgogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kulikuwa na changamoto kubwa ya eneo ambalo Wizara ya Maliasili katika awamu iliyopita ya Uongozi wa Awamu ya Tano, walilitwaa kabisa na kutaka kuligeuza kuwa pori la akiba katika Wilaya ya Longido. Eneo lile ni mahsusi la wafugaji wa Wilaya ya Longido, maeneo ya kuhemea wakati wa kiangazi la kupatia maji na majani, lakini Wizara ikaja na pendekezo bila kuwashirikisha wananchi la kutaka kugeuzwa kuwa pori la akiba. Ni eneo la Game Controlled Area ambalo limekuwepo tangu enzi ya ukoloni na wananchi waliendelea kufuga huku uwindaji ukiendelea bila bughudha, lakini baada ya Waziri kuingia na kupokea hicho kilio amewapa wananchi matumaini kwamba hilo jambo linahitaji kurejelewa na bahati nzuri au mbaya pia taarifa na kilio cha wananchi kimeshafika mpaka Ikulu, kimefika kwa Waziri Mkuu na kwake, lakini ile namna yake ya kusikiliza wananchi ni jambo la kupongeza sana. Nawapongeza sana Wizara ya Maliasili kwa hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nitoe ushauri sasa katika maeneo machache kulingana na hotuba waliyoitoa wenzetu ya bajeti na mambo ambayo yanastahili kufanyiwa marekebisho. Eneo la kwanza hizi kanuni za kifuta jasho na kifuta machozi zinahitaji kurejelewa, kiwango ni kidogo mno na muda wa kusubiri mpaka hata hicho kidogo kinachotolewa kitoke ni muda mrefu mpaka hata inakuwa haina maana tena. Naomba hilo suala lirejelewe na namwomba Waziri atakapokuja kutoa mrejesho hapa hebu atuambie kwamba ni utaratibu gani amejiwekea wa kuongeza kile kipato na kuharakisha ulipwaji wa wale watu ambao wameathiriwa na wanyamapori.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, Serikali iangalie uwezekano wa kupunguza tozo zinazotozwa Kampuni za utalii wa uwindaji. Hiyo tasnia imeshuka kabisa na ukiwasikiliza wawindaji wanasema ni kwa sababu ya tozo, VAT ilipokuwa introduced mwaka 2016, idadi ya watalii imeshuka kutoka 1,500 kwa mwaka mpaka wakafikia kwenye 500 tu kwa mwaka. Mbaya zaidi ulipoingizwa ule mtindo wa kuuza vitalu kwa njia ya mnada vitalu vingi vimekaa bila wawekezaji na mapato ya Serikali na ya wao wenyewe na ya jamii ambayo walikuwa wanaisaidia kupitia ule mfumo wa uwajibikaji kwa jamii pia yameshuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano katika taarifa ya wanaitwa TAHOA, Chama cha Wawindaji; wanasema kwamba katika minada mitatu ambayo imeshatangazwa tangu huo mfumo uanze na vitalu 60 vilivyowekwa mnadani ni 11 tu vimepata wawekezaji vile vingine vikabaki idle kwa sababu hakuna watu waliokuwa na interest navyo. Sasa naomba kuishauri Serikali kwamba wapange tu bei ambayo ni reasonable ili kila mtu anayetaka kitalu kwa sababu kina bei tayari iwekwe price tag kuondoa utata wowote wa rushwa na nini aweze kuingia na mapato yakapatikana badala ya kuvifanya vikose wawekezaji na vikose ulinzi na mazingira yetu yakazidi kuharibika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wa tatu kwenye mfumo wa marejesho ya mapato kwenye WMA’s, wakati corona ilipoingilia Mataifa na pia nchi yetu ikaathirika, mapato yote yanayokusanywa kwenye vyanzo vya hifadhi yakawa yanapelekwa Hazina. Utaratibu wa kurudisha zile fedha zije zisaidie uendeshaji wa WMA, kuwapa vijiji mgao wao, ulivurugika kabisa na WMA nyingi karibu zishindwe ku-operate kwa sababu mfumo ulikuwa haupo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia Waziri atueleze leo kwa sababu najua kilio cha wenye Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori za Jamii kwamba walikuwa wamekwama kabisa katika uendeshaji. Sasa Wizara imeweka mkakati gani wa kuwasaidia, mapato yaweze kurejeshwa na Hazina waweze kujiendesha na wananchi waendelee kunufaika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu wa nne, ni kuimarisha mahusiano baina ya wananchi na maeneo yaliyohifadhiwa. Kwa huu mtindo sasa hivi ulioko wa kwamba TANAPA wakiona eneo ambalo limeiva wanataka tu walinyakue, hautusaidii, inatakiwa washirikishe na watambue uhifadhi jumuishi, uhifadhi wa mseto maana ndiyo itakayotusaidia katika karne hii ya ongezeko la watu na haja ya maeneo mbalimbali kwa matumizi mbalimbali ya binadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niungane na wenzangu katika kuchangia hoja hii iliyopo mezani ya Azimio lililoletwa katika Bunge lako Tukufu la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu Afya ya Mimea, Afya ya Mifugo na Usalama wa Chakula.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kuzipongeza Wizara zote mbili ambazo zimetupa ushirikiano mkubwa katika kuchambua Azimio hili nikimaanisha Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Mifugo na Wizara nyingine ambazo wataalam wake walikuja tulipokuwa tunafanya uchambuzi wa Azimio hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wameshasema yote kuhusiana na faida za kuridhia Azimio hili, lakini pia nipende kusema kwamba kuna hasara tusiporidhia kwa sababu ni makubaliano ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Moja ya hasara ambayo tungepata tungeweza kutengwa, tungetengwa katika baadhi ya vipengele vya hii Itifaki kwamba kuna wakati tunataka kutetea maslahi ya mazao yetu haya, afya ya mimea, mifugo yetu, usalama wa chakula lakini wanaweza wakasema ninyi hamna haki ya kusema kwa sababu hamkuridhia hili Azimio. Hivyo ili twende pamoja kama tulivyokubali kuwa wanachama ni muhimu wote kama Bunge lako Tukufu turidhie leo Azimio hili ambalo tumeshalitafakari, tumeshalidadavua na tumejiridhisha kwamba kuna faida kubwa katika kuliunga mkono.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na kutoa wito kwamba turidhie Azimio hili, napenda tu kutoa maoni na ushauri kwa Serikali, kwa sababu tumegundua katika kuchambua utekelezaji wa Azimio kwamba kuna maeneo ambayo tuna upungufu mkubwa. Moja ya maeneo ambayo kuna upungufu mkubwa katika kusimamia afya na usafi wa mazao yanayohusika ikiwemo kilimo au mazao ya mimea na mifugo na usalama wa chakula ni kwenye hii sekta ya mifugo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna vitendea kazi vingi vimeshatengenezwa nikimaanisha instrument za kusimamia utekelezaji wa Azimio hili lakini pia bado tumegundua kwamba mifumo ya kusimamia na uwezo wa Taasisi za Serikali husika zina upungufu. Hivyo napenda kuisihi Serikali iwekeze kwa dhati katika kujengea uwezo hizo taasisi ili tusije tukasaini ili Azimio tukadhani tumeshafaidika maana yake tutapigika kweli kweli kwani wenzetu walisaini siku nyingi na ina maana wamejipanga. Kwa hiyo, nasi tunatakiwa tujipange, tuwe na sera, tuwe na sheria, tuwe na kanuni, ambazo zitatuongoza katika kuhakikisha kwamba tunafaidika ipasavyo tunapokuwa katika