Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Justin Joseph Monko (16 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa na mimi nafasi ya kuweza kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna inavyoshughulika na masuala ya wananchi kupitia bajeti zake na kupitia watendaji wake wote kwa ujumla. Kwa sababu ya muda wangu mfupi nitajaribu tu kueleza niliyoyaona katika bajeti hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la kilimo; bado kuna tatizo kubwa kwamba tuna uwekezaji mdogo saa wa kilimo. Tunayo maeneo makubwa, mazuri ambayo yanafaa kwa kilimo, tunayo mabonde mazuri ambayo yanafaa katika kilimo cha umwagiliaji, lakini tunachokifanya sasa hivi ni kufanya umwagiliaji kwenye bahari, kumwagilia maji kweye mito, lakini kilimo cha umwagiliaji bado hakijawa na tija katika nchi yetu.

Kwa hiyo, niiombe sana Serikali ijaribu kuwekeza hatuwezi kwenda kwenye hatua ya viwanda ambayo tunazungumza na tumesisitiza kwamba viwanda vyenyewe lazima viwe ni viwanda ambavyo vitatokana na malighafi za ndani. Malighafi hizo ni za kilimo na tumekuwa na uwekezaji mdogo sna katika sekta ya kilimo.

Katika masuala ya elimu, katika hotuba ya Waziri Mkuu tumeona katika masuala ya elimu kwa kweli udahili wa wanafunzi umeongezeka kwa asilimia zaidi ya 35, lakini miundombinu yetu katika shule za msingi hata katika sekondari kwa kweli ina changamoto kubwa. Zipo shule nyingi katika Jimbo langu zina matatizo. Iko shule moja ya Mikuyu ina madarasa mawili, ina choo ambacho ni cha muda, lakini ina darasa kuanzia chekechea mpaka darasa la sita na haina hata ofisi ya walimu, lakini shule hii imesajiliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini iko shule nyingine ambayo iko Mighanji katika Kata ya Ngimu. Shule hii ina wanafunzi wengi, wako wanafunzi wanasoma wanatoka zaidi ya kilometa 11 kwenda kwenye hiyo shule. Wananchi wa vitongoji vya Ngaramtoni wamejitolea kujenga shule lakini bado haijapata usajili. Wanayo madarasa manne lakini sasa hivi imeshindwa kusajiliwa kwa sababu haina lipu, haina sakafu na bado tumeacha watoto wetu wale wadogo wanaendelea kutembea kwa zaidi ya kilometa 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili ni kubwa ukichanganya na tatizo la upungufu wa walimu, kwa kweli limeleta shida sasa katika Jimbo langu na ndiyo mtaona hata matokeo yaliyopita kwa kweli Jimbo letu limefanya vibaya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia shule za sekondari. Tunayo matatizo ya maabara, maabara nyingi katika Jimbo langu hazijakamilika na nilipotembelea katika Jimbo lile nimeona nyingi zinahitaji fedha karibu shilingi milioni 90 kumalizia. Ni nyingi na suala hili sasa hivi katika bajeti ya Halmashauri yenye makusanyo ya ndani ya shilingi bilioni 1.3 haiwezi kufanya jambo lolote. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali ifanye mkakati wa makusudi katika kuhakikisha kwamba inasaidia kumalizia ujenzi wa hizi maabara zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niangalie katika suala la afya. Suaa la afya katika Jimbo langi la Singida Kaskazini poa ni tatizo kubwa. Nina vijiji 84 lakini tuna zahanati 32 tu. Vituo vya afya vilivyopo ni viwili, Kituo cha Mgori na Kituo cha Ilongero. Vituo hivi havitoi huduma ya upasuaji. Kwa bahati mbaya sana vituo vyote viwili havijapata fedha za ukarabati kama ambavyo katika halmashauri nyingine zimepata.

Kwa hiyo, niiombe sana Serikali ifanye haraka kwa sababu Halmashauri hii haina hata hospitali ya wilaya tunategemea Hospitali ya Mtinko ambayo ni hospitali ya mission na wananchi wanapata matatizo sana katika masuala ya matibabu. Viko vijiji vinafuata matibabu kwa zaidi ya kilometa 40. Kiko Kijiji cha Mkulu ambacho makao makuu yake ya kijiji ni kilometa 26. Viko vitongoji vitatu ambavyo viko Mkulu, lakini kijiji chenyewe ni cha Nduamuhanga kiko kilometa 26; na huko ndiko ili zahanati.

Ukitoka hapo ni lazima ukatize kwenye pori, kwenye hifadhi au upite katika Wilaya ya Chemba. Tunahitaji kwa kweli kupata msaada kwa sababu wananchi wale wanahitaji kupata msaada wa haraka ili kusudi waweze kuepukana na matatizo na kuokoa maisha ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije katika suala la barabara. Jimbo la Singida Kaskazini lina mtandao wa barabara wa kilometa 772.39...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, lakini kinachosikitisha barabara hizo zimejengwa kwa kiwango cha changarawe kwa asilimia 8 tu, yaani kilometa 68 kati ya hizo 774.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali iweze kutenga fedha katika bajeti hii inayokuja kuhakikisha kwamba Jimbo hili linasaidiwa. Hatuwezi kuendelea kuwa na barabara za udongo kwa zaidi ya asilimia 91 katika karne hii. Ahsante sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu sana. Nianze kwa kuipongeza sana Serikali, hasa Wizara hii, kwa fedha ambayo imeshatutengea sisi Mkoa wa Singida katika kuboresha miundombinu ya barabara tuliyonayo. Tumeona wameanza kutenga fedha kwa ajili ya feasibility study ya barabara ya kutoka Singida kuelekea Katesh na Singida kuelekea Shelui, sisi wa Mkoa wa Singida tunafurahi sana katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunalo tatizo la reli yetu ambayo imeunganisha kutoka Manyoni kuja Singida Mjini. Reli hii haijafanya kazi tangu mwaka 2009 na kumekuwepo na dhana potofu kwamba baada ya kuwa sasa tumepata barabara za lami basi pengine reli hiyo ilikuwa haiwezi kuzalisha na haiwezi kupata mizigo. Tukumbuke Singida ni katikati ya nchi na sisi pale Singida kwa reli hii kufika pale maana yake tunaweza tukahudumia mizigo inayotoka Simiyu, Shinyanga na Mwanza ili kuweza kuendelea kuokoa barabara hizi ambazo zimekuwa zikiharibika kwa wakati mwingi ambao tumetumia malori kwenye barabara zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Singida Kaskazini pia tunazo barabara zenye shida. Ipo barabara ya kutoka Singida – Ilongero – Mtinko – Mudida inaelekea Haydom, ukiangalia katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri barabara hii sasa naona imetengewa fedha ya kuanzia Karatu – Mbulu, ikishafika pale Haydom inakwenda Sibiti. Sasa barabara hii iko katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi, ilikuwa ni ahadi pia ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne na ahadi ya Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe Wizara iangalie namna ya kufanya feasibility study katika barabara hii ili kuja kuunganisha na Mji wetu wa Singida ili barabara itakapofunguliwa basi wananchi hawa waweze kupata huduma kwa sababu ni barabara muhimu sana inayounganisha miji mingi sana, lakini inaunganisha huduma za muhimu sana, hasa huduma za hospitali kikiwemo Kituo cha Afya cha Ilongero, Hospitali yetu ya Mtinko, lakini tunakwenda Nkungi, lakini kuna Hospitali ya Rufaa ya Haydom.

