Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Nuru Awadh Bafadhili (4 total)

MHE. NURU A. BAFADHILI aliuliza:-
Askari Polisi wengi katika Jiji la Tanga wanaishi uraiani ambapo ni kinyume cha maadili kutokana na ukosefu wa nyumba za kuishi katika kambi zao.
• Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga upya nyumba za askari hao?
• Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwajengea nyumba za ghorofa askari wa Kambi za Chumbageni, Mabawa na Madina Msambweni, ili ziweze kuwaweka askari wengi katika eneo moja, kama ilivyo Kilwa Road Dar es Salaam?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nuru Awadh Bafadhili, Mbunge wa Viti Maalum, lenye kipengele (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uchakavu wa nyumba za kuishi askari katika Jiji la Tanga na maeneo mengine hapa nchini. Katika kukabiliana na tatizo la uchakavu na upungufu wa nyumba za kuishi askari polisi, Serikali ina mpango wa kujenga nyumba mpya katika Jiji la Tanga na maeneo mengine kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaona umuhimu wa kujenga nyumba za ghorofa kwa ajili ya makazi ya askari, kama ilivyojenga nyumba za Kilwa Road Jijini Dar es Salaam, Ziwani kwa upande wa Zanzibar pamoja na Buyekela Mwanza kwa kuwa zina uwezo wa kuchukua familia nyingi katika eneo dogo la ardhi. Aidha, taratibu za ujenzi wa nyumba za kuishi askari polisi Jijini Tanga zitakapoanza wataalam watazingatia ushauri wa Mheshimiwa Mbunge.
MHE. ALFREDINA A. KAHIGI (K.n.y. MHE. NURU A. BAFADHILI) aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani madhubuti wa kuhakikisha vijana wetu wanakuwa na maadili pamoja na silka na desturi za Kitanzania kama walivyo wazazi wao?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nuru Awadhi Bafadhili, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kusisitiza kuwa wazazi na familia kwa ujumla ndiyo walezi wa kwanza wenye jukumu la makuzi ya mtoto kuanzia hatua za awali. Wazazi hufuatiwa na vyombo vya elimu kuanzia elimu ya awali, msingi, sekondari hadi elimu ya juu. Jukumu la kusimamia malezi na makuzi ya watoto na vijana ni pamoja na kuelimisha kwa maneno na vitendo kuhusu utambuzi wa mambo mema na mambo mabaya, mambo yanayofaha na mambo yasiyofaha yanayostahili na yasiyostahili yakiwemo masuala ya mavazi, kauli, staha, mwenendo pamoja na muonekano kwa vijana.
Mheshimiwa Spika, hatua ya awali ya malezi ya makuzi ikishapita ndipo wajibu mkubwa wa Serikali unajitokeza katika ukuaji wa vijana kupitia sera, kanuni, sheria, taratibu pamoja na miongozo na kwa kutumia majukwaa mbalimbali ya elimu na nasaha kama vile semina, warsha, makongamano, mikutano, maonesho pamoja na matamasha.
Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa inayolikabili Taifa letu leo ni athari ya utamaduni wa nje kwa maadili, mila na desturi zetu kupitia muingiliano mkubwa wa watu wa dunia kwa njia ya utalii, biashara na kadhalika, vilevile kupitia maendeleo ya kasi ya TEHAMA. Pamoja na juhudi za Serikali kudhibiti wimbi la utamadunisho hasi nchini kwa kutumia sheria, kanuni na vilevile kuboresha mitaala yetu toka shule ya msingi hadi elimu ya juu ili izingatie elimu ya uraia, utaifa, uzalendo, mchango wa wazazi na wananchi kwa ujumla katika kufanikisha jitihada za Serikali hauna mbadala. (Makofi)
MHE. NURU A. BAFADHILI aliuliza:-
Shule za Serikali na shule binafsi zina mitaala tofauti, je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuwa na mfumo mmoja wa mitaala?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI (K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nuru Awadhi Bafadhili, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtaala hutolewa kwa lengo la kuweka mwongozo mpana wa viwango vya utoaji elimu kwa kuzingatia idadi ya masomo yatakayofundishwa, umahiri utakaojengeka, njia za ufundishaji na kujifunzia, vifaa vya ufundishaji, upimaji, ufuatiliaji na tathmini za mtalaa husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtalaa unaotumika katika shule za Serikali na shule binafsi ni mmoja na wanafunzi wote wanaosoma shule hizo hupata umahiri unaofanana. Aidha, mtalaa ambao ni tofauti ni ile mtu inayotumika katika shule chache za kimataifa (international schools) zilizopo nchini. Mitalaa hii ya kimataifa imeruhusiwa ili kukidhi mahitaji ya raia wa kigeni wanaoishi hapa nchini.
MHE. NURU A. BAFADHILI aliuliza:-

Katika kipindi cha miaka ya 1970 wakati wanafunzi wakienda likizo walimu walikuwa wakienda katika vyuo mbalimbali vilivyokuwa jirani na wilaya zao ili kupewa mafunzo au kupigwa msasa (refresher courses) kiasi kwamba walimu walikuwa wanapata ari ya kufundisha vizuri:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kurudisha utaratibu huo kwa walimu kupigwa msasa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nuru Awadh, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutoa mafunzo endelevu kwa walimu kazini kulingana na upatikanaji wa fedha. Mafunzo hayo yanalenga kuboresha utendaji kazi na kutoa motisha kwa walimu ili kuinua ubora wa elimu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2018/2019, jumla ya walimu wa Shule za Msingi 1,598 wamepata Mafunzo juu ya Ufundishaji na Ujifunzaji wa Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK). Aidha, walimu wa Shule za Msingi 200 na Sekondari 198 wamejengewa uwezo katika Ufundishaji na Ujifunzaji wa somo la Hisabati. Vilevile, walimu wa Elimu Maalum 804 wamejengewa uwezo katika Ufundishaji na Ujifunzaji wa wanafunzi wenye Mahitaji Maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imetenga kiasi cha Sh.502,807,348 kwa ajili ya kufanya mapitio na tathmini ya Vituo vya Walimu (TRC) kwa lengo la kuviwezesha kutoa mafunzo kazini kwa walimu kama ilivyokuwa inafanyika hapo awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali inakamilisha maandalizi ya Kiunzi cha Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini ambacho kitatoa utaratibu wa uendeshaji wa mafunzo hayo ili kuweka msukumo zaidi wa mafunzo kazini. Napenda kutumia nafasi hii kuzihamasisha Halmashauri zote nchini kutenga fedha kwa ajili ya mafunzo kazini kwa ajili ya walimu.