Itifaki hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende basi kujielekeza kwenye maoni na ushauri ambao ningependa niongezee pale ambapo Kamati imeishia kwa upande wa afya na usafi wa mifugo. Kwa kweli hii sekta ya mifugo ni moja ya sekta ambayo ukiachia kazi iliyoanza kufanywa na Serikali ya Awamu ya Tano na hii ya Sita ilikuwa ni kama imesahaulika. Ili basi tufaidike katika kuingia kwenye hii Itifaki ni vizuri na napendekeza kiundwe chombo mahsusi kama ilivyo katika Wizara ya Maliasili, wana chombo mahsusi, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa, tuanzishe Mamlaka ya Uendelezaji wa Miundombinu ya Mifugo Tanzania au kwa Kiingereza tungeweza kusema Tanzania Livestock Infrastructure Development Agency ambayo itakwenda kusimamia mambo mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, ingeweza kusimamia masuala ya masoko ya ndani ya nje maana hatuuzi bidhaa yetu ipasavyo katika masoko ya nje kwa sababu havikidhi viwango. Ingesimamia masuala ya usafirishaji, masuala ya minada kuelekea sehemu za kupakia na kupakua mifugo, ingesimamia machinjio, ingesimamia suala la ngozi kwa sababu kuna ngozi nyingi zinatumwa siku hizi hakuna masoko, ingesimamia masuala ya magonjwa, masuala ya chanjo ya mifugo, ingesimamia masuala mbalimbali pamoja na usimamiaji wa nyanda za malisho, ingekaa na kutengeneza kanuni za kutenga maeneo mahsusi kwa ajili ya wafugaji. Nyanda za mifugo zingeweza kupimwa zingeweza kuwekewa miundombinu ya maji zingeweza kabisa kuwa gazetted kama National Park zilivyokuwa gazetted na tukawa na maeneo ambayo tungeita kwa lugha ya kigeni disease free zone.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Wilaya yangu ya Longido asilimia 95 ni wafugaji, ni mapori yasiyofaa kwa kilimo, ni maeneo ya wafugaji ambayo yangeweza hata kuchukuliwa yakafanywa model ya maeneo mahsusi ya kufuga mifugo na kunenepesha kwa ajili ya soko la Afrika Mashariki na nchi za nje. Kwa bahati nzuri tuna kiwanda kikubwa kile ambacho wawekezaji wamejenga, moja ya viwanda vikubwa sana hapa nchini vya kuchakata bidhaa za mifugo, lakini mpaka sasa hivi kina-operate under capacity kwa sababu hatujajipanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii Itifaki itakapokuwa imeridhiwa na tukawa bado hatujaweza kuimarisha afya ya mifugo yetu tutaendelea kukosa masoko kwa sababu mifugo itakayopita ni ile ambayo imevuka vile viwango. Hii Itifaki ni ya viwango, the whole thing is about standards ya mazao ya mimea, mazao ya mifugo na usalama wa chakula chote tutakachokuwa tunazalisha Tanzania kitakuwa kinapitishwa kwenye hiyo mizania na tusipopita hakuna mahali tutakwenda kama Taifa hata baada ya kusaini Itifaki hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ningeshauri Taifa letu baada ya kuridhia hili Azimio, basi sasa tujifunge mikanda tufuatilie kwa makini dhana ya utekelezaji. Kila sekta, kila taasisi husika ikajengewe uwezo, tukawasomeshe wataalam wetu katika kila fani; mambo ya maabara, afya ya mimea, udongo, mambo haya ya magonjwa ya sumu kuvu yanayoshambulia mazao na kutukosesha soko na kuelimisha wananchi wetu jinsi ya kuzalisha, jinsi ya kuhakiki afya na kutafutia masoko ya ndani na ya nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache, napenda kusema naunga mkono hoja hii iliyo mezani na nalisihi Bunge lako Tukufu liridhie ili tuweze kusonga mbele. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye haya mapendekezo yaliyoletwa ya Mpango wa Serikali wa Miradi itakayotekelezwa mwaka unaokuwa wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naomba nitoe shukrani za pekee kwa niaba ya wananchi wa Longido, kwa ile ziara ya Rais aliyokuja Longido. Imeongeza hamasa kubwa sana, wananchi wamejenga imani kubwa na kiongozi wao na pia kauli alizoziacha pale zimeacha hamasa kubwa na kuwafanya wananchi wa Longido wajue kwamba Rais wao anawapenda, anawajali; na hasa alipokuja kuwakabidhi ile miradi miwili; mradi wa majisafi na salama kutoka Kilimanjaro shilingi bilioni 15 za Serikali zimeleta maji kwenye Tarafa ya Longido karibu yote inakwenda kufikiwa. Ukisikia naongea habari ya shida ya maji, ni kwa sababu wilaya ni kubwa na Tarafa tatu zilizosalia bado zina shida kubwa ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwenye kile Kiwanda cha Nyama, alipotambua kwamba kuna kero ya tozo, ameacha maagizo kwamba zifanyiwe kazi ili viwanda vyetu viweze kuzalisha kwa tija na wafugaji nao waweze kupata mapato mazuri. Namshukuru sana Rais, nampongeza na Waziri wa Fedha na timu yake yote kwa kazi nzuri waliyoileta mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujikita zaidi katika eneo moja tu katika mchango wangu; eneo la sekta ya mifugo. Kabla sijaingia katika hiyo hoja, naomba nitoe angalizo katika moja ya maeneo ya vipaumbele vya huu mpango kwenye miradi yetu ya kimkakati. Nimekuwa nikifuatilia huu Mkutano wa Mabadiliko ya Tabia Nchi unaoendelea kule Scotland, gazeti la The Times la Marekani nadhani kama siku mbili zilizopita, liliandika article iliyosema kwamba, kuna Mataifa 18 na baadhi ya Mabenki na Taasisi wanakwenda kutengeneza deal la kufanya mchakato wa kusitisha matumizi ya nishati inayotokana na makaa ya mawe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ikanifanya nifikirie kuhusu moja ya miradi yetu ya kimkakati hapa nchini ambao ni Mradi wa Mchuchuma na Liganga. Nikasema kwamba basi nitashauri katika kuratibu hii miradi ya kimkakati, basi tuangalie namna ya kuwekeza katika miradi ambayo itakuwa na uendelevu mkubwa na sina shida kama huu mradi wa makaa ya mawe utakuwa viable kwa muda gani, lakini ni vizuri kutathmini. Tusije tukawekeza fedha nyingi katika mradi ambao labda miaka mitatu au minne ijayo dunia itasema makaa ya mawe hayatakiwi tena kwa sababu yanachafua hali ya hewa ,ni moja ya polluter kubwa ambayo inayoleta shida ya mabadiliko ya tabia nchi kwa maana inatoa sumu nyingi inayoingia angani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikasema kwamba basi nishauri tu kwamba katika tu kwamba katika kupanga, mwangalie hilo suala kwa makini, tujue jinsi ya kuiendea hiyo miradi ya kimkakati kwa upande wa makaa ya mawe na ninafahamu pia pale kuna madini ya chuma. Kwa hiyo, pengine tunaweza kuongeza mtaji mkubwa katika kuvuna chuma badala ya kuhangaikia makaa ya mawe.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kiruswa pale nchi jirani Kenya, nadhani Lamu, hivi sasa wanajenga kiwanda kikubwa kitakachotumia Makaa ya Mawe ambacho kitazalisha karibu nusu ya umeme unaohitajika Kenya. Hivi sasa, they are doing it. Hata hivyo, point yako noted. Haya mambo ya dunia wanasema tu, lakini sisi tupo sahihi.