Mheshimiwa Naibu Spika, iko barabara muhimu sana katika Jimbo la Singida Kaskazini, barabara hii ni ya kimkakati hasa upande wa uchumi na barabara hii inatokea Singida Mjini, inapita katika Kata ya Kinyeto – Kinyagigi – Meria – Magojoa – Msange na inakwenda kuunganisha katika Kata ya Itaja katika Kijiji cha Sagara kwenye Barabara Kuu iendayo Katesh, Arusha.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni muhimu sana kiuchumi, sisi ni wazalishaji wakubwa sana wa vitunguu na ni wazalishaji wakubwa sana wa alizeti, tunahitaji kuileta alizeti hii katika kiwanda kilichopo Singida Mjini, lakini pia tunahitaji kusafirisha vitunguu vyetu. Mpaka sasa wanunuzi walio wengi wanashindwa kufika katika maeneo yetu, tunashindwa kuwa na masoko ndani ya Halmashauri yetu kwa sababu barabara zetu ni mbovu na watu wanalazimika kutumia usafiri wa magari madogo madogo na hivyo badala ya wanunuzi kufika kwenye maeneo wanakuja tu wale wafanyabiashara wa kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii pia tuliiombea kwa Mheshimiwa Rais, ina urefu wa kilometa 42 tu na Mheshimiwa Rais alionesha utayari wa kuijenga katika kiwango cha lami. Kwa hiyo, niiombe sana Wizara iiweke katika mpango wa kufanyiwa feasibility study katika kipindi cha mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunayo barabara moja ndogo, ina kilometa tano, sita, ambayo inatoka katika Kijiji cha Sagara inakwenda katika Kijiji cha Gairo na inakwenda kuunganisha katika Kijiji cha Pohama na kutoka hapo inakwenda tena kuunganisha katika Mji wa Katesh. Barabara hii ina matatizo na wananchi wanaoishi katika Vijiji vya Gairo wametengwa na eneo kwa sababu ukitokea Pohama kuna madimbwi na wakati huu wa mvua haipitiki kabisa. Lakini ukitoka Gairo kupanda hapa Sagara kuna mlima mkubwa ukiwa unapanda katika hilo Bonde la Ufa na barabara hii haipitiki kwa kweli kwa vyombo vya moto.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara yetu hii ya Mambo ya Ndani. Nianze kwa kuipongeza Serikali kupitia Wizara yetu ya Mambo ya Ndani kutokana na hali ya usalama wa nchi na wananchi pamoja na mali zao. Jeshi la Polisi pamoja na majeshi mengine ambayo yako chini ya Wizara hii yamefanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo machache ambayo napenda kushauri. Wenzangu waliotangulia wameshaanza kusema, nianzie na Jeshi la Polisi. Jeshi la Polisi pamoja na kwamba wanafanya kazi nzuri, lakini kwa kweli askari wetu hawa wanafanya kazi katika mazingira magumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira ya watumishi wa Jeshi la Polisi ni magumu sana kwa sababu hawana vitendea kazi, usafiri, majengo yao wanayofanyia kazi katika ofisi ni mabovu sana lakini na makazi yao ni duni kabisa na kuwafanya wale watumishi kuwa kama wamekata tamaa. Wakati mwingi inakuwa kama vile wamesahaulika labda kutokana na wingi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda sana nishauri katika bajeti hii ambayo tunaendelea wajaribu kuliangalia. Sasa hivi kama Mheshimiwa Waziri alivyosema tayari kuna ujenzi umeshaanza kwa mfano kule Arusha tukishirikisha wadau. Yako maeneo ambapo wadau wa maendeleo hawa hawana michango mikubwa sana hasa katika sekta hizi za ulinzi na usalama kutokana na mapato yao au jiografia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukitegemea sana wadau wa maendeleo na Serikali tukakaa pembeni tu kwa kweli yako maeneo ambayo wanajeshi wataendelea wetu kupata matatizo makubwa ya vitendea kazi lakini kuendelea kuishi katika maisha duni na hivyo kutoa huduma zilizo duni kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule jimboni kwangu kwa kweli, nilishamwomba hata Mheshimiwa Waziri aweze kufika, vituo vyetu vya polisi vinatia kinyaa. Yako maeneo kwa mfano ukienda katika Kata moja ya Ngimu, kituo cha polisi wamekwenda kukodisha eneo la Serikali ya Kijiji, wamekwenda kukodisha kwenye majengo ya zamani ya Chama cha Mapinduzi na wanashindwa hata kuyakarabati majengo hayo kwa sababu kwa upande mmoja wanaona majengo sio yao na kwa upande mwingine Jeshi letu la Polisi halina fedha za kutosha kuweza kufanya ukarabati wa majengo haya. Matokeo yake ni nini sasa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wale watumishi wanakaa kwenye nyumba za kupanga. Wakati mwingine ni mbali kabisa na maeneo wanakotakiwa kufanya kazi. Jambo hili linarudisha nyuma sana utendaji wa Jeshi letu la Polisi kwa sababu pale ambapo wananchi wanawahitaji kwenye vituo hawawezi kupatikana kwa urahisi. Ukizingatia bado tunalo tatizo la miundombinu ya mawasiliano hata kuwapata askari imekuwa ni shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Wizara ifanye mkakati wa makusudi wa kuhakikisha kwamba tunaboresha sana mazingira ya kufanyia kazi kwa askari wetu ili hizi huduma ambazo tunaziomba za kutoka Jeshi la Polisi za ulinzi na usalama ziweze kupatikana kwa urahisi, lakini tuweze kuwatia moyo askari wetu kufanya kazi ya kuilinda vizuri nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hili ni kubwa. Wamezungumza waliotangulia, hatuna fedha za kupeleka hata mahabusu wetu kwenye mahakama zetu, kwenye Mahakama za Kata wakati mwingine hata kwenye Mahakama za Wilaya na hivyo tunajikuta kwamba haki za wananchi zinacheleweshwa ama hata wakati mwingine zinapotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo vingine havina hata sehemu ya kutunzia mahabusu, tunao ushahidi kabisa kuna maeneo wananchi wamelazimika kwenda kuvamia sehemu hizo na kuwatorosha wahalifu wale ambao walikuwa wanakusudiwa kupelekwa katika vyombo vya kutolea haki. Sasa ni vizuri sana Serikali ikaangalia suala hili na kuona kwamba tunahitaji kwa kweli kuwa na mazingira mazuri ya kufanyia kazi katika vituo vyetu vya polisi kuanzia kwenye kata hata ngazi ya wilaya ili kusudi wananchi waweze kupata haki zao kwa wakati wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana Wizara kuna zoezi la vitambulisho linaendelea na hata kule jimboni kwangu naona sasa wanakwenda na wananchi wanaendelea kupata vitambulisho hivyo. Niombe kasi hii iongezeke na wananchi wapewe taarifa ili katika zile siku ambazo zimepangwa, tuweze kuhakikisha kwamba tunatoa huduma hii kwa haraka na kuhakikisha kwamba wananchi walio wengi wanaostahili kupata vitambulisho wanaweza wakapata vitambulisho kabla wale watendaji wetu hawajahama katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lipo pia suala la namna ya kuwahudumia mahabusu wetu hasa kwenye masuala ya chakula. Tunawategemea sana wananchi wale ambao wapendwa wao wanakuwa wamechukuliwa na bado wako chini ya polisi hawajafikishwa mahakamani kutoa support ya chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengine kwenye jimbo kama la kwangu vituo vya polisi hivi viko vichache mno na unakuta wananchi wale ambao wanatakiwa kuwahudumia ndugu zao wako mbali. Wananchi wanapata tatizo kubwa la kuweza kuwahudumia wale ndugu na wakati mwingine wasipopata nafasi ya kufika pale, askari wetu wanapata shida kubwa sana ya kuhakikisha kwamba mahabusu hawa wanaweza wakapata angalau huduma zile za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Jeshi letu la Polisi na Wizara tuangalie namna ya kuweza kusaidia katika maeneo haya. Kwa sababu hawa wananchi hawajahukumiwa kwamba wametenda makosa, wana haki ya kuendelea kupata chakula, wana haki ya kusikilizwa, zipo haki za kimsingi ambazo wanastahili kuzipata ili kusudi tusianze kuwahukumu kabla hata hawajafika mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni la muhimu sana kwa sababu kesho na keshokutwa na sisi pia, tutakuwa huko, vituo vyetu hali zake ndiyo hizi hakuna hata mahali pazuri pa kuwaweka wananchi. Kwa hiyo, niombe sana Wizara waangalie namna ya kuweza kuboresha miundombinu hii lakini huduma za chakula, mafuta kwa ajili ya askari wetu na vitendea kazi. Hata wale ambao tumewapa pikipiki, tusiwape tu pikipiki tukashindwa kuwapa mafuta na fedha za matengenezo ili waweze kuendelea kufanya patrol maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la usalama barabarani. Nilipongeze sana Jeshi la Polisi, sasa hivi utii wa sheria bila shuruti umeongezeka kwa kiasi kikubwa. Hili ni jambo jema na la kujivunia sana. Pamoja na kwamba yako maeneo mengine bado askari wanafanya kazi za kuvizia ni kutokana na tabia ya sisi madereva ambao wakati mwingine tunalazimika kuanza kuviziwa katika maeneo hayo. Niombe sana Wizara tufanye kazi kubwa na hasa Jeshi la Polisi ya kuendelea kuwaelimisha wenzetu hawa madereva.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii ya kutoa elimu kwa madereva ni muhimu sana kuliko kutoza fine. Pamoja na kwamba nimesikia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri inawezekana kwamba tukakimbilia sana kwenye fine ili kuongeza mapato, njia hii haiwezi ikatufanya tukawa na utii wa sheria bila shuruti. Wako wengine wenye fedha wanavunja sheria kwa makusudi ili kusudi waweze kupigwa fine na wanalipa lakini wanaendelea na uvunjaji wa sheria na maisha ya wananchi wetu yanaendelea kupotea kwa sababu ya madereva wa aina hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Jeshi la Polisi litoe sana elimu kwa madereva hawa kila siku maana ni lazima kukazia maarifa. Madereva hao wanafanya makosa wakati mwingine sio tu kwa sababu wana fedha…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika wizara hii muhimu kabisa ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri anaonesha kabisa kwamba asilimia 65.5 ya wananchi wa Tanzania wanashughulika na kilimo. Ukiangalia katika bajeti ambayo inaombwa na Wizara hii ni ndogo sana ukilinganisha na idadi ya Watanzania hawa. Watanzania hawa ndio ambao tumewaita katika hotuba hii kwamba ni maskini sana. Watanzania hawa ndio ambao wamekuwa wakihangaika kwa muda mrefu na kwa wakati wote huu tumekuwa tukiwatengea fedha kidogo kama ambavyo imeoneshwa katika takwimu. Nisingependa kurejea katika takwimu zilizopo kwa sababu ya muda ambao nimeupata katika kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wetu wa Singida na hususan Jimbo la Singida Kaskazini sisi ni wakulima wa vitunguu na alizeti. Katika taarifa ya Kamati mtaona kwamba nchi yetu inatumia fedha zaidi ya shilingi bilioni 413 kila mwaka katika kuagiza mafuta, lakini hatujaweka mkazo katika zao la alizeti ambalo linalimwa na wananchi wa Mkoa wa Singida na maeneo mengine. Ni kwa nini Serikali imeendelea kutoa fedha za kuagiza mafuta ghafi kwa asilimia 70 badala ya kuwekeza katika kilimo cha alizeti ili wananchi waweze kupata ajira? Kilimo ndicho kinachoajiri idadi kubwa ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amepita katika maeneo mengi akisema yeye ni Rais wa wanyonge, wanyonge wa Tanzania hii wapo katika sekta ya kilimo huko vijijini. Ukienda katika majimbo yale ya vijijini zaidi ya asilimia 90 ya wananchi hawa wanategemea kilimo.


Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunahitaji kuwekeza sana katika kilimo ili kuweza kuwakomboa wananchi hawa ambao wamekuwa wanashinda kwa muda mrefu na kwa kweli hawapati fedha za kuweza kuendesha maisha yao, wameendelea kuwa maskini kwa muda mrefu kwa miaka mingi tangu tumepata uhuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme ukuaji wa sekta ya kilimo ni mdogo sana kama alivyoeleza Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake. Mpaka sasa ni asilimia 3.1; hatuzuiliwi kwenda kwenye asilimia sita kama ukuaji wa uchumi ulivyo, tunahitaji kuwekeza fedha katika sekta hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hotuba hii katika Bajeti Kuu ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba niipongeze Serikali kwa ujumla, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu yote kwa bajeti hizi mbili ambazo wametuletea ambazo zina akisi taswira ya maendeleo ya Taifa letu kwa ujumla. Nawapongeza sana kwa sababu bajeti hizi zimegusa maeneo mengi ambayo yamewagusa wananchi wetu katika sekta mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nianze kwa kupitia ukurasa wa 14 wa kitabu cha Mheshimiwa Waziri ambapo alikuwa ameongelea sana changamoto ambazo zilitukumba hasa katika utekelezaji wa bajeti iliyopita. Changamoto hizo amezitaja hapo, mojawapo ikiwa ni ajira. Tatizo hili la ajira Waheshimiwa Wabunge wengi waliotangulia wameshalizungumza kwamba tunao wahitimu laki nane lakini wanaopata ajira Serikalini ni elfu arobaini tu. Natambua sana kwamba Serikali ndiye mwajiri mkubwa na pamoja na kwamba ni mwajiri mkubwa hawezi akaajiri wahitimu wote ambao wanakuwa wamehitimu katika vyuo vyetu.

Mheshimiwa Spika, tunazo sekta nyingi ambazo zingeweza zikawachukua wanafunzi hawa kwa taaluma hizo ambazo wameshazipata. Moja ya sekta ambazo mimi naiona ni sekta ya kilimo. Sekta ya kilimo ambayo kwa bahati mbaya sana pia imetengewa bajeti ndogo sana katika bajeti ya mwaka 2018/2019 ambayo ni sawa na 0.4 ya bajeti nzima ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sekta ya kilimo ndiyo inayoajiri wananchi wengi sana, zaidi ya asilimia 65. Ni sekta ambayo inagusa wananchi wengi hasa wa vijijini, sawa na kule kwenye Jimbo langu ambako nilipotoka mimi. Hata hivyo utaona kwamba uwekezaji katika sekta ya kilimo umekuwa ni mdogo sana. Matokeo yake tumekuwa na tatizo la ajira, matokeo yake tumekuwa na umaskini mkubwa na mpaka sasa kwa mujibu wa takwimu za Mheshimiwa Waziri hapa tunao maskini wa zaidi ya asilimia 26.4. Tatizo hili ni kubwa, wananchi wengi bado wanaishi chini ya dola moja.

Mheshimiwa Spika, hili ni jambo ambalo linatufanya tuanze kuangalia katika kuwekeza katika sekta ya kilimo ambayo inaweza kabisa ikawagusa wananchi wengi na ikawaondoa wananchi wengi katika dimbwi la umaskini tulionao. Kwa hiyo, ningeishauri sana Serikali ijaribu kuangalia namna ya kuwekeza katika sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano, katika Jimbo langu la Singida Kaskazini sisi ni wazalishaji wakubwa wa mazao ya mahindi, mtama, vitunguu na alizeti. Tunacho kiwanda kikubwa sana cha alizeti Afrika Mashariki ambacho kiko pale Mount Meru; hakina malighafi za kutosha na wananchi wengi wanashindwa kuhamasika kulima kwa sababu wanategemea zaidi tu kilimo cha mvua. Hakuna kilimo cha umwagiliaji ambacho kinaendelea. Ziko skimu za umwagiliaji ambazo hazijafanya kazi kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, nitatolea mfano skimu moja ya umwagiliaji iliyopo katika Kata ya Msange ambayo tangu mwaka 2009 ilishafanyiwa upembuzi, wananchi walishalipwa katika maeneo yaliyozunguka katika lile bwawa, ni skimu ambayo inatarajiwa kuwa na hekari elfu tatu na kuhudumia wananchi zaidi ya elfu kumi.

