Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Advocate Damas Daniel Ndumbaro (3 total)

MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Tano imeusaidia sana Mji wa Songea kwa kuleta ndege za Bombadier ambazo zinatoa huduma zake katika Uwanja wa Ndege wa Songea.
• Je, kwa nini uwanja huo hauongezwi urefu na kufanyiwa ukarabati ili kutoa huduma zaidi na kuruhusu ndege ziweze kutua kwa saa 24?
• Je, kwa nini Serikali haiweki mashine za ukaguzi wa abiria (scanning machine) ili kuondoa adha kwa abiria kukaguliwa mizigo yao kwa kupekuliwa ambapo inadhalilisha na kupoteza muda?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Damas Daniel Ndumbaro, Mbunge wa Songea Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanja cha Ndege cha Songea ni miongoni mwa viwanja 11 nchini vilivyofanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia mradi wa Transport Sector Support Project. Usanifu huu ulikamilika mwezi Juni, 2017 na ulihusisha usanifu wa miundombinu ya viwanja hivi kwa ajili ya upanuzi na ukarabati ili kukidhi mahitaji ya viwanja hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa Wizara yangu, kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), inaendelea na taratibu za kumpata Mkandarasi pamoja na Mhandisi Mshauri kwa ajili ya kazi za awamu ya kwanza za upanuzi na ukarabati wa kiwanja cha ndege cha Songea, ambazo zitahusisha ukarabati wa barabara ya kutua na kuruka ndege, barabara za viungio, maegesho ya ndege, kusimika taa pamoja na mitambo ya kuongozea ndege, hivyo kuruhusu ndege kuruka na kutua kwa saa 24.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara kwa kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imenunua mashine za ukaguzi wa abiria na mizigo kwa ajili ya viwanja vya ndege vya Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma na Songea na tayari mashine hizo zimepelekwa katika viwanja husika, kikiwemo kiwanja cha ndege cha Songea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa mafundi wanaendelea na zoezi la kufunga mashine hizo ambapo tunatarajia ifikapo katikati ya mwezi huu wa Aprili, 2018, kazi ya kufunga mashine hizo itakuwa imekamilika na hivyo mashine hizo kuanza kutumika katika viwanja hivyo, kikiwemo Kiwanja cha Songea.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO (K.n.y MHE. DKT. DAMAS NDUMBARO) aliuliza:-
Wananchi wa Kata ya Matogoro na Kata ya Seedfarm wanaidai Serikali fidia inayotokana na Serikali kutwaa ardhi yao katika Bonde la Mto Ruhira na mpaka sasa bado hawajalipwa fidia ili wapate ardhi mbadala:-
(a) Je, ni lini Serikali itawalipa wananchi hao fidia stahiki?
(b) Je, Serikali ipo tayari kulipa riba inayotokana na ucheleweshaji wa kulipa fidia ya ardhi kwa wananchi hao?
NAIBU WA WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Damas Daniel, Mbunge wa Songea Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli wananchi 803 ambao walikuwa ndani ya mita 60 kutoka kwenye chanzo cha Mto Ruhira walipisha maeneo yao ambapo maeneo hayo kwa sasa yanatumika kama chanzo cha maji kwa wananchi wa Manispaa ya Songea.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2015 Serikali kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Songea ilifanya tathmini ambapo jumla ya kiasi cha Sh.1,477,475,000 zilihitajika kwa ajili kulipa fidia kwa wananchi hao. Mwaka 2018 Serikali ilifanya mapitio ya tathmini ya fidia hiyo ili kuendana na thamani halisi ambapo kwa sasa fidia hiyo imefikia kiasi cha Sh.1,913,832,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inakamilisha taratibu za kulipa fidia hiyo kwa kulipa shilingi milioni 500 katika mwaka wa fedha 2017/2018 na kiasi kilichobakia kitalipwa katika mwaka wa fedha 2018/2019.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO (K.n.y. MHE. DKT. DAMAS D. NDUMBARO) aliuliza:-
Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha maendeleo ya michezo mbalimbali lakini sheria inayosimamia michezo ya mwaka 1967 ina upungufu makubwa sana.
(a) Je, kwa nini Serikali haijatunga sheria mpya ya michezo ambayo itakwenda sambamba na mahitaji ya jamii kwa sasa?
(b) Je, kwa nini Serikali haina bajeti kwa ajili ya Timu za Taifa zinazobeba bendera kwa ajili ya kuitangaza nchi Kimataifa?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba kwa ridhaa yako kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ndumbaro nitoe pongezi kwa Mabingwa wa Ligi ya Tanzania Bara Simba, kwa kufanikiwa kutinga fainali ya michuano ya Sport Pesa Super Cup nchini Kenya. Simba wamethibitisha kuwa hawakupata ubingwa wa Tanzania Bara kwa kubahatisha, bali kwa soka la viwango na sasa wanaingia fainali kupambana na mabingwa wa Kenya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Damas Daniel Ndumbaro, Mbunge wa Songea Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iko katika hatua za mwisho kabisa kukamilisha maboresho ya sera ya michezo ya mwaka 1995 na sera mpya tutakayoipitisha ndani ya mwaka huu, itakuwa msingi wa sheria mpya ya michezo nchini.
b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya michezo nchini ambayo inaendana na ukubwa wa mashindano yanayotukabili. Kwa mfano, mwakani Tanzania ni mwenyeji wa mashindano ya AFCON ya mpira wa miguu kwa vijana chini ya umri wa miaka 17. Hivyo, mbali na vyanzo vingine vya fedha, Bunge hili tukutu limeidhinisha shilingi bilioni moja itumike kuboresha miundombinu ya Kiwanja cha Taifa na Kiwanja cha Uhuru na shilingi 293,619,000 kwa maandalizi mengine yanayohusiana na AFCON.