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Nilitoa tu concern ya kitu nilicho-observe kwamba isije ikatokea ikafika mahali…

MWENYEKITI: Wala, hiyo itawafuata wao, lakini sisi tusonge mbele.

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa hii Sekta ya Mifugo, pia nimeangalia kutokana na uzoefu ambao sasa tunao nikaona kwamba sekta ya mifugo haikui kwa kasi inayostahili na nikaona pengine kuna jambo ambalo lingeweza kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu Mpango uzingatie katika hilo ili na yenyewe iweze kunyanyuka ichangie katika uchumi wa Taifa kwa zaidi ya hii asilimia saba ambayo tunayo sasa hivi, iwepo na kilimo ni asilimia 26, nikasema basi ungeanzishwa Wakala wa Uendelezaji wa Miundombinu ya Mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala huu hautakuwa tofauti na Mawakala wengine ambao tayari tunao. Kwa mfano, tuna REA na mnajua mapinduzi ambayo wimeleta katika nchi yetu katika kusambaza umeme. Tuna Wakala mwingine wa TARURA, mnajua pia kwa kiasi gani imefungua barabara katika nchi yetu. Tunayo RUWASA, tunao umwagiliaji; wameleta mapinduzi makubwa katika sekta ambazo wamesimamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa na Wakala wa Mifugo ambayo itaenda kusimamima, kutengeneza mifuko kama ilivyo katika haya Mawakala mengine, mifuko ambayo itatusaidia sasa kunyanyua Sekta ya Mifugo na kusimamia miundombinu mingi. Naomba nikutajie baadhi ya miundombinu ambayo huu Wakala ungeweze kusimamia kama utaanzishwa. Kuna majosho ya kuogesha mifugo, kuna mengine yamekufa tangu zamani, kumbe wakala ukiwekwa in place itatusaidia sana. Kuna mabwawa na visima vya kunyweshea mifugo, tuna masoko ya mifugo ya awali, ya upili na ile masoko ya mipakani; kuna machinjio, kuna vituo vya kukusanyia maziwa, kuna miundombinu ya usafirishaji wa mifugo na bidhaa zake. Kama kwenye minada, utakuta minada mingi haina ramp ile ya kupakilia na kupakua mifugo. Nyingine, tunahitaji hata kwenda zaidi katika mazao yanayouzwa nje. Kwa hiyo, kuna code chain inayoangalia mazao ya mifugo kule bandarini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo mengine ambayo sasa hivi nchi ina-focus katika kuanzisha industrial packs. Tungekuwa pia na eneo la industrial packs kwa ajili ya mazao…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Hiyo ni kengele ya pili Mheshimiwa Kiruswa.