Mheshimiwa Spika, skimu hii ya umwagiliaji ilianza kutengewa fedha, ilionekana inahitaji fedha zaidi ya bilioni 1.3 tangu bajeti ya 2009/2010. Hadi ninavyoongea hivi sasa skimu hiyo haijafanyiwa chochote hatujapata fedha na wananchi wameendelea kubaki na mpaka sasa tulianzisha tu skimu ndogo ya ekari 25 ya umwagiliaji wa matone ambayo kwa kweli haijaweza kutoa tija kwa wananchi wa Kata ya Msange Maghojoa na Mwasauya.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ombi langu kwa Serikali ni kuweka uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo ambayo inaweza kuwagusa wananchi walio wengi. Tukiwekeza katika kilimo tutakuwa tumewekeza katika kuongeza ajira kwa vijana wetu. Tutakuwa vile vile tumeongeza Pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati tunaongea ukuaji wa uchumi wa asilimia saba, sekta ya kilimo yenyewe inakuwa kwa asilimia 3.7. Ukuaji huu ni mdogo mno na ndiyo maana hali ya umaskini inashindwa kuondoka na wananchi wetu wanazidi kuwa maskini kila siku na hata ukiangalia huduma ambazo wanaendelea kuzipata kule vijijini tunashindwa kwa sababu mapato yetu ni madogo na Serikali haina uwezo wa kuhudumia miradi mingi ya maendeleo. Kwa hiyo, nataka niiombe sana Serikali kuwekeza sana katika hilo.

Mheshimiwa Spika, katika ukurasa wa 61 mpaka 62 ya kitabu cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri wameweka tozo. Toza ushuru wa forodha wa asilimia 25 badala ya sifuri (0) na 10 katika mafuta ghafi ya kula mfano wa alizeti, mawese, soya, mizeituni na kadhalika. Hili ni jambo zuri na lengo hapa ni kujaribu kulinda viwanda vyetu vya ndani. Hata hivyo, tunajiuliza, tozo hizo kwa bidhaa zinazoingia kutoka nje ambazo tumeweka zinawezaje sasa kuwa-encourage wananchi wetu wakaweza kuongeza kipato na kuongeza uzalishaji? Tutakuwa na viwanda vikubwa kama ambavyo tulivyo navyo installed capacity sasa ni kubwa, lakini malighafi zilizopo ni ndogo. Hadi sasa kwa mfano alizeti tunazalisha kati ya tani laki mbili na nusu mpaka tani laki tatu; lakini kiwanda cha Mount Meru pale Singida kinahitaji zaidi ya tani milioni mbili kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, sasa tunahitaji kuwekeza katika mbegu bora zinazotoa mafuta mengi, tunahitaji kuwekeza katika kuwapa wananchi mbegu zilizo bora ili waweze kuongeza tija katika uzalishaji huo. Tukifanya hivyo tutakuwa tumefika mbali na wananchi wetu tutakuwa tumewasaidia sana.

Mheshimiwa Spika, liko jambo lingine ambalo linaambatana na hilo, hasa kwenye upande wa chakula cha mifugo, mfano kuku, ng’ombe na mifugo mingine ambacho kinatokana na mashudu ya alizeti, mashudu ya pamba, Soya na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu lilipitisha zero VAT katika chakula cha mifugo. Hilo ni jambo jema na lengo lake lilikuwa ni katika kuweza kuwasaidia wafugaji. Hata hivyo, tunalo tatizo kwamba zipo malighafi za chakula cha mifugo. Kwa mfano, mashudu ya alizeti, mashudu ya pamba bado yanatozwa VAT kwa sababu msamaha uliotolewa ulikuwa peke yake kwenye HS code ya 23.09 ambao haugusi mashudu haya ambayo yanazungumzwa. Sasa hivi tunavyoongea mashudu haya yanakwenda Kenya yanatengenezwa chakula cha kuku kwa sababu kunakuwa na zero VAT unapo-export, halafu chakula hicho kinarudi tena Tanzania na sisi ndio tunakuja kununua.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo wawekezaji wengi wanaona bora kuwekeza Kenya wakachukua malighafi Tanzania na hatimaye kurudisha chakula hicho Tanzania na sisi tunashindwa kulinda viwanda vyetu, tunakosa ajira na tunakosa mapato. Kwa hiyo niombe sana Serikali iweze kuondoa VAT katika mazao haya ambayo ni input kubwa kwa asilimia 80 katika utengenezaji wa chakula cha mifugo.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JUSTIN M. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda nimshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa mpango huu ambao ametuletea hapa Bungeni ili sisi nasi tuweze kuupitia na kutoa mapendekezo na maoni yetu. Wamefanya kazi kubwa na tunaanza kuona kwamba upo mwanga mkubwa wa kuweza kutekeleza miradi mingi ambayo tumeikusudia na ambayo ipo katika mpango wa miaka mitano wa 2016-2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na suala la ukusanyaji wa mapato. Katika taarifa tulizozipata na za kiutendaji katika mwaka wa fedha 2016/2017 na 2017/2018 zinaonyesha kwa kiasi fulani tumeshindwa kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato. Pamoja na kwamba TRA wamefanya kazi kubwa lakini tumeshindwa kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato na hatimaye mipango au miradi ya maendeleo mingine imeshindwa kufikia asilimia 100 kwa namna tulivyokuwa tumepanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe na nishauri, zipo changamoto ambazo Mheshimiwa Waziri amezitaja, nami nataka nijikite katika baadhi ya changamoto hizo ili kusudi tuweze kuona namna gani ambavyo tunaweza tukapata mapato au kubadilisha mbinu za ukusanyaji wa mapato na kuweka miradi mingine ambayo pia inaweza ikatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ambalo limeelezwa hapa ni ugumu wa ukusanyaji. Tunao ugumu wa ukusanyaji wa mapato kwa sababu ya uwepo wa sekta isiyo rasmi ambapo tunaishindwa kukusanya mapato yake. Nakubaliana na changamoto hii na wewe mwenyewe ni shahidi, mimi natoka Mkoa wa Singida na wewe hapa Dodoma sisi ni wakulima wa alizeti. Tunazo biashara nyingi sana ambazo zinafanyika kwenye barabara. Wakulima wanakwenda wanakamua alizeti, wanaweka kwenye madumu, wanafanya kazi ya kusubiri wanunuzi kwenye barabara zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili likiwekewa utaratibu mzuri tunaweza kabisa tukapunguza ukubwa wa tatizo hili la biashara zisizo rasmi. Mfano tunatumia fedha nyingi sana katika kuingiza mafuta ya kula kutoka nje na sisi ni wazalishaji wazuri wa mbegu za mafuta yakiwemo ya alizeti. Ni kwa nini katika mpango huu tusipunguze kiasi cha fedha za ununuzi wa mafuta na tukawekeza katika ununuzi wa mashine za kufanyia double refining ili kuongeza thamani na ubora wa mafuta yetu tukaweza kuuza kwenye masoko ya ndani na masoko ya nje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwezo wa kukusanya mafuta yote ambayo yanauzwa barabarani na wananchi upo tukiwa na viwanda vya kutosha vya double refining. Tukifanya hivyo tutakuwa tumewatafutia wakulima wetu masoko yenye uhakika maana watakuwa hawana sababu tena ya kusubiri barabarani, wanaweza wakapata masoko kule kule wanakokamua alizeti na viwanda vya double refining vikachukua mafuta yale kwa ajili ya kwenda kuyachakata kwa mara ya pili na yaweze kwenda kwenye masoko ya ndani na nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo, tutakuwa pia tumepunguza changamoto hiyo ambayo imeelezwa katika kipengele cha sita, changamoto ya masoko na bei ndogo za mazao. Wakulima wetu hawa wanapokuwa wanafanya biashara zisizo rasmi wanapoteza muda mwingi. Walioko barabarani walipaswa wauze yale mafuta na waende wakafanye shughuli nyingine badala yake wamekaa wakisubiri na mafuta yanaweza yakakaa kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo changamoto ambayo imeelezwa iliyopunguza mapato yetu, nayo ni kukosekana kwa ajira. Pamoja na juhudi kubwa ambazo Serikali yetu imefanya za kuongeza ajira lakini bado tunao upungufu mkubwa sana wa ajira katika maeneo yetu. Nitatolea mfano katika Halmashauri yangu ya Singida DC, kwenye sekta ya kilimo peke yake tunao watumishi 23 kati ya 105, kwa hiyo, tuna upungufu wa watumishi 88, sekta ya elimu ya msingi tuna watumishi 831 kati ya 1,629, sekta ya mifugo, watumishi 23 kati ya 84 na sekta nyingine nyingi, tunahitaji walimu wa sayansi 70 katika halmashauri pale, kwa hiyo, utaona zipo nafasi nyingi za ajira. Niiombe sana Serikali itenge fedha kwa ajili ya kuajiri kwenye maeneo haya ambayo yana upungufu mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona madhara yake, kwa mfano kwenye sekta ya elimu. Mkoa wa Singida ni moja ya Mikoa ambayo haijafanya vizuri sana kwenye sekta ya elimu lakini tuna upungufu mkubwa wa walimu kama nilivyowaeleza na walimu wengine wanafundisha madarasa zaidi ya wanafunzi 100 hata wengine kufikia 150. Katika hali hii hatuwezi tukatoa elimu iliyo bora na elimu itakayotosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji katika sekta ya kilimo unahitaji kuongezwa. Sekta ya kilimo ndiyo inayochangia sana katika uchumi wa wananchi wadogo. Serikali hii ya Awamu ya Tano ndiyo imejipambanua kuwa Serikali ya wanyonge ambao zaidi wako vijijini. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali, nimuombe sana Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, utakapokuja na mpango tungetarajia tuone asilimia ngapi ya bajeti ambayo itakuwa imetengwa kwenda kwenye sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi tumekuwa tukiomba kufikia asilimia 10 ya bajeti nzima lakini hapa sasa tunaona bajeti ya maendeleo kwa asilimia 37 lakini tungependa tuone sekta ya kilimo, uvuvi na mifugo imetengewa asilimia ngapi. Tumeomba kwa muda mrefu, Mheshimiwa Dkt. Mpango najua wewe ni msikivu, muende mkafanye utaratibu ili kusudi tuweze kugusa maisha ya wananchi walio wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani ya Chama cha Mapinduzi ilisema, tuna umasikini wa asilimia 28.2, kwa hiyo, tunayo kazi kubwa ya kufanya. Bila kugusa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi hatuwezi kugusa kundi hili kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa miradi ya maji, zipo takwimu zimeonyeshwa hapa, viko vituo vingi ambavyo vimeongezeka na mimi niipongeze sana Serikali kwa kuongeza vituo vingi lakini mashaka yangu makubwa ni katika idadi ya wanufaika ambayo imeelezwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Dkt. Mpango kwenye ukurasa wa 31. Inawezekana katika visima mabavyo tumechimba hasa
vijijini, unaweza ukachimba kisima kimoja, visima viwili, visima vile kama tunaweza tukachukulia kwamba ndiyo vinatoa maji safi na salama kwa kijiji kizima tutakuwa tumefanya makosa makubwa sana. Tunataka tuone ni kwa kiasi gani tumetekeleza Ilani ya CCM ya kuweza kusogeza huduma za maji karibu na wananchi angalau kwa mita 400. Basi utakapokuja Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango tuone tumetekeleza Ilani kwa kiasi gani katika eneo hili la miradi ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika sekta ya elimu. Wananchi wetu wamejitahidi kwa muda mrefu zaidi ya miaka mitano katika kujenga miundombinu ya elimu ikiwa ni pamoja na madarasa, nyumba za walimu na maabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali tufanye juhudi za makusudi kukamilisha miradi hii ya wananchi ambayo imekwishakuanza na kuwatia moyo wananchi wetu waendelee kuchangia kwenye miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya kuchangia uliyonipa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nami fursa ya kuchangia katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza kabisa naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Ofisi yake kwa utendaji mahiri wa kusimamia Serikali. Pia nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa namna anavyoiongoza nchi yetu na anavyopambana na rushwa lakini vilevile kufuatilia kwenye miradi ya maendeleo kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu nitazungumzia mambo machache kama matatu, manne hivi. La kwanza kabisa ni suala la kilimo, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ameelezea sana suala la kilimo na vilevile ameelezea suala la Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo - ASDP II ambao pia umekuwa na vipaumbele vingi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba vipaumbele vyote hivyo vitaweza kuwaondolea wananchi umaskini, kuongeza tija, lakini vile vile kuongeza ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika moja ya mpango mkakati ambalo nataka niongelee mimi ni suala la mafuta ya kula. Katika mpango wa ASDP II umewekwa mpango mkakati wa kuongeza zao la mchikichi hapa nchini ili kukabiliana na tatizo la mafuta ya kula na sisi wote ni mashahidi hata bajeti iliyopita nchi yetu inatumia zaidi ya bilioni mia nne kumi na sita kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo moja, zao hili la mchikichi kama ulivyoona katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu linafanyiwa kazi katika mpango ambao umewekwa katika mpango wa miaka mine. Hata hivyo, tunayo mazao mengine ambayo yenyewe yanaweza yakatoa matokeo ya haraka. Moja ya zao ambayo yanaweza matokeo ya haraka ni zao letu la alizeti ambalo linalimwa kwenye mikoa mingi hususani mkoa wetu wa Singida. Kwa bahati mbaya sana sioni mkakati wowote wa kuweza kuhakikisha kwamba zao hili la alizeti, linawekewa mkakati wa kuhakikisha kwamba tunakamua na kupata mafuta ya kutosheleza. Pengine hatuhitaji hata kuwa na bajeti ya ziada tunachohitaji ni kupunguza bajeti ya kununua mafuta kutoka nje ya nchi na kuhakikisha kwamba tunakamua alizeti tuliyonayo nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyozungumza wakulima wetu wanateseka sana kwa soko la alizeti yakiwemo na mazao mengine, sisi kwa Singida tuna zao la vitunguu kwa mfano, hali ni mbaya sana. Pamoja na mkakati mkubwa wa Serikali wa kujenga viwanda na kwa Mkoa wetu wa Singida kwa taarifa zilizopo tumevuka hata lengo la kuwa na viwanda mia moja, ni zaidi ya viwanda mia mbili, lakini bado tunalo tatizo la soko la vitunguu na soko kubwa sana la alizeti. Mpaka sasa wananchi wanahangaika kuuza alizeti yao, wanahangaika kukamua kidogo kidogo na kuweka kwenye madumu, kusimama barabarani na kupoteza muda mwingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niiombe sana Serikali, ili tuweze kupata matokeo ya haraka katika kuendelea kupoteza fedha nyingi za kigeni kuagiza mafuta, ni vyema Mheshimiwa Waziri Mkuu atakapokuja, tuone mkakati, mahususi kwa ajili ya hili zao la alizeti ili kusudi tuweze kuwasaidia wananchi hawa, kwa sababu hili ni zao ambalo ndani ya mwaka mmoja alihitaji kusubiri kama ulivyo mchikichi. Kwa hiyo, wakati tutakapokuwa tunaendelea kusubiri zao la mchikichi ni vema tukajikita kwenye zao la alizeti na mazao mengine ambayo yanaweza kutoa mafuta na matokeo ya haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika sekta ya maji, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, sekta ya maji hasa vijijini imekuwa kutoka asilimia 58.7 na kufikia asilimia 64.8. Kasi hii naiona bado ni ndogo na wananchi wengi bado hawajapata maji. Kwa mkoa wetu wa Singida sisi tumefikia asilimia 49 peke yake kwa upande wa vijijini. Hali hii ni mbaya sana, sasa niiombe Serikali tumebakiwa na mwaka mmoja wa utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo inatutaka tufikie asilimia 85 kwa vijijini na asilimia 95 kwa mijini, tuiombe sana Wizara ya Maji ambayo sasa hivi imechukua jukumu badala ya Halmashauri, watoe vibali kwa ajili ya miradi ya maji iliyopangwa kwa mwaka wa fedha 2018/2019, ili miradi hiyo itangazwe. Hatutaweza kufikia malengo kama Bunge limetenga fedha, halafu Wizara bado haijaweza kutoa vibali na miradi mingi ya mwaka huu wa fedha unaoendelea haijaweza kutolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la uwezeshaji, nilikuwa najaribu kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, wamefanya kazi, lakini kwa kweli bado kuna changamoto nyingi. Ukiangalia kwenye takwimu ambazo zipo katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ukienda kwenye ukurasa kwa mfano wa 28 kupitia TADB zimetolewa shilingi bilioni 107 ambazo zimewanufaisha wananchi kama milioni moja hivi. Ukijaribu kuangalia maana yake ni kwamba ni sawasawa na mwananchi moja kwa wastani amepata shilingi laki moja na mia saba. Ukienda ukurasa wa 34 kupitia SIDO zimetolewa shilingi bilioni 1.74 ambazo zimenufaisha vikundi au wananchi elfu moja na kumi na tatu kwa wastani wa shilingi milioni moja na laki saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukienda kwenye ukurasa wa 66 kwenye upande wa mafunzo hasa kwa vijana ambao ndiyo tatizo kubwa la nchi yetu, tunasema vijana hapa ni asilimia sitini, lakini vijana ambao tumewapa mafunzo nchi nzima ni vijana elfu thelathini na mbili mia tano na sitini na tatu, hapa tunahitaji kuongeza juhudi. Naomba sana Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye inashughulika na masuala ya vijana, tunaendelea kwa kweli kukuza tatizo hili kama tukienda kwa kasi ya kushughulika na vijana elfu thelathini na mbili peke yake ambayo haifikii hata asilimia 0.1. Kwa hiyo, niombe sana, suala hili lirekebishwe na kuhakikisha vijana hawa wanasaidiwa mitaji, wananchi wetu wanaweza wakakopeshwa kwa wingi, siyo kwa kiwango hiki cha nchi nzima, viwango hivi vingeweza kufaa kuzungumza kama viwango vya mkoa na si viwango vya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine la mwisho nisemehe kwa upande wa umeme. Naipongeza sana Serikali kwa juhudi kubwa, Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imeanza sana kupeleka umeme vijijini, lakini niombe sana juhudi hizi ziongezwe, kwa sababu kwa mujibu wa takwimu bado tuko asilimia 47 pekee kwa nchi nzima. Niseme tu kwa Jimbo langu la Singida Kaskazini mimi ni vijiji 19 peke yake kati ya vijiji 53 ambavyo viko kwenye mradi. Ukichukua kwenye vijiji vyote 84 maana yake sisi ni asilimia 22.6, kwa hiyo, kama wastani wa nchi ni asilimia 47 sisi bado tupo chini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Monko.

MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nami fursa ya kuweza kuchangia kwenye wizara zetu mbili hizi, Wizara ya TAMISEMI pamoja na Utumishi na Utawala Bora. Kwanza kabisa ningependa nianze kwa kutoa shukrani nyingi sana kwa Serikali ya Awamu ya Tano kwa juhudi kubwa ambazo inafanya katika kujaribu kutatua matatizo, kero na changamoto walizonazo wananchi wa Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Singida Kaskazini naishukuru Serikali kwa kutupatia fedha kwenye sekta ya afya ambapo tumepata jumla ya shilingi bilioni mbili na milioni 600 kwenye ujenzi wa hospitali ya wilaya pamoja na vituo viwili vya afya. Vile vile kwenye sekta ya elimu tumepata jumla ya shilingi bilioni moja milioni tisa na laki sita. Hizi zote zimekwenda kutatua changamoto mbalimbali kwenye jimbo letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru pia Serikali tulipata fedha za Mfuko wa Jimbo shilingi milioni hamsini na tisa na laki moja ambazo kwa kweli zimekwenda kwa kiasi kikubwa kuchangia changamoto za ujenzi kwenye kata zetu zote 21. Kwa hiyo naishukuru sana Serikali kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Singida Kaskazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi kubwa ambazo Serikali yetu imefanya, ziko changamoto mbalimbali ambazo ningependa nijaribu kuzisemea hasa nikianza na sekta ya elimu. Kwenye sekta ya elimu Mkoa wetu wa Singida bado haufanyi vizuri sana katika masuala ya matokeo, lakini ziko changamoto kadhaa ambazo zinachangia kutokufanya vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya changamoto hizo ni miundombinu. Kazi kubwa ya Serikali imefanyika na hasa kwenye jimbo langu nami nilipata pia shilingi milioni 300 kwenye kujenga maboma 24. Naipongeza sana Serikali kwa hilo. Kwa shule za msingi peke yake yako maboma 68 ambayo wananchi wamekwishayaanzisha kwa muda mrefu na bado hayajakamilika mpaka leo. Ukienda kwenye shule za sekondari, uangalie kwenye shule za sekondari kwenye Jimbo langu pale maboma zaidi ya 69 ya maabara peke yake hapo hujagusa nyumba za Walimu, mabweni, matundu ya vyoo na vitu kama hivyo. Kwa hiyo bado tunayo changamoto kubwa kwa kweli kwenye kuwekeza, Serikali kuwekeza ili kuweza kusaidia juhudi hizi za wananchi. Maboma haya yameanzishwa mengine yana muda mrefu