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi wakala huo uanzishwe, nami naungana na wenzangu katika kusema kwamba Sekta ya Uzalishaji Kilimo na Mifugo ipewe kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumpongeza Waziri kwa hotuba yake nzuri pamoja na Naibu wake, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara kwa kazi kubwa na nzuri wanazofanya kwa nia ya kukuza na kuendeleza sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, pili, napenda kuishukuru Serikali yetu sikivu na kibinafsi na kwa niaba ya wananchi wa Longido namshukuru Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Magufuli kwa maagizo yake ya kuwapelekea chakula wananchi wa Wilaya ya Longido waliokumbwa na uhaba wa chakula cha nafaka ya mahindi kufuatia ukame wa muda mrefu. Rais alitoa maagizo na Serikali kupitia Waziri wa Kilimo waliwatengea na kuwapeleka wananchi wa Longido mahindi ya bei nafuu ya Serikali jumla ya tani 10,000 ambayo yatawatosha hadi msimu ujao wa mvua.

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi na shukurani hizi, naomba sasa nijielekeze kwenye kuchangia hoja ya bajeti ya Wizara ya Kilimo iliyoko mezani mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, kwanza, kuhusu kilimo chenye tija; kwa kuwa bado kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yetu, iko haja ya Serikali kuwekeza katika masuala ya msingi ambayo yakizingatiwa, wakulima wa Tanzania ambao wengi ni wakulima wadogo wadogo wanaotumia zana duni kama majembe ya mkono na plau, zana ambazo kamwe hazitatoa na kutupeleka kwenye mapinduzi ya kilimo chenye tija. Ili tuondokene na kilimo duni, Serikali iongeze bajeti na kuwekeza kwa nguvu zote katika maeneo yafuatayo:-

(a) Kuhakikisha kila Kijiji kina Afisa Ugani;

(b) Kutoa ruzuku ama mikopo ya kuwezesha wakulima kupata na kutumia zana bora za kilimo kama vile power tillers na matrekta na hivyo kutokomeza kabisa matumizi ya majembe ya mkono na plau kama zana za msingi za kilimo; na

(c) Kusambaza pembejeo za kilimo (mbegu bora, mbolea na madawa bora) kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, pili, kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi; kwa kuwa mabadiliko ya tabianchi yamekuwa yakiathiri kwa kiwango kikubwa kilimo kinachotegemea mvua. Nashauri Serikali iongeze bajeti ya kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji. Tanzania tuna maeneo mengi yenye rutuba yanayofaa kwa kilimo isipokuwa changamoto ni vyanzo vya kudumu vya maji ya kuendeshea kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali kufanya usanifu wa kujenga mabwawa ya umwagiliaji na kuboresha skimu za umwagiliaji ili kukuza kilimo chenye tija katika nchi yetu. Hili liende sambamba na kufundisha wataalam wa kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, katika Kata yangu ya Tingatinga Wilayani Longido kuna maombi ya muda mrefu ya bwawa la umwagiliaji kwenye nyanda za chini katika eneo linapotawanyika mikondo ya Mto Simba unaotokea Mlima Kilimanjaro. Survey zilifanyika tunachoomba ni bajeti ya kujenga bwawa hilo.

Mheshimiwa Spika, vilevile naomba kushauri Serikali kuwekeza katika kufanya utafiti na usanifu wa skimu bora za umwagiliaji kwa kutumia maji ya Mto Ngarenanyuki ambayo hufaa sana kwa kilimo cha nyanya, vitunguu, viazi na mboga za aina mbalimbali. Matumizi yasiyo ya kitaalam ya maji ya mto huu kwa sasa yamesababisha maji kutowafikia wakazi wa Vijiji vya Mwendo wa chini hasa wa Kijiji cha Ngareyani kilichopo Wilaya ya Longido.

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali ijenge matanki makubwa ya maji ya umwagiliaji yapitishwe kwenye mabomba hadi kwenye mashamba badala ya mifereji inayotumiwa kwa sasa ambayo huchapusha maji toka mtoni bila kurudisha na kupelekea kukauka kwa mto na uharibifu wa mazingira wa nyanda za mto huu muhimu.

Mheshimiwa Spika, tatu, kuhusu uwekaji wa chakula cha akiba; pamoja na mpango mzuri ulioko tayari wa Serikali kuwa na maghala mikoani kwa ajili ya kuhifadhia chakula cha akiba, naomba niendelee kusisitiza kwa Serikali kuendelea kuona umuhimu wa kuwekeza zaidi katika kuhifadhi chakula kingi zaidi cha akiba (hasa nafaka) kwa ajili ya kukabiliana na uhaba unaoweza kutokea wakati wowote kutokana na kuongezeka kwa kasi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

Mheshimiwa Spika, kwa haya machache, namalizia kwa kutamka kuwa naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza kazi nzuri. Naomba nitangulize kauli ya kusema kuwa naunga mkono hoja na pia niseme kuwa kwa kuwa mimi ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Wizara hii, mengi ya masuala ambayo ningependa kusema nimechangia katika taarifa yetu ya Kamati. Hata hivyo, naomba Waziri anipe ufafanuzi katika maeneo yafuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMAs); naomba ufafanuzi kuhusu suala la kucheleweshwa kwa mgawo wa fedha za WMA (za photographic safari na uwindaji) toka Serikali, sambamba ni vifuta jasho na machozi. Uchelewashaji huu unaathiri shughuli za utaratibu za uhifadhi na miradi ya maendeleo ya vijiji vilivyotenga maeneo yao yahifadhiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ufafanuzi kuhusu utaratibu usiofurahisha jamii wa usimamizi wa shughuli za uwindaji ni kwa nini Game Scouts wa WMA ambao wamekidhi vigezo vya usimamizi, ukaguzi wa utiaji saini vibali vya wawindaji. Hawapewi fursa hiyo watendaji na Idara ya Wanyamapori? Kwa nini wao ndio wasimamie uwindaji ndani ya eneo la WMA wakati Game Scouts walioelimishwa na wanaoaminiwa na jamii wapo? Tena hawa Game Scouts pia wanatambulika na Mkaguzi wa Idara ya Wanyamapori.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jumuiya ya Wanyamapori Enduimet WMA inalalamikia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa sintofahamu ya kushusha daraja eneo lao la uwindaji toka grade one kuwa grade two bila kuwashirikisha wala kuwafahamisha vigezo walivyotumia kuamua kitalu chao cha uwindaji cha Engasurai kushushwa hadhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, athari za kushushwa hadhi kitalu hiki bila ridhaa ya wanajumuiya siyo tu kimewadhalilisha wenye jumuiya bali pia inawapunguzia mapato kwa zaidi ya 50%. Baya zadi ni kwamba Jumuiya ilishaingia mkataba na mwekezaji wa kitalu hiki kwa makubaliano ya kitalu cha daraja la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, adha wanayopata baadhi ya wananchi kutokana na utaratibu unaotumiwa na vikosi vya kudhibiti ujangili kubaini wawindaji haramu. Katika wilaya yangu ya Longido nina orodha ndefu ya watuhumiwa wa uwindaji haramu ambao wamewekwa mahabusu magereza ya Arusha kwa zaidi miaka miwili sasa bila kesi zao kusikilizwa kila mara ni kutajwa tu na kurejeshwa magereza kwa madai kuwa uchunguzi unaendelea. Miongoni mwao wapo wa vijana wa umri mdogo ambao wamerubuniwa, ni watu wenye visa nao. Naomba Mheshimiwa Waziri aunde tume maalum ya kupitia tuhuma za mahabusu wote waliokaa muda mrefu magereza kwa tuhuma za uwindaji haramu bila kesi zao kusikilizwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kanuni za shoroba na maeneo ya mapito ya wanyamapori; napongeza juhudi za Wizara za kutenga masharoba ya kuendeleza uhifadhi katika nchi yetu. Hata hivyo, napendekeza juhudi hizo zishirikishe jamii zinazoishi katika maeneo hayo kwa karibu. Itapenda zaidi wakifanya matumizi bora ya ardhi na kupewa maeneo hayo wayasimamie wao wenyewe kama WMA au misitu asilia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kubadili hadhi maeneo ya hifadhi; hii pia ni dhana yenye tija kwa uhifadhi wa mapori yetu isipokuwa nashauri yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria za Wizara zinazokinzana zirekebishwe kwanza mfano TAMISEMI, Maliasili, Ardhi na Madini. Eneo la Ziwa Natron libaki ni ardhi oevu inayohifadhiwa chini ya jumuiya pendekezwa ya lake Natron WMA.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haya machache, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. DKT. STEPHEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kuungana na Wabunge wenzangu waliopata fursa ya kuchangia hoja iliyoko mezani ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kuipongeza Serikali yetu ya Awamu ya Tano kwa kazi kubwa na nzuri iliyofanyika hadi sasa katika kuliendeleza Taifa letu kijamii na kiuchumi. Kwa hakika chini ya uongozi madhubuti wa Rais wetu mpendwa, Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake yote ikiweko Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara zilizoko chini yake imefanyika kazi iliyotukuka ya kuijenga nchi yetu na kila sekta ni shahidi wa miradi ya kimkakati iliyotekelezwa (afya, ardhi, elimu, habari, kilimo, maji, maliasili, mawasiliano, mifugo, uvuvi, nishati, ustawi wa jamii na kadhalika).

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizi, naomba nichangie hoja moja inayohusu suala la kazi na ajira.

Mheshimiwa Spika, tuna tatizo kubwa katika Halmashauri zetu za ukaimishaji wa watendaji wa nafasi mbalimbali za ajira kwa muda mrefu suala ambalo linadhoofisha utekelezaji wa majukumu na upitishaji maamuzi kwa kiwango kikubwa. Kwa mfano katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido karibu asilimia 50 ya Watendaji wa Vijiji ni watumishi wanaokaimu nafasi hizo tena wengi ni kwa miaka mingi hadi sasa.

Naiomba Serikali kuanzia bajeti hii ihakikishe kuwa nafasi za ajira zinawekewa ukomo wa kukaimu na Serikali itoe pesa za kuajiri na vibali vya kuajiri kwa wakati kwenye Halmashauri husika.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha mchango wangu wa maandishi kwenye Hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Hotuba ya Waziri Mkuu imeangazia kwenye ukurasa wa nane kuhusu hofu inayoendelea kutanda duniani kufuatia kuenea kwa homa kali ya mapafu inayoletwa na virusi vya Korona (COVID 19).

Mheshimiwa Spika, naomba kuishauri Serikali iwaagize viongozi wote wa ngazi zote katika vijiji vyetu, Kata, Tarafa, Wilaya na Mikoa isambaze habari ya kuwaelekeza na kuziagiza kaya zote zenye watu wao wanaoishi au kufanya kazi nchi za jirani ambazo nazo zimeshaingiliwa na janga hili la virusi vya Korona, watu hao wabakie huko huko hadi janga hili lidhibitiwe na wasijaribu kurudi bila kupitia mipaka rasmi (border posts) wapimwe kabla ya kuruhusiwa kwenda makwao.