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa sekta ya afya, ninayo maboma kwa mfano kwenye Kata ya Ngimu liko jengo ambalo lilianzishwa na wananchi kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita na mpaka leo halijaweza kukamilishwa. Ukienda pale Kata ya Makuro vile vile na sasa hivi wananchi wengi wameanza sasa kwenye kata nyingine vile vile, Kata ya Msisi wameanzisha ujenzi wa jengo la kituo cha afya, ukienda Kinyajigi pale wameanzisha. Juhudi hizi za wananchi zinahitaji kuungwa mkono na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ombi langu kwa Serikali ni kwa Serikali kuongeza bajeti hii ya kukamilisha maboma ambayo tayari wananchi wamekwishayaanzisha kwa nyakati tofauti na wamefanya kazi kubwa ili tusiwakatishe tama. Tukumbuke kwamba uwezo wa kuyamaliza majengo yale haupo kwa wananchi kwa sasa kwa sababu miradi mingi ya Serikali ambayo inakwenda iwe ni hospitali za wilaya, vituo vya afya, majengo ya shule wananchi wanatakiwa kuchangia asilimia 20 ya maeneo hayo. Kwa hiyo niombe sana Serikali tuongeze bajeti ya maendeleo katika kukamilisha maboma haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kubwa ambalo linatoa duni kwa kweli kwenye sekta ya elimu lakini vile vile na huduma za afya ni watumishi tulionao kwenye sekta zetu. Nitatolea mfano wa Jimbo langu la Singida Kaskazini, kwenye sekta ya shule ya msingi peke yake tunahitaji waalimu zaidi ya 1,733 hivi tunavyozungumza tuna waalimu 860 sawa sawa na asilimia 49.6.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye sekta nyingine ukienda kilimo unakuta watumishi wako 16, kwenye vijiji 84 na kata 21, ukienda kwenye shule za msingi upungufu wa Walimu na maeneo mengine. Ni kweli Serikali kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri Serikali ilitoa ajira na kwa mwaka uliopita ajira 4,811 za Walimu. Idadi hii ya ajira iliyotoka kwenye sekta ya elimu peke yake ni ndogo sana. Ukijaribu kuangalia kwenye takwimu ambazo zipo za usajili wa wanafunzi kwa mwaka wa jana, mwaka huu ambao ndiyo tunaendelea nao peke yake wamesajiliwa wanafunzi wa elimu ya awali na shule za msingi kwa zaidi ya wanafunzi 2,900,000 ambao peke yake kwa idadi hiyo ilitakiwa wapatikane Walimu ambao watahudumia wanafunzi hao Walimu zaidi ya 65,550.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaona karibu asilimia 36 ya Walimu wote waliojiriwa mwaka jana wanakwenda kufanya kazi tu ya kuelimisha wale wa darasa la awali na darasa la kwanza. Kwa hiyo bado tunalo tatizo kubwa, niombe sana Wizara ya Utumishi pamoja na TAMISEMI ambazo zote bahati nzuri ziko chini ya Ofisi ya Mheshimiwa Rais, waangalie namna ya kuweza kuongeza ajira kwa watumishi hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo twende pamoja na maslahi ya watumishi ambao kama tulivyosema kwa zaidi ya miaka mitatu sasa bado watumishi hawajaongezewa mishahara. Idadi ya Walimu tulionao tukumbuke hawa ni wale ambao tunao kwenye takwimu, wengine wako masomoni, wengine wana mashauri mbalimbali, ninayo, naweza nikatolea mfano wa Shule moja ya Msingi Mwasauya ambayo ina Walimu saba, watatu hawapo, wako masomoni, mmoja tayari ana mashauri, wanaoingia darasani ni Walimu watatu kwa shule nzima yenye wanafunzi zaidi ya 400.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali hii hatutegemei kuwa na miujiza sana ya kufanya vizuri. Kwa hiyo, niombe sana hasa kwa mikoa hii ambayo haifanyi vizuri kama Mkoa wa Singida tupewe kipaumbele cha kupewa watumishi wa kutosha na kuwapunguzia matatizo Walimu hawa ambao wanafanya kazi katika mazingira magumu. Madarasa bado hayatoshi na wengi uwiano kule kwetu unafika mpaka kwa Mwalimu mmoja wanafunzi mpaka zaidi ya 100. Kwa hiyo, naomba sana Wizara iangalie suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la TARURA tunawapongeza sana. Tumeunda Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini lakini nami pia nilikuwa najaribu kuangalia katika mgawanyo wa fedha za TARURA ambao wamekwenda kwenye bajeti ya mwaka huu, yako maeneo mengi ambayo kwa kweli tumepata fedha kidogo. Mkoa wa Singida peke yake tumepata bilioni nne na milioni mia tano, lakini ziko halmashauri hasa kwenye majiji, manispaa moja inapata zaidi ya bilioni saba, zaidi ya bilioni sita wakati Mkoa mzima wa Singida ni bilioni nne na milioni mia tano peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana ndugu Mheshimiwa Jafo, mjaribu kuangalia, tunayo matatizo makubwa sana kwenye barabara zetu kule vijijini na tukiendelea kutoa fedha kiasi kidogo kiasi hiki kwa kweli wananchi wetu watapata matatizo sana. Mimi kwenye jimbo langu yako maeneo mengi, iko barabara ambayo tuliiomba kwa Mheshimiwa Rais kutoka Kinyeto – Kinyagigi – Meria inakwenda mpaka Sagara kule lakini naona haijatengewa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hatujatengewa fedha kwenye baadhi ya madaraja na maeneo mengine, kwa mfano tunalo Daraja la Songa, Kinyeto - Ilongero pale Ntambuko lakini tuna eneo la Mgori – Kikio, haya ni maeneo sugu ambayo tunayo lakini ukienda kwenye fedha ambazo sisi tumetengewa kwenye maeneo hayo ambayo ni ya matengenezo ya dharura sisi maeneo korofi hatujatengewa fedha hata senti moja lakini ukienda pia kwenye marekebisho pale hatujatengewa hata kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana muende mkafanye review ili pia Halmashauri ya Singida DC waweze pia na wao kupata fedha zitakazoweza kutosheleza. Barabara hizi tunazozungumzia ni muhimu sana kwa uchumi wa Jimbo la Singida Kaskazini.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Monko.

MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda sana niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna ambavyo imewekeza kwenye Wizara hii na inavyojitahidi kutatua matatizo yaliyopo katika subsectors hizo tatu ambazo nimezitaja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, pamoja na Manaibu Waziri kwa kazi kubwa ambayo wanafanya na kwa namna ambavyo wanajitahidi sana katika kujibu hoja zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi kubwa ambazo zinafanyika ningependa nichangie katika maeneo machache katika changamoto ambazo tunaziona kutokana na hotuba ya Mheshimiwa Waziri ambayo ameitoa hivi leo asubuhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi kubwa ambayo imeshafanyika, katika hotuba ya Waziri ameainisha baadhi ya maeneo ambayo yamefanyiwa kazi, yakiwemo ujenzi wa barabara kuu, lami lakini barabara za Mikoa kwa ujenzi wa lami na vilevile kwa ujenzi kwa kiwango cha changarawe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia vizuri, katika bajeti ya Mheshimiwa Waziri kazi kweli imefanyika, lakini kwa kweli nimuombe Mheshimiwa Waziri tunahitaji kuongeza kasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kuongeza kasi kubwa kwa sababu kiwango cha barabara ambacho kimekwisha kutengenezwa mpaka kufikia mwezi wa tatu mwaka huu, kwa barabara kuu ni asilimia 31.9 peke yake ambazo zimekwisha kukamilika kwa mujibu wa takwimu ambazo tumezipata kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ukienda kwenye barabara za Mikoa, hali bado iko vilevile, kwa upande wa barabara za lami, tumefikia asilimia 20 na upande wa barabara za changarawe tumefikia asilimia 12. Kwa hiyo, kasi hii hairidhishi sana, pamoja na kwamba tunafanya mambo makubwa, juhudi kubwa zinafanyika lakini kasi hii ni ndogo na maana yake ni kwamba maeneo mengi ambayo yalikuwa yamepangwa kwenye bajeti iliyopita mpaka sasa bado hayajafanyiwa kazi na ukizingatia kati ya mwezi wa nne na mwezi wa sita tumebakiwa na sehemu chache sana, au katika miezi mitatu hii hatuna uwezo wa kukamilisha kwa ukamilifu wake maeneo ambayo yamesalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda pia hata katika ukarabati, hata katika ukarabati utaona tumeweza tu kukarabati barabara zenye urefu wa km 10,000, 968,000 kati ya 34 ambazo zilikuwa zimekusudiwa. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali kutoa fedha kwa ukamilifu ili kusudi miradi ambayo tulikuwa tumeshaipanga katika bajeti iliyopita ya mwaka 2018/2019 iweze kukamilika na tunapokuwa tunapanga kwenye bajeti mpya tuwe na uhakika kwamba zile ambazo tutapitisha kwenye bajeti hii ya mwaka huu wa 2019/2020 tunaweza basi tukapata hizo fedha na zikafanya kazi ambayo imekusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu tunakuwa na mashaka mara nyingi kwamba tunapitisha bajeti hapa lakini baadaye fedha zisipotoka miradi ile haikamilik. Nikitolea mfano wa barabara inayotoka Singida, inayokwenda Hydom mpaka Karatu, barabara hii imekuwa kwa muda mrefu kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa zaidi ya miaka saba, imekuwa ikiahidiwa. Na niseme tu mpaka sasa tunashukuru kwamba tumeona kwamba kuna fedha zimetengwa kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambayo inaanzia pale Singida kwenda mpaka Haydom, na zingine kutoka hydom kwenda karatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niiombe sana Serikali, mara, mwaka wa fedha utakapoanza ni vyema sana shughuli hii ikaanza mara moja ili katika mwaka unaofuata tuweze kutengewa fedha za kujengwa kwa kiwango cha lami kwa kuwa barabara hii ni muhimu sana, hasa kwa wananchi wa Mkoa wa Singida na Mkoa wa Manyara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wote ambao wanategemea kusafirisha mazao yao, lakini barabara hii pia ina huduma nyingi hasa huduma za afya kwa sasa tunajenga Hospitali ya Ilongero pale, ambayo wananchi wengi wataitegemea kupata rufaa kutoka kwenye vituo vya afya, lakini tunayo Hospitali ya Haydom, tunayo Hospitali ya Nkungi na maeneo mengi ambayo sasa ya uzalishaji ambayo yanategemea sana uwepo wa barabara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambasamba na hilo, ipo ahadi ya Rais aliyoitoa pale Mkoani Singida mwaka jana mwezi wa tatu alipotembelea Mkoa wa Singida katika barabara inayotoka Singida mjini, Kinyeto, Merwa inakwenda mpaka Msange inakwenda kuunganisha na barabara kuu inayokwenda Arusha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Wizara hii ikishirikiana na TARURA kutoka TAMISEMI watafuta fedha, watenge fedha ili kusudi upembuzi yakinifu na usanifu wa kina uanze mara moja kwa barabara hii ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais ili wananchi wa Jimbo la Singida Kaskazini waweze kunufaika na uwepo wa barabara ya lami, waweze kusafirisha mazao pamoja na wao wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda katika suala la mawasiliano, kama walivyosema Waheshimiwa Wabunge wenzangu mwaka jana hapa tulitoa orodha ndefu sana, kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge ya maeneo ambayo bado hayana mawasiliano ya kutosha na mimi Jimboni kwangu yako maeneo mengi. Ziko Kata tano zina matatizo makubwa kabisa ya usikivu wa mawasiliano, na wawekezaji hawa wa Makampuni haya hawajaweza kuwekeza kule kwa sababu hawawezi kupata faida kutokana na uchache wa watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niiombe sana Serikali iweze sasa kutumia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote kuhakikisha maeneo haya ambayo hayana mawasiliano yaweze kupata mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la mizani, nimeona kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wameeleza, lakini niisemee mizani ambayo iko katika barabara ya kutoka Singida kwenda Arusha, tunayo mizani pale Mughamo lakini uko mwingine uko Mkoa wa Manyara, mizani hii inafanya kazi masaa kumi na mbili ya mchana peke yake. Mizani hii haina umeme, mizani hii hazina maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hatuna uwezo wa kulinda barabara zetu kwa masaa ishirini na nne, kwa hiyo, niiombe sana Serikali kujaribu kuwekeza katika maeneo haya, kwa sababu wako watu ambao sasa wanakuwa wanasubiri Watumishi wakishaondoka ile saa kumi na mbili. Wanaanza kupitisha magari yenye uzito mkubwa na matokeo yake barabara zinaharibika na pia Serikali inashindwa kudhibiti hali hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo sio kupata fedha za tozo, lakini lengo ni kulinda barabara zetu ili tusiendelee kujirudia na mtaona barabara ile bado ni mpya lakini tayari imekwisha kuanza kupata maeneo ambayo kwa kweli yana upungufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niiombe sana Wizara, kwa unyenyekevu mkubwa, iko pia barabara inayotoka Singida kwenda Ilongero, kwenda Ngamu hii ni barabara ya Mkoa, na inaenda kuunganisha tena kwenye Mkoa wa Manyara. Barabara hii ni muhimu sana kwa wananchi wa Mkoa Singida na Manyara, niombe sasa ilikuwa imetangazwa km 12.6 za ujenzi kutoka Singida kuelekea Ilongero. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mwaka jana ilipotangazwa mwezi wa kumi na moja mpaka sasa, bado hatua za manunuzi hazijakamilika. Nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, aweze kufatilia jambo hili, ili ujenzi wa kiwango cha lami katika barabara hiyo uweze kuanza mara moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja ya Waziri tuweze kupata fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi yote ambayo imepangwa kwa bajeti hii ya mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nami nafasi ya kuweza kuchangia katika mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka wa 2020/2021. Awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, Naibu Waziri pamoja na timu yote na niipongeze Serikali kwa ujumla wake ikiongozwa na Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa namna ambavyo imekuwa ikitekeleza Mpango wa Maendeleo katika bajeti iliyopitia na bajeti hii ambayo inaendelea sasa ya mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona yako mafanikio mengi katika miradi mingi ya kielelezo ukiwepo Mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge au bwawa la Mwalimu Nyerere, tumeona kwenye standard gauge, ununuzi wa ndege, uboreshaji wa miundombinu, lakini zaidi sana katika sekta ya afya tumeona juhudi kubwa sana za ujenzi wa hospitali za wilaya, lakini na vituo vingi vya afya ambavyo kwa kweli vitakwenda kuboresha maisha ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi pia tumeona mchango wa Serikali hii katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali ambayo yameongezeka kwa kiasi kikubwa na inatusaidia sana sisi katika kutekeleza mipango, ukizingatia kwamba mipango mingi sasa ya Serikali tunaipanga kwa kutumia fedha zetu za ndani. Mfano, katika mapendekezo haya ambayo yapo, katika fedha za mpango wa maendeleo zaidi ya bilioni 12.6 za bajeti ya maendeleo zaidi ya trilion 10.1 zitakuwa sasa zinatokana na fedha zetu za ndani. Kwa hiyo tunaipongeza sana Serikali kwa juhudi kubwa ambayo imefanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichangie katika sekta mbalimbali katika kuboresha Mpango wetu wa Maendeleo wa mwaka 2020/2021, nikianzia na sekta ya afya, kama nilivyosema juhudi kubwa imefanyika katika Serikali hii ya Awamu ya Tano, lakini niombe sana katika Mpango huu kazi tulioifanya kwa mfano kwenye vituo vya afya, pamoja na wingi wa vituo vya afya tulivyofanya ukilinganisha na idadi ya Watanzania zaidi ya milioni 55 waliopo sasa, juhudi kubwa bado inatakiwa katika eneo hili. Pia tujue kwamba bila kuwa na afya njema hata kazi zetu na mipango yetu ya maendeleo haiwezi kutufikisha vizuri. Kwa hiyo niiombe sana Serikali na Mheshimiwa Waziri waangalie namna ambavyo wataongeza vituo vya afya. Ushauri wangu katika hili ni kwanza kukamilisha maboma ambayo yamekwishaanzishwa na wananchi wenyewe. Awamu zilizopita ikiwemo Awamu ya Nne ya Mheshimiwa Kikwete tulianza, wananchi wamejitolea sana katika ujenzi wa maboma ya vituo vya afya na maboma mengine kwenye sekta ya elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya afya, kwa mfano katika jimbo langu, yapo boma katika Kata yetu ya Ngimu lakini nyingine Makuro ambayo yamekaa kwa muda ya miaka 10, wananchi hawa wametoa nguvu zao, lakini mpaka leo maboma hayo hayajaweza kukamilika na kwa kweli wananchi wamekuwa wamezidiwa na ukamilishaji wa maeneo hayo kutokana na mipango mingi ambayo tunawapelekea, ukizingatia kwamba kwa kila fedha za Serikali zinazokwenda asilimia 20 ya nguvu za wananchi inahitajika huko. Kwa hiyo niombe sana Serikali ifanye mpango wa makusudi kama ilivyofanya kwenye sekta ya elimu tuweze kukamilisha maboma haya ambayo yapo katika nchi nzima na wananchi walishajitolea katika kuyajenga ili kusudi tuweze kuboresha huduma za . Tunahitaji afya bora na hasa tunahitaji kuzuia vifo vya wa kina mama na watoto wakati wa kujifungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye sekta ya maji; sekta hii ni muhimu sana, kwa kweli tunao uwezo wa kufanya kila kitu, lakini tunaweza tukashindwa kuishi bila maji. Tumewekeza sana katika maeneo mengi, tumewekeza vizuri katika miundombinu, sasa hivi tunaendelea kuwekeza katika miundombinu ya umeme, tunaendelea kuwekeza katika maeneo mengine, lakini maji ambalo ni hitaji la msingi la maisha ya binadamu kwa kweli bado tumekuwa na nguvu kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia katika bajeti ya maji, imekuwa ni kidogo sana na haina uwezo wa kututoa hapa tulipo. Tunajua Ilani ya Chama cha Mapinduzi inataka angalau kwa upande wa vijijini tufikie asilimia 85 mpaka kufikia mwaka unaokuja. Sasa hivi tunaongelea chini ya asilimia 65, utaona kazi hiyo ni ngumu, kazi hiyo ni kubwa, kwa hiyo niombe sana, zitafutwe fedha za maji. Mwaka jana tulikuja na ombi hapa la kuongeza shilingi 50, lakini ombi hilo halikukubaliwa na sisi hatupingani na hilo, lakini madhali vinaweza vikapatikana vyanzo vingine, suala la maji ni la muhimu sana wewe mwenyewe ni shahidi, Mheshimiwa Rais alipotembea kila mahali alipokwenda ni maji, maji, maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji linawagusa sana akinamama ambao ndio wazalishaji wakubwa na wanatumia muda mwingi sana kwenye kutafuta maji na tunaona kwamba takwimu tunazokuwa nazo zinaweza zisiwe za kweli kwa sababu tunadhani kwamba kisima kimoja kinakwenda pale kama kinasema kinahudumia wananchi 250 au wananchi 500 au 600, hizo ndizo takwimu tunazokuwa nazo, lakini utakuta wengine wapo zaidi ya mita 400 ambayo ndiyo sera yetu au Awamu hii ilikuwa imejiwekea, kusogeza huduma karibu na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niiombe sana Serikali, ukienda katika miradi ya vieleleze Sekta ya Maji sio sekta ya muhimu, sio sekta ya kipaumbele. Sasa hili halitupi sisi nafasi ya kuweza kutenga fedha nyingi kwenye kuboresha miundombinu ya maji. Niombe Mheshimiwa Waziri tulipe kipaumbele cha kwanza kabisa sasa hivi kwenye bajeti inayokuja hii ya mwaka 2020/2021 ili tuweze kuwatua akina mama ndoo kichwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata walioko mijini bado hawajapata maji ya kutosha, bado kumekuwa na urasimu mkubwa. Ukiangalia hata katika Mkoa wa Dar es Salaam shida ya maji bado ni kubwa, katika majiji yote shida ya maji bado ni kubwa. Kwa hiyo niombe sana Wizara hii iangalie na niombe sana Sekta ya Maji iwe ni moja ya sekta za kipaumbele katika Taifa letu. Tunaweza hata tukapunguza kwenye maeneo mengine; tunaweza tukaishi bila lami, tunaweza tukaishi bila miundombinu bora huko lakini hatuna uwezo wa kuishi bila maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine lipo katika kilimo; Sekta ya Kilimo inaajiri zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania, wengi wao – asilimia 90 – wanatoka vijijini ambako mimi ni mwakilishi wao, lakini pia wako wakulima ambao wanaishi mijini. Bado mpango wa Serikali haujatenga fedha za kutosha katika kuboresha Sekta ya Kilimo, bado tunahitaji kuongeza fedha, tunahitaji kuongeza uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika mpango ambao umewasilishwa sasa, fedha nyingi zinazotegemewa ni hizi za mpango wa kuendeleza Sekta ya Kilimo ya Awamu ya Pili (ASDP II). Fedha hizi hazitoshi. Fedha hizi zina maeneo maalum, yako mazao mengine ambayo hayawi-covered kabisa kwenye mpango huu. Mpango huu wa ASDP II wenyewe umelenga zaidi kwenye mazao yale ya kimkakati ambayo utakuta ni korosho, pamba, kahawa, chai.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa yapo mazao mengine ambayo kwa kweli yanahitaji yapewe kipaumbele; tuna mazao ya mafuta kama ufuta, alizeti mchikichi, karanga na maeneo mengine. Haya yanahitaji kupewa kipaumbele kwa sababu tunajua kwamba nchi yetu inatumia fedha nyingi, zaidi ya bilioni 410 katika kuagiza mafuta ya kula kila mwaka. Fedha hizi ni nyingi sana, tusipowekeza katika kilimo hatuwezi kuwasaidia wananchi wetu. Huku ndiko wananchi wetu walio wengi tunakotoka sisi wote waliko. Kwa hiyo, niombe sana Sekta ya Kilimo ipewe umuhimu na kipaumbele cha kwanza pia ili kuweza kuboresha maisha ya wananchi wetu kule vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukumbuke kwamba nchi yetu sasa tunakwenda na tunakwenda kwenye uchumi wa kati ambao utaongozwa na uchumi wa viwanda. Viwanda hivi vitahitaji malighafi za kutoka mashambani, viwanda hivi vitahitaji malighafi za mifugo, viwanda hivi vinahitaji malighafi kutoka kwenye uvuvi. Sasa tusipowekeza katika maeneo haya tutajikuta kwamba hatuwezi kufikia malengo yetu vizuri na ndoto ya Mheshimiwa Rais wetu ya kutufikisha uchumi wa kati 2025 haitaweza kutimia kwa sababu ya uwekezaji mdogo katika Sekta ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapozungumzia Sekta ya Kilimo ni pamoja na mifugo vilevile. Tumeona zipo changamoto nyingi, na niipongeze sana Wizara ya Mifugo, sasa hivi wamekuja na utaratibu wa uhimilishaji wa mifugo ambao unawasaidia wafugaji wetu kuwa na mazao bora zaidi.

Kwa hiyo, niombe sana uwekezaji uongezwe katika sekta hizi ikiwa ni pamoja na Sekta ya Uvuvi. (Makofi)

MWENYEKITI: Kengele ya pili imegonga Mheshimiwa.

MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. JUSTIN J MONKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami ya kuchangia katika hotuba ya Bajeti hii ya Wizara ya Kilimo. Natambua kabisa kilimo kwa nchi yetu ya Tanzania ni sehemu muhimu sana kama walivyosema Waheshimiwa Wabunge wengine waliotangulia ndiyo inayoajiri zaidi ya wananchi asilimia 65 na kuhakikisha kwamba inaleta chakula kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukijaribu kupitia katika Bajeti hii ya Kilimo ni ukweli usiopingika kwamba fedha zilizotengwa kwenye Bajeti ya kilimo ni ndogo sana, ni chache sana. Tunajua liko tatizo la Kibajeti na maeneo mengi ni ya kipaumbele, lakini tuiombe Serikali sana ifanye maamuzi ya makusudi kuongeza fedha katika Bajeti hii ya Kilimo. Kwa utaratibu huu tunaokwenda, hizi bilioni mbili, bilioni mia mbili na hamsini na tatu, kwenye Sekta hii yote ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika hazitoshi kututoa hapa tulipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunazungumzia wananchi zaidi ya asilimia 65 na ukiangalia kwenye fedha za maendeleo, huko tena ndiyo kumekuwa hakufai zaidi, kwa sababu fedha nyingi ambazo zimetengwa kwenye upande wa maendeleo zinatoka kwa wafadhili, tunategemea wafadhili kwa zaidi ya asilimia 38, ukienda kwenye umwagiliaji zaidi ya asilimia 91 ya fedha zilizopangwa kwenye umwagiliaji zinatoka kwa wafadhili wa nje, siyo mapato yetu ya ndani, wakati sisi, kwenye Sekta yenyewe ya Kilimo inazalisha kwa zaidi ya asilimia 28 ya pato la Taifa. Kwa hiyo, naiomba sana, Serikali kwa utaratibu huu tunaokwenda nao kwa kutumia fedha za nje, tunaweza tukapata fedha kwa wakati ambao siyo muafaka na matokeo yake kilimo chetu kikaendelea kudidimia na Wizara hii isifanye vizuri.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine kwenye upande wa umwagiliaji, kwa kweli Sekta ya Umwagiliaji imetengewa fedha kidogo sana shilingi bilioni thelathini na saba. Ni fedha kidogo sana ukiangalia na bilioni ishirini na tisa ndiyo zinapelekwa kwenye upande wa maendeleo. Nimejaribu kuangalia hakuna mradi wowote katika Mkoa wa Singida, ambao upo kwenye umwagiliaji, iko miradi michache sana ambayo itatekelezwa kwa fedha hizi kidogo ambazo zipo. Sasa, sisi tunataka kuongeza uzalishaji, wakati huo huo, tunahangaika sana na kujaribu kuona namna ambavyo tunaweza tukahifadhi mazao mengine. Nadhani tungewekeza kwenye Kilimo cha Umwagiliaji na tukawa tunalima mwaka mzima, hata tusingetumia nguvu kubwa sana katika kuhifadhi mazao ambayo tutayahitaji wakati ambao wananchi wanatafuta chakula wakati ambao kimehifadhiwa kwenye maghala, ambao wakati mwingine yako mbali sana na maeneo waliyoko wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nataka niombe, Serikali ifanye juhudi ya makusudi, wamesema Waheshimiwa Wabunge wenzangu, kwenye upande wa umwagiliaji zipatikane fedha angalau zaidi ya bilioni mia tano ambazo zinaweza zikaenda kwenye maeneo mengi ya kuhuisha pamoja na kujenga miundombinu. Kule katika Jimbo langu, yako mabwawa mengi, liko Bwawa la Suke, liko Bwawa la Mgori, liko Masoghweda, liko Kisisi, liko Ntambuko, yako ni maeneo mengi ambayo yanafaa kwa kilimo cha umwagiliaji hata na miradi ya maji. Hata hivyo, hatujaona kwamba tumechukua hatua za makusudi za kutumia maji haya ambayo tayari Mungu ameshatupa bure ili kuweza ku- develop kilimo cha umwagiliaji na kuongeza uzalishaji wetu kupitia huku.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni upande wa masoko; naipongeza na kuishukuru sana Wizara kwa kuweka Kitengo cha Masoko katika Wizara hii ya Kilimo. Kwa sababu tumekuwa tukitegemea sana Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, ambao wakati mwingine hawajui hata ubora wa bidhaa ambazo Wizara ya Kilimo...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. JUSTIN J MONKO: Mheshimiwa Spika, nakushuru sana na naunga mkono hoja, lakini waangalie sana suala la umwagiliaji. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa na mimi nafasi ya kuchangia katika bajeti hii ya Wizara ya Fedha. Nianze kwa kuipongeza sana Wizara kwa bajeti nzuri ambayo wametuletea hapa na nina imani kubwa akiitekeleza hivi wanavyosema, wataweza kututoa hapa tulipo.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge waliotangulia wameanza kuzungumza mengi na mojawapo limekuwa ni Deni la Taifa na mimi niiombe tu Wizara kwa sasa Deni la Taifa kweli pamoja na kwamba limeongezeka, na Mheshimiwa Simbachawene amelielezea vizuri sana kwa sasa lakini tunaona kwamba deni hili linaendelea kuongezeka pamoja na kwamba inafanya miradi mikubwa ambayo kwa kweli tunaihitaji na ni miradi ya kimkakati ya nchi hii.