Mheshimiwa Spika, hofu yangu kubwa ni kwa wale wanaoweza kuamua kurudi nyumbani kwa kupitia njia zisizokuwa rasmi (njia za panya) na kuvuka mipaka na kwenda hadi manyumbani kwao bila kupimwa na ikitokea akaja mtu ambaye ameathirika; atakuja kuambukiza jamii yetu nzima ambayo kama mjuavyo hatuna miundombinu toshelevu na rasilimali za kupambana na gonjwa hili ambalo bado halina dawa wala chanjo.

Mheshimiwa Spika, pia naiomba Serikali iwekeze katika kuweka vifaa vya kupima na kuzuia maambukizi mapya katika vituo vyetu vyote vya kutolea huduma za afya nchini zikiwemo zahanati, vituo vya afya na hospitali zetu za Wilaya na Mikoa ili kuepuka uwezekano wa kutokea kwa mlipuko wa gonjwa hili kama ilivyotokea kwa wenzetu wa mataifa kama China, Italy, Spain na kwingineko.

Mheshimiwa Spika, mwisho napenda kupongeza juhudi zinazoendelea kufanywa na viongozi wetu wa ngazi za Taifa tukiongozwa na Rais wetu mpendwa Dkt. John Joseph Magufuli, Waziri Mkuu, Mheshimiwa Majaliwa Majaliwa na viongozi wetu wa Mikoa, Wilaya, Tarafa, Kata na hata Vijiji katika kuhakikisha kuwa tunafanya kila liwezekanalo kuzuia kuenea kwa homa hii mbaya ya Corona.

Mheshimiwa Spika, pamoja na juhudi hizi nawasihi Watanzania wenzangu tuendelee kumlilia Mwenyenzi Mungu atuondolee janga hili.

Mheshimiwa Spika, kwa haya machache nashukuru kwa kupokea mchango wangu wa maandishi na ninaunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira wa Mwaka 2018
MHE. DKT. STEPHEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi hii ili nami niweze kuungana na Wabunge wenzangu kuchangia katika hii Miswada na naomba nijikite kwenye Muswada wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira. Naomba nianze kwa kutoa maoni ya jumla halafu kulingana na muda nilionao nitapenda kutoa mchango wangu katika vipengele vichache nilivyovi- note katika Muswada husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maoni ya jumla nipende kuwapongeza waliofanya kazi nzuri ya kuandaa Muswada huu na nikiri kwamba, ni Muswada mzuri na ni Muswada unaotuletea sheria ambayo inahitajika sana katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, niseme tu masikitiko yangu kwamba, ingawa Muswada huu ni wa muhimu na unahitajika sana katika nchi yetu, lakini kuna baadhi ya Watanzania ambao kwao ni kama umetangulia kuwafikia kabla ya kinachotungiwa hii sheria hakijawa reality kwao. Kwa mfano kwa jamii za Watanzania wanaoishi katika nyanda za ukame kama Wilaya yangu ya Longido ambapo zaidi ya asilimia 46 ya wakazi wake hawana chanzo chochote kinachoeleweka cha maji hii kwao ni habari njema tu inayoonesha kwamba, siku ndoto yao ya kupata maji itakapotimia angalau kuna kitu ambacho kitawaelekeza namna ya kuyatumia kwa jinsi inavyostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa maoni yangu ya jumla niungane na wenzangu ambao wameangaliza hili suala la adhabu mbalimbali zinazoweza kutolewa kwa matumizi yasiyostahili ya maji. Ningeomba adhabu hizi ziwe categorized, kwa mfano, adhabu za taasisi zinazokiuka misingi iliyowekwa na Muswada huu zipangiwe adhabu yao kulingana na hadhi yao kwamba, ni taasisi. Category nyingine ni matumizi ya kibiashara, kama mtu anayatumia vibaya kwa ajili ya kufanyia biashara, pia adhabu yake ipangwe kulingana na jinsi alivyovunja sheria katika matumizi ya maji yaliyopelekwa mahali pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, category ya mwisho ni kwa watu binafsi, kama offence imetokea kwa mtu binafsi basi adhabu pia ilingane na hadhi ya huyo mtu aliyevunja sheria hiyo na hii ikizingatia kwamba, hata pamoja na kwamba, muswada na sheria inakwenda kuwekwa, imeweka standard pelnaties kwa ajili ya hizi offences, lakini kwa maoni yangu, ningeomba kwa sababu kuna haya mamlaka ambayo yanakwenda kuundwa na hasa hii Mamlaka ya Wakala wa Maji Vijijini, hiyo basi ipewe pia uwezo wa kutunga by laws ambazo zitakuwa ni case by case.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, wale Community Based Water Supply Organization ipewe mamlaka na sheria hii ya kutunga by-laws ya adhabu zinazostahili kulingana na mazingira ya watu husika. Kwa sababu Watanzania wengi watakaokuwa chini ya hiyo asasi ambayo ni ya community based watakuwa ni watu masikini ambao ukiwawekea faini ya shilingi milioni tano ni kama tu imewatangazia kifungo cha maisha au adhabu ya kifo maana kwao shilingi milioni tano ni kitu ambacho hawajawahi kuona na wala kupata au kupokea katika maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kusema kwamba pamoja na uzuri wa Muswada na sheria tunayokwenda kutunga lakini pia kwenye sehemu ya objectives, natamani kuona kauli mbiu inayotangaza kwamba azma na priority yake ya kwanza ni kuhakikisha kwamba kila Mtanzania anapata access ya maji safi na salama ya kutosha ndipo tuweze kupangilia hii miundombinu sasa ya kuyatumia inavyostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa maoni hayo ya jumla, naomba ni-point baadhi ya vipengele ambavyo napenda kuvitolea maoni. Tukienda Sehemu ya Saba tukaangalia Ibara ya 34(3) inasema hivi: “A Community Water Committee shall be the governing body responsible for overseeing operations of the community organization”. Kwa hiyo, kuna Kamati ya Maji ambayo inaundwa na ndiyo itakuwa inaendesha shughuli za huduma ya maji chini ya Wakala wa Maji Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nilipokwenda kuangalia Jedwali la Pili, kwenye kifungu cha 4(5) kinasema kwamba hii Kamati ya Maji ni Bodi ambayo itakuwa inakutana mara mbili kwa mwaka tu. Naomba kupendekeza kwamba kama hawa ndiyo waangalizi wakuu wa huduma ya maji katika jumuiya husika, inakuwaje wakutane mara mbili kwa mwaka wakati shughuli ya maji ni nyeti na mambo yanaweza kujitokeza hapa katikati na uamuzi wao ukahitajika. Ingawa kwenye hiyo schedule wanasema wanaweza kukutana wakati wowote kukiwa na haja kwa nini isiwekwe kabisa kwenye sheria kwamba ni lazima wakutane angalau siyo chini ya mara moja kila baada ya miezi mitatu au kila robo mwaka ili wawe karibu na usimamizi makini wa haya maji tunayotegemea yatakuwepo na watakwenda kusimamamia. Kwa hiyo, naomba badala ya kuwa wanakutana mara mbili kwa mwaka tu kama ilivyobainishwa kwenye Jedwali katika kifungu cha 4(5) iseme kwamba watakutana at least once every quarter.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia katika Ibara ya 35(3) kuhusu viwango vya maji, hapa haijatamkwi bayana kwamba viwango vinapangwa na nani. Napendekeza Community Based Water Supply Organization wao ndiyo wapange viwango na iandikwe kwenye sheria ili kusiwe na mkanganyiko kwamba hizi rate zinawekwa na nani na zinawekwaje na ikiwezekana basi mamlaka ya juu ama Waziri, ama mamlaka ya maji ya ngazi ya kitaifa itoe bei elekezi ili wananchi wasinyanyaswe kwa sababu ya kutokuwepo kwa sheria inayosema utaratibu wa kupata haya maji na kuweka viwango stahiki unawekwa na nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Sehemu ya Nane kwenye suala la financial provisions, nikaangalia kipengele cha vyanzo vya fedha ambayo inaweza ikapatikana kwa ajili ya kuendesha hizi asasi za maji, nikaenda Ibara ya 38(d) nikakuta inasema kwamba ni wajibu wa kila taasisi inapopata fedha kutoka katika vyanzo mbalimbali fedha vya nje kama donations kupata kibali cha Waziri. Sasa najiuliza kuna haja gani, huu urasimu ni wa nini? Kwa mfano, sisi tuna Community Based Water Supply Association akaja mtalii mmoja maana sisi tupo katika eneo la utali akaona mapungufu yaliyoko akaamua kuweka labda dola mia moja elfu ili kuboresha miundombinu tuliyonayo, kuna haja gani ya kupelekea hiyo taarifa kwa Waziri wakati kuna Serikali za Mitaa ngazi ya Halmashauri, kuna hii RUWA – Rural Water Supply Authority na ina Mkurugenzi wake mkuu? Naomba suala hili liangaliwe na atakapokuja baadaye anieleweshe…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Kiruswa.