Mheshimiwa Spika, sasa wito wangu kwa Wizara ni kujaribu kuangalia kwamba deni hili liwe stahimilivu kama wanavyoendelea kusema kwa sababu ukiangalia sasa zaidi ya trilioni 50 wakati sisi uwezo wetu tunakusanya mapato ya ndani kwa trilioni 20, kidogo linakuwa na mashaka na hasa kwa sisi ambao siyo wachumi. Kwa hiyo, niiombe sana Wizara itupie macho kuhusiana na suala hili la Deni la Taifa na kuangalia tusijetukateleza.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni ukusanyaji wa mapato. Tunaipongeza sana Wizara wamefanya kazi nzuri ya kukusanya mapato na mimi nilitaka baadaye Mheshiwa Waziri atakapokuja, mwaka jana tulipitisha hapa, tulitoa msamaha wa kodi kwa mfano kwenye kulipia magari na nini. Nilitarajia sana kuweza kuona kwamba tuone msamaha huo uliotoka, mapato ambayo yalikuwa yamekusanywa yametusaidia kuongeza mapato kwa kiwango gani, lakini sijaliona hilo. Kwa hiyo, tunataka tuone namna ambavyo Wizara hii inaweza ikasimamia mapato hayo ambayo yanatusaidia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali na hata ulipaji wa pensheni, nyongeza hata za mishahara pamoja na mambo mengine ambayo yanatokana na kuongezeka kwa mapato.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninataka nimuombe Waziri atakapokuja tuweze kujua, kitu ambacho Waheshimiwa Wabunge walipitisha mwaka jana hapa kimeleta manufaa gani.

Mheshimiwa Spika, na labda kazi kubwa ambayo Wizara inatakiwa kufanya sasa ni kujaribu kuendelea kuboresha mazingira ya ukusanyaji wa kodi, hasa kwenye maeneo mengi ili wananchi wengi waweze kulipa kodi. Bado wako wananchi ambao wanaendelea kukwepa kodi kwa sababu wakati mwingine mazingira ya ulipaji au kodi zenyewe siyo rafiki. Kwa hiyo, niombe sana Wizara iweze kuboresha kwenye maeneo haya ili wananchi waweze kulipa kodi inavyostahili.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la miradi na hasa miradi ya PPP; hotuba ya Mheshimiwa Waziri imeeleza vizuri sana, na kwamba sasa hivi wana mikakati ya kuweza kuzisaidia Halmashauri ili ziweze kuongeza uwezo wake wa ukusanyaji wa mapato. Kwa hiyo, niombe Wizara iweze kuwasaidia.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu tukiangalia, kwa mfano katika Halmashauri yangu ya Singida DC tuna miradi ambayo tumekwishakuiandika lakini imekwenda kwa muda mrefu na hatujapata fedha. Tumeomba kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa soko pale Njiapanda ya Meriya na andiko hili limekuja muda mrefu, limepita katika hatua mbalimbali katika ngazi za mkoa na limekwishakwenda huko Wizarani, lakini katika bajeti hii sijaona kama limepata kibali cha kupata fedha.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ile bado ni duni sana, mwaka uliopita tulikusanya chini ya shilingi bilioni moja. Kwa hiyo, tunahitaji sana fedha hizi kwa ajili ya miradi hii mkakati ili tuweze kuongeza uwezo wetu na kuweza kuwasaidia wananchi. Kwa sababu mapato ya ndani ya halmashauri yanategemewa sana na vijiji vyetu, yanategemewa sana na akina mama, vijana na walemavu na yanategemewa sana na Waheshimiwa Madiwani katika kutekeleza miradi mbalimbali kule kwenye Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe sana Wizara ijaribu kuliangalia suala hili, ipitie na kama liko tatizo la maandiko ambayo tunaandika kutoka kwenye Halmashauri basi Wizara itusaidie ili maandiko haya na yenyewe yaweze kukidhi vigezo.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Justin Monko.

MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza Serikali na Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa juhudi kubwa ya kuwaletea wananchi miradi ya maji katika maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri bado tunalo jukumu kubwa mbele yetu katika kufikia malengo ya mwaka 2020 ya kutoa huduma ya maji vijijini kwa asilimia 85. Katika Jimbo langu la Singida Kaskazini tunalo tatizo kubwa la maji katika vijiji vyetu na kuwafanya wananchi kuhangaika kutafuta huduma ya maji. Hata katika baadhi ya maeneo yaliyo na vyanzo vya maji, maji hayo siyo safi na salama kwa matumizi ya binadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishukuru sana Serikali kwa kuliweka Jimbo la Singida Kaskazini katika mradi wa matumizi ya teknolojia ya nishati jadidifu ambao tayari umeshaanza katika vijiji vya Ghalunyangu na Mughunga. Pia kwa kutengea fedha shilingi 1,644,481,000 kwa ajili ya miradi ya maji vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, vipo vijiji na vitongoji katika Kata ya Mughunga ambavyo ni kijiji cha Nduamughanga na vitongoji vya Mukulu ambavyo vipo umbali wa kilometa 25 kutoka makao makuu ya kijiji. Maeneo haya hayana huduma ya maji safi na salama. Pia vipo vijiji vya Lamba, Sughana, Misuna, Gairo na vingine vingi katika Jimbo la Singida Kaskazini.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali kuongeza fedha za miradi ya maji ili kupunguza tatizo hili na kufikia malengo tuliyonadi kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa kilimo cha umwagiliaji, ipo miradi mingi ambayo inafaa kwa umwagiliaji ambayo tayari Wizara imeainisha na niombe kupatikana fedha za kutekeleza miradi hii sasa ili iweze kuongeza tija. Miradi ipo maeneo ya Ikhanuda, Itanika, Ngimu, Songambele, Songa, Ndang’onyo na Sagara. Lipo pia Bwawa la Msange ambalo utafiti ambao umeshafanyika na miradi bado haijaanza. Nimuombe Mheshimiwa Waziri aweze kutembelea jimbo langu na kujionea miradi ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 144 kwenye ukarabati wa mabwawa, inaonesha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Singida inatengewa fedha, lakini bwawa hili na vijiji vilivyoainishwa vipo katika Wilaya ya Ikungi, Jimbo la Singida Mashariki. Nimuombe Mheshimiwa Waziri wafanye marekebisho ili yaingizwe mabwawa na vijiji vya Jimbo la Singida Kaskazini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa namna anavyotekeleza miradi ya maendeleo inayowagusa wananchi kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Mheshimiwa Selemani Jafo, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na viongozi wengine wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utawala bora, Wizara imetoa mafunzo kwa watendaji na Wakuu wa Wilaya ili kuboresha utoaji huduma kwa jamii. Ili kuendelea kutoa huduma bora na kutatua kero za wananchi, naiomba Serikali yangu sikivu iwaelekeze watendaji na wakuu hao waliopata mafunzo, kutoa mafunzo kwa walio chini yao na pia katika ngazi za chini ili viongozi hao na wananchi waweze kujua haki na wajibu wao katika kulitumikia Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalo tatizo katika Jimbo langu la Singida Kaskazini ambapo vipo Vijiji viwili vya Nduamughanya na Sagara vikishindwa kutoa huduma bora kutokana na jiografia ya maeneo ya vijiji hivi. Kijiji cha Nduamughanya kilichopo Kata ya Mughunge kina vitongoji vitatu ambavyo vipo umbali wa kilometa 23 kutoka Makao Makuu ya Kijiji vilitengwa na Msitu wa Hifadhi wa Mgori una kilometa 26 ukipita Handa katika Wilaya ya Chemba. Aidha, Kijiji cha Sagara pia kina vitongoji vitatu vilivyo kilometa nne kutoka Makao Makuu ya Kijiji na vimetengwa na mlima wa kuteremka bonde la ufa na hakuna miundombinu ya barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji hivyo vitongoji vyake vinaweza kusajiliwa kuwa kamili kwa maana ya Kijiji cha Mukulu kwa vitongoji vitatu vya Kijiji cha Nduamughanya na Kijiji kipya cha Gairo kwa vitongoji vitatu vya Kijiji mama cha Sagara, vijiji tarajiwa vipya viwili tayari vimekwisha jenga shule za msingi ambazo zimekwishasajiliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sekta ya afya, tunashukuru Serikali kwa kututengea bajeti ya shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa hospitali mpya ya wilaya. Aidha, Halmashauri ya Singida ina vituo viwili tu vya afya (Ilongero na Mgovi) ambavyo havitoi huduma ya dharura ya upasuaji kutokana na kukosa miundombinu na wataalam.

Niiombe Serikali kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya haina hospitali ya wilaya na kwa sasa inategemea hospitali ya Mission ya Mtinko na ya Rufaa ya Mkoa wa Singida ama Hydom Mkoani Manyara. Serikali itoe kipaumbele kwa vituo hivi viwili vya afya kupatiwa fedha za ukarabati na vifaa ili kunusuru maisha ya wananchi zaidi ya 280,000 wa jimbo hili.

Mheshimiwa, Mwenyekiti, zipo changamoto nyingi katika suala la elimu ya msingi na sekondari hasa katika miundombinu ya shule. Zipo shule katika jimbo langu mfano Shule ya Mikuyu iliyopo Kata ya Makuro ina madarasa mawili tu tangu watoto wa awali hadi darasa la sita na imesajiliwa na SG 02/2/040. Kwa sasa ina jumla ya wanafunzi 476, hakuna nyumba hata moja wa Walimu, ina choo cha muda, matundu manne kwa Walimu na wanafunzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ipo shule ya Msingi ya Ntundu, Kata ya Kinyeto yenye wanafunzi zaidi ya 1,600 na vyumba sita tu vinavyotumika, wanafunzi wanasomea nje kwenye eneo la wazi na Mwalimu anazunguka na kibao uwanjani kufundisha. Hili hii haiwezi kuleta maendeleo kwa watoto wetu na kuongeza ufaulu. Niombe Serikali iangalie shule hizi kwa jicho la pekee kusaidia juhudi za wananchi na halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali iangalie juhudi za wananchi katika ujenzi wa maabara nyingi ambazo hazijakamilika, zikamilishwe ili kuanza kutoa huduma kwa kuwa wananchi sasa wana kazi ya kuanzisha ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari kutokana na ongezeko la wanafunzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa miundombinu ya barabara, Jimbo la Singida Kaskazini lenye jumla ya miundombinu ya barabara iliyohakikiwa ya kilometa 772.39 zimekuwa hazipitiki wakati wa mvua kutokana na zaidi ya kilometa 704.28 sawa na asilimia 91.18 kuwa za udongo. Naomba Serikali kwa kweli iweze kuongeza bajeti ili kuongeza urefu wa barabara za changarawe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi wa Tatu, tarehe 11 tulimwomba Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutusaidia kujenga barabara ya kilometa 42 kwa kiwango cha lami inayounganisha Kata za Kinyeto, Kinyagigi, Merya, Maghojoa, Msange na Itaja. Mheshimiwa Rais alikubali kupokea ombi letu na niombe Serikali sasa kutenga bajeti katika mwaka wa fedha 2018/2019 kuanza mchakato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Wizara ya Afya kwa juhudi kubwa zinazoonekana za kuongeza na kuboresha huduma za afya na usafi wa mazingira nchini. Hivyo kwa dhati kabisa naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na kuwatakia utendaji uliotukuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru sana Serikali kwa fedha za ujenzi wa hospitali shilingi bilioni 1.05 na ukarabati wa kituo cha afya cha Mgori shilingi milioni 400 na Msange shilingi milioni 700. Sambamba na mafanikio haya, tulipata pia usajili wa Hospitali ya St. Carolos Mtinko kuwa Hospitali Teule ya Wilaya. Sambamba na upatikanaji wa dawa kwa kiwango cha kuridhisha, hongera sana kwa Mheshimiwa Ummy na timu yake kwa mafanikio haya katika Jimbo la Singida Kaskazini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mafanikio hakukosi kuwa na changamoto, Jimbo la Singida Kaskazini lina wananchi zaidi ya 250,000 ambapo kwa wastani wa watu 5,000 kwa kituo cha afya tuna uhitaji wa zaidi ya vituo vitatu vya afya ili kuboresha utoaji wa huduma za afya. Hivyo niombe Wizara kwa moyo wa dhati kutusaidia fedha za ukarabati kwa kituo cha afya cha Ilongero na angalau ukamilishaji wa majengo yaliyoanzishwa na wananchi kwa Kata za Ngimu na Makuro ambayo yana zaidi ya miaka nane kusubiri kupauliwa. Ningeshauri kwa hatua ya sasa tuombe shilingi milioni 300 kukamilisha hatua ya awali tukisubiri upanuzi katika awamu zinazokuja.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua pia juhudi za Serikali katika kuongeza Watumishi wa Sekta ya Afya, hivyo niombe sana Serikali kutusaidia watumishi katika Hospitali Teule ya Wilaya (St. Carolos Mtinko) na zahanati na kituo cha afya. Vilevile uboreshaji na usimamizi wa Maendeleo ya Jamii unahitajika maana kuna huduma zisizoridhisha kabisa kwa wananchi hasa vijijini. Hii inatokana na usimamizi usioridhisha na ukosefu wa vitendea kazi ambavyo vimekuwa ndiyo visingizio vya kutokutekeleza wajibu wao. Mheshimiwa Waziri tumefanya kazi kubwa ila tusipoangalia watendaji hawa watatuangusha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa wananchi tutaendelea kushiriki katika miradi ya maendeleo inayopata fedha kutoka Serikalini na kuendelea na ujenzi wa zahanati katika vijiji vyetu ili kuunga mkono juhudi za Serikali kuboresha hali ya huduma nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira wa Mwaka 2018
MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika muswada huu ulioko mbele yetu, Muswada wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza nipende kuishukuru Serikali kwa kutuletea Muswada huu wakati huu, ni muswada muhimu ambao unatarajiwa kutunza, kuendeleza, kuboresha na kusimamia huduma za maji na usafi wa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji ni la muhimu sana. Rasilimali maji ni haki ya msingi ya kila mtu katika ulimwengu huu. Kwa hiyo, upo umuhimu wa kuweka utaratibu wa namna ya kuweza kutunza na kushughulikia huduma hizi katika jamii na matumizi yake katika sekta za kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile muswada huu unatuonesha pia umuhimu wa kuweza kuangalia, kuzuia na kudhibiti uchafuzi na uharibifu wa rasilimali maji. Kwa hiyo, ni muswada muhimu sana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu ningependa tuupitie kwa makini ili tuweze kuona kwamba unaweza ukatusaidia katika vizazi vijavyo maana rasilimali maji inazidi kupungua kadri wananchi tunavyoweza kuongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali Maji, Sheria Na. 11 ya mwaka 2009 ambayo inatoa haki kwa wananchi kuvuma maji ya mvua na kuyatumia, kuchimba visima, lakini vilevile sheria hiyo inatambua pia haki ya matumizi ya maji hasa katika vyanzo vile vya kimila ambavyo vinaongozwa na sheria za kimila.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yetu tulipitia muswada huu na kutoa mapendekezo ambayo, naishukuru sana Serikali kwamba kwa kiasi kikubwa sana mapendekezo tuliyotoa kwenye Kamati iliyachukua na imeyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo sheria kwa sasa ambazo zinaongoza matumizi ya maji, rasilimali maji na usafi wa mazingira ikiwemo ya DAWASA. Hata hivyo, sheria hizi zote bado zimeendelea kuwa na changamoto. Zilituletea changamoto kwamba tumekuwa na sheria ambazo zinaweza zikafanya kazi katika eneo moja. Kwa hiyo, umekuwepo umuhimu wa kuwa na sheria moja ambayo inasimamia rasimali maji katika nchi yetu yote kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii pia inakuja kuondoa mgongano ambao tumekuwa nao. Tumekuwa na mgongano katika Wizara ya Maji kama msimamizi wa sera, lakini vilevile Wizara ya TAMISEMI ambayo yenyewe sasa ilikuwa inatekeleza na kuratibu mipango yote ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni sheria ambayo inakuja kutuondolea tatizo hili ambalo tumekuwa nalo. Kwa hiyo, tunategemea baada ya kuwa tumetunga sheria hii, tutaongeza ufanisi, tutaimarisha miradi ya maji na kuifanya miradi ya maji kuwa endelevu. Hivyo basi, siwezi kusita kusema kwamba naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mwenyekiti wa Kamati alivyosema, awali tulipendekeza kubadilisha jina la RUWA kuwa RUWASA kwa maana ya Rural Water Supply and Sanitation Agency ili kusudi kuangalia masuala ya usafi wa mazingira ambayo katika maeneo mengi yamekuwa hayapewi umuhimu. Tunaishukuru sana Serikali kwa kukubali jambo hili na tuna imani kubwa sana kwamba masuala ya usafi wa mazingira yanaweza sasa yakafanyiwa kazi kuhakikisha kwamba yale maji, hata majitaka ambayo tumekuwa nayo yanaweza sasa yakatibiwa na yakawa disposed katika njia iliyo salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Ibara ya 22 pale, inaonesha eneo la hifadhi ya miradi ya maji. Hifadhi ya miradi ya maji kwa mfano kwa bomba ambalo linaanzia kipenyo cha milimita 1,200 kwamba hifadhi hiyo sasa inatakiwa kuwa hifadhi ya mita 30. Maana yake mita 15 upande mmoja na mita 15 upande mwingine. Kwa kipenyo cha mita 10, I mean kipenyo cha mita 400 mpaka 1,200 ni mita 10 kwa maana ya mita tano kwa kila upande na kipenyo cha milimita 150 mpaka 400 kuwa mita nne kwa maana ya mita mbili kila upande.

Mheshimia Mwenyekiti, suala hili ni jema lakini Kamati yetu tuliona kwamba suala hili ni lazima liambatane na fidia kwa wananchi hasa wale ambao tayari wameshamiliki hayo maeneo. Isije ikatumika vibaya kwamba sasa tunatunga sheria ambayo inatoa mamlaka kwa chombo hiki ambacho tunakianzisha kutoa maeneo ya wananchi ambao tayari wanayamiliki kwa maana ya hifadhi ya mabomba ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumependekeza sana kwamba lazima pawepo na fidia stahiki, fidia ya haki, tena kwa wakati kabla ya kutoa eneo hili ambalo ni la hifadhi ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ukienda kwenye ibara ya 50 ambayo yenyewe inashugulikia masuala ya vyanzo; 50(1) inaongelea habari ya vyanzo vya mapato kwa Wakala wa Maji ambao umeanzishwa, RUWASA. Kamati ilipendekeza kwamba ile shilingi 50/= ambayo ni tozo kutoka kwenye mafuta yote ingetoka kwenye Mfuko wa Maji ya kupelekwa kwenye Wakala huu ili kusudi uweze kutekeleza majukumu yake ya kutoa maji katika maeneo ya vijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mazungumzo na Serikali, vilevile tulikubaliana kwamba jambo hili liangaliwe vizuri katika kanuni kwa sababu kwa sasa kinachoonekana chanzo hiki kimekuwa ndiyo kikubwa na chenye uhakika katika sekta ya maji na hata maeneo ambayo yamesemwa ya Mijini, yale ya pembezoni mwa miji bado yana shida kubwa sana ya maji na hivyo kuwa na uhitaji mkubwa sana wa kupata fedha hizi ambazo ndiyo chanzo muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumekubaliana kwamba zitatungwa kanuni ambazo zitaletwa kenye Kamati kabla hazijaanza kutumika ili kusudi tuweze kukubaliana na kuridhia kuona namna ya mgawanyo wa fedha hizo kwa ajili ya huduma za maji. Kwa sababu tunalo tatizo kubwa sana kwenye maeneo ye vijiji na pengine katika maeneo ya pembeni mwa miji ambayo ni peri-urban areas.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia Ibara ya 61 ambayo inaongelea adhabu na makosa mbalimbali, kama walivyoanza kusema wenzangu, tulikuwa na mapendekezo ya adhabu, nasi tuliona kwamba adhabu hizi zilizowekwa kwa kweli ni vyema zikabadilishwa na zikawekwa kwa mtu mmoja na makampuni, tukaangalia kwa watu ambao wanatumia kwa matumizi ya nyumbani lakini na kwa matumizi ya kibiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kama tulivyoeleza kwenye report ya Kamati, kwamba vilevile tuangalie hata uharibifu unaojitokeza ni uharibifu katika aina ya mabomba ya size gani? Isije ikawa mtu amevunja tu bomba la nchi sita, akapigwa shilingi milioni 50 halafu yule aliyekwenda kuvunja bomba kule nchi hata 45 au 50 yeye akaenda akapigwa faini ya shilingi milioni tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tulipendekeza kwamba adhabu hizo zitengwe; na kwa mtu binafsi zisizidi shilingi milioini tano. Kwa hiyo, zianzie shilingi 500,000/= mpaka shilingi milioni tano na kuanzia shilingi milioni tano kwenda kwenye shilingi milioni 50 iwe ni kwa ajili ya taasisi na makampuni na hasa kwa kuzingatia pia ukubwa wa mabomba tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, tumeomba pia tafsiri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa kwa mchango wako.

MHE. JUSTIN J. MONKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)