MHE. DKT. STEPHEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Muswada ulioletwa mezani wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2021 ambao unakwenda sasa kuleta marekebisho na mapendekezo mbalimbali yatakayotuwezesha kutekeleza bajeti tuliyoipitisha hapa juzi na ambayo Watanzania kwa asilimia kubwa wameiunga mkono.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu utakuwa mdogo sana kwa sababu ningependa tu kuchangia juu ya Sheria ya Kodi ya Mapato Namba. 332 na Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta Sura ya 220. Lakini kabla sijachangia hoja zangu mbili katika haya maeneo nilipenda tu nitoe ushauri wa jumla na mtazamo wangu kuhusu dhana ya kulipa kodi katika Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli mimi nilivyokuwa nikiwa mdogo na nikitafakari jinsi kodi inavyochukuliwa katika Taifa letu na labda Mataifa yanayoendelea ni kwamba watu hawapendi kulipa kodi na inawezekana watu hawaelewi umuhimu wa kulipa kodi na kwa sababu pia nimebahatika kupata exposure ya kuishi nchi za wenzetu kila raia anajua umuhimu wa kulipa kodi na kulip akodi ni wajibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini inawezekana pia historia tuliyonayo ni kwamba watu walikuwa hawaoni faida ya kulipa kodi na ndiyo maana wengine wanathubutu kukwepa wanasema hata nikilip ambona bado sina barabara, sina maji, sina umeme. Lakini dhana hii nadhani katika hizi awamu mbili zilizofuatana, Awamu ya Tano ya Serikali yetu na Awamu hii ya Sita kila Mtanzania ni shahidi kwamba mapinduzi makubwa ya ukuaji wa uchumi wet una miundombinu yake ni ushahidi wa kutosha kwamba kodi zetu zinapolipwa zinafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nipende kuwashauri Watanzania kwamba tusione kodi kama ni mzigo na kama ni msalaba ambao tunapikwa bila sababu ya msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo ninapenda pia kuishauri Serikali ijikite katika kuanzisha kampeni kubwa ya Kitaifa ya kutoa elimu ya kodi na isiishie tu katika kutoa elimu ya kodi ikiwezekana iwekwe pia katika mitaala ya elimu kuanzia elimu ya msingi kwenda juu lakini zaidi ya hayo Serikali iweke mkakati wa kusambaza kodi ili kila mtu mwenye hadhi ya kulipa kodi aweze kugawiwa sehemu yake kulingana na kipato chake alipe kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukifanya hivyo, tunaweza tukapunguza mzigo wa kutwisha kodi kubwa kwa baadhi ya watu wachache ambao ndiyo wanalipa kodi katika nchi yetu watu ambao hawafiki hata 5,000,000 ili mzigo upungue na kila mtu alipe kodi kwa kufurahia kama ambavyo waumini katika madhehebu yao huwa wanatoa sadaka kila Jumapili au Ijumaa kwa kufurahia tena bila kulazimisha na mtu yeyote. Kuna Fungu la Kumi, sadaka ya kwanza na ya pili na sijawahi kuona muumini akilalamika. Wanatoa kwa sababu wanaamini kuna baraka wanayokwenda kupata kwa Mwenyezi Mungu. Sisi tunakwenda kupata baraka kwa kukuza uchumi wetu, miundombinu yetu, elimu yetu na afya yetu tunapotoa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo basi sasa nichangie zile hoja zangu mbili katika hiki Kifungu cha 25 ya Muswada wa Sheria ya Fedha 2021 ambapo kuna kodi ya zuio la asilimia 2 katika mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi. Nimesoma pia maelezo ya Waziri akisema kwamba kodi hii haitawagusa wafanyabiashara wadogo, vyama vya ushirika, inakwenda kwa mawakala na makampuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninaomba nijiridhishe na baadae atakapokuja kuhitimisha anisaidie kufafanua kwamba ni kwa jinsi gani atawalinda hawa wadogo wasio na kipato. Kwa mfano, kuna viwanda hivi sasahivi vinajengwa sehemu mbalimbali nchini za kuchakata mazao ya mifugo. Sisi tuna kiwanda katika Wilaya ya Longido cha kuchakata nyama za mifugo. Adha ambayo tumepata tangu kiwanda hiki kianze ni adha ya bei anayonunulia yule mwenye kiwanda mifugo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ikafika mahali tunamuomba afanye utafiti na nchi ya jirani watu walikuwa wanapeleka mifugo mingi Kenya tunakosa mazao mengine yanayotokana na nyam ana ikafika mahali na yeye akaona akaanza kupandisha pole pole bei ya kilo ya nyama lakini malalamiko yake makubwa ni kwamba kodi ya Serikali ndiyo kikwazo. Kulikuwa na utitiri wa kodi nyingi ambazo hata sijaona kama zimeshapunguzwa kwa jinsi ambavyo tumekuwa tukilia katika Bunge hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya mwekezaji nae kutambua umuhimu wa kuongeza ongeza bei ili asikose malighafi ikafika mahali kilo ya nyama ya mbuzi imefika mpaka 7,500 kutoka 6,500 lakini kwa wenzetu nchi ya jirani ni 8,500. Sasa akiona kwamba kuna hii kodi ya zuio la asilimia 2 isije ikatokea kwamba sasa na yeye ama ata-freeze bei hatapandisha tena bei ya bidhaa ya mfugaji ambayo ni mifugo yake ama ataihamishia sasa kwa mfugaji mwenyewe kuhakikisha kwamba sio yeye anayelipa, anakwenda kupunguza bei ya kununulia ile mifugo ili yeye asipate hasara ya hiyo kodi ya zuio.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ningeomba Serikali iangalie namna ambavyo itamhakikishia huyu mfanyabiashara mdogo wa mifugo au mkulima au mvuvi kwamba hizo kodi za zuio asilimia 2 haitakwenda kuhamia kwake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu wa pili kwenye hii Sheria ya Ushirika, ushuru wa barabara na mafuta sura 220 ni ushauri natoa hapa kwamba kwa sababu tuna TARURA na kwa sababu mfumo wa ukusanyaji wa mapato yetu fedha zote zinakwenda kwenye Hazina kuu ya Serikali ningeomba na nimesoma pia kwenye Taarifa ya Kamati ya bajeti kwamba wangeomba kuwe na mfuko maalum mahsusi kwa ajili ya kupokelea hizi fedha zinazokwenda kupatikana kwenye mafuta ya aina zote ambazo zinakatwa shilingi 100.

Mheshimiwa Naibu Spika, huo mfuko ni muhimu sana na tusiishie tu kuwa na mfuko muhimu kwa sababu itakata ile urasimu wa kwenda kuomba fedha mpaka zitoke HAZINA inachukua muda. Kuwekwe pia na Fungu la dharura litakalopelekwa katika kila Halmashauri ili inapotokea dharura mvua imenyesha daraja limekatika barabara fulani haipitiki, badala ya kuingia mlolongo mzima wa kuomba fedha kule Hazina au labda sasa kwenye huu mfuko wawe na fungu lao la dharura kila wakati. Wawe na fungu ambalo watalichomoa tu watengenezee miundombinu iliyoharibika kama mfuko wa dharura.

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria itambue hilo na marekebisho mwende mkarekebishe kidogo kuwe na percent kulingana na mahitaji ya barabara zilizoko katika kila halmashauri ili halmashauri ziweze kuwa na mfuko wake wa dharura wa kunusuru barabara zinapoharibiwa na mvua kwa sababu barabara nyingi ambazo hii fedha inaenda kusimamia kwa asilimia kubwa zitakuwa bado ni zile barabara za changarawe, barabara za udongo ambazo ni rahisi sana kuharibiwa na mabadiliko ya tabianchi inaponyesha mvua wakati wowote.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache napenda kuwapongeza tena Wizara hii ya Fedha na Mipango kwa bajeti nzuri waliyotuletea na hata kwa huu muswada na marekebisho yanayopendekezwa lakini wana kazi kubwa ya kutoa elimu ya kodi na sio elimu ya kodi tu na kufanya marekebisho mbalimbali ambayo Wabunge wenzangu wametangulia kuyasema ili utekelezaji wa hii bajeti ya mwaka 2021/22 uweze kuleta tija ambayo Watanzania wanaitegemea. Ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nashukuru. (Makofi)